05-Sharh Asmaa Allaah Al-Husnaa Wa Swifaatihi: Wasifu Wa ‘Allaamah Abu ‘Abdirrahmaan Naaswir As-Sa’diy (رحمه الله)

Sharh Asmaa Allaah Al-Husnaa Wa Swifaatihi

 

(Maelezo Ya Majina Mazuri Ya Allaah Na Swiffah Zake)

 

Alhidaaya.com

 

05-Wasifu Wa ‘Allaamah Abu ‘Abdirrahmaan Naaswir As-Sa’diy (رحمه الله)

 

 

 

Jina lake ni Abu ‘Abdillaah ‘Abdurrahman bin Naaswir bin ‘Abdillaah bin Naaswir ‘Aliy As-Sa’diy wa kabila la Tamiymiy. Alizaliwa katika jiji la ‘Unayzah, Qasiym mnamo tarehe 12 Muharram, 1307 H. Mama yake alifariki wakati yeye alipokuwa na umri wa miaka mine na baba yake alifariki dunia wakati yeye alipofikisha miaka saba. Hivyo, alikua kama yatima lakini licha ya haya alikuwa na makuzi mema.

 

 

Imaam As-Sa’dy (رحمه الله) alikuwa na akili sana na alihifadhi Qur-aan alipokuwa na umri wa miaka kumi na mmoja na baada ya hapo alitumia muda mwingi akisoma kwa ‘Ulamaa wa nchini mwake. Alijibidiisha masomoni mwake mpaka akafanya vyema katika aina mbalimbali za sayansi ya Kiislamu na alipofikisha umri wa miaka ishirini na mitatu alikuwa tayari akifundisha. Alijitolea kwa hali zote kwa kujifunza na kufundisha mpaka akawa na mamlaka inayoongoza nchini mwake, akiwa pamoja na wanafunzi waliojazana kwake kutoka maeneo yote.

 

 

Imaam As-Sa’dy (رحمه الله) alisoma chini ya ‘Ulamaa waliokuwa wakiongoza katika wakati wake, miongoni mwao alikuwa Shaykh Ibraahiym bin Hamad bin Jaasir; ambaye  Imaam As-Sa’dy alimsifu kuhusu uwezo wake wa juu ya kuhifadhi Hadiyth, taqwa yake na mapenzi yake kwa masikini. Mara nyingi alishuhudia masikini akija kwa Shaykh Ibraahiym naye Shaykh akitoa nguo na kumpa, licha ya yeye mwenyewe kuwa na haja nacho na akiwa masikini hasa.

 

 

Imaam As-Sa’dy (رحمه الله)  alisoma pia chini ya Shaykh Muhammad bin ‘Abdilkariym ash-Shibl, Shaykh Swaalih bin ‘Uthmaan, Hakimu wa ‘Unayzah, Shaykh bin Sa’b Al-Quwayjiriy, Muhammad Al-Amiyn Ash-Shanqiytwiy na wengine.

 

 

Imaam As-Sa’dy (رحمه الله) alijulikana kwa taqwa yake wake, maadili mema na unyenyekevu kwa wadogo, wakubwa, matajiri na masikini. Kila mara alikuwa akipitisha sehemu ya muda wake kukutana na wale waliotaka wakutane naye na alikuwa mkarimu kwa masikini, mayatima na wageni, akiwasaidia kwa kadiri ya uwezo wake.

 

 

Imaam As-Sa’dy (رحمه الله) alibobea katika Fiqhi na Uswuw Al-Fiqhi, hatimaye akawa katika madhehebu ya Hanbal kama walivyokuwa walimu wake wote. 

 

 

Kazi yake ya kwanza katika Fiqhi iliandikwa kwa mtindo wa kimashairi juu ya madhehebu ya Hanbal ambayo ndiyo pia ilikuwa rai yake. Alisoma kazi ya Ibn Taymiyyah na Ibn Al-Qayyim kwa undani na akanufaika kutokana nao. Alipoendelea na masomo yake hakujifunga sana na madhehebu ya Hanbal bali alifuata njia aliyoamini kuwa ilihakikishiwa ushahidi uliokuwa na nguvu zaidi. Hata hivo, kamwe hakuweza kuwalaumu au kuwadharau wale waliofuata madhehebu fulani. Kadhalika alikuwa bingwa katika Tafsiyr, akiwa amesoma kazi nyingi za Tafsiyr na akiwa ameisoma chini ya walimu wake na kwa kweli alihariri Tafsiyr yeye mwenyewe. Wote waliomsikia akikisherehi Kitabu cha Allaah walitamani aendelee kutokana na uzungumzaji wake wa namna ya kushajiisha na faida nyingi alizozipata kutoka katika Aayah za Qur-aan.

 

 

Imaam As-Sa’dy (رحمه الله) alihariri kazi nyingi na miongoni mwake ni zifuatazo:

 

·        تفسير السعدي = تيسير الكريم الرحمن في تفسير كلام المنان

 

·        إرشاد أولى البصائر والألباب لنيل الفقة بأقرب الطرق وأيسر الأسباب

 

·        الدرة البهية شرح القصيدة التائية في حل المشكلة القدرية

 

·        القول السديد شرح كتاب التوحيد 

 

·        التوضيح والبيان لشجرة الإيمان

 

·        القواعد الحسان لتفسير القرآن

 

·        الوسائل المفيدة للحياة السعيدة

 

·        التنبيهات اللطيفة على ما احتوت عليه العقيدة الواسطية من المباحث المنيفة

 

·        رسالة لطيفة جامعة في أصول الفقه المهمة

 

·        بهجة قلوب الأبرار وقرة عيون الأخيار 

 

·        تفسير أسماء الله الحسنى

 

·        منهج السالكين وتوضيح الفقة في الدين

 

·        الفواكه الشهية في الخطب المنبرية والخطب المنبرية على المناسبات

 

·         تيسير اللطيف المنان في خلاصة تفسير القرآن

 

 

Imaam As-Sa’dy (رحمه الله) alifariki hapo ‘Unayzah mnamo mwaka 1376 H Allaah Amrehemu na Amjaalie makazi ya Jannatul-Firdaws. Aamiyn.

 

Share