21-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Ahkaam Za Sa’yi Baina Ya As-Swafaa Na Al-Marwah

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah

 

21-Ahkaam Za Sa’yi Baina Ya As-Swafaa Na Al-Marwah

 

Alhidaaya.com

 

 

Shuruti za Sa’yi

 

Ili Kusai baina ya As-Swafaa na Al-Marwah kuwe sahihi, ni sharti mambo yafuatayo:

 

1- Kufanyike baada ya Twawaaf sahihi –kwa mujibu wa Jumhuri- kama ilivyotangulia.

 

2- Iwe mizunguko saba. Kutoka As-Swafaa hadi Al-Marwah ni mzunguko, na kutoka Al-Marwaa hadi As-Swafaa ni mzunguko na kuendelea. Akifanya shaka kuhusu idadi kabla hajamaliza, ni lazima ajengee dhana katika idadi chache kama ilivyo katika Twawaaf (yaani akishakia kati ya nne na tano, basi afanye kuwa ni nne).

 

3- Aanzie toka As-Swafaa na amalizie Al-Marwah. Akifanya kinyume kwa kuanzia mzunguko wake wa kwanza toka Al-Marwah, basi mzunguko huu hauhesabiki. Lau ataianza mizunguko yake kutokea As-Swafaa na akaumalizia wa saba As-Swafaa, basi wa kwanza hauhesabiki, na atabakiwa na wa saba. [Ibn Hazm alipitikiwa na wazo lenye makosa akadai kwamba mtu atakwenda kasi katika mizunguko mitatu na atatembea kawaida mizunguko minne iliyobakia, na wengine katika hali hiyo hiyo, wameifanya mizunguko kumi na nne, na wote wana makosa kama alivyobainisha Ibn Al-Qayyim katika Az Zaad (2/231)]

 

4- Kusai kufanyike kwenye eneo lake maalum ambalo ni barabara iliyonyooka baina ya As-Swafaa na Al-Marwah.

 

Shuruti hizi zote ni kutokana na alivyofanya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) mwenye kusema:

((خذوا عني مناسككم))

((Jifunzeni kutoka kwangu matendo yenu ya Hajj)). [Al-Majmuw’u (8/95)]

 

 

Sunnah za Sa’yi

 

1- Mwenye Kusai awe na twahara, kwa kuwa ni dhikr kama ilivyo kwenye Twawaaf.

 

2- Aiguse nguzo kabla hajatoka kwenda sehemu ya Kusai kama ilivyo kwenye Hadiyth ya Jaabir.

 

3,4- Anapokurubia As-Swafaa asome:

إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَائِرِ اللَّـهِ 

na atasema:

 

 أبدأ بما بدأ الله به

 

Na hili liko katika Hadiyth ya Jaabir.

 

5,6- Aelekee Qiblah anapokuwa juu ya As-Swafaa na aseme:

 

((لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ وَحْدَهُ لَا شَرِيكَ لَهُ، لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ، وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ، لَا إِلَهَ إِلَّا اللَّهُ وَحْدَه،  اَنْجَزَ وَعْدَهُ وَنَصَرَ عَبْدَهُ وَهَزَمَ الأحْزابَ وَحْدَهُ))

Kisha aombe alitakalo. Atafanya hivi mara tatu.

 

 

7- Atembee kawaida kwenda Al-Marwah na anaweza kupanda (kipando) kama kuna haja. Katika Hadiyth ya Jaabir: ((Kisha aliteremka kuelekea Al-Marwah, na hata miguu yake ilipojikita barabara katika kitovu cha bonde alikwenda kasi kidogo, na miguu ilipopanda alitembea kawaida mpaka akafika Al-Marwah, akafanya juu ya Al-Marwah kama alivyofanya juu ya As-Swafaa)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1297), Abu Daawuwd (1970) na An-Nasaaiy (3062)]

 

Ibn ‘Abbaas amesema alipoulizwa kuhusu Kusai kwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) baina ya As-Swafaa na Al-Marwah akiwa amepanda: ((Hakika watu wengi walimzonga Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) wakisema: Huyu Muhammad, huyu Muhammad, mpaka wakatoka wasichana vigori toka majumbani.. na walipozidi kumzonga, alipanda [mnyama]. Na kutembea kawaida na kwa kasi kidogo ni bora zaidi [kuliko kupanda])). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1264) toka Hadiyth ya Abiy At-Twufayl].

 

8- Kwenda mchakamchaka wa nguvu kidogo kati ya alama mbili za kijani

Hili ni kwa wanaume tu na si kwa akina mama kama katika Twawaaf.

 

9- Kuomba du’aa baina ya As-Swafaa na Al-Marwah kama ilivyothibiti toka kwa Ibn Mas‘uwd kwamba alikuwa anasema:

((رب اغفر وارحم، إتك أنت الأعز الأكرم))

[Hadiyth Swahiyh Marfuw’u. Imekharijiwa na Ibn Abiy Shaybah (4/68) na At-Twabaraaniy katika Ad-Du’aa (870)]

 

10- Afanye juu ya Al-Marwah kama alivyofanya juu ya As-Swafaa kama kusoma, kuleta tahliyl na takbiyr, kuelekea Qiblah na kuomba du’aa.

 

 

 

Share