18-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Swiyaam: I'tikaaf

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Swiyaam

 

18-I’tikaaf

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Maana Yake

 

Ni kulikalia jambo. Aliyejifungia Msikitini na kukaa humo kwa ajili ya ‘ibaadah hujulikana kama mkaaji I’tikaaf  معتكف)  au (عاكف  [Al-Miswbaah Al-Muniyr (2/424) na Lisaan Al-‘Arab (9/252)]

 

Dalili ya uthibitifu wake

 

Imestahabiwa kukaa I’tikaaf katika Mwezi wa Ramadhwaan. Ni kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah aliyesema: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa anakaa I’tikaaf katika kila Ramadhwaan siku kumi, na ulipokuwa mwaka ambao alifariki, alikaa I’tikaaf siku ishirini)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2044).

 

 

I’tikaaf bora zaidi ni ya mwisho wa Ramadhwaan kutokana na yaliyothibiti toka kwa ‘Aaishah kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa anakaa I’tikaaf Kumi la Mwisho la Ramadhwaan mpaka Allaah ‘Azza wa Jalla Alipomfisha. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2026) na Muslim (1172)]

 

Na imethibiti pia kuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikaa I’tikaaf siku kumi za mwisho za Shawwaal kwa ajili ya kulipa I’tikaaf ya Ramadhwaan, kwa kuwa hakukaa masiku hayo I’tikaaf katika Ramadhwaan. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2041) na Muslim (1174)]

 

Ikiwa mtu ameweka nadhiri ya kukaa I’tikaaf siku moja au zaidi, basi ni lazima atekeleze nadhiri yake. Toka kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab kwamba alimwambia Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam): “Ee Rasuli wa Allaah! Hakika mimi nilikuwa nimeweka nadhiri enzi ya ujahilia ya kukaa usiku mmoja I’tikaaf ndani ya Al-Masjid Al-Haraam”. Rasuli akamwambia:

((فأوف بنذرك [فاعتكف ليلة]..))

((Basi tekeleza nadhiri yako [Akakaa I’tikaaf usiku mmoja]..)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2042) na Muslim (1656)]

 

I’tikaaf haifanywi ila ndani ya Msikiti

 

Ni kwa Kauli Yake Ta’aalaa:

((وَلَا تُبَاشِرُوهُنَّ وَأَنتُمْ عَاكِفُونَ فِي الْمَسَاجِدِ))

((Na wala msiwaingilie hali ya kuwa nyinyi ni wenye kukaa i’tikaaf Misikitini)). [Al-Baqarah (2:187)]

 

Na kwa vile Msikiti ulikuwa ndio sehemu ambayo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii sallam) alifanyia I’tikaaf na wakeze vile vile. Na kama ingekuwa inafaa kufanya I’tikaaf mahala pengine, basi wakeze Rasuli wasingefanya I’tikaaf kwenye Msikiti ambapo kuna uzito wa kuweka kambi humo. Na kama ingekuwa inafaa nyumbani, basi wangefanyia humo ijapokuwa mara moja.

 

Jumhuri ya ‘Ulamaa wanasema I’tikaaf inafaa katika Misikiti yote –ingawa wamekhitalifiana katika kushurutisha kama ni Msikiti Mkubwa "جامع" au mfano

wake- kutokana na ujumuishi wa Kauli Yake Ta’aalaa: فِي الْمَسَاجِدِ

 

Watu wamesema: Hakuna I’tikaaf isipokuwa katika Misikiti Mitatu: Al-Masjidul Haraam, Al-Masjid An-Nabawiy na Al-Masjid Al-Aqswaa. Hili limesemwa na Hudhayfah na Sa’iyd. [Bidaayatul Mujtahid (1/466)]

 

Madhehebu ya Jumhuri ndio yenye nguvu zaidi. Ama yanayosimuliwa kwa njia Marfu’u toka kwa Hudhayfah:

((لا اعتكاف إلا في المساجد الثلاثة))

((Hakuna I’tikaaf isipokuwa katika Misikiti Mitatu)). [Imekharijiwa na Al-Bayhaqiy (4/316), na Ismaa’iyl kama ilivyo katika Mu’ujamu Shuyuukhihii (3/721), Adh-Dhahabiy katika As-Siyar (5/81), Ibn Al-Jawziy katika At-Tahqiyq (1181) kupitia kwa Ibn ‘Uyaynah toka kwa Jaami’i bin Abiy Raashid toka kwa Abu Waail toka kwa Hudhayfah ikiwa Marfu’u. Ibn ‘Uyaynah amezozaniwa kwa kuisimulia kwa ‘Abdul Razzaaq (8016), na kupitia kwake At-Twabaraaniy (6/301-302) kwa Sanad yake toka kwa Hudhayfah ikiwa Marfuw’u. Ibraahiym ameifuatilia toka kwa Hudhayfah ikiwa Mawquwf kwa ‘Abdul Razzaaq (8014) na At-Twabaraaniy (9/301)]

 

‘Ulamaa wamekhitalifiana kuhusiana na kuwa Marfuw’u au Mawquwf.

 

Wanawake wanaruhusika kukaa I’tikaaf kwa masharti mawili:

 

Wanawake wanaruhusiwa kufanya I’tikaaf. Toka kwa ‘Aaishah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alidokeza kuwa atafanya I’tikaaf Kumi la Mwisho la Ramadhwaan. ‘Aaishah akamwomba ruksa, naye akamruhusu. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2045) na Muslim (1172)]

 

‘Aaishah amesema tena: ((Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa anakaa I’tikaaf katika Kumi la Mwisho la Ramadhwaan mpaka Allaah Ta‘aalaa Alipomfisha, kisha wakeze walikaa baada yake)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2026) na Muslim (1172)]

 

Kuna masharti mawili ya mwanamke kukaa I’tikaaf:

 

La kwanza: Apate ruksa ya mumewe

 

Kwa kuwa hatoki nyumbani kwake ila kwa idhini ya mumewe. Hadiyth ya ‘Aaishah iliyopita inaeleza kuwa alimwomba ruksa Rasuli kwa ajili ya I’tikaaf, pia Hafswah na Zaynab walifanya hivyo.

 

Faida

 

Mume akimruhusu mkewe kukaa I’tikaaf, je anaweza kumtoa asiendelee?

- Ikiwa I’tikaaf ni ya Sunnah, basi mume ana haki ya kumtoa, kwani Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa sallam) wakati ‘Aaishah alipomwomba ruksa ya kukaa I’tikaaf, kisha akamfuatia Hafswah halafu Zaynab, (Rasuli) alihisi kuwa hawana hasa niya ya kukaa I’tikaaf bali wanataka tu kuwa karibu naye kutokana na wivu wao kwake, akawatoa na kusema:

 

((...آلبر أردن؟ ما أنا بمعتكف..))

((..Je, wamekusudia [kweli] kupata thawabu? Mimi sikai I’tikaaf..)).  [Hadiyth Swahiyh.]

 

-  Ikiwa I’tikaaf yake ni ya waajib (kama ya nadhiri kwa mfano), na nadhiri ikawa ya kufatanisha siku (ameweka nadhiri I’tikaaf ya Kumi la Mwisho) na mumewe akamruhusu, basi hatokuwa na haki ya kumtoa. Na kama hakushurutisha kufuatanisha katika nadhiri yake, basi anaweza kumtoa kisha baadaye akakamilisha nadhiri yake. [Al-Majmuw’u cha An-Nawawiy (6/476)]

 

 

La pili: I’tikaaf yake isiwe sababu ya fitnah

 

Mwanamke atafanya I’tikaaf madamu hakuna fitnah. Na kama fitnah itamtokea yeye au kwa wanaume kutokana na I’tikaaf yake, basi atazuiwa na hatoruhusiwa, kwani Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliwazuia wakeze kukaa I’tikaaf kwa lisilo hilo kama ilivyotangulia katika Hadiyth ya ‘Aaishah.

 

Je ni sharti mtu afunge Swawm ndio akae I’tikaaf?

 

[Faida ya hili mahala pake: Akikaa I’tikaaf kwa isiyo Ramadhwaan kwa ajili ya nadhiri au mfano wake, au alikuwa akila Ramadhwaan kutokana na udhuru na akataka kukaa I’tikaaf]

 

‘Ulamaa wamekhitalifiana katika suala hili kwa kauli mbili:

 

Ya kwanza: I’tikaaf haifai bila Swawm

 

Ni madhehebu ya Abu Haniyfah, Maalik na Ahmad katika moja ya riwaya zake mbili, nayo imesimuliwa toka kwa ‘Aaishah, Ibn ‘Abbaas na Ibn ‘Umar. [Bidaayatul Mujtahid (1/470) na Tahdhiyb As-Sunan (7/104-109)]

 

Dalili zao ni:

 

1- Kuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikaa I’tikaaf katika Mwezi wa Ramadhwaan, na uthibiti wa I’tikaaf haukujulikana ila kwa Swawm, na haikuthibiti toka kwa Nabiy wala kwa yeyote katika Swahaba Zake kuwa walikaa I’tikaaf bila Swawm.

 

2- Ni kutajwa kwa pamoja I’tikaaf na Swawm katika Aayah moja.

 

3- Ni Hadiyth ya ‘Aaishah aliyesema: ((Sunnah kwa mwenye kukaa I’tikaaf asimzuru mgonjwa, asiende kuzika, asimguse mwanamke wala asimwingilie, na wala asitoke kwa haja yoyote isipokuwa ya dharura, na hakuna I’tikaaf isipokuwa kwa Swawm, na hakuna I’tikaaf isipokuwa katika Msikiti Mkubwa)). Imesimuliwa toka kwake ikiwa Marfu’u lakini si Swahiyh. [Isnaad yake ni Jayyid. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (2473) na Al-Bayhaqiy (4/315). Kuna mvutano kuhusiana na kuthibiti neno lake “Sunnah”, bali Ad-Daaraqutwniy amekata kuwa tamko lote limeandikwa toka kwenye maneno ya Az-Zuhriy, lakini Al-Albaaniy amemjibu katika Al-Irwaa (4/140)]

 

Ya pili: Si sharti Swawm kwa ajili ya I’tikaaf bali imestahabiwa

 

Ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy na Ahmad –katika kauli yake mashuhuri- nayo imesimuliwa toka kwa ‘Aliy na Ibn Mas’uwd. Dalili zao ni:

 

1- Kuwa ‘Umar alimwambia Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam): “Ee Rasuli wa Allaah! Hakika mimi nilikuwa nimeweka nadhiri enzi ya ujahilia ya kukaa usiku mmoja I’tikaaf ndani ya Al-Masjid Al-Haraam”. Rasuli akamwambia:

 

(فأوف بنذرك [فاعتكف ليلة]..))

((Basi tekeleza nadhiri yako [Akakaa I’tikaaf usiku mmoja]..)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2042) na Muslim (1656)]

 

Wamesema: Usiku si mahala pa Swawm, na (Rasuli) amejuzisha kufanya I’tikaaf wakati huo.

 

2- Katika riwaya ya Hadiyth ya ‘Aaishah iliyotangulia –kuhusiana na I’tikaaf za wakeze Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam)- akasema Rasuli alipoona vijihema vya wakeze:

 

((آلبر تردن))

((Je, mmekusudia [kweli] kupata thawabu?)). Akaamuru kijihema chake kivunjwe,  akaacha I’tikaaf katika Mwezi wa Ramadhwaan, na akaja kuifanya mwanzoni mwa Mwezi wa Shawwaal)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim kwa tamko hili (1172)]

 

Wamesema: Na Shawaal mosi ni siku ya kula, si halali kufunga.

 

3- Yaliyosimuliwa Marfu’u toka kwa Ibn ‘Abbaas:

 

((ليس على المعتكف صيام إلا أن يجعله على نفسه))

((Si lazima kwa mwenye kukaa I’tikaaf Swawm ila tu kama atajilazimishia Swawm mwenyewe)). Hadiyth hii ni Dhwa’iyf. [Imekharijiwa na Al-Haakim (1/605), Al-Bayhaqiy (4/318) na Ad-Daaraqutwniy (2/199) kwa Sanad Dhwa’iyf]

 

4- I’tikaaf ni ‘ibaadah inayojitegemea yenyewe, hivyo si sharti Swawm iwe ndani yake kama ‘ibaadah nyinginezo.

 

5- I’tikaaf ni kubakia sehemu maalum kwa ajili ya kumfanyia twa’a Allaah, hivyo Swawm si sharti iwe kiunganishi chake.

 

Ninasema: “Linaloonekana kuwa na nguvu ni kwamba si sharti Swawm  ili I’tikaaf ifanyike, bali imestahabiwa. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.

 

Muda wa chini zaidi wa I’tikaaf

 

[Bidaayatul Mujtahid (1/468) na Fat-hul Baariy (4/319)]

 

Jumhuri ya ‘Ulamaa wakiwemo Abu Haniyfah na Ash-Shaafi’iy wanasema kwamba hakuna mpaka wa chini wa muda wa kukaa I’tikaaf. Maalik kasema uchache wake ni mchana na usiku, na imepokewa toka kwake siku tatu, na imepokewa pia toka kwake siku kumi.

 

Linaloonekana ni kuwa mwenye kushikilia kwamba sharti ya I’tikaaf ni Swawm, basi haijuzu kwake kufanya I’tikaaf usiku. Hivyo hana cha uchache wa mchana na usiku kwa kuwa muda wake wa I’tikaaf ni mchana tu.

 

Ninasema: “Linaloonekana kuwa na nguvu ni kuwa uchache wake ni usiku mmoja kutokana na Hadiyth ya ‘Umar wakati Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alipomwamuru atekeleze nadhiri yake, akakaa usiku mmoja. Hili limeelezwa nyuma. Ama kauli ya Jumhuri isemayo kuwa inatosha chini ya usiku mmoja hata kitambo kidogo cha usiku na mchana, hili linahitaji dalili”.

 

Ni wakati gani anaingia mahala pa kufanyia I’tikaaf na wakati gani anatoka?

 

Mwenye kuweka nadhiri kukaa I’tikaaf siku za kuhesabika, au akataka kukaa I’tikaaf siku kumi za mwisho za Ramadhwaan, basi ni Sunnah aingie sehemu ya kufanyia I’tikaaf baada ya Swalaat Al-Fajr mwanzoni mwa masiku haya (ishirini na moja). Hivi ndivyo alivyofanya Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam). Katika Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa): ((Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa anakaa I’tikaaf katika Kumi la Mwisho la Ramadhwaan. Nilikuwa nikimfungia kijihema, akaswali As-Subhi, kisha akaingia ndani yake…)). [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma]

Hii ni kauli ya Al-Awzaa’iy, Al-Layth na Ath-Thawriy.

 

Maimamu wanne na kundi jingine la ‘Ulamaa wanasema kuwa ataingia muda mchache kabla ya kuchwa jua (tarehe 20). Wameiawilisha Hadiyth kuwa na maana kwamba aliingia mwanzo wa usiku, kisha huingia akabakia  peke yake mwenyewe ndani ya kihema baada ya Swalat As-Subh. Wamesema: Kwa kuwa kumi ni jina la idadi ya siku (nights), hivyo ni lazima aanze kabla usiku haujaanza.

 

Ninasema (Abu Maalik): “Hadiyth inalazimu moja kati ya mawili: Ima iwe imeweka sharia ya kukaa I’tikaaf kuanzia usiku –kama walivyosema- na yeye (Rasuli) aliingia ndani ya kijihema chake baada ya Alfajiri, na hii inaleta utata kwa waliozuia kutoka ndani ya ‘ibaadah baada ya kuingia ndani yake.

 

Au iwe imeweka sharia ya kuanza kukaa I’tikaaf baada ya Alfajiri. Na hili linatiliwa nguvu – kwa mimi ninavyoona- na Hadiyth ya Abu Sa’iyd Al-Khudriyy anayesema: ((Tulifanya I’tikaaf pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) katika Kumi la Kati la Ramadhwaan, tukatoka Asubuhi ya ishirini)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2036). Imetangulia nyuma]

 

Tunaelewa kutokana na Hadiyth hii kuwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alipokuwa anakaa I’tikaaf katika Kumi la Kati, alikuwa anatoka kwenye I’tikaaf asubuhi ya tarehe ishirini, na anaingia alfajiri ya tarehe kumi. Na hili linawafikiana na Hadiyth ya ‘Aaishah. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

Ama kutoka kwenye I’tikaaf, kwa mujibu wa kauli ya kwanza, atatoka baada ya Alfajiri ya Siku ya ‘Iyd kwenda sehemu ya kuswalia Swalaatul ‘Iyd, na hili limestahabiwa na Maalik. Na ama kwa mujibu wa kauli ya pili, atatoka baada ya kuchwa jua la siku ya mwisho ya Ramadhwaan. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

Yenye kubatwilisha I’tikaaf

 

I’tikaaf hubatwilika kwa moja ya yafuatayo:

 

(a) Kutoka bila ya udhuru wa kisharia au kwa haja ya dharura

 

Asitoke Msikitini ila kwa jambo lisilo na budi kihisia au kisharia. Mfano wa kwanza (kihisia) ni kutoka ili kupata chakula, kinywaji na kwenda haja ikiwa hili litamwelea uzito kama hakutoka. Na mfano wa pili (kisharia) ni kutoka kwa ajili ya kuoga janaba au kutawadha kama itashindikana kufanya hayo ndani ya Msikiti. Hili halina budi kisharia.

 

Toka kwa ‘Aaishah amesema: ((Na hakika Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa anaingiza kichwa chake –naye yuko Msikitini- nikamchana nywele zake, na alikuwa haingii nyumbani isipokuwa kwa haja anapokuwa yuko kwenye I’tikaaf)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2029) na Muslim (298)]

 

Na tamko lake lishatangulia nyuma lisemalo: ((Sunnah kwa mwenye kukaa I’tikaaf asimzuru mgonjwa, asiende kuzika, asimguse mwanamke wala asimwingilie, na wala asitoke kwa haja yoyote isipokuwa kwa jambo la lazima)).

 

Linatiliwa nguvu na Hadiyth ya ‘Amrah aliyesema: ((‘Aaishah katika I’tikaaf yake alikuwa anapotoka kwenda nyumbani kwake ni kwa ajili ya haja yake tu, humpitia mgonjwa akamjulia hali, naye hupita tu bila kukaa kumuuliza uliza)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na ‘Abdul Razzaaq katika Al-Muswannaf (8055)]

 

Akishurutisha katika niya yake kutoka kwa jambo maalum, kama kushurutisha kwamba atatoka kwenda kuzika au kwenda kazini kwake mchana –kama wafanyavyo baadhi ya wafanyakazi-, ‘Ulamaa wengi wamesema kuwa sharti yake haimfai, na kama atafanya basi I’tikaaf yake itabatilika.

 

Ath-Thawriy, Ash-Shaafi’iy na Is-Haaq –nayo ni riwaya toka kwa Ahmad- wanasema kuwa ikiwa ataweka sharti mwanzoni mwa I’tikaaf yake, basi haibatiliki kwa kitendo chake. Ni kama kushurutisha katika Hajji.

 

(b) Kujimai

 

‘Ulamaa wote kwa sauti moja wanasema mwenye kumwingilia mke wake katika utupu wake naye yuko katika I’tikaaf akikusudia hilo [akijua kuwa yuko I’tikaafni], basi I’tikaaf yake hubatilika. Ni kwa Kauli Yake Ta’aalaa:

((وَلَا تُبَاشِرُوهُنَّ وَأَنتُمْ عَاكِفُونَ فِي الْمَسَاجِدِ))

((Na wala msiwaingilie hali ya kuwa nyinyi ni wenye kukaa i’tikaaf Misikitini)). [Al-Baqarah (2:187)]

 

Jimai imekatazwa kwa umahususi wake katika ‘ibaadah, hivyo kuifanya hubatilisha ‘ibaadah. [Ash-Sharh Al-Mumti’u]

 

Ama kugusana naye bila kufikia upeo wa kujimai, na bila matamanio, basi hakuna ubaya. Ni kama mke kuosha kichwa chake, au kumpa kitu. Na hili ni kwa Hadiyth ya ‘Aaishah aliyesema:

 

((Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa anakiinamishia kichwa chake kwangu na yeye yuko jirani ndani ya Msikiti, nikamchana na mimi nina hedhi)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2029)]

 

Kama itakuwa kwa matamanio, basi hilo ni haramu kwa mujibu wa Aayah hii. Ikiwa atafanya na manii yakamtoka, I’tikaaf yake itaharibika, na kama hayakutoka, basi haitoharibika. Hili limesemwa na Abu Haniyfah na Ash-Shaafi’iy katika moja ya kauli zake mbili. Amesema katika kauli nyingine: Inaharibika katika hali zote mbili, na hii pia ni kauli ya Maalik, kwa kuwa huo ni mgusano ulioharamishwa, hivyo umeharibu I’tikaaf na kuwa sawa na kumwaga.

 

Ibn Qudaamah amesema: “Sisi kwa upande wetu huo ni mgusano, hauharibu Swawm wala Hijja, hivyo hauharibu I’tikaaf, kwa kuwa ni bila matamanio”. [Al-Mughniy (3/199)]

 

Yanayojuzu kwa mwenye kukaa I’tikaaf

 

(a) Kutoka kwa haja ya dharura

 

Ni kama kutoka kwenda kula, au kunywa, au kujisaidia kama itakuwa vigumu kufanya ndani ya Msikiti kama ilivyotangulia.

 

(b) Kujishughulisha na mambo yanayoruhusika

 

Ni kama kumsindikiza aliyemtembelea na kwenda naye hadi kwenye mlango wa Msikiti, au kuzungumza na mtu mwingine.

 

(c,d) Kutembelewa na mkewe, na kubaki naye faragha

 

Mambo matatu haya ya mwisho yamedondolewa toka kwenye Hadiyth ya mke wa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) Bi Swafiyyah: ((Alikwenda kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kumtembelea Msikitini katika Kumi la Mwisho la Ramadhwaan. Akakaa na kuzungumza naye saa, kisha akasimama kuondoka. Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akasimama pamoja naye na kumsindikiza mpaka alipofika mlango wa Msikiti kwenye mlango wa Ummu Salamah..)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2035) na Muslim (2175)]

 

(e) Kuoga na kutawadha ndani ya Msikiti

 

Toka kwa mtu aliyemhudumia Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema: ((Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alitawadha Msikitini wudhuu mwepesi)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Ahmad (5/364) kwa Sanad Swahiyh]

 

Tushaeleza ‘Aaishah kumwosha Rasuli kichwa na kumchana nywele zake.

 

(f) Kufunga hema lake la kukalia I’tikaaf mwisho wa Msikiti

 

Kwa kuwa ‘Aaishah alikuwa akimfungia Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kijihema anapokaa I’tikaaf. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2023)].

Na hilo lilikuwa ni kwa maagizo yake (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam).

[Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1173)]

 

(g) Kuleta tandiko lake au kitanda chake Msikitini

 

Toka kwa Ibn ‘Umar: ((Kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa anapokaa I’tikaaf, hutandikiwa tandiko lake au huwekewa kitanda chake nyuma ya nguzo ya At-Tawbah)). [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na Ibn Maajah (642)]

 

Hili linataarifiwa na yaliyomo ndani ya Hadiyth ya Abu Sa’iyd: ((…inapokuwa asubuhi ya ishirini, tunahamisha vitu vyetu…)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2040)]

 

(h) Kuposa na kufunga ndoa

 

[Al-Muwattwaa (1/318), Al-Muhallaa (5/192) na Al-Mughniy (3/205)]

Hili halina ubaya, kwa kuwa I’tikaaf ni ‘ibaadah isiyozuia kutumia manukato, na kwa hivyo haikuzuia ndoa kama Swawm. Lakini hili limeshurutishwa na kutojimai kama ilivyotangulia.

 

(i) Mwanamke mwenye damu ya istihaadhwah anaruhusiwa kufanya I’tikaaf

 

[Al-Majmuw’u (6/520) na Al-Mughniy (3/209)]

 

Lakini anatakikana ajichunge vizuri ili asije kuchafua Msikiti. Anaweza kutoka ili kubadili na kujisafisha kulinda usafi wa Msikiti.

 

Toka kwa ‘Aaishah amesema: ((Mwanamke mwenye damu ya istihaadhwah katika wakeze wa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikaa pamoja naye I’tikaaf. Alikuwa anaona wekundu na unjano, na huenda tuliweka beseni chini yake naye anaswali)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2037) na Muslim (2476)]

 

Je, inafaa mwenye hedhi kukaa I’tikaaf?

 

Mwenye hedhi kukaa I’tikaaf kunasimamia juu ya masuala mawili.

 

La kwanza: Je, ni lazima I’tikaaf iambatane na Swawm? La pili: Je mwenye hedhi anaingia Msikitini?

 

Anayeona kuwa ni lazima I’tikaaf iambatane na Swawm, basi kwa msingi huo, mwanamke atazuiliwa asikae I’tikaaf kwa kuwa hafungi. Na mwenye kuona kuwa mwenye hedhi haruhusiwi kuingia Msikitini, basi atazuiliwa asifanye I’tikaaf humo. [Jaami’u Ahkaamin Nisaa (2/430)]

 

Masuala haya yamefafanuliwa kwa mapana katika milango yake katika kitabu hiki. Unaweza kurejea huko. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

Faida

 

Mwanamke akikaa I’tikaaf Msikitini atajiwekea uzio wa kumsitiri asionekane

 

Wakeze Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) walipotaka kukaa I’tikaaf, waliamuru vijihema vyao vikafungwa ndani ya Msikiti. Kwa kawaida wanaume huhudhuria Msikitini, hivyo ni bora kwao na akina mama wasionane. Na kama wanawake watatengewa sehemu yao maalum Msikitini, basi ni bora zaidi. [Angalia kitabu changu cha Fiqhu As-Sunnah Lin Nisaa (uk 247) chapa ya At-Tawfiyqiyyah]

 

Kati ya adabu za I’tikaaf

 

Imestahabiwa kwa mwenye kukaa I’tikaaf ajishughulishe na amali za utiifu kwa Allaah kama kuswali, kusoma Qur-aan, kumdhukuru Allaah, kumwomba maghfirah, kuomba du’aa, kumswalia Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam), kuitafsiri Qur-aan, kudurusu Hadiyth na mfano wa hayo.

 

Si jambo zuri kujishughulisha na maneno au vitendo visivyo na faida, au kupafanya mahala pake pa I’tikaaf kuwa baraza ya masuhubiano ya watu, au mkusanyiko wa watembeleaji, au kurefusha sana mazungumzo na wenzake anaofanya nao I’tikaaf. Hii ni aina, lakini I’tikaaf ya Rasuli ni nyingine kabisa.

 

 

 

Share