055 - Ar-Rahmaan

 

 

  الرَّحْمن

 

 

055-Ar-Rahmaan

 

055-Ar-Rahmaan: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

الرَّحْمَـٰنُ ﴿١﴾

1. Ar-Rahmaan.

 

 

 

 

عَلَّمَ الْقُرْآنَ ﴿٢﴾

2. Amefundisha Qur-aan.[1]

 

 

 

خَلَقَ الْإِنسَانَ ﴿٣﴾

3. Ameumba binaadam.

 

 

 

 

عَلَّمَهُ الْبَيَانَ ﴿٤﴾

4. Amemfunza ufasaha

 

 

 

 

الشَّمْسُ وَالْقَمَرُ بِحُسْبَانٍ ﴿٥﴾

5. Jua na mwezi huenda katika hesabu.

 

 

 

 

وَالنَّجْمُ وَالشَّجَرُ يَسْجُدَانِ ﴿٦﴾

6. Na nyota na miti vinasujudu.[2]

 

 

 

 

وَالسَّمَاءَ رَفَعَهَا وَوَضَعَ الْمِيزَانَ ﴿٧﴾

7. Na mbingu Ameziinua na Akaweka mizani.

 

 

 

 

أَلَّا تَطْغَوْا فِي الْمِيزَانِ ﴿٨﴾

8. Ili msivuke mipaka (kudhulumu) katika mizani.

 

 

 

 

وَأَقِيمُوا الْوَزْنَ بِالْقِسْطِ وَلَا تُخْسِرُوا الْمِيزَانَ ﴿٩﴾

9. Na simamisheni uzani kwa uadilifu, na wala msipunguze mizani.

 

 

 

 

وَالْأَرْضَ وَضَعَهَا لِلْأَنَامِ ﴿١٠﴾

10. Na ardhi Ameiweka chini kwa ajili ya viumbe.

 

 

 

 

فِيهَا فَاكِهَةٌ وَالنَّخْلُ ذَاتُ الْأَكْمَامِ ﴿١١﴾

11. Humo mna matunda na mitende yenye mafumba.

 

 

 

 

وَالْحَبُّ ذُو الْعَصْفِ وَالرَّيْحَانُ ﴿١٢﴾

12. Na nafaka zenye makapi na rehani; miti yenye harufu nzuri ya kunukia.  

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿١٣﴾

13. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?[3]

 

 

 

 

 

خَلَقَ الْإِنسَانَ مِن صَلْصَالٍ كَالْفَخَّارِ ﴿١٤﴾

14. Amemuumba binaadam kutokana na udongo wa mfinyanzi unaotoa sauti kama udongo wa kinamo.

 

 

 

 

وَخَلَقَ الْجَانَّ مِن مَّارِجٍ مِّن نَّارٍ ﴿١٥﴾

15. Na Akaumba majini kutokana na mwako wa moto.

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿١٦﴾

16. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

 

رَبُّ الْمَشْرِقَيْنِ وَرَبُّ الْمَغْرِبَيْنِ ﴿١٧﴾

17. Rabb wa Mashariki mbili na Rabb wa Magharibi mbili.

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿١٨﴾

18. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

 

مَرَجَ الْبَحْرَيْنِ يَلْتَقِيَانِ ﴿١٩﴾

19. Ameziachilia bahari mbili zinakutana.

 

 

 

 

بَيْنَهُمَا بَرْزَخٌ لَّا يَبْغِيَانِ ﴿٢٠﴾

20. Baina yake kuna kizuizi, hazivukiani mipaka.

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٢١﴾

21. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

يَخْرُجُ مِنْهُمَا اللُّؤْلُؤُ وَالْمَرْجَانُ ﴿٢٢﴾

22. Zinatoka humo lulu na marijani.

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٢٣﴾

23. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

وَلَهُ الْجَوَارِ الْمُنشَآتُ فِي الْبَحْرِ كَالْأَعْلَامِ ﴿٢٤﴾

24. Na ni Vyake vyombo viendavyo baharini vikiinuliwa tanga kama milima.

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٢٥﴾

25. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ ﴿٢٦﴾

26. Kila aliyekuwa juu yake (ardhi) ni mwenye kutoweka.[4]

 

 

 

 

 

وَيَبْقَىٰ وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ ﴿٢٧﴾

27. Na utabakia Wajihi[5] wa Rabb wako Mwenye Ujalali na Ukarimu.

 

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٢٨﴾

28. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

يَسْأَلُهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ كُلَّ يَوْمٍ هُوَ فِي شَأْنٍ ﴿٢٩﴾

29. Wanamuomba Yeye wote walio mbinguni na ardhini, kila siku Yeye Yumo katika Kubadilisha mambo. 

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٣٠﴾

30. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

سَنَفْرُغُ لَكُمْ أَيُّهَ الثَّقَلَانِ ﴿٣١﴾

31. Tutakukusudieni kwa hisabu enyi aina mbili ya viumbe (majini na wanaadam).

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٣٢﴾

32. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

يَا مَعْشَرَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ إِنِ اسْتَطَعْتُمْ أَن تَنفُذُوا مِنْ أَقْطَارِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ فَانفُذُوا ۚ لَا تَنفُذُونَ إِلَّا بِسُلْطَانٍ ﴿٣٣﴾

33. Enyi jamii ya majini na wanaadam! Mkiweza kupenya kwenye zoni za mbingu na ardhi, basi penyeni. Hamtoweza kupenya isipokuwa kwa mamlaka (ya Allaah).

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٣٤﴾

34. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

 

يُرْسَلُ عَلَيْكُمَا شُوَاظٌ مِّن نَّارٍ وَنُحَاسٌ فَلَا تَنتَصِرَانِ ﴿٣٥﴾

35. Mtapelekewa mwako wa moto juu yenu na shaba iliyoyayushwa, basi hamtoweza kujinusuru.

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٣٦﴾

36. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

 

 

فَإِذَا انشَقَّتِ السَّمَاءُ فَكَانَتْ وَرْدَةً كَالدِّهَانِ ﴿٣٧﴾

37. Zitakapoachana mbingu zikawa rangi ya waridi kama mafuta.

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٣٨﴾

38. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

فَيَوْمَئِذٍ لَّا يُسْأَلُ عَن ذَنبِهِ إِنسٌ وَلَا جَانٌّ ﴿٣٩﴾

39. Siku hiyo hatoulizwa kuhusu dhambi yake binaadam wala jini.

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٤٠﴾

40. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

يُعْرَفُ الْمُجْرِمُونَ بِسِيمَاهُمْ فَيُؤْخَذُ بِالنَّوَاصِي وَالْأَقْدَامِ ﴿٤١﴾

41. Watatambulikana wahalifu kwa alama zao, basi watachukuliwa kwa vipaji vya uso na miguu.  

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٤٢﴾

42. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

هَـٰذِهِ جَهَنَّمُ الَّتِي يُكَذِّبُ بِهَا الْمُجْرِمُونَ ﴿٤٣﴾

43. Hii ni Jahannam ambayo wahalifu wanaikadhibisha.

 

 

 

 

يَطُوفُونَ بَيْنَهَا وَبَيْنَ حَمِيمٍ آنٍ ﴿٤٤﴾

44. Wataizunguka baina yake na baina ya maji yachemkayo yaliyofikia ukomo wa kutokota.

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٤٥﴾

45. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

وَلِمَنْ خَافَ مَقَامَ رَبِّهِ جَنَّتَانِ ﴿٤٦﴾

46. Na kwa mwenye kukhofu kisimamo mbele ya Rabb wake atapata bustani mbili.[6]

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٤٧﴾

47. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

ذَوَاتَا أَفْنَانٍ ﴿٤٨﴾

48. Zilizo na matawi yaliyotanda.

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٤٩﴾

49. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

فِيهِمَا عَيْنَانِ تَجْرِيَانِ ﴿٥٠﴾

50. Mna humo chemchemu mbili zinazopita.

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٥١﴾

51. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

فِيهِمَا مِن كُلِّ فَاكِهَةٍ زَوْجَانِ ﴿٥٢﴾

52. Mna humo kila matunda ya aina mbilimbili.

 

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٥٣﴾

53. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

 

مُتَّكِئِينَ عَلَىٰ فُرُشٍ بَطَائِنُهَا مِنْ إِسْتَبْرَقٍ ۚ وَجَنَى الْجَنَّتَيْنِ دَانٍ ﴿٥٤﴾

54. Wakiegemea kwenye matandiko ya kupumzikia, bitana yake ni kutokana na hariri nzito nyororo, na matunda ya bustani mbili yako karibu na kufikiwa.

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٥٥﴾

55. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

 

فِيهِنَّ قَاصِرَاتُ الطَّرْفِ لَمْ يَطْمِثْهُنَّ إِنسٌ قَبْلَهُمْ وَلَا جَانٌّ ﴿٥٦﴾

56. Mna humo wanawake wenye staha wanaoinamisha macho, hajawabikiri kabla yao binaadam yeyote wala jini.

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٥٧﴾

57. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

 

كَأَنَّهُنَّ الْيَاقُوتُ وَالْمَرْجَانُ ﴿٥٨﴾

58. Kama kwamba hao wanawake ni yakuti na marijani.

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٥٩﴾

59. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

 

هَلْ جَزَاءُ الْإِحْسَانِ إِلَّا الْإِحْسَانُ ﴿٦٠﴾

60. Je, kuna jazaa ya ihsaan isipokuwa ihsaan tu?[7] 

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٦١﴾

61. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

وَمِن دُونِهِمَا جَنَّتَانِ ﴿٦٢﴾

62. Na zaidi ya hizo mbili, ziko bustani mbili zingine.[8]

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٦٣﴾

63. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

مُدْهَامَّتَانِ ﴿٦٤﴾

64. Za rangi ya kijani iliyokoza.

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٦٥﴾

65. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

فِيهِمَا عَيْنَانِ نَضَّاخَتَانِ ﴿٦٦﴾

66. Mna humo chemchemu mbili zenye kububujika kwa nguvu mfululizo.

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٦٧﴾

67. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

فِيهِمَا فَاكِهَةٌ وَنَخْلٌ وَرُمَّانٌ ﴿٦٨﴾

68. Mna humo matunda na mitende na makomamanga.

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٦٩﴾

69. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

فِيهِنَّ خَيْرَاتٌ حِسَانٌ ﴿٧٠﴾

70. Mna humo wanawake wazuri, wema.

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٧١﴾

71. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

حُورٌ مَّقْصُورَاتٌ فِي الْخِيَامِ ﴿٧٢﴾

72. Hurulaini: Wanawake weupe wazuri wa Jannah wenye macho makubwa ya kupendeza, wanaotawishwa katika mahema.

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٧٣﴾

73.  Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

 

لَمْ يَطْمِثْهُنَّ إِنسٌ قَبْلَهُمْ وَلَا جَانٌّ ﴿٧٤﴾

74.    Hajawabikiri kabla yao binaadam yeyote wala jini.

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٧٥﴾

75. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

مُتَّكِئِينَ عَلَىٰ رَفْرَفٍ خُضْرٍ وَعَبْقَرِيٍّ حِسَانٍ ﴿٧٦﴾

76. Wakiegemea kwenye matakia ya kijani na mazulia ya rangi mbalimbali ya hariri mazuri mno yasiyo na kifani.

 

 

 

 

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿٧٧﴾

77. Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?

 

 

 

 

 

تَبَارَكَ اسْمُ رَبِّكَ ذِي الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ ﴿٧٨﴾

78.  Limebarikika Jina la Rabb wako Mwenye Ujalali na Ukarimu.[9]

 

 

 

[1] Amefunza Qur-aan Kwa Binaadam Na Ufasaha:

 

Kuanzia Aayah hii namba (2) na zinazofuatia (3-4), Tafsiyr yake ni kama ifuatavyo:

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Amemfunza binaadam Quraan kwa kuiwepesisha kusomwa kwake, kuihifadhi, na kufahamu maana zake. Akawafunza Waja Wake kuitamka, na Akawasahilishia kufahamu maana zake. Na hii ni Rehma kubwa kabisa kwa Waja Wake kwamba Amewateremshia Quraan kwa lugha ya Kiarabu, kwa maneno bora kabisa, na ubainifu bora kabisa ikijumuisha kila la kheri na kuhadharisha kila la shari. Akamuumba binaadam katika umbo bora kabisa lililo kamilifu na lililoundwa vizuri. Akamuumba binaadam katika ukamilifu kabisa na Akamtofautisha na viumbe vinginevyo kwa kumfundisha kujieleza na kufafanua yaliyomo ndani ya nafsi yake kwa matamshi na maandishi. Uwezo huu ambao Allaah Amempambanua mwanaadam juu ya viumbe vinginevyo, ni katika Neema Zake kubwa kwake. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

[2] Kila Kitu Kinamsujudia Allaah (عزّ وجلّ).

 

Kutokana na taadhima ya Allaah (سبحانه وتعالى) Muumba wa kila kitu, vitu vyote vinamsujudia Yeye Allaah (سبحانه وتعالى).      

 

Rejea Al-A’raaf (7:206), Ar-Ra’d (13:15), An-Nahl (16:48-50), Al-Hajj (22:18).

 

Na miongoni mwa Hadiyth ni hii ifuatayo:

 

حَدَّثَنَا مُحَمَّدُ بْنُ يُوسُفَ، حَدَّثَنَا سُفْيَانُ، عَنِ الأَعْمَشِ، عَنْ إِبْرَاهِيمَ التَّيْمِيِّ، عَنْ أَبِيهِ، عَنْ أَبِي ذَرٍّ ـ رضى الله عنه ـ قَالَ قَالَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم لأَبِي ذَرٍّ حِينَ غَرَبَتِ الشَّمْسُ ‏"‏ تَدْرِي أَيْنَ تَذْهَبُ ‏"‏‏.‏ قُلْتُ اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَعْلَمُ‏.‏ قَالَ ‏"‏ فَإِنَّهَا تَذْهَبُ حَتَّى تَسْجُدَ تَحْتَ الْعَرْشِ، فَتَسْتَأْذِنَ فَيُؤْذَنَ لَهَا، وَيُوشِكُ أَنْ تَسْجُدَ فَلاَ يُقْبَلَ مِنْهَا، وَتَسْتَأْذِنَ فَلاَ يُؤْذَنَ لَهَا، يُقَالُ لَهَا ارْجِعِي مِنْ حَيْثُ جِئْتِ‏.‏ فَتَطْلُعُ مِنْ مَغْرِبِهَا، فَذَلِكَ قَوْلُهُ تَعَالَى ‏  ‏وَالشَّمْسُ تَجْرِي لِمُسْتَقَرٍّ لَهَا ذَلِكَ تَقْدِيرُ الْعَزِيزِ الْعَلِيمِ ‏

 

Amesimulia Abuu Dharr (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliniuliza wakati wa machweo: “Je, unajua jua linapokwenda (wakati wa kuzama kwake)?”  Nikamjibu: “Allaah na Rasuli Wake Wanajua zaidi.” Akasema: “Hakika linakwenda mpaka linasujudu chini ya ‘Arsh, na kutaka idhini kuchomoza tena, nalo linaruhusiwa. Na inachelewa kuwa (itafika wakati ambapo) litakaribia kusujudu lakini sijda yake haitokubaliwa, na litaomba idhini lakini litakataliwa (kutimiza mizunguko yake). Litaambiwa: ‘Rudi ulipotoka’. Hivyo, litachomoza Magharibi. Na hiyo ndiyo Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

وَالشَّمْسُ تَجْرِي لِمُسْتَقَرٍّ لَّهَا ۚ ذَٰلِكَ تَقْدِيرُ الْعَزِيزِ الْعَلِيمِ ﴿٣٨﴾

“Na jua linatembea hadi matulio yake. Hayo ni Takdiri ya Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mjuzi wa yote.” [Yaasiyn 36:38) - Hadiyth ameipokea Imaam Al-Bukhaariy]

 

[3] Majini Wametoa Jibu Bora Kuhusu Neema Za Allaah (عزّ وجلّ):

 

خرجَ رسولُ اللَّهِ صلَّى اللَّهُ علَيهِ وسلَّمَ على أَصحابِهِ، فقرأَ عليهم سورةَ الرَّحمنِ من أوَّلِها إلى آخرِها فسَكَتوا فقالَ: لقد قرأتُها على الجنِّ ليلةَ الجنِّ فَكانوا أحسَنَ مردودًا منكم، كنتُ كلَّما أتيتُ على قولِهِ فَبِأيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ قالوا: لا بشَيءٍ من نِعَمِكَ ربَّنا نُكَذِّبُ فلَكَ الحمدُ

 

Amesimulia Jaabir (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuja kwa Swahaba zake akawasomea Suwrah Ar-Rahmaan kuanzia mwanzoni mwake hadi mwisho wake, wakanyamaza kimya kisha akasema: “Niliwasomea majini usiku wa majini wakawa na mwitiko bora kuliko nyinyi. Kila nilipofikia kusoma Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):

فَبِأَيِّ آلَاءِ رَبِّكُمَا تُكَذِّبَانِ ﴿١٦﴾

“Basi ni zipi katika Neema za Rabb wenu mnazikadhibisha?”

 

Walikuwa wanasema:

 

لا بشَيءٍ من نِعَمِكَ ربَّنا نُكَذِّبُ فلَكَ الحمدُ

Hakuna chochote katika Neema Zako Rabb wetu tunazozokadhibisha, na Himdi ni Zako.” [At-Tirmidhiy na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhiy (3291), Swahiyh Al-Jaami’ (5138)]

 

Tanbihi: ‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusu usahihi wa Hadiyth hiyo. Imaam As-Sa’diy ameinukuu katika Tafsiyr yake, pia imenukuliwa katika Tafsiyr Al-Muyassar, Tafsiyr Ibn Kathiyr.

 

[4] Kila Kitu Kitatoweka Atabakia Allaah (عزّ وجلّ) Pekee:

 

Rejea Ghaafir (40:16) kwenye maelezo bayana.   

 

[5]Aqiydah Sahihi Ya Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa’ah Ni Kuthibisha Sifa Za Allaah.

 

Rejea  Huwd (11:37), Al-Fat-h (48:10) kwenye maelezo bayana na rejea mbalimbali.

 

[6] Jannah (Pepo) Mbili:

 

Kuanzia Aayah hii namba (46) hadi mwisho wa Suwrah hii tukufu, zimetajwa neema za watu wa Jannah. Rejea pia Faatwir (35:33) kwenye faida na rejea mbalimbali zinazotajwa katika Qur-aan kuhusu neema za Jannah.

 

Yaani na yule anayemkhofu Rabb Wake na kukhofu kusimamishwa Kwake, akaacha aliyokatazwa na akatenda aliyoamrishwa, atapata Jannah mbili za dhahabu ambazo vyombo vyake, majengo yake, na kila kilichomo kitakuwa ni mapambo ya dhahabu. Moja ya Jannah mbili, itakuwa ni malipo ya kujiepusha makatazo, na nyengine itakuwa ni (malipo) ya kufanya utiifu (na matendo mema). [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

Na katika Hadiyth:

 

حَدَّثَنَا عَبْدُ اللَّهِ بْنُ أَبِي الأَسْوَدِ، حَدَّثَنَا عَبْدُ الْعَزِيزِ بْنُ عَبْدِ الصَّمَدِ الْعَمِّيُّ، حَدَّثَنَا أَبُو عِمْرَانَ الْجَوْنِيُّ، عَنْ أَبِي بَكْرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ قَيْسٍ، عَنْ أَبِيهِ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ ‏ "‏ جَنَّتَانِ مِنْ فِضَّةٍ، آنِيَتُهُمَا وَمَا فِيهِمَا وَجَنَّتَانِ مِنْ ذَهَبٍ آنِيَتُهُمَا وَمَا فِيهِمَا، وَمَا بَيْنَ الْقَوْمِ وَبَيْنَ أَنْ يَنْظُرُوا إِلَى رَبِّهِمْ إِلاَّ رِدَاءُ الْكِبْرِ عَلَى وَجْهِهِ فِي جَنَّةِ عَدْنٍ ‏"‏‏.‏

 

Amesimulia Abu Bakr Bin ‘Abdillaah bin Qays kutoka kwa baba yake (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Jannah mbili za fedha, vyombo vyake na vilivyomo ndani yake ni fedha pia. Na Jannah mbili za dhahabu, vyombo vyake na vilivyomo ndani yake. Na hakuna kitakachowazuia watu na kumuona Rabb wao katika Jannah ya ‘Adn isipokuwa ni pazia ya kibri iliyo juu ya Wajihi Wake.” [Al-Bukhaariy Kitaab Cha Tafsiyr (65)]

 

[7] Jazaa Ya Ihsaan (Wema):

 

Hakuna malipo kwa mwenye kumwabudu Allaah ipasavyo na kuwanufaisha Waja Wake, isipokuwa Allaah Atamrejeshea uwajibikaje wake huo kwa kumkirimu thawabu kochokocho, Atamfanikishia kufuzu kuliko kukubwa, Atambubujishia neema za kudumu na Atampa maisha mazuri yaliyo salama. Basi Jannah mbili hizi za juu kabisa ni kwa ajili ya waliojikurubisha kwa Allaah.  [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

[8] Zaidi Ya Jannah (Pepo) Mbili:

وَمِن دُونِهِمَا جَنَّتَانِ ﴿٦٢﴾

“Na zaidi ya hizo mbili, ziko bustani mbili zingine.”

 

Yaani: Ambazo majengo yake, vyombo vyake, mapambo yake na yote yaliyomo humo, yatakuwa ni ya fedha. Na hizi zitakuwa kwa ajili ya watu wa kuliani. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

[9] Dhul-Jalaal Wal-Ikraam: Mwenye Ujalali Na Ukarimu, Utukufu.

 

Majina haya Matukufu ya Allaah (عزّ وجلّ), yanamaanisha: Mwenye Ujalali Na Ukarimu, Mtukuka daima, Mwenye Utukufu wa Juu Kabisa, Taadhima, Hadhi.

 

Na kutaja Majina haya katika duaa, ni sababu mojawapo ya duaa kutakabaliwa. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ameamrisha mtu akithirishe kutamka Majina haya kama ilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo:

 

عَنْ أَنَسٍ، أَنَّ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم قَالَ ‏ "‏ أَلِظُّوا بِيَا ذَا الْجَلاَلِ وَالإِكْرَامِ ‏"‏ ‏

Amesimulia Anas (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Dumisheni kwa wingi: Yaa-Dhal-Jalaali wal-Ikraam.” [Swahiyh Sunan At-Tirmidhiy (2797)]

 

 

Share