08-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Kukingwa Na Moto, Maghfirah, Kufishwa Pamoja Na Wema

 

 

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

 

08-Kukingwa Na Moto, Maghfirah Na Kufishwa Pamoja Na Watu Wema

 

 

 

"رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَذا بَاطِلاً سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ * رَبَّنَا إِنَّكَ مَن تُدْخِلِ النَّارَ فَقَدْ أَخْزَيْتَهُ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ * رَّبَّنَا إِنَّنَا سَمِعْنَا مُنَادِيًا يُنَادِي لِلإِيمَانِ أَنْ آمِنُواْ بِرَبِّكُمْ فَآمَنَّا رَبَّنَا فَاغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا وَكَفِّرْ عَنَّا سَيِّئَاتِنَا وَتَوَفَّنَا مَعَ الأبْرَارِ * رَبَّنَا وَآتِنَا مَا وَعَدتَّنَا عَلَى رُسُلِكَ وَلاَ تُخْزِنَا يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّكَ لاَ تُخْلِفُ الْمِيعَادَ"

 

Rabb wetu, Hukuumba haya bure, Utakasifu Ni Wako, basi Tukinge na adhabu ya moto •  Rabb wetu! Hakika Umuingizaye motoni, kwa yakini Umemhizi, na madhalimu hawana wasaidizi wa kuwanusuru •  Rabb wetu! Hakika sisi tumemsikia mwitaji anaita kwenye iymaan kwamba mwaminini Rabb wenu basi tukaamini.   Rabb wetu! Tughufurie madhambi yetu na Tufutie mabaya yetu na Tufishe pamoja na Waumini wema •  Rabb wetu! Tupe pia Uliyotuahidi kupitia Rusuli Wako, wala Usituhizi Siku ya Qiyaamah, hakika Wewe Huendi kinyume na miadi”.  [Aal ‘Imraan (191-194)].

 

Du’aa hizi tukufu zinatoka kwa watu waliojaa iymaan.  Inatakikana kwa kila Muislamu asimame kidogo kuzitaamuli na kuzizingatia kutokana na mengi muhimu yaliyoko ndani yake.

 

Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) alimuuliza Mama yetu Swiddiyqah bint As Swiddiyq (Radhwiya Allaah ‘anhaa):

 

"أَخْبِرِينَا بِأَعْجَبِ شَيْءٍ رَأَيْتِيهِ مِنْ رَسُولِ اللَّهِ ، قَالَ: فَسَكَتَتْ ثُمَّ قَالَتْ: لَمَّا كَانَ لَيْلَةً مِنَ اللَّيَالِيِ قَالَ:  يَا عَائِشَةُ، ذَرِينِي أَتَعَبَّدُ اللَّيْلَةَ لِرَبِّي، قُلْتُ: وَاَللَّهِ إنِّي لَأُحِبُّ قُرْبَك، وَأُحِبُّ مَا يَسُرُّك، قَالَتْ: فَقَامَ فَتَطَهَّرَ، ثُمَّ قَامَ يُصَلِّي، قَالَتْ: فَلَمْ يَزَلْ يَبْكِي حَتَّى بَلَّ حِجْرَهُ، قَالَتْ: وَكَانَ جَالِسًا، فَلَمْ يَزَلْ يَبْكِي حَتَّى بَلَّ لِحْيَتَهُ، قَالَتْ: ثُمَّ بَكَى، فَلَمْ يَزَلْ يَبْكِي حَتَّى بَلَّ الْأَرْضَ، فَجَاءَ بِلَالٌ يُؤْذِنُهُ بِالصَّلَاةِ، فَلَمَّا رَآهُ يَبْكِي قَالَ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، لِمَ تَبْكِي وَقَدْ غُفِرَ لَك مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِك وَمَا تَأَخَّرَ؟ قَالَأَفَلَا أَكُونُ عَبْدًا شَكُورًا؟ لَقَدْ نَزَلَتْ عَلَيَّ اللَّيْلَةَ آيَةٌ وَيْلٌ لِمَنْ قَرَأَهَا وَلَمْ يَتَفَكَّرْ فِيهَا : إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ......."

 

 “Tueleze jambo la ajabu zaidi uliloliona kwa Rasuli wa Allaah.  Anasema: Akanyamaza (kukumbuka moja kati ya mambo hayo) kisha akasema: Ulipokuwa usiku mmoja kati ya nyusiku alisema: Ee ‘Aaishah! Niruhusu nifanye ‘ibaadah usiku huu kwa ajili ya Mola wangu.  Nikamwambia:  Wa Allaah, mimi napenda kuwa nawe karibu, na ninapenda linalokufurahisha. Akaenda kujitwaharisha, kisha akasimama na kuanza kuswali.  Na hakuacha kuendelea kulia mpaka akailowesha nguo yake.  Alikuwa amekaa, na akaendelea kulia mpaka akazitotesha ndevu zake.  Kisha akalia, na akaendelea kulia mpaka akailowesha sakafu.  Halafu Bilaal akaja kumjulisha wakati wa Swalaah.  Alipomwona analia alimwambia:  Ee Rasuli wa Allaah! Kwa nini unalia nailhali wewe umeshasamehewa madhambi yako yaliyopita na yajayo?!  Akamwambia:  Kwa nini nisiwe mja mwingi wa kushukuru! Hakika imeniteremkia usiku huu aayah.  Ole wake atakayeisoma na asiyataamuli yaliyomo humo:  (Akasoma):  Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi, na mabadiliko ya mfuatano wa usiku na mchana; bila shaka ni Aayaat (ishara, zingatio) kwa wenye akili.”  [Imesimuliwa na Ibn Hibaan katika Swahiyh yake.  Al-Albaaniy kasema: Isnaad yake ni nzuri]

 

Yaani, hizi mbingu zilivyonyanyuliwa na zilivyotanuliwa bila mipaka wala bila nguzo, na ardhi ilivyokuwa chini ya mbingu kwa masafa yasiyoweza kukokoteka, mbali na yaliyomo ndani ya viwili hivi na vilivyo baina yake kati ya tunavyovijua na tusivyovijua, bila shaka kwa wenye akili zingativu ni ishara ya wazi ya uwepo wa Allaah Ta’aala.  Wenye akili hawa ni wale wanaomdhukuru Allaah katika hali zao zote kwa siri na hadharani.

 

Na wanatafakuri na kutaamuli uumbaji huu usio na mfano ambao hawezi yoyote kuufanya isipokuwa Allaah Mtukufu.  Hii inadulisha kwamba kutafakuri huku ni katika sifa za Mawalii wa Allaah Ta’aalaa, na pia ni katika ‘ibaadah kubwa kabisa za moyo.  Ni kutafakuri kwa kina kila kile unachokiona kwa macho yako katika maisha yako ya kila siku.  Vyote hivyo vinaonyesha Uwezo wa Allaah na Uumbaji wake usio na kombo.

 

“Subhaanak” ni neno linalotokana na “Tasbiyh”.  Maana yake ni kutakasa na kuweka mbali na ubaya au kasoro.  Tunaposema “Subhaanah”, ni kuwa tunamtakasa Allaah Ta’aalaa kutokana na upungufu au kufanana na Viumbe Vyake.  Tunamtakasa Yeye kuumba kitu kwa mchezo tu bila hikmah au lengo maalum.

 

Maneno yote haya yanaonyesha uzuri wa kutawassuli kwao wakati wa kuomba du’aa kwa kuyaeleza hayo kabla ya kusema ombi lao.  Ni uzuri ulioje wa kuitandaza du’aa kwa tawasuli badala ya kuifupisha!

 

Na baada ya kutafakuri kwa kina, na kumtakasa Allaah kutokana na upungufu au kasoro yoyote, au kufanana na kiumbe Chake chochote, moja kwa moja wakamwomba Allaah Awakinge na adhabu ya moto.   Kisha wakaeleza sababu ya kuomba kinga dhidi ya moto huo wakisema:

 

"رَبَّنَا إِنَّكَ مَن تُدْخِلِ النَّارَ فَقَدْ أَخْزَيْتَهُ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ"

 

“Rabb wetu! Hakika Umuingizaye motoni, kwa yakini Umemhizi. Na madhalimu hawana wasaidizi wa kuwanusuru”.

 

Yaani Umemdhalilisha na Umemkhizi mbele ya halaiki katika “Mahshar”. Atakayekumbwa na hali hiyo, basi hatopata msaidizi yeyote, kwani Ufalme Siku hiyo ni Wake tu Allaah Al-Waahid Al-Qahhaar.  Hiyo ndiyo Siku ambayo Waumini wanaiogopa ya kusimamishwa mbele ya Allaah na kuhisabiwa.  Hao kwa khofu hiyo, jazaa yao itakuwa ni Jannah.

 

 

"وَأَمَّا مَنْ خَافَ مَقَامَ رَبِّهِ وَنَهَى النَّفْسَ عَنِ الْهَوَىٰ • فَإِنَّ الْجَنَّةَ هِيَ الْمَأْوَىٰ"

 

 

“Ama yule aliyekhofu kisimamo mbele ya Rabb wake, na akaikataza nafsi yake na hawaa • Basi hakika Jannah ndio makaazi yake”.  [An-Naazi’aat: (40-41)]

 

 

Na baada ya kuomba kinga dhidi ya moto, wakaendelea kutawassuli zaidi kwa kujieleza kwa Allaah kwamba  wamemsikia mwitaji anaita kwenye iymaan, naye ni Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), nao bila kusita wakamwamini.  Baada ya kujielezea kwa hili, hapo hapo wakaunganisha du’aa ya kuomba waghufuriwe madhambi yao, wafutiwe mabaya yao na wafishwe pamoja na Waumini wema wakisema:

 

"رَبَّنَا فَاغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا وَكَفِّرْ عَنَّا سَيِّئَاتِنَا وَتَوَفَّنَا مَعَ الأبْرَارِ"

 

“Rabb wetu!  Basi Tughufurie madhambi yetu na Tufutie mabaya yetu na Tufishe pamoja na Waumini wema”.

 

Yaani, kwa sababu ya sisi kumsikia Rasuli akiulingania Uislamu, nasi tukamwamini na kukuamini Wewe, basi Tupe haya tuliyoyaomba. Wameitanguliza tawassuli hiyo huku wakijenga dhana njema kwa Allaah ili iwe njia ya kupatiwa lengo lao kuu la kupata maghfira na kuokoka Siku hiyo ya Qiyaamah.

 

Wakaendelea kuomba Allaah Awatekelezee yale Aliyowaahidi kupitia Rusuli Wake ya kuwanusuru, kuwamakinisha ardhini, kuzipata Radhi Zake na Jannah Yake aakhirah.  Na pia Asiwakhizi Siku ya Qiyaamah.  Wakaongezea hapa tawassuli nyingine ya kumwambia Allaah kwamba Yeye Hakhalifu Ahadi Yake.

 

* رَبَّنَا وَآتِنَا مَا وَعَدتَّنَا عَلَى رُسُلِكَ وَلاَ تُخْزِنَا يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّكَ لاَ تُخْلِفُ الْمِيعَادَ"

 

“Rabb wetu!  Tupe pia Uliyotuahidi kupitia Rusuli Wako, wala Usituhizi Siku ya Qiyaamah, hakika Wewe Huendi kinyume na miadi”.

 

Na kutokana na kutawassuli kwao kwa kujieleza kwa mambo tofauti waliyoyafanya, na kutumia kwao Jina la Rabbi linalobeba maana ya ubwana, ulezi na usimamizi kwa viumbe vyote, kuwa kwao na ikhlasi na kuwa na dhana njema kwa Allaah,  Allaah Aliwajibu du’aa yao.

 

Aayah hizi bainifu zinazotufafanulia du’aa njema wanazoziomba watu wenye akili angavu, zinatuhimiza tujitahidi kuziomba kwa unyenyekevu na udhalili. Na kutokana na umuhimu wake, imethibiti kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akizisoma anaposimama usiku.

 

 

Tunajifunza kutokana na du’aa hizi:

 

1-  Kuna umuhimu mkubwa sana wa kutaamuli uumbwaji wa mbingu na ardhi, kwa kuwa Allaah Ta’aalaa Ametaja ndani yake ishara nyingi.

 

2-  Kutaamuli uumbaji wa Allaah kunamfanya Muislamu afanye ‘ibaadah kwa uzuri zaidi ikiwa ni pamoja na dhikri, du’aa, unyenyekevu na iymaan kuongezeka.

 

3-  Fadhla ya kudumu katika kumdhukuru Allaah kwenye hali zote.

 

4-  Umuhimu wa kumtakasa Allaah kutokana na kasoro yoyote au upungufu wowote (Kumsabbih).

 

5-  Viumbe bora watakasifu wakiwemo Watu Wema na Manabii wanahitaji kuomba du’aa ya kulindwa na moto sembuse watu wa kawaida.

 

6-  Du’aa kama inavyokuwa kwa tamko la ombi, inakuwa vile vile kwa tamko taarifu lenye kumaanisha ombi. Ni katika Kauli Yake Ta’aalaa:

 

رَبَّنَا إِنَّكَ مَن تُدْخِلِ النَّارَ فَقَدْ أَخْزَيْتَهُ

 

“Rabb wetu! Hakika Umuingizaye motoni, kwa yakini Umemhizi”… kwa maana:  Usitukhizi, Ukatuingiza motoni.

 

7-   Kumwomba Allaah Ta’alaa mahitajio ya kidini, kidunia na kiaakhirah, ndio du’aa bora zaidi na ya ngazi ya juu zaidi.

 

8-  Ubora wa kuikunjua du’aa badala ya kuifupisha, kwa kuwa kuikunjua kunasisitiza utumwa zaidi wa mja kwa Allaah.  Kila mtu anavyokithirisha kuomba na kurefusha, hapo utumwa wake kwa Allaah unazidi kuongezeka pamoja na shauku.  Pia kunadulisha mtu kutochoka na kukata tamaa, na hili ni katika visababisho vya kujibiwa.

 

9-  Ni vizuri mwombaji ataje baadhi ya Neema za Allaah kwake wakati anapoomba kutokana na Neno Lake Ta’aalaa:

 

"أَنْ آمِنُوا بِرَبِّكُمْ فَآمَنَّا"

 

10-  Mtu kuitaja amali yake njema hakuipomoshi.  Ni kwa Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"أَنْ آمِنُوا بِرَبِّكُمْ فَآمَنَّا"

 

11- Inafaa kutawassal kwa amali njema katika du’aa.  Ni kwa Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"رَبَّنَا إِنَّنَا آمَنَّا"

 

12-  Umuhimu wa kutawassal kwa Allaah kwa kutumia Majina na Sifa Zake.

 

13-  Katika uzuri wa du’aa ni mwombaji kueleza sababu ya ombi lake.  Ni kama walivyosema:

 

  إِنَّكَ مَنْ تُدْخِلِ النَّارَ فَقَدْ أَخْزَيْتَهُ[ ،]إِنَّكَ لَا تُخْلِفُ الْمِيعَادَ  

 

14-  Kusifu sana pamoja na tawassulati kubwa ni sababu kubwa ya kujibiwa du’aa.

 

15-  Uhalali wa kutawassali kwa Allaah kwa kutumia Sifa Zake Kanushi kama vile: "إِنَّكَ لَا تُخْلِفُ الْمِيعَادَ" Hakika Wewe Huendi kinyuke na ahadi.

 

 

 

Share