23-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Kinga Dhidi Ya Udokezi Wa Mashaytwaan

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

23-Kinga Dhidi Ya Udokezi Wa Mashaytwaan

 

 

 

 

"رَبِّ أَعُوذُ بِكَ مِنْ هَمَزَاتِ الشَّيَاطِينِ * وَأَعُوذُ بِكَ رَبِّ أَنْ يَحْضُرُونِ"

 

Rabb wangu! Najikinga Kwako kutokana na udokezi wa mashaytwaan  ●  Na najikinga Kwako Rabb wasinihudhurie”.  [Al-Muuminuuna: (97-98)]    

 

Kwanza, ni muhimu mno kujua kwamba kujilinda kwa Allaah ni katika aina za du’aa.

 

Pili, Allaah kwa Hikmah Yake Ameumba shari katika nyumba hii ya dunia. Ameumba shari kubwa zaidi, chimbuko lake, asili yake na sababu yake kuu ambaye ni shaytwaan aliyewekwa mbali na Rahmah Zake.  Kati ya hikmah za hili, ni kututahini na kutujaribu ili tuweze kukabiliana na shari hizi tuweze kufaulu duniani na aakhirah.  Pepo ya Allaah ni ghali mno, na cha ghali hakiwezekani kupatikana kwa urahisi.

 

Na kwa vile Mashaytwan wanatuona lakini sisi hatuwaoni kama Alivyosema Allaah:

 

"إِنَّهُ يَرَاكُمْ هُوَ وَقَبِيلُهُ مِنْ حَيْثُ لَا تَرَوْنَهُمْ"

 

“Hakika yeye (Ibliys) anakuoneni, yeye na kabila lake (la mashaytwaan) na hali ya kuwa nyinyi hamuwaoni”… Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Ametuamuru tujilinde nao Kwake kutokana na shari yao kubwa iliyo karibu yetu.

 

Katika aayah, wametajwa mashaytwani, na si shaytwani mmoja.  Hii inaonyesha kuwa ni wengi na wako wa aina mbalimbali, na inatupa picha zaidi kuhusu hatari yao kwetu.  Na kwa ajili hiyo, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akijilinda na aina zote za shari za mashaytwaan akisema:

 

"أَعُوذُ بِاللَّهِ مِنَ الشَّيْطَانِ: مِنْ نَفْخِهِ، وَنَفْثِهِ، وَهَمْزِهِ"

 

“Najilinda kwa Allaah na shaytwaan; kutokana na kiburi chake, mashairi yake na ujununi wake”.  [Abu Daawuwd: Kitaabu As-Swalaat]

 

Haya ambayo Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amejilinda nayo, yanaingia kiujumla kwenye udokezi wa mashaytwan uliotajwa kwenye aayah.  Mbali ya udokezi huo, mashaytwaan hawa wanaingia kwenye kila jambo katika mambo yetu.  Na hii ni hatari kubwa sana!  Hilo Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amelieleza akisema:

 

"إنَّ الشَّيْطَانَ يَحْضُرُ أَحَدَكُمْ عِنْدَ كُلِّ شَيْءٍ مِنْ شَأْنِهِ، حَتَّى يَحْضُرَهُ عِنْدَ طَعَامِه..."

 

“Hakika shaytwaan anamhudhuria mmoja wenu kwenye kila jambo katika mambo yake.  Hata anamhudhuria wakati anapokula”.  [Swahiyh.  Imesimuliwa na Jaabir bin ‘Abdillaah]

 

Kila jambo katika jambo lake!  Hebu angalia hatari hii kubwa kwetu!.  Ukila uko nao!  Ukilala uko nao!  Ukiswali uko nao!  Ukiingia msalani uko nao, na hao ni wa aina nyingine!  Na kitambo kibaya na hatari zaidi unachokuwa nao ni pale kabla ya kutoka roho.  Hapa hutumia mbinu zote kukuzuga ili ufe ukiwa si Muislamu.  Tunamwomba Allaah Atupitishe salama hapo.  Ni kwamba shughuli yoyote uifanyayo, basi ujue uko nao!  Hawakuachi!  Ila tu kama utajilinda kwa Allaah.  Na hapo unakuja umuhimu wa kujilinda na kiumbe huyu katika hali zote.

 

Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwafundisha Maswahaba maneno ya kusema wakati wanaposhtuka usingizini.  ‘Abdullaah bin ‘Amri bin Al-‘Aaswiy amesema:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"إذا فَزِعَ أحَدُكم في النوم فَلْيَقُلْ: أَعوذ بكلمات اللَّه التَّامَّة من غضبه، وعِقَابِهِ، وشرِّ عِبادِهِ، ومن هَمَزَاتِ الشَّياطينِ، وأنْ يَحضُرونِ، فإنَّها لَنْ تَضُرَّهُ"

 

“Akishtuka mmoja wenu usingizini basi aseme:  Najilinda kwa Maneno ya Allaah Yaliyotimia kutokana na Ghadhabu Yake na Adhabu Yake, na shari ya waja Wake, na kutokana na uchochezi wa mashaytwaan na kunihudhuria mimi.  Hakika hawatomdhuru”.  [At-Tirmidhiy: Kitaabu Ad-Da’awaat].

 

 

Tunajifunza kutokana na isti’aadhah hii haya yafuatayo:

 

 

1-  Kujilinda kwa Allaah ni katika aina za du’aa, na Mlinzi wa yote ni Allaah Pekee.  Haijuzu kabisa kujilinda kwa asiye Allaah kwani hilo ni katika shari mbaya.  Allaah Anasema:

 

"وَأَنَّهُ كَانَ رِجَالٌ مِنَ الْإِنْسِ يَعُوذُونَ بِرِجَالٍ مِنَ الْجِنِّ فَزَادُوهُمْ رَهَقًا"

 

Na kwamba walikuwa wanaume miongoni mwa wana Aadam wanajikinga na wanaume miongoni mwa majini, basi wakawazidishia madhambi, uvukaji mipaka ya kuasi na khofu.  [Al-Jinn: (06)]

 

2-  Shaytwaan ana hatari kubwa kwa mwanadamu. Anamvizia katika hali zake zote.  Na kwa ajili hiyo, ni muhimu sana kujilinda naye nyakati zote.

 

 

Share