16-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Kusimamisha Swalah Pamoja Na Watoto

 

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

 

16- Kusimamisha Swalah Pamoja Na Watoto

 

 

 

 

"رَبِّ اجْعَلْنِي مُقِيمَ الصَّلَاةِ وَمِن ذُرِّيَّتِي ۚ رَبَّنَا وَتَقَبَّلْ دُعَاءِ"

 

“Rabb wangu! Nijaalie niwe mwenye kusimamisha Swalaah pamoja na baadhi ya dhuria wangu.  Rabb wetu!  Nitakabalie du’aa yangu”.  [Ibraahiym: (40)]

 

Hii pia ni du’aa ya Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis Salaam).  Muislamu anatakikana awe na hima na du’aa hii na ashikamane nayo kutokana na umuhimu wake mkubwa.

 

Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) amemwomba Allaah Amjaalie awe ni mwenye kuihifadhi Swalaah katika wakati wake, nguzo zake na masharti yake pamoja na yote yenye kuifanya Swalaah kuwa kamili yenye kukubaliwa.  Na hapa ameikhusisha Swalaah kutokana na umuhimu wake na kuwa kwake nembo ya iymaan na kichwa cha Uislamu.  Amewaombea pia baadhi ya dhuria wake wawe pia ni wenye kuisimamisha Swalaah kwa ukamilifu wake unaotakikana.  Amewakhusu baadhi ya dhuria wake kwa du’aa hii pasina wengine kwa kujua kwake baada ya kujuvywa na Allaah kuwa baadhi ya dhuria wake hawatosimamisha Swalaah, na wengine watakuwa ni makafiri na wengine mafasiki.

 

Kisha akamwomba Allaah kwa kutumia Jina la Rabbu kuonyesha utumwa wake Kwake na kutawassali kwa Jina hilo Tukufu akimwomba Amtakabalie du’aa yake hii.

 

Du’aa hii ni katika du’aa bora kabisa anazoomba Muislamu kujiombea mwenyewe na wanawe.  Ni uzuri ulioje yeye na wanaye kuwa ni wenye kusimamisha Swalaah kama inavyotakikana!  Haya ni katika mafanikio makubwa kabisa ya kumshukuru Allaah.

 

Faida kutokana na du’aa hii:

 

1-  Umuhimu wa Swalaah. Ameikhusisha hapa pasi na ‘ibaadah nyinginezo.

 

2-   Umuhimu wa kutawassali kwa Urabb wa Allaah Ta’aalaa kwa kuwa kujibiwa du’aa kwalo ni katika mihimili muhimu.

 

3-  Umuhimu wa kukazania jambo katika du’aa.  Katika sentensi moja ya du’aa hii, Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) amekariri neno la Rabb mara mbili.

 

4-  Mwombaji anatakiwa akithirishe kumwomba Allaah Amtakabalie du’aa yake.

 

5-  Kila mwombaji anatakiwa ajiombee mwenyewe, wazazi wake na dhuria wake.

 

6-  Du’aa ndio makimbilio ya Manabii wote, Mitume na Swalihina, bali viumbe vyote.

 

7-  Kama unawajibika kuswali Swalaah tano, basi usivimbe kichwa na kuwadharau wengine wasiowajibika.  Jua kwamba hiyo ni tawfiyq ya Allaah kwako.  Jaribu kuwakumbusha na kuwaombea Allaah Awahidi.  Hao ni nduguzo katika dini ingawa ni mafasiki.

 

8-  Jaribu kuwazoeza watoto Swalaah tokea udogoni mwao.  Uwafundishe pia namna ya kuswali kama inavyotakikana, uwapeleke chuoni wakajifunze Qur-aan kuisoma kwa kurattil, kwani kisomo sahihi ndani ya Swalaah ni katika vipengele vya kuikamilisha.

 

Wewe pia jifunze kuswali Swalaah sahihi.  Watu wazima wengi wanaswali kwa makosa, kisomo chao ni cha mashaka mashaka na hukmu nyingi hawazijui. Tumia muda wako kujifunza yote yanayotakikana katika Swalaah, kwani Swalaah ikikubaliwa, ‘amali zako zote zitakubaliwa, na ikikataliwa, basi ‘amali zako nyingine zote zitakataliwa.  Tahadhari ndugu Muislamu kwa hili.

 

Kama hujui, usione haya kumtaka Shekhe wako akufundishe kivitendo hata kama kwa kumlipa.  Pia ondosha ujinga wa kutoweza kuisoma Qur-aan kama inavyotakikana.  Ni mangapi ya kidunia tunayalipia na kupoteza muda wetu kwayo?!  Chunga sana hatima yako ndugu yangu Muislamu.

                                                                         

 

 

 

Share