20-Sharh Asmaa Allaah Al-Husnaa Wa Swifaatihi: الْقُدُّوسُ - السَّلاَمُ

Sharh Asmaa Allaah Al-Husnaa Wa Swifaatihi

 

(Maelezo Ya Majina Mazuri Ya Allaah Na Swiffah Zake)

 

Alhidaaya.com

 

الْقُدُّوسُ - السَّلاَمُ

 

 

 

الْقُدُّوسُ

Al-Qudduus

Mtakatifu Ametakasika Na Sifa Zote Hasi

 

 

السَّلاَمُ

As-Salaam

Mwenye Amani, Mwenye Kusalimika Na Kasoro Zote

 

 

 

Allaah (سبحانه وتعالى) ni Pekee Aliye Mkubwa na Ameepukana mbali na namna yoyote ya ila, kasoro, au kufanana na kiumbe Chake chochote. Hivyo, Ameepukana mbali na namna yoyote ya upungufu kama Alivyoepukana na Sifa ya kushabihiana Naye au kukaribia hilo katika Sifa Yake yoyote ya ukamilifu.

 

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 

  لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ﴿١١﴾

Hakuna chochote kinachofanana Naye, Naye Ndiye Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote. [Ash-Shuwraa (42): 11]

 

Na Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ ﴿٤﴾

Na wala haiwi Awe na yeyote anayefanana na kulingana Naye. [Al-Ikhlaasw (112): 4]

 

Na Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 رَّبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا فَاعْبُدْهُ وَاصْطَبِرْ لِعِبَادَتِهِ ۚ هَلْ تَعْلَمُ لَهُ سَمِيًّا ﴿٦٥﴾

Rabb wa mbingu na ardhi na vilivyo baina yake; basi mwabudu Yeye tu na dumisha subira katika ‘ibaadah Yake. Je, unamjua yeyote anayefanana Naye (Allaah)?  [Maryam (19): 65]

 

Na Ameonya Allaah (سبحانه وتعالى):

فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا

Basi msimfanyie Allaah waliolingana naye [Al-Baqarah (2):22]

 

Na Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى):

 

يُسَبِّحُ لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ الْمَلِكِ الْقُدُّوسِ الْعَزِيزِ الْحَكِيمِ﴿١﴾

 Vinamsabbih Allaah Pekee vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi, Mfalme, Ametakasika na sifa zote hasi, Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote. [Al-Jumu’ah (62): 1]

 

Na Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى):

 

هُوَ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْمَلِكُ الْقُدُّوسُ السَّلَامُ الْمُؤْمِنُ الْمُهَيْمِنُ الْعَزِيزُ الْجَبَّارُ الْمُتَكَبِّرُ ۚ سُبْحَانَ اللَّـهِ عَمَّا يُشْرِكُونَ﴿٢٣﴾

Yeye Ndiye Allaah Ambaye hakuna Muabudiwa wa haki ila Yeye, Mfalme, Mtakatifu Ametakasika na sifa zote hasi, Mwenye kusalimisha na Amesalimika na kasoro zote, Mwenye kusadikisha ahadi na kuaminisha, Mwenye kudhibiti, kushuhudia, kuchunga na kuhifadhi, Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Jabari, Asiyeshindwa kufanya Atakalo, Mwenye ukubwa na uadhama, Subhaana Allaah! Utakasifu ni wa Allaah kutokana na ambayo wanamshirikisha. [Al-Hashr (59):23]

 

 

 

 

 

 

Share