050 - Qaaf

 

  ق

 

050-Qaaf

 

050-Qaaf: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

ق ۚ وَالْقُرْآنِ الْمَجِيدِ﴿١﴾

1. Qaaf.[1] Naapa kwa Qur-aan Al-Majiyd: Adhimu, Karimu, yenye kheri, Baraka na ilimu tele. 

 

 

 

بَلْ عَجِبُوا أَن جَاءَهُم مُّنذِرٌ مِّنْهُمْ فَقَالَ الْكَافِرُونَ هَـٰذَا شَيْءٌ عَجِيبٌ﴿٢﴾

2. Bali wamestaajabu kwamba amewajia mwonyaji miongoni mwao, wakasema makafiri: Hili ni jambo la ajabu.

 

 

 

أَإِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا ۖ ذَٰلِكَ رَجْعٌ بَعِيدٌ﴿٣﴾

3. Je, hivi tukifa na tukawa udongo (tutafufuliwa)? Ni marejeo ya mbali hayo! [2]

 

 

 

 

قَدْ عَلِمْنَا مَا تَنقُصُ الْأَرْضُ مِنْهُمْ ۖ وَعِندَنَا كِتَابٌ حَفِيظٌ﴿٤﴾

4. Hakika Sisi Tunajua kinachopunguzwa na ardhi kutokana nao, na Tunacho Kitabu kinachohifadhi barabara.

 

 

 

 

بَلْ كَذَّبُوا بِالْحَقِّ لَمَّا جَاءَهُمْ فَهُمْ فِي أَمْرٍ مَّرِيجٍ﴿٥﴾

5. Bali wamekadhibisha haki ilipowajia, basi wao wamo katika jambo la mkorogeko.

 

 

 

 

أَفَلَمْ يَنظُرُوا إِلَى السَّمَاءِ فَوْقَهُمْ كَيْفَ بَنَيْنَاهَا وَزَيَّنَّاهَا وَمَا لَهَا مِن فُرُوجٍ﴿٦﴾

6. Je, hawatazami mbingu juu yao, vipi Tumezijenga na Tumezipamba, na wala hazina mipasuko yoyote!  

 

 

 

 

وَالْأَرْضَ مَدَدْنَاهَا وَأَلْقَيْنَا فِيهَا رَوَاسِيَ وَأَنبَتْنَا فِيهَا مِن كُلِّ زَوْجٍ بَهِيجٍ﴿٧﴾

7. Na ardhi Tumeikunjua na Tukaitupia humo milima thabiti, na Tukaotesha humo kila aina ya mimea ya kupendeza.

 

 

 

 

تَبْصِرَةً وَذِكْرَىٰ لِكُلِّ عَبْدٍ مُّنِيبٍ﴿٨﴾

8. Ni ufumbuzi macho na ukumbusho kwa kila mja mwenye kuelekea kwa Allaah (kwa khofu na matarajio).

 

 

 

وَنَزَّلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً مُّبَارَكًا فَأَنبَتْنَا بِهِ جَنَّاتٍ وَحَبَّ الْحَصِيدِ﴿٩﴾

9. Na Tukateremsha kutoka mbinguni maji yaliyobarikiwa, kisha Tukaotesha kwayo mabustani na nafaka za kuvunwa.

 

 

 

 

وَالنَّخْلَ بَاسِقَاتٍ لَّهَا طَلْعٌ نَّضِيدٌ﴿١٠﴾

10. Na mitende mirefu yenye mashada ya matunda yenye kupangika tabaka tabaka.

 

 

 

رِّزْقًا لِّلْعِبَادِ ۖ وَأَحْيَيْنَا بِهِ بَلْدَةً مَّيْتًا ۚ كَذَٰلِكَ الْخُرُوجُ﴿١١﴾

11. Ni riziki kwa waja. Na Tukahuisha kwayo nchi iliyokufa, hivyo ndivyo kufufuliwa.

 

 

 

 

كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍ وَأَصْحَابُ الرَّسِّ وَثَمُودُ﴿١٢﴾

12. Wamekadhibisha kabla yao (Maquraysh) kaumu ya Nuwh na watu wa Ar-Rass[3] na kina Thamuwd.

 

 

 

 

وَعَادٌ وَفِرْعَوْنُ وَإِخْوَانُ لُوطٍ﴿١٣﴾

13. Na kina ‘Aad na Firawni na ndugu wa Luutw.

 

 

 

 

وَأَصْحَابُ الْأَيْكَةِ وَقَوْمُ تُبَّعٍ ۚ كُلٌّ كَذَّبَ الرُّسُلَ فَحَقَّ وَعِيدِ﴿١٤﴾

14. Na wakaazi wa Al-Aykah[4] na kaumu ya Tubba’[5], wote walikadhibisha Rusuli. Basi likathibiti Onyo Langu.

 

 

 

 

أَفَعَيِينَا بِالْخَلْقِ الْأَوَّلِ ۚ بَلْ هُمْ فِي لَبْسٍ مِّنْ خَلْقٍ جَدِيدٍ﴿١٥﴾

15. Je, kwani Tulichoka kwa uumbaji wa kwanza? Bali wao wamo katika kuchanganyikiwa akili na uumbaji upya (kufufuliwa).

 

 

 

 

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ وَنَعْلَمُ مَا تُوَسْوِسُ بِهِ نَفْسُهُ ۖ وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ﴿١٦﴾

16. Na kwa yakini Tumemuumba binaadam na Tunajua yale inayowaza nafsi yake[6] na Sisi[7] Tuko karibu naye kuliko mshipa wa koo.

 

 

 

إِذْ يَتَلَقَّى الْمُتَلَقِّيَانِ عَنِ الْيَمِينِ وَعَنِ الشِّمَالِ قَعِيدٌ﴿١٧﴾

17. Pale wanapopokea wapokeaji wawili (Malaika) wanaokaa kuliani na kushotoni. 

 

 

 

مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ﴿١٨﴾

18. Hatamki kauli yeyote isipokuwa anaye mchungaji aliyejitayarisha (kurekodi).[8]

 

 

 

 

وَجَاءَتْ سَكْرَةُ الْمَوْتِ بِالْحَقِّ ۖ ذَٰلِكَ مَا كُنتَ مِنْهُ تَحِيدُ﴿١٩﴾

19. Na Sakaaratul-mawt[9] itakapomjia kwa haki. (Itasemwa): Hayo ndiyo yale uliyokuwa ukiyakimbilia mbali.

 

 

 

وَنُفِخَ فِي الصُّورِ ۚ ذَٰلِكَ يَوْمُ الْوَعِيدِ﴿٢٠﴾

20. Na baragumu[10] litapulizwa.  Hiyo ndio Siku ya makamio.

 

 

 

 

وَجَاءَتْ كُلُّ نَفْسٍ مَّعَهَا سَائِقٌ وَشَهِيدٌ﴿٢١﴾

21. Na kila nafsi itakuja pamoja nayo mwendeshaji na shahidi.[11]

 

 

 

 

لَّقَدْ كُنتَ فِي غَفْلَةٍ مِّنْ هَـٰذَا فَكَشَفْنَا عَنكَ غِطَاءَكَ فَبَصَرُكَ الْيَوْمَ حَدِيدٌ﴿٢٢﴾

22. (Aambiwe): Kwa yakini ulikuwa katika mghafala na haya! Basi Tumekuondoshea kifuniko chako, basi kuona kwako leo ni kukali.[12]

 

 

 

 

وَقَالَ قَرِينُهُ هَـٰذَا مَا لَدَيَّ عَتِيدٌ﴿٢٣﴾

23. Na Malaika wake aliyepewa jukumu atasema: Hii (rekodi) iliyoko kwangu imeshatayarishwa.

 

 

 

 

أَلْقِيَا فِي جَهَنَّمَ كُلَّ كَفَّارٍ عَنِيدٍ﴿٢٤﴾

24. (Allaah Atasema): Mtupeni katika Jahannam kila kafiri mno, mkaidi!

 

 

 

 

مَّنَّاعٍ لِّلْخَيْرِ مُعْتَدٍ مُّرِيبٍ﴿٢٥﴾

25. Mzuiaji wa kheri, mwenye kutaadi, mtiaji shaka.

 

 

 

 

الَّذِي جَعَلَ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ فَأَلْقِيَاهُ فِي الْعَذَابِ الشَّدِيدِ﴿٢٦﴾

26. Ambaye amefanya mwabudiwa mwengine pamoja na Allaah, basi mtupeni katika adhabu shadidi.

 

 

 

 

قَالَ قَرِينُهُ رَبَّنَا مَا أَطْغَيْتُهُ وَلَـٰكِن كَانَ فِي ضَلَالٍ بَعِيدٍ﴿٢٧﴾

27. Shaytwaan mwenzake atasema: Rabb wetu! Sikumvukisha mipaka kuasi lakini alikuwa (mwenyewe) katika upotofu wa mbali.[13]

 

 

 

 

قَالَ لَا تَخْتَصِمُوا لَدَيَّ وَقَدْ قَدَّمْتُ إِلَيْكُم بِالْوَعِيدِ﴿٢٨﴾

28. (Allaah) Atasema: Msibishane Kwangu, na hali Nilishakukadimishieni Onyo Langu!

 

 

 

 

مَا يُبَدَّلُ الْقَوْلُ لَدَيَّ وَمَا أَنَا بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ﴿٢٩﴾

29. Haibadilishwi kauli Kwangu, Nami Si Mwenye Kudhulumu katu waja.

 

 

 

 

يَوْمَ نَقُولُ لِجَهَنَّمَ هَلِ امْتَلَأْتِ وَتَقُولُ هَلْ مِن مَّزِيدٍ﴿٣٠﴾

30. Siku Tutakapoiambia Jahannam: Je, umeshajaa? Nayo itasema: Je, kuna ziada yoyote?[14]

 

 

 

 

وَأُزْلِفَتِ الْجَنَّةُ لِلْمُتَّقِينَ غَيْرَ بَعِيدٍ﴿٣١﴾

31. Na italetwa karibu Jannah kwa wenye taqwa isiwe mbali.

 

 

 

 

هَـٰذَا مَا تُوعَدُونَ لِكُلِّ أَوَّابٍ حَفِيظٍ﴿٣٢﴾

32. (Itasemwa): Haya ndiyo yale mliyoahidiwa kwa kila mwenye kurejea kwa Allaah kwa yote, mwenye kuhifadhi vyema (Amri za Allaah سبحانه وتعالى).

 

 

 

 

مَّنْ خَشِيَ الرَّحْمَـٰنَ بِالْغَيْبِ وَجَاءَ بِقَلْبٍ مُّنِيبٍ﴿٣٣﴾

33. Ambaye anamwogopa Ar-Rahmaan akiwa mbali na macho ya watu na akaja na moyo safi mwelekevu.

 

 

 

 

ادْخُلُوهَا بِسَلَامٍ ۖ ذَٰلِكَ يَوْمُ الْخُلُودِ﴿٣٤﴾

34. Iingieni (Jannah) kwa salama. Hiyo ndio siku yenye kudumu.

 

 

 

 

لَهُم مَّا يَشَاءُونَ فِيهَا وَلَدَيْنَا مَزِيدٌ﴿٣٥﴾

35. Watapata humo wayatakayo, na Kwetu kuna ziada (kumuona Allaah عز وجل).[15]

 

 

 

 

وَكَمْ أَهْلَكْنَا قَبْلَهُم مِّن قَرْنٍ هُمْ أَشَدُّ مِنْهُم بَطْشًا فَنَقَّبُوا فِي الْبِلَادِ هَلْ مِن مَّحِيصٍ﴿٣٦﴾

36. Na karne ngapi Tumeziangamiza kabla yao ambao walikuwa wenye nguvu zaidi kuliko wao! Basi walitangatanga sana kwa vishindo katika nchi. Je, walipata mahali popote pa kukimbilia?

 

 

 

 

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَذِكْرَىٰ لِمَن كَانَ لَهُ قَلْبٌ أَوْ أَلْقَى السَّمْعَ وَهُوَ شَهِيدٌ﴿٣٧﴾

37. Hakika katika hayo, bila shaka pana ukumbusho kwa aliye na moyo (wa uzingativu), au akatega sikio kwa makini, naye yu hadhiri kwa moyo wake.

 

 

 

 

وَلَقَدْ خَلَقْنَا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ وَمَا مَسَّنَا مِن لُّغُوبٍ﴿٣٨﴾

38. Na kwa yakini Tumeumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake katika siku sita, na wala Haukutugusa uchovu wowote.

 

 

 

 

فَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ الْغُرُوبِ﴿٣٩﴾

39. Basi subiri juu ya yale wanayoyasema, na Sabbih ukimhimidi Rabb wako kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa.

 

 

 

 

وَمِنَ اللَّيْلِ فَسَبِّحْهُ وَأَدْبَارَ السُّجُودِ﴿٤٠﴾

40.  Na katika usiku Msabbih, na baada ya kila Swalaah.[16]

 

 

 

 

وَاسْتَمِعْ يَوْمَ يُنَادِ الْمُنَادِ مِن مَّكَانٍ قَرِيبٍ﴿٤١﴾

41. Na sikiliza kwa makini Siku atakayonadi mwenye kunadi kutoka mahali pa karibu.

 

 

 

 

يَوْمَ يَسْمَعُونَ الصَّيْحَةَ بِالْحَقِّ ۚ ذَٰلِكَ يَوْمُ الْخُرُوجِ﴿٤٢﴾

42. Siku watakayosikia ukelele kwa haki.[17] Hiyo ndio Siku ya kutoka (makaburini).

 

 

 

 

إِنَّا نَحْنُ نُحْيِي وَنُمِيتُ وَإِلَيْنَا الْمَصِيرُ﴿٤٣﴾

43. Hakika Sisi Tunahuisha na Tunafisha, na Kwetu ndio mahali pa kuishia.

 

 

 

 

يَوْمَ تَشَقَّقُ الْأَرْضُ عَنْهُمْ سِرَاعًا ۚ ذَٰلِكَ حَشْرٌ عَلَيْنَا يَسِيرٌ﴿٤٤﴾

44. Siku itakayowapasukia ardhi[18] (watoke) haraka haraka. Huo ndio mkusanyo, Kwetu ni mwepesi mno.

 

 

 

 

نَّحْنُ أَعْلَمُ بِمَا يَقُولُونَ ۖ وَمَا أَنتَ عَلَيْهِم بِجَبَّارٍ ۖ فَذَكِّرْ بِالْقُرْآنِ مَن يَخَافُ وَعِيدِ﴿٤٥﴾

45. Sisi Tunajua zaidi yale wanayoyasema, na wala wewe si mwenye kuwalazimisha kwa ujabari. Basi mkumbushe kwa Qur-aan anayekhofu Onyo Langu.

 

 

 

[1] الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah):

 

Hizi ni herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Tanbihi ya Al-Baqarah (2:1).

 

[2] Washirikina Hawakuamini Kuwa Watafufuliwa: 

 

Rejea Al-Israa (17: 49) kwenye maelezo bayana na rejea mbalimbali.

 

[3] Watu Wa Ar-Rass: 

 

Ar-Rass ni kisima [Tafsiyr Ibn Kathiyr]. Rejea Al-Furqaan (25:38) kwenye maelezo kuhusu watu wa Ar-Rass.

 

[4] Watu Wa Al-Aykah

 

Watu wa Aykah ni watu wa kichakani katika mji wa Madyan. Ni watu wa Nabiy Shu’ayb (عليه السّلام). Rejea Ash-Shu’araa (26:176) kupata maelezo bayana. 

 

[5] Kaumu Ya Tubba’ Na Nani Tubba’:

 

Rejea Ad-Dukhaan (44:37).

 

[6] Mwanaadam Hahesabiwi Na Allaah Yale Anayoyawaza Nafsini Mwake Madamu Hakuyaongelea Au Kuyatenda:

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Anakhabarisha Uwezo Wake juu ya mwanaadam, kwani Yeye Ndiye Aliyemuumba, hivyo basi amali zake Anazijua vyema hadi kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Anajua yale yanayomnong’oneza nafsini mwake binaadam, yawe ya kheri au ya shari. Na imethibiti katika Swahiyh Hadiyth ifuatayo:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ، يَرْفَعُهُ قَالَ ‏ "‏ إِنَّ اللَّهَ تَجَاوَزَ لأُمَّتِي عَمَّا وَسْوَسَتْ أَوْ حَدَّثَتْ بِهِ أَنْفُسَهَا، مَا لَمْ تَعْمَلْ بِهِ أَوْ تَكَلَّمْ ‏"‏‏.‏

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Hakika Allaah Amesamehe Ummah wangu (zile amali mbaya) ambazo nafsi zao huwanong’oneza au kupendekeza maadamu hawatatenda au kuzungumza.” [Tafsiyr Ibn Kathiyr, Hadiyth Ameipokea Imaam Al-Bukhaariy: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri (83) – Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

 

[7]  “Sisi” Imekusudiwa Ni Malaika:

 

 Yaani: Malaika wa Allaah (سبحانه وتعالى) wako karibu na binaadam kuliko mshipa wa koo wake.

 

Wale walioawilisha “Na Sisi” kukusudia kuwa ni “Ujuzi Wetu”, wamefanya hivyo ili kuepusha kuingia katika fikra ya “Huluwl” ambayo ina maana ya kuchanganyika Allaah na viumbe Vyake lakini Allaah Akabaki kama Alivyo na kiumbe Chake kikabaki kama kilivyo bila mabadiliko yoyote, au “Iltihaad” ambayo ina maana ya kuchanganyika Allaah (سبحانه وتعالى) na Viumbe Vyake na kuwa kitu kimoja kisichoweza kutenganika.  Lakini itikadi hii imekanushwa na ‘Ulamaa wote kwa sauti moja. Allaah Ametakasika, na Ametukuka, na Yuko mbali na yale wanayompachika. Neno “Sisi” halifai kuawiliwa kwa maana ya Ujuzi wa Allaah, kwani Allaah Hakusema: “Na Mimi Niko karibu zaidi naye kuliko mshipa wake wa koo.”

 

Bali Anasema:

وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ﴿١٦﴾

 

Na Sisi Tuko karibu naye kuliko mshipa wa koo.

 

Kama Anavyosema katika hali ya sakaraatul-mawt ya binaadam pindi Malaika Wake wanapotoa roho za wanaadam:

 

وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنكُمْ وَلَـٰكِن لَّا تُبْصِرُونَ ﴿٨٥﴾

Nasi Tuko karibu naye zaidi kuliko nyinyi, lakini hamuoni. [Al-Waaqi’ah (56:85)]

 

 

(Nasi) yaani: Malaika

 

Na vivyo hivyo Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:

 

إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ ﴿٩﴾

“Hakika Sisi Tumeteremsha Adh-Dhikra (Qur-aan) na hakika Sisi bila shaka Ndio Wenye Kuihifadhi.” [Al-Hijr (15:9)]

 

Kwa hiyo Malaika wameteremsha Wahyi, yaani Qur-aan, kwa Idhini ya Allaah (عزّ وجلّ), na vivyo hivyo Malaika wako karibu zaidi na binaadam kuliko mshipa wake wa koo baada ya kuwezeshwa kuwa hivyo na Allaah.  Hivyo basi, Malaika na shaytwaan wananamjua vyema binaadam na wako karibu naye zaidi. Ni kama vile alivyotuambia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ambaye ni swaadiq al-maswduwq (mkweli mwenye kusadikiwa

 

إِنَّ الشَّيْطَانَ يَجْرِي مِنِ ابْنِ آدَمَ مَجْرَى الدَّمِ

“Hakika shaytwaan hutembea katika mwili wa binaadam kama damu inavyotembea katika mishipa.” [Tafsiyr Ibn Kathiyr – Hadiyth katika Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo]

 

[8] Kuchunga Ulimi:

 

Muislamu anapaswa kuwa na kauli njema tu, na anapaswa kuchunga ulimi wake kwa kutokusema neno lolote lile baya, kwa sababu kama Anavosema Allaah (سبحانه وتعالى) katika Aayah hii tukufu kwamba Malaika wanaandika kila neno linalotamkwa, liwe la kheri au shari, hata liwe dogo vipi. Na kuchunga ulimi kumeonywa katika Kauli kadhaa za Allaah (سبحانه وتعالى) ndani ya Qur-aan. Hali kadhaalika, Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ameonya katika Hadiyth mbalimbali, kama katika Hadiyth hii ifuatayo ambayo inatahadharisha jinsi gani neno moja linaweza kusababisha Radhi za Allaah (سبحانه وتعالى) au Hasira Zake:

 

 عن أَبي هريرة رضي اللهُ عنه ، عن النبيّ صلى الله عليه وسلم قَالَ : (( إنَّ العَبْدَ لَيَتَكَلَّمُ بِالكَلِمَةِ مِنْ رِضْوَانِ الله تَعَالَى مَا يُلْقِي لَهَا بَالاً يَرْفَعُهُ اللهُ بِهَا دَرَجاتٍ ، وإنَّ العَبْدَ لَيَتَكَلَّمُ بِالكَلَمَةِ مِنْ سَخَطِ اللهِ تَعَالَى لا يُلْقِي لَهَا بَالاً يَهْوِي بِهَا في جَهَنَّمَ )) . رواه البخاري .

 

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: "Hakika mja huzungumza maneno yenye kumridhisha Allaah (سبحانه وتعالى) bila kuyapa umuhimu wowote, na Allaah Akamnyanyulia kwayo daraja nyingi Na hakika mja huzungumza maneno yenye kumkasirisha Allaah (سبحانه وتعالى) bila kuyapa umuhimu wowote, yakaja kumporomosha ndani ya Jahannam.” [Al-Bukhaariy]

 

Bonyeza viungo vifuatavyo kwenye Makala mbalimbali zenye funzo hili muhimu kabisa:

 

001-Riyaadhw Asw-Swaalihiyn: Mlango Wa Kuharamishwa Kusengenya na Amri ya Kuhifadhi Ulimi

 

44-Riyaadhw Asw-Swaalihiyn: Mlango Wa Amri kwa Mfungaji Kuhifadhi Ulimi Wake na Viungo Vyake kwa Kwenda Kinyume na Matusi na Mfano Wake

 

02-Madhara Ya Ghiybah: Kutunza Ulimi

 

037-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Mwenye Iymaan Kweli Amkirimu Mgeni, Na Aseme Ya Kheri Au Anyamaze

 

086-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Atakayedhamini Ulimi Na Utupu Atadhaminiwa Jannah

 

094-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kuweka Amani Baina Ya Watu Kwa Ulimi Na Kuacha Yaliyoharamishwa

 

 

[9] Sakaraatul-Mawt: Mateso Makali Ya Mauti:

 

Sakaraatul-Mawti ni mateso anayoyapata mtu anayetolewa roho hadi kwamba hulevywa akili kutokana na uzito wa mateso hayo.

 

Na hakuna wa kuepukana nayo kwani hata Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipokaribia kufariki alihisi sakaraatul-mawti kwa dalili ya Hadiyth hii ifuatayo:

 

حَدَّثَنِي مُحَمَّدُ بْنُ عُبَيْدٍ، حَدَّثَنَا عِيسَى بْنُ يُونُسَ، عَنْ عُمَرَ بْنِ سَعِيدٍ، قَالَ أَخْبَرَنِي ابْنُ أَبِي مُلَيْكَةَ، أَنَّ أَبَا عَمْرٍو، ذَكْوَانَ مَوْلَى عَائِشَةَ أَخْبَرَهُ أَنَّ عَائِشَةَ كَانَتْ تَقُولُ إِنَّ مِنْ نِعَمِ اللَّهِ عَلَىَّ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم تُوُفِّيَ فِي بَيْتِي وَفِي يَوْمِي، وَبَيْنَ سَحْرِي وَنَحْرِي، وَأَنَّ اللَّهَ جَمَعَ بَيْنَ رِيقِي وَرِيقِهِ عِنْدَ مَوْتِهِ، دَخَلَ عَلَىَّ عَبْدُ الرَّحْمَنِ وَبِيَدِهِ السِّوَاكُ وَأَنَا مُسْنِدَةٌ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم فَرَأَيْتُهُ يَنْظُرُ إِلَيْهِ، وَعَرَفْتُ أَنَّهُ يُحِبُّ السِّوَاكَ فَقُلْتُ آخُذُهُ لَكَ فَأَشَارَ بِرَأْسِهِ أَنْ نَعَمْ، فَتَنَاوَلْتُهُ فَاشْتَدَّ عَلَيْهِ وَقُلْتُ أُلَيِّنُهُ لَكَ فَأَشَارَ بِرَأْسِهِ أَنْ نَعَمْ، فَلَيَّنْتُهُ، وَبَيْنَ يَدَيْهِ رَكْوَةٌ ـ أَوْ عُلْبَةٌ يَشُكُّ عُمَرُ ـ فِيهَا مَاءٌ، فَجَعَلَ يُدْخِلُ يَدَيْهِ فِي الْمَاءِ فَيَمْسَحُ بِهِمَا وَجْهَهُ يَقُولُ ‏"‏ لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ، إِنَّ لِلْمَوْتِ سَكَرَاتٍ ‏"‏‏.‏ ثُمَّ نَصَبَ يَدَهُ فَجَعَلَ يَقُولُ ‏"‏ فِي الرَّفِيقِ الأَعْلَى ‏"‏‏.‏ حَتَّى قُبِضَ وَمَالَتْ يَدُهُ‏.‏

 

Amesimulia ‘Aaishah (رضي الله عنها): Hakika katika Neema za Allaah juu yangu ni kuwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alifariki nyumbani kwangu katika siku ya zamu yangu wakati akiegemea kifuani kwangu, na Allaah Akajaalia mate yangu yachanganyike na mate yake katika kifo chake. ‘Abdur-Rahmaan akaingia kwangu akiwa na siwaak (mswaki wa Sunnah) mkononi mwake na nikawa nauegemeza (mgongo wa) Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) (dhidi ya kifua changu). Nikamwona Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akiangalia (siwaak) na nilijua kuwa alipenda siwaak nikamwambia: Je, nikuchukulie? Akabetua kichwa kwa kuafiki. Nikachukua na ulikuwa mgumu kwake kuutumia, nikamuuliza: Je, nikulainishie? Akabetua kichwa kukubali. Nikaulainisha na kusafishia meno yake. Mbele yake kulikuwa na gudulia au kopo. Msimuliaji ‘Umar, hana uhakika kama lilikuwa na maji ama laa. Akawa anatumbukiza mkono wake katika maji na kupangusa uso wake kwa maji hayo, akasema:

   لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ، إِنَّ لِلْمَوْتِ سَكَرَاتٍ

“La ilaaha illa-Allaah (Hapana mwabudiwa wa haki ila Allaah)

 

Hakika mauti yana mateso yake.”   Akainua mkono wake (juu) na kuanza kusema: “Kwa Sahibu wa Juu.” Mpaka akafariki, mkono wake ukashuka chini.  [Al-Bukhaariy, Kitaab Al-Maghaaziy (64), Kitabu cha Ar-Riqaaq (81)]

 

Rejea pia Al-Waaqi’ah (56:83) kwenye faida kadhaa na rejea zake.

 

[10] Baragumu Litakapopigwa Siku Ya Qiyaamah:

 

Rejea Az-Zumar (39:68) kwenye maelezo bayana na rejea zake.

 

[11] Mwendeshaji Na Shahidi:

 

Mwendeshaji ni Malaika na shahidi ni amali zake za kheri na shari. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

Na ije kila nafsi, wakiwa pamoja nayo Malaika wawili: mmoja anaiongoza kwenye mkusanyiko, na mwingine anaitolea ushahidi wa liyoyafanya duniani, ya kheri na shari. [Tafsiyr Al-Muyassar]

 

[12] Watu Na Hasa Makafiri Wataona Vizuri Yanayowasubiri Mbele Yao Siku Ya Qiyaamah:

 

 Tafsiyr ya Imaam As-Sa’diy (رحمه الله):

 

لَّقَدْ كُنتَ فِي غَفْلَةٍ مِّنْ هَـٰذَا

“(Aambiwe): Kwa yakini ulikuwa katika mghafala na haya!”

 

Yaani: Siku ya Qiyaamah, mkengeukaji na mkadhibishaji, anaambiwa Siku ya Qiyaamah maneno haya ya kulaumiwa na kukaripiwa: Ulikuwa mkadhibishaji wa haya na ukaacha kuyatendea kazi basi sasa:

فَكَشَفْنَا عَنكَ غِطَاءَكَ

“Tumekuondoshea kifuniko chako.”

 

Kilichofunika moyo wako, ukazidi usingizi wako wa ghafla, na ukaendelea ukengeukaji wako,

 

  فَبَصَرُكَ الْيَوْمَ حَدِيدٌ﴿٢٢﴾

“Basi kuona kwako leo ni kukali.”

 

Atayaona yale yatakayomkirihisha, kumtisha na kumtia khofu, ya aina za adhabu na mateso. 

 

Maelezo haya ya Allaah huenda ikawa anaambiwa mja, kwani duniani alikuwa katika ghafla kutambua sababu ya kuumbwa kwake, lakini Siku ya Qiyaamah ataamka kutoka usingizi wa ghafla, lakini katika wakati ambao hatoweza kujirudi au kufidia wakati alioupoteza.

 

Na yote haya ni matanabahisho na matahadharisho ya Allaah kwa Waja Wake. Anawaonya kwa kuwakhabarisha yatakayowasibu wakadhibishaji Siku hiyo Adhimu. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

Tafsiyr Al-Muyassar:

 

Kwa hakika wewe ulikuwa katika mghafala kuhusu tukio hili unaloliona leo, ewe binaadam! Ndipo Tukakifunua kifuniko chako kilichoziba moyo wako, kughafilika kukakuondokea. Basi leo macho yako, katika unachokishuhudia, ni makali. [Tafsiyr Al-Muyassar]

 

[13] Shaytwaan Atamgeukia Mwanaadam Na Kukanusha Upotoshaji Wake Siku Ya Qiyaamah:

 

Rejea Suwrah Ibraahiym (14:22) kwenye maelezo na rejea mbalimbali.

 

[14] Jahannam Itaomba Wakazi Wake Wa Motoni Wazidi Kuongezwa Kuingizwa Humo:

 

Aayah kadhaa katika Qur-aan zimethibitisha kwamba moto wa Jahannam utajazwa kwa wanaadam na mashaytwaan. Miongoni mwazo ni: Al-A’raaf (7:38), (7:179),  As-Sajdah (32:13). Na katika Hadiyth, ni hii ifuatayo:

 

  عَنْ أَنَسِ بْنِ مَالِكٍ، قَالَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم ‏ "‏ لاَ تَزَالُ جَهَنَّمُ تَقُولُ هَلْ مِنْ مَزِيدٍ حَتَّى يَضَعَ رَبُّ الْعِزَّةِ فِيهَا قَدَمَهُ فَتَقُولُ قَطْ قَطْ وَعِزَّتِكَ‏.‏ وَيُزْوَى بَعْضُهَا إِلَى بَعْضٍ ‏"‏‏.‏ رَوَاهُ شُعْبَةُ عَنْ قَتَادَةَ‏.‏

 

Amesimulia Anas Bin Maalik (رضي الله عنه):  Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: Moto wa Jahannam utaendelea kusema: Je kuna ziyada yoyote (ya viumbe kuingizwa humu)?  Mpaka Allaah (عزّ وجلّ) Atakapoweka Mguu Wake juu yake, hapo (Jahannam) itasema: Imetosha, imetosha (nimeshajaa) kwa Utukufu Wako! Na pande zake zote zitakusanywa pamoja.” [Al-Bukhaariy Kitaab Al-Aymaan Wan-Nudhur (83), Kitaab At-Tafsiyr (65)]

 

 

[15] ‘Aqiydah Ya Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa’ah Kwamba Waumini Watamuona Allaah (عزّ وجلّ) Peponi.

 

Rejea Yuwnus (10:26).

 

[16] Kumsabbih Allaah (سبحانه وتعالى) Baada Ya Kila Swalaah:

 

Imaam Ibn Kathiyr (رحمه الله) amenukuu: Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) amesema kuhusu Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَأَدْبَارَ السُّجُودِ﴿٤٠﴾

“Na baada ya kila Swalaah.”

 

Yaani: Ni tasbiyh za kila baada ya Swalaah. Na hii imethibitishwa na Hadiyth katika Swahiyh mbili:

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ ـ رضى الله عنه ـ قَالَ جَاءَ الْفُقَرَاءُ إِلَى النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم فَقَالُوا ذَهَبَ أَهْلُ الدُّثُورِ مِنَ الأَمْوَالِ بِالدَّرَجَاتِ الْعُلاَ وَالنَّعِيمِ الْمُقِيمِ، يُصَلُّونَ كَمَا نُصَلِّي، وَيَصُومُونَ كَمَا نَصُومُ، وَلَهُمْ فَضْلٌ مِنْ أَمْوَالٍ يَحُجُّونَ بِهَا، وَيَعْتَمِرُونَ، وَيُجَاهِدُونَ، وَيَتَصَدَّقُونَ قَالَ ‏"‏ أَلاَ أُحَدِّثُكُمْ بِأَمْرٍ إِنْ أَخَذْتُمْ بِهِ أَدْرَكْتُمْ مَنْ سَبَقَكُمْ وَلَمْ يُدْرِكْكُمْ أَحَدٌ بَعْدَكُمْ، وَكُنْتُمْ خَيْرَ مَنْ أَنْتُمْ بَيْنَ ظَهْرَانَيْهِ، إِلاَّ مَنْ عَمِلَ مِثْلَهُ تُسَبِّحُونَ وَتَحْمَدُونَ، وَتُكَبِّرُونَ خَلْفَ كُلِّ صَلاَةٍ ثَلاَثًا وَثَلاَثِينَ ‏"‏‏.‏ فَاخْتَلَفْنَا بَيْنَنَا فَقَالَ بَعْضُنَا نُسَبِّحُ ثَلاَثًا وَثَلاَثِينَ، وَنَحْمَدُ ثَلاَثًا وَثَلاَثِينَ، وَنُكَبِّرُ أَرْبَعًا وَثَلاَثِينَ‏.‏ فَرَجَعْتُ إِلَيْهِ فَقَالَ ‏"‏ تَقُولُ سُبْحَانَ اللَّهِ، وَالْحَمْدُ لِلَّهِ، وَاللَّهُ أَكْبَرُ، حَتَّى يَكُونَ مِنْهُنَّ كُلِّهِنَّ ثَلاَثًا وَثَلاَثِينَ ‏"‏‏.‏

Amesimulia Abu Hurayrah (رضي الله عنه): Baadhi ya watu masikini walikuja kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) wakasema: Matajiri watapata madaraja ya juu na watakuwa na starehe za kudumu, na wao wanaswali kama sisi na wanafunga (Swiyaam) kama sisi, wana fedha zaidi ambazo wanazitumia kuhiji na Umrah, na kupigana katika njia ya Allaah na kutoa swadaqah. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Je, nikuelezeeni jambo ambalo mkilifanya mtawafikia wale walio wazidi, na hakuna atakayewashinda, na mtakuwa bora kuliko watu wanaoishi nao isipokuwa wale watakaofanya kama nyie.  Tamkeni

 

سُبْحان الله

Subhaana Allaah

الْحمد لله

AlhamduliLlaah

الله اَكْبَر

Allaahu Akbar

 

mara thelathini na tatu (kila mmoja pekee) baada ya kila Swalaah ya faradhi.” Tukatofautiana na baadhi yetu wakasema:

 

سُبْحان الله

Subhaana Allaah (mara thelathini na tatu)

الْحمد لله

AlhamduliLlaah (mara thelathini na tatu) 

الله اَكْبَر

Allaahu Akbar (mara thelathini na nne).

 

Nikaenda kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Sema:

 

سُبْحَانَ اللَّهِ، وَالْحَمْدُ لِلَّهِ، وَاللَّهُ أَكْبَرُ

Subhaana Allaah, AlhamduliLlaah, Allaahu Akbar

 

Hata zote ziwe mara thelathini na tatu.”  [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

[17] Baragumu Litakalopulizwa Na Malaika Israafiyl:

 

Rejea Az-Zumar (39:68) kwenye maelezo na rejea zake.

 

[18] Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Ni Wa Kwanza Ambaye Ardhi Itampasukia Atoke Kaburini:

 

 

حَدَّثَنَا مُوسَى بْنُ إِسْمَاعِيلَ، حَدَّثَنَا وُهَيْبٌ، حَدَّثَنَا عَمْرُو بْنُ يَحْيَى، عَنْ أَبِيهِ، عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ ـ رضى الله عنه ـ قَالَ بَيْنَمَا رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم جَالِسٌ جَاءَ يَهُودِيٌّ، فَقَالَ يَا أَبَا الْقَاسِمِ ضَرَبَ وَجْهِي رَجُلٌ مِنْ أَصْحَابِكَ‏.‏ فَقَالَ ‏"‏ مَنْ ‏"‏‏.‏ قَالَ رَجُلٌ مِنَ الأَنْصَارِ‏.‏ قَالَ ‏"‏ ادْعُوهُ ‏"‏‏.‏ فَقَالَ ‏"‏ أَضَرَبْتَهُ ‏"‏‏.‏ قَالَ سَمِعْتُهُ بِالسُّوقِ يَحْلِفُ وَالَّذِي اصْطَفَى مُوسَى عَلَى الْبَشَرِ‏.‏ قُلْتُ أَىْ خَبِيثُ، عَلَى مُحَمَّدٍ صلى الله عليه وسلم فَأَخَذَتْنِي غَضْبَةٌ ضَرَبْتُ وَجْهَهُ‏.‏ فَقَالَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم ‏"‏ لاَ تُخَيِّرُوا بَيْنَ الأَنْبِيَاءِ، فَإِنَّ النَّاسَ يَصْعَقُونَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ، فَأَكُونُ أَوَّلَ مَنْ تَنْشَقُّ عَنْهُ الأَرْضُ، فَإِذَا أَنَا بِمُوسَى آخِذٌ بِقَائِمَةٍ مِنْ قَوَائِمِ الْعَرْشِ، فَلاَ أَدْرِي أَكَانَ فِيمَنْ صَعِقَ، أَمْ حُوسِبَ بِصَعْقَةِ الأُولَى ‏"‏‏.

 

Amesimulia Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alipokuwa amekaa, alitokea Myahudi akasema: Ee Abul-Qaasim! Mmoja katika watu wako amenipiga usoni. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akamuuliza: “Ni nani?” Yule Myahudi akasema: Mtu katika Answaar. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Mwite.” (Pindi mtu yule katika Answaar alipofika) Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuuliza, “Je, ulimpiga?” Yule bwana katika Answaar akasema: Nimemsikia sokoni anakula yamini akisema: Naapa kwa Yule Aliyemteua Muwsaa juu ya viumbe!  Nikasema: Ee khabithi! Je, Allaah Amemfadhilisha Muwsaa kuliko Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم)? Nikaghadhibika nikampiga usoni. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Msifadhilishe baina ya Manabii.   Hakika watu Siku ya Qiyaamah watazimia, nami nitakuwa wa kwanza ambaye ardhi itanipasukia.    Nitamkuta Muwsaa ameshika nguzo miongoni mwa nguzo za ‘Arsh. Sijui kama alikuwa miongoni mwa waliozimia au hakuzimia katika zimio la kwanza.” [Al-Bukhaariy Kitaab Al-Khuswuwmaat (44)]

 

 

 

Share