06-Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Zuhd Yake: Ilifika Siku Hapakuwa Na Chakula Nyumbani Mwake Isipokuwa Tende Moja Tu!

Sifa Na Akhlaaq Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

06-Zuhd Yake:

Ilifika Siku Hapakuwa Na Chakula Nyumbani Mwake Isipokuwa Tende Moja Tu!

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Wake zake Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) nao walijifunza Zuhd na wakakhiari hata kujikhini wenyewe kwa kidogo mno walichonacho na badala yake wakawapatia Maskini waliokuja kuomba kwao.  Basi pindi mwanamke maskini mmoja alipofika nyumba ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kuomba Swadaqah au chakula, alimkuta Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) ambaye hakusita kuigawa tende moja iliyokuwa ndio chakula pekee kilichopatika nyumbani mwake:

 

 

 عَنْ عَائِشَةَ رضى الله عنها قَالَتْ: دَخَلَتِ امْرَأَةٌ مَعَهَا ابْنَتَانِ لَهَا تَسْأَلُ، فَلَمْ تَجِدْ عِنْدِي شَيْئًا غَيْرَ تَمْرَةٍ فَأَعْطَيْتُهَا إِيَّاهَا، فَقَسَمَتْهَا بَيْنَ ابْنَتَيْهَا وَلَمْ تَأْكُلْ مِنْهَا، ثُمَّ قَامَتْ فَخَرَجَتْ، فَدَخَلَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم عَلَيْنَا، فَأَخْبَرْتُهُ فَقَالَ:  "‏مَنِ ابْتُلِيَ مِنْ هَذِهِ الْبَنَاتِ بِشَىْءٍ كُنَّ لَهُ سِتْرًا مِنَ النَّارِ"  البخاري و مسلم

Kutoka kwa ‘Aaishah (رضي الله عنها) ambaye amesema: “Mama mmoja pamoja na binti zake wawili walikuja kwangu wakiomba (Swadaqah), lakini hakukuta chochote nilichonacho isipokuwa tende moja. Nikampa naye akaigawanya kwa binti zake, naye mwenyewe hakula chochote, kisha akasimama na akaenda zake.  Kisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akaja nami nikampa taarifa hii. Akasema: “Yeyote anayekabiliwa na mtihani kwa binti zake, naye akawakirimu kwa wema, basi mabinti hao watakuwa ni kinga dhidi ya Moto wa Jahannam.” [Al-Bukhariy, Muslim na wengineo]

 

Kujikhini kwa aina hii ni ‘amali njema kabisa Aipendayo Allaah (سبحانه وتعالى) Ambaye Aliteremsha Aayah kwa sababu ya kisa kilichotokea katika nyumba ya Abuu Twalhah Al-Answaariy na mkewe Ummu Sulaym ambao walijikhini kula chakula ilhali wao walikuwa na njaa, lakini badala yake wakawaachia wageni wao wale. Kisa chao hicho kilimfurahisha mno Allaah (سبحانه وتعالى) hadi kwamba Akateremsha Aayah:    

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ، ‏.‏ أَنَّ رَجُلاً، مِنَ الأَنْصَارِ بَاتَ بِهِ ضَيْفٌ فَلَمْ يَكُنْ عِنْدَهُ إِلاَّ قُوتُهُ وَقُوتُ صِبْيَانِهِ فَقَالَ لاِمْرَأَتِهِ نَوِّمِي الصِّبْيَةَ وَأَطْفِئِي السِّرَاجَ وَقَرِّبِي لِلضَّيْفِ مَا عِنْدَكِ - قَالَ - فَنَزَلَتْ هَذِهِ

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba mtu alilala usiku kama mgeni kwa mtu mmoja katika Answaariy ambaye hakuwa na chakula isipokuwa chakula cha watoto wake akamwambia mkewe: “Laza watoto na zima taa karibisha wageni kwa (chakula) ulichonacho.” Ikateremka kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 وَيُؤْثِرُونَ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ ۚ وَمَن يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ﴿٩﴾

 Na wanawapendelea kuliko nafsi zao japokuwa wao wenyewe wanahitaji. Na yeyote anayeepushwa na ubakhili na tamaa ya uchu wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufaulu. [Al-Hashr: 9]

 

Na Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى):

 

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ وَاسْمَعُوا وَأَطِيعُوا وَأَنفِقُوا خَيْرًا لِّأَنفُسِكُمْ ۗ وَمَن يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ﴿١٦﴾

Basi mcheni Allaah muwezavyo, na sikilizeni; na tiini na toeni (kwa ajili ya Allaah) ni kheri kwa ajili ya nafsi zenu. Na yeyote anayeepushwa na ubakhili na tamaa ya uchu wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufaulu. [At-Taghaabun: 16]

 

 

Naye Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akatufunza kuwa Iymaan haipatikani isipokuwa mtu ampendelee nduguye kile anachokipendelea nafsi yake:

 

 

عَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ (صلى الله عليه و آله وسلم) قَالَ: ((لاَ يُؤْمِنُ أَحَدُكُمْ حَتَّى يُحِبَّ لإِخِيهِ مَا يُحِبُّ لِنَفْسِهِ)) متفق عليه

Imepokelewa kutoka kwa Anas (رضي الله عنه)  kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hatoamini mmoja wenu mpaka ampendelee nduguye anayojipendelea nafsi yake)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Na huko ndio kufikia wema wa uhakika kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 لَن تَنَالُوا الْبِرَّ حَتَّىٰ تُنفِقُوا مِمَّا تُحِبُّونَ ۚ وَمَا تُنفِقُوا مِن شَيْءٍ فَإِنَّ اللَّـهَ بِهِ عَلِيمٌ ﴿٩٢﴾

Hamtoweza kuufikia wema mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda. Na kitu chochote mnachotoa basi hakika Allaah kwacho ni Mjuzi. [Aal-’Imraan 92]

 

Share