028-Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake أسماء الله الحسنى وصفاته: AL-QARIYB

 

أسماء الله الحسنى وصفاته

Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake

 

Alhidaaya.com

 

الْقَرِيب

 

AL-QARIYB

 

 

 

Al-Qariyb: Aliye Karibu daima (kwa ujuzi Wake)

 

 

Jina hili la Allaah ('Azza wa Jalla) la Qariyb limetokea katika Qur-aan likiwa pekee katika Kauli Yake Allaah ('Azza wa Jalla):

 

 

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ﴿١٨٦﴾

Na watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni Niko karibu; Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba. Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka. [Al-Baqarah: 186]

 

 

Na limetokea katika Qur-aan likiwa limeshirkiana na Majina mengineyo katika Kauli Zake Allaah ('Azza wa Jalla):

 

قُلْ إِن ضَلَلْتُ فَإِنَّمَا أَضِلُّ عَلَىٰ نَفْسِي ۖ وَإِنِ اهْتَدَيْتُ فَبِمَا يُوحِي إِلَيَّ رَبِّي ۚ إِنَّهُ سَمِيعٌ قَرِيبٌ ﴿٥٠﴾

Sema: Ikiwa nimepotoka, basi hakika nimepotoka kwa khasara ya nafsi yangu, na ikiwa nimeongoka, basi ni kwa yale Aliyonifunulia Wahy Rabb wangu; hakika Yeye ni Mwenye kusikia yote, Yu Karibu. [Sabaa: 50]

 

Na pia,

 

 

وَإِلَىٰ ثَمُودَ أَخَاهُمْ صَالِحًا ۚ قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ ۖ هُوَ أَنشَأَكُم مِّنَ الْأَرْضِ وَاسْتَعْمَرَكُمْ فِيهَا فَاسْتَغْفِرُوهُ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ ۚ إِنَّ رَبِّي قَرِيبٌ مُّجِيبٌ﴿٦١﴾

Na kwa Thamuwd (Tulimpeleka) ndugu yao Swaalih. Akasema: Enyi kaumu yangu! Mwabuduni Allaah, hamna mwabudiwa wa haki ghairi Yake. Yeye Ndiye Aliyekuanzisheni katika ardhi, na Akakufanyieni makazi humo; basi mwombeni maghfirah, kisha tubieni Kwake. Hakika Rabb wangu Yuko Karibu, Mwenye kuitikia. [Huwd: 61]

 

 

Jina na Sifa hii ya Allaah ('Azza wa Jalla) ni dalili ya ukamilifu na ukaribu wa Allaah ('Azza wa Jalla) kwa waja Wake, na ukaribu na waja ni wa aina mbili.  

 

Kwanza: Ukaribu wa Jumla: Kwa yeyote, kwa elimu Yake, kwa uzoefu Wake, na ulinzi Wake na kushuhudia Kwake, na kuenea kuenea vitu vyote, dhahiri na batini ya hisia na isiyo na hisia Naye Yuko juu ya viumbe Wake. Anasema Allaah ('Azza wa Jalla):

 

 

هُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ۚ يَعْلَمُ مَا يَلِجُ فِي الْأَرْضِ وَمَا يَخْرُجُ مِنْهَا وَمَا يَنزِلُ مِنَ السَّمَاءِ وَمَا يَعْرُجُ فِيهَا ۖ وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ ۚ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿٤﴾

Yeye Ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha Akawa juu (Istawaa) ya ‘Arsh Anajua yale yanayoingia ardhini, na yale yatokayo humo, na yale yanayoteremka kutoka mbinguni, na yale yanayopanda humo, Naye Yu Pamoja nanyi popote mlipo. Na Allaah ni Mwenye kuona yote myatendayo. [Al-Hadiyd: 4]

 

 

Na pia,

 

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۖ مَا يَكُونُ مِن نَّجْوَىٰ ثَلَاثَةٍ إِلَّا هُوَ رَابِعُهُمْ وَلَا خَمْسَةٍ إِلَّا هُوَ سَادِسُهُمْ وَلَا أَدْنَىٰ مِن ذَٰلِكَ وَلَا أَكْثَرَ إِلَّا هُوَ مَعَهُمْ أَيْنَ مَا كَانُوا ۖ ثُمَّ يُنَبِّئُهُم بِمَا عَمِلُوا يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ﴿٧﴾

Je, huoni kwamba Allaah Anajua yaliyomo mbinguni na yaliyomo ardhini? Hauwi mnong’ono wa watatu isipokuwa Yeye ni wa nne wao (kwa ujuzi Wake), na wala watano isipokuwa Yeye ni wa sita wao (kwa ujuzi Wake), na wala chini kuliko ya hivyo, na wala wengi zaidi isipokuwa Yeye Yu pamoja nao (kwa ujuzi Wake) popote watakapokuwa; kisha Siku ya Qiyaamah Atawajulisha yale waliyoyatenda. Hakika Allaah kwa kila kitu ni ‘Aliym. [Al-Mujaadala: 7]

 

 

Pili: Ukaribu maalum: kwa waja Wake, kwa wenye kumuomba, kwa wapenzi Wake, ni ukaribu wenye kuhitajia mapenzi na kunusuru, na kuunga mkono harakati za watu na matulivu yao, na kuitikia du’aa ya waombaji, na kuwataqabalia na kuwalipa waja Wake. Ni ukaribu ambao ukweli wake haufahamiki sawasawa, lakini athari yake inafahamika kwa wema Wake kwa waja Wake, na machungo yake na kuhudhurisha moyo wake katika hali ile aliyepta ukaribu [Tafsiyr Ibn As-Sa’diy (5/491), Al-Haq al-Waadhwih (64) na Fathu Rahiym (44)]

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ﴿١٨٦﴾

Na watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni Niko karibu; Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba. Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka. [Al-Baqarah: 186]

 

 

Na pia

 

  فَاسْتَغْفِرُوهُ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ ۚ إِنَّ رَبِّي قَرِيبٌ مُّجِيبٌ﴿٦١﴾

Basi mwombeni maghfirah, kisha tubieni Kwake. Hakika Rabb wangu Yuko Karibu, Mwenye kuitikia. [Huwd: 61]

 

 

 

Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah; Al-Qariyb:

 

 

1-Ukitaka kuwa karibu na Allaah ('Azza wa Jalla), basi jikurubishe Kwake kwa kumridhisha Yeye Allaah ('Azza wa Jalla) kwa ‘amali Anazozipenda kama kutimiza fardhi khasa kuhifadhi Swalaah na kwa kuiswali kwa wakati wake. Pia kuzidisha ‘ibaadah za Sunnah, kumdhukuru Allaah ('Azza wa Jalla) kwa wingi, na mengineyo mema na ya khayraat Aliyoyaamrisha Yeye na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa sababu kuna ukaribu maalum, uliowekwa kwa wale Waumini ambao hufanya kazi kuufikia, na Allaah ('Azza wa Jalla) Amewawekea daraja maalumu wanaojikurubisha Naye; Anasema:

 

 

وَالسَّابِقُونَ السَّابِقُونَ ﴿١٠﴾ أُولَـٰئِكَ الْمُقَرَّبُونَ ﴿١١﴾ فِي جَنَّاتِ النَّعِيمِ ﴿١٢﴾ ثُلَّةٌ مِّنَ الْأَوَّلِينَ ﴿١٣﴾ وَقَلِيلٌ مِّنَ الْآخِرِينَ ﴿١٤﴾

 

Na waliotangulia mbele, watatangulia mbele. Hao ndio watakaokurubishwa. Katika Jannaat za taanisi. Kundi kubwa katika wa awali. Na wachache katika wa mwishoni [Al-Waaqi’ah: 10 – 14]

 

Ibn Kathiyr amesema kuhusu

وَالسَّابِقُونَ السَّابِقُونَ ﴿١٠﴾ أُولَـٰئِكَ الْمُقَرَّبُونَ ﴿١١﴾

 

Wanaotangulia duniani kutenda khayraat ni kama Alivyoamrisha Allaah ('Azza wa Jalla) katika Aayah kadhaa. [Aal-‘Imraan: (133), Al-Hadiyd: (22)]. Basi atakayetangulia kwa khayraat katika dunia hii atakuwa mwenye kutangulia Aakhirah katika kukirimiwa kwani jazaa ya thawabu inalingana na aina ya ‘amali utendazo, na kama unavyotenda basi nawe utatendewa hivyo hivyo.

 

Akasema pia, wale walio karibu na Allaah ('Azza wa Jalla) ni wale ambao hutekeleza fardhi na wanatekeleza ‘amali za Mustahabb (yanayopendekezwa) na kujiepusha na na nawaahiy (yaliyokatazwa) na yanayochukiza na hata hujiepusha na mambo yaliyohurusika (mubaah: hayana dharura kuyatenda au kuyaacha).    Baadhi ya Salaf wamesema: Wao ni watu wa kwanza kwenda Msikitini na wa kwanza kutoka kwenda jihaad kwa ajili ya Allaah.

 

 

2-Jiandalie Aakhirah yako kwa khayraat za kila aina ili uwe miongoni mwa Al-Muqarrabuwn upate neema zake pindi mauti yatakapokufikia na ili usijekuwa kinyume chake. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Yu Qariyb katika hali ya Sakaraatul-Mawt ya waja, Anabainisha hali ya aina ya watu wawili hao katika Kauli Zake:

 

فَلَوْلَا إِذَا بَلَغَتِ الْحُلْقُومَ ﴿٨٣﴾ وَأَنتُمْ حِينَئِذٍ تَنظُرُونَ ﴿٨٤﴾ وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنكُمْ وَلَـٰكِن لَّا تُبْصِرُونَ ﴿٨٥﴾ فَلَوْلَا إِن كُنتُمْ غَيْرَ مَدِينِينَ ﴿٨٦﴾ تَرْجِعُونَهَا إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٨٧﴾ فَأَمَّا إِن كَانَ مِنَ الْمُقَرَّبِينَ ﴿٨٨﴾ فَرَوْحٌ وَرَيْحَانٌ وَجَنَّتُ نَعِيمٍ ﴿٨٩﴾ وَأَمَّا إِن كَانَ مِنْ أَصْحَابِ الْيَمِينِ ﴿٩٠﴾ فَسَلَامٌ لَّكَ مِنْ أَصْحَابِ الْيَمِينِ ﴿٩١﴾ وَأَمَّا إِن كَانَ مِنَ الْمُكَذِّبِينَ الضَّالِّينَ ﴿٩٢﴾ فَنُزُلٌ مِّنْ حَمِيمٍ ﴿٩٣﴾ وَتَصْلِيَةُ جَحِيمٍ ﴿٩٤﴾ إِنَّ هَـٰذَا لَهُوَ حَقُّ الْيَقِينِ ﴿٩٥﴾ فَسَبِّحْ بِاسْمِ رَبِّكَ الْعَظِيمِ ﴿٩٦﴾

Basi mbona roho ifikapo kooni. Nanyi wakati huo mnatazama. Nasi Tuko karibu naye zaidi kuliko nyinyi, lakini hamuoni. Basi kwa nini ikiwa hamuwajibiki malipo? Muirudishe roho (mwilini mwake), mkiwa ni wakweli? Basi akiwa miongoni mwa waliokurubishwa. Basi mapumziko ya raha na manukato na Jannah ya neema. Na kama akiwa miongoni mwa watu wa kuliani. Basi: Salaam juu yako uliye katika watu kuliani. Na kama akiwa miongoni mwa wakadhibishaji waliopotoka. Basi mapokezi yake ni maji ya moto yachemkayo. Na kuunguzwa na moto uwakao vikali mno. Hakika hii bila shaka ni haki yenye yakini. Basi sabbih kwa Jina la Rabb wako Adhimu, Mkuu kabisa. [Al-Waaqi’ah: 83 – 96]

 

 

 

3-Kumbuka kuwa Qiyaamah kiko karibu, na Allaah ('Azza wa Jalla) Ambaye Al-Qariyb Ametahadharisha ukaribu wake, kwa hiyo usije kughafilika na Qiyaamah ukasahau kujiandaa kwa ajili yake. Anasema Allaah ('Azza wa Jalla):

 

اقْتَرَبَ لِلنَّاسِ حِسَابُهُمْ وَهُمْ فِي غَفْلَةٍ مُّعْرِضُونَ ﴿١﴾

Imewakaribia watu hesabu yao, nao wamo katika mghafala wanakengeuka (na wanapuuza) [Al-Anbiyaa: 1]

 

Na Anasema pia Allaah ('Azza wa Jalla):

 

اقْتَرَبَتِ السَّاعَةُ وَانشَقَّ الْقَمَرُ ﴿١﴾

Saa imekaribia na mwezi umepasuka.  [Al-Qamar: 1]

 

 

4-Unaposibiwa na mithani ukawa katika dhiki, kumbuka kuwa Allaah ('Azza wa Jalla) ni Qariyb nawe kwa ujuzi Wake, kwa hiyo kimbilia kumwelekea Yeye kwa Istighfaar nyingi na kutubia Kwake ili Akuondoshee dhiki zako na Akujaalie faraja. Kisha mnyenyekee na kumlalamikia shida na dhiki zako na kumuomba du’aa kwani Yeye Anajua na Anasikia na Yuko Karibu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)

  فَاسْتَغْفِرُوهُ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ ۚ إِنَّ رَبِّي قَرِيبٌ مُّجِيبٌ﴿٦١﴾

Basi mwombeni maghfirah, kisha tubieni Kwake. Hakika Rabb wangu Yuko Karibu, Mwenye kuitikia. [Huwd: 61]

 

 

5-Itikia wito wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) wa kumwelekea Yeye Pekee katika kumuomba du’aa kwani Yeye ni Qariyb Anaitikia du’aa za wenye kumuomba kama Anavosema:

 

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ﴿١٨٦﴾

Na watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni Niko karibu; Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba. Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka. [Al-Baqarah: 186]

 

Na pia amka usiku wa manane wakati ambao Allaah ('Azza wa Jalla) huwa Qariyb na waje Wake kwa kuteremka mbingu ya dunia kuwasikiliza wenye haja Awataqabalie, wenye kuomba maghfirah Awaghufurie, wenye shida Awaondoshee. Hakika hii ni neema kubwa miongoni mwa neema za Waumini:

 

عنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((يَنْزِلُ رَبُّنَا تَبَارَكَ وَتَعَالَى كُلَّ لَيْلَةٍ إِلَى السَّمَاءِ الدُّنْيَا حِينَ يَبْقَى ثُلُثُ اللَّيْلِ الْآخِرُ يَقُولُ: مَنْ يَدْعُونِي فَأَسْتَجِيبَ لَهُ، مَنْ يَسْأَلُنِي فَأُعْطِيَهُ، مَنْ يَسْتَغْفِرُنِي فَأَغْفِرَ لَهُ)) البخاري و مسلم

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu)  kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Tabaaraka wa Ta’aalaa Huteremka (kwa namna inavyolingana na utukufu Wake) kila siku katika mbingu ya dunia inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba du’aa Nimuitike? Nani Ananiomba jambo Nimpe? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?)) [Al-Bukhaariy, Muslim

 

 

 

6-Tambua kuwa Allaah ('Azza wa Jalla) Yu Qariyb kwa waja Wake kulikoni  mshipa wa koo kama Anavosema:

 

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ وَنَعْلَمُ مَا تُوَسْوِسُ بِهِ نَفْسُهُ ۖ وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ﴿١٦﴾

Na kwa yakini Tumemuumba insani na Tunajua yale yanayowaza nafsi yake, na Sisi Tuko karibu naye kuliko mshipa wa koo. [Qaaf: 16]

 

Hivyo basi, tahadhari kutenda maovu kwa siri au kwa dhahiri na hata kutamka kauli ovu, au hata neno moja kwa sababu linarekodiwa na Malaika Aliowapa kazi hiyo. Anaendelea kusema hayo katika Suwrah hiyo tukufu ya Qaaf:

 

إِذْ يَتَلَقَّى الْمُتَلَقِّيَانِ عَنِ الْيَمِينِ وَعَنِ الشِّمَالِ قَعِيدٌ﴿١٧﴾ مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ﴿١٨﴾

 

Pale wanapopokea wapokeaji wawili (Malaika) wanaokaa kuliani na kushotoni. Hatamki kauli yeyote isipokuwa anaye mchungaji aliyejitayarisha (kurekodi). [Qaaf: 17 – 18]

 

 

 

7-Timiza adabu za kuomba du’aa kwa Allaah ('Azza wa Jalla), yaani unapomuomba du’aa Allaah ('Azza wa Jalla), usiombe kwa sauti kubwa ya kusikika kwa watu amekataza hivyo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Akataja Jina na Sifa hii tukufu ya Qariyb katika Hadiyth;

 

 

عَنْ أَبِي مُوسَى الأَشْعَرِيِّ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) قَالَ: كُنَّا مَعَ رَسُولِ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) فَكُنَّا إِذَا أَشْرَفْنَا عَلَى وَادٍ هَلَّلْنَا وَكَبَّرْنَا. ارْتَفَعَتْ أَصْوَاتُنَا فَقَالَ النَّبِيُّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم)َ: ((يَا أَيُّهَا النَّاسُ ارْبَعُوا عَلَى أَنْفُسِكُمْ فَإِنَّكُمْ لاَ تَدْعُونَ أَصَمَّ ولاَ غَائِبًا إِنَّهُ مَعَكُمْ ، إِنَّهُ سَمِيعٌ قَرِيبٌ تَبَارَكَ اسْمُهُ وَتَعَالَى جَدُّهُ))

 

Amesimulia Abu Muwsaa Al-Ash’ariyy (رضي الله عنه): Tulikuwa pamoja na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na tukawa kila tukipanda bonde, tunafanya tahliyl (Laa Ilaaha Illa-Allaah), na tunaleta takbiyr (Allaahu Akbar). Zikapanda sauti zetu, na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Enyi watu, zihurumieni nafsi zenu, kwani hamumwombi kiziwi wala asiyekuwepo, hakika Yeye Yupo nanyi (kwa Ujuzi Wake), hakika Yeye Ni Mwenye Kusikia yote, Yupo Karibu, Limebarikika Jina Lake na Umetukuka Ujalali Wake.” [Al-Bukhaariy]

 

 

 

 

Share