Hakimu Wa Kiislamu (Mwenendo Wa Kesi Baina Ya Shari'ah Na Sheria)

 

Hakimu Wa Kiislamu

 

Mwenendo Wa Kesi  Baina Ya Shari’ah Na Sheria

 

Imekusanywa Na:  Naaswir Haamid

 

Na Kupitiwa Na Abuu 'Abdillaah 1430H/2009M

 

Share

001-Hakimu Wa Kiislamu: Dibaji

 

DIBAJI

 

Sifa zote ni Zake Allaahu Bwana wa viumbe vyote. Na rahma na amani ziwe juu ya Nabii Wake msema kweli mwaminifu, na juu ya Maswahaba wake na wale waliowafuata kwa wema hadi siku ya Qiyaamah.

Waba'adu...

Kwanza kabisa napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa ndugu yetu Naaswir Haamid kwa kujitolea kwake kuifanikisha shughuli hii pevu na ngumu. Bila shaka ni kazi ambayo inahitaji umakinifu na subira ya hali ya juu kabisa kutokana na ugumu wake. Nina matumaini makubwa kwamba kazi yake hii ya kukusanya mwenendo wa kesi baina ya Shari'ah na Sheria, itakuwa na manufaa makubwa kabisa kwa Waislamu wote Waswahili kwa vizazi vya sasa na vijavyo mpaka siku ya Qiyaamah. Tunamwomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Azijaalie thawabu za kazi yake hii ziwe katika mizani ya mema yake katika siku hiyo ambayo mali wala watoto hawatafaa kwa chochote ila kwa mtu aliyemjia Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa moyo usio na doa.

Mimi kwa upande wangu nikiwa kama mpitiaji, nahisi jukumu ni kubwa sana la kuhakikisha kuwa kila kitu ni madhubuti na barabara na hakuna dosari wala kasoro yoyote. Nahisi jukumu hili ni zito mno kwanza kabisa mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na kisha kwa wasomaji. Lakini nimekuwa nikijipa moyo kuwa kwa hali yoyote ile, bin Aadam ni bin Aadam tu, hakosi kasoro wala makosa. Wakati wote nimekuwa nikilikumbuka neno Lake Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) katika Aayah ya 286 ya Suratul-Baqarah:

{{Mola wetu! Usituchukulie tukisahau au tukikosea}}

Upitiaji wa kazi hii ni mgumu kwa sababu ya kuzichunguza pokezi za Hadiyth zilizotumika. Kwani kama tujuavyo kwamba, kuna Hadiyth nyingi za uongo ambazo amezushiwa Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na hapo ndipo ugumu wenyewe ulipojikita.

Narudia tena nikisema kuwa bin Aadam hakosi kasoro au upungufu. Bila shaka msomaji kwa hali yoyote, anaweza kukuta dosari kadhaa katika kazi hii pale ambapo pengine tumepitikiliwa au tumeghafilika. Tutashukuru sana kama atachangia kwa kututanabahisha na kutuelezea maoni yake, kwani hilo litazingatiwa kuwa ni mchango wake yeye pia katika kazi hii itakayowanufaisha wengi kwa miaka na miaka.

 

Abu 'Abdillaah

01 Muharram 1430

01/01/2009

 

Share

002-Hakimu Wa Kiislamu: Shukurani

 

SHUKRANI

 

 

 إنَّ الْحَمْدَ لِلَّهِ نَحْمَدُهُ وَنَسْتَعِينُهُ وَنَسْتَغْفِرُهُ وَنَعُوذُ بِاللَّهِ مِنْ شُرُورِ أَنْفُسِنَا وَمِنْ سَيِّئَاتِ أَعْمَالِنَا مَنْ يَهْدِهِ اللَّهُ فَلَا مُضِلَّ لَهُ وَمَنْ يُضْلِلْ فَلَا هَادِيَ لَهُ وَأَشْهَدُ أَنْ لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ وَحْدَهُ لَا شَرِيكَ لَهُ وَأَشْهَدُ أَنَّ مُحَمَّدًا عَبْدُهُ وَرَسُولُهُ. اللّهُـمَّ صَلِّ عَلـى مُحمَّـد، وَعَلـى آلِ مُحمَّد، كَمـا صَلَّيـتَ عَلـى إبْراهـيمَ وَعَلـى آلِ إبْراهـيم، إِنَّكَ حَمـيدٌ مَجـيد ، اللّهُـمَّ بارِكْ عَلـى مُحمَّـد، وَعَلـى آلِ مُحمَّـد،  كَمـا بارِكْتَ عَلـى إبْراهـيمَ وَعَلـى آلِ إبْراهيم، إِنَّكَ حَمـيدٌ مَجـيد .

أمّاَ بعد, إِنَّ أَصْدَقَ الْحَدِيثِ كِتَابُ اللَّهِ وَأَحْسَنَ الْهَدْيِ هَدْيُ مُحَمَّدٍ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَ سَلَّم,  وَشَرَّ الْأُمُورِ مُحْدَثَاتُهَا وَكُلَّ مُحْدَثَةٍ بِدْعَةٍ وَكُلَّ بِدْعَةٍ ضَلَالَةٍ وَكُلَّ ضَلَالَةٍ فِي النَّارِ

 

Vyovyote nitakavyojitahidi kumshukuru Mola wangu Mtukufu kwa Neema na Fadhila Zake, basi shukurani hizo hazitafikia chembe ya usawa wa Neema na Fadhila hizo, kwani hakuna awezaye kuzihesabu. Lakini sina budi kutaja shukurani zangu Kwake kwa kuniwezesha kuifanikisha kazi hii.

 

Kwa hakika mengi ninayapatia katika kujifunza kwangu. Ni katika pirika pirika hizi ndipo nilipotambua kwamba nina mzigo mkubwa mno kwa jamii inayonizunguka. Hicho kidogo nilichojifunza kwa hakika wengi hawakielewi. Ndio nikachukua jitihada za kuwafikishia Waislamu wenzangu ili waelewe yale yanayowazunguka katika mambo ya Sheria. Na ukweli ni kwamba, Waislamu wengi sio wenye kuipigia mbizi nyanja hii.

  

Bila ya shaka ni wajibu wa kila Muislamu kujifunza Uislamu wake ili aweze kufahamu yale ya halali na haramu. Hapo ndipo ataweza kuzichunga amali zake kwa lengo la kupata mafanikio duniani na Akhera. Na tunatamka kwamba hakuna njia iliyo sahihi ya wanaadamu kuifuata isipokuwa ni njia ya Uislamu. Ni Uislamu wetu ndio utatupatia mafanikio makubwa.

  

Hamu, utashi na matamanio makubwa yalinizidi ya kuipatia jamii yetu msaada wa masuala ya Sheria nilipokuja kujua kwamba wanafunzi wengi wanapata taabu katika somo hili kutokana na elimu hii kukuwepo katika lugha ya Kiarabu na Kiingereza. Halikadhalika, wana jamii wengi ninaokutana nao Mahkamani ni wenye kukosa ufahamu wa masuala haya ya Sheria.

 

Pia sina budi kukiri kwamba kitabu hiki ni zao la bidii na juhudi ya muda mrefu usiopungua miezi kumi na nane.

 

Lakini nisingeliweza kuikamilisha kazi hii bila ya usaidizi na ushauri wa ndugu yangu katika Uislaam, Muhammad Baawaziyr. Namshukuru kwa nasaha, ushauri, na namna alivyonitia moyo na ari kwa ajili ya kuitenda kazi hii. Shukurani na du’aa zangu za dhati zimfikie na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Amlipe kwa juhudi yake kubwa anayochangia katika kazi hii, Aamiyn.

 

Pia shukurani zangu kwa familia yangu, nikianza na mama  yangu, kisha kwa baba yangu, Dr. Hamed R. H. Hikmany ambaye amenipa wasaa wa kila aina kuniwezesha kutekeleza kazi hii, kunitayarishia na kuninunulia vitabu pamoja na vifaa vinavyohitajika kuiwezesha kazi hii itendeke kwa hali na mali. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Awalipe wazee wangu Pepo ya Firdaws, Aamiyn.  Pili shukurani nyingi kwa tashji’i kubwa na uvumilivu wa hali ya juu kutoka kwa Ahli yangu ambaye amenisaidia kwa kiasi kikubwa na amenipa fursa ya kutosha ya kushughulika na majukumu haya matukufu bila kuchoshwa wala kuvunjika moyo. Namuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Amlipe malipo mema, Ambariki, Amuongoze na Amzidishie elimu ya dini yake na taqwa. Aamiyn.

 

Shukurani za dhati pia kwa Ukhti yetu katika Uislaam Ummu Iyyaad ambaye amenipa fursa na ruhusa adhimu ya kutumia rejeo za kazi zake. Namuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Amjaalie tawfiyq na Amfanyie wepesi katika kazi zake hizi. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Azijaalie kazi zake zizae matunda ya khayr kwa familia yake na jamii nzima.

 

Namuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Aijaalie kazi hii ilete manufaa makubwa kwa jamii yetu, iwe ni sababu ya wengi kupata haki zao. Aijaalie iwe ni ufunuo kwa wale waliozama katika ujahili wa kufuata Umagharibi zaidi kuliko Uislamu wao. Aijaalie iwe ni alhidaaya (uongofu) wao kwa Idhni Yake.

 

Namuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anitakabalie amali hii iwe nzito katika mizani ya mambo mema siku ya Qiyaamah.  Aamiyn Yaa Rabbal ’Aalaamiyn.

 

 

Naaswir Haamid

01 Muharram 1430H – 01/01/2009M

 

 

 

Share

003-Hakimu Wa Kiislamu: Umuhimu Na Faida Ya Kujifunza Sheria

 

UMUHIMU NA FAIDA YA KUIFAHAMU SHERIA

 

 

Uislamu umejengwa kwa mihimili mikuu kutoka katika Qur-aan na Sunnah ya Bwana wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Yeyote anayefuata nje ya mfumo huu basi atawajibika kueleza ni kwa nini alifanya hivyo. Kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) zinathibitisha: 

 

{{Bila shaka Dini (ya haki) mbele ya Allaah ni Uislamu. Na waliopewa Kitabu (Mayahudi na Manaswara) hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ilimu. (Walikhitalifiana) kwa sababu ya uhasidi uliokuwa baina yao. Na anayezikataa Aya za Allaah (Allaah Atamuadhibu huko Akhera), na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.}}

[Suratu al-'Imraan: 19]

 

{{Na anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa katika wenye khasara (kubwa kabisa).}}

[Suratu al-'Imraan: 85]

 

{{Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na kukutimizieni neema Yangu, na Nimekupendeleeni Uislamu uwe Dini yenu.}} [Surratu al-Maaidah: 3]

 

Kwa hakika Aayah hizo hapo juu zinatudhihirishia kwamba, Uislamu ndio Dini ya haki ya kufuatwa na viumbe vyote. Kupitia Uislamu wetu huu, ndio tunapata mfumo mzima wa maisha. Haitakikani kwa Muislamu kuwa na khiyari ya Uislamu wake; iwe ni kiuchumi, kisiasa au kijamii. Taratibu zote za maisha ya Muislamu yatakiwa kuegemezwa kupitia kwenye Uislamu wake. Ndipo hata tunapoona kwamba hata mwenendo wa kusikiliza na kutolea hukumu kwenye migogoro yatakikana kufuata mkondo wa Uislamu. Naye Allaah Ametuthibitishia hili kwa kauli Yake:

 

{{Enyi mlioamini! Ingieni katika hukumu za Uislamu zote…}}

[Suratu al-Baqarah: 208]

 

Waislamu wanashurutishwa kuitakidi amri zote za Uislamu kuwa ni stahiki juu yao kufuatwa. Wala si katika Muumini mwenye kuzikubali baadhi na kuzikataa baadhi. Hii ndio njia sahihi ya Uislamu. Hivyo basi, mwenye kutaka mafanikio duniani na Akhera anawajibika kushikamana na kamba ya Allaah Mtukufu.

 

Kabla ya kuja Uislamu, kulikuwa na upotevu wa hali ya juu kabisa; upotevu huu ama ulikuwa wa kuteleza na kuvuka mipaka katika kutafuta njia za kujikurubisha kwa Mola, au kwa kupotoka na kupindukia mipaka katika kumfuata Shaytwaan.

 

Ukaja Uislamu ukakuta upotevu na makosa katika utaratibu ulio nje ya maumbile ya mwanaadamu, haki ikifanywa batili na kinyume chake. Hivyo, jambo la kwanza ulilolifanya Uislamu ni kutengeneza sehemu hii muhimu ya Shari’ah. Sehemu hii ilitengenezwa kwa misingi mbali mbali ya Kishari’ah ambayo kupitia huko masala ya lipi la kufuatwa na lipi la kuepukwa yakatengenea.

 

Uislamu ukarudisha mambo haya kwenye asili yake, na kuweka mizani ya uadilifu na vipimo vya kupimia lililo halali na haramu. Kwa hivyo, Ummah wa Nabii Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ukawa katikati baina ya wale waliopotea na wale walioongoka. Yaani ukawa Ummah wa wastani na bora kuliko Ummah zote zilizopita, kama ulivyosifiwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni Umma bora ulioletwa kwa wanaadamu:

 

{{Nyinyi ndio Ummah bora kuliko ummah zote zilizodhihirishiwa watu (ulimwenguni) – mnaamrisha yaliyo mema na mnakataza yaliyo maovu, na mnamwamini Mwenyezi Mungu.}} [Suratu al-Ímraan: 110]

 

Na kwa hakika sio kazi nyengine tunayoifanya kwa wana jamii isipokuwa ni kujiengua miongoni mwa wenye kula khasara kutokana na kupoteza muda pamoja na kuacha kuamrisha mema na kukatazana maovu:

 

{{Kuwa binaadamu yuko katika hasara.}}

 

{{Isipokuwa wale walioamini na wakafanya vitendo vizuri, na wakausiana (kufuata) haki na wakausiana (kushikamana) na subira (kustahamiliana).}} [Suratul-Ásr: 2-3]

 

Ni wajibu wa Muislamu kuelewa kwamba kutafuta elimu ndani ya Uislamu ni faradhi kama ilivyo faradhi ya Swalah. Kwa hakika hawapo sawa wale wenye kujua na wasiojua:

 

{{Je wanalingana wale wanaojua na wale wasiojua?}} [Az-Zumar: 9]

 

Allaah pia Anaelezea daraja ya wale waliopata elimu:

 

{{“Atawainua Mwenyezi Mungu wale walioamini miongoni mwenu, na wale waliopewa elimu wana daraja kubwa.}} [Al-Mujaadalah: 11]

 

Pia Kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) anatufahamisha kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((Kutafuta elimu ni faradhi juu ya kila Muislamu.)) [Ibn Maajah, Shaykh Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Sunnan Ibn Maajah].

 

 

Hakika mwenye kuitafuta elimu hurahisishiwa njia ya kwenda Peponi kama alivyosema kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mwenye kupita katika njia inayoshikamana ndani yake na elimu, Atamrahisishia Mwenyezi Mungu njia ya Peponi.)) [Al-Bukhaariy]

 

Na katika mapokezi mengine, amesimulia Abu Hurayrah:

 

Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Yeyote anayetoka katika njia akiitafuta kutokana nayo (njia hiyo) elimu, Humrahisishia Mwenyezi Mungu njia ya Peponi.)) [Imepokelewa na Muslim]

 

Elimu ndani ya Uislamu sio tu kusoma Qur-aan kama kasuku. Bali ni kuielewa, kuifanyia kazi pamoja na Sunnah alizokuja nazo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na ni nani anayesema kwamba elimu katika Uislamu ni ile tu inayomfikisha msomaji kuvaa vilemba vikubwa?! Uislamu umeweka kipaumbele katika elimu zote, iwe ni yenye kutoa vifungu vya sheria ama ni yenye kutibu ama inayorusha roketi na kadhalika. Tunatamka kwa vinywa vipana kwamba, elimu yoyote ambayo itakuwa na manufaa kwa Waislamu wenyewe na Ummah huu wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) basi tutaisaka, tutaisoma na tutaifanyia kazi kwa bidii zote bi idhni Llaah!

 

Uislamu umehimiza kusoma, na ndani ya hiyo elimu kuna mambo ya Shari’ah ambayo sio vyema kwa Muislamu kuiacha nyuma kwa kigezo kwamba haifanyiwi kazi. Popote inapopatikana fursa ya kuitumia basi na itumike Shari’ah. Muislamu anatakiwa kugida kila anachoweza kutokana na elimu aliyotuachia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

Imesimuliwa na Abu Muusa: Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Mfano wa uongofu na elimu ambayo Allaah Amenileta (kuifikisha) ni kama mvua kubwa inayoanguka juu ya ardhi, baadhi yake katika ardhi yenye rutba imenyonya maji ya mvua na ikaleta (kutokana nayo) mimea na majani kwa wingi. (Na) baadhi yake (ardhi) ilikuwa nzito na ikazuia maji ya mvua (kupenya katika ardhi) na Allaah Akawanemeesha watu kutokana nayo na wakaitumia kwa kunywa, kunyweshea wanyama wao na kwa ajili ya umwagiliaji na kilimo kwenye ardhi hiyo. (Na) baadhi yake (ardhi) ilikuwa sio yenye rutuba ambayo haikuweza kukamata maji wala kutoa mimea (hivyo ardhi hiyo haikutoa faida yoyote). (Ardhi) Ya mwanzo ni mfano wa mtu anayetambua dini ya Allaah na akapata faida (kutoka na elimu) ambayo Allaah Ameishusha kupitia kwangu (Mitume na wanazuoni) na akaisomesha kwa wengine. (Ardhi) Ya mwisho ni mfano wa yule mtu asiyeijali na hachukui (hafuati) uongofu wa Allaah Alioushusha kupitia kwangu (Ni mfano wa hiyo ardhi isiyo na rutuba).)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy]

 

Udhalilifu tunaoupata hivi leo katika ulimwengu huu unatokana na kukosa elimu sahihi pamoja na kutoisimamisha hiyo elimu tunayoifuata. Maadui zetu wametugawa na tugawika vipande vipande kama kigae kilichovunjika. Hatukumalizia hapo tu, bali tukachaguliwa elimu za kuzisoma na zipi za kusimamisha. Hatimaye, tukawa hatusemi wala kutetea isipokuwa kile tulichokisoma mashuleni kupitia mitaala ya kikafiri.

 

Ukweli ni kwamba kuna fadhila kubwa za kusoma. Mwenye elimu ndani ya Uislamu umemtukuza zaidi kuliko yule anayefanya ibada bila ya elimu. Fadhila hizi hazikuishia hapo tu, bali huombewa maghfira na viumbe vyote vilivyomo mbinguni na ardhini:

 

Kutokana na Abu Umaamah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) amesema: Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Fadhila za mwenye elimu juu ya mwenye kufanya ibada kama fadhila za aliye chini yenu))

Kisha akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Hakika ya Mwenyezi Mungu na Malaika Wake na viumbe vya mbinguni na ardhini hata wadudu ndani ya mashimo yao na hata samaki wanamswalia mwenye kusomesha watu khayr.)) [Imepokewa na At-Tirmidhiy]

 

Qur-aan na Sunnah pia zinatuonesha kwamba mali na watoto havina umuhimu mbele ya elimu, kwani hata Mitume hawakurithisha mali kwa taifa lao isipokuwa elimu. Elimu ndio mirathi waliyotuachia Mitume wetu, kwani wao hawarithishi makasri wala dhahabu wala pesa:

 

Kutokana na Abu Dardaai (Radhiya Allaahu ‘Anhu) amesema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mwenye kuifuata njia kuitafua elimu, Allaah Humfanyia wepesi njia ya Peponi, na hakika ya Malaika wanagubika mbawa zao kwa mwenye kutafuta elimu, wapo radhi kwa anayoyafanya, na hakika ya mwanazuoni anaombewa maghfira kwa aliyepo katika mbingu na ardhi hata samaki baharini, na fadhila za mwanazuoni juu ya mwenye kufanya ibada ni kama fadhila za mwezi juu ya nyota nyengine, na hakika ya wanazuoni ni warithi wa Mitume, na hakika Mitume hawarithishi dinari wala dirham, na hakika (wao) wanarithisha elimu. Basi yeyote atakayechukua (elimu hiyo), amechukua kitu bora.)) [Imepokewa na Abu Daawuud na Tirmidhiy]

 

Leo ulimwengu wetu umegubikwa na tatizo la kuwaweka madarakani  viongozi wenye ukosefu wa elimu sahihi na wasio wacha Mungu, waliopo ni wachache sana wenye sifa hizo, ama wengi ni wenye elimu ya kubahatisha, wenye kutumia elimu yao kwa maslahi ya kilimwengu na wenye kutumiwa kuuvuruga Uislamu.

 

Imesimuliwa na 'Abdullaah bin 'Amr bin Al-'Aas kwamba: Nimemsikia Mjumbe wa Allaah akisema:

((Allaah haichukui elimu kwa kuichukua kutoka kwa (mioyo ya) watu, lakini anaichukua kwa kufariki Maulamaa hadi hakuna yeyote (‘Aalim) atakayebaki, watu watawafanya viongozi wao wajinga ambao watakapoulizwa watatoa fatwa zao bila ya elimu. Hivyo watapotea na watawaongoza watu kwenye upotevu)) [Al-Bukhaariy]

 

Elimu na Uislamu ni vitu vinavyokwenda sambamba ndani ya mfumo wetu huu wa maisha hapa duniani. Kuna khayr kubwa kwa yule mwenye kupatiwa elimu inayotokana na diyn hii ya Uislamu, kwani zipo elimu nyingi na chungu nzima zisizo na asili yoyote na Uislamu. Mfano wa somo la historia kuwasomesha wanafunzi ya kwamba binadamu asili yake ni sokwe! Subhaana Allaah.

 

Mu'aawiyah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) amesimulia kutoka kwa Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Mwenyezi Mungu Akimtakia khayr (mja Wake) Humpa ufahamu (elimu) katika diyn.)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Kazi hizi tuzifanyazo kwa jamii si chochote ila ni kutafuta radhi za Muumba. Kwani hili ni jukumu la kila Muislamu kumsomesha mwenziwe kwa kile alichokipata. Hata gari la shilingi milioni mia moja halina thamani mbele ya yule aliyemuongoza mja mmoja tu:

 

Kutokana na Sahal bin Sa'ad (Radhiya Allaahu ‘Anhu) amesema: Hakika ya Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kumwambia 'Aliy (Radhiya Allaahu ‘Anhu):

((Ninaapa kwa Allaah kwamba Akimuongoza Allaah mja kupitia kwake mtu mmoja ni bora kwake kuliko ngamia mwekundu.)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Pia katika Hadiyth nyengine, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema mwenye kulingania uongofu, atapata ujira wa anayemfuata bila ya kupunguziwa chochote:

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) amesema: Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Yeyote anayelingania katika uongofu, atakuwa na ujira mfano ujira wa anayemfuata, hatapunguziwa kutokana ujira huo chochote.)) [Muslim]

 

Muhimu kuelewa kwa makini kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amempatia dhamana ya moto kwa yule anayemsingizia uongo:

 

Kutokana na 'Abdullaah bin 'Amruu bin Al-'Aas (Radhiya Allaahu ‘Anhuma) amesema: Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Fikisheni kutoka kwangu japo Aayah (moja), na hadithieni habari za Bani Israaiyl wala hakuna kosa, na yeyote atakayenizulia uongo moja kwa moja, basi ajitayarishie makaazi yake ndani ya moto.)) [Imepokelewa na Al-Bukhaariy]

 

Hichi ni kibarua kikubwa kwa waandishi wa Kiislamu, kwani Ulimwengu wa Hadiyth umejaa simulizi za uongo chungu nzima. Hata hivyo, tunarudia kusema kwamba mwenye kutafuta elimu Allaah Humfanyia wepesi mambo yake.

 

Ni mengi ambayo tunayasikia na kuyasoma kutoka vyanzo mbalimbali. Uislamu kwa upande wake umehimiza Muislamu kusoma na kusomesha. Kuifikisha elimu kwa wengine ndio jamii inapotengenea. Elimu hii ifikishwe bila ya kujali huyo unayemfikishia iwapo anaelewa au laa:

 

Kutoka kwa Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu ‘Anhu) amesema: Nimemsikia Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

((Mwenyezi Mungu Amemtakia khayr aliyesikia maneno kutoka kwetu, basi akayafikisha kama alivyoyasikia, pengine aliyefikishiwa ni mjuzi kuliko aliyefikisha.)) [Imepokewa na at-Tirmidhiy]

 

Ndio maana waandishi kadhaa wanahitaji mawazo ya wengine. Kwa sababu huenda huyo anayefikishiwa elimu ni mjuzi zaidi kuliko mfikishaji. Na tunasema kwamba, muongozo uliomo ndani ya kitabu hichi cha Mwenendo wa Kesi Baina ya Shari’ah (za Allaah) Na sheria (za mwanaadam) si jambo geni wala sio jipya. Wapo wajuzi zaidi wa kuandikia maelezo haya kwani wao ni wenye elimu zaidi. Tunachokifanya ni kufikisha kwa jamii ili upatikane ufahamu kwa wepesi huku tukipatiwa fafanuzi za makosa yetu. Kwani kila binaadamu ni mwenye kukosea.

 

Ufikishaji huu kama tulivyosema awali, ni mzigo kwa aliyepatiwa elimu. Kwani kuna adhabu kubwa mbele ya Allaah kwa anayeficha elimu sahihi. Adhabu ambayo ni ya kurajmiwa kama anavyofanyiwa punda au farasi au ngo'mbe kwa kuingiziwa kamba puani aendeshwe kwa namna bwana anavyotaka. Ni udhalilifu wa aina gani huu kwa mwenye kuficha elimu?

 

Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Mwenye kuulizwa juu ya elimu akaificha, atafungwa mdomo na kifungo cha moto siku ya Qiyaamah.)) [Imesimuliwa na Abu Hurayrah; Imepokewa na Ahmad na at-Tirmidhiy]

 

Tuweke akili sawa kwamba kutafuta elimu kwa kupata cheo hapa duniani sio sahihi kabisa. Tusome elimu kwa ajili ya kupata radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Kwani hapo tutapata yote – dunia na Akhera.

 

Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Mwenye kujifunza elimu (isiyokuwa) ya kutafuta fadhila za Allaah 'Azza wa Jalla, hajifunzi isipokuwa kupata cheo ndani ya dunia, hatoipata (hata) harufu ya Pepo siku Qiyaamah.)) [Imesimuliwa na Abu Hurayrah; Imepokewa na Abu Daawuud]

 

Muislamu wa kweli hatosheki katika kufanya khayr, na hakuna fadhila kubwa kama za kuitafuta elimu pamoja na kuisomesha.

 

Kutoka kwa Abu Sa'iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ‘Anhu) amesema: Amesema Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Hatosheki Muumini katika (kutenda) khayr mpaka atakapomalizia Peponi.)) [Imepokewa na at-Tirmidhiy]

 

Na hivyo tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ajaalie kazi hizi za kuifikishia jamii elimu sahihi ni yenye manufaa. Manufaa ambayo yatajaalia kuzaa matunda hapa duniani pamoja na hapo tutakapokuwa katika maisha ya barzakh (kaburini). Hii ni kwa uthibitisho wa Hadiyth aliyonukuliwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

 

((Atakapokufa mwanaadamu hukatika amali zake isipokuwa mambo matatu: swadaqah yenye kuendelea, au elimu yenye kumnufaisha, au mtoto mwema anayemuombea.)) [Imesimuliwa na Abu Hurayrah; Imepokelewa na Muslim]

 

Kwa upande wa Tawhiyd tunaelezwa kwamba Shahadah ya Mwenyezi Mungu Ndiye Anayestahiki kuabudiwa na kwamba Muhammad ndiye Mjumbe Wake wa mwisho inafanyiwa kazi kwa kufuata Shari’ah ya Kiislamu. Hata kwa wasiokuwa Waislamu walio chini ya himaya ya Taifa la Kiislamu (dhimmi) wanawajibika kufuata Shari'ah hizi:

 

Imesimuliwa na Ibn 'Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma): Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Nimeamrishwa (na Allaah) kupigana dhidi ya watu hadi waape kwamba hakuna mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mjumbe Wake, na kusimamisha Swalah na kutoa Zakaah, hivyo wakiyatekeleza hayo, basi maisha yao na mali zao zinahifadhiwa kutokana na mimi isipokuwa kwa Shari’ah za Kiislamu na hisabu yao itafanywa na Allaah.)) [Al-Bukhaariy]

 

Shari’ah hizo ni lazima zitokane na Qur-aan pamoja na Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwani Shari’ah yoyote isiyotokana na Muumba basi hiyo haifai kufuatwa na yaeleweka kuwa ni baatwil kwani itakuwa inaenda kinyume na maumbile (fitrah) ya mwanaadamu.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Yeyote anayeweka masharti (Shari’ah) ambayo hayamo ndani ya Kitabu cha Allaah, masharti yake yatakuwa si sahihi hata kama atayalazimisha mara mia moja.)) [Imesimuliwa na mama wa Waumini 'Aaishah; Imepokewa na Al-Bukhaariy]

 

Na kutoa hukumu kwa mujibu wa Shari’ah za Allaah ndio mwenendo unaotakiwa kufuatwa na kuhimizwa kutekelezwa. Kisa hichi ni vyema tukakinukuu ili kufahamu ni namna gani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa makini kabisa katika kusimamisha hukumu za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

 

Imesimuliwa na Abu Hurayrah na Zayd bin Khaalid al-Juhaani: Bedui mmoja alikuja na kusema: "Ewe Mjumbe wa Allaah! Hukumu baina yetu kwa mujibu wa Shari’ah za Allaah." Mpinzani wake akasimama na kusema: "Yupo sahihi. Hukumu baina yetu kwa mujibu wa Shari’ah za Allaah.' Bedui akasema: "Mwanangu wa kiume alikuwa ni mfanyakazi akifanya kazi kwa bwana huyu, na akatenda kitendo cha ndoa kisicho halali na mkewe. Watu wameniambia kwamba mwanangu apigwe mawe hadi kifo; hivyo kwa uzito wa hilo, nikalipa fidia ya mbuzi mia moja na mtumwa wa kike ili kumuokoa mwanangu. Kisha nikawauliza wanazuoni ambao walisema: "Mwanao apigwe mijeledi mia moja na atengwe kwa mwaka mmoja." Mtume akasema:

((Hapana shaka nitahukumu baina yenu kwa mujibu wa Shari’ah za Allaah. Huyo mtumwa wa kike na mbuzi mia moja warudi kwako, na mwanao atastahiki mijeledi mia moja na mwaka mmoja wa kutengwa.)) Baadaye akamuamrisha mtu:

((Ewe Unays! Nenda kwa mke wa huyu (mtu) na mpige mawe hadi afariki.)) Hivyo, Unays akaenda na kumpiga mawe hadi kufa. [Al-Bukhaariy]

 

Kufuata Shari’ah sio tu kazi ya Hakimu, bali hata kwa mashahidi na wenye kupeleka kesi zao wanawajibika kuwa makini katika kufuata mwenendo sahihi utakaopelekea hukumu ya haki na uadilifu kutolewa. Mwenendo huu ni pamoja na kufuata maelekezo ya Mahkama iliyo 'aadil pamoja na kujiweka mbali na vitendo vya dhulma kama vile utapeli, wizi na rushwa.

 

Juu ya migogoro na migongano yote inayotokezea baina ya watu, la muhimu ni kukumbuka kwamba Muumba wetu ni Ghafuurun Rahiym (Mwenye Kuswamehe na Mwenye Huruma). Kama Yeye Mola wetu yupo tayari kutupokelea dhambi zetu hata ziwe na ukubwa wa mbingu na ardhi, kwanini basi wanaadamu wanashindwa kuwa wasemehevu baina yao? Ni vyema tukajifunza kutokana na kisa kifuatacho:

 

Binti wa An-Nadr alivunja jino la mtoto wa kike, jamaa wa Ar-Rabi’ wakaomba jamaa wa mtoto wa kike kukubali Irsh (fidia kutokana na maumivu) na kumsamehe (mtenda kosa), lakini wakakataa. Hivyo, walikwenda kwa Mtume aliyeamrisha kufanya kisasi. Anas bin An-Nadr akauliza: "Ewe Mjumbe wa Allaah! Je jino la Ar-Rabi’ litavunjika?" "Hapana kwa Yule Aliyekuleta wewe pamoja na Ukweli, jino lake halitavunjika." Mtume akasema:

((Ewe Anas! Shari’ah ya Allaah inaamrisha kisasi)) Baadaye jamaa za mtoto wa kike wakakubali na kumsamehe. Mtume akasema:

((Kuna baadhi ya watumwa wa Allaah, ambao wakila kiapo kwa jina la Allaah, kinajibiwa na Allaah, (yaani kiapo chao kinatimizwa)) Anas akaongeza: "Watu wameelewana na kukubali Irsh." [Imesimuliwa na Anas; Imepokelewa na Al-Bukhaariy]

 

Bahati mbaya ndani ya jamii za Waislamu, utakuta migogoro isiyo na kichwa wala miguu. Waislamu wanafika kupelekeshana Mahakamani kwa sababu ya nazi zenye kuhesabika na kugombania ulezi wa mtoto wa mwaka mmoja? La hawla walaa quwwata illa bi Llaah! Hii ni aibu na fedheha kubwa. Waislamu wanatakiwa kuwa ni mfano kwa wasio Waislamu kwa kuwa na moyo wa kusamehe na huruma. Njia hii itarahisisha kutatua migogoro pamoja na kupunguza magonjwa yanayotokana na kuweka kitu moyoni sana kama presha au magonywa ya moyo.

 

 

 

 

Share

004-Hakimu Wa Kiislamu: Taratibu Za Utendaji Katika Kukusanya Kitabu Hiki

 

TARATIBU ZA UTENDAJI KATIKA

KUKIKUSANYA KITABU HICHI

 

 

Ni jambo linaloeleweka ya kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ameziweka kanuni za ulimwengu huu katika aina mbili. Aina ya mwanzo ni ile ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ndiye Mwendeshaji wa kila kitu, kwa mfano mwenendo wa jua na mwezi. Aina ya pili ni ile ambayo mwanaadamu anahitajika kuzifuata kanuni Alizowekewa na Muumba wake. Hizi nazo pia zimegawika sehemu mbili. Sehemu ya mwanzo ni kanuni ambazo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Amekwisha zitolea hukumu, kwa mfano taratibu za uendeshaji wa makosa ya jinai kama vile zinaa na ulevi. Sehemu ya pili ni zile ambazo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ameziwacha wazi kwa wanaadamu kuzitolea ufafanuzi kwa kutumia vyanzo vya Qur-aan na Sunnah. Hapa ndipo tunapopata tawi la mwenendo wa kesi.

 

Qur-aan ni mwongozo wa Uislamu ikifafanuliwa vyema kwa kutumia Sunnah ya Habibul-Mustafa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa kutumia Sunnah hii ndipo tunapata fursa ya kutolea fafanuzi baadhi ya vifungu vya Shari’ah ya Kiislamu. Wanavyuoni kwa kupitia vikao vyao Shuura na mamlaka ya Shari’ah ndogo za Kiislamu pia wameweza kutumia fursa zao katika kutolea maelezo mwenendo huu wa kesi.

 

Mwenendo wa kesi ni ule utaratibu wa kushughulikia migogoro. Katika kitabu chetu hichi tumetumia zaidi kesi baina ya wanaadamu wenyewe sio yale makosa ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Amekwishayatolea maamuzi kama vile zinaa na ulevi. Ingawa kwa upande fulani mifano ya huduud (jinai zenye hukumu zake) imeelezewa ili kupata ladha baina ya jinai na madai pamoja na kuweka wazi hoja kwa lengo la kueleweka vyema.

 

Kazi ya kukusanya vyanzo vya Shari’ah sio kazi nyepesi hata kidogo. Ikikumbukwa kwamba Uislamu unaruhusu kanuni zake kufafanuliwa kupitia vyanzo vikuu vya Shari’ah ambavyo ni Qur-aan na Sunnah. Halikadhalika ni dhambi kubwa kumzulia Muumba maelezo ambayo Hajayatoa na vivyo hivyo kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Kazi hii ya kukusanya Shari’ah hizi tunaifanya baina ya hadhari mbili kama zilivyoelezwa ndani ya Qur-aan:

 

{{Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na anayemtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, (Mwenyezi Mungu) Atamwingiza katika Bustani zipitazo mito mbele yake; wakae humo milele. Na huko ndiko kufaulu kukubwa.}} [Suratun-Nisaa: 13]

 

Aayah hiyo ya juu inatuhimiza kumtwii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Utiifu huu ndio unatupelekea kuchambua maelezo ya Shari’ah ili kupata muongozo ulio adilifu usioendana na dhulma. Kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa pamoja wameiharamisha dhulma.

 

Lakini Aayah inayofuatia ya Suratun-Nisaa inaeleza kwamba mwenye kumuasi Yeye Muumba pamoja na Mtume Wake basi wajitayarishie makaazi ya Motoni:

 

{{Na anayemwasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na kuiruka mipaka Yake, (Mwenyezi Mungu) Atamwingiza Motoni, huko atakaa milele, na atapata adhabu zifedheheshazo.}} [Suratun-Nisaa: 14]

 

Kumzulia vifungu vya Shari’ah Muumba na Mtume Wake ni dhambi kubwa mbele ya Mola Mlezi na ni uasi mbaya dhidi ya Uislamu. Malipo yake ndio huo Moto ufedheheshao. Ni kusema kwamba, uangalifu wa hali ya juu unahitajika katika kutoa maelezo ya masuala ya Shari’ah ya Kiislamu. Kwani kutojali mipaka ya Mola Mlezi katika ufafanuzi huu kutasababisha Muislamu kuporomoka katika uasi.

 

Inaeleweka pia kwamba mwenye kumuongoza Muislamu mwenziwe katika khayr atapata naye malipo sawa sawa na yule mwenye kuifanya hiyo khayra, na mwenye kumuongoza mtu katika upotovu naye atapata malipo sawa. Hivyo, tumechukua jukumu kubwa la kuutolea ufafanuzi Ummah wa Kiislamu haswa kwa wazungumzaji wa Kiswahili. Lakini, tutakuwa mas-uul iwapo kitabu hichi kitakuwa ni sababu ya Waislamu kupotea (Allaah Atulinde na kuangamia huku). Na iwapo itabainika mbele ya Mahkama ya Mola wa Mbingu na Ardhi kwamba kitabu hichi kimepoteza zaidi kuliko kuongoza basi adhabu kubwa itatuwajibikia juu yetu. Hakika hizi kazi sio katika masuala ya kuyavamia na kuyachezea hata kidogo!

 

Juu ya yote hayo, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anamlipa mja wake kutokana na niyah. Wala hakuna kitu muhimu anachohitajika Muislamu kukichunga kama niyah yake kama alivyosema Abu Sufyaan bin Sa'iyd ath-Thawriy (Rahimahu Allaahu):

 

((Hakuna kitu ninachojishughulisha nacho zaidi kuliko niyah yangu.))[1]

 

Hivyo tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kupitia nia zetu za khayr kujaalia kazi hii ni miongoni mwa zitakazofanya mizani ya ‘amali njema kupanda juu.

 

Upotevu mkubwa uliowakumba Waislamu wa leo ni kutokana na kuacha mafunzo sahihi ya Kiislamu. Walianza kudharau fardhi ya elimu wakatumbukia katika udhalilifu wa hali ya juu. Waislamu wakajikuta hawaelewi baina ya mwenendo wa Kiislamu na ule usio kuwa wa Kiislamu. Hata migogoro yao imekuwa ikisimamiwa katika taratibu zilizo nje ya Uislamu.

 

Tunaamini kwamba, iwapo Muislamu atasoma kwa ajili ya Allaah na kuelewa vyema mafunzo ya Shari’ah za Kiislamu atakuwa mbali katika kumuasi Mola wake. Na iwapo atateleza basi Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa Rahmah Zake Atamuongoza katika uongofu.

 

Inakuwa ni jambo la kusikitisha kwa mtu aliyebobea katika fani ya Shari’ah anapomuona mtu akikosa haki yake kwa kukosa tu kufuata taratibu sahihi za kufungua kesi. Hili katika Uislamu laweza kuepukwa, lakini kwa masikitiko makubwa hizi ni njia ambazo weledi wa Shari’ah wamekuwa wakizitumia. Na ndio sababu ya Waislamu kukosa haki zao za msingi.

 

Waislamu haiwaisaidii kukaa kitako na kutosimamia haki zao kwa hoja ya kwamba Mahkama za leo sio za Kiislamu. Ni kupitia Mahkama hizi hizi twaweza kwa kutumia hizo hizo Sheria walizoziweka wanaadamu kuweza kujitetea. Kujitetea huku kunawezekana kusiwe na mafanikio lakini dhimma mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) itakuwa imepunguwa kwa kiwango kikubwa. Tukielewa kwamba ndani kabisa katika vifungu vya Sheria alivyovitunga mwanaadamu ni vyenye kudai haki na uadilifu. Hivi ndivyo vifungu ambavyo vitatumika kudai haki zetu. Kinyume cha vifungu hivi, ni vile visivyoendana kabisa na Uislamu, basi hivyo vitakataliwa na kutosimamiwa.

 

Ni kawaida ya kesi kufunguliwa baada ya kutokezea mgogoro. Ndipo hapa ambapo Muislamu anatakiwa aelewe nini na wapi anakwenda kukidai. Baadaye utafuata utaratibu wa kulisikiliza dai na kutolea ushahidi. Hatimaye hukumu itatolewa na upande usioridhika kupatiwa haki ya rufaa. Hizi ni taratibu ambazo kitabu hichi kimejitahidi kuyatolea ufafanuzi.

 

Utaratibu uliotumika katika kukikusanya kitabu hichi ni kuchukua fafanuzi na maelezo kutoka Shari’ah na baadaye kuyatafutia kulingana kwake na Sheria za nchi. Shari’ah kwa hapa tunakusudia zile za Kiislamu wakati Sheria ni hizi azitungazo mwanaadamu.

 

Halikadhalika, Sheria sio zile tu zilizopitishwa na Bunge ama Baraza la Wawakilishi. Bali pia zinaambatana na hukumu zinazotolewa na Mahakimu. Hivyo, iwapo Hakimu aliwahi kutoa hukumu hapo kabla, ikitokea tena kesi kama hiyo kwa pande (za watu) zilizo tofauti anahitajika kutumia uzoefu wa hukumu ile ile iliyopita. Hivyo, kitabu hiki kimekusanya hukumu za kesi tofauti zilizowahi kusomwa hapa Afrika Mashariki, Uingereza na pia India.

 

Kitabu hiki kimetoa maelezo pia kwa Hakimu. Kwa mfano uteuzi na wajibu wake katika misingi ya Uislamu. Kwa upande wa Zanzibar, kuna kanuni na muongozo maalum unaohitajika kufuatwa na Mahakimu pamoja na wafanyakazi wengine wa Mahkama. Anahitajika kutojishirikisha katika rushwa wala kupendelea upande mmoja. Namna anavyohitajika kuwa ni mambo mengi. Wajibu wa kufuata muongozo huu umo ndani ya Sheria ya Tume ya Uajiri ya Mahkama ya mwaka 2003 ya Zanzibar.

 

Ili kukifanya kitabu kuwa na maelezo mafupi yenye maelezo ya kina, imebidi kutumia vifupisho vya maneno. Mfano wa vifupisho vilivyotumika ni kama ifuatavyo:

 

 

KIINGEREZA:

 

 

KIFUPISHO

KIREFU

MAANA

 

Cr.

 

Criminal

Jinai

E. A.

 

East Africa

Afrika Mashariki

E. A. C. A.

 

East African Court of Appeal

Mahkama ya Rufaa ya Afrika Mashariki

 

O.

Order

Kanuni

 

r.

Rule

Amri

 

R.

Republic

Jamhuri

 

S.

Section

Kifungu

 

V.

Versus

Dhidi ya

 

 

 

KISWAHILI:

 

 

KIFUPISHO

KIREFU

 

J.

Juzuu

 

uk.

Ukurasa

 

 

 

Halikadhalika, kwa lengo la kurahisisha marejeo pamoja na kutoa fafanuzi katika vipengele tofauti, kitabu hiki tumekigawa katika sura mbali mbali. Maelezo ya sura hizi ni kama zifuatazo:

 

Sura Ya Kwanza imesawazisha kwa kutolea fafanuzi za baadhi ya maneno muhimu na yaliyotumika sana ndani ya kitabu hiki. Bila ya shaka msomaji anaweza kukutana na maneno asiyoyaelewa maana yake kutokana na kitabu hiki kujikita katika mambo ya Shari’ah na Sheria kwa pamoja.

 

Sura Ya Pili ya kitabu hiki ndio imeanza kuingia rasmi katika mambo ya kesi kwa kutolea maelezo ya namna ya kufungua kesi na nani anastahiki kufungua kesi.

 

Sura Ya Tatu inaeleza kuhusu hati. Hizi ni zile hati (summons) anazopatiwa mtu na kuwajibika kufika Mahkamani katika tarehe iliyopangwa na wakati utakaoelezwa ndani ya hati hizo.

 

Sura Ya Nne inafafanua namna ya kusikiliza kesi. Hii ndio sura inayoeleza wapi Mahkama inaweza kukaa, wajibu wa hakimu kusikiliza maelezo ya pande zote za kesi, hatma ya yule anayekataa kujibu na namna gani ya kushugulikia kesi ambayo upande mmoja umekubali kushindwa, na imemalizia sura hii kwa kutoa maelezo ya kuakhirisha kesi.

 

Sura Ya Tano imekusanya maelezo ya ushahidi katika kesi. Sura hii imeanza kwa kutolea ufafanuzi wa dhana ya ushahidi, baadaye imeendelea na kufafanua kuhusu kiapo na nani anawajibika kuapa na nani anawajibika kuthibitisha malalamiko yake. Katika kesi kunawezekana kukakuwepo na mtaalamu wa masuala fulani, hili limeelezwa ndani ya sura hii pia. Sura ya tano imeangalia namna ya kumfahamu shahidi anayeletwa mbali, huu ni ufahamu wa khulqa zake na namna ya utoaji ushahidi wake. Ama maelezo mengine muhimu katika sura hii ni kuhusu ushahidi wa kimazingira na kutengua ushahidi wa mwenye kujirudi. Sura hii ya tano inamalizia na maelezo kuhusu namna na wakati gani wa kutoa tafsiri.

 

Sura Ya Sita kwa upande wake imetengwa kwa kutolea maelezo ya hukumu. Haya ni maelezo kuhusu namna ya kuitayarisha hukumu, namna ya kuisoma. Kwa kile kinachofuata baada ya kusomwa hukumu ni kikaza hukumu, rufaa, mapitio na marejeo. Hakimu amepewa mamlaka ya kutoa mawazo yake binafsi, hili limewekwa ndani ya sura hii ya sita. Suluhu ni katika njia nyepesi na salama ya kumaliza kesi. Hivyo, kitabu hiki hakijaacha kufafanua suluhu ndani ya sura hii. Maelezo mengine ni ushauri wa wanazuoni na kizuizi cha kufungua kesi kutokana na kupita muda mrefu.

 

Sura Ya Saba inaeleza kuhusu wafanyakazi wa mahkama, hawa ni wale makarani, wataalamu, wafasiri na wengineo.

 

Sura Ya Nane ambayo ni ya mwisho inamalizia na hitimisho.

 

Kwa mtiririko wa sura hizi pamoja na maelezo yake, tunatumai kwamba itaeleweka kiasi fulani kuhusu utendaji wa kazi hii na maelezo tuliyoyagusia mwanzoni katika kuwa makini pamoja na kuichunga niyah.



[1] Shaykh Bakr bin 'AbdiLlaah Abu Zayd, Sharhu Hilyat Twaalib al-'Ilmi, Iliyoshereheshwa na Shaykh Muhammad bin Swaalih al-'Uthaymiyn, Chapa ya Daaru Ibnul Haytham, Misri, (2002).

Share

005-Hakimu Wa Kiislamu: Vitabu Vya Marejeo

 

VITABU VYA MAREJEO

 

 

Bila ya shaka hakuna kazi inayonasibiana na Uislamu ikakamilika bila ya kurejea maneno matukufu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Nayo ni Qur-aan Tukufu. Kwa kuwafanyia wepesi wasomaji wa Kiswahili, tumetumia maneno ya Kiswahili bila ya kuweka zile Aayah asili. Hili ni vyema likawashajiisha wasomaji kurudia Aayah za Qur-aan moja kwa moja. Kwani fadhila za kuisoma Qur-aan zinapatikana kwa kurudia Aayah asili katika lugha ya Kiarabu kama zilivyoteremshwa.

 

Kwa ajili ya kufanikisha utendaji wa kazi hii vyema, imenibidi kurejea zaidi katika vitabu vya Kiingereza na baadhi ya vitabu vya Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kamusi imetumika kwa ajili ya maana na uchambuzi wa neno kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili.

 

Ama sheria nimetumia zaidi kutoka Zanzibar. Ingawa kwa kiwango kikubwa sheria za Tanzania Bara, Kenya, Uganda, India na nyinginezo zinafanana kutokana na kutawaliwa na Muingereza ambaye aliziwasilisha sheria hizi kwa koloni zake. Sio mambo yote ndani ya sheria hizi ambayo yanafanana na mazingira ya Shari’ah za Kiislamu. Hivyo, imenibidi kutumia baadhi tu ya vifungu nilivyohisi vinafanana na Shari’ah. Hata hivyo, bado imebaki kazi kubwa kwani sio vifungu vyote nilivyofanikisha kuvinukuu. Hii ni kutokana na muda pamoja na kujizuia kukifanya kitabu hichi kuwa kirefu mno.

 

 

QUR-AAN TAFSIYR YA KISWAHILI

 

Shaykh Abdullah Saleh Al-Farsy, Qur-aan Takatifu, (1994).

 

 

HADIYTH

 

Imaam Abiy Zakariyyah Yahya bin Sharaf an-Nawawiy ad-Damshiqiy, Riyaadhu as-Swaalihiyna, Daarul-Kitaabul-'Alamiyyah, Bayruut – Lubnaan, (1985).

 

Al-Haashimiy, Mukhtaar ahaadiyth an-Nabawiyyah.

 

Duktuur Mustafa Dayb Matn al-Ghaayatu wa at-Taqriyb, (1978).

 

 

 

SHARI’AH[1]

 

Fundamentals Of An Islamic Constitution, Extract From The Concept Of Islamic State, Treatise, Islamic Council Of Europe – 1st Ed. 1979.

 

'Abdur-Rahiym, The Principles of Islamic Jurisprudence, Afif Printers, Delhi, India, 2nd Ed. 1994.

 

G. M. Azad, Judicial System of Islam, Afif Printers, Delhi, India, 1st. Ed. 1994.

 

 

SHERIA[2]

 

B. D. Chipeta, A Handbook For Public Prosecutors, Tanzania, 1979.

 

B. D. Chipeta, A Magistrate's Manual, T. M. P Book Department, Tabora, Tanzania.

 

B. D. Chipeta, Civil Procedure In Tanzania, A Student's Manual, Dar es Salaam University Press Ltd, Dar es Salaam, Tanzania, 2002.

 

Dr. Avtar Singh, Principles Of The Law of Evidence, Central Law Publications, Allahabad, India, 13th Ed. 2002.

 

 

SHERIA ZA ZANZIBAR

 

Interpretation Decree, Chapter 1, (1953).

Courts Decree, Chapter 3, (1923).

Jurisdiction Decree, Chapter 4, (1934).

Evidence Decree, Chapter 5, (1917).

Evidence (Banker's Book) Decree, Chapter 6, (1949).

Oaths Decree, Chapter 7, (1917).

Civil Procedure Decree, Chapter 8, (1917).

Limitation Decree, Chapter 12, (1917).

Arbitration Decree, Chapter 25, (1928).

Contract Decree, Chapter 149, (1917).

Land Tribunal Act, Act 12 of 1994.

 

 

KAMUSI YA KIARABU - KIINGEREZA  

 

Hans Wehr – Edited by   J   Milton Cowan, A Dictionary Of Modern Written Arabic - Arabic-English, 3rd Ed. (1976).

 

 

KAMUSI YA KIINGEREZA - KISWAHILI

 

A Standard English-Swahili Dictionary. Oxford University Press, (1996).



 



[1] Ni vyanzo vya sheria vinavyotokana na misingi mikuu ya sheria za Kiislamu kutoka kwenye Qur-aan na Sunnah pamoja na vyanzo vyengine vidogo kama Qiyaas, Ijma’ na vyenginevyo.

 

[2] Kwa mnasaba wa sehemu hii, tunalifasili neno hili kuwa: Ni sheria ambazo zimetungwa na mwanaadamu zinazodai kuwa hazina uhusiano wa dini yoyote kwa ajili ya kuweka misingi na kanuni za maisha ya mwanaadamu hapa duniani.

 

Share

006-Hakimu Wa Kiislamu: Yaliyomo: (Mwenendo Wa Kesi Baina Ya Shari'ah Na Sheria)

 Hakimu Wa Kiislamu (Mwenendo Wa Kesi Baina Ya Shari'ah Na Sheria)

YALIYOMO

 

SURA YA KWANZA: UTANGULIZI

 

Mamlaka Ya Kutoa Amri Na Hukumu

 

Nukuu Ndani Ya Baadhi Ya Vitabu

 

Shari’ah Dhidi Ya Sheria

 

Dhana Ya Mwenendo Wa Kesi

 

Masharti Ya Uteuzi Wa Hakimu Wa Kiislamu

 

Wajibu Wa Hakimu

 

Fafanuzi Za Maneno

 

 

SURA YA PILI: UFUNGUZI WA KESI

 

Nani Anayeweza Kudai?

 

Uteuzi Wa Mahkama Inayofaa

 

 

Dai Lazima Litimize Kanuni Zake

 

Kuunganisha Kwa Pande Za Watu

 

Utaratibu Pale Mdaiwa Anapoishi Nje Ya Mpaka

 

 

SURA YA TATU: HATI

 

Nyaraka

 

Wito Kwa Mdaiwa

 

Ushahidi Wa Wito

 

Kutotii Kwa Mdaiwa Na Kuvamia Eneo La Mdaiwa

 

Kufika Mdaiwa Mahkamani

 

Majibu Kwa Njia Ya Kujitoa

 

 

SURA YA NNE: KUSIKILIZA KESI

 

Sehemu Ya Mahkama

 

Hamna Hukumu Bila Ya Kusikilizwa

 

Hukumu Dhidi Ya Upande Mmoja - Al-Qadhaa ‘Ala al-Ghaib

 

Mdaiwa Kukataa Kujibu

 

Kukubaliana Na Madai (Admission)

 

Kusikiliza Dai

 

Kuakhirisha Na Kuchelewesha Haki

 

 

SURA YA TANO: USHAHIDI

 

Dhana Ya Ushahidi

 

Kuthibitisha (Onus Of Proof)

 

Mawazo Ya Mtaalamu (Expert’s Opinion)

 

Tazkiyah

 

Mashahidi Wa Mdai Na Mdaiwa

 

Nukuul (Kiapo)

 

Masharti Ya Kuwa Shahidi

 

Kuulizia Uwezo Wa Shahidi

 

Kiapo Cha Moja Kwa Moja Na Tetesi

(Direct And Hearsay Testimony)

 

Kiapo Ni Lazima Kiendane Na Madai

 

Kuchagua Ushahidi

 

Ushahidi Wa Hali Halisi (Tahkiim-ul-Haal)

 

Ushahidi Wa Kimazingira (Circumstantial Evidence)

 

Kutengua Kiapo/Ushahidi (Retraction)

 

Kizuio (Estoppel)

 

Tafsiri

 

 

SURA YA SITA: HUKUMU

 

Hukumu

 

Kutoa Hukumu

 

Athari Ya Maoni Binafsi Ya Hakimu

 

Kikaza Hukumu (Execution Of Decree)

 

Marejeo (Reference) Na Mapitio

 

Amri Ndogo Ndogo (Ancillary Orders)

 

Kizuizi (Time Barred)

 

Ushauri Wa Wanazuoni

 

Suluhu (Arbitration)

 

 

SURA YA SABA: WAFANYAKAZI WA MAHKAMA

 

 

SURA YA NANE: HITIMISHO

Share

007-Hakimu Wa Kiislamu: Sura Ya Kwanza

 

SURA YA KWANZA

 

UTANGULIZI

 

 

Mamlaka Ya Kutoa Amri Na Hukumu

 

Qur-aan Tukufu inasema:

 

{{Haikuwa hukumu ila hii ya Mwenyezi Mungu tu. Ameamrisha msimuabudu yeyote isipokuwa Yeye tu.}} [12:40]

 

Aayah hii inatuonesha wazi kwamba mamlaka ya kutoa amri na hukumu ni ya Kwake pekee Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Amri hii sio tu kwenye sheria, lakini pia inagusa nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kiutawala. Yeye Allaah Ndiye Pekee wa kutoa amri na kanuni za kila kitu. Qur-aan inasema:

 

{{Fahamuni kwamba (ni Kwake tu Mwenyezi Mungu) na amri zote ni Zake (Mwenyezi Mungu) Ametukuka kabisa Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote.}} [7:54]

 

Bila ya shaka yoyote, mamlaka ambayo Qur-aan imeeleza kwa Allaah, sio tu kwenye utawala, bali hata kwa sheria. Qur-aan inaeleza hili:

 

{{Na wasiohukumu kwa yale Aliyoteremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio makafiri.}} [5:44]

 

 

Nukuu Ndani Ya Baadhi Ya Vitabu

 

Dhana hii ya mamlaka ya Allaah katika sheria ndio msingi mkuu wa Uislamu. Hakika wanachuoni wote wa Kiislamu wanakubaliana kwamba mamlaka ya sheria ni ya Kwake pekee Allaah. Hivyo, kwa mfano ndani ya kitabu chake maarufu: Al-Ihkaam fiy Usuul al-Ahkaam, ambacho kinahusu misingi ya Fiqh, mwanachuoni Amidiy ameandika kama ifuatavyo:

 

"Tambua kwamba, hakuna isipokuwa Allaah ndiye Mtawala na hamna amri inayofaa zaidi kutekelezwa ila iliyotolewa na Yeye"

 

Shaykh Muhammad Khadhiri, mwanachuoni wa Kimisri kwenye Misingi ya Shari’ah ya Kiislamu, anasema ndani ya kitabu chake cha Uswuul al-Fiqhi:

 

"Kwa vile amri ni za Kwake pekee Allaah, hakuna anayepaswa kutoa Amri ila Yeye. Hii ni nukta ambayo Waislamu wote wanakubaliana nayo."

 

Profesa Twaaha al-'Alwaaniy amenukuliwa akisema yafuatayo ndani ya kitabu chake cha Uswuul al-Fiqhi al-Islaamiy:

 

"Kuanzisha vifungu vya Shari’ah, kuamuru sheria kufuatwa, kuweka kanuni na amri, na kufasili mifumo; ni kazi ambayo ni maalumu kwa Allaah pekee. Yeyote anayejipa na kuandikia kazi hizi zaidi ya Allaah, ametenda dhambi ya shirk. Kwani, kufanya hivyo amekwenda kinyume kabisa na imani ya Upweke wa Allaah Tawhiyd."



 

Shari’ah Dhidi Ya Sheria

 

Ulimwengu wa leo una Shari’ah na Sheria. Shari’ah ni zile sheria za Kiislamu na Sheria ni zile zinazotungwa na mwanaadamu zisizo na msingi wa dini.

 

Kwa upande wa kesi, kuna kesi za madai (civil) na kesi za jinai (criminal). Kesi za madai ni migogoro baina ya pande mbili zilizofungua kesi. Kawaida kesi hizi hufunguliwa na wananchi wenyewe. Mfano A amemtukana jirani yake na pia rafiki yake wa enzi aitwae B. Hapa kama B amekasirishwa na maneno ya A, atafungua kesi dhidi ya A kuhusiana na madai yake.

 

Ama kesi za jinai, ni makosa dhidi ya Serikali, hivyo hufunguliwa na kusimamiwa kesi hizi na Serikali yenyewe. Kwa mfano makosa ya jinai kama wizi, ubakaji, ujambazi, utapeli, ulaji rushwa na mengineo.

 

Tumetoa maelezo haya ili kuonesha tofauti baina ya neno Shari’ah na Sheria ambayo tunayatumia kwenye kitabu hiki. Ni vyema pia tukiweka wazi kwamba kitabu chetu kitajikita zaidi kwenye mwenendo wa kesi za madai (civil procedure).

 

 

Mwenendo Wa Kesi Za Madai

 

Mwenendo wa kesi ni utaratibu wa hatua baada ya hatua katika kusuluhisha migogoro baina ya pande mbili kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa. Utawala wa haki unapatikana kutokana na mwenendo huru wenye maridhiano. Hivyo, pale mwenendo wa kesi utakapoegemezwa kwenye upendeleo, rushwa, ujinga wa kutoifuata sheria, basi hapo hapatakuwa na utawala wa haki.

 

Utawala wa haki chini ya Uislamu unaweza tu kutambuliwa na kusifiwa kwa watu wanaofahamu Qur-aan na Sunnah pamoja na maelezo ya Fiqhi. Kuna tofauti na yapo mengine yamefanana baina ya mwenendo wa Sheria na Shari’ah.

 

Maelezo yaliyomo ndani ya kitabu hiki yanachambua zaidi kuonesha uwiano uliopo baina ya pande hizi mbili za sheria. Lengo kuu likiwa ni kutenda haki na uadilifu kupitia mwenendo wa kesi.

 

 

Masharti Ya Uteuzi Wa Hakimu Wa Kiislamu

 

Ama kuhusu sifa za kuteuliwa kushikilia nafasi ya Hakimu wa Kiislamu, maelezo yafuatayo yanapatikana ndani ya Qur-aan na Sunnah:

 

a) {{Hakika Mwenyezi Mungu Anakuamrisheni kuzirudisha amana kwa wenyewe (wanaozistahiki). Na mnapohukumu baina ya watu mhukumu kwa haki.}} [4:58]

 

b) {{Hakika wale waliosema: "Mola wetu ni Mwenyezi Mungu," kisha wakatengenea, hawatakuwa na hofu (siku ya kufa kwao wala baadaye) wala hawatahuzunika).}} [46:13]

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

a) "Viongozi wenu walio bora ni wale muwapendao na wanaokupendeni na muwaombeao (kheri) na wanaokuombeeni (kheri), (lakini) viongozi wenu waovu kabisa ni muwachukiao na wanaokuchukieni na munaowalaani na wanaokulaanini" (Muslim)

 

b) "Naapa kwa Allaah, hatumpatii yeyote, shughuli za serikali yetu kwa yeyote anayeomba (dhamana) hiyo au aliye na uchu wa (dhamana) hiyo." (Al-Bukhaariy na Muslim)

 

c) "Tunawatambua wanaoomba cheo (cha kutoa haki na dhamana) kama ni asiye muaminifu." (Abu Daauud)

 

Sio tu Qur-aan na Sunnah, lakini pia taariykh yetu inathibitisha kwamba Uislamu haukubaliani na fikra ya mtu kuomba dhamana ya uongozi. Hivyo tunaelezwa na Qalqashandi:

 

"Imesimuliwa na Abu Bakr kwamba alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na uteuzi wa dhamana za uadilifu na haki. Alijibu: "Hivyo ni vya wale wasioshabikia navyo na wasio na uchu navyo; hivyo ni kwa wale wanaovikimbia mbali na sio wale wanaovikimbilia; hivyo ni kwa wale wanaopatiwa (bila ya kuviomba) na sio kwa wale wanaodai kuwa ni haki yao." [1]

 

Qur-aan inaeleza kwamba:

 

{{Wale ambao Tukiwamakinisha, (Tukiwaweka uzuri) katika ardhi husimamisha Swalah na wakatoa Zakaah na wakaamrisha yaliyo mema na wakakataza yaliyo mabaya. Na marejeo ya mambo ni kwa Mwenyezi Mungu.}} [22:41]

 

Aayah hiyo hapo juu inafafanua vipengele muhimu vya uadilifu kwa viongozi na wananchi pia. Vipengele hivyo muhimu ni kama vifuatavyo:

 

1. Waislamu wanawajibika kumtii Allaah na Mtume Wake, mmoja mmoja na kwa pamoja pia, na utiifu huu upewe kipaumbele kwa kila mtu mwengine. Bila shaka, utiifu kwa watu wengine unakuja baada ya kumtii Allaah na Mtume na sio kabla, na hili ni la lazima sio hiari.

 

Aayah na Hadiyth zifuatazo zinathibitisha hilo lisemwalo juu:

 

a) {{Haiwi kwa mwanamume aliyeamini wala kwa mwanamke aliyeamini, Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wanapokata shauri, wawe na hiari katika shauri hilo. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, hakika amepotea upotofu (upotevu) ulio wazi (kabisa).}} [33:36]

 

b) {{Na wasiohukumu kwa yale Aliyoteremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio makafiri …Na wasiohukumu kwa yale Aliyoteremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio madhalimu …Na wasiohukumu kwa (kufuata) yale Aliyoteremsha Mwenyezi Mungu basi hao ndio waasi.}} [5: 44, 45, 47]

 

c) "Muislamu ni lazima asikilize na amtii mtawala iwapo atakubaliana kwa aliloamrishwa na atalikataa, alimuradi tu hakuamrishwa kutenda dhambi. Kwa hali hiyo, asimsikilize wala asimtii." (Al-Bukhaariy na Muslim)

 

d) "Hata kama mtumwa aliye na sura mbaya atachaguliwa kuwa mtawala wenu na akatekeleza matakwa yenu kwa mujibu wa mafundisho ya Kitabu na Sunnah, ni lazima mumsikilize na mumtii." (Al-Bukhaariy na Muslim)

 

e) "Hakuna utiifu mbele ya dhambi…" (Al-Bukhaariy na Muslim)

 

f) "Hakuna utiifu kwa wanaomuasi Allaah" (Atw-Twabaraaniy)

 

Vipengele vilivyotajwa hapo juu kutoka Qur-aan na Sunnah vinaonesha wazi kwamba Mahakimu hawana haki ya kutoa hukumu kinyume na mafundisho ya Qur-aan na Sunnah na kama watafanya hivyo, Waislamu hawana ulazima kuwatii. Sio hilo tu, ukweli ni kwamba watakuwa wapo kwenye msimamo sahihi iwapo hawatowatii na wala hawatakuwa wametenda dhambi. Juu ya hivyo, iwapo jambo lolote litathibitishwa kuwa sahihi kwa mujibu wa muongozo wa Qur-aan na Sunnah haliwezi kutupwa na Hakimu wala kiongozi yeyote wa Serikali au sheria ya nchi.

 

Kwa maana hiyo, ni amri au sheria iliyopitishwa ndio yenye kugongana na Shari’ah – na sio Shari’ah – hilo liwekwe pembeni na litamkwe kuwa ni lenye kwenda kinyume – batili ultra vires.

 

2. Wakati huo huo, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe ameeleza ni wakati gani vipengele hivi vinaweza kuwekwa pembeni. Anasema:

 

a) "Pale watu wanapofanya hivi (yaani, wakisimama imara katika utawala wa Allaah na ukweli wa Utume, wakasimamisha Swalah na kutoa Zakaah), watahifadhiwa maisha yao kutokana na mimi (yaani Mahkama/Dola) isipokuwa wanapotenda kosa la jinai dhidi ya Shari'ah ya Kiislamu. Ama kwa uchambuzi wa nia zao, Allaah pekee Anaweza kuwa Hakimu." (Al-Bukhaariy na Muslim).

 

b) "Yeyeote anayeitamka (Kalimah ya Tawhiyd) analazimika kuhifadhiwa maisha na mali yake, alimuradi tu hajiwajibishi kwa madhambi mbele ya (Shari'ah za) Allaah, na Allaah Pekee ndio Mwenye kuhukumu niyah." (Al-Bukhaariy na Muslim)

 

Hadiyth hizi zinahakikisha hifadhi ya maisha, mali na heshima ndani ya mipaka ya Shari’ah na fikra zake. Mipaka ya hifadhi hii chini ya Shari’ah inapanuliwa hata kwa wasio Waislamu wote, ambao wanaishi chini ya himaya ya Dola la Kiislamu, hupatiwa haki sawa ambazo Waislamu wanazipata.

 

3. Ama kwa upande wa utaratibu au mwenendo wa kufuata kutimiza haki, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameeleza kanuni ifuatayo:

 

"Watu wawili wanapofikisha mgogoro kwako kwa kutolewa maamuzi, usitoe hukumu isipokuwa tu pale utakapowasikiliza sawa sawa wote." (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na Ahmad).

 

Katika kesi aliyohukumu Sayyidna 'Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu) ametengeneza kanuni ifuatayo:

 

"Kwa mujibu wa Shari’ah ya Kiislamu, hakuna atakayefungwa bila ya kutenda haki (kisawasawa kwake)." (Maalik; Muwatta)

 

Tunajifunza kutoka maelezo yaliyomo ndani ya Muwatta kwamba, katika sehemu mpya zilizotekwa za Iraaq, baadhi ya watu walianza kufitinisha na kutengeneza tuhuma za uongo mmoja dhidi ya mwengine, na kwa mtindo huu, waliweza kuwapeleka wengi jela. Malalamiko hayo yalipofikishwa mbele ya Sayyidna 'Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu), alitoa amri hiyo hapo juu. Ina maana kwamba hakuna mtu atakayefungwa bila ya utaratibu maalum wa mwenendo wa kesi ndani ya Mahkama na bila ya kumpatia fursa nzima ya kujitetea.

 

4. Pale Khawaarij wasioamini Dola yoyote walipoibuka kutaka kufanya mapinduzi wakati wa ukhalifa wa Sayyidna 'Aliy (Radhiya Allaahu ‘Anhu), aliwaandikia:

 

"Mnaweza kuishi na kuhama sehemu yoyote muipendayo, alimuradi tu hamumwagi damu na kueneza migogoro na kuhifadhi uhaini. Lakini mukitiwa hatiani kwa kosa lolote miongoni mwa haya, nitapigana vita dhidi yenu." (Ash-Shawkaaniy, Nayl al-Awtaar)

 

Kutokana na maelezo haya, inaonekana wazi kwamba dhana ya uadilifu ya Kiislamu hairuhusu Hakimu kupewa mamlaka ya kukamata au kufunga au kuua au kutoa haki za imani, maoni, mawazo ya mtu yeyote bila ya kufuata Shari'ah madhubuti zinazokutana kwenye uadilifu.

 

Juu ya hivyo, tunajifunza kutokana na vyanzo sahihi kwamba Uislamu hauruhusu ubaguzi baina ya Hakimu na watu wa kesi kwa mnasaba wa Shari'ah, haki na uadilifu. Kunatakiwa kuwepo na ibakie kuwepo sheria iliyo sawa, mwenendo sawa na Mahkama sawa kwa hao wote. Kabla ya kifo chake, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alijiwasilisha yeye mwenyewe kwa kuridhia dai lolote ambalo mtu anawezekana kuwa nalo dhidi yake. Halikadhalika, Sayyidna 'Umar alimlazimisha Jabalah bin Aiham Ghassani, mkuu wa kabila, kuthibitisha dai la mtu dhidi yake. Pia, alikataa kukubaliana na ombi la 'Amr bin al-'Aas kwenye kugawa kategoria (kuweka ubaguzi) kwa lengo la kulinda heshima za watawala. Sio hilo tu, mtawala alimpatia kila mtu haki ya kumfungulia kesi ndani ya Mahkama ya kawaida.

 

 

Wajibu Wa Hakimu

 

Lengo kuu la ofisi ya Hakimu ni kutenda haki kwa uwazi na azma njema. Mwenendo ulioelezwa humu ni msaada wa wanachuoni mbalimbali ili kuwanufaisha wale wenye kiu ya elimu ya haki na uadilifu kwa mujibu wa Shari’ah. Sio lengo kabisa kwa Hakimu wa Kiislamu kuwa mjinga, mpokea rushwa na asiyetenda haki.

 

Ni vyema tukabainisha ya kwamba hamna utaratibu na mwenendo rasmi wa kesi utakaoelezwa moja kwa moja, isipokuwa njia yoyote itakayopelekea haki kutendeka na kuwatosheleza pande mbili zenye kudai haki, basi hio njia tutaikamata na kuibainisha kuwa ni sahihi kwa Uislamu. Bila ya shaka, Hakimu anateuliwa akiwa ni mjuzi wa mambo, hivyo yafaa kutumia hukumu zilizopita precedence kwenye uamuzi wa migogoro mipya.

 

Mengi yameelezwa na wanachuoni wetu kuhusu Hakimu wa Kiislamu, lakini ni machache yaliyoelezwa kuhusiana na taratibu za kazi yake ya Ki-Shari’ah. Huenda hili lilitendeka kwa sababu mbili. Kwanza, wanachuoni walielekeza nguvu zaidi katika Shari’ah na sio mwenendo wa Shari’ah kwa kuwanufaisha wanajamii na Hakimu. Pili, jamii ya enzi za Maswahaba na Matabi'ina ni tofauti sana na ya kwetu. Sasa, idadi ya watu imeongezeka, matatizo yamezidi kuwa magumu kutokana na siasa za kutungwa na misimamo ya uchumi yenye uoni wa mambo ya anasa. Ni kwa sababu hizo, mwenendo wa kesi za sasa katika Shari’ah ni wenye kupatiwa maelezo ya kina, uchambuzi na fafanuzi za jumla jamala ili kuondosha migogoro, dhana mbovu na itikadi au mila zisizo sahihi.

 

Pamoja na kuangalia mahitaji ya karne yetu hii, kitabu hiki kimekusanya muongozo wa Qur-aan, Sunnah, majadiliano na fafanuzi za wanachuoni, kwa kuchukua maelezo ya hapa na pale ili ipatikane picha nzuri ya namna Hakimu wa Kiislamu anavyotakiwa kutenda na kupambanua baina ya mwenendo wa kesi za Shari’ah na Sheria.

 

Mifano mingi iliyoelezwa humu, yaweza kwa kiasi kikubwa kutendeka chini ya Taifa la Kiislamu liliopo zama za awali za Uislamu. Hata hivyo, mengi yaweza kufanyiwa kazi kwa Hakimu wa Kiislamu hata kama akiwa ameteuliwa kushikilia wadhifa huo akiwa yupo ndani ya taifa lisilo la Kiislamu. Ingawa hiyo Sheria anayoisimamia haina msingi wa maadili bora wala kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), lakini lengo la Shari’ah na Sheria linafanana kuwa ni kutenda haki na uadilifu. Kinachoharibu upande wa Sheria ni kubeza taratibu za Shari’ah pamoja na kutengua maadili kama mzizi wa sheria.

 

Kuna faida kubwa ya kuitafsiri barua ya Sayyidna ‘Umar kwa Abu Muusa al-Ash’ari (Radhiya Allaahu ‘Anhuma). Barua hii itatusaidia sana kuchora ramani ya kitabu hiki:

 

1.     Hakika Hakimu ana majukumu mazito na njia yake inayofanana kwa vitendo.

2.     Elewa mgogoro ulioletwa mbele yako, kwa sababu kuitamka hukumu iliyo ya haki bila ya kuifanyia kazi haitokuwa na maana.

3.     Waone wote walio mbele yako ni sawa, wakusanye Mahkamani na hukumu (itolewe wazi) ili aliye juu asiwe na matumaini ya dhulma, na aliye chini asikose imani ya hukumu yake.

4.     Wajibu wa kuthibitisha ni kwa yule aliyedai au kutuhumu, na kiapo ni kwa yule anayekataa.

5.     Suluhisho baina ya Waislamu ni halali, isipokuwa kwa suluhisho litakalofanya halali kuwa haramu na haramu kuwa halali.

6.     Yule ambaye anaelemea ushahidi usiokuwepo, muwekee muda; kama ataleta ushahidi wake ndani ya kipindi hicho, mpe haki yake iwapo anastahiki, kama akishindwa kufanya hivyo, igeuze hukumu dhidi yake. Hili ni ombi la mwisho na uwazi utakaoondosha giza.

7.     Jiepushe na hukumu yako ya jana ambayo baadaye umetanabahi kwenye akili yako na ukaongozwa njia sahihi kurudi kwenye hukumu ya haki, kwa sababu haki inasimamishwa (daima), na hakuna chochote kinachobatilisha kilicho haki, kwa sababu ni bora kurejea kwenye usahihi kuliko kuendelea na lisilo sahihi.

8.     Ushahidi wa Waislamu wote unatumika kwenye kesi ya mtu mwengine yeyote, isipokuwa ushahidi wa aliyetumikia hukumu ya kesi ya huduud[2] au amewahi kujaribu kutoa ushahidi wa uongo, au ushahidi wa yule anayeshukiwa kuwa ni jamaa au anayehusiana naye.

9.     Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anaelewa siri zilizofichikana ndani ya nafsi za waja Wake na Ameweka gamba juu yao kwenye huduud, isipokuwa litakalodhihirika kupitia ushahidi au kiapo.[3]

 

 

Fafanuzi Za Maneno

 

Shari’ah: Ni vyanzo vya sheria vinavyotokana na misingi mikuu ya sheria za Kiislamu kutoka kwenye Qur-aan na Sunnah pamoja na vyanzo vyengine vidogo kama Qiyaas, Ijma’ na vyenginevyo.

 

Sheria: Kwa mnasaba wa kitabu hiki, tunalifasili neno hili kuwa: Ni sheria ambazo zimetungwa na mwanaadamu zinazodai kuwa hazina uhusiano wa dini yoyote kwa ajili ya kuweka misingi na kanuni za maisha ya mwanaadamu hapa duniani. Neno hili "Sheria" limeanza kutumika zaidi kuanzia Sura ya Pili ili kupambanua baina ya sheria za Kiislamu na zile zinazotungwa na mwanaadamu.

 

Hakimu: Ni mtu mwenye mamlaka ya kubainisha wapi ilipo haki, kuisimamia na kuifanyia kazi hiyo haki. Neno 'Hakimu' ndani ya kitabu hiki linaenda sambamba na neno 'Mahkama'. Kwa mfano tunaposema 'Mahkama itaamrisha….' ina maana ya 'Hakimu ataamrisha…'

Pia 'Hakimu' lina maana sawa na 'Qaadhi' ingawa 'Qaadhi' linatumika sana kwa Mahkama za Kiislamu kinyume na 'Hakimu' ambalo linatumika katika Mahkama mbalimbali nchini Tanzania. Ni vyema tukaeleza kwamba 'Qaadhi' sio tamko lililo takatifu kutoka Qur-aan Tukufu. Taariykh inaonesha kuwa 'Qaadhi' ilianza kipindi cha utawala wa Ufalme wa Umayyah (Umayyad Dynasty) na kazi zake zilikuwa ni kusimamisha haki na kutoa ufafanuzi kwenye vipengele vya Sháriah. 'Qaadhi' waliwajibika kutumia Qur-aan na Sunnah.

Dai (Da’wa): Inatafsiriwa kama ni kuomba kwa nguvu za Ki-Shari’ah kutoka kwa yule mtu anayedai kuwa na haki dhidi ya mwengine mbele ya Hakimu.

 

Mdai (Muddai’i): Mtu anayefanya maombi anaitwa mdai. Pia huitwa Mlalamikaji.

 

Mdaiwa (Muddaa’ ‘alayhi): Yule mtu anayefanyiwa dhidi yake hayo maombi anaitwa mdaiwa. Pia anaitwa Mlalamikiwa.

 

Wadaawa: Mdai na mdaiwa wanapounganishwa kwa kuwaelezea pamoja, hutumika neno la wadaawa. Hivyo, wadaawa ni mdai/wadai pamoja na mdaiwa/wadaiwa.

 

Kwa uwazi, anayedai ndie mdai, anayedaiwa ni mdaiwa na hicho kinachodaiwa ndio dai. Kwa mfano A ametukanwa na B, A atafungua kesi ya kutukanwa kutoka kwa B. Hivyo, A ni mdai (aliyetukanwa), B ni mdaiwa (aliyetukana), na tendo la kutukanwa ndio dai lenyewe.

 

Kwa maana nyengine, anayedai ni mtu anayewajibika kuacha dai (kufuta kesi) kama akipenda na mdaiwa ni mtu asiyeweza kufanya hivyo kwa mapenzi yake kukimbia shauri lililowekwa mbele ya Hakimu. Hivyo, mdaiwa ni mtu aliyekuwa na uwezekano wa kukubali madai bila ya kuwasilisha ushahidi.

 





[1] Qalqashandi, Subh al-A'sha, J. 1, uk. 240.

[2] Kesi za jinai katika Shari’ah kama wizi, zinaa, unywaji pombe n.k.

[3] Angalia Al-Bayhaqiy; As-Sunan Al-Kubraa, X, uk. 150.

Share

008-Hakimu Wa Kiislamu: Sura Ya Pili

 

SURA YA PILI

 

UFUNGUZI WA KESI

 

 

Nani Anayeweza Kudai?

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatueleza kuwa mtoto kabla kubaleghe, mtu aliye kwenye usingizi na mwenda wazimu hawaandikiwi dhambi. Hivyo hawawezi kwa nafsi zao kuingia kwenye masuala ya mikataba au ufunguzi wa kesi au kudaiwa.

Mtoto mdogo na yule asiyekuwa na akili, hawawezi kufungua kesi bila ya kusimamiwa na mlezi au msimamizi. Mada hii imeelezwa vyema na wanachuoni tofauti.

 

Dai linaweza tu kufunguliwa na mtu mwenye akili timamu. Hivyo, dai la mtoto au mwendawazimu halitosikilizwa isipokuwa kupitia kwa mlezi, wala shauri halitosikilizwa dhidi yake bila ya kuwa na mwakilishi.

 

Sheria inaruhusu kuwepo msimamizi wa mtoto na mwenda wazimu. Kesi yoyote ya mtoto mdogo itafunguliwa kwa jina lake lakini itasimamiwa na mlezi wake.[1] Mahkama itakaporidhika kwamba mdaiwa ni mtoto mdogo au mwenda wazimu, wala hana mtu wa kuisimamia kesi yake, itateuwa mtu anayefaa kuwa ni wakala wake.[2] Hata hivyo, msimamizi huyo ni lazima awe ni mwenye umri wa mtu mzima na wala asiwe na nia mbaya juu ya usimamizi wake.[3]

 

 

Uteuzi Wa Mahkama Inayofaa

 

Mtu ambaye anataka dai lake lisikilizwe, kwanza kabisa ateue Mahkama inayofaa, ile ambayo ina nguvu ya Kisheria kusikiliza lalamiko hilo. Uteuzi wa Mahkama inayofaa ni jambo jepesi chini ya mfumo wa Kiislamu.

 

Isipokuwa kwa sasa, nguvu za Kisheria za Hakimu fulani zitakuwa zimebanwa kulingana na amri ya uteuzi wake ambapo amepatiwa aina fulani tu za kesi anazozitolea hukumu. Mdai anawajibika kupeleka maombi yake kwenye Mahkama ambayo mipaka yake ya kisheria anaishi yeye na mdaiwa wake. Na haitoleta tofauti yoyote kwenye sehemu hii kuhusu kiini kikuu cha madai.

 

Kwa mfano, ardhi ipo sehemu nyengine au mtu ambaye amedaiwa anaishi kwenye nguvu za Kisheria za Hakimu mwengine. Zote kwa pamoja, zitakuwa na nguvu sawa sawa mbele ya Mahkama. Kitakachotofautiana ni thamani ya ardhi hiyo.

 

Kesi yoyote kwa mujibu wa Sheria itafunguliwa kwenye Mahkama yenye mamlaka ya kuisikiliza. Madai hayo ni lazima yawe ndani ya mipaka ya Mahkama hiyo.[4] Pale ambapo dai ni la thamani ya kitu kisichohamishika kama vile ardhi iliyopo kwenye mamlaka ya Mahkama nyengine, inaruhusika kufungua kesi hiyo kwenye Mahkama yoyote yenye mamlaka ya kusikiliza madai ya ardhi kama hiyo.[5] Inapotokezea hitilafu ya eneo la ardhi iwapo lipo ndani ya mamlaka ya Mahkama Y au Mahkama X. Moja kati ya Mahkama hizo, itaweka kumbukumbu ya maelezo hayo na kuisikiliza kesi hiyo kama vile imo ndani ya mamlaka yake. Pingamizi ya kwamba Mahkama haikuweka kumbukumbu hiyo itatupiliwa mbali na Mahkama ya juu pale itakapokatiwa rufaa ikiwa tu Mahkama hiyo iliendelea kusikiliza kesi hiyo kwa lengo la kutenda haki na uadilifu. [6]

 

 

 

Dai Lazima Litimize Kanuni Zake

 

Al-Mawardi anajishughulisha na mada hiyo kwenye kitabu maalum chenye jina la Sayr ad-Dalawa-Safari - Kuhusu Mwenendo Wa Kesi. Kwa mujibu wa al-Mawardi na Ibn Qudaamah, madai ni lazima yawe kwa maandishi[7].

 

Wakati wa kipindi cha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Makhalifa waongofu, madai mengi yakitolewa hukumu kwa njia ya mdomo na amri kupitishwa bila ya shaka kwa mdomo. Siku zilivyoenda mbele na kufanya maandiko kuwa rahisi, wanachuoni wakapendekeza kwamba madai na hukumu zake ziwe kwa maandishi.

 

Hata hivyo, ni vizuri kufafanua kwamba Qur-aan tukufu inatilia mkazo zaidi kufanya shughuli zenye mnasaba wa amana kama vile mikataba (na madai) kwa njia ya maandishi, Qur-aan inasema:

 

{{Enyi mlioamini! Mnapokopeshana deni kwa muda uliowekwa, basi iandikeni…}} [2: 282]

 

Kwa kutumia Aayah hiyo, ni usalama zaidi kufanya madai hata katika kuitoa hukumu kwa maandishi.

 

Kuna kanuni nyengine kadhaa ambazo dai ni lazima litimize. Kwa mfano, mtu mmoja au walio wengi dhidi ya yule anayependekezwa au wanaopendekezwa (kudaiwa) a/watambulike. Kitu hicho au hali inayodaiwa ni lazima pia iwekwe wazi na sifa zake zilizokuwa wazi. Kwa mfano, kama ni ardhi, aeleze namna alivyoipata, mipaka yake ni lazima iwekwe wazi ijapokuwa thamani yake haina haja ya kutajwa. Kama dai linahusika na deni, ni lazima aeleze namna lilivyopatikana deni hilo, aeleze kama ni aina ya pesa iliyoazimwa, pesa iliyonunuliwa au mshahara, na nyenginezo na pia thamani yake iwekwe wazi.

 

Kinachodaiwa kiwe kinawezekana kudaiwa, ili kwamba ikiwa haiwezekani kwa mujibu wa uzoefu na hukumu zetu, dai hilo litupwe. Kwa mfano, X anaonesha kuwa na umri wa miaka 35, lakini anadai kuwa ni mkubwa kuliko Y ambaye ni mzee anayefika miaka 60. Au B anayedai C kuwa ni mwanawe, ilhali yatambulika kwa uwazi kuwa C ni mtoto wa A.

 

Maelezo ya madai kama si ya ulinganifu (kigeugeu) na hayana muelekeo wa kutendeka haki yatakataliwa. Kwa mfano, X amekwenda dukani kununua bidhaa, kabla ya kuinunua anadai ni ya kwake. Hapa X atakuwa hana haki ya kudai kutouziwa bidhaa hiyo, kwani hajaenda kununua ila amedai bidhaa isiyo na uhakika wa milki ya X. Lakini, hata hivyo, kama madai ya mdai yatarekebishwa na kueleweka, madai yake yatahitaji kusikilizwa na pingamizi ya kukosekana muelekeo wa kesi haitakuwa na mashiko kwasababu madai yameshafanyiwa marekebisho.

 

Madai yaweza kuwa kwa matamshi au kwa maandishi. Kama ni matamshi, Mahkama itawajibika kuyawekea kumbukumbu.

 

Madai pia ni lazima yaweke wazi vizuri kiini cha madai dhidi ya yule mtu anayedaiwa, inaweza kujaribiwa kwa aidha, kama mtu huyo atakubali tuhuma za madai, ambapo maamuzi yatatolewa dhidi yake. Kama mdaiwa atakana madai hayo, kesi itaendelea dhidi yake kama ni mshindani (khaswm) wa mdai, na mdaiwa ataitwa kuja kujibu hoja. Jaalia, mdai anatamka kwamba wakala wa mdaiwa amenunua bidhaa fulani kutoka kwake, na anadai malipo, lakini mdaiwa anakana dai hilo, mdaiwa atatambulika kuwa ni mshindani na kesi itaendelea dhidi yake. Kwa upande mwengine, kama mdai kiurahisi tu atatuhumu kwamba wakala wa mdaiwa hakulipa malipo na mdaiwa akakataa dai, kesi haitosimama na wala haitasikilizwa kama yalivyo madai ya mdai kwani hayajaweka wazi kiini cha madai dhidi ya mdaiwa. Kwa mfano, mdai ameshindwa kuonesha namna na sababu gani anayostahiki kulipwa malipo kutoka kwa mdaiwa.

 

Hivyo, ni lazima madai yawe na maelezo yote muhimu kuhusiana na kinachodaiwa kwenye kesi pamoja na sababu ya kudai hicho kinachodaiwa na maombi ambayo Mahkama itatakiwa itolee hukumu.

 

Mwandishi wa kitabu cha al-Hidayah anashauri kwamba: pale inapotokezea kwamba kitu kinachodaiwa hakipo na wala hakijulikani, basi madai yatawajibika kutupwa, kwani hayana maelezo ya kinachodaiwa[8].

 

Ibn Farhuun anaweka vipengele vitano vya madai:

 

1)    Kinachodaiwa kijulikane.

2)    Kama mdaiwa atakubali ukweli wa madai, kitulizo (relief) kitolewe.

3)    Madai yasiwe ya uchokozi (madai ya uongo).

4)    Madai yaletwe yakiwa na sababu maalum.

5)    Madai yawe na sababu nzuri ambayo hayatokataa ukweli wake[9].

 

Mwandishi wa al-Hidayah anaendelea kueleza kwamba ikiwa ni kesi ya kitu kinachoweza kuhamishika, basi ni lazima kiletwe Mahkamani (kama inawezekana), ili kiwekwe wazi na kutambuliwa. Kama hakiwezekani kielezwe ukubwa wake, thamani, jinsia, aina na sifa yake zote zielezwe.

 

Kwa kitu kisichohamishika, maelezo ya kina ya mipaka pamoja na watu, unganisha na maelezo ya wanafamilia, namna ya mipaka na walio jirani watajwe. Inatosha kama ni mipaka mitatu tu ya kesi ya ardhi itatajwa, kwa mujibu wa wanachuoni wengi wa wafuasi wa Abu Haniyfah[10]. Wanachuoni wengine kama Ibn Qudaamah na al-Mawardi, wana mtazamo kwamba mipaka yote minne itajwe[11].

 

Sheria kwa upande wake inaeleza kuwa dai ni lazima lipelekwe Mahkamani ama kwa mdomo au maandishi likiwa na maelezo yaliyo wazi ya dai hilo.[12] Madai hayo yawe na kiini chake.[13] Pale mdai anapoegemeza madai yake kwa hoja ya kutenzwa nguvu, makosa ya makusudi, uongo n.k. itamwajibikia kuyaeleza ndani ya madai (pamoja na tarehe kama inahitajika).[14] Baada ya kufunguliwa kesi na kuanza kusikilizwa, madai hayataruhusika kuibua hoja mpya ya dai au kuingiza madai mengine yasiyoendana pamoja na madai yaliyofunguliwa hapo mwanzo.[15] Hata hivyo, Hakimu ana uwezo wa kuamrisha kuondoshwa baadhi ya vifungu vilivyomo ndani ya madai ikiwa anaamini kuwa kubakia kwake vitaifanya Mahkama kutotenda haki na uadilifu au kupelekea kwenye sakata lisilo na msingi.[16]

 

Vifungu vifuatavyo ni lazima vitimizwe ndani ya madai:

 

(a)             jina la Mahkama ambayo dai linapelekwa,

(b)             jina na anwani ya mdai,

(c)             jina na anwani ya mdaiwa,

(d)             kama mdaiwa ni mtoto au mwenda wazimu, ielezwe,

(e)             hoja za kufungua kesi na lini liliibuka,

(f)               hoja za kuonesha kwamba Mahkama inayo mamlaka,

(g)             kitulizo anachodai mdai,

(h)             kama mdai amesamehe kiwango cha dai, ielezwe,

(i)                thamani ya kinachodaiwa kwa mnasaba wa mamlaka na malipo ya Mahkama, yaelezwe.[17]

 

Pale dai linapohusu malipo ya fedha taslim, ni lazima dai lieleze idadi halisi ya fedha inayodaiwa.[18] Na kama ikiwa ni fedha iliyokopeshwa, dai pia liweke wazi maelezo yote yanayohusiana na mkopo huo. Kwa mfano, tarehe ya mkataba, tarehe iliyotakiwa kulipwa, fedha iliyolipwa na iliyokuwa bado (kama ipo).[19] Ama ikiwa ni dai la kitu kisichohamishika kama vile ardhi, dai ni lazima lieleze mipaka ya ardhi hiyo pamoja na nambari za kumbukumbu ya upimaji.[20]

 

 

Kuunganisha Kwa Pande Za Watu

 

Inaweza kutokea kwamba watu wawili au zaidi wamehusika kwenye kuvunja Shari'ah, au wana faida fulani katika kukataa haki ya mdai, wengine ni wengi zaidi kuliko wengine au wote kwa nguvu moja, au zaidi ya mtu mmoja ana faida katika kuanzisha dai. Hapo, suala muhimu linakuja katika uteuzi wa watu na Shari'ah inaweka wazi kanuni kwa lengo la uteuzi huo. Kwa mfano, pale dai linapofanywa kwa madhumuni ya bidhaa mahsusi, yule mtu ambaye anayo milki nayo afanywe kuwa mdaiwa peke yake.

 

Hivyo, kama A amechukua milki ya farasi visivyo halali anayemilikiwa kihalali na B na kumuuza kwa C na B anamtaka farasi wake, B anaweza kumfungulia kesi A na C kwa pamoja, ingawa A ndiye aliyechukua lakini kwa sasa C ndie mwenye milki ya mnyama. Yule mtu ambaye anayo milki, atalazimika kumfungulia kesi mchuuzi wake kwa kurudishiwa thamani aliolipa. Mifano  mengine ni mdhaminiwa aliyeajiriwa, mtu aliyekuwa na nguvu ya kutumia kifaa, na mpangaji, pale mali iliyokuwa kwenye mamlaka yao imechukuliwa visivyo halali na mwengine, wanaweza kumfungulia kesi aliyefanya kosa kwa kurudisha kifaa bila ya kumfanya mmiliki (mfano mdhamini au mpangishaj) kuwa ni upande wa kesi.

 

Kwenye masuala ya mali ya aliyefariki, kanuni ya jumla ni kwamba, mmoja kati ya warithi anaweza kuwa ni mdai au mdaiwa kwa mnasaba wa madai ambayo yanaweza kufanywa kwa niaba au dhidi ya aliyefariki. Isipokuwa pale ambapo dai hilo ni kurudishwa kwa mali maalum kutoka kwa milki ya aliyefariki, ambapo mdaiwa anayefaa ni mtu mwenye kuwa nayo hiyo mali na mrithi asiyekuwa nayo hiyo mali hawezi kufanywa kuwa ni mdaiwa.

 

Ni hivyo hivyo kwa kesi ya kukubali kuwa mrithi, au kuhodhi mali ya aliyefariki, au kuwazuia warithi wengine. Mmoja kati ya warithi atakuwa na nguvu ya kufungua kesi kwa niaba yaaliyefariki kwa kitu ambacho kilikuwa ni haki yake aliyefariki kutoka kwa mdaiwa, kwa muundo wa deni au mfano wa hiyo haki au wajibu kwa aliyefariki kutoka kwa mdaiwa. Kama dai litatimizwa, maamuzi yatatolewa kwa mali anayostahiki kwa faida ya warithi wote. Mdai yeye mwenyewe, hata hivyo, ataruhusika kuitambua sehemu yake ya urithi.

 

Mfano: Kama X ana dai la pesa dhidi ya mali iliyoachwa na aliyefariki Y, anaweza kuthibitisha dai lake mbele ya warithi A, B au C (mmoja tu kati ya warithi). Ikiwa kama X amehodhi (ameitia mkononi) au hahodhi (hajaitia mkononi) sehemu yoyote ya mali ya aliyefariki Y. Ingawa kukubali kwa mmoja kati ya hao warithi kwamba X anahodhi au hahodhi mali ya aliyefariki Y, hakutowafunga warithi wengine wasidaiwe na X. Kama mmoja kati ya A, B au C hatokubali dai, na X atathibitisha dai lake mbele ya A, B au C, maamuzi yatapitishwa dhidi ya warithi wote na warithi wengine hawatolazimika kumtaka X kuthibitisha dai lake dhidi yao kwa mnasaba wa sehemu ya urithi wao. Hata hivyo, wapo wazi (A, B au C) kukubaliana na maamuzi hayo kwa maombi ya kujitoa kwenye madai (ili wawe na kesi tofauti).

 

Wenye hisa wanapokuwa wengi katika mali mahsusi lakini sio kwa haki ya kurithi, mmoja kati ya wenye hisa hawezi kuwakilisha wengine kama ni mdaiwa katika kesi kwa mnasaba wa mali hiyo, lakini kama atalalamikiwa na kufunguliwa kesi peke yake, maamuzi yaweza kutolewa dhidi yake kwa kiwango cha hisa zake.

 

Mwananchi wa eneo anaweza kufungua kesi kwa mali au suala lenye manufaa ya jamii nzima kama vile bughudha za walevi zinazotokana na klabu inayopigisha miziki usiku kucha (public nuisance); na maamuzi kumpendelea yeye yatatolewa kwa manufaa ya wananchi wote wa eneo hilo. Kwenye kesi kuhusiana na kitu chenye manufaa ya jamii ambacho kinatumiwa na watu wa vijiji viwili, kama vile mkondo au kisima, inatosha kwa baadhi ya watu wa kila kijiji kuwa ni wahusika, isipokuwa pale Mahkama itakapoweka idadi maalum ya watu. Idadi inapozidi mia moja, inatambulika ya kwamba hakuna kizuizi.[21]

 

Sheria inaeleza kwamba kuunganishwa kwa pande za wadai tofauti inawezekana ndani ya kesi moja. Kesi ambayo haki au fidia kwa mnasaba wa tendo au makubaliano yamefanywa, ikiwa kwa pamoja, au mmoja mmoja.[22]

 

Masharti muhimu ambayo yameeleza kwamba ni lazima yathibiti yamo ndani ya kesi ya Stroud dhidi ya Lawson[23], ambayo Mahkama iliamuru:

 

"Inatosha kwamba masharti haya yatimizwe, ni kusema kwamba, haki ya kitulizo (relief) inayodaiwa kuwepo kwa kila mdai iwe kwa mnasaba kwamba imetokana na mauziano hayo hayo, na pia kwamba kuwe na hoja moja ya msingi, ili kwamba kesi iwe ndani ya kanuni hiyo hiyo."

 

Mdai anaweza kuunganisha wadaiwa kwa kufuata masharti maalum yaliyoelezwa hapo juu.[24] Hata hivyo Hakimu anayo nguvu ya kumtoa mdai au mdaiwa yeyote iwapo ni kwamba huenda kuunganishwa huko kutaishushia heshima pande nyengine.[25]

 

 

Utaratibu Pale Mdaiwa Anapoishi Nje Ya Mpaka

 

Kwa mujibu wa hukumu za jumla katika Shari’ah zinazopatikana kwa kufananisha (al-Qiyaas), maamuzi ya Hakimu yanamfunga mdaiwa ambaye anaishi ndani ya mipaka yake. Lakini kwa mujibu wa hiari ya wanachuoni ambao wanakubaliana na Maswahaba na warithi wao na inaegemezwa kwenye dharura, kama mdaiwa yupo ndani ya mipaka ya Hakimu mwengine, mdai anaweza kufungua kesi yake katika Mahkama ndani ya mipaka hiyo anayoishi na mashahidi wake wanapatikana.[26] Hakimu ambaye kesi imefunguliwa katika Mahkama yake, anaweza kuweka kumbukumbu ya ushahidi na halikadhalika kutoa amri yake ikiangaliwa kwamba mdaiwa aliyeshindwa kufika aidha ameteua wakala kumwakilisha yeye au Mahkama yenyewe imeteua mtu kuangalia faida yake.

 

Lakini usahihi wa uteuzi wa Mahkama wa wakala, kwa ajili ya mdaiwa kwa kesi kama hiyo haionekani kuwa haina mashaka. Kama ushahidi uliotolewa na mdai huthibitisha kesi yake, Mahkama inaweza kuweka kumbukumbu kwa yale iliyoyaona na kutoa hukumu na baada ya mali kuizuia na kudhibiti kumbukumbu mbele ya mashahidi wawili kwa Hakimu ambaye ndani ya mipaka yake, mdaiwa anaweza kupatikana. Kama mdaiwa asiyehudhuria hajawakilishwa na wakala wake, Mahkama ambayo imefunguliwa kesi, inaweza kama ikichagua kufanya hivyo, kuweka kumbukumbu wa ushahidi na kuupeleka kwa Hakimu wa sehemu ambayo mdaiwa anaishi, kwa minajili ya Hakimu huyo kupitisha amri hiyo mbele ya mdaiwa.

 

Mienendo hii inaruhusiwa kwa kesi tu zinazohusiana na kutoa haki binafsi, kama vile kurudisha deni, kuthibitisha ndoa au uzazi (mfano mtoto A ni wa mzazi B), kurudisha mali isiyohaulishika (non transferable) na mfano wa hayo na sio kwenye masuala ya hadd (jinai) na kulipiza kisasi.

 

Ama kwa upande wa Sheria inaeleza kwamba hati ya madai inaweza kupelekwa kwa mdaiwa ikiwa yupo au hayupo ndani ya mipaka ya Mahkama iliyoitoa hiyo hati. Hati hivyo itapelekwa kwenye mipaka ya Mahkama ambayo mdaiwa anaishi na Mahkama hiyo itaifanyia kazi kama vile imeitoa binafsi. Baadaye itaweka kumbukumbu pamoja na mwenendo wowote uliotumia na kuirudisha Mahkama iliyoitoa.[27]

 

 

[1] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XXXVI, r. 1.

[2] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XXXVI, r. 3 (1).

[3] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XXXVI, r. 4 (1).

[4] Sheria ya Mwenendo wa Madai, S. 10 – 11.

[5] Sheria ya Mwenendo wa Madai, S. 12.

[6] Sheria ya Mwenendo wa Madai, S. 13

[7] (a) al-Mawardi; Adaab Al-Qaadhi, II, uk. 330-355 (b) Ibn Qudamah, Akhbaar Al-Qudhaat, IX, uk. 84.

[8] Al-Marghinani; Al-Hidayah, II, uk. 201.

[9] Ibn Farhuun, Tasbirah, I. uk. 86-88.

[10] Al-Murghinani; Al-Hidayah; II, uk. 201-202.

[11] (a) Ibn Qudamah; Akhbaar Al-Qudat, IX, uk. 85-86 (b) Al-Mawardi; Adab Al-Qaadhi, II, uk. 330.

[12] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. IV, r. 1.

[13] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. VI, r. 2.

[14] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. VI, r. 4.

[15] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. VI, r. 7.

[16] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. VII, r. 16.

[17] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. VII, r. 1.

[18] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. VII, r. 2.

[19] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. VII, r. 3.

[20] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. VII, r. 4.

[21] Al-Majallah, uk. 277-278.

[22] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. I, r. 1

[23] Stroud V. Lawson, (1898) W Q. B. 44, uk. 52.

[24] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. 1, R. 3 na 5.

[25] Angalia kesi ya The Bank of India V. Shah, (1965) E. A. 18.

[26] Al-Hidayah, Juzuu ya VI, uk. 381-390.

[27] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. V, r. 21-22

 

Share

009-Hakimu Wa Kiislamu: Sura Ya Tatu

 

SURA YA TATU

 

HATI

 

 

 

Nyaraka

 

Mara nyengine, hati za karatasi zinakubaliwa kama ni mbadala wa kiapo cha mdomo. Lakini Mahkama hairuhusiwi kutoa maamuzi kwa kutegemea tu hati iliyopigwa muhuri au hati nyengine yoyote. Hadi pale inapoonekana kuwa ipo huru na udanganyifu na iwe ni kawaida ya watu kuingia kwenye mauziano kwa njia za hati. Kwa mfano, hati rasmi na kumbukumbu za Mahkama iliyo adilifu zinaweza kukubaliwa. Madaftari ya hisabu yaliyowekwa kwenye biashara na hati zilizotolewa mbele ya mashahidi wawili, pia zinaweza kutumika kama ni ushahidi.[1]

 

Ndani ya Sheria ya Ushahidi inaruhusu hati kuwasilishwa Mahkamani kama ni sehemu ya ushahidi. Hati hizi zipo za aina mbili. Aina ya kwanza ni zile za msingi (primary) ambazo ni za asili na aina ya pili ni zile ambazo zinathibitisha kuwepo hiyo aina ya kwanza (secondary). Kwa mfano nakala ya cheti cha ndoa inaweza kuwa ni ithbati kwamba kipo cheti halisi cha ndoa. Hivyo, nakala kwa hapa ni aina ya pili na kile cheti halisi ndio aina ya kwanza.[2] Pia maelezo ya mdomo juu ya kuthibitisha ukweli wa hati unatambulika kuangukia aina ya pili ya ushahidi wa hati.[3] Hakuna hati inayoruhusiwa kuthibitishwa Mahkamani isipokuwa pale yatakapotolewa maelezo ya shahidi.[4]

 

 

Wito Kwa Mdaiwa

 

Ni lazima Mahkama itoe wito kwa mdai pale taratibu za kufungua kesi zinapokamilika. Hata hivyo, wanachuoni hawakutoa maelezo ya kina kuhusiana na utoaji wa wito kwa mdai, isipokuwa Ibn Qudaamah na al-Khassaaf.[5]

 

Utaratibu wa wito wa kufika Mahkamani kwa mdaiwa unajulikana kwa al-Adwa wa l-l’adu (Bidii ya kumtafuta mdaiwa) na kuegemezwa hoja hiyo kwa Abu Yuusuf, ambaye ameeleza kwamba pale kesi inapofunguliwa Mahkamani na mdaiwa kutambuliwa kuwa anaishi mji huo huo, wito huo utapelekwa pamoja na aliyefungua kesi na tarishi ambao watamleta mdaiwa yeye binafsi au wakala wake.

 

Kwa mujibu wa Abu Yuusuf, utaratibu wa al-‘Adwa wa l-l’ada una msingi kutoka Istihsaan[6] na sio Qiyaas[7], na Maswahaba walifanya hivyo na hakuna aliyeukataa.[8]

 

Azad anaendelea kusema kwamba; inapotokea kuwa mdaiwa anaishi nje ya mji, kwa usafiri wa siku nzima. Hakimu ataandika ushahidi uliotolewa na mdai na kisha kumpelekea mdaiwa, akimpa amri ya kufika na kujibu madai. Kwa mujibu wa Ibn Qudaamah na al-Khassaf, maelezo hayo yanatolewa kutoka kwenye maamuzi precedence tofauti yaliyotolewa kutoka kwa Makhalifa waongofu.

 

Kwa mujibu wa kifungu 20 cha Sheria ya Mwenendo wa Madai ya Zanzibar, Mahkama kama ikipenda inaweza kutoa hati ya wito kwa mdaiwa pale kesi inapofunguliwa. Hati hiyo ni lazima iwe na saini ya Hakimu (au ofisa yeyote aliyeteuliwa na Hakimu kutia saini) pamoja na muhuri wa Mahkama.[9] Hati hiyo ni lazima imuelekeze mdaiwa huyo kufika yeye mwenyewe au kuwakilishwa na wakala wake. Pia kuna utaratibu maalum wa kumtafuta ili kumpata mdaiwa pale anapojaribu kukimbia sheria. Mfano anaweza kupelekewa afisa maalum kumuita[10], ikishindikana atabandikiwa hati hiyo mlangoni mwake.[11]

 

 

Ushahidi Wa Wito

 

Wito wowote unaopelekwa kwa mdaiwa kumtaka afike Mahkamani ni lazima uwe na ithibati kwamba umetoka Mahkamani na ni amri ya Hakimu. Hivyo, wito huo uwe na ushahidi wa Hakimu (mfano saini) na nembo ya Mahkama ukipelekwa na tarishi.

 

Itakapotokezea mdaiwa kutoweza kufika kwa sababu za msingi kama ugonjwa au wanawake wa mila ambao wamezuiwa kabisa kutoka, hawatapelekewa wito. Badala yake, kamati itaundwa ambayo itamtembelea mtu huyo aliyetajwa na atakuwepo Hakimu au naibu wake aliyepewa nguvu kuwa naibu. Kamati itaandika maelezo ya mdaiwa huyo na kuyafikisha Mahkamani. Kama mdaiwa wa namna hiyo atateua wakili, basi kamati haitaandika maelezo ya mdaiwa.

 

Imaam ash-Shafi’iy anakubaliana na Hakimu kuhamia kwenye eneo la mdaiwa ikiwa anayedaiwa ni mwanamke. Ametumia kisa cha Unays aliyeamrishwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Nenda ewe Unays kwa mwanamke wa (kesi hii) hili, akikubali (tuhuma za zinaa nje ya ndoa), mpige mawe hadi kufa.”[12]

 

Sheria ya Mwenendo wa Madai inaeleza kama ilivyo hapo juu. Hivyo, ni lazima wito uwe na saini pamoja na muhuri wa Mahkama.[13] Halikadhalika nakala moja ya wito itarejeshwa Mahkamani ikionesha jina na saini ya mpokeaji, tarehe na wakati ilipopelekwa.[14] Sheria pia haimlazimishi mwanamke aliyefungika na mila kufika Mahkamani. Hawa ni wale wanawake ambao hawaruhusiki kutoka nje kwa mujibu wa mila na tamaduni zao.[15]

 

 

Kutotii Kwa Mdaiwa Na Kuvamia Eneo La Mdaiwa

 

Kama mdaiwa bila ya sababu za msingi atakataa kufika Mahkamani hali ya kuwa amepelekewa wito rasmi wa kumtaka afike. Hakimu ataandika maelezo hayo pamoja na ushahidi wa mashahidi wawili. Hakimu atamtaarifu walii (mkuu wa mamlaka ya shehia/kata/eneo/kijiji) na gharama za utaratibu huo utakuwa ni juu ya mdaiwa mwenyewe. Ataadhibiwa kwa mijeledi au kifungo kulingana na amri ya Hakimu, kwa sababu ameshindwa kufuata amri ya Hakimu, na hivyo mdaiwa amedharau Mahkama.

 

Mdaiwa atawajibika kuadhibiwa kwa kutofika Mahkamani siku aliyopangiwa kufika ikiwa amepokea na kuukubali wito. Ni kosa la jinai kuidharau Mahkama na atawajibika kuadhibiwa. Hata hivyo, adhabu ya aliyekataa kupokea wito na kutofika ni kubwa kuliko kwa mtu aliyepokea na kukataa kufika[16].

 

Kama mdaiwa atajificha na kumkimbia tarishi, Hakimu atamuandikia walii kwa lengo la kumfikisha.

 

Itakapotokezea kutolewa habari kwamba mdaiwa aliwahi kuonekana kwa ushahidi wa mdai na walii ambaye ameshindwa kumfikisha mdaiwa Mahkamani. Na kama upo ushahidi wa kuwa yupo nyumbani kwake, basi Hakimu atatoa amri ya kuizingira nyumba yake na kugeuzwa jela kwa siku tatu. Kila siku ataulizwa, kama akikaidi itaendelelea hadi siku ya pili, ataulizwa tena, akikaidi, utaratibu huu utaendelea hadi siku ya tatu. Ikifika siku ya tatu bado amekaidi kufika Mahkamani. Hakimu atamteua wakili aisimamie kesi kwa niaba ya mdaiwa.

 

Lakini kwa mujibu wa al-Mawardi kwenye kesi ya mdaiwa kutotii amri ya kufika Mahkamani. Hakimu anaweza kutumia moja kati ya njia zifuatazo:

 

1)    Kumlazimisha kwa msaada wa tarishi kufika Mahkamani.

2)    Kuihamisha kesi yake mamlaka ya juu ambayo itamlazimisha kufika Mahkamani.

3)    Kuteua watu wawili waadilifu ambao watamwita mbele ya mlango wa nyumba yake kufika Mahkamani na kujibu madai[17].

 

Kwa maoni ya Maliki anaeleza kwamba, Hakimu asimlazimishe mdaiwa, isipokuwa kama Hakimu ataridhika kwamba masuala ya fedha yalifanyika baina ya mdai na mdaiwa. Kwa sababu mtu anaweza tu kufungua kesi ili kumtia doa mwenziwe. Hata hivyo, Ibn Qudaamah[18] hakubaliani na mawazo haya kwani anasema kuwa mdaiwa ni lazima alazimishwe kufika Mahkamani.

 

Al-Khassaaf anasema kwamba wanachuoni wetu wanaruhusu kufanya uvamizi kwenye eneo la mdaiwa wa fedha (mwenye deni) ambaye kwa makusudi anajificha. Hakimu Abu Yuusuf ameshawahi kutumia njia hii. Kwa maelezo ya as-Sarkhasi, utaratibu huu haufai.

 

Mfumo wa kuvamia kwenye kesi kama hii utakuwa kama ifuatavyo:

 

Hakimu atawapeleka watu wawili madhubuti, matarishi, wanawake na wahudumu. Matarishi watasimama kuizunguka nyuma ili kama akitoroka wamkamate. Wanawake na wahudumu wataingia ndani kumtafuta ili kumtoa hata kama amefichwa na wanawake wa familia yake.

 

Kwa kutetea hoja hiyo, al-Khassaaf ametoa vigezo vya Makhalifa waongofu, lakini uvamizi waliofanya unahusu maeneo yanayotuhumiwa kwa jinai, kama ulevi na kucheza dansi.

 

Ikiwa kwa njia hizo zote hazijafanikisha kumleta mdaiwa Mahkamani, Hakimu ataandika ushahidi uliotolewa na mdai na akiukubali ushahidi huo atatoa hukumu ya upande mmoja (bila ya kumsikiliza mdaiwa)[19].

 

Maelezo yote hapo juu yanaonesha wazi kwamba Mahakimu wa mwanzo wa Kiislamu walikuwa na hadhari kuhusiana na wito na huduma hizo. Ilikuwa ni wajibu wa Mahkama ya mamlaka ya juu kumtaarifu mdaiwa kuhusiana na hatua hiyo ili aweze kufika Mahkamani kujibu madai. Tofautisha na maoni ya Joseph Schacht kama ifuatavyo:

 

“Shari’ah za Kiislamu bado zinatumia njia za zamani za kuanzisha vitendo, ambavyo vinahusisha mdai kumkamata mdaiwa na kumburuza mbele ya Jaji (Hakimu)”[20].

 

Sheria inaruhusu kubandikwa hati ya wito kwenye nyumba ya mdaiwa. Njia hii hufuatwa iwapo Mahkama imeamini kwamba mdaiwa anakwepa kupatiwa wito huo au iwapo hapatikani kabisa au ameshindwa yeye binafsi au wakala wake kupokea wito huo.[21]Iwapo mpeleka notisi ametumia taratibu ya kuibandika hati ya wito, atatakiwa kula kiapo au Mahkama inaweza kumuamuru kwenda Mahkama nyengine ili kuthibitisha maelezo yake.[22]

 

Mahkama inaweza kuamuru mambo yafuatayo juu ya mtu ambaye amepatiwa hati ya wito na ameshindwa kufuata amri ya kufika:

 

a)    Kutoa hati ya kukamatwa (arrest warrant)

b)    Kushikilia na kuiuza mali yake/zake

c)     Kumtoza faini

d)    Kuamuru kuwasilisha dhamana ya mali na atakaposhindwa atahukumiwa kifungo cha jela kisichokuwa cha jinai (civil prison).[23]

 

Kufika Mdaiwa Mahkamani

 

Pale madai yatakapotolewa na kukamilisha taratibu kama zilivyo hapo juu na kuithibitisha Mahkama kwamba kweli ipo kesi ya kujibu. Mara nyengine, madai huweza kuwa hayana msingi na kupelekea kutupwa.[24] Prima facie, Hakimu atamuamuru mdaiwa kufika na kujibu madai.

 

Kila dai linalofunguliwa mbele ya Hakimu, ni lazima lifuate taratibu maalum za Sheria. Dai lililofuata taratibu za Sheria katika ufunguzi wake, itamlazimu mdaiwa kufika mbele ya Hakimu kujibu madai. [25]

 

 

Majibu Kwa Njia Ya Kujitoa

 

Pale wadaawa wanapofika Mahkamani, mdai ataulizwa kueleza kesi yake na kama ameweka kwa maandishi madai yake ayathibitishe. Baadaye Mahkama itamuita mdaiwa kutoa jibu lake, kama ina lazima. Mdaiwa kiurahisi anaweza kukataa dai hilo au kujitetea kwa njia ya kujitoa (daf’a). Ndani ya majibu kwa njia ya kujitoa inakuwa na madai ambayo yanaletwa mbele na mdaiwa mwenyewe, ambayo inatosa kujibu madai ya mdai. Kwa mfano, mtu anapodai kwa mwengine idadi fulani ya pesa kama ni deni analomdai, na mdaiwa kueleza kwamba alikuwa akidaiwa pesa hiyo lakini ameshalipa au mdai amemsamehe deni hilo au kwamba yeye na mdai wamewafikiana kulimaliza au kiasi hicho hakikuwa ni deni lakini ni gharama ya bidhaa fulani, ambazo yeye mdaiwa amenunua kwa ajili ya mdai. Kama mdaiwa atathibitisha dai lake la kujitoa, kesi ya mdai itafeli.

 

Pale mdaiwa anapobisha dai hilo, mdai ataitwa ili kuthibitisha madai yake. Kama mdai ataweza kutoa ushahidi wa kutosha unaokubalika, atalazimika kupatiwa maamuzi kwa ajili yake na kama si hivyo, anaweza tu kuita upande wa pili kuchukua kiapo kuthibitisha kukataa kwake. Kama upande wa pili utachukua kiapo, dai hilo dhidi yake litatupwa, lakini kama atakataa kula kiapo, utatolewa uamuzi wa hukumu. Hakimu, kwa mujibu wa hukumu za zamani precedence, anaweza kuegemeza amri zake kwenye uoni wake binafsi wa ukweli. Lakini siku hizi, anasema mwandishi wa Durru’l-Mukhtaar, hili halitokubaliwa kwa sababu ya maofisa kushiriki kwenye rushwa.[26]

 

Sheria inaeleza kwamba, mdaiwa atahitajika kuwasilisha majibu ya madai siku ya mwanzo ya kusikilizwa kesi yake au pale Mahkama itakapoamuru vyenginevyo.[27]

 

Mdaiwa katika kesi anaweza kujitoa dhidi ya madai ya mdai, kwa msingi wa kudai haki au dai. Kujitoa kwake hakutakuwa na ulazima kwamba iwe ni kwa misingi ya kulipwa au kutolipwa haki yake. Kujitoa huku kutakuwa na nguvu kama vile ni dai la pingamizi na Hakimu anaweza kutamka hukumu ya mwisho.

 

Iwapo kujitoa kwa mdaiwa kumezuiliwa na Mahkama au haiwezekani kwa mujibu wa hati ya mdai, mdaiwa atatakiwa kufungua dai jengine jipya kwa ajili ya kujitoa.

 

Iwapo imethibiti kwamba dai la kujitoa kwa mdaiwa ni la msingi, Mahkama inaweza kutoa amri ya kumvua mdaiwa dhidi ya madai ya mdai. Mahkama pia inaweza kuamuru malipo yoyote kutoka kwa mdai kwenda kwa mdaiwa.[28]

 





[1] Fataawa ‘Alamgiri, Juzuu ya III, uk. 584; al-Majallah, uk. 297; pia angalia Sheria ya Ushahidi ya Daftari la Benki, Sura ya 6, S. 3 – 6.

[2]  Sheria ya Ushahidi, S. cha 63

[3] Sheria ya Ushahidi, S. 63 (e)

[4] Sheria ya Ushahidi, S. 67

[5] Azad, Judicial System of Islam, uk. 80.

[6] Twaha Jaabir al-Alwany katika kitabu cha Uswuulul al-Fiqh ametafsiri Al Istihsaan: Kuikubali Qiyaas-kufananisha ambayo inaonekana kuwa juu kisheria kwa kulinganisha na mfananisho ulio dhahiri. Ni katika maelezo hayo ambapo al Istihsaan inakuja kwa mara kadhaa kutafsiriwa kama ni “Hiari ya Mwanachuoni”.

[7] Qiyaas: inahusu suala kwa kulifananisha na jengine, pia suala hilo linazungumzwa ndani ya Qur-aan au Sunnah.

[8] Azad, Judicial System of Islam, uk. 81.

[9] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. V, r. 1 (2) na (3).

[10] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. V, r. 16.

[11] Ibid, O. V, r. 17.

[12] Azad, Judicial System of Islam, uk. 83.

[13] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. V, r. 10; angalia pia Sheria ya Mahkama ya Ardhi no. 12 ya 1994, S. 23 – 25.

[14] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. V, r. 18.

[15] Sheria ya Mwenendo wa Madai, S. 111 (1).

[16] Azad, Judicial System of Islam, uk. 82.

[17] Azad, Judicial System of Islam, uk. 83.

[18] Azad, Judicial System of Islam, uk. 83.

[19] Ibn Qudamah; Akhbaar al-Qudhaat, IX, uk. 109.

[20] An Introduction to Islamic Law, uk. 16.

[21] Sheria ya Mwenendo wa madai, O. V, r. 17 na 20.

[22] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. V, r. 19.

[23] Sheria ya Mwenendo wa Madai, S. 24.

[24] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. VII, r. 12.

[25] Sheria ya Mwenendo wa Madai, S. 19 na 20.

[26] Durru’l-Mukhtaar’, Juzuu ya IV, uk. 391, pia Raddu’l-Mukhtaar.

[27] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. VIII, r. 1.

[28] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. VIII, r. 6 (1) na (8).

Share

010-Hakimu Wa Kiislamu: Sura Ya Nne

 

SURA YA NNE

 

 

KUSIKILIZA KESI

 

 

 

Sehemu Ya Mahkama

 

Sehemu yoyote inaweza kutangazwa kama ni Mahkama ya Hakimu ikiwa ni eneo lililo wazi na rahisi kuingilika kwa jamii (open court). Utawala wa haki unaweza kufanywa Msikitini kwa mujibu wa wanachuoni wa Hanafi. Lakini ash-Shafi’iy halikubali wazo hili, ana fikra za wale watu waliokuwa ni wanafiki na wanawake walio ndani ya kipindi chao cha hedhi. Al-Kasam na al-Marghinani, wakilipinga wazo la Hanafi, wametoa hoja zao kwamba; ni vyema ikatengwa sehemu nyengine isiyokuwa Msikiti kuwa ni Mahkama ya Hakimu.[1]

 

Kwa upande mwengine, Sheria inaeleza kwamba ni lazima kesi isikilizwe kwenye Mahkama ya wazi[2] isipokuwa pale Mahkama inaporidhika ya kwamba haitotenda haki iwapo kesi itasikilizwa humo.[3] Hivyo, Mahkama itakuwa na uwezo wa kusiliza kesi sehemu nyengine yoyote baada ya kuweka kumbukumbu za hoja na sababu ya kutosililiza kesi hiyo Mahkama ya wazi.

 

 

Hamna Hukumu Bila Ya Kusikilizwa

 

Lengo kuu la hapa ni kuwapa haki ya kusikilizwa pande zote mbili za kesi (mdai na mdaiwa) ili kuondosha hukumu itakayotolewa kwa maelezo ya upande mmoja. Kanuni hii imechukuliwa kutoka Hadiyth iliyotolewa na ‘Aliy bin Abii Twaalib (Radhiya Allaahu ‘Anhu) alipopatiwa muongozo kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa mnasaba wa uteuzi wake nchini Yemen kushikilia mamlaka ya kutoa hukumu:

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimpeleka (Sayyidna ‘Aliy) Yemen kama ni Qaadhi. Nilisema: “Ewe Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)! Umenipeleka mimi na bado mdogo na sina elimu kuhusu qadhiya (kesi)”. Akasema: “Allaah Atakuongoza kutamka hukumu sahihi. Pande mbili zenye khitilafu zinapokutana mbele yako usihukumu kwa mmoja mpaka umsikilize mwengine. Huenda, kwa kutumia mwenendo huu, sababu za hukumu zitakuwa wazi juu yako” ‘Aliy akasema, baada ya kufuata muongozo huu, sikupata kuwa na shaka yoyote kuhusu hukumu niliyotoa.”[4]

 

Sheria inaeleza kwamba hakuna ruhusa ya kutoa hukumu kwa upande mmoja hadi pale hati ya taarifa inapotolewa kwa upande ulioshindwa kuhudhuria. Hii itampa nafasi kwa mara nyengine kuhudhuria Mahkamani.[5]

 

 

Hukumu Dhidi Ya Upande Mmoja - Al-Qadhaa ‘Alaa al-Ghaib

 

Ibn Qudaamah ambaye ni mwanachuoni wa Hanbali ana maelezo ya kwamba hukumu kuhusiana na haki za wanaadamu zaweza kutolewa dhidi ya aliyeshindwa kuhudhuria Mahkamani. Ametumia Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

Hind alisema: “Ewe Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Abu Sufyaan ni mtu bakhili na hanipatii kitakachonitosheleza mimi na watoto wangu” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Chukua kitakachokutosheleza wewe na mtoto wako wa kiume kulingana na mahitaji (yenu).”[6]

 

Pia Qudaamah anaeleza kwamba; hukumu ambayo imetolewa ya upande mmoja na bila ya kumpatia nafasi ya kumsikiliza mdaiwa iwekwe pembeni ikiwa tu, kama ghaaib (asiyekuwepo Mahkamani) atatokezea Mahkamani na kuthibitisha kwamba ushahidi uliotolewa na mashahidi hao, haukubaliki kwa Mahkama.

 

Ibn Qudaamah pia anaeleza kwamba, kwa mujibu wa wanachuoni walio wengi kuwa, hukumu iliyotolewa upande mmoja sio sahihi ikiwa mdaiwa yupo ndani ya mji.[7]

 

Hadiyth aliyotumia Ibn Qudaamah sio amri ya kisheria iliyotolewa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ni kipande cha ushauri wa Kishari’ah na maelezo ya dini ili kuwapatia Waislamu muongozo kuhusiana na wale ambao hawapo tayari kufika Mahkamani kutoa ushahidi wao kwa kuegemea sababu zisizo msingi. Maelezo ya Ibn Qudaamah yanakataliwa kwa kutumia Hadiyth ifuatayo:

 

Ibn ‘Abbaas amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kama watu watapewa kulingana na misingi ya madai yao, watadai damu na mali za wengine, lakini jukumu la kiapo ni juu ya mdaiwa”[8]

 

Kwa upande wa madhehebu ya Hanafi, mwanachuoni wa Kihanafi aitwae Al-Marghinani anakubali kwamba hukumu ya upande mmoja sio sahihi isipokuwa iwe mbele ya wakala wa yule asiyehudhuria.[9] Ibn Farhaan na Maaliki wote wanakubali mawazo ya Ibn Qudaamah.[10]

 

Al-Mawardi ametenga kurasa kadhaa kuhusiana na hili na kutoa mjadala mrefu chini ya mada inayoitwa Al-Qadhaa ‘Alaa al-Ghaib – Hukumu Dhidi ya asiyekuwepo. Al-Mawardi ambaye anafuata misimamo ya ash-Shafi’iy, ana mawazo ya kwamba hukumu dhidi ya mtu asiyekuwepo Mahkamani ni sahihi, ikiwa ni kwa qadhiya ya mali inayo au isiyo hamishika. Cha muhimu, ni hiyo hukumu iwe ndani ya misingi ya haki za binaadamu.[11]

 

Kwa Maalik, hukumu kama hiyo ni sahihi katika mali inayohamishika na batili kwa mali zisizohamishika.[12]

 

Hukumu dhidi ya asiyekuwepo Mahkamani lakini yupo ndani ya mji sio sahihi kwa mafundisho ya ash-Shafi’iy. Lakini hukumu hiyo hiyo ni sahihi kwa mujibu wa Ibn  Shubrumah, Ahmad na Is-haaq kama ilivyotolewa maelezo na Al-Mawardi bin Shubrumah ambaye amesema kwa mujibu wa al-Mawardi: “Nitatoa hukumu dhidi ya mtu aliyekuwa nyuma ya ukuta mwengine na ambaye hayupo mbele yangu.”[13]

 

Al-Mawardi baada ya kutoa maelezo ya wanachuoni wakubwa wakubwa, amekubaliana na mawazo ya ash-Shafi’iy kwamba; kama ushahidi mzuri utakaotolewa dhidi ya asiyekuwepo Mahkamani, haki ikathibitika, kutolea hukumu kesi hiyo ni sahihi.

 

Azad ambaye ni mwanachuoni wa Kihanafi ameeleza kwamba pande zote ni lazima ziwepo Mahkamani. Amenukuu kwa kuikataa hoja za watu wa ash-Shafi’iy kwa kutumia Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya kwamba walikwenda watu wawili kufanya ahadi mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili kutimiza malengo yao kwenye siku fulani. Mmoja wao hakutimiza ahadi hii, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatoa hukumu na amri dhidi ya yule aliyeshindwa kutimiza ahadi. Azad ameitolea maelezo Hadiyth kuwa haina mnasaba wa hoja za al-Mawardi.[14]

 

Azad anaendelea kutoa hoja kuwa mawazo ya al-Mawardi hayakubaliki kwa karne ya leo. Kwani kipindi cha wanachuoni wa mwanzo, msafara wa mji mmoja kwenda mwengine ulikuwa ni mgumu. Hivyo wanachuoni wakaegemea kwa hukumu kwa aliye mbali (qadhaa ‘ala al-ghaibu) ili kufikia haki. Mahanafi wameingiza na kutumia mwenendo mwengine kwamba pale mdaiwa anaishi kwa muda au maisha yake yote ni maeneo ya mbali na Mahkama, mdai anaruhusika kuiwasilisha kesi yake na kutoa ushahidi na kuangalia kwa makini kuhusiana na ukweli wa ushahidi, atapeleka kumbukumbu za ushahidi wa kesi kwa Hakimu ambaye huyo mdaiwa anaishi.[15]

 

Azad anamaliza kwa kusema kuwa hukumu ya upande mmoja (kama ikishindikana hizo taratibu hapo juu) inaweza kutolewa ikiwa mdaiwa yupo nje ya mji na ameondoka wala hakusudii kurudi siku za mbele. Hata hivyo, mdai ataamrishwa kuweka dhamana (rehani) kama mdaiwa atatokea siku za mbele na kuthibitisha sababu na uhalali wake.[16]

 

Sheria kwa upande wake inaeleza kuwa pale ambapo mdai amefika Mahkamani lakini mdaiwa hakufika, Mahkama inaweza kuendelea na kesi kwa kumsikiliza mdai na kutolea uamuzi wa upande mmoja iwapo tu mdaiwa alipata wito wa kumuita Mahkamani. Ikiwa haikuthibiti kwamba hati ya wito ilipelekwa, Mahkama itaamuru kutolewa kwa hati ya pili ya kumuita mdai. Mahkama pia inaweza kuakhirisha kesi iwapo mdaiwa hakupatiwa muda muafaka wa taarifa ya kufika Mahkamani.[17]

 

Iwapo Mahkama imetoa amri ya kusikilizwa upande mmoja, mdaiwa anaweza kupinga hukumu hiyo[18] au kutoa sababu ya msingi ya kutohudhuria kwake na Mahkama ikamuamuru kusikilizwa kesi yake kana kwamba alikuwepo siku ya mwanzo.[19]

 

Mdai anaposhindwa kufika Mahkamani lakini mdaiwa amefika, Mahkama inaweza kulifuta dai lake (mdai) na hataruhusiwa kufungua dai jengine jipya kama hilo. Hata hivyo, mdai anapowasilisha sababu ya msingi ya kutohudhuria kwake, amri ya kulifuta dai la mdai linaweza kuwekwa upande.[20]

 

Kwa upande wa kesi yenye mdai au mdaiwa zaidi ya mmoja, na baadhi yao tu wamehudhuria, Mahkama itaendelea na kesi kama vile wapo Mahkamani.[21] Na iwapo mdai na mdaiwa kwa pamoja wameshindwa kufika Mahkamani bila ya sababu ya msingi, Mahkama itaamua kuifuta kesi ama kuwapatia wito mwengine ama kuwalazimisha kufika Mahkamani.[22]

 

 

Mdaiwa Kukataa Kujibu

 

Wanachuoni wa Hanafi wanasema kwamba pale mdaiwa anapoitwa na kuukubali wito wa kufika Mahkamani, lakini akakataa kuzungumza mbele ya Mahkama (kudharau) na kukataa kujibu madai ya mdai, Hakimu atampeleka jela mpaka pale atakapokuwa tayari kujibu madai ya mdai. Ama wanachuoni wa Kishafi’iy kwa mujibu wa al-Mawardi, wanasema kwamba mdaiwa hatofungwa, lakini hukumu itatolewa dhidi yake.

 

Utaratibu wa kutolea hukumu dhidi ya anayeshindwa kuwasilisha majibu ya madai unaenda sambamba ndani ya Sheria. Kwani mdaiwa anaposhindwa kuyawasilisha majibu yake ndani ya muda aliopatiwa, Mahkama itatoa amri kwa upande mmoja.[23]

 

 

Kukubaliana Na Madai (Admission)

 

Kwa ujumla, Mahkama inakubali mdaiwa kukariri madai (kukubali ukweli wa mdai) bila ya kuhitaji ushahidi mwengine kutoka kwa mdai. Lakini kukubali huko kwa mdaiwa kuwe kumefanywa kwa hiari. Hata kama kumefanywa kwa kutumia nguvu, haitokuwa na nguvu mbele ya Shari'ah. Wala isiwe imefanywa kwa ubishi au mzaha.

 

Pale mdaiwa anapokubali madai ya mdai na ukweli wake wa mdai, Hakimu atatoa amri ya hukumu itakayompendelea mdai.

 

Sheria pia inakubaliana na upande wowote kukubali madai ya upande wa pili.[24] Kwa mfano mdaiwa anaweza kukubaliana na madai kwamba alishindwa kulilipa deni la mdai. Baada ya Mahkama kupokea hati inayoonesha upande mmoja kukubaliana na madai ya upande mwengine, Hakimu atatoa hukumu inayoona inafaa.[25]

 

 

Kusikiliza Dai

 

Kanuni zinaweka wazi kuhusiana na kulisikiliza dai. Kanuni muhimu na ya moja kwa moja kwa suala hili ni kwamba dai lazima lisikilizwe mbele ya wadaawa au wawakilishi wao. Mdai, kama ataweza, anaweza kumleta mdaiwa pamoja naye mbele ya Mahkama pale tu anapoleta dai lake. Kama hatoweza kumleta mdaiwa, Mahkama ni lazima itoe hati ya kumuita ili afike Mahkamani. Kama mdaiwa atakataa kufika, atapelekewa hati ya wito mara tatu pamoja na hati ya madai katika nyakati tofauti na kama tu bado hajafika, ataarifiwa kwamba Mahkama itateuwa wakala kwa niaba yake na dai likiwa na ushahidi litasikilizwa. Kama bado tu hajafika wala kumleta mwakilishi wake, basi Mahkama yenyewe itateuwa mtu kuangalia faida yake, na baada ya kulisikiliza dai na ushahidi mbele ya pande hizo, pamoja na kuangalia vyema ushahidi, itatoa maamuzi. Ama akitokea wakati pale inapotolewa hukumu dhidi ya upande mmoja (ex-parte), na kupinga usahihi wa maamuzi, ataruhusiwa kujibu dai, na utetezi wake utasikilizwa. Kama madai yake yatakubaliwa, maamuzi yatawekwa pembeni.

 

Hakuna utaratibu wa Mahkama kuteua wakala kusimamia kesi ya yule anayeshindwa kufika Mahkamani kwa upande wa Sheria.

 

 

Kuakhirisha Na Kuchelewesha Haki

 

Aidha, ujio wa kesi ulikuwa ni mchache kwenye kipindi cha wanachuoni wa mwanzo ama kwa sababu nyenginezo, ndio maana hawakusema kitu kuhusiana na kuakhirisha kesi hivyo kuchelewesha katika kutenda uadilifu.

 

Katika barua ya ‘Umar kwa Abu Muusa (Radhiya Allaahu ‘Anhuma), kama ilivyoelezwa awali, tunaweza kusema kwamba Hakimu atumie akili yake na hekima zake zote katika kesi ambayo ni yenye ujanja na ugumu na anaweza kuakhirisha tamko la hukumu hadi afikie hitimisho lililokuwa sahihi.

 

Pale ambapo mdai hana mashahidi wake, wanachuoni wamesema kwamba Hakimu anaweza kusubiri mpaka wafike mashahidi mbele yake kwa muda wa siku tatu.[26]

 

Ama kwa Sheria ni lazima ziwepo sababu za msingi kabla ya kuakhirisha kesi. Kwani haki inayocheleweshwa kutolewa inasababisha haki kukosekana (justice delayed is justice denied). Hata hivyo, Hakimu amepewa nguvu ya kuakhirisha kesi hadi wakati anapoona inafaa. Mahkama inaweza kuakhirisha kuisikiliza kesi mara kwa mara. Katika kila siku inayoikhirishwa kesi, ni lazima Mahkama ipange tarehe nyengine kwa ajili ya pande za kesi kufika kusikiliza kesi yao. Hakutakuwa na ruhusa kwa Mahkama kuakhirisha kesi iwapo imeanza kusikilizwa hadi mashahidi wote wapatiwe haki ya kusikilizwa. Hata hivyo, Mahkama inapokuwa na sababu ya msingi, inaweza kuakhirisha kusikiliza mashahidi hadi siku inayofuata na ni lazima iweke kumbukumbu ya sababu ya kuakhirisha huku.[27]

 

Iwapo muda muwafaka umetolewa na Mahkama, hakutakuwa na ruhusa ya kuakhirisha kesi kwa upande ulioshindwa kuwasilisha ushahidi, au mashahidi au kufanya jambo lolote aliloamrishwa.[28]

 

Upande wowote utakaoshindwa kujibu masuala yaliyoulizwa, na ambayo Mahkama inaamini anaweza kujibu, Mahkama inaweza kuakhirisha kesi hadi siku nyengine, na kutoa muongozo wa mtu huyo aliyeshindwa kujibu kufika Mahkamani.[29] Iwapo hakufika siku iliyotajwa bila ya sababu ya msingi, Mahkama inaweza kutamka hukumu, au kutoa amri yoyote inayoona inafaa.[30]

 





[1] Azad, Judicial System In Islam, uk. 96.

[2] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XXI, r. 5

[3] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XXX. r. 6.

[4] Al-Bayhaqiy, as-Sunan al-Kubra, X, uk. 137. Pia angalia al-Jami’, I, uk. 171 na Mishkaat al-Masaabih, al-Khaatib at-Tibirizi, uk. 325.

[5] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XI, r. 15.

[6] Al-Mughni, IX, uk 109, uk. 110.

[7] Al-Mughni, IX, uk. 109-111.

[8] Muslim, Sahiih.

[9] (a) Al-Murghinani, al-Hidaaya, II, uk. 142 (b) Pia angalia Ibn Qudaamah, Akhbaar al-Qudhaati, IX, uk. 109.

[10] (a) Ibn Farhuun, Tasbiirah, I, uk. 86-88 (b) Al-Hilli, Sharai’ al-Islaam.

[11] Al-Mardhi, Adaab al-Qaadhi, II, uk. 304-326.

[12] Al-Mawardi, Adaab al-Qaadhi, II, uk. 307.

[13] Al-Mawardi, Adaab al-Qaadhi, II, uk. 311.

[14] Azad, Judicial System of Islam, uk. 78-79.

[15] (a) Azad, Judicial System of Islam, uk. 80 (b) Angalia pia kitabu cha Kitaab al-Qaadhi ilaa al-Qaadhi kuhusiana na kumbukumbu za kesi kwa Hakimu mwengine.

[16] Azad, Judicial System of Islam, uk. 80.

[17] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XI, r. 6.

[18] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XI, r. 14

[19] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XI, r. 8.

[20] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XI, r. 9 – 10.

[21] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XI, r. 11 – 12.

[22] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XI, r. 13.

[23] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. VIII, r. 10.

[24] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XIV, r. 1

[25] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XIV, r. 6.

[26] Kwa mifano, angalia al-Marghinani; al-Hidayah, III, mjadala kuhusiana na Shahadah, uk. 155-156.

[27] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XX, r. 1.

[28] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XX, r. 3.

[29] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XII, r. 4 (1)

[30] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XII, r. 4 (2)

 

Share

011-Hakimu Wa Kiislamu: Sura Ya Tano

 

SURA YA TANO

 

USHAHIDI

 

 

Dhana Ya Ushahidi

 

Ushahidi ni tendo la kisheria na inaangukia chini ya fungu la habari akhbarah. Pale haki inapotokana na tukio la kiasili au tendo la mwanaadamu, Taifa inayoiwakilisha jamii ndio itakuwa na wajibu wa kuelezea ukweli wa namna ilivyotokea. Pale ukweli unapoibua haki ya mtu ulio dhahiri, Taifa linaichukua haki hiyo wenyewe (by its own motion). Kwa mfano, yatambulika kwamba nyumba A, B, X, Y na K zilivunjwa kutokana na kujengwa shule na Taifa hilo. Au, mwananchi Z, S, D, na O waliuawa kutokana na vita vilivyopiganwa na Taifa hilo.

 

Lakini, kwa kesi yoyote, ofisa wa Taifa, ambaye ni Hakimu, kama yeye mwenyewe hana uelewa binafsi wowote wa tukio, ni lazima ategemee maelezo ya shahidi. Habari hii, yaweza kuelezwa kwa njia ya matamshi ya aliyeuona ukweli huo au kwa alama au dalili traces zilizotokea pale pale wakati wa tukio. Ni ukweli ulio dhahiri kwamba haitowezekana kutoa maelezo yakinifu kama dalili au alama zimetoweka au zimeondolewa kwa makusudi. Hivyo, hakutakuwa na njia rahisi ya kupinga ukweli huo, kama ushahidi unajulikana wazi na Taifa au Hakimu.[1]

 

Kama ukweli ulio wazi umesababisha haki fulani kudaiwa, ni haki na pia ni wajibu wa kila mwananchi aliyeona kutoa habari kwa Mahkama na Taifa kwa jumla. Lakini, shahidi anaweza (kutokana na kukosa maadili) kuchagua kutotoa habari sahihi kwa yaliyotokea na tendo hilo pekee laweza kutambulika kuwa ni habari. Wajibu wa kutoa ushahidi sahihi unatambulika kuwa ni wa sifa isiyokamilika kwa namna ambayo binaadamu amejaa kasoro. Kwa mujibu wa wanachuoni wa Kiislamu, kiapo cha uongo hakitambuliki kuwa ni ushahidi, kwa vile lengo kuu la kutoa habari ni kuweka wazi wa lililotokea. Ukweli ni kwamba, kwa mujibu wa hao wanachuoni, kiapo, ushahidi au habari za uongo ni mkanganyo wa ushahidi.

 

Mahitaji ya ushahidi mara nyingi yanaibuka pale ukweli unaojadiliwa unatokana na haki ya A dhidi ya B na B akabisha. Na kwa vile ni uoni halisi wa ushahidi kwamba unatoa habari ya ukweli ili ipatikane athari kwa anayepaswa kuipata kwa uadilifu. Wanachuoni wa Kiislamu, wanasema kwamba kutoa ushahidi ni haki ya mtu aliyeona tukio ili kumuathiri yule anayedaiwa. Kazi ya Hakimu kwa hapa ni kuupa nguvu za kisheria ushahidi uliotolewa ukiwa na habari au thibati. Haki ya Hakimu ni kupatiwa ushahidi wa kweli (shahaadah). Lakini, kwa vile ni kawaida ya wanaadamu kutotoa habari sahihi ama ikiwa kwa makosa ya kuona kwake au kwa sababu ya kukosa maadili mema, ni mzigo mkubwa kwa Shari’ah kuchukua hadhari kwa lengo la kuikinga Mahkama isiburuzwe na uongo.

 

Hakutakuwa na mgongano wa ushahidi iwapo habari zote zilizotolewa ni za ukweli, ingawa kunaweza kutokea mgongano wa matamko, ambapo moja kati ya tamko laweza kuitwa ushahidi, na tamko jengine kuwa ni uongo au kosa. Kwa mnasaba wa uongo au kosa, haiwezekani kuwa ni haki au wajibu wa mtu yeyote kutamka mbele ya Mahkama na wala Mahkama haitakuwa na mamlaka ya kukubali. Hivyo kwa msingi wa wanachuoni wa Kiislamu, ushahidi kuhusiana na ukweli ni lazima uegemee upande mmoja. Kwa kubainisha kanuni hizi, Shari’ah inatengeneza kanuni namna itakayoweza kuondosha makosa na uongo. Baadhi ya mambo haya ni ya mwenendo, lakini mengine yanaonesha asili na umbali wa kiapo kuwa ni tendo la kisheria.

 

 

Kuthibitisha (Onus Of Proof)

 

Hadiyth maarufu na muhimu ambayo inatoa mwangaza juu ya vipengele vya kuthibitisha ni:

 

“Jukumu la kuthibitisha (al-Bayyinah) lipo kwa mdai na kiapo kifanywe kwa mdaiwa.”[2]

 

Neno “Bayyinah” ndani ya Hadiyth linatokana na mzizi wa neno “bayaan”, ambalo linamaanisha kuelezea kwa uwazi kabisa. Hivyo, kwa mujibu wa Hadiyth, inampasa juu ya mdai kuifanya kesi yake kuwa nzuri kwa kutoa maelezo kamili ya madai, kuvipambanua vifungu vyote vya ushahidi vinavyowezekana kutolewa na kutoa hoja za nguvu na za kulazimisha. Maelezo hayo yanatupelekea ya kwamba mdai anaweza kutoa ushahidi wa maandiko (documentary evidence), ushahidi wa mazingira (circumstantial evidence) (mambo yote yapasavyo ambavyo si dhahiri au hakika ila huelekea kuwa kwa mambo na hali zilivyokuwa) na mawazo ya mtaalamu kwa lengo la kuthibitisha madai yake.

 

Kwenye kisa maarufu ambacho kilikuwa baina ya Zabriqan bin Badr na Hutay’ah. Ambapo ilidaiwa kwamba Hutay’ah aliandika shairi lenye kumtusi Liwali Zabriqan. ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akamwita Hassaan bin Thaabit, mshairi maarufu na mzuri kabisa, kutoa mawazo ya kitaalamu. Hutay’ah ameripotiwa kusema:

 

Weka rehani iliyo juu,

Usisafiri kwenye ujasusi wao huo,

Hakika wewe ndie mtafunaji,

Mvaaji baada ya sura mpya.

 

Hassaan akaamua kwamba Hutay’ah alikuwa mkosa kwa kusingizia uongo. Kwa maamuzi haya, Hutay’ah aliadhibiwa.[3]

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesimuliwa akisema kama ilivyopokewa na Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘Anha):

 

“Mimi ni binaadamu tu na nyinyi mnaleta migogoro yenu kwangu mimi, mukiwa wenye fasaha katika viapo vyenu kuliko wengine, ili ya kwamba nitoe hukumu kwa niaba yenu kwa mujibu wa ninayoyasikia kutoka kwenu. Hivyo, vyovyote nitakavyoamua kwa yeyote, ambapo kwa haki ni ya ndugu yake, asichukue kwani simpatii chochote ila kipande cha moto.”[4]

 

Kutokana na Hadiyth hii na kwa mujibu wa madai ya wadaawa, inaruhusiwa na ni vyema madai yakapelekwa Mahkamani kwa kesi ambayo inakuwa kubwa siku hadi siku. Hata hivyo, wadaawa wanahimizwa kuwa wakweli kwenye viapo.

 

Sheria inaeleza kuwa mtu yeyote anayehitajia Mahkama kutoa hukumu ya suala lenye haki ama wajibu, atahitajika kuthibitisha kwa kutumia hoja zake alizo nazo mkononi.[5] Mtu yeyote anayelazimika kuthibitisha hoja zake, ndiye atakayeambiwa kwamba mzigo wa kuthibitisha upo juu yake.[6] Ni kusema kwamba, mzigo wa kuthibitisha upo kwa yule ambaye iwapo hajathibitisha hoja zake atashindwa kesi yake.[7] Iwapo kuna mtu yeyote mwenye ushahidi nje ya pande za kesi (mdai au mdaiwa) atawajibika kutoa ithibati.[8] Kwa mtu ambaye hatambuliki iwapo ni yuhai au maiti, na imeelezwa kwamba yupo hai ndani ya kipindi cha miaka 30, mzigo wa kuthibitisha utakuwa juu ya yule mwenye kudai kwamba hayupo hai.[9] Katika suala la kwamba mtu fulani anamiliki mali, mzigo wa kuthibitisha kwamba hamiliki ni kwa yule anayedai hana milki ya mali hiyo.[10]

 

Mahkama inaweza kuthibitisha kuendelea kuwepo kwa kitu ambacho kinaamini kilitendeka, kwa kuzingatia matokeo asili, tabia za kibinaadamu na biashara za binafsi au za umma, katika mahusiano ya suala la kesi hiyo.[11] Kwa mfano kuna dhana kwamba shughuli za kijamii zinatayarishwa vizuri, kwamba kila mtu anayetuhumiwa na kosa la jinai kuwa ni msafi hadi ithibitishwe vyenginevyo, kwamba kitu fulani kinachothibitishwa kuwepo kinatambulika kuwa kipo hadi ithibitishwe kinyume chake.

 

 

Mawazo Ya Mtaalamu (Expert’s Opinion)

 

Ibn Farhuun ameelezea mada mahsusi kwenye fikra za kitaalamu katika kitabu cha Tabsiirah. Anasema kwamba mawazo ya mwandishi wa ramani za majengo/mjenzi katika kesi za ujenzi (migogoro kuhusiana na nyumba, kuta, paa n.k.), mawazo ya mfanyabiashara katika kesi za bei na thamani ya vitu na mawazo ya mtu wa sayansi ya utabibu yanaruhusiwa kwa mujibu wa wanachuoni walio wengi.[12]

 

Muongozo kutoka Sheria unaeleza kwamba Mahkama itakapohitaji kupata mawazo juu ya jambo geni, au la sayansi au sanaa, au uandishi wa hati, au alama za dole, mawazo ya jambo hilo kutoka kwa wataalamu wa jambo hilo yatatambulika kuwa yanafaa. Watu wanaotoa ushahidi wa mambo haya wanaitwa wataalamu.[13]

 

 

Tazkiyah

 

Kuchunguza sifa za shahidi (tazkiyah) ni kazi ya Hakimu, ambayo si rahisi kama inavyoonekana. Aidha, shahidi ni wa tabia nzuri au laa, hawezekani kutambulika kwa jamii zetu za leo. Watu hawasemi kitu kuhusiana na jamii za waovu. Na ni nani aliyelindwa kutokana na dhambi isipokuwa Mitume? Ibn Farhuun kuhusiana na hili anaeleza njia nyepesi kwamba shahidi anapofika mbele ya Hakimu, ni lazima aandike jina lake, wazee wake, anuani yake ya ukaazi, msikiti anaoswali, sura yake, uwezo wake, kazi yake na kama nyumba anayoishi ni ya kwake au laa.[14] Maelezo haya yanarahisisha kazi ya tazkiyah.

 

Sheria inaeleza kwamba, utakuwepo utaratibu wa kuwachunguza mashahidi ndani ya sheria za mwenendo wa jinai au madai.[15]

 

Katika siku ya mwanzo ya kusikiliza kesi, au wakati mwengine wowote, upande wowote wa kesi uliofika Mahkamani unaweza kuchunguza upande wa pili. Hakimu pia atakuwa na fursa ya kuchunguza pande za kesi. Uchunguzi huu unaweza kufanywa kwa wadaawa ama kwa mashahidi wao.[16]

 

 

Mashahidi Wa Mdai Na Mdaiwa

 

Pale mdaiwa anapokataa madai yaliyoletwa na mdai. Mdai ataleta ushahidi kwa mujibu wa Shari'ah. Hakimu baada ya hapo atawafanyia mashahidi tazkiyah (kuwachunguza tabia na ukweli wao) kama iilivyoelezwa vizuri na wanachuoni, baadaye atausikiliza ushahidi wao.

 

Iwapo mdai ameshindwa au hakuweza kuleta ushahidi thabiti, Hakimu kwa maelekezo ya mdai, atamlazimisha mdaiwa kuapa kama ilivyotajwa ndani ya Hadiyth na vitabu vya Fiqh. Al-Mawardi ameshauri kwamba ikiwa mdai hatodai kiapo kutoka kwa mdaiwa, madai yake yatatupwa[17].

 

Sheria kwa upande wake inaeleza kwamba mtu yeyote atawajibika kuthibitisha jambo isipokuwa pale anaposhindwa kufahamu suala lililoulizwa au kushindwa kujibu kutokana na suala lenyewe kuwa ni la kumshushia heshima.[18]

 

Mtu aliye na ugonjwa wa akili (mwenda wazimu) hazuiliki kutoa ushahidi iwapo amelielewa suala aliloulizwa. Atazuiliwa iwapo tu haelewi suala aliloulizwa.[19]

 

Shahidi asiyeweza kuzungumza (bubu), atatoa ushahidi wake kwa njia yoyote nyengine inayoweza kueleweka, iwapo kwa ishara au kwa maandishi. Lakini maandishi yake ni lazime yatiwe saini yake mbele ya Mahkama. Ushahidi unaotolewa wa maandishi kutoka kwa bubu unatambulika kuwa ni ushahidi wa mdomo.[20]

 

Upande wowote wa kesi kutoka kwa mdai au mdaiwa unaweza kuwasilisha shahidi. Shahidi huyo atawajibika kujibu masuala yatakayoulizwa kutoka kwa aliyemfikisha Mahkamani. Baadaye atawajibika kujibu masuala kutoka kwa upande wa pili unaopingana naye. Upande uliomfikisha shahidi huyo Mahkamani utapatiwa fursa tena ya kumuuliza masuala. Hii itampatia fursa upande uliomfikisha shahidi Mahkamani kurekebisha kosa lolote.[21]

 

Mfano A ni mdai na B ni mdaiwa, A amemfikisha C kuwa ni shahidi wake, na B amemfikisha D, E na F kama ni mashahidi wake. A ataanza kumuuliza shahidi wake C, baadaye B ataendelea kumuuliza masuala shahidi C, A atapatiwa tena fursa ya mwisho kumuuliza shahidi wake C. Utaratibu huu ndio utatatumika kwa A dhidi ya mashahidi D, E na F.

 

 

Nukuul (Kiapo)

 

Kanuni kuu iliyopo kwa Shari’ah ya Kiislamu kuhusiana na ushahidi ni kwamba, agizo au amri ya Mahkama iegemezwe inavyowezekana kwenye uhakika na sio kubahatisha. Wale ambao ni wazoefu wa mfumo wa mwenendo wa kileo, wameganda kufikiria kwamba kanuni hizi, ambazo zinaacha kidogo au kutokana na nguvu yoyote Mahkama katika kuzichunguza sifa na uaminifu wa kiapo. Hata hivyo, mengi ambapo wanajaribu kudhania kuyabania, yanapelekea kwa upande fulani kuwa na athari kwenye kesi nyingi katika kuyakataa malengo yao wenyewe. Kwa upande mwengine, inaweza kuzungumzwa kwamba kanuni za mwenendo wa Shari'ah za Kiislamu zinapelekea kumaliza haraka migongano na madai, ambapo mifumo ya sasa ya mwenendo na kesi umebanwa kutofanikisha hili.

 

Pale itakapotokezea kuwepo majibizano ya madai na tuhuma nyenginezo, pande zote mbili watalazimika kuleta ushahidi na kutoa kiapo iwapo hawakuweza kuleta ushahidi thabiti. Lakini nini itakuwa khatamu ya kesi? Hii itategemea na uzuri wa kesi na asili ya kila kesi. Na hakuna utaratibu maalum kuhusiana na viapo vya pamoja (tahaluf).

 

Mdai anapokataa kuchukua kiapo, kesi itahukumiwa dhidi yake. Hata hivyo, Imaam ash-Shafi’iy anaeleza kuwa kwenye kesi hii, hukumu, haitatolewa kumpendelea mdai mpaka yeye mwenyewe (mdai) aape[22]. Katika ushahidi wao, ash-Shafi’iy anatumia Hadiyth maarufu ya Sayyidna ‘Uthmaan kupeleka malalamiko mbele ya Khaliyfah Sayyidna ‘Umar dhidi ya Miqdaad (Radhiya Allaahu ‘Anhum). Miqdaad akashikilia ‘Uthmaan athibitishe. Sayyidna ‘Umar akakubaliana naye kwa kusema: “Miqdaad ametenda (amesema) kwa mujibu wa haki (kweli).

 

Kwa upande wa Hanafi, wanatumia Hadiyth inayosema “Jukumu la kuthibitisha ni juu ya mdai na kiapo kichukuliwe na mdaiwa.”[23]

 

Kwa ushahidi wa Hanafi, wametumia kesi ya Hadhramawt iliyoletwa mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ni vyema ikaelezwa kama ilivyopokelewa na Muslim:

 

Watu wawili, mmoja kutoka Hadhramawt, na mwengine kutoka Kindah walifika mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Muhadhrami akasema: Ewe Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mtu huyu amevamia ardhi yangu! Yule Mkindi akajibu: “Ardhi hii inayodaiwa ni ya kwangu ndani ya mamlaka yangu na Muhadhrami hana haki ya kudai kutokana na ardhi hiyo.” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia Muhadhrami: “Una ushahidi wowote?” Akasema “Hapana” Mtume akasema “Utahukumiwa kwa kiapo cha mdaiwa” Muhadhrami akasema, “Ewe Mtume wa Allaah! Mtu huyo sio muadilifu, hivyo kiapo cha uongo hakina tofauti kwake.” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Hata hivyo, ni lazima ukubali maelezo yake chini ya kiapo.”[24]

 

Sarakhsi alipojadili mada hii, ametoa maelezo mazuri kwamba kiapo sio dalili ya kuthibitisha madai. Ni ushahidi pekee utakaokubaliwa kuthibitisha ukweli wa madai. Pale mdaiwa anapochukua kiapo, inamaanisha kwamba madai ya mdai hayajakubaliwa (na mdaiwa). Vivyo hivyo, kwa mdai kutoa kiapo, hakitothibitisha kesi yake.[25]

 

Kiapo kinaruhusiwa chini ya Sheria ya Fafanuzi – Interpretation Decree, Cap. 1, Laws of Zanzibar.[26] Sheria inaeleza kwamba, Mahkama inaweza kwa wakati unaoona unafaa, kuamuru maelezo ya hoja fulani yatolewe kwa kiapo, au kwamba kiapo cha shahidi yoyote kilichoandikwa kitolewe kwa kusomwa.[27]

 

 

Masharti Ya Kuwa Shahidi

 

Ukirudia sababu za watu kudanganyika hadi kusema uongo au yale mazingira yanayomzuia kutoa habari sahihi na yenye kufaa. Abu Yuusuf ana maoni kwamba, mtu yeyote mwenye tabia njema na mkweli ataruhusika kuwa ni shahidi hata akiwa ni masikini mwenye maisha duni.

 

Shari’ah inasisitiza juu ya masharti kadhaa ambayo Hakimu wa Kiislamu anatakiwa ayaangalie:

 

(1) Uhuru wa upendeleo na kuchukia; hivyo kiapo hakikubaliki kwa baba juu ya mtoto na kinyume chake, cha mtumwa juu ya bwana wake, kwa pande ambazo wanategemea kesi yao moja, cha mtu ambaye ana uhasidi wa upande wa pili, cha asiyekuwa Muislamu dhidi ya Muislamu na vyenginevyo.

 

(2) Utegemezi wa jumla kuhusu tabia; hivyo watu wenye shughuli zenye maadili mabaya, kama vile wataalamu wa kucheza miziki, watu wanaojulikana kuwa ni waongo, walevi au wacheza kamari, watu wasiokuwa na tabia njema kwa kujihusisha na vitendo vilivyo nje ya misingi ya Uislamu vinavyotolewa adhabu ya hadd, kama mtu ambaye ni faasiq kinyume na a’adil. Au mfano wa wale ambao tabia zao mbovu zipo juu ukilinganisha na zile nzuri. Maafisa wala rushwa walioajiriwa kwa malengo ya kunyanyasa, hawakubaliki kuwa ni mashahidi.

 

(3) Ufahamu na uwezo wa kuelewa; hivyo, mtoto mdogo, mwenda wazimu, au kipofu kwenye masuala ambayo yanahitaji kuthibitishwa kwa kiapo cha kuona, wote hawa wanakuwa hawafai kutoa ushahidi.

 

Kwa kuzuia maafa zaidi dhidi ya uwezekano wa makosa au kiapo cha uongo na pia kwa sababu huenda kwa upande mwengine kukawa na majibizano yasio na lazima. Kiapo cha shahidi mmoja kwa kawaida kinatambulika kuwa hakitoshelezi kuthibitisha dai. Hivyo, madai yaliomo kwenye masuala ya haki za watu, kwa mfano uzuiaji wa biashara isiyo na maadili haitumii kiapo hicho cha ahad. Ama baadhi ya masuala ambayo wanawake pekee wanaelewa, kama vile mtoto fulani amezaliwa na mwanamke fulani, yanaweza kuthibitishwa hata kwa kiapo cha mwanamke mmoja.

 

Masuala ambayo yanaangukia kwenye haki za umma na kuhitaji uthibitisho kamili ulio wa kweli, kama vile makosa yanayopelekea adhabu ya hadd yanaweza tu kuthibitishwa kwa ushahidi wa mashahidi wawili wa kiume na kwa kesi nyengine, ambayo ni ya uzinifu kwa mashahidi wanne wa kiume. Mwanamke anatambulika kuwa na uwezo wa chini katika masuala ya kutoa ushahidi kwa sababu ya sifa yake dhaifu.

 

Sheria inaeleza kwamba shahidi anaweza kukanywa na upande wa pili wa kesi au kwa upande uliomuita. Kukanywa huku ni katika njia zifuatazo:

 

a)    kwa ushahidi wa mtu ambaye amethibitisha kwamba shahidi huyo hafai kuaminiwa.

 

b)    amepokea hongo, rushwa au aina nyengine yoyote ya laghai ili kutoa ushahidi wake

 

c)     kwa maelezo yake yoyote ya hapo kabla yanayoonesha kukhitalifiana na maelezo anayoendelea kuyatoa sasa

 

d)    anapohusishwa na tuhuma za kuwa ni mwenye tabia mbaya kabisa kwa mfano ubakaji.[28]

 

 

Kuulizia Uwezo Wa Shahidi

 

Jambo muhimu ni Mahkama kupata maelezo ya kanuni ambazo zimewekwa kwa lengo la kuiongoza Mahkama kuelewa sifa zinazofaa kwa shahidi na ukweli wa matamko yake, pia kwa lengo la kuongoza dhidi ya uwezekano wa Mahkama kuyumbishwa kutokana na kiapo chake. Juhudi pia zinafanyika ili kuzuia uwezekano wa Mahkama kuitwa ili kuamua baina ya madai yenye viapo vyenye mgongano kwenye kesi ambapo wadaawa wanatoa tuhuma zenye mgongano na kila mmoja anaelemea kutetea tuhuma zake, kanuni zimewekwa kwa ule ushahidi unaoweza kukubalika.

 

Ni moja kati ya kanuni muhimu kwa Hakimu, kama shahidi aliyeletwa mbele na upande wa kesi kwa kutoa ushahidi utakaotambulika kuwa wa kweli, ametoa ushahidi unaotakikana dhidi ya upande wa pili na huo upande wa pili ukapinga ushahidi huo kwa madai kwamba ushahidi wake ni wa uongo au kwa hoja ya shahidi kusahau tukio, kuulizia kuhusiana na uwezo wa shahidi na zaidi ni ukweli wa yeye kuwa ni mtu wa kusahihisha. Kuulizia huku kufanywe na yeye Hakimu aidha binafsi au Mahkamani kwa msaada wa watu anaowatambua kuwa wanaweza kutegemewa na wenye kuielewa hali ya maisha na sifa za shahidi aliyetajwa. Upande mwengine pia unao uhuru wa kutoa dharura au pingamizi (jarh, ta’an) kwa ushahidi huo. Kwa kuonesha kwamba shahidi huyo hakubaliki kwa sababu ya kuwa na upendeleo, chuki binafsi au sababu nyenginezo. Uchunguzi ulio wazi kwa sifa za shahidi kwa kutumiwa kigezo cha namna ulivyo Uislamu siku za mwanzo, inasemekana kwamba ushahidi wake utatolewa kwa sababu ya kubishana na bughudha.[29]

 

Kama shahidi ni mgeni kwenye sehemu anayoishi Hakimu huyo na ndani ya mipaka yake ya Kishari'ah, basi Hakimu atalazimika kufanya uchunguzi kwa kumuulizia. Mahakimu pia wanalazimika kuweka kumbukumbu (register) za watu wanaotambulka kuwa ni ‘aadil au watu wenye kusahihisha. Pia Hakimu alipitie register hilo kila baada ya kipindi fulani.

 

Hakuna Sheria ya moja kwa moja kuhusiana na uwezo wa shahidi katika kesi. Wala hakuna kanuni juu ya kueleza uzito wa ushahidi pamoja na kupata maelezo yake. Kila kesi ina sifa yake maalum, na kila moja ni lazima isomwe vyema ili kufikia haki.[30]

 

Lengo la kesi ni kufikia kwenye ukweli, na ukweli unapatikana ndani ya ushahidi wa mashahidi. Katika kuamua iwapo Hakimu amuamini ama asimuamini shahidi, Hakimu anasaidiwa pamoja na mambo mengine, kuangalia khulqa ya shahidi. Hii ni namna ya shahidi anavyojitambulisha na anavyozungumza wakati wa kutoa ushahidi wake. Pia Hakimu anaweza kuangalia kujiamini kwa shahidi, utulivu, uoni na mfano wa hayo.

 

 

Kiapo Cha Moja Kwa Moja Na Tetesi

(Direct And Hearsay Testimony)

 

Kwa ujumla, kiapo cha moja kwa moja peke yake kina thamani ya kuthibitisha. Hivyo, kama ni jambo linawezekana kuonekana, au kama lina matamshi ya maneno kwa mtu aliyezisikia, ni lazima ushahidi uthibitishwe na shahidi aliyeona kwa macho (eyewitness). Lakini mara nyengine kiapo kisichokuwa cha moja kwa moja pia kinatumika. Kwa mfano, ukweli wa ubaba, uzazi, kifo, ndoa, uteuzi wa Hakimu, inawezekana kuthibitishwa na mtu aliyepokea habari kwa mnasaba wake kutoka kwa watu wenye sifa za kutegemewa.[31] Hata kwa masuala ya matamko mepesi ya shahidi kwamba amesikia kadha na kadha, hayatokubalika lakini aweza kuelezea ukweli wenyewe. Kwa mfano, kwamba siku ya tarehe kadha na kadha, alikuwepo Hakimu wa sehemu fulani, au fulani na fulani alikufa katika tarehe fulani. Ijapokuwa maarifa yake yataegemezwa kwenye tetesi. Kwa maneno mengine, habari zake ni lazima ziwe zimeleta imani fulani ndani ya akili yake ili kukubalika na yeye mwenyewe kama ni maarifa. Pia, kama atasema: “Sikuona hili, lakini ninalitambua” na ikabainika ni kweli, maelezo hayo yatakubalika. Ushahidi kama huo, pia unakubalika kuthibitisha ukweli wa mali kuwa ni waqfu, lakini sio kuthibitisha masharti ya ruzuku hiyo.[32] Kama mtu atamuona mwengine amehodhi mali asiyekuwa mtumwa, atalazimika kuthibitisha hilo kwa kueleza kwamba; inamilikiwa na mtu aliyehodhi, kwa sababu kuhodhi kuna maanisha umiliki.[33]

 

Inawezekana kutokea mara nyengine kwamba watu hao walioshuhudia mauziano au mabadilishano, hawatokuwepo kwa hoja ya kufariki kwao au kuwa kwao masafa ya mbali na kwamba haiwezekani kuwafikisha Mahkamani. Basi ushahidi unawezekana kupokewa kutoka kwa mtu aliyewasiliana na hao mashahidi waliofariki kama wapo mbali, kwamba walishuhudia mauziano hayo. Huu unaitwa “ushahidi juu ya kiapo” (shahaadatu ‘ala shahaadat), na unaruhusika na wanachuoni kwenye kutenda uadilifu kwa sababu ya dharura.[34]

 

Katika Sheria, ushahidi wa moja kwa moja ni ule ambao unalingana na tukio. Kwa mfano kusikika kwa sauti ya mlipuko ni ushahidi wa hoja ya nyumba kuingia moto. Pia, iwapo mtu ameona huo mlipuko ukitokea na kutolea kiapo basi itatambulika kuwa ni ushahidi wa moja kwa moja.[35]

 

Maandishi yanaweza kuthibitishwa na shahidi aliye na maandishi hayo. Ushahidi wa kutumia mdomo (oral) unaweza kuthibitishwa na mtu ambaye ameambiwa hayo maneno.

 

Hadi hapa, ushahidi wa kuthibitisha usio moja kwa moja ni wa tetesi. Kifungu 60 cha Sheria ya Ushahidi kinahitaji kwamba ushahidi wa mdomo katika kesi zote uwe ni wa moja kwa moja, hivyo ni kusema, shahidi ni lazima awe na ufahamu wa moja kwa moja wa hoja anayoyathibitisha. Kwa mfano, suala ni namna moto ulivyoanza kuwaka. Mtu aliyeuona moto ukianza kwa mlipuko anaweza kutoa ushahidi wa tukio hili, kwa sababu yeye ana ufahamu wa tukio hilo. Iwapo katika pita pita zake amemwambia mtu kuhusiana na mlipuko, mtu huyo aliyeelezwa hawezi kutoa ushahidi wa mlipuko kwa sababu ufahamu wake si chochote ila ni tetesi. Ila tu anaweza kutoa ushahidi kwamba aliambiwa kuhusu huo moto.

 

 

Kiapo Ni Lazima Kiendane Na Madai

 

Kiapo cha kisheria ni lazima kiendane na madai, vyenginevyo hakitakuwa na athari. Kwa mfano, pale dai ni kwamba mali imekuwa ikihodhiwa na mdai kwa miaka isiyozidi miwili na mashahidi wake wanasema kwamba, imekuwa mali yake kwa zaidi ya miaka miwili, hakitoruhusiwa. Ingawa, kama wangelisema kwamba mali hiyo inahodhiwa na mdai kwa chini ya miaka miwili, kiapo hicho kisingelikataliwa. Kwa sababu, ujuzi wao unawezekana umepunguwa.

 

Vile vile, kama mdai anadai shilingi milioni moja na mashahidi wanasema ni nusu yake, ushahidi utakaokubalika ni wa shilingi laki tano, na hautokubaliwa kama watasema ni zaidi ya milioni. Chukulia mfano, dai la A ni shilingi milioni moja kwa mali iliyouzwa, na mashahidi wakaeleza kwamba B anadaiwa zaidi ya shilingi milioni moja kwa A kama ni deni, hautakubaliwa.[36] Vile vile, kama kutakuwa na mgogoro wa kiapo miongoni mwa mashahidi wa mdai, ushahidi huo utatupiliwa mbali. Kama ushahidi utapingana na ukweli ulio wazi au unaonekana, hautakuwa na nguvu.

 

Kwa upande wa Sheria inaeleza kwamba kiapo ni lazima kiendane na hoja (madai) zilizoletwa kutoka kwa mdai ama mdaiwa, na hayo madai yawe yale ambayo anaweza kuyathibitisha hata kwa kiapo.[37]

 

 

Kuchagua Ushahidi

 

Chukulia mfano, wadaawa wote wanafanya tuhuma zenye kugongana ulio sahihi na asili kwa mnasaba wa jambo hilo hilo, na wote wapo tayari kutoa ushahidi. Suala linalokuja hapa; ni ushahidi wa nani utakaochukuliwa au kusikilizwa? (Tarji’uilil-bayyinah). Kwa ujumla, kanuni ni kwamba, ushahidi wa yule ambaye tuhuma inaendana na hali iliyo hakika (istis-haab al-haal) utakubaliwa. Kama tulivyoona, Mahkama haiwezi kusikiliza ushahidi kwa kukubaliana na madai ya wote. Kwa sababu, madai ya mmoja ni lazima yatakuwa ni uongo ama dhaifu na kiapo cha ushahidi huo, hakiwezi kuwa ni taarifa au habari au ushahidi.

 

Hivyo, kama mtu atapendelea kutoa ushahidi kwamba mtu alikuwa na afya nzuri kipindi fulani na yule anayepingana anataka kuthibitisha kwamba baadaye alizidiwa na homa na kupelekea kifo. Ikiwa hakuna ushahidi mwengine, ushahidi wa mwanzo utakubaliwa dhidi ya ushahidi wa pili. Sababu ni kwamba; kutokana na kutokuwepo ushahidi wa suala hilo, mtu huyo atatambulikana kuwa yuhai. Vile vile, ushahidi wa mtu anayetaka kuthibitisha kwamba mtu aliyekuwa na uwezo wa kuelewa, atasikilizwa kama ni uchaguzi dhidi ya yule anayedai kwamba alikuwa ni mwendawazimu au mpungufu wa akili katika kipindi fulani. Ushahidi kwamba bidhaa fulani ilinunuliwa, utakubaliwa kama ushahidi kwamba ilikuwa ni zawadi au amana au kodi. Na ushahidi kwamba ilikodiwa utakuwa ni uchaguzi dhidi ya kwamba ilikuwa ni amana.

 

Kama pande zote mbili wanahodhi bidhaa fulani na mmoja wao akadai kwamba bidhaa hiyo ni yake peke yake na mwengine akadai kwamba ni yao wote, ushahidi wa mwanzo utasikilizwa. Sababu ni kwamba, haki yake inakubaliwa na ushahidi wa pili. Kama, kwa upande mwengine, wote wanadai kila mmoja ana haki peke yake, wataamuliwa kuwa ni dai la wamiliki kwa pamoja, kwani hakuna hoja ya uchaguzi wa ushahidi wa mmoja dhidi ya mwengine.

 

Ndani ya Sheria, inaeleza kwamba hoja (ushahidi) ni zile ambazo zinathibitishwa mbele ya Mahkama. Kwa mfano, mtu amesikia sauti ya kitu au kuona mtu ni hoja. Au kwamba kuna vitu fulani vimehifadhiwa katika mfumo maalum katika sehemu maalum ni hoja. Hoja yenye mgogoro ni ile ambayo inabishaniwa na pande zote mbili. Hivyo, ni kazi ya Hakimu kuchagua maelezo anayoamini kuwa ni sahihi. Kwa mfano, A anaeleza kuwa hataki kuirejesha amana aliyompatia B. Kwa upande wa B, yeye anasema kuwa hana hiyo amana kabisa.[38]

 

Ni lazima Hakimu aweke kumbukumbu pale ambapo suala linapokataliwa kuulizwa (objection) kwa shahidi kutoka kwa pande yoyote au na wakili, na Mahkama ikaruhusu kufanya hilo. Kumbukumbu atakayoiweka Hakimu ni lazima ioneshe suala, jibu na pingamizi.[39]

 

Hakimu ni lazima azingatie mwenendo wa shahidi na aweke kumbukumbu maelezo yake anayotoa wakati wa kuulizwa masuala.[40] Iwapo atashindwa kuweka kumbukumbu ya maelezo, Hakimu ni lazima aandike sababu ya kushindwa huko.[41]

 

 

Ushahidi Wa Hali Halisi (tahkiymul-haal)

 

Kwenye baadhi ya kesi, ambapo pande zote mbili hawakufanikiwa kuwasilisha ushahidi wa kutosha, lakini kuna uwezekano wa mmoja wao kuwa na ushahidi wa kukusanya vipande vipande vya tokeo kwenye hali halisi (tahkiymul-haal). Basi huo ushahidi unaotokana na hali halisi utakubaliwa.

 

Kwenye kesi kama hizo, Shari’ah inaweza kumlazimisha mtu aliyetoa ushahidi huo, kufanya kiapo na mara nyengine hatolazimika.

 

Kwa mfano, pale ambapo kuna mgogoro baina ya mume na mke kuhusiana na bidhaa fulani ndani ya nyumba, kama ni bidhaa ya panga na mshale na mfano wake. Vitadhaniwa kuwa ni vya mume na tamko lake litakubaliwa na hukumu itatolewa kwa faida yake. Hukumu itatolewa ikiwa tu mke ameshindwa kuwasilisha ushahidi wowote na mume yupo tayari kula kiapo. Mfano huo huo unaweza kudhaniwa kwa faida ya mke kwa mnasaba wa vifaa vya jikoni, zulia na mfano wake.

 

Kama mfadhili atafungua kesi ya kurudishiwa zawadi aliyoitoa na aliyefadhiliwa akasema zawadi imemalizika (perished) tamko la mfadhiliwa litakubaliwa bila ya kiapo. Kama ni mdhaminiwa, tamko lake litakubaliwa kama atakula kiapo. Kama mjane atadai kuwa ni Muislamu kabla ya kifo cha mumewe aliyekuwa ni Muislamu, lakini warithi wakasema kwamba alikuwa si Muislamu tokea kabla ya kifo, tamko la warithi litakubaliwa. Sababu ni kwamba, tamko la mjane akiwa yeye ni Muislamu litashikana na madai ya warithi pale atakapofika Mahkamani na kutoa ushahidi.[42]

 

Mara nyengine, pande za kesi kuhusiana na mauziano haziwezi kukubaliana na wala yeyote kati yao hayupo tayari kutoa ushahidi, lakini wote wapo tayari kula kiapo kwa mnasaba wa kutilia nguvu madai. Mahkama itatupilia mbali mauziano hayo. Kwa mfano, mnunuzi na muuzaji wa bidhaa hawawezi kukubaliana na dai la bei ya kilichouzwa, na hamna aliye tayari kutoa ushahidi, lakini wote wapo tayari kula kiapo kutilia nguvu madai yao, Mahkama itatupilia mbali madai hayo. Sababu ni kwamba, hakuna msingi wa kupendelea tamko dhaifu la mmoja dhidi ya mwengine.


Imeamuliwa ndani ya Sheria kwamba, mazingira ambayo yatamtia mtu hatiani ni lazima yathibitishwe, na mazingira hayo yakhitimishe asili ya kosa. Kusiwe na pengo baina ya tokeo moja na jengine (mnyororo wa ushahidi – chain of evidence). Pia, mazingira yanayothibitishwa ni lazima yaendane pamoja tu na dhana ya kosa la jinai la mtuhumiwa na wala isiwe inagongana na usafi wake (innocence).[43]

 

Ushahidi Wa Kimazingira (Circumstantial Evidence)

 

Ukiacha ushahidi wa mwanaadamu, ukweli na kimazingira Qariynah inawezekana kutegemewa kama ni ushahidi. Lakini ushahidi wa kimazingira utachukuliwa kuwa na nguvu, pale tu ambapo unafikia kikomo cha uhalisi (Qaati’atan). Kwa mfano, kama mtu ameonekana akitoka kwenye nyumba isiyokaliwa na watu, mwenye khofu na wasiwasi huku amekamata kisu chenye damu, na ndani ya nyumba kuna mwili wa mtu aliyeuawa kwa kukatwa shingo. Mazingira yote haya, yatachukuliwa kuwa ni ushahidi kwamba, mtu huyo aliyeonekana akitoka, amemuua.[44]

 

Mahkama inaweza kwa upande wa Sheria, kuamini hoja fulani ingalipo. Ushahidi huo unaweza kuwa umetokana na tukio asili, tabia za mwanadamu na biashara za kibinafsi au kijamii kwa mnasaba wa kesi iliyo mkononi. Kwa mfano, mtu aliye na bidhaa zilizoibiwa mara tu baada ya kutokezea wizi atakuwa ama ni mwizi au amepokea mali ya wizi.[45]

 

 

Kutengua Kiapo/Ushahidi (Retraction)

 

Kiapo kinaweza kutenguliwa na shahidi mwenyewe kwa kubadili kile alichotolea ushahidi. Kutengua huko ni lazima kufanywe Mahkamani, vyenginevyo, hautakuwa na nguvu yoyote. Kama mashahidi watabadili ushahidi kabla ya amri kutolewa, ushahidi utabadilishwa. Lakini baada ya maamuzi kutolewa, hautaathiri amri. Kama kutengua kumefanyika pale ambapo amri ishatolewa, na kwa upande fulani ushahidi uliotolewa na kutumika kutolea amri, umesababisha hasara yoyote, mashahidi watahusika ipasavyo na hasara hiyo.

 

Sheria inaeleza kwamba njia kuu ya kuuangusha ushahidi unaotolewa na shahidi ni kwa kuoanisha maelezo yake yanayojigonga. Iwapo matamshi yake aliyotoa hapo kabla yanagongana na ushahidi, matamshi hayo ni lazima yaandikwe.[46]

 

Utenguzi wa ushahidi pia unafanywa kwa ushahidi uliotolewa na pande za kesi ukiwa tofauti. Kwa mfano, shahidi mmoja anaeleza kwamba tokeo lilitokea mchana, na mwengine anasema limetokea wakati wa usiku, na ilikuwa giza sana wala haiwezekani kuona kitu.

 

 

Kizuio (Estoppel)

 

Mara nyengine, hakuruhusiwi kutolewa ushahidi au ukweli fulani kwa mnasaba wa tabia ya anayetaka kutoa ushahidi huo. Hii inaitwa (Bayaanu adh-Dharuurah) lenye kuendana na kizuio. Kwa mfano, kama mmiliki wa mali fulani, amemuona mtu mwengine, akiuza mali hiyo na kunyamaza kimya, hataruhusiwa kuthibitisha kwamba mtu huyo aliyekuwa akiuza hakumpa mamlaka ya kufanya hivyo.

 

Sheria inaeleza kwamba, pale ambapo mtu kwa tamko au tendo kwa makusudi kabisa ameruhusu mtu mwengine kuamini jambo kuwa ni kweli na kulitendea kazi kwa kuamini huko, iwapo yeye mwenyewe ama ni wakala wake, hataruhusiwa katika kesi yoyote kukataa ukweli wa jambo hilo.[47]

 

Mfano, kwa makusudi kabisa, A anampelekea B kuamini kwamba ardhi aliyonayo A ni ya kwake na hivyo kumtapeli B kuingia kwenye mauziano na kulipia hiyo ardhi. A hataruhusiwa katika kesi hii kukataa ukweli wa kujaribu kumtapeli B.

 

 

Tafsiri

 

Kwa mujibu wa al-Hilli na Ibn Qudaamah, tafsiri ya maandiko iliyofanywa na watu wawili walio waadilifu inaruhusiwa kutumika Mahkamani.[48]

 

Sheria kwa upande wake pia inaruhusu kufasiriwa hati pale itakapoona kuna haja ya kufanya hivyo.[49] Pale ushahidi utakapowekwa kumbukumbu kimaandishi kwa lugha ya Kiingereza, Mahkama inaweza kuamuru kufasiriwa kwa maandishi hayo kwa yule wakili au mtu asiyeelewa Kiingereza.[50] Kazi ya kufasiri maandishi pia utafanywa kwa shahidi ambaye haelewi lugha iliyoandikwa kwenye hati.[51]

 





[1] Al-Majallah, uk. 289.

[2] Al-Bayhaqi, as-Sunan al-Kubra, X, uk. 250.

[3] Ahmad Hassan az-Zayyat; Tariykh Adab ‘Arbai, uk. 209.

[4] Bukhari, ash-Shaib, II, uk. 1085.

[5] Sheria ya Ushahidi, S. 101

[6] Sheria ya Ushahidi, S. 102

[7] Sheria ya Ushahidi, S. 103

[8] Sheria ya Ushahidi, S. 106

[9] Sheria ya Ushahidi, S. 107

[10] Sheria ya Ushahidi, S. 110

[11] Sheria ya Ushahidi, S. 114

[12] Ibn Farhuun, Tabsirah, II, uk. 74-77.

[13] Sheria ya Ushahidi, S. 45

[14] Ibn Farhuun, Tabsirah, I, uk. 243.

[15] Sheria ya Ushahidi, S. 138

[16] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XII, r. 2

[17] Al-Mawardi; Adab al-Qaadhi, uk. 350.

[18] Sheria ya Mwenendo wa Madai, S. 118 (1)

[19] Sheria ya Mwenendo wa Madai, S. 118 (2)

[20] Sheria ya Mwenendo wa Madai, S. 119

[21] Sheria ya Mwenendo wa Madai, S. 137 na 138

[22] Al-Mawardi; Adaab al-Qaadhi, uk. 350.

[23] Al-Marghinanani; al-Hidayah, II, uk. 203. Angalia pia Sahihi Muslim.

[24] Shaih, I, uk. 80.

[25] As-Sarkhasi; K. al-Mabsuut, XVI, uk. 116-120.

[26] Angalia ukurasa wa 6, S. cha 2 cha Sheria hii.

[27] Sheria ya Mwenendo wa madai, O. XXII, r. 1

[28] Sheria ya Ushahidi, kifungu 155 (1)

[29] Fathul-Qaadir, Juzuu ya VI, uk. 458-459; Hidayah, Juzuu ya VI, uk. 458-459.

[30] R. V. Madhub Chunder (1874) 21 W. R. Cr. 13, 19 (India).

[31] Hidayah, Juzuu ya VI, uk. 466-467; pia angalia al-Majallah, uk. 287-288.

[32] Hidayah, Juzuu ya VI, uk. 469.

[33] Hidayah, Juzuu ya VI, uk. 522-523.

[34] Hidayah, Juzuu ya VI, uk. 522-523.

[35] Sheria ya Ushahidi, S. 3

[36] Al-Majallah, uk. 291.

[37] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XXII, r. 3 (1)

[38] Sheria ya Ushahidi, kifungu 3

[39] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XXI, r. 11

[40] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XXI, r. 12

[41] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XXI, r. 13

[42] Hidayah, Juzuu ya VI, uk. 425.

[43] R. V. Harishchandra Ladaku Thange, Supreme Court of India, Justices Arijit Pasayat and P.  P. Naolekar, India's National Newspaper, 04/Sept/2007.

[44] Al-Majallah, uk. 297.

[45] Sheria ya Ushahidi, S. 114

[46] Angalia kesi ya Matofali V. R. (20 E. A. C. A. 232)

[47] Sheria ya Ushahidi, S. 115

[48] (a) Ibn Qudamah; Akhbar al-Qudat, IX, uk. 100 (b) Ibn Farhuun; Tabsirah, I, uk. 86-88.

[49] Sheria ya Ushahidi, S. 162 (3)

[50] Sheria ya Mwenendo wa Madai, S. 117

[51] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XXI, r. 9

Share

012-Hakimu Wa Kiislamu: Sura Ya Sita

SURA YA SITA

 

HUKUMU

 

 

Hukumu

 

Hukumu (hukm) inatolewa tafsiri kuwa ni kile ambacho kinasuluhisha au kinamaliza mgogoro. Hukumu inaweza kuwa ni ya maelekezo, inayomuelekeza yule aliyeshindwa (judgement-debtor) kumpa chochote kwa aliyeshinda (judgement-creditor). Au kuzuia, kama pale kesi inapoamuliwa dhidi ya mdai ikiwa kwamba hana mamlaka ya kupatiwa haki aliyodai. Hukumu na amri za Mahkama ni lazima ziheshimiwe.

 

Pale hukumu inapotolewa, suala linaibuka, nani inayemshika hukumu ama amri hiyo? Ni kwamba inawashika wadaawa na pia wale ambao Shari'ah inawaruhusu kuwakilisha, lakini sio kwa wengine. Ama baina yao, suala linaamuliwa kuwa limekhitimishwa na kwamba haiwezi kusikilizwa baadaye (res judicata), isipokuwa kwa kesi maalum. Hivyo, hukumu kwa mnasaba wa mali dhidi ya mtu mwenye kuihodhi hiyo mali, inamshika huyo anayehodhi mali hiyo yeye peke yake na wale wanaopata manufaa nayo hiyo mali kutoka kwake lakini sio wengine.[1]

 

Hata hivyo, kwa mujibu wa Rukuu’l-Islaam, hukumu dhidi ya mtu mwenye kuhodhi mali anayedai kwamba mali hiyo ni waqf inawafunga watu wote. Lakini sio hivyo kwa maoni ya Abu Layth na Sadnu’sh-Shahiid.[2] Na kama ilivyotajwa, hukumu dhidi ya mrithi wa wasia, kuzungumza ukweli, inaifunga mali ya urithi.

 

Hukumu ya Mahkama inaweza kuwa batili katika mazingira fulani. Kwa mfano, kama imekwenda kinyume na Shari'ah maalum kama haki za msingi (mfano haki ya kusikilizwa) au kama imeegemezwa katika ushahidi usiokubalika kutumika Mahkamani au kama imempendelea mtu ambaye Hakimu ana faida naye, kama vile baba, mama, mke au watoto.

 

Sheria kwa upande wake pia inaweka pingamizi ya kufunguwa kesi ambayo imeshatolewa hukumu hapo kabla. Pingamizi hii ni kwa wadaawa wale wale na madai yale yale yaliyofunguliwa kwenye Mahkama nyengine.[3] Kwa mfano, A mdai na B ni mdaiwa, A anadai B kuvunja makubaliano ya mkataba. Mahkama X ikaamua B kumlipa fidia A kutokana na kuvunja mkataba huo. Mahkama Y ambayo ina hadhi sawa na Mahkama X (kwa mfano zote ni Mahkama za Wilaya) haiwezi kuisikiliza tena kesi baina ya A na B kwani imekwishatolea ufumbuzi. Isipokuwa B anaweza kukata rufaa katika Mahkama ya juu (kwa mfano Mahkama ya Mkoa).[4]

 

 

Kutoa Hukumu

 

Hukumu iwe kwa maandishi kwa mujibu wa mawazo ya wanavyoni. Al-Bayhaqiy amenukuu Hadiyth inayosema kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamrisha kuandikiwa wakfu kwa ajili ya Ansaar (wasaidizi wa Muhajiriyn huko Madiynah). Waliomba kwamba hiyo iandikwe kwa ndugu zao wa Ki-Quraysh. Hivyo al-Bayhaqiy amesema kwamba Hakimu anaweza kuandika hukumu yake kwa upande wenye kesi pale anapoombwa.[5]

 

Ibn Qudaamah, hata hivyo, ana mawazo ya kwamba nakala mbili za hukumu zitayarishwe, moja itunzwe chumba cha kumbukumbu (diwaan) na nyengine kama ikiombwa ipelekwe kwa aliyeshinda kesi.[6]

 

Al-Kasaniy, ameeleza tabia ya mwenendo wa Kimahkama enzi za leo, kumbukumbu ya madai pamoja na tarehe iandikwe kwanza, kisha majina ya mashahidi na kisha majibu. Kumbukumbu hii inawekewa mtindo wa mwezi au mwaka, kwenye mkoa au kesi au faili (linaloitwa qimatrah) ikiwa na muhuri wa Mahkama.[7]

 

Sheria inaeleza kwamba, Hakimu atatamka hukumu pale kesi itakaposikilizwa. Baadaye itafuatia amri ya hiyo hukumu.[8] Masharti mengine muhimu yanayoeleza namna ya kutayarisha hukumu ni kama yafuatayo:

 

  1. Ni lazima itamkwe hadharani (open court)
  2. Iwe kwa maandishi
  3. Hakimu hana ruhusa ya ya kuiacha hukumu kusomwa na msaidizi wake
  4. Iwe na tarehe
  5. Isainiwe na Hakimu
  6. Iwe na maelezo ya kesi
  7. Namna alivyofikia kwenye hukumu hiyo (maoni ya Hakimu)
  8. Ioneshe maamuzi aliyofikia
  9. Sababu ya maamuzi hayo kufikiwa hivyo
  10. Hoja za msingi na namna ilivyozichunguza hoja hizo[9]

 

 

Athari Ya Maoni Binafsi Ya Hakimu

 

Kwa mujibu wa wanachuoni walio wengi, Hakimu anaweza kuihukumu kesi kulingana na uelewa wake binafsi wa ukweli wa kesi. Abu Haniyfah anasema kwamba, uamuzi kama huo unakubalika kwenye kesi tu ambapo ukweli ulitambulika kwenye uelewa binafsi wa Hakimu baada ya kuteuliwa kushika ofisi.[10]

 

Hakimu Abu Yuusuf ana mawazo kwamba, uamuzi huo ni sahihi isipokuwa katika kesi za jinai (kama uzinifu, wizi n.k.)[11]

 

Maalik kwa upande wake, anakataa Hakimu kutumia uelewa wake binafsi wa kesi.[12]

 

Al-Mawardi ametoa mawazo kwamba, Hakimu aitamke ndani ya hukumu iwapo amefikia uamuzi wa kesi hiyo kwa mujibu wa uelewa wake binafsi wa kesi hiyo.[13] Wanachuoni wengine wanakubali Hakimu kutumia uelewa wake binafsi bila ya kikwazo au lawama.[14]

 

Sheria kwa upande wake inaruhusu kuwepo maoni binafsi ya Hakimu. Hata hivyo, wakati wa kuisoma hukumu ni lazima Hakimu aeleze maoni hayo na sababu ya kuyaingiza hadi kufikia hukumu hiyo anayoitoa.[15]

 

 

Kikaza Hukumu (Execution Of Decree)

 

Hii ni hati inayotolewa baada ya hukumu kusomwa ili kuifanyia kazi hukumu hiyo kwa vitendo. Mfano hukumu ya kuruhusu kuvunja nyumba, kikaza hukumu chake ni hati ya kuivunja nyumba hiyo.

 

Hukumu bila ya kufanyiwa kazi, haina nguvu kama alivyosema ‘Umar kumwambia Abu Muusa al-Ash’ariy kama ilivyoelezwa mwanzo wa kitabu hiki. Kwa mujibu wa al-Marghinani, kikaza hukumu kitolewe na Mahkama hiyo hiyo iliyotoa hukumu. Kwa sababu hukumu bila ya kuifanyia kazi haikutani na haki inayostahiki. Kama Hakimu ametoa kikaza hukumu na kuiacha izagae ofisini, Hakimu atakayerithi ataifanyia kazi, kuwa nayo na kuipa nguvu kikaza hukumu hicho kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa na waliomtangulia kwa lengo la kufanyiwa mapitio.

 

Pale hukumu inapotolewa kwa upande wa kesi, Shari’ah pia inatoa ruhusa ya kuifanyia kazi na kuiwasilisha kwa wakala wa Mahkama hiyo kwa kuipa nguvu (tafiydh). Hukumu ni lazima ikaziwe kwa kumlazimisha aliyeshindwa kuifuata na ulazima huo kwa kawaida unafanyiwa kazi kwa kumpeleka jela mshindwa hadi atii.

 

Kama hukumu inaweza kuthibitishwa kwa kupelekwa mali maalum au kwa uuzaji wa mali ya aliyeshindwa, Mahkama itatoa amri kwa kupelekwa jela au kuuzwa. Hili litafanywa, pale tu, mshindwa kwa hali nyengine hatimizi hukumu.[16] Kwenye ukazaji wa hukumu ya pesa, mshindwa atafungwa jela iwapo atarudisha nyuma jitihada za kuifanyia kazi hukumu; lakini kama ataweza kuithibitisha Mahkama kwamba hana mali au uwezo, hakutakuwa na sababu ya kufungwa jela. Kama Mahkama hiyo itatambua kwamba mshindwa ameficha mali yake au amekataa kulipa kiwango kilichotajwa ndani ya hukumu, ingawa ana uwezo wa kulipa, basi atafungwa jela hadi alipe. Lakini, kama Hakimu anaona kwamba aliyeshindwa amesota sana jela, ataachiwa huru.

 

Kwa upande wa Sheria, tunaona kwamba mshindi anahitajia kuandika barua ya maombi kwa Hakimu ili kuifanyia kazi hukumu iliyotolewa. Barua hiyo ioneshe mambo yafuatayo:[17]

 

  1. Nambari ya kesi
  2. Majina ya pande za kesi (mdai na mdaiwa)
  3. Tarehe ya hukumu
  4. Iwapo imependekezwa rufaa yoyote
  5. Iwapo yamefanywa malipo kwa Mahkama au baina ya wadaawa
  6. Iwapo kuliwahi kufanywa ombi kama hili hapo kabla
  7. Kiwango cha pesa (malipo au fidia) kilichotozwa
  8. Jina la yule aliyeshindwa kesi
  9. Msaada wa mahkama katika kuifanyia kazi hukumu hiyo:

a)    Iwapo kwa kufikisha mali Mahkamani

b)    Kuiuza mali

c)     Kuteuliwa kwa mpokeaji

d)    Iwapo Mahkama tayari imeshatoa maelekezo

 

 

Marejeo (Reference) Na Mapitio (Review)

 

Shari’ah inaruhusu mapitio ya hukumu kwenye kesi ambapo imekiuka kanuni za Shari’ah, hapo kesi itasikilizwa tena kwa mara nyengine.

 

Wanachuoni hawakujihusisha na marejeo za kesi kwenda Mahkama nyengine au mapitio kwa chini zaidi. Muongozo kuhusiana na hili, unaweza kuchukuliwa kutokana na simulizi refu iliyopokewa na Waki’ katika Akhbaar-al-Qudhaah ambapo ‘Aliy ameripotiwa kusema kwa wenye kugombana ambapo kesi ilihukumiwa na yeye:

 

Ikamateni hukumu yangu kwa muda, mpaka mukutane mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuhukumu kesi yenu.[18]

 

Kutokana na mapokezi haya, tunaweza kuamua kwamba:

 

1)  Amri ya muda inaruhusika (ad interim injuctions), na

2)  Hakimu anaweza kuwasilisha kesi kwenye mamlaka ya juu ikiwa haiangukii kwenye uwezo wake wa Kimahkama au ameona ni vyema kuamuliwa na mamlaka ya juu.

 

Maneno ya ‘Umar katika barua yake kwenda kwa Abu Muusa al-Ash’ariy inasema:

 

Jiepushe na hukumu yako ya jana, ambayo umetanabahi kwenye akili yako na ukaongozwa njia sahihi kurudi kwenye hukumu ya haki, kwa sababu haki inasimamishwa, na hakuna chochote kinachobatilisha kuliko haki, kwa sababu ni bora kurejea kwenye usahihi kuliko kuendelea na lisilo sahihi.

 

Kwa mujibu wa al-Marghinani, ni mzigo juu ya kila Hakimu kusimamia na kuipa nguvu kikaza hukumu cha Hakimu mwengine, isipokuwa kama ama hicho kikaza hukumu kitakuwa ni kinyume na hukumu za Qur-aan au Sunnah, au maamuzi dhidi ya makubaliano ya wanachuoni.[19]

 

Kwa ujumla, si vizuri kumpinga Hakimu aliyetangulia kutoa hukumu nyengine juu ya kigezo cha tofauti za mawazo kwa mnasaba wa mada ya Kishari'ah kama ilivyoshauriwa ndani ya al-Jaami’ as-Saghiyr ya Muhammad na kunukuliwa na al-Marghinani ndani ya al-Hidayah.[20]

 

Al-Hilli anasema kwamba Hakimu aliyemrithi Hakimu aliyeondoka, akiona makosa fulani ndani ya maamuzi ya baadhi ya Mahakimu, Hakimu aliyerithi anaweza kufanyia kazi kikaza hukumu kwa niaba yake.[21]

 

Sheria inaeleza kwamba Hakimu anaweza kumuomba Hakimu aliye juu yake kuipitia kesi. Kwa mfano Hakimu wa Wilaya kumuomba Hakimu wa Mkoa kumpatia maoni.[22]

 

Iwapo upande mmoja wa kesi umeona kwamba haujatendewa haki, unaweza kuomba mapitio katika Mahkama iliyoitoa hukumu yake. Utaratibu huu unaweza kufanywa iwapo hukumu yake ilitoa nafasi ya rufaa au haikutoa.[23]

 

Mahakama Kuu inaweza kuamrisha kupatiwa jalada la kesi kutoka Mahkama zilizo chini yake. Mahkama Kuu inaweza kuamrisha vyenginevyo iwapo itatambulika mambo yafuatayo:

 

  1. Iwapo Hakimu ametumia nguvu zisizo zake (unauthorized jurisdiction)
  2. Ameshindwa kutumia ipasavyo nguvu aliyopatiwa
  3. Amefanyia kazi nguvu zake kwa njia zisizo sahihi[24]

 

 

Amri Ndogo Ndogo (Ancillary Orders)

 

Mahkama imepewa nguvu ya kutoa amri ndogo kwa malengo ya kukitunza kiini kikuu cha mzozo. Kwa mfano inawezekana kutokea kwamba wadaawa wote wana malengo ya faida katika mali fulani, waweza pia kuwa hawapo mbele ya Mahkama na pirika zao hazijulikani. Kwa kadhia kama hizo, Mahkama inalinda hifadhi za faida za wengine kwa kuteuwa mpokeaji au kwa kuchukua ulinzi kutoka kwa upande wenye kuihodhi. Kwa mfano, kama mali imehodhiwa na mtu, na mtu mwengine anatoa ushahidi kwamba ni mali ya baba yake aliyefariki na kumuacha yeye na ndugu aliyepotea. Hakimu anapotengeneza hukumu kuhusiana na nyumba hiyo kwa faida ya mdai, ni lazima, kwa mujibu wa Abu Haniyfah, awache gharama nyengine kwenye mikono ya mtu aliyeihodhi, bila ya kuchukua ulinzi kutoka kwake.[25] Lakini kwa mujibu wa wafuasi wa Abu Haniyfah, kama mtu mwenye kuihodhi mali atatoa ukweli wa mgogoro kwamba ilimilikiwa na aliyefariki, ni lazima iondoshwe kutoka kwenye mikono yake na ikabidhiwe kwa mtu muadilifu ili kuikamata kwa niaba ya mrithi asiyekuwepo.

 

Hivyo hivyo, ni lazima Mahkama ichukue ulinzi pale inapoamrisha mume kulipia huduma kwa mwanamke anayedaiwa kumkimbia mke huyo.

Hakimu ndani ya Sheria anaweza kutoa amri nyengine ndogo ndogo ambazo anaamini zinafaa. Kwa mfano amri ya kuizuia mali, kufanya jambo, kumuamuru mtu kula kiapo juu ya mtu fulani anayehusiana na mali.[26]

Kuna kesi ambazo zinatolewa amri ya kuuzwa mali kabla ya kumaliza kesi (interlocutory orders). Hizi ni mali ambazo zinaweza kuhamishika. Kwa mfano katika kesi ya gari baina ya A na B, ambayo kwa amri ya Mahkama gari hiyo imehodhiwa kabla ya hukumu (attached before judgement). A ambaye gari hiyo imesajiliwa kwa jina lake, anakhofu kwamba kwa kipindi ambacho kesi itakuwa imesimama, gari hiyo inaweza kuharibika au kufisidika thamani yake. Katika hali kama hiyo, A anaweza kuomba kwa Hakimu kwamba gari hiyo iuzwe mara moja.[27]

 

Kizuizi (Time Barred)

 

Ni utaratibu wa nchi nyingi kuweka kipindi cha kuzuia kusikiliza kesi. Ili kwamba; kama mdai atakuja Mahkamani baada ya kumalizika kipindi kilichotajwa, kesi yake haitosikilizwa.

 

Ni kawaida kuwepo uteuzi wa Hakimu ambaye anakuwa na mamlaka fulani tu kwenye kutolea hukumu. Kwa mfano Hakimu kwa ajili ya migogoro ya ndoa, mirathi tofauti na yule wa masuala ya nyumba, ardhi, jinai nk. Hali kadhalika, amri ya kumzuia Hakimu asisikilize kesi itakayovuka kipindi kinachotakiwa ipo ndani ya mamlaka yake. Kwa mfano, A kudai kuibiwa mazao yake miaka 15 iliyopita.

 

Wasomi wa leo, wamekubaliana kwamba amri kama hiyo ni kwa mujibu wa kanuni za Shari’ah za Kiislamu.[28] Dhana ya kale ya Shari’ah, hapana shaka ilikuwa kwamba haki ya mtu haitopotea kwa sababu ya kupita muda na kwamba ni mashaka kwa Hakimu kusikiliza dai lake.[29] Hata hivyo, inawezekana kwamba, kuanzishwa kwa Shari’ah ya kizuizi ni kielelezo cha nguvu kwa ukweli kwamba Shari’ah kwa kipindi kirefu, imekuwa inatafuta njia za kujifananisha na mazingira ya wakati na Shari’ah haijakataa kanuni hii.[30]

 

Sheria ya Kuzuia Kufunguliwa Kesi[31] Mahkamani imeweka jedwali ambalo linaonesha aina tofauti ya kesi, na kizuizi cha idadi ya siku kwa ajili ya kufungulia kesi. Kwa mfano A ameingiliana mkataba wa ujenzi na B, B ameshindwa kuondosha mabaki ya vifaa vilivyotumika katika ujenzi. A akitambua kwamba ni wajibu wa B kuifanya kazi na bila ya kufungua kesi ndani ya siku tisiini (90) atazuiliwa kumdai fidia B katika Mahkama.[32]

 

 

Ushauri Wa Wanachuoni

 

Hakimu anaweza kuwaendea wanachuoni kwa ajili ya ushauri kama vile Mufti na Maulamaa kuhusiana na vifungu vya Shari’ah. Jambo hili sio tu linaruhusiwa bali kupendekezwa na wanachuoni. Fikra hii pia inathibitishwa na mapokezi kutoka kwa Maswahaba ambayo inawekwa hapa chini kwa manufaa zaidi:

 

‘Uthmaan bin Affaan alimuomba ‘Abd Allaah bin ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhuma) akamate nafasi ya kuwa Hakimu kwa ajili ya watu. Lakini ‘Abd Allaah akamuomba mkuu wa majeshi kumuweka mbali na kazi hiyo. Khaliyfah alimuuliza sababu kuu itakayomkubalisha kukubali cheo hicho ambapo baba yake amekuwa nacho. Ibn ‘Umar alisema:

 

“Kama kulikuwa na hitilafu yoyote kwa baba yangu, alikuwa akimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), lakini mimi sioni mtu yeyote wa kumuuliza.”[33]

 

Tumeona kwamba Shari'ah inaruhusu Hakimu kumuomba Hakimu mwenziwe kupata ushauri wa kesi aliyonayo mkononi. Lakini pia Sheria inaruhusu kuwepo kwa washauri ama wazee wa busara katika jopo la Mahkama.[34]

 

Mahkama inaruhusiwa kwa nguvu ilizopatiwa, kumteua mtu yeyote atakayefaa kuishauri katika kesi. Pia pande za kesi zinaweza kutoa ombi kama hili. Mshauri wa Mahkama anaweza kuwa ni mmoja au zaidi. Hakimu ni lazima aweke kumbukumbu ya ushauri huo. Hata hivyo, mshauri huyo hatokuwa na sauti katika maamuzi (hukumu) ya Mahkama.[35]

 

 

Suluhu (Arbitration)

 

Suluhu ni kinyume cha hukumu, kwani suluhu ni maridhiano ya kumaliza kesi kwa pande zote mbili bila ya kutezwa nguvu. Ama hukumu hutolewa ikiushinikiza upande ulioshindwa kuifuata.

 

Shari’ah ya Kiislamu inaruhusu pande za kesi zinazogombana kuhusu madai juu ya mali fulani na haki binafsi nyengine kupeleka malalamiko yao kwa msuluhishi/mpatanishi (arbitrator). Kwa maarufu, inajulikana kama ni tahkiym. Msuluhishi ni lazima awe na sifa zinazofanana na kuchukua kiti cha Uhakimu, kwani hakika, anafanya kazi kama ya Hakimu, lakini dhimmi[36] anaweza kuteua mtu wa imani kama zake kuwa msuluhishi.

 

Kwenye makosa ya jinai yanayoadhibiwa kwa hadd na kisasi, suluhu hairuhusiwi. Msuluhishi amepewa nguvu ya kusikiliza ushahidi na kuapisha viapo kama ilivyo Mahkamani na kwa suluhu ya msuluhishi iliyopelekwa Mahkamani ili kupata ridhaa na usajili wa Mahkama. Hukumu ya suluhu hiyo itatolewa kwa mujibu wa vifungu vyake ikiwa tu haipingani na Shari’ah.

 

Kwa upande wa Sheria, Mahkama katika hali ambayo wadaawa hawajateua msuluhishi, inaweza kuteua msuluhishi wa kesi ya wadaawa pale inapoona inafaa.[37]

 

Pale ambapo wadaawa wameafikiana, wanaweza kuteua msuluhishi kabla ya kutamkwa hukumu katika Mahkama. Maombi hayo yanatakiwa kuwa kwa maandishi, na yanatakiwa kutiwa saini na msuluhishi. Msuluhishi huyu anateuliwa kwa makubaliano ya wadaawa. Mahkama inaweza kuweka muda wa kufikia suluhu hiyo.[38]

 

 

[1] Fataawa ‘Alamgiri, Juzuu ya III, uk. 525.

[2] Fataawa ‘Alamgiri, Juzuu ya III, uk. 526.

[3] Sheria ya Mwenendo wa madai, S. 6 (1).

[4] Sheria ya Mwenendo wa madai, S. 72.

[5] Al-Bayhaqiy, as-Sunan al-Kubra, X, uk. 131.

[6] Ibn Qudaamah, Akhbar al-Qudat, IX, uk. 75.

[7] Al-Kasaniy; K. Bada’ia as-Sanaia, VII, uk. 12.

[8] Sheria ya Mwenendo wa Madai, S. 25

[9] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XXIII, r. 2-3

[10] Al-Mawardi; Adaab al-Qaadhi, II, uk. 369.

[11] Al-Mawardi; Adaab al-Qaadhi, II, uk. 370.

[12] Al-Mawardi; Adaab al-Qaadhi, II, uk. 370.

[13] Al-Mawardi; Adaab al-Qaadhi, II, uk. 377.

[14] Muhammad Sangalaji, Qadhaa daar Islam, uk. 140.

[15] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XXIII, r. 3 (2)

[16] Fataawa ‘Alamgiri, Juz. ya 3, uk. 501-502.

[17] Sheria ya Mwenendo wa Madai, O. XXIV, r. 7-8

[18] Waki’, Akhbaar-al-Qudhaah, I, uk. 97.

[19] Al-Marghinani; al-Hidayah, II, uk. 144-145.

[20] Al-Marghinani; al-Hidayah, II, uk. 144-145. Kwa maelezo angalia as-Sarkhasi; K. al-Mubsuut, XVI, uk. 84.

[21] Al-Hilli, K. Sharai’ al-Islam, uk. 315.

[22] Sheria ya Mwenendo wa Madai, S. 88

[23] Sheria ya Mwenendo wa Madai, S. 89

[24] Sheria ya Mwenendo wa Madai, S. 90

[25] Al-Hidayah, Juzuu ya VI, uk. 430.

[26] Commonwealth Consolidated Acts, Proceeds of Crime Act 2002, section 39.

[27] B. D. Chipeta, Civil Procedure In Tanzania, Dar es Salaam University Press Ltd, Tanzania, 2002.

[28] Raddu’l-Mukhtaar, Juzuu ya IV, uk. 377-371.

[29] Raddu’l-Mukhtaar, Juzuu ya IV, uk. 377-379.

[30] Abdur-Rahiym, The Principles Of Islamic Jurisprudence, toleo la mwanzo, (1991), uk. 356.

[31] Rudia Limitation Decree, chapter 12

[32] Limitation Decree, S. 3, jedwali I, uk. 10. Angalia pia Sheria ya Mikataba – Contract Decree, chapter 149.

[33] Mapokezi hayo yamepokewa na at-Tirmidhiy lakini mapokezi yaliyotolewa hapa yamepokewa na al-Khaatib at-Tibriyz ndani ya Mishkaat al-Masaabih, uk. 325. Hata hivyo, Tibriyz hakutoa chanzo.

[34] Rudia Sheria ya Mahkama ya Ardhi – Zanzibar, no. 12 ya 1994, S. 4 (1), 5 (1), 6 (2) na 37.

[35] Sheria ya Mwenendo wa Madai, S. 118; Angalia pia Sheria ya Mahkama, Sura ya 3, O. XXII

[36] Raia asiyekuwa Muislamu anayeishi katika taifa la Kiislamu.

[37] Sheria ya Usuluhishi, S. 7

[38] Rudia Sheria ya Mwenendo wa Madai, kifungu 66, Jedwali ya Tatu, S. 1-5, uk. 350

Share

013-Hakimu Wa Kiislamu: Sura Ya Saba

 

SURA YA SABA

 

WAFANYAKAZI WA MAHKAMA

 

 

Wanachuoni wanakubaliana kwamba ni lazima akuwepo karani anayeweza kuandika na awe ndani ya sehemu ya jamii ili kusaidia kazi ya kutoa hati za wito. Awe ni mtu mwenye kuisimamisha na kuifuata Shari’ah na amri zake kuhusiana na vikaza hukumu. Bila ya kusahau, ni lazima karani awe ni mtu anayeaminika na mwenye elimu nzuri ya Fiqhi na akae sehemu ambayo Hakimu atamuona nini anachoandika.

 

Kwa mujibu wa Sheria ya Mahkama, Jaji Mkuu anaweza kuteua watu kwa idadi yoyote kuwa ni wasajili, makarani, wadhamini, wafasiri na maofisa wengine wanaohitajika na Mahkama yoyote. Msajili wa Mahkama Kuu anaweza kuwataka wateuliwa hao kula kiapo.[1]

 





[1] Sheria ya Mahkama, S. 25 na 26.

Share

014-Hakimu Wa Kiislamu: Sura Ya Nane

 

SURA YA NANE

 

HITIMISHO

 

 

Maelezo yote haya, ingawa yamekusanywa kwa juhudi kubwa kutoka kwenye vyanzo mbali mbali, yanaonesha ukweli ya kwamba muundo na utaratibu wa Kishari’ah siku za mwanzo za Uislamu haukuwa mwepesi kama wengi wanavyofikiria. Hapana shaka, haukuwa utaratibu wenye mazonge yanayohusisha mbinu nyingi za kitaalamu zisizosaidia kitu kusuluhisha matatizo. Hata hivyo, ukosefu wa maelezo kamili na ya moja kwa moja ni miongoni mwa matatizo ya wanahistoria na wanachuoni wetu.

 

Siku za leo, kuna mawazo mengi kwamba maelezo hayo ndani ya Shari’ah, khasa mwenendo wa Mahkama, zinachukuliwa na kuazimwa kutoka sheria ya Kirama na sheria za Sasanide.[1] Pia inasemwa kwamba Hadiyth zinatungwa ili kuzifanya hizo kanuni zilizoazimwa ziwe za Kiislamu. Lakini wanachuoni wa Kiislamu wanatetea kwamba Hadiyth hizo ni sahihi, na ni maneno hasa ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yaliyofikishwa kwa uangalifu wa hali ya juu kutoka kwa wasomi na wacha Mungu.

 

Tukiachilia mbali mgongano huu, ambao ni nje ya kazi hii, sasa tugeukia kwenye mada ambayo Uislamu ni msingi wa maisha na sio msingi wa mwenendo wa kesi. Uislamu mara zote unatoa mwangaza ili wafuasi wake wabakie ndani ya mhimili sahihi wa mafunzo ya Kiislamu. Uislamu, tokea mwanzo, pamoja na hitilafu tulizonazo, unatufunza kuwa na mwenendo maalumu wa maisha, kuweka mbele umoja.

 

Kutumia njia za kisasa na mitindo mipya ya kazi hakika ni tendo la Kiislamu. Kama Waislamu wa leo wanapigana kwa kutumia bunduki, sayansi na teknolojia, basi wasizuiliwe kwenda kinyume na waliowatangulia ambao walipigana kwa silaha na mapanga. Kupigana sehemu iliyo wazi ulikuwa ni mtindo wa Waarabu lakini pale Salmaan al-Faarisiy alipotoa wazo la kwamba handaki lichimbwe, ambalo ni mtindo wa vita vya Wafursi, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alilikubali kwa vile ilikuwa ni njia bora ya kushinda vita hivyo. Na ni nani aliyesema kwamba yote ni makosa kwa Wakristo, Wayahudi, Waarabu, Warumi na Wafursi kutokana na uoni wa Kiislamu? Lile lililokuwa ni kosa juu yao liliwekwa, linawekwa na litaendelea kuwekwa wazi na kwa nguvu zote kupingwa na Uislamu. Ama lililokuwa zuri kwao wao linakubaliwa kwa uwazi.

 

Uislamu unahimiza kusoma yote ambayo ni mazuri na yenye manufaa kutoka kwa watu wengine. Ingawa Waislamu walishindwa kupata ridhaa ya Mola wao, lakini ilikubalika (kutokana na Shuura waliyoifanya) kwamba mateka wa vita vya Badr wawafundishe watoto wa Kiislamu namna ya kuandika. Wanachuoni kadhaa wamenukuliwa wakitoa ushauri: “Tafuta elimu hata iwe China”.[2]

 

Ndani ya kuta za mwenendo wa Kishari’ah sio dhambi kuomba muongozo kutoka sheria nyengine na kutumia vifungu vyote ambavyo haviendi kinyume wala vyenye kuchukiza dhidi ya mafundisho ya Kiislamu.



[1] Kwa mifano angalia: Goldziher, Introduction Of Islamic Theology And Law – Utangulizi Wa Dhana Ya Kiislamu Na Sheria (Tafsiri ya Kiingereza imefanywa na Andras na Ruth Hamori) uk. 44.

[2] Hii kwa wengi inajulikana kuwa ni Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), lakini ukweli si Hadiyth ni maneno tu ya kutungwa yanayotumika sana kwa kuhamasishia watu elimu.

Share