06-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Kuandikwa Pamoja Na Wenye Kushuhudia Haki

 

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

06- Kuandikwa Pamoja Na Wenye Kushuhudia Haki

 

 

 

"رَبَّنَا آمَنَّا بِمَا أَنزَلَتْ وَاتَّبَعْنَا الرَّسُولَ فَاكْتُبْنَا مَعَ الشَّاهِدِينَ"

 

Rabb wetu! Tumeamini Uliyoyateremsha na tumemfuata Rasuli, basi Tuandike pamoja na wanaoshuhudia (haki).  [Aal ‘Imraan: (53)]

 

Du’aa hii iliombwa na wafuasi na wasaidizi waaminifu wa Nabiy ‘Iysaa ‘Alayhis Salaam wajulikanao kama “Al-Hawaariyyuwn”.  Wameitwa hivi kutokana na usafi na weupe wa iymaan zao kwa Allaah Mtukufu wakawa katika daraja za juu kabisa za usafi kwa nje yao na ndani yao.

 

Du’aa yao hii wameianza kwa kutumia Jina Takatifu la Allaah la Rabb wakisema:

 

"رَبَّنَا آمَنَّا بِمَا أَنْزَلْتَ"

 

Rabb wetu! Tumeamini Uliyoyateremsha”.

 

Waombaji wengi wakiwemo Mitume, Manabii na Waumini wema walikuwa wakitawassal kwa Allaah Ta’aalaa kwa kutumia Jina hili.  Hili linaonekana pia kwenye du’aa nyingi zilizoko ndani ya Qur-aan Tukufu na hususan Aayah za mwisho za Suwrat Al-Baqarah.

 

Kisha wakaanza kujieleza wakisema kwamba wao wameamini yale yote Aliyoyateremsha katika Injiyl, na wamemfuata Rasuli wao ‘Iysaa (‘Alayhis Salaam) katika yale yote aliyowaletea – na haya yote Allaah Anayajua-  na kwa ajili hiyo basi wanamwomba Awaandike pamoja na wenye kushuhudia.  Na hii ndiyo iymaan kamili, kwani iymaan ndio msingi wa kila kitu, na ndiyo inayotangulizwa kabla ya yote.  Kwanza kumwamini Allaah, kuamini Ubwana Wake, kuamini Uungu Wake na kuamini Majina Yake na Sifa Zake Tukufu.

 

Wamekusanya katika du’aa yao hii tawassulati mbalimbali adhimu; tawassuli kwa Ubwana wa Allaah, iymaan yao pamoja na matendo yao mema.  Baada ya kujieleza kwao huko, mwisho wakataja ombi lao.  Wakamwomba Allaah Awaandike pamoja na wenye kushuhudia.  Hawa ni wale wenye kushuhudia haki, walioikubali tawhiyd, waliowasadiki Mitume, waliofuata Maamrisho ya Allaah na kujiepusha na makatazo Yake.  Wakamwomba Allaah Awajumuishe katika kundi moja na hawa na Awakirimu pamoja nao.

 

Hili ndilo ambalo kila mmoja wetu anatakiwa aliombe na alipupie ili kuwa katika kundi hilo la wenye kushuhudia.

 

Tunajifunza kutokana na du’aa hii:

 

1-  Kwamba iymaan ni lazima ikusanye yote Aliyoyateremsha Allaah.

 

2-  Mtu kujishuhudishia mwenyewe kwamba yeye ni Muumini au ni Muislamu au mfano wa hayo, hakuzingatiwi kama ni riyaa na hususan katika kumfuata Rasuli na yote aliyokuja nayo. Kwa kuwa hilo lina faida, nayo ni kumtia nguvu mfuatwa.

 

3-  Kuna umuhimu mkubwa wa kutawassal kwa Allaah kwa wasiylah zaidi ya moja. Manabii walitawassal kwa Allaah kwa wasiylah mbili kuu ambazo ni kumwamini Yeye na kufuata yote Aliyowateremshia.

 

 

4-  Muislamu awe na pupa ya kusuhubiana na watu wema, kwa kuwa katika hilo kuna utengefu kwake duniani na aakhirah.

                                                                         

 

 

 

 

 

 

 

Share