22-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Kuomba Mtoto

 

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

 

22-Kuomba Mtoto

 

 

 

"رَبِّ لا تَذَرْنِي فَرْدًا وَأَنتَ خَيْرُ الْوَارِثِينَ"

 

Rabb wangu! Usiniache pekee.  Nawe Ndiye Mbora wa wenye kubaki”.  [Al-Anbiyaa: (89)].

 

 

Hii ni du’aa nyingine ya Nabiy Zakariyyaa (‘Alayhis Salaam).  Ndani ya maneno yake kwa mujibu wa aayah, ipo du’aa ya kuomba mtoto.  Ni muundo mzuri murua uliojaa adabu katika kuwasilisha ombi kwa Mola wa walimwengu.

 

Katika du’aa hii anasema:  “Ee Rabbi wangu!  Usiniache mpweke bila mtoto wala wa kunirithi, kwani Wewe Ndiye Mbora Utakayesalia baada ya viumbe vyote kufa”.

 

Hapa amemsifu Allaah kwa Sifa hiyo ya kubakia milele bila mwisho sambamba na ombi lake hilo la kutaka aruzukiwe mtoto wa kumrithi baada ya yeye kufa na kuendeleza mema yake.

 

Na hapo hapo Allaah Akamjibu ombi lake hilo, na Akamruzuku Nabiy mwema Aliyemuita Yahyaa.  Si hivyo tu, bali Alimpa mkewe uzazi mwingi baada ya kuwa tasa kuonyesha Ukamilifu wa Uwezo Wake Ta’aalaa Ambaye hakuna kiwezacho kumshinda ardhini na mbinguni.  Anatuambia:

 

"فَاسْتَجَبْنَا لَهُ وَوَهَبْنَا لَهُ يَحْيَىٰ وَأَصْلَحْنَا لَهُ زَوْجَهُ"

 

“Basi Tukamuitikia na Tukamtunukia Yahyaa, na Tukamtengenezea mke wake”.  [Al-Anbiyaa: (90)]

 

Kisha Allaah Ta’aalaa Akabainisha sababu ya kwa nini Alimjibu du’aa Akisema:

 

"إِنَّهُمْ كَانُوا يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَيَدْعُونَنَا رَغَبًا وَرَهَبًا ۖ وَكَانُوا لَنَا خَاشِعِينَ"

 

Hakika wao walikuwa wakikimbilia katika mambo ya khayr na wanatuomba kwa raghba na khofu, na walikuwa wenye kutunyenyekea”.  [Al-Anbiyaa: (90)]

 

Kuharakia mambo ya kheri ni katika sababu za kujibiwa du’aa ya Muislamu. Hawa walikuwa wakiyaharakia mambo yote ya kheri kwa aina zake na maumbo yake yote katika nyakati zake bora.  Si hivyo tu, bali walikuwa wakiyatenda kwa ufanisi utakiwao huku wakiwa wanyenyekevu katika hali zote na katika nyakati zote.  Na hili ndilo ambalo Muislamu anatakiwa aliige toka kwa watu hawa wema.

 

Katika aayah, tamshi la kuomba limekuja kwa muundo wa kitenzi cha wakati uliopo “wanatuomba” kwa faida mbili:

 

Ya kwanza:  Ni kwamba walikuwa wakikithirisha sana hilo na kudumu nalo.

Ya pili:  Kuleta picha yao nzuri katika akili zetu.  Ni kama vile msemeshwa anaiona picha yao hivi sasa ikimwathiri na kumfanya aige kitendo chao hicho.

 

 

Tunajifunza yafuatayo kutokana na du’aa hii:

 

 

1-  Muislamu hatakiwi kukata tamaa kwa jambo lolote.  Ni lazima awe na yakini kamili kuwa Allaah Ana uwezo wa kulifanya lisilowezekana kwa nadhari zetu kuwa linawezekana.

 

 

2-  Kuruzukiwa watoto ni katika neema kubwa.  Neema hiyo hukamilika ikiwa watoto ni wema watakaowafaa wazazi duniani na aakhirah.

 

 

3-  Miongoni mwa sababu za kujibiwa du’aa ni kuwa na shime na mambo ya kheri kwa mujibu wa uwezo wa mtu, na kudumu kumwomba Allaah nyakati zote na mahala popote.

 

 

4-  Du’aa huombwa kwa raghba ya kuomba maslaha ya dunia na aakhirah, na khofu ya kuomba hifadhi ya mambo yanayoogopwa ya duniani na ya aakhirah.

 

 

5-  Unyenyekevu ni dalili ya iymaan ya kweli ya mja kwa Mola wake.

 

 

 

 

Share