038 - Swaad

 

   ص

 

038-Swaad

 

 

038-Swaad: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

 

ص ۚ وَالْقُرْآنِ ذِي الذِّكْرِ ﴿١﴾

1.  Swaad.[1] Naapa kwa Qur-aan iliyojaa ukumbusho na taadhima.

 

 

 

 

بَلِ الَّذِينَ كَفَرُوا فِي عِزَّةٍ وَشِقَاقٍ ﴿٢﴾

2. Bali wale waliokufuru wamo katika majivuno na upinzani.

 

 

 

 

كَمْ أَهْلَكْنَا مِن قَبْلِهِم مِّن قَرْنٍ فَنَادَوا وَّلَاتَ حِينَ مَنَاصٍ ﴿٣﴾

3. Karne ngapi Tumeziangamiza kabla yao, wakaomba uokozi, lakini hakukuwa tena na wakati wa kuokoka.

 

 

 

 

وَعَجِبُوا أَن جَاءَهُم مُّنذِرٌ مِّنْهُمْ ۖ وَقَالَ الْكَافِرُونَ هَـٰذَا سَاحِرٌ كَذَّابٌ ﴿٤﴾

4. Na wakastaajabu kwamba amewajia mwonyaji miongoni mwao. Na makafiri wakasema: Huyu ni mchawi muongo.[2]

 

 

 

 

أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ ﴿٥﴾

5. Amewafanya waabudiwa kuwa ni Ilaah Mmoja?  Hakika hili bila shaka ni jambo la ajabu mno!

 

 

 

 

وَانطَلَقَ الْمَلَأُ مِنْهُمْ أَنِ امْشُوا وَاصْبِرُوا عَلَىٰ آلِهَتِكُمْ ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ يُرَادُ ﴿٦﴾

6. Na wakaondoka wakuu miongoni mwao wakisema: Nendeni zenu na subirini juu ya waabudiwa wenu, hakika hili bila shaka ni jambo linalokusudiwa (ubaya).

 

 

 

 

مَا سَمِعْنَا بِهَـٰذَا فِي الْمِلَّةِ الْآخِرَةِ إِنْ هَـٰذَا إِلَّا اخْتِلَاقٌ ﴿٧﴾

7. Hatukusikia haya katika mila ya mwisho, haya si chochote isipokuwa ni jambo lililozushwa tu.

 

 

 

 

أَأُنزِلَ عَلَيْهِ الذِّكْرُ مِن بَيْنِنَا ۚ بَلْ هُمْ فِي شَكٍّ مِّن ذِكْرِي ۖ بَل لَّمَّا يَذُوقُوا عَذَابِ ﴿٨﴾

8. Eti ameteremshiwa ukumbusho yeye tu miongoni mwetu? Hapana! Wao wamo katika shaka na Ukumbusho Wangu, bali hawajaonja bado Adhabu Yangu.

 

 

 

 

أَمْ عِندَهُمْ خَزَائِنُ رَحْمَةِ رَبِّكَ الْعَزِيزِ الْوَهَّابِ ﴿٩﴾

9. Au wanazo hazina za Rehma za Rabb wako Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwingi wa Kutunuku?

 

 

 

 

أَمْ لَهُم مُّلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا ۖ فَلْيَرْتَقُوا فِي الْأَسْبَابِ ﴿١٠﴾

10. Au wana ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyo baina yake? Basi na wapande katika njia (kufika huko watawale).

 

 

 

 

جُندٌ مَّا هُنَالِكَ مَهْزُومٌ مِّنَ الْأَحْزَابِ ﴿١١﴾

11. (Wao ni) vijiaskari watakaoshindwa huko katika makundi.

 

 

 

 

كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍ وَعَادٌ وَفِرْعَوْنُ ذُو الْأَوْتَادِ ﴿١٢﴾

12. Walikadhibisha kabla yao watu wa Nuwh, na kina ‘Aad, na Firawni mwenye askari washupavu na nguvu kubwa.[3] 

 

 

 

وَثَمُودُ وَقَوْمُ لُوطٍ وَأَصْحَابُ الْأَيْكَةِ ۚ أُولَـٰئِكَ الْأَحْزَابُ ﴿١٣﴾

13. Na kina Thamuwd na watu wa Luutw, na watu wa Al-Aykah.[4] Hayo ndio Makundi.

 

 

 

إِن كُلٌّ إِلَّا كَذَّبَ الرُّسُلَ فَحَقَّ عِقَابِ ﴿١٤﴾

14. Hakuna hata mmoja wao isipokuwa waliwakadhibisha Rusuli, basi ikahakikika Ikabu Yangu.[5]

 

 

 

 

وَمَا يَنظُرُ هَـٰؤُلَاءِ إِلَّا صَيْحَةً وَاحِدَةً مَّا لَهَا مِن فَوَاقٍ ﴿١٥﴾

15. Na hawangojei hawa isipokuwa ukelele angamizi mmoja tu usio na kurudishwa wala taakhira.

 

 

 

 

وَقَالُوا رَبَّنَا عَجِّل لَّنَا قِطَّنَا قَبْلَ يَوْمِ الْحِسَابِ ﴿١٦﴾

16. Na wanasema: Rabb wetu! Tuharakizie fungu letu (la adhabu) kabla ya Siku ya hesabu.[6]

 

 

 

اصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَاذْكُرْ عَبْدَنَا دَاوُودَ ذَا الْأَيْدِ ۖ إِنَّهُ أَوَّابٌ ﴿١٧﴾

17. Subiri kwa yale wanayoyasema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Na mkumbuke Mja Wetu Daawuwd mwenye nguvu. Hakika yeye ni mwingi wa kutubia na kurejea Kwetu.[7]

 

 

 

إِنَّا سَخَّرْنَا الْجِبَالَ مَعَهُ يُسَبِّحْنَ بِالْعَشِيِّ وَالْإِشْرَاقِ ﴿١٨﴾

18. Hakika Sisi Tulitiisha milima iwe pamoja naye ikisabbih jioni na baada ya kuchomoza jua.

 

 

 

 

وَالطَّيْرَ مَحْشُورَةً ۖ كُلٌّ لَّهُ أَوَّابٌ ﴿١٩﴾

19. Na ndege waliokusanywa. Wote walikuwa ni watiifu mno kwake.  

 

 

 

 

وَشَدَدْنَا مُلْكَهُ وَآتَيْنَاهُ الْحِكْمَةَ وَفَصْلَ الْخِطَابِ ﴿٢٠﴾

20. Na Tukamtilia nguvu ufalme wake, na Tukampa hikmah, na umaizi wa kukata hukumu.

 

 

 

 

وَهَلْ أَتَاكَ نَبَأُ الْخَصْمِ إِذْ تَسَوَّرُوا الْمِحْرَابَ ﴿٢١﴾

21. Na je, imekujia khabari ya wenye kupinzana waliporuka ukuta kuingia chumba cha kuswalia?  

 

 

 

 

إِذْ دَخَلُوا عَلَىٰ دَاوُودَ فَفَزِعَ مِنْهُمْ ۖ قَالُوا لَا تَخَفْ ۖ خَصْمَانِ بَغَىٰ بَعْضُنَا عَلَىٰ بَعْضٍ فَاحْكُم بَيْنَنَا بِالْحَقِّ وَلَا تُشْطِطْ وَاهْدِنَا إِلَىٰ سَوَاءِ الصِّرَاطِ ﴿٢٢﴾

22. Walipomuingilia Daawuwd akafazaika kutokana nao! Wakasema: Usikhofu!  (Sisi ni) wapinzani wawili; mmoja wetu amemdhulumu mwenziwe, basi hukumu baina yetu kwa haki, na wala usipendelee, na tuongoze katika njia ya sawa.

 

 

 

 

 

إِنَّ هَـٰذَا أَخِي لَهُ تِسْعٌ وَتِسْعُونَ نَعْجَةً وَلِيَ نَعْجَةٌ وَاحِدَةٌ فَقَالَ أَكْفِلْنِيهَا وَعَزَّنِي فِي الْخِطَابِ ﴿٢٣﴾

23. Hakika huyu ni ndugu yangu, ana kondoo majike tisiini na tisa, nami nina kondoo jike mmoja. Naye akaniambia: Nikabidhi huyo awe katika amana yangu, na amenishinda kwa maneno. 

 

 

 

 

قَالَ لَقَدْ ظَلَمَكَ بِسُؤَالِ نَعْجَتِكَ إِلَىٰ نِعَاجِهِ ۖ وَإِنَّ كَثِيرًا مِّنَ الْخُلَطَاءِ لَيَبْغِي بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَقَلِيلٌ مَّا هُمْ ۗ وَظَنَّ دَاوُودُ أَنَّمَا فَتَنَّاهُ فَاسْتَغْفَرَ رَبَّهُ وَخَرَّ رَاكِعًا وَأَنَابَ ۩﴿٢٤﴾

24. (Nabiy Daawuwd) akasema: Kweli amekudhulumu kwa kukuomba kondoo wako kuongezea kondoo wake. Na hakika washirika wengi hufanyiana baghi[8] (dhulma) wao kwa wao isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema, na hao ni wachache. Daawuwd akahisi kwamba Tumemtia mtihanini, basi akamwomba Rabb wake maghfirah na akaporomoka kusujudu na akarudi kwa Allaah (kwa tawbah na ibaada).[9]

 

 

 

 

فَغَفَرْنَا لَهُ ذَٰلِكَ ۖ وَإِنَّ لَهُ عِندَنَا لَزُلْفَىٰ وَحُسْنَ مَآبٍ ﴿٢٥﴾

25. Tukamghufuria hayo. Na hakika yeye bila shaka ana makurubisho na marejeo mazuri Kwetu.

 

 

 

 

يَا دَاوُودُ إِنَّا جَعَلْنَاكَ خَلِيفَةً فِي الْأَرْضِ فَاحْكُم بَيْنَ النَّاسِ بِالْحَقِّ وَلَا تَتَّبِعِ الْهَوَىٰ فَيُضِلَّكَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ الَّذِينَ يَضِلُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ لَهُمْ عَذَابٌ شَدِيدٌ بِمَا نَسُوا يَوْمَ الْحِسَابِ ﴿٢٦﴾

26.  Ee Daawuwd!  Hakika Tumekujaalia uwe Khalifa katika ardhi. Basi hukumu baina ya watu kwa haki, na wala usifuate matamanio yakakupoteza Njia ya Allaah. Hakika wale wanaopotea Njia ya Allaah watapata adhabu kali kwa sababu ya kusahau kwao Siku ya hesabu.

 

 

 

 

وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاءَ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا بَاطِلًا ۚ ذَٰلِكَ ظَنُّ الَّذِينَ كَفَرُوا ۚ فَوَيْلٌ لِّلَّذِينَ كَفَرُوا مِنَ النَّارِ ﴿٢٧﴾

27. Na wala Hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake bila kusudio. Hiyo ndio dhana ya wale waliokufuru. Basi ole wao wale waliokufuru kwa moto utakaowapata.

 

 

 

 

أَمْ نَجْعَلُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ كَالْمُفْسِدِينَ فِي الْأَرْضِ أَمْ نَجْعَلُ الْمُتَّقِينَ كَالْفُجَّارِ ﴿٢٨﴾

28. Je, Tuwafanye wale walioamini na wakatenda mema kama mafisadi katika ardhi? Au Tuwafanye wenye taqwa kama waovu?

 

 

 

 

كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ مُبَارَكٌ لِّيَدَّبَّرُوا آيَاتِهِ وَلِيَتَذَكَّرَ أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿٢٩﴾

29. Kitabu Tumekiteremsha kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) chenye Baraka, ili wapate kuzingatia kwa makini Aayaat zake, na ili wapate kukumbuka wenye akili.

 

 

 

 

وَوَهَبْنَا لِدَاوُودَ سُلَيْمَانَ ۚ نِعْمَ الْعَبْدُ ۖ إِنَّهُ أَوَّابٌ ﴿٣٠﴾

30. Na Daawuwd Tukamtunuku Sulaymaan. Uzuri ulioje wa mja! Hakika yeye ni mwingi wa kutubia.[10]

 

 

 

إِذْ عُرِضَ عَلَيْهِ بِالْعَشِيِّ الصَّافِنَاتُ الْجِيَادُ ﴿٣١﴾

31. Alipohudhurishiwa jioni farasi wasimamao kidete tayari kukimbia kwa kasi.

 

 

 

فَقَالَ إِنِّي أَحْبَبْتُ حُبَّ الْخَيْرِ عَن ذِكْرِ رَبِّي حَتَّىٰ تَوَارَتْ بِالْحِجَابِ ﴿٣٢﴾

32. Akasema: Hakika mimi nimependelea mapenzi ya vitu vizuri badala ya kumdhukuru Rabb wangu mpaka (jua) likatoweka.

 

 

 

 

رُدُّوهَا عَلَيَّ ۖ فَطَفِقَ مَسْحًا بِالسُّوقِ وَالْأَعْنَاقِ ﴿٣٣﴾

33. (Akasema) warudisheni kwangu! Akaanza kuwapapasa miguu na shingo.

 

 

 

 

وَلَقَدْ فَتَنَّا سُلَيْمَانَ وَأَلْقَيْنَا عَلَىٰ كُرْسِيِّهِ جَسَدًا ثُمَّ أَنَابَ ﴿٣٤﴾

34. Na kwa yakini Tulimtia mtihanini Sulaymaan, na Tukamtupia juu ya kiti chake mwili kisha akarejea kutubia.[11]

 

 

 

 

قَالَ رَبِّ اغْفِرْ لِي وَهَبْ لِي مُلْكًا لَّا يَنبَغِي لِأَحَدٍ مِّن بَعْدِي ۖ إِنَّكَ أَنتَ الْوَهَّابُ ﴿٣٥﴾

35. Akasema: Rabb wangu! Nighufurie, na Nitunukie ufalme asiupate mtu yeyote baada yangu. Hakika Wewe Ndiye Mwingi Wa Kutunuku.[12]

 

 

 

 

فَسَخَّرْنَا لَهُ الرِّيحَ تَجْرِي بِأَمْرِهِ رُخَاءً حَيْثُ أَصَابَ ﴿٣٦﴾

36. Basi Tukamtiishia upepo unaokwenda kwa amri yake polepole popote anapotaka kufika.

 

 

 

وَالشَّيَاطِينَ كُلَّ بَنَّاءٍ وَغَوَّاصٍ ﴿٣٧﴾

37. Na mashaytwaan, kila ajengaye na mpiga mbizi.

 

 

 

 

وَآخَرِينَ مُقَرَّنِينَ فِي الْأَصْفَادِ ﴿٣٨﴾

38. Na wengineo, wafungwao minyororoni.

 

 

 

 

هَـٰذَا عَطَاؤُنَا فَامْنُنْ أَوْ أَمْسِكْ بِغَيْرِ حِسَابٍ ﴿٣٩﴾

39. (Tukasema): Hiki ni Kipawa Chetu, basi toa au zuia bila ya hesabu.

 

 

 

 

وَإِنَّ لَهُ عِندَنَا لَزُلْفَىٰ وَحُسْنَ مَآبٍ ﴿٤٠﴾

40. Na hakika yeye bila shaka ana makurubisho Kwetu na marejeo mazuri.  

 

 

 

 

وَاذْكُرْ عَبْدَنَا أَيُّوبَ إِذْ نَادَىٰ رَبَّهُ أَنِّي مَسَّنِيَ الشَّيْطَانُ بِنُصْبٍ وَعَذَابٍ ﴿٤١﴾

41. Na mkumbuke Mja Wetu Ayyuwb alipomwita Rabb wake: Hakika mimi amenigusa shaytwaan kwa tabu na adhabu.[13]

 

 

 

 

ارْكُضْ بِرِجْلِكَ ۖ هَـٰذَا مُغْتَسَلٌ بَارِدٌ وَشَرَابٌ ﴿٤٢﴾

42. (Akaambiwa): Piga piga ardhi kwa mguu wako!  Hii (chemchemu); maji baridi ya kuogea na ya kunywa.

 

 

 

 

وَوَهَبْنَا لَهُ أَهْلَهُ وَمِثْلَهُم مَّعَهُمْ رَحْمَةً مِّنَّا وَذِكْرَىٰ لِأُولِي الْأَلْبَابِ ﴿٤٣﴾

43. Na Tukamtunukia ahli zake na wengine mfano wao pamoja nao ikiwa ni Rehma kutoka Kwetu, na ni ukumbusho kwa wenye akili.

 

 

 

 

وَخُذْ بِيَدِكَ ضِغْثًا فَاضْرِب بِّهِ وَلَا تَحْنَثْ ۗ إِنَّا وَجَدْنَاهُ صَابِرًا ۚ نِّعْمَ الْعَبْدُ ۖ إِنَّهُ أَوَّابٌ ﴿٤٤﴾

44. Na (akaambiwa): Chukua mkononi mwako kicha cha vijiti na upigie navyo, na wala usivunje kiapo. Hakika sisi Tulimkuta mwenye subira mno, mja mwema kabisa, hakika yeye ni mwingi wa kutubia.

 

 

 

 

وَاذْكُرْ عِبَادَنَا إِبْرَاهِيمَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ أُولِي الْأَيْدِي وَالْأَبْصَارِ ﴿٤٥﴾

45. Na wakumbuke Waja Wetu: Ibraahiym, na Is-haaq, na Ya’quwb, wenye nguvu na busara.

 

 

 

إِنَّا أَخْلَصْنَاهُم بِخَالِصَةٍ ذِكْرَى الدَّارِ ﴿٤٦﴾

46. Hakika Sisi Tumewakhitari kutokana na ikhlasi zao kwa kuwapa sifa khalisi ya ukumbusho wa Aakhirah.

 

 

 

وَإِنَّهُمْ عِندَنَا لَمِنَ الْمُصْطَفَيْنَ الْأَخْيَارِ ﴿٤٧﴾

47. Na hakika wao Kwetu bila shaka ni miongoni mwa waliokhitariwa na walio bora kabisa.

 

 

 

 

وَاذْكُرْ إِسْمَاعِيلَ وَالْيَسَعَ وَذَا الْكِفْلِ ۖ وَكُلٌّ مِّنَ الْأَخْيَارِ ﴿٤٨﴾

48. Na wakumbuke Ismaaiyl na Alyasa’ na Dhul-Kifli[14], na wote hawa ni miongoni mwa walio bora kabisa.

 

 

 

 

هَـٰذَا ذِكْرٌ ۚ وَإِنَّ لِلْمُتَّقِينَ لَحُسْنَ مَآبٍ ﴿٤٩﴾

49. Huu ni ukumbusho. Na hakika wenye taqwa bila shaka wana mahali pazuri kabisa pa kurejea.

 

 

 

جَنَّاتِ عَدْنٍ مُّفَتَّحَةً لَّهُمُ الْأَبْوَابُ ﴿٥٠﴾

50. Jannaat za kudumu milele, zitakazofunguliwa milango yote kwa ajili yao.

 

 

 

مُتَّكِئِينَ فِيهَا يَدْعُونَ فِيهَا بِفَاكِهَةٍ كَثِيرَةٍ وَشَرَابٍ ﴿٥١﴾

51. Wakiegemea humo, wakiagizia humo matunda mengi na vinywaji.

 

 

 

 

وَعِندَهُمْ قَاصِرَاتُ الطَّرْفِ أَتْرَابٌ ﴿٥٢﴾

52. Na pamoja nao wanawake wenye staha wanaoinamisha macho, wa hirimu moja.

 

 

 

هَـٰذَا مَا تُوعَدُونَ لِيَوْمِ الْحِسَابِ ﴿٥٣﴾

53. Haya (yaliyotajwa) ndiyo mnayoahidiwa (enyi wenye taqwa) kwa ajili ya Siku ya hesabu.

 

 

 

إِنَّ هَـٰذَا لَرِزْقُنَا مَا لَهُ مِن نَّفَادٍ ﴿٥٤﴾

54. Hakika hii bila shaka ni Riziki Yetu, haina kumalizika.

 

 

 

هَـٰذَا ۚ وَإِنَّ لِلطَّاغِينَ لَشَرَّ مَآبٍ ﴿٥٥﴾

55. Ndio hivi! Na hakika wenye kupinduka mipaka katika kuasi, bila shaka wana mahali pabaya mno pa kurejea.

 

 

 

جَهَنَّمَ يَصْلَوْنَهَا فَبِئْسَ الْمِهَادُ ﴿٥٦﴾

56. Nayo ni Jahannam, wataingia kuungua. Basi pabaya palioje mahali pa kupumzikia![15]

 

 

 

هَـٰذَا فَلْيَذُوقُوهُ حَمِيمٌ وَغَسَّاقٌ ﴿٥٧﴾

57. Ndio hivi! Basi wayaonje maji yachemkayo na usaha.

 

 

 

 

وَآخَرُ مِن شَكْلِهِ أَزْوَاجٌ ﴿٥٨﴾

58. Na (adhabu) nyinginezo za mfano wake na aina yake. 

 

 

 

 

هَـٰذَا فَوْجٌ مُّقْتَحِمٌ مَّعَكُمْ ۖ لَا مَرْحَبًا بِهِمْ ۚ إِنَّهُمْ صَالُو النَّارِ ﴿٥٩﴾

59. (Wataambizana): Hili ndilo kundi litakaloingia pamoja nanyi. Hawana makaribisho mazuri. Hakika wao wataingia kuungua motoni.

 

 

 

 

قَالُوا بَلْ أَنتُمْ لَا مَرْحَبًا بِكُمْ ۖ أَنتُمْ قَدَّمْتُمُوهُ لَنَا ۖ فَبِئْسَ الْقَرَارُ ﴿٦٠﴾

60. (Waliofuata wapotofu) watasema: Bali nyinyi hakuna makaribisho mazuri kwenu!  Nyinyi ndio mliotutangulizia haya. Basi ubaya ulioje makazi ya kustakiri!

 

 

 

قَالُوا رَبَّنَا مَن قَدَّمَ لَنَا هَـٰذَا فَزِدْهُ عَذَابًا ضِعْفًا فِي النَّارِ ﴿٦١﴾

61. Watasema: Ee Rabb wetu! Yule aliyetuletea haya, basi Mzidishie adhabu maradufu katika moto.

 

 

 

وَقَالُوا مَا لَنَا لَا نَرَىٰ رِجَالًا كُنَّا نَعُدُّهُم مِّنَ الْأَشْرَارِ ﴿٦٢﴾

62. Na watasema: Tuna nini! Mbona hatuwaoni watu tuliokuwa tukiwahesabu kuwa ni miongoni mwa waovu?

 

 

 

أَتَّخَذْنَاهُمْ سِخْرِيًّا أَمْ زَاغَتْ عَنْهُمُ الْأَبْصَارُ ﴿٦٣﴾

63. Tuliowafanya vichekesho, au yamepotea tu macho yetu tusiwaone? 

 

 

 

 

إِنَّ ذَٰلِكَ لَحَقٌّ تَخَاصُمُ أَهْلِ النَّارِ ﴿٦٤﴾

64. Hakika hayo bila shaka ni kweli; makhasimiano ya watu wa motoni.

 

 

 

قُلْ إِنَّمَا أَنَا مُنذِرٌ ۖ وَمَا مِنْ إِلَـٰهٍ إِلَّا اللَّـهُ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ ﴿٦٥﴾

65. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Hakika mimi ni mwonyaji tu. Na hakuna Muabudiwa wa haki yeyote isipokuwa Allaah Mmoja Pekee, Asiyepingika.

 

 

 

 

رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا الْعَزِيزُ الْغَفَّارُ ﴿٦٦﴾

66. Rabb wa mbingu na ardhi na vilivyo baina yake, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwingi wa Kughufuria.

 

 

 

 

 

قُلْ هُوَ نَبَأٌ عَظِيمٌ ﴿٦٧﴾

67. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Hii (Qur-aan) ni khabari muhimu adhimu.

 

 

 

 

أَنتُمْ عَنْهُ مُعْرِضُونَ ﴿٦٨﴾

68. Nyinyi mnaikengeuka.

 

 

 

 

مَا كَانَ لِيَ مِنْ عِلْمٍ بِالْمَلَإِ الْأَعْلَىٰ إِذْ يَخْتَصِمُونَ ﴿٦٩﴾

69. Sikuwa mimi na ilimu yoyote kuhusu wakuu watukufu (Malaika) wanapokhasimiana na kujadiliana.

 

 

 

 

إِن يُوحَىٰ إِلَيَّ إِلَّا أَنَّمَا أَنَا نَذِيرٌ مُّبِينٌ ﴿٧٠﴾

70. Haifunuliwi Wahy kwangu isipokuwa ya kwamba: hakika mimi ni mwonyaji mbainishaji.

 

 

 

 

إِذْ قَالَ رَبُّكَ لِلْمَلَائِكَةِ إِنِّي خَالِقٌ بَشَرًا مِّن طِينٍ ﴿٧١﴾

71. Pale Rabb wako Alipowaambia Malaika: Hakika Mimi Namuumba mtu kutokana na udongo.

 

 

 

 

فَإِذَا سَوَّيْتُهُ وَنَفَخْتُ فِيهِ مِن رُّوحِي فَقَعُوا لَهُ سَاجِدِينَ ﴿٧٢﴾

72. Basi Nitakapomsawazisha na Nikampuliza humo roho Niliyoiumba, basi mwangukieni kumsujudia.

 

 

 

 

فَسَجَدَ الْمَلَائِكَةُ كُلُّهُمْ أَجْمَعُونَ ﴿٧٣﴾

73. Wakamsujudia Malaika wote pamoja.

 

 

 

 

 

إِلَّا إِبْلِيسَ اسْتَكْبَرَ وَكَانَ مِنَ الْكَافِرِينَ ﴿٧٤﴾

74. Isipokuwa Ibliys, alitakabari na akawa miongoni mwa makafiri.

 

 

 

 

 

قَالَ يَا إِبْلِيسُ مَا مَنَعَكَ أَن تَسْجُدَ لِمَا خَلَقْتُ بِيَدَيَّ ۖ أَسْتَكْبَرْتَ أَمْ كُنتَ مِنَ الْعَالِينَ ﴿٧٥﴾

75. (Allaah) Akasema: Ee Ibliys! Nini kilichokuzuia usimsujudie Niliyemuumba kwa Mikono Yangu?[16] Je, umetakabari, au umekuwa miongoni mwa waliojitukuza?

 

 

 

 

 

قَالَ أَنَا خَيْرٌ مِّنْهُ ۖ خَلَقْتَنِي مِن نَّارٍ وَخَلَقْتَهُ مِن طِينٍ ﴿٧٦﴾

76. (Ibliys) akasema: Mimi ni bora kuliko yeye, Umeniumba kutokana na moto, naye Umemuumba kutokana na udongo.

 

 

 

 

قَالَ فَاخْرُجْ مِنْهَا فَإِنَّكَ رَجِيمٌ ﴿٧٧﴾

77. (Allaah) Akasema: Basi toka humo, kwani hakika wewe umetokomezwa mbali na kulaaniwa.

 

 

 

وَإِنَّ عَلَيْكَ لَعْنَتِي إِلَىٰ يَوْمِ الدِّينِ ﴿٧٨﴾

78. Na hakika Laana Yangu iko juu yako mpaka Siku ya malipo.

 

 

 

 

قَالَ رَبِّ فَأَنظِرْنِي إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ ﴿٧٩﴾

79. (Ibliys) akasema: Rabb wangu! Basi Nipe muhula mpaka siku watakayofufuliwa.

 

 

 

 

قَالَ فَإِنَّكَ مِنَ الْمُنظَرِينَ ﴿٨٠﴾

80. (Allaah) Akasema: Hakika wewe ni miongoni mwa waliopewa muhula.

 

 

 

 

إِلَىٰ يَوْمِ الْوَقْتِ الْمَعْلُومِ ﴿٨١﴾

81. Mpaka siku ya wakati maalumu.

 

 

 

 

قَالَ فَبِعِزَّتِكَ لَأُغْوِيَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٨٢﴾

82. (Ibliys) akasema: Naapa kwa Utukufu Wako. Hakika nitawapotosha wote.[17]

 

 

 

 

إِلَّا عِبَادَكَ مِنْهُمُ الْمُخْلَصِينَ ﴿٨٣﴾

83. Isipokuwa Waja Wako miongoni mwao waliokhitariwa kwa ikhlasi zao.

 

 

 

 

قَالَ فَالْحَقُّ وَالْحَقَّ أَقُولُ ﴿٨٤﴾

84. (Allaah) Akasema: Basi haki (ndio Kiapo Changu), na haki Naisema!

 

 

 

 

 

لَأَمْلَأَنَّ جَهَنَّمَ مِنكَ وَمِمَّن تَبِعَكَ مِنْهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٨٥﴾

85. Bila shaka Nitaijaza Jahannam kwa wewe na wote waliokufuata miongoni mwao.

 

 

 

 

قُلْ مَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُتَكَلِّفِينَ ﴿٨٦﴾

86. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Sikuombeni ujira wowote juu ya hili, na wala mimi si miongoni mwa wenye kujidai kuzusha chochote kisichohusu.

 

 

 

 

إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ لِّلْعَالَمِينَ ﴿٨٧﴾

87. Haikuwa hii (Qur-aan) isipokuwa ni ukumbusho tu kwa walimwengu.

 

 

 

 

 

وَلَتَعْلَمُنَّ نَبَأَهُ بَعْدَ حِينٍ ﴿٨٨﴾

88. Na bila shaka mtakuja kujua khabari zake baada ya muda.[18]

 

 


 

[1] الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah):

 

Hizi ni herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Tanbihi ya Al-Baqarah (2:1).

 

[2] Makafiri Kumsingizia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  Kila Aina Ya Sifa Mbaya:

 

Rejea Al-Furqaan (25:4-8) kwenye maelezo na rejea mbalimbali kuhusu washirikina kumpachika Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kila aina ya sifa ovu pamoja na kuipachika Qur-aan. Walisema ni mchawi, kuhani, mshairi, majinuni, mtungaji na ameibuni Qur-aan na sifa nyenginezo.

 

Rejea pia Asw-Swaaffaat (37:36).

 

[3] Awtaad Maana Zake:

 

‘Ulamaa wametaja maana mbalimbali kuhusu neno hili kama ifuatavyo: Askari washupavu na nguvu kubwa [Tafsiyr As-Sa’diy]. Nguvu kubwa mno [Tafsiyr Al-Muyassar]. Ufalme thabiti wa nguvu [Ibn ‘Abbaas]. Nguvu na mashambulizi ya nguvu [Adhw-Dhwahaak]. Na wengine wamesema ni vigingi. Na wengineo wametaja maana zinazokaribiana na maana hizo.

 

[4] Watu Wa Al-Aykah:

 

Watu wa Aykah ni watu wa kichakani wa Nabiy Shu’ayb (عليه السّلام). Rejea Ash-Shu’araa (26:176). 

 

[5] Tofauti Baina Ya Ikabu Na Adhabu:

 

Rejea Al-Hashr (59:4).

 

[6] Ada Ya Makafiri Kuhimiza Adhabu

 

Rejea Al-Anfaal (8:32), Al-Hajj (22:47), Ash-Shuwraa (42:18).

 

[7] Miongoni Mwa Fadhila Za Nabiy Daawuwd (عليه السّلام) :

 

Aayah hii (17) hadi (20) zinataja baadhi ya fadhila za Nabiy Daawuwd (عليه السّلام) . Rejea pia Sabaa (34:10).

 

[8] Maana Ya Baghyun/Baghaa Katika Qur-aan:

 

Rejea Ash-Shuwraa (42:14) kupata maana zake mbalimbali.

 

[9] Sujuwd Ya Nabiy Sulaymaan (عليه السّلام) Na Sujuwd Ya Tilaawaah (Kusoma Qur-aan)

 

Bonyeza kiungo kifuatacho kupata faida:

034-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swalaah: Sijdah Ya Kisomo

Wamekhitilafiana ‘Ulamaa kuhusu Sijdah ya Tilaawah (kusoma Qur-aan) ya Aayah hii, lakini imethibiti kusujudu mtu anaposoma Aayah hii kutokana na Hadiyth zifuatazo ambazo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alisujudu:

 

أَخْبَرَنِي إِبْرَاهِيمُ بْنُ الْحَسَنِ الْمِقْسَمِيُّ، قَالَ حَدَّثَنَا حَجَّاجُ بْنُ مُحَمَّدٍ، عَنْ عُمَرَ بْنِ ذَرٍّ، عَنْ أَبِيهِ، عَنْ سَعِيدِ بْنِ جُبَيْرٍ، عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ، أَنَّ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم سَجَدَ فِي ‏{‏ ص ‏}‏ وَقَالَ ‏ "‏ سَجَدَهَا دَاوُدُ تَوْبَةً وَنَسْجُدُهَا شُكْرًا ‏"‏ ‏.‏

 

Amesimulia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alisujudu katika Suwrah Swaad akasema: “Alisujudu Daawuwd kama ni tawbah (kutubia) nasi tunasujudu kama shukurani.” Sunan An-Nasaaiy na ameisahihisha Al-Albaaniy - Swahiyh An-Nasaaiy (956)]

 

Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas aliyesema: “Swaad si katika mahala palipothibiti na kukokotezewa kusujudu, lakini mimi nilimwona Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akisujudu hapo.” [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1069), Abu Daawuud (1409) na At-Tirmidhiy (577)]

 

Duaa ya kusoma katika Sajdah ya Tilaawah, Rejea An-Najm (53:62).

 

[10] Fadhila Za Nabiy Sulaymaan (عليه السّلام):

  

Kuanzia Aayah hii (31) hadi (40), zinatajwa fadhila za Nabiy Sulaymaan (عليه السّلام).  Rejea pia Suwrah Sabaa (34:12-14) kwenye fadhila zake kama hizo na nyenginezo.

 

Rejea pia An-Naml (27:10-19). Na humo katika Suwrah An-Naml, kisa chake ni kuanzia Aayah namba (10) hadi (40) anaposhukuru Neema na Fadhila za Allaah juu yake. Kisha kisa kinaendelea hadi Aayah namba (44).

 

[11] Nabiy Sulaymaan (عليه السّلام) Alitiwa Mtihanini Kwa Kiapo Chake Alichoapa Bila Kusema In Shaa Allaah.

 

Rejea Al-Kahf (18:23)  kwenye Hadiyth inayotaja hayo.

 

Na Tafsiyr ya Aayah:

 

Hakika Tulimpa mtihani Sulaymaan na Tukamrushia kwenye kiti chake kipande cha mtoto aliyezaliwa katika kipindi alichoapa kuwa atawapitia wake zake na kila mmoja katika wao atamzalia shujaa atakayepigana katika njia ya Allaah na hakusema In Shaa Allaah (Allaah Akitaka).  Akawapitia wake zake wote, na hakuna hata mmoja katika wao aliyeshika mimba isipokuwa mmoja aliyezaa mtoto nusu. Kisha Sulaymaan alirudi kwa Rabb Wake, akatubia. [Tafsiyr Al-Muyassar] 

 

[12] Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Ameheshimu Duaa Ya Nabiy Sulaymaan (عليه السّلام):

 

حَدَّثَنَا إِسْحَاقُ بْنُ إِبْرَاهِيمَ، قَالَ أَخْبَرَنَا رَوْحٌ، وَمُحَمَّدُ بْنُ جَعْفَرٍ، عَنْ شُعْبَةَ، عَنْ مُحَمَّدِ بْنِ زِيَادٍ، عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ، عَنِ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ ‏ "‏ إِنَّ عِفْرِيتًا مِنَ الْجِنِّ تَفَلَّتَ عَلَىَّ الْبَارِحَةَ ـ أَوْ كَلِمَةً نَحْوَهَا ـ لِيَقْطَعَ عَلَىَّ الصَّلاَةَ، فَأَمْكَنَنِي اللَّهُ مِنْهُ، فَأَرَدْتُ أَنْ أَرْبِطَهُ إِلَى سَارِيَةٍ مِنْ سَوَارِي الْمَسْجِدِ، حَتَّى تُصْبِحُوا وَتَنْظُرُوا إِلَيْهِ كُلُّكُمْ، فَذَكَرْتُ قَوْلَ أَخِي سُلَيْمَانَ رَبِّ هَبْ لِي مُلْكًا لاَ يَنْبَغِي لأَحَدٍ مِنْ بَعْدِي"‏‏.‏ قَالَ رَوْحٌ فَرَدَّهُ خَاسِئًا‏.‏

Amesimulia Abu Hurayrah: Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Jana usiku Jini mkubwa (‘Ifriyt) kati ya majini alinijia ili anivurugie Swalaah yangu (au alisema jambo linalolingana na hilo) lakini Allaah Aliniwezesha kulishinda. Nilitaka kulifunga katika moja ya nguzo za Msikiti ili nyote mlione asubuhi lakini nilikumbuka kauli ya kaka yangu Sulaymaan (kama ilivyo ndani ya Qur-aan) :

 

قَالَ رَبِّ اغْفِرْ لِي وَهَبْ لِي مُلْكًا لَّا يَنبَغِي لِأَحَدٍ مِّن بَعْدِي ۖ

“Akasema: Rabb wangu! Nighufurie, na Nitunukie ufalme asiupate mtu yeyote baada yangu.” [Swaad: (35)]

 

[13] Nabiy Ayyuwb (عليه السّلام) Mitihani Yake Na Subira Yake:

 

Nabiy Ayyuwb (عليه السّلام) alifikwa na mitihani ya kila aina; aliuguwa maradhi miaka kumi na nane, na akafikwa na msiba wa kuondokewa na watoto na mali yake yote. Lakini juu ya hivyo alivumilia bila ya kulalamika, bali aliendelea bila ya kusita na ibaada zake na huku akimshukuru Allaah (سبحانه وتعالى) hadi mwishowe aliomba duaa hiyo.

 

[14] Dhul-Kifl Ni Nabiy Au Mja Mwema:

 

Rejea Al-Anbiyaa (21:85).

 

[15] Mateso Na Adhabu Za Watu Wa Motoni:

 

Rejea An-Nabaa (78:21) kwenye rejea mbalimbali na maelezo bayana kuhusu aina za mateso na adhabu za watu wa motoni.

 

[16] Aqiydah Sahihi Ya Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa’ah Ni Kuthibisha Sifa Za Allaah Kama Mikono Yake:.

 

Rejea Al-Fat-h (48:10), Al-Maaidah (5:64), Az-Zumar (39:67).

 

[17] Shaytwaan Ameahidi Kuwapotosha Wanaadam:

 

Rejea Suwrah Ibraahiym (14:22) kwenye maelezo bayana na rejea mbalimbali kuhusu shaytwaan anavyowapotosha wanaadam na jinsi anavyowakanusha na kujitenga nao inapofika adhabu au itakapokuwa Siku ya Qiyaamah.

 

[18]  Wakati Makafiri Watakapokuja Kujua Khabari Za Ukweli Wa Qur-aan:

 

‘Ulamaa wa Tafsiyr wamesema:  

 

Makafiri watakuja kujua ukweli wa Qur-aan na yaliyotajwa ndani yake ambayo hawakuyaamini, pindi Qur-aan itakaposadikishwa na watu ukweli wake, na pindi Uislamu utakaposhinda wakaingia watu katika Dini makundi kwa makundi, na pia pindi watakapoiona adhabu na njia za kurudi kwa Allaah zikawakatia. Na baadhi ya Salaf wamesema: (i) Baada ya mauti. (ii) Siku ya Qiyaamah.  (iii) Itakapomfikia mtu ilimu ya yaqini baada ya kufariki. [Tafsiyr Al-Muyassar, Tafsiyr As-Sa’diy, Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

 

 

 

Share