089-Asbaabun-Nuzuwl: Al-Baqarah Aayah 089: وَلَمَّا جَاءَهُمْ كِتَابٌ مِّنْ عِندِ اللَّـهِ مُصَدِّقٌ لِّمَا مَعَهُمْ

 

أسْبابُ النُّزُول

Asbaabun-Nuzuwl

(Sababu Za Kuteremshwa Suwrah Na Aayaat Za Qur-aan)

Imekusanywa na: Alhidaaya.com

 

 

Al-Baqarah Aayah 89: Na kilipowajia Kitabu kutoka kwa Allaah kisadikishacho...

 

 

وَلَمَّا جَاءَهُمْ كِتَابٌ مِّنْ عِندِ اللَّـهِ مُصَدِّقٌ لِّمَا مَعَهُمْ وَكَانُوا مِن قَبْلُ يَسْتَفْتِحُونَ عَلَى الَّذِينَ كَفَرُوا فَلَمَّا جَاءَهُم مَّا عَرَفُوا كَفَرُوا بِهِ ۚ فَلَعْنَةُ اللَّـهِ عَلَى الْكَافِرِينَ ﴿٨٩﴾

89. Na kilipowajia Kitabu kutoka kwa Allaah kisadikishacho yale yaliyo pamoja nao, na japokuwa kabla ya hapo walikuwa wakiomba ushindi dhidi ya wale waliokufuru; basi yalipowajia yale waliyokuwa wakiyatambua waliyakanusha, basi laana ya Allaah iwe juu ya makafiri.

 

 

Sababun-Nuzuwl:

Aayah hii imeteremka kuhusu Mayahudi kama alivyohadithia ‘Aaswim bin ‘Umar bin Qataadah kuhusu watu katika kaumu yake ambao walisema: Katika ambayo yaliyotuitia katika Uislaam kwa Rahmah ya Allaah (تعالى), na Akaiongoza kwetu, ni pale tulipokuwa tukisikia kutoka Mayahudi, wakati sisi tulikuwa washirikina waabudu masanamu, na Ahlul-Kitaab walikuwa ndio wenye ‘ilmu tusiyokuwa nayo sisi. Na ikawa inaendelea shari baina yetu na wao, basi ilikuwa pale tunapopata (matatizo) kutoka kwao kwa baadhi ya waliyoyachukia, walituambia: Hivi karibuni anakaribia kutumwa Nabiy, basi sasa tutawaua mauwaji ya ‘Aad na Iram, na yeye atakuwa pamoja nasi. Ikawa tunasikia sana hilo. Kisha Allaah Alipomtuma Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  tukamuitikia alipotuitia kwa Allaah  (تعالى)na tukatambua waliyokuwa wakituahidi. Tukawakimbilia na tukamwamini, lakini wao wakamkanusha. Na hapo zikateremshwa Aayaat za Al-Baqarah kuwazungumzia wao: Na kilipowajia Kitabu kutoka kwa Allaah kisadikishacho yale yaliyo pamoja nao, na japokuwa kabla ya hapo walikuwa wakiomba ushindi dhidi ya wale waliokufuru; basi yalipowajia yale waliyokuwa wakiyatambua waliyakanusha, basi Laana ya Allaah iwe juu ya makafiri” (2: 89) [Amepokea Ibn Is-haaq katika Siyrah]

 

Sababun-Nuzuwl: Pia, Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما)  amehadithia kwamba: Mayahudi walikuwa wakimuomba Allaah (kuletwa kwa Nabiy Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) ili wapate ushindi juu ya (Qabila la) Aws na Khazraj kabla ya kutumwa kwake Nabiy. Kisha Allaah Alipomtuma kwa Waarabu, wakamkanusha na kukataa kwamba walikuwa wakimzungumza. Basi Mu’aadh bin Jabal na Bishr bin Al-Baraa bin Ma’ruwr kutoka Bani Salamah waliwaambia: Enyi Mayahudi! Mcheni Allaah na ingieni katika Uislamu, kwani mlikuwa mkimuomba Allaah kuja kwa Muhammad wakati sisi tulikuwa bado makafiri na nyinyi mlikuwa mkituambia kwamba atatumwa na mkatuelezea sifa zake kwetu. Salaam bin Mushkim kutoka Bani An-Nadhwiyr akajibu: Hakuleta lolote tunalolitambua, wala si yeye ambaye tulikuwa tukikutajieni. Hapo Allaah Akateremsha Aayah kuhusu kauli yao. Na kilipowajia Kitabu kutoka kwa Allaah kisadikishacho yale yaliyo pamoja nao… (2:89) [Ameipokea Ibn Ishaaq- Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

Share