05-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Watoto Wema

 

 

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

05-Watoto Wema

 

 

 

"رَبِّ هَبْ لِي مِن لَّدُنْكَ ذُرِّيَّةً طَيِّبَةً إِنَّكَ سَمِيعُ الدُّعَاءِ"

 

Rabb wangu! Nitunukie kutoka Kwako kizazi chema, hakika Wewe Ni Mwenye Kusikia du’aa yangu”.  [Aal ‘Imraan: (38)]

 

Nabiy Zakariyya (‘Alayhis Salaam) alipoona kwamba Allaah Ta’aalaa Anamruzuku Maryam matunda ya msimu wa baridi wakati wa kipindi cha joto, na matunda ya majira ya joto kipindi cha baridi, hapo alitamani kupata mtoto. Wakati huo alikuwa ni mzee ambaye mifupa yake imedhoofu na nywele zimejaa mvi.  Pamoja na hali hiyo, mkewe pia alikuwa ni tasa.  Lakini kutokana na ukamilifu wa iymaan yake na dhana yake njema kwa Mola wake juu ya ukamilifu wa Uwezo Wake, alielekea kumwomba bila kuchelewa.

 

Akamwomba Mola wake, akamwita mwito wa siri kama Alivyosema Allaah katika Suwrat Maryam:

 

"إِذْ نَادَى رَبَّهُ نِدَاءً خَفِيًّا"

 

Alipomwita Rabb wake mwito wa siri”.  [Maryam: (3)]

 

Tunamwona akimwomba Allaah Amtunuku, kwa kuwa kutunuku ni ihsani anayofanyiwa mtu bila ya mkabala wowote au kwa njia isiyo ya kawaida.  Na hili linanasibiana na hali yake ya utu uzima na utasa wa mkewe ambaye hazai. Ni kana kwamba amesema:  “Nipe mimi bila kupitia njia zilizozoeleka”.  Yeye hapa hakuangalia njia wala visababisho kwa mazingira yake ya kawaida, bali alimwangalia Muumba wake na Mpatishaji wake.  Na hii ndio iymaan safi ya kweli kwa Allaah Ta’aalaa, na ndio dhana njema ya mja kwa Mola wake.

 

Katika du’aa yake hii, Nabiy Zakariyyah ‘Alayhis Salaam amemwomba Allaah Amtunuku watoto wema. Hakuomba tu watoto, bali kafungamanisha ombi lake hilo na wema.  Wema huu ni wa hapa duniani na aakhirah.  Wema uwe katika maneno yao, matendo yao na hata pia katika miili yao.  Ni wema wa kihisia na kidhahania.

 

Du’aa yake ameimalizia kwa kusema:  “Hakika Wewe Ni Mwenye Kusikia maombi”.  Hapa anatoa sababu ya ombi lake.  Kana kwamba anasema:  “Mimi sikukimbilia Kwako na kukuomba isipokuwa kwa kujua kwangu kwa yakini kwamba Wewe Unajibu maombi na wala Humwangushi mtu”.  Kaimalizia kwa Jina Lake Tukufu la “Mwenye Kusikia” ambalo Linanasibiana na ombi lenyewe.   Na hapo moja kwa moja ikamjia bishara ya kukubaliwa ombi lake.

 

Tunajifunza kutokana na du’aa hii:

 

1-  Kwamba viumbe wote wakiwemo Mitume na Manabii wanamhitajia Allaah Ta’aalaa.  Wanahitajia kumwomba katika hali zao zote.

 

2-  Haitakikani mtu aombe tu mtoto, bali aombe watoto wema.  Watoto tu wanaweza kuwa fitnah na kiini cha matatizo kwake yeye mwenyewe.  Watoto wema watamfaa duniani na aakhirah.

 

3-  Dhana njema kwa Allaah ni ‘ibaadah njema pia.  Allaah Humlipa Mja Wake na Humpa kwa mujibu wa nguvu ya dhana yake njema Kwake.  Kutokana na dhana yake njema kwa Allaah, Zakariyah alimwomba Allaah hapo hapo kutokana na yale aliyoyaona kwa Maryam, na Allaah Akamjibu hapo hapo.

 

4-  Mwenye kutamani jambo kubwa, au akaona kitu kikubwa anachokitamani, basi aelekee hapo hapo kwa Allaah amwombe, na wala asicheleweshe.  Nabiy Zakariyyah alipoyaona ya Maryam, hapo hapo akaomba la kwake analolitamani ambalo alikuwa amelikatia tamaa kutokana na hali yake na hali ya mkewe.

 

5-  Hapa kuna kiashirio kwamba du’aa inarejesha qadhwaa.  Hii ni kwa vile, kwa sababu za kawaida tu, mwanamke tasa na mzee hawazai.  Naye alipomwomba Allaah Amruzuku mtoto, bishara ilikuwa moja kwa moja.

 

"فَنَادَتْهُ المَلائِكَةُ"

 

“(Hapo hapo) Malaika akamwita”.

 

6-  Umuhimu wa kutawassal kwa Majina Matukufu ya Allaah pamoja na Vitendo Vyake. Aliposema: هَبْ لِي “Nitunuku”, hapo alitawassal kwa Sifa ya Allaah ya Kutunuku, nayo ni Sifa ya kivitendo, na inanyambulika kutokana na Jina lake la “Al-Wahhaab”.

 

7-  Kwa kutajwa kisa hiki cha ajabu pamoja na ombi jema la Zakariyyah, tunatakiwa tusikate kabisa tamaa na Fadhla za Allaah na Rahma Zake.

 

8-  Inapendeza kuomba du’aa kwa siri.  Hili limeashiriwa na Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"إِذْ نَادَى رَبَّهُ نِدَاءً خَفِيًّا"

 

Alipomwita Rabb wake mwito wa siri.

 

9-  Katika njia bora kabisa za kumfikia Allaah, ni mwombaji kutawassal Kwake kwa kuelezea udhaifu wake, uhitajio wake Kwake na udhalili wake ingawa yote hayo Allaah Anayajua.  Lakini hapa ni kama anakiri hilo kwa kinywa chake kwamba yeye hawezi lolote ila kwa Nguvu na Msaada Wake Allaah.  Angalia Nabiy Zakariyyah anavyojieleza:

 

"رَبِّ إِنِّي وَهَنَ الْعَظْمُ مِنِّي وَاشْتَعَلَ الرَّأْسُ شَيْبًا"

 

Rabb wangu! Hakika mimi mifupa imeninyong’onyea na kichwa kimeng’aa mvi.”  [Maryam: (04)]

 

10-  Kumshtakia Allaah hakupingani na subira, bali ni ukamilifu wa utumwa kwa Allaah Ta’aalaa.

 

 

 

Share