02-Fadhila Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Miujiza Yake: Muujiza Wa Al-Israa Wal-Mi’raaj

Fadhila Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم

02-Miujiza Yake: Muujiza Wa Al-Israa Wal-Mi’raaj

 

Alhidaaya.com

 

 

Muujiza wa Al-Israa wal Mi’raaj ni muujiza mwengineo mkubwa katika miujiza ya Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّم). Tukio la Israa wal Mi’raaj halikuwa ni tukio la kawaida bali lilikuwa ni tukio la muujiza adhimu ambao umedhihirisha Utukufu usio na mithali, na Uwezo mkubwa wa Allaah (سُبْحانَهُ وَتَعالى).  Alimwongoza Rasuli Wake (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّم) na Akadhihirisha dalili mojawapo ya Unabiy wake kwa watu khasa washirikina wa Makkah ambao hawakumwamini bali walimkanusha na kumtesa na kumdhikisha kutokana na Risala yake aliyotakiwa na Allaah (سُبْحانَهُ وَتَعالى) Aibalighishe kwao.

 

Ni muujiza mashuhuri unaotambulikana na walimwengu kutokana na ajabu ya muujiza huu wa kuweza kusafirishwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّم) katika safari ya usiku mmoja kutoka Makkah kupita Baytul-Maqdis (Jerusalem), kisha kufikia mbingu ya saba na kurudi Makkah siku hiyo hiyo.

 

Anasema Allaah (سُبْحانَهُ وَتَعالى):

 

سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الْأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ لِنُرِيَهُ مِنْ آيَاتِنَا ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ ﴿١﴾

Utakasifu ni wa Ambaye Amemsafirisha usiku mja Wake kutoka Al-Masjid Al-Haraam mpaka Al-Masjid Al-Aqswaa ambao Tumevibariki vilivyoko pembezoni mwake; ili Tumuonyeshe baadhi ya Aayaat (miujiza, ishara, dalili) Zetu. Hakika Yeye (Allaah) ni Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote. [Al-Israa: 1]

 

Al-Israa wal Mi’raaj ni tukio ambalo limempatia Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّم) hadhi kubwa ulimwenguni, hadhi ya kumfikisha mahali ambako hakuna mwana-Aadam aliyewahi kufikia nako ni Sidrat Al-Muntahaa huko mbingu ya saba.   

 

Al-Israa wal Mi’raaj ni muujiza ambao wana-Aadam wamestaabishwa na wengine kuduwaa kwa kutafakari jinsi gani inawezekana safari ya mtu kwa usiku mmoja kusafiri mji hadi mji, kisha mpaka kupanda mbinguni na kufikia mbingu ya saba na kuongea na Rabb wake. Wanaoitilia shaka ni makafiri, ama Waumini hawana shaka nayo safari hiyo kwa sababu Iymaan zao zimethibiti katika kila jambo alokuja nalo Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّم). Juu ya hivyo imetajwa na Allaah (عَزَّ وَجَلَّ) Ambaye ni Al-Qaadir (Mweza wa kila kitu) katika Qur-aan Anaposema:

 

 

وَلَقَدْ رَآهُ نَزْلَةً أُخْرَىٰ ﴿١٣﴾ عِندَ سِدْرَةِ الْمُنتَهَىٰ ﴿١٤﴾ عِندَهَا جَنَّةُ الْمَأْوَىٰ ﴿١٥﴾ إِذْ يَغْشَى السِّدْرَةَ مَا يَغْشَىٰ ﴿١٦﴾ مَا زَاغَ الْبَصَرُ وَمَا طَغَىٰ ﴿١٧﴾ لَقَدْ رَأَىٰ مِنْ آيَاتِ رَبِّهِ الْكُبْرَىٰ ﴿١٨﴾

 

Na kwa yakini amemuona (Jibriyl) katika uteremko mwingine. Kwenye mkunazi wa mpaka wa mwisho kabisa. Karibu yake kuna Jannah ya Al-Ma-waa. Ulipoufunika mkunazi huo unachokifunika. Jicho lake halikukengeuka wala halikupinduka mipaka. Kwa yakini aliona miongoni mwa Aayaat (ishara, dalili) za Rabb wake kubwa kabisa. [An-Najm: 13- 18]

 

Matukio yafuatayo kwa kifupi yalitokea katika safari hiyo kuu ya Israa wal Mi’raaj:

 

 

1-Safari ya usiku mmoja kuanzika Masjid Al-Haram Makkah kupitia Baytul-Maqdis Jerusalem, kupanda mbinguni hadi mbingu ya saba na kuongea na Allaah (سُبْحانَهُ وَتَعالى).

 

 

2-Kuwasalisha Manabii wote pindi alipofika Baytul-Maqdis.

 

 

3-Katika kila mbingu alionana na Manabii; Aadam, ‘Iysaa na Yahyaa, Yuwsuf, Idriys, Haaruwn, Muwsaa, (عَلَيْهِم السَّلام) hadi kumfikia Nabiy Ibraahiym (عَلَيْهِ السَّلام) ambaye alikuwa mbingu ya saba.

 

 

3-Alipokutana na Nabiy Muwsaa (عَلَيْهِ السَّلام) mbingu ya sita alimnasihi arudi kwa Allaah (عَزَّ وَجَلَّ) ili amuombe Ampunguzie idadi za Swalaah aliyofaridhishwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّم) na Ummah wake kuanzia khamsini kwa siku hadi kufikia tano kwa siku.  

 

4-Jibriyl alipofikia Sidrat Al-Muntahaa huko mbingu ya saba, alimwacha Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّم) aendelee akaongea na Allaah (عَزَّ وَجَلَّ), ilhali yeye Jibriyl (عَلَيْهِ السَّلام) alibakia nyuma.

 

 

4-Allaah (عَزَّ وَجَلَّ) Alifaridhisha nguzo ya Kiislaam ambayo ni Swalaah tano kwa siku.

 

 

5-Neema za Jannah (Pepo) alizoziona Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّم) akanusa harufu yake.

 

 

6-Kuona kwake Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّم) Moto wa Jahannam na matukio mbalimbali aliyoyaona, yaliyothibiti katika Hadiyth za Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّم), yakiwemo adhabu za watu wa matendo mbali mbali ya madhambi kama kula ribaa, ghiybah (kusengenya), wazinifu n.k.

 

 

7-Baada ya kurudi Makkah, washirikina wa Makkah kutokumwamini Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّم).

 

8-Abu Bakr Asw-Swiddiyq alimwamini mojamoja kwa moja na ndipo alipopata laqab yake hiyo ya Asw-Swiddiyq (mkweli).

 

Kwa faida nyenginezo bonyeza viungo vifuatavyo:

 

Tukio la Israa Na Mi'iraaj

 

Muujiza Wa Al-Israa Wal-Mi'raaj Na Mafunzo Yake

 

Israa Na Mi'iraaj: Kisa Cha Abu Bakr Asw-Swiddiyq (رضي الله عنه)

 

 

Share