31-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Hajj Na 'Umrah: Kutekeleza ‘Umrah Na Fadhila Zake

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Hajj Na ‘Umrah

 

31-Kutekeleza ‘Umrah Na Fadhila Zake

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Taarifu yake

 

Maana ya العمرة katika lugha ni ziara, au kupakusudia mahala paliposhamiri. Imeitwa hivi kwa kuwa inafanywa katika umri wote.

 

Ama kisharia, ni kuikusudia Al-Ka’abah kwa ajili ya Nusuk ambayo ni Kutufu na Kusai. [Mughnil Muhtaaj (1/460) na Kash-Shaaful Qina’a (2/436)]

 

 

Hukmu yake

 

‘Ulamaa wamekhitalifiana katika hukmu ya ‘Umrah kwa aliyewajibikiwa na Hajj katika kauli mbili:

 

Ya kwanza: ‘Umrah ni waajib mara moja tu katika umri wote

 

 

Ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy katika moja ya kauli zake mbili., na moja ya riwaya mbili toka kwa Ahmad. Imesimuliwa toka kwa  ‘Umar, Ibn ‘Abbaas, Zayd bin Thaabit, Ibn ‘Umar na kundi la Masalaf.  Ni kauli pia ya Ahlu Adh-Dhwaahir. [Al-Ummu (2/132), Al-Majmuw’u (7/3,7), Al-Mughniy (3/218), Al-Inswaaf (3/387) na Al-Muhallaa (7/360)]

 

 

Hoja zao ni:

 

1- Kauli Yake Ta’aalaa:

((وَأَتِمُّوا الْحَجَّ وَالْعُمْرَةَ لِلَّـهِ))

((Na timizeni Hajj na ‘Umrah kwa ajili ya Allaah)). [Al-Baqarah (2:196)]

 

2- Hadiyth ya ‘Aaishah aliyesema: ((Ee rasuli wa Allaah! Je ni waajib kwa wanawake Jihaad? Akasema:

((نعم عليهن جهاد لا قتال فيه: الحج والعمرة))

((Na’am, ni juu yao Jihaad isiyo na mapigano ndani yake; Hajj na ‘Umrah)). [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh. Imekharijiwa na Ahmad (6/71) na Ibn Maajah (2901). Al-Irwaa (981) amesema: “Na hii Isnaad yake ni Swahiyh juu ya sharti ya Masheikh wawili. Ninasema: “Hadiyth iliyopo kwa Al-Bukhaariy (1520) na An-Nasaaiy (5/86) haikutaja ‘Umrah, na matokeo ya Hadiyth ni mamoja, hivyo uthibiti wa tamko hilo utafitiwe. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”]

 

Neno lake (عليهن) linadulisha ulazima.

 

3- Hadiyth ya Adh-Dhubaa bin Ma’abad amesema: ((Nilimwendea ‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhu) nikamwambia: Ee Amiyrul Muuminiyn. Hakika mimi nimesilimu. Na mimi nimekuta Hajj na ‘Umrah zimefaradhiwa kwangu, nami nimezinuwia. Akamwambia:

((هديت لسنة نبيك))

((Umehidiwa kwenye Sunnah ya Nabiy wako)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na An-Nasaaiy (2/13-14), Abu Daawuwd (1799) na Ibn Maajah (2970). Angalia Al-Irwaa (2970)]

 

 

4- Jumhuri wanasema ‘Umrah ni Hajj ndogo. [Angalia Al Fat-h (6/322,8)/172) na Tafsiyr At-Twabariy (10/75)]

 

Ya pili: ‘Umrah ni Sunnah na si waajib 

 

Ni madhehebu ya Abu Haniyfah na Maalik. [Al-Mudawwanah (1/370), Fat-hul Qadiyr (2/306) na Al-Badaai’u (3/1320)]

 

Ni kauli kongwe ya Ash-Shaafi’iy, riwaya nyingine toka kwa Ahmad, nayo imesimuliwa toka kwa Ibn Mas-‘uwd, na chaguo la Sheikh wa Uislamu Ibn Taymiyah. Hoja zao ni:

 

 

1- Yaliyosimuliwa toka kwa Jaabir: ((Kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) aliulizwa, je ‘Umrah ni waajib? Akasema:

((لا، وأن تعتمروا فهو أفضل))

((Hapana, mkifanya ‘Umrah, basi hilo ni bora kwenu)). [Hadiyth Dhwa’iyf. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (939)]

 

2- Yaliyosimuliwa kwa njia Marfuw’u toka kwa Twalha:

((الحج جهاد، والعمرة تطوع))

((Hajj ni Jihaad, na ‘Umrah ni kujitolea [Sunnah])). [Hadiyth Dhwa’iyf. Imekharijiwa na Ibn Maajah (2989)]

 

 

3- ‘Umrah na Hajj ni ‘ibaadah mbili za jinsi moja. Ukiifanya kubwa, basi ndogo inakuwa si waajib. Ni kama kutawadha pamoja na kuoga, ingawa kutawadha pamoja na kuoga ni bora zaidi na ukamilifu zaidi. [Majmuw’u Al-Fataawaa (26/9)]

 

Na hivi ndivyo alivyofanya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam), lakini aliwaamuru kufanya Tamattu’u, na akasema:

((دخلت العمرة في الحج إلى يوم القيامة))

((‘Umrah imeingia ndani ya Hajj mpaka Sikuya Qiyaamah)). [Hadiyth Swahiyh. Takhriyj yake imetajwa nyuma]

 

 

4- Kwamba ndani ya ‘Umrah hakuna tendo lolote zaidi ya matendo yaliyomo kwenye Hajj, na matendo hayo ya Hajj Allaah Ameyafaradhisha mara moja tu, na si mara mbili. Hivyo tunapata kujua kuwa Allaah Hakufaradhisha ‘Umrah. [Majmuw’u Al-Fataawaa (26/8)]

 

 

Ninasema: “Ama Hadiyth ambazo kundi la pili limezitolea ushahidi, hakuna Hadiyth yoyote kati yake ambayo ni Swahiyh. Pamoja na hivyo, hoja za wenye kusema ‘Umrah ni waajib (ambao ni kundi la kwanza) pia haziko dhahiri bayana kuwajibisha ‘Umrah. Tukichukua Kauli Yake Ta’aalaa:

 

وَأَتِمُّوا الْحَجَّ وَالْعُمْرَةَ لِلَّـهِ

tutaona kwamba uwajibu wa hapa ni wa kutimiza matendo kwa aliyeanza kutekeleza ‘ibaadah hizo mbili. Ama katika kuanza, Allaah Amewajibisha Hajj tu Aliposema:

 

 وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ

((Na kwa ajili ya Allaah, imewajibika watu watekeleze Hajj))

 

Na hakuwajibisha ‘Umrah. Ama kusema ‘Umrah ni Hajj ndogo, Ibn Taymiyah ameufanya usemi huu kuwa hoja dhidi ya wenye kusema ni waajib na si hoja ya kutilia nguvu usemi wao, kwa kuwa wanaposema Hajj ndogo, itamaanisha kuwajibishwa Hajj mbili (ndogo na kubwa), nalo ni jambo ambalo haliwezekani.

 

Muhimu, la salama na la akiba zaidi, ni kuitekeleza ‘Umrah bila kuiacha kutokana na uwezekaniko wa kuthibiti ziada ya neno “’Umrah” katika Hadiyth ya ‘Aaishah (iliyotangulia nyuma), na uwezekaniko wa kuwa muradi wa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

 دخلت العمرة في الحج كهاتبن

((‘Umrah imeingia ndani ya Hajj kama viwili hivi))

 

Kuwa uwajibu wa ‘Umrah ni kama wa Hajj, na kwa kuwa kutenda kwa kutegemea dalili za uwajibu, dhima husalimika kwazo kwa mujibu wa Ijma’a. Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.

 

Fadhila ya ‘Umrah

 

[Irshaadus Saariy ‘Anil Wajiyz (uk. 266)]

 

‘Umrah ni katika ‘Ibaadah zilizotukuka sana, na ni miongoni mwa vikurubisho bora kabisa ambavyo Allaah Huwapandishia kwavyo Waja Wake daraja na kuwaporomoshea kwavyo makosa. Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) ameihimizia kwa maneno na kivitendo.

 

1- Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

 

((العمرة إلى العمرة كفارة لما بينهما))

((‘Umrah hadi ‘Umrah, ni kafara ya yaliyo kati yake)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1773) na Muslim (1349)]

 

2- Na amesema:

 

((تابِعُوا بَيْنَ الْحَجِّ وَالْعُمْرَةِ، فَإِنَّهُمَا يَنْفِيَانِ الْفَقْرَ وَالذُّنُوبَ كَمَا يَنْفِي الْكِيرُ خَبَثَ الْحَدِيدِ والذهب والفضة))

((Fatanisheni baina ya Hajj na ‘Umrah, kwani viwili hivi huondosha umasikini na madhambi, kama vile mivukuto [ya mhunzi] inavyoondosha uchafu wa chuma, dhahabu na silva)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (807) na An-Nasaaiy (5/115). Angalia Swahiyh Al-Jaami’u (2899)]

 

3- Nabiy (‘Alayhis Swalaat was Salaam) alifanya ‘Umrah, na Swahaba wake wakafanya ‘Umrah pamoja naye wakati wa uhai wake na baada ya kufariki kwake.

 

 

Wakati wake

 

Inajuzu kufanya ‘Umrah katika siku zote za mwaka –kwa mujibu wa kauli ya Jumhuri- isipokuwa katika siku za Ramadhwaan inakuwa ni bora zaidi. Ni kwa kauli yake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam)

((عُمرَةٌ في رمَضَانَ تَعدِلُ حجة - أو حَجَّةً مَعِي))

((‘Umrah katika Ramadhwaan inalingana [kwa thawabu] na Hijjah - au kuhiji pamoja nami)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1782) na Muslim (1256)]

 

 

‘Umrah inajuzu kabla ya Hajj

 

Toka kwa ‘Ikrimah bin Khaalid: ((Kwamba alimuuliza Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) kuhusu kufanya ‘Umrah kabla ya Hajj akajibu: Hakuna ubaya kuifanya, kwani Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alifanya ‘Umrah kabla hajahiji)). [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1774)]

 

Je, ni sharia kufanya ‘Umrah mara kwa mara?

 

Kukariri ‘Umrah kunakuwa katika hali mbili:

 

Hali ya kwanza: Kuirudia rudia katika mwaka mmoja kwa safari za kwenda na kurudi

 

‘Ulamaa wamekhitalifiana kwa kauli mbili kuhusu hali hii: [Majmuw’u Al-Fataawaa (26/267) na kurasa zinazofuatia, na Al-Majmuw’u cha An-Nawawiy (7/140)]

 

Kauli ya kwanza:  Ni makruhu. Ni kauli ya Hasan, Ibn Syriyna na An-Nakha’iy, ni madhehebu ya Maalik, na chaguo la Sheikh wa Uislamu.

 

Hoja yao ni kuwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) na Swahaba wake hawakufanya ‘Umrah mara mbili kwa mwaka. Hivyo ni makruhu kuzidisha zaidi ya walivyofanya. Pia, ‘Umrah ni Hajj ndogo, na Hajj haifanywi katika mwaka ila mara moja tu, na hivyo hivyo ‘Umrah.

 

Kauli ya pili: Inajuzu na ni Sunnah. Ni madhehebu ya Jumhuri wakiwemo ‘Atwaa, Twaawuws, ‘Ikrimah, Ash-Shaafi’iy na Ahmad. Imesimuliwa pia toka kwa ‘Aliyy, Ibn ‘Umar, Ibn ‘Abbaas na ‘Aaishah.

 

Hoja yao ni kuwa ‘Aaishah kwa amri ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alifanya ‘Umrah mara mbili katika mwezi mmoja; ‘Umrah yake ambayo ilikuwa pamoja na Hajj, na ‘Umrah aliyoinuwia toka At-Tan-’iym (baada ya kumalizika Hajj).

 

Pia wametolea dalili Hadiyth isemayo:

((العمرة إلى العمرة كفارة لما بينهما))

((Umrah hadi ‘Umrah, ni kafara ya yaliyo kati yake)). [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma kidogo]

 

Na Hadiyth ya ‘Aaishah: ((Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alifanya ‘Umrah mbili: ‘Umrah katika Dhul- Qa-’adah, na ‘Umrah katika Shawwaal)). [Isnaad yake ni Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1991) na Al-Bayhaqiy (5/11)]

 

Ninasema: “Ninaloliona linaniridhisha ni kuwa madhehebu ya Jumhuri ndiyo yenye nguvu. Kwani ‘Umrah ni ‘amali ya kheri, na halikuja katazo lolote la kuwa isirudiwe rudiwe. Na kuifanyia Qiyaas kwa Hajj –kuwa ni mara moja tu- hakufai, kwa kuwa ‘Umrah haikuwekewa wakati maalum kinyume na Hajj. Isitoshe,  Hajj haiwezekaniki ikakariri katika mwaka mmoja. Hivyo kuilinganisha na ‘Umrah hakufai. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

Hali ya pili: Kuirudia rudia kwa safari moja

 

Makhitalifiano katika suala hili ni mfano wa makhitalifiano yaliyo kabla yake. Na kauli yenye nguvu hapa ni kuwa si sharia mtu kufanya ‘Umrah nyingi katika safari moja kama wafanyavyo watu wengi leo ambao wanatoka kwenda hadi At-Tan-‘iym –baada ya Hajj mfano- kisha wanafanya ‘Umrah. Hili Rasuli hakulifanya, bali ((‘Umrah zote za Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alizifanya akiwa ndani ya Makkah. Na yeye alikaa Makkah baada ya wahyi kuanza kumshukia kwa miaka kumi na tatu, na haikunukuliwa kamwe toka kwake kuwa alifanya ‘Umrah akitoka nje ya Makkah katika muda wote huo. Na ‘Umrah aliyoifanya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) na akaiwekea sharia, ni ‘Umrah ya mtu anayeingia Makkah, na si ‘Umrah ya mtu aliye ndani ya Makkah, kisha akatoka kwenda nje ya mipaka ya Haram ili akahirimie. Na hili hakulifanya yeyote wakati wa uhai wake isipokuwa ‘Aaishah peke yake kati ya wengineo waliokuwa pamoja naye, kwa kuwa yeye alikuwa amehirimia ‘Umrah akapata hedhi, na Rasuli akamwamuru, akachanganya Hajj ndani ya ‘Umrah, na akawa ni mwenye kufanya Qiraan. Akahisi ukakasi wenzake kurudi wakiwa wamefanya Hajj kando na ‘Umrah kando, na yeye kafanya ‘Umrah ndani ya Hajj yake. Akamwomba kaka yake aende naye At-Tan-‘iym ili akahirimie ‘Umrah huko)). [Irshaadu As-Saariy ‘anil Wajiyz (uk. 266)]

 

Isitoshe, kihakika, Kutufu Nyumba ni bora zaidi kuliko Kusai, na ni vyema zaidi kuliko kutaabika kutoka kwenda hadi At-Tan-‘iym ili kuhirimia ’Umrah mpya. Na kwa sasa inajulikana vizuri kabisa kuwa muda ambao mtu anautumia katika kutoka kwenda At-Tan-‘iym ili ahirimie ‘Umrah mpya, anaweza kwa muda huo kuzunguka Al-Ka’abah mamia ya mizunguko.

 

Ninasema: “Hili ni kwa yule aliyefanya ‘Umrah kabla ya Hajj na akataka –baada ya Hajj- kuikariri tena ‘Umrah yake, au alikuwa amefanya ‘Umrah na akataka kufanya tena. Ama mwenye hali kama ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) ambapo hakuweza kufanya ‘Umrah kabla ya Hajj, basi hakuna ubaya kufanya ‘Umrah baada ya kumaliza Hajj yake kwa kuzifanyia kazi dalili zote. [Haya kayasema Al-‘Allaamah Ibn Baaz (Rahimahul Laah) kama ilivyo katika Kitabu cha Tawdhwiyhul Ahkaam cha Bassaam (3/247)]. Na hii ni kauli wastani zaidi katika suala hili. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

Nguzo za ‘Umrah

 

1- Kuhirimia

 

2- Kutufu

 

3- Kusai

 

Mwenye kuacha nguzo yoyote kati ya hizi, basi ‘Umrah yake haitimu.

 

Waajibaat za ‘Umrah

 

1- Kuhirimia toka kwenye Miyqaat

 

Ni lazima kwa anayetaka kufanya ‘Umrah ahirimie toka kwenye Miyqaat kama anaishi nje ya eneo la Miyqaat. Na kama anaishi ndani ya eneo la Miyqaat, basi atahirimia toka nyumbani kwake. Ama mkazi wa Makkah, huyo atatoka kwenda nje ya mipaka ya Haram (At-Tan-‘iym au kwingineko) na atahirimia kutoka huko kama alivyofanya ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa).

 

2- Kunyoa au kupunguza

 

 

Share