04-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Nyoyo Zisipotoshwe

 

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

 

Alhidaaya.com

 

04-Nyoyo Zisipotoshwe

 

 

"رَبَّنَا لاَ تُزِغْ قُلُوبَنَا بَعْدَ إِذْ هَدَيْتَنَا وَهَبْ لَنَا مِن لَّدُنكَ رَحْمَةً إِنَّكَ أَنتَ الْوَهَّابُ"

 

Rabb wetu! Usizipotoe nyoyo zetu baada ya kuwa Umetuhidi, na Tutunukie kutoka Kwako rahmah. Hakika Wewe Ni Mwingi wa Kutunuku na Kuneemesha”.  [Aal ‘Imraan: (08)]

 

Kuthibiti katika dini, iymaan na njia iliyonyooka ni takwa muhimu ambalo Muislamu anatakiwa amwombe Mola wake wakati wote.  Na kulipata takwa hili hakuwi ila kwa tawfiyq toka kwa Allaah Mtukufu.  Kutokana na umuhimu wake, hata Rasuli mwenyewe alikuwa akikithirisha kuomba akisema:

 

"اللَّهُمَّ مُصَرِّفَ الْقُلُوبِ صَرِّفْ  قُلُوبَنَا عَلَى طَاعَتِكَ"

 

“Ee Allaah! (ee) Mwenye kuzigeuza nyoyo, Zigeuze nyoyo zetu ziwe juu ya utiifu Kwako”.  [Sunan At-Tirmidhiy]

 

Na alikuwa pia anaomba:

 

"يَا مُقَلِّبَ الْقُلُوبِ ثَبِّتْ قَلْبِي عَلَى دِينِكَ"

 

“Ee Mwenye Kuzipindua nyoyo, Uthibitishe moyo wangu juu ya Dini Yako”. [Swahiyh Muslim: Kitaabul Qadar]

 

Na baada ya kuomba kukitwa nyoyo zao juu ya iymaan, hawatosheki na hilo, bali pia wanamwomba Allaah Awatunuku Rahma Zake toka Kwake. Wanamwomba Rahma Zake pana jumuishi zitakazowafanya kupata nuru ya iymaan, tawhiyd na maarifa ndani ya nyoyo zao, na kupata pia utiifu kamili wa viungo.   Miongoni mwa matokeo ya rahmah hii ni kudumu juu ya uongofu hapa duniani, na kuzipata neema za kudumu huko aakhirah.  Na kwa ajili hiyo, du’aa hii ya kuomba rahmah imekuja kwenye aayah nyingi ndani ya Qur-aan Tukufu.  Kuzipata rahmah hizi za Allaah ni ufaulu mkubwa mno kwa Muislamu, kwa kuwa hata kuingia Peponi kunasimamia juu ya msingi wa kuzipata rahmah.  Bila rahmah hakuna Pepo, hata mtu awe na mema ya kiasi gani.  Hata Rasuli mwenyewe anasema kuwa hawezi kuingia Peponi ila baada ya kufunikwa na Rahma za Allaah.

 

Kutokana na haya, inatubainikia umuhimu wa kukithirisha kuomba Rahmah za Allaah ili tuweze kufaulu hapa duniani na kesho aakhirah, na tuweze kuingia Peponi kwa Rahmah hizo.

 

Kutokana na du’aa hii tunajifunza haya yafuatayo:

 

1-  Mwanadamu hana uwezo wa kuumiliki moyo wake, kwani moyo huu uko kati ya Vidole Viwili katika Vidole vya Allaah ambapo Anaugeuza Anavyotaka. Hili limethibitishwa na Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Hivyo ni muhimu sana kukithirisha du’aa hii ili moyo uthibiti katika iymaan na wala usiyumbe yumbe au kutoka nje ya duara la iymaan.

 

2-  Kumwomba Allaah kuthibiti juu ya iymaan ni moja kati ya makusudio makubwa anayotakiwa Muislamu ayapupie.

 

3-  Muislamu anatakiwa azihudhurishe wakati wote Neema za Allaah kwake.

 

4-   Umuhimu wa kutawassal kwa Allaah kupitia Neema Zake kwa kusema: “Baada ya kutuhidi”.

 

5-  Viumbe wote hawana budi ila kumwomba Rabbi wao katika kuwaletea manufaa na kuwaondoshea madhara.

 

 

 

Share