069 - Al-Haaqah

 

   الْحآقَّة

 

069-Al-Haaqah

 

069-Al-Haaqqah: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

 

الْحَاقَّةُ﴿١﴾

1.   Tukio la haki lisiloepukika![1]

 

 

 

 

مَا الْحَاقَّةُ﴿٢﴾

2. Ni nini tukio la haki lisiloepukika?

 

 

 

 

وَمَا أَدْرَاكَ مَا الْحَاقَّةُ﴿٣﴾

3. Na nini kitakachokujulisha nini tukio la haki lisiloepukika?

 

 

 

 

كَذَّبَتْ ثَمُودُ وَعَادٌ بِالْقَارِعَةِ﴿٤﴾

4. Kina Thamuwd na ‘Aad walikadhibisha tukio lenye kugongagonga na kutia kiwewe nyoyo.[2]

 

 

 

 

 

فَأَمَّا ثَمُودُ فَأُهْلِكُوا بِالطَّاغِيَةِ﴿٥﴾

5. Ama kina Thamuwd, wao waliangamizwa kwa ukelele mkali uliovuka mipaka.

 

 

 

 

وَأَمَّا عَادٌ فَأُهْلِكُوا بِرِيحٍ صَرْصَرٍ عَاتِيَةٍ﴿٦﴾

6. Na ama kina ‘Aad, hao waliangamizwa kwa upepo mbaya wa sauti na baridi kali, uvumao kwa nguvu.

 

 

 

 

سَخَّرَهَا عَلَيْهِمْ سَبْعَ لَيَالٍ وَثَمَانِيَةَ أَيَّامٍ حُسُومًا فَتَرَى الْقَوْمَ فِيهَا صَرْعَىٰ كَأَنَّهُمْ أَعْجَازُ نَخْلٍ خَاوِيَةٍ﴿٧﴾

7. Aliwalazimishia nyusiku saba na michana minane mfululizo, basi utaona watu humo wameanguka chini kama kwamba ni magogo ya mitende iliyo mitupu.

 

 

 

 

فَهَلْ تَرَىٰ لَهُم مِّن بَاقِيَةٍ﴿٨﴾

8. Basi je, unaona mabakio yao yoyote?

 

 

 

وَجَاءَ فِرْعَوْنُ وَمَن قَبْلَهُ وَالْمُؤْتَفِكَاتُ بِالْخَاطِئَةِ﴿٩﴾

9. Na akaja Firawni na wale walio kabla yake, na (watu wa) miji iliyopinduliwa chini juu kwa sababu ya hatia zao.

 

 

 

فَعَصَوْا رَسُولَ رَبِّهِمْ فَأَخَذَهُمْ أَخْذَةً رَّابِيَةً﴿١٠﴾

10. Basi wakamuasi Rasuli wa Rabb wao, Akawachukua mchukuo uliopindukia ukali.

 

 

 

إِنَّا لَمَّا طَغَى الْمَاءُ حَمَلْنَاكُمْ فِي الْجَارِيَةِ﴿١١﴾

11. Hakika Sisi, pale maji yalipopinduka mipaka, Tulikubebeni katika merikebu.[3]

 

 

 

لِنَجْعَلَهَا لَكُمْ تَذْكِرَةً وَتَعِيَهَا أُذُنٌ وَاعِيَةٌ﴿١٢﴾

12. Ili Tuifanye kuwa ni ukumbusho kwenu, na ibakie kumbukumbu katika sikio (la wenye kuzingatia) linalobakisha kumbukumbu.

 

 

 

 

 

فَإِذَا نُفِخَ فِي الصُّورِ نَفْخَةٌ وَاحِدَةٌ﴿١٣﴾

13. Basi litakapopulizwa baragumu mpulizo mmoja.[4]

 

 

 

وَحُمِلَتِ الْأَرْضُ وَالْجِبَالُ فَدُكَّتَا دَكَّةً وَاحِدَةً﴿١٤﴾

14. Na ardhi na milima ikaondolewa kisha ikapondwa mpondo mmoja.

 

 

 

فَيَوْمَئِذٍ وَقَعَتِ الْوَاقِعَةُ﴿١٥﴾

15. Basi siku hiyo ndio litatokea tukio la kutokea.

 

 

 

 

وَانشَقَّتِ السَّمَاءُ فَهِيَ يَوْمَئِذٍ وَاهِيَةٌ﴿١٦﴾

16. Na mbingu zitararuka, kwani siku hiyo zitakuwa dhaifu sana.

 

 

 

 

 

وَالْمَلَكُ عَلَىٰ أَرْجَائِهَا ۚ وَيَحْمِلُ عَرْشَ رَبِّكَ فَوْقَهُمْ يَوْمَئِذٍ ثَمَانِيَةٌ﴿١٧﴾

17. Na Malaika watakuwa pembezoni mwake,[5] na watabeba ‘Arsh[6] ya Rabb wako juu yao siku hiyo (Malaika) wanane.[7]

 

 

يَوْمَئِذٍ تُعْرَضُونَ لَا تَخْفَىٰ مِنكُمْ خَافِيَةٌ﴿١٨﴾

18. Siku hiyo mtahudhurishwa, halitofichika tendo lenu lolote la siri.

 

 

 

فَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ فَيَقُولُ هَاؤُمُ اقْرَءُوا كِتَابِيَهْ﴿١٩﴾

19. Basi ama yule atakayepewa kitabu chake kuliani mwake, atasema: Hebu chukueni someni kitabu changu![8]

 

 

إِنِّي ظَنَنتُ أَنِّي مُلَاقٍ حِسَابِيَهْ﴿٢٠﴾

20. Hakika mimi niliyakinisha kuwa hakiki mimi ni mwenye kukutana na hesabu yangu!

 

 

فَهُوَ فِي عِيشَةٍ رَّاضِيَةٍ﴿٢١﴾

21. Basi yeye atakuwa katika maisha ya kuridhisha.

 

 

فِي جَنَّةٍ عَالِيَةٍ﴿٢٢﴾

22. Kwenye Jannah ya juu.[9]

 

 

قُطُوفُهَا دَانِيَةٌ﴿٢٣﴾

23. Matunda yake ya kuchumwa yako karibu.

 

 

 

 

كُلُوا وَاشْرَبُوا هَنِيئًا بِمَا أَسْلَفْتُمْ فِي الْأَيَّامِ الْخَالِيَةِ﴿٢٤﴾

24. (Wataambiwa): Kuleni na kunyweni kwa furaha kwa yale mliyoyatanguliza katika siku nyingi zilizopita.

 

 

 

 

وَأَمَّا مَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِشِمَالِهِ فَيَقُولُ يَا لَيْتَنِي لَمْ أُوتَ كِتَابِيَهْ﴿٢٥﴾

25. Na ama yule atakayepewa kitabu chake kushotoni mwake, atasema: Ee! Laiti nisingelipewa kitabu changu![10]

 

 

 

وَلَمْ أَدْرِ مَا حِسَابِيَهْ﴿٢٦﴾

26. Na wala nisingelijua hesabu yangu!

 

 

 

يَا لَيْتَهَا كَانَتِ الْقَاضِيَةَ﴿٢٧﴾

27. Ee! Laiti yangelikuwa (mauti) ndio kumalizika kwangu.

 

 

 

 

مَا أَغْنَىٰ عَنِّي مَالِيَهْ ۜ﴿٢٨﴾

28. Haikunifaa mali yangu.

 

 

 

هَلَكَ عَنِّي سُلْطَانِيَهْ﴿٢٩﴾

29. Madaraka yangu yamenitoweka.

 

 

 

خُذُوهُ فَغُلُّوهُ﴿٣٠﴾

30. (Patasemwa): Mchukueni, na mfungeni pingu.

 

 

 

ثُمَّ الْجَحِيمَ صَلُّوهُ﴿٣١﴾

31. Kisha kwenye moto uwakao vikali mno muingizeni aungue.

 

 

 

 

ثُمَّ فِي سِلْسِلَةٍ ذَرْعُهَا سَبْعُونَ ذِرَاعًا فَاسْلُكُوهُ﴿٣٢﴾

32. Kisha mtieni pingu katika minyororo yenye urefu wa dhiraa sabini.

 

 

 

 

 

إِنَّهُ كَانَ لَا يُؤْمِنُ بِاللَّـهِ الْعَظِيمِ﴿٣٣﴾

33. Hakika yeye alikuwa hamuamini Allaah Mwenye Taadhima.[11]

 

 

 

 

وَلَا يَحُضُّ عَلَىٰ طَعَامِ الْمِسْكِينِ﴿٣٤﴾

34. Na wala hahamasishi kulisha masikini.

 

 

 

 

فَلَيْسَ لَهُ الْيَوْمَ هَاهُنَا حَمِيمٌ﴿٣٥﴾

35. Basi leo hapa hatokuwa na rafiki wa dhati.

 

 

 

 

وَلَا طَعَامٌ إِلَّا مِنْ غِسْلِينٍ﴿٣٦﴾

36. Wala chakula isipokuwa usaha (wa walio motoni).

 

 

 

 

لَّا يَأْكُلُهُ إِلَّا الْخَاطِئُونَ﴿٣٧﴾

37. Hawakili chakula hicho isipokuwa wenye hatia.

 

 

 

 

فَلَا أُقْسِمُ بِمَا تُبْصِرُونَ﴿٣٨﴾

38. Basi Naapa kwa yale mnayoyaona.[12]

 

 

 

 

وَمَا لَا تُبْصِرُونَ﴿٣٩﴾

39. Na kwa yale msiyoyaona.

 

 

 

إِنَّهُ لَقَوْلُ رَسُولٍ كَرِيمٍ﴿٤٠﴾

40. Hakika hii (Qur-aan) bila shaka ni kauli ya Rasuli Mtukufu.

 

 

 

 

وَمَا هُوَ بِقَوْلِ شَاعِرٍ ۚ قَلِيلًا مَّا تُؤْمِنُونَ﴿٤١﴾

41. Na si kauli ya mshairi. Ni machache sana yale mnayoamini.

 

 

 

 

وَلَا بِقَوْلِ كَاهِنٍ ۚ قَلِيلًا مَّا تَذَكَّرُونَ﴿٤٢﴾

42. Na wala si kauli ya kahini. Ni machache sana yale mnayokumbuka.

 

 

 

تَنزِيلٌ مِّن رَّبِّ الْعَالَمِينَ﴿٤٣﴾

43.  Ni uteremsho kutoka kwa Rabb wa walimwengu.

 

 

 

وَلَوْ تَقَوَّلَ عَلَيْنَا بَعْضَ الْأَقَاوِيلِ﴿٤٤﴾

44. Na lau kama (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) angetutungia baadhi ya kauli.

 

 

 

لَأَخَذْنَا مِنْهُ بِالْيَمِينِ﴿٤٥﴾

45. Bila shaka Tungelimchukua kwa Mkono wa kuume.

 

 

 

ثُمَّ لَقَطَعْنَا مِنْهُ الْوَتِينَ﴿٤٦﴾

46. Kisha bila shaka Tungelimkata mshipa mkubwa wa moyo wa uhai.

 

 

 

فَمَا مِنكُم مِّنْ أَحَدٍ عَنْهُ حَاجِزِينَ﴿٤٧﴾

47. Basi hakuna mmoja yeyote kati yenu angeliweza kutuzuia naye.

 

 

 

 

وَإِنَّهُ لَتَذْكِرَةٌ لِّلْمُتَّقِينَ﴿٤٨﴾

48. Na hakika hii (Qur-aan) bila shaka ni ukumbusho kwa wenye taqwa.

 

 

 

 

وَإِنَّا لَنَعْلَمُ أَنَّ مِنكُم مُّكَذِّبِينَ﴿٤٩﴾

49. Na hakika Sisi bila shaka Tunajua kwamba miongoni mwenu wako wenye kukadhibisha.

 

 

 

 

وَإِنَّهُ لَحَسْرَةٌ عَلَى الْكَافِرِينَ﴿٥٠﴾

50. Na hakika hii (Qur-aan) bila shaka itakuwa ni majuto makubwa juu ya makafiri.

 

 

 

وَإِنَّهُ لَحَقُّ الْيَقِينِ﴿٥١﴾

51. Na hakika hii (Qur-aan) ni haki ya yakini.[13]

 

 

 

فَسَبِّحْ بِاسْمِ رَبِّكَ الْعَظِيمِ﴿٥٢﴾

52. Basi sabbih kwa Jina la Rabb wako Adhimu.

 

 

 

[1] Al-Haaqqah Ni Katika Majina Ya Siku Ya Qiyaamah:

 

Rejea Al-Qiyaamah (75;1) kwenye majina mengineyo ya Siku ya Qiyaamah.

 

[2] Makafiri Wa Nyumati Za Nyuma Na Aina Za Adhabu Zao:

 

Kuanzia Aayah hii namba (4) na zifuatazo hadi namba (12) zinataja baadhi ya nyumati za awali na adhabu zao baada ya kukadhibisha Risala ya Allaah kupitia Rusuli Wake. Rejea Al-‘Ankabuwt (29:40) kwenye uchambuzi na maelezo yao kwa mukhtasari kuhusu kufru, shirki na kukadhibisha kwao na maangamizi yao pamoja na rejea zake mbalimbali.

 

[3] Merikebu Ya Nabiy Nuwh (عليه السّلام):

 

Ni merikebu ya Nabiy Nuwh (عليه السّلام). Rejea Al-‘Ankabuwt (29:40).

 

[4] Mipulizo Ya Baragumu Ya Kutokea Qiyaamah:

 

Kuanzia Aayah hii namba (13) hadi namba (18) yanazungumziwa matukio yatakayotokea Siku ya Qiyaamah mpaka Atakapoteremka Allaah (عزّ وجلّ) kuwafanyia hesabu waja.

 

Rejea Az-Zumar (39:68) kwenye maelezo yake na faida kadhaa. Rejea pia An-Naml (27:87).

 

[5] Kuteremka Malaika Kutoka Mbinguni Siku Ya  Qiyaamah Kisha Allaah (عزّ وجلّ)  Kuwahukumu Viumbe:

 

Rejea Al-Furqaan (25:25), Al-Fajr (89:22), Al-Baqarah (2:210), Al-An’aam (6:158).

 

[6] ‘Arsh Ya Ar-Rahmaan (Kiti Cha Enzi) Ni Tofauti Na Viti Vya Enzi Vya Wafalme Duniani:

 

Kuna kauli mbili kuhusu ‘Arsh hiyo ya Allaah (سبحانه وتعالى) watakayoibeba Malaika Siku ya Qiyaamah, kama alivyosema Imaam Ibn Kathiyr kwamba, inaweza kuwa imekusudiwa ni ‘Arsh Adhimu ya Allaah. Au ‘Arshi (ni Kiti cha Enzi) ambacho kitawekwa Siku ya Qiyaamah kwa ajili ya kuhukumiwa watu. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

Rejea Twaahaa (20:5) kwenye maelezo bayana na faida muhimu zenye kuhusiana na ‘Aqiydah ya Muislamu kuhusu ‘Arsh ‘Adhimu ya Allaah (سبحانه وتعالى).   

 

Hata kama imekusudiwa katika Aayah hii kuwa ni Kiti cha Enzi kitakachowekwa kwa ajili ya watu kuhukumiwa, basi pia haikujulikana kayfiyah (namna yake) na hakiwezi kufanana na kiti cha enzi cha wafalme, kama vile kiti cha Malkia Balqees wa Sabaa kilichotajwa katika Suwrah An-Naml (27:23), (27:38) (27:41-42). Au pia kiti cha enzi cha Nabiy Yuwsuf (عليه السّلام), rejea Suwrah Yuwsuf (12:100).

 

[7] Malaika Watakaobeba ‘Arsh Ya Allaah (عزّ وجلّ):

 

Rejea Ghaafir (40:7) kwenye Hadiyth inayotaja sifa za Malaika wanaobeba ‘Arsh ya Allaah (عزّ وجلّ).

 

[8] Watakaopewa Vitabu Vyao Kuliani:

 

Kuanzia Aayah hii namba (19) hadi namba (24) zinaelezwa hali za watakaopewa vitabu vyao kuliani mwao. Wametajwa pia katika Suwrah Al-Inshiqaaq (84:7-9).         

 

[9] Daraja Za Jannah:

 

Rejea Al-Muuminuwn (23:11) kwenye Hadiyth inayotaja daraja za Jannah, na Jannah ya Al-Firdaws kuwa ni ya juu kabisa, na nasaha ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa Muumini kuwa, anapoomba Jannah, aombe Jannah ya Al-Firdaws.  

 

[10] Watakaopewa Vitabu Vyao Kushotoni Mwao:

 

Kuanzia Aayah hii namba (25) hadi namba (37) zinaelezwa hali za watakaopewa vitabu vyao kushotoni mwao. Wametajwa pia katika Suwrah Al-Inshiqaaq (84:10-15).

 

[11] Adhimu:

 

Ni Sifa ya Allaah (سبحانه وتعالى) ambayo maana zake ni: Mwenye Taadhima, Utukufu, Mkubwa na Mkuu kabisa Aliyetukuka, Mwenye Ujalali, Ukarama.

 

[12]  Allaah (سبحانه وتعالى) Anaapia Kuthibitisha Ukweli Wa Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) Na Kuwaraddi Washirikina Waliompachika Sifa Ovu Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Pamoja Na Qur-aan:

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Anaaapia kwa vitu vinavooonekana na visivyooonekana katika Aayah hii namba (38-39), na jibu la kiapo ni Aayah zinazofuatia namba (40-43) za kumthibitisha Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم)  na kuithibitisha Qur-aan Tukufu kuwa ni Uteremsho kutoka Kwake, na kuwaraddi washirikina wa Makkah kwa dhulma zao za kumpachika sifa ovu Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) pamoja na Qur-aan Tukufu.  Rejea pia Al-A’raaf (7:184), Atw-Twuwr (52:29), Sabaa (34:46), Yaasiyn (36:70), Al-Qalam (68:2), At-Takwiyr (81:22). Rejea pia Al-Furqaan (25:4), kwenye uchambuzi na maelezo bayana na rejea mbalimbali za sifa ovu kama hizo za mshairi na kahini zilizotajwa katika Aayah namba (41-42).

 

[13] Haqq Ya Yakini:

 

Haqq ya yakini (ukweli wa yakini) yaani: Kiwango cha juu cha ilimu, kwani kiwango cha juu cha ilimu ni yakini ambayo ni ilimu iliyo madhubuti, isiyoyumba wala kutetereka. Kuna viwango vitatu vya yakini, kila kimoja ni cha juu zaidi kuliko cha kabla yake: (i) Ilimu ya yakini, ambayo ni ilimu inayopatikana kutokana na khabari. (ii) Jicho la yakini, ambayo ni ilimu inayotambulika kwa maono na kuona. (iii) Ukweli wa yakini, ambao ni ujuzi unaotambulika kwa hisia ya kuonja na kuvaana na kitu.  

 

Na hivi ndivyo ilivyo Qur-aan Tukufu. Ilimu yote iliyomo humo inaungwa mkono na uthibitisho wa uhakika na dalili za wazi kabisa, na yeyote anayepitia hayo yaliyomo ya uhakika wa ujuzi wa imaan atapata yakini ya kweli. [Tafsiyr As-Sa’diy]

 

 

 

Share