Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti

 

Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti

 

 

Mwandishi: Mahmuwd Bin Al-Jamiyl

 

Mfasiri: Abuu Sumayyah

 

Imepitiwa Na: Abu 'Abdillaah

 

 

 

بسم الله الرحمن الرحيم

 
 
 
UTANGULIZI:
 
 
Shukrani ni za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), swala na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) Aali zake, sahaba zake na wote wenye kufuata uongofu na njia yake.
 
Risala hii fupi yenye kubainisha mambo yanayomfaa maiti katika kaburi lake na akhera yake kwa idhini ya Mola wake. Risala hii inakusanya mambo yote yenye kufanywa na watu wanaomhusu maiti na kwa wenye kumtakia kheri maiti wao katika walio hai. Hali kadhalika inakusanya baadhi ya yanayotakiwa kufanywa na mtu aliye hai kwa ajili ya nafsi yake ili imnufaishe yeye kwa Allaah baada ya kifo chake.
 
Katika risala hii nimetanabahisha baadhi ya matendo na amali ambazo hazimfai maiti bali si hivyo tu huenda amali hizo zikamdhuru ikiwa amefanya kabla ya kifo chake au kutoka kwa jamaa zake anapokuwa katika sakarati mauti na baada ya kifo chake.
 
Baada ya hayo sala na salamu kwa Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) aali zake, sahaba zake na Alhamdulillah Rabil 'Aalamiyn.
 
 

 

Share

01-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Anapougua Maradhi anayohofiwa kufa nayo

Anapougua Maradhi anayohofiwa kufa nayo
 
Mja anapougua na maumivu ya ugonjwa huo yakazidi ni ishara na onyo anayotoa Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa waja wake akiwakumbusha na kifo, ni ishara vile vile akiwaonyesha waja wake kuwa Yeye yu karibu mno nao na hayuko mbali kabisa, hivyo basi na waja hao kwa ishara hizi na watende matendo ambayo yatawakurubisha kwa Mola wao na yatakayowafaa baada ya kifo chao.
 
Katika jumla ya mambo ambayo yanampasa mgonjwa kufanya pindi maradhi yake yanaposhtadi na kukurubia kifo chake ni haya yafuatayo:
Share

02-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kuridhika na kuwa na subira kwa Qadar ya Allah (Subhaanahu wa Ta'ala)

Kuridhika na kuwa na subira kwa Qadar ya Allah (Subhaanahu wa Ta'ala)
 
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, ‘ Ajabu kwa mambo ya muumini, kila kitu kwake ni la kheri, na hiyo ni kwa muumini peke yake tu, yakimfika yenye kufurahisha hushukuru na hiyo huwa ni kheri kwake, na yakimsibu madhara husubiri na hivyo kuwa ni kheri kwake’ (Muslim)
 
Waliokuwa pambizoni mwake ni juu yao kumkumbusha hilo mara kwa mara na wamhimize nalo bali waoneshe mfano kwake katika kusubiri na kuridhisha.
Share

03-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kumdhania mema Allah (Subhaanahu wa Ta'ala)

 
Kumdhania mema Allah (Subhaanahu wa Ta'ala)
 
Ni juu ya mja Muumini kumdhania mema Mola wake Mtukufu haswa zaidi ikiwa anakaribia kukutana nae Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “ Amesema Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) mimi ni mwenye dhana njema kwa mja wangu” (Bukhari na Muslim)
Vile vile katika hadithi nyingine Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “Asife mmoja wenu ila awe ni mwenye dhana njema kwa Mola wake” (Muslim)
 
Katika jumla ya kumdhania vizuri Mola wako ni kuhisi ukarimu wake na fadhila zake, asimuhisi Mola wake kuwa ni dhalimu, bali amuhisi kuwa Mwenyezi Mungu anamtakia kheri katika maradhi yake hayo.
 
Mgonjwa katika hali yake ya maradhi azidishe khofu kwa Mola wake kwa madhambi aliyokuwa nayo na atarajie hali kadhalika rehema ya Mola wake Mtukufu. Khofu, matumaini na matarajio katika moyo wake ya kusamehewa madhambi pamoja na ulimi wake kuuharakisha kwa istighfaar na toba na dua kwa ajili yake ni sababu kubwa kabisa kuifanya dhana yake kwa Mola wake kuwa nzuri hivyo basi na Mola wake hawezi kuangusha dhana yake hiyo na matarajio yake kwake hivyo basi matokeo yake ni kuwa Mwenyezi Mungu nae atampa amani kwa anachokihofia.

Share

04-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Asitamani Mauti

 
Asitamani Mauti
 
Kadiri mgonjwa atakavyohisi uchungu katika maradhi yake haimpasi yeye au hata jamaa zake kutamani yamfike mauti.
 
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, ‘Asitamani mmoja wenu mauti kwa dhara au ugonjwa uliomsibu, ikiwa hapana budi kufanya hivyo basi na aombe dua hii, ‘Ee, Mola wangu nihuishe maadamu maisha yangu yatakuwa na kheri nami, na nifishe ikiwa kufa kwangu itakuwa ni kheri kwangu (kuliko kuishi kwangu)” (Bukhari na Muslim)
 
Ikiwa mja ni mwema basi ziada ya umri wake itakuwa ni kuongeza wema wake juu ya wema aliokuwa nao, na ikiwa ni mja muovu basi yale maumivu ayapatayo katika ugonjwa wake humuondolea madhambi yake na hiyo vile vile ni fursa yake ya kutubia na kurejea katika Istighfar kwa yale aliyepetuka mipaka katika haki ya Allah (Subhaanahu wa Ta'ala).
 
Amesema tena Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) “ Mbora katika watu ni yule mwenye umri mrefu na matendo yake yakawa mazuri” (Tirmidhi na Ahmad)
Share

05-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kutekeleza haki za watu

 
Kutekeleza haki za watu:
 
Hapana shaka kuwa katika mambo ambayo yatamfaa mja baada ya kifo chake ni kuhakikisha kuwa katika mwisho wa uhai wake amesharejesha haki za watu, na aombe kwa wale ambao wana haki zao kwake wachukue haki zao hizo, au aliovunja heshima/ hadhi warejeshe heshima hizo kabla hajafariki au mfano wa mambo kama hayo au vinginevyo apate msamaha kutoka kwa watu hao.
 
Akishindwa kufanya hivyo kwa sababu nyingi mfano kwa udhaifu aliokuwa nao, au kwa maradhi yake au vile vile kutokuwepo wenye haki hizo, au kutokuwepo kwa haki hizo kwake yeye, ikiwa hali ndivyo hivyo ilivyo basi wakiwepo jamaa zake wenye kutaka kumnufaisha basi na watoe haki hizo na kuwapa wenyewe kabla ya kifo chake na ikishindikana lifanyike baada ya kifo chake.
 
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “Mwenye haki ya nduguye kwake kamvunjia heshima na hadhi yake au ana deni la mtu basi na arejeshe haki hizo kabla ya kufika siku ambayo haitakubaliwa dinari au dirhamu yake, akiwa ana amali njema alizofanya basi zitachukuliwa amali hizo na kupewa huyo sahibu yake, ikiwa hana amali njema alizofanya basi atapewa maovu ya sahibu yake.”
Share

06-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Nia na usia wa kurejesha haki

 
 
Nia na usia wa kurejesha haki:
 
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “ Sio haki kwa Muislamu ambae zitampita siku mbili na ana kitu anataka kuusia ila usia ule utakuwa umeandikwa kichwani mwake.” Baada ya kusikia hadithi hii Umar bin Khatab akasema, ‘ Haikunipitia mimi hata siku moja baada ya kusikia hadithi hii ila nilikuwa tayari nimeshatayarisha usia wangu.’ (Bukhari na Muslim)
 
Ikiwa mja ni mdaiwa na hana mali ya kulipa deni hilo ni juu yake aweke nia ya kulipa deni hilo na akokoteze kwa kumuomba Mwenyezi Mungu amsaidie alilipe deni hilo na aandike usia kwa jamaa zake kumlipia deni hili.
Share

07-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kinachotakiwa kiwepo katika usia:

 
Kinachotakiwa kiwepo katika usia:
 
Katika masiku haya ambayo sheria imekuwa inavunjwa na haifuatwi hali kadhalika ujahili kuenea kila upande na elimu ya dini kuwa ni chache yampasa Muislamu ausie katika yale mambo ambayo yatamkosha yeye kwanza na kufuatwa isivyo, hili litamuokoa na wengine kumfuata katika makosa haswa katika mambo yanayohusu mauti, swala ya jeneza na mambo yenye kuhusiana nayo, hivyo anatakiwa ausie kufuatwa kwa sunna na kuacha bid’a, maasi na chochote kilichozushwa katika dini katika mambo hayo; kama vile kuomboleza kwa sauti na makelele, kujipiga, na kuomba maombi ya kijahili. Ni juu ya mwenye kuusia ausie kukataza mambo haya na ajiepushe nayo na awahadharishe jamaa zake na ubaya na uovu wake.
 
Wakati fulani Abu Musa aliugua na kuhisi maumivu makubwa, kwa maumivu hayo akazimia ilhali kichwa chake kipo chini ya uangalizi wa mwanamke mmoja katika jamaa zake, mwanamke yule baada ya kuona hali ya Abu Musa akapiga kelele kwa nguvu lakini Abu Musa hakuweza kusema kitu kwa hali aliyokuwa nayo, baada ya kuzindukana akasema, ‘Mimi najikosha kwa yale aliyojikosha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) kwani Mtume alijikosha na haya yafuatayo (hakuyataka kabisa yatokee): As-Swaliqah; yaani mtu mwenye kunyanyua sauti yake kwa juu wakati wa msiba, na Al-Haaliqah; mwenye kunyoa nywele zake wakati wa msiba na Ash-Shhaqah; anayerarua na kuchana nguo zake wakati wa kuomboleza.” (Bukhari na Muslim)
 
Ni juu ya wasia unaotolewa kuhusu mali na vitu uzingatie kwanza kulipa madeni au amuusie katika wale ambao hawarithi theluthi katika mali yake kwa sharti kuwa isipatikane madhara katika kuusia huko.
Share

08-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Wasia kwa wasiorithi katika ndugu na jamaa wa karibu

 
Wasia kwa wasiorithi katika ndugu na jamaa wa karibu:
 
 
Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala) amesema, “Mnalazimishwa mmoja wenu anapofikwa na mauti, kama akiacha mali kufanya wasia kwa wazazi (wake) na jamaa (zake) kwa namna nzuri inayokubaliwa na Sheria. Ni wajibu haya kwa wamchao Mungu.” (2:180)
 
Katika aya hii ni wajibu kuusia kwa kiasi cha mali kwa jamaa wa karibu ikiwa mtu huyo ni mwenye wasaa na uwezo wa hilo.
 
Share

09-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Hakuna kuusiwa mali mwenye kurithi

 
 
Hakuna kuusiwa mali mwenye kurithi:
 
 
Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala) ameshatoa haki kwa kila mwenye kurithi nasibu yake, kama vile tunavyojifunza hayo katika surat Nisaa na sura nyinginezo. Haifai kuzidisha au kupunguza kile alichoweka Mwenyezi Mungu katika sheria yake tukufu, hivyo basi mwenye kutaka atoe usia basi na atoe kwa wale ambao hawarithi kisheria.
 
 Imethibiti kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “ Mwenyezi Mungu amempa kila mwenye haki haki yake anayostahiki hivyo hausiwi (mali) mwenye kurithi.” (Abu Daud)
 
Share

10-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Usia kwa theluthi ya mali au chini ya hapo

 
Usia kwa theluthi ya mali au chini ya hapo:
 
 
Inajuzu kuusia mali theluthi moja tu, haifai kuzidisha zaidi ya hapo, ni vizuri zaidi ikawa ni chini ya theluthi.
 
Sa’ad bin Waqas (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema, ‘Nilikuwa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) katika hijja ya kuaga (Hijjatul wadaa) nikaugua maradhi ambayo yalinikurubisha na mauti, Mtume akaja kunitembelea, nikamwambia, ‘Ee, Mtume mimi nina mali nyingi na sina mrithi zaidi ya binti yangu mmoja, je, niusie kwa theluthi mali yangu? Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akasema, “Hapana” nikasema, ‘kwa sehemu ya mali’? Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akasema, “Hapana” nikasema, “ Theluthi ya mali yangu?” Mtume akasema, “theluthi, theluthi ni nyingi, ee, Sa’ad kuwaacha warithi wako mali nyingi, matajiri ni bora kwako kuliko kuwaacha kama mzigo wakiomba omba watu.” Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akaendelea kusema, “Ee, Sa’ad hutotoa utakachokitoa kwa kutamani ujira wa Mwenyezi Mungu ila Mwenyezi Mungu atakulipa kwa hilo, kiasi hata tonge unalompa mkeo.” (Bukhari na Muslim)
 
Share

11-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kuacha kufanya maovu (madhara) katika kuusia

 
Kuacha kufanya maovu (madhara) katika kuusia:
 
 
 Katika mambo ambayo hayatakiwi kufanyika wakati unapousia ni kuwausia baadhi ya warithi kwa yasiyokuwa haki zao. Au kutoa usia kuwa mmoja katika warithi wake asirithi nayo ni haramu na kinyume na hukumu na sheria ya Allah (Subhaanahu wa Ta'ala).
 
Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) amesema, “…Baada ya kutoa vilivyousiwa au kulipa deni, pasipo kuleta dhara…” (4:12)
 
Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) kuwa amesema, “Hakuna dhara au kudhuriana, atakayefanya madhara basi Mwenyezi Mungu atamdhuru, na atakayefanya ugumu basi Mwenyezi Mungu atamfanyia ugumu.”
Share

12-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kutokutekeleza Usia wenye madhara

Kutokutekeleza Usia wenye madhara:
 
 
Mja atakapousia usia ambao ndani yake mna madhara kwa mfano; kuwazuilia watu wake haki na kuwapa wasiostahiki haki hiyo, au kuusia katika vitu ambavyo ni bid’a na kinyume na sheria wakati wa kupeleka jeneza na kuswalia, hali kadhalika wakati wa kuzika kwa mfano kuusia watu waomboleze kwa makelele na mfano wa hayo, basi ni juu ya kila aliyehudhuria katika usia huo amtanabahishe kwa hilo ili aweze kutubia na kulibadilisha atakapokufa kabla ya hilo kufanyika basi jamaa zake warejeshe haki hizo kwa wanaohusika na kutokutekelezwa kwa usia huu wenye dhulma na uovu ndani yake. Haki za Allah ni kubwa zaidi kuliko haki ya maiti wao juu yao, hakuna utiifu wa kumtii mja katika kumuasi Allah (Subhaanahu wa Ta'ala).
 
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “ Atakayezua jambo katika dini yetu hii ambalo halipo basi atarejeshwa nalo.” (Bukhari na Muslim)
 
Umran bin Hiswin (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema, ‘Mtu mmoja aliwaacha huru watumwa sita alipokuwa anataka kufa, wakaja warithi wake katika mabedui wakaenda kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) na kumueleza jambo hilo, Mtume akawauliza “Kafanya hivyo!” akaendelea kusema, “lau tungelijua hilo tusingemswalia” akasema Umar, ‘Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akawafanyia kura baina yao kisha akawaacha huru wawili na wanne akawarejesha kwa watu wao.” (Ahmad na Muslim)  
 
Share

13-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Baadhi ya matendo yenye kumfaa maiti

 
Baadhi ya matendo yenye kumfaa maiti:
 
 
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “Anapokufa mwana adamu amali zake zote zinakatika isipokuwa mambo matatu: sadaka yenye kuendelea, elimu yenye kunufaisha na mtoto mwema ambae atamuombea mzazi wake (baada ya kifo chake).” (Muslim)
 
Vile vile katika hadithi nyingine amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam), “Hakika katika amali njema ambazo zitamfuatia muumini (baada ya kifo chake) ni mambo haya yafuatayo: elimu aliyoifundisha na akaieneza, mtoto mwema aliyemuacha au msahafu aliouacha kama mirathi au msikiti alioujenga au nyumba ya kupumzikia (wanakaa) walioharibikiwa safari, mto aliotengeneza njia yake au sadaka aliyoitoa kutoka katika mali yake alipokuwa na afya yake njema na pindi alipokuwa hai na baada ya mauti yake.” (Ameifanyia tahsiin Albani)
 
 
Hii ni mifano mizuri kabisa ya wema na sadaka yenye kuendelea. Mifano hii ina manufaa mengi katika maisha ya muumini na baada ya kifo chake.
 
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “ Ni nani miongoni mwenu aliyepambazukiwa akiwa amefunga? Abubakar akajibu, ‘Mimi’ Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akauliza tena, “Ni nani miongoni mwenu aliyeshuhudia Jeneza?” Abubakar akajibu, ‘Mimi’. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akauliza tena, “Ni nani miongoni mwenu aliyelisha masikini?” Abubakar akajibu, ‘Mimi’ baada ya hapo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akasema, “Hazikusanyiki amali njema hizi kwa mtu siku moja ila mtu huyo ataingia peponi.” (Muslim)
 
Hali kadhalika amesema tena Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam), “Atakayeshuhudia jeneza kisha akaliswalia basi atapata Qiirati moja, na mwingine akalishuhudia hadi akazikwa atapata Qiirati mbili.” Pakaulizwa na hizo Qiirati mbili ni nini? Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akajibu, “ni mfano wa milima miwili mikubwa” (Bukhari na Muslim)
 
Katika riwaya nyingine “ kila Qiirati moja ni sawa na mlima Uhud”  
 
 Milango ya kheri ni mingi sana mfano ya milango hiyo ni katika swala, kutoa sadaka, kufanya dhikri tofauti, kuhiji kwa mwenye uwezo, kwenda kufanya Umra (ziara au hija ndogo), kuwafanyia wema wazazi wako wawili, kuunga udugu (kuwatembelea ndugu na kuishi nao vizuri), kupigana jihadi, kujifunza na kufundisha na kadhalika katika kheri kuna milango zaidi ya hii na Mwenyezi Mungu ameahidi watu kulipwa mema.
 
Share

14-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kauli ya Mwisho ya Mtu kuwa ni Laa ilaha illa llahi

 
Kauli ya Mwisho ya Mtu kuwa ni Laa ilaha illa llahi :
 
 
Mja atakapohisi sakaraatul maut na kukaribia mwisho wake katika maisha haya ya dunia basi na ahudhurishe katika moyo wake hisia hizo na aelekee kwa Mola wake akiwa na mapenzi na khofu kwake na akithirishe kauli ya ‘Laa ilaha illa llah’ ili ahitimishe itikadi yake kwa kauli hiyo ya Tawhid.
 
Watu wote watakaokuwa karibu yake katika hali hiyo ya sakaraatul maut wamkumbushe hilo na wamwambie aliseme kwa upole ili Mwenyezi Mungu amuwafikishe kulitamka.
 
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “Walakinieni watu wenu wanaokaribia kufa Laa ilaha illa llah   (Muslim)
 
Katika riwaya nyingine ya Ibn Hibaan amesema,“ Atakaye tamka maneno yake ya mwisho Laa ilaha illa llah ataingia peponi siku moja katika dahr hata likimpata litakalompata.”
 
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema katika hadithi nyingine kuwa, “Atakayekufa na hali amekufa akifahamu kuwa hakuna Mola Apasae kuabudiwa kwa haki ila Allah basi mtu huyo ataingia peponi.” (Muslim)
 
Hali kadhalika katika hadithi yake nyingine amesema kuwa, “Atakayekufa na hakumshirikisha Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) na kitu chochote ataingia peponi.” (Muslim)
 
Katika Musnad ya Imam Ahmad imepokewa kuwa, “Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) alimtembelea mgonjwa katika Ansaar akasema kumwambia yule mgonjwa, “Ee, mjomba sema, ‘Laa ilaha illa llah’ akasema (mpokeaji kuwa mtu huyu alikuwa ni mjomba au ami), “ni mjomba au baba mdogo” akasema, ‘bali ni mjomba’ akasema, “nikakhiyarishwa niseme, “Laa ilaha illa llah” Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akasema, “Naam.”
 
 
Katika hadithi nyingine sahihi iliyokuwa ni mashuhuri zaidi imepokewa kuwa, “Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) alimwambia Ami yake Abi Talib alipokuwa katika sakaratul maut, “Ewe ami yangu sema, Laa ilaha illa llah, neno litakalo kufanya upate shufaa ya Allah (Subhaanahu wa Ta'ala).”
Share

15-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kumuombea kheri Mwenye kufa

 
Kumuombea kheri Mwenye kufa:
 
 
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “Mtakapokuwa mnamuombea anayekaribia kufa au aliye shakuwa maiti muombeeni kheri kwani Malaika huitikia Amin kwa yale mnayoyaomba.” (Muslim)
Share

16-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kumfunga macho na kumuombea atakapokufa

 
Kumfunga macho na kumuombea atakapokufa:
 
 
Imam Muslim amepokea, ‘Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) aliingia kwa Abu Salama macho yake yakiwa yamekodoka, akamfunga kisha akasema, “Hakika roho inapochukuliwa hufuatiwa na macho” akasikia kelele kutoka kwa watu wa Abu Salama, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akasema kuwaambia, “Msijiombee ila muombe dua njema, hakika malaika huitikia Amin kwa yale mnayoyaomba.” Kisha akasema tena, “Ee, Mwenyezi Mungu msamehe Abu Salama na nyanyua hadhi yake pamoja na waongofu, na uwaache baada yake pamoja na waliotangulia, utusamehe sisi na yeye Ee, Mola wa ulimwengu, lipanue kaburi lake na uliwekee nuru.”
Share

17-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Je, Surat Yaasin husomwa kwa maiti?

 
Je, Surat Yaasin husomwa kwa maiti?
 
 
Imezoeleka kwa watu wengi hupenda kusoma surat Yasin kwa mtu anayekufa na baada ya kufa kwake na katika kaburi lake vile vile. Hakika jambo hili ni jambo lisilofaa na katika maeneo haya, hakuna fadhila zozote anazopata kwa kusomwa kwa surat Yasin. Hakika kusomwa kwake katika sehemu hizi ni Bid’a haimfai maiti kitu.
Share

18-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kulipa Deni kwa mali ya Maiti

 
Kulipa Deni kwa mali ya Maiti:
 
 
Ni juu ya jamaa za maiti kumlipia maiti madeni anayodaiwa katika mali ya maiti, kama atakuwa ameacha mali hata ikibidi kutolewa mali yote isibakie kitu baada ya kutolewa madeni.
 
Kutoka kwa Sa’ad bin Al-Atwal (Radhiya Allaahu 'anhu) alisema kuwa nduguye alifariki akaacha dirham mia tatu, hali kadhalika alikuwa ameacha watoto. Sa’ad akasema, ‘ Nilitaka mali ile iwafae wale watoto wake yule aliyefariki, Sa’ad akasema, ‘Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akaniambia, “hakika ya nduguyo ni mfungwa wa deni analodaiwa, mlipie deni hilo.” Nikajibu, ‘Ee, Mtume wa Allah, nimeshamlipia deni lake ila ilbaki Dinari mbili ambazo nimempa mkewe na hana bayina kwake, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akasema, “mpe hakika yeye ni mwenye haki nazo.” (Ibn Majah, Ahmad na wengineo)
Share

19-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kujitolea kwa kumlipia madeni Maiti

 
Kujitolea kwa kumlipia madeni Maiti:
 
 
Pindi atakapokufa maiti na ameacha madeni anayodaiwa na hakuacha mali ya kutosha kulipa madeni yale inapendeza watu wajitolee kumlipia madeni yale anayodaiwa.
 
Kutoka kwa Salama bin Al-akwaa (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema, ‘tulikuwa tumekaa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) zama ilipokuja jeneza na kutakiwa kuswalia, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akauliza je, ana madeni? Wakajibu, ‘Hana’. Mtume akauliza tena je, ameacha chochote? Wakajibu, ‘Hapana’. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akamswalia. Kisha likaja Jeneza lingine wakasema Ee, Mtume Tuswalie maiti huyu, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akauliza, “Je, amewacha madeni?” wakajibu, ‘Ndiyo’ akauliza tena, “Je, amewacha chochote? Wakajibu, ‘Ndio ameacha Dinari tatu.’ Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akamswalia.
Kisha likaja jeneza la tatu, watu wakamuomba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) aswalie, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akauliza, ‘Je, amewacha kitu.’ Wale watu wakajibu, ‘hakuacha chochote.’ Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akawauliza tena, “Je, amewacha madeni?” wakamjibu, ‘Ndio, anadaiwa Dinari tatu.’ Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akawaambia, “Mswalieni Sahibu yenu.” Abu Qatada akasema, “Ee Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) mswalie nami nitamlipia hilo deni lake hilo.” (Bukhari)
 
 
 Katika mapokezi mengine imepokewa kuwa Mtume hakumswalia hadi Abu Qatada alipomlipia lile deni alilokuwa anadaiwa yule maiti.
 
Hadithi hizi na mfano wake zina tupa dalili za wazi kuwa deni lisipolipwa linamzuilia maiti kheri nyingi sana na si hivyo tu, hali kadhalika inamzuilia na kuingia peponi, kama tunavyojifunza katika hadithi sahihi kuwa mtu mmoja alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam), ‘Je, nikiuliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu (jihadi ya vita) nikapambana na nikawa sijarudi nyuma Je, nitaingia peponi? Akawa anauliza hivyo mara tatu na Mtume humjibu, “Ndiyo” alipoondoka Mtume akamuita kisha akamwambia, “ila ukiwa una madeni, kwani Jibril ameniambia hivyo sasa hivi.”
 
Share

20-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Walii kumlipia deni maiti

Walii kumlipia deni maiti:
 
 
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) alipokuwa analetewa mtu aliyekufa mwenye madeni huuliza, “Je, ameacha wa kumlipia deni lake?” akiambiwa kuwa ameacha wa kumlipia humswalia lakini kama hajaacha huwaambia sahaba zake, “Mswalieni sahibu yenu.” Mwenyezi Mungu alipomfungulia yeye na Waislamu nchi nyingi zikawa katika himaya ya Uislamu akawa anasema, “Mimi ni wa mwanzo kuliko waumini wengine katika jambo hilo, hivyo atakayekufa na akaacha deni basi ni juu yangu mimi kulilipa deni hilo, na atakayeacha mali basi mali hiyo ni ya warithi wake.” (Bukhari na Muslim) 
Share

21-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kuacha kuomboleza kwa sauti ni rehema kwa maiti

 
Kuacha kuomboleza kwa sauti ni rehema kwa maiti:
 
Tunasoma katika sahihi mbili kuwa, ‘Umar bin Al-Khattab (Radhiya Allaahu 'anhu) alipochomwa kisu, Hafswa, mwanae wa kike akaanza kuomboleza kwa nguvu. Umar akamwambia Hafswa, ‘Ewe Hafswa je hukumsikia Mtume akisema, ‘Mwenye kuliliwa na watu huadhibiwa.’ Na Suhaib akaliliwa vile vile na waliokuwa wanaomboleza namna hiyo wakawa wanalia kwa kusema, ‘Ewe ndugu yangu aa aaah, ewe jamaa yangu aaa aaah, Umar akasema, “Ewe, Suhaib, Je, hujui kuwa mwenye kuliliwa huadhibiwa.’
Katika sahihi mbili, ‘Kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “Hakika maiti huadhibiwa kwa kilio cha jamaa zake.”
Katika Riwaya ya Muslim, “Maiti huadhibiwa kaburini kwa kuliliwa na ndugu zake.”
Abdullah bin Rawaha (Radhiya Allaahu 'anhu) alizimia, Amrah dada yake Abdullah akaanza kulia kwa kusema, ‘Wajabalaah, na kadha wa kadha, alipozindukana Abdullah bin Rawaha akasema, ‘ulichokifanya na ulichokisema nimeambiwa, Je, wewe ndivyo ulivyo? Alipofariki Abdullah dada yake hakumlilia tena.’ (Bukhari)
Share

22-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kilio chenye kukubaliwa kisheria

Kilio chenye kukubaliwa kisheria:
 
Hapana shaka kuwa msiba unapomfika mtu wa kufiliwa kwa mpenzi wake, jamaa zake na ndugu wa karibu unakuwa ni mkubwa kwa mtu na unaweza kumchanganya mtu na hilo ni jambo la kawaida, dini yetu tukufu haiendi kinyume na hisia za kimaumbile za mwanadamu lakini pamoja na hivyo huzielekeza hisia hizo katika sehemu itakiwayo bila ya kumchukiza na kumkasirisha Allah (Subhaanahu wa Ta'ala).
Katika sahihi mbili tunasoma kadhalika, ‘Kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) alipofiwa na mwanawe Ibrahim alilengwa na machozi kisha akasema, “Hakika jicho hutoa machozi, na moyo unahuzunika, hatusemi ila kile chenye kumridhisha Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) na hakika kuachana nawe Ibrahim tunahuzunika.”
 
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) alijiwa na baadhi ya wajukuu zake akiwa katika hali ya kifo, akalia akaulizwa, ‘Ni nini Ee Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam)? mtume akajibu, “hii ni huruma na Mwenyezi Mungu huwahurumia waja wake wenye kuwahurumia wenzao.” (Bukhari na Muslim)
Ama hadithi nyingine katika hadithi kama hizi, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) alisema, “ Si katika sisi anayechana nguo, kujipiga mashavu na akapiga kelele za Jaahiliya.” (Bukhari na Muslim) Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) ametuelezea kuwa mambo haya ni katika mambo ya wakati wa ushenzi (Jaahiliya) na ni mambo ya kikafiri.
 
Share

23-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kutangaza kifo kwa ajili ya maslaha

 

Kutangaza kifo kwa ajili ya maslaha:

 

 

Hakika kutangaza kifo cha Muislamu ni jambo lisilohimizwa kisheria, kutangazwa kifo cha Muislamu ni kwa haja kwa wale watakaomuosha, watakaomkafini, watakaomswalia na watakaomzika. Njia zinazoruhusiwa kisheria zitatumika kwa haja bila ya kuwepo kwa Taklifu yoyote kwa mfano: watu kujulishana huo msiba, au kwa njia ya simu kama ilivyo siku hizi, vile vile inajuzu kutumia vipaza sauti (microphone) kwa haja inayolazimu kama kutumika vijijini bila ya kuzidisha zaidi ya kutaja kifo chake na wakati wa kuswaliwa na mfano wa hayo.

Katika siku ambayo Mtume aliomboleza kifo cha Najashi siku aliyokufa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) alikwenda katika mswala, akawapanga safu kisha akafanya takbir mara nne (Bukhari na Muslim)

Hali kadhalika alipoomboleza viongozi wa vita vya Mu’ta, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) alisema, “Zaid alichukua bendera kisha akauawa baada ya hapo akachukuwa Jaafar nae akauawa kisha akachukuwa Abdullah bin Rawaaha naye akauawa…” (Bukhari)

Share

24-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kutangazwa kifo kwa lengo la kumuombea

Kutangazwa kifo kwa lengo la kumuombea:
 
Inajuzu kutangazwa kwa kifo cha Muislamu kwa lengo la kumuombea dua kutoka kwa wanawe, nduguze, jamaa na jirani zake. Katika Musnad ya Imam Ahmad kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) alisema, “Je, nikujulisheni kuhusu jeshi lenu lenye kupambana? Lilikwenda likakutana na adui, Zaid akafa shahidi, wakamuombea kwa Mwenyezi Mungu na watu wakamuombea, kisha bendera ikashikwa na Jaafar bin Abi Talib nae akapigana na watu kwa ushujaa mkubwa akafa shahidi, nashuhudiwa shahada yake hiyo, wakamuombea, kisha bendera ikashikwa na Abdullah bin Rawaaha akapigana kwa ushujaa nae akafa shahidi, watu wakamuombea…”
Katika sahihi mbili: kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) alipoomboleza kifo cha Najashi alisema, “Muombeeni msamaha ndugu yenu kwa Mola wenu.”
Share

25-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Maombolezo yaliyoharimishwa

 

Maombolezo yaliyoharimishwa:

 

Huku ni kuomboleza kijaahiliya, kama vile kutaja amali za aliyefariki kama kutaja mazuri yake, ushujaa wake na mengine aliyoyafanya, kama vile tuonavyo leo hii katika magazeti na majarida au katika matangazo mbali mbali. Haya ndiyo maombolezo ya Kijaahiliya ambayo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) ametukataza, na jambo hili linaingia katika jumla ya maombolezo na kelele ambazo zinamdhuru maiti na watu wake wala hayawanufaishi na chochote.

Share

26-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kutaja mazuri ya maiti na kuacha mabaya yake

 

Kutaja mazuri ya maiti na kuacha mabaya yake:

 

 

Ikiwa hapana budi kumzungumzia maiti ni bora wamzungumzie mazuri yake ikiwa maiti huyo ni katika jumla ya sifa aliyokuwa nayo na kuacha kuzungumzia mabaya yake ikiwa ni mtu mwenye mabaya, kwani hayo mazuri ndiyo yatakayomnufaisha yeye kwa Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) na asisingiziwe yasiyokuwa ya kwake.

Tunajifunza katika hadithi ya Bukhari na Muslim: kuwa kuna wakati lilipita jeneza na watu wakamtaja mazuri ya yule maiti, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akasema, “Amestahiki, amestahiki, amestahiki” jeneza lingine likapita na watu wakataja mabaya ya yule maiti wa pili, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akasema, ““Amestahiki, amestahiki, amestahiki” Umar akauliza, ‘Fidia iwe juu yako kwa baba yangu na mama yangu, ilipita jeneza watu wakamtaja kwa kheri ukasema, “Amestahiki, amestahiki, amestahiki” lilipopita jeneza la pili akatajwa vibaya ukasema, “Amestahiki, amestahiki, amestahiki” Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akasema, “Mtakayemtaja kwa kheri amestahiki pepo, na mtakayemtaja kwa shari amestahiki moto, nyie ni mashahidi wa Allah katika ardhi, nyie ni mashahidi wa Allah katika ardhi.”

 

 

Share

27-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kuoshwa maiti upesi

 
Kuoshwa maiti upesi:
 
 
Katika mambo ya kheri ambayo humfikia maiti ni kufanya upesi katika kumtayarisha kwa kumkosha, kumkafini na kumzika.
 
Katika kuoshwa vinachungwa vifuatavyo:
 
· Idadi ya kuoshwa iwe ni mara tatu na zaidi ikibidi kwa haja kwa sharti kuwa idadi hiyo iwe ni witri: tatu, tano au saba na mfano wa haya.
 
· Itumike majani ya mkunazi au sabuni katika kila anapokoshwa ili kumsafisha vizuri zaidi.
 
· Muoshaji atumie sabuni au mfano wake kama vile siku hizi gloves inavyotumika na kuwepo na sitra yenye kumfunika maiti baada ya kuvuliwa nguo.
 
· Ni vizuri kutia kafuri katika maji haswa katika josho la mwisho au mafuta mazuri maadamu sio haramu, na inapokuwa ni haramu basi hayafai.
 
· Kucha za mwanamke zitapunguzwa na kuoshwa vizuri, hali kadhalika nywele zake kuchanwa na kufungwa vifundo vitatu nyuma yake.
 
·  Aanze kukosha sehemu za kulia kwanza na sehemu za udhu
 
·  Mwanamume hukosha wanaume, mwanamke hukosha wanawake, mume humuosha mkewe na mke humkosha mumewe.
 
·  Shahidi, aliyekufa katika vita hakoshwi.
Share

28-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kinachomlazimu mwenye kukosha

 
Kinachomlazimu mwenye kukosha:
·         Ni vizuri muoshaji awe ni mwenye kujua zaidi Sunna za josho na matendo yake katika jamaa na ndugu wa karibu zaidi wa maiti au mtu mwingine katika watu wenye elimu na fadhila.
·         Ni juu ya muoshaji kusitiri aibu za maiti, haifai kuhadithia anachokiona kwake, ama akiona kizuri kwa maiti basi na aseme hamna neno katika kuelezea ya kheri.
·         Ni juu ya mkoshaji katika tendo lake hili au amali yake hii njema ya kukosha anayofanya atarajie radhi za Allah (Subhaanahu wa Ta'ala)
Share

29-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kumkafini na kumpamba maiti

 
Kumkafini na kumpamba maiti:
 
 
Baada ya kumkosha maiti kinachofuatia ni kumpamba, kwa kauli yake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) aliyoisema, “Atakapomkafini mmoja wenu nduguye basi na ampambe.”
Kinachochungwa katika kumvisha sanda (kafini) maiti ni haya yafuatayo:
1.     Fungu la mali ya maiti ndilo litumike katika jambo hili kama atakuwa amewacha mali.
2.     Limsitiri kiwiliwili chake chote bila ya kufanyika kwa israfu.
3.     Kitambaa chenyewe kiwe ni cheupe na kinapendeza kikiwa ni cha pamba.
4.     Kutokuvishwa sanda katika vitu vilivyoharimishwa kama vile hariri, kwani hiyo ni haramu kwa mwanamume, kwa mwanamke ni halali katika hali ya kawaida lakini ikitumika kama sanda inakuwa ni katika israfu.
5.     Maiti avishwe sanda kuanzia moja hadi tatu, haifai kuzidisha zaidi ya hapo. Inapendeza zaidi kuwa ni tatu tu.
6.     Muhrim atakapokufa atazikwa kwa nguo zake mbili alizofia nazo.
7.     Shahidi atazikwa kwa nguo zake alizofia nazo bila ya kukoshwa.
8.     Sanda itakapokuwa ni ndogo na fupi basi kichwa cha maiti kitasitiriwa na kutawekwa katika miguu yake majani ya idhkhir au majani mengine yoyote.
Share

30-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Je, maiti itahamishwa kutoka katika nchi aliyofia na kupelekwa nchini kwake?

Je, maiti itahamishwa kutoka katika nchi aliyofia na kupelekwa nchini kwake?
 
Mtu anaweza kufa katika nchi isiyokuwa ile anayoishi au katika kijiji chake, kiasi cha kuwa wakati mwingine ikahitajika kumsafirisha kumrudisha katika nchi yake ya asili au ile anayoishi (ambapo ndipo penye watoto wake, ndugu na jamaa zake) je, jambo hilo linafaa kisheria?
Jibu: jambo hilo halifai kisheria kwani huchelewesha kuzikwa kwa maiti, kisha baada ya hapo ni kinyume na Sunna.
Imepokewa kutoka kwa Aisha (Radhiya Allaahu 'anhu) kuwa nduguye mmoja alikufa katika sehemu iitwayo Waadil Habasha akahamishwa kutoka sehemu ile, Aisha akawaambia waliomhamisha, ‘Linanihuzunisha (nyie kufanya hivyo) ni vizuri kama angezikwa sehemu ile aliyofia.’
Share

31-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kulisindikiza Jeneza

Kulisindikiza Jeneza:
 
 
Hii ni moja katika haki miongoni mwa haki za Waislamu kwa nduguye kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam), “Haki ya Muislamu kwa nduguye Muislamu ni tano: Kujibu salamu, kumtembelea mgonjwa, kulisindikiza jeneza, kuitikia mwito na kumuombea mwenye kupiga chafya.” (Bukhari na Muslim)
Mambo yafuatayo huchungwa katika kubeba Jeneza:
·         Jeneza kubebwa mabegani, sio vizuri kubebwa kwa gari ila itakapokuwa ni dharura.
·         Lifuatwe kuanzia nyumbani, kuswaliwa hadi anapomalizwa kuzikwa.
·         Kumpeleka kwa mwendo wa haraka lakini sio kulikimbiza jeneza.
·         Inajuzu kuwa mbele ya jeneza au nyuma yake, kuliani mwake au kushotoni mwake, ila aliyepanda gari au mnyama anatakiwa akae nyuma ya jeneza.
·         Haifai kufuata kwa maombolezo na makelele, au kwa kubeba vijinga vya moto au kufuatwa na wanawake au kwa sauti hata ikiwa ni kwa kufanya dhikri. Mfano wa hayo; kilichoenea miongoni mwa watu wanapobeba jeneza husema, ‘wahidu’ yaani semeni, ‘Laa ilaha illa llah’ hii ni miongoni mwa bid’a na ni makosa katika kusindikiza jeneza kufanya hivyo. Na katika jumla ya makosa mengine hali kadhalika ni kuwa kwa wale wanaobeba jeneza kwa gari huweka kaseti na radio yenye kusoma Qur’an au kutoa khutuba, hili nalo halifai na ni kinyume na Sunna katika kulifuata jeneza ni vizuri watu wakawa na subira, kuwa na mazingatio katika tukio hili zima kwani aliyebebwa leo ni ndugu yao na kesho atabebwa yeye.
Share

32-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Swala ya Jeneza

 
Swala ya Jeneza:
 
 
Suala hili la kuswaliwa maiti ni katika jambo kubwa ambalo maiti ananufaika nalo. Hivyo basi katika wale wanaopenda maiti wao wafaidike na hili ni vizuri wakaona kuwa idadi ya wanaomswalia maiti ni wengi tena wengi wao ni wale wema Mukhliswiin miongoni mwao. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “ Hakuwa maiti atakayeswaliwa na watu wanaofika mia moja na wote wakamuombea isipokuwa Mwenyezi Mungu atakubali maombezi yao.” (Muslim). Hali kadhalika katika hadithi nyingine tena Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “Hakuwa Muislamu aliyekufa na watu wakasimama katika jeneza lake wakafikia arobaini hawamshirikishi Mwenyezi Mungu na chochote ila Mwenyezi Mungu atakubali maombezi yao.” (Muslim)
Share

33-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Sifa ya swala ya Jeneza

 
Sifa ya swala ya Jeneza:
 
 
·         Inapendeza idadi ya wenye kumswalia kuwa wengi na safu zikaongezeka nyuma ya jeneza.
·         Atakayeongoza swala ya kumswalia maiti awe ni Imam au naibu wake au yule mwenye uwezo zaidi wa kusoma Qur’an, au awe mwenye kuijua Sunna zaidi au vinginevyo awe ni yule aliyekuwa mkubwa zaidi kwa umri.
·         Inapendeza swala iwe nje ya msikiti karibu na anapoishi na hufaa ndani ya msikiti kwa haja.
·         Imamu husimama usawa wa kichwa cha maiti mwanamume au katikati ya kiwiliwili (kiunoni) mwa maiti mwanamke.
·         Jeneza huwekwa kiasi cha kuwa kichwa cha maiti huwa kuumeni mwa Imamu akiwa anaelekea Qibla.
·         Imamu hunyanyua mikono yake katika takbira ya kwanza tu au katika takbira zote, na maamuma humfuata imamu wake.
·         Imamu hunyanyua sauti yake kwa takbira, lakini maamuma hanyanyui sauti yake.
·         Imamu baada ya takbira ya kwanza atasoma suratul Fatiha, ama baada ya takbira ya pili atamswalia Mtume kama ilivyo katika tashahhud, katika takbira ya tatu na ya nne atamuombea maiti dua maalum kisha atawaombea waislamu wote.
·         Inapendeza dua zitakazosomwa ni zile ambazo zimepokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) vinginevyo basi dua zozote zile zinazotaka maghfira na rehma kwa maiti.
·         Akimaliza swala atatoa salamu mara moja tu kuumeni au akipenda atatoa salamu mbili.
·         Inajuzu kuzidisha takbira na dua.
·         Hakuna kurukuu na kusujudu katika swala ya jeneza na ni wajibu mtu kuchukua udhu wake.
 
Share

34-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Dua zilizopokelewa katika dua za Jeneza

Du'aa zilizopokelewa katika dua za Jeneza:
 
 
Kutoka kwa 'Awf bin Maalik (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema, ‘Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) aliliswalia Jeneza nikahifadhi du'aa yake alipokuwa akiomba,
 
 
اللهُـمِّ اغْفِـرْ لَهُ وَارْحَمْـه، وَعافِهِ وَاعْفُ عَنْـه، وَأَكْـرِمْ نُزُلَـه، وَوَسِّـعْ مُدْخَـلَه، وَاغْسِلْـهُ بِالْمـاءِ وَالثَّـلْجِ وَالْبَـرَدْ،
وَنَقِّـهِ مِنَ الْخطـايا كَما يُنَقََّ الـثَّوْبُ الأَبْيَـضُ مِنَ الدَّنَـسْ، وَأَبْـدِلْهُ داراً خَـيْراً مِنْ دارِه، وَأَهْلاً خَـيْراً مِنْ أَهْلِـه،
وَزَوْجَـاً خَـيْراً مِنْ زَوْجِه،  وَأَدْخِـلْهُ الْجَـنَّة، وَأَعِـذْهُ مِنْ عَذابِ القَـبْر وَعَذابِ النّـار
 
“Allahumma ighfir lahu warhamhu, Waafihi waafu anhu, wa’akrim nuzulahu, wawasigh madkhalahu, wa’aghsiluhu bil maai wathalji walbarad, wanaqihi minal khatwaaya kama Yunaqa thawbul abyadhu mina ddanas, wa abdil-hu daaran khayran min daarihi, wa ahlan khayran min ahlihi, wazawjan khayran min zawjihi, wa adkhil-hul Jannah, wa a'idh-hu min ’adhabil Qabri, wamin 'adhaabin nnaar.”Anaendelea kusema Maalik, ‘Nikatamani kuwa mimi ndio niwe yule maiti anayeswaliwa.”  
 
Kutoka kwa Zaid bin Rukaana bin Abdul Mutwalib amesema, ‘Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) anaposimama kuliswalia jeneza husema, “Allahumma abduka wa ibn Amatak ahtaaj ila rahmatika, wa anta ghaniyu ‘an 'adhaabihi, Inn kaana muhsinan fazid fi hasanaatih, wain kaana musiian fatajaawaz ‘anhu.” (Al-Haakim)
Wakati fulani aliulizwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu), ‘Ni vipi kuswalia Jeneza? Abu Hurayrah Allahumma inahu 'abdika wa ibn 'abdika wa ibn amatika, kaana yashhadu an laa ilaaha illa Allaahu, wa ana Muhammadan 'abduka wa rasuuluka, wa anta a’lamu bihi, Allahumma in kaana muhsinan fazid fii hasanaatih wa in kaana musiian fatajaawaz 'an sayiatihi, Allahumaa laa tuharimna ajrahu wala tuftina ba'dahu.” (Maalik)
 
Share

35-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kulipeleka upesi Jeneza

 

 

Kulipeleka upesi Jeneza:

 

 

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “Lipelekeni upesi jeneza likiwa ni la mtu mwema basi mtakuwa mnamuwahisha kwenye kheri yenyewe na likiwa kinyume na hivyo basi mnaondosha shari kwenye mabega yenu.” (Bukhari na Muslim)

Katika hadithi nyingine amesema, “Litakapowekwa jeneza na watu wakaweka katika mabega yao, basi likiwa ni la mtu mwema litasema, “Nipelekeni, likiwa la mtu asiye mwema litasema, “Ole wangu wananipeleka wapi?! Kila kitu kinasikia sauti ile isipokuwa mwana adamu tu na lau akilisikia basi atapata mshtuko mkubwa unaoweza kumuangusha ….(saaka).” (Bukhari)

 

Share

36-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Muda unaokatazwa kuswalia jeneza na kuzika

 

Muda unaokatazwa kuswalia jeneza na kuzika:

 

Kutoka kwa Uqbah bin ‘Amir (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema, ‘Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) ametukataza kuswalia na kuzika maiti katika nyakati tatu; pindi linapochomoza jua hadi linapotulia juu, pindi jua linapokuwa katikati hadi linapopinda, pindi jua linapoanza kuzama hadi linapokuwa limezama kabisa.’ (Muslim)

Nyakati zenyewe ni hizi: linapochomoza hadi baada yake kama dakika ishirini hivi hadi nusu saa, kabla ya Swala ya Adhuhuri kwa dakika ishirini hadi inapoadhiniwa adhuhuri, kabla ya Maghrib hadi linapozama kabisa jua.

Share

37-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kumuombea maiti baada ya kuzika

 

Kumuombea maiti baada ya kuzika:

 

 

Ilikuwa ndio ada ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) anapomaliza kuzika akisimama kaburini na husema, “Nyote muombeni Mwenyezi Mungu amsamehe ndugu yenu na amfanye thabiti kwani hivi sasa anahojiwa.” (Abu Daud na wengineo)

 

Share

38-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Je, Dua ya pamoja husihi?

 

 

Je, Dua ya pamoja husihi?

 

 

Tunajifunza kulingana na hadithi iliyopita makosa mbali mbali yenye kufanywa na watu wengi wanaposimama makaburini mmoja wao anasimama na kuanza kuomba dua kwa sauti kubwa na wengine huitikia Amin, ilivyo kama tunavyojifunza katika hadithi iliyotangulia ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) aliwaamrisha masahaba zake wamtakie maghfira maiti wao kila mmoja katika nafsi yake na amuombe Mwenyezi Mungu amthibitishe pindi atakapoulizwa na malaika wawili.

 

Share

39-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Je, maiti hulakiniwa majibu ya Malaika wawili?

 

Je, maiti hulakiniwa majibu ya Malaika wawili?

 

Imepokewa hadithi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam): Kuwa maiti anapowekwa kaburini humjia malaika wawili wakali na humweka kitako na huanza kumhoji: ni nani Mola wako? Ni ipi dini yako? Ni nani Mtume wako? Baada ya maswali hayo kila mja atajibu kulingana na maisha yake yalivyokuwa hapa duniani na Mwenyezi Mungu atawapa Ithbati wale wote waliokuwa wakimuamini yeye kwa kauli iliyo thabiti katika maisha haya ya dunia na huko akhera, na dhalimu atakuwa katika upotevu na Mwenyezi Mungu hufanya ayatakayo.

Maiti hanufaiki na Talqin ya walio hai kwake kama wanavyofanya wengine baada ya kuzika, mtu anasimama kaburini kisha anasema, ‘Ee, fulani bin fulani watakapokujia malaika wawili na wakakuuliza ni nani Mola wako, sema, Mola wangu ni Allah …’ jambo hili halikuthibiti kufanywa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) au hata masahaba zake, lingekuwa ni jambo la kheri basi lingefanywa na hao wa mwanzo, maadamu hawakufanya basi atakayefanya atakuwa amefanya bid’a, na kila bid’a ni upotevu na kila upotevu ni katika moto. Hili si katika jambo ambalo litakalomnufaisha maiti. Hadithi iliyotangulia haina maelezo zaidi ya kumuombea na kumtaka awe thabiti katika kauli yake na sio kumlakinia kaburini.

Share

42-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kutoa mkono wa pole (Taazia)

 

 

Kutoa mkono wa pole (Taazia):

 

 

Ni vizuri kuwapa pole wafiwa ili kuwaliwaza na kuwahimiza subira na kuridhika kwa yale aliyotaka Allah (Subhaanahu wa Ta'ala), hivyo basi kuwapunguzia huzuni waliyokuwa nayo na kumbashiria malipo ya wanaosubiri. Ni vizuri zaidi kutumia matamko aliyotumia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) na aliyotufundisha katika kutoa mkono wa pole au atakachoweza mtu maadam hakuna makosa ndani yake.

 

Share

43-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Je, kunafaa kukusanyika kwa ajili ya Taazia?

 

Je, kunafaa kukusanyika kwa ajili ya Taazia?

 

 

Mkusanyiko wa namna hii haufai; sio makaburini au sehemu yoyote maalum kwa ajili ya tukio hilo. Ama baadhi ya watu wenye kutaka kheri katika jamaa za maiti husimama safu moja ndefu makaburini, na hivyo huja watu mmoja mmoja wenye kutoa mkono wa pole kisha wakawasalimia na kuwapa mkono wa pole wafiwa mmoja mmoja. Jambo hili pamoja na kuwa makusudiwa yake ni kuondosha bid’a ya kukusanyika majumbani kwa ajili ya taazia ila nalo ni katika makosa na hayajathibiti katika Sunna na hayakufanyika wakati wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) na hata wakati wa masahaba zake. Jambo hili lina ugumu katika utekelezaji wake kwani watu wa maiti katika kutekeleza kwake yawahitajia kusimama muda mrefu kusubiri mkono wa pole kutoka kwa waliohudhuria mazishi, hii ni taklifu ambayo haitakiwi waipate wafiwa. Linaloweza kufanyika ni kuwa watu hupeana pole popote pale penye wasaa bila ya taklifu kwa pande zote mbili.

 

Share

44-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Je, wafiwa huwatengenezea wahani chakula?

 

 

Je, wafiwa huwatengenezea wahani chakula?

 

 

Haifai kwa wafiwa kutengeneza chakula kwa wahani, lakini kinyume chake ndio sahihi wao ndio wenye haja haswa ya kutengenezewa chakula kwa msiba waliokuwa nao, huzuni ambayo inawafanya kukosa hamu ya kula, hivyo basi ni katika Sunna kwa jamaa wa karibu wa maiti (wasio kuwa wafiwa wa daraja la mwanzo) pamoja na majirani zao kuwatengenezea wafiwa chakula kitakachowatosheleza.

Share

45-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Matamko ya taazia ni haya yafuatayo

 
Matamko ya taazia ni haya yafuatayo:
 
Mtume aliagizwa mara moja kwa mmoja wa wanawe hali ya kuwa ana mtoto anayetaka kufa, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akasema, “Hakika ni cha Allah alichokichukuwa na ni chake alichokitoa, na kila kitu mbele yake kinakwenda kwa muda maalum, hivyo subiri na ujitathmini.” (Bukhari)
Hali kadhalika siku moja Mtume alimuona mwanamke fulani akilia kaburini, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akamwambia, “Mche Mwenyezi Mungu na usubiri.”
 
Share

46-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Matamko yaliyokatazwa

Matamko yaliyokatazwa:
 
 Imezoeleka kwa baadhi ya watu kumwambia mfiwa aliyefiliwa na mtu wa karibu yake maneno haya, ‘Yaliyobaki yawe katika maisha yako’ haya ni matamko yasiyotakiwa kwani yaweza kufahamika maana yake kuwa, ‘kuwa maiti hakukamilisha umri wake, na kuwa kuna umri wake ambao hakuishi, hivyo basi huomba baki ya umri ambao hakuishi uende kwa jamaa na ndugu zake walio hai. Mwenyezi Mungu amebainisha kuwa ajal ya mtu itakapofika haicheleweshwi wala haiwahi saa wala dakika, kwa hivyo tena hakuna tena baki ya Umri wa yule aliyekufa.
 
Share

47-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Dua za Waislamu zinamnufaisha maiti

 

Dua za Waislamu zinamnufaisha maiti:

 

Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala) amesema, “Na waliokuja baada yao wanasema: Mola wetu Mlezi! Tughufurie sisi na ndugu zetu waliotutangulia katika Imani, wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu undani kwa walio amini. Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe ni Mpole na Mwenye kurehemu.” (59:10)

Katika hadithi yake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “maombi ya Muislamu kwa nduguye ni yenye kujibiwa, katika kichwa chake kuna malaika aliyewakilishwa kila atakapomuombea nduguye kheri anasema malaika yule: Amin, nawe upate kama hivyo (ulivyomuombea nduguyo).” (Muslim)

Share

48-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kumlipia maiti saumu

 

Kumlipia maiti saumu:

 

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “ Atakayekufa ilhali kaacha deni la funga basi na alipiwe na walii wake.” (Bukhari na Muslim)

Katika sahihi mbili tunasoma: kuwa mwanamke fulani alisafiri baharini akapanda chombo akanadhiria kwa Mwenyezi Mungu kuwa akimuokoa atafunga mwezi mzima, Mwenyezi Mungu akamuokoa lakini hakufunga hadi alipofariki. Wakaja jamaa zake wa karibu kama sio dada yake basi alikuwa ni bintie akaenda kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akamueleza kuhusu ile nadhiri ya funga ya mama yake. Mtume akamuuliza, “Je, unaonaje je, angelikuwa anadaiwa na mtu si ungemlipia deni lile?” yule binti akajibu, ‘Ndio’ kisha Mtume akamwambia, “basi mlipie funga yake.” Hali kadhalika linaingia hapo funga zote za wajibu na za kunadhiria.

Share

49-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kumlipia maiti nadhiri

 

Kumlipia maiti nadhiri:

 

 

Sa’ad bin ‘Ubada alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam), ‘Hakika mama yangu amefariki na alinadhiria? Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamjibu, “Mlipie nadhiri yake au tekeleza nadhiri yake.”

 

Share

50-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kumtolea sadaka maiti

 

Kumtolea sadaka maiti:

 

Tunasoma katika sahihi mbili kuwa: mtu mmoja alisema, ‘Mama yangu alijisahau na lau angeliweza kusema angetoa sadaka, je, atapata ujira nikimtolea sadaka?’ Mtume akajibu, “Ndio atapata ujira na malipo kwa sadaka hiyo.” Hali kadhalika tunasoma katika sahihi ya Bukhari kuwa, “Sa’ad bin ‘Ubada alifiliwa na mama yake wakati hayupo, akasema, ‘Ee, Mtume wa Allah, mama yangu amefariki nami sipo, je, itamfaa lau nikimtolea sadaka? Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akajibu, “Ndio (atanufaika kwa sadaka hiyo)” kisha Sa’ad akasema kama ni hivyo, ‘Basi nakushuhudia kuwa ukuta wenye mitende mingi ni sadaka yake.’

 

Share

51-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kutoa sadaka mali ambayo haikuusiwa

 
Kutoa sadaka mali ambayo haikuusiwa:
 
 
Muslim amepokea kuwa: kuwa mtu mmoja alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam), ‘Baba yangu amefariki na ameacha mali ambayo hakuusia chochote; Je, nikitoa sadaka mali hiyo itamsaidia kumpunguzia madhambi yake au je, atapata malipo kwa jambo hilo? Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akajibu, “Ndiyo.”  
 
Share

52-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kuacha huru mtumwa, kutoa sadaka na kuhiji humnufaisha Muislamu

 

 

Kuacha huru mtumwa, kutoa sadaka na kuhiji humnufaisha Muislamu:

 

 

Abu Daud na wengineo wamepokea kuwa, “ ‘Al-Aas bin Wail As-sahami aliusia waachwe huru watumwa mia moja, mwanawe Hisham akawaacha huru watumwa hamsini tu. Mwanawe mwingine aitwae Amruu akataka kuwaacha wale watumwa wengine hamsini waliobakia, akaenda kwanza kumuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam). alipomfikia akamuuliza, ‘Ewe Mtume wa Allah, hakika baba yangu ameusia waachwe huru watumwa mia moja, lakini ndugu yangu Hisham amewaacha watumwa hamsini tu, hivyo wamebaki hamsini. Je, niwaache huru? Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akajibu, “lau baba yenu angelikuwa Muislamu na mkaacha huru watumwa au mkamtolea sadaka au mngelimhijia basi angenufaika na hayo na malipo yake yangemfikia.”

 

Share

53-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kumhijia asiyehiji

 

 

Kumhijia asiyehiji:

 

 

Imepokewa na Bukhari kuwa: mwanamke kutoka kabila la Juhayna alikwenda kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam), akamuuliza, ‘Mama yangu aliweka nadhiri kuwa atahiji lakini hakuhiji hadi alipofariki, je, nimuhijie? Mtume akamjibu, “Ndio, mhijie, je, huoni kuwa kama mama yako angekuwa anadaiwa ungelipia deni lake? Tekeleza deni la Mwenyezi Mungu na Yeye ndiye Mwenye haki ya kulipwa deni lake.”

Katika Sahihi Muslim inasmuliwa kuwa mwanamke kutoka kabila la Khath’am alisema, ‘Baba yangu ni mzee sana na ana faradhi ya Hijja ambayo hakuitekeleza naye hawezi kukaa juu ya mgongo wa mnyama. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akamjibu, “Mhijie.”

Katika hadithi nyingine sahihi iliyokuwa mashuhuri, ‘kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) alimsikia mtu akisema, ‘Labaika Allahumma kwa Shubruma, Mtume akamwambia mtu yule, ‘Je, huyo Shubruma ni nani? Yule mtu akajibu, ‘Ni ndugu au jamaa yangu wa karibu.’ Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akamuuliza, ‘Je, wewe mwenyewe umehiji.? Yule mtu akajibu, ‘hapana.’ Hapo Mtume akasema, “Jihijie mwenyewe kwanza kisha muhijie Shubrama.”

 

 

Share

54-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Au kijana mwema atakayemuombea dua

 
Au kijana mwema atakayemuombea dua:
 
Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala) amesema, “…Na useme: “Mola wangu! Warehemu (wazee wangu) kama walivyonilea katika utoto.” (17:24)
Nae Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “atakapokufa mwanadamu matendo yake yote hukatika ila hubakia mambo matatu; sadaka yenye kuendelea, elimu yenye kunufaisha au kijana mwema atakayekuombea dua.” (Bukhari na Muslim)
Ama Abu Daud na Ibn Majah nao wamepokea kutoka kwa Abu Usaid Malik Ibn Rabia Assaidy amesema, ‘Tulipokuwa kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) alitokea mtu mmoja wa kabila la Salama, mtu yule akamuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam), ‘Je, kuna kilichobakia katika wema ninaoweza kuwafanyia wazazi wangu baada ya kifo chao? Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akajibu, “Ndio, kuwaombea dua na msamaha kwa Mwenyezi Mungu, kutekeleza ahadi ulizowapa baada ya kifo chao, kutembelea wagonjwa hali kadhalika kuwatembelea jamaa na ndugu ambayo haiwezikani bila ya wewe kuwa mtoto wao, na kuwakirimu rafiki zao.”
 
Share

55-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Je, husomewa Qur’an na Al-Faatiha?

 
Je, husomewa Qur’an na Al-Faatiha?
 
Ni jambo ambalo limezoeleka kwa watu wengi kusema, ‘Al-Faatiha kwa roho ya fulani, au kusoma surat Yaasin katika kaburi la maiti, au kusoma baadhi ya aya au sura katika Qur’an na huleta nakala za misahafu kuwagawia watu wengine watumie katika kusoma pale kaburini, wengine hujenga hema kubwa baada ya kifo na baada ya hapo linakuwepo kila alhamisi ya mwanzo na ya pili ya kifo chake na arbaini na kumbukumbu ya mwaka ya kifo chake bali haiishii hapo na katika misimu mbali mbali kumbukumbu yake inaendelea na katika hali hizo hukodiwa mtu maalum ambaye atasoma Qur’an na watu hukusanyika. Kila inapokuwa jamaa wafiwa wana mali nyingi na watu wenye hadhi katika jamii basi yule msomaji wa Qur’an anayekodishwa huwa ni maarufu zaidi na mahema yenye kufungwa au kumbi zenye kukodishwa huwa ni kubwa na ghali zaidi. Mali nyingi hutumiwa katika shughuli hizi na malipo atakayelipwa huyo msomaji wa Qur’an ili kuzihuisha siku hizo za kumbukumbu itakuwa ni kubwa sana kwa kusoma robo ya Qur’an mbali na gharama nyingine ambazo wanatakiwa walipe wafiwa. La shaka kuwa mambo haya ni kinyume kabisa na sheria ya dini ya Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) katika nyanja mbali mbali mfano:
·         Kinyume na Sunna katika kuacha kufanya Istighfaar iliyokokotezwa kisheria na dua zilizothibiti hadi kuzua matendo na maneno ambayo Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala) hakuteremsha.
·         Katika kufanya mambo kama haya mtu anakuwa anajiingiza katika israfu, na haya yamekatazwa na Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) pamoja na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam), kwa mfano tunasoma katika Qur’an: “…na wala msifanye ubadhirifu. Kwa hakika Yeye hapendi wanao fanya israfu. (7:31) hali kadhalika katika sura nyingine tunajifunza, “ Hakika wabadhirifu ni ndugu wa Mashetani…” (17:27) mambo haya ni katika mambo ya bid’a na haramu iweje mtu akadhani mambo kama haya yatamfaa maiti?! Huku ni kukuza mambo na kukumbusha huzuni kila mara na kujeruhi donda linalokaribia kupona. Huenda ikapelekea kila Alhamisi hizo za kumbukumbu na kila vikao hivi vinapofanyika watu wakawa wanalia kila wanapokutana. Haya si katika mambo yenye kufaa kufanywa.
 
Share

56-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Je, huswali swala yake na ya babake au hufunga kwa funga yao?

Je, huswali swala yake na ya babake au hufunga kwa funga yao?
 
 
Amesema Imam Muslim katika utangulizi wa sahihi yake, ‘Amesema Muhammad kuwa, nimemsikia Abu Ishaka ibrahim bin Issa Attwalaqaan akisema, ‘Nilimuuliza Abdullah bin Mubaarak, ‘Ewe, Abu AbduRahman! Vipi kuhusu ile hadithi inayosema, “Hakika katika wema mzuri zaidi kufanya baada ya wema ni kuwaswalia wazazi wako pamoja na swala yako, na kuwafungia saumu pamoja na saumu yako.” Akasema kuwa, ‘Abdullah bin Muba’rak akasema, ‘Ewe, Abu Ishaka hadithi hii imetoka kwa nani? Akajibu, ‘Ni katika hadithi ya Shihaab bin Kharaash.’ Abdullah bin Muba’raka akasema, Huyu ni mtu anayeaminika’ Je, imetoka kwa nani?’ Nikasema, ‘Kutoka kwa al-Hajjaj bin Di’nar. Abdullah akasema, Huyu nae anaaminika’ Je, kutoka kwa nani? Nikasema, ‘kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam)’. akasema Abdullah bin Mubarak, ‘Ewe, Abu Ishaka hakika baina ya al-Hajjaj bin Di’nar na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) mafaawidh tanqatwih fiiha ahnaaq al-Matwy  lakini katika sadaka hakuna tofauti. Hapa Abdullah bin Mubaarak (rehema ya Allah iwe juu yake) anakusudiwa kuonesha kuwa hadithi yenyewe ni dhaifu lakini ile sehemu yenye kutaja sadaka ni sahihi hakuna tofauti miongoni mwa watu wenye elimu katika kujuzisha sadaka lakini si swala.
 
Share

57-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kuzuru kaburi lake na kumuombea

 

 

Kuzuru kaburi lake na kumuombea:

 

 

Ziara ya makaburi ni jambo lililoruhusiwa kisheria, ni jambo lenye faida kwa walio hai ili wawaidhike na iwakumbushe na akhera ajue mwenye kuzuru kaburi kuwa hapo alipo nduguye naye atakuwamo siku moja. Hali kadhalika faida nyingine ni kuwaombea nduguze waislamu na huyo maiti wake. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “Nilikuwa nimewakataza kwanza kuzuru makaburi lakini kuanzia sasa yatembeleeni.” (Muslim) katika lafdhi nyingine hadithi inasema, “Kwani huko kuzuru makaburu hukukumbusheni na akhera.” (Ahmad)

 

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) wakati fulani alilitembelea kaburi la mama yake akalia na walio pambizoni mwa Mtume nao wakalia sana kisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akasema, “Nilimuomba idhini Mola wangu nimuombee msamaha kwake lakini Mwenyezi Mungu hakunipa idhini hiyo, nikamuomba nilitembelee kaburi lake akanipa idhini, tembeleeni makaburi kwani huko kunawakumbusheni na mauti.” (Muslim)

Share

58-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Je, ni ruhusa kwa wanawake kutembelea makaburi?

 
Je, ni ruhusa kwa wanawake kutembelea makaburi?
 
 

Wakati tunazungumzia suala hili yapasa kuangalia sura nyingi kama hizi zifuatazo:

Kwanza: Haifai kwa wanawake kusindikiza maiti na kuzika kwa mujibu wa maneno ya Ummu Atwiya (Radhiya Allaahu 'anhu), “Tumekatazwa kusindikiza jeneza walam yuuzam alayna. (Bukhari na Muslim)
Pili: inafaa kwa mwanamke kuzuru makaburi baada ya kuzika, ili kumuombea maiti, kwa sharti kuwa azingatie hukumu za kisheria kama vile kujisitiri vizuri, kuacha kupiga makelele katika bid’a na maasi. Katika hili wanawake na wanaume wanakuwa sawa sawa kulingana na kauli yake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam), “Nilikuwa nimewakataza kwanza kuzuru makaburi lakini kuanzia sasa yatembeleeni.” (Muslim)
 
Tatu: kinachokatazwa kwa wanawake ni ziara za mara kwa mara makaburini, kwani ziara hizo za mara kwa mara hupoteza haki nyingi pamoja na udhaifu wa mwanamke katika mas’ala mazima ya misiba na kupiga mayowe na kujigaragaza kwa kuombeleza na mfano wa mambo kama hayo. Kama ilivyopokelewa katika hadithi nyingine inayosema, “Mwenyezi Mungu amewalaani wanawake wenye kwenda mara kwa mara makaburini.”
Share

59-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Matamko yanayotumika katika kuwaombea wafu makaburini

Matamko yanayotumika katika kuwaombea wafu makaburini:
 
Imepokewa katika sahihi Muslim kuwa, ‘Aisha (Radhiya Allaahu 'anhu) alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) Je, tunatakiwa tuseme nini kuwaombea waliokwisha zikwa makaburini?’ Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akamwambia, “ Sema, 
 
 
السَّلامُ عَلَـيْكُمْ أَهْلَ الدِّيارِ مِنَ المؤْمِنيـنَ وَالْمُسْلِمينَ، وَإِنّا إِنْ شاءَ اللهُ بِكُـمْ لاحِقُـونَ

( وَ يَرْحَمُ اللَّهُ الْمُسْتَقْدِمِينَ مِنَّاوَالْمُسْتَأْخِرِينَ) نَسْـاَلُ اللهَ لَنَـا وَلَكُـمْ العَـافِيَةَ.                                             

Assalaam ala ahli diyaar minnal muuminina wal muslimina, wainna inshaAllah bikum llahiquuna.”          wayarhamu llaha al-Mustaqdimiina minna wal musta’khirina, Nas-alu Allaaha Lana wa lakum Al-'Aafiyah
 
“Amani ishuke juu yenu watu wa nyumba za waumini na waislamu, nasi apendapo Mwenyezi Mungu  tutakutana nanyi, tunamuomba Mwenyezi Mungu  atusamehe, sisi na nyinyi.  [Na Mwenyezi Mungu awarehemu wa mwanzo na wa mwisho] namuomba Mwenyezi Mungu  atupe sisi nanyi afya njema.
 
 Mtume anapokuwa kwake alikuwa akitoka usiku wa mwisho na akisema, “Assalamu alaykum dara Qawmi Muuminiin, Wa’atakum maa Tad’uuna Ghadan Muajala’n, Wainna InshaAllah bikum Laahiquun, Allahumma ghfir Liahli Baqiih Al-Gharqad.” (Muslim)
 
Share

60-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Je, Yafaa kusoma Qur’an Makaburini?

 

Je, Yafaa kusoma Qur’an Makaburini?

 

Hili ambalo halikufanywa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam), hakuliamrisha lakini aliamrisha tu kusomwa dua na kuwaombea maghfira kwa Mwenyezi Mungu. Hakupenda watu wasome Qur’an makaburini kwa hadithi yake aliyosema, “Msizifanye nyumba zenu makaburi, kwani shetani hukimbia na huchukizwa na nyumba ambayo itasomwa surat Baqara.” Kadhalika haifai kuswali makaburini, hata ikiwa swala hiyo ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'ala). Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) amesema, “ Swalini nyumbani kwenu wala msizifanye nyumba zenu makaburi.” (Muslim) vile vile amesema, “mmoja wenu kukaa katika jiwe la moto akaunguza nguo yake na moto ule ukaingia katika ngozi yake ni bora kwake kuliko kukaa juu ya kaburi.” (Muslim) hali kadhalika amesema, “Msiswali makaburini na msikae juu yake.” (Muslim)

Share

61-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kuzuru makaburi wakati wa matukio maalum

 
Kuzuru makaburi wakati wa matukio maalum:
 
Watu wengi wamefanya mazoea ya kuzuru makaburi nyakati maalum; kwa mfano wakati wa iddi mbili, katika mwezi wa Rajab, katika siku za Alhamisi na mfano wa hayo katika masiku na miezi ambayo watu wamefanya kuwa ni za matukio maalum. Katika masiku hayo watu ambao huenda kufanya ziara makaburini huandaa chakula maalum na kugawa kwa watu wa makaburi na wengine huchukua hata radio, t.v na hupitisha masiku ya sikukuu ya iddi makaburini; wakiimba, kucheza na kufanya laghwi na lahwi na wakasahau kabisa hali za watu wa makaburi na kuwaombea dua kwa Mwenyezi Mungu kinyume chake wanawaudhi na wanawabughudhi watu wa makaburi.
Hii ni bid’a na ni katika mambo yenye kuzushwa. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) hakufanya wala hakuamrisha lakini kinyume chake ameyakataza, haiwanufaishi waliokuwa hai au waliokuwa wafu. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) aliwahi kusema, “Msifanye kaburi langu kuwa ni mahali pa kurudiwa rudiwa.” Kwa maana msizowee kulizuru katika masiku maalum. Ikiwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) analisemea kaburi lake sembuse makaburi ya watu wengine ndio haswa ya mwanzo kuhadharishwa.
Kwa mja ambae anataka kheri kwa ajili ya nafsi yake basi na ajitahidi kuchunga matumizi ya wakati wake asije kutumia katika lahwi na laghwi na mchezo na maasi na mambo yote yaliyo munkari hata atakapomjia malaika wa mauti anakuwa ameshafanya maandalizi wala hajutii wakati wake uliopita, yaliyopita hayarudi, mtu ajitahidi kila analolifanya ahakikishe kuwa linaingia katika mizani ya mambo yake ya kheri na kupunguza mambo ya shari, jitahidi ufanye litakalokufaa kwa siku yako ya mwisho.
Allahumma hdi Qawmi fainahum laa Yaalamun
Ee, Mwenyezi Mungu waongoze watu wangu kwani wao ni watu wasiojua.
Na utusamehe sisi na maiti wetu Ee, Mola wa walimwengu.
Natoshelezwa na haya machache na kumswalia Mtume wetu Muhammad na Aali zake na sahaba zake.
 
 
Share