Kutoa Zakaah (Zakaatul-Maal)

Share

001-Kutoa Zakaah: Yaliyomo

Share

002-Kutoa Zakaah: Utangulizi

 

Kutoa Zakaah: Utangulizi

 

Alhidaaya.com

 

Kutoa Zakaah ni nguzo ya tatu ya Islam.Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Nguzo za Uislaam ni tano. Shahada kuwa hapana muabudiwa wa haki ila Allaah, na kwamba Muhammad ni Rasuli wa Allaah, na Kusimaamisha Swalaah, na Kutoa Zakaah, na Kufunga mwezi wa Ramadhwaan na Kuhiji Makkah kwa mwenye uwezo wa kufika huko".

 

Kufaridhishwa kwa Zakaah ni jambo muhimu na tukufu sana kwa Waislam kwa sababu ya wingi wa faida yake na kwa ajili ya haja kubwa ya kuwepo kwa jambo hilo, kutokana na masikini na mafakiri wanaohitajia sana msaada wa ndugu zao wenye uwezo, kwani katika Kutoa Zakaah uhusiano mzuri unajengeka baina ya Waislam matajiri na Waislam masikini, na hii ni kwa sababu siku zote moyo wa mtu huelekea na kumpenda yule anayemfanyia wema na ihsani. Zakaah inasaidia pia katika kuzisafisha na kuzitakasa nyoyo.

 

Allaah Anasema:

خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا

Chukua (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) katika mali zao Swadaqah, uwatakase na ziwazidishie kwazo.  [At-Tawbah: 103]

 

Katika kutoa Zakaah au Swadaqah kunaizoesha nafsi katika kuwapendelea kheri watu wenye haja na katika kuwaonea huruma na pia kunaipatia nafsi baraka nyingi kutoka kwa Allaahu Subhanaahu wa Ta’aalaa.

 

Allaah Anasema:

وَمَا أَنفَقْتُم مِّن شَيْءٍ فَهُوَ يُخْلِفُهُ وَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ

Na kitu chochote mtoacho, basi Yeye Atakilipa, Naye ni Mbora wa wenye kuruzuku. [Sabaa: 39]

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Allaahu Anasema: 'Ee mwana Aadam, toa na sisi tutakupa"

 

Anasema Ibn Uthaymiyn:

"Kutoa Zakaah ni jambo liliofaradhishwa katika Uislam, na ni nguzo muhimu sana baada ya Shahada mbili na Swalaah, na dalili ya kuwajibika kwake imo ndani ya Qur-aan na pia katika mafundisho ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), pamoja na ijmai ya Waislam, na yeyote anayeikanusha nguzo hii anakuwa Kafir aliyertadi katika Uislaam, na hukumu yake ni kutubishwa, na akitubu anasamehewa. Ama akikataa kutubu na akaendelea kuikanusha basi hukmu yake ni kuuliwa. Ama anayeifanyia ubakhili au akapunguza katika Zakaah yake, huyo anakuwa miongoni mwa madhalimu wanaostahiki adhabu ya Allaahu.

 

Allaahu Anasema:

 

وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلاَ يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللّهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ. يَوْمَ يُحْمَى عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَى بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ هَـذَا مَا كَنَزْتُمْ لأَنفُسِكُمْ فَذُوقُواْ مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ

Na wale wanaorundika dhahabu na fedha na wala hawazitoi katika njia ya Allaah, basi wabashirie adhabu iumizayo.  Siku zitakapopashwa katika Jahannam, na kwazo vikachomwa moto vipaji vyao, na mbavu zao, na migongo yao (wakiambiwa): Haya ndiyo mliyoyarundika kwa ajili ya nafsi zenu. Basi onjeni yale mliyokuwa mkiyarundika. [At-Tawbah - 34 - 35]

 

 "Miongoni mwa faida za kutoa Zakaah anazozipata mtu katika dini yake" anaendelea kusema Shaykh Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah), "Ni kuitimiza nguzo katika nguzo za Kiislam, jambo litakalomletea mtu furaha katika dunia yake na katika akhera yake, na pia inazidi kumkaribisha mja kwa Rabb wake na kumuongezea Imani, kama ilivyo katika mambo yote ya kumtii Allaahu Subhanaahu wa Ta’aalaa."

 

Share

003-Kutoa Zakaah: Maana Ya Zakaah

 

Kutoa Zakaah:Maana Ya Zakaah

 

Alhidaaya.com

 

 

Zakaah ni ile haki Aliyoifaradhisha Allaah kwa Muislam katika mali yake anayotakiwa kuwapa wanaostahiki. Neno Zakaah, katika lugha (katika kamusi ya lugha ya Kiarabu) maana yake ni 'Kujitakasa', kwa sababu anayetoa Zakaah anataraji kuitakasa mali yake, nafsi yake na kupata baraka kutoka kwa Rabb wake.

 

Allaah Anasema:

خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا

Chukua (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) katika mali zao Swadaqah, uwatakase na ziwazidishie kwazo. [At-Tawbah: 103]

 

Zakaah ni nguzo ya tatu ya Uislaam iliyofaradhishwa katika Qur-aan tukufu na katika mafundisho ya Nabiy mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na kwa sababu ya umuhimu wake, Allaah ameitaja mara themanini na mbili katika Qur-aan kwa kuifuatanisha pamoja na Swalaah.

 

Imepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema:

 

"Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomteua Muadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa gavana wa nchi ya Yemen na kadhi wao alimwambia:

 

"Unakwenda katika nchi ya watu wa Ahlul Kitab, kwa hivyo (kwanza) walinganie katika shahada ya Laa ilaaha illa Allaah na kwamba mimi ni Rasuli wa Allaah, wakitii juu ya hilo, wafundishe kuwa Allaah amewafaradhishia Swalaah tano mchana na usiku, wakitii juu ya hilo, wafundishe kuwa Allaah amewafaradhishia Swadaqah (Zakaah) za mali zao, zichukuliwe kutoka kwa matajiri wao na kurejeshewa masikini wao, na kama wakitii juu ya hilo, usije ukachukuwa mali zao zenye thamani, na uiogope dua ya aliyedhulumiwa, kwani hapana kizuizi baina yake (dua hiyo) na baina ya Allaah". [Imesimuliwa na Ma-Imaamu wote wa Hadiyth]

 

Imesimuliwa pia na At-Twabaraaniy kutoka kwa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Allaah amewafaradhishia matajiri wa Kiislam katika mali zao kiasi cha kuwatosha masikini wao. Na (masikini) wasingepata tabu ya njaa na mavazi isipokuwa kutokana na ubakhili wa matajiri wao. Jueni kuwa Allaah atawahesabia hesabu nzito sana na atawapa adhabu iumizayo".

 

Share

004-Kutoa Zakaah: Kufaradhishwa Zakaah

 

Kutoa Zakaah: Kufaradhishwa Zakaah

 

Alhidaaya.com

 

 

Zakaah imefaradhishwa wakati Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa Makkah katika siku za mwanzo za Uislaam, lakini hapakuwekwa Nisaab, (kiwango cha mali ambacho mtu akiwa nacho kwa muda wa mwaka analazimika kuitolea Zakaah), wala kiasi cha kulipa, isipokuwa waliachiwa Waislam wenyewe kukisia kiasi cha kutoa.

 

Katika mwaka wa Pili baada ya Hijrah, ilifaradhishwa kiasi chake katika kila aina ya mali na kubainishwa vizuri.

 

Share

005-Kutoa Zakaah: Umuhimu Wake (Katika Qur-aan)

 

Kutoa Zakaah: Umuhimu Wake (Katika Qur-aan)

 

Alhidaaya.com

 

 

Katika Qur-aan tukufu na katika Mafundisho ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), yamo mafunzo mengi yanayopendekeza Kutoa Zakaah na yanayowakemea wale wasioitoa.

 

Katika Qur-aan Allaah Anasema:

خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا

Chukua (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) katika mali zao Swadaqah, uwatakase na ziwazidishie kwazo. [At-Tawbah: 103]

 

Na maana yake ni "Chukua ee Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Swadaqah maalum kutoka katika mali za Waislam na uwape wanaostahiki ili wenye mali 'wasafike' kutokana na uchafu wa ubakhili na tamaa, na kutokana na ubaya wa kuwanyima masikini haki zao na pia 'uwatakase' nafsi zao kwa Swadaqah hizo na wapate baraka za Rabb wao ili waweze kupata furaha za hapa duniani na za huko Aakhirah.

 

Na Akasema:

 

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ. آخِذِينَ مَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ إِنَّهُمْ كَانُوا قَبْلَ ذَلِكَ مُحْسِنِينَ. كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ. وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ. وَفِي أَمْوَالِهِمْ حَقٌّ لِّلسَّائِلِ وَالْمَحْرُومِ

Hakika wenye taqwa watakuwa katika Jannaat na chemchemu.  Wakichukua yale Atakayowapa Rabb wao. Hakika wao walikuwa kabla ya hapo ni wahisani. Walikuwa kidogo tu katika usiku wakilala kwa raha. Na kabla ya Alfajiri wakiomba maghfirah. Na katika mali zao kuna haki maalumu kwa mwenye kuomba na asiyeomba. [Adh-Dhaariyaat: 15-19]

 

Katika Aayah hii Allaah Anatuelezea juu ya wale atakaowaingiza katika bustani Zake na chemchem, kwa sababu walipokuwa huko duniani walikuwa wenye kulala muda mfupi sana nyakati za usiku, na sehemu kubwa ya usiku, walikuwa wakiswali, na nyakati za kabla ya kuingia alfajiri walikuwa wakiomba maghfira huku wakijikurubisha kwake Subhanaahu wa Ta’aalaa.

 

Walikuwa pia watu wenye kutoa katika mali zao kuwapa fakiri na maskini, wenye kuomba na wasiyo omba huku wakiwaonea huruma.

 

Na Allaah Akasema pia:

 

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاء بَعْضٍ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُقِيمُونَ الصَّلاَةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَيُطِيعُونَ اللّهَ وَرَسُولَهُ أُوْلَـئِكَ سَيَرْحَمُهُمُ اللّهُ إِنَّ اللّهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ

"Na Waumini wanaume na Waumini wanawake ni marafiki wandani wao kwa wao, wanaamrisha mema na wanakataza munkari na wanasimamisha Swalaah na wanatoa Zakaah na wanamtii Allaah na Rasuli Wake. Hao Allaah Atawarehemu. Hakika Allaah ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote". [At-Tawbah - 71]

 

Share

006-Kutoa Zakaah: Umuhimu Wake (Katika Sunnah)

 

Kutoa Zakaah: Umuhimu Wake (Katika Sunnah)

 

Alhidaaya.com

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Mambo matatu naapa juu yake na nakuhadithieni Hadiyth muihifadhi (vizuri).

 

Mali haipungui kwa kutoka Swadaqah, na mtu anapodhulumiwa akasubiri, basi Allaah humuongezea utukufu, na mtu anapojifungulia mlango wa kuombaomba, basi Allaah humfungulia mlango wa ufakiri". [At-Tirmidhiy kutoka kwa Abuu Kabshah Al-Anmaary (Radhwiya Allaahu ‘anhum)]

 

Na kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa; Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Hakika Allaah anazikubali Swadaqah na anazipokea kwa mkono wake wa kuume na anailea kama mmoja wenu anavyomlea nyumbu wake mpaka tonge (anayoitoa Swadaqah) inafikia ukubwa wa jabali Uhud". [Ahmad - At-Tirmidhiy na ameisahihisha]

 

Hadiyth hii inatujulisha kuwa mtu anapotoa Zakaah au Swadaqah, basi Zakaah hiyo inaingia mikononi mwa Allaah Subhanaahu wa Ta’aalaa kwanza, kabla haijaingia mikononi mwa masikini anayepewa, ikitufahamisha jinsi gani Allaah anavyoitukuza ‘Ibaadah hii ya Kutoa Zakaah na jinsi anavyompenda mja wake mwenye kutoa Zakaah au Swadaqah hata akaipokea kwa mikono yake Mwenyewe Subhanaahu wa Ta’aalaa kwanza, akaizidisha jaza yake na kuifanya iwe na ukubwa wa Jabali Uhud.

 

Anasema Waki’iy:

 

"Hadiyth hii pia inasadikisha kauli yake Subhanaahu wa Ta’ala katika Qur-aan pale Aliposema:

 

أَلَمْ يَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ هُوَ يَقْبَلُ التَّوْبَةَ عَنْ عِبَادِهِ وَيَأْخُذُ الصَّدَقَاتِ

Je, hawajui kwamba Allaah Ndiye Anayepokea tawbah ya waja Wake, na Anapokea Swadaqah. [At-Tawbah: 104]

 

Na Aliposema:

يَمْحَقُ اللَّـهُ الرِّبَا وَيُرْبِي الصَّدَقَاتِ ۗ 

Allaah Huifuta baraka (mali ya) ribaa na Huzibariki swadaqah.[Al-Baqarah - 276]

 

Imepokelewa kuwa Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:

 

"Mtu mmoja kutoka katika kabila la Bani Tamiym alimwendea Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwambia:

 

"Ee Rasuli wa Allaah, mimi nina mali nyingi na nina jamaa wengi na wageni huja kwangu kwa wingi. Kwa hivyo nijulishe nini nifanye na vipi nitowe?"

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

 

"Utoe Zakaah kutoka katika mali yako, kwa sababu hiyo ni tohara itakayokutahirisha, na uwaendee watu wako (ndugu zako wa nasaba), na uijue haki ya masikini na ya jirani na ya muombaji". [Ahmad]

 

Na Kutoka kwa Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Mambo matatu naapa juu yake, Allaah hawezi kumfanya aliye na sehemu yake katika Uislam akawa sawa na yule asiye na sehemu. Na sehemu za Uislaam ni tatu. Swalaah, Funga na Zakaah. Na Allaah Anapokuwa pamoja na mja wake hapa duniani, basi huko akhera hamuachi akawa na mwengine asiyekuwa Yeye. Na mtu anayewapenda watu hapa duniani, basi siku ya Qiyaamah Allaah Atamjaalie awe pamoja nao…" [Ahmad]

 

Na kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:

 

"Mtu mmoja alimuuliza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam);

"Ee Rasuli wa Allaah; Unasemaje juu ya mtu anayetoa Zakaah ya mali yake?"

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

"Atakayetoa Zakaah ya mali yake, keshaiondoa shari yake".

 

Share

007-Kutoa Zakaah: Wasiotoa Zakaah (Katika Qur-aan)

 

Kutoa Zakaah: Wasiotoa Zakaah (Katika Qur-aan)

 

Alhidaaya.com

 

Allaah Anasema:

 

وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلاَ يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللّهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ. يَوْمَ يُحْمَى عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَى بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ هَـذَا مَا كَنَزْتُمْ لأَنفُسِكُمْ فَذُوقُواْ مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ

Na wale wanaorundika dhahabu na fedha na wala hawazitoi katika njia ya Allaah, basi wabashirie adhabu iumizayo. Siku zitakapopashwa katika Jahannam, na kwazo vikachomwa moto vipaji vyao, na mbavu zao, na migongo yao (wakiambiwa): Haya ndiyo mliyoyarundika kwa ajili ya nafsi zenu. Basi onjeni yale mliyokuwa mkiyarundika. [At-Tawbah: 34 – 35]

 

Na akasema:

 

وَلاَ يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللّهُ مِن فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَّهُمْ بَلْ هُوَ شَرٌّ لَّهُمْ سَيُطَوَّقُونَ مَا بَخِلُواْ بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَلِلّهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَاللّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ

Wala wasidhani kabisa wale wanaofanya ubakhili kwa yale Aliyowapa Allaah katika fadhila Zake kwamba hayo ni khayr kwao, bali ni shari kwao. Watafungwa kongwa yale waliyoyafanyia ubakhili Siku ya Qiyaamah. Na ni Wake Allaah Pekee urithi wa mbingu na ardhi. Na Allaah kwa yale myatendayo ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [Aal-‘Imraan: 180]

 

Katika aya hii, Allaah Amesema "Watafungwa kongwa" badala ya "Watakuja kufungwa kongwa".

 

kwa ajili ya kutujulisha ukaribu wa mtu kukumbana na adhabu hizo. Kwa sababu mtu akeshakufa tu Qiyaamah chake kishasImaama, na kuanzia hapo mpaka siku ya Qiyaamah ataanza kukumbana na baadhi ya adhabu kutokana na yale maovu aliyoyatenda.

 

Wangapi wametoka majumbani mwao kwa miguu yao wenyewe, wakarudishwa wakiwa wamebebwa. Wangapi walifunga wenyewe vifungo vya suruali zao, wakaja kufunguliwa na waoshaji maiti.

 

Mwanaadamu anapotafakari juu ya wale wanaobebwa juu ya majeneza kila siku na kupelekwa makaburini wakiacha mali zao nyingi nyuma yao, mali zitakazokuja kufaidiwa na warithi, ataona namna gani yeye alivyohangaika kuichuma mali hiyo na nani atakayekuja kufaidika nayo, na nani atakayehesabiwa juu ya mali hiyo.

 

Ikiwa mali imepatikana kwa njia zisizokuwa za halali au ikiwa mali hiyo haikutolewa ndani yake haki ya Allaah, basi mali hizo watasatarehe nayo warithi, na yule aliyechuma ndiye atakayeulizwa naAllaah na kuhesabiwa.

 

Allaah Subhanaahu wa Ta’aalaa Akamaliza Aayah hii kwa kusema:

 

وَلِلّهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَاللّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ

"Na urithi wa mbingu na ardhi ni wa Allaah. NaAllaah ana khabari za yote mnayoyafanya."

 

Na maana yake ni kuwa hata kama utawaachia mali hiyo watu wako, wao pia watakuja kufa na watakaokuja baadaye nao watakufa, na mwisho kabisa hapana atakayebaki isipokuwa Allaah Subhanaahu wa Ta’aalaa, siku atakayozirithi mbingu na ardhi na kila kilicho juu yake.

 

Share

008-Kutoa Zakaah: Wasiotoa Zakaah (Katika Sunnah)

 

Kutoa Zakaah: Wasiotoa Zakaah (Katika Sunnah)

 

Alhidaaya.com

 

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Atakayepewa mali kisha asitoe Zakaah yake, basi mali hiyo Siku ya Qiyaamah itageuzwa kuwa joka dume lenye upara, mwenye madoa mawili machoni (kutokana na wingi wa sumu aliyonayo), atajizungusha katika mwili wa mtu huyo, kisha atamkaba shingoni huku akimwambia:

"Mimi ndiyo hazina yako uliyokuwa ukiikusanya, mimi ndiyo mali yako", kisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaisoma Aayah hii:

 

وَلاَ يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللّهُ مِن فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَّهُمْ

Wala wasidhani kabisa wale wanaofanya ubakhili kwa yale Aliyowapa Allaah katika fadhila Zake kwamba hayo ni khayr kwao.  [Aal-‘Imraan: 180]

[Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Na kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) amesema kuwa; Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Enyi watu wa Madina, mambo matano mkija mkapewa mtihani juu yake na kuteremshiwa - Najikinga kwa Allaah yasije yakakukuteni - Hautoenea uzinzi katika kaumu mpaka wakafikia kujitangazia, (isipokuwa) yatakuja kuenea kwao maradhi (aina mpya) ambayo hayajakuwepo kwa waliowatangulia, na hawatopunjwa watu katika vipimo na katika mezani isipokuwa wataletewa umasikini na shida ya kupatikana vitu, na dhulma ya ufalme. Na watakapoacha (watu) kutoka Zakaah ya mali zao, watanyimwa mvua, na lau kama si kwa ajili ya wanyama, basi isingenyesha mvua. Na watakapovunja ahadi ya Allaah na ahadi ya Rasuli wake, watasalitishiwa adui asiyekuwa mwenzao achukuwe baadhi ya vilivyo mikononi mwao. Na ikiwa viongozi wao hawatahukumu kwa kitabu cha Allaah, basi vitafanywa vita vyao viwe baina yao" [Ibn Maajah – Al-Bazaar na Al-Bayhaqiy]

Share

009-Kutoa Zakaah: Hukmu Ya Asiyetoa Zakaah

 

Kutoa Zakaah: Hukmu Ya Asiyetoa Zakaah

 

Alhidaaya.com

 

 

Kutoa Zakaah ni fardhi, na ni katika mambo waliyokubaliana 'Ullamaa wote kuwa yeyote anayeikanusha fardhi hii anakuwa kesha toka katika dini akiwa ni kafiri aliyertadi, isipokuwa kama mtu huyo ni Muislam mpya, na kwa ajili hiyo husameheka kutokana na kutoelewa kwake.

 

Ama yule anayeacha kutoa Zakaah lakini wakati huo huo hakanushi kuwajibika kwake, huyo anapata dhambi ya kuacha kuitoa, lakini kuacha huko hakumtoi katika dini, isipokuwa ikiwa anaishi katika nchi inayohukumiwa na shariy’ah ya Kiislam, basi anayehukumu atatakiwa aichukuwe Zakaah hiyo kwa nguvu.

 

Ipo ikhtilafu baina ya 'Ulamaa iwapo anayeacha kutoa Zakaah atozwe gharama kwa kuacha kwake huko kwa ajili ya kumtia adabu, na gharama yenyewe ni kuchukuliwa nusu ya mali yake, na hii inatokana na Hadiyth iliyotolewa na Imaam Ahmad na Annasaiy na Abu Daawuud na Al-Haakim na Al-Bayhaqiy kutoka kwa Bahza bin Hakim kutoka kwa baba yake kutoka kwa babu yake kuwa amesema:

 

"Nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

 

"…Atakayekataa (kutoa Zakaah) tutaichukuwa (kwa nguvu, na pia tutachukua) pamoja na nusu ya mali yake haki katika haki ya Rabb wetu Mtukufu na watu wa Aali Muhammad si halali kwao kuchukuwa chochote katika hiyo (Zakaah)".

 

[Amesema Imaam Ahmad kuwa isnadi ya Hadiyth hii ni sahihi na amesema Al Hakim kuwa hii ni Hadiyth sahihi].

 

Hata hivyo wapo baadhi ya maulamaa walioidhoofisha Hadiyth hii na wengine wakasema kuwa hukmu hii ilifutwa baadaye, wakiegemea baadhi ya Hadiyth zinazoelezea juu ya baadhi ya watu waliochelewa kulipa Zakaah na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwachukulia nusu ya mali zao.

 

Ama ikiwa watu watakataa kutoa Zakaah wakiwa wanaelewa kuwa ni jambo la wajibu, na ikiwa zipo nguvu za kuweza kupambana nao, basi watapigwa vita mpaka wakubali kuitoa. Na hii inatokana na Hadiyth iliyosimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim kuwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Nimeamrishwa nipambane na watu mpaka watowe shahada ya; Laa ilaaha illa Allaah Muhammadan RasuluLLaah, na wasimaamishe Swalaah na watoe Zakaah. Wakishafanya hivyo, damu yao na mali yao zitakingika kwangu isipokuwa katika kulipa haki za Kiislam, na hesabu yao iko kwa Allaah".

 

Imeelezwa na Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa; Alipofariki Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Abuu Bakr akawa (Khalifa), baadhi ya waarabu walikataa kutoa Zakaah, na Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alitayarisha jeshi la kupambana nao.

‘Umar akasema (kumuuliza Abuu Bakr):

 

"Vipi unataka kupigana vita na watu (Waislam), wakati Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

 

"Nimeamrishwa nipambane na watu mpaka watowe shahada ya; Laa ilaaha illa Allaah na atakayetamka hayo itakingika kwangu mali yake na nafsi yake isipokuwa katika haki yake (anayodaiwa au kisasi kwa makosa aliyofanya), na hesabu yake iko kwa Allaah?”

 

Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema:

"Wa-Allaahi nitampiga vita yeyote atakayetenganisha baina ya Swalaah na Zakaah, kwa sababu Zakaah ni katika 'haki yake' (shahada hiyo). Wa-Allaahi lau kama wataacha kunipa mbuzi mdogo (na katika riwaya nyingine 'Kamba') iliyokuwa ikilipwa wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ningewapiga vita kwa kukataa kwao kuitoa".

 

‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema:

 

"Wa-Allaahi nilipoona kuwa Allaah amemfungulia Abu Bakr kifua chake aamue kuwapiga vita, nikajuwa kuwa yuko katika haki".

[Muslim - Abuu Daawuud - na At-Tirmidhiy na Maimaamu wengine wa Hadiyth]

 

Share

010-Kutoa Zakaah: Wanaowajibika Kutoa

 

Kutoa Zakaah: Wanaowajibika Kutoa

 

Alhidaaya.com

 

 

- Muislam anayemiliki Niswaab, nacho ni 'Kiwango maalum cha mali’ kilichowekwa na shariy’ah katika aina yoyote ile ya mali inayowajibika kuitolea Zakaah.

 

- Niswaab hiyo lazima iwe ishatolewa ndani yake mahitajio ya dharura ya lazima kama vile chakula, mavazi, makazi, vyombo vya nyumbani, chombo cha usafiri na vyombo vyake vya kufanyia kazi, madeni n.k.

 

- Lazima kiwango hicho kiwe kimemilikiwa kwa muda wa mwaka mzima (mwaka wa Kiislam) bila kupungua katika wakati wowote ule ndani ya mwaka huo, na kama kitapungua katika wakati wowote ule kabla ya kutimia mwaka, basi hesabu nyingine mpya itaanzwa kuanzia pale kinapokamilika tena Kiwango hicho.

 

Amesema Imaam An-Nawawiy:

 

"Madhehebu yetu na madhehebu ya Imaam Malik na Ahmad na ya ‘ulamaa walio wengi ni kuwa; Mali inayotolewa Zakaah kwa ajili yake, kama vile dhahabu, fedha na wanyama wa kufugwa, lazima kiwango chake kibaki kwa muda wa mwaka mzima bila kupungua. Na wakati wowote ule kitakapopungua, basi mwaka wake unakatika, na wakati wowote ule kitakapotimia tena, unaanza kuhesabiwa mwaka mwingine".

 

Ama Abuu Haniyfah anasema:

 

"Kinachotakiwa ni kuwepo kwa Kiwango (Niswaab) mwanzo wa mwaka na mwisho wake, na haidhuru iwapo kitapungua katikati ya mwaka, hata kama mtu alikuwa nazo Dirham mia mbili kisha zikapotea zote katikati ya mwaka na akabakiwa na dhirham moja tu, au kama alikuwa na kondoo arubaini wakapungua na akabaki mmoja tu, kisha mwisho wa mwaka akaweza kumiliki (Dirham) mia mbili kamili au (kondoo) arubaini kamili, basi itawajibika Zakaah kwa vyote".

 

Masharti haya hayahusiani na Zakaah za mazao na matunda, kwa sababu vitu hivyo Zakaah yake inatolewa siku ya mavuno.

 

Allaah Anasema:

وَآتُواْ حَقَّهُ يَوْمَ حَصَادِهِ

"Na toeni haki yake (Zakaah) siku ya kuvunwa kwake". [Al-An’aam: 141]

 

Share

011-Kutoa Zakaah: Mtoto Na Mpungufu Wa Akili

 

Kutoa Zakaah: Mtoto Na Mpungufu Wa Akili

 

Alhidaaya.com

 

 

Inamuwajibikia aliyekabidhiwa mali ya yatima au ya mtu mwenye upungufu wa akili kuitolea Zakaah mali hiyo ikifikia kiwango chake.

 

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amru (Radhwiya Allaahu ‘anhu), anasema kuwa; Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Mwenye kumlea yatima mwenye mali, basi aifanyie biashara mali hiyo na asiiache mpaka ikamalizika kwa kuliwa na Swadaqah (Zakaah)".

 

Anasema Shaykh Sayyid Saabiq katika Fiqhis Sunnah kuwa; Isnadi yake ina udhaifu ndani yake. Akaendelea kusema:

 

“Anasema Al-Haafidh kuwa Hadiyth hii ina ushahidi kuwa ni 'Mursal' iliyorushwa moja kwa moja mpaka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) bila ya kutaja isnadi. Ama Imaam Ash-Shaafi’iy ameikubali (hadithi hii) kwa sababu zipo Hadiyth nyingi zinazoelezea juu ya kuwajibika kwa Zakaah katika mali yoyote ile.  Anasema Imaam At-Tirmidhiy kuwa wanavyuoni wamekhitalifiana juu ya kuwajibika kuitolea Zakaah mali ya yatima,” amemaliza kusema Shaykh Sayyid Saabiq.

 

Share

012-Kutoa Zakaah: Mwenye Deni

 

Kutoa Zakaah: Mwenye Deni

 

Alhidaaya.com

 

Mwenye kumiliki kiwango kinachomwajibisha kutoka Zakaah, na wakati huo huo anadaiwa, kwanza anatoa kiasi cha deni analodaiwa, kisha anailipia Zakaah mali iliyobaki ikiwa bado inafikia kiwango cha kutolewa Zakaah. Ama ikiwa mali iliyobaki haifikii kiwango, basi hatoi Zakaah, kwa sababu wakati huo anahesabiwa kuwa ni mtu fakiri, na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 

"Hatoi Swadaqah (Zakaah) isipokuwa mtu tajiri". [Ahmad]

 

Na amesema:

 

"Ichukuliwa (mali ya Zakaah) kutoka kwa matajiri wao na kurudishiwa mafakiri wao".

 

Share

013-Kutoa Zakaah: Aliyefariki

 

Kutoa Zakaah: Aliyefariki

 

Alhidaaya.com

 

 

Anasema Sayyid Saabiq katika Fiqhis Sunnah kuwa, katika madhehebu ya Maimaam Ash-Shaafi’iy na Ahmad na Abuu Thawr, ni kuwa mtu akifarki na akaacha deni la Zakaah, basi inawajibika katika mali yake kwanza kutolewa deni la Zakaah, tena iwe kabla ya kutimizwa wasia alioacha na kabla ya urithi kugawiwa.

 

Allaah Anasema:

 مِن بَعْدِ وَصِيَّةٍ يُوصِي بِهَا أَوْ دَيْنٍ ۗ

"Baada ya kutoa wasia aliousia (maiti) au kulipa deni". [An-Nisaa: 11]

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Deni la Allaah linastahiki zaidi kulipwa". Na Zakaah ni deni la Allaah.

 

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema:

 

“Mtu mmoja alikuja kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

"Mama yangu amefariki na anadaiwa saumu ya mwezi mzima, je nimlipie?"

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza:

"Mama yako angelikuwa na deni ungemlipia?"

Akasema:

"Ndiyo, ningemlipia".

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

"Basi deni la Allaah linastahiki zaidi kulipwa". [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Share

014-Kutoa Zakaah: Niyah

 

Kutoa Zakaah: Niyah

 

Alhidaaya.com

 

 

Zakaah ni ‘Ibaadah, na kwa ajili hiyo kutia Niyyah ni jambo muhimu kama ilivyo katika ‘Ibaadah yoyote ile. Na Niyah ni kitu cha moyoni na hakina uhusiano na ulimi, na kusudi lake ni kuwa mtu anapotoa Zakaah akusudie kuitoa kwa ajili ya Allaah.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Hakika ya amali yoyote ni kutokana na Niyyah, na mtu hulipwa kutokana na Niyyah yake".

 

Share

015-Kutoa Zakaah: Kutoa Panapowajibika

 

Kutoa Zakaah: Kutoa Panapowajibika

 

Alhidaaya.com

 

 

Inawajibika kuitoa Zakaah wakati wake unapowadia, na haijuzu kuichelewesha isipokuwa kwa dharura inayokubalika.

 

Kutoka kwa Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) amesema kuwa; Nabiy (Swalla Alaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Haichanganyiki mali pamoja na Zakaah isipokuwa itaiangamiza", na katika riwaya nyingine;

 

"Inakuwa ishakuwajibikia katika mali yako kuitolea Zakaah, kisha usiitoe, kwa hivyo (mali ya) haramu (isiyotolewa Zakaah) inaiangamiza (mali ya) halali". [Ash-Shaafi’iy na Al-Bukhaariy katika 'At-Taariykh']

Share

016-Kutoa Zakaah: Kuitanguliza

 

Kutoa Zakaah: Kuitanguliza

 

Alhidaaya.com

 

 

Inajuzu kuitanguliza na kuitoa kabla ya kufikia wakati wake hata kabla ya miaka miwili.

 

Anasema Ash-Shawkaaniy katika kitabu chake 'Naylul-Awtaar';

 

"Wanachuoni wengi kama vile Az-Zuhriy na Al-Hassan Al-Baswriy na Maimaam Ash-Shaafi’iy na Ahmad na Abuu Haniyfah wamejuzisha kuitanguliza Zakaah kabla ya kufikia wakati wake".

 

Ama Imaam Maalik na Sufyaan Ath-Thawriy na baadhi ya Wanachuoni wengine wameona kuwa haijuzu kuitanguliza kabla ya wakati wake, wao wameziegemea zile Hadiyth zinazowajibisha kutoa Zakaah baada ya kukamilika mwaka.

 

Anasema Ibn Rushd:

 

"Ikhtilafu iliyopo baina ya Wanachuoni ni kuwa - Zakaah ni ‘Ibaadah au haki iliyowajibishwa kupewa masikini. Wanaosema kuwa Zakaah ni ‘Ibaadah, wao wameifananisha na Swalaah na wakasema kuwa haiwezekani kutolewa kabla ya kufikia wakati wake.

Ama wale wenye kuona kuwa ni haki iliyowajibika, wamejuzisha kuitoa kabla ya kufikia wakati wake ikiwa mtu mwenyewe amejitolea kufanya hivyo".

 

Ama Imaam Ash-Shaafi’iy ameegema madai yake katika riwaya inayosema kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwahi kuchukua katika mali ya Al-‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na kuitolea Zakaah kabla ya kufikia wakati wake.

 

Share

017-Kutoa Zakaah: Kuomba Du’aa

 

Kutoa Zakaah: Kuomba Du’aa

 

Alhidaaya.com

 

Inapendeza kumuombea dua mtoaji Zakaah, pale anapoitoa.

 

Allaah Anasema:

خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا وَصَلِّ عَلَيْهِمْ إِنَّ صَلاَتَكَ سَكَنٌ لَّهُمْ

Chukua (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) katika mali zao Swadaqah, uwatakase na ziwazidishie kwazo na waombee du’aa (na maghfirah). Hakika du’aa yako ni utulivu kwao. [At-Tawbah: 103]

 

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin Abi ‘Awfiy amesema:

 

“Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapoletewa mali ya Zakaah akisema: "Allaahumma swalliy ‘alayhim". Na baba yangu siku moja alimpelekea mali ya Zakaah akasema: "Allaahumma swalliy ‘alaa aali Abi ‘Awfiy". [Ahmad na wengineo].

 

Imepokelewa kutoka kwa Waail bin Hujr kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuombea mtu mmoja aliyeleta ngamia wa Zakaah akasema:

 

"Allaahumma Baarik fiyhi wa fiy ibilihi". (Allaah mbariki yeye na katika ngamia wake)

 

Anasema Imaam Ash-Shaafi’iy:

 

"Ni Sunnah kwa Imaam anapopokea mali ya Zakaah kumuombea dua mtoaji kwa kumwambia: "Aajaraka Allaahu fiyma a’atwayta, wa baarik laka fiyma abqayta".

 

(Allaah akupe ujira mwema katika ulichotoa na akubarikie katika kilichobaki).

 

Share

018-Kutoa Zakaah: Mali Inayotolewa Zakaah

Mali Inayotolewa Zakaah

 

1.. Dhahabu na Fedha

2. Mazao na Matunda

3. Mali ya Biashara

4. Wanyama wa kufugwa

 

Share

019-Kutoa Zakaah: Dhahabu Na Fedha

 

Kuota Zakaah: Dhahabu Na Fedha

 

Alhidaaya.com

 

 

Allaah Anasema:

 

هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ﴿٣٣﴾ وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلاَ يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللّهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ. يَوْمَ يُحْمَى عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَى بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ هَـذَا مَا كَنَزْتُمْ لأَنفُسِكُمْ فَذُوقُواْ مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ. يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ كَثِيرًا مِّنَ الْأَحْبَارِ وَالرُّهْبَانِ لَيَأْكُلُونَ أَمْوَالَ النَّاسِ بِالْبَاطِلِ وَيَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۗ وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلَا يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ﴿٣٤﴾

Yeye Ndiye Aliyemtuma Rasuli Wake (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kwa mwongozo na Dini ya haki ili Aishindishe juu ya dini zote, japo watakirihika washirikina. Enyi walioamini! Hakika wengi katika Wanazuoni Marabai wa dini (zao) na Wamonaki wanakula mali za watu kwa batili, na wanazuia njia ya Allaah. Na wale wanaorundika dhahabu na fedha na wala hawazitoi katika njia ya Allaah, basi wabashirie adhabu iumizayo.  [ At-Tawbah: 33-34]

 

Kwa hivyo mwenye kumiliki viwili hivyo (Dhahabu au Fedha) ikiwa ni katika mfumo wa pesa au mikufu au vipande (vinoo), ikitimia Niswaab yake na kukamilisha mwaka na akawa hana deni, wala shida yoyote inayokubalika, anawajibika kuitolea Zakaah yake.

 

Wakati Wa Nabiy(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa Sallam)

 

Wakati wa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), watu wa Bara Arabu walikuwa wakifanya biashara zao kwa njia ya kubadilishana bidhaa, na hawakuwa wakitumia pesa isipokuwa wachache sana walioweza kumiliki pesa za dhahabu na za fedha zilizokuwa zikitumika katika nchi za jirani.

 

Pesa zilizotengenezwa kwa dhahabu zilikuwa zikiitwa Dinari, na zilikuwa zikiletwa kutoka nchi za Warumi kama vile Byzantine na nyenginezo, na walikuwa pia wakitumia pesa zilizotengenezwa kwa fedha zilizokuwa zikiitwa Dirham.

 

Kwa vile pesa hizo zilikuwa zikiwafikia zikiwa na uzito mbali mbali, na kiasi mbali mbali, nyengine ndogo ndogo na nyengine kubwa kubwa, na hazikuwa na kiasi maalum wala uzito maalum, kwa hivyo watu wa Makkah hawakuwa wakizitumia kama zinavyotumiwa pesa za kawaida, bali walikuwa wakizipima na kuzipa thamani maalum waliyokubaliana.

 

Miongoni mwa vipimo walivyokuwa wakitumia ilikuwa ratili, ambayo wakati huo ilikuwa na uzito wa wakia kumi na mbili na walikuwa pia wakitumia vipimo vya Mithqaal.

 

Kutokana na kipimo cha Mithqaal, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

 

"Haitolewi Zakaah ikiwa dhahabu haikutimia Mithqaal ishirini."

 

Karatasi za benki (Bank notes) zinazopigwa chapa na serikali tofauti ulimwenguni, hupigwa chapa kulingana na Dhahabu na Fedha inayomiliki serikali hizo, ama sivyo serikali yoyote masikini au yenye madeni ingelipiga chapa idadi ya noti yenye thamani kubwa kuliko dhahabu waliyo nayo na kuweza kulipa madeni yao na kujitajirisha.

 

Niswaab Yake

 

Dhahabu hailipiwi kitu mpaka ifikie Niswaab yake na imilikiwe (Niswaab hiyo) kwa muda wa mwaka (Mwaka wa Kiislam).

 

Niswaab ya dhahabu ni mithqaal 20 au gramu 92 au Tola71/2 au wakia 3. (Baadhi ya Wanachuoniwanasema kuwa Niswaab yake ni gramu 85 au Tola 5 au wakia 2), na hii inatokana na ugumu wa kuweza kukisia bei ya vipimo vilivyokuwa vikitumika wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na vinavyotumika wakati wetu huu. Hapana hitilafu juu ya kiwango cha Mithqaal 20 isipokuwa hitilafu ipo katika kuifasiri Mithqaal katika vipimo vya kisasa.

 

Inapofikia kiwango hicho, na kubaki muda wa mwaka, unaichukua na kuipeleka kuipima kwa sonara au kwa wajuzi, na baada ya kuijua thamani yake unailipia 2.5% (mbili unusu katika mia) ya thamani ya dhahabu yote.

 

Niswaab Ya Dhahabu Ndiyo Niswaab Ya Pesa Za Kawaida.

 

Kwa mfano katika nchi ya UAE, bei ya gramu tisini na mbili ya dhahabu ni Dh. 2575/-

Kwa hivyo hicho ndicho kiwango cha kuanzia kulipia Zakaah. Na dhahabu yako inapofikia kiwango hicho unailipia Dh. 64/- ambayo ni mbili unusu katika mia ya thamani hiyo. Dhahabu inapozidi, na Zakaah yake inaongezeka.

 

Unailipia thamani ya dhahabu tu bila kuhesabu ujira wa mfuo au kazi ya mkono au thamani ya nakshi zake. (Gharama za ufulishaji hazimo).

 

Fedha

 

Niswaab ya fedha ni mithqaal 140 au Tola 36 au wakia 141/2.

Ikifikia kiwango hicho na ikamilikiwa muda wa mwaka, inalipiwa moja katika arubaini au mbili unusu katika mia ya thamani yake.

Share

020-Kutoa Zakaah: Zakaah Ya Deni (Mwenye Kudai)

 

Kutoa Zakaah: Zakaah Ya Deni (Mwenye Kudai)

 

Alhidaaya.com

 

Wanachuoni wameigawa deni katika hali mbili.

 

1. Ikiwa anayedaiwa ni mtu tajiri au mtu muaminifu, deni hilo litachukuliwa mfano wa pesa zilizowekwa dhamana katika benki ambapo wakati wowote mtu anaweza kuzipata au ana uhakika wa kulipwa deni lake.

 

Katika hali hii zipo rai tatu.

 

a) Ya kwanza ni kuwa mwenye kudai anatakiwa ailipie mali hiyo Zakaah yake, juu ya kuwa halazimiki kuilipia mpaka pale atakapozipata na wakati huo atailipia pamoja na Zakaah ya siku zote za nyuma.

b) Ya pili ni kuwa analazimika kuilipia Zakaah yake kila unapotimia mwaka, kwa sababu pesa hizo zitahesabiwa mfano wa pesa zilizowekwa benki, na hii ni kwa sababu aliyekopeshwa ni mtu tajiri au muaminifu kiasi cha kuwa ana uhakika wa kulipwa au wa kuzipata pesa zake hizo wakati wowote ule anapozitaka.

c) Rai ya tatu ni kuwa hazilipii mpaka pale atakapolipwa deni hilo, na hapo atazilipia Zakaah ya mwaka ule mmoja tu.

 

Anasema Imaam Muhammad bin Uthaymiyn (Rahimahu Allaah):

 

"Rai ya mwanzo, nayo ni kuilipia Zakaah ya miaka yote pale atakapozipata pesa zake ni bora zaidi na inakubalika zaidi".

 

2. Ikiwa anayedaiwa ni mtu masikini au mtu asiyekuwa muaminifu, haimuwajibikii mwenye kudai kuzitolea Zakaah pesa hizo mpaka atakapozipata na kubaki nazo muda wa mwaka mzima kisha atazilipia Zakaah ya mwaka huo tu, ambao mali yake hiyo ilibaki kwake kama kawaida ya utoaji wa Zakaah.

 

Anasema Imaam Muhammad bin Uthaymiyn (Rahimahu Allaah):

 

"Haijuzu kumdai au kumlazimisha mtu masikini au kumshitaki na hatimaye kumuingiza jela na kumtenganisha na watu wake ikiwa mtu huyo kweli hana uwezo wa kulipa deni, na ikiwa mtu huyo hafanyi ujanja wa kuchelewesha makusudi, na badala yake tunatakiwa tumsitahamilie mpaka pale Allaah Atakapomfariji.

 

Allaah Anasema:

 

وَإِن كَانَ ذُو عُسْرَةٍ فَنَظِرَةٌ إِلَى مَيْسَرَةٍ وَأَن تَصَدَّقُواْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿٢٨٠﴾ وَاتَّقُواْ يَوْمًا تُرْجَعُونَ فِيهِ إِلَى اللّهِ ثُمَّ تُوَفَّى كُلُّ نَفْسٍ مَّا كَسَبَتْ وَهُمْ لاَ يُظْلَمُونَ ﴿٢٨١﴾

Na ikiwa (mdaiwa) ni mwenye hali ngumu, basi (mdai) angoje mpaka afarijike. Na mkifanya deni kuwa ni swadaqah basi ni khayr kwenu mkiwa mnajua. Na iogopeni Siku mtakayorejeshwa ndani yake kwa Allaah, kisha kila nafsi italipwa kamilifu iliyoyachuma nao hawatodhulumiwa. [Al-Baqarah: 280-281]

 

Mtu akisema:

 

"Pesa zangu kwanini nisizidai?", Anaendelea kusema Imaam Ibn ‘Uthaymiyn,

"Tunamwambia:

Ni kweli pesa zako, lakini wewe mwenyewe ndiye uliyemkopesha pesa hizo. Pale alipokujia kutaka kukukopa ungelimtafutia udhuru wowote ule, kisha ukampa kiasi chochote cha mali ikiwa kama ni msaada (Swadaqah) tu kutoka kwako, basi yasingekukuta haya. Lakini umkopeshe na hali unajuwa kuwa mtu huyu ni masikini, kisha akishindwa kukulipa ukamshitaki, umtie jela na kumtenganisha na mke na watoto wake, jambo hilo ni haramu kabisa na haijuzu kwa Muislam kulitenda". [Mwisho wa maneno ya Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah)].

 

Share

021-Kutoa Zakaah: Zakaah Ya Mapambo

 

Kutoa Zakaah: Zakaah Ya Mapambo

 

Alhidaaya.com

 

 

‘Ulamaa wamekhitalifiana katika kuzitolea Zakaah dhahabu na fedha za mapambo.

 

Wapo waliosema kuwa dhahabu au fedha ya kujipamba inapofikia Niswaab yake lazima itolewe Zakaah yake, na hawa wameegemeza Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema kumwambia mwanamke mmoja aliyemvisha mwanawe mkufu wa dhahabu akamwambia:

 

"Unailipia Zakaah yake?"

Akasema:

"La, hatuilipii"

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

"Huogopi Allaah akakuvalisheni mikufu ya Moto? Zilipie Zakaah yake". [Ahmad]

 

Na pia Hadiyth iliyosimuliwa na Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) aliposema:

 

"Aliingia chumbani kwangu Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaniona nimevaa pete za fedha. Akaniuliza:

"Nini hiki Ee ‘Aaishah?"

Nikamwambia:

"Nimezitengeneza ili nijipambe kwa ajili yako ee Rasuli wa Allaah".

Akasema:

"Unazilipia Zakaah yake?"

Nikasema:

"Hapana."

Akasema:

"Hiyo inatosha kwa (kukupatia adhabu ya) Moto". [Abuu Daawuwd – Ad-Daaraqutniy na Al-Bayhaqiy]

 

Ama wale wanaosema kuwa Dhahabu ya mapambo hailipiwi Zakaah, wao wameegemeza hoja zao katika Hadiyth iliyosimuliwa na Al-Bayhaqiy inayosema:

 

"Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliulizwa juu ya mapambo:

"Yanatolewa Zakaah?

Akasema:

"La, hayatolewi"

Akaulizwa:

"Hata kama thamani yake itafikia Dinari elfu moja?'

Akasema:

"Zaidi" (hata kama zaidi ya thamani hiyo)

 

Na pia Hadiyth iliyomo katika Muwataa, kitabu cha Imaam Maalik inayosema:

 

"Bibi ‘Aaishah alikuwa akiwalea wana wa kaka yake mayatima na walikuwa na mapambo na hakuwa akiyatolea Zakaah.”

 

Atakayezichunguza Hadiyth hizi na zile, ataona kuwa zile zinazolazimisha kuitolea Zakaah dhahabu au fedha ya mapambo ndizo zenye nguvu zaidi na zenye uhakika zaidi kuliko zisizolazimisha - Wa-Allaahu A'lam.

 

Share

022-Kutoa Zakaah: Zakaah Ya Biashara

 

Kutoa Zakaah: Zakaah Ya Biashara

 

Alhidaaya.com

 

Hukmu Yake

 

Wapo baadhi ya Wanachuoni ambao ni wachache sana wanaosema kuwa hapana dalili ya kuwa mali ya biashara inatolewa Zakaah, lakini dalili zilizomo ndani ya Qur-aan na Sunnah zinaleta maana kinyume na rai zao.

 

Allaah Anasema:

خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا وَصَلِّ عَلَيْهِمْ إِنَّ صَلاَتَكَ سَكَنٌ لَّهُمْ

Chukua (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) katika mali zao Swadaqah, uwatakase na ziwazidishie kwazo na waombee du’aa (na maghfirah). Hakika du’aa yako ni utulivu kwao. Allaah ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote. [At-Tawbah - 103]

 

Aayah hii inaleta maana ya ujumla kuwa Zakaah inatakiwa itolewe kutoka katika mali zao (Matajiri), mali ya aina yoyote ile ikiwemo mali ya biashara, bila kufafanua aina ya mali hiyo.

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Ichukuliwe kutoka kwa matajiri wao na kurudishiwa mafakiri wao".

 

Kwa hivyo dalili hizi zinatujulisha kuwa mali yoyote ile, ikiwemo mali ya biashara, lazima itolewe Zakaah, na kwamba Zakaah hiyo ichukuliwe kutoka kwa matajiri, na bila shaka wafanya biashara ni matajiri, na kwamba irudishwe kwa masikini. Muhimu mali hiyo iwe imekifikia kile kiwango cha kutolewa Zakaah (Niswaab) na imekamilisha muda wa mwaka.

 

Namna Ya Kutoa Zakaah Ya Biashara

 

Mwenye kumiliki mali ya biashara iliyofikia Niswaab, akishakamilisha mwaka anatakiwa ahesabu mali yake yote aliyokuwa nayo kwa ajili ya biashara. Kama ni mfaya biashara wa nyumba, basi azihesabu nyumba zake (zile tu alizozitayarisha kwa ajili ya biashara), au ardhi au vyombo vya nyumbani, magari au nguo au biashara ya aina yoyote ile. Atavihesabu vitu alivyokuwa navyo kwa ajili ya biashara pamoja na kuzihesabu pesa zote alizonazo kwa ajili ya biashara kisha atazitolea Zakaah yake, nayo ni mbili unusu katika mia au moja katika arubaini.

Atafanya hesabu hiyo bila kujali kama wakati wowote ule ndani ya mwaka ule pesa hizo zilipungua au kuongezeka.

 

Kumbuka

 

Ikumbukwe kuwa vitakavyohesabiwa (katika Zakaah ya Biashara) ni vitu vilivyotayarishwa kwa ajili ya biashara tu.

 

Kwa mfano mtu anamiliki magari hata yakifikia idadi ya magari kumi au zaidi, au atataka kuuza gari lake mwenyewe kwa ajili ya kulibadilisha tu na kununua gari jengine au ardhi au nyumba au chochote kile, ikiwa anataka kuuza kwa ajili ya kutaka kununua kingine badala yake au kwa ajili ya mahitajio mengine yasiyokuwa ya kibiashara, basi mali hiyo haitolei Zakaah ya biashara, na hii ni kwa sababu Niyah ya kuviuza vitu hivyo si kwa ajili ya biashara.

 

Kumbuka pia kuwa Zakaah inatolewa kutokana na asili ya chochote kilichoongezeka kutokana mali hiyo wakati wowote ule katika mwaka. Ama kile kilichoongezeka kutokana na asili nyingine, basi mwaka wake unaanza kuhesabiwa kuanzia siku ile iliyoongezeka mali hiyo.

 

Kwa mfano:

 

Mfanya biashara alikuwa akiendela kupata faida katika biashara yake na kufikia kiasi cha Shilingi laki kumi, kisha katika mwezi wa mwisho au hata katika siku ya mwisho kabla ya kutimia mwaka, akapata faida kiasi cha Shilingi laki saba, pesa zote hizo zitahesabiwa pamoja na Zakaah ya biashara ya mwaka huo, kwa sababu asili yake (faida iliyopatikana) inatokana na biashara hiyo anayoitolea Zakaah.

 

Mfano mwingine:

 

Mfanya biashara alikuwa akiendelea kupata faida katika biashara yake na kufikia kiasi cha shilingi laki kumi, kisha katika mwezi wa kumi na mbili au katika siku ya mwisho au siku yoyote ile ndani ya mwaka huo kabla ya kuingia muda wa kulipa Zakaah ya mwaka ule, mtu huyo akarithi mali au pesa kutoka kwa jamaa yake aliyefariki kiasi cha Shilingi milioni moja.

 

Pesa hizo alizorithi hazitohesabiwa katika Zakaah ya mwaka huo, bali ataanza kuzihesabia mwaka wake mpya kuanzia siku ile alizozipata pesa hizo. Kwa sababu asili ya pesa hizo hazitokani na biashara ile anayoitolea Zakaah, bali inatokana na asili nyingine, ambayo ni urithi.

 

Wenye Kupokea Mishahara

 

Kwa kawaida mwenye kupokea mshahara pesa zake huongezeka na kupungua katika miezi mbali mbali. Kwa vile itakuwa vigumu kwake kuweka hesabu ya kila mwezi pale zinapokamilisha Niswaab au kuongezeka pale zinapopungua, wanavyuoni wakasema kuwa mtu huyo ataanza kuuhesabu mwaka wake kuanzia siku ile aliyoweza kutimiza Niswaab, na kuanzia mwezi huo, atakuwa akiitolea Zakaah mali yake kila anapotimiza mwaka.

Share

023-Kutoa Zakaah: Zakaah Ya Mazao

 

Kutoa Zakaah: Zakaah Ya Mazao

 

Alhidaaya.com

 

Allaah Amewajibisha kuyatolea Zakaah mazao Aliposema:

 

وَهُوَ الَّذِي أَنشَأَ جَنَّاتٍ مَّعْرُوشَاتٍ وَغَيْرَ مَعْرُوشَاتٍ وَالنَّخْلَ وَالزَّرْعَ مُخْتَلِفًا أُكُلُهُ وَالزَّيْتُونَ وَالرُّمَّانَ مُتَشَابِهًا وَغَيْرَ مُتَشَابِهٍ كُلُواْ مِن ثَمَرِهِ إِذَا أَثْمَرَ وَآتُواْ حَقَّهُ يَوْمَ حَصَادِهِ

Naye (Allaah) Ndiye Ambaye Aliyezalisha mabustani yanayotambaa na yasiyotambaa. Na mitende na mimea yakitofautiana kwa ladha yake, na zaytuni na makomamanga yanayoshabihiana na yasiyoshabihiana. Kuleni katika matunda yake yanapotoa mazao na toeni haki yake (Zakaah) siku ya kuvunwa kwake. [Al-An’aam: 141]

 

Katika kuifasiri Aayah hii amesema Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu):

 

'Haki yake, ni Zakaah yake iliyofaradhishwa".

 

Wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Zakaah ya mazao ilikuwa ikitolewa katika Mahindi, Ngano, Mtama, Tende na Zabibu na wengine wakaongeza 'Mchele' na wengine wakasema kuwa Zakaah ya mazao inatolewa katika chakula chochote kile kinachoweza kubaki muda mrefu kama vile mwaka au zaidi bila kuharibika.

 

Matunda, hayakuwa yakitolewa Zakaah isipokuwa Tende na Zabibu. Matunda mengine hayakuwa yakitolewa Zakaah isipokuwa kama matunda hayo ni kwa ajili ya biashara, basi hapo itatolewa Zakaah ya biashara na si Zakaah ya Mazao. Zakaah ya Mazao inatolewa siku ya kuvuna na kabla ya kuuzwa wala kuliwa na si lazima itimie mwaka.

 

Niswaab Ya Mazao

 

Mazao hayatolewi Zakaah mpaka yatimie Wiski tano yakiwa safi bila magamba. Kama hayajasafishwa, basi lazima yatimie wiski kumi.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Chini ya Wiski tano haitolewi Zakaah". [Imaam Ahmad na Al-Bayhaqiy]

 

Wiski 5 ni sawa na pishi 300, kwa sababu wiski moja ni sawa na pishi sitini kwa pishi iliyokuwa ikitumika wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na pishi sitini mara tano ni sawa na pishi mia tatu.

 

Kwa vipimo vya kisasa:

 

"Niswaab ya mazao ni Wisqi 5. Moja ni kilo 60 yaani kilo 300. Kilo moja ni ratili 13/4 (ratili mbili kasorobo) (300 mara 13/4 = ratili 525).

Kilo karibu ni sawa na pishi ya mbao (vibaba vinne)."

 

Kwa hivyo mazao yakifikia pishi 300 au ratili 525 yanakuwa yamefikia Niswaab yake (kiwango chake) na yatatolewa Zakaah yake ambayo ni moja juu ya kumi (one tenth), hii ikiwa mazao hayo yanapata maji yake bila kuyahangaikia, yaani kama vile kunyeshewa na mvua au maji ya mito au chemchem n.k.

 

Ama ikiwa mkulima anayatilia maji yeye mwenyewe kwa kuyahangaikia maji hayo, basi Zakaah yake itapungua na itakuwa ni nusu ya moja juu ya kumi.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Kilichonyeshewa na mvua au maji yanayopita (waadi) au yaliyotwama (Zakaah yake ni) moja katika kumi na kilichomiminiwa maji nusu ya moja katika kumi". [Al-Bukhaariy na wengineo].

 

Allaah Ameamrisha kuitoa Zakaah ya mazao; "Siku ya kuvuna kwake", na maana yake ni; kabla hakijaliwa wala kugawiwa chochote kile ndani yake, na ikiwa mtu amekwishafanya hivyo kwa kusahau, basi itambidi akisie kile alichotoa au alichouza na akitolee Zakaah yake.

 

Ama kile alichokula mkulima kabla ya kuvuna, hakimo katika hesabu. Alipoulizwa Imaam Ahmad juu ya wanachokula wenye ardhi kabla ya mavuno alisema:

 

"Hapana neno ikiwa atakula katika mazao yake kiasi anachohitajia".

 

Anasema Shaykh Sayyid Saabiq katika Fiqhis Sunnah:

 

"Kauli hii pia imetamkwa na Imaam Ash-Shaafi’iy na Al-Layth na Ibn Hazm'.

Ama Imaam Malik na Imaam Abuu Haniyfah wanasema:

"Anachokula mtu katika mazao yake kabla ya mavuno atahesabiwa katika Niswaab" [Mwisho wa maneno ya Sayyid Saabiq].

 

Toeni Katika Vizuri

 

Baadhi ya wenye kumiliki mitende walikuwa wakitoa Zakaah yao ya mazao katika tende au zabibu au mazao yasiyokuwa mazuri. Walikuwa wakichagua mazao yasiyokuwa mazuri na kuyatolea Zakaah, na yale mazuri walikuwa wakichukua wenyewe.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ أَنفِقُواْ مِن طَيِّبَاتِ مَا كَسَبْتُمْ وَمِمَّا أَخْرَجْنَا لَكُم مِّنَ الأَرْضِ وَلاَ تَيَمَّمُواْ الْخَبِيثَ مِنْهُ تُنفِقُونَ وَلَسْتُم بِآخِذِيهِ إِلاَّ أَن تُغْمِضُواْ فِيهِ وَاعْلَمُواْ أَنَّ اللّهَ غَنِيٌّ حَمِيدٌ

Enyi walioamini! Toeni katika vizuri mlivyochuma na katika ambavyo Tumekutoleeni kutoka katika ardhi. Na wala msikusudie vibaya kutoka humo mkavitoa na hali nyinyi wenyewe si wenye kuvichukuwa isipokuwa kuvifumbia macho. Na jueni kwamba hakika Allaah ni Mkwasi, Mwenye kustahiki kuhimidiwa. [Al-Baqarah: 267]

 

Anasema Imaam Ash-Shawkaaniy:

 

"Hii ni dalili kuwa, haijuzu mtu kuwapa watu Zakaah katika yale mazao mabovu na yasiyokuwa mazuri."

 

Share

024-Kutoa Zakaah: Zakaah Ya Wanyama Wa Kufugwa

 

 

Zakaah Ya Wanyama Wa Kufugwa

 

Alhidaaya.com

 

 

Wanyama wanaofugwa wanalazimika kutolewa Zakaah kwa masharti yafuatayo:

1.  Lazima watimie Niswaab

2.  Wakamilishe mwaka

3.  Wawe wanyama wa kufugwa.

 

Wanyama wasiokuwa wa kufugwa kama vile wa kupandwa au wanaotumiwa kwa kubeba mizigo au kwa kilimo n.k. Hawa hawatolewi Zakaah.

Wanyama wanaotolewa Zakaah ni Ngamia, Ng'ombe, Mbuzi na Kondoo.

 

Zakaah Ya Ngamia

 

Ngamia hawatolewi Zakaah mpaka watimie watano. Wakitimia watano wa kufugwa hadi tisa na kutimiza mwaka chini ya milki ya mtu, basi atawatolea mbuzi mmoja.

 

Wakitimia ngamia 10 mpaka 14 atawatolea mbuzi wawili.

 

Na hivyo hivyo kila wakizidi ngamia watano ataongeza mbuzi mmoja.

Wakitimia ngamia 25 mpaka 35 atatoa mtoto wa ngamia jike aliyekamilisha mwaka na kuingia mwaka wa pili au mtoto wa ngamia dume aliyekamilisha mwaka wa 2 na anaingia wa 3.

 

Kuanzia ngamia 36 mpaka 45 atatoa mtoto wa ngamia jike aliyekamilisha miaka 2 na keshaingia wa 3.

 

Kuanzia ngamia 46 mpaka 60 atatoa mtoto wa ngamia jike aliyekamilisha miaka 3 na kuingia wa 4.

 

Kuanzia ngamia 61 mpaka 75 atatoa mtoto wa ngamia jike aliyekamilisha miaka 4 na kuingia mwaka wa 5.

 

Kuanzia ngamia 76 mpaka 90 atatoa watoto wa ngamia wawili jike waliokamilisha miaka miwili na kuingia wa tatu.

 

Kuanzia ngamia 91 mpaka 120 atatoa watoto wa ngamia wa kike wawili waliotimia miaka 3 na kuingia mwaka wa 4.

 

Wakizidi kuliko hapo, basi katika kila ngamia 40 atatoa mtoto wa ngamia wa kike aliyekamilisha miaka 2 na kuingia wa 3. Na katika kila ngamia 50 waliozidi kuliko hapo atatoa mtoto wa ngami wa kike aliyekamilisha miaka 3 na kuingia wa nne.

 

Anasema Sayyid Saabiq katika Fiqhis Sunnah:

"Hawatolewi Zakaah ngamia dume ikiwa wapo wa kike, lakini anatolewa mtoto wa ngamia wa kiume aliyetimia miaka miwili na kuingia wa tatu ikiwa hajapatikana wa kike aliyekamilisha mwaka na kuingia wa pili.

 

 

Zakaah Ya Ng’ombe

 

Ng'ombe hawatolewi Zakaah mpaka watimie 30 wa kufugwa. Wanapotimia 30 mpaka 39 wa kufugwa na kukamilisha mwaka, atatolewa ndama aliyekamilisha mwaka mmoja.

 

Wakitimia ng'ombe 40 mpaka 59 atatolewa ndama asiyepungua umri wa miaka miwili.

 

Wakitimia ng'ombe 60 mpaka 79 atatolewa ndama wawili wa mwaka mmoja.

 

Kutoka hapo, kila wakizidi ng'ombe 30, ataongeza kutoa ndama wa mwaka mmoja.

 

Na kila wakizidi ng'ombe 40 atawatolea ndama wa miaka miwili.

 

 

Zakaah Ya Mbuzi

 

Mbuzi hawatolewi Zakaah mpaka watimie 40, na wakitimia arubaini mpaka 120 wa kufugwa na kukamilisha mwaka kwa mwenye kuwamiliki, atawatolea mtoto wa mbuzi wa mwaka mmoja.

 

Hatowatolea tena mpaka wafikie idadi yao mbuzi 121.

 

Wakiongezeka na kutimia 121 mpaka 200, atawatolea mtoto wa miaka miwili.

 

Kuanzia mbuzi 201 mpaka 300 atawatolea kondoo watatu.

 

Wakizidi kuliko mbuzi 300, basi atawatolea kondoo mmoja katika kila mbuzi mia waliozidi.

 

Inaruhusiwa pia kutoa mbuzi badala ya kondoo.

 

Wanyama Wengine

 

Wanyama wengine wasiokuwa hawa kama vile farasi, nyumbu, punda na wengineo, hawatolewi Zakaah isipokuwa kama ni kwa ajili ya biashara.

  

 

Share

025-Kutoa Zakaah: Zakaah Ya Madini Ya Kale

Zakaah Ya Madini Ya Kale

 

Madini inayotolewa ardhini kama vile petroli, gesi, shaba, chuma n.k, hivi vyote havitolewi Zakaah, isipokuwa dhahabu na fedha tu na tushaelezea hapo mwanzo namna ya kutoa Zakaah yake. Ama vilivyobaki vinatolewa Zakaah ya biashara baada ya kuchimbuliwa au kutolewa na kuuzwa.

 

Share

026-Kutoa Zakaah: Zakaatul Fitwr

 

Kutoa Zakaah: Zakaatul Fitwr

 

Alhidaaya.com

 

 

Imefaridhishwa katika mwezi wa Sha'abani mwaka wa 2 baada ya Hijrah (baada ya kuhamia Madiynah). Rasuli wa wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifaridhisha Zakaatul Fitwr ili iitakase saumu kutokana na dhambi ndogo ndogo zilizopatikana ndani ya mazungumzo na matendo. Na wakati huo huo Zakaah hiyo iwe msaada kwa mafakiri na wasiojiweza katika kuisherehekea Sikukuu.

 

 

Imepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema:

"Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifaridhisha Zakaah ya Fitwr kwa ajili ya kumtakasa aliyefunga kutokana na dhambi ndogo ndogo za mazungumzo na matendo, na ili wafaidike masikini. Atakayeitoa kabla ya Swalaah (ya 'Iyd) inakubaliwa kama Zakaah ya Fitwr na atakayeitoa baada ya Swalaah inakubaliwa kama Swadaqah ya kawaida." [Abuu Daawuwd – Ibn Maajah na Ad-Daaraqutniy]

 

Alikuwa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akitoa Zakaah ya Fitwr siku ya mwisho ya mwezi wa Ramadhwaan kabla ya Swalaah ya Idi kuswaliwa. [Abuu Daawuwd na Ibn Maajah na Al-Hakim]

 

 

Kila aliyefunga Mwezi wa Ramadhwaan mwenye kumiliki chakula cha kumtosha kwa muda wa siku moja, inamwajibikia kutoa Zakaatul Fitwr, nayo ni pishi ya tende au pishi ya ngano au pishi ya shaiyri. Anatakiwa atowe kwa ajili yake na kwa ajili ya kila anayemtegemea kama vile wanawe, wakeze nk. na kuwapa masikini ili nao wapate kufurahi katika Siku ya Sikukuu.

Kwa vipimo vya kisasa, pishi moja ya mbao iliyokuwa ikitumika wakati wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kiasi cha kilo 2.

 

Zakaah hii ni wajibu kwa kila Muislam mdogo na mkubwa, mwanamume au mwanamke.

 

Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:

"Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amefaridhisha kwa kila mtu kutoa Zakaatul Fitwr katika mwezi wa Ramadhwaan, pishi ya tende (au) pishi ya shaiyri, ikiwa yeye ni mtumwa au mtu aliye huru, mwanamume au mwanamke, mdogo au mkubwa miongoni mwa Waislam". [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Hikmah Yake

 

Zakaatul Fitwr ilifaridhishwa katika mwezi wa Sha'baan mwaka wa pili baada ya Hijrah kwa ajili ya kumtwahirisha aliyefunga kutokana na makosa yoyote yale aliyotenda katika mwezi wa Ramadhwaan pale alipokuwa amefunga, kama vile mazungumzo ya upuuzi au madhambi, na wakati huo huo Zakaah hiyo itawafaa masikini na wahitaji ili nao wapate kufurahi pamoja na Waislam wenzao siku ya Sikukuu.

 

 

Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:

 

"Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amefaridhisha Zakaatul Fitwr kwa ajili ya kumtahirisha aliyefunga kutokana na maneno ya upuuzi au madhambi madogo madogo na ili masikini nao wapate chakula. Atakayeitoa (Zakaah hiyo) kabla ya Swalaah (ya 'Iyd) inakubaliwa Zakaah yake, ama atakayeitoa baada ya Swalaah (ya 'Iyd), itahesabiwa kama ni Swadaqah ya kawaida tu". [Abuu Daawuwd na Ibn Maajah na Ad-Daaraqutniy]

 

Mwenye Kuitoa

 

Anayeitoa Zakaah hiyo ni mtu aliyefunga. Anajitolea yeye mwenyewe, mkewe na watoto wake wanaomtegemea na anawatolea pia wote wale wanaomtegemea wakiwemo watumishi wake.

 

Kiasi Chake

 

Iliyowajibishwa katika Zakaatul Fitwr ni pishi ya ngano au ya shaiyri au ya tende au zabibu au mchele au mahindi na vinginevyo vilivyo na mfano huo katika vyakula.

 

Imaam Abuu Haniyfah peke yake amejuzisha kutoa pesa zenye thamani hiyo badala ya kutoa nafaka panapo udhuru

 

Wakati Wa Kuitoa

 

Wanachuoni wengi wamekubalina kuwa Zakaatul Fitwr itolewe katika Ramadhwaan ya mwisho, lakini wamekhitalifiana juu ya wakati maalum unaowajibika kuitoa.

 

Wapo waliosema kuwa wakati unaowajibika kuitoa ni pale jua la Ramadhwaan ya mwisho linapozama, na wengine wakasema kuwa wakati wake ni kuanzia baada ya kuingia alfajiri ya siku ya Sikukuu.

 

Kutokana na hitilafu hii tunapata faida ya kuwajibika kumtolea Zakaah hiyo mtoto aliyezaliwa kabla ya kuingia alfajiri ya siku ya Sikukuu na baada ya jua kuzama, je mtoto huyo anatolewa Zakaah?

 

Kwa wale wenye kufuata rai kuwa wakati wa kuitoa Zakaah hiyo ni pale jua la siku ya Ramadhwaan ya mwisho kuzama, mtoto huyo hatolewi Zakaah kwa sababu amezaliwa baada ya kumalizika wakati wa kuwajibika, na kwa wenye kufuata rai ya pili, kwa sababu amezaliwa kabla ya wakati unaomwajibika.

 

Kuitanguliza

 

Wanachuoni wengi wanakubali kuwa Zakaatul Fitwr inaweza kutangulizwa na kutolewa kabla ya wakati wake kwa siku moja au mbili.

 

Hadiythi iliyopokelewa kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) inasema:

 

"Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuamrisha kuitoa Zakaatul Fitwr kabla ya watu kutoka msikitini (katika Swalaah ya ‘Iyd)".

 

Anasema Naafi’ (Radhwiya Allaahu ‘anhu):

"Ibn ‘'Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akiitoa kwa siku moja au siku mbili kabla ya Siku ya Sikukuu".

 

Ama zaidi ya hapo, Wanachuoni wamekhitalifiana.

 

Imaam Abuu Haniyfah amesema:

"Inaweza kutolewa wakati wowote ule katika mwezi wa Ramadhwaan".

 

Imaam Ash-Shaafi’iy amesema:

"Inajuzu kuitoa (hata) katika siku za mwanzo za mwezi wa Ramadhwaan".

 

Imaam Maalik amesema:

"Inajuzu kutanguliza kwa siku moja au mbili kabla ya Sikukuu".

 

Lakini Wanachuoni wote wamekubaliana kuwa haijuzu kuiahirisha na kuitoa baada ya ‘Iyd.

 

Share

027-Kutoa Zakaah: Swadaqah

 

Kutoa Zakaah: Swadaqah

 

Alhidaaya.com

 

Swadaqah

Muislam anaipa mali yake mtazamo wa aina nyingine kabisa tofauti na asiyekuwa Muislam, kwani dini ya Kiislam inampa kila mtu haki ya kutafuta mali na kufanya biashara ya halali na kuwa tajiri anayeweza kumiliki mali nyingi. Isipokuwa baada ya kuimiliki mali hiyo, analazimika kuwapa maskini Zakaah, ambayo ni haki yao maalum waliyopangiwa na Mola wao Subhanaahu wa Ta’aalaa.

 

Wakati huo huo Muislam anatakiwa ajipatie thawabu nyingi zaidi na ajiepushe na shari nyingi pamoja na kuwasaidia ndugu na jamaa zake, na masikini waislamu wenzake wenye kuhitaji, kwa kutoa kiasi kingine katika mali zao kwa hiari yao wenyewe na kwa kiasi anachokitaka mwenyewe, na hii inaitwa 'Swadaqah'.

 

Kinyume na njia inayotumika katika nchi za Kikoministi za kuwanyang'anya matajiri mali zao kwa nguvu na kuwapa masikini, kitendo cha dhulma na cha ufisadi, kwa sababu binaadamu kwa kawaida wanakhitalifiana katika ujuzi na katika jitihada zao, na kwa ajili hiyo lazima wahitalifiane katika ujira na mapato yao, kwani katika kuwafanya watu wote wawe sawa katika mapato, utakuwa unamweka katika daraja moja mvivu na mwenye kujitahidi, hodari na asiyekuwa hodari, mtaalamu na asiyekuwa mtaalamu.

 

Hii ikiwa mali hiyo wanayonyang'anywa matajiri wanapewa kweli masikini na wale wanaostahiki, na ikiwa watu wote watakuwa sawa kweli, lakini uhakika wa mambo umethithibitisha kuwa yanayotendeka ni kinyume kabisa na maneno yao, kwani wao huwanyang'anya mali matajiri na kuwapa viongozi wa vyama vyao pamoja na vibaraka wao.

 

Allaah Anasema:

مَّا أَفَاء اللَّهُ عَلَى رَسُولِهِ مِنْ أَهْلِ الْقُرَى فَلِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ وَلِذِي الْقُرْبَى وَالْيَتَامَى وَالْمَسَاكِينِ وَابْنِ السَّبِيلِ كَيْ لَا يَكُونَ دُولَةً بَيْنَ الْأَغْنِيَاء مِنكُمْ

Ngawira Aliyotoa Allaah kwa Rasuli Wake kutoka kwa watu wa hivi vijiji ni kwa ajili ya Allaah na Rasuli na kwa ajili ya  jamaa wa karibu, na mayatima, na masikini na msafiri aliyeharibikiwa, ili isiwe mzunguko wa zamu baina ya matajiri tu miongoni mwenu.

[Al-Hashr: 7]

 

Allaah katika Aayah hii anatujulisha kuwa jamaa na mayatima na masikini na wasafiri walioharibikiwa wana haki zao katika mali zetu, na anawakataza matajiri wasiifanye mali ikawa kinyang'anyiro baina yao tu na kusahau haki za wengine.

 

Muislam pia anatakiwa aitumie mali yake katika kuijenga akhera yake na kujitayarishia Jannah yake.

 

Allaah Anasema:

وَابْتَغِ فِيمَا آتَاكَ اللَّهُ الدَّارَ الاخِرَةَ وَلَا تَنسَ نَصِيبَكَ مِنَ الدُّنْيَا وَأَحْسِن كَمَا أَحْسَنَ اللَّهُ إِلَيْكَ وَلَا تَبْغِ الْفَسَادَ فِي الاَرْضِ إِنَّ اللَّهَ لَا يُحِبُّ الْمُفْسِدِينَ

Na tafuta katika yale Aliyokupa Allaah makazi ya Aakhirah. Na wala usisahau fungu lako katika dunia. Na fanya ihsaan kama Alivyokufanyia Allaah ihsaan, na wala usitake ufisadi ardhini. Hakika Allaah Hapendi mafisadi. [Al-Qaswasw: 77]

 

Haya ndiyo mafundisho ya Kiislam yaliyo kinyume kabisa na mafundisho ya mafisadi wanaojishughulisha na kukusanya mali tu na kurimbika, na wakati huo huo yanatufundisha kuwa Musilam hatakiwi abaki msikitini tu akifanya ‘Ibaadah bila kujishughulisha na elimu pamoja na kufanya biashara, na kuwaachia makafiri peke yao katika uwanja wa elimu na biashara na viwanda, na kwa ajili hiyo wanapata nguvu ya kututawala kiuchumi na kielimu, bali Muislam anatakiwa asiisahau pia sehemu yake ya dunia.

 

Allaah Anasema:

وَلا تَنسَ نَصِيبَكَ مِنَ الدُّنْيَا وَأَحْسِن كَمَا أَحْسَنَ اللَّهُ إِلَيْكَ

Na tafuta katika yale Aliyokupa Allaah makazi ya Aakhirah. Na wala usisahau fungu lako katika dunia. Na fanya ihsaan kama Alivyokufanyia Allaah ihsaan, [Al-Qaswasw: 77]

 

Dini ya Kiislam inatutaka tuwe msitari wa mbele katika kutoa, na Allaah amewaahidi khayr nyingi wale wanaotoa katika njia Yake.

 

Allaah Anasema:

مَّثَلُ الَّذِينَ يُنفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ فِي سَبِيلِ اللّهِ كَمَثَلِ حَبَّةٍ أَنبَتَتْ سَبْعَ سَنَابِلَ فِي كُلِّ سُنبُلَةٍ مِّئَةُ حَبَّةٍ وَاللّهُ يُضَاعِفُ لِمَن يَشَاء وَاللّهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ

Mfano wa wale wanaotoa mali zao katika njia ya Allaah ni kama mfano wa punje moja ya mbegu iliyotoa mashuke saba, katika kila shuke kuna punje mia. Na Allaah Humzidishia Amtakaye; na Allaah ni Mwenye wasaa, Mjuzi wa yote. [Al-Baqarah: 261]

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

 

"Hakika ya Swadaqah inazima ghadhabu ya Rabb na inamuondolea maiti adhabu" [At-Tirmidhiy]

 

Na akasema:

 

"Haipiti asubuhi wanayoiamkia watu, ila Malaika wawili wanateremka. Mmoja wao anasema: "Allaah muongezee mtoaji badala ya kile anachokitoa". Na mwengine anasema: "Allaah mharibie mali yake (usiite baraka) aliyeacha kutoa ".  [Muslim]

 

Aina Za Swadaqah

Swadaqah haina maana ya kutoa pesa tu au kumsaidia mtu, bali Swadaqah ziko aina nyingi sana.

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Kila Muislam anatakiwa atoe Swadaqah".

Wakasema:

"Ee Rasuli wa Allaah, asiyekuwa na mali (je)?"

Akasema:

"Afanye kazi kwa mikono yake, ajisaidie nafsi yake kisha atoe Swadaqah".

Wakasema:

"Ikiwa hajapata?"

Akasema:

"Amsaidie mwenye shida".

Wakasema:

"Asipompata?"

Akasema:

"Afanye mema na aache shari, kwani akifanya hivyo anaandikiwa (thawabu ya) Swadaqah".

[Al-Bukhaariy na wengineo]

 

Na katika riwaya nyingine amesema:

"Kila siku jua linapochomoza nafsi inaandikiwa juu ya kila inachotenda (katika thawabu ya) Swadaqah. Katika hayo ni kuwapatanisha wawili wanaogombana (anaandikiwa mtu thawabu ya kutoa) Swadaqah. Akimsaidia mtu kumnyanyua ili aweze kumpanda mnyama wake, anaandikiwa Swadaqah, akimnyanyulia mzigo wake, Swadaqah, kuondoa udhia barabarani, Swadaqah, neno jema, Swadaqah, na kila hatua anayokwenda msikitini Swadaqah". [Ahmad na wengineo]

 

Na akasema:

"Kati yenu kama yupo mwenye kuuogopa moto, basi atoe Swadaqah walau kwa nusu ya tende, na asiyepata, basi kwa neno jema”. [Ahmad na Muslim]

 

Na akasema:

"Siku ya Qiyaamah Allaah Atasema:

"Ee mwana Aadam, niliumwa (kwa nini) hukunitembelea?"

Atasema (mwana Aadam):

"Ee Rabb, vipi nitakutembelea na wewe ni Mola wa Ulimwengu?"

Atasema:

"Hukujua kuwa mja wangu fulani alikuwa akiumwa na hukumtembelea? Ama ungelimtembelea, ungelinikuta kwake. Ee mwanaadamu nimekuomba chakula na wewe hukunilisha?"

Atasema:

"Ee Rabb wangu, vipi nitakulisha na wewe ni Rabb wa ulimwengu wote?"

Atasema:

"Hukujuwa kuwa fulani alikuomba chakula na hukumpa. Huelewe kuwa ungelimpa chakula, ungelikikuta kwangu?

Ee mwanaadamu, nilikuomba maji hukunipa".

Atasema:

"Ee Rabb wangu, vipi nitakunywesha nawe ni Rabb wa Ulimwengu wote?"

Atasema:

"Mtu fulani alikuomba maji, na wewe hukumpa. Ama ungelimpa ungeyakuta hayo kwangu".

[Muslim]

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema pia:

"Mtu hapandi kitu au halimi kitu kisha mwana Aadam akala katika mazao hayo au mnyama au chochote ila ataandikiwa kwa ajili yake Swadaqah". [Ahmad na At-Tirmidhiy]

 

Na akasema:

"Kila wema ni Swadaqah, na katika wema ni kumkabili mwenzio kwa uso wa bashasha… (uso mkunjufu)." [Ahmad na At-Tirmidhiy]

 

Wenye Kustahiki Zaidi

Watu wako, mkeo na watoto wako pamoja na ndugu zako wa nasaba ndio wanaoistahiki zaidi Swadaqah yako.

 

Nabiy(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Mmoja wenu akiwa fakiri, basi ajitosheleze nafsi yake, kinachozidi awape watoto wake, kinachozidi, awape ndugu zake wa nasaba, na kikizidi basi atoe huku na kule". [Ahmad na Muslim]

 

Hukumu ya Swadaqah inahitilafiana na ya Zakaah, kwani mali ya Zakaah haijuzu kupewa asiyekuwa Muislam, lakini Swadaqah anaweza kupewa asiyekuwa Muislam.

 

Allaah Anasema:

وَيُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلَى حُبِّهِ مِسْكِينًا وَيَتِيمًا وَأَسِيرًا

Na wanalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini na mayatima na mateka. [Ad-Dahar: 8]

 

Neno lililotumika kwa 'wafungwa', katika aya hii ni 'Asiyran', na maana yake ni mateka wa kivita ambaye bila shaka ni kafiri aliyetekwa baada ya kupigana vita dhidi ya Waislam, lakini juu ya hivyo Allaah anawasifia Waislam wanaowalisha chakula wafungwa hao.

 

Kuiharibu Swadaqah

Haijuzu kumsimbulia au kumdharau anayepokea Swadaqah kwa sababu kilichomfanya akubali kuipokea Swadaqah hiyo ni umasikini wake, na mtu kumtakabaria masikini ni dhambi kubwa sana, na anapofanya hivyo thawabu zake zinapotea bure.

Allaah Anasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ لاَ تُبْطِلُواْ صَدَقَاتِكُم بِالْمَنِّ وَالأذَى كَالَّذِي يُنفِقُ مَالَهُ رِئَاء النَّاسِ وَلاَ يُؤْمِنُ بِاللّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ

Enyi walioamini! Msibatilishe swadaqah zenu kwa masimbulizi na udhia kama yule ambaye anatoa mali yake kwa kujionyesha kwa watu wala hamwamini Allaah na Siku ya Mwisho.

[Al-Baqarah: 264]

 

 

Kutoa Katika Mali Ya Haramu

 

Allaah haikubali Swadaqah ikiwa inatokana na mali ya haramu. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Enyi watu! Allaah ni mzuri na hakubali isipokuwa kizuri tu".

 

Imesimuliwa kuwa siku moja mtu mmoja aliiba tufaah kisha akaliuza, na pesa alizopata akawagawia masikini.

 

Habari zilipomfikia Qaadhi wa mji huo, akamwita na kumuuliza:

"Kwa nini umeiba kisha ukazigawa Swadaqah pesa za mali ya wizi?"

Yule mtu akajibu:

"Kwa sababu Allaah Anasema:

مَن جَاء بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا وَمَن جَاء بِالسَّيِّئَةِ فَلاَ يُجْزَى إِلاَّ مِثْلَهَا

Atakayekuja kwa ‘amali njema basi atapata (thawabu) kumi mfano wa hiyo. Na Atakayekuja kwa ovu basi hatolipwa ila mfano wake... [Al-An’aam: 160]

 

Kwa hivyo, akaendekelea kusema mtu Yule aliyeiba tufaa: ‘Kutokana na aya hii, mimi nilipoiba tufaa nilifanya kitendo kibaya nikalipwa dhambi moja tu sawa na tufaa moja nililoiba, lakini nilipowagawia masikini nilifanya kitendo chema nikalipwa mara kumi, na thawabu 10 nilizozipata kwa kuligawa tufaa lile,ukitoa ile dhambi moja ya kuiba, nitabakiwa na thawabu tisa"

Qaadhi akamwambia:

"Lakini umesahau jambo moja ewe ndugu Muislam, (Allaah ni mwema, na hakubali isipokuwa chema tu).”

 

Kuwasaidia Wanyama

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema kuwaambia Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum):

"Mtu mmoja aliyekuwa akitembea, alishikwa na kiu, akaona kisima mbele yake, akateremka na kunywa maji ndani yake kisha akatoka. Alipokuwa akitoka alimuona mbwa akihema kwa kiu. Yule mtu akasema; "Bila shaka mbwa huyu ameshikwa na kiu kama nilivyoshikwa mimi. Akateremka (tena) kisimani, akajaza maji kiatu chake, kisha akamshika kichwa chake mbwa yule na kumnywesha.

Akashukuriwa na Allaah na kughufuriwa".

Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhu) wakasema:

"Hata katika wanyama tunapata thawabu?"

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

"Katika kila chenye uhai mna thawabu". [Al-Bukhaariy]

 

Swadaqatun Jaariyah

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Mwanaadamu anapokufa, amali zake zote zinakatika isipokuwa tatu. Swadaqatun Jaariyah (Swadaqah inayoendela), au elimu yenye kunufaisha watu, au mtoto mwema anayemuombea". [Ahmad na Muslim]

 

Kushukuru

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Atakayekufanyieni wema mlipeni, na ikiwa hamna cha kumlipa, basi muombeeni dua mpaka muhisi kuwa mumemlipa". [Abuu Daawuwd na An-Nasaaiy]

 

Imesimuliwa na Imaam Ahmad kutoka kwa Al-Ash’ath bin Qays kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Hamshukuru Allaah yule asiyewashukuru watu." [Ahmad]

 

Na akasema:

 

"Aliyetendewa jema, akasema kumwambia aliyemtendea: “Jazaaka Allaahu khayran', (Allaah  Akujaze khayr), huyo amekwisha shukuru kama inavyotakikana".

 

Share

028-Kutoa Zakaah: Wanaostahiki Zakaah

 

Kutoa Zakaah: Wanaostahiki Zakaah

 

Alhidaaya.com

 

Swadaqah ya kawaida, anapewa mtu yeyote hata akiwa si Muislam, ama Zakaatul Fitwr wanapewa watu wa aina mbili tu, nao ni masikini na mafakiri Waislam.

Zakaatul Maal (Zakaah ya mali), hii wanapewa aina 8 tu ya Waislamu waliowataja na Allaah katika kitabu chake kitukufu Aliposema:

 

إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاء وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللّهِ وَابْنِ السَّبِيلِ فَرِيضَةً مِّنَ اللّهِ وَاللّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ

 

 "Swadaqah hupewa (watu hawa):-

1. Mafakiri na

2. Masikini na

3. Wanaozitumikia na

4. Wanaotiwa nguvu nyoyo zao (juu ya Uislam) na

5. Katika kuwapa uungwana watumwa na

6. Katika kuwasaidia Wenye deni na

7. Katika (kutengeneza) Mambo aliyoamrisha Allaah na

8. Katika (kupewa) Wasafiri (walioharibikiwa).

 ۖ فَرِيضَةً مِّنَ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ

Ni faradhi itokayo kwa Allaah.  Na Allaah ni Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote". [At-Tawbah: 60.]

 

Ayakayeichunguza aayah hii utaona kuwa Allaah ametumia neno 'Lil' katika kuwataja watu aina nne wa mwanzo wanaostahiki kupewa Zakaah. Na hii inaitwa Laam ya tamliyk, na maana yake ni kuwa lazima kuwamilikisha watu wa aina nne wa mwanzo (yaani kuwapa mikononi mwao) Zakaah yao.

 

Allaah Anasema:

إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاء وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ

Hakika Zakaah ni kwa ajili ya mafakiri na masikini na wanaozitumikia, na wanaotiwa nguvu nyoyo zao (katika Uislamu). [At-Tawbah: 60]

 

Ama katika aina nne waliobaki, Allaah ametumia neno 'Fiy'. Na kwa kutumia neno hilo Allaah hatulazimishi, kuwamilikisha kwa kuwapa Zakaah yao mikononi mwao.

 

Allaah Anasema:

وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللّهِ وَابْنِ السَّبِيلِ

Na kuwakomboa mateka, na wenye deni na katika njia ya Allaah na msafiri (aliyeharibikiwa). [At-Tawbah: 60]

 

Kwa hivyo katika aina nne za mwisho, kwa mfano kama unataka kumsaidia mwenye deni, hulazimiki kumpa pesa hizo mkononi mwake, bali unaweza kwenda kumlipia deni hilo moja kwa moja bila ya kumkabidhi mdaiwa huyo pesa hizo mkononi mwake. Hata hivyo, ukitaka unaweza pia kumkabidhi mweyewe mkononi mwake.

 

Ukitaka kuzitumia pesa za Zakaah katika njia ya Allaah, unaweza kununua kwa mfano silaha na kuwakabidhi wapiganaji 'Mujaahidiyn' au unaweza kuzitumia katika njia ya Allaah bila ya kumkabidhi mtu pesa hizo mkononi mwake, wakati huo huo unaweza ukitaka kuwakabidhi wanaohusika au wajuzi ili ipate kutumika kwa usahihi zaidi.

  

Mafakiri Masikini

 

Juu ya kuwa watu wamehitalifiana juu ya nani masikini na nani fakiri, lakini kwa ujumla hawa ni watu ambao wanachokipata hakiwatoshi katika matumizi yao ya kila siku.

 

Mtu anaweza kuwa masikini hata kama anapata mshahara mkubwa lakini wakati huo huo ana watoto wengi au wazee na ndugu wanaomtegemea anaowajibika kuwatizama, au ana madeni kiasi ambapo juu ya kuwa anapata mshahara mkubwa, pesa hizo hazimtoshi kuwalisha watu wake hao.

 

Kwa ajili hiyo juu ya tofauti iliyopo baina ya masikini na fakiri katika sharhi yake, lakini katika kuhitajia kwao msaada, wote wawili wapo katika hali moja.

 

Zipo Hadiyth zinazotujulisha kuwa wapo baadhi ya masikini wenye kustahi kuombaomba juu ya shida kubwa walokuwa nazo. Waislam wanatakiwa wawachunguze watu wa aina hii na kuwasaidia na wasiwaache mpaka hali zao zikawa mbaya.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 

"Masikini si yule anayeomba akapewa tende moja au mbili akaondoka, au tonge moja au mbili, lakini masikini wa kweli ni yule anayejizuwia. Someni mkitaka (kauli ya Allaah isemayo):

 

التَّعَفُّفِ تَعْرِفُهُم بِسِيمَاهُمْ لاَ يَسْأَلُونَ النَّاسَ إِلْحَافًا

"Utawafahamu kwa alama zao hawawaombi watu wakafanya ung'ang'anizi".

 

Anayepewa Zakaah ni Masikini au Fakiri Muislam tu, ama Masikini au Fakiri asiyekuwa Muislam hapewi katika mali ya Zakaah, na kama Fakiri asiyekuwa Muislam atahitajia msaada, basi atapewa katika mali ya Swadaqah na si ya Zakaah.

 

Wenye Kuzitumikia

 

Wanaozitumikia Zakaah ni wale waliopewa jukumu la kuipokea, kuikusanya kutoka kwa matajiri na wenye kazi ya kuihifadhi, waandishi, na wenye kuigawa, wakiwemo wachungaji wa wanyama wa Zakaah.

 

Ili waweze kupewa katika Mali ya Zakaah, watu hao lazima wawe Waislam, na wasiwe katika wale walioharamishwa kupokea Zakaah katika watu wa Ahlul Bayt ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Banu 'Abdil-Muttalib ambao tutawataja baadaye.

 

Katika wanaoitumikia Zakaah, hata akiwa mtu tajiri basi anastahiki kupewa katika mali hiyo, na ikiwa mtu wa aina hiyo amepewa na wakubwa wanaohusika na akawa hana haja nayo mali hiyo, basi aichukuwe na kuwagawia anaowataka au kumnunulia zawadi anayemtaka.

 

Imepokelewa kuwa ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipokuwa akifanya kazi ya kukusanya mali ya Zakaah, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimpa katika mali hiyo.

‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema:

"Mimi najitolea tu na sina haja ya kulipwa, mpe mwenye kuzihitajia zaidi kuliko mimi".

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

"Alichokupa Allaah katika mali hii bila ya wewe mwenyewe kuiomba, uichukue na uitumie au itolee Swadaqah." [Al-Bukhaariy na An-Nasaaiy]

  

Wenye Kutiwa Nguvu

 

Hawa ni watu wanaopewa katika mali ya Zakaah kwa ajili ya kulainishwa nyoyo zao na kutiwa nguvu kutokana na udhaifu wa nyoyo hizo, na wengine hupewa kwa ajili ya kuwaepusha Waislam na shari zao, au kuwavutia katika kuupenda Uislam na kuupa nguvu.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwapa wakubwa wa makabila ya kiarabu na hasa makabila ya kibedui kwa ajili ya kuwapendekeza katika Uislaam.

 

Imepokelewa kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimpa mtu mmoja aitwae Swafwaan bin Umayyah ngamia wengi sana katika ngamia wa ngawira waliopatikana katika vita vya Hunain, na Safwan huyu alikuwa mkubwa wa kabila lake.

 

Safwaan alikuwa wakati huo bado hajasilimu, na alipopewa mali hiyo, akarudi kwa watu wake na kuwaambia:

 

"Enyi watu wangu, ingieni katika dini ya Kiislam, kwani Muhammad anatoa utoaji wa mtu asiyeogopa ufakiri".

 

(Mwenye kuchunguza, ataona kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwatendea makabila ya Kibedui tofauti na anavyowatendea watu wa mijini. Alikuwa akiwachukulia kwa akili zao. Na hii ni kwa sababu Mabedui ni watu wagumu sana kufahamu. Hata katika kuuliza masuali, Mabedui walikuwa wakimuuliza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) masuali na kujibiwa, wakati masuali hayo hayo wangeuliza Swahaba wanaokaa mjini (Radhwiya Allaahu ‘anhum), basi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angekasirika nayo masuali hayo).

 

Wakati wa ukhalifa wake Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akiendelea kuwapa watu wa aina hii, lakini ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) siku moja alikataa kutoa, akawaambia:

 

"Hii Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikupeni kwa ajili ya kuzizowesha nyoyo zenu na kuzilainisha, lakini sasa Allaah amekwishautukuza Uislam na hatuna haja nanyi tena, mkitaka ingieni katika Uislam, na kama hamtaki basi baina yetu na baina yenu ni panga. Allaah Amesema:

وَقُلِ الْحَقُّ مِن رَّبِّكُمْ فَمَن شَاء فَلْيُؤْمِن وَمَن شَاء فَلْيَكْفُرْ

Na sema: Hii ni haki kutoka kwa Rabb wenu. Basi anayetaka aamini, na anayetaka akufuru. [Al-Kahf: 29]

 

Anasema Sayyid Saabiq katika Fiqhis Sunnah:

 

"Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikubaliana na ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) katika uamuzi wake huo, na hapana hata Sahaba mmoja (Radhwiya Allaahu ‘anhum) aliyepinga. Na hii ni katika Ijtihadi zake ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu), na hata makhalifa waliokuja baada yake, Uthmaan na Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhum) hawakuwapa tena watu wa aina hii katika mali ya Zakaah.

 

Hata hivyo," anaendela kusema Shaykh Saabiq, "hii haimaanishi kuwa watu wa aina hii wasipewe, na Imaam yeyote yule atakayetawala na akaona kuwa ipo haja ya kuwapa watu wa aina hii, basi atawapa kwa sababu dalili ipo katika Qur-aan na Sunnah.”

 

Katika Kugomboa

 

Uislaam umeijaalia ‘Ibaadah hii ya kuwagomboa mateka na watumwa kuwa ni kitendo kinachompatia mtu thawabu nyingi sana na kumuingiza katika Jannah za Allaah Subhanaahu wa Ta’aalaa.

 

Kutoka kwa Al-Barra-a (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema:

"Mtu mmoja alikuja kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwambia:

"Nijulishe juu ya amali (njema) itakayonikurubisha na Jannah na kunibaidisha na Moto".

Akasema:

"Waachie huru watu na wagomboe watumwa".

Akauliza (tena):

"Ee Rasuli wa Allaah, si yote hayo yanabeba maana moja tu?"

Akasema:

"La, (sivyo), 'kuwaachia huru' ni kujihusisha peke yako katika kuwaacha huru, na 'kuwagomboa' ni kusaidia katika kulipa thamani ya kuwagomboa". [Ahmad na Ad-Daaraqutniy].

 

Wakati ule ilikuwa mtumwa anaweza kuandikiana na kukubaliana kuwa atakapoweza kulipa malipo fulani katika muda fulani, ataachwa huru. Kwa hivyo Waislam walitakiwa wawasaidie watu wa aina hiyo kwa kuwalipia kiasi hicho ili waweze kujigomboa.

 

Kumsaidia Mwenye Deni

 

Hawa ni wale wenye madeni makubwa wakashindwa kuyalipa kutokana na kula hasara katika biashara zao nk. Sharti madeni hayo yawe katika mambo ya halali au yatokane na maasi aliyotubu nayo mtu huyo.

 

Imepokelewa kutoka kwa Imaam Ahmad na Abuu Daawuwd na Ibn Maajah na At-Tirmidhiy, kutoka kwa Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

 

"Mas-alah (ya kuwasaidia wenye madeni), hayawi halali isipokuwa katika mambo matatu; aliye fakiri sana, au mwenye deni zito sana, au mwenye kudaiwa damu (ya diya - fidiya).”

 

(Huyu ni mtu aliyejikuta amebebeshwa deni la diya kutokana na ndugu yake au jamaa yake aliyeuwa kwa bahati mbaya. Ikiwa hajalipa diya hiyo, basi ndugu yake huyo au jamaa yake atauliwa kwa ajili ya kulipa kisasi)

 

Katika Kutengeneza

 

(Fiy sabiyli-LLaah), ‘ulamaa wengi wanasema kuwa haya ni mambo yanayohusiana na vita vya Jihadi tu pamoja na watu wanaopigana vita hivyo.

 

Hawa wana sehemu yao katika mali ya Zakaah wanayopewa hata kama askari mpiganaji Jihadi ni tajiri anayejiweza.

 

Vitu vinavyonunuliwa kutokana na pesa za Zakaah kwa ajili ya vita, kama vile farasi, panga, n.k. lazima virudishwe katika nyumba ya hazina ya Waislam (Baytul maal) baada ya kumalizika kwa vita.

Kadhaalika, ‘ulamaa wengi wanaonelea kuwa kusaidia mtafutaji elimu ya Dini "Twaalibul-'Ilm" inaingia katika "Fiy sabiylil-LLaah". Na utafutaji elimu ya Dini ni katika jambo tukufu sana.

  

Katika Kupewa Wasafiri

 

Msafiri aliyeishiwa na pesa akawa hana njia nyingine ya kupata pesa za matumizi, huyu anapewa katika mali ya Zakaah, sharti safari yake hiyo iwe katika mambo ya twa'a na si katika kumuasi Rabb wake, hata akiwa msafiri huyo huko kwao alikotoka ni mtu tajiri mwenye mali nyingi.

 

Share

030-Kutoa Zakaah: Walioharimishwa Kupewa

Kutoa Zakaah: Walioharimishwa Kupewa

 

Alhidaaya.com

 

 

1.    Kafiri

 

Katika Hadiyth iliyotangulia, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Zichukuliwe kutoka kwa matajiri Wao na kurejeshewa masikini Wao"

  

Na maana yake ni kuwa:-

 

Zichukuliwe kutoka kwa matajiri wa Kiislam na kupewa masikini wa Kiislam.

 

 

2.    Bani Hashim

 

Nao ni watoto wa Aliy na Aqiyl na Jaafar na Al ‘Abbaas na Al Harith (Radhwiya Allaahu ‘anhum).

 

Nabiy (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

 

"Swadaqah haijuzu kupewa kwa watu wa Muhammad". [Muslim]

 

‘Ulamaa wamekhatalifiana juu ya ukoo wa Bani Al Muttalib, iwapo nao pia hawapewi katika mali ya Zakaah au wanapewa. Imaam Ash-Shaafi’iy amesema kuwa hawa nao wasipewe katika mali ya Zakaah, na hii inatokana na Hadiyth iliyotolewa na Imaam Ash-Shaafi’iy na Imaam Ahmad na Imaam Al-Bukhaariy kutoka kwa Jubair bin Mut’am aliposema:

 

"Siku ya Khaybar (baada ya kumalizika vita hivyo), Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliikusanya upande mmoja sehemu ya ngawira ya watu wa ukoo wake katika Bani Haashim na ya Bani Al-Muttwalib na akawaacha (watu wa kabila lake) katika Bani Nawfal na Bani ‘Abdu Shams. Tukamwendea mimi na ‘Uthmaan bin ‘Affaan na kumuuliza:

 

"Ee Rasuli wa Allaah hawa ni Bani Haashim na sisi hatukanushi fadhila zao kutokana daraja yako mbele ya Allaah, lakini vipi hawa ndugu zetu katika Bani Al Mutwalib, umewaingiza wao ukatuacha sisi wakati nasaba yao na yetu juu yako ni sawa sawa?"

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

 

"Sisi na Bani Mutwalib hatujafarikiana katika ujahilia wala katika Uislaam, bali sisi na wao ni kitu kimoja". Akaviingiza vidole vyake vya mkono wa kulia ndani ya vidole vya mkono wa kushoto na kuvichanganya."

 

Kutokana na ushahidi huu, baadhi ya maulamaa wakasema; 'Bani Mutwalib nao pia wanaingia katika kuharamishiwa kupewa katika Mali ya Zakaah".

 

 

3.    Baba Na Watoto

Haijuzu mtu kumpa katika mali ya Zakaah baba yake, mama yake, watoto wake na babu zake, na hii ni kwa sababu mtoaji Zakaah anawajibika kuwatizama watu hao na kuwapa katika mali yake, na kwa ajili hiyo, watu hao wanalazimika kuwa matajiri kutokana na utajiri wake.

 

 

4.    Mke

Haijuzu mtu kumpa mkewe katika mali ya Zakaah, na jambo hili linakubaliwa na ‘ulamaa wote na hii ni kwa sababu mtu anawajibika kumtizama na kumpa mkewe katika mali yake kama anavyowajibika kuwapa wazee wake wawili akiwa anao uwezo huo.

 

Anasema Ibnul Mundhir:

 

"Isipokuwa kama mke ana deni, basi hupewa Zakaah katika ile sehemu ya kuwasaidia wenye madeni kwa ajili ya kulipa deni hilo".

 

Ama ikiwa mke ni tajiri mwenye uwezo wa kutoa Zakaah, basi yeye anarushusiwa kumpa mumewe katika mali ya Zakaah kutokana na kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

 

"Amesema kweli Ibn Mas’uud, mumeo na mwanao wanastahiki zaidi kuwapa Swadaqah". [Al-Bukhaariy]

 

 

5.  Haijuzu kuitumia mali ya Zakaah kwa ajili ya kujikurubisha kwa Allaah kama vile kujenga misikiti, kununua misahafu, kununua vifaa vya kusaidia kuosha maiti nk. Na hii ni kwa sababu Allaah kwa hekima yake keshazitaja na kuzisherehesha njia za kutoka Zakaah katika aya iliyotangulia ya Suwrah At-Tawbah na akaikamilisha aayah hiyo kwa kusema;

 

  ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ

Na Allaah ni Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote. [At-Tawbah: 60]

 

Share

031-Kutoa Zakaah: Watu Wema

 

Kutoa Zakaah: Watu Wema

 

Alhidaaya.com

 

 

Zakaah anapewa Muislam anayeistahiki akiwa Muislam huyo ni mtu mwema au mtu asi, isipokuwa mtu asi hapewi katika mali ya Zakaah ikiwa itajulikana kwa uhakika kuwa atakuja kuitumia mali hiyo katika kuuendeleza uasi wake. Ikijulikana kwa uhakika kuwa ataitumia mali hiyo katika kumuasi Allaah, basi mtu huyo atanyimwa, ama ikiwa hayajulikani hayo, au ikijulikana kuwa ataitumia mali hiyo katika shida zake, basi hapo atapewa.

 

Hata hivyo ni bora kwa mtoaji Zakaah aihusishe mali hiyo kwa kuwapa watu wema au maulamaa wanaostahiki wanaoifayia kazi elimu yao, kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Walisheni chakula chenu wacha wa Allaah na mnaowajuwa katika walioamini (kweli)". [Ahmad]

 

Anasema Ibn Taymiyah:

 

"Asiyeswali hapewi katika mali ya Zakaah mpaka pale atakapotubu akawa anaswali."

 

Anasema Sayyid Saabiq:

 

"Katika kundi hilo wanaingia pia wale wanaomuasi Allaah bila kujali wala kuona haya, na kuendelea kuzama katika maasi huku nyoyo zao zikiwa ziAsh-Shaafi’iysidika na dhamiri zao zimekwisha haribika".

 

Hawa hawapewi katika mali ya Zakaah isipokuwa kama Zakaah hiyo itawasaidia katika kuwaongoza mwongozo ulio sahihi au itawasaidia katika kutoka hali yao hiyo.

 

Share

032-Kutoa Zakaah: Kuinunua Zakaah

 

Kutoa Zakaah:Kuinunua Zakaah

 

Kuinunua Zakaah

 

Alhidaaya.com

 

 

Nabiy (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amekataza mtu kuinunua Zakaah yake. Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhwiya Llaahu ‘anhu), amesema:

 

"‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alimtoa farasi wake Swadaqah fiy sabiyli Llaah, kisha akamkuta farasi huyo anauzwa na akataka kumnunua. Akamuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya jambo hilo, akamwambia:

 

"Usimnunue na wala usirudie (kutaka kuimiliki tena) Swadaqah yako" [Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo]

 

Baadhi ya maulamaa wakasema kuwa kukataza huko ni kwa ajili ya kujiepusha tu, na si kwa ajili ya kuharamisha, wakiegemea Hadiyth nyingine inayoruhusu mtu kuipokea Swadaqah yake kama zawadi itokayo kwa masikini aliyempa.

 

Share

033-Kutoa Zakaah: Kuisafirisha Zakaah

 

Kutoa Zakaah: Kuisafirisha Zakaah

 

Alhidaaya.com

 

 

‘Ulamaa wengi wamekubali kuwa mali ya Zakaah (Zakaatul Maal - si Zakaatul Fitwr) inaweza kusafirishwa na kutolewa katika nchi nyingine kwa wanaoistahiki zaidi ikiwa watu wa mji anaoishi mtoaji hawaihitajii zaidi mali hiyo. Ama ikiwa katika nchi hiyo wapo wanaoihitajia, basi zipo Hadiyth zinazotujulisha kuwa Zakaah ya kila nchi wanapewa masikini wake.

 

Katika madhehebu ya Imaam Abu Haniyfah, wao wanasema:

 

"Ni Makruuh kuisafirisha mali ya Zakaah isipokuwa ikiwa kwa ajili ya kumsaidia ndugu wa nasaba mwenye kuihitajia, na hii inatokana na umuhimu wa kuunganisha undugu huo, au pia kwa ajili ya watu wenye shida sana katika watu wa nchi yake, au kwa ajili ya kuiondoa kutoka nchi ya kikafiri na kuipeleka katika nchi ya kiislam."

 

Madhehebu ya Imaam Ash-Shaafi’iy yanasema:

 

"Haijuzu kuisafirisha mali ya Zakaah na inawajibika kutolewa katika nchi iliyochumwa mali hiyo isipokuwa pakikosekana wenye kuihitajia Zakaah hiyo katika nchi hiyo".

 

Mu’aadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipewa ugavana wa nchi ya Yemen na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na alipotawala ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alimuacha Mu’aadh aendelea kuwa gavana wa nchi hiyo. Lakini Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipompelekea ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) theluthi ya mali ya Zakaah, ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikataa kuzipokea akamwambia:

 

"Sikukupeleka uwe mchotaji (wa mali) wala mpokeaji wa kodi, bali nimekupeleka kwa ajili ya kuchukua mali (ya Zakaah) kutoka kwa matajiri wao na kuzirudisha kwa masikini wao".

 

Mu’aadh (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema:

 

"Nisingekuletea ila kwa sababu sikumpata (masikini) anayezistahiki kuzichukua".

 

Share

034-Kutoa Zakaah: Kuidhihirisha Zakaah

 

Kuidhihirisha Zakaah: Kuidhihirisha Zakaah

 

Alhidaaya.com

 

 

Inazuju kwa mtoaji kuidhihirisha au kuitoa kwa siri Zakaah yake, yote sawa ikiwa anachokitowa ni Swadaqah ya kawaida au Zakaah ya mali, ingawaje kuitoa kwa siri ni bora zaidi.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

إِن تُبْدُواْ الصَّدَقَاتِ فَنِعِمَّا هِيَ وَإِن تُخْفُوهَا وَتُؤْتُوهَا الْفُقَرَاء فَهُوَ خَيْرٌ لُّكُمْ

Mkidhihirisha swadaqah basi ni vizuri hivyo, na mkizificha na kuwapa mafakiri, basi hilo ni khayr kwenu. [Al-Baqarah: 271]

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Watu saba Allaah  Atawafunika katika kivuli Chake, Siku ambayo hakutokuwa na kivuli ila kivuli Chake: Imaam muadilifu, kijana ambaye amekulia katika ‘Ibaadah ya Rabb wake, Mtu ambaye moyo wake umeambatana na Misikiti, watu wawili wanaopendana kwa ajili ya Allaah; wanakutana kwa ajili Yake na wanafarikiana kwa ajili Yake, mwanamme aliyetakwa na mwanamke mwenye hadhi na mrembo wa kuvutia akasema: "Mimi namkhofu Allaah!" Mtu aliyetoa Swadaqah yake akaificha hadi kwamba mkono wake wa kushoto usijue nini ulichotoa mkono wake wa kulia, na mtu aliyemdhukuru Allaah kwa siri macho yake yakatokwa machozi." [Al-Bukhaariy - Muslim na Imaam Ahmad]

 

 

Share