21-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Kukiri Kosa Kwa Kumtakasa Allaah

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

21- Kukiri Kosa Kwa Kumtakasa Allaah

 

 

 

 

"لا إِلَهَ إِلا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ"

 

“Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Subhaanak! Utakasifu ni Wako, hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu”.  [Al-Anbiyaa: (87)]

 

Dhulma maana yake ni kukiweka kitu mahala pasipo pake;  ima kwa kukipunguza au kukiongeza, au kukitoa nje ya wakati wake au mahala pake. Dhulma ziko za aina tatu:

 

Ya kwanza:  Dhulma kati ya mtu na Allaah Ta’aalaa.  Dhulma kubwa hapa ni shirki na ukafiri.

 

Ya pili:  Dhulma kati ya mtu na mtu.

 

Ya tatu:  Dhulma kati ya mtu na nafsi yake mwenyewe.

 

Hii ni du’aa ya Nabiy Yuwnus (‘Alayhis Salaam). Allaah ‘Azza wa Jalla Alimtuma kwa watu wa Naynawa nchini Iraki.  Akawalingania wamwamini Allaah na wamwabudu, lakini watu hao walikataa na kubobea zaidi kwenye ukafiri.  Akawaahidi kwamba adhabu ya Allaah itawashukia baada ya siku tatu. Naye akatoka kujitenga nao akiwa amewaghadhibikia kabla Allaah Hakumwamuru kufanya hivyo huku akidhani kwamba Allaah Hatomtia mtihanini.  Watu wake hao walipopata uhakika kuwa Nabiy wao ameondoka na kuwaacha na huku wanajua kwamba Nabiy hasemi uongo, walitoka pamoja na watoto wao, wanyama wao na mifugo yao kwenda jangwani.  Huko wakamwomba Allaah msamaha kwa unyenyekevu mkubwa na kumlilia.  Allaah Akawaondoshea adhabu waliyoahidiwa.  Allaah Anasema:

 

" فَلَوْلَا كَانَتْ قَرْيَةٌ آمَنَتْ فَنَفَعَهَا إِيمَانُهَا إِلَّا قَوْمَ يُونُسَ لَمَّا آمَنُوا كَشَفْنَا عَنْهُمْ عَذَابَ الْخِزْيِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَمَتَّعْنَاهُمْ إِلَى حِينٍ"

 

“Basi kwa nini usiweko mji mmoja ukaamini na iymaan yake ikawafaa - (haukutokea) isipokuwa kaumu ya Yuwnus.  Walipoamini, Tuliwaondoshea adhabu ya hizaya duniani, na Tukawasterehesha mpaka muda maalumu”. [Yuwnus: (98)]

 

Ama Yuwnus, yeye alikwenda na kupanda jahazi pamoja na watu wengine. Jahazi likazidiwa uzito na wakahofia kughariki.  Ikabidi wapige kura ya kumtosa mtu mmoja baharini.  Kura ikaangukia kwa Yuwnus, lakini walikataa kumtosa.  Wakairudia mara tatu, lakini ikaangukia kwake vile vile.  Allaah Anasema:

 

"فَسَاهَمَ فَكَانَ مِنَ الْمُدْحَضِينَ"

 

“Akapiga kura ya vishale, akawa miongoni mwa walioshindwa”[As-Swaaffaat: (141)] 

 

Yuwnus akajitupa mwenyewe baharini.  Allaah Akampelekea nyangumi mkubwa, Akamwamuru asimle bali ammeze tu ili tumbo lake liwe ni jela kwake. Hapo akawa ndani ya magiza matatu;  la tumbo la nyangumi, la bahari na la usiku.  Naye bila kuchelewa akaelekea kwa Mola wake kumwomba Amwokoe toka ndani ya zahama hii ngumu akisema:

 

"لا إِلَهَ إِلا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ"

 

“Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Subhaanak!  Utakasifu ni Wako, hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu”.

 

Naye Allaah Ta’aalaa Akamkubalia du’aa yake na kumwokoa toka ndani ya tumbo hilo.

 

Ameitaja dhulma kwa nafsi yake mwenyewe, na kwamba yeye mwenyewe amepita njia ya wenye kujidhulumu wenyewe.  Naye hakuomba toka kwa Allaah msamaha kwa tamko wazi la kuomba ili kumhisisha kwamba yeye ni mwovu dhalimu, naye ndiye aliyejiletea madhara kwa nafsi yake mwenyewe na Allaah Hakumdhulumu.  Ni kana kwamba anamwambia Allaah Ta’aalaa: “Ukiniadhibu, basi ni kutokana na Uadilifu Wako, na kama Utanisamehe, basi ni kutokana na Rahma Zako”.

 

 

Du’aa hii imekusanya mambo matatu makuu:

 

 

1-  Imethibitisha Uungu wa Allaah ‘Azza wa Jalla; (Laailaaha illaa Anta).

 

2-  Imethibitisha ukamilifu wa kumtakasa Allaah na kila kasoro;  (Subhaanak).

 

3-  Kukiri kosa na kuomba maghfirah kwa kusema kwamba yeye amekuwa katika madhalimu kwa kosa tu la kuondoka kabla ya kupewa idhini na Allaah.

 

Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:

 

1-  Du’aa kama inavyokuwa kwa tamko wazi la ombi, inakuwa vile vile kwa tamshi la kuashiria.

 

2-  Tamshi hili limekusanya adabu za du’aa na sababu za kujibiwa.  Inapendeza kama Muislamu atalikithirisha wakati anapoomba du’aa na hususan anapozongwa na matatizo na misukosuko.

 

3-  Ndani yake kuna tawhiyd kamili na iymaan kwa Allaah.  Inapendeza kwa mwombaji ayajumuishe haya kwenye du’aa yake yoyote.

 

4-  Kuna dalili kwamba kumsabbih Allaah kunatakikana zaidi mtu anapokabiliwa na misukosuko mikubwa, ghamu na hamu.  Ni kama Anavyosema Allaah:

 

"وَلَقَدْ نَعْلَمُ أَنَّكَ يَضِيقُ صَدْرُكَ بِمَا يَقُولُونَ * فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَكُنْ مِنَ السَّاجِدِينَ"

 

“Na kwa yakini Tunajua kwamba kifua chako kinadhikika kwa yale wanayoyasema  ●  Basi sabihi na mhimidi Rabb wako na uwe miongoni mwa wanaosujudu”.  [Al-Hijri: (97)]

 

 

5-  Kwamba tawhiyd, iymaan kamili na kukiri madhambi ni moja ya sababu kubwa za kuokoka kutokana na maafa ya dunia na aakhirah.

 

6-  Madhambi ni katika sababu kubwa zinazopelekea kuondoka neema na kuandamwa mtu na nakama.

 

7-  Majanga yanayomwandama mtu sababu yake ni kutowajibika ipasavyo na makalifisho ya kisheria.

 

8-  Viumbe wote vyovyote daraja zao ziwavyo, wanamhitajia Allaah.  Hivyo ni lazima wakimbilie Kwake Pekee.

 

 

 

Share