017 - Al-Israa

 

 

الإِسْرَاء

 

017-Al-Israa

 

017-Al-Israa: Utangulizi Wa Suwrah

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ لِنُرِيَهُ مِنْ آيَاتِنَا ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ ﴿١﴾

1. Utakasifu ni wa Ambaye Amemsafirisha usiku Mja Wake kutoka Al-Masjid Al-Haraam mpaka Al-Masjid Al-Aqswaa ambao Tumebariki pembezoni mwake, ili Tumuonyeshe baadhi ya Aayaat (Ishara) Zetu (kubwa mno)[1] Hakika Yeye (Allaah) Ni Mwenye Kusikia yote, Mwenye Kuona yote.

 

 

 

وَآتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ وَجَعَلْنَاهُ هُدًى لِّبَنِي إِسْرَائِيلَ أَلَّا تَتَّخِذُوا مِن دُونِي وَكِيلًا ﴿٢﴾

2. Na Tumempa Muwsaa Kitabu na Tukakifanya mwongozo kwa wana wa Israaiyl kwamba: Msimfanye yeyote badala Yangu kuwa ni mtegemewa.

 

 

 

ذُرِّيَّةَ مَنْ حَمَلْنَا مَعَ نُوحٍ ۚ إِنَّهُ كَانَ عَبْدًا شَكُورًا ﴿٣﴾

3. Enyi kizazi cha ambao Tuliwabeba pamoja na Nuwh (katika jahazi). Hakika yeye alikuwa mja mwingi wa shukurani.  

 

 

 

وَقَضَيْنَا إِلَىٰ بَنِي إِسْرَائِيلَ فِي الْكِتَابِ لَتُفْسِدُنَّ فِي الْأَرْضِ مَرَّتَيْنِ وَلَتَعْلُنَّ عُلُوًّا كَبِيرًا ﴿٤﴾

4. Na Tuliwajulisha wana wa Israaiyl katika Kitabu kwamba: Bila shaka mtafanya ufisadi katika ardhi mara mbili, na kwa hakika mtapanda kiburi cha dhulma na kutakabari kukubwa.

 

 

 

فَإِذَا جَاءَ وَعْدُ أُولَاهُمَا بَعَثْنَا عَلَيْكُمْ عِبَادًا لَّنَا أُولِي بَأْسٍ شَدِيدٍ فَجَاسُوا خِلَالَ الدِّيَارِ ۚ وَكَانَ وَعْدًا مَّفْعُولًا ﴿٥﴾

5. Basi utakapowadia wakati wa mara ya kwanza yao (fisadi mbili) Tutakutumieni Waja Wetu wenye nguvu kali za kupigana vita, waingie kusaka nyumba kwa nyumba.[2]  Na hii ni ahadi, lazima itekelezwe.

 

 

 

ثُمَّ رَدَدْنَا لَكُمُ الْكَرَّةَ عَلَيْهِمْ وَأَمْدَدْنَاكُم بِأَمْوَالٍ وَبَنِينَ وَجَعَلْنَاكُمْ أَكْثَرَ نَفِيرًا ﴿٦﴾

6. Kisha Tukakurudishieni nguvu zenu dhidi yao, na Tukakuongezeeni mali na wana, na Tukakufanyeni wengi zaidi kwa idadi na nguvu.

 

 

 

إِنْ أَحْسَنتُمْ أَحْسَنتُمْ لِأَنفُسِكُمْ ۖ وَإِنْ أَسَأْتُمْ فَلَهَا ۚ فَإِذَا جَاءَ وَعْدُ الْآخِرَةِ لِيَسُوءُوا وُجُوهَكُمْ وَلِيَدْخُلُوا الْمَسْجِدَ كَمَا دَخَلُوهُ أَوَّلَ مَرَّةٍ وَلِيُتَبِّرُوا مَا عَلَوْا تَتْبِيرًا ﴿٧﴾

7. (Na Tukasema): Mkifanya ihsaan basi mnanjifanyia ihsaan kwa ajili ya nafsi zenu wenyewe, na mkifanya uovu, basi hasara ni juu yake. Na utakapowadia wakati wa mara ya pili, (Tutakutumieni tena maadui) ili wadhalilishe nyuso zenu, na ili waingie Msikitini (Bayt Al-Maqdis) kama walivyouingia mara ya kwanza, na ili wateketeze kila walichokiteka kwa mateketezo makubwa.

 

 

 

عَسَىٰ رَبُّكُمْ أَن يَرْحَمَكُمْ ۚ وَإِنْ عُدتُّمْ عُدْنَا ۘ وَجَعَلْنَا جَهَنَّمَ لِلْكَافِرِينَ حَصِيرًا ﴿٨﴾

8. Asaa Rabb wenu Akakurehemuni. Na mkirudi (kwenye ufisadi na dhulma), Nasi Tutarudi (kukuadhibuni). Na Tumeifanya Jahannam kwa makafiri kuwa ni gereza.

 

 

 

إِنَّ هَـٰذَا الْقُرْآنَ يَهْدِي لِلَّتِي هِيَ أَقْوَمُ وَيُبَشِّرُ الْمُؤْمِنِينَ الَّذِينَ يَعْمَلُونَ الصَّالِحَاتِ أَنَّ لَهُمْ أَجْرًا كَبِيرًا ﴿٩﴾

9. Hakika hii Qur-aan inaongoza katika yaliyonyooka kabisa,[3] na inawabashiria Waumini wanaotenda mema kwamba watapata ujira mkubwa.

 

 

 

وَأَنَّ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ أَعْتَدْنَا لَهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا ﴿١٠﴾

10. Na kwamba wale wasioamini Aakhirah Tumewaandalia adhabu iumizayo. 

 

 

 

وَيَدْعُ الْإِنسَانُ بِالشَّرِّ دُعَاءَهُ بِالْخَيْرِ ۖ وَكَانَ الْإِنسَانُ عَجُولًا ﴿١١﴾

11. Na binaadam huomba shari kama vile aombavyo kheri. Na binaadam ni mwenye pupa mno.

 

 

 

وَجَعَلْنَا اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ آيَتَيْنِ ۖ فَمَحَوْنَا آيَةَ اللَّيْلِ وَجَعَلْنَا آيَةَ النَّهَارِ مُبْصِرَةً لِّتَبْتَغُوا فَضْلًا مِّن رَّبِّكُمْ وَلِتَعْلَمُوا عَدَدَ السِّنِينَ وَالْحِسَابَ ۚ وَكُلَّ شَيْءٍ فَصَّلْنَاهُ تَفْصِيلًا ﴿١٢﴾

12. Na Tumejaalia usiku na mchana kuwa ni Aayah (Ishara, Alama) mbili. Tukafuta Aayah ya usiku na Tukajaalia Aayah ya mchana kuwa ni ya mwangaza ili mtafute Fadhila kutoka kwa Rabb wenu, na ili mjue idadi ya miaka na hesabu (nyinginezo). Na kila kitu Tumekifasili tafsili ya waziwazi kabisa.

 

 

 

وَكُلَّ إِنسَانٍ أَلْزَمْنَاهُ طَائِرَهُ فِي عُنُقِهِ ۖ وَنُخْرِجُ لَهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ كِتَابًا يَلْقَاهُ مَنشُورًا ﴿١٣﴾

13. Na kila binaadam Tumemuambatanishia amali zake alizokadariwa (kuzitenda) shingoni mwake. Na Tutamtolea Siku ya Qiyaamah kitabu akikute kimekunjuliwa.[4]

 

 

 

اقْرَأْ كِتَابَكَ كَفَىٰ بِنَفْسِكَ الْيَوْمَ عَلَيْكَ حَسِيبًا ﴿١٤﴾

14. (Ataambiwa): Soma kitabu chako! Nafsi yako inakutosheleza leo kukuhesabu.[5]

 

 

 

مَّنِ اهْتَدَىٰ فَإِنَّمَا يَهْتَدِي لِنَفْسِهِ ۖ وَمَن ضَلَّ فَإِنَّمَا يَضِلُّ عَلَيْهَا ۚ وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ ۗ وَمَا كُنَّا مُعَذِّبِينَ حَتَّىٰ نَبْعَثَ رَسُولًا ﴿١٥﴾

15. Anayehidika, basi anahidika kwa manufaa ya nafsi yake. Na anayepotoka, basi anapotoka kwa hasara yake. Na wala mbebaji (wa dhambi) hatobeba mzigo wa mwengine. Na Hatukuwa Wenye Kuadhibu mpaka Tupeleke Rasuli.

 

 

 

وَإِذَا أَرَدْنَا أَن نُّهْلِكَ قَرْيَةً أَمَرْنَا مُتْرَفِيهَا فَفَسَقُوا فِيهَا فَحَقَّ عَلَيْهَا الْقَوْلُ فَدَمَّرْنَاهَا تَدْمِيرًا ﴿١٦﴾

16. Na Tunapotaka kuangamiza mji, Tunawaamrisha wastareheshwa wake wa anasa za dunia, nao wakaendelea kufanya ufasiki humo, na hapo ikastahiki juu yake kauli (ya adhabu), kisha hapo Tunaudamirisha kwa mateketezo makubwa.

 

 

 

وَكَمْ أَهْلَكْنَا مِنَ الْقُرُونِ مِن بَعْدِ نُوحٍ ۗ وَكَفَىٰ بِرَبِّكَ بِذُنُوبِ عِبَادِهِ خَبِيرًا بَصِيرًا ﴿١٧﴾

17. Ni nyumati nyingi sana Tumeziangamiza baada ya Nuwh. Na Rabb wako Anatosheleza kabisa Kuwa Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri, Mwenye Kuona dhambi za Waja Wake. 

 

 

 

مَّن كَانَ يُرِيدُ الْعَاجِلَةَ عَجَّلْنَا لَهُ فِيهَا مَا نَشَاءُ لِمَن نُّرِيدُ ثُمَّ جَعَلْنَا لَهُ جَهَنَّمَ يَصْلَاهَا مَذْمُومًا مَّدْحُورًا ﴿١٨﴾

18. Yeyote anayetaka (starehe za dunia) ipitayo upesi upesi Tunamharakizia humo Tuyatakayo, kwa Tumtakaye. Kisha Tutamjaalia Jahannam aingie na kuungua hali ya kuwa mwenye kushutumiwa na kufukuziliwa mbali. 

 

 

 

وَمَنْ أَرَادَ الْآخِرَةَ وَسَعَىٰ لَهَا سَعْيَهَا وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَأُولَـٰئِكَ كَانَ سَعْيُهُم مَّشْكُورًا ﴿١٩﴾

19. Na anayetaka Aakhirah na akaifanyia juhudi inayostahiki kufanyiwa, naye ni Muumin, basi hao juhudi zao ni za kushukuriwa.[6]

 

 

 

 

كُلًّا نُّمِدُّ هَـٰؤُلَاءِ وَهَـٰؤُلَاءِ مِنْ عَطَاءِ رَبِّكَ ۚ وَمَا كَانَ عَطَاءُ رَبِّكَ مَحْظُورًا ﴿٢٠﴾

20.  Wote hao Tunawakunjulia - hawa na hao - katika Hiba za Rabb wako. Na hazikuwa Hiba za Rabb wako zenye kuzuiliwa.

 

 

 

انظُرْ كَيْفَ فَضَّلْنَا بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ ۚ وَلَلْآخِرَةُ أَكْبَرُ دَرَجَاتٍ وَأَكْبَرُ تَفْضِيلًا ﴿٢١﴾

21. Tazama vipi Tulivyowafadhilisha baadhi yao juu ya wengineo. Na bila shaka Aakhirah ni yenye daraja kubwa zaidi na fadhila kubwa zaidi.

 

 

 

لَّا تَجْعَلْ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ فَتَقْعُدَ مَذْمُومًا مَّخْذُولًا ﴿٢٢﴾

22. Usifanye pamoja na Allaah mwabudiwa mwengine, ukaja kushutumiwa na kutelekezwa mbali (motoni).[7]

 

 

 

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۚ إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُل لَّهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا ﴿٢٣﴾

23. Na Rabb wako Ameamuru kwamba: Msiabudu isipokuwa Yeye Pekee na kuwafanyia ihsaan wazazi wawili.[8] Kama mmoja wao akifikia uzee naye yuko pamoja nawe, au wote wawili basi usiwaambie, Uff![9] Na wala usiwakemee, na waambie maneno ya heshima.

 

 

 

وَاخْفِضْ لَهُمَا جَنَاحَ الذُّلِّ مِنَ الرَّحْمَةِ وَقُل رَّبِّ ارْحَمْهُمَا كَمَا رَبَّيَانِي صَغِيرًا ﴿٢٤﴾

24. Na wainamishie bawa la unyenyekevu kwa huruma, na useme: Rabb wangu! Warehemu kama walivyonilea udogoni.

 

 

 

رَّبُّكُمْ أَعْلَمُ بِمَا فِي نُفُوسِكُمْ ۚ إِن تَكُونُوا صَالِحِينَ فَإِنَّهُ كَانَ لِلْأَوَّابِينَ غَفُورًا ﴿٢٥﴾

25. Rabb wenu Anajua zaidi yaliyomo katika nafsi zenu. Mkiwa ni Swalihina basi hakika Yeye daima Ni Mwingi wa Kughufuria wenye kutubia kila mara Kwake.

 

 

 

وَآتِ ذَا الْقُرْبَىٰ حَقَّهُ وَالْمِسْكِينَ وَابْنَ السَّبِيلِ وَلَا تُبَذِّرْ تَبْذِيرًا ﴿٢٦﴾

26. Na mpe jamaa wa karibu haki yake, na masikini, na msafiri (aliyeharibikiwa), na wala usifanye ubadhirifu[10] wa ufujaji mkubwa. 

 

 

 

إِنَّ الْمُبَذِّرِينَ كَانُوا إِخْوَانَ الشَّيَاطِينِ ۖ وَكَانَ الشَّيْطَانُ لِرَبِّهِ كَفُورًا ﴿٢٧﴾

27. Hakika wabadhirifu wamekuwa ni ndugu wa mashaytwaan, na shaytwaan amekuwa ni mwingi wa kumkufuru Rabb wake.

 

 

 

وَإِمَّا تُعْرِضَنَّ عَنْهُمُ ابْتِغَاءَ رَحْمَةٍ مِّن رَّبِّكَ تَرْجُوهَا فَقُل لَّهُمْ قَوْلًا مَّيْسُورًا ﴿٢٨﴾

28. Na kama unajikurupusha nao na huku unatafuta Rehma ya Rabb wako unayoitaraji, basi sema nao kauli laini.

 

 

 

وَلَا تَجْعَلْ يَدَكَ مَغْلُولَةً إِلَىٰ عُنُقِكَ وَلَا تَبْسُطْهَا كُلَّ الْبَسْطِ فَتَقْعُدَ مَلُومًا مَّحْسُورًا ﴿٢٩﴾

29. Na wala usifanye mkono wako kama uliofungwa shingoni mwako (ubakhili), na wala usiukunjue wote kabisa (kwa israfu) ukaja kubakia mwenye kulaumiwa, mwenye kufilisika.

 

 

 

إِنَّ رَبَّكَ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ وَيَقْدِرُ ۚ إِنَّهُ كَانَ بِعِبَادِهِ خَبِيرًا بَصِيرًا ﴿٣٠﴾

30. Hakika Rabb wako Anamkunjulia riziki Amtakaye na Humkadiria kwa kipimo (Amtakaye). Hakika Yeye daima kwa Waja Wake Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na za siri, Mwenye Kuona yote.

 

 

 

 

وَلَا تَقْتُلُوا أَوْلَادَكُمْ خَشْيَةَ إِمْلَاقٍ ۖ نَّحْنُ نَرْزُقُهُمْ وَإِيَّاكُمْ ۚ إِنَّ قَتْلَهُمْ كَانَ خِطْئًا كَبِيرًا ﴿٣١﴾

31. Na wala msiue watoto wenu kwa kukhofia ufukara. Sisi Tunawaruzuku wao na nyinyi. Hakika kuwaua imekuwa ni hatia kubwa.

 

 

 

وَلَا تَقْرَبُوا الزِّنَىٰ ۖ إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاءَ سَبِيلًا ﴿٣٢﴾

32. Na wala msiikaribie zinaa. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya kabisa.

 

 

 

وَلَا تَقْتُلُوا النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّـهُ إِلَّا بِالْحَقِّ ۗ وَمَن قُتِلَ مَظْلُومًا فَقَدْ جَعَلْنَا لِوَلِيِّهِ سُلْطَانًا فَلَا يُسْرِف فِّي الْقَتْلِ ۖ إِنَّهُ كَانَ مَنصُورًا ﴿٣٣﴾

33. Na wala msiue nafsi ambayo Allaah Ameiharamisha (kuiua) isipokuwa kwa haki. Na atakayeuliwa kwa kudhulumiwa, basi Tumemfanya mrithi wake awe na mamlaka.  Lakini asipindukie mipaka katika kuua. Hakika yeye atasaidiwa (kwa sharia).

 

 

 

وَلَا تَقْرَبُوا مَالَ الْيَتِيمِ إِلَّا بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ حَتَّىٰ يَبْلُغَ أَشُدَّهُ ۚ وَأَوْفُوا بِالْعَهْدِ ۖ إِنَّ الْعَهْدَ كَانَ مَسْئُولًا ﴿٣٤﴾

34. Na wala msiikaribie mali ya yatima isipokuwa kwa njia ya ihsaan mpaka afikie umri wa kupevuka. Na timizeni ahadi, hakika ahadi itakuwa ni ya kuulizwa.

 

 

 

وَأَوْفُوا الْكَيْلَ إِذَا كِلْتُمْ وَزِنُوا بِالْقِسْطَاسِ الْمُسْتَقِيمِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا ﴿٣٥﴾

35. Na timizeni kamilifu kipimo mnapopima, na pimeni kwa kipimo cha sawasawa. Hivyo ni kheri na bora zaidi matokeo yake.

 

 

 

وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ ۚ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَـٰئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْئُولًا ﴿٣٦﴾

36. Na wala usifuate usiyo na ilimu nayo. Hakika masikio na macho na moyo; vyote hivyo vitaulizwa.

 

 

 

وَلَا تَمْشِ فِي الْأَرْضِ مَرَحًا ۖ إِنَّكَ لَن تَخْرِقَ الْأَرْضَ وَلَن تَبْلُغَ الْجِبَالَ طُولًا ﴿٣٧﴾

37. Na wala usitembee katika ardhi kwa majivuno. Hakika wewe huwezi kupasua ardhi, na wala huwezi kufikia urefu wa milima.

 

 

 

كُلُّ ذَٰلِكَ كَانَ سَيِّئُهُ عِندَ رَبِّكَ مَكْرُوهًا ﴿٣٨﴾

38. Yote hayo, uovu wake umekuwa ni wa kukirihisha mbele ya Rabb wako.

 

 

 

ذَٰلِكَ مِمَّا أَوْحَىٰ إِلَيْكَ رَبُّكَ مِنَ الْحِكْمَةِ ۗ وَلَا تَجْعَلْ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ فَتُلْقَىٰ فِي جَهَنَّمَ مَلُومًا مَّدْحُورًا ﴿٣٩﴾

39. Hayo ni miongoni mwa hikmah ambayo Amekufunulia Wahy Rabb wako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Na wala usifanye pamoja na Allaah mwabudiwa mwengine ukaja kutupwa katika Jahannam hali ya kuwa mwenye kulaumiwa na kufukuziliwa mbali. 

 

 

 

أَفَأَصْفَاكُمْ رَبُّكُم بِالْبَنِينَ وَاتَّخَذَ مِنَ الْمَلَائِكَةِ إِنَاثًا ۚ إِنَّكُمْ لَتَقُولُونَ قَوْلًا عَظِيمًا ﴿٤٠﴾

40. Je, Rabb wenu Amekukhitarieni watoto wa kiume na Yeye Amejichukulia Malaika watoto wa kike? Hakika nyinyi mnasema kauli nzito mno![11]

 

 

 

وَلَقَدْ صَرَّفْنَا فِي هَـٰذَا الْقُرْآنِ لِيَذَّكَّرُوا وَمَا يَزِيدُهُمْ إِلَّا نُفُورًا ﴿٤١﴾

41. Na kwa yakini Tumesarifu namna kwa namna katika hii Qur-aan ili wakumbuke, lakini haiwazidishii ila kukimbia (haki) kwa chuki.

 

 

 

قُل لَّوْ كَانَ مَعَهُ آلِهَةٌ كَمَا يَقُولُونَ إِذًا لَّابْتَغَوْا إِلَىٰ ذِي الْعَرْشِ سَبِيلًا ﴿٤٢﴾

42. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Kama wangelikuwa pamoja Naye waabudiwa kama wasemavyo, basi hapo wangelitafuta njia ya kumfikia Mwenye ‘Arshi.[12]

 

 

 

سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يَقُولُونَ عُلُوًّا كَبِيرًا ﴿٤٣﴾

43. Ametakasika Allaah na Ametukuka kutokana na wanayoyasema ya uongo na dhulma kubwa ya hali ya juu kabisa!

 

 

 

تُسَبِّحُ لَهُ السَّمَاوَاتُ السَّبْعُ وَالْأَرْضُ وَمَن فِيهِنَّ ۚ وَإِن مِّن شَيْءٍ إِلَّا يُسَبِّحُ بِحَمْدِهِ وَلَـٰكِن لَّا تَفْقَهُونَ تَسْبِيحَهُمْ ۗ إِنَّهُ كَانَ حَلِيمًا غَفُورًا ﴿٤٤﴾

44. Zinamsabihi mbingu saba na ardhi na waliomo humo. Na hakuna kitu chochote isipokuwa kinasabihi na kumhimidi Yeye, lakini hamzifahamu tasbihi zao. Hakika Yeye Ni Mvumilivu, Mwingi wa Kughufuria.

 

 

 

وَإِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآنَ جَعَلْنَا بَيْنَكَ وَبَيْنَ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ حِجَابًا مَّسْتُورًا ﴿٤٥﴾

45. Na unaposoma Qur-aan Tunajaalia baina yako na baina ya wale wasioamini Aakhirah kizuizi kinachofunika (akili wasiifahamu).

 

 

 

وَجَعَلْنَا عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ أَكِنَّةً أَن يَفْقَهُوهُ وَفِي آذَانِهِمْ وَقْرًا ۚ وَإِذَا ذَكَرْتَ رَبَّكَ فِي الْقُرْآنِ وَحْدَهُ وَلَّوْا عَلَىٰ أَدْبَارِهِمْ نُفُورًا ﴿٤٦﴾

46. Na Tumetia juu ya nyoyo zao vifuniko wasiifahamu, na katika masikio yao uziwi.[13] Na unapomtaja Rabb wako katika Qur-aan Pekee wanageuza migongo kukimbia (haki) kwa chuki.

 

 

 

نَّحْنُ أَعْلَمُ بِمَا يَسْتَمِعُونَ بِهِ إِذْ يَسْتَمِعُونَ إِلَيْكَ وَإِذْ هُمْ نَجْوَىٰ إِذْ يَقُولُ الظَّالِمُونَ إِن تَتَّبِعُونَ إِلَّا رَجُلًا مَّسْحُورًا ﴿٤٧﴾

47. Sisi Tunajua zaidi kile wanacholenga kukisikiliza pale wanapokusikiliza kwa makini, na wakati wanaponong’ona.  (Na Tunajua pia) wanaposema madhalimu: Hamfuati isipokuwa mtu aliyefanyiwa sihri.

 

 

 

انظُرْ كَيْفَ ضَرَبُوا لَكَ الْأَمْثَالَ فَضَلُّوا فَلَا يَسْتَطِيعُونَ سَبِيلًا ﴿٤٨﴾

48. Tazama vipi walivyokupigia mifano wakapotoka, basi hawawezi kupata njia (ya kuwahidi).

 

 

 

وَقَالُوا أَإِذَا كُنَّا عِظَامًا وَرُفَاتًا أَإِنَّا لَمَبْعُوثُونَ خَلْقًا جَدِيدًا ﴿٤٩﴾

49. Na wakasema: Je, hivi sisi tukiwa mifupa, na mapande yaliyosagika sagika, je, hivi sisi hivyo tutafufuliwa katika umbo jipya?[14]

 

 

 

قُلْ كُونُوا حِجَارَةً أَوْ حَدِيدًا ﴿٥٠﴾

50. Sema: Kuweni mawe au chuma.

 

 

 

أَوْ خَلْقًا مِّمَّا يَكْبُرُ فِي صُدُورِكُمْ ۚ فَسَيَقُولُونَ مَن يُعِيدُنَا ۖ قُلِ الَّذِي فَطَرَكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ ۚ فَسَيُنْغِضُونَ إِلَيْكَ رُءُوسَهُمْ وَيَقُولُونَ مَتَىٰ هُوَ ۖ قُلْ عَسَىٰ أَن يَكُونَ قَرِيبًا ﴿٥١﴾

51. Au umbo katika vile vinavyohisiwa vikubwa (au vigumu) katika vifua vyenu. Basi watasema: Nani atakayeturudisha (kuwa hai?). Sema: Ni Yule Aliyekuanzisheni mara ya kwanza! Basi watakutingishia vichwa vyao na kusema: Lini hayo?! Sema: Asaa yawe karibu.

 

 

 

يَوْمَ يَدْعُوكُمْ فَتَسْتَجِيبُونَ بِحَمْدِهِ وَتَظُنُّونَ إِن لَّبِثْتُمْ إِلَّا قَلِيلًا ﴿٥٢﴾

52. Siku Atakayokuiteni, nanyi mtamuitika huku mkimhimidi, na mtaona kama vile hamkubakia (duniani) isipokuwa kidogo tu.

 

 

 

وَقُل لِّعِبَادِي يَقُولُوا الَّتِي هِيَ أَحْسَنُ ۚ إِنَّ الشَّيْطَانَ يَنزَغُ بَيْنَهُمْ ۚ إِنَّ الشَّيْطَانَ كَانَ لِلْإِنسَانِ عَدُوًّا مُّبِينًا ﴿٥٣﴾

53. Na waambie Waja Wangu waseme maneno yaliyo mazuri zaidi. Hakika shaytwaan anachochea baina yao. Hakika shaytwaan kwa binaadam daima ni adui bayana.[15]

 

 

 

رَّبُّكُمْ أَعْلَمُ بِكُمْ ۖ إِن يَشَأْ يَرْحَمْكُمْ أَوْ إِن يَشَأْ يُعَذِّبْكُمْ ۚ وَمَا أَرْسَلْنَاكَ عَلَيْهِمْ وَكِيلًا ﴿٥٤﴾

54. Rabb wenu Anakujueni vizuri zaidi. Akitaka Atakurehemuni au Akitaka Atakuadhibuni. Na Hatukukutuma (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kuwa mlinzi wao.

 

 

 

وَرَبُّكَ أَعْلَمُ بِمَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۗ وَلَقَدْ فَضَّلْنَا بَعْضَ النَّبِيِّينَ عَلَىٰ بَعْضٍ ۖ وَآتَيْنَا دَاوُودَ زَبُورًا ﴿٥٥﴾

55. Na Rabb wako Anawajua vilivyo waliomo katika mbingu na ardhi. Na kwa yakini Tumewafadhilisha baadhi ya Manabii juu ya wengineo. Na Tukampa Daawuwd Zabuwr.

 

 

 

قُلِ ادْعُوا الَّذِينَ زَعَمْتُم مِّن دُونِهِ فَلَا يَمْلِكُونَ كَشْفَ الضُّرِّ عَنكُمْ وَلَا تَحْوِيلًا ﴿٥٦﴾

56. Sema: Iteni wale ambao mnadai (ni waabudiwa) pasi Naye, basi hawamiliki uwezo wa kukuondosheeni dhara wala kuihamisha (kwa mwengine).

 

 

 

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ يَدْعُونَ يَبْتَغُونَ إِلَىٰ رَبِّهِمُ الْوَسِيلَةَ أَيُّهُمْ أَقْرَبُ وَيَرْجُونَ رَحْمَتَهُ وَيَخَافُونَ عَذَابَهُ ۚ إِنَّ عَذَابَ رَبِّكَ كَانَ مَحْذُورًا ﴿٥٧﴾

57. Hao wanaowaomba (wao wenyewe) wanatafuta kwa Rabb wao njia ya kujikurubisha, yupi miongoni mwao awe karibu zaidi, na wanataraji Rehma Yake, na wanakhofu Adhabu Yake. Hakika Adhabu ya Rabb wako ni ya kutahadhariwa daima.[16]

 

 

 

وَإِن مِّن قَرْيَةٍ إِلَّا نَحْنُ مُهْلِكُوهَا قَبْلَ يَوْمِ الْقِيَامَةِ أَوْ مُعَذِّبُوهَا عَذَابًا شَدِيدًا ۚ كَانَ ذَٰلِكَ فِي الْكِتَابِ مَسْطُورًا ﴿٥٨﴾

58. Na hakuna mji wowote isipokuwa Sisi Tutauangamiza kabla ya Siku ya Qiyaamah, au Tutauadhibu adhabu kali. Hayo yameandikwa katika Kitabu (Lawh Al-Mahfuwdhw)[17].

 

 

 

وَمَا مَنَعَنَا أَن نُّرْسِلَ بِالْآيَاتِ إِلَّا أَن كَذَّبَ بِهَا الْأَوَّلُونَ ۚ وَآتَيْنَا ثَمُودَ النَّاقَةَ مُبْصِرَةً فَظَلَمُوا بِهَا ۚ وَمَا نُرْسِلُ بِالْآيَاتِ إِلَّا تَخْوِيفًا ﴿٥٩﴾

59. Na hakuna kinachotuzuia kuleta Aayaat (Ishara, Dalili, Miujiza) isipokuwa ni kuwa watu wa awali waliikadhibisha. Na Tuliwapa kina Thamuwd ngamia jike kuwa dalili dhahiri lakini wakamdhulumu. Na Hatupeleki Aayaat (Ishara, Miujiza) isipokuwa kwa ajili ya (kuonya na) kukhofisha (ili wazingatie).[18]

 

 

 

وَإِذْ قُلْنَا لَكَ إِنَّ رَبَّكَ أَحَاطَ بِالنَّاسِ ۚ وَمَا جَعَلْنَا الرُّؤْيَا الَّتِي أَرَيْنَاكَ إِلَّا فِتْنَةً لِّلنَّاسِ وَالشَّجَرَةَ الْمَلْعُونَةَ فِي الْقُرْآنِ ۚ وَنُخَوِّفُهُمْ فَمَا يَزِيدُهُمْ إِلَّا طُغْيَانًا كَبِيرًا ﴿٦٠﴾

60. Na (kumbuka ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Tulipokuambia: Hakika Rabb wako Amekwishawazunguka watu. Na Hatukuijaalia ndoto ambayo Tulikuonyesha isipokuwa ni mtihani kwa watu, na mti uliolaaniwa katika Qur-aan.[19] Na Tunawatisha, basi haiwazidishii isipokuwa upindukaji mipaka mkubwa wa kuasi.

 

 

 

وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ قَالَ أَأَسْجُدُ لِمَنْ خَلَقْتَ طِينًا ﴿٦١﴾

61. Na pindi Tulipowaambia Malaika: Msujudieni Aadam. Wakasujudu isipokuwa Ibliys. Akasema: Je, nimsujudie Uliyemuumba kwa udongo?[20]

 

 

 

قَالَ أَرَأَيْتَكَ هَـٰذَا الَّذِي كَرَّمْتَ عَلَيَّ لَئِنْ أَخَّرْتَنِ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ لَأَحْتَنِكَنَّ ذُرِّيَّتَهُ إِلَّا قَلِيلًا ﴿٦٢﴾

62. (Ibliys) akasema: Unamwona huyu ambaye Umemkirimu zaidi yangu! Basi Ukiniakhirisha mpaka Siku ya Qiyaamah, bila shaka nitaangamiza kabisa kizazi chake isipokuwa wachache.

 

 

 

قَالَ اذْهَبْ فَمَن تَبِعَكَ مِنْهُمْ فَإِنَّ جَهَنَّمَ جَزَاؤُكُمْ جَزَاءً مَّوْفُورًا ﴿٦٣﴾

63. (Allaah) Akasema: Nenda! Kwani atakayekufuata miongoni mwao, basi hakika Jahannam ni jazaa yenu, jazaa timilifu.

 

 

 

وَاسْتَفْزِزْ مَنِ اسْتَطَعْتَ مِنْهُم بِصَوْتِكَ وَأَجْلِبْ عَلَيْهِم بِخَيْلِكَ وَرَجِلِكَ وَشَارِكْهُمْ فِي الْأَمْوَالِ وَالْأَوْلَادِ وَعِدْهُمْ ۚ وَمَا يَعِدُهُمُ الشَّيْطَانُ إِلَّا غُرُورًا ﴿٦٤﴾

64. Na wachochee kilaini uwawezao miongoni mwao kwa sauti yako, na wakusanyie kikosi chako cha farasi, na askari wako waendao kwa miguu, na shirikiana nao katika mali na watoto na waahidi. Lakini shaytwaan hawapi ahadi isipokuwa ni udanganyifu.[21]

 

 

 

إِنَّ عِبَادِي لَيْسَ لَكَ عَلَيْهِمْ سُلْطَانٌ ۚ وَكَفَىٰ بِرَبِّكَ وَكِيلًا ﴿٦٥﴾

65. Hakika Waja Wangu huna mamlaka juu yao. Na Rabb wako Anatosheleza Kuwa Mtegemewa wa yote.

 

 

 

 

رَّبُّكُمُ الَّذِي يُزْجِي لَكُمُ الْفُلْكَ فِي الْبَحْرِ لِتَبْتَغُوا مِن فَضْلِهِ ۚ إِنَّهُ كَانَ بِكُمْ رَحِيمًا ﴿٦٦﴾

66. Rabb wenu Ndiye Ambaye Anakuendesheeni merikebu baharini ili mtafute Fadhila Zake. Hakika Yeye Ni Mwenye Kukurehemuni.

 

 

 

وَإِذَا مَسَّكُمُ الضُّرُّ فِي الْبَحْرِ ضَلَّ مَن تَدْعُونَ إِلَّا إِيَّاهُ ۖ فَلَمَّا نَجَّاكُمْ إِلَى الْبَرِّ أَعْرَضْتُمْ ۚ وَكَانَ الْإِنسَانُ كَفُورًا ﴿٦٧﴾

67. Na inapokuguseni dhara baharini wale mnaowaomba hupotea isipokuwa Yeye Pekee. Anapokuokoeni katika ardhi kavu mnakengeuka. Na binaadam amekuwa ni mwingi wa kukufuru, asiyeshukuru.

 

 

 

أَفَأَمِنتُمْ أَن يَخْسِفَ بِكُمْ جَانِبَ الْبَرِّ أَوْ يُرْسِلَ عَلَيْكُمْ حَاصِبًا ثُمَّ لَا تَجِدُوا لَكُمْ وَكِيلًا ﴿٦٨﴾

68. Je, mmeaminisha kwamba (Allaah) Hatokudidimizeni upande wowote wa ardhi kavu, au Hatokuleteeni tufani ya mawe, kisha hamtopata wa kumtegemea? 

 

 

 

أَمْ أَمِنتُمْ أَن يُعِيدَكُمْ فِيهِ تَارَةً أُخْرَىٰ فَيُرْسِلَ عَلَيْكُمْ قَاصِفًا مِّنَ الرِّيحِ فَيُغْرِقَكُم بِمَا كَفَرْتُمْ ۙ ثُمَّ لَا تَجِدُوا لَكُمْ عَلَيْنَا بِهِ تَبِيعًا ﴿٦٩﴾

69. Au je, mmeaminisha kwamba (Allaah) Hatokurudisheni huko (baharini) mara nyingine, kisha Akakutumieni kimbunga cha upepo Akakugharikisheni kwa sababu ya kufru yenu kisha hamtopata mteteaji wa kukunusuruni Nasi? 

 

 

 

وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آدَمَ وَحَمَلْنَاهُمْ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ وَرَزَقْنَاهُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ وَفَضَّلْنَاهُمْ عَلَىٰ كَثِيرٍ مِّمَّنْ خَلَقْنَا تَفْضِيلًا ﴿٧٠﴾

70. Na kwa yakini Tumewakirimu wana wa Aadam, na Tukawabeba katika ardhi kavu na baharini, na Tukawaruzuku katika vizuri na Tukawafadhilisha juu ya wengi miongoni mwa Tuliowaumba kwa ufadhilisho mkubwa.[22]

 

 

 

يَوْمَ نَدْعُو كُلَّ أُنَاسٍ بِإِمَامِهِمْ ۖ فَمَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ فَأُولَـٰئِكَ يَقْرَءُونَ كِتَابَهُمْ وَلَا يُظْلَمُونَ فَتِيلًا ﴿٧١﴾

71. Siku Tutakayoita watu wote pamoja na rekodi zao za matendo (au Nabii wao).[23] Basi atakayepewa kitabu chake kuliani mwake, hao watasoma kitabu chao na wala hawatodhulumiwa kadiri ya uzi katika kokwa ya tende. 

 

 

 

 

 

وَمَن كَانَ فِي هَـٰذِهِ أَعْمَىٰ فَهُوَ فِي الْآخِرَةِ أَعْمَىٰ وَأَضَلُّ سَبِيلًا ﴿٧٢﴾

72. Na atakayekuwa kipofu katika hii (dunia) basi yeye Aakhirah atakuwa kipofu na atapotea zaidi njia. 

 

 

 

وَإِن كَادُوا لَيَفْتِنُونَكَ عَنِ الَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ لِتَفْتَرِيَ عَلَيْنَا غَيْرَهُ ۖ وَإِذًا لَّاتَّخَذُوكَ خَلِيلًا ﴿٧٣﴾

73. Na hakika walikaribia kukukengeusha (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) na yale Tuliyokufunulia Wahy ili upate kututungia mengineyo. Basi hapo ndipo wangelikufanya rafiki mwandani.

 

 

 

وَلَوْلَا أَن ثَبَّتْنَاكَ لَقَدْ كِدتَّ تَرْكَنُ إِلَيْهِمْ شَيْئًا قَلِيلًا ﴿٧٤﴾

74. Na lau kama Hatukukuthibitisha, kwa yakini ungelikaribia kuelemea kwao kidogo.

 

 

 

إِذًا لَّأَذَقْنَاكَ ضِعْفَ الْحَيَاةِ وَضِعْفَ الْمَمَاتِ ثُمَّ لَا تَجِدُ لَكَ عَلَيْنَا نَصِيرًا ﴿٧٥﴾

75.  Hapo basi bila shaka Tungelikuonjesha (adhabu) maradufu ya uhai na (adhabu) maradufu ya mauti kisha usingelipata wa kukunusuru Nasi.

 

 

 

وَإِن كَادُوا لَيَسْتَفِزُّونَكَ مِنَ الْأَرْضِ لِيُخْرِجُوكَ مِنْهَا ۖ وَإِذًا لَّا يَلْبَثُونَ خِلَافَكَ إِلَّا قَلِيلًا ﴿٧٦﴾

76. Na hakika walikaribia wakusumbue mno katika ardhi ili wakutoe humo. Na hapo wao wasingelibakia baada yako isipokuwa kidogo tu.

 

 

 

سُنَّةَ مَن قَدْ أَرْسَلْنَا قَبْلَكَ مِن رُّسُلِنَا ۖ وَلَا تَجِدُ لِسُنَّتِنَا تَحْوِيلًا ﴿٧٧﴾

77. (Hiyo ndiyo) desturi ya Tuliowatuma kabla yako miongoni mwa Rusuli Wetu. Na wala hutopata mabadiliko katika desturi Zetu.[24]

 

 

 

 

أَقِمِ الصَّلَاةَ لِدُلُوكِ الشَّمْسِ إِلَىٰ غَسَقِ اللَّيْلِ وَقُرْآنَ الْفَجْرِ ۖ إِنَّ قُرْآنَ الْفَجْرِ كَانَ مَشْهُودًا ﴿٧٨﴾

78. Simamisha Swalaah jua linapopinduka hadi kiza cha usiku na (refusha) Qur-aan ya (Swalaah ya) Alfajiri. Hakika Qur-aan ya Alfajiri ni yenye kushuhudiwa.

 

 

 

وَمِنَ اللَّيْلِ فَتَهَجَّدْ بِهِ نَافِلَةً لَّكَ عَسَىٰ أَن يَبْعَثَكَ رَبُّكَ مَقَامًا مَّحْمُودًا ﴿٧٩﴾

79. Na katika usiku, amka uswali (tahajjud)[25] kwa kuisoma (Qur-aan) ikiwa ni ziada kwako. Asaa Rabb wako Akakuinua cheo cha kuhimidiwa (kusifika).[26]

 

 

 

 

وَقُل رَّبِّ أَدْخِلْنِي مُدْخَلَ صِدْقٍ وَأَخْرِجْنِي مُخْرَجَ صِدْقٍ وَاجْعَل لِّي مِن لَّدُنكَ سُلْطَانًا نَّصِيرًا ﴿٨٠﴾

80. Na sema: Ee Rabb wangu! Niingize mwingizo wa kheri na Nitoe pa kutokea pa kheri na Nijaalie kutoka Kwako (hoja au) mamlaka yenye kunusuru.[27]

 

 

 

وَقُلْ جَاءَ الْحَقُّ وَزَهَقَ الْبَاطِلُ ۚ إِنَّ الْبَاطِلَ كَانَ زَهُوقًا ﴿٨١﴾

81. Na sema: Haki imekuja, na ubatili umetoweka. Hakika ubatili ni wenye kutoweka daima.[28]

 

 

 

وَنُنَزِّلُ مِنَ الْقُرْآنِ مَا هُوَ شِفَاءٌ وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ ۙ وَلَا يَزِيدُ الظَّالِمِينَ إِلَّا خَسَارًا ﴿٨٢﴾

82. Na Tunateremsha katika Qur-aan ambayo ni shifaa na rehmakwa Waumini na wala haiwazidishii madhalimu isipokuwa khasara.[29]  

 

 

 

وَإِذَا أَنْعَمْنَا عَلَى الْإِنسَانِ أَعْرَضَ وَنَأَىٰ بِجَانِبِهِ ۖ وَإِذَا مَسَّهُ الشَّرُّ كَانَ يَئُوسًا ﴿٨٣﴾

83. Na Tunapomneemesha binaadam, hukengeuka na kujitenga mbali, lakini inapomgusa shari, huwa mwenye kukata tamaa.[30]

 

 

 

قُلْ كُلٌّ يَعْمَلُ عَلَىٰ شَاكِلَتِهِ فَرَبُّكُمْ أَعْلَمُ بِمَنْ هُوَ أَهْدَىٰ سَبِيلًا ﴿٨٤﴾

84. Sema: Kila mmoja anatenda kwa namna yake. Basi Rabb wenu Anamjua zaidi yule aliyehidika zaidi katika njia (ya haki).

 

 

 

وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الرُّوحِ ۖ قُلِ الرُّوحُ مِنْ أَمْرِ رَبِّي وَمَا أُوتِيتُم مِّنَ الْعِلْمِ إِلَّا قَلِيلًا ﴿٨٥﴾

85. Na wanakuuliza kuhusu Ruwh[31] (roho). [32] Sema: Roho ni katika Jambo la Rabb wangu. Na hamkupewa ujuzi isipokuwa kidogo tu.[33]

 

 

 

وَلَئِن شِئْنَا لَنَذْهَبَنَّ بِالَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ ثُمَّ لَا تَجِدُ لَكَ بِهِ عَلَيْنَا وَكِيلًا ﴿٨٦﴾

86. Na kama Tungelitaka, bila shaka Tungeliondosha yale Tuliyokufunulia Wahy, kisha usingelipata kwa haya, mtegemewa wa kukunusuru Nasi.

 

 

 

إِلَّا رَحْمَةً مِّن رَّبِّكَ ۚ إِنَّ فَضْلَهُ كَانَ عَلَيْكَ كَبِيرًا ﴿٨٧﴾

87. Isipokuwa Rehma kutoka kwa Rabb wako. Hakika Fadhila Zake juu yako daima ni kubwa.

 

 

 

قُل لَّئِنِ اجْتَمَعَتِ الْإِنسُ وَالْجِنُّ عَلَىٰ أَن يَأْتُوا بِمِثْلِ هَـٰذَا الْقُرْآنِ لَا يَأْتُونَ بِمِثْلِهِ وَلَوْ كَانَ بَعْضُهُمْ لِبَعْضٍ ظَهِيرًا ﴿٨٨﴾

88. Sema: Ikiwa watajumuika wanaadam na majini ili walete mfano wa hii Qur-aan, hawatoweza kuleta mfano wake na japokuwa watasaidiana wao kwa wao.[34]

 

 

 

وَلَقَدْ صَرَّفْنَا لِلنَّاسِ فِي هَـٰذَا الْقُرْآنِ مِن كُلِّ مَثَلٍ فَأَبَىٰ أَكْثَرُ النَّاسِ إِلَّا كُفُورًا ﴿٨٩﴾

89. Na kwa yakini Tumesarifu namna kwa namna hii Qur-aan kwa watu, kwa kila mfano, lakini watu wengi wamekataa kabisa (haki; hawakukubali) isipokuwa kukufuru tu.

 

 

 

وَقَالُوا لَن نُّؤْمِنَ لَكَ حَتَّىٰ تَفْجُرَ لَنَا مِنَ الْأَرْضِ يَنبُوعًا ﴿٩٠﴾

90. Na wakasema: Hatutakuamini (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) mpaka utububujie kutoka ardhini chemchemu.[35]

 

 

 

أَوْ تَكُونَ لَكَ جَنَّةٌ مِّن نَّخِيلٍ وَعِنَبٍ فَتُفَجِّرَ الْأَنْهَارَ خِلَالَهَا تَفْجِيرًا ﴿٩١﴾

91. Au uwe na bustani ya mitende na mizabibu, kisha utububujie mito kati yake mbubujiko mkubwa.

 

 

 

أَوْ تُسْقِطَ السَّمَاءَ كَمَا زَعَمْتَ عَلَيْنَا كِسَفًا أَوْ تَأْتِيَ بِاللَّـهِ وَالْمَلَائِكَةِ قَبِيلًا ﴿٩٢﴾

92. Au utuangushie mbingu vipande vipande kama ulivyodai, au umlete Allaah na Malaika uso kwa uso.

 

 

 

أَوْ يَكُونَ لَكَ بَيْتٌ مِّن زُخْرُفٍ أَوْ تَرْقَىٰ فِي السَّمَاءِ وَلَن نُّؤْمِنَ لِرُقِيِّكَ حَتَّىٰ تُنَزِّلَ عَلَيْنَا كِتَابًا نَّقْرَؤُهُ ۗ قُلْ سُبْحَانَ رَبِّي هَلْ كُنتُ إِلَّا بَشَرًا رَّسُولًا ﴿٩٣﴾

93. Au uwe na nyumba ya dhahabu, au upande mbinguni. Na wala hatutoamini kamwe kupanda kwako mpaka ututeremshie kitabu tukisome.  Sema: Utakasifu ni wa Rabb wangu! Kwani mimi nimekuwa nani isipokuwa ni binaadam (na) Rasuli!

 

 

 

وَمَا مَنَعَ النَّاسَ أَن يُؤْمِنُوا إِذْ جَاءَهُمُ الْهُدَىٰ إِلَّا أَن قَالُوا أَبَعَثَ اللَّـهُ بَشَرًا رَّسُولًا ﴿٩٤﴾

94. Na hakuna kilichowazuia watu wasiamini ulipowajia mwongozo isipokuwa husema: Je, Allaah Ametuma binaadam kuwa ni Rasuli?

 

 

 

قُل لَّوْ كَانَ فِي الْأَرْضِ مَلَائِكَةٌ يَمْشُونَ مُطْمَئِنِّينَ لَنَزَّلْنَا عَلَيْهِم مِّنَ السَّمَاءِ مَلَكًا رَّسُولًا ﴿٩٥﴾

95. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Kama ingelikuwa katika ardhi kuna Malaika wanatembea kwa utulivu na amani, basi bila shaka Tungeliwateremshia kutoka mbinguni Malaika kuwa ni Rasuli.

 

 

 

قُلْ كَفَىٰ بِاللَّـهِ شَهِيدًا بَيْنِي وَبَيْنَكُمْ ۚ إِنَّهُ كَانَ بِعِبَادِهِ خَبِيرًا بَصِيرًا ﴿٩٦﴾

96. Sema: Anatosheleza Allaah kuwa Shahidi baina yangu na baina yenu. Hakika Yeye daima Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na za siri za Waja Wake, Mwenye Kuona yote.

 

 

 

وَمَن يَهْدِ اللَّـهُ فَهُوَ الْمُهْتَدِ ۖ وَمَن يُضْلِلْ فَلَن تَجِدَ لَهُمْ أَوْلِيَاءَ مِن دُونِهِ ۖ وَنَحْشُرُهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ عَلَىٰ وُجُوهِهِمْ عُمْيًا وَبُكْمًا وَصُمًّا ۖ مَّأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۖ كُلَّمَا خَبَتْ زِدْنَاهُمْ سَعِيرًا ﴿٩٧﴾

97. Na ambaye Allaah Amemhidi, basi huyo ndiye aliyehidika. Na Anayempotoa, basi hutowapatia rafiki walinzi pasi Naye. Na Tutawakusanya Siku ya Qiyaamah juu ya nyuso zao[36] (wakiwa) vipofu, mabubu na viziwi, makazi yao ni (moto wa) Jahannam, kila ukififia Tutawazidishia moto uliowashwa vikali mno.

 

 

 

ذَٰلِكَ جَزَاؤُهُم بِأَنَّهُمْ كَفَرُوا بِآيَاتِنَا وَقَالُوا أَإِذَا كُنَّا عِظَامًا وَرُفَاتًا أَإِنَّا لَمَبْعُوثُونَ خَلْقًا جَدِيدًا ﴿٩٨﴾

98. Hiyo ndiyo jazaa yao kwa kuwa wao walizikanusha Aayaat (na Ishara, Hoja, Dalili) Zetu na wakasema: Je, hivi sisi tukiwa mifupa na mapande yaliyosagika sagika, hivi kweli sisi tutafufuliwa katika umbo jipya?[37]

 

 

 

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّ اللَّـهَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ قَادِرٌ عَلَىٰ أَن يَخْلُقَ مِثْلَهُمْ وَجَعَلَ لَهُمْ أَجَلًا لَّا رَيْبَ فِيهِ فَأَبَى الظَّالِمُونَ إِلَّا كُفُورًا ﴿٩٩﴾

99. Je, hawajaona kwamba Allaah Ambaye Ameumba mbingu na ardhi Ni Mweza wa Kuumba mfano wao?  Na Amewawekea muda maalumu usio na shaka? Lakini madhalimu wamekataa kabisa hawana isipokuwa kukufuru tu.

 

 

 

قُل لَّوْ أَنتُمْ تَمْلِكُونَ خَزَائِنَ رَحْمَةِ رَبِّي إِذًا لَّأَمْسَكْتُمْ خَشْيَةَ الْإِنفَاقِ ۚ وَكَانَ الْإِنسَانُ قَتُورًا ﴿١٠٠﴾

100. Sema: Ingekuwa nyinyi mnamiliki hazina za Rehma ya Rabb wangu bila shaka hapo mngelizuia kuzitumia kwa ajili ya kukhofu (zisimalizike). Na binaadam amekuwa ni mchoyo kupindukia.

 

 

 

وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَىٰ تِسْعَ آيَاتٍ بَيِّنَاتٍ ۖ فَاسْأَلْ بَنِي إِسْرَائِيلَ إِذْ جَاءَهُمْ فَقَالَ لَهُ فِرْعَوْنُ إِنِّي لَأَظُنُّكَ يَا مُوسَىٰ مَسْحُورًا ﴿١٠١﴾

101. Na kwa yakini Tulimpa Muwsaa Aayaat (Ishara, Dalili, Miujiza) tisa bayana.[38] Basi waulize wana wa Israaiyl alipowajia, na Firawni akamwambia: Hakika mimi nakuona ewe Muwsaa kuwa umerogwa.

 

 

 

قَالَ لَقَدْ عَلِمْتَ مَا أَنزَلَ هَـٰؤُلَاءِ إِلَّا رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ بَصَائِرَ وَإِنِّي لَأَظُنُّكَ يَا فِرْعَوْنُ مَثْبُورًا ﴿١٠٢﴾

102. (Muwsaa) akasema: Kwa yakini umekwishajua kwamba hakuna Aliyeteremsha haya isipokuwa Rabb wa mbingu na ardhi kuwa ni dalili za kuonekana dhahiri, na hakika mimi bila shaka nakuona ewe Firawni kuwa umekwisha angamia.

 

 

 

فَأَرَادَ أَن يَسْتَفِزَّهُم مِّنَ الْأَرْضِ فَأَغْرَقْنَاهُ وَمَن مَّعَهُ جَمِيعًا ﴿١٠٣﴾

103. Basi akataka awasumbue na kuwafukuza katika ardhi, Tukamgharikisha yeye na waliokuwa pamoja naye wote.

 

 

 

وَقُلْنَا مِن بَعْدِهِ لِبَنِي إِسْرَائِيلَ اسْكُنُوا الْأَرْضَ فَإِذَا جَاءَ وَعْدُ الْآخِرَةِ جِئْنَا بِكُمْ لَفِيفًا ﴿١٠٤﴾

104. Na Tukawaambia baada yake wana wa Israaiyl: Kaeni katika ardhi, na itakapokuja ahadi ya Aakhirah Tutakuleteni nyote pamoja kwa makundi mchanganyiko.

 

 

 

وَبِالْحَقِّ أَنزَلْنَاهُ وَبِالْحَقِّ نَزَلَ ۗ وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا مُبَشِّرًا وَنَذِيرًا ﴿١٠٥﴾

105. Na kwa haki Tumeiteremsha (Qur-aan), na kwa haki imeteremka. Na Hatukukutuma (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) isipokuwa ni mbashiriaji na mwonyaji tu.

 

 

 

وَقُرْآنًا فَرَقْنَاهُ لِتَقْرَأَهُ عَلَى النَّاسِ عَلَىٰ مُكْثٍ وَنَزَّلْنَاهُ تَنزِيلًا ﴿١٠٦﴾

106. Na Qur-aan Tumeigawanya sehemu mbali mbali ili uwasomee watu kwa kituo, na Tumeiteremsha kidogo kidogo.[39]

 

 

 

قُلْ آمِنُوا بِهِ أَوْ لَا تُؤْمِنُوا ۚ إِنَّ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ مِن قَبْلِهِ إِذَا يُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ يَخِرُّونَ لِلْأَذْقَانِ سُجَّدًا ﴿١٠٧﴾

107. Sema: Iaminini au msiamini. Hakika wale waliopewa ilimu kabla yake wanaposomewa (Qur-aan) wanaporomoka kifudifudi wanasujudu.

 

 

 

وَيَقُولُونَ سُبْحَانَ رَبِّنَا إِن كَانَ وَعْدُ رَبِّنَا لَمَفْعُولًا ﴿١٠٨﴾

108. Na wanasema: Utakasifu ni wa Rabb wetu, hakika Ahadi ya Rabb wetu lazima itimizwe.

 

 

 

وَيَخِرُّونَ لِلْأَذْقَانِ يَبْكُونَ وَيَزِيدُهُمْ خُشُوعًا ۩﴿١٠٩﴾

109. Na wanaporomoka kifudifudi huku wanalia na inawazidishia unyenyekevu.

 

 

 

قُلِ ادْعُوا اللَّـهَ أَوِ ادْعُوا الرَّحْمَـٰنَ ۖ أَيًّا مَّا تَدْعُوا فَلَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ ۚ وَلَا تَجْهَرْ بِصَلَاتِكَ وَلَا تُخَافِتْ بِهَا وَابْتَغِ بَيْنَ ذَٰلِكَ سَبِيلًا ﴿١١٠﴾

110. Sema: Muiteni Allaah au muiteni Ar-Rahmaan[40], vyovyote mtakavyomwita basi Yeye Ana Majina Mazuri kabisa.[41] Na wala usisome (Qur-aan) kwa sauti ya juu katika Swalaah yako wala usiiteremshe sana, bali shika njia ya wastani baina yake. [42]

 

 

 

وَقُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي لَمْ يَتَّخِذْ وَلَدًا وَلَمْ يَكُن لَّهُ شَرِيكٌ فِي الْمُلْكِ وَلَمْ يَكُن لَّهُ وَلِيٌّ مِّنَ الذُّلِّ ۖ وَكَبِّرْهُ تَكْبِيرًا ﴿١١١﴾

111. Na sema: AlhamduliLLaah (Himidi Anastahiki Allaah) Ambaye Hakujifanyia mwana na wala Hakuwa na mshirika katika ufalme, na wala Hakuwa dhalili hata Awe (Anahitaji) mlinzi (na msaidizi), na mtukuze matukuzo makubwa kabisa.[43]  

 

[1] Safari Ya Al-Israa Na Al-Mi’raaj:

 

Maana Ya Al-Israa kilugha: Ni safari ya usiku.

 

Kiistilahi: Ni safari ya baadhi ya usiku mmoja, ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) yeye mwenyewe kwa mwili wake na akili zake na roho yake kuanzia Masjid Al-Haraam (Msikiti Mtukufu - Makkah) kufika Masjid-Al-Aqswaa (Msikiti wa Mbali -Al-Quds) na kurejea kwake Makkah usiku huo huo. Alisafiri akiwa ameambatana na Malaika Mtukufu Jibriyl (عليه السّلام) kwa kipando cha mnyama wa ajabu mwenye umbo la kuvutia kabisa aliyejulikana kwa Al-Buraaq.

 

Maana Ya Al-Mi’raaj kilugha: Ni kupanda juu.

 

Kiistilahi: Ni kupanda kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) mbinguni kuanzia Masjid Al-Aqaswaa hadi kufika mbingu ya saba.

 

Maana ya Al-Buraaq kilugha ni: Mwale unaotoka katika mwanga.

 

Kiistilahi: Ni kama alivyoelezea Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  katika Hadiyth:

“Nililetewa Al-Buraaq, mnyama mrefu wa umbo na mweupe, ni mkubwa kiasi zaidi ya punda  lakini ni mdogo kuliko nyumbu, ambaye anapokwenda mbio hatua yake ni upeo wa macho yake. Nilimpanda mnyama huyo mpaka nikafika Al-Masjid Al-Aqswaa huko Al-Quds (Jerusalem). Hapo nilimfunga pale mahali ambapo Manabii wengine walikuwa wakifunga wanyama wao.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Matukio ya safari hii tukufu ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ya Al-Israa na Al-Mi’raaj yameelezewa kwa tafasili katika Hadiyth ndefu ya [Al-Bukhaariy] Na Hadiyth kadhaa nyenginezo za tukio tukufu la Al-Israa Wal Mi’raaj zimethibiti; mojawapo inaeleza kuwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliswali na Manabii wengine hapo katika Msikiti wa Al-Aqswaa na yeye akiwa Imaam kwa kauli Yake (صلى الله عليه وآله وسلم): “Kisha niliingia Al-Masjid Al-Aqswaa, nikaswali rakaa mbili.” [Swahiyh Muslim] 

 

Msikiti wa Al-Aqswaa umekuwa na sifa ya kuwa ni kituo cha Manabii wote, toka enzi ya Al-Khaliyl Ibraahiym (عليه السّلام). Hivyo Manabii wote walikusanyika hapo na Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) akawa Imaam wao. Hii ni dalili juu ya cheo kikubwa alicho nacho Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) ambaye ni Nabiy wa mwisho miongoni mwa Manabii wengine (عليهم السّلام). [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

Rejea pia An-Najm (53:1-18) Aayah zinazoelezea bado tukio hili na Allaah (سبحانه وتعالى) kumuunga mkono kuwa Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) ni mkweli na hakukadhibisha tukio hili.

 

Kwa maelezo bayana rejea Alhidaaya.com makala zifuatazo:

Muujiza Wa Al-Israa Wal-Mi'raaj Na Mafunzo Yake

Tukio la Israa Na Mi'iraaj

[2] Waliotumwa Kuwadhalilisha Baniy Israaiyl:

 

Wafasiri wamekhitilafiana kuhusu nani hao waliotumwa kuwadhalilisha Baniy Israaiyl? Ambalo hawakukhitilafiana ni kuwa watu hao walikuwa ni makafiri. Ima ni watu kutoka Iraq, au Jazeera, au kwingineko. Watu hawa Allaah Aliwapa nguvu dhidi ya Baniy Israaiyl wakati walipokithiri kutenda maasia, wakaacha kutekeleza sharia zao nyingi na wakadhulumu kwenye nchi. Imaam As-Sa’diy amesema walikuwa ni makafiri. [Tafsiyr As Sa’diy]

 

Ibn Kathiyr amesema: Wamekhitilafiana Wafasiri wa Salaf na waliotangulia kuhusu ni nani waliopelekewa watu wa kuwaadhibu na kuwadhalilisha Ibn ‘Abaaas na Qataadah wamesema: Ni Jaaluwt Al-Jazariy na askari wake, walitumiwa mwanzo wakadhalilishwa, kisha zamu ikawa yao baada ya hapo wakapata nguvu. Lakini katika vita, Daawuwd alimuua Jaaluwt. Na ndiyo sababu Allaah Akasema: Kisha Tukakurudishieni nguvu zenu dhidi yao. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

[3] Qur-aan Inaongoza Katika Njia Iliyonyooka:

Rejea Suwrah Fusw-Swilat (41:44) kwenye maelezo bayana.

 

[4] Amali Kuambatanishwa Shingoni:

 

Amali zinazoambatanishwa shingoni mwa binaadam, ni amali za kheri au shari alizokadariwa au alizojaaliwa binaadam kuzitenda kwa khiyari yake mwenyewe. Amali hizo zimeambatanishwa shingoni mwake na zitamhusu yeye pekee, kwa maana, hatahesabiwa kwa matendo ya mtu mwengine wala mwengine hatahesabiwa kwa matendo yake yeye. Rejea Az-Zalzalah (99:6-8), Al-Kahf (18:49), Qaaf (50:17-18), Al-Infitwaar (82:10-12).

 

Na kuhusu kukunjuliwa kitabu cha matendo, rejea At-Takwiyr (81:10), Al-Anbiyaa (21:104).

 

[5] Binaadam Hataweza Kukanusha Ovu Lolote Alilolitenda Duniani:

 

Aayah hii inahusiana na Aayah iliyotangulia. Na hapa, Allaah (سبحانه وتعالى) Anabainisha kuwa hakuna mtu atakayeweza kukanusha jambo lolote lile ovu alilolitenda, kwani ataambiwa asome mwenyewe kitabu chake! Kamwe hatoweza kukanusha jambo, kwani hata viungo vya binadaam vitashuhudia matendo yake aliyoyatenda duniani. Rejea Yaasiyn (36:65), An-Nuwr (24:24), na Fus-swilat (41:20-22).

 

[6] Juhudi Za Muumini Na Mavuno Ya Aakhirah:

 

Rejea Ash-Shuwraa (42:20).

 

[7] Makatazo Na Maamrisho Ya Allaah (سبحانه وتعالى) Kuanzia Aayah Ya (22) Hadi Ya (39):

 

Kuanzia Aayah hii ya (22), Allaah (سبحانه وتعالى) Anaanza katazo la kutokumshirikisha Yeye na chochote. Kisha Anaendelea kutaja maamrisho na  makatazo mengineyo mbalimbali hadi Aayah ya (39) ambayo Anamalizia pia kwa kutoa amri na tahadharisho la kutokumshirikisha Yeye (سبحانه وتعالى).     

 

[8] Kuwafanyia Ihsaan Wazazi Wawili:

 

Rejea Luqmaan (31:14) na Al-Ahqaaf (46:15) kwenye maelezo bayana na fadia tele:

 

[9] Uff (Neno La Kudhihirisha Karaha)

 

Ni neno la kuudhika na kuonyesha karaha ya kiwango cha chini kabisa. Na linaweza kuwa kwa kauli au kwa ishara ya kuchukizwa au kutokuridhika na jambo. Yaani, usionyeshe hata kidogo kuwa umechukizwa au umeudhika nao au hukuridhika na wazazi.

 

[10] Tofauti Ya Israfu Na Ubadhirifu:

 

Israfu inaweza kuwa na maana ya kuvuka mipaka kwa kutenda dhambi. Mfano ni katika Kauli za Allaah (سبحانه وتعالى) katika Suwrat za Yaasiyn (36:19), Al-A’raaf (7:81), Al-Anbiyaa (21:9) na nyenginezo kadhaa.

 

Kuna ujumuishi na umahususi baina ya israaf (israfu) na tabdhiyr (ubadhirifu), kwani huweza kuja pamoja baadhi ya nyakati zikawa na maana moja, na iliyo jumuishi zaidi ambayo ni israaf, inaweza ikabaki yenyewe na maana yake ya asili.

 

Na pia inaweza kuwa kwa maana ya kuvuka kikomo cha matumizi ya pesa katika mambo yanayoruhusika kama chakula, nguo na kadhalika. Kwa lugha nyingine, ni kuitumia Neema ya Allaah (سبحانه وتعالى) zaidi ya kiwango cha mahitaji ya mtu. Mfano ni mtu kununua nguo nyingi akawa hazivai baadhi yake. Au mtu kununua chakula zaidi ya anachokihitaji, kisha akala cha kumtosha, na kinachobakia kikaharibika akakitupa.  Rejea Al-‘Araaf (7:31).

 

Ama Tabdhiyr (ubadhirifu), hii inahusiana na mali tu bila ya upindukaji mipaka ya maasi. Kwa maana nyingine, tabdhiyr  ni utumiaji wa mali katika kisichojuzu (cha haramu), ni sawa utumiaji uwe mdogo kama kutumia pesa kununulia sigara, pombe na kadhalika. Au uwe mkubwa, kama vile mtu kufunga safari za starehe zenye  maasi. Pia utumiaji wa mali katika shughuli kwa ajili ya kujionyesha na kujifakharisha. Na hili ni tatizo ambalo linaendelea kutendeka katika jamii zetu za Kiislamu. Mfano utaona katika shughuli za ndoa, mali nyingi zinatumika kufanya mambo ya ziyada ya shughuli hizo, na mambo mengineyo ni ya haramu kama kuweka bendi za muziki na mambo mengineyo ya kuwaigiza  makafiri. Na zaidi huwa ni  kwa ajili ya kujionyesha, kujifakharisha na kushindana; kila mmoja amshinde mwengine katika shughuli yake aonekana amefanya jambo kuu kuliko mwenziwe.  

 

Yote mawili, israfu na tabdhiyr (ubadhirifu), ni utumiaji wa Neema za Allaah (سبحانه وتعالى) katika yasiyomridhisha. Lakini binaadam akumbuke na atambue kuwa  atakuja kuulizwa na Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kila neema aliyonayo; ameipataje na ameitumiaje. Rejea Suwrah At-Takaathur (102). Na mali ni katika mambo manne ambayo mwanaadam lazima atasimamishwa kuulizwa Siku ya Qiyaamah. Hadiyth ifuatayo imethibitisha:

 

عَنْ أَبِي بَرْزَةَ الأَسْلَمِيِّ (رضي الله عنه)  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((لاَ تَزُولُ قَدَمَا عَبْدٍ يَوْمَ الْقِيَامَةِ حَتَّى يُسْأَلَ عَنْ عُمُرِهِ فِيمَا أَفْنَاهُ، وَعَنْ عِلْمِهِ فِيمَ فَعَلَ، وَعَنْ مَالِهِ مِنْ أَيْنَ اكْتَسَبَهُ وَفِيمَ أَنْفَقَهُ وَعَنْ جِسْمِهِ فِيمَ أَبْلاَهُ))  رواه الترمذي وقال: حديث حسن  صحيح

Amesimulia Abuu Barzah Al-Aslamiyy (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Nyayo za mja hazitoondoka (Siku ya Qiyaamah) mpaka aulizwe juu ya umri wake alivyoumaliza, ilimu yake alivyoifanyia, mali yake ameichuma kutoka wapi na ameitumia kwa mambo gani, na mwili wake aliutumia kwa kazi gani.” [At-Tirmidhiy na amesema: Hadiyth Hasan Swahiyh]

 

[11] Kauli Nzito Mno Kumsingizia Allaah (سبحانه وتعالى) Kuwa Ana Wana Wa Kike!

 

Mbingu na majabali yanakaribia kupasuka kwa kauli nzito ya usingiziaji kama huu: Rejea Maryam (19:88-95).

 

Na usingiziaji mwengine ni kudai kwamba Malaika ni banaati (wana wa kike) wa Allaah (سبحانه وتعالى)! Rejea Asw-Swaaffaat (37:149-156), Az-Zukhruf (43:19), na An-Nahl (16:57-59).

 

Na kwa ujumla, usingiziaji wa kuwa Allaah (سبحانه وتعالى) Ana mwana umetajwa kwenye An-Nisaa (4:171), na Al-Maaidah (5:73-75).

 

[12]  Makafiri Wangelitafuta Njia Ya Kufikia Katika ‘Arsh Ya Allaah (عزّ وجلّ)

 

Imaam As-Sa’diy amesema: Yaani wangechukua njia ya kumfikia Allaah (سبحانه وتعالى)  kwa kumwabudu, na kurudia Kwake, na kujikurubisha Kwake. Basi vipi mja faqiri ambaye anaona shida ya ufaqiri wake amwabudu mungu mwengineo pamoja na Allaah? Hii hapana isipokuwa dhulma katika dhulma kubwa na ujinga ulio mkubwa kabisa. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

Yaani: Wanatafuta njia na wanajitahidi kumshinda Allaah (سبحانه وتعالى), kwa hivyo ama wapande wawe juu Yake, lakini Anayetukuka na kushinda na kudhibiti ni Rabb Mwabudiwa. Ama wanajua na  wanakiri kwamba miungu yao wanayoiabudu badala ya Allaah imetiishwa na hawana uhusiano wowote na jambo hilo. Basi kwa nini waliwachukua wakiwa katika hali hii? Hii itakuwa kama Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى) katika Al-Muuminuwn (23:91).  [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

[13] Nyoyo Za Makafiri Zimefunikwa Na Masikio Yana Uziwi:

 

Rejea Al-An’aam (6:25), Fusw-Swilat (41:5), Al-Kahf  (18:57).

 

[14] Kufufuliwa Ni Katika Nguzo Sita Za Imaan Na Katika Mambo Ya Ghaibu. Makafiri Hawakuamini Kwamba Watafufuliwa:

 

Aayah hii na zinazofuatia hadi ya (59) na pia Aayah ya (98), zinataja kuwa makafiri hawakuwa wanaamini kabisa kwamba watafufuliwa Siku ya Qiyaamah na kwamba watarudi kuwa katika umbo jipya. Rejea Al-An’aam (6:29), Ar-Ra’d (13:5), Qaaf (50:3), Al-Muuminuwn (23:35-37), (23:82-83), Asw-Swaaffaat (37:16-17). Na hawakuamini kwamba watakusanywa na kusimamishwa kuhesabiwa matendo yao, ilhali Allaah (سبحانه وتعالى) Amethibitisha hilo katika Qur-aan kwamba Atafufua viumbe vyote na watahesabiwa matendo yao na kulipwa wanavyostahiki kulipwa. Miongoni mwa Kauli Zake Allaah (سبحانه وتعالى) kuhusu hayo ni katika Suwrah za Yaasiyn (36:48-54), (36:77-83), Al-Waaqi’ah (56:47-50), Al-Hajj (22:5–7), na At-Taghaabun (64:7), Al-Qiyaamah (75:36-40). Na iweje Allaah (سبحانه وتعالى) Asiweze kuwafufua ilhali hilo ni jambo jepesi kabisa kama Anavyosema katika Kauli Zake, katika Suwrah za Luqmaan (31:28), na Ar-Ruwm (30:27). Na Anasema kuwa uumbaji Wake wa mbingu na ardhi ni mkubwa zaidi kulikoni kumuumba mwanaadam, rejea Kauli Yake katika Ghaafir (40:57). Hali kadhaalika, Hadiyth kadhaa za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) zimethibitisha jambo hili la kufufuliwa Siku ya Qiyaamah na kuhesabiwa matendo. Na kuamini Aakhirah na matukio yake kama ya kufufuliwa ni mojawapo ya nguzo sita za imaan. Na haya ni katika mambo ya ghaibu ambayo kuyaamini ni  katika sifa kuu za Muumini. Na Allaah (سبحانه وتعالى) Amelitilia umuhimu mkubwa hadi kwamba likawa ni jambo la kwanza kutangulizwa katika Suwrah ya pili ya Qur-aan.  Rejea Al-Baqarah (2:3) kwenye maelezo bayana kuhusu yepi ya ghaibu.

 

[15] Shaytwaan Huchochea Waja Wa Allaah Na Ni Adui Bayana!: 

 

Rejea Suwrah hii Aayah (64) na Suwrah Ibraahiym (14:22) kwenye rejea nyenginezo za kutahadharishwa na shaytwaan.

 

[17] Al-Lawh Al-Mahfuwdh (Ubao Uliohifadhiwa): Rejea Ar-Ra’d (13:39).

 

[19] Ndoto Aliyoonyeshwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Na Ni Mti Wa Az-Zaqquwm:

 

Ndoto aliyoonyeshwa katika safari ya muujiza ya Al-Israa Wal-Mi’raaj [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

Mti huo ni Mti wa Az-Zaqquwm ambao ni mti ulioko katika Moto wa Jahannam. [Tafsiyr As-Sa’diy, na Ibn Kathiyr]. Rejea Ad-Dukhaan (44:43-46), na Asw-Swaaffaat (37:62-68).

 

[20] Allaah (سبحانه وتعالى) Kuwaamrisha Malaika Wamsujudie Binaadam Wakasujudu Wote Isipokuwa Ibliys:

 

Rejea Al-Baqarah (2:34), Al-A’raaf (7:11-18), Al-Hijr (15:28-40), Swaad (38-37-85).

 

[21] Njia Za Shaytwaan Kuwachochea Wanaadam:

 

Kuhusu Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

وَاسْتَفْزِزْ مَنِ اسْتَطَعْتَ مِنْهُم بِصَوْتِكَ  

“Na wachochee kilaini uwawezao miongoni mwao kwa sauti yako.”

 

Mujaahid amesema: Ni upuuzi na nyimbo (muziki). [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

Na Imaam As-Sa’diy amesema: Aayah hii inamhusu kila anayelingania maasi. Na maana yake ni kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Amewafanyia mtihani Waja Wake kwa adui huyu wa wazi, anayewaitia katika kumuasi Allaah (سبحانه وتعالى)  kwa maneno yake na matendo yake.

 

Hii ni pamoja na kila uasi unaohusiana na mali zao na watoto wao, kama vile kuzuia Zakaah, kutokutimiza kafara, na haki za wajibu. Pia, kutokuwafunza adabu njema Watoto, kutokuwalea malezi mema ya kheri, na kutowaongoza njia ya kuepuka shari.  Kadhalika, kuchukua mali za watu bila ya haki (kwa dhulma), au kuiweka mali mahala pasipostahiki, au kutumia chumo haramu kujinufaisha.

 

Bali Mufassiruna wengi wameeleza kwamba kutokupiga BismiLLaahi wakati wa kula au kunywa au kufanya jimai, yote hayo yanaingia katika kushirikiana na shaytwaan katika mali na watoto, na kwamba kama mtu hakupiga BismiLLaahi katika haya, basi shaytwaan hushirikiana naye kama ilivyoelezwa katika Hadiyth. [Imaam As-Sa’diy]

 

عَنْ عِيَاضِ بْنِ حِمَارٍ الْمُجَاشِعِيِّ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ ذَاتَ يَوْمٍ فِي خُطْبَتِهِ ‏"‏ أَلاَ إِنَّ رَبِّي أَمَرَنِي أَنْ أُعَلِّمَكُمْ مَا جَهِلْتُمْ مِمَّا عَلَّمَنِي يَوْمِي هَذَا كُلُّ مَالٍ نَحَلْتُهُ عَبْدًا حَلاَلٌ وَإِنِّي خَلَقْتُ عِبَادِي حُنَفَاءَ كُلَّهُمْ وَإِنَّهُمْ أَتَتْهُمُ الشَّيَاطِينُ فَاجْتَالَتْهُمْ عَنْ دِينِهِمْ وَحَرَّمَتْ عَلَيْهِمْ مَا أَحْلَلْتُ لَهُمْ وَأَمَرَتْهُمْ أَنْ يُشْرِكُوا بِي مَا لَمْ أُنْزِلْ بِهِ سُلْطَانًا

Hadiyth ya ‘Iyaadhw bin Himaar Al-Mujaashi’iyy  (رضي الله عنه): Kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alisema siku ile katika khutba yake: “Jueni na tambueni kwamba hakika Rabbi wangu Ameniamuru niwafundisheni  msiyoyajua katika mambo Aliyonifundisha hivi leo. (Hayo Aliyonifundisha ni): Mali yoyote Niliyomtunuku mja basi ni halali yake, na hakika Mimi Nimewaumba Waja Wangu wote wakiwa safi wenye kuelemea haki, lakini mashaytwaan wakawajia, wakawaengua mbali na dini yao, lakini pia wakawaharamishia Niliyowahalalishia, na wakawaamuru wanishirikishe Mimi kwa mambo ambayo Sikuteremsha kwayo dalili.” [Muslim]

 

Rejea Suwrah Ibraahiym (14:22) na rejea nyenginezo zilizotajwa humo za jinsi shaytwaan anavyokanusha wanaadam aliowapoteza na matahadharisho ya kumfuata shaytwaan.

 

[22] Wanaadam Kukirimiwa Na Kutukuzwa Na Allaah (سبحانه وتعالى):

 

Haya ni kutokana na Ukarimu Wake Allaah (سبحانه وتعالى) kwao, na Ihsaan Yake bila ya kipimo, kwani Amewatukuza wanaadam kwa sifa zote za utukufu. Akawatukuza kwa ilimu na akili, na kuwatumia Rusuli, na kuwateremshia Vitabu, na kuwajaalia miongoni mwao kuwa ni awliyaa (vipenzi) na waliotakaswa, na Akajaalia neema za dhahiri na za kufichika. [Imaam As-Sa’diy]

 

[23] Maana Ya إمام  )Imaam(:

 

Imaam ina maana kadhaa. Rejea An-Nahl (16:120).

 

 ‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusu maana ya بِإِمَامِهِمْ   katika Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

يَوْمَ نَدْعُو كُلَّ أُنَاسٍ بِإِمَامِهِمْ ۖ

Siku Tutakayoita watu wote pamoja na rekodi zao za matendo (au Nabii wao).”

 

Mujaahid na Qataadah wamesema ni Nabii wao kutokana na Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى) katika Suwrah Yuwnus (10:47).

 

Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما)  amesema: Ni Kitabu cha amali zao walizozitenda duniani. Na wamesema hivyo pia Abu Al-‘Aaliyah,   Al-Hasan na Adhw-Dhwahaak, na kwamba hii ni kauli iliyo na nguvu kabisa, na wakataja Kauli za Allaah (سبحانه وتعالى) katika Yaasiyn (36:12), Al-Kahf (18:49), Al-Jaathiyah (45:28-29).

 

Lakini hii haipingani pia na kuja kwa Nabii wao pindi Allaah (سبحانه وتعالى) Atakapohukumu nyumati zote Siku ya Qiyaamah, kwa sababu hakuna budi aweko wa kushuhudia amali zao kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى) katika Suwrah Al-Baqarah (2:143), An-Nisaa (4:41), Al-Hajj (22:78), Az-Zumar (39:69-70) na Al-Jaathiyah (45:28). Lakini hapa imekusudiwa Kitabu cha amali, ndio maana Allaah (سبحانه وتعالى) Anamalizia kusema katika Aayah hii:

 

يَوْمَ نَدْعُو كُلَّ أُنَاسٍ بِإِمَامِهِمْ ۖ فَمَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ فَأُولَـٰئِكَ يَقْرَءُونَ كِتَابَهُمْ وَلَا يُظْلَمُونَ فَتِيلًا ﴿٧١﴾

“Siku Tutakayoita watu wote pamoja na rekodi zao za matendo (au Nabii wao). Basi atakayepewa kitabu chake kuliani mwake, hao watasoma kitabu chao na wala hawatodhulumiwa kadiri ya uzi katika kokwa ya tende.”  [Al-Israa (17:71)]

 

[24] Desturi Ya Allaah (سبحانه وتعالى) Kuwaadhibu Makafiri Na Kuwajaalia Ushindi Waumini: Rejea Aal-‘Imraan (3:137), Yuwsuf (12:109).

 

[25] Fadhila Za Qiyaamul-Layl (Kisimamo Cha Usiku):

 

Fadhila za Qiyaamul-Layl (kisimamo cha usiku) kufanya ibaada zimetajwa katika Qur-aan na Sunnah sehemu nyingi. Rejea As-Sajdah (32:17), Adh-Dhaariyaat: (51:15-19), Al-Furqaan (25:63-64), Az-Zumar (39:9), Aal-‘Imraan (3:17), (3:113), Al-Muzzammil: (73:2).

 

[26] مَقَامًا مَّحْمُودًا : Maqaaman Mahmuwdan:: (Cheo Cha Kuhimidiwa)

 

“Maqaamun Mahmuwdun” ni cheo cha kuhimidiwa (kusifiwa). Ni cheo ambacho Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) ataomba Uombezi Mkuu "الشَّفَاعَةُ العُظْمَى" ili mambo yafunguke baada ya watu kuchoshwa na kutaabika mno na kisimamo kirefu cha kusubiri hisabu Siku ya Qiyaamah. Kwanza, watu watamwendea Nabiy  Aadam (عليه السّلام) wamtake aombe Shafaa’ah ili mambo yafunguke, naye atatoa udhuru, kisha watamwendea Nabiy Nuwh  (عليه السّلام), kisha Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام), kisha Nabiy Muwsaa (عليه السّلام), na Nabiy ‘Iysaa  (عليه السّلام), lakini wote watatoa nyudhuru. Hatimaye wataelekezwa waombe  kwa Sayyid (Bwana) wa wana wa Aadam yaani Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم), ili Allaah Awarehemu kutokana na khofu ya hali ya juu na dhiki ya  Siku hiyo. Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) atawaombea Shafaa’ah kwa Rabb wake, na Allaah (عزّ وجلّ) Atamuitikia na Atamsimamisha mahali patakapotamaniwa na kila wa mwanzo na wa mwisho, na itakuwa ni fadhila kwake juu ya viumbe wote. [Tafsiyr As-Sa’diy] 

 

Duaa Baada Ya Adhaan Kumuombea Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Maqaamun Mahmuwdun Ili Upate Shafaa-ah (Uombezi) Wake:

 

Amesimulia Jaabir Bin ‘Abdillaah (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Atakayesema baada ya kusikia Adhaana:

 

اللَّهُمَّ رَبَّ هَذِهِ الدَّعْوَةِ التَّامَّةِ وَالصَّلاَةِ الْقَائِمَةِ آتِ مُحَمَّدًا الْوَسِيلَةَ وَالْفَضِيلَةَ وَابْعَثْهُ مَقَامًا مَحْمُودًا الَّذِي وَعَدْتَهُ

Ee Rabb wa wito huu uliotimu, na Swalaah ya kudumu! Mpe Muhammad Wasiylah na daraja ya juu zaidi, na Mfufue Umpe Maqaam ya kuhimidiwa Uliyomwahidi.

 

Basi hapo atastahiki kupata Shafaa’ah (uombezi) yangu Siku ya Qiyaamah.”

 [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (614), Abuu Daawuwd (529), At-Tirmidhiy (211) na An-Nasaaiy (2/27)]

 

[27] Kuingizwa Pa Kheri Na Kutolewa Pa Kheri:

 

Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

رَّبِّ أَدْخِلْنِي مُدْخَلَ صِدْقٍ وَأَخْرِجْنِي مُخْرَجَ صِدْقٍ وَاجْعَل لِّي مِن لَّدُنكَ سُلْطَانًا نَّصِيرًا ﴿٨٠﴾

“Ee Rabb wangu! Niingize mwingizo wa kheri na Nitoe pa kutokea pa kheri na Nijaalie kutoka Kwako (hoja au) mamlaka yenye kunusuru.”

 

Yaani: Fanya kokote niingiako na kokote nitokako kuwe ni kwa ajili ya kukutii Wewe na kuzitafuta Radhi Zako. Na hii ni kwa sababu ya kujumuisha kwake kumtakasia Allaah na kuafikiana na Amri Yake (ya kuomba duaa hii).

 

Na:

وَاجْعَل لِّي مِن لَّدُنكَ سُلْطَانًا نَّصِيرًا ﴿٨٠﴾

“Na Nijaalie kutoka Kwako (hoja au) mamlaka yenye kunusuru.”

 

Yaani: Hoja ya dhahiri kabisa, na uthibitisho usio na shaka kwa yote ninayoyaendea na ninayoyaacha.

 

Na hii ndiyo hali ya juu kabisa Anayoiteremsha Allaah (عزّ وجلّ)  kwa mja, nayo ni kuwa, hali zake zote zinakuwa ni kheri na zenye kumkurubisha kwa Rabb wake, na pia anakuwa na  dalili na ushahidi wa wazi kabisa katika hali zake zote. Na  hiyo inajumuisha ilimu yenye manufaa, na amali njema, kwa kuyajua yote hayo vyema kwa dalili zake na ushahidi wake. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

[28] Haki Itabakia Na Ubatili Utatoweka:

 

Amesimulia ‘Abdullaah Bin Mas’uwd (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliingia Makkah (mwaka wa kuiteka) na yalikuwepo masanamu mia tatu na sitini kwenye Al-Ka‘bah. Akaanza kuyagonga na bakora iliyokuwa mkononi mwake, huku anasema:

 

جَاءَ الْحَقُّ وَزَهَقَ الْبَاطِلُ ۚ إِنَّ الْبَاطِلَ كَانَ زَهُوقًا ﴿٨١﴾

“Haki imekuja, na ubatili umetoweka. Hakika ubatili ni wenye kutoweka daima.” [Al-Israa (17:81)]

 

Na:

جَاءَ الْحَقُّ وَمَا يُبْدِئُ الْبَاطِلُ وَمَا يُعِيدُ ﴿٤٩﴾

“Haki imekuja, na ubatilifu hausimamishi (tena chochote), na wala haurudishi (kitu).” [Saba-a (34:49)] [Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo]

 

Rejea pia Saba-a (34:49).

 

[29] Qur-aan Ni Shifaa (Poza, Tiba), Mawaidha, Mwongozo, Rehma:

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Anatuambia kwamba Kitabu Chake, Alichomteremshia Rasuli Wake Muhammad, (صلى الله عليه وآله وسلم), nayo ni Qur-aan ambayo:

 

لَّا يَأْتِيهِ الْبَاطِلُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَلَا مِنْ خَلْفِهِ ۖ تَنزِيلٌ مِّنْ حَكِيمٍ حَمِيدٍ﴿٤٢﴾

“Hakitokifikia ubatili mbele yake wala nyuma yake. Ni Uteremsho kutoka kwa Mwenye Hikmah wa yote, Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa kwa yote.” [Fusw-Swilat (41:42)]

 

Ni shifaa (poza, tiba) na rehma kwa Waumini. Yaani: Inawaondolea yale yaliyomo ndani ya nyoyo zao za shaka, unafiki, shirki, kuchanganyikiwa na kuelemea ubatilifu. Qur-aan inaponya yote hayo. Pia ni rehma ambayo kwayo mtu hupata imaan na hikma na kutafuta wema. Haya ni kwa wale tu wanaoiamini na kuikubali kuwa ni ya haqq (kweli), ni shifaa (poza na tiba) na rehma kwa watu kama hao. Ama kafiri ambaye anajidhulumu nafsi yake kwa ukafiri wake, anapoisikia Qur-aan haimzidishii isipokuwa kujitenga nayo, kuikadhibisha, na kufru (kuikanusha).  Tatizo liko kwa kafiri mwenyewe, sio kwa Qur-aan, kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

قُلْ هُوَ لِلَّذِينَ آمَنُوا هُدًى وَشِفَاءٌ ۖ وَالَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ فِي آذَانِهِمْ وَقْرٌ وَهُوَ عَلَيْهِمْ عَمًى ۚ أُولَـٰئِكَ يُنَادَوْنَ مِن مَّكَانٍ بَعِيدٍ﴿٤٤﴾

“Sema: Hii (Qur-aan) kwa walioamini ni mwongozo na shifaa. Na wale wasioamini, wana uziwi masikioni mwao nayo ni upofu kwao. Hao wanaitwa kutoka mahali mbali.” [Fusw-Swilat (41:44)]

 

Rejea Suwrah hiyo ya Fusw-Swilat (41:44) na Yuwnus (10:57-58) kwenye uchambuzi kuhusu Qur-aan kuwa ni shifaa (poza na tiba), mawaidha na rehma kwa Waumini.

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَإِذَا مَا أُنزِلَتْ سُورَةٌ فَمِنْهُم مَّن يَقُولُ أَيُّكُمْ زَادَتْهُ هَـٰذِهِ إِيمَانًا ۚ فَأَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا فَزَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَهُمْ يَسْتَبْشِرُونَ﴿١٢٤﴾ وَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ فَزَادَتْهُمْ رِجْسًا إِلَىٰ رِجْسِهِمْ وَمَاتُوا وَهُمْ كَافِرُونَ﴿١٢٥﴾

Na inapoteremshwa Suwrah, basi miongoni mwao wako wanaosema: Nani kati yenu imemzidishia (Suwrah) hii imaan? Ama wale walioamini huwazidishia imaan nao wanafurahia. Na ama wale ambao katika nyoyo zao mna maradhi, huwazidishia rijs (unafiki, shaka n.k.) juu ya rijs yao, na wakafa hali wao ni makafiri.” [At-Tawbah (9:124-125)].

 

Na kuna Aayah nyingi zinazotaja haya. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

Rejea Suwrah hiyo ya At-Tawbah (9:124-135) kwenye maelezo kuhusu Qur-aan inaposomwa, inawazidisha Waumini imaan. Ama kafiri na wenye maradhi katika nyoyo zao, haiwazidishii ila rijs (unafiki, shaka kufru n.k).

 

[30] Hali Ya Binaadam Asiyekuwa Muumini Anapopatwa Dhara:

 

Rejea Yuwnus (10:12).

 

[31] Maana Za Ruwh Katika Qur-aan:

 

Rejea An-Nahl (16:2).

 

[32] Roho Ni Jambo La Allaah Pekee:

 

Sababu ya kuteremka Aayah hii inapatikana Alhidaaya.com 085-Asbaabun-Nuzuwl: Al-Israa Aayah 085: وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الرُّوحِ ۖ قُلِ الرُّوحُ مِنْ أَمْرِ رَبِّي وَمَا أُوتِيتُم مِّنَ الْعِلْمِ إِلَّا قَلِيلًا

 

Ulamaa wamekhitilafiana kuhusu roho ilokusudiwa: Kuna waliosema ni roho za binaadam, au Jibriyl au Malaika?

 

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ، قَالَ كُنْتُ أَمْشِي مَعَ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم فِي حَرْثٍ بِالْمَدِينَةِ وَهْوَ مُتَّكِئٌ عَلَى عَسِيبٍ، فَمَرَّ بِقَوْمٍ مِنَ الْيَهُودِ فَقَالَ بَعْضُهُمْ لِبَعْضٍ سَلُوهُ عَنِ الرُّوحِ‏.‏ وَقَالَ بَعْضُهُمْ لاَ تَسْأَلُوهُ عَنِ الرُّوحِ‏.‏ فَسَأَلُوهُ فَقَامَ مُتَوَكِّئًا عَلَى الْعَسِيبِ وَأَنَا خَلْفَهُ، فَظَنَنْتُ أَنَّهُ يُوحَى إِلَيْهِ فَقَالَ ‏((‏وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الرُّوحِ قُلِ الرُّوحُ مِنْ أَمْرِ رَبِّي وَمَا أُوتِيتُمْ مِنَ الْعِلْمِ إِلاَّ قَلِيلاً‏))‏ فَقَالَ بَعْضُهُمْ لِبَعْضٍ قَدْ قُلْنَا لَكُمْ لاَ تَسْأَلُوهُ‏.‏

Amesimulia ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه): Nilikuwa natembea na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) katika mashamba ya Madiynah, naye alikuwa akitembea kwa kuegemea kuti la mtende. Mara akalipita kundi la Mayahudi na wao wakaambizana wamuulize kuhusu roho. Baadhi yao wakasema: Msimuulize kuhusu roho. Lakini wakamuuliza. Akainuka kwa kutegemea kuti la mtende, nami niko nyuma yake, nikidhani kuwa anateremshiwa Wahyi. Kisha akasoma:

 

وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الرُّوحِ ۖ قُلِ الرُّوحُ مِنْ أَمْرِ رَبِّي وَمَا أُوتِيتُم مِّنَ الْعِلْمِ إِلَّا قَلِيلًا ﴿٨٥﴾

“Na wanakuuliza kuhusu roho. Sema: Roho ni katika amri ya Rabb wangu. Na hamkupewa ujuzi isipokuwa kidogo tu.”

 

Hapo baadhi ya Mayahudi wakasema (kuwaambia wenzao): “Si tulikuambieni kuwa msimuulize (hamkusikia)?”

[Al-Bukhaariy – Kitaab At-Tawhiyd]

 

[34] Changamoto Kwa Makafiri Walete Mfano Wa Qur-aan Lakini Hilo Ni Mustahili:

 

Rejea Yuwnus (10:38), Al-Baqarah (2:23-24), Atw-Twuwr (52:33-34), Huwd (11:13-14). Rejea pia Al-An’aam (6:93) ambako kumetajwa waongo waliodai Unabii.

 

[35] Washirikina Kudai Kutumiwa Rasuli Asiyekuwa Binaadam:

 

Kuanzia Aayah hii (90) hadi (93) washirikina wa Makkah wanadai kuteremshiwa mambo ya ajabu kabisa yote kumpinga Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa kuwa yeye ni binaadam. Lakini Allaah (سبحانه وتعالى) Anawahoji kwa dalili za nguvu kabisa katika Aayah namba (95).

 

Na hii ndio ada ya washirikina kutowaamini Rusuli wao kwa sababu tu ni binaadam.

 

Na washirikina wa kaumu za kale walidai hivyo pia. Basi wao na hawa wa Makkah madai yao kama haya kutaka kuteremshiwa asiyekuwa binaadam yalilingana. Rejea Huwd (11:27), Ibraahiym (14:10), Al-Anbiyaa (21:3), Al-Muuminuwn: (23:24),  (33-34), (47). Rejea pia Al-Furqaan (25:7), Ash-Shu’araa (26:154), (186). Pia Yaasiyn (36:15), Al-Qamar (54:24) na At-Taghaabun (64:6).

 

[36] Makafiri Watakusanywa Juu Ya Nyuso Zao Siku Ya Qiyaamah:

 

Rejea Al-Furqaan (25:34).

 

[37] Makafiri Hawakuamini Kwamba Watafufuliwa: Rejea Aayah kwenye Suwrah hii ya Al-Israa (17:49).

 

[38] Miujiza Tisa Ya Allaah Kwa Watu Wa Firawni: Rejea Al-A’raaf (7:130).

 

[39] Hikma Ya Qur-aan Kuteremshwa Kwa Vituo Na Kidogo Kidogo:

 

Kuna hikma kadhaa za kuteremshwa

Qur-aan kwa vituo na kidogo kidogo. Miongoni mwazo ni: kuwasahilishia Swahaba hukmu za makatazo ya maasi waliyokuwa nayo katika Ujaahiliyyah:

 

Rejea Alhidaaya.com Makala ya: Hikmah Ya Kuteremshwa Qur-aan Kidogokidogo Wakati Mbali Mbali.

 

Moja ya hikma ni kuwavutia watu kuingia katika Dini kwa kufuata maamrisho yake na makatazo yake polepole, na hii ni njia itumikayo na yenye matunda katika daawah.  Kwani ingelikuwa ni kufuata makatazo yote na kufuata maamrisho yote kwa pamoja, basi ingelikuwa ni vigumu sana watu kufuata,  na ndio maana kwa muda wa miaka kumi Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipokuwa Makkah, hakukuwa na zaidi ya kuwaita watu kuingia katika Dini. Neno la  “Laa ilaah illa-Allaah” ndilo lililokuwa lengo, hakukuwa na amri za fardhi yoyote wala hukmu zozote.

 

Mfano, makatazo ya ulevi, kwa vile ulevi ulikuwa ni moja ya maasi makuu, na hata baada ya kuja Uislamu, baadhi ya Swahaba walikuwa bado wakilewa. Hii ni kwa sababu ilikuwa ni ada na desturi zao walizozirithi katika ujaahiliyyah kama zilivyo desturi nyinginezo walizokuwa nazo kama kuwaua watoto wa kike, kuwanyima urithi wanawake n.k. Ukaja Uislamu na kuondosha dhulma zote hizo.  Hivyo, jambo kama ulevi lilihitajika hikma ya kuukataza kwa polepole na ndio maana tunaona kwamba kuna Aayah tatu zinazohusiana na makatazo ya ulevi. Ilianza kwanza kwa kutaja madhara yake na manufaa yake, kisha polepole hadi kukataza kabisa. Hadiyth ifuatayo imethibitisha hayo:

 

حَدَّثَنَا إِبْرَاهِيمُ بْنُ مُوسَى، أَخْبَرَنَا هِشَامُ بْنُ يُوسُفَ، أَنَّ ابْنَ جُرَيْجٍ، أَخْبَرَهُمْ قَالَ وَأَخْبَرَنِي يُوسُفُ بْنُ مَاهَكَ، قَالَ إِنِّي عِنْدَ عَائِشَةَ أُمِّ الْمُؤْمِنِينَ ـ رضى الله عنها ـ إِذْ جَاءَهَا عِرَاقِيٌّ فَقَالَ أَىُّ الْكَفَنِ خَيْرٌ قَالَتْ وَيْحَكَ وَمَا يَضُرُّكَ قَالَ يَا أُمَّ الْمُؤْمِنِينَ أَرِينِي مُصْحَفَكِ‏.‏ قَالَتْ لِمَ قَالَ لَعَلِّي أُوَلِّفُ الْقُرْآنَ عَلَيْهِ فَإِنَّهُ يُقْرَأُ غَيْرَ مُؤَلَّفٍ‏.‏ قَالَتْ وَمَا يَضُرُّكَ أَيَّهُ قَرَأْتَ قَبْلُ، إِنَّمَا نَزَلَ أَوَّلَ مَا نَزَلَ مِنْهُ سُورَةٌ مِنَ الْمُفَصَّلِ فِيهَا ذِكْرُ الْجَنَّةِ وَالنَّارِ حَتَّى إِذَا ثَابَ النَّاسُ إِلَى الإِسْلاَمِ نَزَلَ الْحَلاَلُ وَالْحَرَامُ، وَلَوْ نَزَلَ أَوَّلَ شَىْءٍ لاَ تَشْرَبُوا الْخَمْرَ‏.‏ لَقَالُوا لاَ نَدَعُ الْخَمْرَ أَبَدًا‏.‏ وَلَوْ نَزَلَ‏.‏ لاَ تَزْنُوا‏.‏ لَقَالُوا لاَ نَدَعُ الزِّنَا أَبَدًا‏.‏

 

Ametuhadithia Ibraahiym bin Muwsaa, ametujulisha Hishaam bin Yuwsuf, kwamba Ibn Jurayj amewajulisha amesema: Amesema au amenijulisha Yuwsuf bin Maahak kuwa alipokuwa pamoja na ‘Aaishah Mama wa Waumini  (رضي الله عنها), mara akaja kwake mtu kutoka Iraaq, akamuuliza: Ni kafani (sanda) gani iliyo bora zaidi? Akasema (رضي الله عنها): Allaah Akurehemu! Itakusaidia nini kujua hilo (ukiwa maiti sanda yoyote utakafiniwa nayo)?! Akasema: Ee Mama wa Waumini, nionyeshe Mswahafu wako. Akasema (رضي الله عنها): Kwa nini? Akasema: Huenda nikaukusanya na kuipanga Qur-aan kulingana nayo, kwani watu wanaisoma pamoja na Suwrah zake sio kwa mpangilio wa sawasawa. Akasema (رضي الله عنها): Haijalishi ni sehemu gani unayosoma mwanzo. (Fahamu kuwa) kitu cha kwanza kuteremshwa kwayo ni Suwrah za al-Mufaswswal (fupi fupi) ambazo kumetajwa ndani yake Jannah na Moto. Na watu wanapokuwa wamekomaa na nafsi zao kutulia juu ya hilo, Aayah kuhusiana na halali na haramu ziliteremshwa. Na lau ingeteremshwa mwanzo (kwa mfano): “Msinywe pombe (mvinyo)”, watu wangesema: “Hatutaacha kunywa (pombe)”. Na lau kungeteremshwa: “Msizini”, watu wangesema: “Hatutaacha kuzini”.  [Al-Bukhaariy]

 

[40] Washirikina Walipinga Jina La Ar-Rahmaan: 

 

Rejea pia Al-Furqaan (25:60).

 

Sifa hii ya Rahmah ni ya dhati Yake Allaah ambayo haiwezi kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى). Makafiri wa Makkah hawakupenda Sifa na Jina hili la Ar-Rahmaan. Basi wakakataa kuliandika katika mkataba wa Hudaybiyah, pale Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipomuamrisha mwandishi wa mkataba andike “BismiLLaah (Kwa Jina la Allaah) Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rehma) Ar-Rahiym (Mwenye kurehemu).” Wakasema: “Andika: Biismika-Allaahumma.”  Hapo Allaah (سبحانه وتعالى) Akateremsha:

قُلِ ادْعُوا اللَّـهَ أَوِ ادْعُوا الرَّحْمَـٰنَ ۖ أَيًّا مَّا تَدْعُوا فَلَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ ۚ  

“Sema: Muiteni Allaah au muiteni Ar-Rahmaan, vyovyote mtakavyomwita basi Yeye Ana Majina Mazuri kabisa.”  [Al-Israa: 110]

[Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

Na ndio maana Suwrah za Qur-aan zinaanza na BismiLLaah ambayo inataja Majina Yake Mawili ya Ar-Rahmaan na Ar-Rahiym. Pia Allaah (سبحانه وتعالى) Ametanguliza katika ufunguzi wa Suwrat Al-Faatihah Akaanza na Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rehma) na Ar-Rahiym (Mwenye Kurehemu).

 

Na Imaam As-Sa’diy amefafanua: “Sema, ee Rasuli kuwaambia washirikina wa watu wako waliokupinga kutumia kwako “Yaa Allaah”, “Yaa Rahmaan”, katika duaa zako. Muiteni Allaah au muiteni Ar-Rahmaan kwani kwa Majina yoyote Yake mkimuomba huwa mnamuomba Rabb Mmoja, kwa kuwa Majina Yake yote ni Mazuri. [Tafsiyr Al-Muyassar]

 

[41] Majina Mazuri Kabisa Ya Allaah (سبحانه وتعالى): Rejea Faharasa ya Majina Mazuri Kabisa Ya Allaah Na Sifa Zake.

 

[43] Allaah Yu Mmoja Pekee Hana Mwana Wala Mshirika Wala Msaidizi Basi Mtukuze Matukuzo Makubwa Kabisa:

 

Washirikina walidai na kumsingizia Allaah (سبحانه وتعالى) kwamba Ana mwana na kwamba Anao wasaidizi na walinzi kwa ajili ya usimamizi wa Ufalme Wake kana kwamba Hana uwezo wa kutekeleza usimamizi wa Ufalme Wake, kwa hiyo Anahitajia wasaidizi na walinzi. Basi Allaah (سبحانه وتعالى) Anakusha hilo, kwani Ufalme wa mbingu na ardhi ni Wake wote Yeye (سبحانه وتعالى). Naye Yuko Pekee Hana mwana wala mshirika wala msaidizi. Yeye ni Mkwasi, Hahitaji chochote kwa viumbe, bali wao  mafakiri ndio wenye kumhitaji, na wao ndio wenye udhalili. Hivyo, Allaah Anaamrisha kumhimidi Yeye na kumsifu na kumtukuza kwa Majina Yake Mazuri Kabisa na Sifa Zake Kamilifu. Basi mtukuze kwa matukuzo makubwa kabisa ya Ujalali na Utukufu Wake. AlhamduliLlaah, Yeye ni Allaahu Akbar (Mkuu wa Dhati kwa Sifa na Matendo).   

 

 

 

Share