29-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Kutohizishwa Siku Ya Qiyaamah

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

 

29-Kutohizishwa Siku Ya Qiyaamah

 

 

 

"وَلا تُخْزِنِي يَوْمَ يُبْعَثُونَ * يَوْمَ لَا يَنْفَعُ مَالٌ وَلَا بَنُونَ * إِلَّا مَنْ أَتَى اللَّهَ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ"

 

“Na wala Usinihizi Siku watakayofufuliwa  •  Siku hayatofaa mali wala watoto  •  Isipokuwa yule atakayemfikia Allaah na moyo uliosalimika”.  [Ash-Shu’araa: (87-89)].

 

Huu ni mwendelezo wa du’aa zilizotangulia za Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis Salaam).  Anamwomba Allaah Asimkhizi Siku ya Qiyaamah watu wakatapofufuliwa.  Khiizaya ni udhalili na unyonge.  Anaomba akingwe na udhalili na unyonge wa Siku hiyo.  Hakuna udhalili na unyonge wa mfano wa Siku hiyo.  Watu watanyongeka na kudhalilika kutokana na kashfa ya madhambi yao makubwa waliyokuwa wakiyafanya kwa siri na dhahiri. Madhambi hayo yatawatesa mno kabla ya adhabu yenyewe kuwafikia.  Na hata hii pia ilikuwa ni du’aa ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyekuwa akiomba:

 

" اللَّهُمَّ لا تُخْزِنِي يَوْمَ الْقِيَامَةِ , وَلا تُخْزِنِي يَوْمَ الْبَأْسِ ؛ فَإِنَّ مَنْ أَخْزَيْتَهُ يَوْمَ الْبَأْسِ فَقَدْ أَخْزَيْتَهُ

 

“Ee Allaah! Usinikhizi Siku ya Qiyaamah, wala Usinikhizi Siku ya adhabu kali, kwani Utakayemkhizi Siku ya adhabu kali, basi kwa hakika Umemkhizi”.  [Riwaayah ya Imam Ahmad.  Al-Arnaauwtw kasema ni Swahiyh katika Musnad wa Ahmad]

 

Halafu akataja sababu ya ombi lake hilo kwa Siku hiyo ngumu akisema: “Siku hayatofaa mali wala watoto  ●  Isipokuwa yule atakayemfikia Allaah na moyo uliosalimika”.  Kwa maana kuwa hakuna chochote kitakachoweza kumkinga mtu na adhabu ya Allaah hata kama ataijaza ardhi dhahabu na watu isipokuwa atakayemjia Allaah na moyo uliosalimika na kila mabaya, maradhi ya shubha kama shirki, shaka, unafiki, na kushabikia mambo ya bid’a, hawaa za kinafsi na mengineyo angamizi.  Moyo umetajwa hapa kwa kuwa ndio chimbuko la uzuri na ubaya wa kiwiliwili cha mtu.  Ukiwa salama, basi viungo vyote vinakuwa salama, na ukiharibika basi viungo vyote vinaharibika.  Na hili ndilo lililokuwa ombi la Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) la kuwa na moyo salama. Alikuwa akiomba:

 

"اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ الثَّبَاتَ فِي الْأَمْرِ، وَالْعَزِيمَةَ عَلَى الرُّشْدِ، وَأَسْأَلُكَ شُكْرَ نِعْمَتِكَ، وَحُسْنَ عِبَادَتِكَ، وَأَسْأَلُكَ قَلْبًا سَلِيمًا، وَلِسَانًا صَادِقًا"

 

“Ee Allaah!  Hakika mimi nakuomba uthabiti katika jambo (Dini ya Allaah) bila kutetereka, na azima ya kupania mambo ya kheri yenye kufaulisha.  Na ninakuomba kuzishukuru Neema Zako, kukuabudu kama inavyotakikana, na ninakuomba moyo uliosalimika na ulimi usemao kweli”.  [Sunan An-Nasaaiy.  Al-Arnaauwtw kasema ni Hasan Lighayrih]

 

 

Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:

 

 

1-  Kuwa inapendeza zaidi kwa mwombaji akusanye katika du’aa yake kheri za dunia na aakhirah, na nyumba ya aakhirah iwe ndio makusudio yake makuu.

 

 

2-  Mwombaji amwombe Allaah Amzidishie ‘ilmu na hikmah kwa yatakayomnufaisha katika dini yake, dunia yake na aakhirah yake.

 

 

3-  Mwombaji anatakiwa amwombe Allaah Ta’aalaa Amjaalie kuwa pamoja na watu wema duniani na aakhirah.  Pia Amruzuku utajo mwema hapa duniani kutokana na faida zifuatazo:

 

 

(a) Kufanywa kiigizo chema na watu.

 

 

(b) Kuombewa du’aa na watu.

 

 

(c) Kukubaliwa kirahisi katika ushahidi, kutoa nasaha, kutatua migogoro na kadhalika.

 

 

4-  Umuhimu wa kutawassal kwa Sifa za Allaah Ta’aalaa ikiwemo Sifa ya kivitendo ya Kutunuku kama ilivyo katika du’aa nyingi za Qur-aan Tukufu. Katika hili kuna ukamilifu wa adabu, utukuzaji na usifuji kwa Allaah Ta’aalaa.

 

 

5-  Kutaja sababu ni katika uzuri wa du’aa.

 

 

6-  Ni vizuri kwa mwombaji awaombee wazazi wake wawili hata kama hawako kwenye hali ya uongofu au hali tengefu.

 

 

7-  Manabii na Mitume wote wanaiogopa Siku ya Qiyaamah.

 

 

8-  Moyo ni kinofu muhimu zaidi mwilini. Kikiwa kizima, basi mwili wote unapata uzima, na kikiharibika, nao mwili wote unaharibika.

 

 

9-  Mja anatakiwa asighurike kwa matendo yake. Ikiwa Imamu wa Manabii ambaye amepewa mambo makubwa ya kuhimidiwa anaiogopa Siku hiyo, basi  sisi ndio tunatakiwa tuiogope zaidi.

 

 

Share