10-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Kuepushwa Kuwa Kundi Moja Na Madhalimu

 

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

                  

10-Kuepushwa Kuwa Kundi Moja Na Madhalimu

 

 

"رَبَّنَا لاَ تَجْعَلْنَا مَعَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ"

 

“Rabb wetu! Usitujaalie kuwa pamoja na watu madhalimu”.   [Al-A’araaf: (23)]

 

Hii ni du’aa ya watu wa “Al-A’araaf”, napo ni mahala kati ya Pepo na moto.  Si mahala pa kutulia hapo, bali ni pa watu ambao mema yao yamelingana na mabaya yao.  Watakaa hapo kwa muda Aupendao Allaah, kisha hatimaye wataingia Peponi baada ya roho kuwa juu juu.  Watakuwa wakiogopa hata kutupa jicho kuwaangalia watu wa motoni kutokana na kitisho kikubwa cha moto wenyewe na hali za waliomo humo.  Hapo macho yao yatageuziwa huko waangalie, na kutokana na watakayoyaona, ndipo wataomba du’aa hii Allaah Asiwapeleke huko wakajumuika na hao madhalimu. 

 

"وَإِذَا صُرِفَتْ أَبْصَارُهُمْ تِلْقَاءَ أَصْحَابِ النَّارِ قَالُوا رَبَّنَا لَا تَجْعَلْنَا مَعَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ"

 

“Na yatakapogeuzwa macho yao kuelekea watu wa motoni watasema: Rabb wetu! Usitujaalie kuwa pamoja na watu madhalimu”.   [Al-A’araaf: (47)]

 

Hakika ni kisimamo kigumu mno hapo!  Hali hii inatuzindusha kuwa tujitahidi kiasi tuwezavyo kufanya amali zote njema ili mizani yetu iwe nzito tusije kukwama hapo, na tujiepushe na yote mabaya hata kama tunayaona ni madogo vipi.  Pengine tasbiyha moja tu inaweza ikailaza miyzaan akaokoka mtu, au kosa moja dogo tu linaweza kupindua mizani na kumfanya mtu kuingia Motoni. Tusidharau jema lolote, tusidharau baya lolote.

 

Muumini anatakiwa aendelee kumwomba Allaah Ta’aalaa Asimjaalie kuwa pamoja na watu madhalimu hapa duniani na huko aakhirah.  Anatakikana aepukane nao hapa hapa duniani ili asije kuwa nao kundi moja Siku ya Qiyaamah, kwani watakuwa mahala pabaya kabisa kwenye adhabu ya kuwadhalilisha.

 

 

Tunajifunza kutokana na du’aa hii:

 

1-  Kwamba Muislamu anatakiwa ajiepushe na kila lile litakalompelekea katika hatima mbaya ya kuishilia Jahannam –tunajilinda nayo kwa Allaah- katika maneno, vitendo na mwenendo.

 

2-  Muislamu anatakiwa akithirishe kuomba du’aa hii muhimu kwa kuwa imekusanya ndani yake kuomba kinga ya hatima mbaya zaidi.

 

3-  Muislamu ajiepushe awezavyo kushirikiana na madhalimu kwa kuwa atakuwa pamoja nao ndani ya moto.

 

4-  Dhulma si tu kuchukua mali za watu kinyume na sheria, bali ni kila kitendo kitakachomsababishia mtu kuishilia pabaya.  Kwani dhulma ni kukiweka kitu mahala ambapo si pake.  Ukiweka utupu wako sehemu isiyo halali, basi umedhulumu, ukipetuka Mipaka ya Allaah, basi umedhulumu na kadhalika. Allaah Alipomkataza Baba yetu Aadam asile mti Alimwambia:  “Wala msiukaribie mti huu, mtakuwa katika madhalimu”.  Mtu akifanya katazo lolote hata la kidunia, au akavunja sheria, basi anakuwa amejidhulumu mwenyewe kwa kuwa atakabiliwa na vyombo vya sheria.  Na siku hiyo, kila dogo na kubwa litahisabiwa, na hatima ya mtu itakuwa kwa mujibu wa matokeo ya hisabu.

 

 

 

Share