158-Asbaabun-Nuzuwl: Al-Baqarah Aayah 158: إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَائِرِ اللَّـهِ

 

أسْبابُ النُّزُول

Asbaabun-Nuzuwl

(Sababu Za Kuteremshwa Suwrah Na Aayaat Za Qur-aan)

Imekusanywa na: Alhidaaya.com

 

 

 

Al-Baqarah Aayah 158: Hakika Asw-Swafaa na Al-Marwah ni katika alama za Allaah...

 

 

 إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَائِرِ اللَّـهِ ۖ فَمَنْ حَجَّ الْبَيْتَ أَوِ اعْتَمَرَ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِ أَن يَطَّوَّفَ بِهِمَا ۚ وَمَن تَطَوَّعَ خَيْرًا فَإِنَّ اللَّـهَ شَاكِرٌ عَلِيمٌ ﴿١٥٨﴾

158. Hakika Asw-Swafaa na Al-Marwah ni katika alama za Allaah. Basi yeyote anayehiji kwenye Nyumba hiyo au akatekeleza ‘Umrah basi hakuna lawama kwake kutufu (vilima) viwili hivyo. Na atakayejitolea kufanya khayr basi hakika Allaah ni Mwenye kupokea shukurani, Mjuzi wa yote.

 

Sababun-Nuzuwl: 

 

Aayah hii imeteremka kuwazungumzia baadhi ya Swahaba (رضي الله عنهم) ambao walihisi uzito Kutufu baina ya Swafaa na Marwah, kwa sababu (Kutufu huko) kulikuwa ni katika ‘ibaadah za enzi ya jaahiliyyah. Washirikina walikuwa wameweka sanamu lao linaloitwa Manaat, wakiliabudu, wakilifanyia Hijjah ya kijahiliyyah na wakilizunguka. Ulipokuja Uislamu walimuuliza Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu hilo. Ndipo hapo Allaah Akateremsha Aayah hii (2:158) [Al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها)].  Rejea Utangulizi wa Tarjama, tanbihi katika Kufasiri Qur-aan kwa kauli za Swahaba  (رضي الله عنهم).

 

Pia, sababu nyingine ni pale iliposhuka Aayah inayoamrisha Kutufu Al-Ka’bah. Ilikuwa haikutajwa katika Qur-aan Kutufu Swafaa na Marwah. Swahaba wakasema: Ee Rasuli wa Allaah! Tulikuwa tunatufu Swafaa na Marwah, na Allaah Ameteremsha kuhusu Kutufu Nyumba (Al- Ka’bah). Basi je itakuwa dhambi kwetu Kutufu Swafaa na Marwah? Hapo Allaah Akateremsha Aayah hii: Hakika Asw-Swafaa na Al-Marwah ni katika Alama za Allaah…” (2:158) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Pia ‘Aaswim bin Sulaymaan (رضي الله عنه)  amehadithia kwamba: Nilimuuliza Anas bin Maalik   (رضي الله عنه)  kuhusu Swafaa na Marwah, akasema: Tulikuwa tunaona kuwa hilo ni jambo la ujaahiliyyah. Kisha ulipokuja Uislamu tukazuia  Kutufu Vilima Viwili hivyo) ndipo Allaah (سبحانه وتعالى) Akateremsha: Hakika Asw-Swafaa na Al-Marwah ni katika Alama za Allaah…” (2:158) [Al-Bukhaariy]

 

 

 

 

Share