03-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Mema Ya Dunia Na Aakhirah

 

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

03-Mema Ya Dunia Na Aakhirah

 

 

 

 

 

"رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الآخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّار"

 

Rabb wetu! Tupe katika dunia mazuri na katika Aakhirah mazuri na Tukinge na adhabu ya moto”.  [Al-Baqarah: (201)]

 

Du’aa hii ndani yake kuna kukiri “Rubuwbiyyah Kuu” ya Allaah Ta’aalaa yenye kuwajibikiana na kumpwekesha Yeye tu katika Uungu.  Hili ndilo linalotakikana kwa mwenye kuomba du’aa, ahudhurishe maana hizi njema za Umola Wake Ta’alaa kwa Viumbe Vyake vyote, nalo ni jambo ambalo linamfanya mja awe mnyenyekevu na mwenye kuonja ladha ya kunong’onezana na Mola Wake katika du’aa kama hii ambayo hailingani na kitu chochote katika anavyovipenda.

 

Katika du’aa hii, anaomba kheri zote za dunia kwa tamshi fupi kabisa na maneno machache mno.  Du’aa hii imekusanya kheri zote za dunia anazozitamani mtu, kwani mema katika “Tupe katika dunia mazuri” yanajumuisha matakwa yote mema ya hapa duniani ikiwa ni pamoja na afya njema, nyumba pana yenye wasaa, mke mwema au mume mwema au watoto wema, riziki kunjufu, elimu nufaishi, amali njema, kipando maridhawa, usalama na amani na mengineyo muhimu katika maisha yetu.

 

Ama mema ya aakhirah, hayo bila shaka ni Pepo, kwani ambaye hatoipata Pepo Siku hiyo, basi huyo amenyimwa kheri zote.  Kadhalika, kupata amani kutokana na fazaa kubwa ya kisimamo cha Qiyaamah, kufanyiwa wepesi hisabu, kuweko katika Kivuli cha Allaah huku wengine wakitaabika na kuteseka na mengineyo mengi mema ya Siku hiyo kwa waja wema.

 

Ama “na Utukinge na adhabu ya moto”, hii inajumuisha kutuwepesishia sababu zake hapa duniani, kujiepusha na maharamisho na madhambi, kuwa na tawhiyd safi, kujiepusha na bid’a na kufuata yale yote aliyokuja nayo Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Na kwa vile du’aa hii imekusanya maombi yote ya kidunia na kiaakhirah, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikithirisha kuiomba.  Anas (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema: “Ilikuwa ndio du’aa anayoiomba zaidi Rasuli”.

 

Na Anas akamuiga Rasuli katika hilo, na akawa haiachi katika du’aa zozote anazoziomba. Baadhi ya Maswahaba walimwomba awaombee, naye akawaombea kwa du’aa hii iliyobarikiwa.

 

Tunajifunza kutokana na du’aa hii:

 

1-  Kwamba tuombe kheri zote za dunia na aakhirah.

 

2-  Tunapoomba tutawassal kwa Sifa za kivitendo za Allaah Ta’aalaa kama hapa “Tukinge”.

 

3-  Mtu halaumiwi kuomba kheri za dunia pamoja na kheri za aakhirah.

 

4-  Kila mmoja wetu anahitajia mema ya dunia na mema ya aakhirah.

 

5-  Uzuri wa du’aa ni iwe yenye kukusanya utashi:  “Tupe duniani mema na aakhirah mema”, na khofu pia:  “Utukinge na adhabu ya moto”.  Hii inamfanya mtu kuwa kati ya khofu na matumaini.

 

6-  Umuhimu wa kuomba kwa du’aa zilizomo kwenye Qur-aan Tukufu.  Du’aa hizi ni toshelezi na jumuishi kwa matakwa yote anayoyatamani mtu katika dini yake, dunia yake na aakhirah yake.  Muislamu anatakiwa awajibike nazo pamoja na zile zilizopokelewa toka kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) badala ya kutumia du’aa za kutungwa na watu ambazo mara nyingi zinakuwa na maneno yasiyomridhisha Allaah Ta’aalaa.

 

 

Share