02-Sharh Asmaa Allaah Al-Husnaa Wa Swifaatihi: Dibaji Ya Mfasiri Wa Kitabu Cha Kiingereza Kutoka Kiarabu

Sharh Asmaa Allaah Al-Husnaa Wa Swifaatihi

 

(Maelezo Ya Majina Mazuri Ya Allaah Na Swiffah Zake)

 

Alhidaaya.com

 

01-Dibaji Ya Mfasiri Wa Kitabu Cha Kiingereza Kutoka Kiarabu

 

 

 

Himdi na shukurani zote ni kwa Allaah. Tunamhimidi, tunamwomba msaada na maghfirah. Anayeongozwa na Allaah hakuna wa kumpotosha na ambaye Allaah Anamwacha apotee, hakuna wa kumwongoza. Nashuhudia kwamba hapana apasaye  kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah Peke Yake, hana mshirika na nashuhudia kwamba  Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) ni Mja na Rasuli Wake.

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:

 

وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا ۖ وَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ ۚ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٨٠﴾

Na Allaah Ana Majina Mazuri kabisa, basi muombeni kwayo. Na waacheni wale wanamili katika kukadhibisha Majina Yake, watalipwa yale waliyokuwa wakiyatenda. [Al-A’raaf (7): 180]

 

 

Kutoka katika vituo vitukufu na vya juu zaidi vya utambuzi ni kumjua Allaah (سبحانه وتعالى), kupitia uzuri Wake. Hii ndiyo elimu waliyo nayo wasomi wa uumbwaji huu. Wote wanamjua kupitia miongoni mwa Sifa Zake lakini wenye utambuzi kamilifu zaidi ni wanomjua kupitia ukamilifu Wake, Utaadhima (Utukufu) Wake na Uzuri Wake. Hakuna chenye kufanana Naye katika Sifa Yake yoyote ile, na kama utachukulia kuwa uumbaji Wake ulikuwa katika namna bora sana, na ukataka kujaribu na kulinganisha jumla ya uzuri Wake wake wa ndani na wa nje na uzuri wa Allaah (سبحانه وتعالى), ulinganisho huo utakuwa hafifu kuliko tochi yenye mwangaza hafifu kuwashwa mkabala na  kisahani kinachowaka cha jua.

 

Inatosha kujua uzuri Wake kwamba kama kizuizi Chake kingeondolewa, kila kitukufu cha Dhati Yake kinawafikia viumbe Wake kingefutika kabisa. Inatosha kujua kuwa uzuri wote, wa nje na ndani, unaopatikana ulimwenguni humu na Aakhirah, ni matokeo ya athari ya kazi Yake, hivyo, ni nini basi anachoweza mtu kuhisi kuhusu uzuri wa Ambaye uzuri huu umetoka Kwake? Inatosha kujua uzuri Wake kuwa, Kwake ndipo ilipomiliki taadhima yote kikamilifu, nguvu na uwezo wote kikamilifu, ukarimu wote, upaji wote, elimu yote na Rahmah yote.

 

 

Kutoka katika Nuru ya Dhati Yake kiza chote hutiwa nuru, kama Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alivyosema pindi alipoomba du’aa huko Twaaif:

 

 

أَعُوذُ بِنُورِ وَجْهِكَ الَّذِي أَشْرَقَتْ لَهُ الظُّلُمَات وَصَلَحَ عَلَيْهِ أَمْر الدُّنيْا وَالآخِرَة

 

Najikinga kwa Nuru ya Wajihi Wako inayotia Nuru kiza na juu yake mambo ya duniani na Aakhirah hupangiliwa.[1]

 

 

‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه) amesema: “Hapana usiku na mchana pamoja kwa Rabb Wako, Nuru ya mbingu na ardhi huja kutokana na Nuru ya Dhati yake.”[2] Kwa hivyo, Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) ni Nuru ya mbingu na ardhi na katika Siku ya Hukmu, pindi Atakapohukumu watu, Nuru Yake itaiangaza dunia.

 

 

Mojawapo katika Majina Yake ni Al-Jamiyl (Mzuri), Imesimuliwa kutoka kwa Ibn Mas’uwd (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kuwa amesema:

 

الله جَمِيلُ يُحِبُّ الْجَمال

((Allaah ni Jamiyl (Mzuri) na Anapenda uzuri))” [Muslim]

 

 

Uzuri Wake ni hatua nne, uzuri wa Dhati Yake, uzuri wa Sifa Zake, uzuri wa Vitendo Vyake na uzuri wa Majina Yake.

 

 

Majina Yake yote ni mazuri, Sifa Zake zote ni kamilifu, matendo Yake yote yameegemea katika hikma safi kabisa, ni zenye manufaa, za haki na pia ni Rahmah.

 

 

Hivyo, ni juu ya mja kujua kuwa hakuna apasaye kuabudiwa kwa haki ghairi Yake Allaah (سبحانه وتعالى), ni juu yake kumpenda Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) kwasababu Yeye ni Yeye na kwa sababu ya ukamilifu Wake. Pia ni juu ya mja kujua kuwa kwa ukweli hakuna anayemfadhili mmojawapo kwa kila namna ya baraka za nje na ndani isipokuwa Yeye Allaah (عز وجل) na kwa hivyo anapaswa ampende Yeye kwa hili pia, na amsifu Yeye. Hivyo, mja anapaswa ampende Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) kwa sababu ya mambo yote haya mawili. [Ibn Al-Qayyim, Al-Fawaaid (uk 258)]

 

 

 

Katika kushikamana na mahimizo ya hapo juu, tasnifu hii imedondolewa kutoka katika maneno ya ufunguzi ya Imaam Naaswir As-Sa’diy (رحمه الله) katika Tafsiyr yake ya Qur-aan, Tafsiyr Al-Kariym Ar-Rahman, ambamo kwa ufupi na kwa vizuri ameeleza Majina hayo ya Allaah yanayojitokeza katika Qur-aan. Baada ya kila maelezo, mwandishi ameongeza baadhi ya Aayah za Qur-aan kuonesha matumizi ya Jina fulani mahsusi. Inapaswa itambulike kuwa mwandishi  (رحمه الله)  ametaja tu Majina yanayojitokeza katika Qur-aan na idadi yake kwa ujumla inafikia themanini na tisa kwa mtazamo wake. Majina ya ziada yaliyotajwa katika Qur-aan yameongezwa kutokana na kazi ya Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (رحمه الله) katika Qawaaidul-Muthlaa fiy SwifaatiLLaah wa Asmaaihil-Husnaa na kuleta jumla ya mia moja na tatu.

 

 

Kabla ya kuendelea na makala au kitabu hiki, itakuwa ni jambo la manufaa kuleta baadhi ya kanuni za ujumla kuhusu Majina ya Allaah (عز وجل)[3]

 

 

i-Majina Yote Ya Allaah Ni Mazuri Na Makamilifu

 

 

Hii ni kwa sababu yanaunda maelezo kamilifu na Sifa zisozo na ila hata kidogo, wala hazina japo uwezekano wa kuwa na kasoro. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ

Na Allaah Ana Majina Mazuri kabisa. [Al-A’raaf (7): 180]

 

 

 

ii-Majina Ya Allaah Ni Halisi Na Maelezo Halisi

 

 

Ni Majina halisi kulingana na kukuwa yanamaanisha Dhati ya Allaah (عز وجل) na maelezo kulingana na maana zake; Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:

 

وَهُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٨﴾

Naye Ndiye Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Al-Ahqaaf (46):8]

 

Na Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَرَبُّكَ الْغَفُورُ ذُو الرَّحْمَةِ ۖ

Na Rabb wako ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye Rahmah. [Al-Kahf (18):58]

 

 

Hivyo Aayah ya pili inathibitisha kuwa Mwenye Rahmah ni Ambaye Ana Sifa hiyo na ameelezwa kwa Rahmah. Hapo pia kuna muwafaka wa wanaisimu kuwa neno

 

عليم

‘Mjuzi’

 

Hupewa mwenye ujuzi tu.

 

Na neno la

سميع

‘Mwenye kusikia’

 

 

Hupewa mwenye kusikia tu, na kuendelea.

 

 

 

iii-Ikiwa Jina La Allaah Linajulisha Maelezo Elekezi

 

 

Ni muhimu kuthibitisha mambo matatu:

 

1-Jina hilo hasa

 

2-Sifa inayojulishwa na Jina hilo

 

3-Hukmu na matumizi ya lazima yaliyomo (katika kutajwa kwa Jina hilo)

 

 

Hii ndiyo sababu ‘Ulamaa wameeleza kuwa adhabu iliyowekwa kwa waporaji wa njiani imeondolewa ikiwa watatubu, kwa mujibu wa kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

 

إِلَّا الَّذِينَ تَابُوا مِن قَبْلِ أَن تَقْدِرُوا عَلَيْهِمْ ۖ فَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٣٤﴾

Isipokuwa wale waliotubia kabla ya kuwashinda nguvu basi jueni kwamba hakika Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Al-Maa-idah (5): 34]

 

 

Hii ni kwasababu, kidokezo muhimu kwa Majina haya mawili, ni kuwa Allaah (سبحانه وتعالى) Amewaghufuria dhambi zao na Amewaonyesha Rahmah kwa kuwaondolea kutumika adhabu waliyowekewa.

 

 

Halikadhalika, neno la

 

السميع

‘Mwenye kusikia yote daima’

 

 

Linashurutisha kuwa unathibitisha Jina hili, Sifa ya Kusikia na kidokezo cha lazima kuwa Anasikia yote, ya siri na dhahiri.

 

 

Ikiwa jina si elekezi, basi ni muhimu tu kuthibitisha mambo ya mawili ya mwanzo yaliyotajwa hapo juu. Kwa mfano, Jina

 

الحيّ

 

‘Aliye Hai daima’

 

 

Ni muhinu kuthibitisha Jina hili na Sifa inazohusiana nayo ya uhai.

 

 

 

iv- Jina La Allaah Linaweza Kujulikana Kwa Kupitia Wahy Tu

 

 

 

Hii ni kwasababu hakuna njia ya kiakili tu ya kuyajua. Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:

 

وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ ۚ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَـٰئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْئُولًا ﴿٣٦﴾

Na wala usifuatilie usiyo na elimu nayo. Hakika masikio na macho na moyo; vyote hivyo vitaulizwa. [Al-Israa (17) :36]

 

 

 

v-Majina Ya Allaah Hayajafungika Kwa Idadi Yoyote

 

  

Hii inatokana na Hadiyth Swahiyh ya Ibn Mas’uwd (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akiomba:

 

للَّهُمَّ إِنِّي عَبْدُكَ، وَابْنُ عَبْدِكَ، وَابْنُ أَمَتِكَ، نَاصِيَتِي بِيَدِكَ، مَاضٍ فِيَّ حُكْمُكَ، عَدْلٌ فِيَّ قَضَاؤُكَ، أَسْأَلُكَ بِكُلِّ اسْمٍ هُوَ لَكَ سَمَّيْتَ بِهِ نَفْسَكَ، أَوْ عَلَّمْتَهُ أَحَدًا مِنْ خَلْقِكَ، أَوْ أَنْزَلْتَهُ فِي كِتَابِكَ، أَوْ اسْتَأْثَرْتَ بِهِ فِي عِلْمِ الْغَيْبِ عِنْدَكَ، أَنْ تَجْعَلَ الْقُرْآنَ رَبِيعَ قَلْبِي، وَنُورَ صَدْرِي، وَجَلَاءَ حُزْنِي، وَذَهَابَ هَمِّي

Ee Allaah hakika mimi ni mja Wako, mtoto wa mja Wako, mtoto wa kijakazi Chako, utosi wangu uko Mikononi Mwako, yaliyopita kwangu yako katika hukumu Yako, ni usawa kwangu kunihukumu Kwako, nakuomba kwa kila Jina ambalo ni Lako Ulilojiita  Mwenyewe au Uliloliteremsha katika Kitabu Chako, au Ulilomfundisha yeyote yule kati ya viumbe Vyako, au Ulilolihifadhi Wewe Mwenyewe (na kujihusisha kulijua) katika ’ilmu ya ghayb Kwako, nakuomba Ujaalie Qur-aan kuwa ni rabiy' (uhuisho, raha, furaha na ustawisho) wa moyo wangu na nuru ya kifua changu, na ufumbuzi wa  huzuni yangu, na sababu ya kuondoka wahka wangu kujifunza.” [Ameipokea Ahmad (1/391) [452], Al-Haakim (1/509) na ameisahihisha Al-Albaaniy katika As-Silsilah Asw-Swahiyhah (199) na Al-Kalimi Atw-Twayyib (124)]

 

Haiwezekani kuyafungia Majina hayo ambayo Allaah (سبحانه وتعالى) Ameyahifadhi Kwake katika ghaibu kwa kuweka idadi au kuyaenea. Kuhusu Hadiyth inayotaja Majina tisini na tisa, maana yake ni kuwa, mwenye kuyahifadhi, kuyaelewa na kuyatumia katika maisha yake ya kila siku, idadi hii ya majina, ataingia Jannah (Peponi).

 

 

 

 

[1] ‘Aliy Hasan: Imesimuliwa na Is-haaq, As-Siyrah, Atw-Twabariy., Taaryikh na vingine na Hadiyth hii si Swahiyh kwa mukhutasari.

 

[2] ‘Aliy Hasan: Imesimuliwa na Atw-Twabariy, Al-Kabiyr (8886) na wengine na imetolewa kuwa Swahiyh na Ibn Taymiyyah, Majmuw’ Fataawaa (6/3910).

 

[3] Imefupishwa kutoka Ibn ‘Uthaymiyn, Qawa-idul-Muthlaa fiy SwifaatiLLaah wa Asmaaihil-Husnaa

 

 

Share