Kukata Undugu

  

 

KUKATA UNDUGU

 

MUONEKANO WAKE, SABABU NA NJIA ZA KUTIBU

 

قطيعة الرحم, المظاهر, الأسباب,  سبل العلاج

 

تأليف محمد بن ابراهيم الحمد

 

Mfasiri:  Haliymah ‘Abdullaah Husayn

 

Share

00-Kukata Undugu: Faharasa

 

FAHARASA

 

01. Utangulizi

02. Madh-har ya kukata undugu

03. Sababu za kukata undugu

   - Ujinga

   - Udhaifu wa Uchamungu

   - Kibri

   - Kupotea muda mrefu

   - Kulaumu sana

   - Kujikalifisha

   - Kutowajali wanaokuzuru

   - Ubakhili

   - Kuchelewa kugawa mirathi

   - Ushirika baina ya wanandugu

  - Kujishughulisha na dunia

  - Talaka baina ya Ndugu

  - Kuwa mbali na uvivu katika ziara

  - Kuwa karibu katika makazi

  - Kutokuwa na subra kwa Ndugu

  - Kuwasahau baadhi ya Ndugu katika mialiko

  - Hasadi na chuki

  - Mizaha mingi

  - Umbeya na uchonganishi

  - Tabia mbaya ya baadhi ya wake

04. Tiba ya ukataji undugu

  - Ni nini kuunga undugu?

  - Kwa kitu gani unaunga undugu?

05. Fadhila za kuunga undugu

06. Vitu vinavosaidia kuunga undugu

 

Share

01-Kukata Undugu: Utangulizi

 

 

Utangulizi

 

 

Shukrani zote njema ni za Allaah rehema na amani zimuendee Mtume wa Allaah na watu wake, Maswahaba na waliomfuata, ama baada:

 

Kukata undugu ni dhambi kubwa na kosa kubwa inafungua mafungamano inakata vizuizi inaeneza uadui na chuki inahalalisha kukatana na kuhamana.

 

Kukata undugu kunaondosha mazoea na mapenzi kunaidhinisha laana na kuharakisha adhabu, kunazuia kushuka rehma na kuingia peponi, na kunakufanya uwe mpweke na dhalili, pia inakuvutia huzuni zaidi, ikikutokea balaa unategemea kwa nani kheri na wema inakuzidishia zaidi maumivu.

 

Dhambi hii Amekemea Allaah katika Kitabu Chake:

 

“Basi yanayotarajiwa kwenu mkitawala ndio mfisidi katika nchi na mwatupe jamaa zenu?

 

“Hao ndio Mwenyezi Mungu Aliowalaani, na Akawatia uziwi, na Akawapofoa macho yao.”   Muhammad: 22-23

 

Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):

 

“Haingii peponi mkata undugu.”   

 

Share

02-Kukata Undugu: Madh-har Ya Kukata Undugu

 

 

MADH-HAR YA KUKATA UNDUGU

 

Kukata undugu ni katika mambo yaliyoenea katika jamii ya Waislam, na haswa haswa katika wakati huu uliotawaliwa na mada (kupenda mali) kumepungua kutembeleana na kuungana watu wengi wamepoteza haki hii na kupituka, Allaah ndiye mwenye kutegemewa.

 

Kukata undugu kunaonekana kwa njia nyingi watu wengine hawawajui ndugu zao wa karibu kwa kuwaunga kwa mali au vyeo au tabia inapita miezi na huenda miaka hajawatembelea wala kuwafanyia wema, kuzidisha mapenzi, au kupeana zawadi au kuwazuilia dhara au maudhi, huenda yeye mwenyewe akawaudhi kwa maneno au matendo au vyote.

 

Na kuna watu hawashirikiani na ndugu zao katika furaha wala kuwaliwaza wala kuwapa sadaka maskini wao bali utamkuta anawatanguliza wengine katika kuwaunga.

 

Na katika watu wanawaunga ndugu zao pindi wakiwaunga na anawakata wakimkata huu si uungaji bali ni kulipa mema kwa mfano wake na hili linatokea kwa ndugu wa karibu na wengineo kulipa mema sio kwa ndugu peke yao.

 

Na muunga undugu wa kweli ni yule aungae nduguze kwa ajili ya Allaah, wakimuunga au wasimuunge.

 

Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):            

 

(Sio muungaji kwa kutoa lakini muungaji ni yule ambaye ukikatwa undugu wake anauunga) Al-Bukhaariy

 

Na katika ukataji undugu unawakuta baadhi ya watu ambao Allaah Amewapa elimu na kulingania wa mbali na anaghafilika na kuwalingania watu wake (nduguze) na hili halitakikani; watu wa karibu ni bora kwa kuwaamrisha  mema.

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kumwambia Nabii wake Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):

 

“ Na uwaonye jamaa zako walio karibu nawe.” Ash-Shua’raa: 214

 

Na katika madh-har ya ukataji undugu unakuta baadhi ya familia kubwa anatokea mwenye elimu au mtu mwema au mlinganiaji unamuona anakubalika zaidi na kuheshimika na watu wengine wala hapati katika familia yake ila kukanushwa na kupingwa jambo ambalo linamshushia utukufu wake kumdhoofisha nguvu zake na kupunguza athari yake.

 

 Na katika madh-har ya kukata undugu kuwagawanya ndugu na kuvunja nguvu zao.

 

Share

03-Kukata Undugu: Sababu Za Kukata Undugu

 

SABABU ZA KUKATA UNDUGU

 

 

1. UJINGA

 

Ujinga unapelekea kukata undugu.

 

 

2. UDHAIFU KATIKA UCHA MUNGU (TAQWA)

 

Itakapodhoofika Ucha Mungu hajali mtu kukata Aliyoamrisha Allaah kuunga wala hatamani ujira wa uungaji na hajali matokeo ya ukataji.

 

 

3. KIBRI

 

Baadhi ya watu wakipata cheo cha juu au akapata nafasi nzuri au akawa mfanyibiashara mkubwa anafanya kibri kwa ndugu wa karibu; anaacha kuwatembelea na kuwapenda anaona yeye ndiye mwenye haki na yeye ni bora kutembelewa na kuijiwa.

 

 

4. KUPOTEA KWA MUDA MREFU

 

Kuna baadhi ya watu wanawapotea ndugu zao muda mrefu anaanza kusema nitawazuru mpaka anazoea kuwa mbali nao na anawakata.

 

 

5. KULAUMU SANA

 

Baadhi ya watu anapofanyiwa ziara na mmoja wa ndugu baada ya kupoteana muda mrefu, anamshushia mvua ya lawama na amepuuza katika haki yake na anafanya taratibu katika kumzuru hili linapelekea ndugu kuogopa kumzuru kwani atalaumiwa.

 

 

6. KUJIKALIFISHA ZAIDI

 

Mwingine anapozuriwa na ndugu anajilazimisha kuliko inavyohitajika na anajitia hasara kwa mali nyingi anajiandaa kumkirimu na anaweza kuwa hali yake ni duni. Hivyo ndugu anapunguza ziara anaogopa kumtia nduguye katika matatizo.

 

 

7. KUTOWAJALI WANAOKUZURU

 

Miongoni mwa watu, anapotembelewa na ndugu hajali wanapozungumza, hawasikilizi katika mazungumzo yao, wala hafurahii kuja kwao, wala hawashukuru kwa kuja kwao, hawapokei kwa furaha, anajivuta jambo linalopelekea ndugu kutomtembelea.

 

 

8. UCHOYO NA UBAHILI

 

Baadhi ya watu Allaah Anapowaruzuku mali au cheo anawakimbia ndugu, sio kwa kibri, ila anaogopa kufungua mlango na nduguze wataanza kumtembelea na kutaka msaada au linginelo.

 

Badala awafungulie mlango awakaribishe na awahudumie kwa analoweza au kuomba samahani kwa asiloliweza, bali anawaepuka anawahama ili wasimsumbue kwa kutaka misaada mingi kama anavyodai.

 

Ni nini faida ya mali au cheo akiwanyima nduguze?

 

Amesema Zuhayr bin Abi Sulma:

 

ومن يك ذا فضل فيبخل بفضله

علي قومه يستغن عنه ويذ مم

 

“Mwenye kuwa na uwezo akafanya ubahili kwa watu wake, akafaidika nao mwenyewe na kulaumiwa.”

 

 

Na uzuri ulioje wa aliyoyasema Al-Baaruudiy:

 

فلا تحسبن المال ينفع

اذا هو لم تحمد قراه العشائر

 

“Usihesabie (usidhani) mali inanufaisha, ikiwa yeye hatosifiwa na wa karibu”

    

Na katika yaliyosemwa:

 

ومن ذا الذي ترجو الأباعد نفعه

اذا كان لم يصلح عليه الأقارب

 

“Ni kitu gani tunachosubiria wa mbali kutunufaisha, ikiwa ndugu wa karibu hawawezi kutunufaisha?”

 

 

9. KUCHELEWESHA KUGAWA MIRATHI

 

Inaweza kuwa baina ya ndugu Mirathi haijagaiwa ama kwa uvivu wao au baadhi wana makusudi ya kuchelewesha au mfano wake.

 

Kila unapochelewa ugawaji wa Mirathi na muda kupita, kunaenea uadui na bughdha baina ya ndugu huyu anataka haki yake katika Mirathi atajirike, mwengine anakufa, na wanapata tabu walio baada yake kukusanya wakala wapate fungu lao, mwengine anamdhania mwenzie vibaya, yanazidi matatizo na inaenea kuhamana.

 

 

10. USHIRIKA BAINA YA NDUGU

 

Mara nyingi ndugu wanashirikiana katika mradi au shirika fulani bila kuafikiana katika misingi madhubuti na bila ya kusimamia Ushirika kwa uwazi, bali kwa kuridhishana ya uongo na kutodhaniana vizuri.

 

Uzalishaji utakapoongezeka na kutanuka mzunguko wa kazi, kunazuka hitilafu na ubaya pia dhana mbaya, na haswa ikiwa wana uchache wa Ucha Mungu na kujitolea au ikiwa baadhi yao wanang’ang’ania rai zao au upande mmoja ukawa unashughulika zaidi.

 

Na hapa uhusiano unakuwa mbaya na kufarakana na inaweza kufikia kushtakiana mahakamani.

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

 

“ … Na hakika washirika wengi hudhulumiana wao kwa wao, isipokuwa walioamini na wakatenda mema. Na hao ni wachache…” Swaad: 24.

 

 

11. KUSHUGHULIKA NA DUNIA

 

 

12. TALAKA BAINA YA NDUGU

 

Inaweza kutokea talaka baina ya ndugu, yanazidi matatizo baina ya ndugu zao ama kwa sababu zinazohusiana na talaka au mengineo.

 

 

13. UMBALI WA MASAFA NA KUFANYA UVIVU KATIKA ZIARA

 

 

14. KUWA KARIBU KATIKA MAKAZI BAINA YA NDUGU

 

Huenda hili likasababisha kukatana. Imepokelewa kutoka kwa ‘Umar bin Al-Khattwwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

 

“Waamrisheni wenye undugu watembeleane wala wasiwe majirani.”

 

Ameongezea Ghazaali kutokana na maneno ya ‘Umar “amesema hivyo kwani ukaribu unaleta msongamano katika haki na huenda likarithisha chuki na kukatana.”

 

Amesema Aktham bin Asw-Swayfi:

 

“Kuweni mbali katika majumba  kuweni karibu katika mapenzi.”

 

Kisha kuwa karibu katika masafa kunaweza kusababisha matatizo, na yanatokea matatizo kwa sababu inaweza kuwa baina ya watoto mashindano na yanaweza kuhama hadi kwa wazazi, kila mzazi anajitahidi kumtetea mwanae na kunaanza uadui na mwisho kutengana.

 

 

15. UCHACHE WA KUWASTAHAMILIA NDUGU NA KUWASUBIRIA

 

Baadhi ya watu hawawezi kustahamili kitu kidogo kutoka kwa ndugu kosa dogo tu au kulaumiwa na mmoja wa ndugu anafanya haraka kukatana na kuhamana.

 

 

16. KUWASAHAU NDUGU KATIKA SHUGHULI NA HARUSI

 

Inaweza kuwa kwa mmoja wa wanafamilia ana harusi au sherehe fulani, anawaalika ndugu kwa mdomo au kadi au kwa simu, huenda akamsahau mmoja katika ndugu au huenda aliyesahauliwa ni dhaifu wa nafsi au ana tabia ya dhana mbaya; anafasiri kusahaulika kwamba wamempuza na kumdharau anaamua kwa dhana hiyo kuwahama.

 

 

17. HASADI

 

Kuna aliyeruzukiwa elimu au cheo au mali au kupendwa, na wengine unakuta anawahudumia ndugu zake anawafungulia moyo wake mwema, kwa hilo huenda baadhi ya ndugu wakawa wanamhusudu na wanamsababishia uadui na kutia shaka katika uaminifu wake.

 

 

18. MIZAHA MINGI

 

Mizaha mingi ina athari mbaya,huenda ikatoka neno la kujeruhi kwa mtu, hachungi hisia za wengine, ikampata mtu anayeathirika haraka, ikazaa chuki bughdha kwa muongeaji.

Na hili linatokea sana baina ya ndugu kwa kukutana kwao sana.

 

Amesema Ibn ‘Abdil-Bariy:

 

“Kundi la Ulamaa limechukia kuzama katika mizaha, kutokana na mwisho mbaya…”

 

 

19. UCHONGANISHI

 

Katika watu kuna ambaye katika tabia yake Allaah Atuepushe anaharibu uhusiano ulio baina ya wapendanao, unamkuta anapupia baina ya wapendanao kuwatenganisha na kuchafua usafi wao, ni ndugu wangapi wametengana kutokana na mchonganishi, mmbeya.

 

Anasema Al-‘Aashiy:

 

“Mwenye kumtii mchonganishi hatomuachia rafiki hata kama alikuwa ni kipenzi aliye karibu.”

 

 

20. TABIA MBAYA KATIKA BAADHI YA WAKE

 

Baadhi ya watu wanaweza kuwa na mtihani na mke mwenye tabia mbaya hawezi kumstahamilia yeyote, hataki ndugu au yeyote washirikiane naye kwa mumewe, anamzuia akitaka kuwakaribisha, na wanapomzuru ndugu wa mume haonyeshi furaha, hili linasababisha ndugu kukatana.

 

Baadhi ya waume wanampa uongozi mke akiwaridhia ndugu zake anawaunga na ndugu asiowataka mke anawakata na huenda akamtii katika kuwakata wazazi.

 

Share

04-Kukata Undugu: Tiba Ya Kukata Undugu

 

TIBA YA KUKATA UNDUGU

 

Tumeona kukata undugu na madhara yake na baadhi ya sababu zinazopelekea hilo.

Ikiwa mambo ni hivyo, hapana budi kwa mwenye akili atahadhari na kukata undugu, na ajiepushe na sababu zinazopelekea hilo na ajue ukubwa wa undugu apupie sababu za kuunga achunge adabu zinazopasa kuchunga pamoja na Ndugu.

 

Ni nini kuunga undugu?

 

Na kwa vitu gani inakuwa?

 

Na ni nini fadhila zake?

 

Na ni njia zipi na sababu zinazosaidia hilo?

 

Na ni adabu zipi zinapasa kuzichunga pamoja na Ndugu wa karibu?

 

 

NI NINI KUUNGA UNDUGU?

 

Kuunga undugu ni kinyume cha kuhamana.

 

Kuunga undugu ni kuwafanyia wema ndugu wa karibu kwa nasaba au kwa ukwe kuwafanyia huruma upole na kuchunga hali zao hata wakiwa mbali na wakafanya vibaya au wakakukata.

 

 

NI KWA LIPI INAKUWA KUUNGA UNDUGU?

 

Kuunga undugu kwa mambo mengi inakuwa kwa kuwatembelea kuwajulia hali kuwaulizia kuwapa zawadi na kuwaweka kuendana na daraja zao na kuwapa sadaka mafakiri wao kuwafanyia upole matajiri wao kuwaheshimu wakubwa kuwaonea huruma wadogo na madhaifu pia kuwasiliana nao kwa barua simu kuwafanyia ziara kuwakaribisha kuwapokea vizuri kuwatukuza kuwanyanyua katika mambo yao na kumuunga anayekukata.

 

Inakuwa pia kushirikiana nao katika furaha kuwaliwaza katika matatizo kuwaombea dua kuwasafishia vifua kuwapatanisha waliogombana kuwa na pupa ya kuthibitisha mahusiano kuwatembelea wagonjwa wao kuwaitikia wito.

 

Na kubwa katika kuunga undugu, apupie mtu kuwalingania katika uongofu kuwaamrisha mema kuwakataza maovu.

 

Na undugu huu utaendelea ukiwa mwema wenye kutengamaa.

 

Ama ikiwa ndugu kafiri au muovu inakuwa kumuunga kwa kuwapa mawaidha na kuwakumbusha na kujitolea kwa juhudi katika hilo.

 

Ukiona wanakupinga au kukufanyia makusudi au ukijiogopea kupotea nao basi wahame vizuri bila kuwafanyia maudhi na uzidishe kuwaombea du’aa huenda Allaah Akawaongoza kwa baraka ya du’aa zako. Na ukipata fursa ya kuwalingania mara kwa mara itumie.

 

Na inapendezeshwa katika kuwalingania ndugu na kuwapa nasaha ufanye wema katika kuamiliana nao utumie upole hikma na mawaidha mazuri wala usiingie nao katika mjadala ila kwa uchache na kwa wema kwani walinganiaji wengi athari yao katika familia na kabila ni ndogo. Na hili linatokea kwa walinganiaji hawafanyi upande huu kuwa ni muhimu kuwalingania ndugu wangetafuta njia wangefaulu na kuwaathiri, mfano kuwanyenyekea, kuwajali, kuwaunga, kujipendezesha kwao.

 

Na ni juu ya familia au kabila wawaheshimu wenye elimu katika familia kuwasikiliza na kutowadharau.

 

Ikitokea hili katika familia watakuwa huru katika kupanda kufikia ukamilifu na fadhila.

 

Share

05-Kukata Undugu: Fadhila Za Kuunga Undugu

 

FADHILA ZA KUUNGA UNDUGU

 

1. Kuunga undugu ni alama ya kumuamini Allaah na siku ya mwisho:

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):

“Mwenye kumuamini Allaah na siku ya mwisho amkirimu mgeni wake, na mwenye kumuamini Allaah na siku ya mwisho aunge undugu wake.” Al-Bukhaariy.   

 

 

2. Ni sababu ya kuzidi umri na kukunjuliwa rizki.

 

Kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):

“Mwenye kupenda kutanuliwa rizki yake, na azidishiwe baraka katika umri wake aunge undugu wake.” Al-Bukhaariy

 

Na kuongezewa umri ni kubarikiwa kupewa nguvu katika mwili akili kuwa salama na maisha mazuri (chakula bora, hewa safi)

 

3. Mwenye kuunga undugu anakuwa karibu na Allaah

 

Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):

“Hakika Allaah Ameumba viumbe mpaka Alipomaliza ulisimama undugu, ikasema; huyu amesimama anajikinga Kwako na anayemkata, Akasema ndio hivi huridhii Nikimuunga anayekuunga na Ninamkata anayekukata? Akasema sawa. Akasema hilo lako (umekubaliwa ombi lako).” Al-Bukhaariy.

 

4. Kuunga undugu ni sababu kubwa ya kuingia peponi

 

 Kutoka kwa Abu Ayuub al- Answaariy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba mtu alisema;

“Ewe Mtume wa Allaah, nifahamishe tendo litakaloniingiza peponi na litakaloniepusha na moto.” Akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam): “Umuabudu Allaah wala Usimshirikishe na chochote, usimamishe Swalaah utoe Zakaah na uunge undugu” Al-Bukhaariy.

 

5. Kuunga undugu ni katika kumtii Allaah, kwani unafuata uloamrishwa.

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

 

 “Na wale ambao huyaunga Aliyoamrisha Mwenyezi Mungu yaungwe, na wanaikhofu hisabu mbaya.” Ar-Raa’d: 21

 

6. Nayo ni katika mazuri ya dini, Uislam ni dini ya kuunganisha dini ya wema huruma inaamrisha undugu na inakataza kukatana.

 

Inapelekea makundi ya Waislam wenye kushikamana kuzoeana kuoneana huruma kinyume na vikundi vingine visivyochunga haki hii wala kutilia umuhimu.

 

7. Sheria zote za dini za mbinguni zimeafikiana kuhusu kuunga undugu na kuhadharisha ukataji wake. Na hili linaonesha umuhimu wake.

 

8. Kuunga undugu kunapelekea kutajwa vizuri na kusifiwa hata watu wa enzi ya ujahilia (ujinga) walikuwa wanawasifia waunga undugu.

 

9. Kunapelekea wema na ni dalili ya uzuri wa nafsi na ukweli katika kuishi na watu. Palisemwa asiyewafaa ndugu zake hawezi kukufaa…

 

10. Inaeneza upendo baina ya ndugu.

 

Kwasababu inaenea mapenzi na mazoea mazuri, ndugu wanakuwa kitu kimoja, hivyo maisha yao yanakuwa safi na furaha inazidi.

 

11. Kunyanyuliwa muunga undugu.

 

Mwanadamu akiwaunga Ndugu zake,na akachunga katika kuwatukuza, watamkirimu, watamheshimu, watakuwa ni wenye kumsaidia.

 

12. Kuwa na cheo wenye kuungana.

 

Ndugu wenye kuungana kupendana wataheshimika kila mtu ataogopa kuwafanyia ubaya kinyume na hivyo wakikatana kufanyiana vitimbwi watadharaulika watadhalilika baada ya utukufu na kuwa juu. 

Share

06-Kukata Undugu: Vitu Vinavyosaidia Kuunga Undugu

 

VITU VINAVYOSAIDIA KUUNGA UNDUGU

 

Kuna adabu ziinazopasa kufuatwa pamoja na ndugu

 

1. Kufikiria athari zinazoendana na undugu na mwisho mzuri ni kitu kikubwa inapasa tufuatilie.

 

2. Kutazama mwisho mbaya wa ukataji undugu na hilo ni kufikiria yatakayoletwa na ukataji undugu ikiwa ni pamoja na matatizo, majuto, hasara, n.k. Ukifikiria hayo, itakusaidia uepuke kukata undugu.

 

3. Kutaka msaada kwa Allaah Kwa kumuomba Akuwezeshe katika kuunga undugu.

 

4. Kubadilisha mabaya ya ndugu kwa ihsaan. Hili linabakisha mapenzi na linahifadhi yaliyo baina ya ndugu katika makubaliano. Na linakupunguzia mwanaadamu unayopata katika ubaya wa ndugu.

 

Na kwa hilo, alikuja mtu kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema: “Ewe Mtume wa Allaah, mimi nina ndugu nawaunga wananikata, nawafanyia wema na wao wananifanyia maovu, nawa mpole kwao wananifanya mjinga. Akasema “ikiwa uko kama unavyosema kanakwamba unawalisha majivu ya moto, na hutoacha kuwa unaungwa mkono na Allaah, ukidumu kwa hilo.

 

5. Kukubali udhuru wao wakikosea au kuomba msamaha.

 

Na uzuri unaotajwa katika hilo ni yaliyomfika Nabii Yuusuf na nduguze. Baada ya yote waliyomfanyia alikubali walipoomba msamaha na akawaombea Allaah Awasamehe wala hakuwagombeza kwa makosa yao.

 

6. Kuwasamehe na kusahau aibu zao hata kama hawajaomba msamaha na hilo linaonesha ukarimu wa nafsi.

 

7. Unyenyekevu na tabia laini

 

 Hilo linapelekea ndugu kumpenda mtu na kuwa karibu naye.

 

8. Kufungua macho na kutoshughulika na mambo mengine au makosa madogo sio kila uonalo unatoa kasoro, itakufanya ugombane kila mara.

 

9. Kujitolea kadri ya uwezo wako ikiwa ni cheo nafsi au mali.

 

10. Kutotaka wakusifie au wakulipe mfano wa uliyowafanyia

 

11. Kutuliza nafsi na kuridhika na kidogo kutoka kwa ndugu.

 

12. Kuchunga hali zao na kujua hisia zao na kuwaweka kuendana na daraja zao. Wako miongoni mwa ndugu mwenye kuridhia kitu kidogo, inamtosha ukimtembelea mara moja kwa mwaka, au inamtosha ukiongea naye kwa simu, mwengine inamtosha kwa ukunjufu wa uso na kuongea naye, mwengine haridhiki mpaka umzuru (umtembelee) mara kwa mara. Hivyo ishi na mtu jinsi alivyo ili ubakishe upendo.

 

13. Kuacha kuwabebesha ndugu wasiyoyaweza na kuwaondolea mazito.

 

14. Kujiepusha kulaumu sana.

 

Mpaka wazoee ndugu kumijia na kufurahi nae, mkarimu ni yule anayewapa watu haki zake na ananyamazia haki zake asipotekelezewa. Hata kukiwa na kosa inayohitaji kukemewa basi iwe kwa upole.

 

15. Kuvumilia lawama za ndugu na kuwabeba vizuri.

 

Mwenye akili na malezi mazuri anapolaumiwa na mmoja katika ndugu anachukulia vizuri na anaona anampenda, hivyo anamtaka msamaha kupunguza hasira zake na inaonesha anataka amtembelee ndio maana analaumu.

 

16. Kuwa kati na kati katika mizaha na ndugu kuchunga hali zao na kujiepusha kuwatania wasiopenda hilo.

 

17. Kujiepusha na ugomvi na majadiliano mengi haya yote inarithisha bughdha, ubinafsi na inachafua mahusiano.

 

18. Kuharakisha kuwapa zawadi ikitokea migongano na ndugu. Zawadi zinaleta upendo na kuepusha dhana mbaya.

 

19. Aweke akilini mwanaadamu kwamba ndugu ni pande la nyama kutoka kwake kwa hiyo hana budi kuwa nao wala hawezi kujivua wakitukuka wao ndio kutukuka kwake wakidhalilika ndio kudhalilika kwake.

 

20. Ajue kuwa kuwafanyia uadui ndugu ni shari na balaa mwenye kufaidika kwa hili ni mwenye hasara na mwenye kushinda ni mwenye kushindwa.

 

21. Kuchunga katika kuwakumbuka ndugu katika sherehe na matukio mbalimbali. inatakiwa mtu aandike majina na namba za simu za ndugu na azihifadhi ili iwe rahisi kuwakumbuka anapowahitaji. Na anapomsahau mmoja wao amwendee amwombe msamaha na amridhishe kadri ya uwezo wake.

 

22. Kupupia kupatanisha.

 

Inapasa aliyepata bahati ya kupendwa katika familia arekebishe panapotokea matatizo kwani mzozo usiposuluhishwa moto wake utawaenea wote.

 

23. Kuharakisha kugawa mirathi.

 

Ili kila mmoja achukue fungu lake na kusienee ugomvi na madai na kuwe na mafungamano baina ya ndugu.

 

24. Kupupia uhusiano mzuri na maafikiano katika ushirika.

 

Wakiingia ndugu katika kushirikiana kila mmoja achunge waelewane katika mambo yao na yawe na kujitolea na upendo kushauriana na kuhurumiana ukweli na amana na kila mmoja ampendelee mwenzie analopendelea nafsi yake na kila mtu ajue wajibu wake na wa mwenzie.

Kama inavyopendezwa wajadiliane matatizo kwa uwazi wapupie kufikia muafaka na ikhlaas katika kazi na kusamehe vitu vidogo, pia waandike maafikiano yao.

 

25. Mikutano ya mara kwa mara.

 

Iwe kila mwezi au mwaka kukutana huku kuna kheri nyingi watu wanajuana, wanaungana, wanapeana naswaha na haswa haswa wasimamizi wakiwa ni wenye elimu.

 

26. Sanduku la wanandugu.

 

Ambalo hukusanywa michango ya ndugu yenye wasimamizi katika familia ili atakapohitaji mmoja katika wanafamilia mali kwa ajili ya ndoa au lingine wanafanya haraka kujua hali yake na kumsaidia; hili linazalisha mapenzi na kuikuza.

 

27. Kielekezo cha ndugu.

 

Inapendeza baadhi ya ndugu waweke kielekezo maalum ndani yake kuna namba za ndugu za simu kisha ichapishwe na kugawanyiwa ndugu wote, hili linasaidia kuwaunganisha na inamkumbusha mtu ndugu zake akitaka kuwasalimia au kuwaita katika mjumuiko na harusi.

 

28. Tahadhari na kuwatia uzito ndugu.

 

Na hilo ni kuwa mbali na kila sababu inayopelekea hilo, unajiepusha na kuwatia uzito wasiokuwa na uwezo na usiwalaumu kwa wasiyoyaweza.

 

29. Mashauriano baina ya ndugu

 

Inapendekezwa kwa ndugu kuwa na kikao cha majadiliano au kuwa na viongozi watakaowaendea wakati wa tatizo ili wapate wazo moja na linalomridhisha Allaah, inatakiwa viongozi hao wawe wapole wenye uoni na rai nzuri.

 

30. Mwisho ichungwe katika hilo, uwe undugu unawakaribisha kwa Allaah kwa ikhlaas bila kumshirikisha na kuwe kusaidiana katika wema na Uchamungu. Isikusudiwe ujinga wa kijahilia.

 

Mwisho tunamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na kumtakia rehma na amani Mtume wetu.

 

Pia nachukua fursa hii kuwashukuru wote waliosaidia katika kupitia.

 

 

Ndugu msomaji unaruhusiwa kutuma maoni na kurekebisha panapostahili Ukamilifu ni  wa Allaah pekee, na kama tunavyofahamu upana wa Lugha ya Kiarabu na ufinyu wa Lugha ya kiswahili.

 

Share