33-Imaam Ibn 'Uthaymiyn: Ana Umri Wa Sitini Na Tano Sasa Anapata Damu Inayoendelea Miaka Mitatu Nini Hukmu Ya Swawm?

 

 

Fataawaa Mas-ala 60 Kuhusu Hedhi Na Nifaas

 

33-Ana Umri Wa Sitini Na Tano Sasa Anapata Damu Inayoendelea Miaka Mitatu

Nini Hukmu Ya Swawm?

 

Imaam Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu-Allaah)

 

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

 

Nina mama yangu mzazi mwenye umri wa miaka sitini na tano na ana muda wa miaka ipatayo kumi na tisa hajapata mtoto na sasa hivi damu inamtoka yapata muda wa miaka mitatu. Hivi inaelekea maradhi haya aliyapata wakati ule na hivi karibuni kuna Swiyaam je unamnasihi nini au tufanye nini?

 

 

JIBU:

 

Katika hali hii kwa mwanamke huyu ambaye amepatwa damu ya kuendelea, hukmu yake ni kuacha Swalaah na Swawm kwa muda wa ada yake ya zamani kabla ya kutokea kwa tukio hili. Kwa mfano, ikiwa hedhi yake ilikuwa inamjia mwanzo wa mwezi kwa muda wa siku sita, basi itabidi akae siku sita ya kila mwanzo wa mwezi asiswali na asifunge. Baada ya siku hizo kumalizika akoge na aswali na afunge.

 

Namna ya Swalaah kwa huyu na mfano wake ni: Kuosha sehemu zake za siri vizuri sana na atawadhe wakati ule inapoingia wakati wa Swalaah ya faradhi, na kwa hali hii ili kuondosha mashaka juu yake ni kujumuisha Swalaah ya Adhuhuri na Alasiri na Maghribi pamoja na ‘Ishaa, ili iwe kufanya kwake hivi,  ni moja kwa Swalaah zake mbili; Swalaah ya Adhuhuri na Alasiri, na moja kwa ajili ya Swalaah ya Magharibi na ‘Ishaa na moja kwa ajili ya Swalaah ya Alfajiri; badala ya kufanya hivyo mara tano kwa siku, atafanya mara tatu tu.

 

Narejea kusema tena kwa mara ya pili: Anapotaka kujitoharisha atakosha sehemu zake za siri vizuri na kukausha kwa nje kwa kipande cha nguo au mfano wake hadi nje pakauke, kisha atatawadha na kuswali. Ataswali Adhuhuri rakaa nne, Alasiri rakaa nne, Maghrib tatu, ‘Ishaa nne na Alfajiri mbili, na hatopunguza Swalaah kwa kufupisha kama wanavyodhani baadhi ya watu. (Bali kuunganisha zikiwa kamilifu).

 

 

Hata hivyo inajuzu kukusanya Adhuhuri na Alasiri, Maghrib na ‘Ishaa. Adhuhuri na Alasiri ima iwe kutanguliza au kuchelewesha na kadhalika Maghrib na ‘Ishaa kwa kutanguliza au kuchelewesha na akitaka kuswali Sunnah kwa udhu huu hakuna neno.

 

Share