09-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Bila Maghfirah Na Rahma Hatima Ni Khasara

 

                       

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

09-Bila Maghfirah Na Rahma Hatima Ni Khasara

 

 

 

"رَبَّنَا ظَلَمْنَا أَنفُسَنَا وَإِن لَّمْ تَغْفِرْ لَنَا وَتَرْحَمْنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ"

 

Rabb wetu! Tumedhulumu nafsi zetu, na basi Usipotughufuria na Ukaturehemu, bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliokhasirika”. [Al-A’araaf: (23)].

 

Du’aa hii ya barakah ni ya baba na mama yetu Aadam na Hawaa (‘Alayhimas Salaam).  Inatuonyesha namna ya kutubia na kurejea kwa Allaah baada ya kufanya makosa.  Na kwa ajili hiyo, Allaah Ameitaja ili iwe ni mwangaza kwetu mpaka Siku ya Qiyaamah.

 

Katika du’aa hii, baba yetu na mama yetu baada ya kukiri kwamba wamezidhulumu nafsi zao, wameomba kwanza wasamehewe na kisha warehemewe, yaani wameomba maghfirah kabla ya rahmah, kwa kuwa rahmah haipatikani ila kwa maghfirah.  Na mpangilio huu umekuja kwenye aayaati nyingi ndani ya Qur-aan Tukufu.  Na ndio maana kuomba maghfirah kumehimizwa sana ndani ya Qur-aan na faida zake nyingi kutajwa ndani yake pamoja na kwenye Hadiyth za Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Tunajifunza kutokana na du’aa hii:

 

1-  Kwamba kukiri kwanza kosa kisha kukubali kujidhulumu kabla ya kuomba msamaha, kuna matarajio makubwa zaidi ya kukubaliwa du’aa.

 

2-  Umuhimu wa kutawassali kwa Jina la Allaah la Rabb wakati wa kuomba du’aa.

 

3-  Du’aa hii imekusanya aina nne za tawassul:

 

Kwanza:  Kutawassali kwa Jina la Rabb.

 

Pili:  Kutawassali kwa hali ya waombaji kwa kukiri kwao:  “Tumezidhulumu nafsi zetu”.

 

Tatu:  Kulitegemeza jambo kwa Allaah waliposema:  “Na kama Hutotughufuria na Kuturehemu”.

 

Nne:  Kuelezea hatima yao itakavyokuwa kama Hatowasamehe na Kuwarehemu, nayo ni kwamba watakuwa wenye kukhasirika.

 

 

4-  Du’aa hii ni katika miundo bora zaidi ya kuomba maghfirah.  Allaah Ndiye Aliyemfundisha Aadam ‘Alayhis Salaam na itaendelea kuombwa mpaka Siku ya Qiyaamah.

 

 

5-  Ukamilifu wa du’aa ni mwombaji kukusanya kati ya utashi, hofu na tawbah. Hapa ni pale waliposema:

 

 "وَإِنْ لَمْ تَغْفِرْ لَنَا وَتَرْحَمْنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ"

 

6-  Dhambi lolote ni lazima tulikuze na tulione kubwa, kwani dhambi lolote kwa haki ya mkubwa ni kubwa.

 

 

7-  Du’aa ndio makimbilio kwa Manabii na Mitume wote.  Hakuna awezaye kughafilika nayo au kutoijali isipokuwa waovu.

 

 

 

Share