051-Riyaadhw Asw-Swaalihiyn: Mlango Wa Kuwa na Matumaini

 

Riyaadhw Asw-Swaalihiyn

 

باب الرجاء

051-Mlango Wa Kuwa na Matumaini

 

Alhidaaya.com

 

قَالَ الله تَعَالَى:

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٥٣﴾

Sema: Enyi waja Wangu ambao wamepindukia mipaka juu ya nafsi zao: Msikate tamaa na rahmah ya Allaah; hakika Allaah Anaghufuria dhambi zote; hakika Yeye Ndiye Mwenye kughufuria, Mwenye kurehemu. [Az-Zumar: 53]

 

وَهَلْ نُجَازِي إِلَّا الْكَفُورَ ﴿١٧﴾

Na Hatuadhibu isipokuwa anayekufuru. [Sabaa: 17]

 

إِنَّا قَدْ أُوحِيَ إِلَيْنَا أَنَّ الْعَذَابَ عَلَىٰ مَن كَذَّبَ وَتَوَلَّىٰ ﴿٤٨﴾

Hakika tumefunuliwa Wahy ya kwamba adhabu itakuwa kwa yule atakayekadhibisha na akakengeuka. [Twaahaa: 48]

 

وَرَحْمَتِي وَسِعَتْ كُلَّ شَيْءٍ ۚ  ﴿١٥٦﴾

Na rahmah Yangu imeenea kila kitu. [At-A'raaf: 106]

 

 

 

Hadiyth – 1

وعن عبادة بن الصامتِ رضي الله عنه، قَالَ : قَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم  : (( مَنْ شَهِدَ أنَّ لا إلهَ إلاَّ اللهُ وَحْدَهُ لا شَرِيكَ لَهُ ، وَأنَّ مُحَمداً عَبْدهُ ورَسُولُهُ ، وَأنَّ عِيسى عَبْدُ اللهِ وَرَسُولُهُ وَكَلِمَتُهُ ألْقَاهَا إِلَى مَرْيَمَ ورُوحٌ مِنْهُ ، وَأنَّ الجَنَّةَ حَقٌّ ، وَالنَّارَ  حَقٌّ ، أدْخَلَهُ اللهُ الجَنَّةَ عَلَى مَا كَانَ مِنَ العَمَلِ )) مُتَّفَقٌ عَلَيهِ .

وفي رواية لمسلم : (( مَنْ شَهِدَ أنْ لا إلَهَ إلاَّ اللهُ وَأنَّ مُحَمَّداً رَسُولُ اللهِ ، حَرَّمَ اللهُ عَلَيهِ النَّارَ )) .

Imepokewa kutoka kwake 'Ubaadah bin Saamit (Radhwiyah Allaahu 'anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mwenye kushuhudia kuwa hapana apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allaah Peke Yake hana mshirika, kuwa Muhammad ni mja na Rasuli Wake, na kuwa 'Iysa ni mja wa Allaah na Rasuli Wake, na ni Neno Lake Alilotia kwa Maryam na roho toka kwake, na kuwa Pepo ni kweli, na Moto ni kweli, Allaah atamwingiza Peponi kwa amali alizokuwa akifanya." [Al-Bukhaariy na Muslim]

Katika riwaayah ya Muslim: "Mwenye kushuhudia kuwa hapana Mola isipokuwa Allaah, na kuwa Muhammad ni Rasuli wa Allaah, Allaah atamharamishia Moto."

 

 

 

Hadiyth – 2

وعن أَبي ذررضي الله عنه، قَالَ : قَالَ النَّبيّ صلى الله عليه وسلم : (( يقول الله (عزّ وجلّ) : مَنْ جَاء بالحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أمْثَالِهَا أَوْ أزْيَد ، وَمَنْ جَاءَ بالسَيِّئَةِ فَجَزاءُ سَيِّئَةٍ سَيِّئَةٌ مِثْلُهَا أَوْ أغْفِرُ . وَمَنْ تَقَرَّبَ مِنِّي شِبْراً تَقَرَّبْتُ مِنْهُ ذِرَاعاً ، وَمَنْ تَقَرَّبَ مِنِّي ذِرَاعاً تَقَرَّبْتُ مِنْهُ بَاعاً ، وَمَنْ أتَانِي يَمْشِي أتَيْتُهُ هَرْوَلَةً ، وَمَنْ لَقِيني بِقُرَابِ الأرْض خَطِيئةً لا يُشْرِكُ بِي شَيئاً ، لَقِيتُهُ بِمِثْلِهَا مَغفِرَةً )) رواه مسلم .

Imepokewa kutoka kwa Abu Dharr (Radhwiyah Allaahu 'anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: Amesema Allaah Ta'aalaa: "Mwenye kuleta jema atapata mara kumi mfano wake au zaidi, na Mwenye kuleta ovu, malipo yake ni uovu mfano wake au Namsamehe. Na Mwenye kunikaribia kwa shubiri, Nitamkaribia kwa dhiraa. Na mwenye kunikaribia kwa kutembelea, Nitamjia kwa kukimbia, Mwenye kukutana nami kwa madhambi ujazo wa ardhi, na asinishirikishe na chochote, Nitakutana naye kwa msamaha kama huo." [Muslim] 

 

 

Hadiyth – 3

وعن جابر رضي الله عنه، قَالَ : جاء أعرابي إِلَى النَّبيّ صلى الله عليه وسلم ، فَقَالَ: يَا رَسُول الله ، مَا الموجِبَتَانِ؟ قَالَ : (( مَنْ مَاتَ لاَ يُشْرِكُ بالله شَيئاً دَخَلَ الجَنَّةَ ، وَمَنْ مَاتَ يُشْرِكُ بِهِ شَيْئاً دَخَلَ النَّار )) رواه مسلم .

Imepokewa kutoka kwa Jaabir (Radhwiyah Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Alikuja Bedui kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alahi wa aalihi wa sallam) na kuuliza: "Ee Rasuli wa Allaah! Ni vitu gani viwili vinavyomfanya mtu aingie Peponi au Motoni?" Akasema (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Yeyote anayekufa hakumshirikisha Allaah na chochote ataingia Peponi na mwenye kuaga dunia huku anamshirikisha Allaah basi ataingia Motoni." [Muslim]

 

 

Hadiyth – 4

وعن أنس رضي الله عنه : أن النَّبيّ صلى الله عليه وسلم  ومعاذ رديفه عَلَى الرَّحْل ، قَالَ : (( يَا مُعَاذُ )) قَالَ : لَبِّيْكَ يَا رَسُول الله وَسَعْدَيْكَ ، قَالَ : (( يَا مُعَاذُ )) قَالَ : لَبَّيْكَ يَا رَسُول الله وَسَعْدَيْكَ ، قَالَ : (( يَا مُعَاذُ )) قَالَ : لَبِّيْكَ يَا رَسُول الله وسَعْدَيْكَ ،   ثَلاثاً ، قَالَ : (( مَا مِنْ عَبْدٍ يَشْهَدُ أن لا إلهَ إلاَّ الله ، وَأنَّ مُحَمَّداً عَبْدُهُ وَرَسُولُهُ صِدْقاً مِنْ قَلْبِهِ إلاَّ حَرَّمَهُ الله عَلَى النَّار )) قَالَ : يَا رَسُول الله ، أفَلاَ أخْبِرُ بِهَا النَّاس فَيَسْتَبْشِروا ؟ قَالَ : (( إِذاً يَتَّكِلُوا )) فأخبر بِهَا مُعاذٌ عِنْدَ موتِه تَأثُّماً . مُتَّفَقٌ عَلَيهِ .

Imepokewa kutoka kwa Anas (Radhwiyah Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Mu'aadh akiwa nyuma yake, wakiwa juu ya kipndo, aliita: "Ee Mu'aadh!" Naye akajibu: "Labbaika Ee Rasuli wa Allaah wa Sa'dayka." Aliita (tena): "Ee Mu'aadh!" Naye akajibu: "Labbaika Ee Rasuli wa Allaah wa Sa'dayka." (Aliita hivi) mara tatu, kisha akasema: "Hakuna yeyote anayekiri kwa moyo na akatamka kwa ulimi kuwa hakuna Mola anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Allaah na Muhammad ni mja na Rasuli wa Allaah kwa ukweli wa moyo wake isipokuwa Allaah Atamharamishia moto." Akasema: "Ee Rasuli wa Allaah niwaeleze watu kwa hilo wakafurahi?" Akanijibu: "Kama utawaambia watabweteka!" Na hilo Mu'aadh alilieleza wakati wa kufa kwake kwa kuhofia kupata dhambi (ya kuficha mafundisho)." [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Hadiyth – 5

وعن أَبي هريرة رضي الله عنه- أَوْ أَبي سعيد الخدري رضي الله عنهما - شك الراوي - ولا يَضُرُّ الشَّكُّ في عَين الصَّحَابيّ ؛ لأنَّهُمْ كُلُّهُمْ عُدُولٌ – قَالَ : لَمَّا كَانَ غَزوَةُ تَبُوكَ ، أصَابَ النَّاسَ مَجَاعَةٌ ، فقالوا : يَا رَسُول الله ، لَوْ أذِنْتَ لَنَا فَنَحرْنَا نَواضِحَنَا فَأكَلْنَا وَادَّهَنَّا ؟ فَقَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم: (( افْعَلُوا )) فَجاء عُمَرُ رضي الله عنه ، فَقَالَ : يَا رَسُول الله ، إنْ فَعَلْتَ قَلَّ الظَّهْرُ ، وَلَكِن ادعُهُمْ بفَضلِ أزْوَادِهِمْ ، ثُمَّ ادعُ الله لَهُمْ عَلَيْهَا بِالبَرَكَةِ ، لَعَلَّ الله أنْ يَجْعَلَ في ذلِكَ البَرَكَةَ . فَقَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم : (( نَعَمْ )) فَدَعَا بِنَطْع فَبَسَطَهُ ، ثُمَّ دَعَا بِفضلِ أزْوَادِهِمْ ، فَجَعَلَ الرَّجُلُ يَجيءُ بكَفّ ذُرَة وَيَجيءُ بِكَفّ تمر وَيجيءُ الآخرُ بِكِسرَة حَتَّى اجْتَمَعَ عَلَى النّطعِ مِنْ ذلِكَ شَيء يَسيرٌ ، فَدَعَا رَسُول الله صلى الله عليه وسلم بِالبَرَكَةِ ، ثُمَّ قَالَ : (( خُذُوا في أوعِيَتِكُمْ )) فَأَخَذُوا في أوْعِيَتهم حَتَّى مَا تَرَكُوا في العَسْكَرِ وِعَاء إلاَّ مَلأوهُ وَأَكَلُوا حَتَّى شَبعُوا وَفَضَلَ فَضْلَةٌ فَقَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم : (( أشْهَدُ أنْ لا إلهَ إلاَّ اللهُ وَأنّي رَسُولُ الله ، لا يَلْقَى الله بِهِما عَبْدٌ غَيْرَ شَاكٍّ فَيُحْجَبَ عَنِ الجَنَّةِ )) رواه مسلم .

Imepokewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiyah Allaahu 'anhu) au Abu Sa'iid Al-Khudriy (Radhwiyah Allaahu 'anhu), mpokezi ana shaka na wala shaka haidhuru katika Swahaba yoyote, kwani wote ni waadilifu: "Ilipokuwa Vita vya Taabuk, watu walipatwa na njaa, wakasema: "Ee Rasuli wa Allaah! Lau ungeruhusu kuchinja ngamia wetu, tule na kutumia mafuta yake." Akasema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Fanyeni hivyo." Akaja 'Umar (Radhwiyah Allaahu 'anhu) na kusema: "Ee Rasuli wa Allaah! Ikiwa tutafanya hivyo vipando vitapungua, lakini waitishe chakula chao cha ziada, Kisha muombe Allaah awabarikie hicho. Huenda Allaah akawatilia baraka." Akasema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Ndio." Akaitisha busati la ngozi akalitandika, kisha akaomba watu walete vyakula vilivyozidi. Watu wakaleta vyakula, mtu analeta kifumba cha mahindi, mwingine analeta tende, mwingine analeta kipande cha mkate, Vyakula hivyo vikakusanywa katika busati hilo. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akakiombea baraka, kisha akasema: "Chukueni katika vyombo vyenu." Wakachukua katika vyombo vyao, hadi hakukubakia chombo katika kambi isipokuwa wakajaza vyombo vyao vyote katika kambi. Hapo wakala mpaka wakashiba, kingine kikabaki. Akasema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Nashuhudia ya kwamba hapana Mola isipokuwa Allaah, na mimi ni Rasuli wa Allaah. Hatokutana mja na Allaah akiwa na kauli hizi mbili na hana shaka yoyote, kisha akazuiwa kuingia Peponi." [Muslim]

 

 

 

Hadiyth – 6

وعن عِتْبَانَ بن مالك رضي الله عنه وَهُوَ مِمَّن شَهِدَ بَدراً ، قَالَ : كنت أُصَلِّي لِقَوْمِي بَني سَالِم ، وَكَانَ يَحُولُ بَيْنِي وبَيْنَهُمْ وَادٍ إِذَا جَاءتِ الأَمْطَار ، فَيَشُقُّ عَلَيَّ اجْتِيَازُهُ قِبَلَ مسْجِدِهم ، فَجِئتُ رسولَ الله صلى الله عليه وسلم فقلت لَهُ : إنّي أنْكَرْتُ بَصَرِي وَإنَّ الوَادِي الَّذِي بَيْنِي وبَيْنَ قَومِي يَسيلُ إِذَا جَاءتِ الأمْطَارُ فَيَشُقُّ عَلَيَّ اجْتِيَازُهُ فَوَدِدْتُ أنَّكَ تَأتِي فَتُصَلِّي في بَيْتِي مَكَاناً أتَّخِذُهُ مُصَلّى ، فَقَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم : (( سَأفْعَلُ )) فَغَدَا رسولُ الله صلى الله عليه وسلم وَأَبُو بكر رضي الله عنه بَعْدَ مَا اشْتَدَّ النَّهَارُ ، وَاسْتَأذَنَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم فَأذِنْتُ لَهُ ، فَلَمْ يَجْلِسْ حَتَّى قَالَ : (( أيْنَ تُحِبُّ أنْ أُصَلِّيَ مِنْ بَيْتِكَ ؟ )) فَأشَرْتُ لَهُ إِلَى المَكَانِ الَّذِي أُحبُّ أنْ يُصَلِّيَ فِيهِ ، فَقَامَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم فَكَبَّرَ وَصَفَفْنَا وَرَاءَهُ فَصَلَّى رَكعَتَينِ ثُمَّ سَلَّمَ وَسَلَّمْنَا حِينَ سَلَّمَ فَحَبَسْتُهُ عَلَى خَزيرَةٍ تُصْنَعُ لَهُ ، فَسَمِعَ أهلُ الدَّارِ أنَّ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم في بَيْتِي فَثَابَ رِجالٌ مِنْهُمْ حَتَّى كَثُرَ الرِّجَالُ في البَيْتِ ، فَقَالَ رَجُلٌ : مَا فَعَلَ مَالِكٌ لا أرَاهُ ! فَقَالَ رَجُلٌ : ذلِكَ مُنَافِقٌ لا يُحِبُّ الله ورسولَهُ ، فَقَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم : (( لا تَقُلْ ذلِكَ ، ألاَ تَرَاهُ قَالَ : لا إلهَ إلاَّ الله يَبْتَغي بذَلِكَ وَجهَ الله تَعَالَى )) فَقَالَ : اللهُ ورسُولُهُ أعْلَمُ أمَّا نَحْنُ فَوَاللهِ مَا نَرَى وُدَّهُ وَلاَ حَدِيثَهُ إلاَّ إِلَى المُنَافِقينَ ! فَقَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم : (( فإنَّ الله قَدْ حَرَّمَ عَلَى النَّارِ مَنْ قَالَ : لا إلهَ إلاَّ الله يَبْتَغِي بذَلِكَ وَجْهَ الله )) مُتَّفَقٌ عَلَيهِ .

Imepokewa kutoka kwa 'Itbaan bin Maalik (Radhwiyah Allaahu 'anhu) miongoni mwa waliohudhuria Badr, amesema: Nilikuwa nikiswali na watu wangu Bani Saalim baina yangu na wao kuna bonde, mvua ikinyesha linafurika na huwa tabu kwangu kwenda msikitini. Nikaenda kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) nikasema: "Macho yangu ni dhaifu na bonde lililopo baina yangu na watu wangu linafurika ikinyesha mvua hivyo nashindwa kulivuka, Hivyo Napenda uje uswali nyumbani sehemu ninayotumia kuswalia." Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Akasema: "Nitafanya." Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaja na Abu Bakr (Radhwiyah Allaahu 'anhu) baada jua kuwa juu. Rasuli wa Allaah (Swallah Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akabisha nikamkaribisha, Hakukaa hadi akasema: "Ni wapi unapopenda niswali nyumbani kwako?" Nikamuashiria sehemu nilipenda aswali. Akasimama Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akapiga takbira tukasimama nyuma yake, Akaswali rakaa mbili kisha akatoa salamu, nasi tukatoa salamu baada yake. Nikamzuia kwa sababu ya chakula anachoandaliwa. Watu wa mji wakasikia kuwa Rasuli wa Allaah yupo nyumbani kwangu wakaja watu wengi hadi wakajaa nyumbani, Akasema mtu mmoja: "Maalik amefanya nini simuoni?" Akasema mwingine: "Yule ni mnafiki hampendi Allaah na Rasuli Wake." Akasema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Usiseme hivyo, kwani humuoni amesema Laa Ilaaha Illa Allaah akitaka radhi za Allaah Ta'aalaa?", Akasema: "Allaah na Rasuli Wake wanajua zaidi. Ama sisi hatuwaoni marafiki zake wala mazungumzo yake isipokuwa ya wanafiki." Akasema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Hakika amemharamishia moto mwenye kusema Laa Ilaaha Illa Allaah hatafuti kwa hilo isipokuwa radhi ya Allaah." [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

Hadiyth – 7

وعن عمر بن الخطاب رضي الله عنه ، قَالَ : قدِم رَسُول الله صلى الله عليه وسلم بسَبْيٍ فَإِذَا امْرَأةٌ مِنَ السَّبْيِ تَسْعَى ، إِذْ وَجَدَتْ صَبياً في السَّبْيِ أخَذَتْهُ فَألْزَقَتهُ بِبَطْنِهَا فَأَرضَعَتْهُ ، فَقَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم: (( أتَرَوْنَ هذِهِ المَرْأةَ طَارِحَةً وَلَدَها في النَّارِ ؟ )) قُلْنَا : لاَ وَاللهِ . فَقَالَ : (( للهُ أرْحَمُ بِعِبَادِهِ مِنْ هذِهِ بِوَلَدِهَا )) مُتَّفَقٌ عَلَيهِ.

Imepokewa kutoka kwa 'Umar bin Al-Khattaab (Radhwiyah Allaahu 'anhu) amesema: "Waliletwa mateka wa vita kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Kulikuwa na mwanamke akizunguka kutafuta mwanae. Akampata katika mateka akamchukua akamuweka tumboni mwake, akamnyonyesha. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: "Je, munamuona huyu mwanamke anaweza kumtia mtoto wake motoni?" Tukasema: "La! Wa-Allaahi." Akasema: "Allaah ana huruma zaidi kwa waja wake kuliko huyu kwa mtoto wake." [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Hadiyth – 8

وعن أَبي هريرة رضي الله عنه ، قَالَ : قَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم: (( لَمَّا خَلَقَ الله الخَلْقَ كَتَبَ في كِتَابٍ ، فَهُوَ عِنْدَهُ فَوقَ العَرْشِ : إنَّ رَحْمَتِي تَغْلِبُ غَضَبي )) .

وفي رواية : (( غَلَبَتْ غَضَبي )) وفي رواية : (( سَبَقَتْ غَضَبي )) مُتَّفَقٌ عَلَيهِ .

Imepokewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiyah Allaahu 'anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Pindi Allaah Alipoviumba viumbe, Aliandika katika kitabu, ambacho kipo Kwake juu ya 'Arshi Yake: Hakika rehema Yangu inashinda ghadhabu Yangu." 

Na katika riwaayah nyingine: "Imeshinda ghadhabu Yangu."

Na katika riwaayah nyengine: "Imepita ghadhabu Yangu." [Al-Bukhaariy, Muslim na At-Tirmidhy]

 

 

Hadiyth – 9

وعن أَبي هريرة رضي الله عنه ، قَالَ : سَمِعْتُ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم، يقول : (( جَعَلَ الله الرَّحْمَةَ مِئَةَ جُزْءٍ، فَأمْسَكَ عِنْدَهُ تِسْعَةً وَتِسْعِينَ، وَأنْزَلَ في الأرْضِ جُزْءاً وَاحِداً، فَمِنْ ذلِكَ الجُزءِ يَتَرَاحَمُ الخَلائِقُ، حَتَّى تَرْفَعَ الدَّابّةُ حَافِرهَا عَنْ وَلَدِهَا خَشْيَةَ أنْ تُصِيبَهُ )) .

وفي رواية : (( إنّ للهِ تَعَالَى مئَةَ رَحمَةٍ ، أنْزَلَ مِنْهَا رَحْمَةً وَاحِدَةً بَيْنَ الجنِّ وَالإنس وَالبهائِمِ وَالهَوامّ ، فبها يَتَعاطَفُونَ ، وبِهَا يَتَرَاحَمُونَ ، وبِهَا تَعْطِفُ الوَحْشُ عَلَى وَلَدِهَا ، وَأخَّرَ اللهُ تَعَالَى تِسْعاً وَتِسْعينَ رَحْمَةً يرْحَمُ بِهَا عِبَادَهُ يَوْمَ القِيَامَة )) مُتَّفَقٌ عَلَيهِ .

ورواه مسلم أيضاً مِنْ رواية سَلْمَانَ الفارِسيِّ رضي الله عنه ، قَالَ : قَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم: (( إنَّ للهِ تَعَالَى مِئَة رَحْمَةٍ فَمِنْهَا رَحْمَةٌ يَتَرَاحمُ بِهَا الخَلْقُ بَيْنَهُمْ ، وَتِسْعٌ وَتِسعُونَ لِيَومِ القِيَامَةِ )) .

وفي رواية : (( إنَّ الله تَعَالَى خَلَقَ يَوْمَ خَلَقَ السَّمَاواتِ وَالأَرْضَ مَئَةَ رَحْمَةٍ كُلُّ رَحْمَةٍ طِبَاقُ مَا بَيْنَ السَّماءِ إِلَى الأرْضِ ، فَجَعَلَ مِنْهَا في الأرضِ رَحْمَةً فَبِهَا تَعْطفُ الوَالِدَةُ عَلَى وَلَدِهَا ، وَالوَحْشُ وَالطَّيْرُ بَعْضُهَا عَلَى بَعْض ، فَإذا كَانَ يَوْمُ القِيَامَةِ أكملَهَا بِهذِهِ الرَّحمَةِ ))

Imepokewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiyah Allaahu 'anhu) amesema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: Allaah Amefanya rehema kuwa sehemu mia moja, Akabakia na sehemu tisini na tisa, Akateremsha ardhini sehemu moja, katika sehemu hiyo viumbe wanahurumiana, mpaka mnyama anainua kwato zake akihofia kumdhuru mwanae."

Katika riwaayah nyengine: "Hakika Allaah Ta'aalaa ana rehma mia moja, katika hizo ameteremsha rehma moja baina ya majini na wanadamu, wanyama na wadudu. Katika hiyo rehma wanasikitiana, wanahurumiana, mnyama pori anamhurumia mwanae. Allaah Amebakisha rehema tisini na tisa Arawarahamu nazo waja Wake Siku ya Qiyaamah." [Al-Bukhaary, Muslim na At-Tirmidhy]

Amepokea Muslim Hadiyth kutoka kwa Salmaan Al-Faarisy; Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Hakika Allaah Ta'aalaa ana rehema mia moja, miongoni mwa hizo ni rehema moja, wanahurumiana viumbe baina yao, tisini na tisa ni kwa ajili ya Siku ya Qiyaamah." 

Katika riwaayah nyingine: "Hakika Allaah Ta'aalaa ameumba siku Aliyoumba mbingu na ardhi rehema mia moja; kila moja ni baina ya mbingu na ardhi. Akajalia katika ardhi rehema Mama anamhurumia mwanae, na wanyama na ndege wanahurumiana wao kwa wao, Ikifika Siku ya Qiyaamah, Allaah ataikamilisha kwa rehema hii." 

 

 

Hadiyth – 10

وعن أَبي هريرة رضي الله عنه، عن النَّبيّ صلى الله عليه وسلم فيما يحكِي عن ربهِ تبارك وتعالى ، قَالَ: (( أذْنَبَ عَبْدٌ ذَنْباً ، فَقَالَ : اللَّهُمَّ اغْفِرْ لِي ذَنْبِي ، فَقَالَ الله تَبَاركَ وَتَعَالَى : أذنَبَ عبدي ذَنباً ، فَعَلِمَ أنَّ لَهُ رَبّاً يَغْفِرُ الذَّنْبَ ، وَيَأْخُذُ بالذَّنْبِ ، ثُمَّ عَادَ فَأذْنَبَ ،   فَقَالَ : أيْ رَبِّ اغْفِرْ لِي ذَنْبي ، فَقَالَ تبارك وتعالى : أذنَبَ عبدِي ذَنباً ، فَعَلِمَ أنَّ لَهُ رَبّاً ، يَغْفِرُ الذَّنْبَ ، وَيَأْخُذُ بالذَّنْبِ ، قَدْ غَفَرْتُ لِعَبْدِي فَلْيَفْعَلْ مَا شَاءَ )) مُتَّفَقٌ عَلَيهِ .

Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiyah Allaahu 'anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anayohadithia kutoka kwa Mola wake (Tabaaraka wa Ta'aalaa) kuwa Amesema: "Mja amefanya dhambi, akasema: "Ee Mola wangu nisamehe dhambi yangu." Akasema Allaah (Tabaaraka wa Ta'aalaa): "Mja Wangu amefanya dhambi, akajua kuwa anaye Mola anayesamehe dhambi, na anayehesabu dhambi." Kisha akarudi akafanya dhambi, akasema: "Ee Mola Wangu nisamehe dhambi yangu." Akasema Allaah (Tabaaraka wa Ta'aalaa): "Mja Wangu amefanya dhambi, akajua kuwa anaye Mola anayesamehe dhambi, na anayehesabu dhambi." Kisha akarudi akafanya dhambi, akasema: "Ee Mola Wangu nisamehe dhambi yangu."Akasema Allaah (Tabaaraka wa Ta'aalaa): "Mja Wangu amefanya dhambi, akajua kuwa anaye Mola anayesamehe dhambi, na mwenye kuhesabu dhambi. Nimemsamehe mja Wangu dhambi zake, hivyo afanye anavyotaka." [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

Hadiyth – 11

وعن أَبي هريرة رضي الله عنه، قَالَ : قَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم: (( والَّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ ، لَوْ لَمْ تُذْنِبُوا ، لَذَهَبَ الله بِكُمْ ، وَجَاءَ بِقَومٍ يُذْنِبُونَ ، فَيَسْتَغْفِرُونَ الله تَعَالَى ، فَيَغْفِرُ لَهُمْ )) رواه مسلم .

Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiyah Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu ipo mikononi Mwake kwamba lau hamngekuwa mkifanya dhambi Allaah angewaondosha na Akawaleta watu ambao watafanya dhambi na kisha wataomba msamaha kwa Allaah (Ta'aalaa) Naye atawasamehe." [Muslim]

 

 

Hadiyth – 12

وعن أَبي أيوب خالد بن زيد رضي الله عنه، قَالَ : سَمِعْتُ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم، يقول : (( لَوْلاَ أنَّكُمْ تُذْنِبُونَ ، لَخَلَقَ الله خَلْقاً يُذْنِبُونَ ، فَيَسْتَغْفِرونَ ، فَيَغْفِرُ لَهُمْ )) رواه مسلم .

Imepokewa kutoka kwa Abu Ayub Khalid bin Zaiyd (Radhwiyah Allaahu 'anhu) amesema: "Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: "Msingekuwa mnafanya dhambi basi Allaah angewaumba viumbe wenye kufanya madhambi kisha wataomba toba na Allaah atawasamehe." [Muslim]

 

 

Hadiyth – 13

وعن أَبي هريرة رضي الله عنه، قَالَ : كُنَّا قُعُوداً مَعَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم، مَعَنَا أَبُو بَكْرٍ وَعُمْرُ رضي الله عنهما ، في نَفَرٍ فَقَامَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم مِنْ بَيْنِ أظْهُرِنَا ، فَأبْطَأَ عَلَيْنَا فَخَشِينَا أنْ يُقتطَعَ دُونَنَا ، فَفَزِعْنَا فَقُمْنَا فَكُنْتُ أوَّلَ مَنْ فَزِعَ فَخَرَجْتُ أبْتَغِي رسولَ الله صلى الله عليه وسلم، حَتَّى أتَيْتُ حَائِطاً للأنْصَارِ ... وَذَكَرَ الحَدِيثَ بِطُولِهِ إِلَى قوله : فَقَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم: (( اذهَبْ فَمَن لَقِيتَ وَرَاءَ هَذَا الحَائِطِ يَشْهَدُ أنْ لا إله إلاَّ الله ، مُسْتَيقِناً بِهَا قَلبُهُ فَبَشِّرْهُ بِالجَنَّةِ )) رواه مسلم .

Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayrah(Radhwiyah Allaahu 'anhu) amesema: Tulikuwa tumekaa pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na pamoja nasi kulikuwa na Abu Bakr na 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhummaa) miongoni mwa Swahaaba wengine Alisimama Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baina ya migongo yetu na akakawia sana, hivyo tukawa na hofu kubwa sana kuhusu usalama wake. Hapo tulisimama ili kumtafuta, nami ndiye niliyekuwa wa mwanzo kuwa na hamu hiyo. Niliinuka ili kumtafuta Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), mpaka nikafika kwenye ukuta wa Ansaar. Hapa aliitaja Hadiyth kwa urefu na ukamilifu wake mpaka katika kauli yake: Akasema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Nenda nyuma ya ukuta huu umbashirie Pepo kila utakayekutana naye huku anashuhudia ya kwamba hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah." [Muslim]

 

 

 

Hadiyth – 14

وعن عبد الله بن عمرو بن العاص رضي الله عنهما : أنَّ النَّبيّ صلى الله عليه وسلم تَلاَ قَولَ الله (عزّ وجلّ) في إبراهيم صلى الله عليه وسلم: ( رَبِّ إِنَّهُنَّ أَضْلَلْنَ كَثِيراً مِنَ النَّاسِ فَمَنْ تَبِعَنِي فَإِنَّهُ مِنِّي ) [ إبراهيم : 36 ] الآية ، وقَولَ عِيسَى صلى الله عليه وسلم: ( إِنْ تُعَذِّبْهُمْ فَإِنَّهُمْ عِبَادُكَ وَإِنْ تَغْفِرْ لَهُمْ فَإِنَّكَ أَنْتَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ) [ المائدة : 118 ] فَرَفَعَ يَدَيهِ وَقالَ : (( اللَّهُمَّ أُمّتي أُمّتي )) وبَكَى ، فَقَالَ الله (عزّ وجلّ) : (( يَا جِبْريلُ ، اذْهَبْ إِلَى مُحَمَّدٍ -وَرَبُّكَ أعْلَمُ - فَسَلْهُ مَا يُبْكِيهِ ؟ )) فَأتَاهُ جبريلُ ، فَأخْبَرَهُ رسولُ الله صلى الله عليه وسلم، بِمَا قَالَ - وَهُوَ أعْلَمُ - فَقَالَ اللهُ تَعَالَى : (( يَا جِبريلُ ، اذْهَبْ إِلَى مُحَمّدٍ ، فَقُلْ : إنَّا سَنُرْضِيكَ في أُمّتِكَ وَلاَ نَسُوءكَ )) رواه مسلم .

Imepokewa kutoka kwake 'Abdillaahi bin 'Amru bin al-'Aasw (Radhwiyah Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisoma kauli ya Allaah ('Azza wa Jalla) kuhusu Ibraahiym (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Rabb wangu! Hakika hao (masanamu) wamepoteza wengi kati ya watu. Basi atakayenifuata, huyo ni katika mimi." [Ibraahiym: 36] Na kauli ya 'Iyssaa (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Ukiwaadhibu, basi bila shaka hao ni waja Wako; na Ukiwaghufuria basi hakika Wewe Ndiye Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote." [Al-Maaidah: 118] Nabiy alinyanyua mikono yake na kusema: "Ee Mola wangu! Ummah wangu, Ummah wangu", na akaanza kulia. Akasema Allaah ('Azza wa Jalla): "Ee Jibriyl! Nenda kwa Muhammad na Rabb wako ni mjuzi zaidi na umuulize ni kipi kinachomliza (yaani analia kwa nini)?" Jibriyl ('Alayhi sallaam) alikuja kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), naye akamwambia alichokisema na Allaah anajua zaidi. Akasema Allaah Ta'aalaa: "Ee Jibriyl! Nenda kwa Muhammad na umwambie: 'Hakika tutakufanya uridhike kwa Ummah wako na hatutakufanya uhuzunike'." [Muslim]

 

 

 

Hadiyth – 15

وعن معاذ بن جبل رضي الله عنه، قَالَ : كُنْتُ رِدْفَ النَّبيِّ صلى الله عليه وسلم عَلَى حِمَارٍ ، فَقَالَ : (( يَا مُعَاذُ ، هَلْ تَدْرِي مَا حَقُّ الله عَلَى عِبَادِهِ ؟ وَمَا حَقُّ العِبَادِ عَلَى الله ؟ )) قُلْتُ : اللهُ وَرَسُولُهُ أعْلَمُ . قَالَ : (( فإنَّ حَقَّ اللهِ عَلَى العِبَادِ أنْ يَعْبُدُوهُ ، وَلاَ يُشْرِكُوا بِهِ شَيئاً ، وَحَقَّ العِبَادِ عَلَى اللهِ أنْ لاَ يُعَذِّبَ مَنْ لا يُشْرِكُ بِهِ شَيئاً ))  فقلتُ : يَا رَسُول الله ، أفَلا أُبَشِّرُ النَّاسَ ؟ قَالَ : (( لاَ تُبَشِّرْهُمْ فَيَتَّكِلُوا )) مُتَّفَقٌ عَلَيهِ .

Imepokewa kutoka kwa Mu'aadh bin Jabal (Radhwiyah Allaahu 'anhu) amesema: Nilikuwa nimepanda nyuma ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya punda, akaniambia: "Ee Mu'aadh! Unajua haki ya Allaah na Rasuli Wake wanajua zaidi." Akasema: "Hakika haki ya Allaah juu ya waja Wake wamuabudu wala wasimshirikishe na chochote. Na haki ya waja kwa Allaah, ni kumuadhibu asiyemshirikisha na chochote." Nikasema: "Ee Rasuli wa Allaah! Je nisiwabashirie wakabweteka." [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Hadiyth – 16

وعن البراءِ بن عازب رضي الله عنهما ، عن النَّبيّ صلى الله عليه وسلم، قَالَ : (( المُسْلِمُ إِذَا سُئِلَ في القَبْرِ يَشْهَدُ أنْ لاَ إلَهَ إلاَّ الله ، وَأنّ مُحَمّداً رَسُول الله ، فذلك قوله تَعَالَى: ( يُثَبِّتُ اللهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي  الآخِرَة ) [ إبراهيم : 27 ] )) مُتَّفَقٌ عَلَيهِ.

Imepokewa kutoka kwa Al-Baraa'a bin 'Aazib (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Muislamu atakapoulizwa kaburini, anashuhudia kuwa hapana Mola isipokuwa Allaah, na kuwa Muhammad ni Rasuli Wake, hiyo ni kauli Yake Ta'aalaa: "Allaah Huwathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika uhai wa dunia na Aakhirah." [Ibraahiym: 27] 

 

 

Hadiyth – 17

وعن أنس رضي الله عنه ، عن رَسُول الله صلى الله عليه وسلم ، قَالَ : (( إنّ الكَافِرَ إِذَا عَمِلَ حَسَنَةً ، أُطعِمَ بِهَا طُعْمَةً مِنَ الدُّنْيَا ، وَأَمَّا المُؤْمِنُ فَإنَّ الله تَعَالَى يَدَّخِرُ لَهُ حَسَنَاتِهِ في الآخِرَةِ ، وَيُعْقِبُهُ رِزْقاً في الدُّنْيَا عَلَى طَاعَتِهِ )) .

وفي رواية : (( إنَّ الله لاَ يَظْلِمُ مُؤْمِناً حَسنَةً يُعْطَى بِهَا في الدُّنْيَا ، وَيُجْزَى بِهَا في الآخِرَةِ . وَأَمَّا الكَافِرُ فَيُطْعَمُ بِحَسَنَاتِ مَا عَمِلَ للهِ تَعَالَى في الدُّنْيَا ، حَتَّى إِذَا أفْضَى إِلَى الآخرَةِ ، لَمْ يَكُنْ لَهُ حَسَنَةٌ يُجْزَى بِهَا )) رواه مسلم .

Imepokewa kutoka kwa Anas (Radhwiyah Allaahu 'anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Hakika kafiri akifanya jema, hulishwa chakula duniani, Ama Muumini Allaah Ta'aalaa anamuwekea amali yake njema Aakhirah, na anampa riziki hapa duniani kwa sababu ya utiifu wake." 

Na katika riwaayah nyengine: "Hakika Allaah hamdhulumu Muumini aliyefanya mambo mema anampa duniani, na kumlipa nayo nayo Aakhirah. Ama kafiri analishwa kwa mema aliyoyafanya kwa ajili ya Allaah duniani; hadi akifika Aakhirah, hawi na mema yoyote ya kulipwa huko." [Muslim]

 

 

Hadiyth – 18

وعن جابر رضي الله عنه ، قَالَ : قَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم: (( مَثَلُ الصَّلَوَاتِ الخَمْسِ كَمَثَلِ نَهْرٍ جَارٍ غَمْرٍ عَلَى بَابِ أحَدِكُمْ يَغْتَسِلُ مِنْهُ كُلَّ يَوْم خَمْسَ    مَرَّات )) رواه مسلم .

Imepokewa kutoka kwa Jaabir (Radhwiyah Allaahu 'anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema: "Mfano wa Swalaah tano ni kama mfano wa mto mkubwa unaopita mbele ya mlango wa mmoja wenu, ambaye atakuwa anajiosha kila siku mara tano." [Muslim].

 

 

Hadiyth – 19

وعن ابن عباس رضي الله عنهما ، قَالَ : سَمِعْتُ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم، يقول : (( مَا مِنْ رَجُلٍ مُسْلِمٍ يَمُوتُ ، فَيقُومُ عَلَى جَنَازَتهِ أرْبَعونَ رَجُلاً لاَ يُشْرِكُونَ بِاللهِ شَيئاً ، إلاَّ شَفَّعَهُمُ اللهُ فِيهِ )) رواه مسلم .

Imepokewa kutoka kwa Ibn 'Abbaas (Radhwiyah Allaahu 'anhummaa) amesema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: "Hakuna Muislamu yeyote ambaye anaaga dunia, wakasimama watu arobaini kumswalia (Swalaah ya Jeneza) wasiomshirikisha Allaah na chochote isipokuwa Allaah anakubali maombi yao." [Muslim]

 

 

Hadiyth – 20

وعن ابن مسعود رضي الله عنه، قَالَ : كُنَّا مَعَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم في قُبَّة نَحْوَاً مِنْ أربَعِينَ ، فَقَالَ : (( أتَرْضَونَ أنْ تَكُونُوا رُبُعَ أهْلِ الجَنَّةِ ؟ )) قُلْنَا : نَعَمْ . قَالَ :  (( أتَرْضَوْنَ أنْ تَكُونُوا ثُلُثَ أهلِ الجَنَّةِ ؟ )) قُلْنَا : نَعَمْ ، قَالَ : (( وَالَّذِي نَفْسُ مُحَمّدٍ بيَدِهِ ، إنِّي لأَرْجُو أنْ تَكُونُوا نِصْفَ أهْلِ الجَنَّةِ وذلك أنَّ الجنَّةَ لاَ يَدْخُلُهَا إلاَّ نَفْسٌ مُسْلِمَةٌ ، ومَا أنْتُم في أهْلِ الشِّركِ إلاَّ كَالشَّعْرَةِ البَيْضَاءِ في جلدِ الثَّورِ  الأَسْوَدِ ، أَوْ كَالشَّعْرَةِ السَّودَاءِ في جلدِ الثَّورِ الأحْمَر )) مُتَّفَقٌ عَلَيهِ .

Na imepokewa kutoka kwa Ibn Mas'uud (Radhwiyah Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Tulikuwa takriban watu arobaini katika nyumba ndogo pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: "Je, mtaridhia kuwa robo ya watu wa Peponi?" Tulisema: "Ndio." Akasema: "Je, mtaridhia kuwa thulithi ya watu wa Peponi?" Tulisema: "Ndio." Akasema: "Naapa kwa ambaye nafsi ya Muhammad ipo mkononi Mwake, hakika nina matarajio kuwa nyinyi mtakuwa nusu ya watu wa Peponi. Na hiyo kwa sababu ya kuwa hataingia Peponi ila nafsi ya Muislamu. Na idadi yenu kulinganishwa na watu wa shirki ni kama nywele nyeupe katika ngozi ya fahali mweusi, au nywele nyeusi katika ngozi ya fahali mwekundu." [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Hadiyth – 21

وعن أَبي موسى الأشعري رضي الله عنه، قَالَ : قَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم : (( إِذَا كَانَ يَوْمُ القِيَامَةِ دَفَعَ اللهُ إِلَى كُلِّ مُسْلِم يَهُودياً أَوْ نَصْرانِياً ، فَيَقُولُ : هَذَا فِكَاكُكَ مِنَ النَّارِ )) .

وفي رواية عَنْهُ ، عن النَّبيّ صلى الله عليه وسلم، قَالَ : (( يَجِيءُ يَوْمَ القِيَامَةِ نَاسٌ مِنَ المُسْلِمينَ بِذُنُوبٍ أَمْثَال الجِبَالِ يَغْفِرُهَا الله لَهُمْ )) رواه مسلم .

Imepokewa kutoka kwa Abu Muwsaa Al-Ash'ariy (Radhwiyah Allaahu 'anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Itakapokuwa siku ya Qiyaamah Allaah atampa kila Muislamu Yahudi au Mnasara, Atasema: 'Hii ni fidiya yako na Moto'." 

Katika riwaayah yake nyingine: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Watakuja watu Siku ya Qiyaamah miongoni mwa Waislamu na madhambi mfano wa mlima, Allaah atawasamehe (madhambi yao hayo)." [Muslim]

 

 

Hadiyth – 22

وعن ابن عمر رضي الله عنهما ، قَالَ : سَمِعْتُ رسولَ الله صلى الله عليه وسلم،   يقول : (( يُدْنَى المُؤْمِنُ يَوْمَ القِيَامَة مِنْ رَبِّهِ حَتَّى يَضَعَ كَنَفَهُ عَلَيهِ ، فَيُقَرِّرُهُ بذُنُوبِهِ ، فيقولُ : أتعرِفُ ذَنْبَ كَذَا ؟ أتَعرفُ ذَنْبَ كَذَا ؟ فيقول : رَبِّ أعْرِفُ ، قَالَ : فَإنِّي قَدْ سَتَرْتُهَا عَلَيْكَ في الدُّنْيا ، وَأنَا أغْفِرُهَا لَكَ اليَومَ ، فَيُعْطَى صَحيفَةَ    حَسَنَاتِهِ )) مُتَّفَقٌ عَلَيهِ .

Imepokewa kutoka kwa Ibn 'Umar (Radhwiyah Allaahu 'anhummaa) amesema: Nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akisema: "Muumini atasogezwa karibu na Mola wake Siku ya Qiyaamah na kumfunika kwa sitara Yake. Atamuulizia dhambi zake, Atasema:, 'Unajua dhambi kadhaa? Unajua dhambi kadhaa?' Atasema: 'Mola wangu najua, Atasema: Mimi nimekusitiri duniani, Nami ninaisamehe kwako leo. Atapewa sahifa ya mema yake." [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Hadiyth – 23

وعن ابن مسعود رضي الله عنه: أنَّ رَجُلاً أصَابَ مِن امْرَأة قُبْلَةً ، فَأتَى النَّبيَّ صلى الله عليه وسلم فَأخْبَرَهُ ، فَأنْزَلَ الله تَعَالَى : ( وَأَقِمِ الصَّلاةَ طَرَفَيِ النَّهَارِ وَزُلَفاً مِنَ اللَّيْلِ إِنَّ الْحَسَنَاتِ يُذْهِبْنَ السَّيِّئَات ) [ هود : 114] فَقَالَ الرجل: أَليَ هَذَا يَا رَسُول الله ؟ قَالَ : (( لجميعِ أُمَّتِي كُلِّهِمْ )) مُتَّفَقٌ عَلَيهِ .

Imepokewa kutoka kwa Ibn Mas'uud (Radhwiyah Allaah 'anhu) kuwa : Mtu mmoja alimbusu mwanamke ajnabi, akaja kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kumwelezea hilo. Allaah Ta'aalaa akateremsha: "Na simamisha Swalaah katika ncha mbili za mchana na sehemu ya kwanza ya usiku; hakika mema yanaondosha maovu." [Huwd: 114]. Akasema yule mtu: "Ee Rasuli wa Allaah! Je, hili ni langu?" Akasema: "Ni kwa Ummah wangu wote." [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Hadiyth – 24

وعن أنس رضي الله عنه، قَالَ: جاء رجل إِلَى النَّبيّ صلى الله عليه وسلم ، فَقَالَ : يَا رَسُول الله، أَصَبْتُ حَدّاً ، فَأَقِمْهُ عَلَيَّ ، وَحَضَرَتِ الصَّلاةُ ، فَصَلَّى مَعَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم ، فَلَمَّا قَضَى الصَّلاةَ ، قَالَ : يَا رَسُول الله ، إنِّي أصَبْتُ حَدّاً فَأقِمْ فيَّ كِتَابَ الله . قَالَ : (( هَلْ حَضَرْتَ مَعَنَا الصَّلاةَ )) ؟ قَالَ : نَعَمْ . قَالَ : (( قَدْ غُفِرَ لَكَ )) مُتَّفَقٌ عَلَيهِ .

Imepokewa kutoka kwa Anas (Radhwiyah Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Alikuja mtu kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kuuliza: "Ee Rasuli wa Allaah! Nimefanya kosa la kusimamishiwa hadd, kwa hivyo isimamishe." Wakati wa Swalaah ulifika, naye (huyo mtu) akaswali pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Baada ya swalaah alisema tena: "EeRasuli wa Allaah! Nimefanya kosa la kusimamishiwa hadd kwa hivyo isimamishe kulingana na Kitabu cha Allaah." Akasema (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Je, umeswali na sisi?" Akasema: "Ndio." Akasema (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Hakika umesamehe (kosa lako hilo)." [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Hadiyth – 25

وعن أنس رضي الله عنه ، قَالَ : قَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم : (( إنَّ الله لَيرْضَى عَنِ العَبْدِ أنْ يَأكُلَ الأَكْلَةَ ، فَيَحْمَدُهُ عَلَيْهَا ، أَوْ يَشْرَبَ الشَّرْبَةَ ، فَيَحْمَدُهُ عَلَيْهَا )) رواه مسلم

Na imepokewa kutoka kwa Anas (Radhwiyah Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Hakika Allaah anamridhia mja anayekula chakula na baadae akamuhimidi (akamshukuru Allaah) au akanywa kinywaji kisha akamuhimidi kwa ajili ya kupata kinywaji hicho." [Muslim] 

 

 

Hadiyth – 26

وعن أَبي موسى رضي الله عنه  ، عن النَّبيّ صلى الله عليه وسلم ، قَالَ : (( إنَّ الله تَعَالَى يَبْسُطُ يَدَهُ باللَّيلِ ليَتُوبَ مُسِيءُ النَّهَارِ ، وَيَبْسُطُ يَدَهُ بالنَّهَارِ لِيَتُوبَ مُسِيءُ اللَّيلِ ، حَتَّى تَطلُعَ الشَّمْسُ مِنْ مَغْرِبِهَا )) رواه مسلم .

Imepokewa kutoka kwa Abu Muuwsaa 'Abdillahi bin Qays al-Ash'ariy (Radhwiyah Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Hakika Allaah Ta'aalaa hunyoosha mkono Wake usiku wapate kutubia mpaka jua lichomoza upande wa magharibi." [Muslim]

 

 

Hadiyth – 27

وعن أَبي نجيح عمرو بن عَبَسَة - بفتح العين والباءِ - السُّلَمِيِّ رضي الله عنه، قَالَ : كُنْتُ وأنَا في الجاهِلِيَّةِ أظُنُّ أنَّ النَّاسَ عَلَى ضَلاَلَةٍ ، وَأَنَّهُمْ لَيْسُوا عَلَى شَيْءٍ ، وَهُمْ يَعْبُدُونَ الأَوْثَانَ ، فَسَمِعْتُ بِرَجُلٍ بِمَكَّةَ يُخْبِرُ أخْبَاراً ، فَقَعَدْتُ عَلَى رَاحِلَتِي ، فَقَدِمْتُ عَلَيهِ ، فإِذَا رسولُ الله  صلى الله عليه وسلم مُسْتَخْفِياً ، جرَءاءُ عَلَيهِ قَومُهُ ، فَتَلَطَّفَتُ حَتَّى دَخَلْتُ عَلَيهِ بِمَكَّةَ ، فَقُلْتُ لَهُ : مَا أنْتَ ؟ قَالَ : (( أنا نَبيٌّ )) قُلْتُ : وما نبيٌّ ؟ قَالَ : (( أرْسَلَنِي الله )) قُلْتُ : وبأيِّ شَيْء أرْسَلَكَ ؟ قَالَ : (( أَرْسَلَنِي بِصِلَةِ الأرْحَامِ ، وَكَسْرِ الأَوْثَانِ ، وَأنْ يُوَحَّدَ اللهُ لاَ يُشْرَكُ بِهِ شَيْء )) قُلْتُ : فَمَنْ مَعَكَ عَلَى هَذَا ؟ قَالَ : (( حُرٌّ وَعَبْدٌ )) ومعه يَوْمَئذٍ أَبُو بكرٍ وبلالٌ رضي الله عنهما ، قُلْتُ : إنّي مُتَّبِعُكَ ، قَالَ : (( إنَّكَ لَنْ تَسْتَطيعَ ذلِكَ يَومَكَ هَذَا ، ألا تَرَى حَالي وحالَ النَّاسِ ؟ وَلَكِنِ ارْجعْ إِلَى أهْلِكَ فَإِذَا سَمِعْتَ بي قَدْ ظَهرْتُ فَأتِنِي )) قَالَ : فَذَهَبْتُ إِلَى أهْلِي وقَدِمَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم  المَدِينَةَ حَتَّى قَدِمَ نَفَرٌ مِنْ أهْلِي المَدِينَةَ ، فقلتُ : مَا فَعَلَ هَذَا الرَّجُلُ الَّذِي قَدِمَ المَدِينَةَ ؟ فقالوا : النَّاس إلَيهِ سِرَاعٌ ، وَقَدْ أرادَ قَومُهُ قَتْلَهُ ، فلَمْ يَسْتَطِيعُوا ذلِكَ ، فقَدِمْتُ المدينَةَ ، فَدَخَلْتُ عَلَيهِ ، فقلتُ : يَا رَسُول الله أَتَعْرِفُني ؟ قَالَ : (( نَعَمْ ، أنْتَ الَّذِي لَقَيْتَنِي بمكّةَ )) قَالَ : فقلتُ : يَا رَسُول الله ، أخْبِرنِي عَمَّا عَلَّمَكَ الله وأَجْهَلُهُ ، أخْبِرْنِي عَنِ الصَّلاَةِ ؟ قَالَ : (( صَلِّ صَلاَةَ الصُّبْحِ ، ثُمَّ اقْصُرْ عَنِ الصَّلاَةِ حَتَّى تَرْتَفِعَ الشَّمْسُ قِيدَ رُمْحٍ ، فَإنَّهَا تَطْلُعُ حِينَ تَطلُعُ بَيْنَ قَرْنَيْ شَيطَان ، وَحينَئذٍ يَسجُدُ لَهَا الكُفَّارُ ، ثُمَّ صَلِّ فَإنَّ الصَلاَةَ مَشْهُودَةٌ مَحْضُورةٌ حَتَّى يَسْتَقِلَّ الظِّلُّ بالرُّمْحِ ، ثُمَّ اقْصُرْ عَنِ الصَّلاةِ ، فَإنَّهُ حينئذ تُسْجَرُ جَهَنَّمُ ، فإذَا أقْبَلَ الفَيْءُ فَصَلِّ ، فَإنَّ الصَّلاةَ مَشْهُودَةٌ مَحضُورَةٌ حَتَّى تُصَلِّي العصرَ ، ثُمَّ اقْصرْ عَنِ الصَّلاةِ حَتَّى تَغْرُبَ الشَّمْسُ ، فإنَّهَا تَغْرُبُ بينَ قَرْنَيْ شَيطانٍ ، وَحِينَئذٍ يَسْجُدُ لَهَا الكُفّارُ )) قَالَ : فقلتُ : يَا نَبيَّ الله ، فالوضوءُ حدثني عَنْهُ ؟ فَقَالَ : (( مَا مِنْكُمْ رَجُلٌ يُقَرِّبُ وَضُوءهُ ، فَيَتَمَضْمَضُ وَيسْتَنْشِقُ فَيَسْتَنْثِرُ ، إلاَّ خَرَّتْ خَطَايَا وَجْهِهِ مِنْ أطْرَافِ لِحْيَتِهِ مَعَ المَاءِ ، ثُمَّ يَغْسِلُ يديهِ إِلَى المِرفقَيْن ، إلاَّ خَرَّتْ خَطَايَا يَدَيْهِ مِنْ أنَامِلِهِ مَعَ الماءِ ، ثُمَّ يَمْسَحُ رَأسَهُ ، إلاَّ خرّتْ خطايا رأسِهِ من أطْرَافِ شَعْرِهِ مَعَ الماءِ ، ثُمَّ يغسل قدميه إِلَى الكعْبَيْنِ ، إلاَّ خَرَّتْ خَطَايَا رِجلَيْهِ مِنْ أنَاملِهِ مَعَ الماءِ ، فَإنْ هُوَ قَامَ فَصَلَّى ، فَحَمِدَ الله تَعَالَى ، وأثنى عَلَيهِ ومَجَّدَهُ بالَّذي هُوَ لَهُ أهْلٌ ، وَفَرَّغَ قلبه للهِ تَعَالَى ، إلاَّ انْصَرفَ مِنْ خَطِيئَتِهِ كهيئته يَومَ وَلَدتهُ أُمُّهُ )) .

فحدث عَمرُو بن عَبسَة بهذا الحديث أَبَا أُمَامَة صاحِب رَسُول الله صلى الله عليه وسلم ، فَقَالَ لَهُ أَبُو أُمَامَة : يَا عَمْرُو بنُ عَبسَة ، انْظُر مَا تقولُ ‍! في مقامٍ واحدٍ يُعْطَى هَذَا الرَّجُلُ ؟ فَقَالَ عَمْرٌو : يَا أَبَا أُمَامَة ، لقد كَبرَتْ سِنّي ، وَرَقَّ عَظمِي ، وَاقْتَرَبَ  أجَلِي ، وَمَا بِي حَاجَةٌ أنْ أكْذِبَ عَلَى اللهِ تَعَالَى ، وَلا عَلَى رَسُول الله صلى الله عليه وسلم ، لَوْ لَمْ أسمعه مِنْ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم ، إلاَّ مَرَّةً أَوْ مَرَّتَينِ أَوْ ثَلاثاً – حَتَّى عَدَّ سَبْعَ مَرَّات – مَا حَدَّثْتُ أبداً بِهِ ، وَلكنِّي سمعتُهُ أكثَر من ذلِكَ . رواه مسلم .

Imepokewa kutoka kwa Abu Najiih 'Amru bin 'Asabah As-Sulamiy (Radhwiyah Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Katika siku zangu za Ujahiliyyah nilikuwa nadhani kuwa watu wapo katika upotevu na wao hawakuwa katika kitu chochote (katika kufuata Dini ya haki). Watu wakati huo walikuwa wakiabudu masanamu. Nilisikia habari ya kwamba yupo mtu Makkah aliyekuwa akieleza kuhusu jambo jipya. Nilipanda kipandio changu na nikaelekea Makkah na nilipofika nilikutana na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye alikuwa akifanya mambo yake kwa siri kwa sababu ya mateso kutoka kwa watu wake. Nilijificha mpaka nikapata nafasi ya kukutana naye hapo Makkah, na hapo nikamuuliza: "Wewe ni nani?" Akasema: "Mimi ni Nabiy" Nikasema: "Na Nabiy ni nini?" Akasema: "Nimetumwa na Allaah." Nikasema: "Amekutuma na kitu gani?" Akasema: "Amenituma kuunganisha kizazi, na kuvunja masanamu, na kumpwekesha Allaah wala asishirikishwe na chochote." Nikamuuliza: "Na ni akina nani ambao wako nawe juu ya hili?" Akasema: "Watu walio huru pamoja na watumwa." Na wakati huo alikuwa pamoja na Abu Bakr na Bilaal. Nikasema: "Mimi nakufuata wewe." Akasema: "Hakika wewe huwezi kufanya hivyo sasa, je huoni hali yangu na watu? Lakini nenda zako kwa familia yako na pindi utakaposikia ya kuwa nimefaulu katika jukumu basi wakati huo njoo kwangu." Kwa hali hiyo nilirudi kwa familia na watu wangu na Rasuli wa Allaah alihama Madinah. Nilibaki pamoja na familia yangu na huku ninafuatilia habari na nikawa nawauliza watu kuhusu Rasuli wa Allaah mpaka baadhi ya watu wangu walipozuru Madinah. Nikawauliza (waliporudi): "Huyu mtu aliyehamia Madinah amefanya nini?" Wakasema: "Watu wanakwenda kwake kukubali ujumbe wake (kusilimu) japokuwa watu wake walikuwa wanataka kumuua lakini wakashindwa." Niliwasili Madinah na nikafika kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na kumuuliza: "Ee Rasuli wa Allaah! Je, unanifahamu?" Akasema: "Ndio, wewe ni yule uliyenikuta Makkah." Nikasema: "Ee Rasuli wa Allaah! Nijulishe yale aliyokuelimisha Allaah ambayo siyajui na unipe habari ya Swalaah?" Akasema: "Swali Swalaah ya Asubuhi (Swalatul Fajr), kisha jiweke kando (usiswali) mpaka jua liwe limepanda juu ya mbingu kiasi cha mkuki, kwani linapochomoza linachomoza baina ya pembe mbili za Shetani na wakati huo ndio makafiri wanalisujudia. Baada ya hapo unaweza kuswali, kwani Swalaah inashuhudiwa na inahudhuriwa na Malaika mpaka kivuli cha mkuki kiwe sawa (kwa kupotea) na urefu wa mkuki. Baada ya hapo usiswali, kwani wakati huo Moto uantiwa kuni (za kuuwakisha). Kivuli kitakaporefuka basi Swali, kwani Swalaah inashuhudiwa na ianhudhuriwa na Malaika mpaka wakati wa Alasiri. Baada ya hapo jiepushe kuswali mpaka machweo, kwani jua linakuchwa (linazama) baina ya pembe mbili za Shetani na wakati huo makafiri wanalisujudia." Hapo nikasema: "Ee Nabiy wa Allaah! Wudhu', nihadithie kuhusu hilo." Akasema: "Hakuna mtu yeyote ambaye atachukua maji ya kutawadhia, akasukutua na kusafisha pua yake isipokuwa madhambi ya pua na modomo wake yanaoshwa na kutolewa nje. Kisha anapoosha uso wake kama alivyoamrisha Allaah isipokuwa madhambi yake ya uso yanadondoka pembezoni mwa ndevu zake pamoja na maji. Kisha anaosha mikono yake mpaka vifundoni, isipokuwa hudondoka madhambi ya mikono yake kwenye vidole pamoja na maji. Kisha anapaka kichwa chake, isipokuwa hutoka madhambi yote ya kichwa kutoka katika mwisho wa nywele pamoja na maji hayo. Kisha anaosha miguu yake mpaka vifundoni isipokuwa makosa yote ya miguu hufutwa pamoja na maji yanapotoka. Na hapo anaposimama kuswali, akamuhimidi Allaah Ta'aalaa, akamsifu na kumtukuza kwa lile ambalo Yeye ndiye Mwenyewe (anastahiki zaidi) na akaufanya moyo wake unyenyekee kikamilifu kwa ajili ya Allaah Ta'aalaa isipokuwa makosa yake yote hufutwa akawa yuko katika hali kama ile siku aliyezaliwa na mamake. Pale 'Amru bin 'Abasah alipomuhadithia Hadiyth hii Abu Umamah, Swahaaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), Abu Umamah alimwambia: "Ee 'Amru: "Ee Abu Umamah! Hakika nimekuwa mzee na mifupa yangu imekauka na ajali yangu imekaribia (kufa kwangu) na wala sina haja yeyote ya kusema uwongo juu ya Allaah Ta'aalaa wala juu ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Lau kama sikumsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mara moja au mbili au tatu na akahesabu mpaka kufika mara saba nisingekuwa ni mwenye kumhadithia yeyeote milele lakini nimesikia zaidi ya hivyo." [Muslim]

 

 

Hadiyth – 28

وعن أَبي موسى الأشعري رضي الله عنه، عن النَّبيّ صلى الله عليه وسلم، قَالَ : (( إِذَا أرادَ الله تَعَالَى رَحمةَ أُمَّةٍ ، قَبَضَ نَبيَّهَا قَبْلَها ، فَجعلهُ لَهَا فَرطاً وسلَفاً بَيْنَ يَديْهَا ، وإذَا أرادَ هَلَكَةَ أُمَّةٍ ، عَذَّبَهَا وَنَبِيُّهَا حَيٌّ ، فَأهلكَها وَهُوَ حيٌّ يَنظُرُ ، فَأقرّ عَينَهُ بهلاكِها حِينَ كَذَّبُوهُ وَعَصَوا أمْرَهُ )) رواه مسلم .

Imepokewa kutoka kwa Abu Muuwsaa Al-Ash'ariy (Radhwiyah Allaahu 'anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Anapotaka Allaah Mtukufu rahma kwa watu, Humfisha Nabiy wao kabla yao, na kufanya ishara, na mtangulizi siku ya mwisho; na Anapotaka Kuangamiza watu, Huwaadhibu na Nabiy wao yu hai, na Huwaangamiza Nabiy wao akiwatazama, Hutuliza jicho lake kwa kuangamia kwao, kwa kumkadhibisha kwao na kuasi amri yake." [Muslim]

 

 

 

 

 

Share