30-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Kuzinduliwa Kuzihisi Na Kuzishukuru Neema

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

 

30- Kuzinduliwa Kuzihisi Na Kuzishukuru Neema

  

 

 

 "رَبِّ أَوْزِعْنِي أَنْ أَشْكُرَ نِعْمَتَكَ الَّتِي أَنْعَمْتَ عَلَيَّ وَعَلَى وَالِدَيَّ وَأَنْ أَعْمَلَ صَالِحًا تَرْضَاهُ وَأَدْخِلْنِي بِرَحْمَتِكَ فِي عِبَادِكَ الصَّالِحِين"

 

“Rabb wangu!  Nipe ilhamu na uwezo nishukuru Neema Yako ambayo Umenineemesha juu yangu na wazazi wangu, na nipate kutenda mema Utakayoridhia, na Niingize kwa Rahmah Yako katika Waja Wako Swalihina. [An-Naml: (19)]

 

Hii ni du’aa ya Nabiy Sulaymaan (‘Alayhis Salaam).  Allaah Alimpa Utume na ufalme, Akamfundisha lugha za ndege, naye akawa ni mwingi wa kushukuru neema zote hizo.

 

Katika du’aa hii, amemwomba Allaah Amzindushe na Ampe tawfiyq ya kuendelea kuzishukuru Neema Zake kwake zisizokokoteka wala kuhesabika. Katika hili amewajumuisha pia wazazi wake wawili kwa ajili ya kukithirisha neema hizo, kwani neema aliyo naye yeye manufaa yake yanarejea kwao vile vile.

 

Huu ndio ukamilifu na uzuri wa kushukuru Neema za Allaah ambapo neema kubwa zaidi ni Uislamu ambao ni tunu isiyolinganishwa na chochote Aliyotutunukia sisi Allaah bila kumwomba.  Na wengi neema hii hawaihisi wala hawaithamini kabisa. Mtu Muislamu lakini Uislamu hataki kujifunza.  Anaitupa bahati kubwa aliyonayo mkononi.

 

 

Kadhalika, amemwomba Allaah Mtukufu Amwezeshe kutenda amali yoyote ile njema ya kumridhisha Allaah iwe kwa ulimi, kwa moyo, au kwa viungo.  Si kila amali aifanyayo mtu inamridhisha Allaah Subhaanah kwani inaweza kuwa na mapungufu ya riyaa, kujiona, shirki na kadhalika.  Mtu lazima ajiepushe na hayo na aifanye amali yake kwa ikhlasi safi.

 

Akamwomba pia Amuingize Peponi Nyumba ya Rahmah Zake pamoja na Waja Wake wema ambapo haingii yeyote isipokuwa kwa Rahma za Allaah na si kwa amali zake vyovyote ziwavyo.  Na ndipo akaomba akisema:  “Na Niingize kwa Rahmah Zako”, na si kwa amali zangu, pamoja na Waja Wako wema kwenye Jannaat Zako za daraja ya juu kabisa ambazo haingii isipokuwa Swalihina.

 

 

Nabiy huyu ameomba ukamilifu wa furaha za dunia na aakhirah ambazo ni:

 

 

- Kuwezeshwa kuzishukuru Neema za Allaah zisizokokoteka.

 

 

- Kufanya ‘amali zenye kuridhiwa.

 

 

- Kusuhubiana na viumbe wema.

 

 

Kuna faida kadhaa kutokana na du’aa hii:

 

 

1-  Umuhimu wa kumwomba Allaah Atusaidie katika kumtii na hususan kumshukuru ambako kunawajibisha kuzilinda neema za dunia na aakhirah.  Na haya ndiyo makusudio ambayo Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiyaomba akisema:

 

"اللَّهُمَّ أَعِنِّي عَلَى ذِكْرِكَ وَشُكْرِكَ وَحُسْنِ عِبَادَتِكَ"

 

“Ee Allaah!  Nisaidie katika kukudhukuru, kukushukuru na kukuabudu itakikanavyo”.  [Abuu Daawuwd: Kitaabul Witr.  Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh]

 

 

2-  Neema ya Uislamu ndio neema kubwa zaidi kuliko zote.  Na kwa ajili hiyo, Rasuli (Swalla Allaah (‘Alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimwomba Allaah Ta’aalaa Amtimizie na Amhifadhie neema hii akisema:

 

"اللهمَّ احْفَظْنِي بِالإسلامِ قائِمًا ،واحْفَظْنِي بِالإسلامِ قاعِدًا ،واحْفَظْنِي بِالإسلامِ رَاقِدًا"

“Ee Allaah!  Nijaalie mwenye kushikamana na Uislamu katika hali ya kusimama kwangu, Nijaalie mwenye kushikamana na Uislamu katika hali ya kukaa kwangu, na Nijaalie mwenye kushikamana na Uislamu katika hali ya kulala kwangu”.  [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Swahiyhul Jaami’i].

 

 

3-  Sifa ya kuridhia ni katika Sifa za Allaah Ta’aalaa.  Nayo ni Sifa ya kivitendo inayohusiana na Matakwa Yake ‘Azza wa Jalla.

 

 

4-  Kuziamini Sifa za Allaah Ta’aalaa ni chachu ya ‘amali na kauli njema.

 

 

5-  Sifa ya utumwa kwa Allaah ndio sifa kubwa zaidi kuliko zote.

 

 

6-  Umuhimu wa kuomba kusuhubiana na kuwa pamoja na Swalihina.

 

 

7-  Kuzingatia zaidi kuzitengeneza ‘amali na vitendo na maneno ili zikubaliwe na ziridhiwe na Allaah Ta’aalaa.

 

 

8-  Inapendeza zaidi kwa mwombaji awajumuishe wazazi wake wawili ndani ya du’aa yake kutokana na fadhila kubwa yao kwake.

 

 

9-  Wazazi wawili ni miongoni mwa neema kubwa zaidi za Allaah kwa mtu.

 

 

10-  Umuhimu wa kuomba du’aa za Qur-aan kwa kuwa zimekusanya maneno mafupi yenye maana pana.

 

 

Share