11-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Kuandikiwa Mema Ya Dunia Na Ya Aakhirah

 

 

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

                                 

11- Kuandikiwa Mema Ya Dunia Na Ya Aakhirah

 

 

 

"أَنتَ وَلِيُّنَا فَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَا ۖ وَأَنتَ خَيْرُ الْغَافِرِينَ  • وَاكْتُبْ لَنَا فِي هَـٰذِهِ الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الْآخِرَةِ"

 

“Wewe Ni Mlinzi wetu, basi Tughufurie na Turehemu, Nawe Ni Mbora wa wenye kughufuria •  Na Tuandikie katika dunia hii mazuri na katika Aakhirah”.  [Al-A’araaf (155-156)]

 

Hii ni du’aa iliyoombwa na Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam).  Aliiomba pale alipokwenda na watu wema 70 katika Baniy Israaiyl kwa ajili ya miadi maalum na Allaah ili kumwomba msamaha baada ya kuabudu ndama.  Walipofika mahala pa miadi, watu wake hao walimwambia Muwsaa:  “Hatutokuamini mpaka tumwone Allaah wazi wazi, kwani wewe umezungumza Naye, basi tuonyeshe nasi tumwone”.  

 

Hapo ikawachukua radi na umeme angamizi wakafa.  Na Muwsaa (‘Alayhis Salaam) akaomba du’aa hii.  Akamwomba Allaah Awaghufirie madhambi yao na Awarehemu kwa Rehma Zake ambazo zimekienea kila kitu.  Akatanguliza du’aa kwa Jina Tukufu la Allaah la “Al-Waliyy” lenye maana ya kuwa Allaah Ndiye Mwenye Kuyasimamia mambo ya viumbe vyote ya duniani na aakhirah, na Ndiye Mwenye Kuwalinda na Kuwahifadhi.  Akatanguliza pia kiwakilishi “Wewe” ili  iwe ni ufunguo wa kupenyeza ombi lake la maghfirah na rahma.  Hii ni adabu njema kabisa ya kutawassali kwa Majina ya Allaah Mtukufu.

 

Kisha baada ya kuomba maghfirah na rahmah, akamwomba Allaah Awaandikie mema hapa duniani na aakhirah.  Ameomba kuandikiwa kwa kuwa chenye kuandikwa kinakuwa ni cha kudumu, cha kuendelea na chenye kukariri mara kwa mara.  Ama kitu cha muda tu, hicho hakiandikwi.  Na mema ni neno jumuishi kwa kila lile analolitamani mtu katika dini yake, dunia yake na aakhirah yake.

 

 

Tunajifunza katika du’aa hii:

 

 

1-  Kwamba mwombaji anatakiwa atumie matamshi matukufu zaidi, maana nzuri zaidi na utukuzo kwenye du’aa yake.  Ni kama kutumia kiwakilishi cha “Wewe” kwa Allaah Mtukufu.

 

 

2-  Kutawassali kwa Jina kati ya Majina Matukufu ya Allaah kama "الولي" .  Ni kama ilivyo katika aayah: "وَلِيُّنَا".

 

 

3-  Kuzingatia maombi yenye umuhimu zaidi ya kidunia na kiaakhirah.  Nayo ni kuomba maghfirah na rahmah.  Ni kama pale waliposema: "فاغفر لنا وارحمنا".

 

 

Share