Wasifu Wa Maswahaba Kumi Waliobashiriwa Pepo

  

 

Wasifu  Wa  Maswahaba

 

Kumi

 

Waliobashiriwa

 

Pepo

 

 

Al-Khansaa Book Centre.

 

 

 

Wasifu wa Maswahaba Kumi Waliobashiriwa Pepo

 

 

 

 

 

© Al-Khansaa Book Centre.

 

 

 

 

 

 

Chapa ya

Kwanza, Machi 2011

 

 

 

 

 

Kimeandikwa na: Idara ya Utafiti ya Darussalam

 

 

 

Kimefasiriwa kwa Lugha ya Kiswahili na:

 

Hassan Athman Mnjeja

 

Kimepitiwa na:

Abu Sumayyah na Yassin Kachechele

 

 

Typesetting:

 

Al-Khansaa Book Centre,

S.L.P 78397,

Dar es Salaam,

Tanzania.

 

 

Kimechapishwa na:

 

Al-Khansaa Book Centre,

Dar es Salaam,

Tanzania.

 

 

 

 

 

 

 

Haki Zote Zimehifadhiwa.

 

 

“Muhammad ni Mtume wa Allaah. Na walio pamoja naye wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao. Utawaona wakiinama na kusujudu wakitafuta fadhila na radhi za Allaah. Alama zao zi katika nyuso zao, kwa athari ya kusujudu. Huu ndio mfano wao katika Taurati. Na mfano wao katika Injili ni kama mmea ulio toa chipukizi lake, kisha ukalitia nguvu, ukawa mnene, ukasimama sawa juu ya ubuwa wake, ukawafurahisha wakulima, ili kuwakasirisha kwa ajili yao makafiri. Allaah Amewaahidi walioamini na wakatenda mema katika wao msamaha na ujira mkubwa.” (48:29)  

 

 

 

  

 

Share

01-Wasifu Wa Maswahaba Kumi Waliobashiriwa Pepo: Faharisi

 

 

Yaliyomo

 

1. Abu Bakr As-Swiddiyq (Radhiya Allaahu 'Anhu) .......................

Aliyebashiriwa Pepo..........................................................................

Jina Lake Na Nasaba Yake.................................................................

Umbile  Lake....................................................................................

Kuzaliwa  Kwake..............................................................................

Kurejea Kwake Kwenye Uislamu........................................................

As-Swiddiyq (Msema Kweli)..............................................................

Kurejea Kwa Baba Yake Katika Uislamu..............................................

Kurejea Kwa Mama Yake Katika Uislamu.............................................

Kuhajiri............................................................................................

Hijra................................................................................................

Fadhila Za Wahamaji (Muhajirina)......................................................

Habari Za Peponi Zinazofurahisha.......................................................

Siku Ya Kutawafu Mjumbe Wa Allaah..................................................

Utume Wake.....................................................................................

Hotuba Yake Baada Ya Kiapo Cha Utiifu...............................................

Vita Dhidi Ya Walioritadi....................................................................

Vita Vya Buzakhah............................................................................

Vita  Ya  Al-Yamamah.......................................................................

Ukusanyaji Wa Qur-aan Tukufu Kuwa Mus-haf Mmoja..........................

Hadhi  Yake......................................................................................

Imani  Naye.....................................................................................

 

 

2. ‘Umar Bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu 'Anhu) ................

Aliyebashiriwa Pepo.....................................................................

Kuzaliwa Na  Malezi Yake.............................................................

Umbile  Lake................................................................................

Kurejea Kwenye Uislamu...............................................................

Kuhama  Kwake  (Kuhajir).............................................................

Kulingana  Na  Qur-aan  Takatifu.................................................

Kuchaguliwa  Kuwa   Khalifa........................................................

Mwenye Nguvu Na Muaminifu......................................................

Mwasisi  (Mtangulizi)...................................................................

Matendo  Ya  Ibada.......................................................................

Tabia  Yake...................................................................................

Kujinyima  Anasa..........................................................................

Kuwajali  Raia  Zake......................................................................

Kubashiriwa  Pepo..........................................................................

Kufa  Kwake  Shahidi....................................................................

 

 

3. ‘Uthmaan  Bin  'Affaan (Radhiya Allaahu 'Anhu) .....................

Jina Lake Na Ukoo Wake.................................................................

Ukoo  Wake...................................................................................

Maumbile Yake...............................................................................

Kurejea  Katika  Uislamu.................................................................

Kuhajiri Kwake...............................................................................

Mwandishi  Wa  Wahyi....................................................................

Aliyekusanya  Qur-aan  Tukufu........................................................

Kutoa Katika Njia Ya Allaah.............................................................

Kisima Cha Rumah.........................................................................

Upanuzi Wa Msikiti Wa Mtume.........................................................

Ukarimu Wake................................................................................

Kujinyima  Anasa  Za  Dunia............................................................

Kujitambua.....................................................................................

Ukhalifa.........................................................................................

Ushindi Katika Utawala wake............................................................

Kufa Shahidi...................................................................................

 

 

4. ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu 'Anhu) .........................

Ambaye Amebashiriwa Pepo.............................................................

Kuzaliwa  Kwake.............................................................................

Kusilimu  Kwake.............................................................................

Umbile  Lake...................................................................................

Ndoa  Yake......................................................................................

Kubashiriwa Pepo............................................................................

Ujasiri  Wake...................................................................................

Elimu  Yake......................................................................................

Tathmini Yake..................................................................................

Abu Turaab......................................................................................

Kufa  Shahidi...................................................................................

 

5. Twalhah bin ‘Ubaydullaah (Radhiya Allaahu 'Anhu)..................

Ambaye Alibashiriwa Pepo................................................................

Jina Lake.........................................................................................

Mama Yake......................................................................................

Maumbile Yake.................................................................................

Kurejea Katika Uislamu.....................................................................

Hijrah..............................................................................................

Kubashiriwa Pepo.............................................................................

Twalhah (Radhiya Allaahu 'Anhu) Nguli Jasiri.....................................

Siku Ya Badr....................................................................................

Siku Ya Uhud...................................................................................

Ahadi Ya Kifo...................................................................................

Twalhah Alirehemewa.........................................................................

Twalhah Alikuwa Mmoja Wa Waliotimiza Majukumu Yake.......................

Ukarimu Wake wa Kutumia Katika Njia Ya Allaah................................

Sadaka na Kuunga Udugu................................................................

Niitie Watu Wangu..........................................................................

Kutopendelea...................................................................................

Mapenzi Yake Kwa Mjumbe wa  Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aaalihi

Wa Sallaam).....................................................................................

1.Nitolewe Muhanga..........................................................................

2.Maneno ya Mtu:.............................................................................

Kumtaja Kwa Mazuri.........................................................................

Umauti  Wake..................................................................................

Kifo  Chake......................................................................................

 

 

Share

02-Wasifu Wa Maswahaba Kumi Waliobashiriwa Pepo: Maelezo Ya Wachapishaji

 

 

Maelezo Ya Wachapishaji

 

 

 

Tunamhimidi Allaah. Tunamtukuza Yeye, tunamwomba Msamaha na tunaomba hifadhi Yake kutokana na mwelekeo wa kifisadi na kutokana na uovu wa amali mbaya.

 

 

 

Adui mkubwa wa Uislamu ni Shaytwaan. Huja na sura ya hadaa na hutumia juhudi zake zote kuwatoa Waislamu kwenye dini yao na katika misingi na mafundisho yake adhimu. Makafiri wanatishika kwa mwenendo wa maisha ya Waislamu ambao hauna dosari wala usio fedhehesha. Wanajua fika kuwa madhali Waislamu wanashikamana na dini yao, juhudi zote za kuwapotosha hazitofanikiwa kwa sababu Uislamu ndiyo chimbuko la uwezo wao. Uislamu ni dini inayomuinua mtu binafsi kuwa juu na mwenye kuheshimika. Na kwa sababu hii, Uislamu unashambuliwa kwa kila njia na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na wasio kuwa Waislamu (makafiri). Ni jambo rahisi kuwapotosha vijana na kuwatoa katika mambo yenye manufaa na kuwatia katika maangamizi, maisha yaliyo kinyume na Uislamu. Kwa kufuata mwongozo wa Uislamu, tuna muadhimisha Muumba wetu, Allaah na tunakuwa mfano bora kwa binadamu wengine.

 

 

 

Adui (Shaytwaan) ana jaribu kutushawishi tuone ya kuwa maisha ya dunia ndiyo njia pekee ya kupata uwezo na mafanikio. Upotoshaji huo unakusudia kuwashawishi Waislamu waone ya kuwa udhaifu wao una sababishwa na kufuata dini yao, maamrisho yake na misingi yake. Vyombo vya habari pia huitwa viburudishaji, ni vinara vya kuchafua akili za vijana; kwahiyo familia za Kiislamu ziwe macho kutambua uwezo wa viburudishaji kuwapotosha vijana wetu kwa kuwatoa kwenye maadili mema bila wao kujua. Badala ya kuiga haiba ya Mtume Muhammad ambayo haina walakini, bila kujitambua wanaiga tabia mbaya wanazoziona kwenye sinema au runinga, na hivi ndivyo wanavyotekwa na Shaytwaan.

 

 

 

Waislamu imara wana uwezo wa kukhitari kati ya haiba na uigizaji na akabaki na msimamo, ambapo wale dhaifu na wajinga ni rahisi kupotoshwa. Inatupasa kuongeza juhudi hasa katika zama hizi kuzungumza na vijana wetu, na hata sisi watu wazima lazima turejee kwa mashujaa wakuu wa Kiislamu waliopita ambao walijenga utamaduni wenye nguvu na uliotukuka katika tamaduni zingine. Ambao waliitoa jamii kutoka ujahili na kuingiza katika Uislamu ambao ulibadilisha maisha yao kwa kiwango kikubwa. Huu ni utamaduni unaojumuisha shani ya maadili ya Muislamu na maendeleo ya kimaisha sawia.

 

 

 

Tunataka kukiwasilisha kitabu hiki, “LULU ZENYE THAMANI–Wasifu wa Maswahaba kumi waliobashiriwa Pepo.” Kwa vijana wetu kuwa urithi kwao kwa matarajio kuwa wataendelea kutafuta thamani ya kweli ambayo Uislamu unataka kuifikia. Ndani yake kuna mifano ya kuigwa badala ya ubandia, na mafisadi walio wasilishwa kwetu na makafiri.

 

 

 

Abdul Malik Mujahid

 

MENEJA MKUU

 

DARUSSALAM

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Maelezo Ya Wachapishaji (Chapa ya Kiswahili)

 

 

 

Kitabu hiki ni miongoni mwa vitabu muhimu sana kwa wasomaji wa lugha hii ya Kiswahili.

 

 

 

Ni vitabu vichache vinavyozungumzia wasifu wa maswahaba kwa lugha hii ya kiswahili bali ni vichache zaidi vilivyochambua (kwa ushahidi) bila ya ziada ya maneno ya kufurahisha watu wala nuksani.

 

 

 

Hizi ni zama ambazo vigezo bora vimewapotea watu, watu huiga wanavyoviona, wanavyovisoma na wanavyosikia kwa watu. Hakuna kigezo kizuri kama kile alitotuachia Mtume na nyota zilizowakilishwa na maswahaba zake. Hao ndio wa kufuatwa na kuigwa.

 

 

 

Qadhwaa na Qadar ya Allaah ndio iliyowachagua maswahaba zake  kusuhubiana na Mtume Muhammad na usuhuba ule uliwafanya kuwa ni watu walioshiba na kupata maadili yaliyokuwa bora kabisa kutoka kwa mbora wa viumbe vya Allaah. Ilifikia wakati ambao Qur-aan ilikuwa ikionekana katika vitendo vya kila siku katika maisha yao.

 

 

 

Hiyo ndio hali aliyowaachia Mtume na kutuachia kwani yeye kadhalika alikuwa hivyo na Bi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kuthibitisha hilo anamwambia Swahaba aliyetaka kujua tabia ya Mtume ilivyokuwa na kumwambia asome Qur-aan kwani ndio ilivyokuwa tabia ya Mtume.

 

 

 

Waislamu hatuna budi kujifunza tabia nyingi nzuri waliotuachia mashujaa wa Ummah huu na kitabu hiki kinawasilisha hayo.

 

 

 

Abu Summayyah

 

 

 

Al-Khansaa Book Center

 

 

Share

03-Wasifu Wa Maswahaba Kumi Waliobashiriwa Pepo: Utangulizi

 

Utangulizi

 

Roho ya binadamu hujitahidi kupata furaha kwa juhudi zote. Kwa bahati mbaya watu wanapokuwa katika juhudi hizo hupata matatizo na maafa. Na haya hujiri mtu anapoacha kufuata mwongozo wa Uislamu na hasa kwa mtu anayedhani kuwa kiasi kubwa cha mali ndio utatuzi wa mikasa aliyonayo. Mwana falsafa mkubwa aliyeitwa Aristotle alisema kuwa furaha inapatikana kupitia tafakuri juu ya Mungu (Allaah) na kwa kuishi maisha yenye nidhamu. Hapana maelezo mazuri juu ya Uislamu kuliko kauli isemayo, “Kuwa ni Njia ya maisha yenye Nidhamu.”

 

Maswahaba wa Mjumbe wa Allaah walikuwa watambuzi wa ukweli huu. Hivyo, walimridhisha Allaah, na kufanya hivyo, walipata furaha na maendeleo katika maisha yao. Katika jumuiya ya Kiislamu, utajiri unagawanywa. Wale wenye kingi wanagawana kingi, na wale wahitaji wanapewa sehemu. Tunapomridhisha Allaah, mizani zetu za amali njema zinajaa na Pepo ndio tuzo yetu siku ya Hesabu. Je, kuna tuzo na mahali bora zaidi kuliko Peponi?

 

Jihadi inaweza kuwa tukio la kila siku, Maswahaba walikuwa wapanda farasi mchana na jioni waliitumia kufanya ibada. Walikuwa watu wa kusali, kufunga, kutoa sadaka, wakarimu wa kweli. Waliokuwa safi (wasiofanya dhambi), waaminifu na wacha-Mungu. Walikuwa watu waliomudu kudhibiti fikra zao, mwili na hasira. Hawakuridhisha utashi wa nafsi zao. Walijishughulisha kuwalisha wenye njaa. Yote tuliyo yadhukuru ni Jihadi.

 

Mwito wa Jihadi (yaani vita au mapambano) uliponadiwa, Maswahaba walikuwa tayari wamejitolea muhanga kwa kila kitu; mali zao, maisha yao, na waliziacha familia zao majumbani.

 

Hawakuogopa kifo kwa sababu hawakujua njia bora ya kufa zaidi ya kupigana kulinda haki za Kiislamu au maadili yaUislamu.

 

Na hii ndio maana halisi ya shahada, La ilaaha illa Allaah (hapana apasae kuabudiwa ila Allaah), Allaah aliwaruzuku furaha ya kweli na Pepo kama malipo ya uaminifu katika njia yake.

 

Pepo ni makazi ya mwisho na ya kudumu ya waumini na wacha-mungu. Kuna Maswahaba wengi waliobashiriwa Pepo kwa kutambua ibada zao na hadhi ya juu.  Tunapo kitalii kitabu hiki tutapata fursa ya kujifunza habari zao. Na kwa kufanya hivyo tutajifunza njia ya kwenda Peponi.

 

Share

04-Wasifu Wa Maswahaba Kumi Waliobashiriwa Pepo: Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu 'Anhu) - 1

 

 

 

1. Abu Bakr As-Swiddiyq Aliyebashiriwa Pepo.

 

 

Linapotajwa jina la As-Swiddiyq tunapata tafakuri ya watu wenye mwenendo na maadili mema. Moyo utachangamka na kuvutiwa na As-Swiddiyq (mkweli).

 

Abu Bakr As-Swiddiyq alikuwa rafiki wa Mjumbe wa Allaah Muhammad tokea ujana wake mpaka alipozeeka. Alikuwa mwenza mwaminifu wakati wa raha na wakati wa shida. Alikuwa akiitwa ‘mwaminifu’ ambaye alimwamini Mtume wakati wengine wakimpa mgongo (wakimkana). Imani yake ilikuwa thabiti, na alifahamika kwa umbuji wa lugha na kwa kuamiliana vizuri na watu. Alifahamika sana kwa ukarimu wake; na utajiri wake ulikuwa wa jamii ya waumini.

 

Ilikuwa heshima kwake kwa Allaah kuteremsha aya hii;

“Ikiwa nyinyi hamtamnusuru Mtume , basi Allaah Alikwishamnusuru walipomtoa waliokufuru, naye ni wa pili katika wawili walipo kuwa katika pango, naye akamwambia sahibu yake: Usihuzunike. Hakika Allaah yu pamoja nasi. Allaah Akamteremshia utulivu Wake, na Akamuunga mkono kwa majeshi msioyaona, na akalifanya neno la waliokufuru kuwa chini, na Neno la Allaah kuwa ndilo juu. Na Allaah ndiye Mwenye nguvu Mwenye hikima.” (9: 40).

 

Kisa cha Hijrah na siku walizokaa pangoni ni mfano wa somo lililoonesha usuhuba unavyoweza kuwa na nguvu.

 

Alikuwa kiumbe wa Allaah aliyependwa sana na Mjumbe wa Allaah na alielezewa kama ifuatavyo:

“Alikuwa dhaifu kimwili lakini mwenye nguvu katika mambo ya Allaah , alikuwa mnyofu katika nafsi yake lakini aliyetukuka mbele za Allaah . Alitukuzwa mbele za watu, na alifadhilishwa katika mioyo yao.”

 

Wanyonge waliimarishwa kwa ushawishi wake. Abu Bakr alikuwa chimbuko la matumaini wakati wa hali ngumu. Alikuwa kimbilio na mhimili wa Waislamu wakati akiishi nao. Alidharau maisha ya dunia, na akajiweka mbali na jambo lolote ambalo halikuwamo katika mafundisho ya Mtume Alikuwa msomi mashuhuri wa dini ambaye alibadilishana mawazo na watu na alikuwa mcheshi. Alikuwa na imani thabiti kuliko watu wote, alikuwa na imani safi na alikuwa mkweli sana. Alikuwa rahimu kwa kila mtu, hasa kwa Waislamu. Kulipokuwa na kukengeuka dhidi ya Uislamu alilia; na Uislamu uliposhambuliwa aliunguruma kama simba tayari kuihami dini na watu aliowapenda sana. Endapo aliyedhalilishwa ni mwanamke au mtoto au mnyonge, alikuwa wa kwanza kukusanya watu kwenda kwenye mapambano.

 

Hebu fikiri, hadhi ya Uislamu ingekuwaje kama asingewahofisha wasaliti? Ujasiri wake na ulezi wake alivifanya kuwa umoja na nguvu. Alikuwa Zaydi ya mtu wa kawaida.

 

Huyu ndiye Abu Bakr aliyekuwa mbora wa Waislamu baada ya kurejea katika Uislamu, na alibakia hivyo mpaka Allaah Alipomukhitari (Alipotwaa roho yake).

 

Ni muhali kudhukuru mema yote na uadilifu wa Abu Bakr ndani ya kurasa chache. Kwa hiyo inatosheleza kutaja sifa chache kwa matarajio ya kuwa zitawahamasisha wale wanaotafuta ukweli.

 

 

Jina Lake na Nasaba Yake

 

 

Jina lake ni ‘Abdullaah bin Abu Quhaafah, ‘Uthmaan bin ‘Aamir bin ‘Amr bin Ka’b bin Sa’d bin Taim bin Murrah bin Ka’b. Nasaba yake inakutana na ile ya Mjumbe wa Allaah kwa Murrah.

Lakabu yake ilikuwa ‘Atiyq (aliyeokolewa Motoni). Watu wana maoni tofauti kuhusiana na jina lake. Baadhi wanasema kuwa ni kwa sababu ya vitendo vyake na majadiliano na watu kwa tabia iliyotukuka. ‘Wengine wanasema ni kwa sababu ya nasaba yake sharifu, kwa kuwa hakuwa na dosari au alikuwa nazo chache. Inasemekana kuwa lakabu hiyo alipewa na Mtume .

’Aaishah alisema: “WaLlaahi, nilipokuwa chumbani mwangu na Mjumbe wa Allaah na Maswahaba wake walikuwa uani, tulitenganishwa na pazia. Abu Bakr aliingia ndani na Mtume alisema, ”Yeyote atakaye kuridhishwa kwa kumwangalia mtu aliyeokolewa na Moto, amuangalie Abu Bakr.”

 

‘Abdullaah ni jina alilopewa na wazazi wake lakini jina ‘Atiyq ndilo liliolokuwa likitumika sana. Katika baadhi ya masimulizi katika zama za jahiliya alikuwa akijulikana kama ‘Abdul Ka’bah lakini aliposilimu aliitwa, ‘Abdullaah. ’’Abdullaah bin Az-Zubayr alisema

“Jina la Abu Bakr lilikuwa ‘Abdullaah. Mtume alimwambia: ‘Umeokolewa na Moto’ Kwa sababu hiyo aliitwa “Atiyq.”

 

Mama yake aliitwa Saalima bint Sakhr bin ‘Amr bin Ka’b. Lakabu yake ilikuwa Ummul-Khayr (Mama wa Kheri) na alikuwa binamu ya baba yake.

 

 

Umbile Lake

 

 

Abu Bakr alikuwa na hali nzuri ya wastani, mwembemba, mgongo ulipinda kidogo, na alikuwa na uso mwembemba na macho makubwa yaliyoingia ndani. Paji la uso wake lilijitokeza kidogo, na alitia nywele zake hinna iliyochanganywa Katam.

 

 

Kuzaliwa  Kwake

 

 

Abu Bakr alizaliwa miaka miwili na miezi kadhaa baada ya kuzaliwa Mtume katika mji wa Makkah. Aliishi hapo mpaka alipokuwa kijana (barobaro). Hakuondoka mpaka alipoanza biashara, na kisha alihamia Madina pamoja na Mtume Alikuwa mmoja wa matajiri wa Makkah na alifahamika kwa ukarimu wake, heshima na tabia njema. Alikuwa akipendwa na watu wa jahiliya na alikuwa msimamizi wa diya na madeni.

 

Hali ilikuwa hivyo kwa sababu Maquraysh hawakuwa na mfalme wa kuwatawala. Kila kabila ilikuwa na kiongozi ambaye alitawalia mambo yao. Mathalan Banu Hashim walikuwa na jukumu la kuwapa mahujaji chakula na maji. Banu 'Abdid-Daar walikuwa na jukumu la kuangalia mambo mengine yaliyohusu utunzaji wa Ka’bah (Nyumba ya Allaah Hapana mtu aliyeruhusiwa kuingia ndani ya Ka’abah bila ruhusa ya Banu ‘Abdud-Daar.

 

Kuibeba bendera wakati wa vita lilikuwa jukumu lao pamoja na Darun–Nadwah (mahala Maquraysh wakikutana kujadili masuala muhimu).

 

Abu Bakr alijishughulisha sana na biashara zake. Akiutumia vizuri muda wake na hakupoteza muda wake kufanya mambo yasiyo na maana. Ambapo wengine wakinywa pombe au wakijishughulisha na ufisadi, uzinzi na madhambi mengine. Abu Bakr alikuwa mwanaume aliyejipambanua kwa daraja na hadhi.

Abu Bakr aliona faraja kuwa na kijana kama yeye ambaye alikuwa na maadili mema. Mtu ambaye aliyeacha kuabudia masanamu, asiye kunywa pombe na ambaye hakupoteza ujana wake katika ufedhuli. Kijana huyo alikuwa Muhammad bin ‘Abdillaah bin ‘Abdul-Muttwalib ambaye Abu Bakr alimwona kuwa rafiki bora. Vivyo hivyo Muhammad aliona kwa Abu Bakr yaliyomfanya awe karibu naye na kumpenda. Jamii ilipendezewa na usuhuba wao. Abu Bakr aliutumia muda wake na mapumziko kujifunza koo za makabila ya Kiarabu mpaka akawa mjuzi wa tawi hili la elimu mpaka akawa bingwa wa nyanja hii.

 

 

Kurejea Kwake Kwenye Uislamu

 

 

Haishangazi Abu Bakr kuwa mtu wa kwanza kusilimu, na pia sio ajabu kuwa alikuwa wa kwanza kumwamini Mjumbe wa Allaah .

Kuna mambo mawili yaliyomfanya Abu Bakr kuharakisha kuukubali Uislamu.

  • Kupenda mambo mazuri, na
  • Urafiki wake na Mjumbe wa Allaah .

Abu Bakr alikuwa na wema wa asili ambao uliwafanya watu kutenda mema. Alijiepusha na yale mambo ambayo yangechafua hadhi yake.

 

Moyo wake ulikuwa sawa na ardhi yenye rutuba ambayo inatoa matunda mengi. Maji yalitononeshwa na busara za Uislamu ambazo aliamua kuzifuata. Uislamu ukifanya hulka yake kuwa nzuri. Kamilifu, ya ukweli, ya haki na imara. Ukarimu wake katika njia ya Allaah haukuwa na mfano. Kwa ufupi, kila tabia na mwenendo mzuri unajumuishwa katika hiba yake.

 

Mvuto mwingine uliomsukuma Abu Bakr kufuata njia ya Uislam ni urafiki wake na Mjumbe wa Allaah Muhammad. Haina maana aliamini kwa kumpendezesha rafiki yake.

 

Hapana! Hakuamini kwa sababu ya urafiki wao bali ni kutokana aliyojifunza na yaliyompendeza kwa Mtume ndiyo yaliyomkurubisha katika Uislamu na Allaah.  Aliuona Uislamu kwa uwazi, kwa sababu aliiona tabia njema ya Mtume Urafiki wake na Mtume haukuwa katika nje na wakati huo huo waliheshimiana na kusaidiana. Alimpenda Mtume na alimuona kuwa ni mshauri wake mkuu. Walipishana miaka miwili katika umri wao, na hili lilifanya wafahamiana bila kuwepo ushindani au ubandia. Naye Abu Bakr alikuwa na muda wa kumjua Mtume pia. Alifarijika kumwona kuwa ni mkweli na mwaminifu. Kwa hiyo alimtambua kuwa ni Mtume na hakuona dosari yoyote kwake. Aliona ni mfano uliokuwa unatembea katika yote aliyokuwa akihubiri kuhusu Uislamu. Kutokana na sababu hiyo haikuwa ajabu kwa Abu Bakr kuwa mtu wa kwanza kumwamini Muhammad na kumuunga mkono.

 

Muhammad alipotoa ujumbe kwa Abu Bakr akimwalika yeye na watu wengine kuyaacha masanamu yao, Abu Bakr hakusita, na alikuwa mtu wa mwanzo kusilimu. Mtume Muhammad rafikiye alifurahi sana.

 

Mjumbe wa Allaah akizungumzia kurejea kwa Abu Bakr kwenye Uislamu, alisema,

 

“Sijapata kumlingania mtu kwenye Uislamu na asiwe na wasiwasi, Abu Bakr alikuwa wa mwanzo kutokuwa na wasiwasi.”

Kuna Hadiyth nyingi zinazothibitisha ya kuwa Abu Bakr alikuwa wa mwanzo kati ya wanaume huru kumwamini Mtume kama ilivyo. Khadija alikuwa mwanamke wa mwanzo kumwamini. ‘Aliy bin Abi Twaalib  akiwa miongoni mwa vijana, na Zayd bin Haarithah miongoni mwa watumwa wa mwanzo kuingia katika Uislamu.

 

Kusilimu kwa Abu Bakr kuliunufaisha Uislamu, kwa sababu alikuwa mtu maarufu sana hapo Makkah ambaye alikuwa tajiri na aliyependwa sana na watu. Alikuwa muhubiri mzuri wa Uislamu kwa sababu watu walimheshimu, na walivutiwa sana na tabia yake. Kwa hakika maswahaba wengi walirejea katika Uislamu kupitia kwake.

Baadhi yao ni: Az-Zubayr bin Al-’Awwaam, ‘Uthmaan bin ‘Affaan, Talha bin ‘Ubaydullaah, Sa’d bin Abi Waqqaas na ‘Abdur-Rahmani bin ‘Awf . Kwa njia hii, kurejea kwa Abu Bakr katika Uislamu kuliwaleta watu wengi katika Uislamu. Waislamu lazima wawe wema na waamiliane kwa uzuri na watu wengine kama njia ya kuwavuta watu wazuri, na kunyanyapaa watu waovu kunasaidia kuepusha uovu. Ni kama fumbo la mti wenye matunda mengi ambao mizizi yake ni imara katika ardhi na matawi yake yanafikia juu mawinguni. Unazaa matunda wakati wote katika mwaka. Kinyume na hivi, ni mshikamano wa watenda maovu ambao ni kama fumbo la mti mwovu ambao hauzai chochote isipokuwa matunda mabaya yasiyolika.

 

 

As-Swiddiyq (Msema Kweli)

 

 

Alipewa jina la As-Swiddiyq (msema kweli) kwa sababu ya kutokuwa na wasiwasi wa kumwamini Mjumbe wa Allaah . Ibn Is-haaq alisema kwa mamlaka ya Al-Hasan Al-Baswriy na Qataadah, Alijulikana kwa jina hilo kwa mara ya mwanzo asubuhi ya Israa (safari kutoka Makkah mpaka Quds [Jerusalem]) kisha Mi’iraaj (kurufaishwa mbinguni). Kwa mamlaka ya Bi ’Aaishah aliyesema: “Makafiri walimwendea Abu Bakr na kumwambia, Rafiki yako amefikwa na jambo gani? Anadai ya kuwa usiku uliopita alikwenda (Quds) Jerusalem (na akarejea usiku ule ule)” Akauliza? Amesema hivyo? Wakasema, ‘Ndiyo’. Abu Bakr akawambia: Amesema kweli, na ninaamini ufunuo atakao kuja nao kutoka mbinguni. Kwa hiyo kutokana na msimamo huo aliitwa As-Swiddiyq.”

 

Kuna Hadiyth nyingi zinazothibitisha kuwa Jibriyl na Mtume walimpa jina hili. Kwa mamlaka ya Abu Hurayrah aliyesema: “Mjumbe wa Allaah alipofika Dhi Tuwa wakati akirejea kutoka Mi’iraaj safari ya Usiku, alimwambia malaika Jibriyl: “Ewe Jibriyl! Watu wangu hawatoniamini.’ Alimwambia,”Abu Bakr anakuamini, Yeye ni As-Swiddiyq.”

 

Kuna Hadiyth nyingine inayothibitisha kuwa Jibriyl ndiye aliyempa jina hili. Kwa mamlaka ya An-Naazil bin Sawah ambaye alisema:

 

“Tulimwambia ‘Aliy ‘Ewe Khalifa wa Waumini! Tueleze juu ya Abu Bakr alisema: “Huyu ni mtu aliyepewa As-Swiddiyq kwa ulimi wa Jibriyl na Muhammad. Alikuwa Khalifa wa Mjumbe wa Allaah aliyemchagua kwa ajili ya dini yetu, hivyo tunaridhika naye kwa maisha yetu ya dunia.”

 

Kwa mamlaka ya Hakam bin Sa’d ambaye alisema: “Nilimsikia ‘Aliy akiapa ya kuwa jina la ‘As-Swiddiyq, (Abu Bakr) alipewa na Allaah :

 

 

Kurejea Kwa Baba Yake Katika Uislamu

 

 

Baba yake alikuwa ‘Uthmaan bin ‘Aamir akijulikana kama Abu Quhaafah. Alirejea kwenye Uislamu siku Makkah ilipokombolewa na akala kiapo cha utii kwa Mjumbe wa Allaah na kipindi cha Ukhalifa wa Abu Bakr Alifariki dunia wakati wa Ukhalifa wa ‘Umar

 

Sasa tumsikilize Asmaa bint Abi Bakr akitusimulia juu ya kurejea baba yake kwenye Uislamu.

 

“Mjumbe wa Allaah aliposimama Dhi–Tuwa, Abu Quhaafah alimwambia binti yake mdogo kabisa,’Ewe binti! Nisindikize safari yangu ya Abu Qubays kwa kuwa alikuwa kipofu kwa hiyo binti alimsindikiza. Alimwambia ‘Ewe binti, unaona nini? Alijibu: “Naona mkusanyiko wa watu wengi. Akamwambia, ‘Hawa ni farasi. Akajibu, ‘Namwona mtu akienda mbele na nyuma.’ Akasema, Huyu ndiye anayewaongoza na anakuwa mbele yao.’ Kisha akasema:  ‘WaLlaahi wametawanyika”, Akasema: ‘WaLlaahi! Wapanda farasi wameendelea na safari. Alirejea naye nyumbani wakiwa njiani, mpanda farasi alikutana naye, na alipomwona msichana amevaa kidani cha fedha, alikichukua.

 

Asmaa alisema: “Mjumbe wa Allaah alipoingia Makkah na kisha kuingia katika nyumba ya Allaah , Abu Bakr alimjia akimwongoza baba yake. Mjumbe wa Allaah alipomwona Abu Bakr akamwambia; ‘Ingekuwa vema kama ungelimwacha nyumbani mpaka nije kwake. Abu Bakr alijibu; “Ewe Mjumbe wa Allaah! “Analazimika kuja kwake kuliko wewe kwenda kwake.” Kisha Abu Bakr alimkalisha mbele ya Mjumbe wa Allaah Mjumbe wa Allaah alikigusa kifua chake kisha akamwambia, ‘Rejea katika Uislamu’ na alirejea katika Uislamu.

 

 

Kurejea Kwa Mama Yake Katika Uislamu

 

 

Mama yake akiitwa Salma bint Sakhr. Alikuwa miongoni mwa Waislamu wa mwanzo, na alikufa katika hali nzuri ya Uislamu. ’Aaishahh anasimulia kisa kifuatacho: “Maswahaba wa Mjumbe wa Allaah ambao idadi yao ilikuwa 39, walijumuika katika nyumba ya Darul-Arqam. Abu Bakr alimsisitizia Mjumbe wa Allaah ajitokeze mbele ya watu. Mjumbe wa Allaah alisema:

“Kwa hakika sisi ni wachache ewe Abu Bakr” Aliendelea kumchagiza mpaka Mjumbe wa Allaah alikubali na Waislamu walitawanyika Msikitini (Nyumba ya Allaah ).

 

Abu Bakr alisimama na alianza kuwaasa watu na Mjumbe wa Allaah alikuwa amekaa. Kwa hiyo, Abu Bakr alikuwa mtu wa kwanza kuwalingania watu katika dini ya Allaah na Mjumbe Wake hadharani. Makafiri walikasirika na kuwashambulia Waislamu. Abu Bakr alipigwa vibaya. Mwovu na fedhuli, ‘Utbah bin Abi Rabi’ah alimpiga kwa kobadhi mpaka Abu Bakr akajeruhiwa sana kiasi cha kushindwa kutofautishwa kati ya pua na uso. Banu Taym, jamaa zake Abu Bakr, walikuja kuwazuia makafiri kuendelea kumpiga. Walimpeleka Abu Bakr nyumbani, na wakarejea Msikitini huku wakiapa: ‘WaLlaahi, iwapo Abu Bakr atafariki dunia, tutamwua ‘Utbah.’

 

Walirejea nyumbani kwa Abu Bakr na Abu Quhaafah alimsemesha Abu Bakr mpaka akajibu. Aliporejewa na fahamu, alisema: ”Mjumbe wa ‘Allaah amefanya nini?”

Walimlaumu na kumkaripia.Waliondoka na kumwambia mama yake Ummul-Khayr amlishe na ampe kinywaji.

 

 

Abu Bakr aliendelea kuuliza: ‘Mjumbe wa Allaah amefanya nini?’ Mama yake akamwambia: ‘WaLlaahi sijui alichofanywa rafiki yako?’ Abu Bakr akamwambia, ‘Nenda kwa Umm Jamiyl bint Al-Khattwaab na umuulizie habari zake.’ Alipofika kwa Umm Jamiyl, alimwambia; ‘Kwa hakika, Abu Bakr anakuuliza juu ya Muhammad bin ‘Abdillaah.’ Umm Jamiyl alijibu ‘Simjui Abu Bakr wala Muhammad bin ‘Abdillaah, lakini kama unataka niende kwa mwanao, nitafuatana nawe.’ Alisema, ‘Ndiyo.’ Kwa hiyo Umm Jamiyl alifuatana naye na walimkuta Abu Bakr anakaribia kukata roho. Umm Jamiyl aliangua kilio na kusema: hakika watu waliokuumiza ni waasi, na namwomba Allaah Mlezi Akulipizie kisasi.’ Abu Bakr aliendelea kuuliza: ’Mjumbe wa Allaah anafanya nini?’ Alijibu: ‘Mamako huyu hapa anakusikiliza’. Abu Bakr akamwambia: ‘Usimhofie’ Akajibu, ‘Afya yake ni njema’. Akauliza tena, ‘Yuko wapi?’ Alijibu, ‘Katika nyumba ya Al-Arqam.’ Akasema: ‘WaLlaahi sitoonja chakula wala maji mpaka niende alipo’. Walimwambia asubiri mpaka watu watulie. Kulipotulia, alitoka akimwegemea mama yake na Umm Jamiyl. Alipoingia kwa Mjumbe wa Allaah alimbusu, na Mjumbe wa Allaah alifurahi sana.

 

Abu Bakr alimwambia: ‘Ningependa baba yangu na mama yangu watolewe muhanga, mimi sina tatizo isipokuwa yule mwovu (‘Utbah) amejeruhi uso wangu. Huyu ni mama yangu, maridhia kwa wazazi wake, nawe umetukuzwa (umebarikiwa). Kwa hiyo mkaribishe kwa Allaah, na umwombee kwa Allaah Amwokoe na adhabu ya Moto. Mtume alimkaribisha katika Uislamu naye aliupokea Uislamu.

 

Walikaa na Mjumbe wa Allaah kwa mwezi mmoja, na jumla yao walikuwa wanaume 39. Hamzah naye alirejea katika Uislamu siku ambayo “Abu Bakr alipigwa.

 

 

Kuhajiri

 

 

Mateso ya makafiri yaliposhitadi, Mjumbe wa Allaah aliwapa ruksa ‘Waislamu kuhajiri. Abu Bakr alipoomba ruksa ya kuondoka, Mjumbe wa Allaah alimwambia:

“Usifanye haraka. Inaweza kuwa Allaah atakuchagulia mwenza.” Abu Bakr alitarajia ya kuwa mwenza atakuwa Mjumbe wa Allaah mwenyewe, kwa hiyo alinunua vipando viwili kwa madhumuni hayo.

 

‘Aaishah anasema: “Mtume alikuwa akija kwenye nyumba ya baba yangu mapema asubuhi au jioni. Siku ile aliyeruhusiwa na Allaah kuhajiri, alitujia mchana. Abu Bakr aliondoka alipokaa juu ya kitanda na kumpisha Mtume Hapakuwa na mtu nyumbani isipokuwa Asmaa na mimi. Mtume alimwambia Abu Bakr ‘Waondoshe uliokuwa nao.’ Alisema, ‘Ewe Mjumbe wa Allaah! Hawa ni mabinti zangu. Kuna jambo gani?’ Mjumbe wa Allaah alijibu: ‘Allaah Ameniruhusu nihajiri’. Abu Bakr akasema: ‘Je, nifuatane nawe?’ Ewe Mjumbe wa Allaah? Alijibu ‘Ndiyo’. WaLlaahi sijapata kumwona mtu akitoa machozi kwa furaha kama nilipomwona baba yangu siku ile akitokwa na machozi ya furaha.”

 

 

Hijra

 

 

Mtume na Abu Bakr walimkodi ‘Abdullaah bin Urayqit ambaye alikuwa kafiri, kuwaongoza katika safari yao. Walimpa vipando viwili avichunge mpaka wakati utakapowadia. Hapana aliyeijua safari yao isipokuwa ‘Aliy bi Abi Twaalib, Abu Bakr As-Swiddiyq na familia ya Abu Bakr

 

Mtume na Abu Bakr walianza safari yao. Waliingia katika pango linaloitwa Thawr jirani ya Makkah. Kutokana na mapenzi yake kwa Mtume Abu Bakr alikuwa wa kwanza kuingia pangoni isije kuwa kulikuwa na mnyama pori mle ndani, alimkinga Mtume ili asimhatarishe maisha yake.

 

Abu Bakr alimtaka mwanae ‘Abdullaah asikilize waliyokuwa wakiyasema watu, na aje kwake kuwaelezea waliyokuwa wakijadili watu kuhusu kadhia hii. Alimtaka ‘Aamir bin Fuhayrah, mtumwa wake, awachunge kondoo wale mchana na jioni awapeleke pangoni kwa sababu mbili:

1.  Kuwakamua na kunywa maziwa yao.

2.  Kufuta nyoyo za ‘Abdullaah anapokuja kuwapasha habari.

 

Baada ya siku tatu watu walikata tamaa ya kuwatafuta. Mwongozaji (‘Abdullaah bin Urayqit) alikwenda pangoni na farasi watatu.

Asmaa bint Abi Bakr aliwaletea chakula. Wakati mmoja aliposahau Al-Isam (mkanda wa kubebea chakula) alichukua mkanda wake na kuukata. Alipewa lakabu ya Dhatun–Nitwaqayn (mwenye mikanda miwili) baada ya tukio hilo.

 

Makafiri walipopoteza matumaini ya kumkamata Mjumbe wa Allaah na Maswahaba zake, walitangaza zawadi nono ya ngamia 100 kwa yeyote atakayemshika. Waliangalia nyayo lakini walichanganyikiwa. Mmoja ya watu hodari wa kufuatilia nyayo alikuwa Suraaqah bin Malik.

 

Kwa msaada wake waliweza kupanda mlima alipokuwa Mtume na Maswahaba wake. Walipita mlango wa pango mara nyingi bila kutambua ya kuwa ndani mlikuwa na watu kwa sababu Allaah aliwafisha utambuzi na uoni wao ili kumhifadhi Mjumbe wa Allaah . Abu Bakr alimwambia Mtume: “WaLlaahi, kama mmoja wao angeangalia chini ya miguu yake, angetuona.”

Mtume alimwambia:

“Unafikiria nini juu ya (watu) wawili na Allaah ni watatu wao? Katika mapokezi mengine ya Muhammad bin Sinaan, iliyosimuliwa na Anas kuwa Abu Bakr alisema:

“Nilimwambia Mtume nilipokuwa pangoni, kama mmoja wao angeangalia chini ya miguu yake, angetuona.”Alisema, ‘Ewe Abu Bakr! Unafikiria nini juu ya (watu) wawili ambapo watatu wao ni Allaah?”

 

Watu wa Al-Madiynah walipopata habari ya kuwa Mtume alikuwa anaondoka Makkah, walimsubiri kwa hamu. Wakati mwingine ilikuwa asubuhi wakati jua lilikuwa kali. Siku ambayo Mjumbe wa Allaah alipowasili Al-Madiynah, mtu wa kwanza kumwona alikuwa Ya’aquub ambaye alijua kuwa watu wa Madiynah walikuwa wakimsubiri, alisema kwa sauti.

 

“Enyi Answaar! Yule mliyekuwa mkimsubiri amewasili: Kwa hiyo walitoka nje na kumlaki Mtume pamoja na Mwenzake chini ya kivuli cha mtende. Watu wengi wa Madiynah hawakumfahamu Mjumbe wa Allaah hivyo walijumuika ili wamfahamu. Kivuli kiliposogea, Abu Bakr alisimama kutengeneza kivuli kwa nguo yake. Kwa kitendo hicho walimfahamu Mjumbe wa Allaah Muhammad

 

 

Share

05-Wasifu Wa Maswahaba Kumi Waliobashiriwa Pepo: Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu 'Anhu) - 2

 

 

Fadhila za Wahamaji (Muhajirina)

 

 

Kuna Aayah na Hadiyth nyingi zinazotaja fadhila za wahamaji (Muhajirina) Mmoja wao ni Abu Bakr ‘Abdullaah bin Abi Quhaafah Al-Taymy Kauli ya Allaah inasema,

“Wapewe mafakiri Wahajiri waliotolewa majumbani mwao na mali yao kwa ajili ya kutafuta fadhila kutoka kwa Allaah na radhi Zake, na wanamsaidia Allaah na Mtume Wake. Hao ndio wakweli.” (59: 8)

 

Na vile vile katika Kauli ya Allaah :

“Ikiwa nyinyi hamtamnusuru Mtume, basi Allaah Alikwishamnusuru walipomtoa waliokufuru, naye ni wa pili katika wawili walipo kuwa katika pango, naye akamwambia sahibu yake: Usihuzunike. Hakika Allaah Yu pamoja nasi. Allaah Akamteremshia utulivu Wake, na akamuunga mkono kwa majeshi msiyoyaona, na akalifanya neno la waliokufuru kuwa chini, na Neno la Allaah kuwa ndilo juu. Na Allaah ndiye Mwenye nguvu Mwenye hikima.” (9: 40)

 

‘Aaishah, Abu Sa’id na Ibn ‘Abbaas walisema; “Abu Bakr alikuwa pangoni na Mtume katika pango la Ath-Thawr, Makkah).” (Al-Bukhaariy).

 

 

Habari za Peponi Zinazofurahisha

 

 

Mtume asiyezungumza kwa utashi wake, alimletea Abu Bakr habari zinazofurahisha za Peponi zaidi ya mara moja.

 

Anas bin Malik alisimulia: Hakika, Mtume, Abu Bakr ‘Umar na ‘Uthmaan walipanda mlima Uhud wakati mlima ukitetema, na hapo Mjumbe wa Allaah alisema: “Kuwa madhubuti ewe Uhud. Kuna Mtume, mtu mwaminifu mmoja, na mashahidi wawili wamesimama juu yako.” (Al-Bukhaariy Hadiyth Na. 3675).

 

Bila shaka yeyote alikuwa anamkusudia Abu Bakr kwa kauli yake: “Mtu mwaminifu” Imeridhiwa kuwa waaminifu na wa kweli ni miongoni mwa wenye haki ya kuwemo Peponi kwa mujibu wa maandiko ya Qur-aan kama Mola Alivyosema:

“Na wenye kumtii Allaah na Mtume , hao wa pamoja na wale aliowaneemesha Allaah miongoni mwa Manabii, na Masiddiqi, na Mashahidi, na Watu wema. Na uzuri ulioje kuwa pamoja na watu hao! “ (4: 69).

 

Abu Hurayrah alisimulia kuwa Mjumbe wa Allaah alisema: “Yeyote atakayetoa aina mbili ya vitu kama sadaka katika njia ya Allaah, ataitwa kwenye lango la Peponi na ataambiwa: “Ewe mtumwa wa Allaah! Neema iko hapa’ Yeyote aliyekuwa miongoni waliokuwa wakisimamisha Swalah, ataitwa kwenye lango la Swalah. Abu Bakr As-Swiddiyq na yeyote aliyekuwa miongoni mwa walioshiriki katika Jihaad, ataitwa kwenye lango la Jihaad, na yeyote ambaye alikuwa miongoni mwa wafungaji, ataitwa kwenye lango la Ar-Rayyaan; yeyote aliyekuwa miongoni mwa waliokuwa wakitoa As-Swadaqah, ataitwa kwenye, lango la As-Swadaqah.” Abu Bakr alisema: “Waruhusu wazazi wangu watolewe muhanga kwa ajili yake, Ewe Mjumbe wa Allaah! Hatopata dhiki yule atakayeitwa kwenye milango hiyo. Je, yupo atakayeitwa kwenye milango yote hiyo?”Mtume alijibu, “Ndiyo, na nataraji utakuwa mmoja wao.”

 

 

Siku ya Kutawafu Mtume

 

 

Waislamu walipata majonzi makubwa siku alipofariki dunia Mtume ‘Umar bin Al-Khattwaab aliathirika sana kiasi cha kuchomoa upanga wake na kusema: “Iwapo nitamsikia yeyote akisema kuwa Mjumbe wa Allaah amefariki dunia, nitakata shingo yake.”

 

Mjumbe alitumwa kwa Abu Bakr Yule mtu alipomwona Abu Bakr, alilia. Abu Bakr alimwuliza: “Una jambo gani? Mtume amefariki dunia?” Yule mtu alisema: “’Umar bin Al-Khattwaab anasema: “Sitomsikia yeyote akisema Mjumbe wa Allaah amefariki dunia bila kutaka kukata shingo yake.”

 

Abu Bakr aliingia ndani ya nyumba ambapo Mtume alilazwa na kufunikwa nguo. Alimbusu na alitoka nje na kuwasomea Aayah ifuatayo:-

“Na Muhammad hakuwa ila ni Mtume tu. Wamekwishapita kabla yake Mitume. Je, akifa au akauwawa ndiyo mtageuka mrudi nyuma? Na atakayegeuka akarudi nyuma huyo hatamdhuru kitu Allaah. Na Allaah Atawalipa wanaomshukuru.” (3: 144)

 

Na Aayah:

“Ni nani itakayemfikia adhabu ya kumhizi, na itakayemshukia adhabu ya daima.” (39: 30).

Kisha akasema: “Yeyote aliyekuwa akimwabudu Muhammad afahamu kuwa Muhammad amefariki dunia. Na yeyote aliyekuwa anamwabudu Allaah, afahamu ya kuwa Allaah ni wa milele na hatokufa.” ‘Umar alisema, “WaLlaahi! Inakuwa kama sikuwahi kuzisoma Aayah hizi mpaka leo.”

 

 

Utume Wake

 

 

Mjumbe wa Allaah hakuwahi kumteua kati ya Maswahaba zake kuwa Khalifa. Lakini katika siku zake za mwisho, alisema kama ilivyoelezwa katika Hadiyth ifuatayo:

“Amri aliyopewa Abu Bakr kuwaswalisha watu.”

‘Aaishah alisema: “Kwa uhakika, Abu Bakr ana moyo laini na kila wakati hulia. “Mjumbe wa Allaah alisema: “Mwamuru Abu Bakr awaswalishe watu.” Alijibu, “Kwa hakika Abu Bakr ana moyo laini, na atakaposimama katika nafasi yako, watu hawatomsikia: Akaendelea kusema: “Muamuru Abu Bakr awaswalishe watu. Wewe ni sawa na mwanamke kwenye kisa cha Yuusuf.”

 

Kwa hiyo, mjumbe (aliyetumwa kuwasilisha amri ya Mjumbe wa Allaah kuwaongoza watu katika Swalah) alifika kwa Abu Bakr na kumfahamisha juu ya suala lile. Hivyo ‘Abu Bakr ndiye aliyewaswalisha watu wakati wa uhai wa Mtume.

 

Baadhi ya Wanachuoni wamehitimisha kuwa kuanzia wakati ule na tukio lile la Mjumbe wa Allaah alimpasisha Abu Bakr kuwa Khalifa, kwa kuwa kuwaswalisha watu ni jukumu la kwanza na muhimu kwa Khalifa.

 

Baada ya Mtume kufariki dunia Al-Answaar (Waungaji mkono watu wa Madiynah) walijumuika chini ya kivuli cha Banu Saa’idah na kusema: “Sa’d bin Ubaidah atapewa Ukhalifa.”

 

Al-Muhajirina (Waliohamia Madiynah kutoka Makkah) walipata habari za mkusanyiko wa kuchagua Khalifa, nao walikwenda kuhudhuria. Mmoja wa Answaar alitoa hutuba. ‘Umar bin Al-Khattwaab   alitaka kutoa hutuba, lakini Abu Bakr alimwashiria akae kimya, na alifanya hivyo. Abu Bakr alisimama na kuhutubia. Hakuzoza jambo juu ya mema ya Answaar.

 

Alisema:

“Mnafahamu ya kuwa Mjumbe wa Allaah alisema:

“Endapo watu wangechukua bonde maalumu, na Answaar wakachukua jengine. Ningechukua bonde la Answaar. Nilichosema kuhusiana nanyi ni maadili yenu mema. Lakini Waarabu hawakujua kadhia hii isipokuwa Ma-Quraysh kwa sababu wao ni bora kuliko Waarabu wengine kwa wema. Nimewachagua watu hawa wawili kwa ajili ya kiapo cha utii. Kwa hiyo kuleni kiapo cha utii.”

Aliushika mkono wa ‘Umar bin Al-Khatwab na Abu ‘Ubaydah bin Al-Jaraah

 

Abu Bakr alipomaliza hatuba yake, Answaar walipendekeza kuwa na Ma-amir wawili, mmoja kutoka ‘Answaar na mwingine kutoka Mahajirina.

 

‘Umar alisema: “Mnajua ya kuwa Mjumbe wa Allaah alimuamuru Abu Bakr awaswalishe watu? Wakasema, “Ndiyo, hapana shaka.” Kawaambia “Nani atapewa kipaumbele; mtu mwingine asiyekuwa yule aliyetangulizwa na Mtume ?  Wakajibu: “Hayupo: (hapana)”.

 

Abu Bakr alisimama na kumwambia ’Umar Nyoosha mikono yako ili tule kiapo cha kukukutii” Lakini ‘Umar alikataa, na mkono wa Abu Bakr ili kula kiapo cha kumtii. Usayd bin Hudayr na Bashir bin Sa’d alimpa ahadi ya utiifu Abu Bakr na watu wengine waliohudhuria walifanya hivyo pia. Kwa hiyo wote Answaar na Muhajirina walichukua ahadi ya kumtii Abu Bakr Siku iliyofuatia, watu walijumuika kwa ajili ya Swalah. Abu Bakr alipopanda juu ya mimbari, kila mtu alikula kiapo cha kumtii.

 

 

Khutbah Yake Baada ya Kiapo Cha Utiifu

 

 

Abu Bakr alipochaguliwa kuwa Khalifa, alipanda juu ya mimbari kutoa hotuba, na alipokuwa akifanya hivyo, alionyesha mwenendo mwema. Aliheshimiwa kama Swahaba mwenye cheo. Alionyesha heshima na kumcha Allaah.

 

Baada ya kumshukuru Allaah alisema:

“Enyi watu! Nimechaguliwa kuwa Khalifa, hata hivyo mimi sio bora kuliko nyie. Kwa hiyo, kama nikipatia katika hukumu, niungeni mkono; vinginevyo mna haki ya kunikosoa. Ukweli ni uaminifu, na kuongopa ni uasi. Wadhaifu miongoni mwenu watapata nguvu mpaka nitakapowapoka haki zao; ambao watu wenye nguvu miongoni mwenu ni dhaifu kwangu mpaka nitakapowapoka haki yao, Allaah akipenda. Msiache Jihaad (kupigana kwa ajili ya Allaah ). Hapana watu waliacha Jihaad bila kughadhibikiwa na Allaah Nitiini wakati namtii Allaah na Mjumbe Wake. Nikiwaasi, nami sina haki ya kutiiwa.”

 

Kisha aliwaamuru wasimame ili waswali kwa kusema: “Simameni kwa ajili ya Swalah, na Allaah Awanyeshee huruma zake.”

 

Abu Bakr alihofia sana majukumu makubwa aliyobeba kama Khalifa, Qays bin Abu Hazm alisema: Nilipokuwa nimekaa na Abu Bakr Khalifa wa Mjumbe wa Allaah mwezi mmoja baada ya kutawafu Mtume . Kuliadhiniwa na watu walijumuika. Ilikuwa mara ya kwanza kusomwa Adhaana. Abu Bakr alipanda kweye mimbari, na akamtukuza Allaah. Kisha akasema:

“Enyi watu natamani mtu mwingine angepewa haya madaraka. Kama mmenitaka nitawale kama alivyofanya Mtume wenu, itakuwa nje ya uwezo wangu kwa sababu yeye alikuwa amehifadhiwa, na muhimu Zaidi alikuwa akipokea wahyi.”

 

 

Vita Dhidi Ya Walioritadi

 

 

Baada ya kufariki dunia Mtume, makabila mengi ya Kiarabu katika sehemu nyingi waliritadi (walibadili imani) isipokuwa Kaskazini mwa Madiynah ambapo makabila yaliona jeshi la Usaamah walitanabahi kuwa kama Waislamu wasinge kuwa na nguvu wasingeweza kusonga mbele umbali ule dhidi ya jeshi kubwa kama Usaamah alivyofanya. Kwa Abu Bakr halikuwa na jambo la muhimu zaidi ya mantiki. Ulikuwa ni uamuzi wa Mtume, na kwa hiyo ilikuwa lazima uheshimiwe bila kujali matatizo au vikwazo. Maagizo yake yalikuwa “Nilitumaini mbele jeshi la Usaamah. Naapa kwa Allaah iwapo mbwa mwitu watanishambulia, sitosita kupeleka jeshi. Kwani sitobadilisha maamuzi yaliyofanywa na Mjumbe wa Allaah .

 

Wartadi walikuwa makundi mawili.

·         Kundi la kwanza liliritadi kwa hofu na waliwafuata Mitume wa uongo, kama vile Musaylimah, Tulayhah na kadhalika.

 

·         Kundi jengine halikuacha Uislamu na waliendelea kuamini ya kuwa: “Hapana apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah, na kuwa Muhammad ni mtumwa Wake na Mjumbe wake. Hata hivyo, walikataa kutoa Az-Zakaah. Mgogoro wa kundi hili ulipelekwa kusuluhishwa kwa Khalifa (Abu Bakr).

 

‘Umar bin Al-Khattwaab  alikuwa mmoja na Maswahaba walioitwa kusikiliza mgogoro.

Abu Bakr alipinga kwa nguvu zake zote, alisimama imara kama jabali.

Hakuogopa Lolote na wakati huo alitoa hutuba yake maarufu:

“WaLlaahi, kama waliniamini hatamu ya mnyama waliyokuwa wakimpa Mjumbe  wa Allaah , nitapigana mpaka waisalimishe,

‘Umar alimwambia:

“Unawapigaje ambapo Mtume alisema: “Nimeamrishwa (na Allaah) kuwapiga wale wanaopigana, mpaka waseme: La illaha illAllaah (hapana mwenye haki ya kuabudiwa ila Allaah ). Na yeyote aliyesema, ataokoa maisha yake na mali yake, kwa kutovunja shari’ah (haki na hali zitakazonifanya aadhibiwe kwa haki (bila uonevu), na hesabu yake itakuwa kwa Allaah ”

 

Abu Bakr alisema:

“WaLlaahi! Nitawapiga wale wanaotofautisha kati ya Swalah na Zakaah, kwa kuwa Zakaah ni haki ya lazima kuchukuliwa kutokana na mali (kwa mujibu wa Amri ya Allaah). WaLlaahi! Watakapokataa kunilipa hata ugwe waliokuwa wakitoa zama za Mjumbe wa Allaah, nitawapiga mpaka watoe walichozuia.”

    

Maswahaba wa Mtume walikuwa na rai kuwa Abu Bakr aamiliane na makafiri kwa upole, ‘Umar alikuwa mmoja wao. Alimwambia:

“Ewe Khalifa wa Mjumbe wa Allaah !  Kuna mpole na mwenye huruma kwa watu.”

 

Abu Bakr alikasirika na kumwambia:

“Nilitarajia msaada wako, lakini umeniacha mkono. Je, inafaa kuwa wakorofi katika siku za ujahili na dhaifu katika Uislamu? Wahyi umesimama, na sasa Dini imekamilika. Inahoofika wakati bado niko hai! Kama Mjumbe wa Allaah asingesema: Isipokuwa lile lililofaradhishwa.’ Kwa hali hiyo, tutasimamisha Swalah, na kuwalipa masikini haki yao. WaLlaahi, hata kama watu wote wasinisaidie, nitapigana nao peke yangu.” Wasaidizi wa waasi (murtadi) waliona uchache wa askari wa Kiislamu, Madiynah baada ya kutoka kwa jeshi la Usaamah. Hali hii iliwafanya washambulie.

 

Abu Bakr alikuwa amechukua tahadhari, hivyo aliwatuma baadhi ya Maswahaba kwa makabila yaliyokuwa jirani ambao wangeshambulia Madiynah, na makabila hayo yalipigwa.

 

Abu Bakr aliongeza jeshi lililokuwa na Answaar na Muhajirina mpaka alipofika Naq (kauli ya Najd). Wakazi wa jangwani walikimbia pamoja na watoto wao. Watu walimtaka Abu Bakr arejee Madiynah na ateue kamanda mpya wa jeshi. Alimteua Khalid bin Al-Waliyd na akamwambia:

         

“Watu watakaporejea kwenye Uislamu na wakalipa haki za masikini, iwapo mmoja wenu anataka kurejea na arejee.”

         

Abu Bakr alirejea Madiynah wakati jeshi la Usaamah lilikuwa limepata ushindi. Jeshi la Usaamah lilipopumzika, Abu Bakr alikusanya vikosi kumi na moja chini ya Khaalid bin Al-Waliyd, ‘Ikrimah bin Abu Jahl., ‘Amr bin Al-‘As, Sawayd bin Maqrin, Al-‘Ala Bin al-Haddramiy na wengineo.

 

 

Vita Vya Buzaakhah

         

Vita vya Buzaakhah vilikuwa vita maarufu dhidi ya makafiri. Abu Bakr alimuelekeza Khalid bin Al-Waliyd kupigana dhidi ya Mtume mwingine na bandia aliyeitwa Tulayhah bin Khuwaylid Al-Asadi.

         

Abu Bakr alimwamuru ‘Adiy bin Haatim aende Tay (kabla ya kumwamuru Khaalid bin Al-Waliyd Alimwamuru ‘Adiy aanzie Tay, kisha aelekee Buzaakhah na kisha Al-Batah. Aliambiwa hata kama alipata ushindi, hakutakiwa kuondoka mpaka apewe rukhsa na Abu Bakr Ki-istratejia, Abu Bakr alisema watoke na jeshi wakakabiliane na jeshi pinzani lililoongozwa na Khaalid bin Al-Waliyd kama njia ya kuwahofisha.

 

 

Vita Ya Al-Yamaamah

 

Al-Yamaamah ilikuwa nchi ya asili ya Banu Haniyfah iliyopo katikati ya Rasi ya Arabia, Kaskazini ya Najraan. Lilikuwa eneo lenye mimea mingi na mitende mingi na hapo ndipo Khaalid bin Al-Waliyd alipigana dhidi ya Musaylimah, mzandiki mkubwa. Musaylimah alikuwa miongoni mwa wasaidizi wa Banu Haniyfah ambao walikwenda kwa Mjumbe wa Allaah (mwaka wa makaimu). Aliporejea, alijidai kuwa mwenza wa Mjumbe na akawaongeza watu wake kwenye bid’ah na kuwaweka mbali na Uislamu.

         

Baada ya kifo cha Mtume , Abu Bakr alimtuma ‘Ikrimah bin Abi Jahl na kisha akamtuma Shurahbiyl bin Hasanah kupigana na Musaylimah, lakini Ikrimah alishindwa. Abu Bakr alimuelekeza Shurahbiyl kwa watu wa Oman, na alimwamuru akae mpaka Khaalid atakapoungana naye wampige Musaylimah kwa pamoja.

         

Jeshi la Waislamu lilipokabiliana na jeshi la Musaylimah, Zayd bin Al-Khattwaab alikuwa upande wa kulia kwa Khaalid na Abu Hadhayfah bin ‘Utbah alikuwa upande wa kushoto. Bendera la Answaar lilibebwa na Thaabit bin Qays bin Shammar bendera la Muhajirina lilibebwa na Saalim (mtumwa aliyeachwa huru na Abu Hadhayfah) Wafuasi wa Musaylimah walikuwa elfu kumi ambao walipigana kwa nguvu.   

 

Waislamu walipigana mpaka wakakaribia kushindwa. Baadhi ya Waislamu walihisi hatari ya kushindwa kutokana na ukubwa wa jeshi la adui, kwa hiyo wakapeana moyo kuwa imara katika mapambano. Thaabit bin Qays alisema:

“Ee Allaah! Nakanusha yale wayafanyayo (yaani watu wa Al-Yamaamah) na nakuomba msamaha kwa yote wayafanyayo (yaani Waislamu).

Kisha alimshambulia adui na kumuua. Zayd bin Al-Khattwaab alisema:

“WaLlaahi, sitozungumza tena mpaka nimshinde.” Vita iliendelea kuwa kali na Saalim, Abu Hudhayfah na Zayd bin Al-Khattwaab waliuawa.

 

Khaalid bin Al-Waliyd alitanabahi ya kuwa kusingekuwa na ushindi wa uhakika mpaka wamwue Musaylimah. Kwa hiyo alishambulia huku akipiga ukulele… Kila mtu aliyejitokeza aliuawa. Musaylimah na aliokuwa nao baada ya kuona hali ile walikimbilia bustanini. Al-Bara’ bin Maalik alisema:

“Enyi Waislamu! Nitupeni ndani ya bustani. Waislamu walisita kwa kumwogopa, lakini walifuata amri yake, na alitupwa ndani ya bustani mpaka akapigana vita kali Musaylimah aliuawa. ‘Wahshi (mtumwa aliyeachwa huru na Jubayr, aliyemuua Hamzah  ‘ami yake Mtume, siku ya Uhud) alimuua Musaylimah waliuawa kwa sababu jeshi la Waislamu lilikuwa imara. Allaah Aliwasaidia mpaka wakamshinda adui.

 

 

Ukusanyaji Wa Qur-aan Tukufu Kuwa Mus-haf Mmoja

         

Matokeo ya vita vilivyopiganwa kati makafiri na Waislamu, Maswahaba maarufu wa Mtume waliuawa. Miongoni mwao ni wale waaminifu waliohifadhi Qur-aan Takatifu. ‘Umar alichelea kuwa maandishi ya Qur-aan yangepotea kama vifo hivyo vingeendelea, na alimtaka Abu Bakr atoe amri ya kukusanywa kwa Qur-aan Tukufu ambako kutafanywa mara moja. Abu Bakr hakupenda kufanya jambo ambalo Mtume hakulifanya mwenyewe, lakini alijua ya kuwa ‘Umar alikuwa sahihi, vinginevyo Qur-aan ingeweza kupotea baada ya muda. Abu Bakr alikubaliana na fikra za ‘Umar hivyo alimuamuru Zayd bin Thaabit akusanye matini ya Qur-aan.

 

Alisimulia Zayd bin Thaabit (mwandishi wa Qur-aan Tukufu). “Abu Bakr As-Swiddiyq aliniita wakati watu wa Yamaamah walipouawa (yaani Maswahaba wengi wa Mtume waliopigana na Musaylimah). Nilikwenda kwake na nilimkuta ‘Umar bin Al-Khattwaab amekaa naye. Abu Bakr aliniambia, “‘Umar alikuja kwangu na kuniambia:

“Qur-aan wengi walifariki dunia (yaani waliohifadhi Qur-aan) siku ya vita ya Yamaamah na nachelea wengi wao wanaweza kuwa mashahidi katika vita vingine na sehemu kubwa ya Qur-aan hupotea. Kwa hiyo, nakushauri wewe (Abu Bakr) utoe amri Qur-aan ikusanywe.” Nilimwambia ‘Umar: ‘Unawezaje kufanya jambo ambalo Mjumbe wa Allaah hakulifanya?”  ‘Umar alijibu: ‘WaLlaahi, hili jambo zuri la kufanywa, “‘Umar aliendelea kunishawishi nikubali pendekezo lake mpaka Allaah Alipofungua kifua changu na kuanza kuona uzuri wa rai ya ‘Umar. “Kisha Abu Bakr aliniambia, “Wewe ni kijana mwerevu, na hatuna shaka nawe. Ulikuwa ukiandika Ufunuo Mtakatifu kwa kuongezwa na Mjumbe wa Allaah kwa hiyo tafuta maandiko ya Qur-aan na yakusanye yawe kitabu kimoja.”

 

WaLlaahi! Kama wangeniamuru kuhamisha moja ya milima, isingekuwa mizito katika ombi hili. Kisha nilimwambia Abu Bakr,” Utafanyaje jambo ambalo Mtume hakulifanya?” Abu Bakr  aliendelea kunishawishi nikubaliane na rai yake mpaka Allaah Alipofunua kifua changu kwa kile alichofunua kifua cha Abu Bakr na ‘Umar  Kwa hiyo nilianza kuitafuta Qur-aan na kuikusanya kutokana (na yale yaliyoandikiwa juu yake) makuti ya mtende, mawe meupe membamba na kutoka kwa watu waliojua kwa moyo, mpaka nilipoipata ayah ya mwisho ya Surat Al-Tawbah kwa Abi Khuzaimah Al-Answaari, na Aya hiyo niliikuta kwake tu. Aya yenyewe ni hii:

“Hakika amekwishakujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini ni mpole na mwenye huruma.

Basi wakigeuka, wewe sema: Allaah Ananitosheleza. Hapana mungu isipokuwa Yeye tu. Mimi namtegemea Yeye, na Yeye ndiye Mola Mlezi wa Kiti Kikuu cha Enzi.” (9: 128,129).

 

Muswada kamili na Qur-aan ulibaki kwa Abu Bakr mpaka alipofariki dunia, kisha akawa kwa ‘Umar mpaka alipofariki dunia, kisha kwa Hafswah, binti ya ‘Umar. (Al-Bukhaariy, Hadiyth Na. 4986).

 

Ilisimuliwa kwa mamlaka ya ‘Aliy:

“Malipo bora juu ya (ukusanyaji wa) Mushaf yamwendee Abu Bakr Alikuwa na mwanzo kurekodi Qur-aan Tukufu.”

 

 

Hadhi  Yake

 

Hapana shaka kuwa Abu Bakr alikuwa na hadhi ya kipekee miongoni mwa Maswahaba wa Mjumbe Kuna Hadiyth nyingi zinazothibitisha ya kuwa alikuwa anapendwa Zaidi na Mtume Kuna Hadiyth nyingi zinazothibitisha ya kuwa alikuwa anapendwa Zaidi na Mtume na alikuwa rafiki yake kabla na baada ya kutangaza Uislamu. Mtume hatosahau kuwa alikuwa wa mwanzo kusilimu. Maswahaba walijua hadhi yake kwa Mtume na walijua alivyotumia kwa ajili ya Dini. Ni kwa sababu hii walimheshimu sana na wakaweka hadhi yake kwenye ndimi na mioyo yao. Wakati wote alikumbukwa na kusemwa kwa heshima na uchaji wake. Alimpenda kwa sababu mbili. Ya kwanza, kwa sababu ya tabia yake kama vile ukarimu, wema, ukweli, msafi (asiye na dhambi kubwa) na kuwa wa kwanza katika Uislamu na ya pili mapenzi kwa Mtume

 

Amr bin Al-‘Aas alisema:

“Mtume alinitumia kamanda wa jeshi aliyeitwa Dhatus–Salaasil. Nilimwuliza: “Nani unayempenda zaidi? Akajibu, ‘Aaishah. Nikamwambia, ‘Katika wanaume’ Akajibu “Baba Yake.” Kisha nikasema: ‘Kisha nani? Akajibu: ‘‘Umar bin Al-Khattwaab . Kisha Mtume aliwataja wanaume wengine.”

           

Mtume katika Hadiyth nyingi anawafafanulia Maswahaba sababu ya kumpenda zaidi Abu Bakr. Msikilize asemavyo.

“Kwa uhakika Allaah alinituma kwenu. Mkaniambia: ‘Unasema uongo’, ambapo Abu Bakr (aliniamini na) akawambia watu, ‘Anasema kweli, na akanifariji.” Kisha alisema mara mbili, “Basi hamuachi kumdhuru mwenzangu?” Baada ya pale hapana aliye mdhuru Abu Bakr. (Al-Bukhaariy 2661.)

         

Shukrani za Mtume zinaweza kuonekana katika kauli yake:

“Abu Bakr amenipendelea kwa mali yake na usuhuba wake. Kama ningetakiwa kuwa na Khaliyl miongoni mwa binaadamu, bila shaka ningemchukua Abu Bakr lakini udugu wa Kiislamu na urafiki unatosha. Fungeni milango yote ya Msikiti isipokuwa ule wa Abu Bakr.” (Al Bukhaariy 3654.)

         

Kwa mamlaka ya ‘Abdullaah bin Shaqiyq ambaye alisema ya kuwa alimwambia ‘Aaishah:

“Nani kati ya Maswahaba wa Mjumbe wa Allaah alipendwa sana naye?” Alijibu, “Abu Bakr” Nilisema, “Kisha nani?” Alijibu “‘Umar” Nikasema “Kisha nani?” Alijibu, “Abu ‘Ubaydah” nilimwambia kisha nani?” Alinyamaza kimya. (Sunan At-Tirmidhiy 3657.)

 

Daraja ya Abu Bakr ilikuwa ya juu baada ya Mitume (kwa ubora).

“Alisimulia Ibn ‘Umar. Tulikuwa tukiwalinganisha watu kuona ni yupi bora wakati wa uhai wa Mjumbe wa Allaah Tulimwona Abu Bakr kuwa bora zaidi, kisha ‘Umar na kisha ‘Uthmaan ”

         

Inafahamika ya kuwa Mtume alipenda na kuchukia kwa ajili ya Allaah. Kwa hiyo mfahamu ya kuwa hadhi ya Abu Bakr ilipokuwa ya juu mbele ya Allaah kwa kuwa ilikuwa juu kwa Mtume

 

Mjumbe wa Allaah alisema:

“Kwa hakika watu wenye daraja la chini watawaona wale wenye daraja la juu kama muonavyo nyota zing’arazo upeo wa macho. Na kwa hakika, Abu Bakr na ‘Umar ni miongoni mwa hao.”

 

 

Imani  Naye

 

Kutokana na kuwa karibu na Mtume tunaona tabia ya Abu Bakr ilikuwa uaminifu wake, ukweli na kupenda haki. Alitegemewa kwa masuala ya sekula na Dini na aliamuru Abu Bakr aongoze Swalah alipokuwa mgonjwa sana. Watu wote walichukulia tukio hilo kuwa Abu Bakr atakuwa Khalifa, kwa kuwa kuswalisha watu ni jukumu la Khalifa. Hili linathibitishwa na maneno ya Mtume:

“Sijui nitakuwa nanyi kwa muda gani, kwa hiyo fuateni mwongozo wa watu wawili watakaochukua uongozi baada yangu”, na akamnyooshea kidole Abu Bakr na ‘Umar.” (At- Tirmidhiy 3664.)

         

Hivi Mjumbe wa Allaah anawaamuru watu wafuate uongozi wa mtu yeyote isipokuwa yule mwenye kuaminika.

         

‘Aaishah amesema kuwa Mtume alisema,

“Hainipitikii akilini ya kuwa mtu mwingine angekuwa Imaam katika Swalah, wakati Abu Bakr alikuwa miongoni mwao.”

 

Ibn ‘Abbaas alisimulia ya kuwa Mtume alisema:

“Kama ningetakiwa kuwa na Khalili, ningemchukua Abu Bakr, lakini yeye ni ndugu yangu na mwenzangu (katika Uislamu)” (Al-Bukhaariy).

 

Na Ayyuub alisimulia ya kuwa Mtume alisema,

“Kama ningetakiwa kumchagua Khalili, ningemchukua yeye (yaani Abu Bakr) kuwa Khalili, lakini udugu wa Kiislamu ni bora.” (Al-Bukhaariy).

 

Kuna Hadiyth nyingine inayothibitisha uaminifu huu. Jubayr bin Mut’im alisimulia.

         

Mwanamke alifika kwa Mjumbe wa Allaah na kuzungumza naye. Alimtaka aseme hoja yake, na alisema; “Nitafanya nini. Ewe Mjumbe na Allaah, nitakapokuja nikakukosa?” (kama alikuwa na maana, “Nikikuta umefariki dunia) Alimjibu “Usiponikuta, nenda kwa Abu Bakr.” (Al-Bukhaariy Hadiyth Na. 3659)

 

 

Uaminifu huu wa Mjumbe wa Allaah ulipenya nyoyo za Waislamu. Kutokana na hali hiyo watu wengi walikuta kigogo cha utii na akapata uungwaji mkono, na maazimio ambayo yaliathiri kwa kiasi kikubwa kukua kwa dola ya Kiislamu.

 

 

Share

06-Wasifu Wa Maswahaba Kumi Waliobashiriwa Pepo: ‘Umar Bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘Anhu) - 1

 

2. ‘Umar Bin Al-Khattwaab  (Radhiya Allaahu ‘Anhu) Aliyebashiriwa Pepo

 

 

Jina lake lilikuwa ‘Umar bin Al-Khattwaab bin Nufayl bin ‘Abdil-‘Uzza Qurayshiy Al-’Adawiy. Lakabu yake ilikuwa Abu Hafsw. Alikuwa na udugu na Mtume kwa kizazi chake cha nane.

Mama yake alikuwa Hantamah bint Haashim bin Al-Mughirah bin ‘Abdillaah bin ‘Umar bin Makhzuum na alikuwa binamu wa Abu Jahal.

 

 

Kuzaliwa Na Malezi Yake

 

 

Alizaliwa miaka mitatu baada ya mwaka wa ndovu, na alikuwa miongoni mwa Maquraysh wema. Alikuwa balozi wa Maquraysh. Kila ulipotokea ugomvi kati ya Maquraysh na makabila mengine, walikuwa wakimtuma ‘Umar kama Mjumbe (balozi) wao. Aidha walikuwa wakimtuma katika mikutano ya majigambo iliyokuwa ikifanyika katika zama za jahiliya.

         

‘Umar alipobaleghe, baba yake alimfunza kuchunga ngamia. Hii ilionekana amali nzuri lakini inayochosha. Al-Khattwaab alimfundisha mwanae kuvumilia ugumu uliotokana na kazi hiyo. Kila ‘Umar alipochoka na kutaka kupumzika, baba yake alimhimiza na kumtaka avumilie matatizo, na hivyo akamfunza kuwa mvumilivu. Sehemu ‘Umar aliyochungia wanyama wake iliitwa Daghnan.

         

Baada ya kuteuliwa kuwa Khalifah, mara moja alipita malishoni, na alisema. “Allaah Aliyetukuka, Inashangaza mabadiliko ya majaaliwa! Nilikuwa nikiwalisha wanyama wangu hapa, katika malisho haya huku nimevaa shati la sufu. Nilipochoka, baba akinipiga. Sasa mimi ni mtawala, na hapana aliye juu yangu isipokuwa Allaah.”

         

Katika ujana wake, alifanya shughuli zilizofanywa na Waarabu wa daraja la juu. Alishughulikia nasaba (kizazi), mieleka, kuendea khutbah rasmi na ubingwa wa kupanda farasi. Baadaye alikuwa bingwa na kutambua nasaba na mpiga mieleka asingeshindika. Alikuwa akishindana mieleka katika uwanja wa ‘Ukaaz.

         

Wakati huo huo alijifunza kusoma na kuandika, na alikuwa mmoja wa watu kumi na saba wa kabila la Quraysh walioweza kusoma na kuandika.

 

 

Umbile  Lake

 

‘Umar alikuwa na rangi nzuri ya uso, kipara, ndevu nyingi na alikuwa mrefu. Watu wanasema alipokuwa akitembea utadhani alipanda mnyama. Ndevu zake zilikuwa ndefu na mvi kwenye ncha zake.

 

 

Kurejea Kwenye Uislamu

 

Siku moja ‘Umar alichukua panga lake na kutoka nje. Alikutana na mtu wa Banu Zuhrah na kumwuliza: Unakwenda wapi ewe ‘Umar?”

Alijibu:

“Nakwenda kumuua Muhammad.”

Yule mtu akamuuliza:

“Unajihakikishiaje usalama kwa Banu Haashim na Banu Zuhrah utakapomuua?”

‘Umar alimwambia yule mtu:

“Nikuambie jambo litakalokufadhaisha Ewe ‘Umar! Dada yako na shemeji yako wamerejea katika Uislamu na wameitelekeza dini unayoiamini.”

‘Umar alikwenda moja kwa moja nyumbani kwa dada yake na akamkuta mwanaume Muhajirina. Jina lake Khabbaab. Khabbaab aliposikia sauti ya ‘Umar, alijificha ndani ya nyumba.

“‘Umar aliingia na kumkuta dada yake na mumewe, na alisema:

“Nimesikia nini ndani ya nyumba hii?” Walikuwa wakisoma Surah Twa-haa (Sura Na. 20 ya Qur-aan Tukufu). Walijibu.

“Hapana, tulikuwa tunazungumza tu.”

“Nina wasiwasi ya kuwa mmeacha dini yenu.” Mume wa dada yake (shemeji) alimwambia.”

“Je, Ungeweza kugundua ukweli kama dini ingelikuwa tofauti na yako?”

‘Umar alimpiga sana, dada yake alifika na kumsukuma ‘Umar ili asiendelee kumpiga mumewe. ‘Umar alimpiga sana dada yake mpaka akatoka damu usoni.

Dada yake ‘Umar alimwambia kaka yake kwa hasira:

“Huoni ya kuwa ukweli upo katika dini nyingine minghairi ya dini yako? Nakiri ya kwamba hapana mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Allaah, na ninakiri ya kwamba Muhammad ni Mjumbe na mtumwa Wake.”

 

‘Umar alisema:

“Nipe ulichonacho ili niweze kukisoma.” ‘Umar alikuwa anajua kusoma na kuandika. Dada yake alimwambia: “Wewe si twahara, na hutakiwi kukigusa, mpaka utakapotwharika. Wale waliotakaswa ndio wanaogusa Qur-aan. Nenda kaoge au katawadhe (Wudhuu).

Kwa hiyo alikwenda kupata Wudhuu, na kisha alianza kusoma mpaka alipofikia:

“Hakika Mimi ndiye Allaah. Hapana mungu ila Mimi tu. Basi niabudu Mimi, na usimamishe Swalah kwa ajili ya kunikumbuka Mimi.” (20: 14)[1]. [usahihi wa kisa hiki una mashaka, maelezo zaidi chini]

 

Kutokana na hayo ‘Umar alitambua ukweli. Alisisitiza kutangaza ukweli japokuwa Waislamu walikuwa dhaifu katika zama zile.

Ibn ’Umar alisema: ‘Umar aliporejea kwenye Uislamu (na kutangaza habari zile) aliuliza: “Nani aliyekuwa mbora wa kuwalingania watu?” Watu walijibu: “Jamiyl bin Ma’mar Al-Jumahi.”

 

Ibn ‘Umar  alisema:

“Kwa hiyo baba yangu alitoka nikamfuata. Nilikuwa mkubwa nakuelewa yaliyokuwa yakisemwa. ‘Umar alikutana na Jamiyl na kumwambia: “Lazima uwe na uwezo wa kupata habari za kusilimu kwangu.”

 

Jamiyl hakuchelewa. Alichukua joho lake na kutoka nje. “‘Umar na mimi tulimfuata ambapo Jamiyl alisimama katika mlango wa Al-Ka’bah na kupiga ukelele.

 

“Enyi Maquraysh! ‘Umar ameasi (ameacha dini ya mababu zake).”

‘Umar  alimwambia:

“Umesema uongo, lakini nimesilimu.” Baadhi ya Maquraysh walimshambulia ‘‘Umar  na walipigana naye mpaka akaanguka.

 

 

Al-Faaruuq

           

Mjumbe wa Allaah aliwapa majina maalum baadhi ya Maswahaba ili kuelezea baadhi ya mwenendo wao. Mathalan, AsaduLlaah (Simba wa Allaah) kwa Hamzah , SayfuLlaah (Upanga wa Allaah) kwa Khaalid bin Waliyd na Al-Faaruuq (mpambanuzi wa yaliyo sahihi na batili) kwa ‘Umar.

           

‘Umar  anasimulia kisa kinachohusu kupewa jina la Al-Faaruuq;

“Hamzah alirejea kwenye Uislamu siku tatu kabla yangu. Kisha, Allaah Aliufungua moyo wangu katika Uislamu. Baada ya kutamka shahada. Nilimwambia Mjumbe wa Allaah. “Hatuko kwenye ukweli ima tunaishi ama tunakufa?” Mjumbe wa Allaah alisema: “Ndiyo bila shaka, mko katika ukweli ima mko hai au mmekufa. “

‘Umar alisema: “Kwa nini tunajificha kama ndiyo hivyo? Kwa yule aliyekutuma na ukweli, lazima tutoke nje. Kwa hiyo tulitoka nje katika safu mbili. Hamzah aliiongoza moja na mimi niliongoza ya pili mpaka tukaingia Msikitini.”

‘Umar  aliendelea kusema.

“Maquraysh waliniangalia na wakamwangalia Hamzah, utusi utusi ulikuwa mbele yao. Mjumbe wa Allaah alinipa jina la Al-Faaruuq kuanzia pale.”

 

 

Kuhama  Kwake  (Kuhajiri)

 

 

Mateso ya makafiri yalipozidi sana, na njia za kuwatesa Waislamu zilipokuwa hazivumiliki baada ya kifo cha Abu Twaalib, ‘ami yake Mtume, Waislamu waliruhusiwa kuhajiri huku wakiacha nyuma mali zao Makkah na wakitarajia malipo na furaha ya mbele Siku ya Qiyaamah.

           

Kutokana na kuwaogopa makafiri, Waislamu walikuwa wakihama kwa siri. ‘Umar ndiye aliyekuwa mtu pekee ambaye hakumwogopa yoyote, na alihama bila kificho.

           

Ali bin Abi Twaalib  alisema:

“Sikumfahamu mtu aliyehama kwa dhahiri isipokuwa ‘Umar bin Al-Khattwaab. Alipokuwa tayari kuhama, alichomoa upanga wake, akachukua upinde mabegani mwake na akachukua mishale mkononi mwake. Alikwenda Al-Ka’bah ambapo alitufu na wakuu wa Kiquraysh walikuwepo. Kisha alikwenda Maqaam Ibraahiym, aliswali rakaa mbili kwa unyenyekevu mkubwa, na alisema:

“Nyuso hizi zitafedheheshwa. Yeyote anayetaka mama yake afikwe na msiba, basi anifuate nyuma ya milima ile.

‘Aliy  alisema:

“Watu wote dhaifu walimfuata, na aliwafundisha yale ambayo yangewasaidia, na wakaelekea Madinah.”

 

 

Kulingana  na  Qur-aan  Takatifu

 

 

Qur-aan Takatifu iliteremshwa na kufanana na fikra (utashi) wa ndani na ‘Umar , zaidi ya mara moja: Anas bin Maalik  alisimulia ya kuwa ‘Umar alisema:

“Allaah alijibu maombi (du’aa) yangu kuhusu mambo matatu: Maqaam Ibraahiym, Hijaab kwa mwanamke wa Kiislamu, na kuhusu mateka wa Vita vya Badr.”

 

Katika siku ya Badr, Allaah Aliwapa ushindi Waislamu dhidi ya makafiri, ambapo makafiri sabini waliuawa, na wengine sabini walichukuliwa mateka. Mtume alishauriana na Abu Bakr, ‘Umar na ‘Aliy juu ya mateka hao.

Abu Bakr alisema:

“Hao ni binamu zetu, ndugu zetu na jamaa zetu. Nashauri uchukue fidia kutoka kwao ili tujiimarishe zaidi ya hayo Allaah Aliyetukuka anaweza kuwaongoza na wakatuunga mkono.”.

Mtume alisema:

“Unaonaje? Ewe kijana wa Al-Khattwaab!”

‘Umar alisema:

“WaLlaah, naona kinyume cha anavyoona Abu Bakr. Nakuomba unipe fulani bin fulani (jamaa wa ‘Umar) ili nimkate shingo yake, ‘Aqiyl (kaka yake ‘Aliy) mpe ‘Aliy amkate shingo yake, na mpe Hamzah kaka yake (fulani bin fulani) amkate shingo yake. Allaah Anajua kuwa hatukuwa na huruma na makafiri. Na hao niliowataja ndio viongozi  na watukufu wao.”

 

Mjumbe wa Allaah alimili kwa rai ya Abu Bakr na akachukua fidia kutoka kwa mateka. Allaah Mtukufu Aliteremsha Aayah ifuatayo kuthibitisha rai ya ‘Umar.

“Haimfalii Nabii yeyote kuwa na mateka mpaka awe ameshinda baraabara katika nchi. Mnataka vitu vya dunia, na Allaah anataka Akhera. Na Allaah ni Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye hikima.” (8: 67)[2]

 

‘Umar bin Al-Khattwaab alisema:

“Ewe Mjumbe wa Allaah! Utaifanya Maqaam Ibraahiym kuwa sehemu ya Swalah.”

Allaah Mtukufu aliteremsha Aayah ifuatayo:

“Na kumbukeni tulipoifanya ile Nyumba (ya Al-Ka’abah) iwe pahala pa kukusanyikia watu na pahala pa amani. Na alipokuwa akisimama Ibraahiym pafanyeni pawe pa kuswalia. Na tuliagana na Ibraahiym na Ismaa’iyl: Itakaseni Nyumba yangu kwa ajili ya wanaoizunguka kwa kutufu na wanaojitenga huko kwa ibada, na wanaoinama na kusujudu.”(2: 125).

 

‘Umar bin Al-Khattwaab alisema:

“Pia nilisema: ‘Ewe Mjumbe wa Allaah! Watu wazuri na wabaya wamekuzuru! Utawaamrisha akina mama na Waumini wajisitiri (wavae Hijaab)! Kwa hayo Aayah Takatifu ya Al-Hijaab iliteremshwa.”[3]

 

Ilisimuliwa ya kuwa Qur-aan Takatifu ililingana (ilisadifu) na rai ya ‘Umar katika hali 21. Hii ni dalili ya wazi aliyoruzukiwa ‘Umar na Allaah. Mjumbe wa Allaah alisema:

“Bila shaka Allaah ameandika ukweli katika ulimi na moyo wa ‘Umar.”

Ibn ‘Umar alisema:

“Hapana jambo lililowafika watu nao pamoja na ‘Umar wakalizungumzia isipokuwa Qur-aan iliteremshwa kulingana na aliyoyasema ‘Umar.

 

 

Kuchaguliwa Kuwa Khalifa

 

 

Abu Bakr alipohisi ya kuwa kifo kilikuwa kikimjongelea, alishauriana na Maswahaba kuhusu atakayechukuwa uongozi baada yake. Aliwajua maswahaba wote na alimjua aliyefaa zaidi. Alijua ya kuwa ‘Umar alikuwa mkweli wa dhati, na alimjua ya kuwa anaheshimika, hivyo alimpendekeza kuwa Khalifa, lakini halikuwa jukumu lake kuamua. Kwa hiyo aliwaita Maswahaba kutaka ushauri. Aliwaambia:

“Ninakufa, kwa hiyo lazima tumchague Khalifa anayefaa.”

Maswahaba wakamwambia:

“Uamuzi ni wako.”

Abu Bakr  akaanza kushauriana na Maswahaba juu ya ‘Umar

‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf alisema:

“Yeye ni bora kuliko umdhaniavyo.”

 ‘Uthmaan alisema:

“Najua ya kuwa anachokificha ni bora kuliko anachokidhihirisha na hapana kati yetu aliye bora kuliko yeye.”

‘Aliy alisema:

“‘Umar ni kama ulivyomuelezea.” Usayd bn Hudayr alisema:

“Allaah Amuongeze awe mwema baada yako, kwani anachokificha ni bora kuliko anachodhirisha. Hapana anayeweza kumzidi katika suala hili.”

Mmoja wao alimwambia Abu Bakr:

Utamjibu nini Mola iwapo atakuuliza: Ulimteua vipi na ilhali ulimjua kuwa ni mkali?”

Abu Bakr alimjibu:

“Ningesema: Ee Allaah, Nimemteua mbora kuliko wote.” Kisha alimwamuru ‘Uthmaan aandike Agizo la kumteua ‘Umar kuwa Khalifa.

 

 

Mwenye Nguvu Na Muaminifu

             

Du’aa ya kwanza aliyoomba ‘Umar baada ya kuchaguliwa ni msaada na ulinzi kutoka kwa Allaah:

“Ee Allaah! Mimi ni mkali, naomba unifanye mpole. Mimi ni dhaifu hivyo nipe nguvu. Na mimi ni bakhili, nifanye mkarimu”.

         

Kwa kuwa alijua umuhimu wa Baytul Maal (hazina ya serikali) kwa mtawala kuidhibiti, alisema:

“Ee Allaah! Nimekuwa kama mlezi wa yatima. Nikiwa tajiri wa wastani. Sitochukua mshahara. Na ikiwa vinginevyo. Nitachukua kiasi cha kukidhi haja.”

         

Wakati fulani ‘Umar aliugua, alitakiwa kutumia asali kama dawa, na ilikuwepo chupa kubwa iliyojaa asali katika hazina ya dola (Baytul Maal). ‘Umar  alipanda juu ya mimbari na alisema:

“Mkiniruhusu nichukue nitafanya hivyo. Vinginevyo ni haramu kwangu.” (Walimruhusu).

‘Umar alikuwa mwangalifu katika utunzaji wa mali ya ummah kwa kuweka kumbukumbu sahihi.

         

Abu Bakr alisimulia ya kuwa aliingia kwa ‘Umar wakati wa kukusanya Zakaah siku ya jua kali, alimkuta ‘Uthmaan amekaa chini ya kivuli. Ali na ‘Umar  walikuwa wamesimama juani wakirekodi rangi na umri wa ngamia wa Zakaah. ‘Aliy alipomwambia ‘Uthmaan “Hajasikia msemo wa binti wa Shu’ayb akimweleza baba yake’;

“Akasema mmoja katika wale wanawake: Ewe baba yetu! Muajiri huyu. Hakika mbora wa kumuajiri ni mwenye nguvu na muaminifu.” (28: 26)?”

‘Aliy alimnyooshea kidole ‘Umar  alimwambia:

“Huyu ana nguvu na mwaminifu.”

 

‘Umar alipotaka kuwadhibu watu kwa jambo lolote, alianza na ‘ailah yake. Aliwakusanya na kuwambia:

“Watu wamewaangalia kama ndege wanaowinda wanavyowaangalia wanyama. WaLlaahi, iwapo nitamsikia mmoja wenu anafanya ninalotaka kulikataza, nitampa adhabu maradufu.”

 

Alikuwa akifuatilia hali za raia wake. Twalhah alimwona akiingia katika nyumba usiku wa kiza, na kisha akaingia nyumba nyingine. Asubuhi aliingia ndani ya nyumba na kumkuta ajuza kipofu asiyejiweza. Alimuuliza: “Una habari gani juu ya mtu anayekuzuru kila mara?” Alijibu: “Huwa ananitembelea kila mara kukidhi mahitaji yangu na kuniondolea machungu.”

         

Aliwahudumia raia zake wa Dola ya Kiislamu kutokana na kumcha Allaahna alikuwa akisema:

“Kwa jina la Yule aliye mtuma Muhammadkwa ukweli, iwapo ngamia aliibiwa katika Euphrates, nachelea Allaahasije akaitaka familia ya Al-Khattwaab kuwajibika kwa sababu hiyo.”

 

 

Mwasisi (Mtangulizi)

         

‘Umar alikuwa mwasisi wa mambo mengi:-

·         Alikuwa wa mwanzo kuitwa “Kiongozi wa Waumini” (Amiyrul–Muuminiyn) aliwambia: “Nyie ni waumini, na mimi ni Kiongozi.”

·         Kwa mara ya mwanzo, watu walimwita, “Khalifa wa Khalifa wa Mjumbe wa Allaah

·         ‘Umar alikuwa na mwanzo kufanya mwaka wa mwandamo kuwa kalenda rasmi ya Waislamu.

·         ‘Umar alikuwa wa mwanzo kuanzisha mfumo wa wizara za serikali ambapo mishahara na kumbukumbu za wafanyakazi wa dola na askari zilianzishwa. Pia alianzisha mfumo wa kuweka kumbukumbu za taarifa alizotuma kwa Magavana na wakuu wa nchi.

·         ‘Umar alikuwa na mwanzo kuunda jeshi la polisi ili kulinda usalama.

·         ‘Umar alikuwa wa mwanzo kuamuru sala ya Taraweeh kwa jamaa Msikitini.

·         ‘Umar alikuwa wa mwanzo kuwatia adabu watu waliokosea. Fimbo yake ilikuwa inatisha kuliko mapanga.

 

 

[1] Kisa hiki cha kurejea katika Uislamu kwa ‘Umar hakijachukuliwa kama Hadiyth Sahihi. Ilikusanywa na Al-Bayhaqiy katika Ad-Dalaail 3/219) na Ibn Sa’d klatika Al-Twabaqaat (23.267) na Al-Haakim katika Al-Mustadrak (4/95) kwa kupitia Is-haaq bin Yuusuf Al-Azraq, alisema:”Al-Qasim bin ‘Uthmaan alitusimulia kwa mamlaka ya Anas bin Maalik.”

Isnad hizi ni dhaifu. Udhaifu wake unatokana na Al-Qaasim bin ‘Uthmaan Al-Basr. Ad-Daaraqutniy anasema katika Sunan yake: “Hadiyth hii ni dhaifu.” Al-Haafidh anasema katika Al-Lisaan (4/542) kuwa Imam Al-Bukhaariy alisema. “Anayo Hadiyth ambayo haikuungwa mkono na wote” Adh-Dhwahaak anasema katika Miyzaan Al-l’tidaal (3/375) katika kitabu wasifu wake: “Alimsimulia Is-haaq Al-Azraq Hadiyth, na kisa cha kusilimu kwa ‘Umar kinaonekana kuwa dhaifu.

 

[2] Tafsir Ibn Kathiyr.

[3] Ar–Riyadh An-Nadim 2/287.

 

 

Share

07-Wasifu Wa Maswahaba Kumi Waliobashiriwa Pepo: 'Umar Bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu 'Anhu) - 2

 

Matendo ya Ibada

 

‘Umar aliyasabilia maisha yake yote kwa Allaah. Kauli yake na kukaa kimya kwake vilitawaliwa na utashi wa Allaah. Furaha na ghadhabu yake ikiwa ni pamoja na kuchukia kwake rushwa, ilikuwa imepunguzwa ukali chini ya mwongozo wa Uislamu, na hakuwa mkali na katili kwa yoyote. Dhamira yake za amali zake zilielekezwa kupata radhi ya Allaah, Muumba Wake. ‘Umar  alifikia daraja hii ya wema kutokana na subira na uthibiti katika uchaji Mungu.

 

Sa’iyd bin Al-Musayyib alisema:

    

“‘Umar alipendelea kuswali usiku wa manane.”[1].

“‘Umar akipenda kufanya amali zilizomkurubisha na Allaah”, Anas alisimulia.

 

Mjumbe wa Allaah aliwauliza  Maswahaba zake: “Nani anatarajia kufunga leo?” ‘Umar alijibu, “Mimi.” Mjumbe wa Allaah alisema: “Nani aliyesindikiza jeneza leo?” ‘Umar alijibu: “Mimi.”Alisema: “Pepo ni yako.”[2]

Hadithi hii inatajwa katika uadilifu wa Abu Bakr

 

 

Tabia Yake

 

Isipokuwa ‘Umar alikuwa na uhusiaho mzuri na Mtume kwa kuwa Mtume alimwoa binti yake Hafswah, na zaidi ya hayo alikuwa mtu wa ukoo mtukufu, na alikuwa Jemadari wa Waumini hakuwa na kiburi. Kinyume chake, ‘Umar alikuwa na staha. ‘Abdullaah bin ‘Abbaas alisimulia kisa kinachoonesha kuwa alikuwa hivyo na alisema”

 

Al-‘Abbaas alikuwa na mchirizi nyumbani kwake. Siku moja Al-‘Abbaas alichinja kuku wawili. Ilikuwa siku ya Ijumaa na ‘Umar alivaa kanzu mpya na alielekea Msikitini. Wakati akiwa njiani kuelekea Msikitini, maji yaliyochanganyika na damu ya kuku wale kutoka katika mchirizi yalichafua kanzu ya ‘Umar .

‘Umar aliamuru mchirizi ule ufukiwe. Kisha alirejea nyumbani kwake kubadilisha nguo na akawaswalisha watu.

 

Al-‘Abbaas alimwendea na kumwambia: “WaLlaahi, ulikuwepo alipouweka Mtume” ‘Umar alimwambia Al-‘Abbaas: “Nakutaka upande mgongoni  mwangu mpaka mchirizi utakaporejeshwa pahala alipouweka Mjumbe wa Allaah” Kwa hiyo Al-’Abbaas  alifanya hivyo.[3]

 

Hadiyth hii inaonesha kuwa alikuwa mwenye staha, na hakuwa mkorofi wala fedhuli. Inadhihirisha mapenzi ya dhati na kumheshimu Mtume.

 

Kuna Hadiyth nyingine inayoonesha tabia yake ya kati na kati. Alipokwenda Syria, askari walikutana naye amevaa kikoi, makobadhi na kilemba. Alipofika kwenye ardhi yenye maji maji, alishuka, na akashika makobadhi mkononi na akashika kichwa cha mnyama wake na kuvuka maji. Aliambiwa, “Ewe Jemadari wa Waumini! Inafaa kwa askari wa makasisi wa Syria kukutana nawe katika hali hiyo?” Alijibu:

 

“Kwa uhakika Allaah Ametutukuza kwa Uislamu. Kwa hiyo hatutatafuta utukufu kutoka sehemu nyingine.”[4]

 

Dalili nyingine ya unyofu wake ni pale alipokuja kwa ‘Aliy bin Abi Twaalib na alimwambia:

“Kwa nini hukutuma mtu aniite?”

‘Umar alijibu:

“Nawajibika zaidi kuja kwako.”

Siku moja, alipokuwa Khalifa alikuwa akibeba kiriba cha maji, aliulizwa:

“Moyo wangu unakuwa ukinishawishi, hivyo nataka kuuadibisha.”[5]

 

 

Kujinyima  Anasa

         

‘Umar alijulikana kwa bidii yake kwenye Dini. Twalhah bin ‘Ubaydullaah alisema:

“‘Umar hakututangulia kuingia katika Uislamu au katika kuhajiri, lakini alikuwa ameyapa nyongo maisha ya dunia, na alipenda maisha ya Akhera zaidi. Siku moja, Hafswah bintiye alimwambia:

 

“Ewe Jemadari wa Waumini.”Hapana madhara endapo utavaa nguo nzuri kuliko hizi na kula mlo kamili, kwa sababu Allaah Amekujaalia vya kutosha na zaidi.”

Alimwambia:

“Hukumbuki ya kuwa Mjumbe wa Allaah na Abu Bakr walivyokuwa wakiteseka?” Alianza kuwataja mpaka alipolia. Kisha alisema:

“WaLlaahi, nitashirikiana nao maisha magumu waliyokabiliana nayo mpaka nitakapoungana nao katika daraja za juu (bora).

Abu ‘Uthmaan alisema:

“Nilimwona ‘Umar akitupa Jamrah ilhali amevaa Izaar (kikoi) yenye kiraka.”[6]

Anas  alisema:

“Niliona viraka vinne katika shati la ‘Umar.”

‘Abdullaah bin ‘Aamir alisema:

“Tulitoka kwenda Hija na ‘Umar bin Al-Khattwaab, hatukusimika hema mpaka tuliporejea. Tulipotaka kupumzika, tulitandika mkeka, na tulitandaza shuka kwa ajili ya kivuli chini ya mti.”[7]

 

 

Kuwajali  Raia  Zake

 

‘Umar  alikuwa akijishughulisha sana na mambo ya raia zake. Alikuwa akiwakagua, aliwasaidia na akitatua matatizo yao. Mara nyingi akijichosha kwa kuwafikiria wengine. Kichocheo cha nguvu zake kilikuwa kwa ajili ya Akhera, na alisema:

“Iwapo nitalala mchana, raia zangu wanaweza kudhuriwa, na iwapo nitalala usiku naweza kukasirika.”

Siku moja, ‘Umar alikwenda sokoni na kijana wa kike alimfuata na kumwambia:

“Ewe Kamanda wa waumini! Mume wangu amefariki, na nina watoto wadogo. Nachelea waonaje wakapotea. Mimi ni binti ya Khifaf bin Ayman Al-Ghifaariy ambaye alikuwa pamoja na Mjumbe wa Allaah katika Al-Hudaybiyah.

Alimwambia:

“Karibu ndugu!”

Alipakia kwenye ngamia magunia makubwa mawili ya chakula na nguo. Alimpa yule mwanamke na kumwambia:

“Chukua, na Allaah Atakupa kingine kabla ya kumalizika hiki.”

Mwanaume aliyeshuhudia hilo alimwambia:

“Umempa kingi ewe Kamanda wa Waumini!” Alijibu:

“Nataraji uondokewe na mama yako. Namkumbuka baba yake na binamu yake walipokuwa wakiizingira ngome kwa muda mrefu mpaka Allaah Alipowapa ushindi, na tukachukua ngawira zake.

 

Siku moja kikundi cha wafanya biashara kilifika msikitini, ‘Umar alimwambia ‘Abdur-Rahmaan “uwalinde usiku wa leo.”

Waliwalinda usiku kucha huku wakimwomba Allaah awaruzuku. Usiku ule alisikia mtoto akilia na akafuatilia ile sauti ya kilio cha mtoto, alimkuta na mama yake. Alimwambia:

“Muogope Allaah, na umtendee wema mwanao.” Kisha alirejea 

mahala pake. Kabla ya kuingia alfajiri, alimsikia tena yule mtoto akilia, na akaenda kumwangalia:

 

“Je, mama si mama mwema? Huyu mtoto ana matatizo gani?”

Mama alijibu”

“Ewe mtumwa wa Allaah! Namlazimisha aache kunyonya lakini hataki.”

Akamwuliza sababu ya kufanya vile. Alisema, kwa sababu ‘Umar hatengi posho ila kwa walioacha ziwa.”

Alimwuliza:

“Mtoto ana umri gani?” Alijibu: “Miezi kadhaa.”

Alimwambia:

“Mapenzi yakafike. Usimwachishe kunyonya kwa lazima.” Aliswali Subhi, watu hawakuelewa kisomo chake wakati akiswali Subhi kutokana na kulia sana. Alipotoa At-Tasliym alisema:

“Ni jinsi gani ‘Umar anafadhaishwa! Ni watoto wangapi wameteseka au kufariki dunia?”

 

Kisha alimtaka mpiga mbiu atangaze kuwa ni marufuku kwa wanawake kuwaachisha ziwa watoto wao mapema. Akaamuru ya kuwa posho ilipwe kwa kila mtoto anayezaliwa, na akapeleka nakala ya shar’ah hiyo sehemu zote za dola.[8]

 

‘Usiku mmoja alipokuwa akivinjari, alisikia sauti za watoto waliokuwa wakilia, ‘Umar alijongelea nyumba ile na kusema:

“Ewe mjakazi wa Allaah! Watoto hawa wana shida  gani?”

 

Alijibu: “Wanalia kwa kuwa wana njaa.” ‘Alisema: “Je vipi chungu kilichopo  jikoni?”

 

Alijibu: “Ni chungu chenye maji ili watoto wadhani kuwa kimejaa samli, unga na tende. Nafanya hivi mpaka walale.”

 

‘‘Umar alikaa na kulia. Alikwenda kwenye ghala la chakula na akachukua gunia lenye unga, samli, tende, nguo na fedha na kulijaza pomoni.

 

Alimwambia Aslam (Mtunza ghala) ‘Nibebeshe mgongoni’ Aslam alijibu: “Hapana nitalibeba badala yako, Ewe Jemadari wa Waumini!”  (‘Umar) Alimwambia, “Yaani mama yako akukose Ninawajibika kwao Siku ya Qiyaamah.” Alibeba lile gunia na kulipeleka kwa yule mama. Alichanganya samli, tende na unga kisha akaanza kupika na baada ya kuiva aliwapakulia ili wale. Hakuondoka mpaka alipowaona watoto wakila na kucheza.

Alimwambia Askari:

“Unajua kwa nini sikuondoka mpaka walipokula?” Alijibu,”Hapana, Ewe Jemadari wa Waumini!” Alimwambia: “Nilipowaona wanalia, nilichukia sana na sikutaka kuondoka mpaka nipate utulivu.

 

 

Kubashiriwa  Pepo

 

Kuna Hadiyth nyingi zinazombashiria Pepo.

Ibn ‘Umar alisimulia, Mtume alimwona ‘Umar amevaa kanzu nyeupe na akamwambia”:

“Ni mpya au imefuliwa?”

Ibn  ‘Umar alisema:

“Sikusikia jibu la ‘Umar.”

Mtume alimwambia:

“Vaa nguo mpya, ishi kwa furaha na kufa ukiwa shahidi. Nakuombea Allaah Akupe utulivu wa macho hapa duniani na kesho Akhera.”

‘Umar  alisema:

“Na wewe pia, Ewe Mjumbe wa Allaah”

 

 Abu Muusa alisimulia:

Siku moja, nilikuwa pamoja na Mtume katika bustani ya Al-Madiynah, mtu mmoja alipobisha hodi. Mtume alisema:

“Mfungulie mlango na mpe bishara za Peponi.” Kwa hiyo nilimfungilia, kumbe alikuwa Abu Bakr, hivyo nikampa bishara za Peponi.

 

Mtu mwingine alikuja na kuomba ruhusa ya kuingia.

Mjumbe wa Allaah Alisema.

“Mfungulie mlango na mpe habari za kufurahisha za Peponi.”

Alikuwa ‘‘Umar. Nilimfungulia na nikampa habari njema za Peponi.

 

Kisha mtu wa tatu alikuja na kuomba rukhsa ya kuingia Mjumbe wa Allaah alikuwa ameegemea, alikaa amenyooka na alisema:

“Mfungulie mlango na mweleze mazuri ya Peponi kwa wema wake na mateso yatakayomfika.”

Alikuwa ‘‘Uthmaan na nilimfungulia mlango na nikambashiria Pepo, na nikamweleza aliyoyasema Mjumbe wa Allaah.

’Uthmaan alisema:

“Msaada unatakiwa kuombwa kwa Allaah Pekee.” (Al-Bukhaariy).

 

Katika masimulizi mengine Anas alisema, Abu Bakr, ‘Umar, ‘Uthmaan walipanda mlima wa Uhud. Mlima ulipotetemeka Mjumbe wa Allaah alisema:

“Tulia, Uhud, kwa sababu kuna Mtume, mkweli mmoja na mashahidi wawili juu yako.” (Al-Bukhaariy).

 

Mu’adh bin Jabal alisimulia: 

Kwa uhakika ‘Umar ni mmoja wa wakazi wa Mtume na aliwaelezea aliona nini kwenye ndoto zake, na wakati mwingine alipokuwa macho. Mjumbe wa Allaah alisema:

“Nilipokuwa Peponi niliona Qasri na niliuliza: “Ni la nani hili?” Nilijibiwa: ‘Ni kwa ajili ya ‘Umar bin Al-Khattwaab.”[9]

 

 

Baadhi ya Hadiyth za Mtume Kuhusiana Naye

 

Mtume alisema:

“Miongoni mwa ummah kabla yenu walikuwepo Muhaddathun (watu walipata ufunuo, japokuwa hawakuwa miongoni mwa Mitume. Na kama yupo mtu wa aina hiyo miongoni mwa wafuasi (ummah) wangu, ni ‘Umar.”[10]

 

Anas  alisimulia ya kuwa Mtume alimzungumzia Abu Bakr na ‘Umar .

“Hawa ndio mabwana wa watu wa Peponi miongoni mwa watu wa mwanzo na wa mwisho isipokuwa Mitume na Manabii (At-Tirmidhi).

Mtume alisema:

“Kuna mtu anayechukia uongo. Huyo ni ‘Umar bin Al-Khattwaab Mtume pia alisema:

 

Bila shaka, Allaah Aliwapa malaika watu wa ‘Arafah kwa ujumla, na akampa ‘Umar pekee.”

 

Aidha Mtume alisema:

“Hamtapata mateso endapo mtu huyu atakuwa miongoni mwenu (akimkusudia ‘Umar) ”[11]

 

Mtume alimwambia ‘Umar

“Naapa kwa Yule Ambaye roho yangu iko Mikononi Mwake, Shaytwaan akuonapo njiani, yeye huchukua njia nyingine tofauti na yako.”[12]

Mtume alisema:

“Aliyekuwa na shauku ya juu kwa Dini ya Allaah ni ‘Umar.”[13]

 

Mtume alisema:

“Kwa uhakika, Allaah Ameandika ukweli katika ulimi wa moyo wa ‘Umar.”

 

Baadhi ya kauli za Maswahaba kumhusu ‘Umar

 

Abu Bakr alisema:

“Hapana mtu kwenye uso wa dunia ninayempenda zaidi ya ‘Umar.”

 

Ibn ‘Umar alisema”

“Sijapata kumwona yeyote mighairi ya Mjumbe wa Allaah aliye mkali na mkarimu kuliko ‘Umar.”

 

Ibn Mas’uud alisema:

“Watu wema wanapotajwa, na ‘Umar hutajwa. Alikuwa na maarifa mengi juu ya Kitabu cha Allaah na Dini ya Allaah.”

 

Hudhayfah alisema:

“Sikumjua mtu aliyeogopa lawama za Allaah zaidi ya ‘Umar.”

 

 

Kufa Kwake Shahidi

 

‘Umar bin Al-Khattwaab aliuawa na Abu Lu-u lu-u ambaye alikuwa mtumwa wa Al-Mughiyrah bin Sh’bah alikuwa mateka wa vita.

Alikwenda kwa ‘Umar kulalamikia juu ya kodi kubwa hivyo, alimwambia: “Unacholipa si kikubwa.”

 

Aliondoka na ‘Umar Kisha alichukua jambia lenye ncha tatu na kulificha mpaka alfajiri ambapo ‘Umar angeamsha watu kwa ajili ya Swalah ya Subhi, na alimchoma mara tatu. Pigo moja lilikuwa chini ya kitovu ndilo lilosababisha kifo. Kisha aliwachoma watu kumi na mmoja baada ya ‘Umar kisha alijiua.

 

‘‘Uthmaan bin ‘Affaan alisema: “Nilikuwa mtu wa mwisho kusema na ‘Umar akiwa hai, nilimwona alipokuwa akiweka kichwa chake kwenye paja la mwanae, ‘Abdullaah, huku akimwambia, “Acha shavu langu liwe juu ya ardhi, na ‘Abdullaah alisema: Mapaja yangu na ardhi yote ni sawa.” Alimwambia: Liache shavu langu liwe juu ya ardhi. Mama yako awe mkiwa” Kisha nikamsikia akisema: “Ole wangu, na ole wenu yangu ikiwa Allaah hatonisamehe; mpaka roho yake ilipotolewa.”

 

‘Umar alimtuma mtoto wake, ‘Abdullaah kwa ‘Aaishah kumwomba idhini ya kumzika pembeni mwa Mtume na Abu Bakr. Alitoa rukhusa na alizikwa pembeni ya rafiki zake wawili akiwa na umri wa miaka 63. Alikuwa Khalifa wa miaka kumi, miezi minne na siku kadhaa.



[1] Swifatus –Safwah.

[2] Ar-Riyaadh An-Nadirah 2/364.

 

[3] Swifatus-Safwah  2/128

[4] Swifatus-Safwa, 2/380.

[5] Siyar A’laam An-Nubalaa.

[6] Usdul-Ghaabah

[7] Swifatus -Safwah 1/126.

 

[8] Swifatus –Safwah 1/126.

 

[9] Majma’ Az-ZawAaid  9/1446

[10] Al -Bukhaariy

[11] Ar-Riyadh An-Naadirah.

[12] Al-Bukhaariy

[13] At-Tirmidhiy, Hadiyth Na. 3790.

22 At-Trirmidhiy 5/607.

 

Share

08-Wasifu Wa Maswahaba Kumi Waliobashiriwa Pepo: 'Uthmaan Bin 'Affaan (Radhiya Allaahu 'Anhu) - 1

 

‘Uthmaan Bin ‘Affaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu) Ambaye Alibashiriwa Pepo

 

 

Jina Lake Na Ukoo Wake

 

Jina lake ni ‘Uthmaan bin ‘Affaan bin Abul-‘Aas bin Umayyah bin ‘Abdus Shams, alikuwa Mquraysh wa Bani Umayyah. Ukoo wake na ule wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) unakutana kwa ‘Abdu Manaaf

 

Alizaliwa katika mji wa Twaaif miaka sita baada ya mwaka wa Ndovu, sawa na 576 M Mama yake aliitwa Arwaa bint Kuraya bin Habiyb bin Abdus Shams, na bibi yake alikuwa Al-Baydha bint ‘Abdil-Muttwalib bin Haashim, shangazi wa Mjumbe wa Allaah.

 

 

Ukoo Wake

 

‘Uthmaan alipewa lakabu ya Abu ‘Abdillaah (Baba ‘Abdullaah) na Abu ‘Amr. ‘Abdullaah alikuwa mtoto kwa Ruqayyah bintiye Mjumbe wa Allaah. ‘Abdullaah alifariki dunia alipokuwa na umri wa miaka sita yaani, mwaka wa nne wa Hijriyyah.

 

Aidha ‘Uthmaan alipewa lakabu ya Dhun-Nurayn (mwenye nuru mbili) kwa sababu aliwaoa Ruqayyah na Umm Kulthuum mabinti wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alikuwa mtu pekee aliyeoa mabinti wawili wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Maumbile Yake

 

‘Uthmaan hakuwa mrefu wala mfupi, alikuwa mzuri wa sura na nywele rangi ya njano na ndevu nzito. Alikuwa na mifupa mikubwa na mabega mapana.

 

Alifahamika kwa ndevu zake za rangi ya njano, alikuwa na nywele nyingi na nywele nyuma ya masikio yake.

 

‘Abdullaah bin Hazm alisema:

“Nilimwona ‘Uthmaan. Sijawahi kumwona mwanaume au mwanamke mwenye sura nzuri kama yake.”[1]

 

 

Kurejea Katika Uislamu

 

Si jambo la kushangaza kuwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kurejea katika Uislamu. Alikuwa amemiliki kufanya vizuri, na kwa maumbile yake hakupenda jambo lililokusudiwa kushusha heshima ya mtu.

 

Alifahamika kwa hayaa zake, na alikuwa na sifa nzuri hata kabla ya kusilimu. Kila mara akihudhuria mikutano ya watu wa hadhi yake. Mara nyingi alikuwa akipatikana nyumbani kwa Abu Bakr As-Swiddiyq, pahala walipokuwa wakikutana watukufu wa Kiquraysh.

 

Abu Bakr alikuwa rafiki kwa watu wake kutokana na kujiweka na watu wa kawaida na utu wake. Alikuwa mtu mtukufu miongoni mwa Maquraysh, na alikuwa anajua miamala mibovu ya watu wake. Waheshimiwa na Kiquraysh wakienda kwake kwa haja mbali mbali. Alikuwa na ujuzi na mweledi wa mambo mengi, na alikuwa na lugha ya umbuji iliyowafanya watu wengi wamwamini. Abu Bakr aliwaalika katika Uislamu watu waminifu. ‘Uthmaan bin ‘Affaan alikuwa miongoni mwa wale walioalikwa na Abu Bakr kurejea katika Uislamu. Alimwambia:

“Ole wako, ‘Uthmaan! WaLlaahi, wewe ni mtu mwenye busara na mwerevu unayetofautisha haki na batili. Masanamu mnayoyaabudu ni mawe yasiyosikia, hayaoni wala hayana faida wala madhara!”

‘Uthmaan alisema”

“Ndiyo hasa. WaLlaahi, si chochote lakini ni kama ulivyosema.”

Abu Bakr alisema.

“Huyu Muhammad bin ‘Abdillaah, ambaye Allaah Alimtuma kuwa Mjumbe kwa binadamu wote. Je, ungependa kuja kumsikiliza?”

‘Uthmaan alijibu:

“Ndiyo, Ninataka.”

Walipokuwa katika hali hiyo, Mjumbe wa Allaah alifika akifuatana na ‘Aliy bin Abi Twaalib aliyekuwa amebeba kanzu. Abu Bakr alipomwona akija, alimsogeza karibu yake na kumnong’oneza kitu. Alikaa kitako na alimwambia ‘Uthmaan:

“Ewe ‘Uthmaan! Mjibu Allaah kuhusiana na Pepo Yake. Mimi ni Mjumbe wa Allaah kwako na Viumbe Wake.”

‘Uthmaan alisema:

“WaLlaahi baada ya kusikia maneno hayo, sikuweza kujizuia ila kurejea katika Uislamu, na nikatamka Shahada: “Nakiri kwa moyo ya kuwa hapana apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allaah, na kuwa Muhammad ni Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Mjumbe Wake.”

 

 

Kuhajiri Kwake

 

Mateso waliyofanyiwa Waislamu na makafiri wa Makkah yalitofautiana kulingana na hadhi ya mtu. Wanyonge kama vile; watumwa na watumwa walioachwa huru waliteswa sana. Makafiri walijitahidi kuwakashifu na kuwazuia kuukubali Uislamu. Hoja ya mbinu hiyo ilikuwa kuwashajiisha wadogo kuwa dhidi yao.

Ama watu watukufu, kama wale wa makabila yenye nguvu, machifu wa makabila yao walitekeleza jukumu hilo. Adhabu ilikuwa kupigwa au kuwekwa kizuizini.

 

‘Uthmaan aliporejea katika Uislamu, ‘ammi yake Al-Hakam bin Abil-‘Aasw bin Umayyah alimfunga mnyororo na kumwambia:

“Je unaitelekeza dini ya mababu zako na kufuata dini ya mzushi? WaLlaahi, sitokufungua mpaka utakapoacha dini uliyoingia.”

‘Uthmaan alijibu:

WaLlaahi sitoiacha wala kusogea inchi moja kutoka katika dini hiyo.”

Al Hakam alipoona anang’ang’ania katika dini yake, aliondoka.

 

Makafiri hawakuacha kuwatesa na kuwaadhibu Waislamu. Mjumbe wa Allaah alipoona yaliyokuwa yakiwasibu Waislamu, na kuwa hakuweza kuwatetea, aliwambia:

“Itakuwa vema kwenu kuhamia (kukimbilia) Ethiopia, kwa kuwa kuna Mfalme anayewatendea vizuri watu (raia) wake. Ni nchi ya ukweli, na nataraji Allaah Atawawezesha kwenda huko.”[2]

 

Baada ya maelezo hayo, Waislamu walikwenda Ethiopia wakikimbia mateso na wakikimbilia kwa Allaah pamoja na dini yao. Hawa walikuwa Waislamu wa mwanzo kuhama.

 

Juu ya kuhama kwa ‘Uthmaan na mkewe, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

“Allaah awe pamoja nao, kwa kuwa ‘Uthmaan alikuwa wa mwanzo kukimbilia kwa Allaah baada ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Luut.

 

 

Kubashiriwa Pepo na Ushahidi

 

Abu Muusa alisimulia.

Siku moja, nilikuwa nimekaa katika bustani na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Al-Madiynah, alipokuja mtu na kuomba ruhusa ya kuingia.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

“Mfungulie lango, na umbashirie Pepo.” Kwa hiyo nilimfungulia, alikuwa Abu Bakr, nilimbashiria Pepo. Mtu mwingine alikuja na kuomba ruhusa ya kuingia. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Mfungulie lango, na umbashirie Pepo.”Alikuwa ‘Umar. Nilimfungulia, na nikampa habari njema za Peponi. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ameegemea kisha akasimama wima na kusema:

“Mfungulie lango, na mbashirie Pepo na utukufu utakaomshukia.” Alikuwa ‘Uthmaan.  Nilimfungulia lango na nikampa habari njema za Peponi, na nikamwambia aliyodhukuru Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

’Uthmaan alisema; “Allaah pekee Ndiye Anayestahili kuombwa msaada.”[3]

 

Katika mapokezi mengine Anas alisema:

“Mjumbe wa Allaah, Abu Bakr, ‘Umar na ‘Uthmaan walipanda Mlima Uhud. Mlima ulipotetema, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

“Nyamaza (tulia) Ewe Uhud kwa sababu kuna Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), mkweli na Mashahidi wawili juu yako.”

 

Hadiyth ya tatu iliyosimuliwa na Sa’iyd bin Zayd inaeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:-

“Abu Bakr yumo Peponi. ‘Umar yumo Peponi. ‘Uthmaan yumo Peponi. ‘Aliy yumo Peponi. Twalhah yumo Peponi. Az-Zubayr yumo Peponi. ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf yumo Peponi, na Sa’d yumo Peponi.”

 

Sa’iyd  aliongezea kusema:

“Na kama utapenda nikutajie mwingine, Nitakutajia.” Kisha akajitaja.”[4]

 

 

Mwandishi wa  Wahyi

 

Zaidi ya sifa bainifu njema za ‘Uthmaan alikuwa mmoja wa waandishi wa wahyi. Alisimulia ‘Aaishah:

“Nilimwona Mjumbe wa Allaah akiegemeza paja lake kwa ‘Uthmaan, nilipokuwa nikimfuta jasho usoni mwake wahyi ulipokuwa ukimteremkia alimwambia ‘Uthmaan: “Ewe ‘Uthmaan andika, WaLlaahi, mja huyo ana hadhi mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wa Allaah, na Allaah Aliridhia kutukuzwa kwake!

 

Alisimulia Ja’far bin Muhammad kwa mamlaka ya baba yake”

“Kila Mjumbe wa Allaah alipokaa, Abu Bakr alikuwa kuliani kwake, ‘Umar alikaa kushotoni kwake na ‘Uthmaan alikaa mbele yake, kwa sababu alikuwa katibu myeka wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).”

 

 

Aliyekusanya Qur-aan Tukufu

 

Wakati wa kupeleka jeshi Armenia, kulikuwa na majeshi mawili ya Waislamu. Moja lilitoka Syria na jengine kutoka Iraaq. Hudhayfah bin Al-Yamaani alishiriki katika jeshi hilo na aligundua tofauti katika matamshi ya baadhi ya maneno katika Qur-aan.

 

Watu wa Kuufah walisoma Qur-aan kwa mujibu wa mapokezi ya ‘Abdullaah bin Mas’uud ambapo watu wa Syria walisoma kwa mujibu wa mapokezi ya Ubay bin Ka’b

 

Hudhayfah alichelea tofuati hizo, hivyo alikwenda kwa ‘Uthmaan Khaliyfah na kumwambia:

“Ewe Jemedari wa Waumini! Okoa hili taifa kabla hawajatofuatiana wao kwa wao juu ya Kitabu chao, kwa sababu Mayahudi na Wakristo walitofuatiana kuhusu vitabu vyao.”

 

‘Uthmaan alitoa khutbah ambapo alisema:

“Enyi watu! Miaka michache imepita tangu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amefariki dunia, na mwatofautiana kuhusu Qur-aan, nasema: “Haya ni masimulizi ya Ubay na yale ni masimulizi ya ‘Abdullaah, kwa hiyo miongoni mwao watasema” WaLlaahi, huzisoma vizuri Aayah kadhaa wa kadhaa. Kwa hiyo, nawaalika kila mmoja wenu kuileta, endapo mna sehemu ya Kitabu cha Allaah.”

 

Watu walileta vipande vya karatasi au vipande vya ngozi vilivyoandikwa juu yake mpaka akikusanya vya kutosha.

Kisha ‘Uthmaan aliwaita walioleta ngozi na vipande vya karatasi na alimwuliza kila mmoja”

“Je uliisikia hii kutoka kwa Mjumbe wa Allaah na je, alikusomea?”

Mtu alijibu: “Ndiyo” Baada ya kusema hayo, alisema, “Nani mwandishi mzuri?”

Walijibu “Sa’iyd bin Al-‘Aasw.”

‘Uthmaan alisema:

“Sa’iyd atoe Imla na Zayd aandike.”

Kwa ajili hiyo Misahafu iliandikwa na kugawanywa kwa watu.[5]

 

‘Uthmaan alimtuma Hafswah bint ‘Umar mkewe Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amletee hati iliyokunjwa inakiliwe kwenye Msahafu, kisha alirejeshewa.

Hati zilizokunjwa ziliandikwa wakati wa ukhalifa wa Abu Bakr baada ya vita ya Al-Yamamaah wakati Maswahaba wengi waliohifadhi Qur-aan walikufa shahidi.

 

Wakati huo ‘Umar alimwambia Abu Bakr, “Maswahaba wengi waliohifadhi Qur-aan waliuawa siku ya Al-Yamaamah, nachelea kusije kupotea kitu katika Qur-aan. Kwa hiyo nakutaka uamuru ukusanyaji wake.

 

Kwa matokeo hayo, Abu Bakr alimwambia Zayd bin Thaabit akusanye kutokana na ngozi, kutoka Al-Asab (matawi ya mtende yaliyoondolewa majani yake, ambapo sehemu ya Qur-aan iliandikwa juu yake na kutoka mioyo ya Ummah na Kiislamu. Zile hati zilizokusanywa alikuwa nazo Abu Bakr na kisha ‘Umar alipofariki dunia zilitunzwa na Hafswah bint ‘Umar. Kisha ‘Uthmaan alizichukua na alimwamuru Zayd bin Thaabit, Abdullaah bin Az-Zubayr, Sa’iyd bin Al-Aasw, ‘Abdur-Rahmaan bin Al-Haarith bin Hishaam azinakili katika Mus-haf.

Kwa hiyo ‘Uthmaan aliwapa maelekezo yafuatayo:-

“Endapo mtatofuatiana juu ya kitu chochote, kiandikeni kwa mujibu wa lugha ya Kiquraysh kwa sababu ilishushwa kwa lugha hiyo.”

 

Hivyo walifanya, baada ya kunakili hati zilizokunjwa (scrolls), ‘Uthmaan alizirejesha kwa Hafswah na kisha akapeleka nakala ya Msahafu kwa kila jimbo na aliamuru aina nyengine ya Mus-haf ichomwe moto. Ulimwengu wa Kiislamu unashukuru kwa kitendo hiki cha ‘Uthmaan.

 

Iwapo tungeorodhesha aliyofanya ‘Uthmaan katika njia ya Allaah tungeweza kutengeneza orodha kamili. Hapa inatosha kutaja matukio matatu ambayo ni ushahidi ulio wazi juu ya utoaji wake mkubwa kwa ajili ya Allaah.

 

 

Kutoa Katika Njia ya Allaah

 

Kuliandaa jeshi kwa Vita ya Taabuuk

Vita ya Taabuuk inaitwa ‘Vita ya majonzi baada ya kauli ya Allaah. (9:117).

 

“Allaah Amekwishapokea toba ya Nabii na Wahajiri na Ansari waliomfuata katika saa ya dhiki, pale baada ya kukaribia nyoyo za baadhi yao kugeuka. Basi akapokea toba yao, kwani hakika Yeye kwao wao ni Mpole na ni Mwenye kuwarehemu.” (9: 117)

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwataka watu kuelekea vitani na aliwafahamisha sehemu waliyokuwa wakienda ili wajiandae. Aliwanasihi watu wa Makkah na makabila ya Kiarabu kupigana na akawataka watu kutoa sadaka na akawataka watoe katika njia ya Allaah. Watu wengi waliitikia kwa kutoa mali nyingi kama sadaka.

 

Wa kwanza kutoa sadaka yake alikuwa Abu Bakr ambaye alitoa mali yake yote iliyofikia Dirham 4000.

’Umar alitoa nusu ya mali yake.

‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf alitoa wakia (ounce) 200 za dhahabu na fedha.

‘Aaswim bin ‘Adiy wasaqi 70 za tende.

‘Uthmaan alitoa zana kwa thuluthi ya jeshi (1/3), ngamia 950 na farasi 50.

Ibn Is-haaq alisema: “‘Uthmaan alitoa kiasi kikubwa kwa kulipa jeshi zana za kivita. Hapana aliyetoa zaidi yake katika njia hii. Alipeleka dinari elfu moja na kuziweka juu ya paja la Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “‘Uthmaan hawezi kudhuriwa na chochote kuanzia siku ya leo.” (At-Tirmidhiy).

 

 

Kisima cha Rumah

 

Kuna tukio jingine linaloonesha mapenzi ya hali ya juu na huruma huyu Swahaba.

Mali zote za dunia si chochote ikilinganishwa na alichoahidi na Allaah. Waja wake walitumia miongoni mwa alivyowapa.

Muhajirina walipofika Madiynah walipata matatizo ya ukosefu wa maji ya kutosha. Mtu mmoja katika Banu Ghifaar alikuwa na kisima kikiitwa ‘Rumah’ na akiuza kiriba kimoja cha maji kwa Mudd moja.”

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwuliza:

“Je unakiuza kwa chemchemi ya Peponi?” Yule mtu alijibu: “Ewe Mjumbe wa Allaah! Sina kitu zaidi ya hiki, siwezi kufanya hivyo.”

‘Uthmaan alipofahamishwa hilo, alikinunua kwa dirham 35,000 na alimwambia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) “Je mtapewa chemchemi Peponi, kama nitatoa Bishr kama ulivyofanya?” Mjumbe wa Allaah alisema: “Ndiyo.”

‘Uthmaan alimwambia: “Nimeshakinunua, na nawapa Waislamu.[6] Abu Hurayrah alisema; “‘Uthmaan alinunua Pepo mara mbili” Siku ya Rumah na ile “Siku ya Huzuni[7]

 

 

Upanuzi wa Msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

 

Siku moja watu walialikwa kuchangia ununuzi wa kipande cha ardhi kilichokuwa karibu na Msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili upanuliwe. Kama ada, ‘Uthmaan alikwenda kuinunua ile ardhi na iliunganishwa na Msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Qataadah alisimulia: Kulikuwa na ardhi jirani na Msikiti. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Nani atakinunua, na atapewa kingine Peponi.

 

 

Hayaa/Soni

 

‘Uthmaan alikuwa mwingi wa haya, na soni humfanya mtu awe mzuri, awe mwanaume au mwanamke. Na kwa ‘Uthmaan ndiyo iliyomfanya kuwa safi na mbali na mambo ambayo yangemchafulia sifa yake. Hayaa ilikuwa ni sifa yake kubwa hata hivyo alikuwa mtu mashuhuri pamoja na kuwa na soni.

 

Al-Hasan akielezea hayaa (soni) yake: “Angekuwa ndani ya nyumba na milango imefungwa na angekuwa anavua nguo ili kujimwagia maji mwilini. Soni ilimzuia kusimama wima.”[8]

 

Alikuwa na soni ya kipekee. ‘Uthmaan hakuwa na hayaa mbele ya watu tu bali alikuwa na hayaa hata kwa majini wasioonekana na Malaika ambao walikuwa wanaishi. Kwa hiyo alikuwa na soni iliyoenea kote. Anas alisimulia ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

“Mkarimu zaidi katika ummah wangu ni Abu Bakr. Mkali zaidi katika masuala ya dini ya Allaah ni ‘Umar. Na mwenye soni ya ukweli ni ‘Uthmaan.”[9]

 

Mtu mwenye soni kwa kawaida huchunga ulimi wake na ni mwenye bashasha, na anapozungumza huchagua maneno ili asimuudhi yeyote. Sifa hii inamfanya mtu aheshimiwe katika hivyo watu waliamiliana nao na ‘Uthmaan alikuwa mwenye uadilifu na staha.

‘Aishah alisema:

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ameegemea nyumba yake na miguu na mapaja yakiwa wazi.

Abu Bakr na ‘Umar waliomba rukhsa ya kuingia, na walipoingia, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alibaki katika hali ile ile. Waliteta na kisha ‘Uthmaan aliomba rukhsa ya kuingia. Papo hapo Mjumbe wa Allaah alikaa wima na kujifunika. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ‘Uthmaan waliteta. Alipotoka, nilimwuliza. “Ewe Mjumbe wa Allaah! Abu Bakr na ‘Umar waliingia, lakini hukukaa wima. Lakini alipoingia ‘Uthmaan ulikaa wima na kujifunika.” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimjibu: nisimwonee hayaa mtu anayeonewa hayaa na Malaika?”[10]

 



[1] Al-Mu’jam Al-Kabir

[2] As-Siyrah An-Nabawiyyah ya Ibn Hishaam

[3] Al-Bukhariy na Muslim

[4] ‘Usudul Ghaabah 3/580

[5] Imeripotiwa na Ibn ‘Asaakir

[6] Siyar A’laam An-Nubalaa’

[7] Al-Haakim 3/107 (Ni wazi kuwa maneno ya Abu Hurayrah hapana maana ya kuwa Mtume alikuwa akiuza Pepo kama ilivyofanywa na Makasisi wa kanisa la Roma (R.C.), ‘Uthmaan alistahili Pepo kutokana na ‘amali zake. Kutokana nazo, mbili zilitajwa na Abu Hurayrah kwa kununua kisima cha Rumah, tunathibitisha ya kuwa ‘Uthmaan alikuwa mtu mkarimu kwa niaba ya Waislamu, na hii, inadhihirisha ya kuwa Imani thabiti kwa Allaah. “Inasemwa ya kuwa yule asiyejali mambo ya Waislamu si miongoni mwao.”

 

[8] Musnad Ahmad 543

[9] Imeripotiwa na Ibn ‘Asaakir

[10] Muslim

Share

09-Wasifu Wa Maswahaba Kumi Waliobashiriwa Pepo: 'Uthmaan Bin 'Affaan (Radhiya Allaahu 'Anhu) - 2

 

Ukarimu Wake

 

Tumeona jinsi ambavyo ‘Uthmaan alivyokuwa tayari kutoa katika njia ya Allaah. ‘Uthmaan hakukoma hapa. Hakuwa kama mvua iliyonyesha katika muda mwafaka. Alifahamika kwa kusaidia masikini na yeyote aliyehitaji msaada wake. Imesimuliwa kwa mamlaka ya Ibn ‘Abbaas.

Ibn ‘‘Abbaas alisema:

 

Wafanya biashara walifika nyumbani kwa ‘Uthmaan na kubisha hodi. Alitoka nje na joho lake ametungika mabegani, aliwauliza, “Mna shida gani?” Walijibu. “Tumepata habari ya kuwa kuna msafara unakuja kwako, una ngano na vyakula.  Tuuzie ili tuweze kuwasaidia masikini wa Madiynah.” ‘Uthmaan aliwajibu. “Ingieni ndani nyote.” Waliingia na kushangaa. Kulikuwa na mizigo elfu moja iliyopakuliwa nyumbani kwa ‘Uthmaan. Aliwaambia,”Mtanilipa kiasi gani kama faida? Walijibu, “Kumi kwa kumi na mbili.“ Aliwambia, “Nimepewa zaidi.” Wakasema, ”Kumi kwa kumi na nne.” Akasema,”Nimepewa zaidi.”   Wakamwambia, “Kumi kwa kumi na tano.” Akasema, “Nimelipwa zaidi.” Wakamwambia, “Nani mwingine aliyekulipa zaidi? Wafanya biashara wote wa Madiynah tuko hapa?” Akasema. “Kila dirham nimelipwa, mara kumi. Je, mnanyongeza yoyote?” Wakajibu. “Hapana.” Akawaambia, ”Nyie ni mashahidi kuwa nimetoa sadaka kwa masikini wa Madiynah.”

 

 

Kujinyima Anasa za Dunia

 

‘Uthmaan alikuwa mfano wa mtu aliyejinyima anasa za dunia na mcha-Mungu. Aliishi maisha ya kawaida. Alikula chakula cha kawaida, na hakufanya israfu katika mavazi na kufuja mali. Alijua ya kuwa Allaah hakujishughulisha na umbile la nje la mtu bali umbile la ndani na nia yake.

 

‘Abdul-Malik bin Shaddad bin Al-Had alisema.       

“Nilimwona ‘Uthmaan Ijumaa moja juu ya mimbari amevaa nguo ya Aden isiyo na thamani zaidi ya dirham nne au tano na kilemba cha Kufi kitochotiwa dai.[1]

Pamoja na kuwa alikuwa Khalifa alilala mchana Msikitini juu ya changarawe.

 

Al-Hasan aliulizwa juu ya wale wanaolala mchana Msikitini. Alijibu, ”Nilimwona ‘Uthmaan bin ‘Affaan akilala mchana Msikitini. Alikuwa Khalifa wa Waislamu wakati huo. Alipoamka kutoka usigizini alikuwa na alama za kokoto kwenye ngozi yake. Watu walisema,”Huyu ni jemadari wa Waislamu. Huyu ni jemadari wa Waislamu.”

                                                                                             

Kwa hiyo, tunaona ya kuwa kujirahisisha na kuipa nyongo dunia ilikuwa hali yake ya kawaida. Aidha alipanda mnyama wa kawaida sio farasi dume.

Imeelezwa kwa mamlaka ya Maymuun bin Mahran:

“Al-Hamdaan aliniambia ya kuwa alimwona ‘Uthmaan akipanda farasi jike na mtumwa wake alipanda nyuma yake.”[2]

 

 

Kujitambua

 

Alikuwa mcha-Mungu na akiogopa Siku ya Malipo.

Kwa mamlaka ya Hani, mtumwa aliyemwacha huru:

“Kila ‘Uthmaan aliposimama mbele ya kaburi, alilia mpaka ndevu zake zikalowa. Aliiogopa Siku ya malipo kwa sababu ni siku ambayo hapana ‘amali zitakazofanywa na kumbukumbu zitakuwa zimefungwa.”

‘Uthmaan alikuwa akisema:

“Kama ningekuwa kati ya Pepo na Moto bila kujua nitaamuriwa kwenda wapi, ningechagua kufanywa jivu kabla ya kujua nitaamriwa kwenda wapi.[3]

 

Abul-Fusayt alisema:

“Siku moja, ‘Uthmaan alimwambia mtumwa wake, “Kwa hakika, mara moja nilikufinya sikio lako, hivyo lipiza kisasi.”Kisha akamwambia yule mtumwa, “Nifinye kwa nguvu kwa kulipiza hapa duniani kunavumilika ya Akhera hayavumiliki.”[4]

         

Kujitambua kwake kulimzuia kusimulia Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Japokuwa alikuwa mtu wa karibu sana. Alikuwa mume wa mabinti mawili wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Ruqayyah na Ummu Kulthum. ‘Amr bin Sa’ad bin Abi Waqqaas alisema ya kuwa alimsikia ‘Uthmaan akisema, “Kinachonizuia kusimulia Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kuogopa kuwa sikuwa msikivu. Nilisikia Hadiyth isemayo: “Yeyote anayezua neno, na akalihusisha nami, atapata makazi yake Motoni.”[5]

 

 

Ukhalifa

 

Baada ya ‘Umar kuchomwa kisu, aliambiwa: “Teua (mrithi) Ewe Jemadari wa Waumini!” ‘Umar alijibu. “Hapana wanaostahiki zaidi katika suala hili kundi hili la watu aliowafia. Aliwataja majina; ‘Aliy,

‘Uthmaan, Az-Zubayr, Twalhah, Sa’ad na ‘Abdu-Rahman.”

Aliendelea kusema: ‘Abdullaah bin ‘Umar (mwanae) awe shahidi (katika uchaguzi) nazingatia ya kuwa hahusiki na kadhia hii.”

 

Lile kundi lililochaguliwa walimchagua ‘Uthmaan kuwa Jemadari wa Waumini na mrithi wa ‘Umar.

 

 

Ushindi Katika Utawala Wake

 

Vita nyingi zilipiganwa na kupatikana ushindi katika sehemu zote, baharini na nchi kavu. Ushindi huo ulidumu kwa miaka kumi mpaka uliposimamishwa na Al-Fitnah (zahama).

 

Maadui wa Uislamu kwa makusudi kabisa waliendelea kufanya fujo na kusita kutekwa na mipaka yao kuingizwa katika ardhi ya Waislamu na majaribio mengi yalisitishwa.

 

Kabla ya kipindi cha ‘Uthmaan, Waislamu waliteka majimbo mengi na kuongeza maeneo mazuri katika dola ya Kiislamu. Waislamu hawakuweza kuacha idadi kubwa ya wanajeshi katika miji na sehemu walizozifungua kwani Waislamu wakati huo walikuwa ni wachache.

 

‘Umar alipouawa, wakazi wa majimbo ya jirani walidhani Waislamu wamekuwa dhaifu. Walidhani sasa ulikuwa muda mwafaka kuanzisha mashambulizi. Walivunja mikataba waliokubaliana na Waislamu, na ‘Uthmaan kama Khalifa, alipambana nao kwa nguvu. Alikusanya majeshi chini ya makamanda wazoefu, na jeshi lilimudu kuleta utulivu kwa mara ya pili huko Persia (Iran), Khurasan, Babul Al-Abwaab, Afrika na Armenia.

 

‘Uthmaan hakufanikiwa kuwashinda maadui tu bali aliongeza ardhi mpya katika dola ya Kiislamu baada ya kushinda vita nyingi.

 

Nchi zifuatazo ziliongezwa katika dola ya Kiislamu.

1.     Katika Afrika, eneo la kuanzia Tripoli mpaka Algeria.

2.     Cyprus (Kuprus) katika Maditerranean.

3.     Mashariki ya Uturuki.

4.     Armenia, na kaskazini mwa Daghustan.

5.     Kapol, na Sind.

 

Vita hivi havikuwa rahisi. Vilikuwa vikali kama ilikuwa baharini au nchi kavu. Inatosha kutaja mfano mmoja tu.

Vita inaitwa Dhatus-Sawari (vita ya mlingoti uliosimikwa). Constantina, mtoto wa Hercules akiwa kamanda katika mwaka wa 31 wa Hijriyah, akitarajia kulipiza kisasi kwa Waislamu, walimshinda katika Afrika. Waislamu wengi waliuawa. Makafiri wasio na idadi pia waliuawa, lakini siku hiyo Waislamu walikuwa na uvumilivu usio na kikomo, na Allaah Aliteremsha ushindi kwa Waislamu.         

 

 

Ustawi wa Jamii Wakati wa Utawala Wake

 

Dola ya Kiislamu ilipanuka sana enzi za Ukhalifa wa ‘Uthmaan Zama zake zilikuwa za ustawi wa jamii na wingi na mali; watu wake walifurahia maisha mazuri na anasa. Muhammad bin Sina alisema”

“Utajiri (mali) uliongezeka wakati wa utawala wa ‘Uthmaan. Mjakazi aliweza kuuzwa kwa kupimwa kwa fedha, farasi kwa dirhamu laki moja na mtende kwa dirham elfu moja.

Al-Hasan alisema: “Chakula kilikuwa kingi wakati wa Ukhalifa wa ‘Uthmaan.”[6]

 

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Akimsifu Wakati Wote.

 

‘Uthmaan alikuwa mwenza wa kudumu wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ingekuwaje kinyume chake? Alikuwa mume wa Ruqayyah na kisha Umm Kulthum baada ya kifo cha Ruqayyah. Alikuwa Swahaba mcha-Mungu na mwenye soni na alipendwa sana na kuwavutia watu wengi. Vipi isingekuwa hivyo, ambapo alitumia mali zake nyingi katika njia ya Allaahambapo hapana aliyekuwa sawa naye katika hili.

 

Kama uthibitisho wa mapenzi hayo, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimwombea sana ‘Uthmaan kwa Allaah kwa du’aa:

”Allaah Akusamehe Ewe ‘Uthmaan kwa yale uliyoyatenda, utakayoyatenda na utakayoyaficha, uliyoyadhihirisha, na yale yatakayokuwepo mpaka Siku ya Hukumu.”

 

Anas alisimulia ya kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema,

“Mtu mkarimu zaidi katika ummah wangu kwa ummah wangu ni ‘Abu Bakr, Mkali zaidi katika Dini ya Allaah ni ‘Umar na mwenye soni ya kweli ni ‘Uthmaan.”

 

Aidha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimzungumzia kwa ‘Aaishah.

“Hutaki nione haya mbele ya mtu anayeonewa haya na malaika?”

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliendelea kusema: “Ewe Allaah!  Nimeridhishwa na ‘Uthmaan na nakusihi uwe radhi naye pia.”[7]

Na pia alisema,

“‘Uthmaan ni mwenye soni zaidi na mkarimu zaidi katika ummah wangu.”[8]

Na pia alisema:

“Mwenye haya zaidi katika ummah wangu ni ‘Uthmaan.”[9]

 

 

Rai za Maswahaba Kuhusiana Naye

 

Kuna masimulizi sahihi kuwa wakati ‘Abu Bakr akimsomea wasia wake ‘Uthmaan kuhusu mrithi wake, alitaja jina la ‘Umar kuwa khalifa wa kumrithi, kisha Abu Bakr alipoteza fahamu.

‘Uthmaan aliandika: “Umar”. Abu Bakr alipozinduka, aliuliza: “Kumeandikwa nini?” ‘Uthmaan alisema: “Umar” Abu Bakr alisema,”Utukufu kwa Allaah ambaye ameutawala mja wake.”

 

Mutarrifu alimsifu ya kuwa alikutana na ‘Aliy ambaye alimwambia: “Ewe Abu ‘Abdullaah!  Kitu gani kilichokuchelewesha? Ni mapenzi kwa ‘Uthmaan? Iwapo unakubali niliyosema (kuhusu kumpenda ‘Uthmaan), utakuwa sahihi kwa sababu alikuwa na shauku ya kuwaunganisha jamaa zake, na anamwogopa sana Allaah[10]

 

Ibn ‘Umar aliripoti, “Wakati wa uhai wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tuliwataka watu wachague kati ya Abu Bakr, ‘Umar na ‘Uthmaan, na watu walimchagua Abu Bakr, ‘Umar na kisha ‘Uthmaan.[11]

 

Ibn Sirin alisema:

“Aliyekuwa na elimu zaidi juu ya ibada za Hijjah alikuwa ‘Uthmaan na kisha Ibn ‘Umar.[12]

 

‘Uthmaan alipochaguliwa kuwa Khalifa, Ibn Mas’uud alisema”

“Tumemchagua mbora wa wote walio hai, na hatukufanya hiyana.”

 

‘Abdullaah bin ‘Umar alisema:

“Wanaume watatu wa Kiquraysh ni wenye sura nzuri zaidi, wenye mwenendo mwema na wenye soni zaidi (sana) Wanapokuambia kitu, basi ni kweli Na ukizungumza nao, hawatokudanganya. Watu hao ni: Abu Bakr, ‘Uthmaan bin ‘Affaan na Abu ‘Ubaydah bin Al-Jarraah.”[13]

 

Masruuq alikutana na Al-Ashtar na kumwambia, “Umemwua ‘Uthmaan?”  Alijibu, “Ndiyo” “WaLlaahi, umemuua na wakati wote alikuwa anafunga na kuswali.”

 

 

Kufa Shahidi

 

Maadui wa ‘Uthmaan walieneza uvumi wa uongo ili watu wawe dhidi yake. Walimshutumu kwa kuwapendelea jamaa zake na kuwa aliwapa vyeo katika ofisi za dola badala ya Maswahaba wengine wa Mjumbe wa Allaah. Walitumia fursa ya hali ya uvumilivu wa ‘Uthmaan na kufululiza kujaribu kuwaridhisha raia wake badala ya kuwa mkali kwao.

‘Abdullaah bin Saba alikuwa mstari wa mbele katika hujuma hii.

 

Kikundi kilitoka Misri kilikwenda kwa ‘Uthmaan huko Madiynah wakimlalamikia Amir wao, ‘Abdullaah bin Sa’da bin Abi Sarh. Aliwapokea na akakubaliana nao kuwa Amir atauzuliwa. Alipofikisha ushauri wao wakamteua Muhammad bin Abi Bakr na akatoa agizo kuhusiana na hilo. Walianza safari ya kurejea kwao Misri. Njiani walimwona kijana aliyepanda farasi huku akimpiga sana. Walimwuliza, kulikoni? Yule kijana aliwajibu:

“Mimi ni tarishi wa Kamanda wa Waumini, amenituma niende kwa Amir wa Misri.”

 

Walipofika walikuta barua (iliyoghushiwa) kutoka kwa ‘Uthmaan kwenda kwa ‘Abdullaah bin Sa’d bin Abi Sarh ikisema:

“ Iwapo fulani na fulani watakuja kwako,  waue kwa kughushi,  puuza barua yao, na endelea na madaraka yako mpaka taarifa nyingine itakapokufikia.”

 

Lile kundi lilihamanika na kurejea Madiynah walipomhoji ‘Uthmaan aliapa kwa jina la Allaah kuwa hakuandika barua ile. Baadaye ilithibitika kuwa Marwaan ndiye aliyeghushi barua ile. Walipomtaka ‘Uthmaan awakabidhi Marwaan, alikataa kwa kuchelea kuwa wangemuua.

Lile kundi likasema”

“Ama tupatie Marwaan au jiuzulu Ukhalifa.”

 

‘Uthmaan alikataa, hivyo walimzingira na kutaka kumuua. ‘Aliy aliwatuma watoto wake wawili Hasan na Husayn ili wamlinde. Az-Zubayr alimtuma mtoto wake ‘Abdullaah, Twalhah na Maswahaba wengine wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pia walituma watoto wao kwa lengo hilo hilo, lakini maasi walipanda ukuta wa nyumba. ‘Uthmaan alikuwa akisoma Qur-aan aliyoipenda sana. Alipokuwa akisoma kimya na unyenyekevu, walimuua. Alikufa na Mus-haf mikononi.

 

Aliuawa tarehe 18 Dhul –Hijjah, mwaka wa 35 H, na alizikwa Al-Baqi’i. Alikuwa na umri wa miaka 82.

 

 



[1] Hilyat Awliya’ 1/60

[2] Hilyat Awliya’

[3] Hilyat Awliya’

[4] Ar-Riyaadh An-Naadirah.

[5] At-Taariykh Al-Kabiyr 2191

[6] Ar-Riyaadh An-Naadirah

[7] Muslim

[8] Muslim

[9] Hilyat Awliyaa’

[10] Swifatus-Safwah.

[11] Al-Bukhaariy 2655

[12] Imeripotiwa na Ibn ‘Asakir

[13] Hilyat Awliyaa’ 1/57

Share