13-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Tamko La Talbiyah

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah

 

13-Tamko La Talbiyah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Maana ya Talbiyah (التلبية) ni kuitikia Wito wa Allaah Ta’aalaa Alioutoa kwa Viumbe Vyake wakati Alipowaita kwenda kuhiji katika Nyumba Yake kupitia ulimi wa Kipenzi Chake Ibraahiym Alayhis Salaam. Na mwitikiaji (الملبي) [Hujaji] ni mwenye kujisalimisha na kuwa mtiifu kwa mwingine kama anavyoburuzwa aliyekunjwa shati kooni. Na maana: Mimi ni mwenye kukujibu Wito Wako, mwenye kujisalimisha kwenye Hukmu Yako, mwenye kutii Amri Yako, mara baada ya nyingine, na nitaendelea kuwa juu ya hayo.

 

Kayaeleza haya Sheikh wa Uislamu (Rahimahu-Allaah) akiizungumzia Hijjah ya Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam (uk. 550).

 

Toka kwa Naafi’i toka kwa Ibn ‘Umar kwamba Talbiyah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) ilikuwa:

 

((لبيك اللهم لبيك، لبيك لا شريك لك لبيك، إن الحمد والنعمة لك والملك، لا شريك لك))

 

Amesema: Na ‘Abdullaah bin ‘Umar alikuwa akiongezea tamko hilo kwa kusema:

 

((لَبَّيْكَ وَسَعْدَيْكَ، وَالْخَيْرُ فِي يَدَيْكَ،  والعمل))

 

[Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1549) na Muslim (1184) na ziada ni yake]

 

Na katika Hadiyth ndefu ya Jaabir: ((..na Rasuli akanyanyua sauti akitamka Tawhiyd akisema:

 

 ((لبيك اللهم لبيك، لبيك لا شريك لك لبيك، إن الحمد والنعمة لك والملك، لا شريك لك،))

 

Na watu wakaitikia kwa sauti kwa hili ambalo wanaliitikia (kivingine na tamko la Rasuli). Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) hakuwajibu kitu, bali aliendelea na Talbiyah yake..)). Hadiyth [Swahiyh. Imetajwa nyuma kamili]

 

Na katika riwaya: ((Na watu wakaitikia kwa sauti kwa hili ambalo wanaliitikia kwa sauti [kinyume na matamshi ya Rasuli]:

((لبيك ذا المعارج، لبيك ذا الفواضل))

Na Rasuli hakujibu….)).  [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1812) na Ahmad (13918)]

 

Na pia imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah kwa njia swahiyh kwamba: ((Ilikuwa ni katika Talbiyah yake –‘Alayhis Swalaat Was Salaam-:

((لبيك إله الحق))

[Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na An-Nasaaiy (2752) na Ibn Maajah (2920)]

 

Ninasema: “Tunapata faida mambo mawili kutokana na Hadiyth hizi:

 

 

1- Inajuzu kuongezea juu ya Talbiyah aliyoileta Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kwa kuwa aliwakubalia Swahaba wake kuongeza kwa yaliyothibiti toka kwa Ibn ‘Umar na wengineo.

 

2- Kutosheka na Talbiyah ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) ni bora zaidi kwa kuwa yeye alishikamana nayo. Ash-Shaafi’iy (Rahimahu-Allaah) amesema: “Kama ataongeza chochote katika Talbiyah cha kumtukuza Allaah, basi hakuna ubaya. Nami napenda mtu atosheke na Talbiyah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) tu”.

 

Na ameungana na madhehebu ya Jumhuri kama ilivyo katika Al Fat-h (3/480).

 

Mwahala Pa Kuleta Talbiyah

 

Imesuniwa kukithirisha kuleta Talbiyah tokea mtu anapohirimia na baada ya hapo wakati wote akiwa juu ya kipando, anatembea, anapanda, anashuka na katika hali zote mpaka atakapotupia Jamarat Al-‘Aqabah –kwa kauli ya Jumhuri- kinyume na Maalik.

 

Katika yanayoonyesha hilo ni kuwa uhalali wa Talbiyah umethibiti katika mwahala pafuatapo:

 

1- Wakati wa kupanda na kushuka njiani

 

Toka kwa Ibn ‘Abbaas ikiwa Marfuu: -katika Hadiyth ya Dajjaal- :

 

((أما موسى كأني أنظر إليه إذا انحدر في الوادي يلبي))

((Ama Muwsaa, kana kwamba mimi ninamwangalia naye anashuka kwenye bonde akipiga Talbiyah)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukaariy (1555) na Muslim (166)]

 

Al-Haafidh kasema: “Hadiyth inatuhabarisha kuwa Talbiyah katika vitovu vya mabonde ni katika mwenendo wa Mitume, na inakokotezeka zaidi wakati wa kuteremka na wakati wa kupanda”. [Fat-hul Baariy (3/485)]

 

 

2- Wakati wa kwenda ‘Arafaat

 

Toka kwa Anas bin Maalik kuwa aliulizwa –naye anatoka asubuhi mapema toka Minaa kwenda ‘Arafaat -kuhusu Talbiyah: Vipi mlikuwa mnafanya na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa wasallam)? Akasema: ((Mwenye kulabbiy alikuwa analeta Talbiyah na hakatazwi, na mwenye kuleta Takbiyr alikuwa analeta Takbiyr na hakatazwi)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1659) na Muslim (1284)]

 

3- Wakati wanapoondoka toka Kisimamo cha ‘Arafah mpaka watakapotupia vijiwe

 

Toka kwa Ibn ‘Abbaas kwamba Usaamah alikaa nyuma ya Nabiy (Swallah Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) [juu ya ngamia wa Nabiy] toka ‘Arafah hadi Muzdalifah, kisha Al- Fadhwl alikaa nyuma ya Nabiy toka Muzdalifah hadi Minaa.  Akasema: Wote wawili wamesema: Nabiy (Swalla  Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) hakuacha kupiga Talbiyah mpaka alipotupia vijiwe Jamaratul Aqabah)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1544) na Muslim]

 

An-Nawawiy kasema: “Na hii ni dalili kuwa ataendelea kuleta Talbiyah mpaka pale atakapoanza kutupia Jamaratul Aqabah asubuhi ya tarehe kumi (Yawm An-Nahr)”. [Yaani, riwaya ya Muslim isemayo: Hakuacha kuleta Talbiyah mpaka alipofika Al Jamarah]

 

 

Na haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy, Sufyaan, Ath-Thawriy, Abu Haniyfah, Abu Thawr, Jumhuri ya ‘Ulamaa katika Swahaba, Taabi’iyna, Fuqahaaul Amswaar na waliokuja baada yao.

 

Ahmad, Is-Haaq na baadhi ya Salaf wamesema: Ataleta Talbiyah mpaka amalize kutupia vijiwe Jamaratul Al-Aqabah. Lakini Jumhuri wamewajibu wakiwaambia kuwa muradi wake ni mpaka atakapoanza kutupia ili riwaya mbili zioanishwe.

Toka kwa Ibn Mas’uwd amesema: ((Nasi tukiwa Muzdalifah, nilimsikia yule ambaye ameteremshiwa Suwrat Al-Baqarah akisema katika sehemu hii tuliposimama:

"لبيك اللهم لبيك"

[Imekharijiwa na Muslim (1383) na An-Nasaaiy (5/265)]

 

Angalizo:

 

Maalik anasema kuwa ataikata Talbiyah wakati wa kuingia Makkah, atatufu na atasai, kisha ataanza tena kuleta Talbiyah hadi Adhuhuri ya Siku ya ‘Arafah. Dalili yao ni Hadiyth ya Naafi’u aliyesema: ((Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) alikuwa anapoingia mwanzoni mwa Al-Haram huacha Talbiyah, kisha hulala Dhuw Tuwaa, halafu huswali huko Asubuhi na huoga, na hueleza kuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alikuwa anafanya hivyo)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1573) na wengineo].

 

Al-Haafidh kasema: “Neno lake: ((alikuwa anafanya hivyo)), linachukulika kuwa linaashiria kitendo chake cha mwisho ambacho ni kuoga. Pia linachukulika kwa vyote, nalo ndilo lenye nguvu zaidi”. [Fat-hul Baariy (3/509)]

 

Lakini yeye amesema (Rahimahu-Allaah): “Inavyoonekana ni kuwa amekusudia kuwa atajizuia kuleta Talbiyah ndani ya Msikiti ambao ameutaja kama Al-Haram, na muradi wa kujizuia na Talbiyah ni kujishughulisha na kutufu na ‘ibaadah nyinginezo, na si kuiacha kabisa.

 

Pia inaonekana kuwa muradi wa kujizuia ni kuacha kuikariri Talbiyah, au kuendelea nayo mfululizo, au kunyanyua sauti katika kuileta, mambo ambayo hufanyika mwanzoni mwa kuhirimia, na si kuiacha kabisa. Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi”.

 

 

 

Share