Matendo Mema Na Athari Yake Katika Utajiri Na Ukunjufu Wa Rizki

 

 

 

 

الأعمال الصالحة وأثرها في الغنى وسعة الرزق – أسعد محمد الطيب

 

Mfasiri Haliymah ‘Abdullaah Husayn

 

 

Share

00-Matendo Mema Na Athari Yake Katika Utajiri Na Ukunjufu Wa Rizki: Faharasa

 

01. Utangulizi

02. Rizki ni makadirio kutoka kwa Allaah

03. Athari ya matendo mema katika rizki

04. Sababu ya kudhikishiwa rizki

05. Mambo yapasayo kuchunga katika kutafuta rizki

06. Faida ya rizki ya halali katika dunia na akhera

07. Madhara ya chumo la halali

 

Share

01-Matendo Mema Na Athari Yake Katika Utajiri Na Ukunjufu Wa Rizki: Utangulizi

 

Utangulizi

 

Shukrani zote zinamstahiki Allaah, tunamtukuza na tunamtegemea, tunaomba msamaha kwake, tunataka kinga kwa Allaah kutokana na shari ya nafsi zetu na matendo maovu yetu aliyeongozwa na Allaah hakuna wa kumpoteza na aliyepotea hakuna wa kumuongoza. Tunashuhudia hakuna mola wa kuabudiwa kwa haki ila Allaah Pekee na tunashuhudia kwamba Muhammad ni Mja Wake na Mtume Wake.

 

Ama baada, ametaja Allaah rizki ya viumbe katika Qur-aan Tukufu sehemu nyingi, na hii ni dalili ya ukubwa wa Allaah Aliyetukuka na nguvu Zake, kwani Ameumba viumbe na Akatawalia rizki zao, pia ni dalili juu ya rehma  kwa waja Wake na ukarimu Wake mkubwa, Naye ni Tajiri hahitaji kitu kwa viumbe, Naye ni Mtoaji kwa wote.

 

Amesema Allaah:

 

“Sikuwaumba majini na watu illa wapate kuniabudu, Sitaki kwao rizki wala Sitaki wanilishe, kwa yakini Allaah Ndiye Mtoaji wa riziki, Mwenye nguvu, madhubuti.” Adh-Dhariyaat: 57

 

Na Amejaalia AllaahAllaah matendo mema yanaendana na imani na ni sharti ya kupata maisha mazuri na malipo mazuri zaidi Akhera, Amesema Allaah :

 

“Mwenye kutenda mema katika mwanaume au mwanamke naye ni Muumin, Tutamuhuisha maisha mema na Tutawalipa ujira wao kwa mema waliyokuwa wakiyatenda.”

 

Hakika maisha yamewahadaa watu wakatopea nafsi zao katika mali, wakawa wanakimbizana kutafuta rizki kwa njia yoyote iwe halali au haramu, wakafuata nafsi zao  maisha yao yakawa dhalili, wakasahau kitabu cha Allaah na Sunnah, ambavyo ndani yake kuna ponyo (tatuzi) na kila kheri, navyo ni njia ya maisha mazuri na rizki pana na kheri nyingi katika dunia na Akhera.

 

Na sababu ya riziki na baraka ni matendo mema.

 

 

Share

02-Matendo Mema Na Athari Yake Katika Utajiri Na Ukunjufu Wa Rizki: Rizki Ni Makadirio Kutoka Kwa Allaah

 

A.    Rizki Ni Makadirio Kutoka Kwa Allaah

 

Allaahu Ameandika riziki za viumbe kabla hajawaumba, kwani elimu ya Allaah imezunguka kila kitu, hakuna kinachotembea ardhini ila imeandikwa riziki yake na ajali yake na vyote vinavyohusiana naye katika dunia na akhera.

 

 Amesema Allaah :

 

“Na hakuna mnyama yeyote (yaani kiumbe chochote) katika ardhi ila riziki yake iko juu kwa mwenyezi Mungu, na Anajua makao yake ya milele na mahali pake pa kupata tu. (napo ni hapa duniani) Yote yamo katika Kitabu kinachodhihirisha (kila kitu).” Huud: 6

 

 Ametupa habari Allaah Yeye ndiye mwenye kusimamia riziki ya viumbe vyote mdogo wao na mkubwa wao wa baharini na nchi kavu.

 

 “na katika mbingu ziko riziki zenu na mliyoahidiwa.” Adh-Dhaariyaat: 22 

 

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin Mas’uud amesema, amesema Mtume:

 

“Hakika mmoja mwenu anakusanywa katika tumbo la mama yake siku arobaini kisha inakuwa pande la damu mfano wa hivyo (siku 40) kisha inakuwa pande la nyama mfano wa hivyo, kisha Allaah Anamtumia Malaika kwa maneno manne, anamwandikia matendo yake, ajali yake, rizki yake, ni muovu au mwema, kisha anampulizia roho. Na mtu atatenda matendo ya watu wa motoni mpaka inakuwa baina yake na kuingia motoni usawa wa dhiraa inamtangulia Kitabu, anatenda matendo ya watu wa peponi na anaingia peponi.

Na kuna mtu anatenda matendo ya watu wa peponi mpaka inakuwa baina yake na kuingia usawa wa dhiraa, inamtangulia Kitabu anatenda matendo ya watu wa motoni akaingia motoni…” Al-Bukhaariy

 

Na kutoka kwa Anas Bin Maalik Amesema, Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):

 

“Hakika Allaah Amemuwakilisha katika tumbo la uzazi Malaika anasema, Ee Mola tone la manii, Ee Mola pande la damu, Ee mola pande la nyama, atapotaka kuliumba anasema ewe Mola ni mwanaume au mwanamke? muovu au mwema? na ipi rizki yake? na ni ipi ajali yake? Anamwandikia hilo katika tumbo la mama yake.” Al-Bukhaariy

 

Share

03-Matendo Mema Na Athari Yake Katika Utajiri Na Ukunjufu Wa Rizki: Athari Ya Matendo Mema Katika Rizki

 

 

B.    Athari Ya Matendo Mema Katika Riziki

 

 

1. Taqwa (Uchaji Allaah) Na Matunda Yake

 

 

 (a) Kufarijika Baada Ya Huzuni Na Kupata Riziki Pasina Kutarajia

 

“Na anayemuogopa Allaah Humtengenezea njia ya kuokoka (katika kila balaa).

 Na Humpa riziki kwa namna asiyoitazamia. Na anayemtegemea Allaah Yeye humtoshea.” Atw-Twalaaq: 2-3

 

Katika aya hii dalili kwamba Allaah Mtukufu Anawafariji wenye matatizo na Anawapa sababu za kupata riziki pasina ya kutegemea na kwa njia wasiyopanga akilini mwao kutokana ucha Allaah wao.

 

 

 (b) Riziki Nyingi Na Pana

 

 Anasema Allaah:

 

“Na kama watu wa miji wangaliamini na kuogopa kwa yakini tungeliwafungulia baraka za mbingu na ardhi, lakini walikadhibisha tukawapatiliza kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.” Al-A’araaf: 96

 

Alitoka ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) anaomba mvua na hakuzidisha zaidi ya kuomba msamaha, aliporudi mvua ikanyesha, wakamwambia hatukukuona ukiomba du’aa ya mvua, akasema hakika nimeomba mvua kwa mawingu yanayoshusha mvua angani kisha akasoma Suratun Nuuh 10-11

 

“Ombeni msamaha kwa Mola wenu hakika Yeye ni mwingi wa msamaha. Atakuleteeni mawingu yanyeshayo mvua nyingi.”

 

 

2. ISTIGHFAAR

 

Matunda Ya Kuomba Msamaha

 

(a) Kukunjuliwa Rizki

 

Anasema Allaah:

 

“Na ili muombe msamaha kwa mola wenu kisha mtubie (mrejee) Kwake. Atakustarehesheni kwa starehe nzuri mpaka muda maalum (mtapoondoka ulimwenguni). Na Atampa (Akhera) kila mwenye fadhila fadhila yake. Na kama mtakengeuka basi nakuhofieni adhabu ya (hiyo) siku kubwa.” Huud: 3

 

Amewaamrisha kuomba msamaha kutokana na dhambi zilizopita na kutubia kwa Allaah, Atawastarehesheni duniani na Akhera.

 

 

(b) Mvua Kunyesha Kwa Mfululizo

 

Anasema Allaah:

 

Na enyi watu wangu ombeni msamaha kwa Mola wenu (kwa mabaya yenu yaliyopita), kisha mtubie Kwake (kwa kufanya mema sasa na kuacha mabaya, Atakuleteeni mawingu yateremshayo mvua tele, na Atakuzidishieni nguvu juu ya nguvu zenu (mlizonazo). Wala msikengeuke kuwa waovu.” Huud: 52

 

 

(c) Kuongezekewa Mali Na Watoto

 

Anasema Allaah:

 

“Nikawaambia, ombeni msamaha kwa Mola wenu hakika Yeye ni Mwingi wa msamaha. Atakuleteeni mawingu yanyeshayo mvua nyingi. Na Akakupeni mali na watoto, na Atakupeni mabustani, na Atakufanyieni mito.” Nuuh: 10-12

 

 

(d) Kupata Riziki Bila Ya Kutarajia

 

Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):

 

“Mwenye kujilazimisha na kuomba msamaha Atamjalia Allaah kwa kila dhiki utatuzi na katika kila shida faraja na Atamruzuku pasina kutarajia.” Abu Daawuud

 

 

3. KUUNGA UDUGU

 

Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kutoka kwa Allaah “Iliambiwa udugu, hivi huridhii nikimuunga anayekuunga na ninamkata anayekukata? akasema ndio naridhia Ee Mola wangu, akamwambia basi ni hivyo.” Al-Bukhaariy

 

Na kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allahu ‘anhu) amesema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):

“Mwenye kufurahi kukunjuliwa katika riziki na kuongezewa umri (kwa kutenda mema) basi na aunge udugu wake.” Al-Bukhaariy

 

 

4. KUMTEGEMEA Allaah

 

Nayo ni sababu muhimu ya kurahisisha rizki.

 

Kutoka kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allahu ‘anhu) amesema, nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akisema:

 

“Lau nyinyi mngemtegemea Allaah ukweli wa kumtegemea Angewaruzuku kama Anavyomruzuku ndege, anatoka asubuhi na njaa anarudi jioni ameshiba.”

 

Katika Hadiyth hii, inatuwekea wazi (Allaah Anajua) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amekataza kukaa na kutotafuta maisha, bali amehimiza kutafuta riziki kwani ndege anatoka asubuhi mapema kutafuta riziki.

 

 

5. SWALAAH

 

Hakika Swalaah inampa Muumini raha na utulivu na furaha. Nayo pamoja na subra ina athari nzuri ya kutatua vikwazo, tabu, na matatizo anayokumbana navyo mwanaadamu.

 

Anasema Allaah:

 

“Enyi mlioamini jisaidieni (katika mambo yenu) kwa subira na Swalaah: bila ya shaka Allaah Yupo pamoja na wanaosubiri.” Al-Baqarah: 153

 

Amesema Sa’iyd bin Jubayr:

“Subra ni kukiri mja kwa Allaah kwa yaliyompata na kutaraji malipo, thawabu kwa Allaah, huenda mtu akafadhaika naye ana haraka asione subira.”

 

Anasema Allaah:

 

“Na waamrishe watu wako kuswali, na uendelee mwenyewe kwa hayo. Hatukuombi riziki bali Sisi ndiyo tunakuruzuku. Na mwisho mwema utawathubutukia wamchao Allaah.” Twaahaa: 132

 

 

6. KUTOA KATIKA NJIA YA ALLAAH

 

Kutoa katika njia (ajili) ya Allaah kuna malipo duniani na Akhera, duniani unapewa badala, baraka, kukunjuliwa katika riziki, ama Akhera ni kupata pepo kwa fadhila na rehma za Allaah.

 

Anasema Allaah:

 

“Enyi mlioamini toeni katika vile vizuri mlivyovichuma, na katika vile Tulivyokutoleeni katika ardhi.Wala msikusudie kutoa vilivyo vibaya hali nyinyi wenyewe msingevipokea isipokuwa kwa kuviangalia (basi Allaah Atapokea vibaya?) basi jueni kwamba Allaah ni Mkwasi na asifiwaye.

Shetani anakuogopesheni ufakara na anakuamrisheni ubakhili,na Mwenyezi Anakuahidini msamaha utokao kwako na ihsani (kubwa pindi mkitoa) na Allaah ni mwenye wasaa mkubwa na mwenye kujua.” Al-Baqarah: 267-268

 

Kwani Shaytwaan anakuogopesheni ufakiri na kuwakhofisha nayo ili mzuie msitoe kwa ajili ya Allaah mlivyo navyo, pia anawaamrisha uovu, maasi, mambo machafu, na Allaah Anakuahidini msamaha.

 

Anasema Allaah:

 

“Sema: “kwa hakika Mola wangu Humkunjulia riziki Amtakaye katika waja Wake, na Humdhikishia (Amtakaye) na chochote mtakachotoa basi Yeye Atakilipa na Yeye ni mbora wa wanaoruzuku.” Sabaa: 39         

 

Chochote mtoacho mtalipwa duniani na Akhera.

 

 

7. HAJJ NA ‘UMRAH

 

 Ibn Mas’uud amesema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam):

 

“Fuatisheni baina ya Hija na ‘Umrah kwani inaondosha umaskini na madhambi kama kutu inavyoondoshwa katika dhahabu na fedha, na Hija iliyokubaliwa thawabu yake ni pepo.”

 

 

8. KUWASAIDIA MADHAIFU NA KUWAJALI

 

Kutoka kwa Mas’ab bin Sa’ad amesema, aliona Sa’ad yeye ni bora kuliko walio chini yake, akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam): “Je, (hamjui kuwa) mnapata ushindi na riziki ila kwa ajili ya madhaifu wenu?”

 

Kutoka kwa Abu Dardaa amesema, nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akisema: “Kwa madhaifu wenu hakika mnaruzukiwa na kupewa ushindi kwa ajili yao.”

 

Amebainisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuwasaidia madhaifu na kuwaheshimu ni sababu ya kuwepesishiwa riziki na kupata ushindi.

 

 

9. DU’AA

 

 Anasema Allaah:

 

“Na kumbukeni (habari hii nayo) aliposema Ibraahiym: “Ee Mola wangu ufanye mji huu (wa Makkah) uwe na salama na uwape wakazi wake matunda wale wanaomwamini Allaah na siku ya mwisho.” (Allaah) Akasema na mwenye kukufuru (pia) nitamstarehesha kidogo kisha nitamsukumiza katika adhabu ya moto napo ni mahali pabaya kabisa pa kurejea." Al-Baqarah: 126

 

Anasema Allaah:

 

“Ee Allaah Mola wetu tuteremshie chakula kutoka mbinguni ili kiwe sikukuu kwa ajili ya mwanzo wetu (nao ni sisi) na wa mwisho wetu (nao ni wafuasi wetu watakaokuja baada yetu wakasikia haya) na kiwe ishara itokayo kwako basi turuzuku kwani Wewe ndie Mbora wa wanaoruzuku.” Al-Maaidah: 114

 

Kutoka kwa Abu Dhari kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) katika aliyopokea kutoka kwa Mola wake Mtukufu amesema:

 

“Enyi waja wangu Mimi nimeharamisha dhulma juu Yangu na Nimejaalia baina yenu haramu msidhulumiane, Enyi waja Wangu, nyote mmepotea ila Niliyemuungoza niombeni uongofu Nitawaongoza,

Enyi waja Wangu nyote mna njaa ila Niliyemlisha, niombeni chakula Nitawapeni,

Enyi waja Wangu nyote mpo tupu ila Niliyemvisha niombeni mavazi Nitawavisheni…” Muslim

 

 

Kutoka kwa Abu Ja’afar kwamba amemsikia Abu Hurayrah akisema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam):

 

“Itakapobakia theluthi ya usiku Anashuka Allaah Mtukufu katika uwingu wa dunia Anasema: “Nani ananiomba Nimjibu, nani ananiomba msamaha Nimsamehe, nani ananiomba riziki Nimpe, nani anataka kuondolewa matatizo Nimuondolee? Anaendelea hivyo mpaka alfajiri.”

 

Kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah amesema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam):

 

“Je, niwajulisheni itakayowaokoa na adui zenu, na itakayowafanyia nzuri rizki zenu? Ni kumuomba Allaah katika usiku wenu na mchana kwani du’aa ni silaha ya Muumin.” Ibn Maajah

 

Share

04-Matendo Mema Na Athari Yake Katika Utajiri Na Ukunjufu Wa Rizki: Sababu Ya Kudhikishiwa Rizki

 

C. SABABU YA KUDHIKISHWA KATIKA RIZIKI

 

Hakika kupata dhiki katika rizki kuna sababu, na Ametupa habari Allaah katika kitabu Chake, na ametufahamisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) kuna amali (matendo) atakayefanya atanyimwa riziki.

 

 

1. KUMKANUSHA ALLAAH (UKAFIRI)

 

Nayo ni sababu kubwa na muhimu katika kudhikishiwa rizki, ama anayesema makafiri wamepewa rizki pana hayo ni kuwasubirisha wazidishe maovu na baada ya hapo Atawaadhibu Allaah.

 

Amesema Allaah:

 

 “Na atakayejiepusha na mawaidha Yangu (haya) basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki na siku ya Qiyaama tunamfufua hali ya kuwa kipofu) Twaahaa: 124

 

Atakuwa na maisha ya shida (duniani, hatopata utulivu wala ukunjufu wa kifua, hata akistarehe atakavyo, akavaa atakacho, aishi anapotaka, hakika moyo wake daima una hofu na dhiki na tabu pia kutangatanga.

 

 

2. MAKOSA NA MADHAMBI

 

Anasema Allaah:

 

“Hayo (ya kuwafika balaa hizi) ni kwa sababu Allaah Habadilishi kabisa neema Alizowaneemeshea watu hata wabadilishe wao yaliyomo moyoni mwao.” Al-Anfaal: 53

 

Anatupa habari Allaah katika ukamilifu wa uadilifu Wake katika hukmu Yake kwamba Allaah Habadilishi neema Aliyomneemesha yoyote ila kwa sababu ya dhambi alizochuma.

 

 

 Kutoka kwa Thawbaan kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) amesema: “Hakika mtu ananyimwa rizki kwa dhambi aliyofanya wala hairudishi Qadar ila du’aa, wala haizidi katika umri ila wema) Musnad Ahmad

 

 

3. ZINAA

 

Anasema Allaah:

 

“Wala msikurubie zinaa hakika hiyo (zinaa) ni uchafu (mkubwa) na ni njia mbaya (kabisa).”  Israa: 32

 

Anasema Allaah Akiwakataza waja Wake zinaa na kutoikaribia.

 

Kutoka kwa Ibn ‘Umar amesema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam):

 

“Zinaa inarithisha umaskini (Ufakiri), dhiki katika rizki, na maradhi mengi ni adhabu kwa ajili ya zinaa.

 

 

4. UBAHILI NA KUTOTOA

 

Amekataza Allaah ubakhili katika sehemu nyingi kwani ni katika sifa mbaya, na mwenye kusifika na tabia hii ameahidiwa maangamivu.

 

Anasema Allaah:

 

“Na wala wasione wale ambao wanafanya ubakhili katika yale Aliyowapa Allaah katika fadhila Zake kuwa ni bora kwao (kufanya ubakhili huko) la, ni vibaya kwao. Watafunwa kongwa (madude ya kunasa shingoni) za yale waliyoyafanyia ubakhili siku ya Qiyaama. Na urithi wa mbingu na ardhi ni wa Allaah. Na Allaah Ana habari za (yote) mnayoyafanya.” Al-'Imraan: 180

 

Yaani asidhani bakhili kukusanya kwake mali kutamfaa bali itamdhuru katika dini yake na huenda ikamdhuru pia duniani.

 

Anasema Allaah:

 

“Loo nyinyi mnaitwa mtoe (mali) katika njia ya Allaah na kuna wengine katika nyie wanafanya ubahili basi afanyaye ubahili anafanya ubakhili huo kwa (kuidhuru) nafsi yake mwenyewe. Na Allaah ni Mkwasi na nyinyi ndio makafiri. Na kama mkirudi nyuma (mkaupa mgongo Uislam), Allaah Ataleta watu wengine badala yenu nao hawatakuwa kama nyinyi (watakuwa bora).” Muhammad: 38

 

Kutoka kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) amesema:

 

“Ogopeni dhulma, hakika dhulma ni viza siku ya Qiyaama, na ogopeni ubakhili kwani umewaangamiza waliokuwa kabla yenu, iliwapelekea kumwaga damu zao na kuhalalisha haramu.”

 

Kutoka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriy amesema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam):

 

“Mambo mawili hayakusanyiki kwa Muumin, ubahili na tabia mbaya.”  At-Tirmidhiy

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah amesema kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) amesema:

 

“Hakuna siku wanayopambazukiwa waja ila Malaika wawili wanashuka anasema mmoja wao, Ee Allaah mpe mtoaji badala, na anasema mwengine, Ee Allaah mpe anayezuia maangamizi.” Al-Bukhaariy

 

Share

05-Matendo Mema Na Athari Yake Katika Utajiri Na Ukunjufu Wa Rizki: Mambo Yapasayo Kuchunga Katika Kutafuta Rizki

 

D. MAMBO YAPASAYO KUCHUNGA KATIKA KUTAFUTA RIZKI

 

CHUMO HALALI

 

Anasema Allaah:

 

“Enyi mlioamini kuleni katika vizuri Tulivyowaruzuku.” Al-Baqarah: 

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah amesema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam):

 

“Enyi watu, enyi watu! Hakika Allaah ni Mzuri hakubali ila vilivyo vizuri, na hakika Allaah Amewaamrisha Waumini Aliyowaamrisha Mitume akasema, “Enyi Mitume kuleni katika vilivyo vizuri na mtende mema, hakika Mimi Najua mnayoyafanya.” Na akasema: “Enyi mlioamini kuleni katika vizuri nilivyowaruzuku.” Kisha akamtaja mtu anaenda safari ndefu nywele zina vumbi ananyanyua mikono yake mbinguni (kuomba), Ee Mola ee Mola, hali ya kuwa chakula chake ni haramu, kinywaji chake ni haramu, na mavazi yake ni haramu na amelelewa kwa haramu, vipi atajibiwa?”

 

Kutoka kwa Anas bin Maalik kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) amesema:

 

“Kutafuta halali ni wajibu kwa kila Muislam.”

 

Share

06-Matendo Mema Na Athari Yake Katika Utajiri Na Ukunjufu Wa Rizki: Faida Ya Rizki Ya Halali Katika Dunia Na Akhera

 

E. FAIDA YA RIZKI YA HALALI DUNIANI NA AKHERA

 

1. FAIDA KATIKA DUNIA

 

(A) KUJIBIWA DUA

 

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas amesema nilisoma hii aya mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam): “Enyi watu kuleni vilivyomo ardhini vilivyo halali vizuri.” akasimama Sa’ad bin Abi waqaas akasema: ewe Mtume wa Allaah niombee Allaah Anijaalie du’aa zangu zijibiwe, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) akamwambia, “Ewe Sa’ad! Kula cha halali utakuwa mwenye kujibiwa du’aa, naapa kwa yule nafsi ya Muhammad ipo mkononi mwake hakika mja ananyakua tonge la haramu kuingiza mdomoni mwake haikubaliwi matendo yake siku arobaini na mja yoyote nyama yake inaota kwa haramu basi moto ni bora kwake.”

 

 

(B) BARAKA KATIKA MALI MKE NA WATOTO

 

(C) RAHA KATIKA NAFSI

 

Anayechunga kula halali anasalimika na midomo ya watu, watakuwa wanamtaja kwa uzuri na watakuwa naye mahusiano mazuri.

 

 

FAIDA KATIKA AKHERA

 

1. KUINGIA PEPONI

 

Kutoka kwa Abu Sa’iid Al-Khudriy amesema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam):

Mwenye kula halali na akatenda katika mwenendo wa Mtume na watu wakasalimika na shari yake ataingia peponi.” At-Tirmidhiy.

 

Wakasema ewe Mtume wa Allaah hilo katika umati wako leo ni wengi. Akasema na itakuwa katika karne baada yangu.

 

 

2. KUSAMEHEWA MADHAMBI

 

 Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam):

 

“Mwenye kulala hali ya kula cha halali alichokichuma analala hali ya kuwa amesamehewa.”

 

 

3. ATAPATA UNAFUU SIKU YA QIYAAMAH (HESABU)

 

4. KUKUBALIWA SADAKA YAKE NA KULIPWA MARADUFU

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah amesema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam):

 

“Mwenye kutoa sadaka usawa wa tende katika chumo la halali na Allaah Hapokei ila vilivyo vizuri, na Allaah Anapokea kwa mkono wa kulia kisha Anamlelea mtoaji, kama mmoja wenu anavyomlea mtoto wa ngamia, mpaka iwe mfano wa jabali.” Al-Bukhaariy

 

 

5. KUJIEPUSHA NA HARAMU

 

Amekataza Allaah chumo la haramu Aliposema,

 

“Enyi mlioamini msiliane mali zenu kwa batili. isipokuwa iwe biashara kwa kuridhiana baina yenu. (hiyo inajuzu) wala msijiue wala msiue (wenzenu). Hakika Allaah ni mwenye kukuhurumieni.

Na atakayefanya haya kwa uadui na dhulma, basi huyo tutamuingiza motoni. Na hayo ni rahisi kwa Allaah.) An-Nisaa: 29-30

 

Anasema Allaah:

 

(Allaah Amehalalisha biashara na Akaiharamisha riba.” Al-Baqarah: 275

 

Amesema Ibn ‘Abbaas: “Ataambiwa mla riba siku ya Qiyaamah chukua silaha yako kwa vita na Allaah.”

 

Share

07-Matendo Mema Na Athari Yake Katika Utajiri Na Ukunjufu Wa Rizki: Madhara Ya Chumo La Haramu

 

MADHARA YA CHUMO LA HARAMU

 

(1). MOJA YA SABABU YA KUINGIA MOTONI

 

 

“Enyi mlioamini, msiliane mali zenu kwa batili, isipokuwa iwe biashara kwa kuridhiana baina yenu. Wala msijiue (wala msiue wenzenu). Hakika Allaah ni mwenye kukuhurumieni. Na Atakayefanya haya kwa uadui na dhulma, basi huyo Tutamwingiza motoni, na hayo ni rahisi kwa Allaah.” An-Nisaa: 29-30

 

 

Kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) alimwambia Ka’ab bin ‘Umar: “Ewe Ka’ab bin ‘Umar,hatoingia peponi ambaye nyama yake imeota kutokana na haramu, na moto ni bora kwake.” Musnad Ahmad

 

 

 Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas amesema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam)

 

 

           

 “Asione vizuri mwenye kukusanya mali isiyo halali yake (isiyo haki yake) akitoa sadaka haitokubaliwa na kinachobakia ni mzigo wa kwendea motoni.”

 

 

(2). HESABU NZITO SIKU YA QIYAAMAH

 

(3). KUTOJIBIWA DU’AA

 

(4). MARADHI YA NAFSI NA MWILI

 

 

3. KUTOHUSUDIANA

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah amesema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam):

 

“Angalieni aliyekuwa chini yenu wala msitazame aliye juu yenu itawapelekea msijizidishie neema ya Allaah.”

 

 

4. KUTOSHEKA

 

Anasema  Allaah:

 

“Wala usifanye mkono wako kama (uliofungwa shingoni mwako wala usiukunjuwe ovyo ovyo, utakuwa ni mwenye kulaumiwa (ukifanya hivyo) na kufilisika (ukiukunjua ovyo ovyo). Israa: 29

 

Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam):

 

“Kuleni, kunyweni, vaeni, toeni sadaka bila israfu wala kujionyesha.” Al-Bukhaariy

 

 

6. KUWA MBALI NA UFEDHULI NA DHULMA

 

Anasema Allaah:

 

“Na saidianeni katika wema na uchaji Allaah, wala msisaidiane katika dhambi na uadui.” Al-Maaidah: 2

 

Neema ya Allaah inapasa kushukuru na katika kushukuru ni kutodhulumu,na kudharau watu, kutoa katika kumtii Allaah na kujisaidia katika njia za kheri sio za dhulma na shari.

 

Anasema Allaah:

 

“Basi Hatukumtuma (Hatukumpeleka) muonyaji katika mji wowote ule ila wenyeji wake wajipatao wakisema “bila shaka sisi tunakataa haya mliyotumwa nao”

Na wakasema “sisi tunayo mali nyingi na watoto wengi wala sisi hatutaadhibiwa.” Sabaa: 34

 

Yaani walijifakharisha kwa wingi wa mali na watoto wakadhani hiyo ni dalili ya kupendwa na Allaah na Anawajali.

 

Anasema Allaah:

 

“Hakika wale waliokufuru hutoa mali zao ili (kuzuilia watu) wasipate kuamini njia ya Allaah basi watazitoa, kisha zitakuwa majuto juu yao kama kisha watashindwa. Na wale waliodumu katika ukafiri watakusanywa katika jahannam (watakaosilimu baadaye Allaah Atawasamehe.)” Al-Anfaal: 36 

 

Anasema Allaah:

 

“Na Tunapomneemesha mwanaadamu, hugeuka na kujitenga upande, (hana haja ya kutuabudu) inapomgusa shari, mara hugeuka akawa na madu’aa marefu marefu.”

Fusswilat: 51

 

Anaonya Allaah katika hizi aya na zinginezo kwa mwenye kutumia neema ya Allaah na mali katika kuwadhulumu watu, na kufanya ufisadi katika ardhi na kiburi kwamba watapata hasira ghadhabu, na adhabu ya Allaah.

 

 Na Qur-aan Tukufu na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) wanatuonyesha yaliyowapata umma zilizopita kama ‘Aad, Thamuud na yaliyowapata waovu kama Fir’awn, Abu Jahal, Qaaruun na wengineo, walipata maangamivu ili iwe ni mazingatio kwa watakaokuja baada yao, na huu ni mwendo wa Allaah katika adhabu kwa wanaokanusha na makafiri mpaka siku ya Qiyaamah.

 

 

WabiLlaahi At-Tawfiyq

 

 

Share