Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako

 

 

 

Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako 

 

 

Mwandishi: ‘Aadil Fat-hi ‘Abdullaah

 

Kimefasiriwa Na: Abu Arwaa

 

 

 

 

 

Share

001-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Utangulii

 

UTANGULIZI

 

Kila jinsi ya sifa njema anastahiki Allaah ambaye Ametufanyia ndoa kuwa ni katika shari’ah ya Dini hii, Akajaalia baina ya wanandoa mapenzi na huruma na Akayafanya hayo kuwa ni dalili na ishara kwa watu wenye kufikiri, Kisha swala na salamu kwa mbora wa viumbe na mpendwa wa kweli Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mbora wa waume, baba bora na aali na sahaba zake wote.

 

Baada ya hayo:

Famiilia ni tofali la jamii, likitengemaa na jamii hutengamaa kwake kutatimia, familia inaweza kukumbwa na matatizo yatakayotikisa nguzo zake, kuharibu mustakabali wake na kuzuia hilo kabla ya kutuka kwake ni bora kuliko kutibu, ndio maana tukaja na kijitabu hiki kwa mwanamke aliyeolewa kwani yeye ndiye mwenye athari kubwa katika kuitengeneza au kuiharibu familia, hadi pale atakapoweka mguu wake na kusimama katika njia ya furaha ya kweli ili aweze kujibu swali ambalo mara nyingi linapita katika akili za wanawake wengi walioolewa; ‘Je, Ni vipi utauteka moyo wa mume wako na kumridhisha Mola wako?

 

Tunamuomba Allaah Mkarimu Anufaishe kwa kitabu hiki kila msomaji, na Atuonyeshe haki na Atuongoze kwenye haki hiyo, atusamehe makosa yetu na kwa hakika yeye ni muweza wa hilo.

 

Tunamuomba Allaah kwa majina Yake matukufu Atusamehe madhambi yetu na makosa yetu, na Atujaalie sisi kuwa funguo za kheri na kufuli za shari na Aturuzuku ukweli wa maneno na matendo.

 

“…Mola wangu Mlezi! Niwezeshe nishukuru neema Zako ulizonineemesha mimi na wazazi wangu, na nitende mema unayo yapenda. Na unitengenezee dhuriya zangu. Hakika mimi nimetubu kwako, na mimi ni miongoni mwa Waislamu.” (46:15)

 

 

‘Aadil Fat-hi ‘Abdullaah

 

Share

002-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Mwanzo Mzuri Wa Maisha Ya Ndoa

 

MWANZO MZURI WA MAISHA YA NDOA

 

Kwa hakika mwanzo mzuri uko katika uchaguzi mzuri, atakayefanya uchaguzi mzuri atakuwa ameweka mguu wake katika njia ya uokozi na furaha.

Uislamu ni dini ya maumbile, umemuongoza mwanamke wa Kiislamu katika misingi sahihi ya kuchagua mume, mwanamke ambae akiongoka kwa uongofu wake basi maisha yao ya ndoa yatakuwa mepesi yenye baraka, na hivyo kuwa na familia njema yenye mapenzi, huruma na mambo mazuri.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, “Atakapokujieni mnayeridhika na dini yake na akhlaqi yake basi muozeni, na kama hamkufanya hivyo itakuwa ni fitna kwenye ardhi na ufisadi mkubwa”[1]

 

Hizi ni sifa za Mume mwema, dini na tabia njema.

 

Angalia ewe dada wa Kiislamu yule anayekuja kukuposa, akiwa mtu mwenyewe amelazimiana na sifa nzuri za Kiislamu na mwenye kuhifadhi Swalah zake, yupo mbali na mambo machafu na watu wenye tabia mbaya na kufuata hawaa, mwenye kusuhubiana na waja wema wa Allaah, hupata chumo la halali basi usimuache mtu huyo.

 

Al-Hasan Al-Baswry amemuusia mtu mmoja kwa kumwambia,

“Muozeshe Binti yako mtu mwenye Dini, Kwani mtu mwenye dini akimpenda binti yako atamkirimu, na akimchukia hatomdhulumu”

 

Baadhi ya watu wanaangalia ndoa kana kwamba ni mkataba wa kibiashara, mshindi na mwenye kupata faida ni yule anayepata kiasi kikubwa cha mali, bila ya kujali matokeo yake mabaya yenye kuangamiza familia, hawajali tabia wala dini ya mume, lakini wanachojali zaidi ni kiasi gani cha mali au fedha alichonacho. Ewe dada wa Kiislamu huu usiwe mtazamo wako kwa mume, ukaonja machungu na hasara kupita kiasi. Angalia tabia yake, maadili aliyokuwa nayo na yasikuhadae mandhari yake ya kupendeza.

 

Mwangalie Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye ni kigezo chetu anapopita mtu mbele ya watu alikuwa akiuliza, “Mnamuonaje mtu huyu, Husema: huyu kwa hakika akiposa ataozeshwa, na akiombewa atakubaliwa, na akisema atasikilizwa, kisha akanyamaza, akapita mtu katika mafukara Waislamu akasema, ‘Mnasemaje katika haya kuhusu huyu? Wakasema, kwa Hakika huyu akiposa haozeshwi, na akiombewa hakubaliwi na akisema hasikilizwi, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, ‘Huyu ni bora ujazo wa ardhi kuliko yule’[2]     

 

Hii haina maana kuwa mimi nakulingania ewe dada yangu Muislamu katika kuchagua mume fukara, lakini kumbuka kuwa fukara mwema ni bora kuliko tajiri muovu. Kama ambavyo mwanamume ana haki ya kuangalia dini ya mwanamke. Ni vyema kwa walii wa mwanamke aangalie dini ya kijana anayekuja kuposa hali yake na tabia zake na pindi atakapomuozesha binti yake mwanamume fasiki, au mwenye bid’ah, basi mtu huyu atakuwa amemkosea binti na yeye mwenyewe.[3]

 

Salafus Swaalih (watangulizi wema) walitupigia mifano mizuri sana katika uchaguzi wa mume mwema, huyu hapa Sa’iyd bin Al-Muswayyib ambaye ni Tabii maarufu, alikuwa ni mwanachuoni mwenye zuhdi, anakataa kumuoza binti yake (ambae watu wanajua uzuri na usomi wake) kwa Waliyd bin ‘Abdil-Malik (mtoto wa Khalifa wa Waislamu wakati ule) na akaamua kumuoza kijana wake kwa mwanafunzi wake ambae akiitwa Abu Wadaa’a kwa Dirham mbili au tatu tu.

 

 

 

[1] Hadiyth hii imepokewa na At-Tirmidhiy na wengineo na ameifanyia Tahsiyn Al-Al-Baaniy

[2] Al-Bukhaariy

[3] Minhaaj al-Qaswidiyn

Share

003-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Upendo Unamaanisha Nini Katika Maisha Ya Ndoa

 

UPENDO NI FUNGUO ZA NYOYO

 

UPENDO UNAMAANISHA NINI KATIKA MAISHA YA NDOA?!!

 

Kwa hakika maisha haya ni:

1- Ikhlaas

2- Upaji

3- Kumpendelea mwenzako

 

Kwa hakika ni kutanguliza haki ya mume kuliko haki yako, ni kujiteremsha ni kujishusha na kiburi chako katikati ya mivutano ili upendo na kufahamiana yachukue nafasi ya ugomvi na mijadala (msuguano).

 

Swahaba Mtukufu Abu Dardaa (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimwambia mke wake maneno yafuatayo:

 

Samehe, utadumisha mapenzi yangu,

                              Wala usizungumze kwa kunibishia ninapo ghadhibika.

 

Wala usinigonge kama mgongo wa dufu hata mara moja,

                                                     Kwani wewe hujui vipi itakavyokuwa.

 

Wala usizidishe malalamiko yakapotea kwa nguvu,

                           Na moyo wangu ukaanza kukukataa na nyoyo hugeuka.

 

Mimi nimeona upendo na maudhi,

                                       Vinapokutana basi mapenzi hayakai huondoka.

 

 

Fahamu ewe dada Muumini kuwa mume wako hatokupenda hadi ahisi kuwa nawe unampenda, mapenzi ni hisia za pande mbili na kubadilishana, siku zote mtu huelekea katika kumpenda mtu kwa kadiri mtu yule atakapoonesha anampenda na kumjali. Maamkizi yenye uchangamfu, kubadilishana zawadi, kuitana kwa majina mazuri na kutabasamu, yote haya hufungua kwa mke upeo mpana wa mapenzi ya kweli na furaha isiyo na kifani na hivyo kumfanya mume kuwa ni kipenzi kizuri zaidi kwa mke wake, kama ilivyo kwa mume kwa mke wake anatakiwa awe ndie kipenzi chake zaidi.

 

Kuna wakati Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa na mtu mmoja anampenda nani zaidi? Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akajibu, kuwa ni Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha).

 

‘Amruu bin Al-‘Aasw amesema,

“Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam.) alinituma na Jeshi tukiwa pamoja na Abu Bakr na ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) niliporejea nilisema, “Ewe Mtume wa Allaah ni mtu gani unayempenda zaidi”?![1]

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akajibu kwa kusema ni, ‘Aaishah, Nikasema: Nakusudia unayempenda kwa wanaume, akajibu, kuwa anampenda Baba yake ‘Aaishah[2]

 

Mapenzi ni mahusiano mazuri, furaha, mahaba, huruma, usamehevu na maghfira, na sio mapenzi kama wanavyosawirisha watu katika baadhi ya visa, wakatengeneza maigizo na kuchora picha (akilini mwao) za kijana kana kwamba ni Nabii katika Manabii au Malaika waliokurubishwa kwa Mwenyezi Mungu kiasi cha kuwa mke atakapoona kwa mumewe kitu kinachomchukiza basi hudhani kuwa maisha ya ndoa yameshindikana na ndoto aliyokuwa nayo imeondoka.

 

Sivyo hivyo kabisa Ewe mke, kwani mifano hiyo haipatikani kabisa katika maisha.

 

Maisha haya ya duniani ni maisha halisi si ya kufikirika au kusadikika, bali ni maisha ambayo kila mtu ana aibu zake, inamtosha mtu kujifakharisha kwa kuhesabika aibu zake.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, “Hambughudhi Muumini mwanamme kumbughudhi Muumini mwanamke kwa tabia yake, kwani akichukizwa na tabia moja ataridhishwa na tabia nyingine”[3]

 

Kadhalika nawe mke utakaposikitishwa na tabia mojawapo ya mume wako basi utaridhika na tabia zake zingine, kumbuka maneno ya Al-Hakiym aliposema,

“Mke anasemaje kuhusu mumewe ambae ameacha wanawake wote na akamchagua yeye tu? Na mwanamke anamfanyia nini mume wake aliyewaacha wazazi wake, marafiki na jamaa zake na hakuridhia kumpata mwenye kumliwaza mwengine zaidi yake”

 

Wewe ndie liwazo la mume wako, mwenza wa mpenzi wako, uzuri ulioje wa ibara ya Qur-aan inayosema,

“…Wao ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao…. (2:187)

 

Katika Aayah nyingine kadhalika,

Na katika Ishara Zake ni kuwa Amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye Amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaofikiri. (30:21)

 



[1]‘Amruu bin Al-‘Aasw wakati huo alikuwa bado mgeni katika Uislam, na akadhani maadamu amepewa uongozi wa jeshi basi yeye ni bora kuliko Abu Bakr na ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) siku moja ‘Amruu alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni mtu anayempenda, Mtume Akamjibu kuwa ni Abu Bakr, ‘Umar, ‘Aliy na ‘Uthmaan. ‘Amruu akatamani asingeuliza swali lile.

[2] Al-Bukhaariy na Muslim

[3] Imepokewa na Muslim

Share

004-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Miongoni Mwa Mapenzi, Ni Wewe Kufurahi Kwa Furaha Yake Na Kuhuzunika Kwa Huzuni Yake

 

MIONGONI MWA MAPENZI NI WEWE KUFURAHI KWA FURAHA YAKE NA KUHUZUNIKA KWA HUZUNI YAKE

 

Kwa hakika jambo kubwa alichukialo mwanamme ni kumuona mke wake akifurahi wakati yeye yupo katika huzuni, au wakati yeye akiwa katika huzuni basi mke wake anakuwa katika furaha. Mambo kama haya yanakuwa ndio sababu ya mume kumchukia na kumtenga mke wake, huenda jambo kama hili likapelekea katika mambo makubwa zaidi hakuna ajuaye isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). 

 

Mwenyezi Mungu Amrehemu mwanamke ambaye kwa kumuangalia tu mume wake na kujua hali yake aliyokuwa nayo basi hujaribu kuwa katika hali yake na akawa ni msaada wake, na jambo hilo la mumewe likawa kubwa katika nafsi yake ikiwa mume wake yupo katika hali ya furaha basi naye atatabasamu mbele ya mumewe na ikiwa ni kinyume chake basi naye huwa kama vile na kujaribu kupunguza kwa kumliwaza mumewe, kumuondolea matatizo, kumpa utulivu wa moyo wake. Hali hii inafanana na ile hali aliyokuwa nayo Mama wa Waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pindi alipojiwa na mume wake; Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na habari ya Wahyi akiwa anatetemeka na kusema,

“Nifunike nifunike kisha akasema, Khadiyjah nina nini? Kisha akamuelezea habari za kule, kisha akasema, ‘Nilikuwa najihofia’. Mama wa Waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) akasema, sivyo kabisa, hiyo ni bishara njema. Mwenyezi Mungu kamwe Hatokutupa, kwa hakika wewe unaunga udugu waliokukata, unasema maneno ya kweli, hauongopi hata mara moja, na unawakirimu wageni, na kumsaidia mtu kupata haki yake.”[1]

 

Je, Umeona ewe mke Muumini, majibu bora kuliko majibu haya? Kwa hakika Mama wa Waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) amestahiki pepo kwa kumliwaza kwake Mtume wa Mwenyezi Mungu na kumpunguzia matatizo yaliyokuwa yakimkabili. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema,

“Niliamrishwa kumpa bishara Khadiyjah kuwa atapata pepo ambayo nyumba yake na nguzo zake ni za lulu ziliyo wazi ndani yake, hamna kelele humo wala usumbufu”[2] 

 

Kwa tendo lile na matendo mengine ya Mama wa Waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ilibidi Mtume ahifadhi wema wa Mama wa Waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) kwa Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) yake yote.

Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) anasema,

“Sikuwahi kumuonea wivu mwanamke yeyote kama nilivyokuwa namuonea wivu Khadiyjah kutokana na kutajwa sana kwa wema na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), siku moja nilimtaja kwa kusema, ‘Una nini kwa mwanamke yule mkongwe mtu mzima’? Si ya kuwa Mwenyezi Mungu Amekuruzuku kilichokuwa cha kheri zaidi?!” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, “WAllaahi hakunibadilishia aliyekuwa mbora kuliko yeye, kwa hakika yeye ndiye aliyeniamini waliponikana watu, aliyenisadiki na kunikubali waliponikadhibisha, akaniliwaza kwa mali yake watu waliponinyima. Na kwa Khadiyjah Allaah Akaniruzuku watoto kinyume cha wanawake wengine.”[3]

 



[1] Al-Bukhaariyna Muslim

[2] Al-Bukhaariyna Muslim

[3] Al-Bukhaariy amepokea Hadiyth hii kwa ufupi na kadhalika wamepokea Hadiyth hii Ahmad na At-Twabaraaniy

Share

005-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Mapokezi Mazuri Huingiza Furaha Moyoni

 

MAPOKEZI MAZURI HUINGIZA FURAHA MOYONI

 

Wakati mume anaporudi nyumbani na kumkuta mumewe amejiandaa na watoto humkabili kwa nyuso za bashasha, jambo hilo humuingizia furaha moyoni mwake. Katika Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tunasoma ya kuwa,

“Atakayekutana na nduguye Muislamu kwa alipendalo ili amfurahishe kwa hilo basi Mwenyezi Mungu Atamfurahisha siku ya Qiyaamah”[1]

 

Ummu Sulaym, mke wa Abu Twalhah pindi alipofiwa na mwanawe aliwaambia watu wa nyumbani kwake,

‘Msimwambie Abu Twalhah hadi mimi mwenyewe nitakapomweleza’ Abu Twalhah aliporejea kutoka katika safari zake akamkuta mkewe katika hali nzuri na sura iliyochangamka. Abu Twalhah akakaribishwa vizuri na kisha wakazungumza wakiwa faragha kiasi cha mume kumaliza haja yake kwa mke wake. Baada ya hapo ndipo alipomweleza habari ya kifo cha mwanawe. Abu Twalhah alikasirika kwa jambo hili (kufichwa habari kwa muda kisha kuelezwa baadaye) kwa hiyo akaenda kushitakia kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Baada ya Mtume kusikia mashitaka yale aliunga mkono kitendo cha mke wa Abu Twalhah na kumwambia, “Mwenyezi Mungu Awabariki kwa usiku wenu ule.”[2]

Alisema kweli Mtume wa Allah na wakabarikiwa kupitia usiku wao ule, watoto kumi na wote wakawa wasomaji wazuri wa Qur-aan.

 

Ewe mke wa Kiislamu! Usiwe kama ambaye humpokea mumewe wakati wa kurudi nyumbani kwa uso uliojawa na huzuni kwa sababu amechelewa kurudi nyumbani, au kwa mapokezi yanayoanza kwa salamu za mashitaka kwa hali yake ya siku ile au ya watoto na matatizo yao. Kwa hakika yote haya yanarudi kwa watoto na huathirika kwa tabia hizi na yanayotokea baina ya wazazi wao hali inayowafanya kuathiri afya zao za nafsi kwa siku za mbele.

 



[1] Imepokewa na At-Twabaraaniy

[2] Al-Bukhaariy Na Muslim

Share

006-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Lawama Nyingi Hukausha Nyoyo

 

LAWAMA NYINGI HUKAUSHA NYOYO

 

Lawama zako zisiwe katika dogo na kubwa, jifunze namna bora ya kusamehe na kukubali mambo mengine bila ya kushindana, kwa hakika maisha ya ndoa huhitajia sana wanandoa kusameheana kuliko jambo lolote lingine.

 

‘Abdullaah bin Ja’afar bin Abi Twaalib alimuusia mwanawe wa kike alipokuwa anaolewa kwa kumwambia,

“Jihadhari na wivu kwani ni ufunguo wa talaka, na jihadhari na lawama nyingi kwani hurithisha maudhi, jilazimishe na kupaka wanja kwa kuwa ni bora na jambo lililo bora zaidi ya manukato ni maji”

 

Kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) naye kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema,

“Je, niwaambieni kuhusu wake zenu peponi? Tukajibu: Ndio ewe Mtume wa Allaah, akasema, Ni wenye upendo na wenye kizazi, atakapoghadhibika au kukosewa, au atakapokasirika mume wake, atasema, “Mkono wangu huu uko juu ya mkono wako, sipaki wanja ukiwa na hasira na macho yangu hayatoona usingizi hadi uridhike”[1]

 

Acha kiburi ewe mke Muumini, na uende kwa mumeo atakapoghadhibika na umridhishe kwani atakupa hadhi na atanyanyua shani yako katika moyo wake na lililo muhimu sana katika yote ni kuwa baada ya hayo utakuwa umepata radhi za Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) kwani radhi za mume ni katika radhi za Allaah (Subhaanahu wa Taala), katika Hadiyth tunasoma, “Mwanamke atakayekufa na mumewe akiwa radhi nae ataingia peponi”

 

Katika Wasia wa Asmaa bint Khaarijah Kwa Mwanae Wakati wa Ndoa Yake:

“Kuwa kwake mume wako ni ardhi, naye atakuwa kwako mbingu, na uwe kwake tandiko atakuwa kwako nguzo, wala using’ang’anie kitu akakuchukia na usiwe mbali nae akakusahau, na akikusogelea msogelee zaidi”

 



[1] At-Twabaraaniy

Share

007-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Je, Tumbo Ni Njia Ya Kuelekea Kwenye Nyoyo

 

JE, TUMBO NI NJIA YA KUELEKEA KWENYE NYOYO?

 

Bila shaka kuwa njaa huzusha mapungufu katika mwili wa mwanaadamu na huathiri hata namna ya kufikiri kwake, huenda akapata dhiki au wakati mwengine furaha, katika hali kama hizo nafsi ikipata inachokitamani na kukipenda miongoni mwa aina za vyakula hufurahi na kwa hiyo humpenda aliyekitengeneza chakula kile.

 

Katika wasia wa Umaamah binti Al-Haarith kwa mwanawe wakati wa ndoa yake:

“Angalia kwa makini wakati wa kula na kulala kwake: kwa hakika njaa nyingi huchoma na kukosesha usingizi na hutia ghadhabu”

 

Kwa hakika mwanamke mwenye kujali wakati wa chakula cha mumewe na akajitahidi kuandaa chakula kizuri zaidi kwa kadiri ya uwezo wake ndie mtu wa karibu zaidi kuupata moyo wa mume wake na heshima yake. Sikusudii wala sipendelei kusema kuwa mwanamke apoteze masaa mengi katika kuandaa chakula, bali apike kile anachokipenda mume wake bila ya kuharibu majukumu yake mengine. 

 

Pindi anaporudi mumewe kutoka kazini na wakati huo huo njaa inamuunguza anakuta chakula kilishaandaliwa na nyumba ni safi na mkewe anamsubiri ili ashirikiane naye chakula, kwa hakika katika hali kama hii ni juu ya Mwenyezi Mungu kuwabarikiri katika mazingira haya mazuri ya kiimani na hii ndio familia iliyobarikiwa.

 

 

Share

008-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Kumtii Mume Huchuma Moyo Wa Mume Na Huondoa Ghadhabu Ya Allaah

 

KUMTII MUME HUCHUMA MOYO WA MUME NA HUONDOA GHADHABU YA ALLAAH (SUBHAANAHU WA TA’ALA)

 

Mwanamke mmoja alikwenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema,

“Mimi ni mwanamke niliyekuja kwako, Jihaad ni faradhi waliyoandikiwa wanaume, wakijeruhiwa hupata thawabu na wakifa huwa hai kwa Mola wao wakiruzukiwa. Ama sisi wanawake ndio wasaidizi wao, je, hatuna ujira kama wanavyopata? Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, “Waambie wanawake wenzako utakaokutana nao kuwa utiifu kwa mume na kujua haki zake ni sawa sawa na Jihaad, ni wachache miongoni mwenu mfanyayo hayo”[1]

 

Kwa hakika kumti mume hulingana na Jihaad katika njia ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), ujira wa anayemtii mume wake na akajua haki zake ni kama ujira wa mwenye kupigana (Mujaahid) katika njia ya Allaah, lakini wanawake wengi hawajui, na utii wa mume humpelekea mkewe peponi. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema, “Pindi mwanamke atakaposwali Swalah zake tano (za faradhi), na akafunga (mwezi wake wa Ramadhaani) na akahifadhi tupu yake, na akamtii mume wake ataingia peponi”[2]

 

Mwanamke mmoja alifika kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mtume akamuuliza,

“Je una mume? Mwanamke yule akajibu, Ndio ninaye, uko vipi naye? Mwanamke akajibu, “Ninamhudumia kadiri ya uwezo wangu ila lile ambalo sina uwezo nalo, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia, “vipi wewe kwake? Mume wako ndio pepo yako na moto wako”[3]

 

Fahamu ewe dada wa Kiislamu kuwa mume wako ndiye pepo na moto wako, kwa mume wako ndio utaingia peponi pindi unapomtii, na kwake ndio utaingia motoni (Mwenyezi Mungu Atukinge na hayo) pindi utakapomuasi.

 

Mtume aliulizwa ni mwanamke gani bora? Mtume akasema,

“Ni yule ambaye akimuangalia anapendeza, na atakapotii pindi atakapoamrishwa, wala asikhalifiane naye katika nafsi yake na mali yake, kwa lile litakalomchukiza”[4]

 

Tukiangalia matatizo mengi yanayokabili familia nyingi utaona kuwa matatizo mengi yanatokana na sababu ya mke kumuasi mume wake, kutokuwa na utii kwa mumewe na kumkhalifu kwa lile lenye kuchukiza, haya yote yanatokana na sababu ya ujinga wa mwanamke na kujua haki za mumewe juu yake au inawezekana kutokana na kiburi alichonacho, wasiwasi wa Shaytwaan na kushawishiwa vibaya ili awafarikishe baina ya mume na mkewe. Yapasa mwanamke kufahamu ya kuwa haki ya mumewe kwake na fadhila zake juu yake ni kubwa mno, kwa dalili ya Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam),

“Lau ingefaa kwa mwanaadamu kumsujudia mwanaadamu mwenzake basi ningeliamrisha kwa mwanamke kumsujudia mumewe kwa ukubwa wa haki yake kwake”[5]

 



[1] Hadiyth hii imepokewa na Al-Bazaar na At-Twabaraniy

[2] Imepokewa na Ahmad na wengineo.

[3] Ahmad na wengineo

[4] Ahmad na wengineo.

[5] Ahmad, An-Nasaaiy na Ibn Maajah

Share

009-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Asiyemshukuru Mume Wake, Hamshukuru Mola Wake

 

ASIYEMSHUKURU MUME WAKE, HAMSHUKURU MOLA WAKE

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema,

“Mwenyezi Mungu Hamuangalii mwanamke ambaye hamshukuru mume wake na wakati huo huo hawezi kufanya lolote bila ya mumewe”[1]

 

Ewe mke mkarimu wa Kiislamu, kwa hakika mume wako anapigana na maisha magumu na kupambana ili kupata tonge la maisha na baada ya hapo anabeba mzigo wa familia, hivyo mdhanie vizuri daima, mshukuru yeye na Mola wako daima, wala usikikosoe kile akiletacho kwa ajili yako na ya familia, usikidharau na kukishusha thamani yake na kutokuridhika kuishi pamoja nae.

 

Tunamuona Mtume wa Mwenyezi Mungu Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) alipokwenda kumtembelea mwanae Ismaa’iyl (‘Alayhis Salaam) na hakumkuta baada ya kufika kwake na kumkuta mke wake, akamuuliza kuhusu hali zao na mke akajibu kuwa wapo katika dhiki, Ibraahiym akajua kuwa mke wa mwanawe hayuko radhi na maisha wanayoishi na mwanawe, hivyo akaamua kumuachia salamu mwanae kwa kumwambia mke wa mwanae, “Akija Ismaa’iyl mpe salamu zangu, na umwambie abadilishe kizingiti cha mlango wake.” Pindi alipokuja Ismaa’iyl, mke wake akamueleza yaliyojiri na kumpa salamu zake ya kuwa amekuja mzee akamuulizia hali yake, na akampa salamu zake na kumtaka Ismaa’iyl abadilishe kizingiti cha mlango, Ismaa’iyl akamwambia mke wake, “Yule ni baba yangu na wewe ni kizingiti cha mlango, nenda kwa jamaa zako”[2]



[1] Ameipokea Al-Haakim na akaisahihisha

[2] Tumeelezea mapokezi yake hapo nyuma

Share

010-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Hamu Yako Kubwa Iwe Kujifanyia Islahi Na Kuendesha Nyumba Yako

 

Hamu Yako Kubwa Iwe Kujifanyia Islahi Na Kuendesha Nyumba Yako

 

 

 

Nafsi ya mwanadamu inapenda uzuri na inapenda kuonesha uzuri kwa anayempenda, tunasoma katika Hadiyth: “Ni yule ambae ukimuangalia atakupendeza.”

 

Kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) vile vile amesema:  “Kwa hakika Allaah Ni Mzuri Anapenda vitu vizuri.”[1]

 

‘Aliy bin Abi Twaalib amesema: “Mbora wa wanawake wenu ni mzuri wa harufu, mwenye kupika chakula kizuri kitamu na akitoa hutoa kwa wastani na akizuia huzuia kwa wastani”

 

Moja katika usia wa Umaamah bint Al-Haarith kwa mwanae Ummu Iyaas bint ‘Awf wakati wa ndoa yake: “Jicho lake lisiangukie kwenye eneo lako lenye kuchukiza, na wala asinuse kwako isipokuwa harufu nzuri.”

 

Kwa hakika usafi binafsi wa mwanamke ni jambo muhimu sana: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza mwanamme kurudi safarini usiku kisha kumgongea mke wake mlango usiku, ili aweze kujitayarisha kwa kuchana nywele na kunyoa vinywele vya mwili.[2]  

 

Katika Hadiyth nyingine tunajifunza: “Usafi unalingania kwenye imani”[3]  

 

Hapa tutaonesha kwa ufupi baadhi ya mambo makhsusi ya mapambo ya mwanamke.[4]

 

1-Kuunga nywele: kuunga nywele za mwanamke kwa nywele nyinginezo ni haramu kwa maafikiano ya Wanachuoni[5] na katika kuziunga na kitu kingine, wanachuoni wametofautiana.

 

2-Kupunguza Nywele: inaruhusiwa kwa kutopungua chini ya masikio mawili, ama chini ya hapo kuna tofauti ya wanachuoni katika hilo.[6]

 

3-Kuondosha Nywele za Uso: Kuna tofauti ya maamuzi ya uhalali na uharamu wake lakini kilichokubaliwa zaidi ni kuwa inafaa, kama haitokuwa tatizo kwa mume (kwa maana akiruhusiwa na mume wake zaidi ikiwa mwanamke huyo kazoea kunyoa mara kwa mara hapo kabla, ikiwa hali haipo dhahiri hivyo yaani mume hakereki na mke kuwa na nywele nyingi basi ni bora aache nywele na asinyoe.[7] WaAllaahu A’alam.

 

4-Kuondosha nyusi: (Ingawa) baadhi ya watu wa madhehebu ya Hanbali na ya Shaafi’iy wanaona kuwa ni sawa kufanya hivyo ikiwa idhini ya mume wake imepatikana na wengineo wanasema kuwa ni haramu kwani imeingia katika jumla ya maana ya An-Nams [8]kwa kuwepo ila nyinginezo sio illa ile ya Taghriyr inayoharamisha kuondosha kwake nyusi. (Pamoja na wanaoona hivyo, ila lililo sahihi kutokana na Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) iliyo wazi ni kuwa jambo hilo ni Haraam; liwe kwa idhini ya mume au bila idhini ya mume)[9]

 

5-Kuondosha Nywele zingine katika mwili.[10]  

 

Kwa ujumla inaruhusiwa bila ya kuwepo mambo yenye kuchukiza. Hivyo inajuzu kwa mwanamke kuondosha nywele zake mwilini mwake kwa njia anayoiona kuwa ni sawa.[11] 

 

Kinachokamilisha pambo la mwanamke na uzuri wake ni uzuri wa nyumba yake, usafi wa makazi yake na kumhudumia mume wake, anaweza kuiga mfano wa Asmaa bint Abi Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhaa) aliposema: “Az-Zubayr alinioa wakati ambapo hakuwa na mali mbali na farasi wake mmoja na ngamia wake anayemnywesha maji, nilikuwa na tabia ya kumlisha farasi wake na kumuongoza na ninamsagia ngamia wake, na ninashona kiriba chake cha maji, ninakanda unga, na nilikuwa nikichukua mbegu kichwani mwangu kwa masafa ya theluthi ya maili (farsakh) nilipumzika na hayo yote pindi baba yangu Abu Bakr aliponitumia mfanyakazi aliyenitosheleza na kumuongoza farasi nikaona kuwa nimekombolewa.”[12]

 

Huu ni mfano wa mwanamke mkweli aliyekuwa akimhudumia mume wake kiasi cha kumuongoza farasi wake na kumsimamia nalo ni jambo lisilowezekana ila kwa wanaume na wanawake majasiri kama Asmaa hadi alipokirimiwa na Allaah kwa kupewa mfanyakazi ili aweze kufanya kazi zingine za kumhudumia mume wake na kusimamia nyumba yake.

 

 

[1]  Imepokelewa na Muslim

 

[2] Al-Bukhaariy na Muslim

 

[3] Imepokewa na At-Twabaraaniy

 

[4] Fungu hili limetoka katika kitabu, ‘Min Qadhwaaaya Az-Ziwaaj’ cha Jaasim bin Muhalhal Al-Yaasin]

 

[5] Angalia Fat-hul Baariy, Juzuu ya 1

 

[6] Swahiyh Muslim, sharh ya An-Nawawi, Juzuu ya 4

 

[7] Naylul Awtwaar cha Ash-Shawkaaniy, Juzuu ya 6

 

[8] Ishara ya Hadiyth   ‘Abdullaah Bin Mas’wud ambaye amesema: “Allaah Amewalaani wenye kuchanja na wenye kuchanjwa, na wenye kunyoa nyusi, na wenye kuchonga meno kwa urembo, na wenye kubadilisha umbile la Allaah” [Imepokewa na Al-Bukhaariy]

 

[9] Maneno ya kwenye mabano ni ya Mpitiaji.

 

[10] Ni juu ya mwanamke mwenyewe kunyoa nywele zake za mwilini na asiifanye kazi hiyo mtu mwengine zaidi yake kwa dalili ya Hadiyth ya Mtume inayosema, “Mwanamme haangalii uchi wa mwanamme mwenzake, na mwanamke haangalii uchi wa mwanamke mwenzake” imepokewa na Muslim na Ahmad

 

[11] Kutoka katika kitabu, ‘Qadhwaaya Az-Ziwaaj’ cha Jaasim bin Muhalhal Al-Yaasin

 

[12] Al-Bukhaariy na Muslim.

 

Share

011-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Mkutano Wenye Mafanikio Ndio Dawa Yenye Kuokoa

 

MKUTANO WENYE MAFANIKIO NDIO DAWA YENYE KUOKOA

 

Katika jambo muhimu sana katika mahusiano ya ndoa na yenye nafasi kubwa kayafanya yawepo na kudumu ni makutano ya kijinsi kati ya wanandoa wawili. Kwa hakika hii ndio dawa ya matatizo yanayozikuta maisha ya ndoa, matatizo mengi katika jumla ya matatizo ya ndoa ni kufeli katika mkutano huu wa ndoa au kuchelewa kwake kutokana na upande mmoja kutohisi chochote.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuhimiza kutumia dawa hiii, kujamiiana na kuingiliana. Mwenyezi Mungu Amelifanya jambo hili lipendwe na watu na Anawalipa watu thawabu kwa kulifanya na ni sadaka na ujira wa ayafanyaye (kwa wanandoa)’[1]. Hapa ndipo panapopatikana ukamilifu wa ladha na kumfanyia hisani mpenzi wako na kulipwa ujira kwa ajili ya hilo, thawabu na sadaka na furaha ya nafsi naye kuweza kuondokana na fikra potofu, hii ni ladha isiyolingana na ladha nyingine yoyote na haswa inapopatikana ukamilifu wake, kila sehemu katika mwili inapopata sehemu ya ladha, basi ndipo ukamilifu wa shughuli hiyo inapofikiwa. Macho yanapomwangalia mke, masikio katika kusikia maneno yake, pua kunusa harufu nzuri na mdomo kubusu na mkono kushika, kila kiungo kinashiriki katika kupata ladha katika ladha kuu inayopata kiwiliwili chake na hii ndio sababu ya mwanamke kuitwa sakan yaani utulivu yaani inatuliza nafsi,

 

“Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu (sakan) kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri. ” (30:21)[2]

 

“Kwa hakika maingiliano baina  ya mume na mazungumzo ya faragha baina yao yakifanyika kwa njia sahihi na nzuri humuongezea mwanamme na mwanamke ukaribu wa kimapenzi na huruma ya kiroho baina yao, huwasaidia na hupumzisha miili yao na huwasahaulisha humumi na matatizo ya kidunia hata ikiwa jambo lenyewe ni la muda mfupi tu. Kadhalika huwapa usingizi mzuri, utulivu, ambao hupatikana kupitia maingiliano haya. Wewe kama mwanandoa una mchango wako katika kufanikisha ukamilishaji na kufikia upeo wa juu katika mafanikio haya, muwafaka wa pamoja kati ya mume na mke ni muhimu katika maingiliano haya muhimu, ni juu yako kama mke kujitahidi kwa kadiri ya hali ya juu kufanikisha jambo hili muhimu, ambalo hupatikana kwa njia ya kuwa wawazi na ushirikiano wa pamoja na mume wako”[3]

 

Uislamu umempa nafasi mwanamme haki ya kuomba unyumba kwa mke wake na ukamhimiza mwanamke kukubali kwa haraka maombi ya mume wake na ukamhadharisha na adhabu mbaya kwa mwenye kukhalifu.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema,

“Mwanamme atakapomtaka mkewe kwa haja yake basi na ampatie na kumfuata hata akiwa jikoni au kwenye tanuri la mkate”[4]

 

Katika Hadiyth nyingine amesema,

“Naapa kwa yule ambaye Nafsi yangu iko mikononi mwake, hakuna mwanamme yeyote atakayemuita mke wake katika kitanda chake na mwanamke yule akakataa, na mwanamme akalala huku akiwa amekasirika basi Malaika watamlaani mwanamke yule hadi kupambazuke”[5]

 

Kadhalika Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemkataza mwanamke kufunga Swawm ya Sunnah bila idhini ya mume wake kwa Hadiyth yake,

“Haiwi Halali kwa mwanamke kufunga sunna na mumewe yupo, isipokuwa kwa idhini yake, wala hatoki nyumbani kwake isipokuwa kwa idhini ya mume wake”[6]

 

Ni vizuri kwa mwanamke kujua kuwa haja ya mume ya kujamiiana nae inaweza kupita haja yake mwanamke kwa mumewe, kwa kuwa vishawishi kwa mwanamme ni vingi sana, mara nyingi fitna hutokea anaponyimwa mume unyumba, bila ya kuwepo kwa udhuru wa kishari’ah na hivyo kusababisha ghadhabu ya Mwenyezi Mungu kwake.

 

Mume asiwe ni mfujaji wa tendo la ndoa bali jambo zuri ambalo dini hii imelingania ni hali ya wastani kwa kila jambo. Kujichosha sana na kuzidisha sana katika kujamiiana ni jambo ambalo halimsaidii mume katika kuwa na siha nzuri. Wanandoa wafahamu ya kuwa jambo ambalo linafanikisha mkutano huu kukua ni kuwepo kwa hamu ya jambo hilo kwa wote wawili, na utangulizi mzuri unatakiwa utoke kwa mume kabla ya jambo lenyewe kuanza, kadhalika kuwekeana wazi na kila mmoja ajue jinsi ya kumuweka sawa mwenzake hadi wafikie kilele cha jambo lenyewe. Katika maingiliano haya ya faragha kati ya mume na mke wasisahau Niyah, na Niyah yenyewe ni, kuwa kila mmoja kumfurahisha mwenzake na kutekeleza haki zake kwake, na yote hayo huwa ni ujira wa sadaka aliyoitaja Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth yake tuliyoitaja hapo nyuma.

 

 





[1] Hii inaashiria ile Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inayosema, “…na mtu kumuingilia mke wake kuna sadaka. Maswahaba wakamuuliza, iweje ewe Mtume wa Allaah, ‘Mtu anastarehe na haja zake na anapata thawabu kwa hilo?’ Mtume akawajibu, ‘Je mnaonaje kama mtu Yule angelifanya kwa haramu je kungekuwa na ubaya?’ Maswahaba wakajibu, ‘Ndio.’ Mtume akasema, ‘vivyo hivyo atakapoweka katika halali atakuwa na ujira’” (Muslim na wengineo)

[2] Angalia kitabu, ‘Rawdhatul Muhibiyn’ cha Ibn Al-Qayyim

[3]Imechukuliwa kutoka katika kitabu, ‘Tuhfatul ‘Aruus’ cha Al-Istanbuliy

[4] Imepokewa na Ahmad

[5] Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim

[6] Al-Bukhaariy na Muslim

Share

012-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Kutoa Siri Ni Khiyana Ya Amana

 

KUTOA SIRI NI KHIYANA YA AMANA

 

Bila ya shaka kuwa mwanamke Muumini ndiye mtu wa karibu sana kwa mume wake, mwanamke huyu, anakuwa ndiye mwanamke aliyefanikiwa katika uhusiano wake wa mapenzi na mume wake. Mtu akiwa na siri kubwa ndani ya moyo wake, pindi anapoibeba siri ile peke yake huhisi kuwa kabeba kitu kizito sana moyoni mwake hadi atakapomuhadithia mtu mwengine ndipo atakapohisi kuwa amepumzika.

Hivyo basi, suala la kuhifadhi siri ni jambo zito kwa mtu na ni amana aliyoichukua. Imepokewa kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema kuwa ikiwa mtu atazungumza na mtu mwengine kisha wakaachana basi huwa ni amana (yaani mazungumzo yale waliyozungumza huwa ni amana kwa kila mmoja). Katika Hadiyth Mtume anasema,

“Hakika katika watu wabaya wenye shari siku ya Qiyaamah ni mtu aliyefanya tendo la ndoa na mke wake kisha mume au mke akatoa siri ile ya mume wake au ya mke wake”[1]

 

Jambo la kuhifadhi siri ni la wajibu kwa mume na mke na ni jambo lililokuwa muhimu sana katika jamii na ndilo linalohifadhi amani na maadili mema katika jamii husika. Kwa hakika kutoa siri za mwanamme ndani ya nyumba yake au mwanamke, matengamano ya mume kwa mkewe, watoto wake, na kila alichokuwa nacho katika mali yake na mengineyo itakuwa ni fedheha kwa watu wengi. Uislamu umemuusia Muislamu kumsitiri na kumfichia siri nduguye Muislamu, na ya kuwa, Muislamu atakayemsitiri nduguye Muislamu basi Mwenyezi Mungu Atamsitiri yeye siku ya Qiyaamah.

 

Pamoja na kuwa kuhifadhi siri kwa ujumla ni jambo muhimu sana na ni wajibu, hata hivyo kuhifadhi siri ya unyumba baina ya mume na mke ni jambo la wajibu zaidi na ni jambo tukufu ambalo halifai kutolewa kwa hali yoyote ile. Ama wajinga wa zama zetu leo hii hawapendezwi na maneno isipokuwa ni maneno haya na yote hayo yanatokana na ukosefu mkubwa walionao wa imani na udhaifu wao.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametahadharisha hali hii ya kutoa siri ya jimai kwa watu, aliposema,

“Huenda mtu akasema anachomfanyia mke wake, na huenda hilo likafanywa na mwanamke pia (watu wakanyamaza baada ya maneno hayo) mwanamke akauliza[2], ee, kweli kabisa na wengi hufanya hivyo katika wanawake na wanaume, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, ‘Basi msifanye hivyo, mfano wa jambo hilo ni kama Shaytwaan aliyekutana na Shaytwaan mwenzake wa kike na akawa anamuingilia hapo njiani na watu wakiwa wanamwangalia”[3] 

 

 





[1] Imepokewa na Muslim

[2] Mwanamke huyu aliyeuliza jina lake ni, Asmaa bint Yaziyd, nae ndiye mpokezi wa Hadiyth hii.

[3] Imepokewa na Ahmad

Share

013-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Ni Wakati Gani Wivu Wako Kwa Mumeo Unakuwa Haufai?

 

NI WAKATI GANI WIVU WAKO KWA MUMEO UNAKUWA HAUFAI?

 

Katika hali ya kawaida kabisa wivu ni jambo linalokubalika, Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Huona wivu, Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inasema,

“Kwa hakika Allaah Huona wivu, na Muumini huona wivu, ama wivu wa Allaah ni Muumini kufanya aliyoharamishiwa na Allaah”[1]

 

Na kama sio wivu tabia nzuri zote na stara katika maisha yangepotea, na mipaka ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ingekiukwa mbele za watu na katika masikio ya watu. Ama ghera ya mke kwa mume wake ni kule kufanya yaliyoharamishwa na Allaah, hii ni ghera inayokubaliwa kishari’ah na ni yenye kupendeza ama nyinginezo ni katika jumla za ghera zenye kukatazwa na haswa ikiwa hazina shaka na tatizo.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema,

“Katika ghera kuna ambazo Anazipenda Allaah, na zingine Anazichukia Allaah, ama ghera Anazozipenda Allaah ni zile ghera zilizojengwa kwa shaka. Ama ghera Anazozichukia ni zile ghera zisizokuwa katika shaka”[2]

 

Jambo la kusikitisha ni kuwa nyumba nyingi zimeangamia na kuanguka kwa sababu ya baadhi za ghera; nayo hutokana na dhana na shaka ambazo si za msingi kabisa, hufuatiwa baada ya dhana na wivu wa namna hiyo ni kujuta nayo ni katika kukhasirika. Asili ya ndoa ni kuwa mwanamke huchagua mwanamme mwema, mwenye kuaminika, kwa maana hiyo hakuna njia au nafasi ya kutia shaka au kumchunguza kila wakati na kumfuatilia kwa kila kitu kwa hoja ya wewe kuwa na wivu. Jihadhari usije ukaiangamiza nyumba yako kwa nafsi yako.

 

Hili ni kwa upande wako kama mke, ama kwa upande wa mume wako na ghera yake juu yako ni juu yake kutekeleza majukumu yako kwa ukamilifu na wakati huo hiyo ghera haitokuwa na nafasi tena.

 

Moja katika majukumu haya ni kujilazimisha kwako na stara, heshima na kulinda utu wako, kisha kutotoka nyumbani kwako bila idhini yake, kisha baada ya hapo, usikae hata mara moja na asiyekuwa maharimu wako. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth yake anasema,

“Jihadharini na kuingia kwa wanawake, Mtu mmoja akauliza ewe Mtume wa Allaah: Je, nikikaa pamoja na shemeji yangu au ndugu wa mume wangu? Mtume akasema, “Shemeji ni mauti.”[3]

 

 


[1] Imepokewa na Al-Bukhaariy

[2] Imepokewa na Ahmad na wengineo

[3] Al-Bukhaariy na Muslim - Mpitiaji

Share

014-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Mume Wangu Ni Bakhili...Nifanyeje?!!

 

MUME WANGU NI BAKHILI…NIFANYEJE?!!!

 

Baadhi ya wake hushitaki na kulalama kwa ubakhili wa waume zao juu yao, malalamiko haya mengi yake si ya kweli, kwani mke hutaka fedha kwa mumewe na ikikosekana kutokana na hali ngumu ya maisha aliyonayo mume basi mke atamtuhumu mumewe kwa ubakhili.

 

Hata hivyo ikiwa mume ni bakhili kweli kwa mke wake na kuto kumpa na kumhudumia mke wake kwa yale aliyoruzukiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa wakati huo mume yule huipelekea nyumba yake katika mawimbi na dhoruba, kwani mke kuhitaji mali humpelekea mwanamke yule katika hatari.

 

Tunamwambia mume huyu, je, hukusoma kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) akiwaelezea waja wake waumini?

“Na wale ambao wanapotumia hawatumii kwa fujo wala hawafanyi ubakhili, bali wanakuwa katikati baina ya hayo.” (25:67)

 

Kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu suala hili,

“Mwenyezi Mungu Atamuuliza kila mchunga kwa alichokichunga, je, amekiweka mahala pake na kuhifadhi au amepoteza, itafikia hadi mtu kuulizwa kuhusu watu wake wa nyumbani”[1]

 

Fahamu ewe mume mkarimu kuwa kutoa kwako kwa ajili ya mke wako na watu wa nyumbani kwako ni sadaka utakayolipwa na Mwenyezi Mungu, katika Hadiyth tukufu ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam),

“Mtu atakapotoa kwa kuwapa watu wa nyumbani kwake akitaraji kulipwa na Allaah itakuwa ni sadaka aliyotoa (atalipwa kwa sadaka hiyo na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala))”[2]

 

Ni juu ya mke kuchunguza na kutafiti ni kwa nini mume wake anakuwa bakhili kwake, huenda akawa anafanya hivyo kutokana na kujua ufujaji wa mke wake, akipewa mali hufuja anachopewa, au huenda kuna sababu zingine binafsi azijuazo kutoka kwa mke wake. ikiwa ubakhili ni katika sifa ya mume wake, basi ni juu ya mke kusubiri na kutaka msaada wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na kujaribu kwa wema kumfanya mume wake aache ubakhili na kumbadilisha kuwa ni mtu karimu mwenye kujitolea.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimpa ruhusa Hind bint ‘Utbah kuchukua mali kutoka kwa mume wake kiasi kinachotosheleza mahitaji yake na wala asizidishe.  Mtume alimwambia hayo kulingana na swali aliloulizwa na Hind,

“Ewe Mtume wa Allaah, kwa hakika Abu Sufyaan ni mtu bakhili hanipi cha kunitosheleza na mtoto wangu ila kile ninachokichukua kutoka kwake bila ya yeye mwenyewe kujua, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia, ‘Chukua kwa wema kile kinachokutosheleza wewe na mwanao’”[3]

 





[1] Imepokewa na Ibn Hibaan

[2] Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim

[3]Imepokewa na Al-Bukhaariy

 

Share

015-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Wewe Ni Mchungaji Katika Nyumba Ya Mume Wako

 

WEWE NI MCHUNGAJI KATIKA NYUMBA YA MUME WAKO, NA UTAULIZWA KUHUSU UCHUNGAJI HUO

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema,

“Ee!! Jueni ya kwamba nyie nyote ni wachunga na kila mmoja ataulizwa alichokichunga, kiongozi wa watu ni mchunga na ataulizwa kwa alichokichunga, na mwanamme ni mchunga wa familia wake na ataulizwa kwa alichokichunga, mwanamke ni mchunga wa nyumba ya mume wake na watoto wake naye ataulizwa alichokichunga, na mtumwa ni mchunga wa mali ya bwana wake naye ataulizwa kuhusu uchungaji wake”[1]

 

Fahamu ewe dada wa Kiislamu kuwa nyumbani kwako kuna majukumu makubwa mno, kwa hivyo yahifadhi vizuri, muhifadhi vizuri mume wako na watoto wako. Hifadhi nzuri ya mali huwa ni katika mipango mizuri bila kufanya ubadhirifu. Ama kuhifadhi watoto maana yake ni kukesha kwa ajili yao ili wapate raha, na kuwalea malezi mema ya imani, ucha Mungu, uadilifu na kutekeleza ahadi.



[1] Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslm

 

Share

016-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Kutekeleza Ahadi Ni Katika Sifa Za Manabii

 

KUTEKELEZA AHADI NI KATIKA SIFA ZA MANABII

 

Kuwa mwadilifu kwa mume wako, na usikufuru namna mnavyoishi naye, na usisahau fadhila mlizofanyiana, kwa hakika haya yanatokana na uzuri wa uangalizi wako wa nyumba yako na kuihifadhi nyumba yako, nayo hupelekea kuokoka na moto.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kuwaambia wanawake,

“Toeni sadaka kwa wingi kwani wengi wenu mtakuwa kuni za motoni!! Mwanamke akauliza, Je, ni kwa sababu gani? Mtume akasema, ‘Kwa sababu hamuachi kulalama sana na mnakufuru maisha yenu ya ndoa, baada ya hapo wakawa wanatoa sadaka vidani vyao na kuweka katika nguo ya Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu)”[1]

 

Kukufuru ndoa maana yake kutotekeleza ahadi, ikiwa mume ameweza kuishi vizuri na mke wake muda wote lakini ikatokezea siku moja akamkosea basi atasahau ihsani aliyofanyiwa muda wote uliopita na atasema, ‘Hakuna hata siku moja aliyonifanyia mema’. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa mtu mwadilifu zaidi na hata baada ya kifo cha mke wake Mama wa Waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha), kwa ajili ya Mama wa Waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwakirimu marafiki wa Mama wa Waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) na akiwatembelea mara kwa mara, ilipotokezea kwa Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kumuonea wivu Mama wa Waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha), Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) akimwambia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa, Mama wa Waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa mwanamke mzee na Mwenyezi Mungu Amembadilishia kilicho bora zaidi yake (yaani Mtume akapewa  Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) baada ya kifo cha Mama wa Waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha). Mtume akamjibu Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kwa kusema, ‘WAllaahi, Mwenyezi Mungu Hakunibadilishia kilicho bora ya Mama wa Waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha).’ Hadiyth hii imetajwa hapo nyuma, baada ya hapo Mtume akawa anamtajia Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) fadhila za Mama wa Waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha).

 





[1] Imepokewa na Al-Bukhaariy

Share

017-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Kukatazwa Kutoroka Katika Nyumba Ya Mume

 

KUKATAZWA KUTOROKA KATIKA NYUMBA YA MUME

 

Huenda mume akatofautiana na mke (jambo hili ni la kawaida na hutokea mara kwa mara) lakini huenda tatizo hili wakati mwingine likawa kubwa kidogo na hivyo mke kughadhibika na kupandwa na Shaytwaan katika akili yake, jambo la kwanza siku zote analofikiria ni kukusanya nguo zake na kurudi kwao.

Kwa hakika hili ni kosa analofanya mke na mara nyingi wanakuwa ni wale walioolewa hivi karibuni, kwa kufanya hivyo mwanamke yule anakuwa amefanya makosa manne na sio moja tu:

1.     Kosa la Kishari’ah: nalo ni lile la kutoka nje ya nyumba bila ya ruhusa ya mume (hakuna sababu yoyote ya kujitetea, eti ‘ulikuwa na ghadhabu’);

2.     Kuweka mazingira yasiyokuwa mazuri katika nyumba anayokwenda, yaani nyumba ya wazazi wake;

3.     Kuenea kwa habari na watu wengine wa nje kujua siri za familia;

4.     Kulifanya tatizo dogo lililotokea kuwa kubwa na kuongeza ugumu katika maisha ya ndoa.

 

Kwa hakika suala la kuhama nyumba yako wewe dada yangu wa Kiislamu si suluhisho la tatizo lililopo, huku ni kuongeza tatizo. Hata hivyo jitahidi kusuluhisha matatizo yako na mume wako vizuri kwa utulivu na muombe Mola wako msamaha. Ikiwa mume wako ameghadhibika muache na mambo yake hadi atakapotulia, kisha mkurubie, na hata ikiwa mkosa ni mume wako katika kutekeleza majukumu yake kwako basi amini ya kuwa utakapomtendea mema na kuwa na subira juu yake basi atakusamehe pindi utakapokuwa mkweli kwa matendo yako yote.

 

Share

018-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Kutaka Talaka Bila Ya Kuwepo Tatizo Ni Jambo Lililoharamishwa Kishari’ah

KUTAKA TALAKA BILA YA KUWEPO TATIZO NI JAMBO LILILOHARAMISHWA KISHARI’AH

Mara nyingi mwanamke anataka talaka kwa mume wake pindi wanandoa wawili wanapomwachia Shaytwaan nafasi na pindi ghadhabu ya mwanamke inaposhtadi, lau angesubiri kidogo na kuzuia ghadhabu zake na kupata utulivu angeona kuwa hakukuwa na sababu ya hilo, talaka si jambo la mzaha wakalichezea wanandoa, akawa mmoja wao akighadhibika anamtishia mwenzake kwa talaka na mwengine akisema anapoghadhibika, ‘Nitaliki’.

 

Wanandoa wanatakiwa kuwa ni werevu kuliko matatizo yanayowakabili, wakishirikiana katika kutatua matatizo na wakifahamiana vizuri kwa hilo, na kila mmoja anajaribu kushusha mahitaji yake na kuachana na misimamo yake ili jahazi lisije likazama. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam.) amemtahadharisha mke asidai talaka kama hamna tatizo la msingi kwa kusema,

“Mwanamke yeyote atakaye talaka kutoka kwa mume wake bila ya tatizo la msingi basi ni haramu kwake kunusa harufu ya pepo”[1]

 

Hata hivyo kungekuwa na jambo lingine linalopelekea jambo hili kwa mfano mume kuwa na tabia mbaya kiasi cha kuwa mke wake hawezi kuvumilia, au ni mtu fasiki asiyetekeleza haki za mke wake na watoto wake, au mfano wa hayo katika mambo yanayofahamika kisheria na desturi.

 

Mke anaweza kudai talaka ikiwa njia zote za kufanya suluhu baina yao ndani ya nyumba na hata nje zimeshindikana ambazo katika utatuzi wenyewe na suluhu yenyewe hushiriki hakimu kutoka upande wa mume na hakimu kutoka upande wa mke kushindikana.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema,

Na mkichelea kuwepo mfarakano baina ya mke na mume basi pelekeni muamuzi kutokana na jamaa za mume, na muamuzi kutokana na jamaa za mke. Wakitaka mapatano Mwenyezi Mungu Atawawezesha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye khabari.(4:35)

 

 

 





[1] Imepokewa na Ahmad na At-Tirmidhiy na wengineo

 

Share

019-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Jamaa Za Mume Wako Ndio Jamaa Zako…Wakirimu

 

JAMAA ZA MUME WAKO NDIO JAMAA ZAKO…WAKIRIMU

 

Kwa hakika miongoni mwa mambo ambayo yananyanyua hadhi na shani yako kwa mume wako ni kuwakirimu jamaa za mume wako na haswa zaidi mama yake mzazi na kutangamana naye matengamano mazuri na kumuita kwa jina analopenda kuitwa nalo na kumsaidia mume wako aweze kuwafanyia wema wazazi wake wawili.

 

Ole wako, tena ole wako, kukikosoa jambo la mama yake kwa mume wako (wala pembeni) jambo hilo hatofurahia na litamkera na kumpa dhiki, jaribu kusubiri kwa muamala wa mama wa mume wako ikiwa hujavutiwa nae au wewe mwenyewe binafsi humpendi na kumbuka ya kuwa, ‘Kama unavyofanya utafanyiwa’ wahurumie watu waliokuwa dhaifu na wazee, na jua ya kwamba chochote utakachowafanyia basi nawe utafanyiwa na watoto wako au wake za wanao.

 

Kadhalika kumbuka kauli ya Allaah,

Na Mola wako Ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa heshima. (17:23)

 

Pamoja na kuwa mume wako ameamrishwa kuwafanyia wema wazazi wake wawili lakini nawe kama mke wake una wajibu wa hilo pia, nalo ni kuhakikisha kuwa unamsaidia mume wako katika kuwafanyia wema wazazi wake wawili, usiwe kikwazo katika kufikia hilo, kama vile wewe kuzua matatizo pamoja na mama yake na kumuweka mume wako katika hali ngumu. Katika kuona kwamba umeshindwa kumsaidia hilo ni pindi mume wako anapokufadhilisha wewe kuliko hata mama yake na hivyo kupata hasara kubwa, na kadhalika hasara hiyo utaipata nawe kadhalika kwani wewe ndie uliyesababisha hilo. Mtu yeyote atakayelingania katika upotofu naye ana dhambi na dhambi za watakaomfuata katika upotofu ule hadi siku ya Qiyaamah, kuwaasi wazazi wawili ni katika madhambi makubwa nayo ni sababu ya kukosa rehema kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

 

Tunasoma katika Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam),

“Watu watatu hawatoingia peponi; Atakayewaasi wazazi wake wawili, Dayuuth[1], na Yule mwenye kujifananisha na wanaume”[2]

 

Je, baada ya hapo dada yangu kuna marejeo mema?!! Kwa hakika kuwakirimu wazazi wawili, na kuwalingania katika kufanya wema ni katika jambo litakalokusaidia katika kupata furaha hapa duniani na Akhera na hivyo kheri itaweze kuenea katika nyumba yenu na rehema na Baraka za Mwenyezi Mungu Hakika Yeye ni Mwingi wa Kuhimidiwa, Mwingi wa Kutukuzwa.

 





[1] Dayuuth ni yule mtu asiyeona wivu kwa mke wake hata akifanya jambo baya

[2] Imepokewa na An-Nasaaiy, Al-Haakim na wengineo

Share

020-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Kumtii Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Kunaingiza Furaha Katika Nyumba

 

KUMTII ALLAAH (SUBHAANAHU WA TA’ALA) KUNAINGIZA FURAHA KATIKA NYUMBA

 

Mara nyingi sisi huwa tunasahau Akhera, lakini haitokezei mtu kusahau kuwanunulia watoto wake nguo mpya za ‘Iyd na hatusahau kamwe kununua aina mbali mbali za vyakula na vinywaji tukitaka kuupokea mwezi mtukufu wa Ramadhaan kila mwaka.

 

Mara nyingi tunashindana ili tuonekane kuwa tuna nyumba nzuri za kisasa zaidi na hili ni jambo zuri halina tatizo lakini Je, tunashindana kwa kiasi hicho hicho kushindania kufanya ‘amali za Akhera nayo ndio amali bora zaidi zinazokusanya maisha mazuri zaidi na ndio maisha halisi.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) anasema,

“…Na katika hayo washindane wenye kushindana.(83:26)

 

Ewe, mke Muumini, Muangalie Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akimgongea mwanae Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha) akiwa na mumewe ‘Aliy usiku akiwaambia wote wawili,

‘Je, Hamswali?!![1] maneno haya yalikuwa ni kulingania katika kushindana katika mambo ya kheri na kujitenga katika kufanya ibada za siri kwa ajili yako ili ikikurubishe kwa Mola wake Mkarimu, kwa hakika Swalah za usiku, hali ya kuwa watu wamelala nyakati hizo ni bora zaidi na zina baraka.

 

Tunasoma katika Hadiyth sahihi kuwa,

“Mwenyezi Mungu Amrehemu mtu aliyesimama usiku akaswali kisha akaamsha familia yake akikataa humwagia maji usoni, kisha Mwenyezi Mungu Amrehemu mwanamke aliyeamka usiku kuswali kisha akamuamsha mume wake akikataa anamwekea maji usoni mwake”[2]

 

Wala sidhani kuwa mke ambae hii ndio hali yake anaweza kuleta matatizo ambayo yakafanya nyumba yao ikawa na migongano na nyufa kubwa, bali jambo la kheri na zaidi ya kheri katika nyumba iliyogubikwa na utiifu, ni kuendelea kuwahimiza katika kufanya mambo ya kheri.

 

 





[1] Al-Bukhaariy na Muslim

[2] Abu Daawuud

Share

021-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Jirani Ana Haki Tusizisahau

 

JIRANI ANA HAKI TUSIZISAHAU

 

Familia ya Kiislamu haiishi peke yake kwa kujitenga na jamii bali ni lazima kuamiliana na jirani. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuusia kuchanganyika na watu na kuwa anayechanganyika na watu na akasubiria maudhi yao ni bora kuliko yule mtu ambaye hatangamani na watu na wala asiyesubiri maudhi yao.[1]

 

Jirani ndiye mtu wa mwanzo anayejiwa na mtu wakati wa shida hivyo kumfanyia wema ni wajibu na miongoni mwa wajibu mkubwa na kumfanyia ubaya ni jambo linalopelekea katika moto na adhabu ya Mwenyezi Mungu.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa,

“Mwanamke fulani namkumbuka kwa wingi wa Swalah zake, Swawm zake na sadaka zake azitoazo lakini anawaudhi jirani zake kwa ulimi wake…Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akajibu, ‘Kwa hakika yeye ni mtu wa motoni’[2]

 

Hata hivyo ni muhimu kutahadhari na jirani muovu ambaye hajali kumuasi Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa uwazi au mchana, na vile vile jirani mzushi (mtu wa bid’ah) ili watoto wasije wakaiga tabia za namna hizi na wakaenda kinyume na shari’ah za Mwenyezi Mungu.

Hata hivyo mlango wa nasaha na kuwaongoza watu hawa haujafungwa na kadhalika ikibidi kujadiliana nao kwa lile lililokuwa zuri hadi Allaah atakapotoa ruhusa ya kuongoka kwao, na siku zote usisahau kuwa, “Dini ni Nasaha.”

 





[1] At-Tirmidhiy

[2] Imepokewa na Ahmad

Share

022-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Kwenye Njia Panda

 

KWENYE NJIA PANDA

 

Ewe, mke Muumini, kila mtu husogea katika furaha lakini wachache ndio wanaopata, wengi wao hukosea njia yake. Ama sisi Waislamu tunajua ya kwamba furaha ya kweli huanzia mwanzo kabisa kwa imani ya mtu kwa Mola wake na utiifu wake na kufuata mfumo na shari’ah Zake.

 

Ukitaka ewe Dada yangu Muumini kupata furaha ya kweli kabisa ni juu yako kubadilisha muelekeo, nayo si mwengine bali utiifu kwa mume wako, huwa ndio chanzo cha utiifu wako kwa Mola wako na kumridhisha mume wako ndio kumridhisha Mola wako na haya ndio ambayo yatakufanya umsamehe makosa yake na kuangalia thawabu kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kabla ya kutaka ujira wa hapa hapa duniani au kuridhia kwa mume wako na kuukabili ubaya uliofanyiwa kwa wema utakaoufanya na yote ni kufuata maelekezo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) aliposema,

“…Pinga uovu kwa lilio jema zaidi. Hapo yule ambaye baina yako naye pana uadui atakuwa kama rafiki jamaa aliye mpole. (41: 34)

 

Hii kwa Yule ambaye ana ugomvi na mwenzake, lakini je kwa yule ambaye ana usuhuba na mwenzake, mapenzi na huruma itakuwaje?!!

 

Wema ni wema ewe dada yangu, hifadhi maneno haya saba yafuatayo yatakufaa na ndio mwisho wa risala yangu hii.

 

1.     Utiifu (kwa Mola wako kisha kwa mume wako kwa sharti utiifu huo kwa mume wako usiwe ni katika kumuasi mola wako);

2.     Kukinai;

3.     Kuwa mwaminifu;

4.     Fanya mambo yako bila ya kujikalifisha, yaani fanya mambo yako kwa wepesi;

5.     Kuwa msafi daima;

6.     Kuwa ni mwenye tabasamu muda wote;

7.     Daima mpendelee mwenzako.

 

 

 

Mwisho Wa Risala Hii

 

 

 

Share