042 - Ash-Shuwraa

 

 

الشُّورى

 

042-Ash-Shuwraa

 

 

042-Ash-Shuwraa: Utangulizi Wa Suwrah

 

 

 Alhidaaya.com

 

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيم

حم﴿١﴾

1. Haa Miym.

 

 

عسق﴿٢﴾

2. ‘Ayn Siyn Qaaaf.[1]

 

 

 

 

كَذَٰلِكَ يُوحِي إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ اللَّـهُ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ﴿٣﴾

3. Hivyo ndivyo Anavyokufunulia Wahy na kwa wale walio kabla yako, Allaah Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote.

 

 

 

لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۖ وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ﴿٤﴾

4. Ni Vyake vilivyomo mbinguni na ardhini, Naye Ni Mwenye ‘Uluwa Uliotukuka, Mwenye Taadhima. 

 

 

 

 

تَكَادُ السَّمَاوَاتُ يَتَفَطَّرْنَ مِن فَوْقِهِنَّ ۚ وَالْمَلَائِكَةُ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَيَسْتَغْفِرُونَ لِمَن فِي الْأَرْضِ ۗ أَلَا إِنَّ اللَّـهَ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٥﴾

5. Zinakaribia mbingu kuraruka moja juu ya nyingine[2], na Malaika wanasabbih na kumhimidi Rabb wao, na wanawaombea maghfirah walioko ardhini. Tanabahi! Hakika Allaah Ndiye Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.[3]

 

 

 

 

وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ اللَّـهُ حَفِيظٌ عَلَيْهِمْ وَمَا أَنتَ عَلَيْهِم بِوَكِيلٍ﴿٦﴾

6. Na wale waliojichukulia badala Yake marafiki wandani na walinzi, Allaah Anayahifadhi matendo yao, nawe si mdhamini wao.

 

 

 

 

 

وَكَذَٰلِكَ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ قُرْآنًا عَرَبِيًّا لِّتُنذِرَ أُمَّ الْقُرَىٰ وَمَنْ حَوْلَهَا وَتُنذِرَ يَوْمَ الْجَمْعِ لَا رَيْبَ فِيهِ ۚ فَرِيقٌ فِي الْجَنَّةِ وَفَرِيقٌ فِي السَّعِيرِ﴿٧﴾

7. Na hivyo ndivyo Tulivyokufunulia Wahy wa Qur-aan ya Kiarabu ili uonye Ummul-Quraa[4] (Mama wa miji [Makkah]), na wale waliozunguka pembezoni mwake, na uonye Siku ya kujumuika isiyokuwa na shaka ndani yake. Kundi litakuwa katika Jannah, na kundi katika moto uliowashwa vikali mno.

 

 

 

 

وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ لَجَعَلَهُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَلَـٰكِن يُدْخِلُ مَن يَشَاءُ فِي رَحْمَتِهِ ۚ وَالظَّالِمُونَ مَا لَهُم مِّن وَلِيٍّ وَلَا نَصِيرٍ﴿٨﴾

8. Na lau Angelitaka Allaah Angeliwafanya ummah mmoja, lakini Anamuingiza Amtakaye katika Rehma Yake. Na madhalimu hawana mlinzi yeyote wala mwenye kunusuru.

 

 

 

 

أَمِ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ ۖ فَاللَّـهُ هُوَ الْوَلِيُّ وَهُوَ يُحْيِي الْمَوْتَىٰ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿٩﴾

9. Je, wamejichukulia badala Yake marafiki wandani na walinzi? Basi Allaah Yeye Ndiye Mlinzi, Naye Ndiye Anayehuisha wafu, Naye juu ya kila kitu ni Muweza.

 

 

 

 

وَمَا اخْتَلَفْتُمْ فِيهِ مِن شَيْءٍ فَحُكْمُهُ إِلَى اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبِّي عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَإِلَيْهِ أُنِيبُ﴿١٠﴾

10. Na katika lolote lile mlilokhitilafiana, basi hukumu yake irejesheni kwa Allaah. Huyo Ndiye Allaah Rabb wangu, Kwake nimetawakali, na Kwake naelekea kwa mambo yangu yote.

 

 

 

 

 

فَاطِرُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ جَعَلَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا وَمِنَ الْأَنْعَامِ أَزْوَاجًا ۖ يَذْرَؤُكُمْ فِيهِ ۚ لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ﴿١١﴾

11. Muanzilishi wa mbingu na ardhi. Amekujaalieni kutokana na nafsi zenu mume na mke, na katika wanyama wa mifugo dume na jike. Anakusambazeni humo. Hakuna chochote kinachofanana Naye, Naye Ni Mwenye Kusikia yote, Mwenye Kuona yote.[5]

 

 

 

 

لَهُ مَقَالِيدُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ وَيَقْدِرُ ۚ إِنَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿١٢﴾

12. Ni Zake funguo za mbingu na ardhi, Anamkunjulia riziki Amtakaye na Humkadiria kwa kipimo (Amtakaye). Hakika Yeye Ni Mjuzi kwa kila kitu.[6]

 

 

 

 

شَرَعَ لَكُم مِّنَ الدِّينِ مَا وَصَّىٰ بِهِ نُوحًا وَالَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ وَمَا وَصَّيْنَا بِهِ إِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ وَعِيسَىٰ ۖ أَنْ أَقِيمُوا الدِّينَ وَلَا تَتَفَرَّقُوا فِيهِ ۚ كَبُرَ عَلَى الْمُشْرِكِينَ مَا تَدْعُوهُمْ إِلَيْهِ ۚ اللَّـهُ يَجْتَبِي إِلَيْهِ مَن يَشَاءُ وَيَهْدِي إِلَيْهِ مَن يُنِيبُ ﴿١٣﴾

13. Amekuamuruni katika Dini yale Aliyomuusia kwayo Nuwh, na ambayo Tumekufunulia Wahy (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), na Tuliyomuusia kwayo Ibraahiym, na Muwsaa na ‘Iysaa kwamba: Simamisheni Dini na wala msifarikiane humo. Yamekuwa magumu kwa washirikina yale unayowalingania. Allaah Anamteua Kwake Amtakaye, na Anamhidi Kwake mwenye kumwelekea.

 

 

 

 

وَمَا تَفَرَّقُوا إِلَّا مِن بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْعِلْمُ بَغْيًا بَيْنَهُمْ ۚ وَلَوْلَا كَلِمَةٌ سَبَقَتْ مِن رَّبِّكَ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى لَّقُضِيَ بَيْنَهُمْ ۚ وَإِنَّ الَّذِينَ أُورِثُوا الْكِتَابَ مِن بَعْدِهِمْ لَفِي شَكٍّ مِّنْهُ مُرِيبٍ ﴿١٤﴾

14. Na hawakufarikiana isipokuwa baada ya kuwajia ilimu kutokana na kufanyiana baghi[7] (uadui (chuki, husuda) baina yao. Na kama si neno lililotangulia (kuakhirisha adhabu) kutoka kwa Rabb wako mpaka muda maalumu uliokadiriwa, basi ingelikidhiwa baina yao. Na hakika wale waliorithishwa Kitabu baada yao bila shaka wamo katika shaka na wasiwasi nayo.  

 

 

 

فَلِذَٰلِكَ فَادْعُ ۖ وَاسْتَقِمْ كَمَا أُمِرْتَ ۖ وَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَاءَهُمْ ۖ وَقُلْ آمَنتُ بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ مِن كِتَابٍ ۖ وَأُمِرْتُ لِأَعْدِلَ بَيْنَكُمُ ۖ اللَّـهُ رَبُّنَا وَرَبُّكُمْ ۖ لَنَا أَعْمَالُنَا وَلَكُمْ أَعْمَالُكُمْ ۖ لَا حُجَّةَ بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمُ ۖ اللَّـهُ يَجْمَعُ بَيْنَنَا ۖ وَإِلَيْهِ الْمَصِيرُ﴿١٥﴾

15. Basi kwa hayo walinganie (ee Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم, na thibiti imara kama ulivyoamrishwa, na wala usifuate hawaa zao. Na sema: Nimeamini Vitabu vyote Alivyoviteremsha Allaah, na nimeamrishwa niadilishe baina yenu. Allaah Ni Rabb wetu na Rabb wenu, sisi tuna amali zetu, nanyi mna amali zenu. Hakuna kubishana baina yetu na baina yenu, Allaah Atatujumuisha baina yetu, na Kwake ndio mahali pa kuishia.

 

 

 

 

وَالَّذِينَ يُحَاجُّونَ فِي اللَّـهِ مِن بَعْدِ مَا اسْتُجِيبَ لَهُ حُجَّتُهُمْ دَاحِضَةٌ عِندَ رَبِّهِمْ وَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ وَلَهُمْ عَذَابٌ شَدِيدٌ﴿١٦﴾

16. Na wale wanaobishana kuhusu Allaah baada ya kuitikiwa, hoja yao ni baatwil mbele ya Rabb wao, na juu yao iko ghadhabu, na watapata adhabu shadidi.

 

 

 

 

 

اللَّـهُ الَّذِي أَنزَلَ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ وَالْمِيزَانَ ۗ وَمَا يُدْرِيكَ لَعَلَّ السَّاعَةَ قَرِيبٌ﴿١٧﴾

17. Allaah Ambaye Ameteremsha Kitabu hiki kwa haki na mizani. Na nini kitakachokujulisha pengine Saa (Qiyaamah) iko karibu?

 

 

 

 

 

يَسْتَعْجِلُ بِهَا الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِهَا ۖ وَالَّذِينَ آمَنُوا مُشْفِقُونَ مِنْهَا وَيَعْلَمُونَ أَنَّهَا الْحَقُّ ۗ أَلَا إِنَّ الَّذِينَ يُمَارُونَ فِي السَّاعَةِ لَفِي ضَلَالٍ بَعِيدٍ﴿١٨﴾

18. Wanaihimiza wale wasioiamini. Na wale walioamini wanaiogopa na wanaitambua kwamba ni haki. Tanabahi!  Hakika wale wanaotilia shaka kuhusu Saa, bila shaka wamo katika upotofu wa mbali.

 

 

 

 

اللَّـهُ لَطِيفٌ بِعِبَادِهِ يَرْزُقُ مَن يَشَاءُ ۖ وَهُوَ الْقَوِيُّ الْعَزِيزُ﴿١٩﴾

19. Allaah Ni Latifu[8] kwa Waja Wake, Anamruzuku Amtakaye, Naye Ndiye Mwenye nguvu zote, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika.

 

 

 

 

مَن كَانَ يُرِيدُ حَرْثَ الْآخِرَةِ نَزِدْ لَهُ فِي حَرْثِهِ ۖ وَمَن كَانَ يُرِيدُ حَرْثَ الدُّنْيَا نُؤْتِهِ مِنْهَا وَمَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِن نَّصِيبٍ﴿٢٠﴾

20. Yeyote atakaye mavuno ya Aakhirah Tutamzidishia katika mavuno yake. Na yeyote atakaye mavuno ya dunia, Tutampa humo, lakini Aakhirah hatokuwa na fungu lolote.[9]

 

 

 

 

أَمْ لَهُمْ شُرَكَاءُ شَرَعُوا لَهُم مِّنَ الدِّينِ مَا لَمْ يَأْذَن بِهِ اللَّـهُ ۚ وَلَوْلَا كَلِمَةُ الْفَصْلِ لَقُضِيَ بَيْنَهُمْ ۗ وَإِنَّ الظَّالِمِينَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ﴿٢١﴾

21. Je, wanao washirika waliowaamuru dini ambayo Allaah Hakuitolea idhini? Na lau si neno la uamuzi, basi jambo lingelimalizwa (hapa duniani) baina yao. Na hakika madhalimu watapata adhabu iumizayo.[10]

 

 

 

 

تَرَى الظَّالِمِينَ مُشْفِقِينَ مِمَّا كَسَبُوا وَهُوَ وَاقِعٌ بِهِمْ ۗ وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فِي رَوْضَاتِ الْجَنَّاتِ ۖ لَهُم مَّا يَشَاءُونَ عِندَ رَبِّهِمْ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَضْلُ الْكَبِيرُ﴿٢٢﴾

22. Utawaona madhalimu ni wenye kuogopa kwa yale waliyoyachuma, nayo yatawafikia tu. Na wale walioamini na wakatenda mema watakuwa katika mabustani yaliyositawi ya Jannah. Watapata wayatakayo kwa Rabb wao, hiyo ndio fadhila kubwa.

 

 

 

 

ذَٰلِكَ الَّذِي يُبَشِّرُ اللَّـهُ عِبَادَهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ ۗ قُل لَّا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ أَجْرًا إِلَّا الْمَوَدَّةَ فِي الْقُرْبَىٰ ۗ وَمَن يَقْتَرِفْ حَسَنَةً نَّزِدْ لَهُ فِيهَا حُسْنًا ۚ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ شَكُورٌ﴿٢٣﴾

23. Hayo ndiyo Aliyowabashiria Allaah Waja Wake wale walioamini na wakatenda mema. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Sikuombeni ujira wowote juu yake isipokuwa mapenzi kwa ajili ya ujamaa wa karibu. Na yeyote anayechuma mazuri, Tutamzidishia humo zuri. Hakika Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mwingi wa Kupokea Shukurani.

 

 

 

 

أَمْ يَقُولُونَ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا ۖ فَإِن يَشَإِ اللَّـهُ يَخْتِمْ عَلَىٰ قَلْبِكَ ۗ وَيَمْحُ اللَّـهُ الْبَاطِلَ وَيُحِقُّ الْحَقَّ بِكَلِمَاتِهِ ۚ إِنَّهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ﴿٢٤﴾

24. Bali wanasema: Amemtungia Allaah uongo? Basi Allaah Akitaka Atapiga mhuri juu ya moyo wako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Na Allaah Anafuta baatwil, na Ataisimamisha haki kwa Maneno Yake. Hakika Yeye Ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.

 

 

 

 

وَهُوَ الَّذِي يَقْبَلُ التَّوْبَةَ عَنْ عِبَادِهِ وَيَعْفُو عَنِ السَّيِّئَاتِ وَيَعْلَمُ مَا تَفْعَلُونَ﴿٢٥﴾

25. Naye Ndiye Ambaye Anapokea tawbah kutoka kwa Waja Wake, na Anasamehe maovu, na Anayajua mnayoyafanya.

 

 

 

 

 

 

وَيَسْتَجِيبُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَيَزِيدُهُم مِّن فَضْلِهِ ۚ وَالْكَافِرُونَ لَهُمْ عَذَابٌ شَدِيدٌ﴿٢٦﴾

26. Na Anawaitikia wale walioamini na wakatenda mema, na Anawazidishia Fadhila Zake. Na makafiri watapata adhabu kali.

 

 

 

 

 

وَلَوْ بَسَطَ اللَّـهُ الرِّزْقَ لِعِبَادِهِ لَبَغَوْا فِي الْأَرْضِ وَلَـٰكِن يُنَزِّلُ بِقَدَرٍ مَّا يَشَاءُ ۚ إِنَّهُ بِعِبَادِهِ خَبِيرٌ بَصِيرٌ﴿٢٧﴾

27. Na lau kama Allaah Angelikunjua riziki kwa Waja Wake, basi wangeruka mipaka katika ardhi. Lakini Anateremsha kwa kadiri ya Akitakacho. Hakika Yeye kwa Waja Wake Ni Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri, Mwenye Kuona yote.

 

 

 

وَهُوَ الَّذِي يُنَزِّلُ الْغَيْثَ مِن بَعْدِ مَا قَنَطُوا وَيَنشُرُ رَحْمَتَهُ ۚ وَهُوَ الْوَلِيُّ الْحَمِيدُ﴿٢٨﴾

28. Naye Ndiye Anayeteremsha mvua baada ya kuwa wamekata tamaa, na Anaeneza Rehma Yake. Naye Ndiye Mlinzi[11], Mwenye Kustahiki Kuhimidiwa kwa yote.

 

 

 

 

وَمِنْ آيَاتِهِ خَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَثَّ فِيهِمَا مِن دَابَّةٍ ۚ وَهُوَ عَلَىٰ جَمْعِهِمْ إِذَا يَشَاءُ قَدِيرٌ﴿٢٩﴾

29. Na katika Aayaat (Ishara, Dalili) Zake, ni uumbaji wa mbingu na ardhi, na Aliowatawanya humo kati ya viumbe vinavyotembea, Naye kuwakusanya Atakapo Ni Muweza.

 

 

 

 

وَمَا أَصَابَكُم مِّن مُّصِيبَةٍ فَبِمَا كَسَبَتْ أَيْدِيكُمْ وَيَعْفُو عَن كَثِيرٍ﴿٣٠﴾

30. Na msiba wowote unaokusibuni, basi ni kwa sababu ya yale iliyochuma mikono yenu, na Anasamehe mengi.

 

 

 

 

وَمَا أَنتُم بِمُعْجِزِينَ فِي الْأَرْضِ ۖ وَمَا لَكُم مِّن دُونِ اللَّـهِ مِن وَلِيٍّ وَلَا نَصِيرٍ﴿٣١﴾

31. Nanyi si wenye kuweza kukwepa ardhini, na wala hamna badala Yake mlinzi yeyote wala mwenye kunusuru.

 

 

 

 

وَمِنْ آيَاتِهِ الْجَوَارِ فِي الْبَحْرِ كَالْأَعْلَامِ﴿٣٢﴾

32. Na katika Aayaat (Ishara, Dalili) Zake ni merikebu zinazotembea baharini kama milima.

 

 

 

 

إِن يَشَأْ يُسْكِنِ الرِّيحَ فَيَظْلَلْنَ رَوَاكِدَ عَلَىٰ ظَهْرِهِ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّكُلِّ صَبَّارٍ شَكُورٍ﴿٣٣﴾

33. Akitaka Anautuliza upepo wa dhoruba zikabaki zimetuama juu ya bahari. Hakika katika hayo mna Aayaat (Ishara, Mazingatio) kwa kila mwingi wa kuvuta subira, mwingi wa kushukuru.

 

 

 

 

أَوْ يُوبِقْهُنَّ بِمَا كَسَبُوا وَيَعْفُ عَن كَثِيرٍ﴿٣٤﴾

34. Au Aziangamize kwa sababu ya waliyoyachuma, na (Akitaka) Anasamehe mengi.

 

 

 

 

وَيَعْلَمَ الَّذِينَ يُجَادِلُونَ فِي آيَاتِنَا مَا لَهُم مِّن مَّحِيصٍ﴿٣٥﴾

35. Na ili wapate kujua wale wanaojadiliana kuzipinga Aayaat (na Ishara, Hoja, Dalili) Zetu, kwamba hawana mahali popote pa kukimbilia.

 

 

 

 

فَمَا أُوتِيتُم مِّن شَيْءٍ فَمَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَمَا عِندَ اللَّـهِ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ لِلَّذِينَ آمَنُوا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ﴿٣٦﴾

36. Na kitu chochote mlichopewa basi ni starehe ndogo za ya uhai wa dunia.  Na yale yaliyoko kwa Allaah ni bora zaidi na ni ya kudumu kwa wale walioamini, na kwa Rabb wao wanatawakali.

 

 

 

 

وَالَّذِينَ يَجْتَنِبُونَ كَبَائِرَ الْإِثْمِ وَالْفَوَاحِشَ وَإِذَا مَا غَضِبُوا هُمْ يَغْفِرُونَ﴿٣٧﴾

37. Na wale wanaojiepusha na madhambi makubwa na machafu[12] na wanapoghadhibika wao wanasamehe.

 

 

 

 

 

وَالَّذِينَ اسْتَجَابُوا لِرَبِّهِمْ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَمْرُهُمْ شُورَىٰ بَيْنَهُمْ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ﴿٣٨﴾

38. Na wale waliomuitikia Rabb wao, wakasimamisha Swalaah, na jambo lao hushauriana baina yao, na kutokana na vile Tulivyowaruzuku wanatoa.[13]

 

 

 

 

وَالَّذِينَ إِذَا أَصَابَهُمُ الْبَغْيُ هُمْ يَنتَصِرُونَ﴿٣٩﴾

39. Na wale wanapokabiliwa na baghi[14] (ukandamizaji na dhulma), wao wanajitetea.

 

 

 

 

وَجَزَاءُ سَيِّئَةٍ سَيِّئَةٌ مِّثْلُهَا ۖ فَمَنْ عَفَا وَأَصْلَحَ فَأَجْرُهُ عَلَى اللَّـهِ ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الظَّالِمِينَ﴿٤٠﴾

40. Na jazaa ya uovu ni uovu mfano wake. Lakini atakayesamehe na akajenga mahusiano mema na aliyemkosea, basi ujira wake uko kwa Allaah. Hakika Yeye Hapendi madhalimu.

 

 

 

وَلَمَنِ انتَصَرَ بَعْدَ ظُلْمِهِ فَأُولَـٰئِكَ مَا عَلَيْهِم مِّن سَبِيلٍ﴿٤١﴾

41. Na bila shaka anayelipiza kisasi baada ya kudhulumiwa, basi hao hawana sababu ya kulaumiwa.

 

 

 

 

إِنَّمَا السَّبِيلُ عَلَى الَّذِينَ يَظْلِمُونَ النَّاسَ وَيَبْغُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ ۚ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ﴿٤٢﴾

42. Hakika sababu (ya kulaumiwa) ni juu ya wale wanaodhulumu[15] watu na wanafanya baghi[16] (ukandamizaji) katika ardhi bila ya haki. Hao watapata adhabu iumizayo.

 

 

 

 

وَلَمَن صَبَرَ وَغَفَرَ إِنَّ ذَٰلِكَ لَمِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ﴿٤٣﴾

43. Na atakayevuta subira na akasamehe, hakika hilo bila shaka ni katika mambo ya kuazimiwa.

 

 

 

 

وَمَن يُضْلِلِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِن وَلِيٍّ مِّن بَعْدِهِ ۗ وَتَرَى الظَّالِمِينَ لَمَّا رَأَوُا الْعَذَابَ يَقُولُونَ هَلْ إِلَىٰ مَرَدٍّ مِّن سَبِيلٍ﴿٤٤﴾

44. Na aliyepotolewa na Allaah basi hatopata rafiki mlinzi (na msaidizi) baada Yake. Na utawaona madhalimu watakapoiona adhabu wakisema: Je, ipo njia yoyote ya kurudi (duniani)?

 

 

 

 

وَتَرَاهُمْ يُعْرَضُونَ عَلَيْهَا خَاشِعِينَ مِنَ الذُّلِّ يَنظُرُونَ مِن طَرْفٍ خَفِيٍّ ۗ وَقَالَ الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ الْخَاسِرِينَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ وَأَهْلِيهِمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ أَلَا إِنَّ الظَّالِمِينَ فِي عَذَابٍ مُّقِيمٍ﴿٤٥﴾

45. Na utawaona wanahudhurishwa (kwenye moto) wakiwa wanyenyekevu kutokana na udhalilifu, wanatazama kwa mtazamo wa kificho. Na watasema wale walioamini: Hakika wenye kukhasirika ni wale waliokhasiri nafsi zao na ahli zao Siku ya Qiyaamah. Tanabahi!  Hakika madhalimu wamo katika adhabu ya kudumu.

 

 

 

 

وَمَا كَانَ لَهُم مِّنْ أَوْلِيَاءَ يَنصُرُونَهُم مِّن دُونِ اللَّـهِ ۗ وَمَن يُضْلِلِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِن سَبِيلٍ﴿٤٦﴾

46. Na wala hawatokuwa na rafiki walinzi wowote wa kuwanusuru badala ya Allaah. Na ambaye Allaah Amempotoa basi hatopata njia (ya kuongoka).

 

 

 

 

اسْتَجِيبُوا لِرَبِّكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ يَوْمٌ لَّا مَرَدَّ لَهُ مِنَ اللَّـهِ ۚ مَا لَكُم مِّن مَّلْجَإٍ يَوْمَئِذٍ وَمَا لَكُم مِّن نَّكِيرٍ﴿٤٧﴾

47. Muitikieni Rabb wenu kabla haijafika Siku isiyo rudishwa nyuma kutoka kwa Allaah. Hamtokuwa na mahali popote pa kukimbilia Siku hiyo na wala hamtoweza kukanusha chochote.

 

 

 

 

فَإِنْ أَعْرَضُوا فَمَا أَرْسَلْنَاكَ عَلَيْهِمْ حَفِيظًا ۖ إِنْ عَلَيْكَ إِلَّا الْبَلَاغُ ۗ وَإِنَّا إِذَا أَذَقْنَا الْإِنسَانَ مِنَّا رَحْمَةً فَرِحَ بِهَا ۖ وَإِن تُصِبْهُمْ سَيِّئَةٌ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيهِمْ فَإِنَّ الْإِنسَانَ كَفُورٌ﴿٤٨﴾

48. Wakikengeuka, basi Hatukutuma (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) uwe mwenye kuwahifadhi. Si juu yako isipokuwa ubalighisho (wa Risala). Na hakika Sisi Tunapomwonjesha binaadam Rehma kutoka Kwetu, huifurahia. Na linapowasibu ovu kwa sababu ya iliyotanguliza mikono yao, basi hakika binaadam ni mwingi wa kukufuru.

 

 

 

 

لِّلَّـهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ ۚ يَهَبُ لِمَن يَشَاءُ إِنَاثًا وَيَهَبُ لِمَن يَشَاءُ الذُّكُورَ﴿٤٩﴾

49. Ni wa Allaah Pekee ufalme wa mbingu na ardhi. Anaumba Atakacho. Humtunukia Amtakaye wana wa kike, na Humtunukia Amtakaye wana wa kiume.

 

 

 

 

أَوْ يُزَوِّجُهُمْ ذُكْرَانًا وَإِنَاثًا ۖ وَيَجْعَلُ مَن يَشَاءُ عَقِيمًا ۚ إِنَّهُ عَلِيمٌ قَدِيرٌ﴿٥٠﴾

50. Au Huwachanganya wa kiume na wa kike, na Humjaalia Amtakaye kuwa ni tasa. Hakika Yeye Ni Mjuzi wa yote, Muweza wa yote.

 

 

 

 

وَمَا كَانَ لِبَشَرٍ أَن يُكَلِّمَهُ اللَّـهُ إِلَّا وَحْيًا أَوْ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ أَوْ يُرْسِلَ رَسُولًا فَيُوحِيَ بِإِذْنِهِ مَا يَشَاءُ ۚ إِنَّهُ عَلِيٌّ حَكِيمٌ﴿٥١﴾

51. Na wala haikuwa kwa mtu yeyote kwamba Allaah Amsemeze isipokuwa kwa Wahy au kutoka nyuma ya kizuizi, au Hutuma Mjumbe (Malaika), kisha Anamfunulia Wahy Ayatakayo kwa Idhini Yake.[17] Hakika Yeye Ni Mwenye ‘Uluwa, Mwenye Hikmah wa yote.

 

 

 

 

وَكَذَٰلِكَ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ رُوحًا مِّنْ أَمْرِنَا ۚ مَا كُنتَ تَدْرِي مَا الْكِتَابُ وَلَا الْإِيمَانُ وَلَـٰكِن جَعَلْنَاهُ نُورًا نَّهْدِي بِهِ مَن نَّشَاءُ مِنْ عِبَادِنَا ۚ وَإِنَّكَ لَتَهْدِي إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ﴿٥٢﴾

52. Na hivyo ndivyo Tulivyokuletea Ruwh[18] (Qur-aan) kutokana na Amri Yetu. Hukuwa unajua nini Kitabu wala imaan lakini Tumeifanya ni Nuru, Tunaongoa kwayo Tumtakaye miongoni mwa Waja Wetu. Na hakika wewe (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) bila shaka unaongoza kuelekea njia iliyonyooka.[19]

 

 

 

 

صِرَاطِ اللَّـهِ الَّذِي لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ أَلَا إِلَى اللَّـهِ تَصِيرُ الْأُمُورُ﴿٥٣﴾

53. Njia ya Allaah Ambaye ni Vyake Pekee vyote vilivyomo mbinguni na vyote vilivyomo ardhini. Tanabahi! Kwa Allaah Pekee yanaishia mambo yote.

 

 

[1] الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah):

 

Hizi ni herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Tanbihi ya Al-Baqarah (2:1).

 

[2] Kuraruka Mbingu Kutokana Na Kumkhofu Allaah Kwa Utukufu Wake: 

 

‘Ulamaa wa Tafsiyr wamesherehesha ifuatavyo:

 

Pamoja na ukubwa wa mbingu na kuwa hazina uhai, lakini zinakaribia kuraruka kutokana na khofu na Utukufu wa Allaah. [Tafsiyr As-Sa’diy]  

 

Zinakaribia mbingu kupasukapasuka, kila moja juu ya ile inayoifuata, kutokana na Utukufu wa Mwingi wa Rehma na Ujalali Wake, Tabaaraka wa Ta’aalaa (Amebarikika na Ametukuka).  [Tafsiyr Al-Muyassar]

 

Na hivyo ni kama Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى) katika Suwrah Al-Hashr (59:21). Rejea huko kupata faida nyenginezo:  

 

Na katika Suwrah Maryam (19) Aayah namba (88-91), imetajwa mbingu kuraruka kutokana na kumzulia Allaah (سبحانه وتعالى) Ana mwana. Rejea huko kwenye Tafsiyr za ‘Ulamaa na faida nyenginezo. 

 

[3] Malaika Wanamhimidi Allaah Na Wanawaombea Maghfirah Walioko Ardhini:

 

Tafsiyr:

 

Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَالْمَلَائِكَةُ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَيَسْتَغْفِرُونَ لِمَن فِي الْأَرْضِ ۗ أَلَا إِنَّ اللَّـهَ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٥﴾

“Na Malaika wanasabbih na kumhimidi Rabb wao, na wanawaombea maghfirah walioko ardhini. Tanabahi! Hakika Allaah Ndiye Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.”

 

وَالْمَلَائِكَةُ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ  

“Na Malaika wanasabbih na kumhimidi Rabb wao.”

 

Kutokana na U’adhwama Wake, Malaika watukufu waliokurubishwa wanamnyenyekea Allaah, na kwa ‘Izza Yake wako tuli hawababaiki, na kwa Uola Wake wanatekeleza Amri Zake zote kwa utiifu wa hali ya juu kabisa. Isitoshe, wanamuadhimisha na kumtakasa Allaah (سبحانه وتعالى) na kila upungufu, na wanamsifu kwa kila sifa za ukamilifu. 

 

وَيَسْتَغْفِرُونَ لِمَن فِي الْأَرْضِ ۗ

“Na wanawaombea maghfirah walioko ardhini.” 

 

Ni kutokana na yale wanayoyafanya ambayo hayaendani na Utukufu na Ukubwa wa Allaah (سبحانه وتعالى) pamoja na kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) ni:

 

  الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٥﴾

“Mwingi wa Kughufuria, Mwenye Kurehemu.”

 

Ambae kama si Maghfirah Yake na Rehma Yake, basi Angewaharakishia Waja Wake adhabu. Ama Allaah kusifika na sifa hizi, baada ya kutaja kwamba Ameteremsha Wahy kwa Rusuli wote kwa ujumla, na kwa Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) khaswa, haya yote ni ishara kwamba katika hii Qur-aan kuna dalili za wazi, na Aayah zinazoonyesha Ukamilifu wa Allaah Muumba, na kwamba Yeye Kuelezewa kwa Majina haya Matukufu Mazuri, kunazijaza nyoyo maarifa ya kumjua, kumpenda, kumuadhimisha, kumtukuza na kumheshimu, na kunamfanya pia mja aelekeze aina zake zote za utumwa wa siri na wa dhahiri Kwake tu Allaah (سبحانه وتعالى), na kwamba katika dhulma kubwa na maneno mabaya, ni kujifanyia mshirika kwa Allaah, kumuabudia asiyekuwa Yeye, vile ambavyo havinufaishi wala havidhuru, bali hivyo ni viumbe ambavyo vinahitajia kwa Allaah kwa hali zao zote. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

[4] Ummul-Quraa (Mama Wa Miji) Ni Makkah:

 

Rejea: Al-An’aam (6:92).

 

[5] Allaah (سبحانه وتعالى) Hafanani Na Yeyote Katika Majina Na Sifa Zake:

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Muumba mbingu na ardhi na Muanzilishi wa kuzitengeneza kwa Uweza Wake na Matakwa Yake na Hikma Yake. Amewapatia nyinyi wake wanaotokana na nyinyi ili mjitulize kwao, na Amewapatia nyinyi Wanyama howa wa kila aina, wa kiume na wa kike. Anawafanya nyinyi muwe wengi kwa kuzaana kwa njia hii ya kutangamana. Hakuna kinachofanana na Yeye (سبحانه وتعالى) na kuwa kama Yeye chochote kile miongoni mwa Viumbe Vyake, si katika Dhati Yake wala Majina Yake wala Sifa Zake wala Vitendo Vyake. Kwani Majina Yake yote ni mazuri na sifa Zake ni sifa za ukamilifu na Utukufu, na kwa Vitendo Vyake (سبحانه وتعالى), Amefanya vipatikane viumbe vikubwa bila ya kuwa na mshirika. Na Yeye Ndiye Mwenye Kusikia na Ndiye Mwenye Kuona. Hakuna chochote kinachofichamana Kwake cha matendo ya Waja Wake na maneno yao, na Atawalipa kwa hayo. [Tafsiyr Al-Muyassar]

 

Rejea pia Huwd (11:37).

 

[6] Allaah Anakunjua Rizki Atakavyo Na Anazuia Atakavyo Kwa Hikma Yake:

 

Rejea Kauli za Allaah (سبحانه وتعالى) katika Suwrah Ar-Ra’d (13:26), Al-Israa (17:30), Al-‘Ankabuwt (29:62), Ar-Ruwm (30:37), Saba-a (34:36), (34:39), Az-Zumar (39:52).

 

Na Tafsiyr ya Aayah hii ni kama ifuatavyo:  

 

لَهُ مَقَالِيدُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ وَيَقْدِرُ ۚ إِنَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿١٢﴾

“Ni Zake funguo za mbingu na ardhi, Anamkunjulia riziki Amtakaye na Humkadiria kwa kipimo (Amtakaye). Hakika Yeye Ni Mjuzi kwa kila kitu.”

 

Anakusudia: Ufalme wa mbingu na ardhi ni Wake, na katika Mikono Yake kuna funguo za rizki na rehma, na neema za wazi na za siri. Viumbe wote ni wenye kumuhitajia Allaah (سبحانه وتعالى) katika kuleta maslahi na kuondosha madhara kwao katika kila hali, na hakuna yeyote anaeweza kufanya hivyo.

 

Na Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Mwenye kutoa na Mwenye kuzuia, Mwenye kudhuru na Mwenye kunufaisha, Ambae kila neema iliyopo kwa waja inatoka Kwake, na hakuna anaeweza kuondosha shari isipokuwa Yeye. Na

 

مَّا يَفْتَحِ اللَّـهُ لِلنَّاسِ مِن رَّحْمَةٍ فَلَا مُمْسِكَ لَهَا ۖ وَمَا يُمْسِكْ فَلَا مُرْسِلَ لَهُ مِن بَعْدِهِ ۚ  ﴿٢﴾

 

“Rehma yoyote Anayoifungua Allaah kwa watu, basi hakuna wa kuizuia, na Anayoizuia, basi hakuna wa kuipeleka baada Yake.” [Faatwir (35:2)]

 

[Rejea pia Faatwir (35:2) kewenye faida]

 

Na ndio maana Anasema:

 

يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ وَيَقْدِرُ ۚ إِنَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿١٢﴾

“Anamkunjulia riziki Amtakaye na Humkadiria kwa kipimo (Amtakaye). Hakika Yeye Ni Mjuzi kwa kila kitu.”

 

Anaiongeza na kumpa rizki kiasi Anachokitaka Amtakaye, na Anaizuia (kuibana) kwa Amtakae, mpaka inakuwa kwa kiasi cha mahitaji yake, na wala Haiongezeki, na haya yote yanakwenda sambamba na Ilimu Yake na Hikma Zake. Na kwa sababu hiyo ndio Anasema:

إِنَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿١٢﴾

“Hakika Yeye Ni Mjuzi kwa kila kitu.”

 

[Tafsiyr As-Sa’diy]

 

[7] Maana Ya Baghyun/Baghaa Katika Qur-aan:

 

Baghyun/Baghaa katika Qur-aan imetumika katika maana mbalimbali. Mfano katika Suwrah hii, baghyun/baghaa imetajwa katika Aayah zifuatazo:

 

Aayah 14: Uadui, chuki, husuda.

 

Aayah 27: Urukaji mipaka.

 

Aayah 39: Ukandamizaji na dhulma.

 

Aayah 42: Ukandamizaji.

 

Aayah nyenginezo zilizotajwa neno hilo la baghyun/baghaa na maana zake ni hizi zifuatazo:

 

(i) Maasi, uovu na ufisadi: Rejea Yuwnus (10:23).

 

(ii) Dhulma, ukandamizaji: Rejea Al-An’aam (6:146), Al-‘Araaf (7:33), Yuwnus (10:90), An-Nahl (16:90), Al-Hujuraat (49:9), Swaad (38:22) (38:24).

 

(iii) Uonevu na kutakabari: Rejea Al-Qaswasw (28:76).

 

(iv) Kuruka mipaka: Rejea Al-Baqarah (2:173).

 

(v) Kukusudia jambo: Rejea Al-A’raaf (7:45).

 

(vi) Chuki, uhasidi: Rejea Al-Baqarah (2:90), (2:213), Aal-‘Imraan (3:19).

 

(vii) Ukahaba: Rejea An-Nuwr (24:33), Maryam (19:20), (19:28).

 

[8] Latwiyf:

 

Rejea Faharasa Ya Majina Mazuri Ya Allaah Na Sifa Zake.

 

[9] Mwenye Kutaka Mavuno Ya Dunia Badala Ya Mavuno Ya Aakhirah:

 

Tafsiyr:

مَن كَانَ يُرِيدُ حَرْثَ الْآخِرَةِ

“Yeyote atakaye mavuno ya Aakhirah.”

 

Malipo na thawabu zake, Akaamini na kuzisadikisha, na akafanya juhudi kwa ajili ya kuzipata.

 

  نَزِدْ لَهُ فِي حَرْثِهِ ۖ  

“Tutamzidishia katika mavuno yake.”  

 

Kwa kumzidishia malipo ya matendo yake, kwa ziada nyingi, kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَمَنْ أَرَادَ الْآخِرَةَ وَسَعَىٰ لَهَا سَعْيَهَا وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَأُولَـٰئِكَ كَانَ سَعْيُهُم مَّشْكُورًا ﴿١٩﴾

“Na anayetaka Aakhirah na akaifanyia juhudi inayostahiki kufanyiwa, naye ni Muumin, basi hao juhudi zao ni za kushukuriwa.” [Al-Israa (17:19)]

 

Pamoja na hilo, ama fungu lake la hapa Duniani hapana budi limfikie.

 

وَمَن كَانَ يُرِيدُ حَرْثَ الدُّنْيَا  

“Na yeyote atakaye mavuno ya dunia.”

 

Yule ambae dunia ndio makusudio na malengo yake, na wala hakufanya (matendo) kwa ajili ya Aakhirah yake, na wala hakuwa akitaraji thawabu ya hayo matendo, na wala hakuogopa madhambi kwa matendo hayo, basi:

 

  نُؤْتِهِ مِنْهَا وَمَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِن نَّصِيبٍ﴿٢٠﴾

“Tutampa humo, lakini Aakhirah hatokuwa na fungu lolote.”

 

 

Fungu lake alilo gaiwa. Hakika ameshanyimwa Jannah na Neema zake, na atakuwa amestahiki moto. Na Aayah hii inafanana sana na Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

 

مَن كَانَ يُرِيدُ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا وَزِينَتَهَا نُوَفِّ إِلَيْهِمْ أَعْمَالَهُمْ فِيهَا وَهُمْ فِيهَا لَا يُبْخَسُونَ﴿١٥﴾ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ لَيْسَ لَهُمْ فِي الْآخِرَةِ إِلَّا النَّارُ ۖ وَحَبِطَ مَا صَنَعُوا فِيهَا وَبَاطِلٌ مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴿١٦﴾

 

“Anayetaka uhai wa dunia na mapambo yake Tutawalipa kikamilifu amali zao humo, nao hawatopunjwa humo. Hao ndio wale ambao hawatokuwa na chochote katika Aakhirah isipokuwa moto. Na yataporomoka yale waliyoyafanya humo (duniani), na yatabatilika yale waliyokuwa wakiyatenda.” [Huwd (11:15-16)]

 

Na Aayah kadhaa zimetaja kustahabu maisha ya dunia badala ya maisha ya Aakhirah, na kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Anaahidi kheri na neema nyingi za kudumu za Aakhirah kuliko za dunia. Miongoni mwazo ni hizi zifuatazo:

 

Suwrah hii Ash-Shuwraa (42:36), Huwd (11:10) (11:15), At-Tawbah (9:38), Yuwnus (10:7), Ibraahiym (14:3), An-Nahl (16:107), Al-Qaswasw (28:60), Az-Zukhruf (43:35), Al-A’laa (87:16-17).

 

[10] Allaah Angetaka Angewaangamiza Washirikina Wote:

 

Tafsiyr:

 

أَمْ لَهُمْ شُرَكَاءُ شَرَعُوا لَهُم مِّنَ الدِّينِ مَا لَمْ يَأْذَن بِهِ اللَّـهُ ۚ  

“Je, wanao washirika waliowaamuru dini ambayo Allaah Hakuitolea idhini?”

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Anakhabarisha ya kwamba washirikina walijifanyia washirika, wakawa wanawapenda na kuwashirikisha katika ukafiri na matendo ya kikafiri. Hao ni katika mashaytwani wa kibinaadam wanaolingania ukafiri katika mambo ya ushirikina na bid-ah, na kuharamisha Alivyovihalalisha Allaah, na kuvihalalisha Alivyoviharamisha Allaah, na mfano wa hivyo, wakiwa wanafanya kwa mujibu wa matakwa na matamanio yao.

 

Pamoja na kwamba dini haiwi isipokuwa kwa mujibu wa Alivyoiweka Allaah, ili waja waifuate, na wajikurubishe Kwake kupitia Dini hiyo. Asili ni kumzuia kila mmoja kutoweka chochote katika yale Aliyoweka Allaah na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم). Sasa itakuwaje kwa hawa mafasiki walioshirikiana na baba zao kwenye ukafiri?!  

 

وَلَوْلَا كَلِمَةُ الْفَصْلِ لَقُضِيَ بَيْنَهُمْ ۗ وَإِنَّ الظَّالِمِينَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ﴿٢١﴾

“Na lau si neno la uamuzi, basi jambo lingelimalizwa (hapa duniani) baina yao. Na hakika madhalimu watapata adhabu iumizayo.”

 

Lau kama si kuwa na muda maalumu ambao Allaah Ameuweka ukitenganisha nyumati mbalimbali, na kwamba Atawachelewesha, (kama si kuwa hilo) wangeangamizwa katika wakati huu uliopo. Angepewa maisha mazuri anaestahiki, na angeangamizwa asiestahiki, kwa ajili zile sababu zinazopelekea kuangamizwa zipo, lakini mbele yao kuna adhabu iumizayo huko Aakhirah kwa hawa na kila aliyedhulumu. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

[11] Al-Waliyyu: (Rafiki Mlinzi, Msaidizi, Msimamizi)

 

Rejea Faharasa ya Majina Mazuri ya Allaah.

 

[12] Kujiepusha Na Machafu:

 

Baadhi ya Hadiyth zilizokataza machafu ni zifuatazo:

 

عَنْ أَبِي اَلدَّرْدَاءِ‏ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏{إِنَّ اَللَّهَ يُبْغِضُ اَلْفَاحِشَ اَلْبَذِيءَ} أَخْرَجَهُ اَلتِّرْمِذِيُّ، وَصَحَّحَهُ

وَلَهُ مِنْ حَدِيثِ اِبْنِ مَسْعُودٍ ‏رَفَعَهُ‏: {لَيْسَ اَلْمُؤْمِنُ بِالطَّعَّانِ، وَلَا اَللَّعَّانُ، وَلَا اَلْفَاحِشَ، وَلَا اَلْبَذِيءَ} وَحَسَّنَهُ، وَصَحَّحَهُ اَلْحَاكِمُ، وَرَجَّحَ اَلدَّارَقُطْنِيُّ وَقْفَهُ

Amesimulia Abuu Ad-Dardaa (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Anamchukia muovu, mwenye maneno mabaya.” [Imetolewa na At-Tirmidhiy na akaisahihisha]

 

Pia amepokea kutoka katika Hadiyth ya Ibn Mas-‘uwd marfuw’: “Muumini si mtukanaji, wala si mlaanifu, wala mchafu, wala si mwenye maneno mabaya.” [Na amesema ni Hasan na akaisahihisha Al-Haakim. Ad-Daaraqutwniy ameitilia nguvu kuwa ni Marfuw’]

 

[13] Miongoni Mwa Sifa Za Waumini Ni Kushauriana Baina Yao:

 

Miongoni mwa sifa za Waumini zimetajwa katika Aayah hii tukufu na mojawapo ni hii ya kushauriana baina yao, sifa ambayo ni jina la Suwrah hii tukufu. Tafsiyr ya Aayah ni kama ilivyoelezewa na Imaam As-Sa’diy (رحمه الله):

 

وَالَّذِينَ اسْتَجَابُوا لِرَبِّهِمْ

“Na wale waliomuitikia Rabb wao.”

 

Na wale walionyenyekea katika kumtii Allaah (سبحانه وتعالى), na wakaitikia daawah Yake, na ikawa makusudio yao ni kumridhisha Allaah na kufaulu kwa kujikurubisha Kwake.

 

Na katika kuitikia na kukubali daawah (wito) wa Allaah ni kutekeleza Swalaah tano na kutoa Zakaah, kwa sababu hiyo, ndio Allaah Akaziunganisha katika kuzitaja ibaada hizi mbili, jambo linalojulisha fadhila na sharafu zake. Akasema:

 

وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ

“Wakasimamisha Swalaah.”

 

Za kusoma kwa sauti na za sauti ya chini, za faradhi na za Sunnah.

 

  وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ﴿٣٨﴾

“Na kutokana na vile Tulivyowaruzuku wanatoa.”

 

Katika utowaji wa waajibu, mfano wa Zakaah na matumizi ya ndugu na familia, na mfano wao, na utoaji mustahab (Sunnah) kama vile kutoa swadaqah kwa watu wote (wasio ndugu).

وَأَمْرُهُمْ شُورَىٰ بَيْنَهُمْ

“Na jambo lao hushauriana baina yao.”

 

Jambo la kidini na kidunia. Hatosheki mtu na rai yake, kwenye jambo lolote lile linalotaka ushirikiano. Na hili halipatikani isipokuwa wakiwa na umoja, upendo na ukamilifu wa akili ya kwamba wanapohitajia jambo lolote lile linalohitaji kufikiria na kupeana rai, huwa wanakusanyika na kushauriana, mpaka ikibainika maslahi, wanaharakisha na kulifanyia kazi. Na jambo hilo ni kama vile rai zao katika Vita na Jihaad, kuwaweka viongozi ama kutoa hukumu, na yasiyokuwa hayo, na kama vile kufanya bah-th (utafiti) kwenye mas-ala ya kidini kiujumla wake, hivyo vyote ni katika mambo yanayohitaji kushirikiana, na kuyafanyia bahth, ili kubainisha usawa Anaoupenda Allaah. Haya yote yanaingia katika Aayah hii. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

[14] Maana Ya Baghyun/Baghaa Katika Qur-aan

 

Rejea Aayah namba (14) ya Suwrah hii Ash-Shuwraa (42) kupata maana zake mbalimbali.

 

[15] Dhulma Ni Dhulumaat (Giza Nene) Siku Ya Qiyaamah:

 

 

عَنْ اِبْنِ عُمَرَ ‏رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا‏ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ‏ صلى الله عليه وسلم ‏{اَلظُّلْمُ ظُلُمَاتٌ يَوْمَ اَلْقِيَامَةِ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

Amesimulia Ibn ‘Umar (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Dhulma ni giza nene Siku ya Qiyaamah.” [Bukhaariy, Muslim]

 

 

Dhulma, maana yake ni kuweka kitu sehemu isiyokuwa yake, au kuficha ukweli ili usitokeze. Katika Siku ya Hukmu (Qiyaamah), dhulma itaonekana na rangi yake itakuwa ni nyeusi. Hadiyth hii inatufundisha kuwa dhulma ni kitu kibaya na ni haramu ikiwa kwa mtu, katika heshima au utajiri wake.

 

019-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Dhulma Irudishwe Duniani Kabla Ya Malipo Ya Aakhirah

 

[16] Maana Ya Baghyun/Baghaa Katika Qur-aan:

 

Rejea Suwrah hii Ash-Shuwraa (42:14) kupata maana zake mbalimbali.

 

[17] Aina Tatu Za Wahy:

 

Na haipasi kwa mtu yeyote katika wanaadam Allaah (سبحانه وتعالى) Aseme naye, isipokuwa kwa njia ya Wahy ambao Allaah (سبحانه وتعالى) Anamtumia, au Aseme naye nyuma ya pazia, kama vile Allaah (سبحانه وتعالى) Alivyosema na Nabiy Muwsaa (عليه السّلام). Au Atume Mjumbe, kama Anavyomtuma Jibriyl  (عليه السّلام)  kwa yule anayetumwa kwake ampelekee Wahy wa kile Allaah (سبحانه وتعالى) Anataka apelekewe, kwa Idhini ya Rabb wake, na sio kwa mapendeleo yake. Hakika Yake Yeye Allaah (سبحانه وتعالى), Yuko juu kwa Dhati Yake, Majina Yake, Sifa Zake na Vitendo Vyake. Amekilazimisha kila kitu, na viumbe vyote vimemdhalilikia, na ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji Wake mambo ya viumbe Vyake. Katika Aayah hii, pana kuthibitisha Sifa ya kusema kwa Allaah (سبحانه وتعالى) kwa namna inayonasibiana na Haiba Yake na ukubwa wa Mamlaka Yake. [Tafsiyr Al-Muyassar]

 

[18] Maana Za Ruwh Katika Qur-aan:

 

Rejea An-Nahl (16:2).

 

[19] Nuru (Mwanga) Ni Njia Moja Tu, Viza Ni Vingi:

 

Rejea Ibraahiym (14:1-2) Kwenye maelezo bayana na faida tele kuhusu Nuru na viza, pamoja na rejea mbalimbali.   

 

 

 

Share