Swabrun Jamiyl (Subira Njema)

  

 

 

Imekusanywa na: Ummu Iyyaad

 

 

 

 

 

Share

00-Swabrun Jamiyl: Utangulizi

 

Swabrun Jamiyl (Subira njema)

 

00-Utangulizi

 

 

 

AlhamduliLLaah, Himdi Anastahiki Allaah Rabb wa walimwengu wote, Swalaah na salaam zimfikie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na jamaa zake, na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na wote waliotangulia kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Muislamu anahitaji subira katika kila jambo zuri au baya na katika kila hali; kwenye furaha na huzuni, siha na maradhi, utajiri na umasikini, neema na dhiki, utiifu na maasi. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَنَبْلُوكُم بِالشَّرِّ وَالْخَيْرِ فِتْنَةً ۖ وَإِلَيْنَا تُرْجَعُونَ

Na Tutakujaribuni kwa mitihani ya shari na kheri. Na Kwetu mtarejeshwa. [Al-Anbiyaa: 35]

 

Dunia ni nyumba ya mtihani ambako mja atakuwa akigeuzwa kukabili hali zote za kheri na shari na hatima yake ni kuelekea kwenye makazi ya malipo kama Anavosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

تَبَارَكَ الَّذِي بِيَدِهِ الْمُلْكُ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿١﴾

Amebarikika Ambaye Mkononi Mwake umo ufalme Naye juu ya kila kitu ni Muweza

 

الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا ۚ﴿٢﴾ 

Ambaye Ameumba mauti na uhai ili Akujaribuni ni nani kati yenu mwenye ‘amali nzuri zaidi. [Al-Mulk: 1–2]

 

Kwa hiyo Muislamu hana chaguo ila asubiri katika mitihani ili apate fadhila tele Alizoahidi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) au sivyo atakuwa miongoni mwa waliokhasirika kama Alivyohukumu Mwenyewe Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  katika Suwratul’Aswr. Pia, Muumini atambue kwamba hakuna mtihani ila Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   Humteremshia mja Wake rahmah na kwa kumpa faraja Naye Haendi kinyume na ahadi Zake. Anasema:

 

فَإِنَّ مَعَ الْعُسْرِ يُسْرًا ﴿٥﴾

Basi hakika pamoja na kila gumu kuna wepesi.

إِنَّ مَعَ الْعُسْرِ يُسْرًا ﴿٦﴾

 

Hakika pamoja na kila ugumu kuna wepesi. [Al-Inshiraah: 5–6]

 

 

Tumenukuu visa kadhaa vilothibiti ili viwe ni mafunzo kwetu na viweze kumthibitisha Muislamu anaposibiwa na mitihani. Juu ya hivyo, tuna mifano bora kabisa vya Rusuli wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  waliokumbana na kila aina ya mitihani, Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Akawasifu kwa subira zao:

 

وَإِسْمَاعِيلَ وَإِدْرِيسَ وَذَا الْكِفْلِ ۖ كُلٌّ مِّنَ الصَّابِرِينَ ﴿٨٥﴾

Na Ismaa’iyl na Idriys na Dhal-Kifli, wote ni miongoni mwa wenye kusubiri. [Al-Anbiyaa: 85]

 

Akamsifu Nabiy Ayyuwb:

 

إِنَّا وَجَدْنَاهُ صَابِرًا ۚ نِّعْمَ الْعَبْدُ ۖ إِنَّهُ أَوَّابٌ ﴿٤٤﴾

Hakika sisi Tulimkuta mwenye subira mno, uzuri ulioje wa mja, hakika yeye ni mwingi wa kurudiarudia kutubia. [Swaad: 44]

 

Na Anasema (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

فَاصْبِرْ كَمَا صَبَرَ أُولُو الْعَزْمِ مِنَ الرُّسُل﴿٣٥﴾ِ

Basi subiri (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kama walivyosubiri wenye azimio madhubuti miongoni mwa Rusuli [Al-Ahqaaf: 35]

 

Hao kama walivyokubaliana Wafasiri baada ya kukhitilafiana kwamba ni Nabiy ‘Ibraahiym, Nuwh, Muwsaa, ‘Iysaa (‘Alayhimus-salaam na Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

 

Tunamuomba Allaah ('Azza wa Jalla) Ajaalie kazi hii iwe kwa ajili ya kupata Radhi Zake Pekee na Ajaalie iwe yenye manufaa kwa ndugu zetu wa Kiislamu na tunamuomba Atughufurie na Atusamehe kwa makosa yoyote yatakayokuwemo.

 

 

 Wa-Swalla-Allaahu ‘alaa Muhammadin wa ‘alaa aalihi wa-Swahbihi wa sallam.

 

 

19 Swafar 1433H -  13 Januari 2012M

Imehaririwa: 2  Jumaada Al-Uwlaa 1439H - 19 Januari 2018

 

 

 

 

 
Share

01-Swabrun Jamiyl: Maana Na Aina Za Subira

 

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)

 

01-Maana Na Aina Za Subira

  

 

Subira imegawika katika sehemu nne:

 

 

1. Subira katika utiifu.

 

Inahusiana na 'amali anazotenda mja kwa kutumia mwili (vitendo vya 'ibaadah) au ulimi wake (kumdhukuru Allaah).

 

 

2. Subira katika maasi.

 

Ni kuacha kutenda jambo lisilokuwa lenye kuridhisha kwa kutumia mwili au ulimi wake. 

 

 

3. Subira katika Qadhwaa na Qadar: (Yaliyohukumiwa na Yaliyokadiriwa) na Allaah:

 

Ni kuzuia nafsi isiungulike au isihamanike au isighadhibike kutokana na mitihani inayomsibu mtu.

 

 

4. Subira kutokana na maudhi ya watu.

 

Ni subira kutokana na maudhi ya watu ni kuzuia nafsi, ulimi na viungo visilipize maovu anayotendewa mtu. Kusubiri kote huko ni kwa ajili ya kupata radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَاصْبِرْ نَفْسَكَ مَعَ الَّذِينَ يَدْعُونَ رَبَّهُم بِالْغَدَاةِ وَالْعَشِيِّ يُرِيدُونَ وَجْهَهُ﴿٢٨﴾ ۖ 

Na isubirishe nafsi yako pamoja na wale wanaomuomba Rabb wao asubuhi kabla jua kucha na jioni, wanataka Wajihi Wake. [Al Kahf: 28]

 

 

Ibnul-Qayyim amemsikia Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah akisema:

 

“Subira katika kutekeleza maamrisho na Allaah ni jambo zito na lilikamilika zaidi kuliko subira katika kujiepusha na yaliyoharamishwa. Kwani maslaha yanayopatikana kwa kutenda maamrisho Yake Allaah yanapendwa zaidi na Allaah kuliko kuacha maasi. Na madhara yanayopatikana kwa kuacha kutekeleza maamrisho ya Allaah ni makubwa na yanachukiza zaidi mbele ya Allaah kuliko madhara ya kuwepo na maasia.” [Madaarij As-Saalikiyn]

 

 

1-Subira Katika Utiifu

 

Kunahitajika subira katika utiifu kwani baadhi ya ‘ibaadah zina tabu na mashaka na nyinginezo zinahitaji imani na azimio la nguvu hata nafsi iridhike. Mfano mtu anapoamka usiku akiwa hakushiba usingizi lakini pamoja na hayo anajitahidi kuamka kwa ajili ya Qiyaamul-layl (kisimamo cha usiku kuswali) au kuamka mapema kwenda Msikitini na pengine hali ya hewa ni baridi kali, au Swawm masiku marefu ya joto kali, au kuitolea mali yake aipendayo Zakaah na Swadaqah, au kuvumilia misukusuko inayopatikana katika kutekeleza ‘ibaada ya Hajj n.k. Yote hayo ni  ‘ibaadah na anaifanya kwa ustahmilivu. Mifano yake ni kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 

وَاسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ ۚ وَإِنَّهَا لَكَبِيرَةٌ إِلَّا عَلَى الْخَاشِعِينَ ﴿٤٥﴾

Na tafuteni msaada kupitia subira na Swalaah; na hakika hilo ni kubwa isipokuwa kwa wanyenyekevu. [Al-Baqarah: 45]

 

وَأْمُرْ أَهْلَكَ بِالصَّلَاةِ وَاصْطَبِرْ عَلَيْهَا﴿١٣٢﴾ ۖ 

Na amrisha ahli zako Swalaah, na dumisha kusubiri kwayo. [Twaahaa: 132]         

 

 تَتَجَافَىٰ جُنُوبُهُمْ عَنِ الْمَضَاجِعِ يَدْعُونَ رَبَّهُمْ خَوْفًا وَطَمَعًا وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ ﴿١٦﴾

Mbavu zao zinatengana na vitanda, wanamuomba Rabb wao kwa khofu na matumaini, na katika yale Tuliyowaruzuku wanatoa.  [As-Sajdah: 16]

 

 

 

2-Subira Katika Maasi

 

Mja anahitaji subira katika maasi kwani binaadamu hukabiliwa na yaliyo haramu na machafu; mfano kula ribaa na mali za mayatima, kuchukua haki za watu ikiwa ni mali au heshima ya mtu, kuzuia ulimi usitaje ya upuuzi au ghibyah (kumteta, kumsengenya mtu), an-Namiymah (kufitinisha) na kila aina ya maneno maovu. Hayo ni baadhi ya mambo ambayo nafsi hutamani kujiridhisha isikie raha na kutimiza matamanio yake, na shaytwaan humtia wasiwasi na kuiamrisha hiyo nafsi itende maovu hayo kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِنَّ النَّفْسَ لَأَمَّارَةٌ بِالسُّوءِ﴿٥٣﴾

Hakika nafsi ni yenye kuamrisha sana maovu. [Yuwsuf: 53]

 

Hapo ndipo mja anapohitajika kufanya jihaad ya nafsi ajizuie na afanye subira na kutokuiendekeza nafsi yake. Imethibiti hili katika Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عَنْ فَضَالَةَ بْنِ عُبَيْدٍ (رضي الله عنه)  أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ فِي حَجَّةِ الْوَدَاعِ: ((أَلاَ أُخْبِرُكُمْ  بالْمؤُمِن؟ مَنْ أَمِنَهُ النَّاسُ عَلَى أَمْوَالِهِمْ وَأَنْفُسِهِمْ  وَالْمُسْلِم  مَنْ سَلِمَ  النَّاسُ  مِنْ لِسَانِهِ وَيَدِهِ وَالْمُجَاهِدُ مَنْ جَاهَدَ نَفْسَهُ فِي طَاعَةِ اللَّهِ  وَالْمُهَاجِرُ مَنْ هَجَرَ الْخَطَايَا وَالذَّنُوبَ)) أحمد والحاكم قال الألباني  "إسناد صحيح" سلسلة الأحاديث الصحيحة

 

Kutoka kwa Fadhwaalah bin ‘Ubayd ((Je, nikujulisheni kuhusu Muumini? Ni yule anayeaminiwa na watu juu ya mali zao na nafsi zao. Na Muislamu ni yule anayeweka amani kwa watu kwa ulimi wake na mkono wake. Na mpiganaji jihaad ni yule anayefanya jihaad ya nafsi yake katika kumtii Allaah, na mhamaji hijrah ni yule anayehama makosa na madhambi)) [Ahmad na Al-Haakim. Kasema Imaam Al-Albaaniy katika Silsilatul-Ahaadiyth Asw-Swahiyhah: “Hii isnaad ni Swahiyh”]

 

 

Ndio maana Jannah (Pepo) ikawa si wepesi kuipata kwani imezungukwa na mazito na magumu (kuyatenda), na moto ukawa wepesi kuufikia kwa kuzungukwa na matamanio kama alivyotuelezea Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth Al-Qudsiy:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ عَنْ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((لَمَّا خَلَقَ اللَّهُ الْجَنَّةَ وَالنَّارَ أَرْسَلَ جِبْرِيلَ إِلَى الْجَنَّةِ فَقَال: انْظُرْ إِلَيْهَا وَإِلَى مَا أَعْدَدْتُ لِأَهْلِهَا فِيهَاز  قَالَ:  فَجَاءَهَا وَنَظَرَ إِلَيْهَا وَإِلَى مَا أَعَدَّ اللَّهُ لِأَهْلِهَا فِيهَا.  قَالَ:  فَرَجَعَ إِلَيْهِ قَالَ: فَوَعِزَّتِكَ لَا يَسْمَعُ بِهَا أَحَدٌ إِلَّا دَخَلَهَا. فَأَمَرَ بِهَا فَحُفَّتْ بِالْمَكَارِهِ. فَقَالَ: ارْجِعْ إِلَيْهَا فَانْظُرْ إِلَى مَا أَعْدَدْتُ لِأَهْلِهَا فِيهَا  قَالَ: فَرَجَعَ إِلَيْهَا فَإِذَا هِيَ قَدْ حُفَّتْ بِالْمَكَارِهِ  فَرَجَعَ إِلَيْهِ فَقَالَ: وَعِزَّتِكَ لَقَدْ خِفْتُ أَنْ لَا يَدْخُلَهَا أَحَدٌ. قَالَ: اذْهَبْ إِلَى النَّارِ فَانْظُرْ إِلَيْهَا وَإِلَى مَا أَعْدَدْتُ لِأَهْلِهَا فِيهَا.  فَإِذَا هِيَ يَرْكَبُ بَعْضُهَا بَعْضًا.  فَرَجَعَ إِلَيْهِ فَقَالَ: وَعِزَّتِكَ لَا يَسْمَعُ بِهَا أَحَدٌ فَيَدْخُلَهَا. فَأَمَرَ بِهَا فَحُفَّتْ بِالشَّهَوَاتِ فَقَالَ: ارْجِعْ إِلَيْهَا فَرَجَعَ إِلَيْهَا فَقَالَ: وَعِزَّتِكَ لَقَدْ خَشِيتُ أَنْ لَا يَنْجُوَ مِنْهَا أَحَدٌ إِلَّا دَخَلَهَا)) الترمذي و قال حديث حسن صحيح – ابو داود والنسائي

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Alipoumba Jannah na moto, Alimtuma Jibriyl Jannah Akimwambia: Iangalie na angalia matayarisho Nliyoyatayarisha kwa ajili ya wakaazi wake. Akasema (Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Kwa hivyo alikuja kuiangalia na kuangalia matayarisho Allaah Aliyofanya kwa ajili ya wakazi wake. Akasema: Akarejea kwa Allaah na kusema: Kwa Utukufu Wako, hakuna atakayesikia (habari yake) ila tu ataingia (Peponi). Kisha Akaamrisha izungushwe (ihusishwe) mambo magumu watu wasiyoyapenda, Akasema: Rejea na angalia yale Niliyoyatayarisha kwa ajili ya wakaazi wake. Akasema: Kisha akarejea na akakuta imezungukwa na mambo magumu watu wasiyoyapenda. Hapo alirejea kwa Allaah na akasema: Kwa utukufu Wako, nina khofu hakuna hata mtu mmoja atakayeingia. Akasema: Nenda motoni ukauangalie na uangalie matayarisho Yangu kwa ajili ya wakaazi wake. Akaona ulikuwa na matabaka moja juu ya tabaka jingine. Akarejea kwa Allaah na akamuambia: Kwa Utukufu Wako hakuna hata mmoja ausikiae (sifa zake) atakayeingia. Kisha Allaah Aliamrisha Uhusishwe na shahawaat (matamanio ya nafsi). Kisha Allaah Akamuambia: Rejea tena (motoni). Alirejea tena na akasema: Kwa Utukufu, wako nakhofia kuwa hapatakuwa na yeyote atakayenusurika nao)) [At-Tirmidhiy akasema ni Hadiyth Hasan, na Abu Daawuwd na An-Nasaaiy]

 

 

 

3-Subira katika Qadhwaa na Qadar (Yaliyohukumiwa na Yaliyokadiriwa) na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

Majaaliwa yanaweza kuwa katika yale ya kheri au ni katika mitihani inayomsibu mtu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَنَبْلُوكُم بِالشَّرِّ وَالْخَيْرِ فِتْنَةً﴿٣٥﴾ ۖ 

Na Tutakujaribuni kwa mitihani ya shari na kheri. [Al-Anbiyaa: 35]

 

فَأَمَّا الْإِنسَانُ إِذَا مَا ابْتَلَاهُ رَبُّهُ فَأَكْرَمَهُ وَنَعَّمَهُ فَيَقُولُ رَبِّي أَكْرَمَنِ ﴿١٥﴾

Basi mwana Aadam pale Rabb wake Anapomtia mtihanini, Akamtakaramu na Akamneemesha, husema: “Rabb wangu Amenitakarimu.”

 

وَأَمَّا إِذَا مَا ابْتَلَاهُ فَقَدَرَ عَلَيْهِ رِزْقَهُ فَيَقُولُ رَبِّي أَهَانَنِ ﴿١٦﴾

Ama Anapomtia mtihanini, Akamdhikishia riziki yake, husema: “Rabb wangu Amenidunisha.” [Al-Fajr: 15–16]

 

Aina hii ya Subira inahusiana pia na aina za misiba inayomsibu mtu ikiwa ni kifo cha mpenzi wake, mali, maradhi, shida, huzuni, dhiki, maafa n.k.  Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَلَنَبْلُوَنَّكُم بِشَيْءٍ مِّنَ الْخَوْفِ وَالْجُوعِ وَنَقْصٍ مِّنَ الْأَمْوَالِ وَالْأَنفُسِ وَالثَّمَرَاتِ ۗ وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ ﴿١٥٥﴾

Na bila shaka Tutakujaribuni kwa kitu katika khofu na njaa na upungufu wa mali na nafsi na mazao. Na wabashirie wenye kusubiri.

 

الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ﴿١٥٦﴾

Wale ambao unapowafika msiba husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.”

 

أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ ﴿١٥٧﴾

Hao zitakuwa juu yao Barakah kutoka kwa Rabb wao na rahmah, na hao ndio wenye kuongoka. [Al-Baqarah: 155–157]

 

 

 

4-Subira Kutokana Na Maudhi ya watu:

 

Miongoni mwayo, inayohitajia subira ya hali ya juu ni dhulma na maudhi ya watu. Na ndio maana Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Ametaja kuwa subira ya aina hii inahitajika azimio la nguvu kuvumilia na kutokulipizia na kusamehe watu wanaosababisha  hayo:

 

وَلَمَنِ انتَصَرَ بَعْدَ ظُلْمِهِ فَأُولَـٰئِكَ مَا عَلَيْهِم مِّن سَبِيلٍ﴿٤١﴾

Na bila shaka anayelipiza kisasi baada ya kudhulumiwa, basi hao hawana sababu ya kulaumiwa.

 

 

إِنَّمَا السَّبِيلُ عَلَى الَّذِينَ يَظْلِمُونَ النَّاسَ وَيَبْغُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ ۚ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ﴿٤٢﴾

Hakika sababu ya kulaumiwa ni juu ya wale wanaodhulumu watu na wanakandamiza katika ardhi bila ya haki. Hao watapata adhabu iumizayo.

 

وَلَمَن صَبَرَ وَغَفَرَ إِنَّ ذَٰلِكَ لَمِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ﴿٤٣﴾

Na atakayevuta subira na akasamehe, hakika hilo bila shaka ni katika mambo ya kuazimiwa. [Ash-Shuwraa: 41–43]

 

 

Juu ya kuwa imeruhusiwa kulipiza dhulma au mateso, lililo bora zaidi ni kuvumilia kwani huko ni kwa ajili ya kupata Radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kutegemea malipo mema. Na juu ya hivyo ni dalili ya taqwa na kuwa na sifa ya ihsaan  ambayo inampatia fadhila Muislamu ya kwamba Allaah Yu pamoja naye daima. Anasema hayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَإِنْ عَاقَبْتُمْ فَعَاقِبُوا بِمِثْلِ مَا عُوقِبْتُم بِهِ ۖ وَلَئِن صَبَرْتُمْ لَهُوَ خَيْرٌ لِّلصَّابِرِينَ﴿١٢٦﴾

Na mkilipiza, basi lipizeni kulingana na vile mlivyoadhibiwa. Na mkisubiri, basi bila shaka hivyo ni bora kwa wenye kusubiri.

 

وَاصْبِرْ وَمَا صَبْرُكَ إِلَّا بِاللَّـهِ ۚ وَلَا تَحْزَنْ عَلَيْهِمْ وَلَا تَكُ فِي ضَيْقٍ مِّمَّا يَمْكُرُونَ﴿١٢٧﴾

Na subiri (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), na haiwi subira yako isipokuwa kupitia kwa Allaah. Na wala usiwahuzunukie, na wala usiwe katika dhiki kutokana na njama wanazozifanya. 

 

 

إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الَّذِينَ اتَّقَوا وَّالَّذِينَ هُم مُّحْسِنُونَ﴿١٢٨﴾

Hakika Allaah Yu Pamoja na wenye taqwa, na wale ambao wao ni wenye kufanya ihsaan. [An-Nahl: 126–128]

 

 

Aina hii ya subira inawahusu pia walinganiaji Dini yetu ya Kiislamu, pale mtu anapoamrisha mema na kukataza maovu kama Luqmaan alipomuusia mwanawe:   

 

يَا بُنَيَّ أَقِمِ الصَّلَاةَ وَأْمُرْ بِالْمَعْرُوفِ وَانْهَ عَنِ الْمُنكَرِ وَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا أَصَابَكَ ۖ إِنَّ ذَٰلِكَ مِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ ﴿١٧﴾

 “Ee mwanangu! Simamisha Swalaah, na amrisha mema na kataza ya munkari, na subiri juu ya yale yatakayokusibu. Hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa. [Luqmaan: 17]

 

 

Na hii ni sifa miongoni mwa sifa za Manabii kwani walivumilia walipokadhibishwa na kuudhiwa na kaumu zao kwa kila aina ya maudhi hadi ikawa ni huzuni kubwa kwao. Nabiy Nuwh ('Alayhis-Salaam) alifanyiwa istihzaai na watu wake. Nabiy Luutw  ('Alayhis-Salaam)    alipata maudhi ya kashfa kutoka kwa watu wake. Nabiy Ibraahiym ('Alayhis-Salaam) aliingizwa kwenye moto na watu wake na akatengwa mbali. Nabiy Yuwsuf ('Alayhis-Salaam) alitaka kuuliwa na nduguze, akaingizwa kisimani, kisha akauzwa kwa bei ndogo mno, kisha akazuliwa kashfa ya mke wa Waziri, akaingizwa jela miaka kadhaa. Nabiy Swaalih ('Alayhis-Salaam) alikadhibishwa na watu wake kuhusiana na miujiza ya ngamia. Nabiy Muwsa ('Alayhis-Salaam) alipata maudhi kuanzia kwa Fir’awn hadi watu wake. Nabiy ‘Iysaa ('Alayhis-Salaam) alipata maudhi na kutaka kuuliwa na watu wake. Na maudhi mengi mbali mbali yalimfikia Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoudhiwa na watu wake Maquraysh wa Makkah hadi kifua chake kikawa na dhiki mno na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akampooza kwa kumwambia:      

 

وَلَقَدْ نَعْلَمُ أَنَّكَ يَضِيقُ صَدْرُكَ بِمَا يَقُولُونَ﴿٩٧﴾

Na kwa yakini Tunajua kwamba kifua chako kinadhikika kwa yale wanayoyasema. [Al-Hijr: 97]

 

Manabii wote hao walivumilia, wakasubiri na wakaweka dhanna nzuri kwa Rabb wao na kuamini waliyoahidiwa na wakaendelea na ulinganiaji wao wa Dini, na wakapata radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na wakawa ni wenye kushinda na kufaulu duniani na Aakhirah.

 

Share

02-Swabrun Jamiyl: Fadhila Za Subra Katika Qur-aan

 

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)

 

 

02-Fadhila Za Subra Katika Qur-aan

 

 

 

Subira imetajwa katika Qur-aan mara nyingi mno kama walivyonukuu ‘Ulamaa. Wengine wamesema kwamba imetajwa zaidi ya mara themanini kwa kusifiwa wale wenye kuvumilia mitihani inayowasibu. Ama kwa ujumla, subira imetajwa katika Qur-aan zaidi ya mara mia.

 

 

Zifuatazo ni baadhi ya fadhila za subira katika Qur-aan:

 

 

1.  Wenye kusubiri hupata mapenzi ya Allaah:

وَاللَّـهُ يُحِبُّ الصَّابِرِينَ ﴿١٤٦﴾

Na Allaah Anapenda wanaosubiri. [Aal-‘Imraan: 146]

 

 

2.  Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Yu pamoja nao daima:

إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الصَّابِرِينَ﴿٤٦﴾

Hakika Allaah Yu Pamoja na wanaosubiri. [Al-Anfaal: 46]

 

 

3. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Amewajumuishia mambo matatu ya bishara njema; Baraka (na maghfirah), rahmah Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na uongofu.

 

وَلَنَبْلُوَنَّكُم بِشَيْءٍ مِّنَ الْخَوْفِ وَالْجُوعِ وَنَقْصٍ مِّنَ الْأَمْوَالِ وَالْأَنفُسِ وَالثَّمَرَاتِ ۗ وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ ﴿١٥٥﴾

Na bila shaka Tutakujaribuni kwa kitu katika khofu na njaa na upungufu wa mali na nafsi na mazao. Na wabashirie wenye kusubiri.

الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ﴿١٥٦﴾

 

Wale ambao unapowafika msiba husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.”

 

أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ ﴿١٥٧﴾

 

Hao zitakuwa juu yao Barakah kutoka kwa Rabb wao na rahmah, na hao ndio wenye kuongoka. [Al-Baqarah: 155-157]

 

 

4. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameahidi kuwalipa malipo mazuri kabisa kwa sababu ya kusubiri kwao katika utiifu.

 

 وَلَنَجْزِيَنَّ الَّذِينَ صَبَرُوا أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴿٩٦﴾

Na kwa yakini Tutawalipa wale waliosubiri ujira wao kwa mazuri zaidi ya yale waliyokuwa wakitenda. [An-Nahl: 96]

 

 

 

5. Wenye kusubiri wameahidiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  malipo mema yasiyohesabika.

 

  إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ ﴿١٠﴾

Hakika wanaosubiri watalipwa kikamilifu ujira wao bila ya hesabu. [Az-Zumar: 10]

 

 

6. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameambatanisha subira na mafanikio na Amewaahidi kufuzu.

 

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اصْبِرُوا وَصَابِرُوا وَرَابِطُوا وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٢٠٠﴾

Enyi walioamini! Subirini na zidini kuvuta subira na bakieni imara na mcheni Allaah ili mpate kufaulu. [Aal-‘Imraan: 200]

 

إِنِّي جَزَيْتُهُمُ الْيَوْمَ بِمَا صَبَرُوا أَنَّهُمْ هُمُ الْفَائِزُونَ ﴿١١١﴾

Hakika Mimi Nimewalipa leo (Jannah) kwa yale waliyokuwa wakisubiri; hakika wao ndio wenye kufuzu. [Al-Muuminuwn: 111]

 

 

7. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amewasifu kuwa ni miongoni mwa wakweli waliosadikisha na wenye taqwa.

 

وَالصَّابِرِينَ فِي الْبَأْسَاءِ وَالضَّرَّاءِ وَحِينَ الْبَأْسِ ۗ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ صَدَقُوا ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُتَّقُونَ ﴿١٧٧﴾  

na wanaosubiri katika dhiki za ufukara na maafa ya magonjwa na njaa na katika vita. Hao ndio waliosadikisha na hao ndio wenye taqwa. [Al-Baqarah: 177].

 

 

 

8. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameahidi maghfirah na ujira mkubwa kwa wenye kusubiri na wakatenda mema.

 

إِلَّا الَّذِينَ صَبَرُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أُولَـٰئِكَ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَأَجْرٌ كَبِيرٌ﴿١١﴾

Isipokuwa wale waliosubiri na wakatenda mema hao watapata maghfirah na ujira mkubwa. [Huwd: 11]

 

 

 

9. Wanaovumilia wamehusishwa na uongozi wa Dini na kuwa ni wenye yakini kuhusu yaliyoteremshwa kwao na Rabb wao.

 

 وَجَعَلْنَا مِنْهُمْ أَئِمَّةً يَهْدُونَ بِأَمْرِنَا لَمَّا صَبَرُوا ۖ وَكَانُوا بِآيَاتِنَا يُوقِنُونَ ﴿٢٤﴾

Na Tukawajaalia miongoni mwao Maimamu wanaongoza kwa amri Yetu waliposubiri; na walikuwa wakiziyakinisha Aayaat (ishara) Zetu. [As-Sajdah: 24]

 

 

10. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Ameifanya subira kuwa ni kinga kubwa kwa maadui na hila zao kama walivyoaahidiwa Maswahaba katika vita vya Uhud.

 

 وَإِن تَصْبِرُوا وَتَتَّقُوا لَا يَضُرُّكُمْ كَيْدُهُمْ شَيْئًا ۗ إِنَّ اللَّـهَ بِمَا يَعْمَلُونَ مُحِيطٌ ﴿١٢٠﴾

((Na mkisubiri na mkawa na taqwa haitokudhuruni chochote katika hila zao. Hakika Allaah ni Mwenye kuyazunguka wayatendayo. [Aal-‘Imraan: 120]

 

 

 

11. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Ameifanya kuwa ni jambo la kutakwa msaada pamoja na nguzo ya Swalaah na kuwasifu kuwa wenye kuvumilia ni wenye sifa ya unyenyekevu.

 

 وَاسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ ۚ وَإِنَّهَا لَكَبِيرَةٌ إِلَّا عَلَى الْخَاشِعِينَ ﴿٤٥﴾

Na tafuteni msaada kupitia subira na Swalaah; na hakika hilo ni kubwa isipokuwa kwa wanyenyekevu. [Al-Baqarah: 45]

 

 

 

12. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amewasifu wenye kuvumilia misiba, maudhi na dhulma kwamba hilo ni jambo kuu la kuazimiwa.

 

وَلَمَن صَبَرَ وَغَفَرَ إِنَّ ذَٰلِكَ لَمِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ﴿٤٣﴾

Na atakayevuta subira na akasamehe, hakika hilo bila shaka ni katika mambo ya kuazimiwa. [Ash-Shuwraa: 43]

 

 

 

13.  Wenye kuvumilia bila shaka watapewa kheri nyingi na wenye hadhi kubwa.

 

 وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا الَّذِينَ صَبَرُوا وَمَا يُلَقَّاهَا إِلَّا ذُو حَظٍّ عَظِيمٍ﴿٣٥﴾

Na hapewi hayo isipokuwa wale waliovuta subira, na hapewi hayo isipokuwa mwenye fungu adhimu. [Fusswilat: 35]

 

 

 

14. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Ameambatanisha ushindi kwa subira na taqwa.

 

بَلَىٰ ۚ إِن تَصْبِرُوا وَتَتَّقُوا وَيَأْتُوكُم مِّن فَوْرِهِمْ هَـٰذَا يُمْدِدْكُمْ رَبُّكُم بِخَمْسَةِ آلَافٍ مِّنَ الْمَلَائِكَةِ مُسَوِّمِينَ ﴿١٢٥﴾ 

Bali, ndio! Mkisubiri mkawa na taqwa na wakakujieni kwa ghafla hivi (kukutekeni); Rabb wenu Atakuongezeeni nguvu kwa Malaika elfu tano waliotiwa alama ya ubora. [Aal-‘Imraan: 125]

 

 

 

15. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amesifu kila ambaye ananufaika na Aayah Zake na akaathirika na mawaidha kwamba ni mwingi wa kusubiri na kushukuru:

 

 إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّكُلِّ صَبَّارٍ شَكُورٍ﴿٣٣﴾

Hakika katika hayo mna Aayaat (zingatio, ishara) kwa kila mwingi wa kuvuta subira na mwingi wa kushukuru. [Ash-Shuwraa: 33]

 

 

16.  Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amemsifu Nabiy Ayyuwb (‘Alayhis Salaam) kwa subira yake kuwa ni mja mzuri alioje.

 

 إِنَّا وَجَدْنَاهُ صَابِرًا ۚ نِّعْمَ الْعَبْدُ ۖ إِنَّهُ أَوَّابٌ ﴿٤٤﴾

Hakika sisi Tulimkuta mwenye subira mno, uzuri ulioje wa mja, hakika yeye ni mwingi wa kurudiarudia kutubia. [Swaad: 44]

 

 

 

17.  Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amehukumu kukhasirika kwa mwana Aadam pindi asipokuwa miongoni mwa wenye kuusia subira na akavumilia  mwenyewe pia:  

 

وَالْعَصْرِ ﴿١﴾

Naapa kwa Al-‘Aswr (zama).

إِنَّ الْإِنسَانَ لَفِي خُسْرٍ ﴿٢﴾

Hakika mwana wa Aadam bila shaka yumo katika khasara.

 

إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ ﴿٣﴾

Isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema na wakausiana haki na wakausiana subira. [Suratul-‘Aswr]

 

 

18. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Amewahusisha watu wa kuliani ambao ni watu wa kheri kwamba ni watu wenye subira wenye huruma.

 

 ثُمَّ كَانَ مِنَ الَّذِينَ آمَنُوا وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ وَتَوَاصَوْا بِالْمَرْحَمَةِ ﴿١٧﴾

Kisha akawa miongoni mwa wale walioamini, na wakausiana kusubiri na wakausiana huruma.

 

أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ الْمَيْمَنَةِ ﴿١٨﴾

Hao ndio watu wa kuliani. [Al-Balad: 17-18]

 

 

 

19. Hatimaye huko Aakhirah ambako ndio kwenye maisha ya kudumu na milele wameahidiwa Jannah na Neema zake:

 

 وَجَزَاهُم بِمَا صَبَرُوا جَنَّةً وَحَرِيرًا﴿١٢﴾

Na Atawalipa kwa sababu ya kusubiri kwao, Jannah na nguo za hariri. [Al-Insaan: 12]

 

 

 

20.  Na pia watabashiriwa Jannah na neema zake na amani kutoka kwa Malaika.

 

 جَنَّاتُ عَدْنٍ يَدْخُلُونَهَا وَمَن صَلَحَ مِنْ آبَائِهِمْ وَأَزْوَاجِهِمْ وَذُرِّيَّاتِهِمْ ۖ وَالْمَلَائِكَةُ يَدْخُلُونَ عَلَيْهِم مِّن كُلِّ بَابٍ﴿٢٣﴾

Jannaat za kudumu milele wataingia pamoja na waliotengenea miongoni mwa baba zao na wake zao na dhuria zao. Na Malaika wanawaingilia katika kila milango.

 

سَلَامٌ عَلَيْكُم بِمَا صَبَرْتُمْ ۚ فَنِعْمَ عُقْبَى الدَّارِ ﴿٢٤﴾

 “Salaamun ‘Alaykum! (Amani iwe juu yenu) kwa yale mliyosubiri.” Basi uzuri ulioje hatima njema ya makazi ya Aakhirah. [Ar-Ra’d: 23-24]

 

 

Lakini si wepesi kuipata Jannah, na miongoni mwa watakaiopata ni wale waja waliosubiri katika kufanya jihaad katika njia ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) wakakumbwa na mitihani na mateso mbali mbali. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Amewatia mtihanini ili Awatambue kama walivumilia kweli:

 

 أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَعْلَمِ اللَّـهُ الَّذِينَ جَاهَدُوا مِنكُمْ وَيَعْلَمَ الصَّابِرِينَ ﴿١٤٢﴾

 

Je, Mnadhani kwamba mtaingia Jannah na hali Allaah Hakudhihirisha wale waliofanya jihaad miongoni mwenu na Akadhihirisha wenye kusubiri? [Aal-‘Imraan: 142]

Share

03-Swabrun Jamiyl: Subira Katika Mitihani Kwa Ujumla

 

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)

 

03 - Subira Katika Mitihani Kwa Ujumla

 

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Hamkalifishi mtu jambo lolote isipokuwa kwa wasaa wake. Na Anapomkidhia mja Wake kufikwa na misiba na mitihani huwa ni kheri kwake kwani malipo yake ni ya duniani na Aakhirah.  Kwa kafiri, misiba na mitihani ni kizuizi kwake kutokuweza kuendelea na shughuli zake za kikawaida. Ama Muumini huwa ni mapumziko ambapo hupata fursa zaidi kumdhukuru Rabb wake kwa kumshukuru, kusubiri na kutegemea malipo ya kufutiwa madhambi yake, au kupandishwa daraja Peponi au kupata mapenzi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  n.k. kama ilivyothibiti katika Qur-aan na Sunnah.

 

 

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ (رضي الله عنه) إِنَّ نَاسًا مِنْ الْأَنْصَارِ سَأَلُوا رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَأَعْطَاهُمْ. ثُمَّ سَأَلُوهُ فَأَعْطَاهُمْ. ثُمَّ سَأَلُوهُ فَأَعْطَاهُمْ حَتَّى نَفِدَ مَا عِنْدَهُ.  فَقَالَ لَهُم حِينَ أَنْفَقَ كُلّ شَيْءٍ بِيَدِه: ((مَا يَكُونُ مِنْ خَيْرٍ فَلَنْ أَدَّخِرَهُ عَنْكُمْ  وَمَنْ يَسْتَعْفِفْ يُعِفَّهُ اللَّهُ  وَمَنْ يَسْتَغْنِ يُغْنِهِ اللَّهُ  وَمَنْ يَتَصَبَّرْ يُصَبِّرْهُ اللَّهُ  وَمَا أُعْطِيَ أَحَدٌ عَطَاءً خَيْرًا وَأَوْسَعَ مِنْ الصَّبْرِ)) متفق عليه

 

Kutoka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: “Watu fulani miongoni mwa Answaar walimuomba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  naye akawapa. Kisha wakamuomba tena naye akawapa. Kisha wakamuomba tena naye akawapa, mpaka akamaliza chote alichokuwa nacho. Akawaambia baada ya kuwa ameshatoa kila kitu: ((Kheri yoyote niliyonayo siwezi kuwanyima, na mwenye kujizuia [kuomba] Allaah Atamjazi kwa kutokuomba, na mwenye kujikwasisha Allaah Atamkwasisha, na atakayejisubirisha Allaah Atampa subira. Hakuna yeyote aliyepewa zawadi bora na ilio kunjufu zaidi kuliko subira)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

La muhimu ni kwamba Muumini avumilie mtihani pale mwanzo anapopata taarifa ya msiba au mtihani. Hivyo ndivyo alivyofunzwa mwanamke aliyekuwa akilia mbele ya kaburi alozikwa kipenzi chake:

 

 

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه)  قَالَ: مَرَّ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِامْرَأَةٍ تَبْكِي عِنْدَ قَبْرٍ فَقَالَ:  ((اتَّقِي اللَّهَ وَاصْبِرِي)) قَالَتْ:  إِلَيْكَ عَنِّي فَإِنَّكَ لَمْ تُصَبْ بِمُصِيبَتِي وَلَمْ تَعْرِفْهُز فَقِيلَ لَهَا: إِنَّهُ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ. فَأَتَتْ بَابَ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَلَمْ تَجِدْ عِنْدَهُ بَوَّابِينَ فَقَالَتْ: لَمْ أَعْرِفْكَ. فَقَالَ: ((إِنَّمَا الصَّبْرُ عِنْدَ الصَّدْمَةِ الْأُولَى)) متفق عليه

 

وفي رواية مسلم "تبكي على صبي لها"

 

Kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu)  amesema: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alimpitia mwanamke analia mbele ya kaburi. Akamwambia: ((Mche Allaah na usubiri!)). Yule mwanamke akasema: “Niondokee, kwani hujafikwa na msiba kama wangu!”  Wala hakumjua. Akaambiwa: “Huyo alikuwa ni Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  Akaenda hadi katika mlango wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na hakuwakuta mabawabu [walinzi] akamwambia: “Nilikuwa sikujua kama ni wewe”. Akamwambia: ((Hakika subira wakati wake ni pale mwanzo wa kupata na msiba)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Na katika riwaayah ya Muslim imesema: “Alikuwa akimlilia mwanawe”

 

 

Katika Hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  zimetajwa fadhila zake mbali mbali ambazo hakika Muumini anapozitambua hutuliza  moyo wake, akapokea majaaliwa aliyokadiriwa na Rabb wake Aliyetukuka akakinai, akaridhika na akashukuru. Hapo ndipo itakapothibiti kwake kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

 

((عَجَبًا لإَمْرِ الْمُؤْمِنِ إِنَّ أَمْرَهُ كُلَّهُ خَيْرٌ, وَلَيْسَ ذَاكَ لإَحَدٍ إلاَّ لِلْمُؤْمِنِ. إِنْ أَصَابَتْهُ سَرَّاءُ شَكَرَ فَكَانَ خَيْرًا لَهُ, وَإِنْ أَصَابَتْهُ ضَرَّاءُ صَبَرَ فَكَانَ خَيْرًا لَهُ)) مسلم

 

((Ajabu ya jambo la Muumin kwamba kila jambo lakeni kheri. Na halipatikani hili isipokuwa kwa Muumin. Anapofikwa na jambo zuri hushukuru nayo ni kheri kwake na anapofikwa na jambo lenye madhara husubiri nayo ni kheri kwake)) [Muslim]

 

 

Miongoni mwa fadhila hizo:

 

 

1-Atakutana na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   akiwa hana tena madhambi:

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه)  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: (( مَا يَزَالُ الْبَلاَءُ بِالْمُؤْمِنِ وَالْمُؤْمِنَةِ فِي نَفْسِهِ وَوَلَدِهِ وَمَالِهِ حَتَّى يَلْقَى اللَّهَ وَمَا عَلَيْهِ خَطِيئَةٌ)) الترمذي وقال حديث حسن صحيح

 

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mtihani utaendelea kumpata Muumini mwanamume na Muumini mwanamke katika nafsi yake na watoto wake, na mali yake mpaka akutane na Allaah akiwa hana dhambi)) [At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth Hasan Swahiyh].

 

 

 

2-Alama ya mapenzi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  - Humtakia kheri mja Anapompa mtihani duniani.

 

 

عَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه)   قَال:َ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم: َ(( إِذَا أَرَادَ اللَّهُ بِعَبْدِهِ الْخَيْرَ عَجَّلَ لَهُ الْعُقُوبَةَ فِي الدُّنْيَا وَإِذَا أَرَادَ اللَّهُ بِعَبْدِهِ الشَّرَّ أَمْسَكَ عَنْهُ بِذَنْبِهِ حَتَّى يُوَافِيَ بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ)) وَ قال النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((إِنَّ عِظَمَ الْجَزَاءِ مَعَ عِظَمِ الْبَلَاءِ وَإِنَّ اللَّهَ إِذَا أَحَبَّ قَوْمًا ابْتَلَاهُمْ فَمَنْ رَضِيَ فَلَهُ الرِّضَا وَمَنْ سَخِطَ فَلَهُ السَّخَطُ)) رواه الترمذي وقال حديث حسن

 

Kutoka kwa Anas kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema: ((Allaah Anapompendelea mja Wake kheri, Humharakishia adhabu duniani. Na Allaah Anapomtakia mja Wake shari Humzuilia dhambi zake hata Amlipe Siku ya Qiyaamah)). Na amesema (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  ((Hakika malipo makubwa kabisa yapo pamoja na mtithani mkubwa, na hakika Allaah Anapopenda watu Huwapa mtihani. Basi atakayeridhika atapata radhi (za Allaah) na atakayechukia atapata ghadhabu)) [At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth Hasan]

 

 

 

3-Alama ya imani

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه)  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ:  ((مَثَلُ الْمُؤْمِنِ كَمَثَلِ الزَّرْعِ لاَ تَزَالُ الرِّيحُ تُمِيلُهُ وَلاَ يَزَالُ الْمُؤْمِنُ يُصِيبُهُ الْبَلاَءُ. وَمَثَلُ الْمُنَافِقِ كَمَثَلِ شَجَرَةِ االأرْزِ لاَ تَهْتَزُّ حَتَّى تَسْتَحْصِدَ)) متفق عليه

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema: ((Mfano wa Muumini ni kama mti ulio na rutuba, upepo unaupiga huku na kule, na ataendelea Muumini kufikwa na mitihani. Na mfano wa mnafiki ni kama mti wa seda [aina ya mti wa mbao ya mkangazi], hautikisiki hadi ung’olewe wote mara moja)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

4-Alama ya taqwa na daraja ya juu mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):  

 

عَنْ سَعْدِ بْنِ أّبِي وّقَّاصٍ (رضي الله عنه)  قَالَ: قُلْتُ يَا رَسُولَ اللَّهِ: أَيُّ النَّاسِ أَشَدُّ بَلآءً؟ قَالَ:  ((الأَنْبِيَاء،  ثُمَّ االأَمْثَلُ فَالأَمْثَلُ، فَيُبْتَلَى الرَّجُلُ عَلَى حَسَبِ دِينِهِ. فَإِنْ كَانَ دِينُهُ صُلْبًا اشْتَدَّ بَلآؤُهُ، وَإِنْ كَانَ فِي دِينِهِ رِقَّةٌ ابْتُلِيَ عَلَى حَسَبِ دِينِهِ. فَمَا يَبْرَحُ الْبَلاَءُ بِالْعَبْدِ حَتَّى يَتْرُكَهُ يَمْشِي عَلَى الْأَرْضِ مَا عَلَيْهِ خَطِيئَةٌ))  أخرجه  الترمذي) وقال: حسن صحيح. وابن ماجه وصححه الألباني 

Kutoka kwa Sa’iyd bin Abi Waqqaasw (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: Nilisema: “Ee Rasuli wa Allaah! Watu gani wanaopata mitihani migumu zaidi? Akasema: ((Manabii, kisha mfano wake, na mfano wake. Hupewa mtihani mtu kulingana na Dini [imani] yake. Ikiwa Dini yake ni imara, mtihani wake huwa mkubwa. Na ikiwa Dini yake ni dhaifu  hupewa mtihani kulingana na Dini yake. Husibiwa sana na mtihani mmojawapo hadi atatembea ardhini bila ya kuwa na dhambi)) [At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth Hasan Swahiyh, Ibn Maajah, na Al-Albaaniy kadhalika kasema ni Swahiyh].    

 

 

Aina yoyote ile ya mtihani huwa ni kheri kwa Muumini, kwani bila ya kufikwa na mitihani haitatambulika imani ya Muumini na pia kusingekuwa na fadhila kama hizo tulizoahidiwa ikiwa ni kwa kupewa mtihani mkubwa mno au mdogo mno kwa kadiri yoyote ile atakayojaribiwa nayo mtu, ikiwa ni wa kuhusu nafsi, kifo, maradhi, maudhi, au kupoteza mali, au maafa, au njaa n.k. Hata uwe mtihani huo japo ni mdogo kiasi cha mwiba, kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنهما)  عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ:  ((مَا يُصِيبُ الْمُسْلِمَ مِنْ نَصَبٍ وَلاَ وَصَبٍ وَلاَ هَمٍّ وَلاَ حُزْنٍ وَلاَ أَذًى وىَ غَمٍّ حَتَّى الشَّوْكَةِ يُشَاكُهَا إِلاَّ كَفَّرَ اللَّهُ بِهَا مِنْ خَطَايَاهُ))

Kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy na Abuu Hurayrah  (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema: ((Muislamu hatopatwa na tabu, wala maradhi, wala hamu wala huzuni wala udhia wala ghamu [sononeko] hata mwiba unaodunga isipokuwa Allaah Humfutia madhambi yake kwa sababu ya hayo)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

Ibnul-Qayyim (Rahimahu Allaah) katika kitabu chake Al-Fawaaid kuhusu maisha haya ya duniani na njia ya kuelekea kwa Allaah na mitihani anayokabiliana nayo Muumini. amesema: “Ee usiyekuwa imara, uko wapi na njia hii? Njia ile ambayo Aadam alitaabika, na Nuwh alilia kwa huzuni, na Al-Khaliyl [Ibraahiym] alirushwa motoni, na Ismaa’iyl alilazwa chini kuchinjwa, na Yuwsuf aliuzwa kwa bei ndogo mno na akabakia jela miaka kadhaa, na Zakariyyah alichinjwa kwa msumeno, na bwana mtawa Yahyaa alichinjwa, Ayyuwb aliteseka na madhara makubwa, na Daawuwd alilia kupita kiasi, ‘Iysaa aliwaponyesha masikini maradhi yao akatembea na mnyama mwitu kwa ajili hiyo, na mateso mangapi ya kila aina aliteseka Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akielekea katika njia? Nawe unaishi kwa burudani na mchezo?”  [Al-Fawaaid 1:42]

 

 

Ndugu Muislamu, kumbuka kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

لَا تَحْسَبُوهُ شَرًّا لَّكُم ۖ بَلْ هُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ﴿١١﴾

Msiichukulie kuwa ni shari kwenu, bali ni kheri kwenu. [An-Nuwr: 11]

 

Na pia:

 

وَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تُحِبُّوا شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٢١٦﴾

 

Na asaa mkachukia jambo na hali lenyewe ni kheri kwenu. Na asaa mkapenda jambo na hali lenyewe ni la shari kwenu. Na Allaah Anajua na nyinyi hamjui. [Al-Baqarah: 216]

 

 

Basi vumilia kwa subira njema ndugu Muislamu na usikate tamaa katika kutaraji rahmah ya Allaah kwani Nabiy Ya’quwb aliwapa usia wanawe alipofikwa na msiba kwamba:

 

وَلَا تَيْأَسُوا مِن رَّوْحِ اللَّـهِ ۖ إِنَّهُ لَا يَيْأَسُ مِن رَّوْحِ اللَّـهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْكَافِرُونَ ﴿٨٧﴾

 

na wala msikate tamaa na faraja ya Allaah; hakika hawakati tamaa na faraja ya Allaah isipokuwa watu makafiri. [Yuwsuf: 87]

 

 

 

 

Share

04-Swabrun Jamiyl: Subira Anaposibiwa Muislamu Na Maradhi

 

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)

 

04 - Subira Anaposibiwa Muislamu Na Maradhi

 

 

 

Muumini anapopata masaibu na mitihani ya maradhi anapaswa kuvumilia kwa kutegemea fadhila ambazo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Ameahidi, pamoja na malipo mema tele, nako ni kwa kuridhika na majaaliwa na si kwa kuchukia na kuhamanika kwani hayatomfaa hayo ila ni kujizidishia maumivu, maradhi na dhiki. Wala haipasi kulaani maradhi kwa vyovyote kwani mja atakuja kukosa fadhila kama alivyofundisha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 

عَنْ جَابِرُ بْنُ عَبْدِ اللَّهِ (رضي الله عنه)  أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ دَخَلَ عَلَى أُمِّ السَّائِبِ أَوْ أُمِّ الْمُسَيَّبِ فَقَالَ:  ((مَا لَكِ يَا أُمَّ السَّائِبِ)) أَوْ ((يَا أُمَّ الْمُسَيَّبِ تُزَفْزِفِينَ؟)) قَالَتْ:  "الْحُمَّى لاَ بَارَكَ اللَّهُ فِيهَا"  فَقَالَ: ((لاَ تَسُبِّي الْحُمَّى فَإِنَّهَا تُذْهِبُ خَطَايَا بَنِي آدَمَ كَمَا يُذْهِبُ الْكِيرُ خَبَثَ الْحَدِيدِ)) مسلم

 

Kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhwiya Allaahu 'anhu)   kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  aliingia kwa Ummu As-Saaib au Ummu Al-Musayyib akasema: ((Je, una nini ee Ummus-Saaib?)) Au ((Ee Ummul-Musayyib; unatetemeka?)) Akasema: “Homa Allaah Asiibariki [ilaaniwe]” Akasema: ((Usiitukane homa kwani inaondosha dhambi za mwana Aadam kama moto unavyoondosha takatataka katika chuma)) [Muslim]

 

 

Basi vuta subira ee ndugu Muumini na mshukuru Rabb wako kwa neema tulizoaahidiwa za kusubiri masaibu ili ufutiwe madhambi yako na uzidishiwe mema yako huko Akhera na upandishwe daraja yako mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   kama ilivyothibiti katika Hadiythi zifuatazo:

 

 

1-Kufutiwa Madhambi Na Kupandishwa daraja:

 

 

 عَنْ عَبْدِ اللَّهِ ابن مَسْعُودٍ (رضي الله عنه)  قَالَ دَخَلْتُ عَلَى رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَهُوَ يُوعَكُ، فَمَسِسْتُهُ بِيَدِي فَقُلْتُ:  "يَا رَسُولَ اللَّهِ، إِنَّكَ لَتُوعَكُ وَعْكًا شَدِيدًا" فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ:  ((أَجَلْ، إِنِّي أُوعَكُ كَمَا يُوعَكُ رَجُلاَنِ مِنْكُمْ)) فَقُلْتُ:  "ذَلِكَ أَنَّ لَكَ أَجْرَيْنِ؟"  فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ:  ((أَجَلْ)) ثُمَّ قَالَ: ((مَا مِنْ مُسْلِمٍ يُصِيبُهُ أَذًى مِنْ مَرَضٍ فَمَا سِوَاهُ إلاَّ حَطَّ اللَّهُ بِهِ سَيِّئَاتِهِ كَمَا تَحُطُّ الشَّجَرَةُ وَرَقَهَا)) متفق عليه

 

Kutoka kwa ibn Mas’uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: “Niliingia kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa anaugua homa. Nikamgusa kwa mkono wangu nikasema: Ee Rasuli wa Allaah! Hakika una homa kali?  Akasema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Ndio! Ninaugua kama wanavyougua wawili wenu)). Nikasema: “Je ni kwa sababu utapata thawabu mara mbili?”  Akasema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  ((Ndio)) kisha akasema: ((Hakuna Muislamu yeyote anayefikwa na dhara kutokana na maradhi au vingineveyo isipokuwa Allaah Atamfutia     madhambi yake mfano wa majani yanavyopuputika mtini)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

Na pia:

 عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) قَالَتْ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ:  ((مَا مِنْ مُصِيبَةٍ تُصِيبُ الْمُسْلِمَ إلاَّ كَفَّرَ اللَّهُ بِهَا عَنْهُ حَتَّى الشَّوْكَةِ  يُشَاكُهَا)) متفق

 

Kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:    ((Hakuna msiba wowote unaomsibu Muislamu isipokuwa tu Allaah Humfutia madhambi hata mwiba unaomchoma))  [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Na pia:

 

عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) قَالَتْ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُول:  ((مَا مِنْ مُسْلِمٍ يُشَاكُ شَوْكَةً فَمَا فَوْقَهَا إِلاَّ كُتِبَتْ لَهُ بِهَا دَرَجَةٌ وَمُحِيَتْ عَنْهُ بِهَا خَطِيئَةٌ)) مسلم

Kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amesema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Muislamu hafikwi na (dhara lolote la) kuchomwa mwiba au zaidi ya hivyo isipokuwa Allaah Atampandisha daraja na Atamfutia madhambi kwa ajili yake)) [Muslim]

 

 

 

2-Kuvumilia ili kupata Jannah:  

 

 

عن عَطَاءُ بْنُ أَبِي رَبَاحٍ قَالَ قَالَ لِي ابْنُ عَبَّاسٍ أَلاَ أُرِيكَ امْرَأَةً مِنْ أَهْلِ الْجَنَّةِ؟ قُلْتُ بَلَى. قَالَ: هَذِهِ الْمَرْأَةُ السَّوْدَاءُ أَتَتْ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَتْ:   إِنِّي أُصْرَعُ وَإِنِّي أَتَكَشَّفُ فَادْعُ اللَّهَ لِي. قَالَ:  ((إِنْ شِئْتِ صَبَرْتِ وَلَكِ الْجَنَّةُ وَإِنْ شِئْتِ دَعَوْتُ اللَّهَ أَنْ يُعَافِيَكِ)) فَقَالَتْ: أَصْبِرُ فَقَالَتْ: إِنِّي أَتَكَشَّفُ فَادْعُ اللَّهَ لِي أَنْ لاَ أَتَكَشَّفَ. فَدَعَا لَهَا  - متفق عليه

 

Kutoka kwa ‘Atwaa bin Abi Rabaah (Radhwiya Allaahu 'anhu)  amesema: “Ibn ‘Abbaas aliniambia: “Je nikuonyeshe mwanamke miongoni mwa watu wa Jannah?” Nikasema: “Ndio” Akasema: Huyu mwanamke mweusi alimwendea Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akasema: “Hakika mimi nina kifafa nami hukashifika   [ninapoanguka] basi niombee kwa Allaah”. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akasema: ((Ukitaka usubiri utapata Jannah, au ukitaka nimuombe Allaah Akuafu)) Akasema: Nitasubiri” Akasema tena: Hakika mimi nakashifika [nikianguka] basi mwombe Allaah nisikashifike” Akamuombea” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

3-Anayepotelewa na macho jazaa yake ni Jannah:

 

 

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه)  قَالَ: سَمِعْتُ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: ((إِنَّ اللَّهَ قَالَ: إِذَا ابْتَلَيْتُ عَبْدِي بِحَبِيبَتَيْهِ فَصَبَرَ عَوَّضْتُهُ مِنْهُمَا الْجَنَّةَ)) يُرِيدُ عَيْنَيْهِ-  البخاري

 

Kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu)   amesema: Nilimsikia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akisema ((Hakika Allaah Amesema: Nitakapomjaribu mja Wangu kwa kukosa vipenzi vyake viwili [macho yake] Nitambadilishia Jannh badala yake)) [Al-Bukhaariy].

 

 

Na kuumwa kuna faida zake ambazo ni:

 

  • Yanampofika maradhi mtu, humfanya atambue kwamba yeye ni dhaifu, hana uwezo wa kujiondoshea dhara inapomfika isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Hapo ndipo hutambua Qadar ya  Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na pia hukumbuka Majina  Yake Mazuri na Sifa Zake mbali mbali; mfano wa sifa mojawapo ya Allaah ni Ash-Shaafi’ [Mwenye Kuponyesha]

 

  • Humfanya mtu aliyekuwa katika ghaflah ya kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  arejee kwa Rabb wake kwa vile Ndiye anayemhitaji zaidi wakati huu, kwani Yeye Subhaanahu wa Ta’aalaa ni Pekee Atakayeweza kumwondoshea dhara. Tajiri awe tajiri vipi lakini yanapomfika maradhi huenda madaktari wakashindwa kumtibu hata kama atatumia mali yake yote ikiwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   Hakutaka apate hiyo shifaa; kwani hakuna shifaa ila shifaa Yake. Hivyo Muumini huwa karibu zaidi na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kwa du’aa zake anazomkabili kumwomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amuondoshee maradhi.

 

  • Muumini anapopatwa na maradhi humfanya atambue neema ya umri wake wa nyuma alipokuwa na afya, na hilo ni jambo la kushukuriwa anapotambua neema ya afya aliyokuwa nayo awali. Na hawezi kutambua na kushukuru yeyote isipokuwa Muumini tu.

 

  • Anapata kujifunza na kujua fadhila za kuugua na maradhi akatambua neema na mazuri aliyoahidiwa kama kufutiwa madhambi n.k. na hapo huzidishia iymaan yake na yaqini kuhusu Aliyoahidi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).    

 

Subira ya hali ya juu kabisa ni subira ya Nabiy Ayyuwb ('Alayhis-Salaam) ambaye alifikwa na mtihani wa kusibiwa mali, watoto na siha. Kwa kuvumilia kwake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Alimrudishia yote aliyoyapoteza. Hiyo ilikuwa ni subira ya aina ya pekee. Pia tunayo mafunzo ya subira kutokana na visa vya Manabii wengineo, Salaf Swaalih [wema waliopita] n.k. 

 

 

 

Share

05-Swabrun Jamiyl: Subira Katika Kuondokewa Na Vipenzi, Jamaa Wa Karibu

 

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)

 

 

05 - Subira Katika Kuondokewa Na Vipenzi, Jamaa Wa Karibu

 

 

Hatima ya mwana Aadam ni kuiaga hii dunia kwa kuwa ni makazi ya muda na starehe ndogo tu kulingana na maisha ya milele Peponi na mazuri yake yaliyoahidiwa katika Qur-aan na Sunnah. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):   

 

 

كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ ۗ وَإِنَّمَا تُوَفَّوْنَ أُجُورَكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۖ فَمَن زُحْزِحَ عَنِ النَّارِ وَأُدْخِلَ الْجَنَّةَ فَقَدْ فَازَ ۗ وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا مَتَاعُ الْغُرُورِ ﴿١٨٥﴾

Kila nafsi itaonja mauti. Na hakika mtalipwa kikamilifu ujira wenu Siku ya Qiyaamah. Basi atakayewekwa mbali na moto na akaingizwa Jannah kwa yakini amefuzu. Na uhai wa dunia si lolote ila ni starehe ya udanganyifu. [Aal-‘Imraan: 185]

 

 

La kutanabahi zaidi ni kwamba hakuna ajuaye wapi au lini mtu itamifikia siku na wakati wake wa kufariki. Hakuna yeyote aliyepewa ujuzi wake hata Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  hakutambulishwa. Na hili ni jambo miongoni mwa mambo matano ambayo Ametaja Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kwamba ujuzi uko Kwake Pekee:

 

إِنَّ اللَّـهَ عِندَهُ عِلْمُ السَّاعَةِ وَيُنَزِّلُ الْغَيْثَ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْأَرْحَامِ ۖ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَّاذَا تَكْسِبُ غَدًا ۖ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ بِأَيِّ أَرْضٍ تَمُوتُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ ﴿٣٤﴾

Hakika Allaah Ana elimu ya Saa na Anateremsha mvua na Anajua yale yaliyomo katika tumbo la uzazi na nafsi yoyote haijui nini itachuma kesho, na nafsi yoyote haijui itafia katika ardhi gani, hakika Allaah ni Mjuzi wa yote, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [Luqmaan: 34]

 

 

Muumini akumbuke kwamba watoto, mke au mume, wazee, ndugu, jamaa wa karibu, marafiki ni amana kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na hizi amana tumepewa ili tuzichunge na ziwe ni utulivu wa nyoyo na viliwazo vya macho yetu. Amana hizi ni mtihani kwetu kutazamwa kama tutazichunga na kutekeleza kama tulivyoamrishwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Hivyo basi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ana haki kuichukua amana Yake wakati wowote ule Alioupanga kumalizika muda wa kuchunga amana hiyo. Na Muumini asichukizwe na majaaliwa ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), bali anapoondokewa na kipenzi chake, aridhike kwa kushukuru na kuvumilia. Pia tumefunzwa kwamba mtu anapopatwa na msiba aombe du’aa ifuatayo ili Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Amjaalie kilicho bora kuliko kilichomuondokea.

 

((إِنَّا لِلَّهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ اللَّهُمَّ أْجُرْنِي فِي مُصِيبَتِي وَأَخْلِفْ لِي خَيْرًا مِنْهَا)) متفق عليه

Innaa liLLaahi wa-innaa Ilayhi raaji’uwn, Allaahumma Ajirniy fiy muswiybatiy wa-Akhlifliy khayram-minhaa

 

((Hakika sisi ni wa Allaah, na hakika sisi Kwake wenye kurejea, ee Allaah, Nilipe kwa msiba wangu na Nipe badala yake kilicho bora kuliko huo [msiba]))  [Muslim]

 

Kadhaalika, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametufunza kumtaazi [kumhani] aliyepatwa na msiba kwa kumuombea:

 

 ((إِنَّ للهِ ما أَخَذ، وَلَهُ ما أَعْـطـى، وَكُـلُّ شَيءٍ عِنْـدَهُ بِأَجَلٍ مُسَـمَّى. فَلْتَصْـبِر وَلْتَحْـتسِبْ))

Inna liLLaahi maa Akhadha walahu maa a’twaa, wakullu shay-in ‘Indahu biajalim-musammaa, faltahtasib waltaswbir

 

((Kwa hakika ni cha Allaah Alichokichukua na ni Chake Alichokitoa, na kila kitu Kwake kina muda maalum,  basi vumilia na taka malipo kwa Allaah)) [Al-Bukhaariy na Ahmad]  

 

 

Naye Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   alipofiwa na kipenzi chake; mwanawe Ibraahiym akiwa ni mtoto mchanga, alihuzunika na kuvumilia subira njema:

 

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه)  قَالَ: دَخَلْنَا مَعَ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَلَى أَبِي سَيْفٍ الْقَيْنِ وَكَانَ ظِئْرًا لإِبْرَاهِيمَ فَأَخَذَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِبْرَاهِيمَ فَقَبَّلَهُ وَشَمَّهُ. ثُمَّ دَخَلْنَا عَلَيْهِ بَعْدَ ذَلِكَ وَإِبْرَاهِيمُ يَجُودُ بِنَفْسِهِ فَجَعَلَتْ عَيْنَا رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ تَذْرِفَانِ فَقَالَ لَهُ عَبْدُ الرَّحْمَنِ بْنُ عَوْفٍ (رضي الله عنه)  وَأَنْتَ يَا رَسُولَ اللَّهِ؟ فَقَالَ: ((يَا ابْنَ عَوْفٍ إِنَّهَا رَحْمَةٌ)) ثُمَّ أَتْبَعَهَا بِأُخْرَى فَقَالَ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((إِنَّ الْعَيْنَ تَدْمَعُ, وَالْقَلْبَ يَحْزَنُ, ولاَ نَقُولُ إِلاَّ مَا يَرْضَى رَبُّنَا, وَإِنَّا بِفِرَاقِكَ يَا إِبْرَاهِيمُ لَمَحْزُونُونَ)) البخاري

Kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu)  ambaye amesema: “Tulingia pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   kwa sonara Abuu Sayfi na alikuwa mume wa mnyonyeshaji Ibraahiym [mtoto wa Nabiy Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam]. Akamchukua na akambusu na kumnusa (kwa kumbusu). Kisha akaingia nyumbani kwa Abuu Sayf na wakati huo Ibraahiym alikuwa katika pumzi yake ya mwisho  na macho ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) yakaanza kutoa machozi. ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf  (Radhwiya Allaahu 'anhu)    akasema: “Hata wewe unalia?” Akasema: ((Ee Ibn ‘Awf! Hii ni rahmah)) Kisha akalia zaidi na akasema: ((Macho yanatoa machozi na moyo unahuzunika lakini hatusemi isipokuwa yanayomidhisha Allaah. Ee Ibraahiym hakika tuna huzuni kwa kufarikiana nawe)) [Al-Bukhaariy]

 

Katika Hadiyth ifuatayo, tunapata mfano mzuri kabisa ya subira kuhusu kisa cha Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) na Abu Twalhah alipofariki mtoto wao ambaye alikuwa mwana pekee walioruzukiwa wakati huo:

 

عَنْ أَنَسِ (رضي الله عنه) قَالَ : كَانَ ابْنٌ لأَبِي طَلْحَةَ يَشْتَكِي ، فَخَرَجَ أَبُو طَلْحَةَ فَقُبِضَ الصَّبِيُّ ، فَلَمَّا رَجَعَ أَبُو طَلْحَةَ قَالَ : مَا فَعَلَ ابْنِي ؟، قَالَتْ أُمُّ سُلَيْمٍ وَهِيَ أُمُّ الصَبِيّ: هُوَ أَسْكَنُ مَا كَانَ،  فَقَرَّبَتْ إِلَيْهِ الْعَشَاءَ فَتَعَشَّى، ثُمَّ أَصَابَ مِنْهَا، فَلَمَّا فَرَغَ قَالَتْ: وَارُوا الصَّبِيَّ، فَلَمَّا أَصْبَحَ أَبُو طَلْحَةَ أَتَى رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَأَخْبَرَهُ فَقَالَ:  ((أَعْرَسْتُمُ اللَّيْلَةَ؟))، قَالَ : نَعَمْ، قَالَ : ((اللَّهُمَّ بَارِكْ لَهُمَا)). فَوَلَدَتْ غُلاَمًا، فَقَالَ لِي أَبُو طَلْحَةَ : احْمِلْهُ حَتَّى تَأْتِيَ بِهِ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، وَبَعَثَ مَعَهُ بِتَمَرَاتٍ  فَقَال:  ((أَمَعَهُ شَيْءٌ ؟)) قَالَ نَعَمْ: تَمَرَاتٌ، فَأَخَذَهَا النَّبِيُّ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَمَضَغَهَا ثُمَّ أَخَذَ مِنْ فِيهِ فَجَعَلَهَا فِي فِي الصَّبِيِّ، ثُمَّ حَنَّكَهُ وَسَمَّاهُ عَبْدَاللَّهِ.   متفق عليه .

 

وَفِي رِواية الْبُخاري: قَالَ ابن عُيَيْنَة:  فَقَالَ رَجُلٌ مِنْ الأَنْصَارِ فَرَأَيْتُ لَهُمَا تِسْعَةَ أَولاَدٍ كُلُّهُمْ قَدْ قَرَأَ الْقُرْآنَ،  يعني منْ أوْلاَدِ عَبْدُ الله الْمَوْلُود.

 

وَفِي رِوَايَة مسلم: 

مَاتَ ابْنٌ لأَبِي طَلْحَةَ مِنْ أُمِّ سُلَيْمٍ فَقَالَتْ لإَهْلِهَا: لاَ تُحَدِّثُوا أَبَا طَلْحَةَ بِابْنِهِ حَتَّى أَكُونَ أَنَا أُحَدِّثُهُ. فَجَاءَ فَقَرَّبَتْ إِلَيْهِ عَشَاءً فَأَكَلَ وَشَرِبَ. ثُمَّ تَصَنَّعَتْ لَهُ أَحْسَنَ مَا كَانَتْ تَصَنَّعُ قَبْلَ ذَلِكَ. فَوَقَعَ بِهَ،  فَلَمَّا أنْ  رَأَتْ أَنَّهُ قَدْ شَبِعَ وَأَصَابَ مِنْهَا قَالَتْ:  يَا أَبَا طَلْحَةَ!  أَرَأَيْتَ لَوْ أَنَّ قَوْمًا أَعَارُوا عَارِيَتَهُمْ أَهْلَ بَيْتٍ فَطَلَبُوا عَارِيَتَهُمْ, أَلَهُمْ أَنْ يَمْنَعُوهَا؟ قَالاَ.  فَقَالَتْ فَاحْتَسِبْ ابْنَكَ. قَالَ فَغَضِبَ ثُمَّ َقَالَ: تَرَكْتِنِي حَتَّى تَلَطَّخْتُ ثُمَّ أَخْبَرْتِنِي بِابْنِي؟ فَانْطَلَقَ حَتَّى أَتَى رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَأَخْبَرَهُ بِمَا كَانَ. فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ:  ((بَارَكَ اللَّهُ لَكُمَا فِي لَيْلَتِكُمَا)) قَالَ: فَحَمَلَتْ قَالَ: فَكَانَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فِي سَفَرٍ وَهِيَ مَعَهُ وَكَانَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِذَا أَتَى الْمَدِينَةَ مِنْ سَفَرٍ لاَ يَطْرُقُهَا طُرُوقًا فَدَنَوْا مِنْ الْمَدِينَةِ, فَضَرَبَهَا الْمَخَاضُ فَاحْتُبِسَ عَلَيْهَا أَبُو طَلْحَةَ،  وَانْطَلَقَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: يَقُولُ أَبُو طَلْحَةَ إِنَّكَ لَتَعْلَمُ يَا رَبِّ إِنَّهُ يُعْجِبُنِي أَنْ أَخْرُجَ مَعَ  رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِذَا خَرَجَ،  وَأَدْخُلَ مَعَهُ إِذَا دَخَلَ،  وَقَدْ احْتَبَسْتُ بِمَا تَرَى.  تَقُولُ أُمُّ سُلَيْمٍ: يَا أَبَا طَلْحَةَ مَا أَجِدُ الَّذِي كُنْتُ أَجِدُ،  انْطَلِقْ فَانْطَلَقْنَا،   وَضَرَبَهَا الْمَخَاضُ حِينَ قَدِمَا فَوَلَدَتْ غُلاَمًا. فَقَالَتْ لِي أُمِّي يَا أَنَسُ لاَ يُرْضِعُهُ أَحَدٌ تَغْدُوَ بِهِ عَلَى رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ،  فَلَمَّا أَصْبَحَ احْتَمَلْتُهُ فَانْطَلَقْتُ بِهِ إِلَى رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ. وَذَكَرَ تَمَامَ الْحَدِيث

Kutoka kwa Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu)  amesema: “Alikuwa mtoto wa Abuu Twalhah akiugua. Abuu Twalhah akasafiri. Mtoto akafariki. Abuu Twalhah aliporudi aliuliza: “Vipi hali ya mwanangu?” Ummu Sulaym - mama wa mtoto - akamwambia: “Ametulia zaidi ya alivyokuwa”. Akampelekea chakula cha jioni akala, kisha akalala na mkewe [wajakamiiana]. Alipomaliza, Ummu Sulaym akamwambia: “Kamzikeni mtoto”. Abuu Twalhah alipopambaukiwa, alimwendea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akamwelezea yaliyotokea. Akamwuliza: ”Je, usiku mlifanya harusi (mlijamiiana)?” Akamjibu: “Ndio”. Akaomba: ((Ee Allaah! Wabarikie)). Akazaa mvulana. Abuu Twalhah akaniambia: “Mbebe  umpeleke kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)”. Akapeleka na tende kadhaa. Akauliza: ((Ana kitu?)) Akajibu: “Ndio, tende kadhaa”  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akazichukua akazitafuna kisha akachukua zile tende zilokuwa mdomoni mwake akazitia katika kinywa cha mtoto, halafu  akamsugulia nazo (ili mtoto afyonze na kumeza) na akampa jina la ‘Abdullaah”    [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

Katika riwaayah nyingine ya Al-Bukhaariy:  “Ibnu ‘Uyaynah amesema: “Mtu mmoja katika Answaar alisema: “Nikawaona watoto tisa wamehifadhi Qur-aan” Yaani watoto wa ‘Abdullaah huyu aliyezaliwa”

 

 

Na katika riwaayah nyingine ya Muslim imesema: “Abuu Twalhah alifiwa na mtoto aliezaa naye kwa Ummu Sulaym. Ummu Sulaym akawaambia jamaa zake: “Msimweleze Abuu Twalhah mpaka mimi niwe ndiye nitakayemweleza” Alivyorudi, akampelekea chakula cha jioni, akala na akanywa, halafu akajipamba kuliko anavyojipamba siku zote. Akamjamii. Ummu Sulaym alipoona kuwa Abuu Twalhah ameshiba na amemjamii alimwambia: “Ee Abuu Twalhah! Niambie lau watu wameazima kitu kwa watu fulani kisha wao wakataka kitu chao kilichoazimwa je, walioazima wana haki ya kuwanyima?” Akajibu: “Hapana!” Akamwambia: “Basi taraji thawabu kwa msiba wa mwanao”. Abuu Twalhah akakasirika na akasema: “Umeniacha mpaka nimejichafua [kwa jimai] halafu ndio unaniambia habari ya mwanangu?”  Akaenda kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamweleza mambo yalivyokuwa. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akawaombea: ((Allaah Awabarikie katika usiku wenu)). Ummu Sulaym akabeba mimba. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa yumo safarini, naye [Ummu Sulaym] yuko naye. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapoingia Madiynah kutoka safari alikuwa haiingii usiku. Wakakaribia Madiynah. Ummu Sulaym akaanza kusikia uchungu wa uzazi. Abuu Twalhah akabaki nyuma. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akaendelea na safari. Abuu Twalhah akasema: “Ee Allaah! Hakika Unajua kwamba mimi hufurahishwa kusafiri pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  anaposafiri, na hupenda kurudi naye anaporudi, na nimezuilika kama Uonavyo”. Ummu Sulaym akasema: “Ee Abuu Twalhah! Sisikii tena uchungu niliousikia, tuondoke!”  Tukaondoka. Akapatwa na uchungu wa kuzaa walipokuwa wameshaingia Madiynah. Akajifungua mvulana. Mama yangu akaniambia: ‘Ee Anas, asinyonyeshwe na yeyote mpaka uende naye kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)”. Kulipopambazuka, nilimbeba nikaenda naye kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)…” Akaendela mpaka mwisho wa Hadiyth.

 

 

Tunapata pia mafunzo kutoka katika kisa cha Ummu Salamah alipofiwa na mumewe na baada ya kuomba du’aa alivyomfunza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaolewa naye (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عَنْ أُمِّ سَلَمَةَ (رَضِيَ الله عَنْهَا) قَالَتْ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) يَقُولُ: ((مَا مِنْ مُسْلِمٍ تُصِيبُهُ مُصِيبَةٌ فَيَقُولُ مَا أَمَرَهُ اللَّهُ،  إِنَّا لِلَّهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ،  اللَّهُمَّ أْجُرْنِي فِي مُصِيبَتِي وَأَخْلِفْ لِي خَيْرًا مِنْهَا،  إلاَّ أَخْلَفَ اللَّهُ لَهُ خَيْرًا مِنْهَا)) قَالَتْ: فَلَمَّا مَاتَ أَبُو سَلَمَةَ قُلْتُ أَيُّ الْمُسْلِمِينَ خَيْرٌ مِنْ أَبِي سَلَمَة أَوَّلُ بَيْتٍ هَاجَرَ إِلَى رَسُولِ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم).  ثُمَّ إِنِّي قُلْتُهَا فَأَخْلَفَ اللَّهُ لِي رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ).  قَالَتْ:  أَرْسَلَ إِلَيَّ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) حَاطِبَ بْنَ أَبِي بَلْتَعَةَ يَخْطُبُنِي لَهُ. فَقُلْتُ:  إِنَّ لِي بِنْتًا وَأَنَا غَيُورٌ فَقَالَ: ((أَمَّا ابْنَتُهَا فَنَدْعُو اللَّهَ أَنْ يُغْنِيَهَا عَنْهَا وَأَدْعُو اللَّهَ أَنْ يَذْهَبَ بِالْغَيْرَةِ))  مسلم

Kutoka kwa Ummu Salamah  (Radhwiya Allaahu ‘anhaa)  amesema: “Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Hakuna Muislamu anayefikwa na msiba akasema Alivyoamrishwa na Allaah: ‘Innaa liLLaahi wa innaa Ilayhi raaji’uwn, Allaahumma Ajirniy fiy muswiybatiy wa-Akhlif-liy khayram-minhaa’   [Hakika sisi ni wa Allaah, na hakika sisi Kwake wenye kurejea, ee Allaah, nilipe kwa msiba wangu na nipe badala yake kilicho bora kuliko huo [msiba)]’, hakuna ila Allaah Atampa kilicho bora kuliko [msiba] huo)). Abuu Salamah alipofariki akasema: Muislamu gani ni bora kuliko Abuu Salamah ambaye familia yake ilikuwa ya kwanza kuhama Hijrah kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)? Kisha nikaisema [du’aa hiyo] na Allaah Akanipa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) badala yake. Akasema: Rasuli wa Allaah, akamtuma Abuu Balta’ah anipose kwake nikasema: Mimi nina binti [anayenitegemea] nami nina tabia ya wivu. Akasema: ((Ama kuhusu binti yake tutamwomba Allaah Amtajirishe kwake [asiwe na jukumu naye], na namuomba Allaah Amuondoshee tabia ya wivu na hamaki)) [Muslim]

 

 

Hadiyth zifuatazo pia zinatupa fadhila za mwenye kusubiri baada ya kufiwa na ahli wake:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ : ((يَقُولُ اللَّهُ تَعَالَى:  مَا لِعَبْدِي الْمُؤْمِنِ عِنْدِي جَزَاءٌ، إِذَا قَبَضْتُ صَفِيَّهُ مِنْ أَهْلِ الدُّنْيَا، ثُمَّ احْتَسَبَهُ إِلاَّ الْجَنَّةُ)) البخاري  

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu)  kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Ta’aalaa amesema: Mja Wangu Muumini hana jazaa Nitakapomchukulia mpenzi wake katika watu wa dunia kisha akatarajia thawabu isipokuwa [atapata] Jannah)) [Al-Bukhaariy]

 

 

عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ (رضي الله عنه)  قَالَ : قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : ((مَا مِنَ النَّاسِ مُسْلِمٌ يَمُوتُ لَهُ ثَلاَثَةٌ مِنَ الْوَلَدِ لَمْ يَبْلُغُوا الْحِنْثَ، إِلاَّ أَدْخَلَهُ اللَّهُ الْجَنَّةَ بِفَضْلِ رَحْمَتِهِ إِيَّاهُمْ))  البخاري  

Kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu)   kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema: ((Muislamu yeyote atakayefiwa na watoto watatu wasiofikia umri wa kubaleghe, Allaah Atamuingiza Jannah kutokana na fadhila ya rahmah Yake kwao)) [Al-Bukhaariy]  

 

 

وعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه)  عَنِ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ : ((لاَ يَمُوتُ لأَحَدٍ مِنَ الْمُسْلِمِينَ ثَلاَثَةٌ مِنَ الْوَلَدِ فَتَمَسَّهُ النَّارُ إلاَّ تَحِلَّةَ الْقَسَمِ))  مسلم

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu)   kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Watoto watatu wakifariki wa Muislamu yeyote, moto hautamgusa isipokuwa kitimizwe kiapo)) [Muslim]

[kiapo cha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Suwrat Maryam Aayah: 71]

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه)  أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ لِنِسْوَةٍ مِنَ الْأَنْصَارِ: ((لاَ يَمُوتُ لِإِحْدَاكُنَّ ثَلاَثَةٌ مِنَ الْوَلَدِ فَتَحْتَسِبَهُ إِلاَّ دَخَلَتِ الْجَنَّةَ))  فَقَالَتِ امْرَأَةٌ مِنْهُنَّ : أَوِ اثْنَيْنِ يَا رَسُولَ اللَّهِ  قَالَ:  ((أَوِ اثْنَيْنِ))  متفق عليه

Kutoka kwa Abuu Huraryah (Radhwiya Allaahu 'anhu)  kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amewaambia wanawake wa Answaar: ((Yeyote miongoni mwenu atakayefiwa na watoto watatu akataraji [malipo], ataingia Jannah)) Akasema mmoja wa wanawake miongoni mwao: “Au hata wawili ee Rasuli wa Allaah?” Akasema ((Au hata wawili)) [Al-Bukhaariy, Muslim] 

 

Anayemshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  katika kifo cha mpenzi wake hujengewa nyumba Peponi inayoitwa Baytul-Hamd:

 

عَنْ أَبِي مُوسَى الأَشْعَرِيِّ (رضي الله عنه)  أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ:  ((إِذَا مَاتَ وَلَدُ الْعَبْدِ قَالَ اللَّهُ لِملاَئِكَتِهِ: قَبَضْتُمْ وَلَدَ عَبْدِي ،  فَيَقُولُونَ: نَعَمْ. فَيَقُولُ: قَبَضْتُمْ ثَمَرَةَ فُؤَادِهِ. فَيَقُولُونَ نَعَمْ. فَيَقُولُ مَاذَا قَالَ عَبْدِي؟ فَيَقُولُونَ: حَمِدَكَ وَاسْتَرْجَعَ. فَيَقُولُ اللَّهُ: ابْنُوا لِعَبْدِي بَيْتًا فِي الْجَنَّةِ وَسَمُّوهُ بَيْتَ الْحَمْدِ))

Kutoka kwa Abuu Muwsa Al-Ash’ariyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Anapofariki mtoto wa mja, Allaah Huwaambia Malaika: Mmechukua roho ya mwana wa mja Wangu? [Malaika] Husema: Ndio! Kisha Husema: Mmechukua tunda la moyo wake! Husema: Ndio. Kisha Husema: Amesema nini mja Wangu? Husema: Amekusifu na amesema kauli ya istirjaa’. Allaah Husema: Mjengeeni mja Wangu nyumba Jannah na iiteni ‘Baytul-Hamd’ [Nyumba ya Shukurani])) [Ahmad, At-Tirmidhiy na ameipa daraja Swahiyh Al-Albaaniy]

 

Istirjaa’ ni kusema [Innaa liLLaahi wa innaa Ilayhi raaji’uwn]

 

Basi uzuri ulioje wa fadhila na malipo mema kabisa kutoka kwa Rabb Mtukufu ambaye Haendi kinyume na ahadi Zake.

 

Mauti ni haki na hapana budi ila kuyakabili kwani dunia ni nyumba ya kupita na Aakhirah ndiko kwenye makazi ya kudumu milele. Bali dunia ni kama shamba la kufanyiwa juhudi kupandikiza mazuri na Aakhirah ndiko kwenye mavuno yake. Na duniani hakuna amana, hugeuka baina ya kheri na shari, baina ya dhiki na furaha, baina ya siha na afya baina ya utajiri na umaskini, hata mtu awe tajiri vipi bila shaka atakumbana na shari au dhiki fulani. Ama Aakhirah tumeahidiwa neema nyingi nzuri kabisa ambazo macho hayajapatapo kuona, wala masikio kusikia, wala kufikiria katika akili ya mwana Aadam. Na huko tumeahidiwa kukutana na vipenzi vyetu waliokuwa na msimamo wa Dini. Na pia kukutana na kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Manabii, na Maswiddiqiyn na Mashuhadaa, na waja wema wengineo. Na madamu hali ni hivyo, basi hakuna khiari ila kuvumilia na kuwa miongoni mwa waliosifiwa kuwa ni wenye kuvuta subira.

 

Kwa hiyo Muumini awe na matarajio ya kuipata Jannah yenye neema tele na kuokoka na moto. Na hilo litathibitika kwa subira kwani ndio ngazi ya kuifikia.

 

Share

06-Swabrun Jamiyl: Subira Katika Kutafuta Elimu

 

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)

 

 

06 - Subira Katika Kutafuta Elimu

 

 

Kutafuta elimu ni waajib kwa kila Muislamu. Na kuifanyia kazi kwa kufuata mafunzo yake, na kuitumia elimu kwa kufunza wengineo yote inahitaji subira; na subira zaidi inahitajika kwa kutokuharakiza kupata matokeo au kutokuchoka au kukata tamaa inapokuwa hali ngumu ambayo mtu hakuitegemea.  

 

Kuchuma elimu ni jambo tukufu kabisa kwa Muislamu kwani inafikisha kumtambua Rabb wake na kuyatambua yampasayo kutenda na yanayopasa kuepukana nayo. Kufanya hivyo ni alama ya kutakiwa kheri na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kama Anavyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما)، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((مَنْ يُرِدِ اللَّهُ بِهِ خَيْرًا، يُفَقِّهْهُ فِي الدِّينِ))   أخرجه الترمذي وغيره وقال: حَدِيثٌ حَسَنٌ صَحِيحٌ

Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa)  kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema: ((Anayekusudiwa kheri na Allaah, [Allaah] Humpa ufaqihi [ujuzi] katika Dini)) [At-Tirmidhiy na wengineo na amesema: Hadiyth Hasan Swahiyh]

 

 

Kheri hiyo ya kupata ujuzi wa Dini inampelekea Muislamu katika kheri kubwa zaidi ya kumfikisha kwenye makazi ya kudumu milele. Kwa hiyo ni dhahiri kuwa elimu ni ufunguo wa Jannah. Amethibitisha hilo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 

عن أَبِي الدَّرْدَاءِ (رضي الله عنه) قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: ((مَنْ سَلَكَ طَرِيقًا يَبْتَغِي فِيهِ عِلْمًا، سَلَكَ اللَّهُ بِهِ طَرِيقًا إِلَى الْجَنَّةِ)) مسلم 

Imepokelewa toka kwa Abuu Ad-Dardaa (Radhwiya Allaahu 'anhu)  amesema: Nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Anayetafuta njia ya kutaka elimu humo, Allaah Humpatia njia ya Jannah [Peponi])) [Muslim]

 

 

Fadhila nyingi mno za mwenye kutafuta elimu zimethibiti katika Qur-aan na Sunnah, ila Muislamu hawezi kuzidiriki bila ya kuwa na subira kwani anahitaji kuwa na uvumilivu katika kila hali atakapokuwa katika safari yake ndefu ya kutafuta elimu hata aweze kuifahamu kwa kina na akamilishe masomo yake. Ndipo tukawa tunahitaji kuomba Du’aa:

 

((الَّلهُمَّ انْفَعْنِي بِمَا عَلَّمْتَنِي وَعَلِّمْنِي مَا يَنْفَعُنِي وَزِدْنِيعِلْمًا))

Allaahumma Anfa’niy bimaa ‘Allamtaniy, wa ‘Allimniy maa yanfa’uniy wa-Zidniy ‘ilmaa.

 

((Ee Allaah, Ninufaishe kwa Unayonifunza, na nielimishe yatakayoninufaisha na nizidishie elimu))  [Swahiyh Ibn Maajah]

 

 

Yafuatayo ni mambo ambayo mtafutaji elimu (mwanafunzi), hana budi nayo na anapaswa kuyavumilia:

 

 

1-Kujifunza Qur-aan Na Hadiyth Pamoja Na Kuzihifadhi

 

 

Qur-aan ni somo linalohitaji subira kwani kuna mashaka ya kujifunza kuzitamka herufi za Qur-aan zipasavyo, kuihifadhi moyoni, na kuifanyia kazi maamrisho yake:

 

عَنْ عَائِشَةَ قَالَتْ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((الْمَاهِرُ بِالْقُرْآنِ مَعَ السَّفَرَةِ الْكِرَامِ الْبَرَرَةِ وَالَّذِي يَقْرَأُ الْقُرْآنَ وَيَتَتَعْتَعُ فِيهِ وَهُوَ عَلَيْهِ شَاقٌّ لَهُ أَجْرَانِ))  

Imetoka kwa mama wa Waumini 'Aaishah  (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema: ((Yule aliyekuwa hodari wa kusoma Qur-aan atakuwa pamoja na Malaika Waandishi wa Allaah watukufu wema, na yule ambaye anaisoma Qur-aan kwa mashaka na huku anajitahidi kwa kudodosa  atapata ujira mara mbili))  [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Hali kadhalika kujifunza na kuhifadhi Hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwani atazihitaji kuzifundisha kwa wengineo; jambo litakalompatia fadhila na malipo mema:

 

 

عن إبْنِ مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) ِ قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولُ الله صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: (( نَضَّرَ اللَّهُ امْرَأً سَمِعَ مِنَّا شَيْئًا فَبَلَّغَهُ كَمَا سَمِعَه، فَرُبَّ مُبَلِّغٍ أَوْعَى مِنْ سَامِعٍ)) وراوه الترمذي وقَالَ : حَدِيثٌ حَسَنٌ صَحِيحٌ  

Imepokelewa toka kwa ibn Mas’uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu)  ambaye amesema: Nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Allaah Amneemeshe mtu aliyesikia kitu kutoka kwetu naye akakifikisha kama alivyosikia. Huenda anayefikishiwa akawa mwenye kufahamu zaidi kuliko aliyesikia)) [At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth Hasan Swahiyh]

 

 

Masomo ya Dini yanahitaji uvumilivu na si pupa ili yathibitike na yafahamike vilivyo. Inahitaji pia kudurusiwa mara kwa mara ili isipotee moyoni baada ya kuthibitika kwani itakapopotea moyoni itakuwa ni khasara kubwa ya kupoteza muda wake wote, na pengine hata kupoteza mali aliyoitumia kwa ajili ya kuichuma elimu hiyo.  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  Ametunasihi:

 

 

عَنْ أَبِي مُوسَى عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((تَعَاهَدُوا الْقُرْآنَ فَوَالَّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ لَهُوَ أَشَدُّ تَفَصِّيًا مِنْ الْإِبِلِ فِي عُقُلِهَا))

Kutoka kwa Abuu Muwsa (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema:   ((Shikameni (dumisheni kuisoma) na Qur-aan, kwa hakika naapa kwa Ambaye nafsi yangu imo Mikononi Mwake, ni wepesi zaidi kukimbia (kupotea akilini) kuliko ngamia anavyochopoka katika kamba yake)) [Al-Bukhariy na Muslim]

 

 

Amesema ‘Umar ibn Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) “Tulikuwa tunahifadhi Aayah kumi na hatukuziendea nyingine mpaka tumezifanyia kazi (hizo kumi)”. Imesimuliwa pia kwamba alihifadhi Suwratul-Al-Baqarah katika muda wa miaka tisa, na hivyo si kwa ajili ya kuhifadhi au kuzijua maana yake tu, bali kuzifahamu kwa bayana na kwa kina na kutekeleza maamrisho yake na   kujiepusha na makatazo yake. Na hivyo ndivyo inavyompasa mwanafunzi au mtafutaji elimu kwani ni miongoni mwa mambo manne yanayowajibika kwa kila Muislamu kujifunza kama alivyoyaasisi Al-Imaam Muhammad ibn Al-Wahhaab katika Kitabu chake ‘Al-Uswuul Ath-Thalaathah’. 

 

 

2- Mwanafunzi Kujifunza Na Kutekeleza Adabu Za Kiuanafunzi:

 

 

Inampasa kwanza mwanafunzi ajifunze adabu za kiuanafunzi na  kuwa na subira pale anapokuwa hakufahamu anayoyaelezea mwalimu wake, na hivyo kwa kutokuuliza maswali mengi wakati mwalimu anaposomesha au kusherehesha darsa, bali asubiri hadi atakapomaliza. Pia awe na heshima mbele ya mwalimu kwa kumkabili kwa upole na adabu, kutimizia anayomwamrisha yanayohusiana na masomo yake. Kadhalika mwanafunzi anapaswa kutekeleza na kufuata taratibu za utafutaji elimu na kuwa na uvumilivu mkubwa katika hilo.

 

 

3-Kuamka Usiku Wa Manane:

 

 

Kufanya juhudi kuamka usiku hakuna budi kwa anayetafuta elimu kwa sababu ndio wakati wenye utulivu na muwafaka zaidi kwa masomo kwani Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):    

 

 إِنَّ نَاشِئَةَ اللَّيْلِ هِيَ أَشَدُّ وَطْئًا وَأَقْوَمُ قِيلًا﴿٦﴾

Hakika kuamka usiku (kuswali) ni uthibiti zaidi wa kuathiri moyo na kuifahamu na unyofu zaidi wa maneno kutua. [Al-Muzzammil: 6]

 

 

Lakini kunahitaji subira kwani kuna mashaka ya kukata mtu usingizi wake wakati watu wamelala. Avute subira kwa kuachilia mbali kitanda chake akaamka na akajiamsha zaidi kwa kutia wudhuu akasimama kuswali kisha akadurusu masomo yake. Anayetafuta elimu hana budi kukosa raha kwani hawezi mtu kuichuma elimu akiwa ameshuhgulishwa na raha za dunia. Imepokelewa kutoka kwa Yahyaa bin Yahyaa At-Tamiymiy amesema: “Abdullaahi bin Yahyaa bin Abi Kathiyr amesema: Nimemsikia baba yangu akisema: “Elimu haiwezekani kwa raha ya mwili” [Imesimuliwa na Muslim katika ‘Kitabu cha Misikiti Na Sehemu Za Swalaah - Mlango wa Swalaah Tano]

 

 

4- Kudurusu Masomo Na Kufanya Utafiti:

 

 

Subira katika kufanya utafiti na kufuatilia elimu japokuwa ni mbali mno pa kuipatia. Maswahaba na waja wema walisafiri maelfu na maelfu ya maili kwa ajili ya kutafuta elimu.

 

 

Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amekusanya maelfu ya Hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   alisema: “Swahibu zangu katika watu wa Makkah walikuwa wakijishughulisha na biashara masokoni, na swahibu zangu katika watu wa Madiynah walikuwa wakijishughulisha na kilimo, lakini mimi nilikuwa masikini niliyetumia muda wangu mwingi kukaa pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Nilikuwa nikihudhuria wasipohudhuria, na nikihifadhi wanaposahau.”

 

 

Imaam Ahmad bin Hanbal alitembea maili thelathini elfu kutafuta Hadiyth na akahifadhi maelfu ya Hadiyth, na akaacha nyuma yake hazina ya Vitabu.

 

Na Jaabir bin ‘Abdillaah alisafiri muda wa mwezi mmoja kwenda Misr kutafuta Hadiyth moja.

 

Imaam An-Nawawy ambaye aliishi muda wa miaka 45 lakini kwa muda huo wa maisha yake mafupi, alikuwa akitumia muda wake wote kutafuta elimu na kuifunza, hata hakuwa akila chakula kizuri na wala hakutamani kuoa.

 

 

 

5-Kuwa na Taqwa Na Utiifu;

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اصْبِرُوا وَصَابِرُوا وَرَابِطُوا وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٢٠٠﴾

Enyi walioamini! Subirini na zidini kuvuta subira na bakieni imara na mcheni Allaah ili mpate kufaulu. [Aal-‘Imraan: 200]

 

 

Huo ni wito kwa Waumini wote, na inawahusu zaidi watafutao elimu kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameihusisha Aayah na mafanikio ya dunia na Aakhirah kwa mambo manne; subira, kuzidi kuvuta subira,  kubakia imara na taqwa. Subira hiyo inajumuisha aina zote za subira; subira katika utiifu, kuacha maasi, kukubali Qadhwaa na Qadar (Yaliyohukumiwa na Yaliyokadiriwa), kuvumilia maudhi ya watu. Na kutafuta elimu kunampeleka mtu kwenye taqwa kwa kuwa atakuwa akitumia wakati wake wote katika kutafuta elimu, kujifunza, kutekeleza ‘ibaadah kusubiri Swalaah baada ya Swalaah, na kila aina ya ‘amali njema.Pia itamwongoza mtu katika tabia za upole, ukarimu n.k. ambazo humkurubisha mja kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Inahitaji pia kujiepusha na maasi kwani atakapoiendekeza mtu nafsi yake atatumbukia kwayo na kushughulishwa nayo hata asiweze tena kuwa na muda wa kutafuta elimu au akose kuwa na taqwa na utiifu. Yote hayo yanahitaji subira.

 

 

6-Kuhudhuria Vikao Vya Darasa, Mihaadhara Na Kusikiliza Kwa Makini”

 

 

Kuvuta subira katika kuhudhuria vikao vya darasa na mihadhara ya Dini hata kama si wakati muwafaka au uliouzoea kama alfajiri au usiku baada ya Swalaah ya ‘Ishaa,  kwa makini japokuwa akili imeshughulishwa na mengineyo. Kubakia hadi mwisho wa darsa ili ufaidikie na yote anayoyafundisha mwalimu japokuwa umechoka au una usingizi.  Aghlabu baadhi ya wanafunzi huanza masomo yao kwa hamu na juhudi kubwa lakini hawafiki hata robo yake huchoka na kukata tamaa kutokana na mashaka wanayokumbana nayo.

 

 

 7-Kuwa na Zuhd (Kuipa dunia mgongo):

 

 

Mwenye kutafuta elimu anapaswa pia kuwa na sifa ya zuhd ambayo inahitaji subira kwa sababu ni kukinaisha nafsi yake na matamanio ya dunia. Na kuipa mgongo dunia si jambo jepesi ila kwa ambaye Allaah Amemrehemu. Zuhd pia inamfanya mtu awe mnyenyekevu na inamjaza mapenzi ya kutangamana na masikini na walio dhaifu wenye taqwa na kuepukana na matajiri ambao wanaoshughulika na starehe za dunia badala ya kushughulika na mambo ya Aakhirah.  Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):   

 

وَاصْبِرْ نَفْسَكَ مَعَ الَّذِينَ يَدْعُونَ رَبَّهُم بِالْغَدَاةِ وَالْعَشِيِّ يُرِيدُونَ وَجْهَهُ ۖ وَلَا تَعْدُ عَيْنَاكَ عَنْهُمْ تُرِيدُ زِينَةَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَلَا تُطِعْ مَنْ أَغْفَلْنَا قَلْبَهُ عَن ذِكْرِنَا وَاتَّبَعَ هَوَاهُ وَكَانَ أَمْرُهُ فُرُطًا ﴿٢٨﴾

Na isubirishe nafsi yako pamoja na wale wanaomuomba Rabb wao asubuhi kabla jua kucha na jioni, wanataka Wajihi Wake. Na wala macho yako yasiwavuke kwa kutaka pambo la uhai wa dunia. Na wala usimtii Tuliyemghafilisha moyo wake na Ukumbusho Wetu akakafuata hawaa zake, na jambo lake limekuwa la kuzidi kuvuka mipaka. [Al-Kahf: 28]

 

 

Kupata mapenzi ya watu atakaowafanyia da’wah ni muhimu kwani kutawajengea imani na mlinganiaji au mwalimu;  na hivyo itasababisha kumsikiliza na kumfuata kwa sababu ya unyenyekevu wake kwao ambao unadhihirisha ikhlaas yake kwao kwa kutokujali manufaa ya kidunia. Juu ya hivyo ni kupata mapenzi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Ameusia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa Ummah wake:

 

 

عَنْ سَهْلِ بْنِ سَعْدٍ السَّاعِدِيِّ (رضي الله عنه) قَالَ: أَتَى النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ رَجُلٌ فَقَالَ: يَا رَسُولَ اللَّهِ ، دُلَّنِي عَلَى عَمَلٍ إِذَا أَنَا عَمِلْتُهُ أَحَبَّنِي اللَّهُ وَأَحَبَّنِي النَّاسُ. فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((ازْهَدْ فِي الدُّنْيَا يُحِبَّكَ اللَّهُ وَازْهَدْ فِيمَا فِي أَيْدِي النَّاسِ يُحِبُّوكَ)) إبن ماجه وغيره بأسانيد حسنة

Imepokelewa toka kwa Sahl bin Sa’iyd As-Saa’idiyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: “Alikuja mtu kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akamwambia: “Ee Rasuli wa Allaah! Nijulishe amali ambayo nikiifanya Allaah Atanipenda na watu pia watanipenda” Akasema: ((Ipe mgongo dunia Allaah Atakupenda, na uvipe mgongo vilivyomo kwa watu, watu watakupenda)) [Ibn Maajah na wengineo kwa isnaad Hasan]

 

 

Basi kuwa na zuhd ee mwanafuzi na daa’iy (mlinganiaji Dini] wakupende watu. Na kuwa na zuhd akupende Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kwani Yeye Hapendi mwenye kuifadhilisha dunia kabla ya Aakhirah, bali Ameilaani hiyo dunia na wakaazi wake isipokuwa watatu:

 

 

عن أبي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَال: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: (( أَلاَ إِنَّ الدُّنْيَا مَلْعُونَةٌ مَلْعُونٌ مَا فِيهَا إِلاَّ ذِكْرُ اللَّهِ ، وَمَا وَالاَهُ ، وَعَالِمٌ أَوْ مُتَعَلِّمٌ)) الترمذي وقال: حَدِيثٌ حَسَنٌ 

Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu)  amesema: “Nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akisema: ((Zindukeni! Dunia imelaaniwa, kimelaaniwa kilichomo humo isipokuwa kumtaja Allaah na jambo linalokaribiana na hilo (la kumtii Allaah), Mwanachuoni na anayejifunza [Dini])) [At-Tirmidhiy na amesema: Hadiyth Hasan]

 

 

Kwa hiyo ukiwa ni mwenye zuhd, ukashughulika kutafuta elimu na moyo wako ukawa umeelemea kwayo na ukajazwa mapenzi yake, shaytwaan hataweza kukughafilisha na dunia. Hutofikiria mali, wala kupata pato lolote kwa kazi yako ya da’awah, wala hutojikalifisha kuishi maisha ya raha, wala hutotamani starehe yoyote, kwani hakuna kitakachokushughulisha ila mambo matatu hayo ambayo yanamhusu mtafutaji elimu, kwa vile muda wako wote utakuwa ni kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), kutafuta elimu na kuifunza au kuibalighisha kwa wengineo, na hayo ni utiifu na ambayo yanahitaji subira ya kweli.  

 

Share

07-Swabrun Jamiyl: Subira Katika Da'wah (Ulinganiaji Wa Dini)

 

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)

 

 

07-Subira Katika Da’wah (Ulinganiaji Wa Dini)

 

 

 

Da’wah katika Dini hii tukufu ina fadhila nyingi mno kama zilivvyothibiti dalili zake katika Qur-aan na Sunnah. Daa’iyah (mlinganiaji) atakapoweza kuitekeleza kazi hii ipasavyo basi hakika atakuwa amebahatika kutekeleza kazi  tukufu  kabisa na ya hadhi  kwake, kwani huko ni kuendeleza majukumu ya Rusuli na Manabii waliowalingania watu wao kufuata haki. Na da’wah ni  amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)    kwa kila Muislamu na kwa hivyo ni jukumu la kila mmoja kulifanyia kazi kwa kuwaita  watu katika Tawhiyd (kumpwekesha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na  kuwakumbusha watu maneno na amri za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na Rasuli Wake    (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ili watu wabakie katika taqwa, iymaan, usalama na amani ya dunia na Aakhirah yao. Ndipo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Akaiambatanisha amri hiyo pamoja na mafaniko ya hakika. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):   

 

وَلْتَكُن مِّنكُمْ أُمَّةٌ يَدْعُونَ إِلَى الْخَيْرِ وَيَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ ۚ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفلِحُونَ ﴿١٠٤﴾

Na watokeze kutoka kwenu umati wa watu unaolingania kheri na unaoamrisha mema na unaokataza munkari. Na hao ndio waliofaulu. [Aal-‘Imraan: 104]

 

Akabainisha pia kwamba bila ya kulingania haki na kuusina na subira ni mambo yatakayomfanya mwana Aadam awe katika khasara [Suwrah Al-Aswr]

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   aliusia kazi hii pale aliposimama katika Jabali la ‘Arafah katika Hijjah yake ya mwisho baada ya kuwapa Maswahaba mawaidha na nasaha zake akahakikisha nao kuwaliza kama alitimizia risalah aliyotumwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa);  wakakiri Maswahaba hilo, kisha akawaamrisha:

 

(( أَلا فَلْيُبَلِّغِ الشَّاهِدُ مِنْكُمُ الْغَائِبَ))

((…basi abalighishe (afikishe ujumbe) aliyekuweko shahidi hapa miongoni mwenu kwa asiyekuweko)) [Al-Bukhaariy]

 

Kwa maana kila mmoja wao aendelee kubalighisha risala na mafunzo yake, kizazi baada ya kizazi mpaka kitakaposimama Qiyaamah. Na akausia pia katika kauli yake nyingine:

 

 ((بَلِّغُوا عَنِّي وَلَوْ آيَةً))

((Fikisheni kutoka kwangu (ujumbe) japo Aayah moja))   [Al-Bukhaariy]

 

 

Kauli hiyo ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inadhihirisha umuhimu mkubwa wa kila Muislamu kuamrisha mema na kukatazana maovu hata ikiwa ni Aayah au Hadiyth moja aliyojifunza kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Kulingania huko kuwe kwa baswiyra (nuru za elimu, dalili, hoja na umaizi) kama Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Alivyomuamrisha Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي﴿١٠٨﴾

Sema: “Hii ndio njia yangu nalingania kwa Allaah, juu ya nuru za elimu na umaizi, mimi na anayenifuata.  [Yuwsuf: 108]

 

 

Na baswiyrah ni elimu sahihi inayopatikana katika vyanzo vya kuaminika na kutoka kwa ‘Ulamaa wenye manhaj ya Salafus-Swaalih (Wema waliotangulia). Baswiyra pia ni hikma kama vile vile Alivyoamrisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ﴿١٢٥﴾

Lingania katika njia ya Rabb wako kwa hikmah na mawaidha mazuri. Na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi [An-Nahl: 125] 

 

 

Na da’wah ndio inayotengeneza Ummah kwa kuwatoa watu kutoka katika kiza kuingia katika Nuru, na  kutoka katika upotofu kuelekea hidaaya,     na kugeuza ubatilifu kwa haki, na kugeuza shari kwa kheri, na ndio maana imeambatinishwa na ukamilifu wa iymaan.

 

كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ﴿١١٠﴾ 

Mmekuwa Ummah bora kabisa uliotolewa (mfano) kwa watu; mnaamrisha mema na mnakataza munkari na mnamwamini Allaah [Aal-‘Imraan: 110]

 

Sharti kuu la da’wah ni kuweko ikhlaas kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).   Na inahitaji daa’iy (mlinganiaji) awe mnyenyekevu kwa   watu anaowalingania ili kusiweko alama ya kiburi, riyaa au aina yoyote ya kujifakharisha. Bali daa’iy awe mwenye tabia njema katika kauli zake na matendo yake:  Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَمَنْ أَحْسَنُ قَوْلًا مِّمَّن دَعَا إِلَى اللَّـهِ وَعَمِلَ صَالِحًا وَقَالَ إِنَّنِي مِنَ الْمُسْلِمِينَ﴿٣٣﴾

Na nani mwenye kauli nzuri zaidi kuliko yule anayelingania kwa Allaah na akatenda mema na akasema: “Hakika mimi ni miongoni mwa Waislamu.” [Fusw-Swilat: 33]

 

 

Na pia inahitaji subira ya hali ya juu kwani daa’iy wa mambo ya haki hataacha kukumbwa na mitihani mbali mbali. Na hiyo ndio jihadi ya kweli kwa kujirekebisha mtu tabia zake, kutumia wakati wake, mali yake na kila neema aliyoruzukiwa na Rabb wake katika kazi hii tukufu. Pia aweze kuvumilia maudhi ya watu, jambo ambalo haliepukani  kwa kila daa’iy. Na hapo inahitaji azimio kubwa la kuendeleza da’wah kama walivyovumilia Rusuli na Manabii. Luqmaan alipompa nasaha mwanawe alimkumbusha kuvuta subira katika kazi hii tukufu:

 

يَا بُنَيَّ أَقِمِ الصَّلَاةَ وَأْمُرْ بِالْمَعْرُوفِ وَانْهَ عَنِ الْمُنكَرِ وَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا أَصَابَكَ ۖ إِنَّ ذَٰلِكَ مِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ ﴿١٧﴾

 “Ee mwanangu! Simamisha Swalaah, na amrisha mema na kataza ya munkari, na subiri juu ya yale yatakayokusibu. Hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa. [Luqmaan: 17] 

 

 

Kwa hiyo daa’iy inampasa afuate nyendo za Rusuli na Manabii anaposibiwa na mitihani ya da’wah khasa kutokana na maudhi ya watu, kwani Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alivumilia mateso na maudhi ya Makafiri, Mayahudi na wanafiki waliomkadhibisha, wakamfanyia kila aina ya istihzai kwa kumwita mwendawazimu, mtungaji mashairi, kahini, mchawi, hata kufika kumpiga mawe lakini alivumilia na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   Akamlinda hadi Akaleta nusra Yake mpaka akasimamisha na kuineza Dini ya Kiislamu. Basi Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  awe ni kigezo bora kwa daa’iy wa Dini hii tukufu na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Haendi kinyume na ahadi Yake Anaposema:

 

 

إِنَّا لَنَنصُرُ رُسُلَنَا وَالَّذِينَ آمَنُوا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيَوْمَ يَقُومُ الْأَشْهَادُ﴿٥١﴾

Hakika Sisi Tutawanusuru Rusuli Wetu, na wale walioamini katika uhai wa dunia na Siku watakayosimama mashahidi. [Ghaafir: 51]

 

 

Kwa ahadi hiyo na nyinginezo za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), ziwe ni matumaini makubwa kwa Muislamu anayelingania watu katika haki na atawakali kwa Rabb wake akitarajia pia malipo mazuri kabisa ya Jannah ambako ndiko kwenye maisha ya milele. Wala hakutakuwa na usalama, amani, furaha wala mafaniko yoyote ila kwa kufuata maamrisho ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  ya kubalighisha risala ya Dini hii tukufu kwa watu wote kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   

 

هَـٰذَا بَلَاغٌ لِّلنَّاسِ وَلِيُنذَرُوا بِهِ وَلِيَعْلَمُوا أَنَّمَا هُوَ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ وَلِيَذَّكَّرَ أُولُو الْأَلْبَابِ﴿٥٢﴾

Hii (Qur-aan) ni ubalighisho wa risala kwa watu, na ili wawaonye kwayo, na ili wapate kujua kwamba hakika Yeye ni Muabudiwa wa haki Mmoja Pekee na ili wakumbuke (na wawaidhike) wenye akili. [Ibraahiym: 52]

 

Maonyo makali yamethibiti katika Qur-aan na Sunnah kwa kutokuitimiza kazi hii tukufu ya kuamrisha mema na kukatazana mema, japokuwa kutakuweko mitihani mbali mbali, na kwa hivyo hapana budi kuvuta subira na kutaraji malipo yake mazuri yasiyokuwa na hesabu.

 

 

 

 

Share

08-Swabrun Jamiyl: Subira Njema Ilivyo Na Daraja Za Subira

Subira njema

 

08 - Subira Njema Ilivyo Na Daraja Za Subira

 

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alimwamrisha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  kuvumilia subira njema kama Anavyosema:

 

 فَاصْبِرْ صَبْرًا جَمِيلًا﴿٥﴾

Basi subiri, subira njema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). [Al-Ma’aarij:  5]

 

Aayah hii tukufu imeteremka kumliwaza Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutokana na maudhi ya makafiri wa Makkah; maudhi ambayo yalimhuzunisha kupita kiasi, yakamtia dhiki. Na alipofariki ‘ammi yake Abuu Twaalib na mkewe Mama wa Waumini Khadiyjah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa)  huzuni juu ya huzuni ikamzidi ndipo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Akamteremshia Suwrat Yuwsuf ambayo ilikuwa ni ukumbusho kwake kwamba si pekee aliyefikwa na mitihani bali Manabii wenzake pia walifikwa na masaibu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kuhusu kauli ya Nabiy Ya’quwb katika Suwrah hiyo:

فَصَبْرٌ جَمِيلٌ﴿١٨﴾

Basi subira njema [Yuwsuf: 18, 83]

 

 Kwa hiyo nini hasa maana ya ‘Swabrun Jamiyl (subira njema)?’ Na je, kuna subira nyinginezo zisizokuwa ni njema? Subira zote zina malipo mema, lakini subira zinakhitilafiana kwa daraja. Salafus-Swaalih (Wema waliotangulia) wamesema: “Hakika subira ni nusu ya iymaan”. Na Ibnul Qayyim amesema katika ‘Madaarijus-Saalikiyn’: “Daraja za subira ni tatu:

 

 

Ya Kwanza: Swabrun biLLaah (Subira kwa Allaah): 

 

Nayo ni subira ya kutaka msaada Kwake Subhaanahu wa Ta’aalaa, na mwenye kuikusudia subira atambue kwamba Allaah Ndiye Mwenye kumpa uwezo wa kusubiri. Na kwamba subira ya mja ni kwa ajili ya Rabb wake na si kwa ajili ya nafsi yake kama Anavyosema Jalla wa ‘Alaa:

 وَاصْبِرْ وَمَا صَبْرُكَ إِلَّا بِاللَّـهِ ﴿١٢٧﴾

Na subiri (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), na haiwi subira yako isipokuwa kupitia kwa Allaah.  [An-Nahl: 127]

 

 

Kwa maana ikiwa Allaah Hatakupa uwezo wa kusubiri hutaweza kusibiri.

 

 

Ya Pili:  Swabrun liLLaah (Subira kwa ajili ya Allaah):

 

Nayo iwe sababu ya subira yako ni mahaba ya Allaah, na kutaka radhi Zake, na kujikurubisha Kwake na si kudhihirisha uwezo wa nafsi, wala kwa kusifiwa na watu kuhusu subira yako n.k., kwa ajili ya manufaa ya kidunia, bali kuvuta subira kwa ajili ya kupata mahaba ya Allaah na kutaka radhi Zake na kujikurubisha Kwake.

 

 

Ya Tatu:  Swabrun Ma’a-Allaah (Subira Pamoja Na Allaah):

 

Iwe hima ya mja ni matakwa na malengo yake ni ya kidini kwa Allaah. Na hukmu zake za kidini, akijisubirisha nafsi yake pamoja na yote hayo, yaani aiweke nafsi yake katika kuthibiti katika amri Zake na mahaba Yake Subhaanahu wa Ta’aalaa. Na subira ya aina hii ndiyo iliyo ngumu kabisa, nayo ndio subira ya Asw-Swswiddiqiyn.

 

 

Na subira ni kubakia katika utiifu, kuacha maasi na kuridhika na majaaliwa. Na hiyo ndio uthibitisho wa iymaan. Inapomfikia mtu neema hushukuru, na unapomsibu msiba husubiri. Hivyo ndivyo inavyopasa kumwabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  katika furaha na misiba, na ndipo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Akajumuisha hayo katika kauli Yake:

 

 إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّكُلِّ صَبَّارٍ شَكُورٍ﴿٥﴾

Hakika katika hayo kuna Aayaat (ishara, zingatio, mafunzo) kwa kila mwingi wa kusubiri na kushukuru. [Ibraahiym: 5, Luqmaan: 31, Sabaa: 19, Ash-Shuwraa:  33]

 

 

Hizo ndizo sifa za mwenye subira njema, aliyekuwa ni mwingi wa kushukuru katika kila hali. Kwa hiyo, maana ya subira njema ni kuvumilia mitihani na masaibu bila ya kulalamika kwa watu, kuhamanika, kuweweseka, kutokuridhika na majaaliwa, au kukata tamaa hata afikie mtu kutaka kujiangamiza. Ni bora aache moyo wake uumie na uhuzunike, jicho lake litoke chozi la kiasi, ulimi wake ujizuie usije kutamka yasiyopasa, lakini abakie mtu katika subira akitegemea malipo mema.

 

 

 Hivyo ndivyo alivyosubiri Nabiy Ya’quwb ('Alayhis-Salaam)   walipomjia wanawe kumpa habari ya mwanawe Yuwsuf kwamba kaliwa na mbwa mwitu na pia alipozuiliwa mwanawe Bin-Yamiyn Misr na wakampasha habari hiyo waliporudi   msafara, hapo   akasema Nabiy Ya’quwb ('Alayhis-Salaam):

 

 فَصَبْرٌ جَمِيلٌ ۖ وَاللَّـهُ الْمُسْتَعَانُ عَلَىٰ مَا تَصِفُونَ﴿١٨﴾

Basi subira njema, na Allaah ni Mwenye kuombwa msaada juu ya mnayoyavumisha.” [Yuwsuf: 18]

 فَصَبْرٌ جَمِيلٌ ۖ عَسَى اللَّـهُ أَن يَأْتِيَنِي بِهِمْ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ ﴿٨٣﴾

Basi subira ni njema. Asaa Allaah Aniletee wote pamoja. Hakika Yeye Ndiye Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote.” [Yuwsuf: 83]

 

 

Subira njema pia ni pale Nabiy Yuwsuf ('Alayhis-Salaam) alipotupwa kisimani na nduguze, akapitishiwa mbele ya wanawake wa mji ili iwadhihirikie uzuri wake wa ajabu hata wakajikata vidole vyao. Kisha akasingiziwa kuwa amemtaka mke wa al-'Aziyz akatiwa jela. Kisha walipokuja ndugu zake kutaka chakula katika hazina iliyoko chini ya milki yake, wakatambuana nao wakakiri makosa yao wakasema:

 

 تَاللَّـهِ لَقَدْ آثَرَكَ اللَّـهُ عَلَيْنَا وَإِن كُنَّا لَخَاطِئِينَ ﴿٩١﴾

 “Tunaapa Allaah! Kwa yakini Allaah Amekustahabu kuliko sisi, nasi bila shaka tulikuwa wakosa.” [Yuwsuf: 91]

 

Naye akawajibu:

 لَا تَثْرِيبَ عَلَيْكُمُ الْيَوْمَ ۖ يَغْفِرُ اللَّـهُ لَكُمْ ۖ وَهُوَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ ﴿٩٢﴾

 “Hakuna lawama juu yenu leo. Allaah Atakughufurieni. Naye ni Mbora zaidi wa kurehemu kuliko wengine wote wenye kurehemu.” [Yuwsuf: 92]

 

 

Na pale Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliporudi Twaaif baada ya kufukuzwa kwa kupigwa mawe akamjia Malaika kumuuliza kama anataka awaangushie majabali mawili watu wa Twaaif waangamizwe. Lakini yeye alikataa akajibu: ((Bali nataraji Allaah Atoe katika migongo yao mwenye kumuabudu Allaah peke Yake bila ya kumshirikisha na chochote)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 Pia subira ya Nabiy Ayyuwb ('Alayhis-Salaam) aliyefikwa na mitihani ya kila aina; maradhi aliyouguwa miaka kumi na nane, msiba wa kuondokewa na watoto na mali yake yote, lakini juu ya hivyo alivumilia bila ya kulalamika, bali aliendelea bila ya kusita na ‘ibaadah zake na huku akimshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) hadi mwishowe aliomba ni:

 

 أَنِّي مَسَّنِيَ الضُّرُّ وَأَنتَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ ﴿٨٣﴾

 “Hakika mimi imenigusa dhara, Nawe Ndiye Mbora zaidi wa kurehemu kuliko wengine wote wenye kurehemu”. [Al-Anbiyaa: 83]

 

 

Nabiy Ibraahiym pia watu wake walipoumuingiza katika moto akavumilia na kutawakali kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ambaye Aliubadilisha moto kuwa baridi. Na pindi alipomlingania baba yake kwa maneno mazuri ya adabu, heshima, hikma na ujuzi aache kuabudu masanamu [Maryam: 41-45]  lakini jibu la baba yake likawa:

 

 أَرَاغِبٌ أَنتَ عَنْ آلِهَتِي يَا إِبْرَاهِيمُ ۖ لَئِن لَّمْ تَنتَهِ لَأَرْجُمَنَّكَ ۖ وَاهْجُرْنِي مَلِيًّا ﴿٤٦﴾

 “Unachukia waabudiwa wangu ee Ibraahiym? Usipokoma, bila shaka nitakupiga mawe; na niondokelee mbali kwa muda mrefu!” [Maryam: 46]

 

 

Juu ya ujeuri na tisho la baba yake, Ibraahiym ('Alayhis-Salaam)  hakulipiza ujeuri bali alivumilia na akamjibu kwa upole kabisa na kumtakia amani:

 

 سَلَامٌ عَلَيْكَ ۖ سَأَسْتَغْفِرُ لَكَ رَبِّي ۖ إِنَّهُ كَانَ بِي حَفِيًّا ﴿٤٧﴾

 “Amani iwe juu yako. Nitakuombea maghfirah kwa Rabb wangu. Hakika Yeye daima kwangu ni Mwenye huruma sana.”

 

 وَأَعْتَزِلُكُمْ وَمَا تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ وَأَدْعُو رَبِّي عَسَىٰ أَلَّا أَكُونَ بِدُعَاءِ رَبِّي شَقِيًّا ﴿٤٨﴾

 “Na natengana nanyi na mnavyoviomba pasi na Allaah; na namuomba Rabb wangu asaa nisijekuwa kwa kumwomba Rabb wangu, mwenye kukosa baraka.” [Maryam: 47-48]

 

 

 Subira Njema Katika Utiifu

 

Subira katika utiifu ni bora zaidi mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kuliko subira katika misiba na mitihani kwa sababu subira ya misiba na mitihani ni subira ya kulazimika mtu kutokana na majaaliwa, kwa maana hana budi nayo wala hana khiari ya kuyakataa. Ama subira katika utiifu na kujiepusha na maasi ni subira ya khiari yake mtu, na hiyo inahitaji azimio la nguvu. Mfano Nabiy Yuwsuf ('Alayhis-Salaam) alipomkataa mke wa al-‘aziyz pale alipomtongoza ilhali mwanamke huyo alikuwa ni mwenye uzuri na mali na kisha walikuwa peke yao wawili chumbani. Hali kama hiyo ni nyepesi kabisa kumpeleka mtu katika maasi, lakini pale mtu anapomlaani shaytwaan na akaacha kuiendekeza nafsi na matamanio, basi hiyo ndio aina ya subira njema.

 

 

Pia, Siku ya Fat-h (ushindi wa) Makkah walipokamatwa makafiri mbele ya Ka’bah baada ya kuwa walimfanyia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kila aina ya maudhi na kila njia za kumzuia asilinganie risala ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), na wakamfukuza Makkah – basi siku hiyo walidhania kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) atalipiza kisasi, lakini aliwaambia: ((Nendeni, nyinyi mmeachiwa huru)) Yaani nimekusameheni [Ar-Rahiyq Al-Makhtuwm] 

 

 Hali kadhalika, kijana anapokuwa hana uwezo wa kuoa, akazuia matamanio yake kwa kufuata amri ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 عن عبد الله بن مسعود (رضي الله عنه) قال: كُنَّا مَعَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ  شباباً لا نجد شيئا   فَقَالَ لَنَا: ((يَا مَعْشَرَ الشَّبَابِ مَنِ اسْتَطَاعَ مِنْكُمُ البَاءَةَ فَلْيَتَزَوَّجْ، فَإِنَّهُ أَغَضُّ لِلْبَصَرِ، وَأَحْصَنُ لِلْفَرجِ، وَمَنْ لَمْ يَسْتَطِيعْ فَعَلَيْهِ بِالصَّوْمِ، فَإِنَّهُ لَهُ وَجَاءٌ.)) رواه البخاري ومسلم .

Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin Mas’uwd   (Radhwiya Allaahu 'anhu)  “Tulikuwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na hali bado ni vijana na hatuna uwezo wa mali. Basi akatuambia: ((Enyi vijana! Mwenye kuweza kuoa na aoe, kwani kuoa kunamsaidia yeye kuinamisha macho yake [kutotazama ya haraam] na kuhifadhi tupu yake [kutofanya zinaa na uchafu mwingine], na yule asiye na uwezo wa kuoa, afunge, maana swawm hupunguza matamanio ya kimwili)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 Zaidi ya hayo ni kwamba  Subira Njema ni pale mwanzo tu pindi mtu anapopata habari ya msiba kama ilivyothibiti katika kisa cha mwanamke aliyekuwa akilia mbele ya kaburi la kipenzi chake.  Rejea Mlango wa ‘Subira Katika Mitihani Kwa Ujumla’

 

 Kauli za Salaf Kuhusu Subira:

 

 ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu):  “Maisha yaliyokuwa bora kabisa kwetu ni yale tuliyokumbana  na subira”

 

Hasan Al-Baswry: “Subira ni hazina miongoni mwa hazina. Lakini Allaah Hampi mtu isipokuwa mja karimu mbele Yake”

 

 ‘Umar bin ‘Abdil-‘Aziyz: “Hakuna neema yoyote Anayomneemsha Allaah mja Wake kisha akaiondoa na badala yake Akambadilishia kwa subira, ila huwa ile Aliyoibadilisha (mtihani na misiba) huwa ni kheri kuliko Aliyoiondoa (neema)”

 

Ibnul-Qayyim katika Madaarij As-Saalikiyn: “Subira imehusishwa na  yakini, iymaan, taqwa, kutawakali, shukurani, ‘amali njema na rahmah. Na ndio maana subira ikawa kama sehemu ya kichwa na iymaan ikawa kama mwili, na hivyo hakuna iymaan kwa asiyekuwa na subira kama vile haiwezekani kuweko mwili bila ya kichwa”

 

 

Share

09-Swabrun Jamiyl: Yapasayo Na Yasiyopasa Wakati Wa Mitihani

 

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)

 

09 - Yapasayo Na Yasiyopasa Wakati Wa Mitihani

 

 

 

Swabrun Jamiyl (subira njema) ni kuzuia ulimi usinene yasiyopasa wala kumshtakia yeyote isipokuwa kumshtakia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), na pia moyo uvumilie asimahanike mtu na kukata tamaa, na viungo visitende yaliyoharamishwa kama kujipigia mashavu na kuchana nguo n.k., basi Muumini anapaswa  kuzingatia na kutekeleza au kujiepusha yafuatayo:

 

 

 1-Kuridhika Na Majaaliwa Na Kusalimu Amri:

 

 

Muumini atambue kwamba kila linalomfika ni majaaliwa yaliyokwishahukumiwa katika Lawhum-Mahfuudhw (Ubao Uliohifadhiwa), kwa hiyo hana budi nayo, bali aridhike nayo apate radhi za Rabb wake na ujira wa kuvumilia. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ﴿٢٢﴾

Hausibu msiba wowote katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa umo katika Kitabu kabla hatujautokezesha. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.

 

لِّكَيْلَا تَأْسَوْا عَلَىٰ مَا فَاتَكُمْ وَلَا تَفْرَحُوا بِمَا آتَاكُمْ ۗ وَاللَّـهُ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ ﴿٢٣﴾

Ili msisononeke juu ya yale yaliyokuondokeeni na wala msifurahie kwa yale Aliyokupeni (Allaah); na Allaah Hapendi kila mwenye kujinata, anayejifakharisha. [Al-Hadiyd: 22-23]

 

 

Bali Muumini anapaswa kuwa na tawakuli na Allaah na akumbuke kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

قُل لَّن يُصِيبَنَا إِلَّا مَا كَتَبَ اللَّـهُ لَنَا هُوَ مَوْلَانَا ۚ وَعَلَى اللَّـهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ﴿٥١﴾

Sema: “Halitusibu (lolote) isipokuwa lile Alilotukidhia Allaah. Yeye ni Maulaa wetu.” Basi kwa Allaah watawakali Waumini. [At-Tawbah: 51]

 

 

Na huko ndiko kuthitibisha iymaan ya Muumini kwa  kuridhika na majaaliwa kama Anavosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa): 

 

 مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۗ وَمَن يُؤْمِن بِاللَّـهِ يَهْدِ قَلْبَهُ ۚ وَاللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ﴿١١﴾

Hausibu msiba wowote isipokuwa kwa idhini ya Allaah. Na yeyote   anayemuamini Allaah, (Allaah) Huuongoza moyo wake. Na Allaah kwa kila kitu ni Mjuzi. [At-Taghaabun: 11]

 

 

 

2- Kutokushitaki Au Kumlalamikia Kwa Watu Masaibu Na Mitihani Bali Kumuomba Allaah:

 

 

Kulalamika au kushitaki kwa watu kunaharibu subira na kumkosesha mtu fadhila zake, kwani anayeshtaki mitihani ya Rabb wake kwa kiumbe huwa amemshtakia ambaye hawezi kumnufaisha au kumuokoa katika mitihani yake. Lililo la busara ni amshtakie Rabb wake Ambaye ni Pekee Mwenye uwezo wa kumteremshia rahamh Akampa faraja.  Mmoja miongoni mwa Salafus-Swaalih alipomuona mtu anamshtakia mwenziwe alimwambia:

 

Vipi unamshtaki Anayekurehemu kwa asiyekuwa na uwezo wa kukurehemu?”

 

Tumepta fundisho bora kutoka kwa Nabiy Ya'aquwb ('Alayhis-Salaam) pale alipojazwa na huzuni kwa kumkumbuka mwanawe mpenzi Yuwsuf na kisha kupotelewa na mwanawe wa pili bin Yamiyn pindi aliposema:

 

 إِنَّمَا أَشْكُو بَثِّي وَحُزْنِي إِلَى اللَّـهِ﴿٨٦﴾

 “Hakika mimi nashitakia dhiki ya majonzi yangu na huzuni zangu kwa Allaah  [Yuwsuf: 86]

 

Lakini inafaa kumshtakia mtu pale anapofikwa na hali ya kuhitaji msaada wa mtu aliojaaliwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na si msaada ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   Pekee Ndiye Mwenye uwezo nao. Mfano, kulalamika dhulma anayotendewa na mwenzake inayoendelea ikiwa anayeshtakiwa ana mamlaka ya kumwepusha na anayemdhulumu, au anapotafuta msaada wa gharama za matibabu ya maradhi yake, au kuomba msaada wa kutatua jambo fulani gumu n.k. kwa kuitikadi kwamba uwezo huo unatokana na Nguvu na Uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Aliomjaalia huyo msaidizi.  

 

 

 

 3- Kuomba Maghfirah Na Toba

 

 

 Huenda ikawa mitihani inayomsibu mtu ni kutokana na madhambi aliyoyatenda hivyo ni vyema arudi kwa Rabb wake kuomba maghfirah na toba. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 ظَهَرَ الْفَسَادُ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ بِمَا كَسَبَتْ أَيْدِي النَّاسِ لِيُذِيقَهُم بَعْضَ الَّذِي عَمِلُوا لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ ﴿٤١﴾

Ufisadi umedhihiri katika nchi kavu na baharini kwa sababu ya yale iliyochuma mikono ya watu ili (Allaah) Awaonjeshe baadhi ya ambayo wameyatenda ili wapate kurejea. [Ar-Ruwm: 41]

 

Na Anasema pia:

 

وَمَا أَصَابَكُم مِّن مُّصِيبَةٍ فَبِمَا كَسَبَتْ أَيْدِيكُمْ وَيَعْفُو عَن كَثِيرٍ﴿٣٠﴾

Na haukusibuni katika msiba wowote basi ni kwa sababu ya yale yaliyochuma mikono yenu, na Anasamehe mengi.  [Ash-Shuwraa: 30]

 

 

 

 4-Kumdhukuru Na Kumshukuru Mno Allaah

 

 

 Kila unapomdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Naye Hukukumbuka. Kauli nzuri iliyoje Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anaposema:

 

 فَاذْكُرُونِي أَذْكُرْكُمْ وَاشْكُرُوا لِي وَلَا تَكْفُرُونِ﴿١٥٢﴾

Basi nidhukuruni na Mimi Nitakukumbukeni; na nishukuruni wala msinikufuru.  [Al-Baqarah: 152]

 

 

Tunajua kwamba kila kheri na shari ni mtihani kwetu, na katika hali zote inatupasa kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  ili kudhihirisha yakini ya kuamini Qadhwaa na Qadar  Rejea Mlango Wa ‘Maana Na Aina Za Subira’. Na hivo ndivyo ilivyo sifa ya Muumini bali huwa ni jambo la kuwastaajibsha wengineo kwa sifa yake hiyo ya ukamilifu wa iymaan:

 

))عَجَبًا لإَمْرِ الْمُؤْمِنِ إِنَّ أَمْرَهُ كُلَّهُ خَيْرٌ، وَلَيْسَ ذَاكَ لإَحَدٍ إلاَّ لِلْمُؤْمِنِ. إِنْ أَصَابَتْهُ سَرَّاءُ شَكَرَ فَكَانَ خَيْرًا لَهُ، وَإِنْ أَصَابَتْهُ ضَرَّاءُ صَبَرَ فَكَانَ خَيْرًا لَهُ)) مسلم

((Ajabu ya jambo la Muumin kwamba kila jambo lake ni kheri. Na halipatikani hili isipokuwa kwa Muumin. Anapofikwa na jambo zuri hushukuru nayo ni kheri kwake na anapofikwa na jambo lenye madhara husubiri nayo ni kheri kwake))  [Muslim]

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Ameahidi kwamba kila mara mja Wake anapomshukuru, Humzidishia neema, na anapokanusha basi ametoa onyo la adhabu kali.

 

 وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكُمْ لَئِن شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ ۖ وَلَئِن كَفَرْتُمْ إِنَّ عَذَابِي لَشَدِيدٌ﴿٧﴾

 

Na pindi Alipotangaza Rabb wenu: “Ikiwa mtashukuru, bila shaka Nitakuzidishieni (neema Zangu); na mkikufuru, basi hakika adhabu Yangu ni kali. [Ibraahiym: 7]

 

 

Na Muislamuu kutokuridhika na majaaliwa ya Allaah, ni aina mojawapo ya kukanusha au kukufuru hukmu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kwani hakuna mtihani au msiba unaomsibu mtu isipokuwa kwa amri Yake. Lililo la muhimu kwa mja ni kusalimu amri, kuridhika na kutegemea malipo mema ya duniani na Aakhirah. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  baada ya kauli Yake kuhusu kifo cha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  wakati walipofadhaika Maswahaba hata wakafikia kutokuamini kuwa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amefariki:

 

 وَمَا مُحَمَّدٌ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِ الرُّسُلُ ۚ أَفَإِن مَّاتَ أَوْ قُتِلَ انقَلَبْتُمْ عَلَىٰ أَعْقَابِكُمْ ۚ وَمَن يَنقَلِبْ عَلَىٰ عَقِبَيْهِ فَلَن يَضُرَّ اللَّـهَ شَيْئًا ۗ وَسَيَجْزِي اللَّـهُ الشَّاكِرِينَ ﴿١٤٤﴾

Na Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) si yeyote isipokuwa ni Rasuli tu. Wamekwishapita kabla yake Rusuli. Je, akifa au akiuawa mtageuka nyuma ya visigino vyenu (mrudi ukafirini)? Na atakayegeuka nyuma ya visigino vyake, basi hatomdhuru Allaah kitu chochote. Na Allaah Atawalipa wenye kushukuru.

 

  

وَمَا كَانَ لِنَفْسٍ أَن تَمُوتَ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ كِتَابًا مُّؤَجَّلًا ۗ وَمَن يُرِدْ ثَوَابَ الدُّنْيَا نُؤْتِهِ مِنْهَا وَمَن يُرِدْ ثَوَابَ الْآخِرَةِ نُؤْتِهِ مِنْهَا ۚ وَسَنَجْزِي الشَّاكِرِينَ ﴿١٤٥﴾ 

Na haiwi kwa nafsi yeyote kufa isipokuwa kwa idhini ya Allaah, imeandikwa muda wake maalumu. Na yeyote anayetaka thawabu za dunia Tutampa katika hizo. Na yeyote anayetaka thawabu za Aakhirah Tutampa katika hizo; na Tutawalipa wanaoshukuru.  [Aal-‘Imraan: 144-145]

 

 

5- Kutokuva Mipaka Ya Shariy’aha Katika Kuombeleza:  

 

 

 Kuombeleza kwa kujipiga mashavuni na kuchana nguo au kulaani wakati, au kupandisha sauti ya kilio na kusema maneno tele na kuojiombea maangamizi n.k. ni miongoni mwa mambo yaliyoharamishwa katika misiba.  

 

 عَنْ عَبْدُ الله ابْن مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ:  ((لَيْسَ مِنَّا مَنْ ضَرَبَ الْخُدُودَ وَشَقَّ الْجُيُوبَ وَدَعَا بِدَعْوَى الْجَاهِلِيَّةِ)) متفق عليه

 

 Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullahi bin Mas’uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  ((Si miongoni mwetu anayejipiga mashavu, akachana nguo na akaomba maombi ya kijahiliya)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 Muislamu ana haki ya kubakia katika huzuni isiyozidi siku tatu. Baada ya hapo inampasa kujirudisha katika hali yake ya kawaida ya kimaisha na si kujiwekea masiku ya kuombeleza. Imekatazwa hayo katika masimulizi yafuatayo:

 

 

عَنْ زَيْنَبَ بِنْتِ أَبِي سَلَمَةَ (رضي الله عنهما) قَالَتْ: دَخَلْتُ عَلَى أُمِّ حَبِيبَةَ (رضي الله عنها) زَوْجِ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ حِينَ تُوُفِّيَ أَبُوهَا أَبُو سُفْيَانَ بْنُ حَرْبٍ، فَدَعَتْ بِطِيبٍ فِيهِ صُفْرَةُ خَلُوقٍ، أَوْ غَيْرِهِ،  فَدَهَنَتْ مِنْهُ جَارِيَةً، ثُمَّ مَسَّتْ بِعَارِضَيْهَا . ثُمَّ قَالَتْ: وَاللَّهِ مَا لِي بِالطِّيبِ مِنْ حَاجَةٍ غَيْرَ أَنِّي سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، يَقُولُ عَلَى الْمِنْبَرِ: ((لا يَحِلُّ لامْرَأَةٍ تُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ أَنْ تُحِدَّ عَلَى مَيِّتٍ فَوْقَ ثَلاثِ لَيَالٍ، إِلا عَلَى زَوْجٍ أَرْبَعَةَ أَشْهُرٍ وَعَشْرًا)) قَالَتْ زَيْنَبُ: فَدَخَلْتُ عَلَى زَيْنَبَ بِنْتِ جَحْشٍ (رضي الله عنها) حِينَ تُوُفِّيَ أَخُوهَا، فَدَعَتْ بِطِيبٍ فَمَسَّتْ مِنْهُ ثُمَّ قَالَتْ: أَمَا وَاللَّهِ مَا لِي بِالطِّيبِ مِنْ حَاجَةٍ غَيْرَ أَنِّي سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ عَلَى الْمِنْبَرِ: ((لا يَحِلُّ لامْرَأَةٍ تُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ أَنْ تُحِدَّ عَلَى مَيِّتٍ فَوْقَ ثَلاثِ لَيَالٍ إِلاَّ عَلَى زَوْجٍ أَرْبَعَةَ أَشْهُرٍ وَعَشْرًا)) متفق عليه

 

Imepokelewa kutoka kwa Zaynab bint Abi Salamah (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amesema: “Niliingia kwa Ummu Habiybah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) mkewe Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alipofiliwa na baba yake Abuu Sufyaan bin Harb. Akaitisha manukato manjano na manukato ya aina nyingine. Akampaka mjakazi wake na akajipaka mashavuni. Kisha akasema: “WaLLaahi sikuwa nina haja ya kujipaka manukato isipokuwa nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema juu ya mimbar: ((Si halali kwa mwanamke anayemwamini Allaah na Siku ya Mwisho kumkalia maiti matanga zaidi ya siku tatu, isipokuwa amkalie mumewe miezi minne na siku kumi)). Zaynab akasema: Kisha nikamwendea Zaynab bint Jahsh (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alipofiliwa na ndugu yake. Akaitisha manukato, akajipaka kisha akasema: “WaLLaahi sikuwa nina haja ya manukato, isipokuwa nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Si halali kwa mwanamke anayemwamini Allaah na Siku ya mwisho kumkalia maiti matanga zaidi ya siku tatu, isipokuwa amkalie mumewe miezi mine na siku kum]i)) [Al-Bukhaariy na Muslim

 

 Hayo ni mafunzo bora ya kufuata na tuchukue mfano wa Nabiy Ya’quwb ('Alayhis-Salaam)

 

Pindi ilipomzidi huzuni yake baada ya kupotelewa na mwanawe Yuwsuf kwa miaka mingi:

 

 وَتَوَلَّىٰ عَنْهُمْ وَقَالَ يَا أَسَفَىٰ عَلَىٰ يُوسُفَ وَابْيَضَّتْ عَيْنَاهُ مِنَ الْحُزْنِ فَهُوَ كَظِيمٌ ﴿٨٤﴾

Akajitenga nao, na akasema: “Ee majonzi yangu juu ya Yuwsuf.” Na macho yake yakageuka meupe kutokana na huzuni, naye huku akiwa amezuia ghaidhi za huzuni. [Yuwsuf: 84]

 

 

 

Share

10-Swabrun Jamiyl: Yanayosahilisha Kuvumilia Mitihani

 

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)

 

10 - Yanayosahilisha Kuvumilia Mitihani

 

 

‘Amali zifuatazo, zitaweza kumsaidia kwa idhini ya Allaah, anayesibiwa na mitihani na huenda zikamfanyia hafifu huzuni zake au maumivu na kila aina ya dhiki zake, na juu ya hivyo akathibitika mtu katika iymaan. Ila yapasa mtu atekeleze kwa yakini na matarijio kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ‘Amali zenyewe zimegawika katika sehemu mbili: (i) ‘Amali Za Kimatendo (ii) ‘Amali za Kimoyo.

 

 

I) ‘Amali Za Kimatendo

 

Ni ‘amali anazotenda mtu kutumia viungo vyake vya mwili kwa kila aina za ‘ibaadah.

 

 

1- Aliyepatwa Mitihani Na Masaibu Asome Qur-aan Kwa Wingi:

 

 Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatueleza kwamba Qur-aan ni shifaa (poza) na rahmah kwa Waumini. Na imethibiti katika Sunnah kwamba Suwrah kadhaa zinatumika kwa Ruqya (kinga na tiba) ya magonjwa, kusahilisha huzuni za misiba, maafa n.k.  Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 وَنُنَزِّلُ مِنَ الْقُرْآنِ مَا هُوَ شِفَاءٌ وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ﴿٨٢﴾

Na Tunateremsha katika Qur-aan ambayo ni shifaa na rahmah kwa Waumini; [Al-Israa: 82]

 

Na Anasema pia (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

قُلْ هُوَ لِلَّذِينَ آمَنُوا هُدًى وَشِفَاءٌ﴿٤٤﴾

Sema: “Hiyo ni kwa walioamini ni mwongozo na shifaa. [Fusswilat: 44]

 

 

 

2 – Aiyepatwa Mitihani Na Masaibu Azidishie Du’aa

 

Du’aa ni ‘ibaadah pekee inayoweza kugeuza majaaliwa ya Muislamu yanayoandikwa na Malaika Wawili katika Kitabu cha matendo, kama ilivyothibiti katika Hadiyth:

 

عَنْ ثَوْبَانَ (رضي الله عنه)  أن النبي (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((لاَ يَرُدُّ الْقَدَرَ إلاَّ الدُّعَاءُ وَلاَ يَزِيدُ فِي الْعُمُرِ إلاَّ الْبِرُّ وَإِنَّ الْعَبْدَ لَيُحْرَمُ الرِّزْقَ بِالذَّنْبِ يُصِيبُهُ))

 

Kutoka kwa Thawbaan (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hairudishwi Qadar ila kwa du’aa, wala hauzidishwi umri ila kwa wema, na hakika mja anaharamishiwa rizki kutokana na dhambi aitendayo)) [At-Tirmidhiy, Ibn Maajah, Ahmad]

 

Du’aa pia inaondosha kila aina ya shari na balaa:

 

عَنْ مُعَاذٍ (رضي الله عنه) عَنْ رَسُولِ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((لَنْ يَنْفَعَ حَذَرٌ مِنْ قَدَرٍ وَلَكِنَّ الدُّعَاءَ يَنْفَعُ مِمَّا نَزَلَ وَمِمَّا لَمْ يَنْزِلْ فَعَلَيْكُمْ بِالدُّعَاءِ عِبَادَ اللَّهِ))

 

 Kutoka kwa Mu’aadh (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Haifai hadhari kutokana na Qadar lakini du’aa inasaidia katika yaliyoteremka na yasiyoteremka, basi juu yenu [jitahidini] kwa du’aa enyi waja wa Allaah))  [Ahmad]

 

 Na Du’aa kadhaa zimethibiti katika Sunnah ambazo Muislamu akizisoma zinamuondoshea huzuni na dhiki, mojawapo ni:

 

 اللَّهُمَّ إِنِّي عَبْدُكَ، وَابْنُ عَبْدِكَ، وَابْنُ أَمَتِكَ، نَاصِيَتِي بِيَدِكَ، مَاضٍ فِيَّ حُكْمُكَ، عَدْلٌ فِيَّ قَضَاؤُكَ، أَسْأَلُكَ بِكُلِّ اسْمٍ هُوَ لَكَ، سَمَّيْتَ بِهِ نَفْسَكَ، أَوْ عَلَّمْتَهُ أَحَدًا مِنْ خَلْقِكَ، أَوْ أَنْزَلْتَهُ فِي كِتَابِكَ، أَوْ اسْتَأْثَرْتَ بِهِ فِي عِلْمِ الْغَيْبِ عِنْدَكَ، أَنْ تَجْعَلَ الْقُرْآنَ رَبِيعَ قَلْبِي ، وَنُورَ صَدْرِي، وَجلاَءَ حُزْنِي ، وَذَهَابَ هَمِّي

 

 Allaahumma inniy ‘abduka wabnu-‘abdika, wabnu-amatika, naaswiyaatiy biyadika, maadhwin fiyya hukmuka, ‘adlun fiyya qadhwaauka, as-aluka bikullismin huwa Laka, sammayta bihi Nafsaka aw-anzaltahu fiy Kitaabika, aw ‘allamtahu ahadan min khalqika, awis-staatharta bihi fiy ‘ilmil-ghaybi  ‘indaka, an-taj’alal-Qur-aana rabiy’a qalbiy, wanuwra swadriy, wajalaa huzniy, wadhahaaba hammiy

 

 ((Ee Allaah hakika mimi ni mtumwa Wako, mtoto wa mtumwa Wako, mtoto wa kijakazi Chako, utosi wangu uko Mikononi Mwako, yaliyopita kwangu yako katika hukumu Yako, ni usawa kwangu kunihukumu Kwako, nakuomba kwa kila jina ambalo ni Lako Ulilojiita kwa Nafsi Yako au Uliloliteremsha katika Kitabu Chako, au Ulilomfundisha yeyote kati ya viumbe Vyako, au Ulilolihifadhi Wewe mwenyewe [na kujihusisha kulijua] katika ilimu iliofichika Kwako, nakuomba Ujaalie Qur-aan kuwa ni rabiy' (uhuisho, raha, furaha na ustawisho) wa moyo wangu na nuru ya kifua changu, na ufumbuzi wa  huzuni yangu, na sababu ya kuondoka wahka wangu.  [Ahmad (1/391, 452), Al-Haakim (1/509) na ameipa daraja Swahiyh Al-Albaaniy]

 

 

 

 3 – Aliyepatwa Mitihani Na Masaibu Akimbilie Kuomba Maghfirah Na Toba

 

Kwa vile huenda ikawa sababu mojawapo ya mitihani na shari inatokana na madhambi ya mtu anayoyatenda, inahitajika kuomba maghfirah na toba ili kujikinga nayo, kwani kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):    

 

وَمَا كَانَ اللَّـهُ مُعَذِّبَهُمْ وَهُمْ يَسْتَغْفِرُونَ﴿٣٣﴾

Na Allaah Hakuwa wa kuwaadhibu hali wao wanaomba maghfirah. [Al-Anfaal: 33]

 

Juu ya hivyo kuomba maghfirah na toba kuna faida nyingi kwa Muislamu kama zilivyothibiti katika Qur-aan na Sunnah. Manabii walipowalingania watu wao waliwanasihi waombe maghfirah na toba ili Allaah   Awajaalie maisha mazuri yenye manufaa, na Awaruzuku neema Zake, na Awazidishie nguvu [Huwd: 2-3, 50-52, Nuwh: 10-12]

 

 

  4- Aliyepatwa Na Mitihani Na Masaibu Akimbilie Swalaah

 

Imepokelewa kutoka kwa Hudhayfah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba:

 

 ((كاَنَ رَسُولُ الله صلى الله عليه وآله وسلم إِذا حَزَبَهُ أمْر فَزِعَ إِلى الصَّلاَة)) أخرجه أبو داود وحسنه الألباني في صحيح أبي داود 1319 

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akizidiwa na jambo la dhiki hukimbilia kuswali.”  [Abu Daawuwd na ameipa daraja ya Hasan Shaykh Al-Albaaniy katika Swahiyh Abi Daawuwd (1319)]

 

 Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anaamrisha kutafuata msaada kutokana na Swalaah na subira:

 

 وَاسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ ۚ وَإِنَّهَا لَكَبِيرَةٌ إِلَّا عَلَى الْخَاشِعِينَ ﴿٤٥﴾

Na tafuteni msaada kupitia subira na Swalaah; na hakika hilo ni kubwa isipokuwa kwa wanyenyekevu.  [Al-Baqarah: 45]

 

 

Imesemakana kwamba Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) alipokuwa safarini akapata habari ya kifo cha kaka yake, alisema neno la istirjaa’ (Innaa-liLLaahi wa innaa Ilyahi Raaji’wn) kisha akaswali rakaa mbili akakaa kitako kirefu, kisha akainuka kuendelea safari yake huku akisoma Aayah hiyo tukufu.

 

 

 

 5 – Aliyepatwa Mitihani Na Masaibu Amdhukuru Allaah Hususan Kwa Tasbiyh

 

 

 Kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kila aina ya dhikru-Allaah ambazo zimethibiti katika Qur-aan na Sunnah. Mfano kumdhukuru kwa Adhkaar ambazo pindi Muislamu anapopatwa janga na balaa, wahka na huzuni; adkhaar hizo zinapatikana katika kitabu cha Hiswnul-Muslim.  Mfano mojawapo ni du’aa ya Nabiy Yuwnus ('Alayhis-Salaam):

 

 لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ 

Hapana muabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Subhaanak! (Utakasifu ni Wako), hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu.  [At-Tirmidhiy, Ahmad, Al-Haakim (Du’aa ya Dhan-Nuwn na pia imo katika Qur-aan Al-Anbiyaa: (87)]

 

 Du’aa hiyo imethibiti kwamba anayeisoma hutakabaliwa haja yake, na pia huondokewa na dhiki au shida zake kwani hivyo ndivyo alivyoomba Nabiy Yuwnus kwa muda masiku au miezi au miaka mpaka akatolewa kwenye dhiki pindi alipokuwa katika kiza tumboni mwa samaki:

 

 وَذَا النُّونِ إِذ ذَّهَبَ مُغَاضِبًا فَظَنَّ أَن لَّن نَّقْدِرَ عَلَيْهِ فَنَادَىٰ فِي الظُّلُمَاتِ أَن لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ ﴿٨٧﴾

Na Dhan-Nuwn (Yuwnus) alipoondoka akiwa ameghadhibika, akadhani kwamba Hatutamdhikisha; akaita katika kiza kwamba: “Hapana muabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Subhaanak! (Utakasifu ni Wako), hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu.”

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akasema:  

 

فَاسْتَجَبْنَا لَهُ وَنَجَّيْنَاهُ مِنَ الْغَمِّ ۚ وَكَذَٰلِكَ نُنجِي الْمُؤْمِنِينَ ﴿٨٨﴾

Basi Tukamuitikia na Tukamuokoa kutokana na ghamu. Na hivyo ndivyo Tuwaokowavyo Waumini. [Al-Anbiyaa: 87-88]

 

Na pindi makafiri wa Makkah walimpotia mtihanini Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kumkanusha na kumfanyia kila aina ya maudhi, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alimuamrisha kuswali na kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) mchana na usiku kwa kuomba maghfirah, kumsabihi, kumhimidi, kumpwekesha, kumtukuza n.k. ili imhafifishie dhiki zake.

 

Ametaja hivyo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Aayah zifuatazo:

 

وَلَقَدْ نَعْلَمُ أَنَّكَ يَضِيقُ صَدْرُكَ بِمَا يَقُولُونَ﴿٩٧﴾

Na kwa yakini Tunajua kwamba kifua chako kinadhikika kwa yale wanayoyasema.

  

فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَكُن مِّنَ السَّاجِدِينَ﴿٩٨﴾

Basi Sabbih kwa Himidi za Rabb wako na uwe miongoni mwa wanaosujudu.

   

وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّىٰ يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ﴿٩٩﴾

Na mwabudu Rabb wako mpaka ikufikie yakini (mauti). [Al-Hijr: 97-99]

 

Na pia:

 

 فَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ غُرُوبِهَا ۖ وَمِنْ آنَاءِ اللَّيْلِ فَسَبِّحْ وَأَطْرَافَ النَّهَارِ لَعَلَّكَ تَرْضَىٰ ﴿١٣٠﴾

Basi subiri juu ya yale wanayoyasema, na sabbih kwa Himidi za Rabb wako kabla ya kuchomoza jua, na kabla kukuchwa kwake. Na katika nyakati za usiku pia sabbih na katikati ya mchana huenda ukapata ya kukuridhisha.  [Twahaa: 130]

 

Na pia:

 

فَاصْبِرْ إِنَّ وَعْدَ اللَّـهِ حَقٌّ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ بِالْعَشِيِّ وَالْإِبْكَارِ﴿٥٥﴾

Basi vuta subira (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), hakika ahadi ya Allaah ni haki, na omba maghfirah kwa dhambi zako, na sabbih kwa Himidi za Rabb wako jioni na asubuhi.  [Ghaafir: 55]

 

Na:

 

 فَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ الْغُرُوبِ﴿٣٩﴾

Subiri juu ya yale wanayoyasema, na sabbih kwa Himidi za Rabb wako kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa.

 

 

وَمِنَ اللَّيْلِ فَسَبِّحْهُ وَأَدْبَارَ السُّجُودِ﴿٤٠﴾

Na katika usiku Msabbih na baada ya kusujudu. [Qaaf: 39-40]

 

Na pia:

 

وَاصْبِرْ لِحُكْمِ رَبِّكَ فَإِنَّكَ بِأَعْيُنِنَا ۖ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ حِينَ تَقُومُ ﴿٤٨﴾

Na subiri (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kwa hukumu ya Rabb wako, kwani hakika wewe uko chini ya Macho Yetu. Na sabbih kwa Himidi za Rabb wako, wakati unapoinuka.

  

وَمِنَ اللَّيْلِ فَسَبِّحْهُ وَإِدْبَارَ النُّجُومِ ﴿٤٩﴾

Na katika usiku Msabbih na zinapokuchwa nyota. [At-Twuur: 48-49]

 

 

 

Kumtakasa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa tasbiyh ni kusema:

 سُـبْحانَ الله 

 

Subhaana-Allaah

 

au

سُبْحانَ اللهِ وَبِحَمْدِهِ سُبْحَانَ اللهِ العَظِيمِ

Subhaana Allaahi Wabihamdihi Subhaana Allaahil-’Adhwiym

Utakasifu ni wa Allaah na Himdi ni Zake, Utakasifu ni wa Allaah Aliye Mtukufu

 

 

Na Kumhimidi ni:

الْحَمْدُ لِلّه

AlhamduliLlaah

 

 au

 

سُبْحَانَ اللهِ، والحَمْدُ للهِ، وَ لاَ إِلَهَ إلاَّ اللهُ واللهُ أَكْبَرُ

Subhaana Allaah, WalhamduliLLaah, wa laa ilaaha illa Allaah, wa Allaahu Akbar

Utakasifu ni wa Allaah na Himdi Anastahiki Allaah, na hapana muabudiwa wa haki  ila ni Allaah, na Allaah ni Mkubwa.

 

 

6 – Aliyepatwa Mitihani Na Masaibu Atoe Sadaka

 

 Imepokelewa kutoka kwa Abuu Umaamah Al-Baahiliy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

   دَاوَوُا مَرْضَاكُمْ بِالصَّدَقَة

 

 ((Watibuni wagonjwa wenu kwa sadaka)) [Hadiyth Hasan -  Swahiyh Al-Jaami’ (3358)]

 

Na kutoa sadaka ni ‘amali inayohitaji subira kwa kutegemea pia malipo mema duniani na Aakhirah. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 مَا عِندَكُمْ يَنفَدُ ۖ وَمَا عِندَ اللَّـهِ بَاقٍ ۗ وَلَنَجْزِيَنَّ الَّذِينَ صَبَرُوا أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴿٩٦﴾

Mlivyo navyo nyinyi vinatoweka, na vilioko kwa Allaah ni vya kubakia. Na kwa yakini Tutawalipa wale waliosubiri ujira wao kwa mazuri zaidi ya yale waliyokuwa wakitenda. [An-Nahl: 96]

 

 

 

II) ‘Amali Za Kimoyo

 

 

Ni ‘amali za kutafakari, kuzingatia na kushukuru, ambazo zitamliwaza aliyefikwa na mitihani kwa kutaraji malipo mema.

 

 

 1- Aliyepatwa Na Mitihani Na Masaibu Hulipwa Malipo ya ‘Ibaadah Alizokuwa Akizitenda Pindi Alipokuwa Katika Siha:

 

Muumini atafakari kwamba anapofikwa na maradhi akawa hawezi kutekeleza ‘ibaadah zake kama alivyokuwa katika hali ya uzima, hupata thawabu zake vile vile kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni Muadilifu kwa kuwa Anajua kwamba lau si kusibiwa na maradhi, Muislamu huyo angeliendeleza ‘ibaadah zake, basi Humpa ujira wake vile vile na juu ya hivyo hupata ujira zaidi wa subira duniani na Aakhirah.

 

 عن أبي موسى الأشعري  (رضي الله عنه)  عن النَّبي (صلى الله عليه وآله وسلم) قال: (( إِذَا مَرِضَ الْعَبْدُ أَوْ سَافَرَ كُتِبَ لَهُ مِثْلُ مَا كَانَ يَعْمَلُ مُقِيمًا صَحِيحًا)) البخاري

 

 Imepokelewa kutoka kwa Abuu Muwsa Al-Ash’ariyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mja anapopatwa maradhi, au akiwa safarini, huandikiwa (thawabu) kama alivyokuwa akitenda akiwa mkaazi na mwenye afya)) [Al-Bukhaariy]

 

وعَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه)  أَنَّ رَسُولَ (صلى الله عليه وآله وسلم) قال: إِذَا ابْتَلَى اللَّهُ الْعَبْدَ الْمُسْلِمَ بِبَلاَءٍ فِي جَسَدِهِ قَالَ لِلْمَلَكِ : اكْتُبْ لَهُ صَالِحَ عَمَلِهِ الَّذِي كَانَ يَعْمَلُ، فَإِنْ شَفَاهُ غَسَلَهُ وَطَهَّرَهُ، وَإِنْ قَبَضَهُ غَفَرَ لَهُ وَرَحِمَهُ)  رواه أحمد في "المسند" (21/268) قال الألباني: حسن صحيح .

 

 Na Imepokelewa kutoka kwa Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Akimjaribu mja Muislamu kwa kumpa mtihani katika mwili wake, Humwambia Malaika: “Mwandikie amali zake njema alizokuwa akizitenda.”  Akimpa shifaa (Akimponyesha) Humwosha na kumtakasa, na Akichukua roho yake, Humghufuria na Akamrehemu)) [Ahmad katika Musnad na amesema Al-Albaani: Hasan Swahiyh]

 

 

2 – Mwenye Kupatwa Mitihani Na Masaibu Ategemee Malipo Ya Aakhirah:

 

Fadhila tele zimethibiti kwa anayevumilia mitihani kwamba malipo yake ni mema yasiyohesabika duniani na Aakhirah [Rejea Mlango Wa: ‘Fadhila Za Subira Katika Qur-aan’ na pia, ‘Subira Katika Mitihani Kwa Ujumla’] Juu ya hayo, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameahidi Jannah (Pepo) ya kudumu iliyojaa neema:

 

 أُولَـٰئِكَ يُجْزَوْنَ الْغُرْفَةَ بِمَا صَبَرُوا وَيُلَقَّوْنَ فِيهَا تَحِيَّةً وَسَلَامًا ﴿٧٥﴾

Hao ndio watakaolipwa maghorofa ya juu (Jannah) kwa kuwa walisubiri, na watapokelewa humo kwa maamkizi na amani.

 

خَالِدِينَ فِيهَا ۚ حَسُنَتْ مُسْتَقَرًّا وَمُقَامًا ﴿٧٦﴾

Ni wenye kudumu humo. Uzuri ulioje wa mahali pa kustakiri na makazi ya kushi daima. [Al-Furqaan: 75-76]

 

 

 

3 – ‘Ibaadah Za Aliyepatwa Na Mitihani Na Masaibu Huwa Za Dhati:

 

Muumini wa kweli anaposibiwa na mitihani na janga, hujikurubisha zaidi kwa Rabb wake kwa kila aina ya ‘ibaadah, na hapo hata du’aa zake huwa ni zile za dhati ndani ya moyo wake uliokuwa na huzuni na dhiki. Na hapo ndipo inapothibiti kumuabudu na kumtaka msaada Pekee Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ ﴿٥﴾

 Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada. [Al-Faatihah: 5]

 

 

 

4 - Mitihani Na Masaibu Ni Kupendwa Na Allaah Kwa Kutanguliziwa Adhabu

 

Tafakari ndugu Muislamu uliyefikwa na mitihani, na shukuru kwamba masaibu yamekufikia ukiwa katika maisha ya dunia; basi omba upasi mtihani wa Aakhirah kwani huko kuna shida na dhiki zaidi.  Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):   

 

 وَلَنُذِيقَنَّهُم مِّنَ الْعَذَابِ الْأَدْنَىٰ دُونَ الْعَذَابِ الْأَكْبَرِ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ ﴿٢١﴾

Na bila shaka Tutawaonjesha adhabu ndogo kabla ya adhabu kubwa huenda wakarejea (kutubia). [As-Sajdah: 21]

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametubashiria hilo:

 

عَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه) قَال:َ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وآله وسلم): َ(( إِذَا أَرَادَ اللَّهُ بِعَبْدِهِ الْخَيْرَ عَجَّلَ لَهُ الْعُقُوبَةَ فِي الدُّنْيَا وَإِذَا أَرَادَ اللَّهُ بِعَبْدِهِ الشَّرَّ أَمْسَكَ عَنْهُ بِذَنْبِهِ حَتَّى يُوَافِيَ بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ)) وَ قال النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((إِنَّ عِظَمَ الْجَزَاءِ مَعَ عِظَمِ الْبَلاَءِ وَإِنَّ اللَّهَ إِذَا أَحَبَّ قَوْمًا ابْتَلاَهُمْ فَمَنْ رَضِيَ فَلَهُ الرِّضَا وَمَنْ سَخِطَ فَلَهُ السَّخَطُ)) رواه الترمذي وقال حديث حسن

 

Kutoka kwa Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Anapompendelea mja Wake kheri, Humharakishia adhabu duniani. Na Allaah Anapomtakia mja Wake shari Humzuilia dhambi zake hata Amlipe Siku ya Qiyaamah)). Na amesema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Hakika malipo makubwa kabisa yapo pamoja na mtihani mkubwa, na hakika Allaah Anapopenda watu Huwapa mtihani. Basi atakayeridhika atapata radhi (za Allaah) na atakayechukia atapata ghadhabu)) [At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth Hasan]

 

 

 

5 – Katika Mitihani na Masaibu, Mtazame Aliye Chini Yako

 

Wana Aadam hawalingani sawa katika neema walizojaaliwa. Basi katika hali ya mitihani na masaibu, Muumini amtazame mwenzake aliye na shida au hali mbaya zaidi kuliko yeye. Kufanya hivyo kutamkumbusha kuwa yeye yuko katika hali bora zaidi na yuko katika neema kuliko nduguye aliye na hali ngumu zaidi. Mfano mgonjwa anapokwenda hospitali kutibiwa, huenda akakuta huko wagonjwa walio na maradhi zaidi kuliko maradhi yake. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha hayo: 

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه)  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وآله وسلم):  ((انْظُرُوا إِلَى مَنْ هُوَ أَسْفَلَ مِنْكُمْ، وَلاَ تَنْظُرُوا إِلَى مَنْ هُوَ فَوْقَكُمْ فَإِنَّهُ أَجْدَرُ أَنْ لاَ تَزْدَرُوا نِعْمَةَ اللَّهِ عَلَيْكُمْ)) متفق عليه وهذا لفظ مسلم.

 وفي رواية البخاري: ((إِذَا نَظَرَ أَحَدُكُمْ إِلَى مَنْ فُضِّلَ عَلَيْهِ فِي الْمَالِ وَالْخَلْقِ فَلْيَنْظُرْ إِلَى مَنْ هُوَ أَسْفَلَ مِنْهُ))

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mtazameni aliye chini yenu wala msimtazame aliye juu yenu kwani (kufanya hivyo) ni haki zaidi msije mkazidharau neema za Allaah juu yenu)) [Al-Bukhaariy na Muslim], hii lafdh ya Muslim.

 

Na katika riwaayah ya Al-Bukhaariy: ((Anapomtazama mmoja wenu aliyefadhilishwa zaidi kwa mali na umbo basi amtazame aliye chini yake))

 

 

 

6 – Mitihani Na Masaibu Humtoa Mtu Kutoka Kwenye Kughafilika Na Huwa Ni Sababu Ya Kuhidika:

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema kuhusu walioghafilika na dunia wakasahau Aakhirah:

 

إِنَّ الَّذِينَ لَا يَرْجُونَ لِقَاءَنَا وَرَضُوا بِالْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَاطْمَأَنُّوا بِهَا وَالَّذِينَ هُمْ عَنْ آيَاتِنَا غَافِلُونَ﴿٧﴾

Hakika wale wasiotaraji kukutana Nasi, na wakaridhika na uhai wa dunia na wakakinaika nayo, na wale ambao wanaghafilika na Aayaat Zetu   [Yuwnus: 7]

 

Anawaonya kwamba hao watakuwa katika maisha ya dhiki na shida na Atawasahaulia mbali kama wao walivyomsahau.

 

 وَمَنْ أَعْرَضَ عَن ذِكْرِي فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنكًا وَنَحْشُرُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ أَعْمَىٰ ﴿١٢٤﴾

 “Na atakayejitenga na ukumbusho Wangu basi hakika atapata maisha ya dhiki, na Tutamfufua Siku ya Qiyaamah hali akiwa kipofu.”

 

قَالَ رَبِّ لِمَ حَشَرْتَنِي أَعْمَىٰ وَقَدْ كُنتُ بَصِيرًا ﴿١٢٥﴾

Atasema: “Rabb   wangu! Kwa nini Umenifufua kipofu, na hali nilikuwa naona?”

 

 قَالَ كَذَٰلِكَ أَتَتْكَ آيَاتُنَا فَنَسِيتَهَا ۖ وَكَذَٰلِكَ الْيَوْمَ تُنسَىٰ ﴿١٢٦﴾

 (Allaah) Atasema: “Hivyo ndivyo, zilikufikia Aayaat Zetu ukazisahau   na kadhaalika leo umesahauliwa.”

  

وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي مَنْ أَسْرَفَ وَلَمْ يُؤْمِن بِآيَاتِ رَبِّهِ ۚ وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَشَدُّ وَأَبْقَىٰ ﴿١٢٧﴾

Na kadhaalika Tutakavyomlipa yule anayevuka mipaka na asiamini Aayaat za Rabb wake. Na bila shaka adhabu ya Aakhirah ni kali zaidi na ni ya kudumu zaidi.  [Twaahaa: 124-127]

 

 

Aghlabu Muislamu anayekuwa katika kughafilika kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kushughulishwa na anasa na starehe za dunia, kisha pindi akipatwa na masaibu, huwa ni sababu ya kumrudisha kwa Rabb wake akatanabahi kwamba yaliyokuwa yakimshughulisha hayatomfaa lolote. Kisha hutekeleza ‘ibaadah zake ipasavyo na hapo basi ndipo hujikurubisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) akatambua ladha ya ‘ibaadah hizo na zikamzidishia iymaan   na mapenzi ya Rabb wake, na kumpenda zaidi Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Dini Yake tukufu. Lakini nasaha kwa kila Muislamu aliyeghafilika akawa mbali na kumdhukuru Allaah kwamba leo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amekupa fursa ya kukutanabahisha ukarudi Kwake baada ya mitihani na misiba. Basi tahadhari usije kurudi katika hali ya mwanzo. Kumbuka kwamba wengine walioaga dunia wakiwa katika mighafiliko ya dunia wameondoka patupu bila ya kuchuma ‘amali za kumtosheleza kwenye safari ndefu ya Aakhiray isiyoepukika.

 

Wewe bado una fursa kwa kuwa umo katika makazi ya kutubia na kutenda ‘amali njema. Kwa hiyo mshukuru Rabb wako kwa kukujaalia mitihani iliyokuzindua kutoka kizani na sasa umo katika mwamko na nuru. Zingatia hayo ndugu Muislamu yasije kukufikia mauti ukatamani kurudishwa duniani ujirekebishe. Majuto utakayoyadhihirisha wakati huo hayatafaa kitu bali utajibiwa:

 

كَلَّا ۚ إِنَّهَا كَلِمَةٌ هُوَ قَائِلُهَا ۖ وَمِن وَرَائِهِم بَرْزَخٌ إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ ﴿١٠٠﴾

 

 “Laa hasha!” Hakika hilo ni neno alisemaye yeye tu.  Na nyuma yao kuna barzakh mpaka Siku watakayofufuliwa. [Al-Muuminuwn: 100]

 

 

7 – Mitihani Na Masaibu Ni Hikma Ya Allaah

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni Mwenye Hikma na Mjuzi. Anapomsibu mja Wake mitihani huenda ikawa ni kheri yake (mja) kama Anavyosema:

 

وَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تُحِبُّوا شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٢١٦﴾

 

Na asaa mkachukia jambo na hali lenyewe ni kheri kwenu. Na asaa mkapenda jambo na hali lenyewe ni la shari kwenu. Na Allaah Anajua na nyinyi hamjui. [Al-Baqarah: 216]

 

 

Rejea kisa cha Nabiy Muwsa ('Alayhis-Salaam)  na Khidhr katika Suwratul-Kahf ambacho kimejaa Hikma za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)    [Al-Kahf: 60-82]

 

 

 

Share

11-Swabrun Jamiyl: Subira Za Wanawake Wema Wa Awali - Haajar Mama Yake Nabiy Ismaa'iyl

 

Swabrun Jamiyl (Subira njema)

 

11 - Subira Za Wanawake Wema Wa Awali: Haajar Mama Yake Nabiy Ismaa’iyl

 

 

 

 

Nabiy Ibraahiym ('Alayhis-Salaam) alihama Shaam kuelekea Makkah akiwa pamoja na mkewe Haajar na mwanawe Ismaa’iyl. Walipofika aliwaacha katika bonde kame, kavu, na lisilokuwa tambarare. Hapakuwa na chakula wala maji, na hapakuwa na watu wanoishi.

 

Haajar alitawakali kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na akavuta subira juu ya kwamba alikuwa na mtoto mchanga aliyekuwa bado akimnyonyesha. Pindi Nabiy Ibraahiym alipoondoka na kuwaacha bondeni Makkah, Haajar alimuuliza: “Ee Ibraahiym, unakwenda wapi na kutuacha katika bonde lisokuwa na watu au chochote (cha kutuwezesha kuishi)?” Akakariri swali lake mara kadhaa, lakini Ibraahiym ('Alayhis-Salaam) hakumjibu wala hakutazama nyuma kwani hivyo ndivyo alivyoamrishwa na Rabb Wake, na hakutaka kufanya kinyume chake. Haajar mwishowe akamuuliza: “Je Allaah Amekuamrisha kufanya hivyo?” Akajibu: “Ndio”. Jibu hilo lilimtosheleza Haajar kwani alijua kwamba ni hukmu ya  Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) akasema: “Basi nenda, hakika Allaah Hatatutekeleza” [Al-Bukhaariy]

 

Nabiy Ibraahiym alimuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

رَّبَّنَا إِنِّي أَسْكَنتُ مِن ذُرِّيَّتِي بِوَادٍ غَيْرِ ذِي زَرْعٍ عِندَ بَيْتِكَ الْمُحَرَّمِ رَبَّنَا لِيُقِيمُوا الصَّلَاةَ فَاجْعَلْ أَفْئِدَةً مِّنَ النَّاسِ تَهْوِي إِلَيْهِمْ وَارْزُقْهُم مِّنَ الثَّمَرَاتِ لَعَلَّهُمْ يَشْكُرُونَ ﴿٣٧﴾

“Rabb wetu! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya dhuria wangu katika bonde lisilokuwa na mmea wowote, kwenye Nyumba Yako Tukufu. Rabb wetu, ili wasimamishe Swalaah na Ujaalie nyoyo za watu zielekee kwao na Uwaruzuku mazao ili wapate kushukuru.” [Ibraahiym: 37]

 

 

Baada ya Nabiy Ibraahiym ('Alayhis-Salaam) kuondoka, haukupita muda Ismaa’iyl akaanza kulia kwa njaa na kiu, hapo Haajar akaanza kutafuta maji mara akitembea kwa kasi,  mara akikimbia baina ya majabali mawili ya Swafaa na Marwah huku akiomba du’aa na kumdhukuru Rabb wake.  Alikaribia kukata tamaa kupata chakula au maji, mara akasikia sauti inayovumavuma. Hapo ndipo alipokuja Jibriyl ('Alayhis-Salaam) akabubujiwa maji ya zamzam kwa amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).   

 

 

Ndege wakaanza kuzunguka katika dimbwi la Zamzam, na watu wa msafara wakatambua kwamba kuna maji, wakayafuata na ndipo wakaweka makazi yao. Hao waliokuwa ni watu katika kabila ya Jurhum waliokuwa safarini kutoka Yemen. Wakabakia hapo, na Haajar na mwanawe wakawa ni wamiliki wa maji hayo katika mji huo mtukufu wa Makkah. Wakaishi nao hadi Ismaa’iyl alipokuwa mkubwa akaoa mwanamke kutoka kabila hilo. Na hapo ndipo kizazi cha Nabiy Ismaa’iyl kilipochipuka hadi kufikia kuzaliwa kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Hizo ni miongoni mwa fadhila kuu kabisa za subira ya Haajar. Juu ya hivyo, ‘ibaadah ya Sa’y baina ya Swafaah na Marwah inatekelezwa na idadi isiyohesabika ya Waislamu tokea zama za kale mpaka leo na itaendelea mpaka Siku ya Qiyaamah, na thawabu zake zikimfikia Haajar.

 

 

 

Share

12-Swabrun Jamiyl: Subira Za Wanawake Wema Wa Awali - Mama Yake Nabiy Muwsaa

 

Swabrun Jamiyl (Subira njema)

 

12 - Subira Za Wanawake Wema Wa Awali -

 

Mama Yake Nabiy Muwsaa

 

 

 

 

Fir’awn alipoota ndoto kuwa atazaliwa mtoto katika wana wa Israaiyl atakayekuwa ni sababu ya kutoweka milki yake na kuangamia kwake, aliamrisha kuua kila mtoto mwanamume anayezaliwa. Mwishowe walikhofia kwamba utafika wakati kutakuweko na wanawake wengi na hakutakuwa na wanaume wa kufanya kazi za kiume. Akaamrisha mwaka mmoja wauliwe watoto wa kiume wote, na mwaka mwengine waachiwe hai. Mwaka aliozaliwa Nabiy Muwsa ('Alayhis-Salaam) ulikuwa ni mwaka wa kuuliwa watoto wanaozaliwa. Mama yake Muwsa alipoibeba mimba yake, tumbo halikutokeza kama mimba za wanawake wengine. Kwa hiyo alisalimika kwani walikuwa wakiingiliwa majumbani kuchunguzwa kama kuna mwanamke mwenye mimba, kisha husubiriwa anapozaa huuliwa mtoto huyo. Mama yake Muwsa alipojifungua alianza kuingiwa na khofu kubwa na huzuni ya kuwa mwanawe atauliwa. Ilipomzidi khofu, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alimpoza moyo wake na Akamtia ilhamu na kumuongoza la kufanya. Kisha Akamuahidi kwamba Atamrudisha mwanawe kwake na juu ya hivyo atarudi akiwa ni Rasuli wa Allaah:

 

 

 وَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ أُمِّ مُوسَىٰ أَنْ أَرْضِعِيهِ ۖ فَإِذَا خِفْتِ عَلَيْهِ فَأَلْقِيهِ فِي الْيَمِّ وَلَا تَخَافِي وَلَا تَحْزَنِي ۖ إِنَّا رَادُّوهُ إِلَيْكِ وَجَاعِلُوهُ مِنَ الْمُرْسَلِينَ ﴿٧﴾

Na Tukamtia ilhamu mama yake Muwsaa kwamba: “Mnyonyeshe. Lakini utakapomkhofia, basi mtupe katika mto na wala usikhofu wala usihuzunike. Hakika Sisi Tutamrudisha kwako, na Tutamfanya miongoni mwa Rusuli”. [Al-Qaswasw: 7]

 

 

Mama yake Muwsa alikuwa akiishi karibu na mto wa Nile. Alichukua kisanduku akamfanyia kama susu la kulalia mtoto. Akalifunga na kamba akawa anamnyonyesha kwa uficho. Ikawa kila anapomjia mtu anayemuogopa humtia mtoto wake katika kisanduku na kumweka katika mto huku akilifunga kamba. Siku moja alisahau kulifunga kamba. Maji yakachukua kisanduku   yakipita nalo mbele ya nyumba ya Fir’awn. Wajakazi wa Fir’awn wakaliona susu wakalibeba mpaka kwa Aasiyah mke wa Fir’awn. Hawakujua kilichomo ndani yake na walikhofu kufungua kwani wangeliingia matatani kufanya hivyo bila ya kupata amri. Kisanduku kilipofunguliwa walimwona mtoto mchanga mzuri ajabu! Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akaujaza moyo wa Aasiyah, mapenzi ya mtoto huyo kwa vile Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  ni Mjuzi wa ya ghaibu, Alijua kuwa Aasiyah ni atakuwa ni Muumini, hivyo Alitaka mtoto huyo awe ni sababu yake ya kutoka katika shirki ya mumewe aingie katika Tawhiyd apate maisha mema ya milele. Na mtoto huyo awe sababu ya kuangamia kwa Fir’awn bila ya yeye kuhisi. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

فَالْتَقَطَهُ آلُ فِرْعَوْنَ لِيَكُونَ لَهُمْ عَدُوًّا وَحَزَنًا ۗ إِنَّ فِرْعَوْنَ وَهَامَانَ وَجُنُودَهُمَا كَانُوا خَاطِئِينَ ﴿٨﴾

Basi wakamwokota watu wa Fir’awn ili awe adui kwao na (sababu ya) huzuni. Hakika Fir’awn na Haamaan na majeshi yao walikuwa wenye makosa. [Al-Qaswasw: 8]

 

 

Kwa maana, Fir’awn alipomuona, alitaka kumuua akikhofu kuwa atakuwa ni yule mtoto aliyemuota ndotoni. Lakini mkewe Aasiyah bint Muzaahim alimkinga na akamwambia mumewe:

 

 قُرَّتُ عَيْنٍ لِّي وَلَكَ ۖ لَا تَقْتُلُوهُ عَسَىٰ أَن يَنفَعَنَا أَوْ نَتَّخِذَهُ وَلَدًا وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿٩﴾

 “Kiburudisho cha macho kwangu na kwako; usimuue, asaa akatufaa, au tumfanye mwana.” Nao hawatambui. [Al-Qaswasw: 9]

 

Subira ya mama yake Muwsa iliendelea kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Kauli Yake:

 

وَأَصْبَحَ فُؤَادُ أُمِّ مُوسَىٰ فَارِغًا ۖ إِن كَادَتْ لَتُبْدِي بِهِ لَوْلَا أَن رَّبَطْنَا عَلَىٰ قَلْبِهَا لِتَكُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٠﴾

Na ukawa moyo uliojaa hisia wa mama yake Muwsaa mtupu! Alikaribia kumdhihirisha (kuwa ni mwanawe) lau kama Tusingeutia nguvu moyo wake ili awe miongoni mwa Waumini.

 

 

وَقَالَتْ لِأُخْتِهِ قُصِّيهِ ۖ فَبَصُرَتْ بِهِ عَن جُنُبٍ وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿١١﴾

Akamwambia dada yake (Muwsaa): “Mfuatilie!”  Akamtazama kwa mbali nao hawatambui.

 

وَحَرَّمْنَا عَلَيْهِ الْمَرَاضِعَ مِن قَبْلُ فَقَالَتْ هَلْ أَدُلُّكُمْ عَلَىٰ أَهْلِ بَيْتٍ يَكْفُلُونَهُ لَكُمْ وَهُمْ لَهُ نَاصِحُونَ ﴿١٢﴾

Na Tulimharamishia akatae kabisa wanyonyeshaji tangu mwanzo, mpaka akasema: “Je, nikuelekezeni kwa watu wa nyumba watakaomlea kwa ajili yenu, nao watakuwa wenye kumweka vyema kidhati?

 

 

فَرَدَدْنَاهُ إِلَىٰ أُمِّهِ كَيْ تَقَرَّ عَيْنُهَا وَلَا تَحْزَنَ وَلِتَعْلَمَ أَنَّ وَعْدَ اللَّـهِ حَقٌّ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿١٣﴾

Basi Tukamrudisha kwa mama yake ili yaburudike macho yake na wala asihuzunike, na ili ajue kwamba ahadi ya Allaah ni kweli, lakini wengi wao hawajui. [Al-Qaswasw: 10-13]

 

 

 Hiyo ndivyo alivyovumilia mama yake Muwsa kufuata amri ya Rabb wake na matokeo yake akatimiziwa ahadi ya kurudishiwa mwanawe ili amnyonyeshe na kisha akapata fadhila kubwa zaidi kwa  kujaaliwa mtoto wake kuwa Nabiy na Rasuli  wa wana wa  Israaiyl. 

 

 

Share

13-Swabrun Jamiyl: Subira Za Wanawake Wema Wa Awali - Aasiyah Aliyekuwa Mke Wa Fir’awn

 

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)

 

13- Subira Za Wanawake Wema Wa Awali: Aasiyah Aliyekuwa Mke Wa Fir’awn

 

 

 

Aasiyah aliishi katika Qasri la fakhari, lilojaa kila aina ya starehe, wakiwemo watumishi tele, na alipata kila alichokitamani. Alikuwa mke wa Fir’awn, Fir’awn aliyejivuna na kutakabari na akavuka mipaka kujifanya yeye ni muabudiwa. Aliwaamrisha watu wake wamwabudu na akawaekea vitisho pindi wakimuasi.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alimtia ilhamu Aasiyah ampende Muwsa pale alipoletewa kisanduku kilichopatikana katika mto wa Nile ambacho  ndani yake alikuwemo Muwsaa akiwa mtoto mchanga. Mtoto huyo alikuwa na nuru usoni mwake, na alimuathiri mno hadi akamuomba Fir’awn asimuue bali wamfanye mwana wao. Akamlea malezi mema yakajengeka mapenzi ya mama na mwana.

 

Muwsaa alipopewa risala (ujumbe) wa kumlingania Fir’awn katika Tawhiyd, Aasiyah alimwamini hapo hapo. Lakini alificha kwanza iymaan yake kwa kumkhofu Fir’awn. Haukufika muda alidhihirisha Uislamu wake. Fir’awn alimtaka arudi katika dini yake ya kumwabudu yeye, akamwekea vitisho na kumtahadharisha adhabu kali. Lakini alithibitika katika iymaan yake ya kufuata haki. Fir’awn akataka ushauri kwa Haamaan (mawaziri wake) wakamshauri amuue Aasiyah. Wakamfunga mikono na miguu yake wakamweka juani. Fir’awn akaamrisha liletwe jiwe kubwa kabisa.  Kisha aulizwe Aasiyah akiwa katika adhabu ya jua na kiu kikali, kwamba nani mwabudiwa wake? Atakapomkubali yeye basi yu angali mke wake, laa sivyo wampige nalo jiwe kumuulia mbali. Aasiyah alithibitika katika iymaan yake, hakujali  kuyaacha maisha ya ufalme aliyokuwa akiishi katika Qasri ambako kulijaa kila aina za starehe. Alilojali zaidi ni kupokea haki aliyokuja nayo Muwsaa na ndugye Haaruwn ya kumpwekesha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Pekee, na kupata radhi Zake atakapokutana Naye Peponi. Katika hali hiyo ya kuadhibiwa na kukaribia mauti, hakutaharuki wala kuhamanika wala kupapatika bali alivuta subira huku akiomba:

 

رَبِّ ابْنِ لِي عِندَكَ بَيْتًا فِي الْجَنَّةِ وَنَجِّنِي مِن فِرْعَوْنَ وَعَمَلِهِ وَنَجِّنِي مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ﴿١١﴾

  “Rabb wangu! Nijengee nyuma Kwako kwenye Jannah na niokoe na Fir’awn na vitendo vyake na niokoe na watu madhalimu.” [At-Tahriym: 11]

 

 

Watu wa Fir’awn walipomjia Aasiyah, macho yake yalikuwa yakitazama nyumba yake ya Peponi aliyokwishaahidiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Akapigwa jiwe, roho yake ikatoka akiwa katika Tawhiyd ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).  

 

Iymaan na subira yake ya hali ya juu imemstahiki kuwa ni miongoni mwa wanawake wanne waliobashiriwa Jannah kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

((أَفْضَلُ نِسَاءِ أَهْلِ الْجَنَّةِ خَدِيجَةُ بِنْتُ خُوَيْلِدٍ وَفَاطِمَةُ بِنْتُ مُحَمَّدٍ وَمَرْيَمُ بِنْتُ عِمْرَانَ وَآسِيَةُ بِنْتُ مُزَاحِمٍ امْرَأَةُ فِرْعَوْنَ))

((Wanawake bora wa Jannah ni Khadiyjah bint Khuwaylid na Faatwimah bint Muhammad, na Maryam bint ‘Imraan, na Aasiyah bint Muzaahim)) [Musnad Ahmad, ameipa daraja ya Swahiyh Shaykh Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaami’ (1135)]

 

 

 

Share

14-Swabrun Jamiyl: Subira Za Wanawake Wema Wa Awali - Maryam Bint ‘Imraan Mama Yake Nabiy 'Iysaa

 

Swabrun Jamiyl (Subira njema)

 

14 - Subira Za Wanawake Wema Wa Awali - Maryam Bint ‘Imraan Mama Yake Nabiy ‘Iysaa

 

 

 

Subira yake ilikuwa ni katika utiifu ambayo ni subira ngumu kabisa kama tulivyotangulia kutaja. Mama yake Hannah bint Faaqudhw alitamani apate mwana wa kiume ili awe msimamizi wa Baytul-Maqdis [Msikiti ulioko Quds, Palestina]. Lakini alijaaliwa mtoto wa kike, akamwita ‘Maryam’. Akalelewa na mjomba wake Nabiy Zakariyyah ('Alayhis-Salaam). Maryam akawa mtiifu, mwenye taqwa ya hali ya juu, mwenye kufanya ‘ibaadah mchana na usiku.   

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akawatuma Malaika wambashirie:

 

وَإِذْ قَالَتِ الْمَلَائِكَةُ يَا مَرْيَمُ إِنَّ اللَّـهَ اصْطَفَاكِ وَطَهَّرَكِ وَاصْطَفَاكِ عَلَىٰ نِسَاءِ الْعَالَمِينَ ﴿٤٢﴾

Na pale Malaika waliposema: “Ee Maryam! Hakika Allaah Amekuteua na Amekutakasa na Amekukhitari juu ya wanawake wa walimwengu.” [Aal-‘Imraan: 42]

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Amemteua Maryam kwa sababu ya  kumtumikia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kwa sababu ya sitara,  heshima na umaasumu wake. Pia kwa sababu ya  kuthibitika kwake katika yakini. Akapata fadhila za kuwa ni miongoni mwa wanawake wanne walio bora kabisa ulimwenguni Taz. Hadiyth katika Subira ya Aasiyah.

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema kuwa Malaika walimuamrisha Maryam akithirishe ‘ibaadah zake na azidishe unyenyekevu, na azidishe kujisalimisha, kusujudu na kurukuu n.k.

 

يَا مَرْيَمُ اقْنُتِي لِرَبِّكِ وَاسْجُدِي وَارْكَعِي مَعَ الرَّاكِعِينَ ﴿٤٣﴾

  “Ee Maryam!  Kuwa mtiifu kwa Rabb wako, na sujudu, na rukuu pamoja na wanaorukuu.” [Aal-‘Imraan: 43]

 

Maryam aliipokea amri hiyo akazidi kuwa katika subira ya utiifu ili adiriki jambo Alilohukumiwa na  Allaah lie ni mtihani wake. Ulikuwa ni mtihani mkubwa mno, lakini ulimpatia daraja tukufu duniani na Aakhirah kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Alionyesha Miujiza Yake na Uwezo Wake wa kumuumba mwana tumboni mwake bila ya kuingiliwa na mwanamume. Akashika mimba baada ya kubashiriwa na Jibriyl ('Alayhis-Salaam) akaridhika na majaaliwa hayo. Ila alitambua kuwa utakuwa ni mtihani mkubwa kwake kumzaa mtoto bila ya kuolewa. Akahofia maudhi ya watu kwa maneno na dhana zao mbaya, jambo ambalo lilihitajia pia subira ya hali ya juu. Aliposhikwa na uchungu uliompeleka katika shina la mtende, alisema:

 

يَا لَيْتَنِي مِتُّ قَبْلَ هَـٰذَا وَكُنتُ نَسْيًا مَّنسِيًّا ﴿٢٣﴾

  “Laiti ningelikufa kabla ya haya na nikawa wa kusahauliwa, aliyesahauliwa kabisa!” [Maryam: 23]

 

Kwa maana: “Natamani nisingelikuwa nimeumbwa nikawa si chochote”  [Kauli ya Ibn ‘Abbaas katika tafsiyr ya Ibn Kathiyr]

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   Akamtuliza khofu yake na sikitiko lake na Akampooza:

 

فَنَادَاهَا مِن تَحْتِهَا أَلَّا تَحْزَنِي قَدْ جَعَلَ رَبُّكِ تَحْتَكِ سَرِيًّا ﴿٢٤﴾

Lakini (muitaji) akamwita kutoka chini yake kwamba: “Usihuzunike! Rabb wako Amekwishakufanyia kijito cha maji.”

 

وَهُزِّي إِلَيْكِ بِجِذْعِ النَّخْلَةِ تُسَاقِطْ عَلَيْكِ رُطَبًا جَنِيًّا ﴿٢٥﴾

 “Na tingisha kwako shina na mtende, litakuangushia tende ziloiva zilizotayari kuchumwa.”

  

فَكُلِي وَاشْرَبِي وَقَرِّي عَيْنًا ۖ فَإِمَّا تَرَيِنَّ مِنَ الْبَشَرِ أَحَدًا فَقُولِي إِنِّي نَذَرْتُ لِلرَّحْمَـٰنِ صَوْمًا فَلَنْ أُكَلِّمَ الْيَوْمَ إِنسِيًّا﴿٢٦﴾

 “Basi kula na kunywa na litue jicho lako. Na utakapokutana na mtu yeyote basi sema: Hakika mimi nimeweka nadhiri ya swawm kwa Ar-Rahmaan hivyo leo sitomsemesha mtu yeyote.”   [Maryam: 24-26]

 

 

Khofu yake ilihakiki baada ya kumzaa ‘Iysaa ('Alayhis-Salaam) na alipokuwa amembeba mbele ya watu wake wakadhihirisha dhana zao alizozikhofia:

 

فَأَتَتْ بِهِ قَوْمَهَا تَحْمِلُهُ ۖ قَالُوا يَا مَرْيَمُ لَقَدْ جِئْتِ شَيْئًا فَرِيًّا ﴿٢٧﴾

Akawafikia watu wake akiwa amembeba (mtoto); wakasema: “Ee Maryam! Kwa yakini umeleta jambo lisilopata kusikika, kuu na ovu mno. 

 

يَا أُخْتَ هَارُونَ مَا كَانَ أَبُوكِ امْرَأَ سَوْءٍ وَمَا كَانَتْ أُمُّكِ بَغِيًّا ﴿٢٨﴾

  “Ee dada wa Haaruwn! Hakuwa baba yako mtu muovu, na wala hakuwa mama yako kahaba.” [Maryam: 27-28]

 

Hali ikawa kama zinavyoendelea Aayah:

 

فَأَشَارَتْ إِلَيْهِ ۖ قَالُوا كَيْفَ نُكَلِّمُ مَن كَانَ فِي الْمَهْدِ صَبِيًّا ﴿٢٩﴾

Akamuashiria. Wakasema: “Vipi tuseme na aliye kwenye susu, bado mtoto?”

 

قَالَ إِنِّي عَبْدُ اللَّـهِ آتَانِيَ الْكِتَابَ وَجَعَلَنِي نَبِيًّا ﴿٣٠﴾

 (Mtoto) Akasema: “Hakika mimi ni mja wa Allaah; Amenipa Kitabu (Injiyl) na Amenijaalia kuwa Nabiy.”

 

وَجَعَلَنِي مُبَارَكًا أَيْنَ مَا كُنتُ وَأَوْصَانِي بِالصَّلَاةِ وَالزَّكَاةِ مَا دُمْتُ حَيًّا ﴿٣١﴾

 “Na Amenijaalia kuwa mwenye kubarikiwa popote nitakapokuweko, na Ameniusia Swalaah na Zakaah madamu niko hai.” 

 

وَبَرًّا بِوَالِدَتِي وَلَمْ يَجْعَلْنِي جَبَّارًا شَقِيًّا ﴿٣٢﴾

 “Na niwe mtiifu kwa mama yangu na wala Hakunijaalia kuwa jabari, muovu.”

 

وَالسَّلَامُ عَلَيَّ يَوْمَ وُلِدتُّ وَيَوْمَ أَمُوتُ وَيَوْمَ أُبْعَثُ حَيًّا ﴿٣٣﴾

 “Na amani iwe juu yangu siku niliyozaliwa, na siku nitakayokufa na siku nitakayofufuliwa hai.” [Maryam: 29-33]

 

 

Juu ya hivyo, dhana, tuhuma na uzushi wa watu wake uliendelea, lakini Maryam aliendelea kuvuta subira akamlea mwanawe ambaye alikuwa ni fadhila kuu juu yake kwamba alikuwa ni miongoni mwa Manabii na Rusuli Watukufu. Na subira hiyo aliihitaji pia mwanawe Nabiy ‘Iyssa ('Alayhis-Salaam) ambaye naye alizuliwa ya kuzuliwa. Lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anathibitisha ukweli wake kuwa ‘Iysaa ni mja Wake:

 

ذَٰلِكَ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ ۚ قَوْلَ الْحَقِّ الَّذِي فِيهِ يَمْتَرُونَ ﴿٣٤﴾

Huyo ndiye ‘Iysaa mwana wa Maryam! Kauli ya haki ambayo wanaitilia shaka.

 

مَا كَانَ لِلَّـهِ أَن يَتَّخِذَ مِن وَلَدٍ ۖ سُبْحَانَهُ ۚ إِذَا قَضَىٰ أَمْرًا فَإِنَّمَا يَقُولُ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴿٣٥﴾

Haiwi kwa Allaah kamwe Ajichukulie mwana yeyote. Subhaanah! (Utakasifu ni Wake). Anapokidhia jambo basi huliambia: “Kun” (Kuwa!) nalo linakuwa!

 

وَإِنَّ اللَّـهَ رَبِّي وَرَبُّكُمْ فَاعْبُدُوهُ ۚ هَـٰذَا صِرَاطٌ مُّسْتَقِيمٌ ﴿٣٦﴾

 (Nabiy ‘Iysaa akasema): “Na kwamba hakika Allaah ni Rabb wangu, na Rabb wenu, basi mwabuduni Yeye (Pekee). Hii ndio njia iliyonyooka.” [Maryam: 34-36]

 

 

 

 

 

 

Share

15-Swabrun Jamiyl: Subira Za Maswahaba - Familia Ya Yaasir (Radhwiya Allaahu 'anhum)

 

Swabrun Jamiyl (Subira njema)

 

15- Subira Za Maswahaba - Familia Ya Yaasir (Radhwiya Allaahu ‘anhum)

 

 

 

  

Yaasir na ndugu yake ‘Abdullaah (ambao asili yao ni kutoka Yemen), na Summayyah ambaye ni mke wa Yaasir, na mtoto wao ‘Ammaar (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kuingia katika Dini ya Kiislamu. Walianza kupata kila aina ya mateso na adhabu lakini nuru ya Uislamu iliyoingia katika nyoyo zao, iliwafanya wastahamili mitihani yote iliyowasibu. Walikuwa wote watatu; Yaasir, ‘Ammaar na Sumayyah (Radhwiya Allaahu ‘anhum) wakitolewa nje wakati wa jua kali sana, wakipelekwa jangwani na kupewa kila aina ya adhabu. Wakati huo Waislam walikuwa bado wachache sana na hawakuwa na nguvu za kuweza kujitetea. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alipokuwa akipita chini ya nyumba yao na kuwasikia wakiadhibiwa, alikuwa akiwaombea du’aa. Siku moja ‘Ammaar  (Radhwiya Allaahu ‘anhu)  alimwambia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Ee Rasuli wa Allaah, adhabu tunayoipata hivi sasa imepindukia mipaka." Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: ((Kuweni na subira enyi familia ya Yaasir, hakika ahadi yenu [jazaa yenu] ni Jannah)) ‘Amru bin Maymun (Radhwiya Allaahu 'anhu)  amesema: “Washirikina walikuwa wakiuunguza mkono wa Yaasir, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akipita kila siku na kuushika mkono huo huku akisema: ((Ee moto kuwa baridi na salama juu ya ‘Ammaar, kama ulivyokuwa baridi na salama juu ya Ibraahiym)).

 

Bibi Sumayyah (Radhhwiya Allaahu ‘anhaa)  pamoja na mumewe, mtoto wao na Waislamu wengi wa mwanzo waliweza kuvumilia tabu nyingi na mateso mengi sana kwa sababu tu walitegemea malipo mema kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Kutokana na iymaan zilizothibiti ndani ya nyoyo zao na baada ya kutambua kuwa hiyo ndiyo njia ya pekee itakayomletea mtu maisha matukufu hapa duniani na kesho Aakhirah, waliridhika kuzipoteza roho zao kwa ajili ya kupata radhi za Rabb wao.

 

Sumayyah bint Khubat alijulikana kwa umaarufu wake (Ummu ‘Ammaar) ni mtu wa mwanzo kufa shahidi kwa ajili ya Uislamu.  Siku moja Abuu Jahal alimuingilia Sumayyah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) na kuanza kumpiga kwa mateke na magumi huku akimtaka amtukane Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na awatukuze miungu ya washirikina wa ki-Quraysh. Lakini Sumayyah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa)  alistahamili adhabu yote hiyo huku akisema: “Ahadun Ahad”.  Neno hilo lilizidi kumtia uchungu Abuu Jahl akawa anaendelea kumpiga Bi Sumayyah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) mpaka akafariki.  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliposikia hayo alisikia uchungu sana, lakini hakuwa na uwezo wa kufanya lolote mbele ya nguvu za makafiri hao, na kwa ajili hiyo akawataka watu wake wahamie nchi ya Uhabeshi (Ethiopia).

 

Ama ‘Ammaar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) siku moja aliteswa sana na makafiri wakamtaka   amtukane Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  na walimwekea kitisho kuwa watamuua. Ikambidi awadanganye kwamba amerudi katika dini yao akamtukana Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ili wasimtese zaidi. Aliporudi kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuelezea juu ya yote hayo, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alimuuliza: ((Lakini vipi ndani ya nafsi yako unajionaje?)) ‘Ammaar akamwambia: “Iymaan imetulia ndani yake”. Hapo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akamwambia: ((Kama watarudia tena basi na wewe rudia)).

 

Ndipo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Alipoteremesha kauli Yake:

 

 

 مَن كَفَرَ بِاللَّـهِ مِن بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ وَلَـٰكِن مَّن شَرَحَ بِالْكُفْرِ صَدْرًا فَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ مِّنَ اللَّـهِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ﴿١٠٦﴾

Atakayemkufuru Allaah baada ya iymaan yake - isipokuwa yule aliyekirihishwa (kukanusha) na huku moyo wake umetua juu ya iymaan - lakini aliyekifungulia ukafiri kifua chake, basi hao juu yao ni ghadhabu kutoka kwa Allaah na watapata adhabu kuu. [An-Nahl: 106]

 

 

 

 

 

Share

16-Swabrun Jamiyl: Subira Za Maswahaba - Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu)

 

Swabrun Jamily (Subira njema)

 

16- Subira Za Maswahaba – Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘anhu)

 

 

 

Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa mtumwa kabla ya Uislamu. Bwana wake aliyemtumikia alikuwa ni Umayyah bin Khalaf anayetokana na kabila la Al-Jumhiy. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoanza kulingania watu katika Dini ya Kiislamu, Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu)  alifurahishwa na habari alizokuwa akizisikia kutoka kwa Abuu Bakr Asw-Swiddiyq  (Radhwiya Allaahu 'anhu)   ambaye alikuwa akiwalingania waliokuwa huru na watumwa. Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu) hakukawia kuingia Usilamu mikononi mwa Abuu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye alimpeleka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  na kuzitamka shahada mbili mbele yake. Akawa miongoni mwa watu wa mwanzo kuingia katika Uislamu.

 

Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu)  naye alipata sehemu kubwa ya adhabu, kwani bwana wake Umayyah bin Khalaf alikuwa mtu khabithi sana. Alikuwa akimtoa nje wakati wa jua kali linalounguza mwili akimvua nguo zake kisha akimlaza juu ya mchanga wa jangwani unaounguza. Kisha akimwekea jiwe kubwa sana juu ya kifua chake huku akimwambia: “Utabaki hivyo hivyo mpaka ufe isipokuwa kama utamkanusha Muhammad na kumtukana kisha urudi tena kuiabudu miungu yako Laata na ‘Uzza." Lakini Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu)   alikuwa akimjibu kwa kusema: “Ahadun Ahad." (Mmoja tu, mmoja tu) akikusudia Allaah. Alipoulizwa: “Kwa nini unaendelea kusema hivyo ‘Ahadun Ahadun’ na hali unajua kuwa maneno hayo yanawaghadhibisha na kwa ajili hiyo wao wataendelea kukuadhibu?" Akajibu: ”Wa-Allaahi kama ningekuwa nalijua neno jingine linaloweza kuwakasirisha zaidi kuliko hilo, basi ningelilitamka." Na neno hilo ‘Ahadun Ahadun’, lilikuwa likimkera sana Umayyah, na kila alipolisikia alipandwa na ghadahbu akawa anampiga Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu)  kama vile mtu aliyepandwa na kichaa! Lakini juu ya hivyo, Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu)  aliendelea kuvuta subira huku akitamka neno lake hilo “Ahadun Ahadun” mpaka Umayyah akashindwa.

 

Ikawa kila siku baada ya kumtesa juani, alikuwa akimfunga kamba shingoni kisha akiwakabidhi watoto wadogo na wendawazimu wamburure Bilaal  (Radhwiya Allaahu 'anhu)  na wazunguke naye mjini Makkah, huku wakimzomea na kumpiga. Lakini alikuwa akiendelea kusema: “Ahadun Ahadun.”

 

Hali iliendelea hivyo hadi siku moja Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu)  alimuona Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu)  katika hali ya mateso hayo, akamwambia Umayyah: "Je, humuogopi Allaah unamtesa namna hii huyu maskini, mpaka lini utaendelea hivi?” Umayyah akamwambia: "Wewe ndiye uliyemharibu huyu, kwa hivyo sasa muokoe wewe kama unaweza." Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu)   akamnunua kwa wakia tano kisha akamuacha huru. Kabla ya hapo, Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu)   alikuwa keshawanunua watumwa sita na kuwaacha huru, na Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu)  alikuwa wa saba.

 

 

Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu)   akaepukana na adhabu, na Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu) bila shaka akapata ujira mkubwa kutoka kwa Rabb wake (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu)   aliendelea na kazi hiyo ya kuwanunua watumwa na kuwaacha huru. ‘Ulamaa wa tafsiri wamekubaliana kuwa Allaah Alimsifia Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu) katika Aayah 17 Suwratul-Layl:  

 

وَسَيُجَنَّبُهَا الْأَتْقَى ﴿١٧﴾

Na ataepushwa nao mwenye taqwa kabisa.

 

الَّذِي يُؤْتِي مَالَهُ يَتَزَكَّىٰ ﴿١٨﴾

Ambaye anatoa mali yake kujitakasa.

 

وَمَا لِأَحَدٍ عِندَهُ مِن نِّعْمَةٍ تُجْزَىٰ ﴿١٩﴾

Na hali hakuna mmoja yeyote aliyemfanyia fadhila yoyote hata amlipe.

 

 

إِلَّا ابْتِغَاءَ وَجْهِ رَبِّهِ الْأَعْلَىٰ ﴿٢٠﴾

Isipokuwa kutaka Wajihi wa Rabb wake Aliyetukuka.

 

 

وَلَسَوْفَ يَرْضَىٰ ﴿٢١﴾

Na bila shaka atakuja kuridhika. [Al-Layl: 17-21]

 

 

 

Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu) akaondoka pamoja na Bilaal  (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwenda kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).  Alipokuwa akiondoka naye, Umayyah akamwambia: "Ondoka naye hapa, Naapa kwa Laata na ‘Uzza, kuwa ungekataa kumnunua kwa wakia tano, basi hata kwa wakia moja tu ningekuuzia!" Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu)   akamjibu: “Lau kama ungelitaka nimnunue kwa wakia mia, basi ningelikupa.”

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alifurahi kupita kiasi alipomuona Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu)  kawa huru, akawabashiria Waislam juu yake na akamfanya baadaye kuwa ni Muadhini wa mwanzo katika Uislam, kwani Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa na sauti nzuri sana na Allaah Akaijaalia sauti hiyo iwe yenye kuleta taathira ndani ya nyoyo za kila mwenye kuisikia.

 

 

Iymaan ya Bilaal na subira yake imempatia fadhila zifuatazo:

 

1. Kupendwa mno na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  pamoja na Maswahaba zake.

 

2. Kuwa ni Muadhini wa kwanza wa Waislamu na hivyo thawabu za Swalaah za Maswahaba alizibeba yeye pia.

 

3. Alikuwa wa kwanza kuadhini juu Ka’bah, pale baada ya kuukomboa mji wa Makkah, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimtaka Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu) apande juu ya Al-Ka’bah na kuadhini.

 

4. Amebashiriwa Jannah na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  kwa kuwa alisikia sauti ya viatu vyake vikiwa mbele yake Peponi. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alipomuuliza ((Nielezee juu ya ‘amali njema kabisa unayoitenda, kwani nimesikia sauti ya viatu vyako vikiwa mbele yangu Peponi?)) Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu)  akajibu: “Ee Rasuli wa Allaah, sijafanya ‘amali yoyote niliyoiona kuwa ni bora kwangu isipokuwa kawaida yangu mimi kila nikitawadha huswali kadiri ninavyojaaliwa kuswali)) Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: ((Hilo ndilo lililokufikisha)) [Al-Bukhaariy]

 

5. Alishiriki katika vita vingi vikiwemo vya Badr na akaweza kumuua aliyekuwa bwana mmiliki wake, Umayyah bin Khalaf ambaye alikuwa akimtesa.

 

6. Alipata heshima kubwa kutoka kwa Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) kwani juu ya kuwa daraja yake ilikuwa ni kubwa mbele ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam),  lakini hakuwa mwenye kiburi wala kujiona wala kutakabari, bali alikuwa mnyenyekevu kwa Waislam wenzake, huku akiichunga nafsi yake.

 

Alifikwa na majonzi makubwa mno alipofariki Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  mpaka akashindwa  kuadhini.

 

Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu) alifariki akiwa shahidi kwani alifanya jihaad kwenda Shaam kupigana vita na akakumbwa na maradhi ya tauni yaliyowaua watu wengi sana huko Shaam. Inasemekana kuwa roho yake ilipokuwa ikimtoka, mkewe alikuwa akimwambia: "Huzuni iliyoje, huzuni iliyoje!” Lakini Bilaal (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa akiyafumbua macho yake akasema: "Bali furaha iliyoje, kesho nitaonana na wapenzi, Muhammad na Maswahaba."

 

 

Share

17-Swabrun Jamiyl: Subira Za Maswahaba - Khabbaab (Radhwiya Allaahu 'anhu)

 

Subira njema

 

17- Subira Za Maswahaba – Khabbaab (Radhwiya Allaahu 'anhu)

 

 

 

Khabbaab (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa ni mtengenezaji panga alizokuwa akiwauzia watu wa Makkah. Alikuwa ni miongoni mwa watu wa mwanzo kuingia Uislamu na akapata mateso kwa ajili ya Dini hii tukufu.

 

Makafiri walipotambua kwamba ameingia katika Dini ya Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  wakaanza kumtesa kwa kumvisha nguo ya chuma na kumlaza katika jua kali. Mara nyingi alilazwa katika mchanga wa moto uliombabua mgongo wake. Alichomwa pia kichwa chake kwa chuma cha moto. Makafiri walichukua vyuma walivyovikuta nyumbani kwake, alivyokuwa akitengenezea mapanga, kisha walivitia   katika moto viwake kisha wakamfunga navyo mwilini, miguuni na mikononi kama minyororo. Lakini alivumilia na mateso yalipomzidi, alimuomba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amwombee pamoja na Waislamu wengineo waliokuwa matesoni. Lakini Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwanasihi wathibitishe iymaan zao katika Dini ya haki na akiwakumbusha fadhila za kusubiri mitihani. 

 

‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu 'anhu) alipokuwa Khalifa wa Waumini, aliwahi kumuuliza Khabbaab (Radhwiya Allaahu 'anhu)  kuhusu mateso aliyoyapata kwa ajili ya kuingia Uislamu. Alipomuonyesha mgongo wake, ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu)   alishtuka na kusema: “Sijapatapo kuona kama hivi kabla!” Khabbaab akasema: “Mwili wangu uliburuzwa katika mrundo wa makaa ya moto hadi damu na mafuta yaliokuwa yakitoka mgongoni mwangu yalikuwa yakizima moto wa makaa.”

 

Alikuwa ni miongoni mwa Waumini dhaifu na masikini kama Bilaal na Suhayl  (Radhwiya Allaahu ‘anhum) ambao makafiri Quraysh walimtaka Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  atengane nao. Lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alimteremshia Rasuli Wake Aayah za Qur-aan kumkataza asiwafuate makafiri. Aayah za Qur-aan zikawanyanyua na kuwapa heshima na utukufu na badala yake ikawa ni kuwadhalilisha makafiri:

 

وَلَا تَطْرُدِ الَّذِينَ يَدْعُونَ رَبَّهُم بِالْغَدَاةِ وَالْعَشِيِّ يُرِيدُونَ وَجْهَهُ ۖ مَا عَلَيْكَ مِنْ حِسَابِهِم مِّن شَيْءٍ وَمَا مِنْ حِسَابِكَ عَلَيْهِم مِّن شَيْءٍ فَتَطْرُدَهُمْ فَتَكُونَ مِنَ الظَّالِمِينَ ﴿٥٢﴾

Na wala usiwafukuze wale wanaomwomba Rabb wao asubuhi na jioni wanataka Wajihi Wake. Si juu yako hisabu yao hata kidogo, na wala hisabu yako si juu yao hata kidogo, hata ukawafukuza; utakuja kuwa miongoni mwa madhalimu.

   

وَكَذَٰلِكَ فَتَنَّا بَعْضَهُم بِبَعْضٍ لِّيَقُولُوا أَهَـٰؤُلَاءِ مَنَّ اللَّـهُ عَلَيْهِم مِّن بَيْنِنَا ۗ أَلَيْسَ اللَّـهُ بِأَعْلَمَ بِالشَّاكِرِينَ ﴿٥٣﴾

Na hivyo ndivyo Tulivyowafanyia mtihani baadhi yao kwa baadhi ili waseme: “Je, hawa ndio wale Aliowafadhilisha Allaah baina yetu?” Je, kwani Allaah Hajui zaidi wanaoshukuru?

   

وَإِذَا جَاءَكَ الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِآيَاتِنَا فَقُلْ سَلَامٌ عَلَيْكُمْ ۖ كَتَبَ رَبُّكُمْ عَلَىٰ نَفْسِهِ الرَّحْمَةَ ۖ أَنَّهُ مَنْ عَمِلَ مِنكُمْ سُوءًا بِجَهَالَةٍ ثُمَّ تَابَ مِن بَعْدِهِ وَأَصْلَحَ فَأَنَّهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٥٤﴾

Na wanapokujia wale wanaoamini Aayaat Zetu basi sema: “Salaamun ‘alaykum! Rabb wenu Ameandika juu ya Nafsi Yake rahmah; kwamba yeyote miongoni mwenu atakayetenda ovu kwa ujahili, kisha akatubia baada yake na akatengenea, basi hakika Yeye ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.” [Al-An’aam: 52-54]

 

Khabbaab (Radhwiya Allaahu 'anhu)  alithibitisha iymaan yake juu ya mateso na adhabu kali. Alishiriki vita vyote pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hadi kufariki kwake. 

 

Hao ni Waislamu wa mwanzo waliotupa mafunzo muhimu ya kuvumilia tabu na mateso kwa ajili ya mapenzi ya Dini yao tukufu. 

 

 

Share

18-Swabrun Jamiyl: Subira Za Maswahaba - Habiyb Bin Zayd Al-Answaariy (Radhwiya Allaahu 'Anhu)

 

Swabrun Jamilyl (Subira njema)

 

18- Subira Za Maswahaba - Habiyb Bin Zayd Al-Answaariy (Radhwiya Allaahu 'Anhu)

 

 

 

Habiyb bin Zayd Al-Answaariy (Radhwiya Allaahu 'anhu) alitumwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  kwa Musaylimah al-Kadhaab kumpelekea majibu ya barua yake aliyomtumia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kukiri urasuli wake wa uongo. Musaylimah alikwishajitangaza kwa watu na wengi kuwa yeye ni rasuli na watu wakaanza kumfuata na kumwamini. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamjibu barua yake kwa kumtaka Musaylimah aache madai yake ya urasuli. Barua hiyo ilimghadhibisha sana Musaylimah akatoa amri afungwe Habiyb (Radhwiya Allaahu 'anhu)  na kupelekwa katika hadhara ya wakuu wake. Akaanza kumuuliza:

 

“Unashuhudia kuwa Muhammad ni Rasuli wa Allaah”

Habiyb  (Radhwiya Allaahu 'anhu) akajibu:  “Ndiyo nashuhudia hivyo”.

Musaylimah akamuuliza: “Na unashuhudia kuwa mimi pia ni rasuli wa Allaah?”

Habiyb akajibu: “Masikio yangu yamezibwa kusikia madai yako hayo”

Akamuuliza tena: “Unashuhudia kuwa Muhammad ni Rasuli wa Allaah?”

Habiyb (Radhwiya Allaahu 'anhu) akajibu tena: “Ndiyo nashuhudia hivyo”.

Musaylimah akamuuliza tena: “Na unashuhudia kuwa mimi pia ni rasuli wa Allaah?”

Habib akajibu tena: “Masikio yangu yamezibwa kusikia madai yako hayo.”

 

Akawa anaendelea kumuuliza hivyo, na kila anapoulizwa Habiyb (Radhwiya Allaahu 'anhu) iwapo anashuhudia kuwa Muhammad ni Rasuli wa Allaah, alikiri. Na anapoulizwa iwapo anashuhudia kuwa Musaylimah pia ni rasuli wa Allaah, alijibu vile vile kuwa yeye kiziwi hasikii madai yake.

 

Mwisho Musaylimah akasema: “Niitieni mshika panga wangu na mpiga mjeledi.”

 

Wakaanza kumtesa Habiyb (Radhwiya Allaahu 'anhu) huku wakimpiga mijeledi na kumkata vipande vipande. Wakaanza kumkata mkono mmoja, ukaanguka chini. Kisha Musaylimah akamuuliza tena maswali yale yale, lakini Habiyb (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa thabiti na kuwapa majibu yale yale. Musaylimah akatoa amri akatwe mkono mwengine ukaanguka mbele ya mkono wa awali uliokatwa. Wakamtesa mpaka akafa shahidi (Radhwiya Allaahu 'anhu). Ummu ‘Ammaarah aliposikia juu ya kuuliwa kwa mwanawe akasema: “Mwanangu keshanitangulia Jannah.”

 

 

 

Share

19-Swabrun Jamiyl: Subira Za Maswahaba - Ka'ab bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'Anhu)

 

Swabrun Jamilyl (Subira njema)

 

19 - Subira Za Maswahaba – Ka’ab Bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘Anhu)

 

 

 

 

Subira yake ilihusiana na Maswahaba watatu (Radhwiya Allaahu ‘anhum) waliofanya makosa ya kutokwenda kupigana vita vya Tabuwk bila ya sababu pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Vilikuwa ni vita ambavyo kwa mara ya kwanza jeshi la Waislam lilijitayarisha kupambana na jeshi kubwa la Warumi katika mwaka wa 9 Hijriyyah wakati wa joto kali sana. Vita hivyo vilivyojulikana kama ni ‘Vita vya Dhiki’. Wanafiki takriban themanini hawakushiriki na wakatoa visingizio mbali mbali. Lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akateremsha Aayah kadhaa za Qur-aan katika Suwratut-Tawbah kuhusu unafiki wao.

 

 

Ka’ab bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa mwenye taqwa na mapenzi ya Allaah na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Alikwishashiriki katika vita vyote pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) isipokuwa vita vya Badr. Na katika vita vya Uhud alimhami Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kubadilishana naye nguo ili maadui wasipate kumuandama na kumuua Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na kwa hivyo, Ka’ab alipata majeraha kumi na moja.

 

 

Kisa chake kuhusu vita vya Tabuwk ni fundisho kubwa kwa Waislamu kujifunza subira katika kutafuta radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) pamoja na kujifunza namna gani Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walikuwa watiifu kwa kiongozi wao na kipenzi chao Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Maswahaba watatu hao (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walivumilia sana katika subira yao wakawa katika dhiki ya nafsi mpaka walihisi kuwa ardhi imewabana kutokana na dhiki. Walitambua kuwa hapana pa kukimbilia isipokuwa Kwake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Kisa chake amekielezea mwenyewe kama alivyokirekodi Imaam Al-Bukhaariy.

 

Anasema Ka’ab (Radhwiya Allaahu 'anhu):

“Sikupata kuwa katika hali nzuri kwa hali na mali kama nilivyokuwa wakati watu wakijitayarisha na vita hivyo. Wa-Allaahi sikupata kukusanya wanyama wawili wa kunipeleka vitani isipokuwa katika vita hivyo. Na ilikuwa kawaida ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anapotaka kupigana vita vyovyote hutoa ishara kama kwamba anataka kupigana vita vingine, (Isipokuwa katika vita hivi hakufanya hivyo kwa sababu ya umbali wa safari na ukali wa joto), mpaka ulipowadia wakati wa vita hivyo vilivyokuwa katika joto kali sana, safari ndefu, pamoja na maadui wengi sana.

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa katika hali ya kujitayarisha, na Waislam pia wakawa katika hali hiyo, na watu walikuwa wengi sana. Nikasema: “Kesho mimi nitajitayarisha nijiunge nao.” Nikawa nakwenda nikirudi bila ya kufanya chochote, huku nikijisemesha nafsini mwangu: “Wakati wowote ninapotaka nitaweza kujitayarisha nijiunge nao.”

 

Nikaendelea na hali hiyo mpaka mambo yalipoanza kupamba moto, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoamua kuondoka asubuhi ya siku ya pili yake pamoja na Waislam, na mimi bado sikuwa nimejitayarisha kwa chochote. Nikasema: “Nitajitayarisha siku ifuatayo baada ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuondoka, au hata baada ya siku mbili kisha nitakutana nao njiani kabla ya wao kuwasili Tabuwk.”

 

Nikatoka asubuhi ya siku ya pili ili nianze kujitayarisha na kununua mahitajio yangu ya vitani, hatimae nikarudi nyumbani bila kufanya chochote. Nikawa katika hali hiyo mpaka zikatufikia habari kuwa Waislam wamekwishawasili Tabuwk na kwamba vita vishaanza, ndipo iliponipitikia niondoke ili niwawahi. Laiti ningefanya hivyo. Lakini sikujaaliwa. Nikawa kila ninapotoka nje ya nyumba yangu na kuonana na watu, ninahuzunika sana na kuona uchungu kwa sababu sikuwa nikimuona mtu yeyote aliye kufu yangu (aliyelingana nami). Sikuwa nikiwaona isipokuwa wale watu waliokuwa wakijulikana kuwa ni wanafiki, au wale waliokuwa na udhuru wa kutokwenda vitani kwa sababu ya umasikini, udhaifu wa hali zao au maradhi.

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuuuliza juu yangu mpaka walipowasili Tabuwk, akasema huku akiwa amekaa pamoja na watu: ((Amefanya nini Ka’ab?)) Mmoja katika watu wa Bani Salamah akasema: "Limemzuia tandiko lake na kuwatazama awapendao." Mu’aadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu 'anhu) akasema: "Maneno mabaya yaliyoje uliyosema! Wa-Allaahi ee Rasuli wa Allaah, sisi tunavyomjua ni mtu anayependa kheri tu." Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akanyamza.

 

 

Niliposikia kuwa misafara inaanza kurudi nikaanza kujisemesha huku nikifikiri uongo upi niuseme hata Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) (anisadiki na) asighadhibike nami? Nikawaendea jamaa zangu wale wenye hekima kutaka ushauri wao. Wakati Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipowasili Madiynah, mimi nilikuwa nishafikia uamuzi kuwa sina budi kumwambia ukweli, na kwamba nikisema uongo sitoweza kuokoka nao. Nikaamua kuwa lazima niseme kweli tu. Asubuhi iliyofuata Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwasili, na ilikuwa kawaida yake anapowasili kwanza huenda Msikitini kuswali rakaa mbili, kisha hukaa hapo muda kidogo kwa ajili ya kusikiliza matatizo ya watu. Wale waliobaki Madiynah wasiende vitani wakaanza kumuendea huku wakimtolea (kila aina ya) udhuru, na walikuwa kiasi cha watu themanini na kidogo hivi. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwakubalia wote udhuru wao na kuwaombea maghfirah na kumuachia Rabb wao ukweli wa udhuru walioutoa. Nilipomsogelea mimi na kumsalimia alitabasamu huku akionyesha dalili ya kughadhibika nami, kisha akaniambia: ((Njoo)) Nikamuendea mpaka nikakaa mbele yake. Akaniuliza: ((Nini kilichokufanya ubaki nyuma, si ulikuwa ushajitolea kupigana?)) Nikamwambia: "Ndiyo, wa-Allaahi ningeulizwa suali hili na mwengine asiyekuwa wewe katika watu wa dunia ningeweza kusalimika kwa kutoa udhuru wowote ule. Lakini nilijishauri sana nikaona kuwa ikiwa nitakutolea udhuru wowote wa uongo leo ukaridhika nami, Allaah Atakujulisha na utakuja kunichukia. Na iwapo nitakuambia ukweli, ukaujua ukweli juu yangu, mimi nategemea msamaha wa Allaah. Wa-Allaahi sikuwa na udhuru wowote, wa-Allaahi sikupata kuwa na nguvu na uwezo wa kifedha kuliko siku niliyokuacha na kubaki nyuma.” Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaniambia: ((Ama huyu amesema kweli. Inuka na ungoje mpaka Allaah Atakapotoa uamuzi wake juu yako)).

 

Nikainuka na kuondoka hapo, na watu wa kabila la Bani Salamah wakainuka kunifuata, wakaniambia: "Wa-Allaahi sisi tunavyokujuwa ni kuwa hujapata kufanya kosa kabla ya hili, kwa nini umeshindwa kutoa udhuru (wowote) kama walivyofanya wengine? Ingelitosha kufuta dhambi yako kwa maghfirah atakayokuombea Rasuli kwa Allaah.” Wakawa wanaendelea kunilaumu mpaka nikafikiria nirudi tena kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kutoa udhuru wowote na kujidanganya nafsi yangu. Kisha nikawaambia: "Yuko mwengine aliyekuwa kama mimi?" Wakasema: "Wawili, wamesema kama ulivyosema na wakaambiwa kama ulivyoambiwa." Nikauliza: "Nani hao?" Wakaniambia: "Muraarah bin Rabiy’ Al-‘Amriy na Hilaal bin Umayyah Al-Waaqifiyy." Hawa ni watu wawili wenye taqwa waliopigana vita vya Badr na walijulikana kuwa ni wenye mfano mwema.

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaamrisha sote watatu tusisemeshwe na mtu.

 

Tukawa tunawaepuka watu na wao wanatuepuka. Haukupita muda watu wakaanza kutubadilikia hata nikaichukia ardhi ikawa kama nisiyoijua. Tukaendelea katika hali hiyo muda wa siku hamsini. Wenzangu walijikalia majumbani mwao wakilizana, lakini mimi nilikuwa kijana zaidi kupita wao na mwenye ustahamilivu zaidi. Nikawa natoka na kuswali Msikitini pamoja na Waislam, huku nikitembea sokoni, lakini hakuna mtu anayenisemesha. Nilikuwa nikimkabili Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumsalimia akiwa amekaa mahali pake baada ya Swalaah, kisha hujiuliza nafsini mwangu: “Mdomo wake ulitikisika kuijibu salamu au haukutikisika?” Mara nyingi huswali karibu yake, na baada ya Swalaah, humtizama kwa kuibiaibia huku nikijishughulisha na du’aa baada ya Swalaah, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa mara nyingine akiniangalia, lakini ninapomuangalia mimi, yeye huugeuza uso wake.

 

Dhiki ya kupigwa pande ilipozidi nikaamua siku moja kwenda nyumbani kwa Abuu Qataadah ambaye ni mtoto wa ‘ammi yangu, na nilikuwa nikimpenda sana. Nikaparamia ukuta, nikaingia uani na kugonga mlango wa nyumba yake, nikaingia ndani na kumsalimia. Wa-Allaahi hakuijibu salamu yangu. Nikamuambia: "Abu Qataadah! Unavyonijua mimi je, simpendi Allaah na Rasuli Wake?" Akanyamaza asinijibu kitu. Nikamuuliza tena suala hilo hilo, akanijibu: “Allaah na Rasuli Wake ndio wanaojua.” Machozi yakanitoka. Nikaondoka na kuruka ukuta nikatoka nje.

 

Siku moja nilipokuwa nikitembea sokoni nikamsikia mmoja katika watu wa Shaam aliyekuja kufanya biashara ya vyakula akisema: “Nani atakayenipeleka kwa Ka’ab bin Maalik?” Watu wakamuelekeza kwangu. Akanijia na kunipa barua iliyotoka kwa mfalme Ghassaan iliyoandikwa yafuatayo: “Nimepata habari kuwa sahibu yako amekupiga pande, na Rabb wako amekufanya usiwe na raha, kwa hivyo njoo kwetu tutakuliwaza.” Nikasema moyoni mwangu: “Huu pia ni mtihani mwengine.” Nikaitumbukiza barua ile ndani ya tanuri la moto na kuiunguza, na ilipofika siku ya arubaini katika zile siku hamsini, mjumbe kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alinijia na kuniambia: "Kwa hakika Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anakuamrisha usimkaribie mkeo”.

Nikamuuliza: “Nimtaliki au nifanyeje?” Akaniambia: “Bali uwe mbali naye na usimkaribie.” Na wenzangu wale wawili wakapewa amri kama niliyopewa mimi. Nikamuambia mke wangu: “Nenda kwa wazee wako na ubaki kwao mpaka Allaah Atakapotoa amri Yake.” Mke wa Hilaal bin Umayyah alikwenda kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuambia: “Ee Rasuli wa Allaah, kwa hakika mume wangu Hilaal ni mtu mzima asiyeweza kujitumikia mwenyewe na hana mfanyakazi wa kumsaidia, utachukizwa iwapo nitabaki kwake na kumhudumia?” Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuambia: ((Hapana [sitochukizwa] lakini asikukaribie)). Akasema: “Wa-Allaahi yeye hana haja ya kufanya jambo lolote. Tokea yalipotokea yaliyotokea, mpaka leo hana isipokuwa kulia tu.”

 

Baadhi ya watu wangu wakaniambia: “Na wewe ungelimuomba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amruhusu mkeo akutumikie kama alivyomruhusu mke wa Hilaal bin Umayyah.” Nikawaambia: “Wa-Allaahi mimi sitomuomba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), sijui atanijibu nini nitakapomuomba, kwa sababu mimi ni kijana bado.” Nikaendelea katika hali hiyo kwa muda wa siku kumi nyingine, mpaka zikakamilika siku hamsini tokea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipowataka watu wasitusemeshe.

 

Baada ya kuswali Swalaah ya Alfajiri ya siku ya hamsini, nikapanda juu ya dari la mojawapo ya nyumba zetu na kukaa. Na wakati nilipokuwa katika hali ile Aliyoisema Allaah kuwa: ((mpaka ardhi ikadhikika kwao juu ya kuwa ni pana)) [At-Tawbah 9: 118] Nikasikia sauti kali ikitokea juu ya jabali ikisema: “Ee Ka’ab pokea bishara njema!” Pale pale nilipo nikaporomoka na kusujudu, nikajua kuwa faraja imekwishawasili. Baada ya Swalaah ya Alfajiri Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwatangazia watu juu ya kusamehewa kwetu na Allaah, na watu wakatoka na kuanza kutupa bishara njema hizo.

 

Wengine wakaja kwangu na wengine wakaenda kwa sahibu zangu. Walikuja wakiwa wamepanda wanyama wao na wengine kwa miguu kwa ajili ya kutupongeza. Na aliponijia yule niliyeisikia sauti yake akinipa bishara njema pale mwanzo, nilimvisha guo langu kama ni zawadi yake. Wa-Allaahi sikuwa nikimiliki isipokuwa nguo hiyo tu, na mimi nikaazima nguo nyingine za kuvaa, kisha nikaelekea Msikitini kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) huku watu wakinijia makundi kwa makundi wakinipongeza na kuniambia: “Tunakupongeza kwa tawbah iliyokuja kutoka kwa Allaah!”   Nilipoingia Msikitini, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa amekaa akiwa amezungukwa na watu, na Twalhah bin ‘Ubaydillaah alikuwa wa mwanzo kunijia mbio na kunipa mkono na kunipongeza. Hakusimama na kunipongeza katika Muhaajiriyn mahali pale isipokuwa Twalhah, sitomsahau kwa tendo lake hilo.

 

Nilipomsalimia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) huku uso wake ukiwa unang'ara kwa furaha, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anapofurahi, uso wake huwa unang'ara mfano wa kipande cha mwezi, akaniambia: ((Pokea bishara njema za kufikiwa na siku bora kupita siku zote tokea ulipozaliwa)) Nikamuuliza: “Msamaha huu umetoka kwako ee Rasuli wa Allaah, au kutoka kwa Allaah?” Akanijibu: ((Bali kutoka kwa Allaah)).  Nikiwa bado nimekaa mbele yake nikamuambia: “Ee Rasuli wa Allaah, kwa ajili ya kutubiwa kwangu huku, nataka kutoa mali yangu yote sadaka kwa ajili ya Allaah.”  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaniambia: ((Zuia mali yako, kwani hiyo ni kheri yako)). Nikamuambia: “Mimi nitazuia sehemu yangu ya Khaybar.”

 

Nikawa kila siku naiambia nafsi yangu: “Allaah Ameniokoa kwa ajili ya kusema ukweli. Kwa ajili hiyo katika maisha yangu sitotamka isipokuwa ukweli tu. Kwani Wa-Allaahi simjui Muislam yeyote aliyepata mtihani mkubwa kutoka kwa Allaah kwa ajili ya kusema ukweli tokea siku niliyozungumza na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mpaka leo hii, kuliko mtihani nilioupata mimi. Na mimi namuomba Allaah Anihifadhi katika siku zangu zilizobaki." Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akateremsha Aayah zifuatazo:

 

لَّقَد تَّابَ اللَّـهُ عَلَى النَّبِيِّ وَالْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ الَّذِينَ اتَّبَعُوهُ فِي سَاعَةِ الْعُسْرَةِ مِن بَعْدِ مَا كَادَ يَزِيغُ قُلُوبُ فَرِيقٍ مِّنْهُمْ ثُمَّ تَابَ عَلَيْهِمْ ۚ إِنَّهُ بِهِمْ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ﴿١١٧﴾

 

Kwa yakini Allaah Amepokea tawbah ya Nabiy na Muhajirina na Answaar ambao wamemfuata (Nabiy صلى الله عليه وآله وسلم) katika saa ya dhiki baada ya nyoyo za kundi miongoni mwao zilikaribia   kuelemea mbali na haki Akapokea tawbah yao. Hakika Yeye kwao ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.

 

وَعَلَى الثَّلَاثَةِ الَّذِينَ خُلِّفُوا حَتَّىٰ إِذَا ضَاقَتْ عَلَيْهِمُ الْأَرْضُ بِمَا رَحُبَتْ وَضَاقَتْ عَلَيْهِمْ أَنفُسُهُمْ وَظَنُّوا أَن لَّا مَلْجَأَ مِنَ اللَّـهِ إِلَّا إِلَيْهِ ثُمَّ تَابَ عَلَيْهِمْ لِيَتُوبُوا ۚ إِنَّ اللَّـهَ هُوَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ﴿١١٨﴾

 

Na (Akapokea tawbah) ya wale watatu waliobaki nyuma (wakajuta mno) mpaka ardhi ikadhikika kwao juu ya kuwa ni pana na zikadhikika nafsi zao, na wakatambua kwamba hakuna pa kumkimbia Allaah isipokuwa kuelekea Kwake; kisha (Allaah) Akapokea tawbah yao, ili watubie. Hakika Allaah Yeye Ndiye Mwingi wa kupokea tawbah, Mwenye kurehemu.

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَكُونُوا مَعَ الصَّادِقِينَ﴿١١٩﴾

 

Enyi walioamini! Mcheni Allaah na kuweni pamoja na wakweli. [At-Tawbah: 117-119]

 

 

Naapa kwa Allaah! Mbali ya (neema) kuwa Allaah Amenihidi katika Uislamu, Hajapata kuniteremshia neema kama neema ya ukweli wangu kuwa sikusema uongo kwa Rasuli wa Allaah, jambo ambalo lingeliniangamiza kama walivyoangamia waliosema uongo, kwani Allaah Amewataja waliosema uongo kwa sifa mbaya kabisa Hajapatapo kumpa sifa hiyo yeyote mwengine, Aliposema:

 

سَيَحْلِفُونَ بِاللَّـهِ لَكُمْ إِذَا انقَلَبْتُمْ إِلَيْهِمْ لِتُعْرِضُوا عَنْهُمْ ۖ فَأَعْرِضُوا عَنْهُمْ ۖ إِنَّهُمْ رِجْسٌ ۖ وَمَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ﴿٩٥﴾

 

Watakuapieni kwa Allaah, mtakaporudi kwao ili muwapuuze. Basi wapuuzeni; hakika wao ni najsi, na makazi yao ni Jahannam. Ni jazaa kwa yale waliyokuwa wakiyachuma.

 

يَحْلِفُونَ لَكُمْ لِتَرْضَوْا عَنْهُمْ ۖ فَإِن تَرْضَوْا عَنْهُمْ فَإِنَّ اللَّـهَ لَا يَرْضَىٰ عَنِ الْقَوْمِ الْفَاسِقِينَ﴿٩٦﴾

 

Watakuapieni ili muwaridhie. Mkiwaridhia, basi hakika Allaah Haridhii watu mafasiki. [At-Tawbah:  95-96]

 

 

Ka’ab akaendelea kusema: “Hali ya sisi watatu ni tofauti na ambao visingizio vyao alivipokea Rasuli wa Allaah walipomuapia. Akafungamana nao kiapo cha utiifu, na akamuomba Allaah Awasamehe. Lakini Rasuli wa Allaah aliacha kesi yetu ibakie kungoja uamuzi mpaka Allaah Alipoitolea hukmu Yake. Na kwa hiyo Akasema Allaah:

((Na [Akapokea tawbah ya] wale watatu walioachwa nyuma [wakajua makosa yao]...))

 

Aliyoyasema Allaah katika Aayah hii haidhihirishi kushindwa kwetu kushiriki vita, ila inahusu kuakhirishwa maamuzi ya Rasuli kuhusu kesi yetu. Ni tofauti na kesi ya waliofungamana naye kiapo akawasamehe kwa kupokea visingizio vyao”.

 

Share

20-Swabrun Jamiyl: Subira Za Swahaabiyaat - Ummu Haarithah (Radhwiya Allaahu 'Anhaa)

 

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)

 

20- - Subira Za Swahaabiyaat - Ummu Haarithah (Radhwiya Allaahu ‘Anhaa)

 

 

Naye ni Ar-Rabiy’ bint Nadhwr bin Dhwamdhwam bin Zayd, shangazi yake Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhum). Mama mzee aliyevuta subira kwa ajili ya kutaka Jannah baada ya kuuliwa mwanawe mpenzi katika vita vya Badr. Waliporudi watu vitani aliangaza huku na kule akimtafuta mwanawe. Waume walirudi kwa wake zao, watoto walirudi kwa wazazi wao. Yeye akangojea na kungojea amuone kipenzi cha moyo wake, lakini Haarithah hakutokea. Akamwendea Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akiwa machozi yamemlenga machoni. Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesimulia: “Ummu Haarithah alikwenda kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  baada ya Haarithah kufa shahidi katika vita vya Badr kwa mshale aliodungwa moyoni na mtu asiyejulikana. Akasema: “Ee Rasuli wa Allaah! Unajua mahali pa Haarithah moyoni mwangu (jinsi alivyo kipenzi kwangu), kwa hiyo ikiwa yuko Jannah, sitomlilia, au sivyo unaona nifanye nini? Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Hakika hizo ni Jannaat nyingi si Jannah [moja] na mwanao amefikia Jannah ya Al-Firdaws ya juu))”.

 

Mama mzee huyo aliposikia jibu hilo, machozi yake yakamkauka akarudi nyumbani kwake akiwa na matumaini ya kuondoka duniani ajumuike na mwanawe huko Peponi. Hakutaka ngawira wala mali, wala lolote bali aliridhika na Jannah. Madamu mwanawe yupo Jannah amestarehe kwa mema waliyobashiriwa mashahidi, basi kumkosa mwanawe duniani hakukuwa na umuhimu tena. Akaendelea kuvuta subira kupata mema yanayodumu milele.

 

 

Share

21-Swabrun Jamiyl: Subira Za Swahaabiyaat - Nusaybah Ummu ‘Ammaarah (Radhwiya Allaahu 'Anhaa)

 

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)

 

21 - Subira Za Swahaabiyaat -  Nusaybah Ummu ‘Ammaarah (Radhwiya Allaahu ‘Anhaa)

 

 

Nusaybah bint Ka’ab Al-Answaariyyah, alijukana pia kwa jina la Ummu ‘Ammaarah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa). Alisilimu aliposikia tu Uislaam. Na alijaaliwa kuwa katika fungamano la kumlinda Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa hali na mali lilojuliakna kwa ‘Bay’atul-‘Aqabah’ (Fungamano la Al-‘Aqabah) la Pili’. Ujumbe upatao wanaume sabiini na wanawake wawili akiwemo yeye kutoka Madiynah walikwenda Makkah kwa siri kukutana na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  kufungamana na ahadi zake. Alishiriki katika vita vingi vikiwemo vita vya Uhud, Hudaybiyah, Khaybar, vita vya Al-Yamaamah na Hunayn. Alihudhuria pia siku ya ‘Bay’atur-Ridhwaan’ (Fungamano la Radhi] pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba wengineo chini ya mti, akaingia katika miongoni mwa wale Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Aliowateremshia kauli Yake:

 

لَّقَدْ رَضِيَ اللَّـهُ عَنِ الْمُؤْمِنِينَ إِذْ يُبَايِعُونَكَ تَحْتَ الشَّجَرَةِ فَعَلِمَ مَا فِي قُلُوبِهِمْ فَأَنزَلَ السَّكِينَةَ عَلَيْهِمْ وَأَثَابَهُمْ فَتْحًا قَرِيبًا﴿١٨﴾

Kwa yakini Allaah Amewawia radhi Waumini walipofungamana nawe ahadi ya utiifu (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) chini ya mti, (Allaah) Alijua yale yaliyomo nyoyoni mwao; basi Akawateremshia utulivu, na Akawalipa ushindi wa karibu. [Al-Fat-h: 18]

 

 

Alibashiriwa Jannah pia pamoja na kuwa karibu na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Alikuwa na mapenzi makubwa mno ya Dini yake na akimpenda mno Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Alikuwa mwanamke shujaa aliyependa jihaad katika njia ya Allaah na kusaidia waliokuwa wakijeruhiwa vitani. Aliposhiriki vita vya Uhud alionyesha ushujaa wake na mapenzi yake ya ajabu ya kumhami Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).  Alipatwa majeraha kumi na mbili. Kisa chake amekisimulia mwenyewe:

“Nilitoka wakati wa asubuhi siku hiyo nikiwa nimebeba birika la maji na kuelekea moja kwa moja penye uwanja wa vita nikajionee mwenyewe yanayotendeka huko. Nikamuona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa kati ya Swahaba zake na wakati huo Waislamu walikuwa wakiwashambulia makafiri na kuwashinda. Ghafla mambo yakabadilika na Waislam wakaanza kushindwa, na kurudi nyuma. Nilipomuona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amezungukwa na maadui, nikautoa upanga wangu na kusimama mbele yake na kuanza kupigana huku na kule. Akatangulia kafiri mmoja anayeitwa Abuu Qamiy-ah huku akisema kwa sauti kubwa: “Nionesheni alipo Muhammad! hatosalimika leo ikiwa mimi nitakuwa salama”. Anasema Nusaybah  (Radhwiya Allaahu ‘anhaa)  “Alipomfikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  na wakati huo alikuwa keshaanguka chini akiwa amejeruhiwa, mimi nikamkabili kafiri huyo akiwa na upanga mkononi nami nikiwa nimesimama baina yake na baina ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) huku akinichoma kwa upanga wake mara nyingi. Nami nikampiga kwa upanga wangu mara nyingi pia, lakini adui wa Allaah yule alikuwa amevaa nguo mbili za chuma.” Mwanawe Nusaybah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) ambaye ni  ‘Abdullaah bin Zayd  (Radhwiya Allaahu 'anhu)  alisema: “Baada ya vita vya Uhud kumalizika niliona majeraha mengi juu ya mwili wa mama yangu Nusaybah, na majeraha mengine yalikuwa makubwa hata ilikuwa ukiweza kuiingiza kiganja cha mkono ndani yake kutazama.”

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alipozungumza juu ya ushujaa wake siku ya Uhud alisema: ((Daraja ya Nusaybah binti Ka’ab leo ni kubwa kuliko fulani na fulani)) Na alikuwa akisema kumwambia Nusaybah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa): ((Nani atakayeweza kustahamili ulivyostahamilia wewe ee Ummu ‘Ammaarah?))  Na Ummu ‘Ammaarah  (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) akawa anamjibu: “Mimi niko tayari kustahamili chochote ee Rasuli wa Allaah, isipokuwa nataka tu uniombee niwe pamoja nawe siku ya Qiyaamah.” Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: ((Bali utakuwa pamoja nami, tena si peke yako, wewe na wanao na familia yako yote. Ee Rabb wangu! mjaalie yeye na familia yake yote wawe pamoja nami Peponi)). Pia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: ((Nilikuwa ninapogeuka kushoto au kulia namuona yeye akipigana kwa ajili yangu)).

 

Nusaybah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alidhihirisha subira yake mara nyingine katika vita vya Al-Yamaamah alipokatwa mkono wake. Vilikuwa ni vita baina ya majeshi ya Kiislamu na majeshi ya Musaylimah Al-Kadh-dhaab wakati wa ukhalifa wa Abuu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu).   Ummu ‘Ammaarah  (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alipomtaka Khalifa wa Waislam ruhusa ili ashiriki vita hivyo, Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu)  alimwambia: “Tunaulewa vizuri ushujaa wako na usatahamilivu wako ee Ummu ‘Aamaarah, ingia vitani ukitaka kwa baraka za Allaah” Ummu Sa’ad bin Ar-Rabiy’ amesema: “Nilimuona Nusaybah bint Ka’ab mkono wake ukiwa umekatika, nikamuuliza: “Lini umekatika mkono wako?” Akanambia: “Siku ya (vita vya) Al-Yamaamah nilikuwa pamoja na watu wa Madiynah, tulipofika katika bustani ya Musaylimah, vita vikali vikapiganwa kwa muda hivi kwa ajili ya kupateka mahali hapo, na Abuu Dujaanah aliuliwa mahali hapo. Kisha nikaingia mimi ndani ya qasri nikimtafuta adui wa Allaah, Musaylimah al-Kadh-dhaab, akanitokea mmoja katika watu wake. Nikapambana naye, akanipiga na kunikata mkono wangu. Basi wa-Allaahi sijauendea kuuokota, nilisonga mbele kumtafuta mpaka nikamuona khabithi yule (Musaylimah) akiwa amekufa, na mwanangu (‘Abdullaah bin Zayd) akiwa karibu yake huku akiufuta upanga wake juu ya mwili wa Musaylimah, Nikamuuliza: “Wewe ndiye uliyemuua?” Akanijibu: “Ndiyo ee mama yangu.” Nikasujudu kumshukuru Allaah.”

 

 

Riwaayah nyingine imesemekana kwamba aliyemuua Musaylimah ni Wahsh bin Harb Al-Habashiyyi na kwa hiyo imesemekana kwamba wote wawli walihusika kumuua adui huyo wa Allaah

 

Share

22-Swabrun Jamiyl: Subira Za Swahaabiyaat - 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'Anhaa)

 

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)  

 

22- Subira Za Swahaabiyaat – Mama Wa Waumini  ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘Anhaa)

 

 

 

 

Kisa kinachojulikana kwa ‘Ifk’ (kashfa ya uzushi) kimekusanywa katika Al-Bukhaariy Amekielezea mwenyewe Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa)

 

“Kila alipotaka Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  kwenda safari alikuwa akipiga kura ya wake zake. Kisha ambaye kura imemuangukia, huwa ndiye anayechukuliwa safarini pamoja naye.

 

Wakati mmoja alipotaka kwenda vitani, kura ikaniangukia mie kwa hiyo nikasafiri na Rasuli wa Allaah. Wakati huo Shariy’ah ya hijaab kwa wanawake ilikuwa imeshaamrishwa, kwa hiyo nikawa nabebwa katika msafara (juu ya ngamia) na nikiteremshwa nayo.

 

Tukaendelea na safari, na Rasuli wa Allaah alipomaliza vita vyake kisha akarudi, tukakaribia Madiynah. Rasuli wa Allaah akaamrisha kuendelea safari usiku. Jeshi lilipoamrishwa kuendelea safari ya nyumbani, niliinuka (kutaka kufanya haja msalani) nikatembea (kutafuta sehemu ya kufanyia haja) hadi nikaliacha (kambi la) jeshi nyuma. Nilipomaliza kujisaidia (msalani), nililiendea msafara wangu lakini kumbe! (mara nikakumbuka!) Kidani changu kilotengenezwa kutokana na aina ya shanga nyeusi kilivunjika. Nikakitafuta hadi kutafuta huko kukanizuia. Watu waliokuwa wakinibeba (katika msafara) wakafika ili kulibeba msafara juu ya ngamia wangu niliyekuwa nimempanda wakidhania kwamba nimo humo. Wakati huo wanawake walikuwa hafifu kwa uzani na hawakuwa wanene kwani walikuwa wakila (chakula) kidogo, kwa hiyo wale watu hawakuhisi kuwa msafara ni hafifu walipounyanyua. Nami nilikuwa bado mwanamke kijana.

 

Wakamwendesha ngamia, wakaendelea. Nami nikakiona kidani changu baada ya jeshi kuondoka. Nikaenda katika kambi yao lakini sikumwona mtu huko kwa hiyo nikaenda mahali nilipokuwa nimekaa (wakati tulipopumzika) nikidhania kwamba watanikosa na watarudi kunitafuta. Nilipokuwa nimekaa mahali pangu, nilisinzia nikalala. Swafwaan bin Al-Mu’attwil As-Sulamiyy Adh-Dhakwaaniy alikuwa nyuma ya jeshi. (alichelewa kuondoka) Akaanza (safari) nyakati ya mwisho ya usiku akafika kituoni pangu wakati wa asubuhi. Akaona umbo la mtu aliyelala. Akanijia na akanitambua baada ya kuniona kwani alikuwa akiniona kabla ya (Shariy’ah ya) ya hijaab. Nikainuka baada ya kauli yake aliyotamka aliponitambua: “Innaa liLLaahi wa innaa Ilayhi raaji’uwn.” Nikajifunika uso wangu kwa nguo yangu na Wa-Allaahi, hakuniambia hata neno moja isipokuwa istirjaa’ah (Innaa liLLaahi wa innaa Ilayhi raaji’uwn) mpaka alimpomwinamisha ngamia aliyekanyaga (chini) miguu yake ya mbele kisha nikampanda. Kisha Swafwaan akaendelea akimuongoza ngamia aliyekuwa amenibeba mimi hadi tukakutana na jeshi lilokuwa limepumzika wakati wa mchana wa joto. Akaangamia aliyekadiriwa kuangamia kiongozi wa ‘ifk’ ambaye ni ‘Abdullaahi bin Saluwl.  Baada ya hapo tukafika Madiynah nami nikawa naumwa mwezi mzima. (Kumbe) Huku watu wakitumbukia katika kusambaza kauli za wazushi wa kashfa nami sikuwa na habari nazo. Lakini kilichonitia shaka wakati naumwa ni kwamba sikuwa napokea tena kutoka kwa Rasuli wa Allaah huruma ile ile niliyokuwa nikiipata wakati nikiumwa (kabla ya uzushi huu wa ifk). Rasuli wa Allaah alikuwa akija kwangu na kuamkia kisha akiongeza kusema: ((Mnaonaje [vipi hali zenu]?)) kisha akiondoka. Hilo lilinitia shaka lakini sikujua kuhusu uovu uliokuwa ukienea mpaka nilipopata nafuu ya ugonjwa wangu.

 

Nikatoka nje pamoja na Ummu Mistwah kuelekea Al-Manaaswi’ mahali ambako tulikuwa tukienda kujisaidia haja. Na ilikuwa hatwendi huko kwa ajili hiyo ila usiku tu. Na hivyo ilikuwa ni kabla ya kuwa na vyoo karibu na nyumba zetu. Desturi hii ililingana na desturi ya Waarabu wa zamani (jangwani au katika mahema) kuhusu kujisaidia haja kubwa kwani tuliichukulia kuwa ni tatizo na madhara kuweko vyoo katika nyumba. Kwa hiyo nikaenda na Ummu Mistwah ambaye ni bint Ruhm bin ‘Abdil-Manaaf na mama yake ni bint wa Sakhr bin ‘Aamir ambaye ni shangazi yake Abuu Bakr As-Swiddiyq, na mwanawe ni Mistwah bin Uthaathah. Tulipomaliza haja zetu, wakati tunarudi nyumbani kwangu, Ummu Mistwah akajikwaa kwa nguo yake akasema: “Aangamizwe Mistwah!” Nikamwambia: “Maovu yaliyoje uliyoyasema! Unamtukana aliyeshiriki katika vita vya Badr?” Akasema: “Ee wee, hukusikia aliyoyasema?” Nikasema: “Amesema nini?” Hapo ndipo aliponitajia kauli za wazushi wa ifk ambazo zilizidisha maradhi yangu. Niliporudi nyumbani, Rasuli wa Allaah alinijia na baada ya kuniamkia akasema: ((Mnaonaje [vipi hali zenu?)) Nikasema: “Utaniruhusu niende kwa wazazi wangu?” Hapo nilitaka kuhakikisha kuhusu habari (hizo za ifk) kutoka kwao. Rasuli wa Allaah akaniruhusu nikaenda kwa wazazi wangu nikamuuliza mama yangu: “Ee mama! Watu wanaongelea kuhusu nini?” Mama yangu akasema: “Ee mwanangu! Chukulia mepesi, kwani hakuna mwanamke mcheshi anayependwa na mumewe ambaye ana wake wengineo pia ila hao wake watamtafutia kasoro!” Nikasema: “Subhaana Allaah! Hivyo kweli watu wamezungumza hayo?” Usiku ule nikawa nalia mno hadi asubui. Machozi yangu hayakusita, wala sikuweza kulala, na asubuhi kukapambazuka nikiwa bado nalia. Wahyi (kutoka kwa Allaah) ulichelewa na Rasuli wa Allaah alimwita ‘Aliy bin Abi Twaalib na Usaamah bin Zayd  (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa  ili kutaka ushauri kuhusu kumtaliki mkewe. Usaamah bin Zayd alimkumbusha Rasuli wa Allaah kuhusu kutokuwa na hatia mkewe na ambayo Nabiy mwenyewe anayayajua katika nafsi yake ya ahli yake kuhusu mapenzi. Akasema: “Ee Rasuli wa Allaah! Yeye ni mkeo, nasi hatujui lolote kuhusu yeye isipokuwa mazuri.”

 

Lakini ‘Aliy bin Abi Twaalib alisema: “Ee Rasuli wa Allaah! Allaah Hakudhikishi jambo, na kuna wanawake tele kama yeye. Lakni ukimuuliza mjakazi wake atakwambia ukweli.”

 ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) akaongezea kusema:

 

Basi Rasuli wa Allaah akamwita Bariyrah akamuuliza: ((Ee Bariyrah! Je, umeona lolote la kukutia shaka [kuhusu ‘Aaishah]?)) Bariyrah akasema: “Naapa kwa Allaah Aliyekutuma kwa haki! Sijapatapo kuona lolote la kumlaumu ‘Aaishah isipokuwa yeye ni msichana asiyepevuka bado ambaye akilala na kuacha unga uliokandwa kwa ajili ya familia yake, bila ya kuuhifadhi, ukaliwa na mbuzi.” 

 

Basi Rasuli wa Allaah akainuka (kuwaelekea) kuwauliza watu nani atakeyelipiza kisasi kwa ‘Abdullaahi bin ‘Ubay bin Saluwl. Rasuli wa Allaah alipokuwa juu ya mimbari akasema: ((Enyi hadhara ya Waislamu! Nani atakayenisaidia kunilipizia dhidi ya mtu aliyenifikishia maudhi ya [kukashifu) ahli yangu? Naapa kwa Allaah, sijui lolote ila mazuri kuhusu ahli yangu, na watu wamemtuhumu mtu (mwanamme) ambaye sijui lolote [baya] isipokuwa mazuri na hajapatapo kuzuru ahli yangu isipokuwa [kunizuru] mimi!))

 

Sa’d bin Mu’aadh al-Answaariy alisimama na kusema: “Ee Rasuli wa Allaah! Naapa nitakulipizia (nitakupumuzisha) naye! Ikiwa ni mtu kutoka kwa (Bani) Al-Aws, basi nitamkatilia mbali kichwa chake; na ikiwa ni kutokana na ndugu zetu Al-Khazraj, basi tupe amri yako nasi tutaitekeleza!”  

 

Hapo Sa’d bin ‘Ubaadah akasimama ambaye ni mkuu wa Khazraj. Na kabla ya tukio hili alikuwa ni mtu mwenye taqwa, lakini alipandwa hamasa (kwa ghera ya kabila lake).

 

Akamwambia Sa’ad (bin Mu’aadh), “Naapa Allaah Aliye hai! Umesema uongo! Hutamuua na wala hutaweza kumuua!”

 

Hapo ‘Usayd bin Hudhwayr, bin ammi wa Sa’d (bin Mu’aadh) alisimama akamwambia Sa’d bin ‘Ubaadah: “Wewe ndiye muongo! Naapa kwa Allaah Aliye hai! Hakika tutamuua, nawe ni mnafiki unayewatetea wanafiki!”

 

Basi makabila mawili ya Al-Aws na Al-Khazraj wakazozana mpaka wakahamasika kupigana huku Rasuli wa Allaah amesimama juu ya mimbari. Rasuli wa Allaah akaendelea kuwanyamazisha mpaka wakawa kimya, naye pia akawa kimya. Siku hiyo niliendelea kulia sana hadi kwamba machozi yangu hayakusita wala sikuweza kulala.

 

Asubuhi yake, wazazi wangu walikuwa pamoja nami na nikalia masiku mawili na mchana mmoja bila ya kulala, machozi ya mfululuzo hadi kulia huko kulikaribia kupasua maini yangu.

 

Walipokuwa nami na huku nikilia, akaja mwanamke wa Answaariy kutaka ruhusa kuniona. Nikamruhusu akaketi na akaanza kulia pamoja nami. Nilipokuwa katika hali ile, Rasuli wa Allaah akatujia na kutuamkia kisha akaketi chini. Hakupata kuketi pamoja nami tokea siku iliyosemwa yaliyosemwa. Alikaa mwezi bila ya kupokea Wahyi kuhusu kesi yangu. Rasuli wa Allaah akatamka shahaadah baada ya kuketi kisha akasema: ((Ee ‘Aaishah! Nimejulishwa kadha na kadhaa kuhusu wewe, na ikiwa wewe ni huna hatia, Allaah Atadhihirisha kutokuwa kwako na hatia. Na ikiwa umetenda dhambi, basi omba maghfirah ya Allaah na utubu Kwake, kwani mja anapokiri madhambi yake akatubia kwa Allaah, basi Allaah Hupokea toba yake)).

 

Rasuli wa Allaah alipomaliza, machozi yangu yalisita moja kwa moja hadi kwamba sikuhisi wala tone moja kutoka. Nikamwambia baba yangu: “Mjibu Rasuli wa Allaah anayoyasema kwa niaba yangu.” Akasema: “Naapa kwa Allaah, sijui la kusema kwa Rasuli wa Allaah!” Kisha nikamwambia mama yangu! “Mjibu Rasuli wa Allaah anayoyasema kwa niaba yangu.” Akasema: “Sijui la kusema kwa Rasuli wa Allaah!” Kwa vile nilikuwa bado mwenye umri mdogo na juu ya kuwa na elimu ndogo ya Qur-aan, nikasema:

 

“Naapa kwa Allaah! Najua mengi uliyoyasikia kuhusu kisa (cha ifk) hadi kwamba imestakiri katika akili zenu na mmeamini. Basi sasa nikikujulisheni kwamba mimi sina hatia, na Allaah Anajua kwamba mimi sina hatia, hamtoniamini. Na nikikiri jambo ambalo Allaah Anajua kwamba mimi sina hatia, mtaniamini. Naapa kwa Allaah! Siwezi kukupatieni mfano isipokuwa wa baba yake Yuwsuf: ((“Basi subira njema, na Allaah ni Mwenye kuombwa msaada juu ya mnayoyavumisha.”)) [Yuwsuf: 18]

 

 

Kisha nikageuka na kulala kitandani mwangu, na wakati huo nilijijua kuwa sina hatia na kwamba Allaah Atadhihirisha kutokuwa kwangu na hatia. Lakini naapa kwa Allaah! Sikufikiria kwamba Allaah Atateremsha Wahyi kwa ajili yangu utakaosomwa (milele), kwani nilijidhania sina thamani hivyo hata nitajwe na Allaah kwa Aayah za kusomwa. Lakini nilitarajia labda Rasuli wa Allaah ataoteshwa ndoto na Allaah kudhihirisha kutokuwa kwangu na hatia. Naapa kwa Allaah! Rasuli wa Allaah hakuwahi kuinuka alipoketi na hakuna aliyeondoka katika nyumba mara Wahyi (kutoka mbinguni) ukamfikia Rasuli wa Allaah. Ukamfikia katika hali ile ile ngumu ya kawaida inayomfikia (anapoletewa Wahyi kutoka mbinguni). Kwa hiyo majasho yakawa yanamwagika chini kama mfano wa lulu, juu ya kwamba ilikuwa siku ya msimu wa baridi, na hivyo ni kwa sababu ya uzito wa kauli (za Wahyi) zilofunuliwa kwake.

 

Baada ya hali hiyo nzito iliyompata Rasuli wa Allaah kumuondokea huku akitabasamu alipokuwa akifunuliwa Wahyi, neno la mwanzo alosema ni:

((‘Aaishah! Allaah Amedhihirisha usafi wako [kutokuwa kwako na hatia])).

 

Mama yangu akaniambia: “Inuka na mwendee.” Nikasema: “Naapa kwa Allaah! Sitomwendea na wala sitomshukuru yeyote isipokuwa Allaah!”

 

Hapo Allaah Akateremsha Wahyi:

 

إِنَّ الَّذِينَ جَاءُوا بِالْإِفْكِ عُصْبَةٌ مِّنكُمْ ۚ لَا تَحْسَبُوهُ شَرًّا لَّكُم ۖ بَلْ هُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۚ لِكُلِّ امْرِئٍ مِّنْهُم مَّا اكْتَسَبَ مِنَ الْإِثْمِ ۚ وَالَّذِي تَوَلَّىٰ كِبْرَهُ مِنْهُمْ لَهُ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿١١﴾

Hakika wale walioleta singizo la kashfa; (kumzulia ‘Aaishah  رضي الله عنها) ni kundi miongoni mwenu. Msiichukulie kuwa ni shari kwenu, bali ni kheri kwenu.  Kila mtu katika wao atapata yale aliyochuma katika dhambi. Na yule aliyejitwika sehemu yake kubwa miongoni mwao atapata adhabu kuu.

 

لَّوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ ظَنَّ الْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بِأَنفُسِهِمْ خَيْرًا وَقَالُوا هَـٰذَا إِفْكٌ مُّبِينٌ ﴿١٢﴾

Kwa nini mlipoisikia (kashfa ya kusingiziwa), Waumini wanaume na Waumini wanawake wasiwadhanie wenzao kheri, na wakasema: “Hii ni kashfa ya kusingizwa iliyo dhahiri?”

 

لَّوْلَا جَاءُوا عَلَيْهِ بِأَرْبَعَةِ شُهَدَاءَ ۚ فَإِذْ لَمْ يَأْتُوا بِالشُّهَدَاءِ فَأُولَـٰئِكَ عِندَ اللَّـهِ هُمُ الْكَاذِبُونَ ﴿١٣﴾

Kwa nini hawakuleta mashahidi wanne? Na kwa vile hawakuleta mashahidi, basi hao mbele ya Allaah ndio waongo.

 

وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ لَمَسَّكُمْ فِي مَا أَفَضْتُمْ فِيهِ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿١٤﴾

Na lau si fadhila ya Allaah juu yenu na rahmah Yake duniani na Aakhirah, bila shaka ingekuguseni adhabu kuu kwa yale mliyojishughulisha nayo kuyaropoka,

 

إِذْ تَلَقَّوْنَهُ بِأَلْسِنَتِكُمْ وَتَقُولُونَ بِأَفْوَاهِكُم مَّا لَيْسَ لَكُم بِهِ عِلْمٌ وَتَحْسَبُونَهُ هَيِّنًا وَهُوَ عِندَ اللَّـهِ عَظِيمٌ ﴿١٥﴾

Mlipoipokea (kashfa ya uzushi) kwa ndimi zenu, na mkasema kwa midomo yenu, yale ambayo hamkuwa na elimu nayo; na mnalidhania ni jambo jepesi; na hali hili mbele ya Allaah ni kubwa mno.

 

وَلَوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ قُلْتُم مَّا يَكُونُ لَنَا أَن نَّتَكَلَّمَ بِهَـٰذَا سُبْحَانَكَ هَـٰذَا بُهْتَانٌ عَظِيمٌ ﴿١٦﴾

Na kwa nini mlipoisikia (kashfa ya kusingiziwa) msiseme: “Haitupasi sisi tuzungumze haya; Subhaanak! Utakasifu ni Wako huu ni usingiziaji wa dhulma mkubwa mno!”

 

يَعِظُكُمُ اللَّـهُ أَن تَعُودُوا لِمِثْلِهِ أَبَدًا إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٧﴾

Allaah Anakuwaidhini msirudie abadani mfano wa haya, mkiwa ni Waumini wa kweli.

 

وَيُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمُ الْآيَاتِ ۚ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿١٨﴾

 

Na Allaah Anakubainishieni Aayaat. Na Allaah Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote.

 

إِنَّ الَّذِينَ يُحِبُّونَ أَن تَشِيعَ الْفَاحِشَةُ فِي الَّذِينَ آمَنُوا لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۚ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿١٩﴾

Hakika wale wanaopenda uenee uchafu wa kashfa kwa wale walioamini; watapata adhabu iumizayo duniani na Aakhirah. Na Allaah Anajua nanyi hamjui.

 

وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ وَأَنَّ اللَّـهَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿٢٠﴾

Na lau si fadhila ya Allaah juu yenu na rahmah Yake, na kwamba Allaah ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu. [An-Nuwr: 11-20]

 

Aayah kumi zote. Alipoteremsha hizo Aayah Allaah, kuthibitisha usafi wangu, Abuu Bakr As-Swiddiyq ambaye alikuwa akimpa swadaqah Mistwah bin Uthaathah kwa vile ni jamaa yake wa uhusiano wa damu na kwa vile alikuwa ni maskini alisema: “Naapa kwa Allaah! Sitompa tena Mistwah chochote baada ya aliyoyasema kuhusu ‘Aaishah” Hapo Allaah Akateremsha Wahyi:

 

وَلَا يَأْتَلِ أُولُو الْفَضْلِ مِنكُمْ وَالسَّعَةِ أَن يُؤْتُوا أُولِي الْقُرْبَىٰ وَالْمَسَاكِينَ وَالْمُهَاجِرِينَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ۖ وَلْيَعْفُوا وَلْيَصْفَحُوا ۗ أَلَا تُحِبُّونَ أَن يَغْفِرَ اللَّـهُ لَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٢٢﴾

Na wala wasiape wale wenye fadhila miongoni mwenu na wenye wasaa wa mali kuwa hawatowapa (swadaqah) jamaa wa karibu, na masikini, na Muhaajiriyn katika njia ya Allaah. Na wasamehe na waachilie mbali. Je, hampendi Allaah Akughufurieni? Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.  [An-Nuwr: 22]

 

 

Abuu Bakr akasema: “Naapa kwa Allaah! Nataka Allaah Anighufurie.” Basi akarudia kumpa Mistwah swadaqah aliyokuwa akimpa kisha akasema: “Naapa kwa Allaah! Sitoacha kabisa kumpa!”

 

‘Aaishah akaendelea kusema: Rasuli wa Allaah alimuuliza Zaynab bin Jahsh pia kuhusu kesi yangu: ((Ee Zaynab! Unajua nini au umeonaje?))

 

Akajibu: “Ee Rasuli wa Allaah! Mimi nahifadhi masikio yangu na macho yangu (kujiepusha kusema uongo). Sijui lolote (baya kuhusu ‘Aaishah) isipokuwa mazuri.” Naye (Zaynab) ndiye miongoni mwa wake za Rasuli wa Allaah, aliyekuwa anayetamani kupokea kutoka kwake fadhila kama nilizokuwa nikizipokea (aliyekuwa na wivu nami).

 

 

Lakini Allaah Alimhifadhi (na uongo) kwa sababu ya huruma yake.

 

Lakini dada yake Hamnah (aliyekuwa akishiriki kwenye hizo tuhuma), aliendelea kugombana naye akaangamizwa kama kama wale waliotunga na kueneza kashfa.”  [Al-Bukhaariy]

Share

23-Swabrun-Jamiyl: Subira Za Swahaabiyaat - Faatwimah Bint Muhammad (Radhwiya Allaahu ‘Anhaa)

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)

 

23  - Subira Za Swahaabiyaat - Faatwimah Bint Muhammad  (Radhwiya Allaahu ‘Anhaa)

 

 

 

Alikuwa ni kipenzi mno wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  hadi kwamba alipokuwa anataka kusafiri huhakikisha kwamba Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) ni wa mwisho kumuaga. Na anaporudi kutoka safarini huenda kwanza Msikitini kuswali rakaa mbili kisha huelekea nyumbani kwa Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kisha ndio huenda kwa wake zake (Radhwiya Allaahu ‘anhunna) Hata aliwahi kusema: ((Faatwimah ni sehemu inayotokana na mimi, atayemghadhibisha amenighadhibisha)).

 

Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alivumilia mno mitihani kadhaa kama  mateso ya baba yake mpenzi na vifo katika familia yake. Mtihani mmojawapo mkubwa aliovumilia ni siku ile ‘Uqbah bin Abi Mu’iytw alipotupa taka juu ya kichwa cha baba yake aliyekuwa amesujudu mbele ya Al-Ka’bah. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliendelea kusujudu na hakuinua kichwa chake mpaka alipokuja Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa)  na kuondoa taka zile.

 

Mtihani mwengine ulikuwa katika siku za mwanzo za kulingania watu katika Uislamu, wakati Waislamu walipogomewa na makafiri Quraysh wa Makkah na kuzungukwa wakiwa katika bonde la Baniy Haashim muda wa miaka mitatu bila kupelekewa chakula. Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alikuwa akiwaona Waislamu wakiwa katika shida na njaa hata ikawabidi kula majani na ngozi. Wakati mwengine kilikuwa kikiwafikia chakula kwa njia ya kufichwa tena kwa siri.  Hali hiyo iliathiri sana siha yake kwani alikuwa na umbo dhaifu tokea utotoni mwake. Lakini pia ilimuongezea iymaan, ushujaa pamoja na ukuaji wa akili na fikra.

 

Alifikwa na misiba mingi ukianza na kifo cha mama yake Khadiyjah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa).  Kifo chake kilitokea katika mwaka uliojulikana ni ‘Aam Al-Huzn (mwaka wa huzuni) kwa kifo hicho cha mama yake. Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) aliweza kuyastahamilia yote hayo, akasubiri na kusimama imara pamoja na baba yake huku akimshughulikia na kumsaidia katika kuliziba pengo la mama yake Khadiyjah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) na kwa ajili hiyo alikuwa akijulikana kwa 'mama wa baba yake.'

 

Misiba mingineyo ni kifo cha dada yake Ruqayyah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa). Kisha katika mwaka wa nane Hijriyyah alifariki dada yake Zaynab (Radhwiya Allaahu ‘anhaa). Na mwaka wa tisa alifariki dada yake mwengine, Ummu Kulthuwm (Radhwiya Allaahu ‘anhaa).

 

Mwisho kabisa ni msiba mkubwa zaidi wa kifo cha baba yake  Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye alifariki siku ya Jumatatu mwezi wa Rabiy’ul Awwal mwaka wa kumi na moja Hijriy. Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alikuwa akimuona baba yake akihangaika alipokuwa akivuta pumzi zake za mwisho, akawa anamwambia: "Masikini baba yangu unataabika."  Na baba yake akawa anamwambia: ((Baba yako hatopata tabu tena baada ya leo ee Faatwimah)).  Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) akawa analia kila anapomuona baba yake akihangaika huku akivuta pumzi zake za mwisho, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa kila anapopata fahamu akimwambia: ((Usilie ee binti yangu, bali nitakapokufa useme: “Innaa liLLaahi wa innaa Ilayhi raaji’uwn)).  Ilipotoka roho yake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaaga dunia, Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alisema: “Ee baba yangu! Umemuitikia Rabb wako, ee baba yangu! Jannah ya Firdaws makazi yako.”

 

Alivumilia pia kuishi maisha ya shida pamoja na mumewe ‘Aliy  (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye alikuwa anapomaliza shughuli zake nje, hurudi nyumbani kumsaidia mkewe kazi za nyumba. Amesema ‘Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhu): “Nilipomuoa Faatwimah hatukuwa tukimiliki zaidi ya ngozi ya kondoo tuliyokuwa tukiitandika wakati wa usiku na kulala juu yake, na wakati wa mchana tulikuwa tukiikalia, na hatukuwa na mfanya kazi wa kutusaidia shughuli za nyumba, na (Faatwimah) alipoletwa nyumbani, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimpa mtungi wa maji na gilasi mbili pamoja na kitambaa na mito miwili iliyojazwa ndani yake majani ya mtende." Aliwahi kutaka msaada kwa baba yake ampatie mtumishi kumsadia kazi za nyumba lakini Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimpa lililo bora zaidi nalo ni kumfunza badala yake aina ya kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).    Alimfunza kwamba pale anapokuwa anataka kulala amsabbih Allaah (Subhaana Allaah) mara thelathini na tatu, amhimidi (AlhamduliLLaah) mara thelathini na tatu, na amtukuze (Allaahu Akbar) mara thelathini na nne. Faatwihmah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alipokea nasaha hiyo akapata usahali katika kazi zake za nyumba pamoja na baraka nyinginezo katika maisha yao.  Na hiyo ni fadhila kuu mojawapo kwake kwamba anachuma thawabu za Waumini wanaoitumia aina hiyo ya tasbiyh mpaka siku ya Qiyaamah.

 

 

 

Share

24-Swabrun Jamiyl: Subira Za Swahaabiyaat -Tamaadhwur Bint As-Sulaymiyyah (Radhwiya Allaahu ‘Anhaa)

 

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)

 

24 - Subira Za Swahaabiyaat  - 

Tamaadhwur Bint As-Sulaymiyyah  (Radhwiya Allaahu ‘Anhaa)

 

 

 

Jina lake hasa ni Tamaadhwur bint 'Amr bin Ash-Shariyd bin Rabaah As-Sulaymiyyah. Alijulikana kwa jina la Al-Khansaa na vile vile Umm Ash-Shuhadaa (mama wa mashahidi) kutokana na watoto wake waliofariki katika jihaad ya kupigana vita. Pia alijulikana kuwa ni mwanamke mwenye haiba nzuri iliyojaa fadhila, tabia njema, ushujaa na subira kubwa.

 

Kabla ya kuingia katika Uislam, alikuwa akitunga mashairi ya beti mbili tatu hadi walipofariki kaka zake Mu'aawiyah na Swakhar bin 'Amr, alifikwa na huzuni kubwa sana hata akawatungia mashairi. Yakawa mashuhuri mno, hata yakazidi kumpatia umaarufu. Na imesemekana kwamba hakuweko mwanamke aliyekuwa hodari wa mashairi kama yeye.

 

Baada ya vifo vya kaka zake, alikuja kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na watu wake wa Banu Sulaym akasilimu. Ilipofika wakati wa vita vya Qaadisiyyah alidhihirisha subira yake kubwa alipokwenda vitani pamoja na watoto wake wanne wa kiume na akawausia kwa kuwaambia maneno haya mazito:

 

"Enyi watoto wangu, naapa kwa Yule Ambaye laa ilaaha illa Huwa (hakuna muabudiwa wa haki ila Yeye), nyinyi ni watoto wa baba mmoja, sikumkhini baba yenu, mmesilimu kwa kutii, mmehama kwa khiari yenu…" Akaendelea kuwanasihi hadi akasema "Mtakapoamka kesho In Shaa Allaah kwa salama, nendeni vitani kupigana na adui zenu, kwani mnajua Aliyowaandalia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  ya thawabu nyingi kwa kupigana na makafiri. Tambueni kuwa nyumba ya milele (Jannah) ni bora kuliko nyumba ya kutoweka (Dunia), Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

   

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اصْبِرُوا وَصَابِرُوا وَرَابِطُوا وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٢٠٠﴾

Enyi walioamini! Subirini na zidini kuvuta subira na bakieni imara na mcheni Allaah ili mpate kufaulu. [Aal-‘Imraan: 200]

 

Wakaenda vitani na alipopata habari ya vifo vyao wote alisema: "AlhamduliLLaah kwa Yule Aliyenipa heshima ya kuuliwa kwao na namuomba Allaah kwa rahma Zake, Aniunganishe nao."

 

Al-Khansaa (Radhwiya Allaahu ‘anhaa)  akaendelea kubakia katika subira na kuthibitisha iymaan yake hadi alipoaga dunia  wakati wa ukhalifa wa 'Uthmaan bin 'Affaan (Radhwiya Allaahu 'anhu).

 

Al-Khansaa (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) ametuonyesha mfano bora kabisa wa Swabrun Jamiyl kwa kuridhika na majaaliwa ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na inapasa mzazi anayefiwa na mwanawe afuate nyayo zake.

 

Share

25-Swabrun Jamiyl: Subira Za Taabi'iyn - Sa'iyd Bin Musayyib (Rahimahu Allaah)

 

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)  

 

25 - Subira Za Taabi'iyn - Sa'iyd Bin Musayyib (Rahimahu Allaah)

 

 

 

Sa’iyd bin Al-Musayyib (Rahimahu Allaah) aliishi maisha ya hali nzuri na alikuwa mwenye hadhi. Hakuwahi kuinamisha kichwa chake kwa mtu yeyote yule, hata kama atapigwa kwa mijeledi au kutishiwa kuuwawa.

 

Hali hiyo ndio iliyomfikia  kutoka kwa Amiyr wa Madiynah katika Ukhalifa wa ‘Abdul-Malik bin Marwaan akimuamuru amfanyie bay’ah (kiapo cha utii) Waliyd bin ‘Abdil-Malik. Alipokataa Sa’iyd kutii kiapo hicho, alitishwa kuuawa. Lakini hakurudisha rai yake pamoja na elimu yake na yale yanayomsubiri na adhabu. Sa’iyd alipoonesha kukataa kwake, walimvua nguo zake na wakampiga mboko hamsini, na wakamzungusha katika soko za Madiynah wakiwa wanasema: “Hii ndio hali ya mwana hezaya!” Sa’iyd akiwajibu huku akijiamini kwa kusema: “Bali ni nani mwana hezaya basi turudishe kwa lile tunalotaka.”

 

‘Abdul-Malik alipojua kilichofanywa na Walii wake wa Madiynah, alimlaumu na akamwandikia:  “Wa-Allaahi, ilikuwa mpate huruma kutoka kwake Sa’iyd, na sio kumpiga, nami najua tofauti iliyopo na kupinga kwake.”

 

Share

26-Swabrun Jamiyl: Subira Za Taabi'iyn - Sa'iyd Bin Jubayr (Rahimahu Allaah)

 

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)  

 

25 - Subira Za Taabi'iyn - Sa'iyd Bin Jubayr (Rahimahu Allaah)

 

 

 

Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) alijitolea maisha yake kwa ajili ya Uislam, na hakumuogopa yeyote ila Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) alizaliwa katika mji wa Kuwfaa. Watu wengi walifaidika na elimu yake iliyojaa faida. Alikuwa  akiwafundisha watu kuhusiana na Dini na dunia yao.

 

Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) alikuwa ni Imaam mkubwa katika maimaam wa Fiqh katika zama za dola ya Umawiyyah kiasi cha kupata ushuhuda wa elimu aliyokuwa nayo kwa ‘Abdullaah bin ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwa uhodari wake wa Fiqh na elimu mbalimbali.

 

Ilikuwa kawaida ya watu wa Makkah wanaokwenda kutembelea wakiwaambia watu wa Kuwfaa: “Si mnae Ibn Ummi Ad-Dahmau.” [wakimkusudia Sa’iyd bin Jubayr.

 

Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) alikuwa ni mtu mwenye umbuji na fasaha, msema kweli, na moyo uliohifadhi, haogopi watawala dhalimu, hanyamazii haki, kwani mwenye kunyamazia haki ni shaytwaan kiziwi.

 

Hajjaaj bin Yuwsuf alimkamata baada ya kumtengenezea tuhuma ya uongo na aliazimia kummaliza. Hata hivyo Hajjaaj hakuweza kufunga mdomo wa Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) katika kuzungumza ukweli kwa kumtisha.

 

Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) alikuwa Muumin mwenye iymaan ya ukweli akifahamu kuwa mauti, uhai na riziki viko katika Mikono ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   na hakuna mwengine mwenye uwezo wa hivyo.

 

Hajjaaj alibadilisha mbinu na akatumia njia ya kumweka mbali na haki Sa’iyd bin Jubayr kwa kumshawishi Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) kwa mali na maslahi ya kidunia kwa kumpa mali nyingi, hata hivyo Imaam huyu badala ya kuchukua mali ile alimpa Hajjaaj darsa ambalo hakuweza kulisahau.

 

Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) alimwambia Hajjaaj: “Ee Hajjaaj! Ikiwa umekusanya mali hii ili ikukinge na fazaa ya Siku ya Qiyaamah, basi ni vizuri, hata hivyo ukae ukifahamu kuwa fazaa moja ya Siku ya Qiyaamah humhizi kila mwenye kunyonyesha kwa kila anachonyonyesha!”

 

Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) alimfahamisha Hajjaaj kuwa mali ni katika njia kubwa ya kutengeneza amali za watu na mambo ya Aakhirah ya mtu, ikiwa mwenye mali hiyo amezikusanya kwa njia ya halali ili imwepushe na fazaa za Siku ya Qiyaamah. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):  

 

يَوْمَ لَا يَنفَعُ مَالٌ وَلَا بَنُونَ ﴿٨٨﴾

 “Siku hayatofaa mali wa watoto.

 

إِلَّا مَنْ أَتَى اللَّـهَ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ ﴿٨٩﴾

 “Isipokuwa yule atakayemfikia Allaah na moyo uliosalimika.  [Ash-Shu’araa: 88-89]

 

Kwa mara nyingine jitihada za Hajjaaj kumshawishi Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) zilishindwa kwani hakuwa ni katika wenye kuabudu dunia na hakuwa katika wale wanaouza Dini yao kwa ajili ya dunia yao. Hajjaaj aliendelea kumtisha Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) kuwa atamkamata na kummaliza na mazungumzo yafuatayo yakawa baina yao:

 

Hajjaaj: “Ole wako ee Sa’iyd!”

 

Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah):  “Ole ni kwa wale waliotoka Jannah na kuingizwa motoni.”

 

Hajjaaj: “Unapendelea nikuue namna gani?”

 

Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah):  “Chagua mwenyewe ee Hajjaaj! Wa-Allaahi huwezi kuniua namna yeyote ile ila kifo kitakuangamiza katika Aakhirah!”

 

Hajjaaj: “Je, unapenda nikusamehe?”

 

Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah):  “Ikiwa ni msamaha basi ni kutoka kwa Allaah, na wewe huna msamaha wala udhuru.”

 

Hajjaaj: “Nendeni mkamuue!”

 

Walipoondoka kwenda kumuua, mwanae Sa’iyd bin Jubayr alilia alipomuona katika hali hiyo, akamwangalia kisha akamwambia: “Nini kinachokuliza? Unalia nini wakati baba yako umri wake ni miaka hamsini na saba!” (kwa maneno hayo) rafiki yake nae akalia.

 

Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) akamwambia: “Kinakuliza nini?”

 

Yule mtu: “Kilichokusibu.”

 

Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah):  “Usilie, katika elimu ya Allaah mambo yalikuwa yawe hivi, kisha akasoma:

 

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ﴿٢٢﴾

Hausibu msiba wowote katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa umo katika Kitabu kabla hatujautokezesha. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi. [Al-Hadiyd: 22]

 

Kisha Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) akacheka na watu wake wakashangazwa na wakamwambia Hajjaaj naye akaamrisha arejeshwe.

 

Hajjaaj akamuliza: “Nini kikuchekeshacho?”

 

Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah)  akajibu; “Nashangazwa na jeuri yako kwa Allaah na huruma Yake kwako.”

 

Hajjaaj akasema: “Muuweni!”

 

Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) akasoma:

 

 

إِنِّي وَجَّهْتُ وَجْهِيَ لِلَّذِي فَطَرَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ حَنِيفًا ۖ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿٧٩﴾

 “Hakika mimi nimeelekeza uso wangu kwa Ambaye Ameanzisha mbingu na ardhi nimeelemea haki, nami si katika washirikina.” [Al-An’aam: 79]

 

 

Hajjaaj: “Mwelekezeni pasipo Qiblah!”

 

Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) akasoma:

 

وَلِلَّـهِ الْمَشْرِقُ وَالْمَغْرِبُ ۚ فَأَيْنَمَا تُوَلُّوا فَثَمَّ وَجْهُ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ وَاسِعٌ عَلِيمٌ ﴿١١٥﴾

Na Mashariki na Magharibi ni ya Allaah; basi popote mnapogeuka kuna Wajihi wa Allaah. Hakika Allaah ni Mwenye wasaa, Mjuzi wa yote [Al-Baqarah: 115]

 

Hajjaaj: “Mpigeni na mlazeni uso chini.”

           

Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) akasoma:

 

مِنْهَا خَلَقْنَاكُمْ وَفِيهَا نُعِيدُكُمْ وَمِنْهَا نُخْرِجُكُمْ تَارَةً أُخْرَىٰ ﴿٥٥﴾

Kutokana nayo (ardhi) Tumekuumbeni, na humo Tutakurudisheni, na kutoka humo Tutakutoeni mara nyingine. [Twaahaa: 55]

 

Hajjaaj: “Mchinjeni!”

 

Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah):  “Ama mini nashuhudia kuwa laa ilaaha illa Allaah (hapana muabudiwa wa haki ila Allaah) Asiye na mshirika, na Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  ni mja Wake na Rasuli Wake.  Ichukue roho yangu ee Hajjaaj, utanikuta nayo Siku ya Qiyaamah.”

 

Kisha Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) akamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   akisema: “Ee Rabbi, Usimsalitishe mtu mwengine ili amuue baada yangu.”

 

Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) Alikufa mwaka 95H. Wamekhitalifiana wanahistoria umri wake wa kufariki; wako wanaosema alifariki akiwa na umri wa miaka 49 na wengine wamesema alikufa akiwa na umri wa miaka 57. Alifariki hali ulimi wake ukimdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).      

 

 

 

 

 

Share

27-Swabrun Jamiyl: Subira Za Maimaam - Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah)

 

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)  

 

27 - Subira Za Maimaam - Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah)

 

    

 

Subira ya Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) ilikuwa zaidi katika kukanusha kwake kuwa Qur-aan imeumbwa.

 

Imepokewa kuwa Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) alimuona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwenye ndoto akimwambia: “Ee Ahmad! Kwa hakika utatahiniwa hivyo subiri Allaah Atanyanyua elimu yako mpaka Siku ya Qiyaamah.”

 

Mtihani ulianza baada ya Maamuwn kushika madaraka ya ukhalifa. Maamuwn alielemea katika rai ya Mu’tazilah na akiwakurubisha katika utawala wake.

 

Mwalimu wa Maamuwn alikuwa ni Abu al-Hudhayl al-‘Allaaf na Qaadhi alikuwa ni Ahmad bin Abi Daawuwd ambao walikuwa viongozi wa Mu’tazilah.

 

Maamuwn alifuata msimamo wa kuwa Qur-aan imeumbwa lakini alijizuia kuwalazimisha watu na Wanachuoni kukamatana na itikadi hiyo potofu kwa kuchelea fitnah. Hata hivyo alishauriwa na Qaadhi wake, Ibn Abi Daawuwd na baraza lake la watu na hata kukinaishwa.

 

Maamuwn akamwandikia gavana wake wa Iraaq, Is-haaq bin Ibraahiym na kumuamuru awakusanye wale wote waliokuwa chini yake miongoni mwa ma-Qaadhi na Wanachuoni na awalazimishe kuwa Qur-aan imeumbwa na atakayekataa afungwe, azuiwe au auliwe.

 

Fitnah hii ikapamba moto huko Iraq. Watu wengi wakafungwa, kuadhibiwa na kuuwawa kwa tendo hilo la Khalifa Maamuwn. Na kuwakaribisha marafiki waovu kiasi cha kumfanya Shaykhul Islaam Ibn Taymiyyah kusema; “Sidhani kama Allaah Atamwacha Maamuwn kwa mtihani aliowaingizia Waislam.”

 

Mtihani wa fitnah hiyo ukawa mkubwa kabisa, Wanachuoni wane walibaki katika msimamo nao ni; Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) na Muhammad bin Nuwh na wengine wawili ambao nao mwishoni walishindwa kuendelea na msimamo wao na kusema kama walivyosema watu.

 

Maamuwn aliamrisha akamatwe Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) na Muhammad bin Nuwh na wapelekwe katika hali ya kufungwa juu ya ngamia mmoja.

 

Muhammad bin Nuwh alifariki njiani kabla ya kufika Twarsuws kwa Maamuwn. Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) alibakia peke yake. Mjumbe kutoka kwa Maamuwn alimjia na kumwambia: “Khalifa amekutayarishia upanga ambao hajawahi kumuulia mtu yeyote!”

 

Imaam Ahmad akasema: “Namuomba Allaah Anitosheleze na msaada Wake.”  Akamuomba Allaahs  akiwa njiani asiuone uso wa Maamuwn na asimkutanishe naye.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alipokea du’aa ile na muda si mrefu ikamfikia habari kuwa Maamuwn kafariki kabla ya Imaam Ahmad kukutana naye. Baada ya habari hiyo Imaam Ahmad alirejeshwa jela kwa mara nyingine.

 

Baada ya hapo ukhalifa ulishikwa na al-Mu’taswim, ambae aliusiwa kumkurubisha Ibn Abi Daawuwd katika majlis yake na kuendelea kushikamana na itikadi ya Uumbwaji wa Qur-aan. Hiyo ndio iliyokuwa itikadi ya watu baada ya hapo, wakati huo Imaam Ahmad akiwa jela.

 

Imaam Ahmad alikuwa jela na al-Mu’taswim alimtoa jela na kumleta katika majlis pamoja na kumuwekea kikao pamoja na Ibn Abi Daawuwd na Wanachuoni (waovu) kuhusu mjadala wa uumbwaji wa Qur-aan, na Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah)  akiwapa dalili zenye kutosheleza kutoka katika Qur-aan yenyewe na Sunnah, na mara kwa mara akiwaambia: “Nipeni dalili kutoka kitabu cha Allaah na Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Siku hiyo majlis ilipita bila muwafaka wowote ule.

 

Mjadala ule uliendelea kwa muda wa siku tatu, Imaam Ahmad akithibiti pale pale penye haki bila kutetereka na kila akiulizwa: “Unasema nini kuhusu Qur-aan?” Hujibu: “Ni maneno ya Allaah yasiyoumbwa. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Anasema:

وَإِنْ أَحَدٌ مِّنَ الْمُشْرِكِينَ اسْتَجَارَكَ فَأَجِرْهُ حَتَّىٰ يَسْمَعَ كَلَامَ اللَّـهِ﴿٦﴾

Na ikiwa mmoja wa washirikina akikuomba umlinde, basi mlinde mpaka asikie Maneno ya Allaah (Qur-aan), [At-Tawbah: 6]

 

Na pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Anasema:

 

الرَّحْمَـٰنُ ﴿١﴾

Ar-Rahmaan.

عَلَّمَ الْقُرْآنَ ﴿٢﴾

Amefundisha Qur-aan. [Ar-Rahmaan: 1-2]

 

 

Na wala Hakusema ‘Khalaqal Qur-aan (Ameumba Qur-aan)’, na pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

 يس ﴿١﴾

Yaa Siyn.

وَالْقُرْآنِ الْحَكِيمِ ﴿٢﴾

Naapa kwa Qur-aan yenye hikmah.   [Yaasiyn: 1-2]

 

Hakusema “Wal-Qur-aanil Makhluwq”.  (Na Qur-aan iliyoumbwa)

 

Baada ya hapo al-Mu’taswim akakusanya Fuqahaa na ma-Qaadhi wote katika nchi wajadiliane na Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) kwa muda wa siku tatu naye mwenyewe akiwepo.

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) alijadiliana nao na kurudisha tuhuma zao dhidi ya Qur-aan kwa hoja thabiti zenye kukata na baada ya hapo al-Mu’taswim akasema: “Ahmad ametushinda!”

 

Wale washawishi na viongozi waovu wakakoleza fitnah ile kwa kumdhihaki Khalifa al-Mu’taswim nao kwa kusema: “Ahmad amewashinda Makhalifa wawili!” Maneno yale yakamkera sana al-Mu’taswim na akashikwa na hasira.

 

Na kwa kulinda hadhi yake akamtishia Imaam Ahmad kumuua. Naye Imaam Ahmad akajibu: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema: ((Si halali damu ya Muislamu aliyeshuhudia Laa ilaaha illa-Allaah, nami ni Rasuli wa Allaah, ila kwa mambo matatu…)). Sasa kwa nini damu yangu iwe ni halaal nami sijaleta katika hayo? Ee Amiyrul Muuminiyn, kumbuka kisimamo chako kwa Allaah  ni kama kisimamo changu sasa hivi kwako.”

 

Baada ya maneno hayo al-Mu’taswim akanyamaza na kulainika. Ibn Abi Daawuwd akaingiza maneno yake na kusema: “Ukimuacha utakuwa umeacha madhehebu ya Maamuwn, au itaendela kusemwa kuwa amewashinda makhalifa wawili.” Hapo tena akaja juu al-Mu’taswim na akaamrisha kurejeshwa jela Imaam Ahmad kwa mara nyingine tena.

 

Siku zikapita na ilipofika Ramadhwaan wakamtoa Imaam Ahmad jela na wakaanza kumpiga hali yakuwa yupo katika Swawm.  Al-Mu’taswim akawaleta wapiga mijeledi na kumpiga na kila mwenye kumpiga Imaam Ahmad mijeledi miwili hurudi nyuma na kwenda mbele mtu mwingine mpya wa kumpiga mijeledi. Na al-Mu’taswim akiwashadidisha kuendelea kupiga huku akisema kwa nguvu: “Allaah Aikate mikono yenu!” Kisha wakamtoa nguo zake na kubakisha kikoi chake tu na kuendelea kumpiga hadi akazimia. Alipozindukana, wakamchukua na kumpeleka nyumbani kwake akiwa hawezi kutembea kwa yaliyomkuta. Jeraha zake zilipopona akaenda Msikitini akitoa darasa zake na kufundisha Hadiyth za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na baada ya muda fitnah ile ikakoma.

 

Baada ya muda al-Mu’taswim akafariki na baada ya hapo akatawala Khalifa al-Waathiq Billaah. Ibn Abi Daawuwd na kundi lake la Wanachuoni waovu wakawasiliana na al-Waathiq ili wamburuze katika fitnah, na kweli fitnah ikarudi kwa mara nyingine isipokuwa al-Waathiq hakushughulika na Imaam Ahmad. Baada ya muda si mrefu Imaam Ahmad akapotea katika ukhalifa wa al-Waathiq kwa muda wa miaka mitano. Mwishoni mwa maisha ya al-Waathiq, alirudi kwa Rabb wake na akaongozwa katika hidaaya. Akaikanusha kauli ya kuwa Qur-aan imeumbwa. Kisha haukupita muda akafariki.

 

Baada ya hapo wakatawala makhalifa wema nao ni Mutawakkil ambaye alitangaza Sunnah na akawaandikia Wanachuoni sehemu mbalimbali kuwa wawakataze watu kujiingiza katika fitnah ile. Kisha tena baada ya muda akatoa tangazo lingine muhimu kwa dola nzima kuachana na bid’ah ile ya itikadi potofu ya kuwa Qur-aan ni kiumbe (imeumbwa). Furaha ikatawala kila sehemu katika dola baada ya tangazo lile, na fitnah na mtihani ule ukaondoka na haki kushinda batili. Ikawa ni hadithi pindi Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) alipokuwa akiulizwa wakati ule wa mtihani: “Ee Aba Abdillaah! Batili imeshinda haki.” Yeye alikuwa akijibu: “Wa-Allaahi batili haiwezi kushinda haki.”

 

Kwa hakika katika masomo muhimu ya mtihani huu, ni kule kuthibiti kwa Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) juu ya haki na kusubiri katika balaa lililomkumba. Kwa hakika Imaam Ahmad alishinda kwa iymaan na ushujaa aliokuwa nao na zikaanguka mbele yake serikali kubwa ulimwenguni katika wakati wake. Na Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) akatoka katika mtihani huu kama vile upanga unapotoka katika ala yake au kama mbalamwezi kwenye usiku wa kiza, na akaweza kuzuia tatizo kubwa ambalo lingeukumba Ummah wa Kiislamu. Na hivyo kubaki ‘Aqiydah ya Ahlu Sunnah Wal-Jamaa’ah ikiwa ni safi isiyochafuliwa na takataka za Muu’tazilah na upotofu wao na wale wote waliowafuata.

 

Siku zikapita na Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) akafariki   kama walivyofariki kabla yake Maamuwn, al-Muutaswim na al-Waathiq na wale majambazi waliojivika jina la uanachuoni nao wakafa mifano ya Ahmad bin Abi Daawuwd na wengineo.

 

Swali linalijitokeza hapa ni kuwa:  Historia imetuhifadhia nini juu ya maisha ya Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) na maisha ya majambazi wale?’ Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) alikuwa ni Mwanachuoni katika Wanachuoni wakubwa wa Kiislamu, katika zama zake, baada ya kifo chake hadi wakati huu tuliokuwa nao.

 

Mwisho wake, jeneza lake lilikuwa ni dalili na alama za Uislamu na elimu yake, vitabu vyake vikabakia hadi kwenye zama zetu leo hii kama kwamba bado anaishi nasi. Kinyume chake historia imetunukulia mwisho mbaya wa wale walioshiriki katika fitnah ile, na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   Atawalipa hapa duniani kabla ya Aakhirah.

 

Ama Qaadhi wa Mu’tazilah Ahmad bin Abi Daawuwd ambaye akitoa fatwa ya ruhusa ya kupigwa kwa ‘Ulamaa na kuwekwa kwao jela na kuwaua, aliulizwa baada ya al-Waathiq kumuua Imaam Ahmad bin Naswri al-Khuza’iy akasema: “Allaah (Amenipiga) Ameniadhibu kwa kupooza!” Mtu huyu alipata shida na tatizo hilo la kupooza akawa kitandani mwake amepotelewa na fahamu kwa muda wa miaka minne kabla ya kufariki kwake.  

 

 

 

 

Share

28-Swabrun Jamiyl: Subira Za Maimaam - Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah)

 

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)  

 

28 -  Subira Za Maimaam - Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah)

 

 

 

Imaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) alikuwa mwenye Iymaan yenye nguvu, mwenye umbuji, jasiri, mwenye elimu nyingi na kubwa.

 

Wakati wake watu wakiogopa dola iliyokuwa na nguvu. Kwa ushujaa wake watu wengi wakashikamana naye na mara kwa mara wakimzunguka na kuwa pamoja naye.

 

Muda mrefu aliokuwa akiutumia Ibn Taymiyyah ulikuwa ni kufundisha Misikitini, na kuwafungua watu kuhusu mambo ya Dini na kubainisha Alichohalalisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na kile Alichoharamisha na kuilinda Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Hata hivyo, maadui wake na washindani wake walimfanyia njama mbalimbali ili wamtege na kumchongea na mtawala wa  Misri na Shaam. Akahamishiwa Misri na akahukumiwa mbele ya ma-Qaadhi na viongozi wakuu wa dola. Alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja na nusu sehemu iiitwayo, Qal’ah, kisha akatolewa jela na ukawekwa mjadala baina yake na viongozi wengine katika washindani wake. Katika mjadala ule Ibn Taymiyyah alishinda. Hata hivyo hawakumuacha na wakamhamishia Shaam kisha akarudi Misri kwa mara nyingine na akafungwa ambapo alihamishiwa Alexandria na kufungwa huko kwa muda wa miezi minane.

 

Mitihani iliendelea na kuendelea kuteswa hadi aliporudi Misri ambapo ilitolewa amri ya mfalme Naaswir Muhammad Qalawuwn kuhusu kutohusika kwake na tuhuma iliyoelekezwa kwake, na akapewa haki ya kuwaadhibu washindani wake waliokuwa sababu ya kuteswa kwake. Hata hivyo, Imaam Ibn Taymiyyah aliwasamehe! Na hivi ndivyo ilivyo adabu ya watu karimu.

 

Ibn Taymiyyah alibakia Cairo na kueneza elimu, akifasiri Qur-aan Tukufu na akiwalingania watu na kushikamana na Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Kisha akahamia Damascus baada ya kuwa mbali nayo kwa muda wa miaka saba hivi. Alipokuwa kule alitoa Fatwa katika mas-alah fulani na Sultani akamuamrisha abadilishe rai yake kuhusu mas-alah hayo, lakini hakujali amri ile na akashikilia rai yake na akasema: “Siwezi kuificha elimu.” Wakamkamata na kumfunga kwa muda wa miezi sita. Kisha akatolewa jela na akaendela kutoa Fatwa zinazolingana na mafundisho ya Qur-aan na Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Mahasimu wake walichukua fursa ya kumfanyia fitna katika fatwa yake inayohusu kufunga safari ya kwenda kutembelea makaburi ya Manabii na waja wema, kwani Ibn Taymiyyah alikuwa na rai kuwa ziara ile si ya wajibu kwa Waislamu. Akafungwa pamoja na nduguye ambaye alikuwa akimhudumia. Pamoja na hayo, hakuacha kuandika, na wakamkataza kufanya hivyo na ndipo alipofungwa na nduguye aliyekuwa akimhudumia kwa hivyo wakataka kuinyamazisha elimu yake isisikike. Vile vile wakamnyang’anya kalamu na karatasi alizokuwa nazo ili asiendelee kuandika elimu yake na kuenea.

 

Azma yake haikuishia hapo kwa kunyang’anywa vifaa vyake akaamua kubadilisha mbinu na kuanza kutumia kuandikia mkaa katika karatasi zilizotapanyika huku na kule.

 

Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) alifariki mwaka 728 Hijriyyah akiwa mwenye kusubiri, Mujaahid akishughulika na elimu. Jeneza lake lilihudhuriwa na Waislamu wapatao laki tano.

Allaah Amruzuku Jannah ya Al-Firdaws. Aamiyn

 

Kwa faida zaidi kuhusu Historia ya Mwanachuoni huyu, soma kitabu hiki muhimu:

 

Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah: Mwanachuoni Wa Wanachuoni (PDF)

 

 

 

Share