Abu Bakr Asw-Swiddiyq (رضي الله عنه)

 

 

Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu)

 

Khalifa Wa Kwanza Aliyeongoka

 

Muhammad Faraj As-Sa'ay (Rahimahu Allaah)

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

 

 

 

Share

01-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Akiutafuta Ukweli Kabla Ya Muhammad ( صلى الله عليه وسلم) kupewa Utume

 

 

01- Abu Bakr Asw  -Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu)

Akiutafuta Ukweli Kabla Ya Muhammad

(Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) Kupewa Utume

 

Alhidaaya.com

 

 

Kabla ya kuja kwa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hapakuwa na wanaomuabudu Allah isipokuwa watu wachache sana wakiwemo wafuatao:

 

Qussa bin Saaida

Zayd bin 'Amr

Waraqah bin Nawfal (aliyekuwa akifuata dini ya Kimasihi) na Abi Qays ibn Anas.

 

Hawa walikuwa wakisema wazi wazi kuwa wao wanamuabudu Allaah wa kweli Rabb wa Ibraahiym ('Alayhis-Salaam).

 

Ma-Quraysh hawakuwadhuru watu hao kwa sababu hawakuwa wakiitukana miungu yao, na pia kwa sababu walikuwa na wafuasi wachache sana waliokuwa wakiwaendea na kuwasikiliza.

Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa miongoni mwa wachache hao.

 

Alikuwa akihudhuria vikao vyao na kuwasikiliza wakizungumza juu ya Allaah wa kweli aliyekuwa akiabudiwa na Ibraahiym na Ismaa'iyl ('Alayhima-salaam), na juu ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye wakati wa kuja kwake umekwishawadia, na kwamba Mtume huyu ndiye atakayewarudisha watu katika ibada ya Allaah mmoja wa kweli.

 

Vikao hivyo ndivyo vilivyomsaidia Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuiona nuru ya Utume kwa haraka, akawa anajitayarisha na kuisubiri.

 

Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa mfanya biashara marufu sana mwenye kujulikana kwa uaminifu wake hapo Makkah, heshima yake ilikuwa kubwa sana baina ya ma-Quraysh, na alikuwa mtu mwenye elimu kubwa ya kuhifadhi nasaba za makabila na mataifa ya Kiarabu, na kwa ajili hiyo alipewa yeye jukumu la kushughulikia mambo ya fidia panapotokea matatizo hayo baina ya makabila..

 

 

Share

02-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Safari Ya Shaam

 

Aliposafiri kwenda Shaam (Syria) akifuatana na wafanya biashara wenzake, Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) aliyakuta yale yale yaliyoko Makkah.

Watu na akili zao, mashujaa, wafasihi wa lugha, washairi wakubwa, walikuwa wakiyaporomokea masanamu na kuyasujudia. Na hali hii ndiyo ilivyokuwa Bara ya Arabuni kote.

Na huko Shaam pia walikuwepo wachache waliokuwa wakizungumza juu ya dini ya Nabii Ibraahiym ('Alayhis-Salaam) na juu ya kumuabudu Mungu wa kweli asiye na mshirika.

Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) akawa anawaendea watu hao na kusikiliza maneno ya Imani kutoka kwao.

Walikuwepo wengine waliokuwa wakisoma Taurati na Injili mfano wa Waraqah bin Nawfal kule Makkah. Hawa walikuwa wakizungumza juu ya dini mpya ambayo muda wake umeshakaribia na juu ya Mtume mpya ambaye wakati wa kuja kwake umeshawadia, na kwamba Mtume huyo atatokea katika nchi ambayo Nabii Ibrahim aliijenga Al-Ka'abah.

Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) akawa anawaza;

Ni kweli Mtume atatokea katika nchi ile iliyojaa watu wanaoabudu masanamu, walevi, wacheza kamari na wauwaji wa watoto wachanga wa kike? Hivyo Kweli anaweza akatokea mtume mahali kama pale penye watu wenye tabia ovu kama zile? 

Alikuwa akijiuliza hivyo nafsini mwake kisha akijijibu mwenywe;

Na kwa nini asitokee Mtume wakati daktari haitwi mpaka pawepo na mgonjwa?

Isitoshe, watu wa Makkah juu ya kuwa na mabaya yote hayo, lakini walikuwa na sifa nyingi njema.

Walikuwa maarufu kuwa ni wasema kweli, na uwongo kwao ulikuwa ni aibu kubwa sana. Ukarimu ulikuwa ni moja ya sifa zao, walikuwa wakiwaambia watumwa wao;

"Atakayeweza kuniletea wageni wengi nitampa uhuru wake".

Watu wenye tabia kama hizi kwa nini asitokee Mtume miongoni mwao?"

Akawa anaikumbuka siku ile Qussa bin Saaida alipoingia ndani ya msikiti wa Al Kaaba bila ya kuwaogopa washrikina huku akisema;

"Labayka Mola wa kweli, Labayka Mola wa kweli, najikinga kwa yule aliyejikinga kwake Ibraahiym".

Yote haya yaliyokuwa yakimpitikia akilini mwake alipokuwa huko Shaam yaliujaza moyo wake shauku kubwa ya kumsubiri Mtume huyu mpya atakayeujaza ulimwengu Nuru ya dini ya Haki na kuwaondolea Makureshi na watu wote balaa hili la kuwasujudia masanamu.

Share

03-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Ikiwa Yeye Amesema Hivyo Basi Mimi Namsadiki

 

Siku zikapita kwa haraka sana, na safari ya kurudi Makkah ikawadia, na usiku kabla ya safari yake, Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliota ndoto ya ajabu sana. Aliota kuwa mwezi umepasuka na vipande vya nuru yake vimeanguka, vikapukutika na kuingia ndani ya kila nyumba ya Makkah.

Asubuhi yake akawaendea wale wacha Mungu aliokuwa akihudhuria darsi zao na kuwauliza juu ya tafsiri ya ndoto yake hiyo, na wote wakamwambia kuwa inaleta bishara njema.

Safari ikaiva. Ngamia wakaanza kuondoka kuelekea Makkah, na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akiielezea safari hiyo alisema:

"Ngamia siku hiyo walikuwa wakitoa sauti za furaha kama kwamba  wanasherehekea sikukuu."

Mara baada ya kuwasili Makkah, wafanya biashara na wanunuzi wa kawaida wakawa wanausogelea msafara huo kwa ajili ya kununua bidhaa zitokazo nchi ya Sham. Wengine walikuwa wakipatana na wengine wakizungumza, wote walikuwa wakipaza sauti zao, na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliwasikia baadhi yao wakizungumza juu ya Mtume mpya aliyedhihiri hapo Makka na namna anavyodai kuwa anapata habari za mbinguni.

Alipounyanyua uso wake akamuona Abu Jahl (Amr ibn Hisham) akimsogelea na kumvamia kwa masuali:

"Umesikia juu ya rafiki yako Muhammad ewe Atiq?" (Atiq lilikuwa jina la kubandikwa la Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu).

Abu Bakr  :      "Amepatwa na jambo gani?"

Abu Jahl :       "Muhammad anadai kwamba eti yeye ni Mtume na kwamba eti anapata habari kutoka mbinguni" .

Abu Bakr :       "Nani anayemletea habari hizo?"

Abu Jahl :       "Anasema eti Malaika aitwaye Jibril."

Abu Bakr :       "Yeye mwenyewe amesema hivyo?"

Abu Jahl :       "Ndiyo! nimemsikia kwa sikio langu."

Abu Bakr :       "Ikiwa yeye mwenyewe ametamka hivyo basi mimi namsadiki."

Abu Jahl hakuweza kustahamili msituko huo na miguu yake ikaaanza kutetemeka, akakaa chini.

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akaona bora kwanza aende nyumbani akawaone watu wake na kuitua mizigo yake, kisha ende nyumbani kwa sahibu yake Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa  aalihi wasallam) na kumsikiliza.

 

Share

04-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Mkweli Mwaminifu

 

Alipokuwa akielekea nyumbani, Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) akawa anaikumbuka siku ilee jiwe jeusi lilipoanguka kutoka mahali pake baada ya kunyesha mvua kali, dhoruba na upepo na mafuriko makubwa, na sehemu kubwa ya msikiti kubomoka.

ma-Quraysh walikubaliana kuujenga upya msikiti huo, lakini mgogoro mkubwa ukazuka wakati wa kulirudisha jiwe jeusi mahali pake, kwani kila kabila lilitaka heshima ya kulirudisha jiwe hilo.

Akawa anakumbuka namna ma-Quraysh walivyokuwa tayari kupigana, pata shika panga mkononi, na mgogoro huo uliendelea muda wa siku tano bila kupatikana suluhisho, mpaka pale aliposimama Aba Umayya Ibn Al Mughira Al Makhzumy na kutoa shauri lake maarufu aliposema;

"Wa mwanzo kuingia msikitini kupitia mlango huu ndiye atakayehukumu baina yetu". 

ma-Quraysh wote kwa pamoja wakalikubali shauri hilo.

 

Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) akawa anakumbuka namna gani ma-Quraysh walivyokaa kimya siku ile wakingoja na kusubiri kwa hamu kubwa nani atakayeingia mwanzo kupitia mlango ule atakayeweza kutoa hukumu itakayowatoa katika janga hilo la kuuwana na kumwaga damu.

Ghafla! Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akatokeza baada ya kuingia kupitia mlango huo, na ma-Quraysh wote kwa pamoja wakapiga ukelele wa furaha huku wakisema;

"Asw-Swaadiq Al-Amiyn" (Msema kweli Mwaminifu),  Sote tuko radhi juu ya uamuzi atakautoa Mkweli Muaminifu".

 

Akawa anaikumbuka miaka 40 alioishi naye akiwa sahibu yake mpenzi, Msema kweli, asiyepata kumsikia hata siku moja akitamka neno la uongo. Hata katika mzaha alikuwa akisema kweli tupu. Kisha akawa anajisemesha nafsini mwake;

"Leo mtu huyu aje aseme uongo, tena juu ya Mwenyezi Mungu? La, haiwezekani kabisa.

Wakati vijana wenzake walipokuwa wakenda ngomani na kuhudhuria sherehe mbali mbali, Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) hakuwa akijishughulisha na mambo hayo, bali alikuwa akisema kuwa yeye hakuumbwa kwa ajili ya mchezo".

 

Share

05-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Abu Bakr ( رضي الله عنه ) Anazitamka Shahada Mbili

 

Yote haya yalikuwa yakimpitia Abu Bakr akilini mwake huku akielekea nyumbani kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kutua mizigo yake, na baada ya kusalimiana na watu wake.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposikia mlango unagongwa akamtaka mkewe Bibi Khadija (Radhiya Allaahu ‘anhu) akatizame nani aliye mlangoni.

Bibi Khadija (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema; "Abu Bakr huyo"

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Mfungulie".

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akaingia, na baada ya kusalimiana akaanza kuuliza;

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu): "Ni kweli wanayosema juu yako?"

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Wanasema nini?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu): "Wanasema kuwa wewe unasema umepata Utume na kwamba unapata

habari kutoka mbinguni."

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Na wewe uliwajibu nini?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu): "Niliwaambia; Ikiwa kweli umesema hivyo basi mimi nasadiki."

Furaha ilimjaa Bwana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na machozi kumlengalenga. Akamkumbatia Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kukibusu kipaji cha uso wake, kisha akakaa na kuanza kumhadithia namna alivyojiwa na Jibriyl katika Pango la Hiraa na jinsi alivyobanwa na Malaika huyo na kumtaka asome aya tano za mwanzo za Suratul 'Alaq:

"Soma kwa jina la Mola wako aliyeumba. Aliyemuumba mwanadamu kwa pande la damu. Soma, na Mola wako mkarimu sana. Ambaye amemfundisha (binadamu ilimu zote hizi kwa msaada) wa kalamu. Amemfundisha mwanadamu (chungu ya) mambo ambayo alikuwa hayajuwi ."

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa akiyasikiliza yote hayo kwa utulivu mkubwa, akatizama chini kwa khushuu, kisha akatamka;

"Ash-hadu al-laa ilaaha Illa Allaah wa ash- hadu annaka RasuluLlaah".

(Nashuhudia kuwa hapana mungu anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah, na nashuhudia kuwa wewe ni mjumbe wa Allaah).

Hivi ndivyo alivyosilimu Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu).

 

 

Share

06-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Abu Bakr ( رضي الله عنه ) Anaanza Kazi Ya Kuwasilimisha Watu

 

Siku ya pili yake Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) aliwasilimisha watano katika mabwana wa kabila la Kikureshi, nao ni 'Uthmaan bin Affan, Az-Zubayr bin 'Awwaam, 'Abdur-Rahmaan bin 'Awf, Sa'ad bin Abi Waqqaasw na Twalhah bin 'UbayduLLaah; akaja nao mpaka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), na wote hawa ni katika wale kumi waliokwisha bashiriwa Pepo .

Siku iliyofuata aliwasilimisha vigogo wengine wanne na kuja nao mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), nao ni 'Uthmaan bin Madh'uwn, Abu 'Ubaydah 'Aamir bin Al-Jarraah, Abu Salamah na Al-Arqam bin Abi Al-Arqam.

Nguvu ya Uislamu ikaongezeka, na Abu Bakr aliitumia mali yake yote katika kuunusuru Uislam na pia nguvu zake na daraja lake mbele ya ma-Quraysh, na vyote hivi vilisaidia sana katika kuujenga na kuuendeleza Uislamu, hata watu wakawa wanasema;

"Wasingeshikamana wawili hawa kama hivi, kwa jambo la upotovu."

 

Share

07-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Nasaba Yake

 

Jina lake ni 'Abdullaah bin 'Uthmaan bin 'Aamir bin 'Amru bin Ka'ab bin Sa'ad bin Tayim bin Murrah bin Ka'ab bi Luay Al-Qurashiy Al-Taymiy, na uhusiano wake na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) unakutana kwa Murrah bin Ka'ab, kwani jina la Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni Muhammad bin 'Abdillaah bin 'Abdil-Muttwalib bin Hsashim bin 'Abdi-Mansaf  bin Qusay bin Kilaab bin Murrah bin Kaa'b.

Jina la baba yake ni 'Uthmaan, lakini alikuwa maarufu kwa jina la Abu Quhaafah, kwa hivyo Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) alikuwa akijulikana kwa jina Ibni Abi Quhaafah, yaani mwana wa Abu Quhaafah.

Mama yake ni Ummul-Khayr – Salmah binti Swakhr bin 'Aamir bin Ka'ab bin Saa'd bin Tayim bin Murrah bin Ka'ab na alikuwa binti 'ammi yake Abu Quhaafah.

 

Share

08-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Watu Wote Wa Nyumba Yake Walisilimu

 

Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) ni Swahaba wa pekee ambaye watu wake wote kuanzia wazee wake na jamii yake yote pamoja na watoto wake waliingia katika Uislamu.

Share

09-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Wakeze Na Wanawe

 

Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) alioa wake wanne;

Wakati wa ujahilia (kabla ya kuja kwa Uislamu) alimuoa Qutaylah binti Sa'ad na akazaa naye 'Abdullaah na Asmaa (Radhiya Allaahu 'anhaa).

'Abdullaah aliingia katika Uislamu tokea siku za mwanzo na alifariki wakati wa ukhalifa wa baba yake.

Asmaa (Radhiya Allaahu 'anhu) ni maarufu kwa jina la 'Dhaat Nitwaqayn', na alipewa jina hilo baada ya kukata 'Nitaaq' mkanda wa kitambaa kinachofungiwa nguo kiunoni na kukifunika chombo kilichotiwa chakula alichokuwa akipelekewa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) pamoja na Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) walipokuwa pangoni wakati wa kuhajir kwenda Madiynah, na alikuwa mkubwa kwa umri kuliko Bibi 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anhaa).

Aliolewa na Az-Zubayr (Radhiya Allaahu 'anhu) walipokuwa Makkah na alizaa naye watoto wengi mpaka alipomuacha akawa anaishi kwa mwanawe 'Abdullaah bin Az-Zubayr (Radhiya Allaahu 'anhumaa) aliyeuliwa Makkah.

Bibi Asmaa (Radhiya Allaahu 'anhaa) aliishi miaka mia, na mwisho wa maisha yake alikuwa kipofu.

 

Wakati wa ujahilia Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) alimuoa pia Umm Rumaan (Radhiya Allaahu 'anhaa) aliyezaa naye 'Abdur-Rahmaan na Bibi 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anhaa) mke wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na alifariki dunia wakati wa uhai wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliyeteremka kaburini kwake siku ya maziko na kumuombea maghfirah.

'Abdur-Rahmaan alipigana vita vya Badr na vita vya Uhud akiwa upande wa makafiri, na kabla ya kuanza vita vya Badr aliita kwa sauti kubwa akitaka mtu yeyote upande wa Waislamu aje kupambana naye na Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) alipotaka kutoka na kupambana na mwanawe huyo, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alimzuia na kumwambia;

"Tuache tukufaidi."

'Abdur-Rahmaan alikuwa shujaa na mtupa mshale mwenye shabaha aliyesilimu baada ya mapatano ya Hudaybiyah (Sulhul-Hudaybiyah), akawa Muislamu mwema aliyepigana vita mbali mbali akiwa upande wa Waislamu, alishiriki katika vita vya Al-Yamaamah chini ya uongozi wa Khaalid bin Waliyd (Radhiya Allaahu 'anhu) wakati majeshi ya Waislamu yalipopambana na majeshi ya Musaylimah Al-Kadhdhaab (Mtume wa uongo), na yeye ndiye mkubwa wa watoto wa Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) na alifariki dunia ghafla mahali panapoitwa Hibsh karibu na mji wa Makka katika mwaka wa 53 H.

Kitabu cha 'Abu Bakr al Siddiq – Muhammad Ridhwa

Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) alimuoa pia Asmaa binti 'Umays (Radhiya Allaahu 'anhaa) baada ya kuuliwa kwa mumewe wa mwanzo Ja'afar bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu 'anhu), wakapata mtoto waliyempa jina la Muhammad bin Abi Bakr.

Abu Bakr alipofariki dunia, Asmaa aliolewa na 'Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu 'anhu) akazaa naye mtoto waliyempa jina la Al-Qaasim.

 

Wakati wa Uislamu Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu) alimuoa pia Habiybah bint Khaarijah bin Zayd bin Abi Zuhayr Al-Khazrajiwakapata mtoto waliyempa jina la 'Aaishah Ummu Kulthuwm aliyeolewa na Twalhah bin 'Ubaydullaah (Radhiya Allaahu 'anhu).

Share

10-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Baadhi Ya Sifa Alizopewa Na Mtume Wa Allaah ( سبحانه و تعالى)

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimpa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) sifa nyingi sana, na zifuatazo ni baadhi chache sana ya sifa hizo;

 

Hakusita Wala Hakurudi Nyuma

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema;

"Mikono yote iliyotunyoshea tushailipa, isipokuwa wa Abu Bakr, msaada alioutowa ni Allaah tu ndiye Atakayemlipa".

"Wote niliowaita katika Uislamu walisita kwanza isipokuwa Abu Bakr, yeye hakusita wala kurudi nyuma, hapo hapo alisilimu."

[Al-Haakim].

 

Usiponikuta, Mwendee Abu Bakr

Mwanamke mmoja alimwendea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa na shida fulani, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyekuwa na shughuli nyingi sana wakati ule akamwambia;

"Nenda urudi siku nyingine".

Yule bibi akamuuliza;

"Nisipokukuta je?"

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia;

"Mwendee Abu Bakr'.

[Al-Bukhaariy]

 

Milango Yote Iliyoelekea Msikitini Ifungwe Isipokuwa Wa Abu Bakr

Siku moja Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipanda juu ya Mimbari na baada ya kumshukuru Allaah na kumpwekesha akasema;

"Allaah Alimshauri mja wake achaguwe iwapo anaitaka dunia au anataka yaliyo kwa Mola wake (anataka kwenda kwa Mola wake), na mja huyo akachagua yaliyo kwa Mola wake."

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliposikia maneno hayo akalia sana huku akisema;

"Kwa baba yangu na mama yangu nakufidia ewe Mtume wa Allaah".

Maswahaba waliohudhuria walishangazwa na kilio chake hicho wakawa wanasema;

'Vipi mtu huyu! Kipi kinachomliza wakati Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuhadithia juu ya mja aliyeshauriwa achague baina ya dunia na baina yaliyo kwa Mola wake na akachagua yaliyo kwa Mola wake?'

Hawakuwa wakijua kuwa aliyeshauriwa ni Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na kwamba alitakiwa achague baina ya kwenda kwa Mola wake au abaki nao duniani, na kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amechagua kwenda kwa Mola wake.

Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema;

"Katika watu walonisaidia sana kwa hali na mali ni Abu Bakr, ingelikuwa naweza kumchagua Khalil (Rafiki), basi angekuwa Abu Bakr, lakini ni undugu katika Uislamu na kupendana. Milango yote iliyoelekea msikitini ifungwe isipokuwa wa Abu Bakr".

[Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Hizi Ni Sifa Za Watu Wa Peponi

Siku moja Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliuliza;

"Yupi kati yenu asubuhi ya leo amefunga?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema;

"Mimi".

Kisha akauliza tena;

"Yupi katika yenu aliyehudhuria mazishi siku ya leo?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema;

"Mimi."

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akauliza tena;

"Yupi kati yenu aliyemlisha masikini siku ya leo?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema;

"Mimi."

Akauliza tena;

"Yupi katika yenu aliyemtembelea mgonjwa?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema;

"Mimi."

Kisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema;

"Hayajumuiki yote haya kwa mtu, isipokuwa ataingia Peponi."

[Muslim]

 

Wewe Ni Swahibu Wangu Penye Hodhi Na Peponi

Kutoka kwa 'Abdullaah bin 'Umar kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu);

"Wewe ni Swahibu yangu penye Hodhi na sahibu yangu wa Pangoni."

[At-Tirmidhiy]

 

Nani Aliye Bora Baada Ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

Siku moja Muhammad bin Hanafiyyah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye ni Mtoto wa 'Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu), alimuuliza babake;

"Nani aliye bora baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ?"

'Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) akajibu ;   Abu Bakr

Akauliza tena ;  Kisha nani

Akajibu ;           Kisha 'Umar

A[l-Bukhaariy]

 

Leo Mnataka Kumuacha Mkono Swahibu Yangu?

Siku moja Abu Bakr na 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhumaa) walijadiliana wakakhitalifiana, na Abu Bakr alimkasirisha 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhumaa) kwa kumwambia maneno yasiyomridhisha. Abu Bakr alimtaka msamaha 'Umar, lakini 'Umar alikataa Kumsamehe, kisha Abu Bakr akenda kumsikitikia Mtume(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

"Allaah keshakusamehe ewe Abu Bakr".

Wakati huo huo 'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyejuta kwa kutomsamehe Swahibu yake, alikuwa akimtafuta ili amtake yeye msamaha na akatokea wakati Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) amekaa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyekuwa amekasirika alipiga magoti mara baada ya kumuona 'Umar, lakini Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipomuona Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika hali ile akamwambia;

"Mimi ndiye niliyemkosea ee Mtume wa Allaah."

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema kumwambia 'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu);

"Allaah Alinituma kwenu nyote, na nyote mlinikadhibisha hapo mwanzo isipokuwa Abu Bakr. Yeye alisema "Swadaqta", basi leo mnataka kumwacha mkono Swahibu yangu?"

Anasema 'Umar bin Al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu);

"Tokea siku ile hapana mtu aliyethubutu kumkasirikia Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu)".

[Al-Bukhaariy]

 

Tulia Ewe Uhud

Siku moja Mtume(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipanda juu ya Jabali Uhud na jabali likatingishika. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akauweka mkono wake mtukufu juu ya jabali hilo huku akiliambia;

"Tulia ewe Uhud! Kwa hakika juu yako yupo Mtume, na Aliyesadiki (Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu)), na mashahidi wawili ('Umar na 'Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhumaa))".

[Al-Bukhaariy]

('Umar na 'Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhum), wote walikufa  mashahidi).

 

Na Amchaye Allaah

Allaah Anasema;     

“Na Amchaye (Allaah) ataepushwa nao (Moto).

Ambaye hutoa mali yake kwa ajili ya kujitakasa.

Na hali ya kuwa hakuna yeyote aliyemfanyia ihsani ili awe anamlipa.

Isipokuwa (anafanya haya) kwa kutaka Radhi ya Mola wake Mtukufu.

Basi atapata la kumridhisha.”

[Al-Layl: 16 – 21]

Maulamaa wa tafsiri wamekubaliana kuwa katika aya hizi Allaah anamsifia Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa sababu sifa zote zilizotajwa zinakwenda sambamba na mwenendo na tabia zake;

Allaah Anasema;

Na Amchaye (Allaah) ataepushwa nao (Moto).”

Hapana shaka kuwa Maswahaba wote ni wachaji Allaah, lakini ukiendelea kuzisoma na kuzichunguza vizuri zaidi aya zilizofuatilia utaona kuwa Allaah Ameongeza sifa nyingine inayomuelezea zaidi Swahaba huyu mtukufu (Radhiya Allaahu ‘anhu).

Allaah Anasema;

“Ambaye hutoa mali yake kwa ajili ya kujitakasa.

Na hali ya kuwa hakuna yeyote aliyemfanyia ihsani ili awe anamlipa.”

Wasfu huu unakubaliana na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) kupita mwengine yeyote kwa sababu yeye ndiye aliyekuwa akitoa mali yake yote kwa ajili ya kuwalisha na kuwavisha masikini pamoja na kuwakomboa Waislam waliokuwa watumwa na kuwaachia huru, yote haya kwa kutaka Radhi za Allaah. Na kisa cha kumkomboa Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) ni maarufu sana.

 

Sitoshindana Naye Tena

'Umar bin Al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) anasema;

“Siku moja Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alituamrisha tutoe Swadaqah, na siku hiyo nilikuwa na Mali (pesa nyingi), Nikasema leo nitamshinda Abu Bakr, nikampelekea Mtume(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nusu ya Mali niliyokuwa nayo.

Mtume(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaniuliza:

“Ahli yako umewabakishia nini?”.

Nikamjibu;

“Nimewabakishia kima kama hiki cha mali (yaani nusu yake)”.

Akaja Abu Bakr na mali yote aliyokuwa nayo, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza;

“Umewabakishia nini ahli yako ewe Abu Bakr”.

Abu Bakr akasema;

“Nimewabakishia Allaah na Mtume wake”.

Nikajisemea moyoni mwangu;

“Sitoshindana naye tena”.

[Abu Daawuwd na Ibni Maajah]

 

Oh! Mtamuua Mtu Kwa Sababu Anasema Mola Wake Ni Allaah?

Katika kuifasiri kauli ya Allaah isemayo;

“Na akasema mtu mmoja Mwislamu aliyekuwa mmoja wa watu wa Fir‘auni afichaye Uislamu wake; Oh! Mtamwua mtu kwa sababu anasema Mola wangu ni Allaah? Na kwa yakini yeye amekujieni kwa dalili wazi wazi zitokazo kwa Mola wenu!”

[Al-Muumin (Ghaafir): 28]

 

Katika kuifasiri aya hii anasema Imaam Al-Qurtwubiy;

Imepokelewa na Imaam Al-Bukhaariy na Muslim kuwa, Urwa bin Az-Zubayr, amesema;

“Nilimuuliza 'Abdullaah bin 'Amr bin Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu); Hebu nihadithie juu ya kubwa kabisa lililomkuta Mtume(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka kwa Mushrikina, akasema;

“Siku moja Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa nje ya Al-Ka'abah, akamtokelea 'Uqbah hbin Abi Mu'ayitw na kumshika mabega yake, kisha akamzungushia nguo shingoni pake na kumbana kwa nguvu kabisa, akatokea Abu Bakr na kumshika mabega yake ('Uqbah) na kumsukumilia mbali na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kisha akasema;

“Oh! Mtamuua mtu kwa sababu anasema Mola wangu ni Allaah?”

Hivi ndivyo alivyosimulia Al-Bukhaariy

Ama Hadiyth iliyopokelewa kutoka kwa At-Tirmidhiy inasema;

“Kutoka kwa Ja'afar bin Muhammad, kutoka kwa babake, kuwa 'Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema;

“Baada ya kufa kwa Abi Twaalib, ma-Quraysh walikusanyika na kutaka kumuuw Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wakamvamia, huyu akimburura na huyu akimsukuma, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawa anaomba  msaada, hapana aliyethubutu kusogea isipokuwa Abu Bakr, aliwaendea akamvuta huyu na kumsukuma yule huku akipiga kelele na kusema;

“Oh! Mtamuua mtu kwa sababu anasema Mola wangu ni Allah? Wa-Allaahi huyu ni Mtume Wake”.

(Ataqtuluuna rajulan an yaquula Rabbiya LLaah? Wa-Allaahi innahu larasuuluhu)

Imepokelewa kutoka kwa Al Bazaar katika Musnad yake kuwa Muhammad Bin 'Aqiyl (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa 'Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akikhutubu akasema;

“Enyi watu! Nani shujaa kupita wote?”

Wakasema;

“Wewe ewe Amiri wa Waislam”

'Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema;

“Ama mimi kila niliyepambana naye nimemshinda, lakini (shujaa kupita wote) ni Abu Bakr. Siku moja tulimjengea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hema kisha tukaulizana; ‘Nani atakayebaki na kumlinda Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ili asije akatokea mmoja katika Mushrikina na kumshambulia, basi Wa-Allaahi hapana aliyeingia isipokuwa Abu Bakr akiunyanyua upanga wake juu ya kichwa cha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kila kafiri aliyejaribu kumsogelea Abu Bakr alikuwa akimrukia (na kumkabili, huyu ni shujaa kupita wote.

Na siku hiyo nilimuona pale alipochukuliwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ma-Quraysh, huyu akimvuta na huyu akimsukuma, hapana aliyesogea siku hiyo isipokuwa Abu Bakr, alisogea akiwapiga na kuwasukuma, huku akisema;

“Ole wenu  Mtamuua mtu kwa sababu anasema Mola wangu ni Allaah? Wa-Allaahi huyu ni Mtume Wake”.

(Waylukum! Ataqtuluna Rajulan an yaquula Rabbiya LLaah?) Wa-Allaahi innahu larasuuluhu))”

Kisha 'Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) akalinyanyua guo alilokuwa amejifunika nalo na kuanza kulia mpaka ndevu zake zikaroa machozi.

 

 

Share

11-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Kuhajir Pamoja Na Swahibu Yake

 

Juu ya kuwa hapana uamuzi mzito kuliko mtu kuamua kuihama nchi yake, kuwaacha watu wake pamoja na nyumba aliyozaliwa ndani yake, na kuyaacha nyuma yote yanayomkumbusha utoto wake, sahibu zake wa utotoni pamoja na kuwa mbali na ardhi aliyocheza na kugaragara juu yake, lakini Waislamu iliwabidi wafanye hivyo baada ya washirikina wa Makkah kuwaonjesha kila aina ya adhabu na kuwazuwia wasiifanye kazi waliyokabidhiwa na Mola wao ya kuilingania dini Yake, dini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala).

Iliwabidi watafute ardhi nyengine, ardhi madhubuti itakayowawezesha kusimama imara juu yake kwa ajili ya kuifikisha kwa watu amana waliyopewa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) na pia kuwawezesha kujilinda kutokana na maadui wa Allaah. Mahali watakapoweza kujitayarisha kwa ajili ya kupigana Jihadi.

Kwa ajili ya lengo hilo adhimu, watu wa Madina walikuwa wakiwasubiri kwa hamu kubwa sana ndugu zao kutoka Makkah, kwani wao ndio waliokuja mahali panapoitwa Mina kwa ajili ya kufungamana na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Mafungamano mawili yaliyokuja kujulikana kwa jina la 'Fungamano la Aqaba' la kwanza na la pili na kumtaka Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ahamie kwao na kumuahidi kuwa watamlinda na kumsaidia katika kuilingania dini hii kwa hali na mali.

Wakati wa kuhama ulipowadia, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), alimwendea Sahibu yake Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kumtaka wafuatane pamoja kuelekea Madina, akamwambia;

"(Assuhba ya Aba Bakr)”.

Kabla ya hapo ma-Quraysh walikwisha amua kumuuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wakihofia kuwa akifanikiwa kuhamia Madiynah itakuwa rahisi kwake kujijenga na kuineza dini aliyokuja nayo na kuipiga vita dini yao iliyo baatwil.

Kwa kusudi hilo, wakatuma vijana kutoka matumbo mbali mbali ya kabila lao na kuwataka wote kwa pamoja wamchome Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa panga zao ili damu yake ichanganyike baina ya matumbo yote hayo, jambo litakalowazuwia jamaa zake wasiweze kudai kulipa kisasi cha mtu wao, na itawabidi waridhike  kwa kulipwa fidia tu.

Jibriyl (‘Alayhis Salaam) alimjulisha Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yote hayo na akamtaka aondoke usiku huo huo kuelekea Madina.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwita 'Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kumwakilisha jukumu la kurudisha amana za watu, akamtaka pia alale juu ya kitanda chake, kisha akatoka huku akiwasomea wale vijana waliokuja kumuwa waliokuwa wakimsubiri nje ya nyumba yake baadhi ya aya za Surat Yaasin, huku akiwanyunyizia mchanga juu ya vichwa vyao na kuwaacha hapo wakiwa wamelala usingizi mzito.

 

Alitoka na kwenda moja kwa moja mpaka nyumbani kwa Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu), na baada ya kumgongea mlango huku akiwa amejifunika uso wake, sahibu yake akatoka, wakaondoka wote kwa pamoja na kuelekea Madina kupitia njia ya pwani pwani kwa ajili ya kuwababaisha makafiri, kwa sababu njia hiyo kwa kawaida haikuwa ikitumiwa na wasafiri wanaokwenda Madina.

Walipowasili penye pango linaloitwa ‘Ghaari Thawr’ wakaingia humo kwa ajili ya kujipumzisha.

Alipokuwa akilichunguza pango hilo, Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akagundua mashimo mengi ndani yake ambayo nyoka, nge au wadudu wabaya wangeweza kupenya kupitia humo. Akachana nguo zake za kujifunikia na kuanza kuyaziba matundu hayo, isipokuwa moja alishindwa kuliziba baada kuishiwa na nguo za kuchana, akakaa karibu yake na kuliziba kwa mguu wake haidhuri adhurike yeye, lakini chochote kisipitie humo na kumdhuru Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitaka kupumzika, akalala karibu na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akiwa ameuweka uso wake mtukufu juu ya paja la Swahibu yake huyo, na haukupita muda wakaanza kusikia sauti za ma-Quraysh waliokuwa wakiwatafuta.

Sauti zikawa zinakaribia, na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu), alipoinama na kutizama nje aliweza kuona namna gani maadui hao walivyo karibu nao, akamwambia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam);

"Mmoja wao akiinama tu, atatuona ."

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia;

"Usihuzunike ewe Abu Bakr, Allaah yupo pamoja nasi, Unaonaje ikiwa wawili, watatu wao ni Allaah?"

 

Allaah Anasema:

"Ikiwa nyinyi hamtamnusuru (Mtume), basi Allaah alikwisha mnusuru walipomtoa waliokufuru, naye ni wapili katika wawili walipokuwa katika pango, naye akamwambia sahibu yake: ‘Usihuzunike. Hakika Allaah yu pamoja nasi’. Allaah akamteremshia utulivu wake, na akamuunga mkono kwa majeshi msiyoyaona, na akalifanya neno la waliokufuru kuwa chini, na Neno la Allaah kuwa ndilo juu. Na Allaah ndiye Mwenye nguvu Mwenye hikima."

 

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akatafunwa na nnge, katika mguu wake ule aliouweka juu ya tundu pale alipoishiwa na vitambaa vya kuzibia. Maumivu yakawa yanazidi, lakini alikhiyari kunyamaza na kustahamili asije akamshughulisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ingawaje alikuwa akijua kuwa sumu inatembea ndani ya damu yake na huenda ikamuua.

Maumivu yalikuwa makali sana hata chozi likamdondoka na kuanguka juu ya uso wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), aliyestuka na kuuliza:

"Kuna nini Abu Bakr, mbona unalia ?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema;

"Nimetafunwa na nnge ee Mtume wa Allaah" .

 Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akainuka na kuushika mguu pale ulipotafunwa, na kumuomba Allaah na hapo hapo sumu hiyo ikatoweka na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akapona.

 

 

Share

12-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Makubaliano ya Hudaybiyah

 

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikua akimfahamu na akimuelewa vizuri sahibu yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)kupita Maswahaba wote (Radhiya Allaahu ‘anhu), na alikuwa na uhakika kuwa yote anayoyasema ni Wahyi utokao kwa Mola wake (Subhaanahu wa Ta'aala.

Katika mwaka wa sita baada ya kuhamia Madiynah, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Maswahaba wake (Radhiya Allaahu ‘anhu) waliondoka Madiynah kuelekea Makkah kwa nia ya kufanya 'Umrah. Wakapiga kambi karibu na mji wa Makkah mahali panapoitwa Al-Hudaybiyah, kisha wakamtuma 'Uthmaan bin 'Affaan (Radhiya Allaahu ‘anhum) ende Makkah kuwajulisha Ma-Quraysh juu ya nia yao hiyo na kwamba hawakuja kwa nia ya kupigana vita.

Ma-Quraysh wakapeleka majeshi yao kutaka kuwazuia, na baada ya majadiliano marefu yaliyopita baina yao, wakaamua kumtuma mjumbe wao aitwaye Suhayl bin 'Amr, aliyeweza kufikia makubaliano na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), yaliyokuja kujulikana kwa jina la Makubaliano ya Al-Hudaybiyah.

Yafuatayo ni baadhi ya shuruti za makubaliano hayo;

·   Waislamu warudi Madiynah mwaka huu na wafanye 'Umrah mwaka ufuatao.

·    Waislamu wanalazimika kumrudisha kwa Makureish yoyote atakayeingia katika dini yao na kukimbilia Madiynah, lakini Ma-Quraysh hawalazimiki kumrudisha atakayetoka katika Uislamu na kukimbilia Makkah.

·   Wasipigane vita kwa muda wa miaka kumi, na wawe wanaendeana watakavyo.

 

Kabla ya mkataba huo kutiwa sahihi (saini), Waislamu walistukia kijana mmoja aitwae Abu Jandal aliyesilimu lakini alikuwa akiishi Makkah akipitishwa mbele yao akiwa amefungwa minyororo shingoni huku na kubebeshwa jiwe kubwa akipiga kelele akiwaomba Waislamu wenzake wamuokoe kutokana na adhabu hiyo.

Kijana huyu Abu Jandal ni mwana wa Suhayl, mjumbe wa Ma-Quraysh katika sulhu hiyo.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), alimuonea huruma kijana huyo, akamtaka Suhayl amruhusu wamchukue kwa sababu mkataba ulikuwa bado haukutiwa saini wala haukupigwa mhuri, lakini baba yake alikataa na kutishia kuuvunja mkataba na kuanzisha vita ikiwa  watajaribu kumchukua kwa nguvu.

Abu Jandal alikuwa akipiga kelele huku akisema;

"Enyi Waislamu wenzangu! mnaniacha nirudi kwa washirikina hawa na mimi nataka himaya yenu?"

Mtume(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia ;

"Kuwa na subira, na Allaah atakujaalia utoke katika janga hilo".

'Umar bin Al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakuweza kuyastahamilia haya, akamuendea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)na kumuuliza;

"Ewe Mtume wa Allaah, wewe si Mtume wa Haki?"

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)akamjibu;

"Ndiyo, ewe 'Umar".

Akauliza tena;

"Kwa nini basi tunakubali kujidhalilisha?"

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)akamwambia;

"Ewe 'Umar, mimi ni Mtume wa Allaah, siwezi kumuasi, na Yeye ndiye atakayetunusuru".

'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) akauliza;

"Si ulituahidi kuwa tutakwenda Makkah na tutatufu katika nyumba kongwe?"

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)akajibu;

"Nilikwambia kuwa ni mwaka huu ewe 'Umar?"

'Umar akajibu;

"La hukusema hivyo."

Mtume(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)akasema;

"Utakwenda Makkah ewe 'Umar na utatufu penye nyumba."

'Umar pamoja na baadhi ya Maswahaba (Radhiya Allaahu 'anhum) hawakuridhika na baadhi ya masharti yaliyokuwemo ndani ya mkataba ule, wao waliona kuwa Waislamu wamekubali kujidhalilisha kwa kuyakubali masharti yote ya makafiri, na hii ni kwa sababu dhahiri yake mkataba huo si mzuri juu ya Waislamu, lakini kwa anayeona mbali mkataba huo ulikuwa ni ufunguzi mkubwa kwa Waislamu, kama alivyosema Allaah katika Suratul Fat-h aya ya mwanzo;

"Bila shaka tumekwishakupa kushinda kuliko dhahiri"

Allaah katika aya hii anatujulisha kuwa kuukubali mkataba huo ni ushindi mkubwa kwa Waislamu, juu ya kuwa dhahiri yake ni kukubali masharti yote ya makafiri, na hii ni inatokana na sababu zifuatazo;

1)      Kutokana na suluhu hiyo, makafiri walifungika wasiweze kupigana vita dhidi ya Waislamu muda wa miaka Kumi.

2)      Katika muda wote huo Waislmu wakawa na uwezo wa kujishughulisha na kuieneza dini yao miongoni mwa makabila mengine ya Bara Arabu, pamoja na nchi za Shaam.

3)      Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)alituma ujumbe kwa wafalme mbali mbali

4)      Wale waliosilimu wasioruhusiwa kukimbilia Madiynah kwa ndugu zao Waislamu, ni bora kwao kubaki Makkah kwa ajili ya kuwalingania watu katika dini ya Kiislam huko Makkah.

5)  Makafiri watakaorudi Makkah iwapo watatoka katika Uislam, hawataudhuru Uislam.

Sababu hizi na nyinginezo ambazo si wasaa wake huu kuzitaja ni dalili kuwa mkataba huo undani wake ulikuwa na manufaa makubwa kwa Waislamu, juu ya kuwa dhahiri yake ni kusalimu amri na kukubali masharti yote ya Ma-Quraysh.

Na hii ndiyo sababu iliyomfanya 'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) asiridhike nao, wala asisimame hapo. Kwani alimwendea pia Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kumuuliza tena masuali yale yale;

"Ewe Abu Bakr, Muhammad si Mtume wa Haki?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu); "Ndiyo"

'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu); "Tukipambana nao makafiri hawa, si atakayekufa upande wetu ataingia Peponi na wao wanaingia Motoni?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu); "Ndiyo".

'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu); "Kwa nini basi tunakubali kujidhalilisha?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu);

"Ewe 'Umar, yeye ni Mtume wa Allaah na hawezi kumuasi, na Allaah ndiye atakayemnusuru, kamatana naye kwani Wallahi yupo katika Haki".

Majibu yale yale ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)kayapata kwa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu), na Allaah akawateremshia Waislamu utulivu nyoyoni mwao.

Allaah anasema;

"Yeye ndiye aliyeteremsha utulivu katika nyoyo za Waislamu ili waongezeke imani juu ya imani yao".

Suratul Fat-h 4

'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema baadaye;

"Nikatambua kuwa ile ndiyo Haki".

Mwaka wa tisa Hijri ndio mwaka ulioitwa 'Mwaka wa Wajumbe' na hii ni kutokana na wajumbe wa makabila mbali mbali ya kiarabu waliokuja kusilimu mbele ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Share

13-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Vita Vya Badr

 

Imani ya Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu)ilikuwa ikijitokeza na kueneza tumaini baina ya watu kila inapotokea shida au dhiki.

Katika vita vya Badr, jeshi dogo sana la Waislamu liliondoka mjini Madiynah kwa nia ya kuuteka msafara mdogo wa kibiashara ukiongozwa na Abu Sufyan unaotokea Syria na kuelekea Makkah, na Waislamu walitegemea kuwa bila shaka msafara huo utakuwa na watu wachache waliokwishachoka baada ya safari ndefu hiyo.

Allaah akawataka Waislamu wauachilie mbali msafara huo na wende kupambana na jeshi kubwa la Ma-Quraysh lililokwishaondoka Makkah kuelekea Madiynah likiwa limejitayarisha kivita na limejizatiti barabara. Na Allaah aliwaahidi Waislam kuwa watawashinda Ma-Quraysh hao juu ya wingi wao.

Idadi ya Waislam ilikuwa mia tatu na kidogo tu, na hawakuwa na silaha nzito isipokuwa panga zao.

Waislamu wakapiga mahema yao katika bonde la Badr na kumtaka Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asiondoke hemani pake iwe itakavyokuwa.

Jeshi kubwa la makafiri likaanza kuhujumu kwa nguvu, na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akihuzunika kila anapoona Muislam anauliwa, na mambo yalipozidi kuwa magumu hata akawa anasikia sauti za panga na kelele na mayowe zikikaribia, akaamua kutoka nje ya hema huku akinyanyua mikono yake mbinguni na kumuomba Mola wake kwa hamasa akisema;

"Mola wangu ikiwa kundi hili litaangamizwa, hutoabudiwa tena ardhini, Mola wangu nipe ushindi ulioniahidi Mola……"

Aliendelea hivyo mpaka  Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipomwendea na kuiweka sawa nguo ya kujifunikia ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) iliyokuwa ikimwanguka huku akimwambia;

"Ewe Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wa Allaah inatosha kuomba, kwani Mola wako atakupa kile alichokuahidi".

Bila shaka Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anaamini kuwa kila alichoahidiwa na Mola wake atakipata, bali hata kabla ya vita hivyo kuanza, yeye ndiye aliyewaonesha Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) mahali watakapoanguka vigogo vya Ma-Quraysh. Aliwaonyesha mahali gani Abu Jahl atauliwa na kuanguka, na akawaonyesha mwahali gani watauliwa na kuanguka vigogo wengine mbali mbali wa ki-Quraysh, na  yote yalitokea kama alivyosema.

Lakini hisia yake juu ya uzito wa mzigo alioubeba na hofu yake katika pambano hili la mwanzo baina ya Imani na Kufru ndiyo iliyomfanya atoke nje ya hema lake na kunyanyua mikono yake juu akiomba kwa hamasa namna ile.

 

 

Share

14-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Imani ya hali ya juu

 

Imani ya hali ya juu kabisa ya Abu Bakr ilionekana pale alipofariki Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)alipokuwa akiumwa maradhi yake ya mwisho, alimtaka Abu Bakr awe anasalisha watu. Siku moja baada ya kuwasalisha Waislam,  Abu Bakr, aliingia chumbani kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)na baada ya kuzungumza naye muda mrefu akamtaka ruhusa arudi nyumbani kwa ajili ya kukidhi haja zake.

Baada ya kumaliza haja zake na alipokuwa akijitayarisha kurudi msikitini, akasikia sauti za watu wanalizana, akazipokea habari za kufariki kwa Mtume wa Allaah huku anakimbia kuelekea msikitini na huku machozi yakimtoka huku akisema;

"Innaa liLLaahi wa innaa ilayhi raaji'uun".

Ndani ya nyumba ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)watu walikuwa mfano wa waliorukwa na akili.

Hata 'Umar bin Al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhum), mwenye nguvu, shujaa, alisimama mbele ya watu panga mkononi huku akisema:

"Wanafiki wanadai kuwa eti Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekufa, Mtume hajafa, bali amekwenda kwa Mola wake kama alivyokwenda Musa mwana wa Imran na atarudi. Sitaki kumsikia mtu akitamka kuwa Mtume amekufa., nikimsikia mtu anasema hivyo nitamkata kichwa chake kwa upanga wangu huu."

Ikiwa hii ni hali ya 'Umar, ilikuwaje basi hali ya walio chini yake? Waislam hawakutegemea kuwa Mtume wao, kipenzi chao, (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)siku moja atakuja kuwatoka, msituko ulikuwa mkubwa sana.

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliingia moja kwa moja chumbani alipolazwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akamfunua uso wake na kuubusu huku akisema;

"Uso wako unapendeza ukiwa uhai au umekufa. Ama kile kifo alichokuandikia Mola wako kimekwishakufikia".

Akaufunika uso wake na kutoka nje na kumkuta 'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) angali anawasemesha watu. Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamtaka anyamaze lakini 'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakunyamaza, na alipomuona hanyamazi akawaelekea watu na kuwaambia;

"Aliyekuwa akimuabudu Muhammad, basi Muhammad kesha kufa, ama aliyekuwa akimuabudu Allaah, basi Allah yu hai na wala hafi."

Kisha akaisoma kauli ya Allaah isemayo:

"Na hakuwa Muhammad ila ni Mtume tu. Wamepita kabla yake Mitume (wengi kabisa). Akifa au akiuawa ndiyo mtarudi nyuma (kwa Visigino vyenu), muwe makafiri kama zamani? Na atakayerudi nyuma kwa visigino vyake hatamdhuru Allaah chochote. Na Allaah atawalipa wanaomshukuru."

Aali Imran- 144

Alipoisikia tu aya hiyo 'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakuweza kusimama, akakaa kitako mfano wa simba aliyenyeshewa mvua. Siku zilizofuata alisema:

"Ilikuwa kama kwamba ninaisikia aya hiyo kwa mara ya mwanzo, miguu haikuweza kunichukua nikajitupa chini na kukaa".

Bukhari.

Ama Ibn 'Abbaas alisema;

"Wallahi ilikuwa kama hawaijui aya hii, na mara walipomsikia Abu Bakr akiisoma, watu wote waliipokea na kila aliyeisikia alikuwa akiisoma na kuirudiarudia".

Bukhari.

Huu ndio ushujaa wa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu), wakati kama huu, umma wote ulipobabaika na kutetereka, akiwemo 'Umar bin Al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu), Abu Bakr Asw-Swiddiyq alikuwa thabiti mfano wa jabali mbele ya kimbunga kilichouvamia umma siku hiyo, na aya aliyoisoma siku ile ikawa inarudiwarudiwa na kila mtu;

"Aliyekuwa akimuabudu Muhammad, basi Muhammad keshakufa, ama aliyekuwa akimuabudu Allah, basi Allah yu hai na wala hafi."

Neno la Tawhiyd, neno la kuuamsha Umma, 'Ikiwa mnamuabudu Allah basi amkeni na muifanye bendera ya Laa ilaaha Illa Allaah ipepee kila mahali. Aamkeni muyaendeleze mapambano yaliyoanzishwa na Mtume wenu huyu mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)'.

Neno hilo liliwaamsha na kuwatanabahisha Waislamu, wakaanza kutimiza wajibu wao, wakamuosha, wakumshughulikia na kumswalia na kumuaga Mtume wao mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

"Je, kusingekuwepo na Abu Bakr, hali ingekuwaje siku hiyo?"

 

 

Share

15-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Siku ya Saqifa

 

Hii ni siku aliyofariki Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na baadhi ya watu wa Madiynah walijikusanya mahali panapoitwa Saqiyfat Bani Saa'dah karibu na Msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ajili ya kufungamana na Swahaba mmoja katika watu wa Madiynah aitwaye Sa'ad bin 'Ubaadah (Radhiya Allaahu ‘anhu)na kumchagua kuwa ni Khaliyfah wa Waislam.

'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu), alipopata habari hizo alimwendea Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu)na kumhadithia yanayotokea, na wote kwa pamoja wakifuatana na Abu 'Ubaydah 'Aamir bin Al-Jarraah (Radhiya Allaahu ‘anhu)wakaelekea huko.

Abu Bakr wala 'Umar hawakuwa na tamaa ya UKhaliyfah kama tutakavyoona, na hii ni kwa sababu walimsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akimkatalia 'Ammi yake Al-'Abbaas, alipomuomba ampe ugavana wa mkoa mmojawapo, na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia;

"Sisi Wa-Allaahi hatumpi utawala mwenye kuuomba wala mwenye kuung'ang'ania."

Na hii ni kwa sababu utawala, si neema wala raha hata mtu aung'ang'anie na kuutaka. Mwenye kuung'ang'ania utawala ni yule asiyeelewa jukumu lake,  ama sivyo asingeutaka. Na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyajua hayo vizuri .

Wengi walibabaika baada ya kuzipokea habari za kifo cha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na miongoni mwao ni watu wa Madiynah  waliojikusanya mahali hapo panapoitwa Saqiyfat Bani Saa'idah, wakasema kuwa; lazima pafanywe haraka kumchagua kiongozi wa umma kabla hapajatokea machafuko, na wakataka kiongozi huyo atoke katika watu wao (awe mtu wa Madiynah), kwa sababu Madiynah ni mji wao, na kwa sababu ya fadhila zao nyingi katika kuunusuru Uislamu, na kwa ajili hiyo wakaamua kumchagua Swahaba huyo aitwaye Sa'ad bin 'Ubaadah (Radhiya Allaahu ‘anhu).

Mara baada ya kuwasili mahali hapo, 'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu)akataka kuuhutubia mkusanyiko huo, lakini Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu), alimvuta nyuma na kumuomba amwachie yeye akhutubie, akajisogeza  mbele na kusema;

"Enyi watu wa Madiynah, hakika hapana fadhila itakayowezwa kutajwa bila ya kutajwa nyinyi ….", akaendelea kuwapa sifa zao walizostahiki, kisha akasema.

"Lakini Khaliyfah wa Waislamu atoke kwetu sisi watu wa Makkah".

Katika kitabu chake kitukufu, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) daima hutanguliza kuwataja watu wa Makkah 'Al-Muhaajiriyn' kabla ya watu wa Madiynah 'Al-Answaar'.

Allaah Anasema;

"Na wale waliotangulia wakawa wa kwanza katika (Uislamu) Muhajiri na Ansari…".

At Tawba-100

Mmoja katika watu wa Madiynah aitwaye Al-Khabbab bin Mundhir (Radhiya Allaahu ‘anhu)akasema;

"Kwetu atoke Amiri na kwenu Amiri".

Akainuka Swahaba mwengine ambaye pia ni katika watu wa Madiynah aitwaye Bashir bin Mubaarak (Radhiya Allaahu ‘anhu)na kusema;

"Enyi Al-Answaar (Watu wa Madiynah), ingawaje sisi tumeipigania dini hii kwa hali na mali, lakini haijuzu kwetu kujifanya bora kuliko wenzetu, sisi tulifanya hayo kwa ajili ya kutaka radhi za Allaah na kumtii Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatokana na kabila la ki-Quraysh, na watu wake ndio wanaostahiki kutuongoza. Allaah Asinijaalie nikapingana nao. Muogopeni Mola wenu enyi watu wa Madiynah na msiwaendee kinyume Al-Muhaajiriyn (watu wa Makkah)".

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu), akaunyanyua juu  mkono wa 'Umar na wa Abu 'Ubaydah 'Aaamir bin Al-Jarraah (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kusema;

"Huyu 'Umar bin Al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuomba Allaah kutokana naye autukuze Uislamu, na huyu Abu 'Ubaydah ambaye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimsifia kuwa ni 'Mwaminifu wa Ummah huu', mimi nimeridhika (achaguliwe) mmoja kati yao, (awe Khaliyfah)"

'Umar aliuchomoa mkono wake kwa nguvu mfano wa mtu aliyeshika jinga la moto na Abu 'Ubaydah akasema;

"La wa-Allaahi! Nina khiyari nikatwe kichwa changu bila ya kutenda dhambi yoyote, lakini sikubali niwe kiongozi wa watu akiwemo Abu Bakr ndani yao. Ewe Abu Bakr, Mtume wa Allaah alikutanguliza wewe utuswalishe, na katika kila kubwa na dogo aliridhika na wewe, basi kwa nini na sisi tusiridhike na wewe? Utandaze mkono wako tufungamane nawe, ew Abu Bakr".

Akautandaza, na katika riwaya zilizo sahihi, wa mwanzo kufungamana naye alikuwa Bashir bin Mundhir ambaye ni mtu wa Madiynah, kisha 'Umar kisha Abu 'Ubaydah kisha wakamvamia Maswahaba wote mmoja baada ya mmoja wakifungamana naye (Radhiya Allaahu 'anhum).

Siku ya msiba mkubwa kupita yote iliyopata kuwatokea Waislamu ilimalizika kwa amani baada ya kuweza kuiondoa khitilafu iliyozuka baina yao, na baada ya kupata matumaini kwa kumuona Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) ndiye aliyeshika hatamu, kwani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anapokuwa anaumwa au anapopatwa na udhuru wowote, alikuwa daima akimtanguliza Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuswalisha watu, kuongoza misafara ya Hajj na kusimamia mambo mbali mbali.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akiumwa katika maradhi yake ya mwisho, alimchagua Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) awaswalishe watu, na bibi 'Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhaa)alipojaribu kumtaka Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumpa 'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) jukumu hilo badala ya baba yake kwa sababu Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa mwingi wa kulia anaposwalisha, Mtum e(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikasirika akamwambia;

"Mwambie Abu Bakr aswalishe watu!"

Share

16-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Mimi Si Mbora Wenu

Siku ya mwanzo ya utawala wake Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu)alipanda juu ya Mimbari ya Msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwakhutubia Ummah aliopewa jukumu la kuwaongoza. Baada ya kupanda ngazi mbili alishindwa kuzikamilisha ngazi zote tatu alizokuwa akizipanda Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), maana aliona kuwa akizikamilisha ngazi zote atakuwa amejiweka daraja moja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Baada ya kuzipanda ngazi hizo akaanza kuhutubia kwa kusema;

"Enyi watu!

'Mimi nimepewa uongozi juu yenu, lakini si mbora wenu.

Nikihukumu sawa, nisaidieni.

Nikihukumu vibaya nirekebisheni.

Hakika aliye dhaifu miongoni mwenu, kwangu mimi ni mwenye nguvu mpaka nimpatie haki yake, na hakika mwenye nguvu miongoni mwenu, kwangu mimi ni dhaifu mpaka niichukue haki ya watu iliyo kwake.

Nitiini iwapo nitamtii Allaah na Mtume Wake, ama nikiasi (amri ya Allaah) basi msinitii.

Umma unapoiacha Jihaad, hudhalilika.

Inukeni mswali, Allaah Akurehemuni".

Hii ndiyo khutbah ya mwanzo ya Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu); khutbah fupi iliyoweka wazi jinsi gani atakavyohukumu.

Alisema;  

'Mimi nimepewa uongozi juu yenu, lakini si mbora wenu'.

 

Aliyasema haya ili kuujulisha Ummah kuwa yeye si Mfalme juu yao bali ni Kiongozi tu, na hivi ndivyo uhusiano utakavyokuwa baina yake na Ummah wake, Kiongozi, Mwalimu, Jemadari, Khaliyfah wao na Mwenzao.

Kwa njia hii aliwajulisha Ummah wake juu ya Dhamana aliyopewa na juu ya kiongozi mwaminifu, vipi anatakiwa awe.

Pia alitaka kuondoa katika fikra zao kwamba, anayehukumu, yupo juu ya shari'ah, na kwamba anaweza akafanya atakavyo, na kwamba hakosi na wala hakosolewi.

Alitaka kuwajulisha kuwa Uongozi si cheo cha kujivunia bali ni dhamana, na Ukhalifa alopewa ni kazi na si kitu cha kujitakabaria mbele ya watu.

"Lakini si mbora wenu"

Katika kitabu chake kiitwacho 'Khulafaa Rrasuul' Mwandishi maarufu Khalid Muhammad Khaalid (Allaah Amrehemu) alisema;

"Huenda akawa Kweli si mbora wao kwa vile yeye ni mwenye kuhukumu, lakini alikuwa mwenye hekima kupita wao na hii ni kwa sababu yeye ni Asw-Swiddiyq, Aliyesadiki ambaye ndani yake amekusanya Kusadiki, Imani, Uaminifu na Uongofu ulomfanya astahiki kuwa Swahibu yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa pangoni.

Alikuwa mwenye hikima kwa sababu alijua kuwa hatokuwa huru mpaka Ummah wake kwanza uwe huru.

Hatokuwa na nguvu mpaka Ummah wake kwanza upate nguvu.

Hatokuwa na Amani mpaka Ummah wake kwanza  upate amani"

 

Share

17-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Kupambana na waliortadi

Baadhi ya makabila yanayoishi mbali na mji wa Madiynah na ambayo yaliingia karibuni tu katika Uislamu, yalianza kufanya uasi na kurtadi mara baada ya kusikia habari za kifo cha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Walirtadi baada ya kukataa kumpa Khaliyfah mpya wa Waislamu mali ya Zakaah kama walivyokuwa wakimpa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Walisema kuwa Allaah katika aya ya 103 ya Suratu Tawbah anasema;

"Chukua Swadaqah katika mali zao, ziwasafishe na kuwatakasa kwa ajili ya hizo (Zakaah) kuwataja kwa vizuri (mbele yangu) na uwaombee dua. Hakika kuwaombea kwako kutawapa utulivu na Allaah ndiye asikiaye na ajuaye."

Waasi hao wakasema:

"Tulitakiwa tutoe Zakaah na kumpa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) apate kututakasa kwa ajili ya hizo Zakaah na kutuombea dua, lakini sasa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kesha kufa na Abu Bakr hawezi kututakasa na kutuombea dua kama alivyokuwa akifanya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa ajili hiyo hakuna tena haja ya kutoa Zakaah."

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu)akaamua kuingia vitani na waasi hao kutokana na sababu mbili;

1-      Aliona kuwa huko ni Kurtadi, kwa sababu Zakaah ni nguzo ya tatu ya Kiislamu na kukataa kuitoa ni kuikataa nguzo hiyo.

2-     Akaona pia kuwa kuyanyamazia mambo hayo kutasababisha kutokea uasi wa aina nyingine, maana watu watakapoona kuwa pana udhaifu katika uongozi, kila mmoja atataka kuiweka sheria mikononi mwake.

''Umar bin Al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu)yeye aliona kuwa kwa vile watu hao wanaukubali Uislamu, bora wasiwapige vita, lakini Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu)aliyekuwa akijulikana kwa upole hakuikubali rai hiyo na akashikilia kupigana na waasi hao.

'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu)akamwambia; "Vipi unapigana vita na watu wanaoikubali shahada ya "Laa ilaaha illa llah" wakati Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema kuwa; atakayeikubali shahada hiyo itahifadhika mali yake na damu yake?

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu)akajibu;

"Lakini si alisema kuwa ni lazima aipe haki yake (shahada hiyo)? Na Zakaah ni katika haki zake." 'Umar
 

Baadhi ya makabila yanayoishi mbali na mji wa Madiynah na ambayo yaliingia karibuni tu katika Uislamu, yalianza kufanya uasi na kurtadi mara baada ya kusikia habari za kifo cha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Walirtadi baada ya kukataa kumpa Khaliyfah mpya wa Waislamu mali ya Zakaah kama walivyokuwa wakimpa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Walisema kuwa Allaah katika aya ya 103 ya Suratu Tawbah anasema;

"Chukua Swadaqah katika mali zao, ziwasafishe na kuwatakasa kwa ajili ya hizo (Zakaah) kuwataja kwa vizuri (mbele yangu) na uwaombee dua. Hakika kuwaombea kwako kutawapa utulivu na Allaah ndiye asikiaye na ajuaye."

Waasi hao wakasema:

"Tulitakiwa tutoe Zakaah na kumpa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) apate kututakasa kwa ajili ya hizo Zakaah na kutuombea du'aa, lakini sasa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kesha kufa na Abu Bakr hawezi kututakasa na kutuombea du'aa kama alivyokuwa akifanya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa ajili hiyo hakuna tena haja ya kutoa Zakaah."

Sayiduna Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu)akaamua kuingia vitani na waasi hao kutokana na sababu mbili;

1-      Aliona kuwa huko ni Kurtadi, kwa sababu Zakaah ni nguzo ya tatu ya Kiislamu na kukataa kuitoa ni kuikataa nguzo hiyo.

2-     Akaona pia kuwa kuyanyamazia mambo hayo kutasababisha kutokea uasi wa aina nyingine, maana watu watakapoona kuwa pana udhaifu katika uongozi, kila mmoja atataka kuiweka sheria mikononi mwake.

''Umar bin Al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) yeye aliona kuwa kwa vile watu hao wanaukubali Uislamu, bora wasiwapige vita, lakini Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa akijulikana kwa upole hakuikubali rai hiyo na akashikilia kupigana na waasi hao.

'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamwambia; "Vipi unapigana vita na watu wanaoikubali shahada ya "Laa ilaaha illa llah" wakati Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema kuwa; atakayeikubali shahada hiyo itahifadhika mali yake na damu yake?

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akajibu;

"Lakini si alisema kuwa ni lazima aipe haki yake (shahada hiyo)? Na Zakaah ni katika haki zake." 'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisema baadaye kuwaambia watu:

"Kisha Allaah alikifungua kifua changu kuikubali rai ya Abu Bakr".

Alisema baadaye kuwaambia watu:

"Kisha Allaah alikifungua kifua changu kuikubali rai ya Abu Bakr".

 

Share

18-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Jeshi La Usaamah

Wakati haya yakitokea, Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliona ni bora kulianzisha tena jeshi la Usaamah (Radhiya Allaahu ‘anhu), jeshi lililoundwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) mwenyewe chini ya uongozi wa Usaamah bin Zeid (Radhiya Allaahu ‘anhu), na jeshi hilo lilikuwa limekwishapiga kambi nje ya Madiynah likijitayarisha kwenda kupigana na Warumi, lakini kutokana na kushtadi kwa maradhi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) jeshi hilo halikuondoka.

Baada ya kifo cha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) jeshi hilo lilirudi tena Madiynah, na Waislamu wakahitilafiana juu ya kulianzisha tena jeshi hilo.

Baadhi ya Waislamu akiwemo 'Umar bin Al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) waliona kuwa si fikra nzuri kulianzisha tena jeshi hilo hasa wakati huu ambapo mji wa Madiynah umo katika hatari ya kuvamiwa na makundi ya waliortadi.

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema;

"Lianzisheni tena jeshi la Usaamah, kwani Wallahi hata kama mbwa wa mwitu wataninyakua basi nitalianzisha tena kama alivyofanya Mtume wa Allaah(Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)."

Alipoona kuwa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) ameshikilia jambo hilo, 'Umar bin Al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema;

"Kwa vile Usaamah ni kijana mdogo sana, basi angalau ungemweka mtu mzima aliongoze jeshi hilo".

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliruka kutoka pale aliposimama na kuzishika ndevu za 'Umar bin Al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu), akamwambia;

"Ole wako ewe Ibnil Al-Khatwtwaab! Amepewa uongozi na Mtume wa Allaah na wewe unanitaka mimi nimuondoe?"

Ndani ya jeshi hilo walikuwemo masahaba wakubwa kama vile 'Umar, 'Uthmaan na wengine (Radhiya Allaahu ‘anhum), na lilipokuwa likiondoka mjini Madiynah, Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akawa analisindikiza huku akitembea kwa miguu na Usaamah (Radhiya Allaahu ‘anhu) akiwa amepanda farasi.

Usaamah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye umri wake haukuzidi miaka kumi na nane wakati ule akasema;

"Ewe Khaliyfah wa Waislamu, bora wewe panda juu ya mnyama huyu na mimi nitakwenda kwa miguu".

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamjibu;

"Wa-Allaahi utabaki juu ya farasi na mimi nitatembea kwa miguu, kwani nitakuwa nimefanya jambo kubwa sana ikiwa nitaitia miguu yangu vumbi angalau kidogo katika njia ya Allaah?."

Kwa vile Abu Bakr alikuwa akiuhitajia ushauri na msaada wa 'Umar katika uendeshaji wa mambo ya Waislamu, na kwa vile 'Umar alikuwa miongoni mwa wanajeshi chini ya uongozi wa Usaamah, ilimbidi Abu Bakr amuombe Usaamah ili amruhusu 'Umar abaki naye Madiynah. Akamnong'oneza sikioni pake na kumwambia;

"Itakuwa vizuri kama utakubali kuniachia 'Umar, maana namhitajia katika kuendesha mambo ya Ummah".

Usaamah (Radhiya Allaahu ‘anhu) akakubali.

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) angeweza kumuamrisha Usaamah (Radhiya Allaahu ‘anhu) juu ya jambo hilo, lakini hakufanya hivyo kwa sababu Usaamah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa mkuu wa jeshi hilo na mwenye haki ya kutoa ruhusa hiyo, na kama Usaamah angelikataa, basi asingemlazimisha.

Na jambo hili la Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuliunda tena jeshi la Usaamah lilisaidia sana kuyavunja nguvu makundi ya waliortadi na kuingiza uoga nyoyoni mwao, maana waasi hao walipoliona jeshi hilo likitoka nje ya Madiynah kuelekea Sham, walisema:

"Wa-Allaahi ungekuwa mji wa Madiynah uko katika udhaifu na hitilafu kama tunavyosikia, basi wasingeweza kulitoa nje jeshi kubwa kama hili kupambana na Warumi".

Baada ya kuwasindikiza mpaka nje kidogo ya mji wa Madiynah, Abu Bakr akalikhutubia jeshi hilo na kulijulisha juu ya misingi ya jeshi la Kiislamu linavyotakiwa liwe.

Baada ya kumshukuru na kumpwekesha Allaah, akasema:

"Msifanye khiyana wala msishambulie bila taarifa (ghadran), wala msikate kate maiti za adui, wala msiue mtoto wala mzee wala mwanamke, wala msiunguze mtende wala msikate mti unaotoa mazao wala msichinje mbuzi wala n'gome wala ngamia isipokuwa kwa ajili ya kula.

Na mtakutana na watu waliojitenga ndani ya hekalu zao kwa ajili ya ibada, basi waacheni hivyo hivyo walivyo."

Kisha akasema: "Nendeni kwa jina la Allaah."

Haya ndiyo maamrisho ya Kiislamu, na hivi ndivyo alivyofundishwa Abu Bakr na Mwalimu wake Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Na hivi ndivyo majeshi ya Kiislamu yalivyokuwa yakifanya kupitia karne zote.

Na waisome historia ya ufunguzi wa Kiislamu kama watakuta yale waliyofanya wao huko Algeria, Bosnia Kosovo, Afghanistan na hivi sasa Palestina. Waislamu wanachinjwa kama mbuzi na kukatwa katwa maiti zao na wengine wamezikwa wakiwa wazima, na wake zao wameingiliwa kwa nguvu na kuharibiwa, kisha wanajidai kuwa wao ni mabingwa wa kugombania haki za binadamu.

 

Share

19-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Alipotoka Kwenda Sokoni

Siku ya pili baada ya kuwa Khaliyfah wa Waislamu, Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alitoka kuelekea sokoni huku akiwa amebeba rundu la nguo.

'Umar bin Khataab na Abu 'Ubaydah (Radhiya Allaahu ‘anhu) walipomwona katika hali hiyo wakamuuliza;

"Unakwenda wapi ewe Khaliyfah wa Mtume wa Allaah?"

Akawajibu;

"Naelekea sokoni".

'Umar akamuuliza;

"Unakwenda kufanya nini sokoni na umepewa u-Khaliyfah juu ya Waislamu?"

Abu Bakr akajibu;

"Wanangu nitawalisha nini?"

'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) akatoa akasema;

"Itakuwa bora kama tutashauriana na Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) waweze kumjaalia Khaliyfah wa Waislamu malipo maalum ili aweze kujihusisha na matatizo ya Ummah".

Maswahaba wote wakakubali ushauri huo.

 

Share

20-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Hali Chakula Cha Haramu

Alikuwa akihiyari kufunga mawe tumboni pake, yamsaidie asihisi njaa kuliko kuingiza tumboni mwake chakula cha haramu.

Katika Swahihul Bukhaariy imeelezwa kuwa;

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu)alikuwa na mfanyakazi, kijana mdogo, na siku moja kijana huyo alikuja na chakula na kumkaribisha Khalifa wa Waislamu (Radhiya Allaahu ‘anhu)aliyekipokea na kula.

Yule kijana akamuuliza Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu)

'Unajuwa kitu gani ulichokula ewe Khalifa wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akauliza;

'Kitu gani?"

Yule kijana akajibu;

"Hapo zamani, zama za ujahilia (kabla ya kuwa Muislamu), niliwahi kumtabiria mtu, na mimi sijui chochote kuhusu utabiri wakati huo, nilimdanganya tu, na tokea siku ile sijaonana na mtu huyo isipokuwa leo, akanipa zawadi yangu (malipo yangu), na 'zawadi yenyewe ni hicho ulichokula."

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu)akaingiza mkono wake kinywani na kuanza kujitapisha kwa nguvu, na yule kijana akamwambia;

'Allaah Akurehemu! Yote haya (unafanya) kwa sababu ya tonge moja tu?'

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu)a kamwambia;

'Wa-Allaahi kama haiwezekani kukitoa mpaka niitoe roho yangu basi nitafanya hivyo, maana nilimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema; "Sehemu yoyote ya mwili iliyojengeka kwa mali ya haramu basi Motoni ndipo panapostahiki kuingizwa mwili huo, na mimi naogopa isiongezeke sehemu yoyote ya mwili wangu kwa tonge hili".

 

Wakati majeshi ya Waislamu yalipokuwa yakisonga mbele kuyashinda majeshi ya Kirumi na kuteka nchi baada ya nchi, huku mali nyingi za ngawira zikiletwa Madiynah, Abu Bakr hakuyumbishwa wala kubabaishwa na yote hayo, bali aliendelea kuhukumu kwa uadilifu na kuishi maisha yale yale na kuvaa nguo zile zile na kula chakula kile kile alichokuwa akila kabla ya kuwa Khalifa.

Alipofariki dunia Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliwacha vitu vifuatavyo;

Ngamia aliyekuwa akimbebea maji, chombo cha kukamulia maziwa ya mnyama, na jokho alokuwa akilivaa anapopokea wajumbe kutoka nje, na alipoviona vitu hivyo 'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alilia sana kisha akasema:

"Wa-Allaahi umekwisha wapa taabu kubwa watakaokuja kuhukumu baada yako."

Alikuwa akisema;

Siku ile alipobashiriwa Pepo na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), Abu Bakr (RadhiyaAllaahu ‘anhu) alisema;

"Wallahi siamini kuwa nitaepukana na adhabu ya Allaah, hata kama mguu wangu mmoja utakuwa ushaingia Peponi, huenda nikawa nimemkosea huyu au yule, kisha uje kutolewa mguu wangu Peponi na kuingizwa Motoni."

Rabi'ah Al-Aslamiy (Radhiya Allaahu ‘anhu) anasema;

"Siku moja nilikuwa nikijadiliana na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu), akaniambia neno lililonichukiza, kisha akajuta na kuniambia;

'Ewe Rabi'ah nirudishie kama nilivyokwambia, upate kulipa kisasi chako'

'Nikamwambia;

Sitofanya hivyo'

Akenda kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na mimi nikamfuata, hata watu wakashangaa wakasema;

'Vipi huyu mtu, yeye anakukosea kisha anakwenda kukushitaki?"

Nikawambia, 'Huyu ni Abu Bakr …'

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaniuliza;

'Ewe Rabi'a,h kuna nini baina yako na Abu Bakr?'

Nikamwambia;

'Ee Mtume wa Allaah, yeye aliniambia neno lililonichukiza akataka nimrudishie ili nimlipize kisasi, nikakataa'.

Mtume akaniambia;

'Ahsante (umefanya vizuri) ewe Rabi'ah, usimrudishie, lakini sema;

'Mungu akusamehe ewe Abu Bakr'

Nikasema, ' Mungu akusamehe ewe Abu Bakr', Abu Bakr akaondoka huku analia".

Musnad Imam Ahmad

Khaalid Muhammad Khaalid katika kitabu cha 'Khulafaar Rasuul', anasema;

"Neno moja tu ulimi uliteleza akalitamka. Halikuwa neno ovu, kwa sababu Abu Bakr haiwezekani atamke neno ovu, lakini neno hilo lilimchukiza Rabia likamsituwa na kumhuzunisha Abu Bakr aliyeshikilia kuwa lazima alipizwe kisasi.

Na kwa nini asifanye hivyo wakati aliwahi kumuona Mtume wa Allaah akifanya hivyo hivyo siku ile alipokuwa akiwapanga majeshi ya Waislamu katika vita, na kwa bahati mbaya alimpiga mtu mmoja kwa nguvu tumboni  pake, na alipohisi kuwa pigo hilo limemuumiza mtu huyo, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)a lipandisha nguo yake na kulifunua tumbo lake na kumtaka mtu yule amrudishie kama alivyompiga."

 

Share

21-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Mkamuaji Maziwa

Kabla ya kupewa Ukhalifa, Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akipenda kwenda kuwasaidia masikini na wazee na vilema, akiwapikia na kuwaoshea vyombo vyao na hata kuwakamulia maziwa.

Siku moja baada ya kuwa Khaliyfah wa Waislamu, alikwenda kuwatembelea baadhi ya wale masikini aliokuwa akiwatumikia, na mara baada ya kugonga mlango wa mojawapo ya nyumba hizo mtoto mdogo alifungua, na alipoulizwa na mamake ;

'Nani anayegonga mlango mwanangu?'

Mtoto akajibu;

'Mkamuaji maziwa amekuja, mama'

Mama alipomwona Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akastuka na kusema;

'Mwanangu, sema 'Khaliyfah wa Waislamu'.

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema;

'Mwache, kwani ameniita kwa jina ninalolipenda kuliko yote'

Alikuwa akiwapenda masikini na akipenda kuwatumikia, na alikuwa akiwapenda watumwa na aliwakomboa wengi kwa mali yake.

Alimkomboa 'Amir bin Fuhayra, Zubayr, Ummu aAbsi na mwanawe, na wengi katika Maswahaba waliokuwa wakiteswa na makafiri wakati ule, na siku ile alipomkomboa Bilaal bin Rabaah (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliambiwa na kafiri aliyekuwa akimtesa na kumuadhibu;

'Ungeniambia huna isipokuwa vijisenti kidogo tu, basi ningekuuzia'

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamjibu;

'Wa-Allaahi ungelitaka hata riali mia za dhahabu basi ningelikulipa'.

Huyu ndiye Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa mwingi wa huruma, mwingi wa kuona haya, hasa anaposifiwa mbele ya watu, alikuwa akisema;

"Mola wangu nijaalie niwe bora kuliko wanavyonifikiria na unisamehe kwa yale wasiyoyajua juu yangu na usinihisabie kwa wanayoyasema."

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alisema juu yake;

"Mwenye huruma kupita wote katika umma wangu Abu Bakr"

Imaam Ahmad na Ibni Habaan.

 

Share

22-Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu): Kufariki Kwake

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa Khalifya hwa mwanzo wa Waislamu na alikuwa amiri wa mwanzo aliyetumwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu kuongoza msafara wa Hajj katika mwaka wa tisa wa Hijri, na alikuwa wa mwanzo kuikusanya Qur-aan na kuiandika katika kitabu kimoja baada ya hapo mwanzo kuwa iliandikwa ndani ya majani, mifupa, vigogo vya miti nk..

Alikuwa akiruhusiwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) yeye na 'Umar bin Al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) kutoa fatwa hata wakati wa uhai wake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

Alifariki dunia siku ya Jumatatu mwezi 13 Jumaadal-Aakhir mwaka wa 13 wa Hijri mwafaka na mwezi wa Agusti mwaka wa 634 akiwa na umri wa miaka 63, na baba yake alifariki baada yake kwa kiasi cha miezi sita.

 

Share