Je Sisi Hatuko Ukingoni Mwa Shimo La Moto?
Hebu tuhisi nini kilitokea nyoyoni mwa Maswahaba wa Mtume (sallallahu alayhi wa sallam) pale waliposikia aya hii waliyosomewa kwa kinywa kitukufu cha Mtume?
“Enyi mlioamini! mcheni MwenyeziMungu kama ipasavyo kumcha; wala msife isipokuwa mmekwishakuwa Waislamu kamili. Na shikamaneni kwa kamba (dini) ya MwenyeziMungu nyote, wala msiachane. Na kumbukeni neema ya MwenyeziMungu iliyo juu yenu. Mlikuwa maadui; naye akaziunganisha nyoyo zenu; hivyo, kwa neema yake, mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto (wa Jahannam), Naye akakuokoeni nalo. Namna hii MwenyeziMungu anakubainishieni Aya zake ili mpate kuongoka.” (3:102-103).
Kabla ya ujumbe wa Uislamu, Uarabuni lilikuwa ni eneo la kutisha, eneo la vurugu na eneo lililoporomoka kimaadili. Makabila yalidumu na uhuru wa kutokuwa na mamlaka yoyote kuu ya kisiasa.
Moja ya taathira mbaya za uhuru huu wa kutokuwa na mamlaka moja ya juu ilikuwa ni ukatili wa kutothamini uhai wa mwanadamu, achilia mbali mali isipokuwa tu mtu labda awe na nasaba na kabila fulani.
Usemi mmoja mashuhuri unaoelezea hali ya mambo katika zama za ujahili unasema hivi: “Mimi niko dhidi ya ndugu yangu, naye kaka yangu yuko dhidi ya binamu zangu, na ndugu na binamu zangu wako dhidi ya mgeni.”
Waliweza kuraruana kwa ajili tu ya maji tu ya kunyweshea wanyama yaliyotekwa kwenye kisima cha mwingine na ugomvi ukaweza kugeuka vita kati ya makabila na makundi. Ugomvi huo ukaendelea hata kwa miaka ukiteketeza jamii ya wanaume wa Arabuni.
Badala ya kujutia jambo hilo, wenyewe walijisifu kwa vita hivyo katika mashairi yao. Hata hivyo, walikuwa ni mashujaa wakubwa ambao walikuwa na sifa muhimu za ujasiri, uhuru, ukarimu na zaidi ya hivyo walikuwa na nyoyo madhubuti zilizokuwa na ukaribu wa ndani na nguvu ya maumbile na zilizoweza kuitakidi jambo na kufa kwa ajili ya jambo hilo.
Lakini nguvu zao zote zilitumika katika mapambano ya wenyewe kwa wenyewe, zikatumika kumsababishia kila mmoja wao moto ambapo wanyonge wakawa chakula cha wababe na asusa ya wenye uwezo
Ni katika zama hizo, MwenyeziMungu, Mwingi wa Rehema, akataka kusamehe makosa ya watu duniani na akawashushia Rehema Yake ya mwisho kwa njia ya mwanadamu aliyebeba ujumbe.
Kwa hekima yenye mvuto, tabia njema na kwa imani isiyoyumba, mtu huyu akaziunganisha nyoyo korofi za watu wake kwa ajili ya kuzisalimisha kwa Mungu Mmoja. Majeshi katili ambayo yalielekeana kupambana, sasa yakaungana pamoja kwa udugu wa Kiislamu.
Mmoja baada ya mwingine, polepole, hatua kwa hatua, watu wakafundishwa kufikiri, kuzungumza na kujiadabisha kwa namna nyingine kabisa. Yakadhihiri mageuzi makubwa na yaliyodumu muda mrefu ambayo mfano wake dunia haijauona tena na kamwe haitauona tena.
Ni kwa msukumo gani nyoyo hizi za waasi, wakorofi na watu wa ajabu ziliweza kufungamanishwa pamoja namna hiyo? Zikashikamanishwa kikamilifu namna hiyo?
Kwa mtu wa nje aliyezitazama nyoyo hizo, hakuna jambo ambalo kwake lingeonekana kuwa muhali kusadikika kama yale maisha mapya ya kila mmoja kumuelekea mwingine, kuelekeana kwa watu wa makabila yaliyokuwa na upinzani ambao, yawezekana, baba zao waliuwana katika zama za ujahili na ndugu zao walitesana.
Badala ya uhasama na vita vya kikatili, wakawa na hali nyingine tofauti kabisa kana kwamba nguvu za kimiujiza zilibadili undani wao. Hapa sasa hebu irejee tena kauli ya MwenyeziMungu, Mwingi wa Rehema na zingatia ni kwa kiasi gani iliwatetemesha maswahaba,
“Na kumbukeni neema ya MwenyeziMungu iliyo juu yenu, mlikuwa maadui, Naye akaziunganisha nyoyo zenu, hivyo, kwa neema Yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto (wa Jahannam), Naye akakuokoeni nalo.(3:103)
Hivi leo, Waislamu duniani kote, wamegawanyika kwa mambo mengi. Baadhi ya mambo hayo ni ya kimaumbile kama vile lugha na utamaduni, na wengine wanajibagua kwa misingi ya kiitikadi na kidini.
Hata katika ulimwengu wa Magharibi ambako Waislamu ni wachache na huku wakiandamwa na kubaguliwa na kwa hali hiyo wana kila sababu ya kuachana na tofauti za kilugha, kiutamaduni na kidini na kuungana kwa kamba moja, eti bado huko nako kuna mgawanyiko mbaya sana miongoni mwa Waislamu!
Kitamathali, na hatujaalii kwa maana halisi, “tuko ukingoni mwa shimo la Moto”. Hitajio letu kubwa kabisa hivi leo ni kutafuta njia za kuungana na kujenga madaraja miongoni mwetu, kati ya kundi moja na jingine.
Badala ya muda wote kutumia bongo zetu kwa ajili kutafutana kasoro miongoni mwetu ndugu wa Kiislamu, tuvumiliane na kusameheana kasoro zetu. Tunahitajika kuelekeana na kuelewana.
Kila Umoja una msingi wake
Lakini kuna changamoto moja hapa. Umoja wowote ule, mshikamano wowote ule, mapenzi yoyote yale, na maelewano yoyote yale lazima yawe na msingi wake na kadri msingi huo unavyokuwa imara ndivyo mafungamano nayo yanavyokuwa imara.
Kwetu sisi Waislamu, msingi wa mafungamano yetu ni utii wetu kwa MwenyeziMungu, mapenzi yetu kwake, mapenzi juu ya dini yake na juu ya Umma mzima wa Kiislamu huku tukizingatia kuwa siku moja sote tutasimama mbele Yake.
Umoja, maelewano na amani miongoni mwa watu ndiyo shabaha ya jamii yoyote ile hususan jamii ya Kiislamu. Kuifikia hali hii ni ishara ya Rehema za Allah kwa jamii hiyo.
MwenyeziMungu anasema,
“Na kama Mola wako angelipenda, angeliwafanya watu wote kuwa umati mmoja. (Angeliwapelekea wote kufuata kitu kimoja). Kwa hivyo wataendelea tu kuhitilafiana”. Isipokuwa wale ambao Mola wako amewarehemu na kwa (rehema) hiyo Mwenyezimungu amewaumba. Na litatimia neno la Mola wako: “Kweli kweli nitaijaza Jahanamu kwa majini na binadamu wote (walio wabaya).” (11:118-119).
Aya hii haina maana ya mgawanyiko bali ina maana ya kukhitalifiana na kutofautiana mambo ambayo kuwepo kwake ni ishara ya rehema ya MwenyeziMungu. Inazungumzia mambo mawili muhimu kuhusiana na tofauti za kidini na kiitikadi.
Si khitilafu na tofauti zote zinazoweza kuondoshwa miongoni mwa watu ulimwenguni. Lakini, kama watu watajisalimisha kikwelikweli kwa MwenyeziMungu, jambo hilo huwa msingi wa umoja ikiwa ni rehema ya Allah.
Akiifafanua aya hii, Ibn Jariir at-Tabari ameeleza katika tafsiri yake kuwa al-Hasan al-Basri amesherehesha kuwa, ‘watu wenye kustahiki rehema za MwenyeziMungu ni wale wasiotofautiana kwa namna ya kuwavuruga.’ Na kwamba Ibn Abbas amesema, ‘MwenyeziMungu kawaumba katika makundi mawili; moja ni la wale wapatao rehema ili wasifarakiane, na jingine ni la wale wasiopata rehema ili wafarakane.
Mitume wote waliwaita watu katika umoja na mshikamano. Akielezea jukumu la Mitume, Imam al-Baghawi amesema, “MwenyeziMungu katuma Mitume wote kusimamisha dini na kuwaleta watu katika jamii moja kuondosha utengano na mfarakano.
Tofauti, mgawanyiko na majadiliano
Tofauti za rai ni kitu cha kawaida na cha lazima. Tofauti hizi zinapokuwa bora, na zinapokuwa na nidhamu na msingi mmoja ambao kila mmoja anauheshimu, basi huitwa khitilafu.
Tofauti zinapoleta fitina, uhasama, makundi na utengano, na zinapovuruga na kuponda misingi ya makubaliano, husababisha mgawanyiko, mfarakano na makundi.
Kwa kuzingatia mafundisho ya Qur’an, wanazuoni wa Kiislamu siku zote wamezitaja na kuzikubali tofauti hizi ambazo baadhi ya wanazuoni hao huziita al-Ikhtilaf at-Tanawwu.(khitilafu ya kutofautiana)
Kwa upande mmoja, MwenyeziMungu na Mtume wake wameonya vikali juu ya mfarakano na utengano ambao unaitwa al-Ikhtilaf at-Tadhdhad (khitilafu ya kufarakana).
Kuna masharti mawili ya kuzuia khitilafu zisilete mfarakano na mgawanyiko; (i) kuchunga misingi ya makubaliano (maafikiano) yaani misingi ya imani inayokubaliwa na wote. (ii) kuacha jukwaa wazi kwa ajili ya majadiliano yenye heshima na uadilifu.
Kuunganisha watu kwa ajili ya Allah
Mafanikio makubwa ya Mtume sallallahu alayhi wa sallam ambayo MwenyeziMungu amemsifu kwayo katika Qur’an ni kwamba, mbali ya kufikisha ujumbe wa MwenyeziMungu, aliweza kuzikamata nyoyo za watu na kujenga mapenzi na umoja miongoni mwao.
“Basi kwa sababu ya rehema itokayo kwa MwenyeziMungu umekuwa laini kwao. Na kama ungekuwa mkali na mwenye moyo mgumu, bila shaka, wangekukimbia. Basi wewe wasamehe na uwaombee msamaha (kwa MwenyeziMungu).....” (3:159).
Mtume sallallahu alayhi wa sallam amekataza na amejitahidi katika maisha yake yote kuondosha chuki na mfarakano miongoni mwa Waumini. Labda mtu anaweza kuuliza hapa, “kwanini isiwe miongoni mwa wanadamu wote?”
Kwa kweli kazi na kusudio la Mtume lilikuwa ni kuwaunganisha wanadamu wote, lakini kuwaunganisha huko ni kwa ajili ya Allah, waungane kwa jina la Allah na kwa ajili ya Allah.
Lakini kama watu walimkadhibisha Allah waziwazi baada ya kupokea ujumbe Wake, basi hapo hapakuwa na msingi wa kujengea umoja. Bali tu yangebakia maisha ya kukaa pamoja kwa kuheshimiana ili njia za kujadiliana na kulinganiana zibakie wazi
Lakini mazingatio yetu katika makala hii, kimsingi, yanaelekezwa kwa wale waliohiyari kuamini na kujinasibu na Umma wa Kiislamu. Misingi miwili ya umoja iliyotajwa mwanzo: kuimarisha imani moja na kustahamilia khitilafu ndiyo ilikuwa sifa kuu ya ulinganiaji ya Mtume sallallahu alayhi wa sallam.
Abu Huraira amesimulia kuwa Mtume wa MwenyeziMungu kasema, “Kwa hakika MwenyeziMungu Anakupendeleeni mambo matatu na hakupendeleeni mambo matatu. Anapenda ibada yenu kwake bila ya kumshirikisha, kwamba mshikamane kwa Kamba ya MwenyeziMungu na kwamba msitengane vikundi-vikundi (msigawanyike). Na hapendi kwenu, utesi, mabishano na isirafu.”
Al-Harith al-Ash’ari amesimulia kuwa Mtume sallallahu alayhi wa sallam kasema, “MwenyeziMungu alimuamrisha Yahya ibn Zakariya kufanya mambo matano na awaamuru Bani Israili wayafanye,.. Nami nakuamrisheni mfanye mambo matano ambayo MwenyeziMungu ameniamrisha; (nayo ni); kusikiliza, kutii, kufanya jihad, kufanya Hijira na kuungana kuwa jamii moja, kwani yeyote anayeiacha jamii, amejivua kamba shingoni hadi airejee...”
Ibn Umar karipoti kuwa Umar aliwahutubia eneo la al-Jabiya akisema “enyi watu! Nasimama miongoni mwenu kama Mtume sallallahu alayhi wa sallam alivyosimama miongoni mwetu pale aliposema, “Nakunasihini muwafuate Maswahaba wangu, na wale watakaowafuata na wale watakaofuata baada ya hao. Lakini baada ya hapo utaenea urongo hadi mtu ataapa lakini kiapo chake hakitapokewa, shahidi atatoa ushahidi lakini ushahidi wake hautakubaliwa...lazima mdumu kama jamii moja na jihadharini na utengano kwani Shetani huwa pamoja na mtu mmoja na huwa mbali zaidi na watu wawili. Yeyote anayetamani starehe za Peponi basi aifuate jamii, na yeyote anayependa mema yake na kuyachukia mabaya yake huyo ni muumini (wa kweli).
Umoja ni sharti muhimu la imani
Fuqaha mashuhuri wa Hanafi, Abu Jafar at-Tahawi katika Kitabu chake “Aqiida at-Tahawiyyah” ambacho ni mashuhuri na kimekubaliwa na kuheshimiwa na madhehebu zote za Waislamu, amesema hivi:
“Sisi twauona umoja (miongoni mwa Waislamu) kuwa ndio Aqida Sahihi na utengano ni upotevu na laana.
Ndiyo sababu wengi miongoni mwa Waislamu huitwa Ahlus Sunna wal Jama’a yaani watu wanaofuata Sunna na kuupa umuhimu umoja na ustawi wa jamii.
Imam Malik amesema: “wema unalemea katika kuwafuata wachaMungu waliotangulia, kuzidisha elimu na ufahamu wa Hadith za Mtume, kushikamana kwa kamba ya MwenyeziMungu, kufuata chochote kinachojenga ujamaa na urafiki na kuepuka chochote kinacholeta mfarakano na utengano isipokuwa kama kinahusu jambo la wazi ambalo MwenyeziMungu na Mtume wake wameliamrisha.
An-Numan ibn Bashiir amesimulia kuwa Mtume wa MwenyeziMungu kasema; “Kuzungumzia neema za Allah ni shukurani na kutofanya hivyo ni ukosefu wa shukurani. Yule asiyeshukuru kwa kidogo hatashukuru kwa kikubwa na yule asiyewashukuru watu, hamshukuru MwenyeziMungu. Jamaa ni neema na utengano ni laana”
Abdullah bin Masoud kasema “Enyi watu! Dumuni na utii na ishikeni jamaa kwani, hii, kimsingi, ndiyo njia ya kufuata kamba ya MwenyeziMungu ambayo ameamrisha kuifuata na jihadharini kuwa chochote ambacho, yawezekana msikipende katika jamaa ni bora kuliko kile mnachoweza kukipenda katika utengano.”
Katika kile kipindi cha kuanguka kwa Waislamu pale vita vya wenyewe kwa wenyewe miongoni mwa viongozi ambapo Waislamu wengine wakaungana na Wakristo dhidi ya ndugu zao Waislamu hali iliyopelekea wafalme wa kikristo kuwashinda Waislamu.
Ibn Abdul Barr, mwanazuoni wa Malik wa Hispania, kasema, “Migawanyiko inayotokea katika Umma miongoni mwa wanazuoni, Masheikh, Maimamu na watu mashuhuri ndiyo ambayo imewawezesha wengine kutawala (duniya). Zaidi ya hivyo huo ni uasi kwa MwenyeziMungu na Mtume Wake.
MwenyeziMungu anasema, “Na kwa wale waliosema: “sisi ni Wakristo,” Tulichukua ahadi kwao, lakini wakaacha sehemu(kubwa) ya yale waliyokumbushwa, kwa hivyo, tukaweka baina yao uadui na bughudha mpaka Siku ya Kiama. Na MwenyeziMungu atawaambia waliyokuwa wakiyafanya.” (5:14).
Kama walivyokuwa watu wa Kitabu waliopita kabla yetu, MwenyeziMungu anatuwaidhi tujihadhari kuwa watu wanapouacha muongozo wa MwenyeziMungu na hukumu Zake na kuona kuwa wanaweza kufanya mambo yao bila ya vitu hivyo, uadui na chuki huwaingia na kuwafanya waishie katika ufisadi na upotevu. Lakini wakiungana, hufanikiwa na kushika uongozi kwani umoja ni rehema na utengano ni laana.”
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


