18-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Hukmu Kiujumla Kuhusu Twawaaf

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah

 

18-Hukmu Kiujumla Kuhusu Twawaaf

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Shuruti Za Kutufu

 

1- Je, mwenye kutufu ni lazima awe twahara?

 

Jumhuri ya ‘Ulamaa –kinyume na Mahanafiy, riwaya toka kwa Ahmad na Ibn Hazm- wanasema kutwaharika na hadathi na najisi ni sharti ya kuswihi Twawaaf. Ikiwa atatufu bila twahara na vitu hivyo, basi Twawaaf yake ni batili, haihesabiwi.

 

Hoja yao ni Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas toka kwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliyesema:

 

((الطواف بالبيت صلاة إلا أن الله أباح فيه الكلام))

((Kutufu Nyumba ni Swalaah isipokuwa Allaah Ameruhusu ndani yake maneno)). [Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (960), An-Nasaaiy (2922), Al-Haakim (1/630) na wengineo. Haifai kuwa Marfuw’u, na sawa ni kuifanya Mawquwf kama alivyoielezea Sheikh wetu katika Kitabu cha Jaami’u Ahkaamin Nisaa (2/515-521), kinyume na Al-‘Allaamah Al-Albaaniy ambaye amesema ni sahihi kuwa Marfuw’u katika Al-Irwaa (1/156)]

 

Hoja hii inapingwa kwa hoja kadhaa:

 

(a) Hadiyth hii haifai kuwa Marfuw’u, na la sawa ni Hadiyth Mawquwf kutokana na maneno ya Ibn ‘Abbaas. Haya yametiliwa nguvu na At-Tirmidhiy, Al-Bayhaqiy, Ibn Taymiyah, Ibn Hajar na Sheikh wetu Mustwafaa Al-‘Adawiy.

 

(b) Hata tukisema ni Swahiyh, lakini hata hivyo, hailazimu kutokana nayo kuwa Twawaaf ifanane na Swalaah katika kila kitu mpaka ishurutishiwe yanayoshurutishwa kwa Swalaah. [Angalia njia za kupambanua kati ya Swalaah na Twawaaf katika Jaami’u Ahkaamin Nisaa (2/522)]

 

(c) Idadi kubwa ya Waislamu ambao idadi yao hakuna aijuaye isipokuwa Allaah ‘Azza wa Jalla, walikuwa wanatufu enzi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) na halikunukuliwa lolote kuwa aliwahi kumwamuru yeyote kati yao atawadhe kwa ajili ya Twawaaf yake, pamoja na kuwepo uwezekano wa wengi wao kuwa walitengukwa na wudhuu, na wengi wao pia kuingia kwenye Twawaaf bila ya wudhuu, na hususan sambamba na msongamano mkubwa katika Twawaaf ya Quduwm na Ifaadhwah. [Jaami’u Ahkaamin Nisaa (2/515) kwa mabadilisho madogo. Angalia Majmuw’u Al-Fataawaa (21/273)]

 

Na kwa ajili hiyo, Sheikh wa Uislamu amesema katika Al-Fataawaa (6/198): “Imebainika kuwa twahara ya hadathi haishurutishwi katika Twawaaf na si wajibu kwayo bila shaka, lakini imesuniwa kuwa na twahara ndogo (wudhuu), kwa kuwa dalili za kisharia zinadulisha kuwa si wajibu kwa Twawaaf, na hakuna katika sharia linalodulisha ulazima wa kuwa na wudhuu”.

 

Na Ibn Hazm (7/179) amesema: “Kutufu Nyumba bila ya twahara kunajuzu”.

 

Ni chaguo pia la Al-‘Allaamah Ibn ‘Uthaymiyn –Allaah Amrehemu- katika Al-Mumti’u (7/300).

 

Ninasema: “Pamoja na kutilia nguvu kujuzu kutufu bila wudhuu, lakini hakuna shaka kuwa ni vizuri kuwa nao kutokana na Hadiyth ya ‘Aaishah aliyesema: ((Jambo la kwanza aliloanza nalo Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) wakati alipokuja ni kuwa alitawadha, kisha akatufu kisha…)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5/16) na Muslim (1235)]

 

Na pia kwa ujumuishi wa dalili zenye kustahabisha kufanya dhikr mtu akiwa na twahara. Lakini pamoja na hivyo, sisi hatuwezi kumlazimisha aliyetengukwa na wudhuu wakati anatufu, aende kutawadha katikati ya msongamano mkubwa bila kuwepo dalili bayana. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.

 

Haya yote ni kuhusu kutwaharika na hadathi ndogo. Ama hadathi kubwa kama hedhi, nifasi na janaba, inavyoonekana ni kuwa ni lazima kujitwaharisha nazo kwa mwenye kutufu kutokana na neno lake Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kwa ‘Aaishah:

 

((افعلي ما يفعل الحاج غير أن لا تطوفي بالبيت))

((Fanya (yote) ayafanyayo mwenye kuhiji isipokuwa tu usitufu Nyumba)). [Hadiyth Swahiyh. Takhriyj yake imetajwa nyuma]

 

Hivyo basi, mwenye kutufu naye ana hadathi kubwa –bila ya udhuru- kisha akarejea kwao, basi hukmu yake ni hukmu ya ambaye hakutufu asilani kwa mujibu wa kauli ya Maalik na Ash-Shaafi’iy. Abu Haniyfah amesema: “Atapeleka mnyama [Makkah], na itamtosheleza”. [At-Tamhiyd cha Ibn ‘Abdul Barr (19/262)]

 

 

2- Kusitiri uchi:

 

Haijuzu kwa yeyote kutufu Nyumba akiwa uchi. Akitufu uchi, haitomtosheleza kwa kauli ya Jumhuri. Ni kwa Neno Lake Ta’aalaa:

 

((يَا بَنِي آدَمَ خُذُوا زِينَتَكُمْ عِندَ كُلِّ مَسْجِدٍ))

((

Enyi wana wa Aadam! Chukueni mapambo yenu (ya mavazi ya sitara na twahara) katika kila mahala pa ‘Ibaadah)). [Al-A’araaf (7:31)]

 

Na kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah: ((Kwamba Abu Bakr As-Swiddiyq (Radhwiya Allaah ‘anhu) alimtuma katika Hajj ambayo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimpa uongozi kwa kundi la watu kabla ya Hajj ya Kuaga Siku ya Kuchinja awatangazie watu:

((ألا لا يحج بعد العام مشرك، ولا يطوف بالبيت عريان))

((Jueni na tambueni! Asihiji mpagani baada ya mwaka (huu), na asitufu mtu Nyumba akiwa uchi)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (369) na Muslim (1347)]

 

‘Ulamaa wa Kihanafiy wamesema: Kusitiri uchi ni lazima katika Twawaaf na si sharti ya kuswihi. Atakayetufu uchi, basi Twawaaf yake itabatwilika kwa maneno ya Jumhuri.

 

Ama kwa Mahanafiy, Twawaaf itaswihi lakini ni lazima achinje.

 

 

3- Twawaaf iwe nje ya Nyumba (Al-Ka’abah)

 

Allaah Ta’aalaa Amesema:

((وَلْيَطَّوَّفُوا بِالْبَيْتِ الْعَتِيقِ))

((na watufu kwenye Nyumba ya Kale [Al-Ka’bah])). [Al-Hajj (22:29)]

 

Na lau atatufu katika “Al-Hijr”, basi Twawaaf yake haiswihi. Na “Al-Hijri” ni sehemu iliyozungushwa nusu duara ukuta pembeni kidogo mwa Al-Ka’abah kwa upande wake wa mashariki. Inaitwa pia “Al-Hatwiym” na “Al-Jadr”.  Kutoswihi huku ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam:

 

((الحجر من البيت))

((Al-Hijr ni sehemu ya Al-Ka’abah)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (876), Abu Daawuwd (2028) na Ibn Maajah (2955). Asili yake ni kutoka Swahiyh Mbili toka kwa ‘Aaishah]

 

“Al-Hijr” ilikuwa ni sehemu ya Al-Ka’abah na Maqurayshi waliiacha kutokana na ufinyu wa fedha za kukamilishia, hivyo wakatosheka kuzungushia sehemu hiyo ya ukuta. Hivyo basi, ili Twawaaf iswihi, ni lazima iwe nje ya kijikuta hicho, na kama si hivyo, itabatilika kwa mujibu wa kauli ya Jumhuri.

 

Ama Mahanafiy, wao wanasema ni lazima atufu upya madhali bado yuko Makkah, na kama amesharejea kwao, basi ni lazima atoe mnyama amtume Makkah.

 

 

4,5- Aanze Twawaaf yake tokea kwenye Jiwe Jeusi (Al-Hajar Al-As-wad) na amalizie na kuanzia mizunguko hapo hapo, na Al-Ka’abah iwe kushotoni mwake

 

Ni kwa Hadiyth ya Jaabir: ((Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alipoingia Makkah, aliliendea Jiwe Jeusi akaligusa kwa mkono, kisha akaenda kwa kuliani mwake, akatembea mwendo kasi kidogo mara tatu [mizunguko mitatu ya mwanzo], na mwendo kawaida mara nne [mizunguko minne ya mwisho])). [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa kamili nyuma pamoja na takhriyj yake]

 

Na hili ni sharti la kutufu kwa Jumhuri kutokana na Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) kuendelea kufanya hivyo, na kwa kuwa pia ni ubainisho wa ujumla wa agizo la Qur-aan la kutufu, na likawa katika uhakika wake. Na kwa neno lake Nabiy:

 

((من عمل عملا ليس عليه أمرنا فهو رد))

((Mwenye kufanya ‘amali yoyote isiyo juu ya amri yetu, basi anarejeshewa mwenyewe)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy katika mlango wa biashara, na Muslim (1718)]

 

 

6- Iwe mizunguko saba kamili

 

Kwa kuwa ndivyo alivyofanya Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akibainisha kipimo kinachotakikana cha Twawaaf kwa mujibu wa Agizo Lake (تعالى)

  ((وَلْيَطَّوَّفُوا))

”Na watufu”,

 

Hivyo inakuwa ni lazima. Na haya ni madhehebu ya Jumhuri. Na kama ataacha hatua moja [ya kumalizia au akaruka ya kuanzia] katika mzunguko wowote, basi mzunguko huo hauhesabiwi.

 

Ama Mahanafiy, wao wamekufanya kuzunguka zaidi ya mara saba kuwa ni nguzo, na chini iliyobaki kuwa ni wajibu, na si nguzo. Na hili linakataliwa kwa kuwa vipimo vya matendo ya’ibaadah havijulikani kwa rai za watu wala ijtihaad, bali ni kwa “Tawqiyf”(Uainisho toka  kwenye Qur-aan na Sunnah) na vyanzo vya kisharia. Ni kama mtu aliyepunguza rakaa moja katika Swalaah yake, Swalaah hii haijuzu. Na kwa ajili hiyo, Al-Kamaal bin Al-Hammaam –ambaye ni katika Fuqahaa wa Kihanafiy- amelikataa hili akisema: “Tunalolifuata ni kuwa haijuzu chini ya saba, wala baadhi yake haziungwi kwa chochote”. [Nihaayatul Muhtaaj (2/409), Badaai’u As-Swanaai’i (2/132) na Fat-hul Qadiyr (2/247)]

 

Akifanyia shaka idadi ya mizunguko

 

Akifanyia shaka ni mizunguko mingapi amezunguka naye bado anatufu, basi atalichukulia la uhakika, nalo ni idadi ndogo [yaani akifanyia shaka kati ya minne au mitano, basi atachukulia ni minne]. Hii ni kauli ya Jamhuiri ya Fuqahaa, na imenukuliwa toka kwa Ibn Al-Mundhir Ijma’a juu ya hilo. [Al-Mughniy (3/378) na Al-Majmuw’u (8/25)]

 

Ninasema: “Lakini kama uhakika wa idadi kubwa utakuwa na nguvu zaidi kwake, basi ataichukulia hiyo hiyo. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.

 

 

7- Kuandamisha kati ya mizunguko

 

Kwa maana ya kutoachanisha mzunguko na mzunguko kwa muda mrefu. Na hili ni sharti la Kutufu kwa ‘Ulamaa wa Kimaalik na Kihanbali. Kuna kauli kwa ‘Ulamaa wa Kishaafi’iy inayosema kuandamisha ni wajibu. Ama kwa ‘Ulamaa wa Kihanafiy na Kishaafi’iy ni Sunnah.

 

Na mwenye kukata Twawaaf yake kwa udhuru kama kwenda haja au kutawadha –kwa mwenye kuliona hilo ni sharti- au kuswali Swalaah ya Faradhi, au kupumzika kutokana na mchoko, basi atakuja kukamilishia idadi aliyofikia. Lakini kama ataikata Twawaaf kipuuzi bila udhuru, basi itabatwilika. [Angalia Al-Muhallaa cha Ibn Hazm (7/180)]

 

 

 

Share