Jihaad

 

 
Jihaad
 
 
Imeandikwa Na: Muhammad Faraj Saalim As-Sa’y
 
1430H/2009M

 

Share

01-Jihaad: Maana Ya Jihaad Na Kuwekewa Shari'ah

 

Maana ya neno Jihaad

 

Neno Jihaad, asili yake linatokana na juhudi, tabu, mashaka. Kwa mfano tunasema; ‘Amejitahidi’, ‘amefanya juhudi’, yaani amezitumia nguvu zake na uwezo wake wote katika kutimiza jambo fulani, na haya yote yanapatikana katika mapambano ya kivita.

 

 

Sheria ya Jihaad

 

Allaah Alimtuma Mtume wake (Swalla AAllaahu ‘alayhi wa sallam) kwa watu wote, akamuamrisha kuwalingania katika uongofu na katika dini ya haki, na wakati wote alipokuwa Makkah alikuwa akiwalingania watu kwa hekima na kwa mawaidha mema, na kwa ajili hiyo ilibidi apambane na kila aina ya uadui, udhia na mateso kutoka kwa watu wa kabila lake baada ya kuuona utukufu na uluwa wao umo hatarini.

 

Wakati wote huo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alimtaka awe akipambana na uadui huo kwa subira, uvumilivu na kwa kusamehe msamaha mzuri.

 

Allaah Anasema:

 

فَاصْفَحِ الصَّفْحَ الْجَمِيلَ

 

“Basi msamehe msamaha mzuri (kila anayekufanyia ubaya).”

Al Hijr – 85

 

Na Akasema:

وَاصْبِرْ لِحُكْمِ رَبِّكَ فَإِنَّكَ بِأَعْيُنِنَا

“Na ungoje hukumu ya Mola wako, na hakika wewe uko mbele ya macho Yetu.”

At-Twuur: 48

 

Na Akasema:

فَاصْفَحْ عَنْهُمْ وَقُلْ سَلامٌ

“Basi wasamehe wewe na uwambie (maneno ya) salama.”

Az-Zukhruf: 89

 

Na Akasema:

قُل لِّلَّذِينَ آمَنُوا يَغْفِرُوا لِلَّذِينَ لا يَرْجُون أَيَّامَ اللَّهِ

“Waambie wale walioamini wawasamehe wale wasioziogopa siku za Allaah (za kuwatia adabu wabaya).”

Al-Jaathiyah: 14

 

Allaah Hakumtaka Mtume wake (Swalla AAllaahu ‘alayhi wa sallam) aukabili ubaya wao kwa ubaya, wala udhia kwa udhia na wala Hakumuamrisha kuwapiga vita wanaoipiga vita da’wah hiyo, au kuwapiga vita wale wanaowatesa Waislamu, bali alikuwa Akimwambia Mtume Wake (Swalla AAllaahu ‘alayhi wa sallam):

 

ادْفَعْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ السَّيِّئَةَ نَحْنُ أَعْلَمُ بِمَا يَصِفُونَ

“Ondosha mabaya (unayofanyiwa) kwa (kulipa) mema; Sisi tunajua wanayoyasema.”

Al-Muminuun: 96

 

Muda wote huo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alimuamrisha Mtume wake (Swalla AAllaahu ‘alayhi wa sallam) apigane Jihaad kwa Qur-aan na kwa hoja zilizo wazi.

 

Allaah Anasema:

وَجَاهِدْهُم بِهِ جِهَادًا كَبِيرًا

“Na ushindane nao kwa (Qurani) hii mashindano makubwa.”

Al-Furqaan: 52

 

Lakini baada ya kupita miaka kumi na tatu huku mateso yakiongezeka, na makafiri kuzidisha uonevu na kuwadhalilisha Waislamu, na hatimaye kufanya njama za kumuua Mtume wa Allaah (Swalla AAllaahu ‘alayhi wa sallam) hata akalazimika kuhamia Madiynah na kuwaamrisha Masahaba wake (Radhiya AAllaahu anhu) pia kuhamia huko, hapo ndipo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alipoteremsha kauli Yake isemayo:

 

وَإِذْ يَمْكُرُ بِكَ الَّذِينَ كَفَرُواْ لِيُثْبِتُوكَ أَوْ يَقْتُلُوكَ أَوْ يُخْرِجُوكَ وَيَمْكُرُونَ وَيَمْكُرُ اللّهُ وَاللّهُ خَيْرُ الْمَاكِرِينَ

“Na (kumbuka ewe Muhammad) walipokufanyia hila wale waliokufuru ili wakufunge au wakuue au wakutoe, na wakafanya hila (zao barabara) Na Allaah akazipindua hila hizo. Na Allaah ni mbora wa kupindua hila (za watu wabaya).”

Al-Anfaal: 30

 

Kisha Akasema:

 

إِلاَّ تَنصُرُوهُ فَقَدْ نَصَرَهُ اللّهُ

“Kama hamtomnusuru (Mtume wa Allaah (Swalla AAllaahu ‘alayhi wa sallam), basi Allaah Alimnusuru.”

At-Tawbah: 40

 

Baada ya kuhamia Madiynah, makao makuu ya dola mpya ya Kiislamu, na baada ya makafiri kuwaendea huko huko na kuwafanyia mbinu na hila mbali mbali, ndipo Allaah Alipotoa amri ya kupigana Aliposema:

 

أُذِنَ لِلَّذِينَ يُقَاتَلُونَ بِأَنَّهُمْ ظُلِمُوا وَإِنَّ اللَّهَ عَلَى نَصْرِهِمْ لَقَدِيرٌ 39 الَّذِينَ أُخْرِجُوا مِن دِيَارِهِمْ بِغَيْرِ حَقٍّ الا أَن يَقُولُوا رَبُّنَا اللَّهُ وَلَوْلا دَفْعُ اللَّهِ النَّاسَ بَعْضَهُم بِبَعْضٍ لَّهُدِّمَتْ صَوَامِعُ وَبِيَعٌ وَصَلَوَاتٌ وَمَسَاجِدُ يُذْكَرُ فِيهَا اسْمُ اللَّهِ كَثِيرًا وَلَيَنصُرَنَّ اللَّهُ مَن يَنصُرُهُ إِنَّ اللَّهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ 40 الَّذِينَ إِن مَّكَّنَّاهُمْ فِي الأَرْضِ أَقَامُوا الصَّلاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ وَأَمَرُوا بِالْمَعْرُوفِ وَنَهَوْا عَنِ الْمُنكَرِ وَلِلَّهِ عَاقِبَةُ الْأُمُورِ 41

“Wameruhusiwa (kupigana) wale wanaopigwa, kwa sababu wamedhulumiwa. Na kwa yakini Allaah ni Muweza wa kuwasaidia.

Ambao wametolewa majumbani (mijini) mwao pasipo haki ila kwa sababu wanasema “Mola wetu ni Allaah.”

Na kama Allaah Asingaliwakinga watu, baadhi yao kwa wengine, bila shaka yangalivunjwa mahekalu na makanisa na nyumba nyengine za ibada na Misikiti ambamo jina la Allaah hutajwa kwa wingi. Na bila shaka Allaah Humsaidia yule anayesaidia dini yake. Hakika Allaah ni Mwenye nguvu na Mwenye kushinda.

Wale ambao tukiwamakinisha (tukiwaweka uzuri) katika ardhi husimamisha Swalah na wakatoa Zakaah na wakaamrisha yaliyo mema na wakakataza yaliyo mabaya. Na marejeo ya mambo ni kwa Allaah.”

Al-Hajj: 39-41

 

Katika aya hizi zimetajwa sababu tatu ambazo kwa ajili yake Allaah Ametoa ruhusa ya kupigana vita:

 

Ya kwanza - Kwa sababu ya kudhulumiwa kwa kushambuliwa na kutolewa majumbani mwao pasipo haki kwa sababu wanasema “Mola wetu ni Allaah”.

 

Ya pili – Lau kama Allaah Asingaliwakinga kwa kuwaamrisha kupigana Jihaad, bila shaka yangalivunjwa mahekalu na makanisa na nyumba nyengine za ibada na Misikiti ambamo ndani yake jina la Allaah hutajwa kwa wingi.

 

Ya tatu – Sababu ya Waislamu kupewa nusura ya Allaah na kumakinishwa (kuwekwa uzuri) katika ardhi ni kwa ajili ya Kusimamisha Swalah na Kutoa Zakaah na Kuamrisha mema na Kukataza mabaya.

 

 

 

 

Share

02-Jihaad: Ni Waajib

Jihaad Ni Waajib

 

Jihaad imefaridhishwa katika mwaka wa pili wa Hijra aliposema Allaah:

 

كُتِبَ عَلَيْكُمُ الْقِتَالُ وَهُوَ كُرْهٌ لَّكُمْ وَعَسَى أَن تَكْرَهُواْ شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ وَعَسَى أَن تُحِبُّواْ شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ وَاللّهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لاَ تَعْلَمُونَ

 

“Mumelazimishwa kupigana vita (kwa ajili ya dini). Nalo ni jambo zito kwenu. Lakini huenda mkachukia kitu nacho ni kheri kwenu. Na huenda mkapenda kitu nacho ni shari kwenu. Na Allaah ndiye anayejua, (lakini) nyinyi hamjui.”

Al-Baqarah: 216

 

Kupigana Jihaad ni Fardhi Kifaayah na wakati mwingine inakuwa Fardhi ‘Ayn.

 

 

Fardhi ‘Ayn

 

‘Fardhi ‘Ayn’ ni yale ambayo kila Muislamu analazimika kuwa nayo au kuyatenda, na hasameheki asiyetenda hata kama kundi la watu wengine watalisimamia jambo hilo na kulikamilisha, kwa mfano; Imani, Swalah, Twahara, Kutoa Zakaah, Kufunga, Kuhiji n.k. Haya yanaitwa Fardhi ‘Ayn na kila Muislamu analazimika kuwa nayo au kuyatenda na si halali kwa mtu yeyote kutoyapa umuhimu.

 

 

Maana Ya Fardhi Kifaayah

 

 

Ama ‘Fardhi kifaayah’ ni yale matendo ambayo Waislamu wanalazimika kuyatenda ingawaje si lazima litendwe na Waisalmu wote, kwani linapotendwa na kundi miongoni mwao, basi waliobaki wanasameheka, kwa mfano,

 

KATIKA DINI:

Kujifunza elimu ya dini kwa ajili ya kuwasomesha wengine, Kumswalia maiti, Kuadhini n.k.

 

KATIKA MAISHA:

Kulima, Utabibu, Ufundi na yaliyo na mfano wake, mambo ambayo yakikosekana, maisha ya wanaadamu yanakuwa hatarini.

 

 

Yanayomhusu Kiongozi

 

Kama vile kuamrisha mema, kukataza mabaya, Kuitisha Jihaad, na Kuyapiga vita maovu na yale yaliyoharamishwa nk.

 

Jihaad inaingia katika Fardhi Kifaayah ambayo haimwajibikii kila mtu iwapo litatokea kundi la watu miongoni mwao litakaloweza kuwapiga vita maadui na kuiondoa shari yao bila kuhitajia msaada wa waliobaki.

 

Katika kutafuta elimu, Allaah Anasema:

 

وَمَا كَانَ الْمُؤْمِنُونَ لِيَنفِرُواْ كَآفَّةً فَلَوْلاَ نَفَرَ مِن كُلِّ فِرْقَةٍ مِّنْهُمْ طَآئِفَةٌ لِّيَتَفَقَّهُواْ فِي الدِّينِ وَلِيُنذِرُواْ قَوْمَهُمْ إِذَا رَجَعُواْ إِلَيْهِمْ لَعَلَّهُمْ يَحْذَرُون

 

“Wala haiwapasi Waislamu kutoka wote (katika miji yao wakaja Madiynah wakaiwacha miji yao mitupi). Lakini kwa nini halitoki kundi (tu) katika kila taifa miongoni mwao (lende Madiynah kwa Mtume) kujitalimisha vyema dini na (kisha wakaja) kuwaonya weziwao (waliosalia makwao) watakapowarudia, ili wapate kujihadharisha (na wao na mabaya).”

At-Tawbah: 122

 

 

Ama kuhusu Jihaad, Allaah Anasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ خُذُواْ حِذْرَكُمْ فَانفِرُواْ ثُبَاتٍ أَوِ انفِرُواْ جَمِيعًا

 

“Enyi Mlioamini! Shikeni hadhari yenu (juu ya maadui zenu msikhadaike). Tokeni (kwenda vitani) makundi moja moja au tokeni nyote pamoja (kama atakavyokuambieni Mtume).”

An-Nisaa: 71

 

Na Akasema:

 

لاَّ يَسْتَوِي الْقَاعِدُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ غَيْرُ أُوْلِي الضَّرَرِ وَالْمُجَاهِدُونَ فِي سَبِيلِ اللّهِ بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ فَضَّلَ اللّهُ الْمُجَاهِدِينَ بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ عَلَى الْقَاعِدِينَ دَرَجَةً وَكُـلاًّ وَعَدَ اللّهُ الْحُسْنَى وَفَضَّلَ اللّهُ الْمُجَاهِدِينَ عَلَى الْقَاعِدِينَ أَجْرًا عَظِيمًا

 

“Hawawi sawa Waislamu wanaokaa wasende vitani, isipokuwa wenye dharura. (Hawawi sawa) na wale wapiganao katika njia ya Allaah kwa mali zao na kwa nafsi zao. Allaah amewafadhilisha katika cheo wale wapiganao katika njia ya Allaah kwa mali zao na kwa nafsi zao kuliko wakaao (wasende kupigana). Ingawa Allaah ameahidi wote (kupata) wema. Lakini Allaah amewafadhilisha – wale wapiganao kuliko wakaao – kwa ujira mkuu.”

An-Nisaa: 95

 

 

Na katika Sahihi Muslim kutoka kwa Abu Sa’iyd Al Khudry (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa; Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alituma ujumbe kwenda kwa watu wa kabila la Hudhayl kuwaambia:

“Atoke (kwenda vitani) katika kila wawili mtu mmoja na ujira watapata wote wawili.”

Sahihi Muslim Kitab al-Imaara – mlango wa Fadhail I’aanat al-ghazi fiy sabili Llaah – Hadiyth nambari 38

 

Na hii ni kwa sababu ikimwajibikia kila mtu, basi mambo mengi ya kidunia yenye maslahi kwa wanaadamu yataharibika, ndiyo maana ikawajibika kwa baadhi yao tu.

 

 

Jihaad Inapokuwa Fardhi

 

Jihaad inakuwa Fardhi ‘Ayn katika sehemu tatu:

 

Ya kwanza – ni pale mwenye kuwajibika kupigana anapokuwa vitani keshasimama katika msitari pamoja na wenzake, hapo analazimika kupigana.

 

Allaah Anasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ إِذَا لَقِيتُمْ فِئَةً فَاثْبُتُواْ

 

 “Enyi mlioamini! Mkutanapo na jeshi (la makafiri) kazaneni barabara (wala msikimbie).”

Al-Anfaal: .45

 

Na Anasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ إِذَا لَقِيتُمُ الَّذِينَ كَفَرُواْ زَحْفاً فَلاَ تُوَلُّوهُمُ الأَدْبَارَ

Enyi Mlioamini! Mkikutana na waliokufuru vitani msiwageuzie mgongo.”

Al-Anfaal: 15

 

 

Ya pili – Adui anapoingia katika nchi ya Kiislamu, wanalazimika watu wote wa nchi hiyo kwa pamoja kutoka na kupambana naye, na si halali kwa mtu yeyote kurudi nyuma asitimize wajibu wake huo wa kupigana na adui, na hii ikiwa haiwezekani kumtoa adui huyo bila kushirikiana wote kwa pamoja.

 

Allaah Anasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ قَاتِلُواْ الَّذِينَ يَلُونَكُم مِّنَ الْكُفَّارِ وَلِيَجِدُواْ فِيكُمْ غِلْظَةً وَاعْلَمُواْ أَنَّ اللّهَ مَعَ الْمُتَّقِينَ

 

“Enyi mlioamini! Piganeni na wale makafiri walio karibu yenu (kwanza kwani ndio wenye madhara na nyinyi zaidi), na wakute ugumu kwenu. Na jueni ya kwamba Allaah yu pamoja na wacha- Mungu.”

At-awbah: 123

 

 

Ya tatu – Mwenye kuhukumu anapotangaza Jihaad analazimika kila mwenye kuwajibika kupigana kuuitikia mwito huo, na haya yanatokana na Hadiyth iliyosimuliwa na Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliposema kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

 

لا هجرة بعد الفتح ولكن جهاد ونية وإذا استنفرتم فانفروا

 

“Hapana kuhajir tena (kutoka Makkah kwenda Madiynah) baada ya Waislamu kuuteka (mji wa Makkah) isipokuwa (kilichokuwepo ni) Jihaad na nia (ya kupigana Jihaad), na mnapoitwa muitikie (mwito).”

Swahiyh al-Bukhaariy – juzu ya 2 Mlango wa ‘Fadhila za Jihaad.’ Hadiyth nambari 2631.

 

Na maana yake ni kuwa mnapotakiwa kwenda kupigana Jihaad, basi lazima muitikie mwito huo.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ مَا لَكُمْ إِذَا قِيلَ لَكُمُ انفِرُواْ فِي سَبِيلِ اللّهِ اثَّاقَلْتُمْ إِلَى الأَرْضِ أَرَضِيتُم بِالْحَيَاةِ الدُّنْيَا مِنَ الآخِرَةِ فَمَا مَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا فِي الآخِرَةِ إِلاَّ قَلِيلٌ

 

“Enyi mlioamini! Mna nini mnapoambiwa “Nendeni (kupigana) kwa ajili ya dini ya Allaah” mnajitia uzito katika ardhi? Je, mumekuwa radhi na maisha ya dunia kuliko ya Akhera? Lakini starehe za maisha ya dunia kwa (mkabala wa maisha ya) Akhera ni kidogo tu.”

At-Tawbah: 38.

 

 

Wanaowajibika Kupigana

 

Anawajibika kupigana Jihaad kila Muislamu mwanamume, mwenye akili timamu, aliyekwishabaleghe, mwenye afya njema mwenye uwezo wa kuwaachia watu wake kiasi cha mali inayowatosha mpaka pale atakaporudi.

 

Kwa hivyo haimwajibikii asiyekuwa Muislamu, mwanamke, mtoto mdogo, mwenda wazimu na mgonjwa, na kwa ajili hiyo hana lawama yeyote katika hawa asipoutikia mwito wa Jihaad kutokana na udhaifu wao au umasikini wao au umri wao au kutokuwa na akili zao ambao huenda kuwepo kwao katika uwanja wa mapambano kukasababisha madhara zaidi kuliko manufaa.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

 

لَّيْسَ عَلَى الضُّعَفَاء وَلاَ عَلَى الْمَرْضَى وَلاَ عَلَى الَّذِينَ لاَ يَجِدُونَ مَا يُنفِقُونَ حَرَجٌ إِذَا نَصَحُواْ لِلّهِ وَرَسُولِهِ مَا عَلَى الْمُحْسِنِينَ مِن سَبِيلٍ وَاللّهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

“Hapana lawama kwa wanyonge, wagonjwa, na wasiopata cha kutumia, maadamu wanamsafia nia Allaah na Mtume Wake. Hapana njia ya kuwalaumu wanao fanya wema. Na Allaah ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.”

At-Tawbah: 91.

 

Na Anasema:

لَيْسَ عَلَى الأعْمَى حَرَجٌ ولا عَلَى الأَعْرَجِ حَرَجٌ وَلا عَلَى الْمَرِيضِ حَرَجٌ

 

“Kipofu hana lawama, wala kiguru hana lawama, wala mgonjwa hana lawama.”

Al-Fat-h: 17.

 

Na kutoka kwa ‘AbdullAah bin ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema:

“Nilipelekwa kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) siku ya Uhud (aniruhusu nikapigane) na wakati huo nilikuwa na umri wa miaka kumi na nne lakini hakuniruhusu.”

Fat-hul Baariy – Sharh ya Swahiyh al-Bukhaariy Juz. 5 Kkitabu cha ‘Ushahidi’, mlango wa ‘kubaleghe kwa watoto na ushahidi wao’.

 

Swahiyh Muslim – Kitabu cha ‘Imaarah’ mlango unaobainisha kubaleghe – Hadiyth nambari 1868

Na hii ni kwa sababu Jihaad ni ibada na haimwajibikii isipokuwa aliyebaleghe.

 

Imeelezwa na Maimam Ahmad na al-Bukhaariy kutoka kwa Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kuwa amesema:

 

“Nilisema (Nilimuuliza) - ewe Mtume wa Allaah; wanawake wanawajibika kupigana Jihaad?” akanijibu: “Jihaad (yao ni ile) isiyokuwa na kuuana ndani yake -  Hija na ‘Umrah.”

Musnad ya Imam Ahmad juz. 6 – Hadiyth za Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha)

Fat-hul Baariy – Sharh ya Swahiyh al-Bukhaariy Juz. 4 mlango wa Hija ya wanawake.

 

Na katika riwaya nyingine kuwa alisema:

“Lakini Jihaad iliyo bora ni Hija iliyokubaliwa.”

 

Imesimuliwa na Al-Waahidiy na As-Suyuutiy katika ‘Ad-Dur al-Manthuur’ kuwa Mujaahid amesema; “Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anha) alisema:

“Ewe Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), (kwa nini) wanaume (tu) wanateka miji (wanapigana Jihaad) na sisi hatuteki na sisi tunapata nusu ya urithi (tu)?”

 

Allaah Akateremsha kauli Yake:

 

وَلاَ تَتَمَنَّوْاْ مَا فَضَّلَ اللّهُ بِهِ بَعْضَكُمْ عَلَى بَعْضٍ لِّلرِّجَالِ نَصِيبٌ مِّمَّا اكْتَسَبُواْ وَلِلنِّسَاء نَصِيبٌ مِّمَّا اكْتَسَبْنَ وَاسْأَلُواْ اللّهَ مِن فَضْلِهِ إِنَّ اللّهَ كَانَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا

“Wala msitamani alicho wafadhili Allaah baadhi yenu kuliko wengine. Wanaume wana fungu katika waliovichuma, na wanawake wana fungu katika waliovichuma. Na muombeni Allaah fadhila Zake. Hakika Allaah ni Mjuzi wa kila kitu.”

An-Nisaa: 32.

 

Imepokelewa pia kutoka kwa Ikrimah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa  alisema:

"Wanawake waliuliza juu ya Jihaad wakasema: “Tunatamani lau Allaah angejaalia na sisi pia tuwe tunapigana Jihaad ili tupate cho chote katika ujira (mwema) kama wanavyopata wanaume.” Ndipo Allaah Alipoiteremsha aya hiyo.

 

Hata hivyo hapana ubaya ikiwa wanawake watatoka kwa ajili ya kuwatibia walioumia au kwa ajili ya shughuli za mfano wake.

 

Kutoka kwa Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

“Siku ya (vita vya) Uhud Waislamu walishindwa wakiwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), nilimuona (siku hiyo) Bibi ‘Aaishah binti Abi Bakr na Ummu Sulayum wakiwa wamekunja mikono ya kanzu zao nikiviona visigino vya miguu yao (huku wakiwa wanakwenda mbio) huku (na kule) wakibeba viriba vya maji migongoni mwao na kuwanywesha watu, kisha wanarudi na kuvijaza tena kisha wanarudi kuwanywesha watu (tena).”

Al-Bukhaariy juz. 2 – Kitabu cha Jihaad, mlango wa ‘Kupigana Jihaad wanawake pamoja na wanaume.’ Hadiyth nambari 2724.

Muslim juz. 3 Mlango wa ‘Kupigana Jihaad wanawake pamoja na wanaume.’ Hadiyth nambari 1811.

 

Kutoka kwa Anas pia anasema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akipigana vita akiwa pamoja na Ummu Sulayum na wanawake wengine katika watu wa Madiynah, waliokuwa wakiwanywesha watu maji na kuwatibia majeruhi.”

Muslim juz. 3 Mlango wa ‘Kupigana Jihaad wanawake pamoja na wanaume.’ Hadiyth nambari 1810.

Abu Daawuud juz. 3 mlango wa ‘Wanawake wanapigana vita’. Hadiyth nambari 2529.

 

At-Tirmidhiy juz. 3 mlango wa ‘Wanawake kwenda vitani’ Hadiyth nambari 1623.

 

 

Ruhusa Ya Wazee

 

Jihaad iliyowajibika haihitajii ruhusa ya wazee, ama Jihaad ya kujitolea lazima ipatikane ruhusa ya wazee wawili au ya mmoja wao.

 

Amesema Ibn Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu):

“Nilimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam); ‘Amali (ibada) ipi inayopendwa zaidi na Allaah?

Akasema:

“Swala katika wakati wake”.

Nikamuuliza (tena):

“Kisha ipi?”

Akaniambia:

“Kuwatii wazee wawili.”

Nikamuuliza (tena):

“Kisha ipi?”

Akaniambia:

 “Jihaad katika njia ya Allaah.”

Swahiyh Al-Bukhaariy juz.1 Kitabu cha ‘Nyakati za Swalah’, mlango wa ‘Fadhila za kusali katika wakati wake’, Hadiyth nambari 504.

Swahiyh Muslim – juz. 1 Kitabu cha ‘Imani’, mlango wa ‘Imani juu ya Allaah ndiyo ‘amali bora kupita zote’, Hadiyth nambari 85

 

Na Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

“Alikuja mtu kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na kumuomba amruhusu kwenda kupigana Jihaad, akamuuliza; ‘Wazee wako wahai?’ Akasema; ‘Ndiyo’, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia: ‘Basi Jihaad yako iwe katika (kuwahudumia) wao’.

Abu Daawuud na An-Nasaaiy na At-Tirmidhiy aliyeisahihisha.

 

Na katika kitabu kiitwacho ‘Shar-atul Islaam’, (imeandikwa):

‘Na haijuzu kwenda kupigana Jihaad isipokuwa yule tu asiyekuwa na matatizo ya kuwahudumia wanawe na wazee wake, kwa sababu hayo ni bora kuliko kupigana Jihaad, bali ndiyo Jihaad iliyo bora.’

(Bila shaka hii ni katika Jihaad isiyowajibika, ama katika Jihaad ya ‘Fardh ‘Ayn’ yaani Jihaad iliyowajibika, basi hapana haja ya kuomba ruhusa kwa mtu yeyote kama ilivyotangulia kuelezwa).

 

 

Kumuomba Ruhusa Mwenye Deni

 

Haruhusiwi kwa anayedaiwa kwenda katika Jihaad isiyowajibika isipokuwa baada ya kumuomba ruhusa mwenye kumdai au aweke rahani mali inayotosheleza kulipa deni hilo au aweke mdhamini, kwa sababu katika Hadiyth ya Abu Qataadah (Radhiya Allaahu ‘anhu) iliyomo ndani ya kitabu cha Imam Ahmad na pia katika Swahiyh Muslim (aliulizwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)):

‘Unaonaje nikiuliwa katika (Jihaad) katika njia ya Allaah, nitasamehewa madhambi yangu yote?’

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:

“Ndiyo (utasamehewa) ikiwa utauliwa ukiwa katika subira huku ukitegemea ujira mwema (kutoka kwa Allaah), isipokuwa (kama una) deni, hakika Jibril ameniambia hayo (hivi punde).”

Ahmad na Muslim

 

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah anamghufiria aliyekufa shahiyd madhambi yake yote isipokuwa deni.”

Pamoja na deni zinaingia pia dhulma alizowadhulumu watu, kama vile kuua na kula mali za watu pasipo haki na mfano wake.

 

 

Msaada Wa Makafiri

 

Inajuzu kutaka msaada wa wanafiki na wavunjao amri katika vita dhidi ya makafiri, na hii ni kwa sababu ‘Abdullaahi bin Ubay na wanafiki wenzake walikuwa wakienda vitani pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), na pia kisa cha Abu Muhjan ath-Thaqafi aliyekuwa mlevi, aliyepigana katika vita dhidi ya dola ya Kifursi ni mashuhuri sana.

Ama kutaka kupigana vita pamoja na makafiri, jambo hili lina khitilafu ndani yake miongoni mwa Maulamaa wa Kiislamu.

 

Ma Imaam Maalik na Ahmad wanasema:

“Haijuzu kutaka msaada wao, wala kusaidia katika jambo lolote.”

 

Imam Maalik akaongeza:

‘Isipokuwa kama watakuwa wakiwahudumia Waislamu tu, hapo inajuzu.’

 

Imam Abu Haniyfah yeye amesema:

“Inawezekana kutaka msaada wao na wanaweza kutoa msaada wowote ule sharti uwe Uislamu ndio wenye nguvu, ama ikiwa ushirikina ndio wenye nguvu, basi inachukiza.”

 

Imam ash-Shaafi’iy yeye anasema:

“Inajuzu kwa masharti mawili;

Kwanza – Waislamu wawe wengi na washirikina wawe wachache.

Pili – Wawe wanajulikana washirikina hao kuwa wana fikra nzuri na muelekeo mzuri juu ya Uislamu. Na watakapotakiwa msaada wao, wasipewe katika sehemu ya ngawira, bali wapewe malipo maalum bila kushirikishwa katika ngawira.”

 

 

Msaada Wa Watu Dhaifu

 

Kutoka kwa Mus'aab bin Sa’ad bin Abi Waqaas amesema:

“Baba yangu alidhani kuwa ana fadhila zaidi kuliko waliokuwa chini yake, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia:

“Kwani mungepata ushindi na kupata riziki bila ya (du’aa za) madhaifu miongoni mwenu?”

Al-Bukhaariy na An-Nasaaiy.

 

Katika An-Nasaaiy imeandikwa kwa lafdhi ifuatayo:

“Hakika Allaah huwanusuru umma huu kwa madhaifu wao, kwa Dua zao na Swala zao na ikhalsi yao.”

 

Na kutoka kwa Abu ad-Darda-a (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

“Nilimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akisema:

“Niitieni masikini wenu, kwa hakika mnapata rizki na mnapata ushindi kwa (dua) za madhaifu wenu.”

Maimamu wote wa Ahlus Sunnah

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Huenda mwenye nywele zilizotimka (kwa umasikini), anayefukuzwa milangoni (kwa kudharauliwa) anapomuomba Allaah Atamkubalia (du’aa yake).”

Ahmad na Muslim

 

 

 

 

Share

03-Jihaad: Wajibu Wa Kuwa Thabiti

 

Wajibu Wa Kuwa Thabiti

 

Muislamu analazimika kuwa thabiti mbele ya adui na ni haramu kwake kurudi nyumba katika mapambano.

Allaah Anasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ إِذَا لَقِيتُمُ الَّذِينَ كَفَرُواْ زَحْفاً فَلاَ تُوَلُّوهُمُ الأَدْبَارَ. وَمَن يُوَلِّهِمْ يَوْمَئِذٍ دُبُرَهُ إِلاَّ مُتَحَرِّفاً لِّقِتَالٍ أَوْ مُتَحَيِّزاً إِلَى فِئَةٍ فَقَدْ بَاء بِغَضَبٍ مِّنَ اللّهِ وَمَأْوَاهُ جَهَنَّمُ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ

“Enyi Mlioamini! Mkutanapo vitani na wale waliokufuru basi msiwageuzie migongo (mkakimbia).

Na atakayewageuzia mgongo wake siku hiyo - isipokuwa kwa mbinu za vita au kuungana na kikosi - basi atakuwa amestahiki ghadhabu ya Allaah. Na pahala pake ni Jahannamu, na huo ni mwisho muovu.”

Al-Anfaal: 15-16

 

Aya hizi zinawajibisha kuwa thabiti katika mapambano na zinaharamisha kurudi nyuma isipokuwa katika hali mbili zifuatazo;

 

Ya kwanza – Kwa ajili ya mbinu za kivita kama vile kuondoka mahali penye hatari zaidi na kukimbilia mahali bora, au kuondoka mahali anapoweza kudhurika kwa urahisi na kukimbilia mahali anapoweza kusitirika, au mahali pa chini na kukimbilia penye muinuko atakapoweza kupambana na adui kwa urahisi zaidi.

 

Ya pili – Kurudi kwa nia ya kuungana na wenzake kwa ajili ya kupambana kwa pamoja dhidi ya adui, au kwa ajili ya kuwasaidia wenzake hao, yote sawa ikiwa wenzake hao wako karibu au wako mbali.

 

Kinyume na hivyo, kurudi nyuma kwa ajili ya kukimbia tu ni mojawapo ya madhambi makubwa sana yatakayompelekea mtu kupata adhabu iumizayo.

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Jiepusheni na mambo saba yaangamizayo.”

Wakamuuliza:

“Ni yepi hayo ewe Mtume wa Allaah?”

Akasema:

“Kumshirikisha Allaah, Uchawi, kuiuwa nafsi iliyoharamishwa na Allaah, kula riba, kula mali ya yatima, kukimbia mnapokutana na adui, na kuwasingizia uongo wanawake waliotakasika wasiojua (maovu)."

 

Uongo Na Hadaa Vitani

 

Inajuzu kufanya hadaa na kusema uongo vitani kwa ajili ya kumbabaisha adui, sharti visitumike (uongo na hadaa) katika kuvunja mikataba na ahadi.

 

Mfano wa hadaa ni pale kiongozi anapomhadaa adui akamfanya adhani kuwa ana jeshi kubwa sana na nguvu nyingi.

Katika hadithi iliyotolewa na Al-Bukhaariy kutoka kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Vita ni hadaa.”

 

Na imetolewa na Muslim katika hadithi ya Ummu Kulthuum bint ‘Uqbah (Radhiya Allaahu ‘anha) kuwa amesema:

“Sijapata kumsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akitoa ruhusa ya kusema uongo juu ya jambo lolote lile katika mazungumzo ya watu isipokuwa katika vita au katika kuleta sulhu baina ya watu na (pia) mtu anapozungumza na mkewe na mwanamke anapozungumza na mumewe.”

 

 

Rehma Vitani

 

Uislamu umeruhusu vita kama ni jambo la dharura na ukaweka vipimo maalumu juu yake, kwa mfano;

 

Asiuliwe isipokuwa anayeshiriki katika vita, ama aliyejitenga asipigane vita, huyo haijuzu kuuliwa au hata kudhuriwa kwa jambo lolote.

 

Imeharamishwa pia kuua wanawake, watoto, wagonjwa, wazee, maulamaa wa dini, wachaji Allaah na waloingia katika sulhu.

 

Imeharamishwa pia kuuharibu mwili wa aliyeuliwa kwa kukatwakatwa, kuuwa wanyama, kufisidi mazao, maji, kuvichafua visima na kubomoa nyumba.

 

Ni haramu pia kuua majeruhi, na kuendeleza chuki, na hii ni kwa sababu vita ni mfano wa opreshen ‘operation’, ambapo anachotakiwa tabibu ni kuyaondoa maradhi tu, na asivuke zaidi ya hapo.

 

Imehadithiwa na Sulaymaan bin Buraydah kutoka kwa kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) anapomchagua kiongozi wa jeshi au wa kikosi, alikuwa akimwita pembeni na kumuusia kumcha Allaah yeye pamoja na maaskari wake, kisha akimwambia:

 

“Piganeni vita kwa jina la Allaah katika njia ya Allaah, piganeni na wanaomkufuru Allaah, piganeni lakini msichupe mipaka, wala msifanye khiyana, wala msiwaharibu maiti kwa kuwakatakata, wala msiuwe watoto.”

 

Amehadithia Nafia kutoka kwa ‘AbduAAllaah bin ‘Umar (Radhiya Allaahu anhu) kuwa katika baadhi ya vita, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alimkuta mwanamke ameuliwa, akakataza kuuliwa kwa wanawake na watoto.

Muslim

 

Amehadithia pia Rawaah bin Rabia’ (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alimuona mwanamke ameuliwa katika mojawapo ya vita alivyoshiriki na huenda akawa ni huyo aliyetajwa katika hadithi iliyotangulia, akasimama mbele ya maiti hiyo kisha akasema:

 

“Hapakuwa na haja ya kumuua mwanamke huyu.” Kisha akawa anaziangilia nyuso za Maswahaba wake kisha akamwambia mmoja wao:

“Kamwahi Khalid bin Walid (umwambie); asiue watoto wala mateka wala mwanamke.”

 

Na katika usia wa Abu Bakr (Radhiya Allaah ‘anhu) alompa ‘Usaamah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipompeleka katika nchi ya Shaam alimwambia:

 

"Msifanye khiyana wala msishambulie bila taarifa (ghadran), wala msikate kate maiti za adui, wala msiuwe mtoto wala mzee wala mwanamke, wala msiunguze mtende wala msikate mti unaotoa mazao wala msichinje mbuzi au n'gome au ngamia ila kwa ajili ya kula. Na mtakutana na watu waliojitenga ndani ya mahekalu yao kwa ajili ya ibada, basi waacheni hivyo hivyo walivyo."

Kisha akasema: "Nendeni kwa jina la Allaah."

 

Na usia kama huu alikuwa akitoa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) na wengine miongoni mwa Makhalifa wa Kiislamu.

 

 

Mwisho

 

 

Share

04-Jihaad: Fadhila Na Thamani Ya Jihaad

Fadhila Za Jihaad

 

Ibada Bora

 

Fadhila zinazopatikana katika Kupigana Jihaad isiyokuwa ya waajib kwa ajili ya kulinyanyua neno la Allaah na kuimakinisha hidaaya Yake juu ya ardhi, na kwa ajili ya kuimakinisha dini ya haki ni nyingi kupita fadhila zinazopatikana katika kuhiji Hija ya nyongeza baada ya mtu kuhiji Hija yake ya lazima, au ‘Umrah ya nyongeza, au Swalah za Sunnah au Swawm ya Sunnah.

 

Juu ya yote hayo, Jihaad imekusanya kila aina ya ibada za kiroho na kiwiliwili, kuikinai dunia, kuihama nchi na kuyahama matamanio na hii ndiyo maana ikapewa jina la ‘Uchaji Allaah’, kwani imekuja katika Hadiyth kuwa:

‘Ucha Mungu wa umma wangu ni Jihaad katika njia ya Allaah.”

 

Na ndani yake mna kuitakasa nafsi, kuitakasa mali, na kumuuzia Allaah nafsi, na haya yote ni matunda ya mapenzi na imani na yakini na kuelekea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

Allaah Anasema:

 

إِنَّ اللّهَ اشْتَرَى مِنَ الْمُؤْمِنِينَ أَنفُسَهُمْ وَأَمْوَالَهُم بِأَنَّ لَهُمُ الجَنَّةَ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللّهِ فَيَقْتُلُونَ وَيُقْتَلُونَ وَعْدًا عَلَيْهِ حَقًّا فِي التَّوْرَاةِ وَالإِنجِيلِ وَالْقُرْآنِ وَمَنْ أَوْفَى بِعَهْدِهِ مِنَ اللّهِ فَاسْتَبْشِرُواْ بِبَيْعِكُمُ الَّذِي بَايَعْتُم بِهِ وَذَلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

 

“Hakika Allaah Amenunua kwa Waumini nafsi zao na mali zao kwa kuwa wao watapata Pepo. Wanapigana katika Njia ya Allaah - wanaua na wanauawa. Hii ni ahadi Aliyojilazimisha kwa Haki katika Taurati na Injili na Qur-aan. Na nani atimizae ahadi kuliko Allaah? Basi furahini kwa biashara yenu mliyo fanya naye. Na huko ndiko kufuzu kukubwa.”

At-Tawbah: 111

 

Dini ya Kiislamu imeitukuza ibada hii ya Jihaad, na ikatunabahisha juu umuhimu wake katika sura nyingi zilizoteremshwa Madina na ikawalaumu wanaoiacha na wanaoipinga na kuwapa sifa za unafiki na wenye maradhi moyoni.

 

 

Watu Bora

 

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Nikujulisheni juu ya aliye bora kupita wote? Mtu aliyeshika hatamu za farasi wake (akimuelekeza) katika njia ya Allaah (kupigana Jihaad). Nikujulisheni juu ya anayefuatia? Mtu aliyejitenga akiwa na mbuzi wake akitoa haki ya Allaah katika mbuzi hao. Nikujulisheni juu ya mtu muovu kupita wote? Mtu anayeombwa kwa jina la Allaah kisha hatoi (juu ya kuwa anao uwezo).”

Alipoulizwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam): ‘Mtu yupi aliye bora?’

Akajibu: “Muislamu anayepigana Jihaad katika njia ya Allaah kwa nafsi yake na mali yake.”

Wakamuuliza: “Kisha yupi?”

Akasema: “Muislamu katika bonde mojawapo akimcha Allaah na anawaepusha watu na shari yake.”

 

 

Pepo Kwa Ajili Ya Mujaahidiyn

 

AmeHadiytha At-Tirmidhiy kuwa mtu mmoja alitamani ajitenge (awe mbali na watu huku akifanya shughuli za ibada peke yake), akamuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) juu ya jambo hilo, na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia:

 

“Usifanye hivyo, kwa sababu mmoja wenu anaposimama (tu) katika njia ya Allaah (wakati wowote anapokuwa katika Jihaad), ni bora kuliko akisali nyumbani kwake muda wa miaka sabini. Hampendi nyinyi Allaah akughufirieni kisha akuingizeni Peponi? Piganeni katika njia ya Allaah. Atakayepigana katika njia ya Allaah (muda wa) kiasi cha kumkamua ngamia maziwa tu, imemwajibikia Pepo.”

At-Tirmidhy

 

 

Daraja Mia Peponi

 

Kutoka kwa Abu Sa’iyd al-Khudry (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

 

“Ewe Abu Sa’iyd! Atakayeridhika kuwa Mola wake ni Allaah, na Islamu dini yake, na Muhammad Mtume wake, amewajibika kuingia Peponi.”

Abu Said akastaajabu kwa maneno hayo akasema:

“Yarudie tena (maneno hayo) kwa ajili yangu ewe Mtume wa Allaah.”

Kisha (Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)) akasema:

“Na mengine anamnyanyua kwayo mja wake daraja mia, na baina ya kila daraja mbili (umbali wake) sawa na umbali wa mbingu na ardhi.”

Akauliza;

“Nini hicho ewe Mtume wa Allaah?”

Akasema:

“Ni Jihaad katika njia ya Allaah, ni Jihaad katika njia ya Allaah.”

Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika huko Peponi zipo daraja mia, Allaah amewatayarishia wapiganao Jihaad katika njia ya Allaah, na baina ya kila daraja mbili umbali wake sawa na umbali wa mbingu na ardhi. Na mnapomuomba Allaah, muombeni (Pepo ya) Al Firdaus, kwani hiyo ipo kati kati ya Pepo, sehemu ya juu ya Pepo, na juu yake ipo Arshi ya Al Rahman, na kutoka hapo inapasuka (inaanzia) mito ya Peponi.”

 

 

Thamani ya Jihaad

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema:

 

“Aliulizwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):

“Kipi chenye thamani kupita Jihaad katika njia ya Allaah?”

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:

“Hamukiwezi.”

Akaulizwa suali hilo mara mbili au tatu na kila anapoulizwa alikuwa akijibu;

“Hamukiwezi.”

Mara ya tatu akasema:

“Mfano wa anayepigana Jihaad katika njia ya Allaah ni mfano wa aliyefunga (aliyebaki akiwa amefunga), (na) akasali nyakati za usiku huku akiomba na kusoma aya za Allaah bila kuchoka katika Sala yake wala kuacha kufunga mpaka atakaporudi yule aliyekwenda kupigana Jihaad katika njia ya Mwenyezi.”

Maimamu watano

 

 

Kufa Shahiyd

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

 

“Hajeruhiwi mtu (anapopigana Jihaad) katika njia ya Allaah, na Allaah anamuelewa kila anayejeruhiwa katika njia ya Allaah, isipokuwa atakuja siku ya kiama huku jeraha lake likiwa linamwaga damu, na rangi ni rangi ya damu lakini harufu ni harufu ya miski.”

 

Amesema Muhammad bin Ibraahiym katika Hadiyth ndefu yenye shairi refu ndani yake kuwa:

 

“Kisha nikakutana na al-Fudhayl bin ‘Iyaadh akanambia:

“Wewe ni katika wanaoandika Hadiyth?”

Nikamwambia; “Ndiyo’.

Akaniambia; “Basi iandike Hadiyth hii (kama) ujira wako kwa kutuletea kitabu cha Abi Abdir-Rahmaan. Kisha al-Fudhayl bin ‘Iyaadh akaanza kunihadithia yafuatayo:

“Amenihadiithia Mansuur bin Al-Muatamir, kutoka kwa Abu Swaalih, kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa mtu mmoja alimwambia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam); “Ewe Mtume wa Allaah nifundishe jambo nitakalopata ndani yake thawabu ya mpigana Jihaad katika njia ya Allaah.”

Akasema:

“Unaweza uwe unaswali (moja kwa moja) bila kuchoka, na ufunge (moja kwa moja) bila kula chakula?”

Akasema:

“Ewe Mtume wa Allaah mimi ni dhaifu nisiyeweza kufanya yote hayo.”

Kisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia:

“Basi naapa kwa yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake, lau kama utafanya yote hayo basi (bado) hutouifikia (daraja) ya mpigana Jihaad katika njia ya Allaah.

Hujaelewa bado kuwa Mpigana Jihaad anapokuwa juu ya farasi (akiwa amekaa tu juu yake) huku amezishika hatamu anaandikiwa thawabu?.”

 

Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliwahi kuwaambia Maswahaba wake:

 

“Walipofariki ndugu zenu katika vita vya Uhud, Allaah alizijaalia roho zao ndani ya mwili (mfano) wa ndege wa kijani wanaiendea mito ya Peponi na wanakula katika matunda yake na wanakaa katika tundu za dhahabu zilizotundikwa katika kivuli cha Arshi. Walipoona ladha nzuri ya vyakula vyao na vinywaji vyao na makazi yao wakasema:

“Nani atakayewajulisha ndugu zetu (waliopo duniani) juu yetu kuwa tuko hai Peponi tunaruzukiwa, ili wasije kufanya ulegevu katika Jihaad?”

Allaah Akasema:

“Mimi nitawajulisha juu yenu.”

 

Ndipo Alipoteremsha kauli Yake:

 

وَلاَ تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ قُتِلُواْ فِي سَبِيلِ اللّهِ أَمْوَاتًا بَلْ أَحْيَاء عِندَ رَبِّهِمْ يُرْزَقُونَ . فَرِحِينَ بِمَا آتَاهُمُ اللّهُ مِن فَضْلِهِ وَيَسْتَبْشِرُونَ بِالَّذِينَ لَمْ يَلْحَقُواْ بِهِم مِّنْ خَلْفِهِمْ أَلاَّ خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلاَ هُمْ يَحْزَنُونَ 0 يَسْتَبْشِرُونَ بِنِعْمَةٍ مِّنَ اللّهِ وَفَضْلٍ وَأَنَّ اللّهَ لاَ يُضِيعُ أَجْرَ الْمُؤْمِنِينَ

 

“Wala kabisa usiwadhanie waliouliwa katika Njia ya Allaah kuwa ni maiti. Bali hao ni wahai, wanaruzukiwa kwa Mola wao Mlezi.

Wanafurahia aliyo wapa Allaah kwa fadhila Yake, na wanawashangilia wale ambao bado hawajajiunga nao, walio nyuma yao, ya kwamba haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika.

Wanashangilia neema na fadhila za Allaah, na ya kwamba Allaah Hapotezi ujira wa Waumini.”

Aal-‘Imraan: 169-171

 

Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

 

“Roho za mashahidi zimo ndani ya miili (mfano wa miili) ya ndege (yenye rangi ya) kijani, wanatembezwa (wanaingia na kutoka) Peponi wanavyotaka.”

 

Na akasema:

 

“Shahidi hahisi maumivu ya kuuliwa ila kama mmoja wenu anavyohisi maumivu ya kufinywa.”

 

Na akasema:

 

“Jihaad iliyo bora, ajeruhiwe farasi wako na imwagike damu yako.”

 

Kutoka kwa Jaabir bin ‘Aatiq kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

 

“Mashahidi ni (aina) saba gheri ya aliyeuliwa katika njia ya Allaah:

Aliyekufa kwa maradhi ya tauni ni shahidi, aliyezama (aliyekufa kwa kuzama) shahidi, mwenye maradhi yanayosibu sehemu za mbavu ni shahidi (aliyekufa kwa maradhi hayo), aliyekufa kwa maradhi  ya tumbo ni shahidi, aliyekufa kwa kuungua - shahidi, aliyekufa kwa kuangukiwa na nyumba - shahidi, na mwanamke aliyekufa katika uzazi - shahidi.”

Ahmad – Abu Daawuud – An-Nasaaiy kwa isnadi iliyo sahihi

 

Na kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Wepi mnaowahesabu kuwa ni mashahidi miongoni mwenu?”

Wakasema:

 

“Ewe Mtume wa Allaah, aliyeuliwa katika njia ya Allaah ni shahidi.”

Akasema:

“Basi mashahidi katika umati wangu watakuwa wachache.”

Wakasema:

“Wepi hao basi ewe Mtume wa Allaah?”

Akasema:

“Atakayeuliwa katika njia ya Allaah ni shahidi, na atakayekufa katika njia ya Allaah ni shahidi (yaani akiwa katika kumtii Allaah), na atakayekufa kwa maradhi ya tauni ni shahidi, na atakayekufa kwa maradhi ya tumbo ni shahidi na aliyezama ni shahidi.”

Muslim

 

Na kutoka kwa Sa’iyd bin Zayd kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayeuliwa kwa ajili ya (kuihami) mali yake ni shahidi, na atakayeuliwa kwa ajili ya (kuipigania) dini yake ni shahidi, na atakayeuliwa kwa ajili ya (kuwahami) watu wake ni shahidi.”

Ahmad na At-Tirmidhiy na akaisahihisha.

 

Wanasema wanavyouni kuwa watu wote hawa wanahesabiwa kuwa ni mashahidi juu ya kuwa hawakufa katika vita vya Jihaad ya kuipigania dini ya Allaah na kuwa siku ya Akhera watapata thawabu sawa na waliokufa katika Jihaad, isipokuwa hapa duniani wataoshwa na kusaliwa (kama maiti wa kawaida).

 

 

Kulinyanyua Neno La Allaah

 

Anayepigana Jihaad ya kweli ni yule ambaye nia yake ni kulinyanyua neno la Allaah na kuinyanyua bendera ya Haki na kuiondoa batili na kujitolea mhanga nafsi yake kwa ajili ya kutaka radhi za Allaah.

Ama ikiwa nia ya kupigana Jihaad ni nyingine katika mambo ya kidunia tofauti na hayo yaliyotajwa, basi hiyo haiwezi kupewa jina la Jihaad.

 

Kwa hivyo atakayepigana kwa ajili ya kupata cheo, au kwa ajili ya ngawira, au apate kuonekana ushujaa wake, au kwa ajili ya kujulikana, basi huyo hana chake katika ujira wowote utokao kwa Allaah na wala hatopata thawabu.

 

Kutoka kwa Abu Musa (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

“Alikuja mtu kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema (akauliza):

“Mtu anapigana kwa ajili ya kujipatia ngawira (mali inayotekwa katika vita), na mwengine apate kusifiwa, na mwengine apate kuonesha ushujaa wake, yupi kati yao (anahesabiwa kuwa) yupo katika njia ya Allaah?”

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:

“Atakayepigana ili neno la Allaah liwe juu, huyo yupo katika njia ya Allaah.”

 

Imesimuiwa na Abu Daawuud na An-Nasaaiy kuwa mtu mmoja alisema:

 

“Ewe Mtume wa Allaah, unaonaje mtu anayepigana kwa ajili ya kutaka ujira na umaarufu, anapata nini?”

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):

“Hapati chochote.”

Akauliza suali hilo mara ya tatu ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipomwambia:

“Hapati chochote. Hakika Allaah haikubali amali (matendo) yoyote ikiwa haikuwa halisi kwa ajili ya kutaka radhi Zake.”

 

Nia ni uhai wa ‘amali yoyote ile, na chochote kinachotendwa bila ya nia basi amali hiyo inakuwa amali isiyo na  uhai wala uzito wowote mbele ya Allaah.

Amesimulia Al-Bukhaariy kutoka kwa Abullaahi bin ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

 

“Hakika ‘amali zote (huhesabiwa kutokana) na nia, na hakika ana kila mja (malipo) ya aliyoyanuwia.”

 

Nia ndiyo yeye kunyanyua daraja ya matendo, kwani mtu anaweza kuifikia daraja ya waliokufa shahidi hata kama hakufa vitani.

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

 

“Atakayemuomba Allaah kwa nia ya kweli afe shahidi, Allaah Atamfikisha katika daraja za waliokufa shahidi hata kama atakufa kitandani pake.”

 

Na akasema:

 

“Hakika katika mji wa Madina kuna makundi ya watu ambao hamkwenda mwendo (yaani vitani), na hamkuyakata mabonde isipokuwa walikuwa mabondeni (sawa kama nyinyi), yamewazuia maradhi.”

 

Ama ikiwa nia ya kupigana Jihaad si kwa ajili ya kutaka radhi za Allaah, bali kwa ajili ya kutafuta manufaa ya kidunia, basi si kama mtu huyo atakosa thawabu tu, bali atakuwa amejitafutia adhabu siku ya Kiama.

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

 

“Nilimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akisema:

“Wa mwanzo kuhesabiwa siku ya Kiama ni mtu aliyekufa shahidi katika vita, ataletwa na kujulishwa neema alizoneemeshwa na baada ya kuzijuwa ataulizwa:

“Umezifanyia kazi gani neema hizi?”

Atasema:

“Nimepigana Jihaad kwa ajili yako mpaka nikafa shahidi.”

Ataambiwa:

“Umesema uongo, bali ulipigana ili pasemwe kuwa wewe ni mjasiri na pashasemwa.”

Kisha pataamrishwa abururwe kwa uso wake na kuingizwa motoni.

Na mtu (mwengine) aliyejifundisha elimu akaijuwa (vizuri), akasoma na Qur-aan, (mtu huyo) ataletwa na kujulishwa neema alizoneemeshwa, kisha ataulizwa;

“Umezifanyia kazi gani neema hizi?”

Atasema:

“Nimejifunza elimu nikafundisha na kwa ajili yako nikasoma Qur-aan.”

Ataambiwa:

“Umesema uongo, bali ulijifunza elimu ili pasemwe kuwa wewe ni aalim. Ukasoma Qur-aan ili pasemwe kuwa wewe ni msomaji mzuri, na pashasemwa.”

Kisha pataamrishwa abururwe kwa uso wake na kuingizwa motoni.

Na mtu (mwengine) Allaah Amempa wasaa, akampa kila aina ya mali, ataletwa na kujulishwa juu ya neema alizoneemeshwa, kisha ataulizwa:

“Umezifanyia kazi gani neema hizi?”

Atasema:

“Sijaacha njia unayopenda mtu atoe katika mali yake ila mimi nimetoa kwa ajili yako.”

Ataambiwa:

“Umesema uongo, bali umetoa ili pasemwe kuwa wewe ni mkarimu na pashasemwa. Kisha pataamrishwa abururwe kwa uso wake na kuingizwa motoni”. 

 

 

Fadhila Za Kulinda Mipaka

 

Kwa kawaida panakuwa na upenyo katika mipaka baina ya ardhi ya Waislamu na ya makafiri, upenyo ambao adui anaweza kuutumia kwa ajili ya kujipenyeza na kuingia ndani ya ardhi ya Waislamu. Kwa hivyo ni wajibu kwa Waislamu kuzilinda vizuri sehemu hizo ili adui asiwezi kuzitumia na kuwashambulia kwa  urahisi.

 

Uislamu umetilia mkazo sana kuzilinda sehemu hizo na pia umetilia mkazo kuwatayarisha Waislamu ili wawe wapiganaji hodari, na kwa ajili hiyo kazi hii ya kulinda kwa ajili ya kupigana Jihaad katika njia ya Allaah ikapewa jina la (Al Ribaat), na uchache wake ni muda wa saa moja na ukamilifu wake ni siku arubaini, na fadhila nyingi sana zinapatikana katika kuzilinda sehemu zenye hatari zaidi.

 

Maulamaa wamekubaliana kuwa fadhila zake ni nyingi kupita fadhila za kuswali Msikiti wa Makkah.

 

Hadiyth zifuatazo zinatujulisha juu ya fadhila za jukumu hili:

 

Kutoka kwa Salmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa alimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akisema:

 

“Ribaat ya siku moja na usiku wake ni bora kuliko kufunga mwezi mzima na kusali usiku wake, na mtu akifa (akiwa katika jukumu hilo), amali zake zitaendelea kuandikwa na riziki yake ataendela kupata na atasalimika na fitna (za kaburi).”

Muslim

 

Na akasema:

 

“Kila maiti amali zake zinakatika ila aliyekufa akiwa analinda mipaka ili adui asiweze kuingia katika nchi ya Kiislamu (Muraabitan), kwa hakika huyu amali zake zinaendelea kuandikwa mpaka siku ya Kiama, na anaepushwa na mitihani ya kaburi.”

 

 

Fadhila Za Kurusha 'Ar-Ramyi'

 

Uislamu umetilia mkazo kujifunza kurusha (mkuki, mshale, kupiga risasi, mabomu nk.), na pia kujifunza fani mbali mbali za kupigana kwa nia ya Jihaad katika njia ya Allaah, na ukapendekeza pia kufanya mazoezi ya viungo na ya kutumia silaha kwa nia hiyo hiyo.

 

Kutoka kwa ‘Uqbah bin ‘Aamir (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

 

“Nilimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akiwa juu ya mimbari akisema:

 

وَأَعِدُّواْ لَهُم مَّا اسْتَطَعْتُم مِّن قُوَّةٍ

 

“Basi waandalieni (wawekeeni tayari) nguvu mnazoweza (silaha).” At-Tawbah: 60

 

‘Hakika nguvu ya kweli ni kurusha, hakika nguvu ya kweli ni kurusha, hakika nguvu ya kweli ni kurusha.”

Muslim

 

Na kutoka kwa ‘Uqbah (Radhiya Allaahu ‘anhu) pia alisema:

 

“Nilimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akisema:

“Mtawezeshwa kuziteka nchi nyingi, mmoja wenu asishindwe kuutumuia mshale wake (asijifunze kuutumia kwa ajili ya mchezo tu – bali kwa ajili ya kupigana Jihaad). Hakika Allaah huwaingiza Peponi watu watatu kwa mshale mmoja - aliyeutengeneza (kwa nia ya Jihaad), anayempa (anayekaa nyuma yake au pamoja naye na kumpa pale mishale inapomalizika), na mrushaji katika njia ya Allaah.”

 

Uislamu umeshadidia sana katika kuchukizwa na mtu anayejifunza kutumia upinde au silaha yoyote kisha akasahau namna ya kuitumia silaha hiyo bila udhuru unaokubalika kishari’ah.

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

 

“Atakayejifunza kutupa, kisha akasahau hayupo pamoja nasi.”

Na akasema:

“Mchezo wowote anaocheza mtu ni batil (yaani hapati thawabu ndani yake), isipokuwa (mchezo wa) upinde (na mshale), na kumzowesha farasi wake (pamoja na kumfundisha), na kucheza na watu wa nyumba yake (kwa kuzungumza na mkewe na kutaniana naye), hayo ni katika mambo ya haki (anayopata thawabu ndani yake).”

 

Anasema Al-Qurtubiy:

 

“Maana ya Hadiyth hii na Allaah ndiye ajuwae zaidi, ni kuwa; Kila mchezo unaopoteza wakati wa mtu usio na faida, hauna thawabu yoyote ndani yake, na kuachana nao ni bora zaidi, isipokuwa mambo matatu haya, juu ya kuwa ni mchezo, lakini yanampatia mtu thawabu kwa sababu ya faida inayopatikana ndani yake. Kwa sababu katika kutumia upinde na mshale na kumfundisha farasi mbinu mbali mbali za kivita, na mtu kuzungumza na kutaniana na mkewe kunaweza kumfanya awe mcha Mungu wa kweli. Na kwa ajili hii mambo matatu haya yakawa yanaweza kumpatia mtu thawabu.”

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alisema:

 

“Enyi wana wa Isma’iyl! rusheni (mishale) kwani baba yenu alikuwa mrushaji.”

 

Na kujifunza kupanda farasi na kutumia silaha ni katika fardhi kifaya inayoweza kuwa fardhi 'ayn.

 

 

 

Share

05-Jihaad: Wajibu Wa Viongozi Wa Jeshi

 

Wajibu Wa Viongozi Wa Jeshi

 

Yafuatayo ni mambo anayowajibika kuwa nayo kiongozi wa jeshi.

 

1.     Kushauriana na wenzake na kutaka rai zao, na asiwe akijiamulia bila kuwashauri, na hii inatokana na kauli ya Allaah Aliposema;

“Na shauriana nao katika mambo.”

Al-‘Imraan: 159

 

Na kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

“Sijapata kumuona mtu anayependa kutaka ushauri wa Maswahaba wake kupita Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).”

Imam Ahmad na Imam Ash-Shaafi’iy (Radhiya Allaahu ‘anhu).

 

2.     Upole na kuwarahisishia mambo. Anasema Mama ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha):

“Nilimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akisema:

“Yeyote atakayepewa uongozi wa umma wangu basi awe mpole juu yao, awe mpole juu yao.”

 

Na imepokelewa kutoka kwa Mu’aqal bin Yasar kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Hapana amiri yeyote aliyepewa uongozi juu ya Waislamu, kisha asijitahidi juu yao (katika kuwa mpole kwao na katika kuwatafutia manufaa) wala asiwanasihi, (kwa kuwaamrisha mema na kuwakataza mabaya) isipokuwa hatoingia Peponi.”

 

Na amesimulia Abu Daawuud kutoka kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akirudi nyuma katika misafara kwa ajili ya kuwasaidia walio dhaifu (kwa kuwashika mikono au kushika hatamu za wanyama wao na kuwatanguliza mbele ili wawe pamoja na wenzao), na kuwapakia juu ya ngamia (wake na wa wengine wendao kwa miguu).”

 

3.     Kuamrisha mema na kukataza maovu ili watu waepukane na kumuasi Allaah.

 

4.     Kulikagua jeshi mara kwa mara apate kuwajuwa vizuri askari wake, na kuwajuwa wale wanaowavunja moyo wenzao wasitake kwenda vitani, na wale wanaosababisha choko choko katika jeshi, kwa kusema kwa mfano; ‘hatuna silaha za kutosha wala nguvu za kutosha.’ Na pia apate kuwajuwa wale wanaotoa siri za jeshi.

 

5.     Kupashana habari na viongozi.

 

6.     Kuchaguwa sehemu zinazofaa kwa ajili ya kupiga kambi.

 

7.     Kutuma wapelelezi kwa ajili ya kujuwa hali za adui.

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa anapotaka kushambulia mahali akiwababaisha adui kwa kuwajulisha kama kwamba anataka kushambulia mahali pengine.

Alikuwa pia akiwatuma wapelelezi wamletee habari za adui, na alikuwa akilipanga vizuri jeshi lake.

 

Amesema Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu):

“Bendera ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ilikuwa nyeusi na ya jeshi ilikuwa nyeupe.”

Abu Daawuud

 

 

 

Usia Kwa Viongozi

 

Kutoka kwa Abu Muusa (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa anapompa uongozi yeyote katika Maswahaba wake katika baadhi ya mambo alikuwa akimwambia:

“Wapeni watu bishara njema (juu ya rehma ya Allaah na kusamehe kwake) wala miswape habari za kuwachukiza (kwa kuwatisha na kuwaogopesha), na mambo muyafanye (yawe) mepesi, msiyafanye (yakawa) magumu.”

 

Na pia kutoka kwa Abu Muusa (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

“Alinituma Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) mimi na Muadh kwenda Yemen akasema:

“Wepesisheni mambo wala msifanye yakawa magumu, wapeni watu bishara njema wala miswape habari za kuwachukiza, wahiyarisheni, na msikhitilafiane.”

Al-Bukhaariy na Muslim

 

Kutoka kwa Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Nendeni kwa jina la Allaah, na kwa ajili ya Allaah, na kwa kufuata mwenendo wa Mtume wa Allaah, wala msimuuwe mzee mkongwe, wala mtoto mdogo, wala mwanamke (ila kama ni mwanajeshi), wala msiendeane kinyume katika ngawira, na mchange pamoja ngawira zenu, na mtengeneze na mfanye mema kwa sababu Allaah anawapenda watendao mema.”

Abu Daawuud

 

 

Usia wa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu)

 

‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimwandikia Sa’ad bin Abi Waqaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) na askari wake wengine akiwausia yafuatayo;:

“Amma baad - Mimi nakuamrisha wewe pamoja na askari ulio nao kumcha Allaah katika kila jambo, kwa sababu kumcha Mungu ni silaha bora kupita zote mbele ya adui, na ni mbinu yenye nguvu kupita zote kati vita. Na nakuamrisha wewe pamoja na ulio nao mchunge msije kufanya maasi kuliko mnavyomchunga adui yenu, kwa sababu madhambi ya wanajeshi yana hatari zaidi juu yao kupita adui wao. Kwa hakika Allaah huwapa ushindi Waislamu kwa sababu maadui ni watu wenye kumuasi Allaah, ama sivyo sisi hatuna nguvu za kuwashinda, kwa sababu idadi yao ni kubwa kuliko idadi yetu, na silaha zao ni kali kupita silaha zetu. Kwa hivyo tukiwa sawa nao katika kufanya maasi, basi wao watatushinda kwa nguvu zao, kwa sababu tunapewa ushindi kutokana na fadhila zetu na si kwa nguvu zetu.

Na mjuwe kuwa katika msafara wenu mna (Malaika) wenye kuhifadhi wanaojuwa kila mnalotenda, kwa hivyo muwaonee haya, na msiwe wenye kumuasi Allaah mkiwa katika njia ya Allaah, na wala msiseme kuwa; ‘Kwa vile adui wetu wana shari kupita sisi kwa hivyo hawataweza kupewa ushindi juu yetu,’ kwani huenda watu wakasalatishiwa (wakapelekewa) na kushindwa na adui aliye mbaya kupita wao kama pale Bani Israil walipomuasi Allaah akawapelekea Majusi (wanaoabudi moto) wakaingia mijini mwao kila upande, ikawa ahadi iliyoyotimizwa.

Muombeni Allaah akusaidieni katika nafsi zenu kama mnavyomuomba akupeni ushindi juu ya adui yenu, namuomba Allaah anipe mimi na nyinyi yote hayo.

Na kuweni wapole kwa Waislamu katika mwenendo wao wala msiwakalifishe mambo mazito yatakayowataabisha.”

 

 

 

Du’aa Wakati Wa Mapambano

 

Mpigana Jihaad anatakiwa amuombe Allaah ampe ushindi kwa sababu ushindi umo mikononi mwake Subhanahu wa Taala, na huu ndio uliokuwa mwenendo wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na mwenendo wa Masahaba baada yake (Radhiya Allaahu ‘‘anhum).

Kutoka kwa Abu Daawuud kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Mawili hayarudi patupu; Dua baada ya muadhini, na (du’aa) katika vita pale wapiganaji wanapovamiana.”

 

Allaah Amesema:

 

إِذْ تَسْتَغِيثُونَ رَبَّكُمْ فَاسْتَجَابَ لَكُمْ

“(Kumbukeni) mlipokuwa mkiomba msaada kwa Mola wenu, naye akakujibuni.”

Al-Anfaal: 9

 

Imepokelewa kutoka kwa (Maimamu) watatu (wa elimu ya hadithi) kutoka kwa ‘Abdullaah bin Abi ‘Aufiy kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) katika siku mojawapo alipokuwa akiwasubiri maadui, alisubiri mpaka wakati wa zawal (kidogo baada ya adhuhuri), kisha akasimama kuwahutubia watu akasema:

“Enyi watu! Msitamani kukutana na adui, na muombeni Allaah usalama, na mtakapokutana naye (adui) basi muwe wenye subira (wavumilivu) na jueni kuwa Pepo ipo chini ya vivuli vya panga.”

 

Kisha akasema:

“Mola wangu uliyekiteremsha kitabu, mwenye kuyasukuma mawingu, uliyewashinda makundi (katika vita vya Ahzaab), washinde na utupe ushindi juu yao.”

 

Na katika du’aa zake wakati wa vita (alikuwa akisema):

“Mola wangu wewe ndiye msaidizi wangu na unipaye ushindi, kwako naelekea na nategemea na kwa ajili yako napigana vita.”

Imepokelewa na Maimaam wa Ahlus-Sunnah

 

 

 

Kupigana Jihaad

 

Dini ya Kiislamu inawaita watu katika uongofu utokao kwa Allaah ili wafaidike na uongofu huo na ili wapate maisha mema ya hapa duniani na ya kesho Akhera.

 

Kwa ajili hiyo Allaah Ameupa Umma wa Kiislamu jukumu la kuinyanyua dini yake, na kuwafikishia watu wahyi wake kwa ajili ya kuuongoza na kuukomboa ulimwengu.

 

Na kwa ajili hii ndiyo umma huu ukawa umma bora kupita umma zote zilizodhihirishiwa watu, na ukawa mbele ya watu wengine ukiongoza mfano wa mwalimu na wanafunzi wake, na kwa ajili hiyo lazima uwe na uwezo wa kujihifadhi na wa kujidumisha, na pia uwezo wa kupambana kwa ajili ya kujipatia haki yake na ili uweze kuchukuwa nafasi yake iliyowekewa na Allaah.

Na kila mwenye kupunguza asitimize wajibu wake katika kujipatia haki yake hiyo, basi anahesabiwa kuwa amefanya makosa makubwa ambayo Allaah humdhalilisha kwayo au kumfutilia mbali.

Uislamu umekataza ulegevu na kutaka amani (kwa makafiri) ikiwa lengo halijafikiwa, kwa sababu kutaka amani katika wakati kama huu haitokuwa na maana yoyote wala tafsiri nyingine isipokuwa ni uoga na kuridhika kuishi kama watu duni.

 

Katika haya Allaah Anasema:

 

فَلا تَهِنُوا وَتَدْعُوا إِلَى السَّلْمِ وَأَنتُمُ الاَعْلَوْنَ وَاللَّهُ مَعَكُمْ وَلَن يَتِرَكُمْ أَعْمَالَكُمْ

“Basi msiregee na kutaka suluhu (piganeni nao maadui zenu) maana nyinyi ndio mtakaoshinda; na Allaah yu pamoja nanyi; wala hatakunyimeni (thawabu za) vitendo vyenu.”

Muhammad: 35

 

Na maana ya neno ‘mtakaoshinda’ maana yake ni kuwashinda na kuwa juu yao katika itikadi, ibada, mwenendo na tabia njema, elimu, na matendo.

Amani ya kweli haipatikani bila ya nguvu na uwezo wa kupigana vita, na hii ndiyo sababu Allaah akaweka sharti kuwa lazima adui aache kuwapiga vita waislamu na kuwafanyia uadui ili dhulma ipate kutoweka juu ya ardhi na ili mtu asiteswe kwa ajili ya dini yake.

Likiwepo mojawapo katika sababu hizo, basi Allaah ametoa idhini ya kupigana vita. (yaani ikiwa waislamu wanapigwa vita au wanadhulimiwa au wanafanyiwa uadui au wanateswa kwa ajili ya itikadi yao basi wanaruhusiwa kupigana vita).

Hapana dini yoyote iliyowapa idhini watu wake kuingia katika mapambano na kupigana vita kwa ajili ya kuisimamisha haki na kwa ajili ya kuwasaidia wanaodhulumiwa na kwa ajli ya kuishi maisha ya kuheshimika isipokuwa dini ya Kiislamu.

Kwa atakayefuatilia aya mbali mbali za Qur-aan tukufu pamoja na maisha ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na ya makhalifa wake (Radhiya Allaahu ‘anhu) atayaona yote hayo kwa uwazi kabisa, kwani Allaah Subhanahu wa Taala anautaka umma huu kutumia nguvu zake zote katika kuyatimiza hayo.

 

Allaah Anasema:

 

وَجَاهِدُوا فِي اللَّهِ حَقَّ جِهَادِهِ

“Na ipiganieni dini ya Allaah kama inavyostahiki (kupiganiwa).”

Al-Hajj: 78

 

Kisha Allaah Subhanahu wa Taala ِAkabainisha kuwa Jihaad ni Imani ya matendo, ambayo bila ya hiyo dini haikamiliki, Akasema:

 

أَحَسِبَ النَّاسُ أَن يُتْرَكُوا أَن يَقُولُوا آمَنَّا وَهُمْ لا يُفْتَنُونَ. وَلَقَدْ فَتَنَّا الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَلَيَعْلَمَنَّ اللَّهُ الَّذِينَ صَدَقُوا وَلَيَعْلَمَنَّ الْكَاذِبِينَ

“Je! Wanadhani watu wataachwa kwa kuwa wanasema: Tumeamini. Nao wasijaribiwe?

Hakika tuliwajaribu walio kuwa kabla yao, na kwa yakini Allaah Atawatambulisha walio wa kweli na atawatambulisha walio waongo.”

Al-‘Ankabuut: 2-3

 

Kisha Akabainisha kuwa hii ndiyo njia aliyowaekea waumini, na kwamba hapana njia nyingine itakayowaletea ushindi na kuwaingiza Peponi, Akasema:

 

أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُواْ الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَأْتِكُم مَّثَلُ الَّذِينَ خَلَوْاْ مِن قَبْلِكُم مَّسَّتْهُمُ الْبَأْسَاء وَالضَّرَّاء وَزُلْزِلُواْ حَتَّى يَقُولَ الرَّسُولُ وَالَّذِينَ آمَنُواْ مَعَهُ مَتَى نَصْرُ اللّهِ أَلا إِنَّ نَصْرَ اللّهِ قَرِيبٌ

“Mnadhani kuwa mtaingia Peponi, bila ya kukujieni kama yaliyo wajia wale walio pita kabla yenu? Iliwapata shida na madhara na wakatikiswa hata Mtume na walio amini pamoja naye wakasema: Lini nusura ya Allaah itakuja? Jueni kuwa nusura ya Allaah ipo karibu.

Al-Baqarah: 214

 

Akawataka Waislamu kujitayarisha vizuri na akawataka pia wawe wenye kutisha mbele ya makafiri, Akasema:

 

وَأَعِدُّواْ لَهُم مَّا اسْتَطَعْتُم مِّن قُوَّةٍ وَمِن رِّبَاطِ الْخَيْلِ تُرْهِبُونَ بِهِ عَدْوَّ اللّهِ وَعَدُوَّكُمْ وَآخَرِينَ مِن دُونِهِمْ لاَ تَعْلَمُونَهُمُ اللّهُ يَعْلَمُهُمْ وَمَا تُنفِقُواْ مِن شَيْءٍ فِي سَبِيلِ اللّهِ يُوَفَّ إِلَيْكُمْ وَأَنتُمْ لاَ تُظْلَمُونَ

“Basi waandalieni nguvu kama muwezavyo, na kwa farasi waliofungwa tayari-tayari, ili kuwatishia maadui wa Allaah na maadui zenu, na wengineo ambao hamwajui, lakini Allaah Anawajua. Na mkitoa chochote katika Njia ya Allaah mtarudishiwa, na wala nyinyi hamtadhulumiwa”.

Al-Anfaal: 60

 

Na namna ya kujitayarisha inategemea wakati na hali ya mambo, na neno ‘nguvu’, maana yake ni kutumia kila njia inayowezekana kutumika kwa ajili ya kumuondoa adui.

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

‘Hakika nguvu ya kweli ni kurusha, hakika nguvu ya kweli ni kurusha, hakika nguvu ya kweli ni kurusha.”

Muslim

 

Na katika kujitayarisha ni kuchukua hadhari na kumuandaa kila mwenye uwezo.

Allaah Anasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ خُذُواْ حِذْرَكُمْ فَانفِرُواْ ثُبَاتٍ أَوِ انفِرُواْ جَمِيعًا

“Enyi mlioamini! Chukueni hadhari yenu! Na mtoke kwa vikosi au tokeni nyote pamoja!

An-Nisaa: 71

 

Na kuchukuwa hadhari hakukamiliki ila kwa kujitayarisha na majeshi yanayoweza kupigana ardhini na baharini na angani.

Allaah akatuamrisha kupambana na adui tukiwa katika hali yoyote ile, iwe ya dhiki au katika neema, nzuri au mbaya, Akasema:

 

انْفِرُواْ خِفَافًا وَثِقَالاً وَجَاهِدُواْ بِأَمْوَالِكُمْ وَأَنفُسِكُمْ فِي سَبِيلِ اللّهِ ذَلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ

“Nendeni mtoke, mkiwa wepesi na wazito, na piganeni Jihaad kwa mali yenu na nafsi zenu katika njia ya Allaah. Haya ni kheri kwenu mkiwa mnajua.”

At-Tawbah: 41

 

Uislamu unategemea zaidi nguvu ya imani kuliko nguvu ya silaha na kwa ajili hiyo unatilia nguvu zaidi mambo ya kiroho na kuiamsha hima na azma ya mpiganaji.

 

Allaah Anasema:

 

فَلْيُقَاتِلْ فِي سَبِيلِ اللّهِ الَّذِينَ يَشْرُونَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا بِالآخِرَةِ وَمَن يُقَاتِلْ فِي سَبِيلِ اللّهِ فَيُقْتَلْ أَو يَغْلِبْ فَسَوْفَ نُؤْتِيهِ أَجْرًا عَظِيمًا. وَمَا لَكُمْ لاَ تُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللّهِ وَالْمُسْتَضْعَفِينَ مِنَ الرِّجَالِ وَالنِّسَاء وَالْوِلْدَانِ الَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا أَخْرِجْنَا مِنْ هَـذِهِ الْقَرْيَةِ الظَّالِمِ أَهْلُهَا وَاجْعَل لَّنَا مِن لَّدُنكَ وَلِيًّا وَاجْعَل لَّنَا مِن لَّدُنكَ نَصِيرًا

“Basi nawapigane katika Njia ya Allaah wale ambao wanaouza uhai wa dunia kwa Akhera. Na anaye pigana katika Njia ya Allaah kisha akauliwa au akashinda basi tutakuja mpa ujira mkubwa.

Na mna nini msipigane katika Njia ya Allaah na ya wale wanao onewa, wanaume na wanawake na watoto, ambao husema: Mola Mlezi wetu! Tutoe katika mji huu ambao watu wake ni madhaalimu, na tujaalie tuwe na mlinzi anaye toka kwako, na tujaalie tuwe na wa kutunusuru anaye toka kwako?”

An-Nisaa: 75-76

 

Na Muislamu anatakiwa awe na subira, kwani kama yeye avyoumia basi adui naye pia anaumia, tena yeye anaumia zaidi kupita wao, na hii ni kwa sababu ya hitilafu kubwa ya malengo yao.

Allaah ِAnasema:

 

وَلاَ تَهِنُواْ فِي ابْتِغَاء الْقَوْمِ إِن تَكُونُواْ تَأْلَمُونَ فَإِنَّهُمْ يَأْلَمُونَ كَمَا تَأْلَمونَ وَتَرْجُونَ مِنَ اللّهِ مَا لاَ يَرْجُونَ

“Wala msifanye uvivu kuwafuatia watu (walio maadui). Kama mmepata maumivu basi wao pia wanapata maumivu kama mnavyoumia. Na nyinyi mnatumai kwa Allaah wasiyoyatumai.”

An-Nisaa: 105

 

Na Akasema:

 

الَّذِينَ آمَنُواْ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللّهِ وَالَّذِينَ كَفَرُواْ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ الطَّاغُوتِ فَقَاتِلُواْ أَوْلِيَاء الشَّيْطَانِ إِنَّ كَيْدَ الشَّيْطَانِ كَانَ ضَعِيفًا

“Walioamini wanapigana katika Njia ya Allaah, na waliokufuru wanapigana katika njia ya upotofu. Basi piganeni na marafiki wa Shetani. Hakika hila za Shetani ni dhaifu.”

An-Nisaa: 76

 

Na maana yake ni kuwa; lengo la Waislamu ni tukufu, na ujumbe wao wanaotaka kuufikisha kwa watu ambao kwa ajili yake wanapigana Jihaad, ambayo ni risala ya haki na ya kheri, nayo ni kulinyanyua juu neno la Allaah ni tukufu pia.

 

Na Muislamu anatakiwa awe mwenye nyoyo thabiti kwenye mapambano.

Allaah Aanasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ إِذَا لَقِيتُمُ الَّذِينَ كَفَرُواْ زَحْفاً فَلاَ تُوَلُّوهُمُ الأَدْبَارَ 15 وَمَن يُوَلِّهِمْ يَوْمَئِذٍ دُبُرَهُ إِلاَّ مُتَحَرِّفاً لِّقِتَالٍ أَوْ مُتَحَيِّزاً إِلَى فِئَةٍ فَقَدْ بَاء بِغَضَبٍ مِّنَ اللّهِ وَمَأْوَاهُ جَهَنَّمُ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ

“Enyi Mlioamini! Mkikutana na walio kufuru vitani msiwageuzie mgongo.

Na atakaye wageuzia mgongo wake siku hiyo - isipo kuwa kwa mbinu za vita au kuungana na kikosi, basi atakuwa amestahiki ghadhabu ya Allaah. Na pahala pake ni Jahannamu, na huo ni mwisho muovu.”

Al-Anfaal: 15-16

 

Kisha Akawajulisha juu ya mahali ilipo nguvu zao za imani Aliposema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ إِذَا لَقِيتُمْ فِئَةً فَاثْبُتُواْ وَاذْكُرُواْ اللّهَ كَثِيرًا لَّعَلَّكُمْ تُفْلَحُونَ. وَأَطِيعُواْ اللّهَ وَرَسُولَهُ وَلاَ تَنَازَعُواْ فَتَفْشَلُواْ وَتَذْهَبَ رِيحُكُمْ وَاصْبِرُواْ إِنَّ اللّهَ مَعَ الصَّابِرِينَ

“Enyi mlioamini! Mkikutana na jeshi, basi kueni imara, na mkumbukeni Allaah sana ili mpate kufanikiwa.

Na mt'iini Allaah na Mtume wake, wala msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu. Na subirini. Hakika Allaah yu pamoja na wanao subiri”

Al-Anfaal: 45-46

 

Kisha Akatujulisha juu ya nafsi ya Muislamu, na kwamba lazima waipigane kwa juhudi zao zote, kwa sababu hawana isipokuwa hiari mbili tu, ama wauwe au wauliwe, Akasema:

 

إِنَّ اللّهَ اشْتَرَى مِنَ الْمُؤْمِنِينَ أَنفُسَهُمْ وَأَمْوَالَهُم بِأَنَّ لَهُمُ الجَنَّةَ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللّهِ فَيَقْتُلُونَ وَيُقْتَلُونَ وَعْدًا عَلَيْهِ حَقًّا فِي التَّوْرَاةِ وَالإِنجِيلِ وَالْقُرْآنِ وَمَنْ أَوْفَى بِعَهْدِهِ مِنَ اللّهِ فَاسْتَبْشِرُواْ بِبَيْعِكُمُ الَّذِي بَايَعْتُم بِهِ وَذَلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

 “Hakika Allaah Amenunua kwa Waumini nafsi zao na mali zao kwa kuwa wao watapata Pepo. Wanapigana katika Njia ya Allaah - wanauwa na wanauwawa. Hii ni ahadi aliyojilazimisha kwa Haki katika Taurati na Injili na Qur'ani. Na nani atimizae ahadi kuliko Allaah? Basi furahini kwa biashara yenu mliyo fanya naye. Na huko ndiko kufuzu kukubwa.

At-Tawbah: 111

 

Akiuwa atapata ushindi, na akiuliwa atakuwa amekufa shahidi na ataingia Peponi.

 

Allaah Anasema:

 

قُلْ هَلْ تَرَبَّصُونَ بِنَا إِلاَّ إِحْدَى الْحُسْنَيَيْنِ

 “Sema; ‘Nyini hamtutazamii sisi ila (kupata) moja katika mema mawili (ima kushinda au kuuawa mkapata Pepo).”

At-Tawbah: 52

 

Anayeuliwa katika Jihaad kwa ajili ya kulinyanyua neno la Allaah hafi akatoweka kama wanavyokufa watu wa kawaida, bali wao wananyanyuliwa na kupelekwa mahali pema zaidi na bora zaidi. Kwa hivyo kufa katika njia ya Allaah maana yake hasa ni kubaki.

Allaah Anasema:

 

وَلاَ تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ قُتِلُواْ فِي سَبِيلِ اللّهِ أَمْوَاتًا بَلْ أَحْيَاء عِندَ رَبِّهِمْ يُرْزَقُونَ. فَرِحِينَ بِمَا آتَاهُمُ اللّهُ مِن فَضْلِهِ وَيَسْتَبْشِرُونَ بِالَّذِينَ لَمْ يَلْحَقُواْ بِهِم مِّنْ خَلْفِهِمْ أَلاَّ خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلاَ هُمْ يَحْزَنُونَ. يَسْتَبْشِرُونَ بِنِعْمَةٍ مِّنَ اللّهِ وَفَضْلٍ وَأَنَّ اللّهَ لاَ يُضِيعُ أَجْرَ الْمُؤْمِنِي

“Wala kabisa usiwadhanie waliouliwa katika Njia ya Allaah kuwa ni maiti. Bali hao ni wahai, wanaruzukiwa kwa Mola wao Mlezi.

Wanafurahia aliyo wapa Allaah kwa fadhila yake, na wanawashangilia wale ambao bado hawajajiunga nao, walio nyuma yao, ya kwamba haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika.

Wanashangilia neema na fadhila za Allaah, na ya kwamba Allaah hapotezi ujira wa Waumini."

Al-‘Imraan: 169-171

 

Allaah siku zote huwa pamoja na wanaopigana Jihaad na wala hawaachi mkono.

Allaah Anasema:

 

إِذْ يُوحِي رَبُّكَ إِلَى الْمَلآئِكَةِ أَنِّي مَعَكُمْ فَثَبِّتُواْ الَّذِينَ آمَنُواْ سَأُلْقِي فِي قُلُوبِ الَّذِينَ كَفَرُواْ الرَّعْبَ فَاضْرِبُواْ فَوْقَ الأَعْنَاقِ وَاضْرِبُواْ مِنْهُمْ كُلَّ بَنَانٍ

“Mola wako Mlezi alipowafunulia Malaika: Hakika Mimi ni pamoja nanyi, basi watieni nguvu walio amini. Nitatia woga katika nyoyo za walio kufuru. Basi wapigeni juu ya shingo na wapigeni kwenye kila ncha za vidole.”

Al-Anfaal: 12

 

Kisha Allaah Anawatayarishia malipo mema hapa duniani na pia malipo mema huko Akhera.

 

Allaah Anasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا هَلْ أَدُلُّكُمْ عَلَى تِجَارَةٍ تُنجِيكُم مِّنْ عَذَابٍ أَلِيمٍ. تُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ وَتُجَاهِدُونَ فِي سَبِيلِ اللَّهِ بِأَمْوَالِكُمْ وَأَنفُسِكُمْ ذَلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ. يَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَيُدْخِلْكُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ وَمَسَاكِنَ طَيِّبَةً فِي جَنَّاتِ عَدْنٍ ذَلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ. وَأُخْرَى تُحِبُّونَهَا نَصْرٌ مِّنَ اللَّهِ وَفَتْحٌ قَرِيبٌ وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ

“Enyi mlioamini! Nikuonyesheni biashara itakayo kuokoeni na adhabu iliyo chungu?

Muaminini Allaah na Mtume wake, na piganeni Jihaad katika Njia ya Allaah kwa mali yenu na nafsi zenu. Haya ni bora kwenu, ikiwa nyinyi mnajua.

Atakusameheni dhambi zenu, na atakutieni katika Mabustani yapitiwayo na mito kati yake, na maskani nzuri nzuri katika Bustani za milele. Huko ndio kufuzu kukubwa.

Na kinginecho mkipendacho, nacho ni nusura itokayo kwa Allaah, na ushindi ulio karibu! Na wabashirieni Waumini!”

Asw-Swaff: 10 – 13

 

Kwa njia hii dini ya Kiislamu iliwalea waliotangulia na ikaweza kuingiza ndani ya nafsi zao imani iliyowawezesha kupambanua baina ya haki na batili na kuwawezesha kupata ushindi na kuziteka nchi na iliwawezesha kuwamakinisha vizuri juu ya ardhi.

Allaah ِِِAnasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تَنصُرُوا اللَّهَ يَنصُرْكُمْ وَيُثَبِّتْ أَقْدَامَكُمْ

“Enyi mlioamini! Mkimnusuru Allaah naye Atakunusuruni na Ataithibitisha miguu yenu.”

Muhammad: 7

 

Na ِAnasema:

 

وَعَدَ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُم فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَى لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُم مِّن بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْنًا يَعْبُدُونَنِي لَا يُشْرِكُونَ بِي شَيْئًا وَمَن كَفَرَ بَعْدَ ذَلِكَ فَأُوْلَئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ

“Allaah Amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyo wafanya makhalifa wa kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia Dini yao aliyo wapendelea, na atawabadilishia amani baada ya khofu yao. Wawe wananiabudu Mimi, wala wasinishirikishe na chochote. Na wataokufuru baada ya hayo, basi hao ndio wapotovu.”

An-Nuur: 55

 

 

 

Share

06-Jihaad: Simba (Mmarekani) Na Chui (Umoja Wa Mataifa)

Simba na Chui

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Mtakapouziana kwa riba, mkajishughulisha na biashara, mkaridhika na kilimo, na mkaiacha jihadi (wakati wenzenu wanauliwa), Allaah atakuteremshieni udhalilifu mtakaoshindwa kuuondoa mpaka (pale) mtakaporudi katika dini yenu.” (Abu Daawuud na Imam Ahmad)

 

Na imetolewa na Muslim na Abu Daawuud na An-Nasaaiy na Al-Haakim na Al-Bayhaqiy kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) pia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Atakayekufa bila kupigana (jihadi) na wala (hata) kumpitikia moyoni mwake (nia ya kupigana) jihadi, (akifa) anakufa akiwa na sehemu ya unafiki.”

   

Waislamu ni umma uliochaguliwa na Allaah kwa ajili ya kuuongoza ulimwengu na walimwengu na kulinyanyua juu neno la Allaah, lakini Waislamu leo wamekuwa watu dhalili kupita umma zote zinazotembea juu ya ardhi. Kila anayetaka kuzifanyia silaha zake majaribio au kujipima nguvu, anazielekeza silaha hizo na nguvu hizo kwa Waislamu. Tumeyaona hayo yakitokea sehemu mbali mbali ulimwenguni, zikiwemo Bosnia, India, Afghanistan, Palastina na sasa Iraq, na hivi karibuni Gaza (Palestina).

 

Kote huko na katika sehemu mbali mbali ulimwenguni Waislamu wanadhalilishwa, wanauliwa, watoto kwa wakubwa, wanawake kwa wanaume, na majumba yao yanabomolewa mbele ya kamera za television na mbele ya macho ya kila mtu, bila watu kujali wala hata nyoyo kusituka. Kisha Waislamu hao hao eti wanakimbilia kupeleka mashitaka yao Umoja wa Mataifa wakitegemea kupata msaada, wakati wote hao (Marekani, Mayahudi na Umoja wa Mataifa) ni kitu kimoja.

 

Na hii inanikumbusha kile kisa cha chui na kima:

Inasemekana kuwa chui alikuwa akipenda kumuonea kima na kumpiga bila sababu yoyote, na kila anapomuona alikuwa akitafuta kisingizio chochote cha kumpiga makofi ya uso kima yule.

Alikuwa mara nyingine akimwambia;

“Kofia yako iko wapi! Mbona leo hujavaa kofia, si nilikwambia lazima uivae? Kesho lazima nikuone nayo,” humwambia hivyo huku akimtandika makofi na mateke.

Siku ya pili kima anapokuja akiwa amevaa kofia, chui yule yule humvamia na humpiga makofi huku akimwambia:

“Kwa nini umevaa kofia! Si nilikwambia usiivae?”  akiivaa anapigwa na asipoivaa anapigwa.

Hali ikaendelea hivyo mpaka siku ile kima alipochoka kuonewa, akaamua kumshitaki chui kwa mfalme simba bila kujuwa masikini kuwa simba na chui wote ni kitu kimoja.

Mfalme simba akamwita chui pembeni na kumwambia kwa kumnong'oneza:

“Wewe vipi ndugu yangu! unampiga mwenzio bila kumtafutia kisingizio kinachokubalika? Tizama mimi kwa mfano; ninapotaka kumpiga punda nafanya nini? Humtuma aniletee matufaha, na yeye bila kuniuliza hukimbia na kuniletea matufaha mekundu, mimi hapo humtandika makofi na kumwambia:

“Nani aliyekuaambia uniletee matufaha mekundu?”

Hapo yeye hukimbia na kurudi haraka akiwa ameniletea matufaha ya kijani, na hapo namtandika tena makofi na kumwambia:

“Nani aliyekwambia uniletee matufaha ya kijani?” na kwa njia hii namtandika makofi kwa raha zangu.”

Chui akaona kuwa hii ni fikra nzuri, akaondoka na kwenda moja kwa moja mpaka kwa kima akamwambia:

“Nenda kaniletee matufaha sasa hivi, tena mbiyo!”

Lakini kima anakhitalifiana na punda, kima alimuuliza chui:

“Unata nikuletee matufaha rangi gani? Mekundu au kijani au manjano?

Chui kuona ameshindwa hila akarudia pale pale:

“Mbona leo hujavaa kofia eh?”, Ngumi! Teke!

 

Na hii ndiyo hali yetu Waislamu baada ya kuyaacha mafundisho ya dini yetu, na kuiacha jihadi na kuyakimbilia maisha ya dunia, Allaah Ametusalitishia udhalili ikawa kila safihi anapotaka kujipima nguvu zake anakuja kututandika sisi ngumi na makofi yake, na sisi tunakimbilia kwa mfalme Simba (Mmarekani) au kwa chui (Umoja wa Mataifa) na kumbe wote hao ni kitu kimoja waliokwishaamua kumpiga vita kila anayetaka kuisimamisha bendera ya Laa ilaaha illa Allaah.

 

Tunamuomba Allaah Atusimamishie kiongozi wa kheri, awe katika utawala wake kiongozi huyo anaheshimiwa kila mwenye kumuogopa Allaah, na anadhalilishwa kila mwenye kumuasi Allaah. Awaunganishe umma chini ya bendera ya Laa ilaaha illa Allaah na kuihuisha Jihadi ambayo kwayo pekee umma huu utarudisha heshima yake - Aamiyn.

 

 

Al-Wahn

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

"Hivi karibuni mtakuja zungukwa na mataifa, mfano wa walaji wanavyokizunguka chakula chao (wanavyokaa kuizunguka sinia ya chakula)." Tukasema: "Kwa sababu ya uchache wetu ewe Mtume wa Allaah siku hiyo?" Akasema: "Hapana, nyinyi siku hiyo mtakuwa wengi, lakini mtakuwa (mumegawanyika) muko mbali mbali mfano wa takataka zinazokumbwa na maji ya mvua. Allaah Ataondoa haiba yenu kutoka katika vifua vya adui yenu, na ataingiza ndani ya nyoyo zenu Al-Wahan (udhaifu)." Mmoja akauliza: "Ewe Mtume wa Allaah, ni kitu gani hiki Al-Wahan?" Akasema: "Kuipenda kwenu dunia na kuyachukia mauti." (Imam Ahmad katika Musnad yake)

 

Hadithi hii ni muujiza katika miujiza ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) juu ya hali yetu hivi sasa. Kama kwamba alipokuwa amekaa pale Msikitini kwake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akihadithia hadithi hii, alikuwa akiiona hali yetu hivi sasa kama tulivyo.

 

Maadui wa Waislamu wanatutuhumu kuwa tunaongezeka kwa wingi, na wanazihadaa serikali zetu zikubali kutupa dawa za kuzuia uzazi. Hii ina maana kuwa idadi yetu inaongezeka, lakini juu ya wingi wetu, hatuna maana yoyote. Hatuna faida yoyote. Maadui wa Allaah wanatuuwa, wanatudhalilisha, wanatutenganisha, wanatugawa, wanatugombanisha, na sisi hatuna la kufanya, bali hatuwezi kufanya kitu. Wanatusukuma wanapotaka, na wanatuendesha wanavyotaka. Tumekuwa mfano wa takataka zinazokumbwa na kusukumwa na maji ya mvua huku na kule.

 

Na muujiza mwingine uliomo ndani ya hadithi hii ni kule kuungana dhidi yetu kwa mataifa yote. Wamarekani, wazungu wa Ulaya, Mayahudi, Wajapani na maadui wa Allaah walioko Magharibi na Mashariki ya ulimwengu, wote wamejikusanya na kutuzunguka, mfano wa walaji wanavyokizunguka chakula chao. Wote wamekula kiapo kuupiga vita Uislamu. Wakati huo huo sisi tumo katika starehe zetu, kama kwamba hapana kinachotokea. Kila mmoja anakiogopea kiti chake, anaiogopea mali yake, anauogopea mustakbali wake, anaiogopea nafsi yake. Tunaipenda dunia na tunayachukia mauti.

 

Tunafaidika na hadithi hii pia ile balagha, ule ubingwa wa kutumia lugha uliotumika katika kuwaelezea maadui wa Allaah, pale (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliposema: "mfano wa walaji wanavyokizunguka chakula chao." Na hii inatuonyesha njaa waliyonayo maadui hawa, na tamaa yao kubwa juu ya mali za Waislamu na utajiri wao. Wanakuja kwa nguvu zao zote na kwa ujabaruti na ujeuri mkubwa na kibri huku wakiwasaidia Mayahudi kwa nguvu zao zote ili waweze kuzinyakua mali hizo na uchumi huo na ardhi.

 

Na muujiza mwengine ni kule kufanya kwao wanavyotaka bila kujali masikitiko yetu wala huzuni zetu wala lawama zetu wala hata vilio vyetu. Wanafanya wanavyotaka. Wanapiga wanavyotaka, wanabomoa wanavyotaka, kama kwamba ardhi yote na Waislamu wote ni milki yao. "Mfano wa walaji wanavyokizunguka chakula chao."

 

Hata Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) walishangazwa waliposkia, wakauliza:

"Kwa sababu ya uchache wetu ewe Mtume wa Allaah siku hiyo?" Walishangaa vipi tutakuwa katika hali hii, vipi maadui wataweza kutupiga wakati idadi yetu ni kubwa kupita yao. Bila shaka tutakuwa wachache wakati huo. Lakini Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akawaambia: "Hapana, (bali) nyinyi siku hiyo mtakuwa wengi, lakini mtakuwa mumefarakana mfano wa takataka zinazokumbwa na maji ya mvua."

 

Izingatie vizuri kauli ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliposema "nyinyi siku hiyo mtakuwa wengi", na hii maana yake ni kuwa mwili wa Waislamu ni mwili mmoja. Tokea wakati ule mpaka wakati huu, sisi sote ni kitu kimoja.

 

"مثل المؤمنين في توادهم وتراحمهم كمثل الجسد الواحد إذا اشتكى منه عضو تداعى له سائر الجسد بالحمى والسهر"

 

Mfano wa Waislamu katika kupendana kwao na kuhurumiana kwao ni mfano wa mwili mmoja, kinapoumia kiungo kimoja basi viungo vyote vilivyobaki vinashirikiana (nacho kiungo hicho) kwa homa na kukesha. (Al-Bukhaariy na Muslim)

 

Hivi ndivyo alivyotufundisha Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)

 

Na katika hadithi hii ya kuzungukwa na maaduwi tunaweza kuujuwa ugonjwa wetu na pia kuijuwa dawa yetu.

 

Maradhi yetu ni kuwa mbali na Allaah, mfarakano wetu, na kuipenda kwetu dunia.

 

Na dawa yetu ni kurudi kwa Mola wetu (Subhaanahu wa Ta’ala). Turudi katika dini yetu. Tuirudishe imani yetu na kumtegemea Allaah peke Yake. Tumuogope Yeye tu, na tuache kuuogopa uluwa na mali na ufalme na vitu kama hivi visivyo na thamani yoyote mbele ya Allaah. Tuache kuuthamini ulimwengu na kuyaogopa mauti.

 

Tuwalee watoto wetu malezi ya Kiislamu na mafundisho ya Allaah na ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Tuwafundishe taariykh yetu.

 

Kurudi kwa Allaah na kurudi katika mafundisho ya dini Yake ndiyo jambo la pekee linaloweza kuturudishia heshima yetu na utukufu wetu.

 

 

 

Share