28-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Hikmah Na Kukutanishwa Na Watu Wema

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

28-Hikmah Na Kukutanishwa Na Watu Wema

 

 

 

"رَبِّ هَبْ لِي حُكْمًا وَأَلْحِقْنِي بِالصَّالِحِينَ* وَاجْعَلْ لِي لِسَانَ صِدْقٍ فِي الآخِرِينَ * وَاجْعَلْنِي مِن وَرَثَةِ جَنَّةِ النَّعِيمِ"

 

“Rabb wangu! Nitunukie hikmah (elimu ya Dini) na Unikutanishe na Swalihina  •  Na Nijaalie kusifika kwa heshima kwa vizazi watakaokuja baadaye  •  Na Nijaalie miongoni mwa warithi wa Jannah ya neema”.  [Ash-Shu’araa: (83-85)].

 

Baada ya Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) kuzielezea Sifa kochokocho za Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa kama kuwa Yeye Amemuumba na Anamwongoza, Anamlisha na Anamnywesha, anapokuwa mgonjwa Anamponyesha, Anamfisha na kisha Atamfufua, na yeye anatumai kuwa Atamghufuria makosa yake Siku ya malipo, baada ya yote hayo, akaleta du’aa yake hii.  Hii ni katika tawassulaat kubwa kabisa zenye kuwajibisha kujibiwa na kukubaliwa du’aa kama tulivyogusia katika du’aa zilizopita.

 

Amemwomba Allaah Amtunukie hikmah.  Hikmah hapa ni kumjua Allaah, kujua Mipaka Yake, na kujua Hukmu Zake.  Yaani anaomba Allaah Amtunuku ‘ilmu ya kujulia ahkaam, halali na haramu ili aweze kuhukumu kwayo baina ya watu.  Hikmah ni jambo la kuliomba sana, kwani mwenye kupewa hikmah anakuwa amepewa kheri nyingi sana kama Alivyolielezea hilo Allaah Ta’aalaa.

 

Amemwomba pia Amkutanishe na Swalihina.  Yaani awe pamoja na watu hao hapa duniani na kesho aakhirah.  Ni kama alivyosema Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati alipokuwa karibu kukata roho:

 

اللَّهُمّ في الرفيق الأعلى

 

“Ee Allaah!  Pamoja na Ar-Rafiyq Al-A’alaa  [Uliowaneemesha katika Manabii, Swiddiyqiyna, Shuhadaa na Swalihina katika daraja za juu za Jannah]”.  [Muslim:  Kitaabu  Fadwaailis Swahaabah]

 

 

Na takwa hili lilikuwa vile vile ni katika maombi ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Alikuwa anaomba:

 

"اللَّهُمَّ تَوَفَّنَا مُسْلِمِينَ، وَأَحْيِنَا مُسْلِمِينَ، وَأَلْحِقْنَا بِالصَّالِحِينَ، غَيْرَ خَزَايَا وَلَا مَفْتُونِين"

 

“Ee Allaah!  Tufishe tukiwa Waislamu, Tuhuishe tukiwa Waislamu, na Tukutanishe pamoja na Swalihina bila kuwa wenye kuhizika wala kufitinika”. [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh]

 

Muislamu anatakiwa asuhubiane na watu wema hapa duniani, kwani rahmah, amani na uongofu vinawazunguka watu hao.  Afanye hivyo ili aweze kusuhubiana nao huko aakhirah na kuwa ngazi moja nao hata kama hakufanya matendo yao kama alivyosema Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"الْمَرْءُ مَعَ مَنْ أَحَبَّ"

 

“Mtu atakuwa pamoja na anayempenda”.  [Al-Bukhaariy 6169 na Muslim 2640]

 

Amemwomba pia Allaah Amjaalie awe mwenye kusifika kwa heshima kwa vizazi watakaokuja baadaye.  Awe na utajo mzuri wa kheri kati ya watu, na sifa njema kwa vizazi vijavyo baada yake.  Utajo mwema huvutia du’aa za watu kwake na kumfanya kiigizo chema kwao.  Na hii ni faida kwao na kwake hadi Siku ya Qiyaamah.  Allaah Ta’aalaa Akamjibu du’aa yake hii, Akampa ‘ilmu kubwa na hikmah, Akamfanya kuwa katika Mitume bora, Akamfanya mwenye kupendwa na kukubalika, na mwenye kutukuzwa na kusifiwa katika mila zote na zama zote.

 

Na kwa muktadha huu, hakuna ubaya mtu kupenda kusifiwa kwa ‘amali zake njema, na kuonekana kwenye ‘amali za Swalihina kama atakusudia kwa hilo Wajihi wa Allaah.  Wanasema:  “Watu wamekufa nailhali wako hai kati ya watu”, yaani kwa kutajwa kwa mema yao, na wasifu wao uliotukuka.

 

Na baada ya Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) kumwomba Allaah furaha ya dunia, alimwomba pia furaha nyingine ya milele akisema:  “Na Nijaalie miongoni mwa warithi wa Jannah ya neema”.  Allaah Akamjibu ombi lake hili, na kuinyanyua ngazi yake juu kwenye Pepo za kudumu milele.  Tunamwomba Allaah Atujaalie tuingie ndani ya du’aa hii ya Khaliylur Rahmaan. Aamiyn.

 

 

Katika hili, Allaah Anawahimiza Waja Wake wawe na hima ya nguvu katika kuomba mfano wa du’aa hizi za barakah zilizokusanya kheri za dunia na aakhirah.

 

 

Share