01-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Al-Faatihah

 

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

 

Suwrah Al-Faatihah:

 

 

"بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ * الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ * الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ * مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ * إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ * اهْدِنَا الصِّرَاط الْمُسْتَقِيمَ * صِرَاطَ الَّذِينَ أَنْعَمْتَ عَلَيْهِمْ غَيْرِ الْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ وَلَا الضَّالِّينَ".

 

“Kwa Jina la Allaah Ar-Rahmaan, Mwenye Kurehemu • Himdi Anastahiki Allaah Rabb wa walimwengu •  Ar-Rahmaan, Mwenye Kurehemu  •  Mfalme wa siku ya malipo  •  Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada  •  Tuongoze njia iliyonyooka  •  Njia ya wale Uliowaneemesha, si ya walioghadhibikiwa wala waliopotea”.  [Al-Faatihah: (1-7)]

 

Du’aa ya kwanza kabisa katika Qur-aan Tukufu iko katika Suwrah hii ya Al-Faatihah.  Hii ndio Suwrah Adhimu kabisa kati ya Suwrah za Qur-aan ambayo Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam ameiita “Ummul Qur-aan” pale aliposema:

 

"الْحَمْدُ لِلَّهِ: أُمُّ الْقُرْآنِ، وَأُمُّ الْكِتَابِ، وَالسَّبْعُ الْمَثَانِي"

 

“Alhamdulil Laahi ni “Ummul Qur-aan, na “Ummul Kitaab” na “As-Sab-‘ul Mathaaniy”.   [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Swahiyh Abiy Daawuwd]

 

Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia Abu Sa’iyd bin Al-Ma’aliy:

 

"لأُعَلِّمَنَّكَ أَعْظَمَ سُورَةٍ فِي الْقُرْآنِ... الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ"

 

“Hakika nitakufundisha Suwrah Adhimu zaidi katika Qur-aan: Alhamdulil Laah Rabbil ‘aalamiyn”.  [Al-Bukhaariy: Kitaabut Tafsiyr].

 

Imeitwa “Ummul Qur-aan” kwa vile inakusanya aina zote tatu za tawhiyd pamoja na du’aa yenye manufaa makubwa zaidi, nayo ni kuomba hidaayah ambayo ndio asili ya furaha na mafanikio katika nyumba mbili za dunia na aakhirah.  Na hapa ni pale unaposoma:

 

"اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ"

 

“Tuongoze njia iliyonyooka”.

 

Mbali na uzito wa du’aa hii, unaposimama ndugu Muislamu kuswali, basi usisahau kuhudhurisha moyo wako kwa kukizingatia kila unachokisoma na kila unachokitenda.  Unaposoma Suwrat Al-Faatihah ujue kwamba Allaah Anakujibisha neno kwa neno.  Ukiyazingatia, basi Naye Atakuzingatia na kukujibu du’aa yako, na usipoyazingatia, basi matunda yake yanakuwa ni madogo mno.  Katika Al-Hadiyth Al-Qudsiy, Allaah Anasema:

 

"قَسَمْتُ الصَّلَاةَ بَيْنِي وَبَيْنَ عَبْدِي نِصْفَيْنِ، وَلِعَبْدِي مَا سَأَلَ، فَإذَا قَالَ الْعَبْدُ:  الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ، قَالَ اللَّهُ تَعَالَى : حَمِدَنِي عَبْدِي، وَإذَا قَالَ:  الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ، قاَلَ اللَّهُ تَعَالَى: أَثْنَى عَلَيَّ عَبْدِي، وَإذَا قَالَ:  مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ، قَالَ : مَجَّدَنِي عَبْدِي،

 

“Nimeigawa Al-Faatihah kati Yangu na Mja Wangu nusu mbili, na Mja Wangu atapata aliloliomba.  Mja akisema:

 

الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ

 

Allaah Ta’aalaa Husema:  Mja Wangu amenihimidi.

 

Na akisema:

الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

 

Allaah Ta’aalaa Husema:  Mja Wangu amenisifu.

 

Na anaposema:

 

مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ

 

Allaah Husema: Mja Wangu amenitukuza”. [Muslim: Kitaabu As Swalaat]

 

Hii ndio nusu ya kwanza ambapo umemhimidi Allaah, umemsifu na umemtukuza.  Hayo yote yanahusiana Naye.

 

Ama nusu ya pili ya kuizingatia zaidi, ni hii ya wewe kumwomba hidaayah.  Na hapo Allaah Husema:  Hili ni kati Yangu Mimi na Mja Wangu, na Mja Wangu atapata aliloliomba.  Na hii ni dhamana Allaah Anatupa kwamba du’aa hii tunayoiomba kila siku katika Swalaah zetu katika Suwrah hii Anatukubalia ikiwa sisi tutaisoma kwa uzingativu, unyenyekevu na ikhlasi, tukijua kwamba tumesimama mbele Yake, Yeye Anatusikiliza, Anatujibisha na Anatuahidi kwamba tuliloliomba tutalipata.  Na kwenye Hadiyth hii, Allaah Ameiita Al-Faatihah kwa jina la Swalaah, kwa kuwa Swalaah haitimii bila kuisoma Al-Faatihah.

 

Hivyo basi, tunapohirimia, tuweke mbali kabisa mawazo yetu na mishughuliko yetu yote ya kidunia na tuizingatie vyema suwrah hii pamoja na yote yanayohusiana na Swalaah.

 

Kuomba hidaayah tunakuhitajia zaidi kuliko kuomba shida zetu zingine zote. Na kwa ajili hiyo, Allaah Mtukufu Ametuwekea Suwrah hii tuisome katika kila rakaa ya Swalaah zetu.  Tumwombe humo hidaayah mara 17 katika Swalaah za faradhi za kila siku kwa moyo uliohudhurishwa, na kwa unyenyekevu na kwenye Swalaah nyingine zote za Sunnah.  Na kwa ajili hiyo, Waumini wenye kuswali kwa khushui katika Swalaah zao, Allaah Amewaeleza kuwa ni katika waliofaulu kutokana na du’aa iliyomo humo na mengineyo yote yaliyokusanywa ndani yake.

 

Muislamu anapoiomba du’aa hii adhimu ni kama vile anasema:  “Ee Rabbi wetu! Tuonyeshe na Tuongoze, na Tupe tawfiyq tushikamane na Njia Yako iliyonyooka ambayo itatufikisha sisi katika Nyumba Yako ya Pepo za neema. Kwani mwenye kuthibiti juu ya njia hiyo hapa duniani, basi unyayo wake utathibiti vyema juu ya Swiraat iliyosimamishwa juu ya mgongo wa Jahannamu.  Na kwa kiasi cha mtu kutembea juu ya njia hii hapa duniani, ndivyo atakavyotembea juu ya njia hiyo ya Swiraat Siku ya Qiyaamah.

 

Kisha du’aa inabainisha njia hiyo tunayoiomba.  Hapo tunasoma na kusema:

 

"صِرَاطَ الَّذِينَ أَنْعَمْتَ عَلَيْهِمْ "

 

“Njia ya wale Uliowaneemesha”.

 

Hapa unatawasali kwa Allaah kwa Neema Zake na kwa ihsani Zake kwa wale Aliowaneemesha kwa kuwapa hidaayah hiyo.

 

Unamwambia Allaah:  Hakika Wewe Umewaneemesha hao kwa kuwapa hidaayah, na bila shaka hilo ni kutokana na Neema Zako kwao.  Basi na mimi Nijaalie nipate sehemu ya neema hii, na Unijaalie niwe miongoni mwa hawa Uliowaneemsha.

 

Watu hawa ni akina nani?  Hawa ni Manabii, Swiddiqina, Mashuhadaa na Swalihina kama Alivyosema:

 

"وَمَنْ يُطِعِ اللَّهَ وَالرَّسُولَ فَأُولَئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللَّهُ عَلَيْهِمْ مِنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاءِ وَالصَّالِحِينَ وَحَسُنَ أُولَئِكَ رَفِيقًا "

 

Na atakayemtii Allaah na Rasuli, basi hao watakuwa pamoja na wale Allaah Aliowaneemesha miongoni mwa Manabii na Swiddiqiyna na Mashuhadaa na Swalihina, na uzuri ulioje kuwa pamoja na hao!”.   [An-Nisaa: (69)]

 

Hili ndilo la kuliomba kwa nguvu zote na kulipigania wakati wote wa umri wetu.  Ni uzuri ulioje kuwa pamoja na hawa!  Beba utajiri wote wa dunia, beba umashuhuri wote wa dunia, beba medali zote za dunia, lakini usipokuwa kwenye kundi hili, basi umekula hasara.  Ndipo hapo unapoomba zaidi usiwe katika kundi la walioghadhibikiwa na waliopotea unaposema:

 

غَيْرِ الْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ وَلَا الضَّالِّينَ

 

“Si ya walioghadhibikiwa wala waliopotea”.

 

Walioghadhibikiwa ni Mayahudi.  Anaingia pia ndani ya kundi hili kila yule aliyeijua haki kisha asiifuate au kuifanyia kazi.  Na waliopotea ni Manasara.  Makundi yote haya mawili yameingia katika hasara kubwa ya kuishia kwenye moto wa Jahannamu.  Na hapa unamwomba Allaah usije kuingia kwenye makundi haya mawili au makundi mengine potovu ambayo mwisho wake ni motoni.

 

Na imesuniwa vile vile kuitikia “aamiyn” ni sawa mtu akiwa anaswali peke yake, au akiwa ni imamu, au akiwa maamuma, na katika hali zote.  Imesimuliwa na Abu Hurayrah kwamba Rasuli wa Allaah amesema:

 

"إذَا أمَّنَ الإمَامُ فَأَمِّنُوا فَإِنَّهُ مَنْ وَافَقَ تَأْمِينُهُ تَأْمِينَ المَلاَئِكةِ غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ"

 

“Imamu akisema “aamiyn”, basi nanyi semeni aamiyn, kwani yeyote ambaye “aamiyn yake itawafikiana na ya Malaika, basi ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia”.  [Al-Bukhaariy: Kitaabul Aadhaan]

 

Mbali na kuongozwa katika njia iliyonyooka uliyoiomba, pia unasamehewa madhambi yako yote ya nyuma kwa kusema tu “aamiyn”.  Ni Rehma iliyoje ya Allaah kwetu sisi!

                                                             

 

 

Share