022 - Al-Hajj

 

الْحَجّ

 

022-Al-Hajj

 

 

022-Al-Hajj:Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمْ ۚ إِنَّ زَلْزَلَةَ السَّاعَةِ شَيْءٌ عَظِيمٌ ﴿١﴾

1. Enyi watu! Mcheni Rabb wenu. Hakika zilizala la Saa ni jambo kuu.[1]

 

 

 

يَوْمَ تَرَوْنَهَا تَذْهَلُ كُلُّ مُرْضِعَةٍ عَمَّا أَرْضَعَتْ وَتَضَعُ كُلُّ ذَاتِ حَمْلٍ حَمْلَهَا وَتَرَى النَّاسَ سُكَارَىٰ وَمَا هُم بِسُكَارَىٰ وَلَـٰكِنَّ عَذَابَ اللَّـهِ شَدِيدٌ ﴿٢﴾

2. Siku mtakapoiona, kila mnyonyeshaji atamsahau anayemnyonyesha, na kila mwenye mimba ataizaa mimba yake, na utawaona watu wamelewa, kumbe hawakulewa lakini ni Adhabu ya Allaah kali! 

 

 

 

وَمِنَ النَّاسِ مَن يُجَادِلُ فِي اللَّـهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَيَتَّبِعُ كُلَّ شَيْطَانٍ مَّرِيدٍ ﴿٣﴾

3. Na miongoni mwa watu kuna ambao wanaobishana kuhusu Allaah bila ya ilimu, na wanafuata kila shaytwaan asi.

 

 

 

كُتِبَ عَلَيْهِ أَنَّهُ مَن تَوَلَّاهُ فَأَنَّهُ يُضِلُّهُ وَيَهْدِيهِ إِلَىٰ عَذَابِ السَّعِيرِ ﴿٤﴾

4. Ameandikiwa (shaytwaan) kwamba atakayemfanya rafiki, basi yeye atampoteza na atamuongoza katika adhabu ya moto uliowashwa vikali mno!

 

 

 

يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِن كُنتُمْ فِي رَيْبٍ مِّنَ الْبَعْثِ فَإِنَّا خَلَقْنَاكُم مِّن تُرَابٍ ثُمَّ مِن نُّطْفَةٍ ثُمَّ مِنْ عَلَقَةٍ ثُمَّ مِن مُّضْغَةٍ مُّخَلَّقَةٍ وَغَيْرِ مُخَلَّقَةٍ لِّنُبَيِّنَ لَكُمْ ۚ وَنُقِرُّ فِي الْأَرْحَامِ مَا نَشَاءُ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ثُمَّ نُخْرِجُكُمْ طِفْلًا ثُمَّ لِتَبْلُغُوا أَشُدَّكُمْ ۖ وَمِنكُم مَّن يُتَوَفَّىٰ وَمِنكُم مَّن يُرَدُّ إِلَىٰ أَرْذَلِ الْعُمُرِ لِكَيْلَا يَعْلَمَ مِن بَعْدِ عِلْمٍ شَيْئًا ۚ وَتَرَى الْأَرْضَ هَامِدَةً فَإِذَا أَنزَلْنَا عَلَيْهَا الْمَاءَ اهْتَزَّتْ وَرَبَتْ وَأَنبَتَتْ مِن كُلِّ زَوْجٍ بَهِيجٍ ﴿٥﴾

5. Enyi watu! Mkiwa mko katika shaka ya kufufuliwa, basi hakika Sisi Tumekuumbeni kutokana na udongo, kisha kutokana na manii, kisha kutokana na pande la damu linaloning’inia, kisha kutokana na kinofu cha nyama kinachotiwa umbo kamili na kisichotiwa umbo kamili, ili Tukubainishieni. Na Tunakikalisha katika fuko la uzazi Tukitakacho mpaka muda maalumu uliokadiriwa. Kisha Tunakutoeni mkiwa watoto wadogo, kisha ili mfikie umri wa kupevuka kwenu. Na miongoni mwenu yuko anayefishwa, na miongoni mwenu yuko anayerudishwa kwenye umri mbaya na dhaifu zaidi hata awe hajui kitu chochote kile baada ya kuwa anakijua. Na utaona ardhi kame, lakini Tunapoiteremshia maji hutikisika na kuumuka, na inaotesha mimea ya kila namna, mizuri yakupendeza.[2]

 

 

 

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ وَأَنَّهُ يُحْيِي الْمَوْتَىٰ وَأَنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٦﴾

6. Hayo (Tuliyoyataja ni dalili) kuwa Allaah Ndiye wa Haki, na kwamba Yeye Anahuisha wafu, na kwamba Yeye juu ya kila kitu Ni Muweza.

 

 

 

وَأَنَّ السَّاعَةَ آتِيَةٌ لَّا رَيْبَ فِيهَا وَأَنَّ اللَّـهَ يَبْعَثُ مَن فِي الْقُبُورِ ﴿٧﴾

7. Na kwamba Saa itafika tu haina shaka ndani yake, na kwamba Allaah Atafufua waliomo makaburini.

 

 

 

وَمِنَ النَّاسِ مَن يُجَادِلُ فِي اللَّـهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَلَا هُدًى وَلَا كِتَابٍ مُّنِيرٍ ﴿٨﴾

8. Na miongoni mwa watu wako wanaobishana kuhusu Allaah bila ya ilimu wala mwongozo wala Kitabu chenye Nuru.

 

 

 

ثَانِيَ عِطْفِهِ لِيُضِلَّ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۖ لَهُ فِي الدُّنْيَا خِزْيٌ ۖ وَنُذِيقُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ عَذَابَ الْحَرِيقِ ﴿٩﴾

9. Mwenye kugeuza shingo yake kwa kibri ili apoteze (watu) Njia ya Allaah. Atapata duniani hizaya, na Tutamuonjesha Siku ya Qiyaamah adhabu ya kuungua.

 

 

 

ذَٰلِكَ بِمَا قَدَّمَتْ يَدَاكَ وَأَنَّ اللَّـهَ لَيْسَ بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ ﴿١٠﴾

10. (Ataambiwa): Hayo ni kwa sababu ya yale iliyotanguliza mikono yako, na kwamba Allaah Si Mwenye Kudhulumu waja katu.

 

 

 

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَعْبُدُ اللَّـهَ عَلَىٰ حَرْفٍ ۖ فَإِنْ أَصَابَهُ خَيْرٌ اطْمَأَنَّ بِهِ ۖ وَإِنْ أَصَابَتْهُ فِتْنَةٌ انقَلَبَ عَلَىٰ وَجْهِهِ خَسِرَ الدُّنْيَا وَالْآخِرَةَ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْخُسْرَانُ الْمُبِينُ ﴿١١﴾

11. Na miongoni mwa watu yuko anayemwabudu Allaah ukingoni. Inapompata kheri hutumainika kwayo, lakini unapompata mtihani hugeuka kurudi kule kwa mwanzo (kwenye kufru).[3] Amekhasirika duniani na Aakhirah. Hiyo ndiyo khasara bayana.

 

 

 

يَدْعُو مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُ وَمَا لَا يَنفَعُهُ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الضَّلَالُ الْبَعِيدُ ﴿١٢﴾

12. Badala ya Allaah, yeye huviomba ambavyo havimdhuru na ambavyo havimnufaishi. Huo ndio upotofu wa mbali.

 

 

 

يَدْعُو لَمَن ضَرُّهُ أَقْرَبُ مِن نَّفْعِهِ ۚ لَبِئْسَ الْمَوْلَىٰ وَلَبِئْسَ الْعَشِيرُ ﴿١٣﴾

13. Humwomba yule ambaye madhara yake yako karibu kuliko manufaa yake. Bila shaka ni mlinzi muovu kabisa, na bila shaka ni rafiki muovu kabisa.

 

 

 

إِنَّ اللَّـهَ يُدْخِلُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَفْعَلُ مَا يُرِيدُ ﴿١٤﴾

14. Hakika Allaah Atawaingiza wale walioamini na wakatenda mema Jannaat zipitazo chini yake mito. Hakika Allaah Anafanya Atakavyo.

 

 

 

مَن كَانَ يَظُنُّ أَن لَّن يَنصُرَهُ اللَّـهُ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ فَلْيَمْدُدْ بِسَبَبٍ إِلَى السَّمَاءِ ثُمَّ لْيَقْطَعْ فَلْيَنظُرْ هَلْ يُذْهِبَنَّ كَيْدُهُ مَا يَغِيظُ ﴿١٥﴾

15. Yeyote yule anayedhani kwamba Allaah Hatomnusuru (Rasuli) duniani na Aakhirah, basi na afunge kitanzi juu, kisha akikate (ajinyoge), na atazame. Je, hila zake zaweza kuondoa yaliyomghadhibisha? 

 

 

 

وَكَذَٰلِكَ أَنزَلْنَاهُ آيَاتٍ بَيِّنَاتٍ وَأَنَّ اللَّـهَ يَهْدِي مَن يُرِيدُ ﴿١٦﴾

16. Na hivyo ndivyo Tumeiteremsha (Qur-aan yenye) Aayaat bayana, na kwamba Allaah Humwongoza Amtakaye.

 

 

 

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَالَّذِينَ هَادُوا وَالصَّابِئِينَ وَالنَّصَارَىٰ وَالْمَجُوسَ وَالَّذِينَ أَشْرَكُوا إِنَّ اللَّـهَ يَفْصِلُ بَيْنَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ ﴿١٧﴾

17. Hakika wale walioamini, na ambao ni Mayahudi, na Wasabai na Manaswara, na Majusi, na wale wanaoshirikisha[4], hakika Allaah Atahukumu baina yao Siku ya Qiyaamah. Hakika Allaah Ni Shahidi juu ya kila kitu.

 

 

 

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ يَسْجُدُ لَهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الْأَرْضِ وَالشَّمْسُ وَالْقَمَرُ وَالنُّجُومُ وَالْجِبَالُ وَالشَّجَرُ وَالدَّوَابُّ وَكَثِيرٌ مِّنَ النَّاسِ ۖ وَكَثِيرٌ حَقَّ عَلَيْهِ الْعَذَابُ ۗ وَمَن يُهِنِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِن مُّكْرِمٍ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَفْعَلُ مَا يَشَاءُ ۩﴿١٨﴾

18. Je, huoni kwamba wanamsujudia Allaah walioko mbinguni na ardhini, na jua, na mwezi, na nyota, na milima, na miti, na viumbe vinavyotembea, na wengi miongoni mwa watu? Na wengi imewastahikia adhabu. Na ambaye Allaah Amemdhalilisha, basi hatopata wa kumthamini. Hakika Allaah Anafanya Atakavyo.[5]

 

 

 

 

هَـٰذَانِ خَصْمَانِ اخْتَصَمُوا فِي رَبِّهِمْ ۖ فَالَّذِينَ كَفَرُوا قُطِّعَتْ لَهُمْ ثِيَابٌ مِّن نَّارٍ يُصَبُّ مِن فَوْقِ رُءُوسِهِمُ الْحَمِيمُ ﴿١٩﴾

19. Hawa ni wapinzani wawili (walioamini na makafiri) wanabishana kuhusu Rabb wao. Basi wale waliokufuru, watakatiwa nguo za moto na watamwagiwa juu ya vichwa vyao maji yachemkayo sana. 

 

 

 

 

يُصْهَرُ بِهِ مَا فِي بُطُونِهِمْ وَالْجُلُودُ ﴿٢٠﴾

20.  Yatayeyushwa kwayo (maji hayo) yaliyomo matumboni mwao na ngozi zao.

 

 

 

وَلَهُم مَّقَامِعُ مِنْ حَدِيدٍ ﴿٢١﴾

21. Na watapata marungu ya chuma.

 

 

 

كُلَّمَا أَرَادُوا أَن يَخْرُجُوا مِنْهَا مِنْ غَمٍّ أُعِيدُوا فِيهَا وَذُوقُوا عَذَابَ الْحَرِيقِ ﴿٢٢﴾

22. Kila watakapotaka kutoka humo kwa sababu ya dhiki, watarudishwa humo, na (wataambiwa): Onjeni adhabu ya kuunguza.

 

 

 

إِنَّ اللَّـهَ يُدْخِلُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ يُحَلَّوْنَ فِيهَا مِنْ أَسَاوِرَ مِن ذَهَبٍ وَلُؤْلُؤًا ۖ وَلِبَاسُهُمْ فِيهَا حَرِيرٌ ﴿٢٣﴾

23. Hakika Allaah Atawaingiza wale walioamini na wakatenda mema Jannaat zipitazo chini yake mito, watapambwa humo kwa vikuku vya dhahabu na lulu, na mavazi yao humo ni hariri.

 

 

 

وَهُدُوا إِلَى الطَّيِّبِ مِنَ الْقَوْلِ وَهُدُوا إِلَىٰ صِرَاطِ الْحَمِيدِ ﴿٢٤﴾

24. Na wataongozwa kwenye kauli nzuri na wataongozwa kwenye njia ya Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa kwa yote.

 

 

 

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا وَيَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ وَالْمَسْجِدِ الْحَرَامِ الَّذِي جَعَلْنَاهُ لِلنَّاسِ سَوَاءً الْعَاكِفُ فِيهِ وَالْبَادِ ۚ وَمَن يُرِدْ فِيهِ بِإِلْحَادٍ بِظُلْمٍ نُّذِقْهُ مِنْ عَذَابٍ أَلِيمٍ ﴿٢٥﴾

25. Hakika wale waliokufuru na wanazuia Njia ya Allaah na Al-Masjid Al-Haraam ambao Tumeufanya kwa watu wote kuwa ni sawasawa; kwa wakaao humo na wageni. Na yeyote anayekusudia humo kufanya upotofu kwa dhulma Tutamuonjesha adhabu iumizayo.

 

 

 

وَإِذْ بَوَّأْنَا لِإِبْرَاهِيمَ مَكَانَ الْبَيْتِ أَن لَّا تُشْرِكْ بِي شَيْئًا وَطَهِّرْ بَيْتِيَ لِلطَّائِفِينَ وَالْقَائِمِينَ وَالرُّكَّعِ السُّجُودِ ﴿٢٦﴾

26. Na (taja) Tulipomwonyesha Ibraahiym mahali pa Nyumba; Al-Ka’bah, (Tukamwambia): Usinishirikishe na chochote, na twaharisha Nyumba Yangu kwa wafanyao Twawaaf, na wanaosimama kuswali na wanaorukuu na kusujudu.[6]

 

 

 

وَأَذِّن فِي النَّاسِ بِالْحَجِّ يَأْتُوكَ رِجَالًا وَعَلَىٰ كُلِّ ضَامِرٍ يَأْتِينَ مِن كُلِّ فَجٍّ عَمِيقٍ ﴿٢٧﴾

27. Na tangaza kwa watu Hajj, watakufikia kwa miguu na juu ya kila ngamia aliyekonda, watakuja kutoka katika kila njia pana za milima zilioko mbali kabisa.

 

 

 

لِّيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ فِي أَيَّامٍ مَّعْلُومَاتٍ عَلَىٰ مَا رَزَقَهُم مِّن بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ ۖ فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْبَائِسَ الْفَقِيرَ ﴿٢٨﴾

28. Ili washuhudie manufaa yao, na walitaje Jina la Allaah katika siku maalumu[7] kupitia yale Aliyowaruzuku kati ya wanyama wenye miguu minne wa mifugo. Basi kuleni sehemu ya nyama yake, na lisheni mwenye shida fakiri.

 

 

 

ثُمَّ لْيَقْضُوا تَفَثَهُمْ وَلْيُوفُوا نُذُورَهُمْ وَلْيَطَّوَّفُوا بِالْبَيْتِ الْعَتِيقِ ﴿٢٩﴾

29. Kisha wajisafishe taka zao na watimize nadhiri zao, na watufu kwenye Nyumba ya Kale (Al-Ka’bah). 

 

 

 

ذَٰلِكَ وَمَن يُعَظِّمْ حُرُمَاتِ اللَّـهِ فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ عِندَ رَبِّهِ ۗ وَأُحِلَّتْ لَكُمُ الْأَنْعَامُ إِلَّا مَا يُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ ۖ فَاجْتَنِبُوا الرِّجْسَ مِنَ الْأَوْثَانِ وَاجْتَنِبُوا قَوْلَ الزُّورِ ﴿٣٠﴾

30. Ndio hivyo iwe.  Na yeyote anayeadhimisha Vitukufu vya Allaah basi hivyo ni kheri kwake mbele ya Rabb wake. Na mmehalalishiwa wanyama wa mifugo isipokuwa wale mnaosomewa. Basi jiepusheni na uchafu wa (kuabudu) masanamu, na jiepusheni na kauli za uongo.

 

 

 

حُنَفَاءَ لِلَّـهِ غَيْرَ مُشْرِكِينَ بِهِ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَكَأَنَّمَا خَرَّ مِنَ السَّمَاءِ فَتَخْطَفُهُ الطَّيْرُ أَوْ تَهْوِي بِهِ الرِّيحُ فِي مَكَانٍ سَحِيقٍ ﴿٣١﴾

31. Huku mkiielemea haki kwa kumwabudu Allaah Pekee bila ya kumshirikisha. Na yeyote anayemshirikisha Allaah, basi ni kama kwamba ameporomoka kutoka mbinguni, wakamnyakua ndege au upepo ukamtupa mahali mbali mno.

 

 

 

ذَٰلِكَ وَمَن يُعَظِّمْ شَعَائِرَ اللَّـهِ فَإِنَّهَا مِن تَقْوَى الْقُلُوبِ ﴿٣٢﴾

32. Hayo ndio hivyo. Na yeyote anayeadhimisha Ishara za Allaah, basi hayo ni katika taqwa ya nyoyo.

 

 

 

لَكُمْ فِيهَا مَنَافِعُ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ثُمَّ مَحِلُّهَا إِلَى الْبَيْتِ الْعَتِيقِ ﴿٣٣﴾

33. Katika hao (wanyama) mnapata humo manufaa mpaka muda maalumu uliokadiriwa. Kisha kuhalalika kwake kuchinjwa ni kwenye Nyumba ya Kale. (Haram ya Makkah).

 

 

 

 

وَلِكُلِّ أُمَّةٍ جَعَلْنَا مَنسَكًا لِّيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ عَلَىٰ مَا رَزَقَهُم مِّن بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ ۗ فَإِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ فَلَهُ أَسْلِمُوا ۗ وَبَشِّرِ الْمُخْبِتِينَ ﴿٣٤﴾

34. Na kwa kila Ummah Tumeweka taratibu za ibaada ili wataje Jina la Allaah kwa yale Aliyowaruzuku ya wanyama wa miguu minne wa mifugo. Kwa hiyo Mwabudiwa wenu wa haki Ni Ilaah Mmoja Pekee, basi jisalimisheni Kwake. Na wabashirie wanyenyekevu.

 

 

 

الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَالصَّابِرِينَ عَلَىٰ مَا أَصَابَهُمْ وَالْمُقِيمِي الصَّلَاةِ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ ﴿٣٥﴾

35. Ambao Anapotajwa Allaah nyoyo zao zinajaa khofu, na wanaosubiri juu ya yale yaliyowasibu, na wanaosimamisha Swalaah na katika vile Tulivyowaruzuku wanatoa.

 

 

 

وَالْبُدْنَ جَعَلْنَاهَا لَكُم مِّن شَعَائِرِ اللَّـهِ لَكُمْ فِيهَا خَيْرٌ ۖ فَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ عَلَيْهَا صَوَافَّ ۖ فَإِذَا وَجَبَتْ جُنُوبُهَا فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْقَانِعَ وَالْمُعْتَرَّ ۚ كَذَٰلِكَ سَخَّرْنَاهَا لَكُمْ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿٣٦﴾

36. Na ngamia na ng’ombe Tumekufanyieni kuwa ni miongoni mwa Ishara za Allaah, kwa hao mnapata kheri nyingi. Basi tajeni Jina la Allaah juu yao wanapopangwa safu (kuchinjwa). Na waangukapo ubavu, basi kuleni sehemu ya nyama yao, na lisheni waliokinai na wanaolazimika kuomba. Hivyo ndivyo Tulivyowatiisha kwa ajili yenu ili mpate kushukuru.

 

 

 

لَن يَنَالَ اللَّـهَ لُحُومُهَا وَلَا دِمَاؤُهَا وَلَـٰكِن يَنَالُهُ التَّقْوَىٰ مِنكُمْ ۚ كَذَٰلِكَ سَخَّرَهَا لَكُمْ لِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ ۗ وَبَشِّرِ الْمُحْسِنِينَ ﴿٣٧﴾

37. Hazimfikii Allaah nyama zake wala damu zake, lakini inamfikia taqwa kutoka kwenu. Hivyo ndivyo Tulivyowatiisha kwenu ili mpate kumtukuza Allaah kwa kuwa Amekuongozeni. Na wabashirie wafanyao ihsaan.

 

 

 

 

إِنَّ اللَّـهَ يُدَافِعُ عَنِ الَّذِينَ آمَنُوا ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ كُلَّ خَوَّانٍ كَفُورٍ ﴿٣٨﴾

38. Hakika Allaah Anawalinda wale walioamini. Hakika Allaah Hampendi kila mwenye tabia ya kukhini, mwingi wa kukufuru.

 

 

 

أُذِنَ لِلَّذِينَ يُقَاتَلُونَ بِأَنَّهُمْ ظُلِمُوا ۚ وَإِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ نَصْرِهِمْ لَقَدِيرٌ ﴿٣٩﴾

39. Wameruhusiwa (kupigana) wale wanaopigwa kwa kuwa wamedhulumiwa. Na hakika Allaah bila shaka Ni Muweza wa Kuwanusuru.

 

 

 

الَّذِينَ أُخْرِجُوا مِن دِيَارِهِم بِغَيْرِ حَقٍّ إِلَّا أَن يَقُولُوا رَبُّنَا اللَّـهُ ۗ وَلَوْلَا دَفْعُ اللَّـهِ النَّاسَ بَعْضَهُم بِبَعْضٍ لَّهُدِّمَتْ صَوَامِعُ وَبِيَعٌ وَصَلَوَاتٌ وَمَسَاجِدُ يُذْكَرُ فِيهَا اسْمُ اللَّـهِ كَثِيرًا ۗ وَلَيَنصُرَنَّ اللَّـهُ مَن يَنصُرُهُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ ﴿٤٠﴾

40. Ambao wametolewa majumbani mwao bila ya haki isipokuwa kwa kuwa tu wanasema: Rabb wetu Ni Allaah. Na lau ingelikuwa Allaah Hawakingi watu baadhi yao kwa wengine, bila shaka yangelivunjwa mahekalu na makanisa, na masinagogi na Misikiti inayotajwa humo Jina la Allaah kwa wingi. Na bila shaka Allaah Atamnusuru yeyote yule anayenusuru Dini Yake. Hakika Allaah bila shaka Ni Mwenye nguvu zote, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika.

 

 

 

الَّذِينَ إِن مَّكَّنَّاهُمْ فِي الْأَرْضِ أَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ وَأَمَرُوا بِالْمَعْرُوفِ وَنَهَوْا عَنِ الْمُنكَرِ ۗ وَلِلَّـهِ عَاقِبَةُ الْأُمُورِ ﴿٤١﴾

41. Ambao Tukiwamakinisha katika ardhi, husimamisha Swalaah na hutoa Zakaah, na huamrisha mema na hukataza munkari. Na kwa Allaah Pekee ndio hatima ya mambo yote.

 

 

 

وَإِن يُكَذِّبُوكَ فَقَدْ كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍ وَعَادٌ وَثَمُودُ ﴿٤٢﴾

42. Na wakikukadhibisha, basi wamekwishakadhibisha kabla yao watu wa Nuwh na ‘Aad na Thamuwd.

 

 

 

وَقَوْمُ إِبْرَاهِيمَ وَقَوْمُ لُوطٍ ﴿٤٣﴾

43. Na watu wa Ibraahiym, na watu wa Luutw.

 

 

 

وَأَصْحَابُ مَدْيَنَ ۖ وَكُذِّبَ مُوسَىٰ فَأَمْلَيْتُ لِلْكَافِرِينَ ثُمَّ أَخَذْتُهُمْ ۖ فَكَيْفَ كَانَ نَكِيرِ ﴿٤٤﴾

44. Na watu wa Madyan. Na Muwsaa alikadhibishwa pia basi Nikawapa muhula makafiri, kisha Nikawachukua. Basi vipi ilikuwa Adhabu Yangu!

 

 

 

فَكَأَيِّن مِّن قَرْيَةٍ أَهْلَكْنَاهَا وَهِيَ ظَالِمَةٌ فَهِيَ خَاوِيَةٌ عَلَىٰ عُرُوشِهَا وَبِئْرٍ مُّعَطَّلَةٍ وَقَصْرٍ مَّشِيدٍ ﴿٤٥﴾

45. Miji mingapi Tumeiangamiza iliyokuwa ikidhulumu, ikaanguka juu ya mapaa yake na kuwa magofu, na visima vilivyohamwa, na makasri madhubuti.

 

 

 

أَفَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَتَكُونَ لَهُمْ قُلُوبٌ يَعْقِلُونَ بِهَا أَوْ آذَانٌ يَسْمَعُونَ بِهَا ۖ فَإِنَّهَا لَا تَعْمَى الْأَبْصَارُ وَلَـٰكِن تَعْمَى الْقُلُوبُ الَّتِي فِي الصُّدُورِ ﴿٤٦﴾

46. Je, basi hawatembei katika ardhi ili wapate kuwa na nyoyo za kuzingatia au masikio ya kusikilizia?[8] Kwani hakika hayapofuki macho, lakini zinazopofuka ni nyoyo zilizomo vifuani.[9]

 

 

 

وَيَسْتَعْجِلُونَكَ بِالْعَذَابِ وَلَن يُخْلِفَ اللَّـهُ وَعْدَهُ ۚ وَإِنَّ يَوْمًا عِندَ رَبِّكَ كَأَلْفِ سَنَةٍ مِّمَّا تَعُدُّونَ ﴿٤٧﴾

47. Na wanakuhimiza adhabu, na hali ya kuwa Allaah Hatokhalifu Ahadi Yake. Na hakika siku moja kwa Rabb wako ni kama miaka elfu katika ile mnayoihesabu.[10]

 

 

 

وَكَأَيِّن مِّن قَرْيَةٍ أَمْلَيْتُ لَهَا وَهِيَ ظَالِمَةٌ ثُمَّ أَخَذْتُهَا وَإِلَيَّ الْمَصِيرُ ﴿٤٨﴾

48. Na miji mingapi Nimeipa muhula hali ya kuwa imedhulumu, kisha Nikaikamata (Kuiadhibu)? Na Kwangu Pekee ni mahali pa kuishia.

 

 

 

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّمَا أَنَا لَكُمْ نَذِيرٌ مُّبِينٌ ﴿٤٩﴾

49. Sema: Enyi watu! Hakika mimi kwenu ni mwonyaji mwenye kubainisha kila kitu.

 

 

 

فَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ ﴿٥٠﴾

50. Basi wale walioamini na wakatenda mema, watapata maghfirah na riziki karimu.

 

 

 

وَالَّذِينَ سَعَوْا فِي آيَاتِنَا مُعَاجِزِينَ أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ الْجَحِيمِ ﴿٥١﴾

51. Na wale waliokwenda mbio katika kupinga Aayaat Zetu, hao ni watu wa moto uwakao vikali mno.

 

 

 

 

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ وَلَا نَبِيٍّ إِلَّا إِذَا تَمَنَّىٰ أَلْقَى الشَّيْطَانُ فِي أُمْنِيَّتِهِ فَيَنسَخُ اللَّـهُ مَا يُلْقِي الشَّيْطَانُ ثُمَّ يُحْكِمُ اللَّـهُ آيَاتِهِ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿٥٢﴾

52. Na Hatukutuma kabla yako Rasuli yeyote wala Nabiy yeyote isipokuwa anaposoma Kitabu cha Allaah au kubalighisha ujumbe, shaytwaan hutupia ya kuvuruga anayoyasoma, lakini Allaah Hufuta yale anayoyatupia shaytwaan kisha Allaah Anathibitisha Aayaat Zake. Na Allaah Ni Mjuzi wa yote, Mwenye Hikmah wa yote.

 

 

 

لِّيَجْعَلَ مَا يُلْقِي الشَّيْطَانُ فِتْنَةً لِّلَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ وَالْقَاسِيَةِ قُلُوبُهُمْ ۗ وَإِنَّ الظَّالِمِينَ لَفِي شِقَاقٍ بَعِيدٍ ﴿٥٣﴾

53. Ili (Allaah) Afanye yale aliyoyatupa shaytwaan kuwa ni fitnah kwa wale wenye maradhi katika nyoyo[11] zao na wale ambao nyoyo zao ni ngumu. Na hakika madhalimu bila shaka wamo katika upinzani wa mbali.

 

 

 

وَلِيَعْلَمَ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ أَنَّهُ الْحَقُّ مِن رَّبِّكَ فَيُؤْمِنُوا بِهِ فَتُخْبِتَ لَهُ قُلُوبُهُمْ ۗ وَإِنَّ اللَّـهَ لَهَادِ الَّذِينَ آمَنُوا إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٥٤﴾

54. Na ili wajue wale waliopewa ilimu kwamba hii (Qur-aan) ni haki kutoka kwa Rabb wao wapate kuiamini, na nyoyo zao zipate kutulia kwayo. Na hakika Allaah Ndiye Anayewaongoza wale walioamini kuelekea njia iliyonyooka.

 

 

 

وَلَا يَزَالُ الَّذِينَ كَفَرُوا فِي مِرْيَةٍ مِّنْهُ حَتَّىٰ تَأْتِيَهُمُ السَّاعَةُ بَغْتَةً أَوْ يَأْتِيَهُمْ عَذَابُ يَوْمٍ عَقِيمٍ ﴿٥٥﴾

55. Na hawatoacha wale waliokufuru kuwa katika shaka nayo (Qur-aan), mpaka iwafikie Saa ghafla, au iwafikie adhabu ya siku kame (isiyokuwa na kheri kwao).

 

 

 

الْمُلْكُ يَوْمَئِذٍ لِّلَّـهِ يَحْكُمُ بَيْنَهُمْ ۚ فَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فِي جَنَّاتِ النَّعِيمِ ﴿٥٦﴾

56. Ufalme Siku hiyo ni wa Allaah Pekee, Atahukumu baina yao. Basi wale walioamini na wakatenda mema, watakuwa katika Jannaat za Neema.

 

 

 

وَالَّذِينَ كَفَرُوا وَكَذَّبُوا بِآيَاتِنَا فَأُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ ﴿٥٧﴾

57. Na wale waliokufuru na wakakadhibisha Aayaat (na Ishara, Dalili, Hoja) Zetu, basi hao watapata adhabu ya kudhalilisha.

 

 

 

وَالَّذِينَ هَاجَرُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ثُمَّ قُتِلُوا أَوْ مَاتُوا لَيَرْزُقَنَّهُمُ اللَّـهُ رِزْقًا حَسَنًا ۚ وَإِنَّ اللَّـهَ لَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ ﴿٥٨﴾

58. Na wale waliohajiri katika Njia ya Allaah, kisha wakauawa, au wakafa, bila shaka Allaah Atawaruzuku riziki nzuri. Na hakika Allaah bila shaka Yeye Ndiye Mbora wa wenye kuruzuku.

 

 

 

لَيُدْخِلَنَّهُم مُّدْخَلًا يَرْضَوْنَهُ ۗ وَإِنَّ اللَّـهَ لَعَلِيمٌ حَلِيمٌ ﴿٥٩﴾

59. Bila shaka Atawaingiza mahala watakapoparidhia. Na hakika Allaah bila shaka ni Ni Mjuzi wa yote, Mvumilivu.

 

 

 

ذَٰلِكَ وَمَنْ عَاقَبَ بِمِثْلِ مَا عُوقِبَ بِهِ ثُمَّ بُغِيَ عَلَيْهِ لَيَنصُرَنَّهُ اللَّـهُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَعَفُوٌّ غَفُورٌ ﴿٦٠﴾

60. Ndivyo hivyo, na yeyote anayejilipizia mfano wa ubaya aliofanyiwa, kisha akaja kufanyiwa baghi[12] (kudhulumiwa) tena, bila shaka Allaah Atamnusuru. Hakika Allaah bila shaka Ni Mwingi wa Kusamehe, Mwingi wa Kughufuria.

 

 

 

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ يُولِجُ اللَّيْلَ فِي النَّهَارِ وَيُولِجُ النَّهَارَ فِي اللَّيْلِ وَأَنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ بَصِيرٌ ﴿٦١﴾

61. Hivyo ni kwa kuwa Allaah Anaingiza usiku katika mchana, na Anaingiza mchana katika usiku, na kwamba Allaah Ni Mwenye Kusikia yote, Mwenye Kuona yote.

 

 

 

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِ هُوَ الْبَاطِلُ وَأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْعَلِيُّ الْكَبِيرُ ﴿٦٢﴾

62. Hivyo ni kwa kuwa Allaah Ndiye wa Haki, na kwamba vile wanavyoomba badala Yake ndiyo batili, na kwamba Allaah Ndiye Mwenye ‘Uluwa Uliotukuka, Mkubwa Kabisa.

 

 

 

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ أَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَتُصْبِحُ الْأَرْضُ مُخْضَرَّةً ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَطِيفٌ خَبِيرٌ ﴿٦٣﴾

63. Je, huoni kwamba Allaah Ameteremsha kutoka mbinguni maji kisha ardhi ikawa chanikiwiti. Hakika Allaah bila shaka ni Mwenye Kudabiri mambo kwa Ulatifu, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri.

 

 

 

لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ وَإِنَّ اللَّـهَ لَهُوَ الْغَنِيُّ الْحَمِيدُ ﴿٦٤﴾

64. Ni Vyake pekee vyote vile vilivyomo mbinguni na vile vilivyomo ardhini. Na hakika Allaah bila shaka Yeye Ndiye Mkwasi, Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa kwa yote.

 

 

 

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ سَخَّرَ لَكُم مَّا فِي الْأَرْضِ وَالْفُلْكَ تَجْرِي فِي الْبَحْرِ بِأَمْرِهِ وَيُمْسِكُ السَّمَاءَ أَن تَقَعَ عَلَى الْأَرْضِ إِلَّا بِإِذْنِهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ بِالنَّاسِ لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿٦٥﴾

65. Je, huoni kwamba Allaah Amevitiisha kwa ajili yenu vile vilivyomo katika ardhi na merikebu zipitazo baharini kwa Amri Yake. Na Anazuia mbingu zisianguke juu ya ardhi isipokuwa kwa Idhini Yake. Hakika Allaah kwa watu ni Mwenye huruma mno, Mwenye Kurehemu.

 

 

 

وَهُوَ الَّذِي أَحْيَاكُمْ ثُمَّ يُمِيتُكُمْ ثُمَّ يُحْيِيكُمْ ۗ إِنَّ الْإِنسَانَ لَكَفُورٌ ﴿٦٦﴾

66. Naye Ndiye Ambaye Anakuhuisheni, kisha Anakufisheni, kisha Atakuhuisheni. Hakika binaadam ni mwingi wa kukufuru.

 

 

 

لِّكُلِّ أُمَّةٍ جَعَلْنَا مَنسَكًا هُمْ نَاسِكُوهُ ۖ فَلَا يُنَازِعُنَّكَ فِي الْأَمْرِ ۚ وَادْعُ إِلَىٰ رَبِّكَ ۖ إِنَّكَ لَعَلَىٰ هُدًى مُّسْتَقِيمٍ ﴿٦٧﴾

67. Kila ummah Tumejaalia taratibu za ibaada wanazozifuata. Basi wasizozane nawe (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kabisa katika jambo hili, na walinganie kwa Rabb wako. Hakika wewe bila shaka uko juu ya mwongozo ulionyooka.

 

 

 

وَإِن جَادَلُوكَ فَقُلِ اللَّـهُ أَعْلَمُ بِمَا تَعْمَلُونَ ﴿٦٨﴾

68. Na wakibishana nawe (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), basi sema: Allaah Anajua zaidi yale mnayoyafanya.

 

 

 

اللَّـهُ يَحْكُمُ بَيْنَكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فِيمَا كُنتُمْ فِيهِ تَخْتَلِفُونَ ﴿٦٩﴾

69. Allaah Atahukumu baina yenu Siku ya Qiyaamah katika yale mliyokuwa mnakhitilafiana.

 

 

 

أَلَمْ تَعْلَمْ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۗ إِنَّ ذَٰلِكَ فِي كِتَابٍ ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ ﴿٧٠﴾

70. Je, hujui kwamba Allaah Anajua yale yote yaliyomo katika mbingu na ardhi? Hakika hayo yamo katika Kitabu. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.

 

 

 

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَمْ يُنَزِّلْ بِهِ سُلْطَانًا وَمَا لَيْسَ لَهُم بِهِ عِلْمٌ ۗ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِن نَّصِيرٍ ﴿٧١﴾

71. Wanaabudu badala ya Allaah ambayo Hakuyateremshia mamlaka, na ambayo hawana ilimu nayo. Na madhalimu hawana yeyote mwenye kunusuru.

 

 

 

وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ آيَاتُنَا بَيِّنَاتٍ تَعْرِفُ فِي وُجُوهِ الَّذِينَ كَفَرُوا الْمُنكَرَ ۖ يَكَادُونَ يَسْطُونَ بِالَّذِينَ يَتْلُونَ عَلَيْهِمْ آيَاتِنَا ۗ قُلْ أَفَأُنَبِّئُكُم بِشَرٍّ مِّن ذَٰلِكُمُ ۗ النَّارُ وَعَدَهَا اللَّـهُ الَّذِينَ كَفَرُوا ۖ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ ﴿٧٢﴾

72. Na wanaposomewa Aayaat Zetu bayana, utatambua katika nyuso za wale waliokufuru karaha. Wanakaribia kuwashambulia wale wanaowasomea Aayaat Zetu. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Je, nikujulisheni yaliyo shari zaidi kuliko hayo kwenu? Ni moto Aliowaahidi Allaah wale waliokufuru. Na ni ubaya ulioje mahali pa kuishia!

 

 

 

يَا أَيُّهَا النَّاسُ ضُرِبَ مَثَلٌ فَاسْتَمِعُوا لَهُ ۚ إِنَّ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ لَن يَخْلُقُوا ذُبَابًا وَلَوِ اجْتَمَعُوا لَهُ ۖ وَإِن يَسْلُبْهُمُ الذُّبَابُ شَيْئًا لَّا يَسْتَنقِذُوهُ مِنْهُ ۚ ضَعُفَ الطَّالِبُ وَالْمَطْلُوبُ ﴿٧٣﴾

73. Enyi watu! Umepigwa mfano basi usikilizeni kwa makini! Hakika wale mnaowaomba badala ya Allaah hawawezi kuumba nzi japo wakijumuika kwa hilo. Na nzi akiwapokonya kitu chochote kile hawawezi kukiambua tena. Amedhoofika mwenye kutaka matilabu na mwenye kutakiwa.[13]

 

 

 

مَا قَدَرُوا اللَّـهَ حَقَّ قَدْرِهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَقَوِيٌّ عَزِيزٌ ﴿٧٤﴾

74. Hawakumkadiria Allaah kama inavyostahiki kumkadiria. Hakika Allaah bila shaka ni Mwenye nguvu zote, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika.

 

 

 

اللَّـهُ يَصْطَفِي مِنَ الْمَلَائِكَةِ رُسُلًا وَمِنَ النَّاسِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ بَصِيرٌ ﴿٧٥﴾

75. Allaah Anakhitari Wajumbe miongoni mwa Malaika na miongoni mwa watu. Hakika Allaah Ni Mwenye Kusikia yote, Mwenye Kuona yote.

 

 

 

يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ ۗ وَإِلَى اللَّـهِ تُرْجَعُ الْأُمُورُ ﴿٧٦﴾

76. Anajua yale yaliyoko mbele yao, na yale yaliyoko nyuma yao. Na kwa Allaah yanarejeshwa mambo yote.

 

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا ارْكَعُوا وَاسْجُدُوا وَاعْبُدُوا رَبَّكُمْ وَافْعَلُوا الْخَيْرَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ۩﴿٧٧﴾

77. Enyi walioamini! Rukuuni, na sujuduni na mwabuduni Rabb wenu, na fanyeni ya kheri ili mpate kufaulu.

 

 

 

وَجَاهِدُوا فِي اللَّـهِ حَقَّ جِهَادِهِ ۚ هُوَ اجْتَبَاكُمْ وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ ۚ مِّلَّةَ أَبِيكُمْ إِبْرَاهِيمَ ۚ هُوَ سَمَّاكُمُ الْمُسْلِمِينَ مِن قَبْلُ وَفِي هَـٰذَا لِيَكُونَ الرَّسُولُ شَهِيدًا عَلَيْكُمْ وَتَكُونُوا شُهَدَاءَ عَلَى النَّاسِ ۚ فَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَاعْتَصِمُوا بِاللَّـهِ هُوَ مَوْلَاكُمْ ۖ فَنِعْمَ الْمَوْلَىٰ وَنِعْمَ النَّصِيرُ ﴿٧٨﴾

78. Na fanyeni Jihaad katika Njia ya Allaah kama inavyostahiki kufanyiwa Jihaad. Yeye Ndiye Amekuteueni, na Hakukufanyieni ugumu wowote ule katika Dini. Mila ya baba yenu Ibraahiym. Yeye (Allaah) Ndiye Aliyekuiteni Waislamu hapo zamani na pia katika hii (Qur-aan). Ili Rasuli (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) awe shahidi juu yenu, nanyi muwe mashahidi juu ya watu.[14] Basi simamisheni Swalaah na toeni Zakaah, na shikamaneni pamoja kwa ajili ya Allaah, Yeye Ndiye Mola Mlinzi wenu. Basi Mzuri Alioje Mola Mlinzi na Mzuri Alioje Mwenye Kunusuru.

 

 

[1] Zilizala (Tetemeko) La Ardhi:

 

Aayah ya (1-2): Mufassiruwn wamekhitilafiana katika kauli mbalimbali kuhusu wakati wa kutokea zilizala hii:

 

(i) Baada ya watu kufufuliwa kutokana na Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِذَا زُلْزِلَتِ الْأَرْضُ زِلْزَالَهَا ﴿١﴾ وَأَخْرَجَتِ الْأَرْضُ أَثْقَالَهَا ﴿٢﴾

“Itakapotetemeshwa ardhi zilzala yake (ya mwisho). Na itakapotoa ardhi mizigo yake.” [Az-Zalzalah (99:1-2)]

 

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَحُمِلَتِ الْأَرْضُ وَالْجِبَالُ فَدُكَّتَا دَكَّةً وَاحِدَةً﴿١٤﴾ فَيَوْمَئِذٍ وَقَعَتِ الْوَاقِعَةُ﴿١٥﴾

“Na ardhi na milima ikaondolewa kisha ikapondwa mpondo mmoja. 15. Basi siku hiyo ndio litatokea tukio la kutokea.” [Al-Haaqqah (69:14-15)]

 

Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

إِذَا رُجَّتِ الْأَرْضُ رَجًّا ﴿٤﴾ وَبُسَّتِ الْجِبَالُ بَسًّا ﴿٥﴾ فَكَانَتْ هَبَاءً مُّنبَثًّا ﴿٦﴾

“Itakapotikiswa ardhi mtikiso mkubwa. Na milima itakapopondwa pondwa. Ikawa chembechembe za vumbi zinazoelea hewani zikitawanyika.” [Al-Waaqi’ah (56:4-6)]

 

(ii)  Zama za mwisho inapokaribia Qiyaamah na ni katika alama za Qiyaamah.

 

(iii) Kabla ya Qiyaamah.

  

(iv) Duniani kabla ya Qiyaamah.

 

Rejea pia Az-Zalzalah (99).

 

[2] Uumbaji Wa Mwanaadam Tumboni Na Kupulizwa Roho Anapofikia Miezi Minne:

 

عَنْ أَبِي عَبْدِ الرَّحْمَنِ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ رضي الله عنه قَالَ: حَدَّثَنَا رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم -وَهُوَ الصَّادِقُ الْمَصْدُوقُ: ((إِنَّ أَحَدَكُمْ يُجْمَعُ خَلْقُهُ فِي بَطْنِ أُمِّهِ أَرْبَعِينَ يَوْمًا نُطْفَةً، ثُمَّ يَكُونُ عَلَقَةً مِثْلَ ذَلِكَ، ثُمَّ يَكُونُ مُضْغَةً مِثْلَ ذَلِكَ، ثُمَّ يُرْسَلُ إلَيْهِ الْمَلَكُ فَيَنْفُخُ فِيهِ الرُّوحَ، وَيُؤْمَرُ بِأَرْبَعِ كَلِمَاتٍ: بِكَتْبِ رِزْقِهِ، وَأَجَلِهِ، وَعَمَلِهِ، وَشَقِيٍّ أَمْ سَعِيدٍ؛ فَوَاَللَّهِ الَّذِي لَا إلَهَ غَيْرُهُ إنَّ أَحَدَكُمْ لَيَعْمَلُ بِعَمَلِ أَهْلِ الْجَنَّةِ حَتَّى مَا يَكُونُ بَيْنَهُ وَبَيْنَهَا إلَّا ذِرَاعٌ فَيَسْبِقُ عَلَيْهِ الْكِتَابُ فَيَعْمَلُ بِعَمَلِ أَهْلِ النَّارِ فَيَدْخُلُهَا. وَإِنَّ أَحَدَكُمْ لَيَعْمَلُ بِعَمَلِ أَهْلِ النَّارِ حَتَّى مَا يَكُونُ بَيْنَهُ وَبَيْنَهَا إلَّا ذِرَاعٌ فَيَسْبِقُ عَلَيْهِ الْكِتَابُ فَيَعْمَلُ بِعَمَلِ أَهْلِ الْجَنَّةِ فَيَدْخُلُهَا)) رواه البخاري ومسلم

Amesimulia Abuu 'Abdir-Rahmaan 'Abdillaah bin Mas-‘uwd (رضي الله عنه):  Ametusimulia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ambaye ni mkweli mwenye kuaminiwa: “Hakika kila mmoja wenu hukusanywa umbo lake katika tumbo la mama yake siku arubaini akiwa ni mkusanyiko wa mbegu (za uzazi za mama na baba), kisha arubaini zifuatazo huwa ni donge la damu, kisha arubaini zijazo huwa pande la nyama, kisha Allaah Humtuma Malaika kwake na kumpulizia roho (yake).  Na (Malaika huyo) anaamrishwa maneno manne: Kuandika rizki yake, ajali yake (umri atakaoishi duniani), amali zake, mtu muovu au mwema. Wa-Allaahi! Naapa kwa Yule Ambaye hakuna muabudiwa wa haki isipokuwa Yeye, hakika mmoja wenu huenda afanye amali za watu wa Jannah hadi ikawa baina yake na Jannah ni dhiraa, na kile kilichoandikwa kikathibiti, akafanya amali ya watu wa motoni akaingia motoni. Na mmoja wenu hufanya amali za watu wa motoni hadi ikawa baina yake na moto ni dhiraa, na hapo kile kilichoandikwa kikathibiti, akafanya amali ya watu wa Jannah akaingia Jannah.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Rejea pia Al-Muuminuwn (23:12), Ghaafir (40:67).

 

[3] Kuwa Baina Ya Imaan Na Kufru Pindi Mtu Anapopata Mitihani:

 

حَدَّثَنِي إِبْرَاهِيمُ بْنُ الْحَارِثِ، حَدَّثَنَا يَحْيَى بْنُ أَبِي بُكَيْرٍ، حَدَّثَنَا إِسْرَائِيلُ، عَنْ أَبِي حَصِينٍ، عَنْ سَعِيدِ بْنِ جُبَيْرٍ، عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ ـ رضى الله عنهما ـ قَالَ ‏ ‏وَمِنَ النَّاسِ مَنْ يَعْبُدُ اللَّهَ عَلَى حَرْفٍ‏ ‏ قَالَ كَانَ الرَّجُلُ يَقْدَمُ الْمَدِينَةَ، فَإِنْ وَلَدَتِ امْرَأَتُهُ غُلاَمًا، وَنُتِجَتْ خَيْلُهُ قَالَ هَذَا دِينٌ صَالِحٌ‏.‏ وَإِنْ لَمْ تَلِدِ امْرَأَتُهُ وَلَمْ تُنْتَجْ خَيْلُهُ قَالَ هَذَا دِينُ سُوءٍ‏.‏

 

Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما)  kuhusiana na Aayah hii na ifuatayo:

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَعْبُدُ اللَّـهَ عَلَىٰ حَرْفٍ ۖ  

Na miongoni mwa watu yuko anayemwabudu Allaah ukingoni.”  [Al-Hajj (22:11-12)]

 

Akasema: “Alikuwa mtu akija Madiynah, na ikiwa mkewe atazaa mtoto wa kiume na farasi wake vile vile akazaa, husema: “Dini hii (ya Kiislamu) ni nzuri.” Lakini ikiwa mkewe atakosa kuzaa na farasi wake vile vile akakosa kuzaa, basi husema: “Dini hii (ya Kiislamu) ni mbaya.” [Al-Bukhaariy]

 

[4] Wasabai, Majusi Na Washirikina:

 

Wasabai:

 

Maana yake kiasili ni ‘kutoka.’ Inasemekana “Fulani alitoka katika dini moja hadi nyingine.” Imaam Atw-Twabariy (رحمه الله)  amesema: “Ni mtu mpya katika dini, kama mtu aliyeritadi kutoka katika Dini ya Kiislamu. Na kila anayetoka katika dini akaingia katika dini nyengine basi Waarabu wanasema Swaabia. Na nyota hung’aa zinapotoka kutoka katika miinuko yake.”

 

Ama kuhusu imaan na itikadi zao, Salaf wamekhitilafiana katika semi mbalimbali, miongoni mwazo ni:

‘Umar na Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما)  wamesema: “Hao (Wasabai) ni Watu wa Kitabu.” Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما)  amesema: “Haijuzu dhabihu zao wala kuingiliana nao.” Na Sufyaan amepokea kutoka kwa Layth kutoka kwa Mujaahid kwamba “Wasabai ni watu baina ya Mayahudi na Majusi, hawana dini.” Na Qataadah amesema: “Wasabai ni watu wanaoabudu Malaika.”

 

Majusi:

 

Majusi ni waabudu moto ambao wanaamini kwamba miungu ni aina mbili: Mungu wa nuru na mungu wa giza. Itikadi yao imepotoshwa hadi kwamba kaka anaweza kufunga ndoa na dada yake.

 

Washirikina:

 

Ni washirikina wa Makkah waliokuwa wanaabudu masanamu, na inajumuisha washirikina wowote wengineo katika nchi yoyote ile wasiotajwa humo.

 

[5] Kila Kitu Kinamsujudia Allaah (سبحانه وتعالى):

 

Kutokana na taadhima ya Allaah (سبحانه وتعالى) Ambaye ni Muumba wa kila kitu, vitu vyote vinamsujudia na kumsabihi Yeye Allaah (سبحانه وتعالى).      

 

Rejea An-Nahl (16:48-50), Ar-Ra’d (13:15), na Al-Israa (17:44).

 

Na Hadiyth ifuatayo inathibitisha jua kumsujudia Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 حَدَّثَنَا مُحَمَّدُ بْنُ يُوسُفَ، حَدَّثَنَا سُفْيَانُ، عَنِ الأَعْمَشِ، عَنْ إِبْرَاهِيمَ التَّيْمِيِّ، عَنْ أَبِيهِ، عَنْ أَبِي ذَرٍّ ـ رضى الله عنه ـ قَالَ قَالَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم لأَبِي ذَرٍّ حِينَ غَرَبَتِ الشَّمْسُ ‏"‏ تَدْرِي أَيْنَ تَذْهَبُ ‏"‏‏.‏ قُلْتُ اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَعْلَمُ‏.‏ قَالَ ‏"‏ فَإِنَّهَا تَذْهَبُ حَتَّى تَسْجُدَ تَحْتَ الْعَرْشِ، فَتَسْتَأْذِنَ فَيُؤْذَنَ لَهَا، وَيُوشِكُ أَنْ تَسْجُدَ فَلاَ يُقْبَلَ مِنْهَا، وَتَسْتَأْذِنَ فَلاَ يُؤْذَنَ لَهَا، يُقَالُ لَهَا ارْجِعِي مِنْ حَيْثُ جِئْتِ‏.‏ فَتَطْلُعُ مِنْ مَغْرِبِهَا، فَذَلِكَ قَوْلُهُ تَعَالَى ‏  وَالشَّمْسُ تَجْرِي لِمُسْتَقَرٍّ لَهَا ذَلِكَ تَقْدِيرُ الْعَزِيزِ الْعَلِيمِ ‏

Amesimulia Abuu Dharr (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliniuliza wakati wa machweo: “Je, unajua jua linapokwenda (wakati wa kuzama kwake)?”  Nikamjibu: Allaah na Rasuli Wake wanajua zaidi. Akasema: “Hakika linakwenda mpaka linasujudu chini ya ‘Arsh, na kutaka idhini kuchomoza tena, nalo linaruhusiwa. Na inachelewa kuwa (itafika wakati ambapo) litakaribia kusujudu lakini sijda yake haitokubaliwa, na litaomba idhini lakini litakataliwa (kutimiza mizunguko yake). Litaambiwa: ‘Rudi ulipotoka’. Hivyo, litachomoza Magharibi. Na hiyo ndiyo Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

وَالشَّمْسُ تَجْرِي لِمُسْتَقَرٍّ لَّهَا ۚ ذَٰلِكَ تَقْدِيرُ الْعَزِيزِ الْعَلِيمِ ﴿٣٨﴾

“Na jua linatembea hadi matulio yake. Hayo ni Takdiri ya Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mjuzi wa yote.” [Yaasiyn 36:38) - Hadiyth ameipokea Imaam Al-Bukhaariy]

Kuhusu Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

وَكَثِيرٌ حَقَّ عَلَيْهِ الْعَذَابُ ۗ

 Na wengi imewastahikia adhabu.”

 

Ina maana wale ambao hawataki kusujudu. [Ibn Kathiyr (6:540)]

 

[6] Aayah Zinazohusiana Na Manaasik Za Hajj:

 

Aayah hii hadi namba (37) zinataja kuhusu Manaasik za Hajj. Rejea pia Al-Baqarah (2:125), (2:196-203).

 

[7] Kumdhukuru Allaah Siku Maalumu:

 

Ni siku kumi bora kabisa za Allaah ambazo ni tarehe 1 hadi 10 Dhul-Hijjah kama alivyosema Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما). Ama siku za kuhesabika, rejea Al-Baqarah (2:203).

 

[8] Kutembea Katika Ardhi Kupata Mafunzo Na Mazingatio:

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Anawataka watu watembee katika ardhi wapate mafunzo na mazingatio, na wapate kutambua hatima ya waliokadhibisha.  Rejea Yuwsuf (12:109), Faatwir (35:43-44), Al-An’aam (6:11), Al-Kahf (18:55), na Aal-‘Imraan (3:137). 

 

[9] Maana Ya Kupofuka Moyo:

 

Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

فَإِنَّهَا لَا تَعْمَى الْأَبْصَارُ وَلَـٰكِن تَعْمَى الْقُلُوبُ الَّتِي فِي الصُّدُورِ ﴿٤٦﴾

Kwani hakika hayapofuki macho, lakini zinazopofuka ni nyoyo zilizomo vifuani.”

 

Maneno haya yametumiwa kwa njia ya sitiari na si kwa maana halisi kuwa moyo upofoke. Kwa kuwa moyo unachukuliwa kuwa ni kitovu cha imaan na taqwa. Rejea Al-Baqarah (2:2) kupata maana ya taqwa. Rejea pia Al-Maaidah (5:41) kuhusu moyo kutokuwa na imaan. Na nyoyoni ndimo ambamo kuna hisia za kiakili na kimaadili. Basi maneno haya yametumiwa kuashiria kwamba ukaidi wao umewazuia kuhisi na kutenda kwa busara, kwani japokuwa wana nyoyo, lakini hawafahamu Rejea Al-A’raaf (7:179). Wala nyoyo hizo haziwezi kuzingatia Qur-aan kwani kama zimefungiwa kufuli. Rejea Muhammad (47:24). Na rejea Aal-‘Imraan (3:7) kulikotajwa watu wenye upotofu katika nyoyo zao kwa kufuata fitnah na mambo yenye shaka, na matamanio na kuacha yaliyo haqq. 

 

Na katika Qur-aan, kumetajwa maradhi ya nyoyoni ambayo ni kufru, shirki, unafiki, shaka, matamanio, ukaidi wa kukubali haqq, maasi na kila aina ya maovu. Rejea Suwrah Muhammad (47:20) kwenye uchambuzi na maelezo bayana na rejea mbalimbali za kuhusu nyoyo zenye maradhi.

 

Kinyume chake ni nyoyo zenye imaan, taqwa, khofu, unyenyekevu na yote yenye hisia nzuri na maadili mema. Rejea Suwrah hii Al-Hajj Aayah (54), Al-Anfaal (8:2-4). Rejea pia Ar-Ra’d (13:28) Anaposema Allaah (سبحانه وتعالى) kuwa kwa Dhikru-Allaah nyoyo hutulia! Na Aayah nyingine nyingi mno ambazo zimetaja nyoyo njema zilizosalimika ambazo Siku ya Qiyaamah ndizo zitakazowafaa watu. Rejea Asw-Swaffaat (37:84). Rejea pia Ash-Shu’araa (26:88-89) kwenye ufafanuzi na maelezo kuhusu moyo uliosalimika.

 

[10] Ada Ya Washirikina Na Makafiri Kuhimiza Adhabu Au Qiyaamah.

 

Hawa wakanushaji (washirikina na makafiri) wanakuhimiza adhabu kwa sababu ya ujinga wao, na dhulma yao, na ukaidi wao, na kudhania kwao kuwa Allaah Hatoweza, na kuwakanusha kwao Rusuli Wake.  Lakini Allaah Haendi kinyume na Ahadi Yake, na yale Aliyoyaahidi lazima yatokee na hakuna atakayeweza kuzuia. Ama kuhimiza kwake, sio juu yako ee Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) wala kusikushughulishe kuhimiza kwao wala kudhania kwao kwamba Tutashindwa, kwani mbele yao kuna Siku ya Qiyaamah ambayo watajumuika wa mwanzo wao na wa mwisho wao, na watalipwa kwa amali zao, na adhabu ya kudumu iumizayo itawapata tu, ndio maana Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:

وَإِنَّ يَوْمًا عِندَ رَبِّكَ كَأَلْفِ سَنَةٍ مِّمَّا تَعُدُّونَ ﴿٤٧﴾

Siku moja kwa Rabb wako ni kama miaka elfu katika ile mnayoihesabu.”  Kutokana na urefu wake na hali ngumu na shida zake. Basi ni sawasawa tu ikiwafika adhabu duniani au wakiakhirishiwa adhabu, kwani Siku hiyo ni lazima tu waidiriki. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

Rejea pia Swaad (38:16), Al-Anfaal (8:32-33)

 

Na wakiulizia lini Qiyaamah kitatokea: Rejea Al-Mulk (67:25), Al-A’araaf (7:187), Al-Ahzaab (33:63), An-Naazi’aat (79:42), na Ash-Shuwraa (42:18).

 

[11] Maradhi Ya Nyoyo: Rejea Aayah namba (46) ya Suwrah hii.

 

[12] Maana Ya Baghi Katika Qur-aan:

 

Rejea Ash-Shuwraa (42:14) kupata maana zake mbalimbali.

[13] Mifano Ya Hikmah Anayopiga Allaah (سبحانه وتعالى): Rejea Al-A’raaf (7:40).

 

[14] Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  Atakuwa Shahidi Kwa Ummah Wake Wa Kiislamu Na Ummah Wa Kiislamu Watakuwa Mashahidi Kwa Rusuli Waliotangulia Kwamba Wamebalighisha Ujumbe. 

 

Rejea Al-Baqara (2:143), An-Nisaa (4:41), Al-Hajj (22:78), Az-Zumar (39:69-70) na Al-Jaathiyah (45:28).

 

 

Share