14-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Kufishwa Na Uislamu Na Kuunganishwa Na Watu Wema

                                                                       

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

 

14-Kufishwa Na Uislamu Na Kuunganishwa Na Watu Wema

 

 

 

"تَوَفَّنِي مُسْلِمًا وَأَلْحِقْنِي بِالصَّالِحِينَ"

 

“Nifishe hali ya kuwa Muislamu na Unikutanishe na Swalihina”. [Yuwsuf: (101)]

 

Du’aa hii ya barakah ni ya Nabiy Yuwsuf (‘Alayhis Salaam) aliyomwomba Mola wake ilipotimia kwake neema ya kukutana na kujumuika na wazazi wake na nduguze, pamoja na neema ya Utume na Ufalme.  Alimwomba Mola wake ‘Azza wa Jalla, kama Alivyomtimizia neema hizo hapa duniani, Amtimizie pia huko aakhirah, na Amfishe hali ya kuwa ni Muislamu wakati atakapokufa, na Amkutanishe na Swalihina ambao ni pamoja na nduguze Manabii na Mitume Rehma na Amani za Allaah ziwe juu yao wote.

 

 

Hii inatuonyesha umuhimu wa du’aa, na kwamba du’aa ndio mwenendo wa Manabii na Mitume wote (‘Alayhimus Swalaat was Salaam), na ndio makimbilio yao wakati wa dhiki na faraja na katika hali zao zote.  Na kwamba du’aa inatakikana iwe ndio makimbilio ya mja katika maisha yake na katika mambo yake yote, na kila dogo lake na kila kubwa lake.

 

 

Du’aa hii ameianza kwa kutaja Jina Tukufu la Allaah la Rabb na kuelezea Neema Alizoneemeshwa na Allaah ya kupewa ufalme na kufundishwa kutegua ndoto. Kisha akaandamiza Sifa nyingine ya Allaah ya uumbaji wa mbingu na ardhi na halafu Jina la “Al-Waliyy” (Mlinzi na Msaidizi).  Hizi zote ni katika tawassulaat na adabu njema za kuomba du’aa, na ni mihimili ya kujibiwa.  Haya yote yanadhihirika katika aayah kamili isemayo: 

 

"رَبِّ قَدْ آتَيْتَنِي مِنَ الْمُلْكِ وَعَلَّمْتَنِي مِن تَأْوِيلِ الْأَحَادِيثِ ۚ فَاطِرَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَنتَ وَلِيِّي فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۖ تَوَفَّنِي مُسْلِمًا وَأَلْحِقْنِي بِالصَّالِحِينَ" 

 

“Rabb wangu! Kwa yakini Umenipa utawala, na Umenifunza katika tafsiri za masimulizi (ya ndoto na matukio). Muanzilishi wa mbingu na ardhi. Wewe Ni Mlinzi, Msaidizi wangu duniani na Aakhirah. Nifishe hali ya kuwa Muislamu na Unikutanishe na Swalihina”.  [Yuwsuf: (101)]

 

Amemwomba Allaah Amkite na Amthibitishe imara juu ya Uislamu mpaka Atakapomfisha.  Hali hii inahitajia Msaada wa Allaah na tawfiyq kutoka Kwake, na mja anatakiwa afuate na ashikamane na miongozo yote ya kumfanikishia hilo huku Akimwomba Allaah Amwafikishe hilo.  Na mtu kufa na Uislamu wake na tawhiyd safi, ni katika mafanikio makubwa ambayo sote tunatakikana tuyaendee mbio.  Hiyo ndiyo “Husnul Khaatimah”.  Tuendelee pia kumwomba Allaah Atuepushe na fitnah ya uhai na fitnah ya wakati wa kufa ambapo shaytwaan hufanya juhudi zake zote za mwisho za kumteteresha Muislamu na iymaan yake ili afe kafiri.  Tunaomba salama.

 

Hata Rasuli mwenyewe, pamoja na kwamba ndiye Kipenzi cha Allaah na mwisho wa Manabii na Mitume, alikuwa akimwomba Allaah Amkite na Amthibitishe juu ya Uislamu mpaka afe.  Alikuwa anasema:

 

"يا وليَّ الإسلام وأهله، مسكني بالإسلام حتى ألقاك عليه"

“Ee Mlinzi (na Msimamizi) wa Uislamu na watu wake! Nikite na Nithibitishe kwenye Uislamu mpaka Nikutane Nawe nikiwa bado niko nao”.  [Imesimuliwa na Anas bin Maalik na kukharijiwa na At-Twabaraaniy]

 

Kisha Nabiy Yuwsuf (‘Alayhis Salaam) akamwomba Allaah Amkamilishie neema hizi kwa kumkutanisha na watu wema katika Pepo ya Kudumu.

 

Faida ya du’aa hii:

 

Du’aa hii imejumuisha:

 

1-   Kukiri tawhiyd.

 

2-  Kujisalimisha kwa Rabb ‘Azza wa Jalla.

 

3-  Kudhihirisha uhitajio wa mja Kwake.

 

4-  Kujiweka mbali na ulinzi usio wa Allaah.

 

5-  Kufa juu ya Uislamu kuwa ndio lengo kuu la Muislamu, na kwamba hilo liko mkononi mwa Allaah tu, na si mkononi mwa kiumbe chochote.

 

6-  Kukiri marejeo ya aakhirah.

 

7-  Kuomba usuhuba wa watu wema.

 

Share